Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mohamed Omary Mchengerwa (15 total)

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Wilaya ya Rufiji ni Wilaya kongwe. Ni miongoni mwa Wilaya za awali, ina miaka zaidi ya 55 toka izaliwe lakini kutokana na mgawanyo wa Wilaya, Wilaya hii imebaki kuwa ni Wilaya pekee ambayo haina Mahakama ya Wilaya. Wananchi wangu wanalazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 100 kufuata huduma za Mahakama ya Wilaya. Je, ni lini Serikali itakuwa na mpango wa kujenga Mahakama ya Wilaya kuwasaidia wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji?
Mheshimiwa Naibu Spika, tofauti ya mshahara kati ya Hakimu na Jaji ni kubwa sana na kazi wanazofanya Mahakimu takribani ni kubwa kuliko wanazofanya Majaji. Nataka nifahamu Serikali inajipanga vipi kuboresha maslahi ya Mahakimu katika suala zima la mishahara, msaada wa nyumba (house allowance) pamoja na non-practicing allowance kwa Mahakimu nchi nzima?
WAZIRI WA SHERIA NA KATIBA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuchomekea maslahi ya Jimbo lake la Rufiji katika swali hili. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara inaelewa hali maalum ambayo Jimbo lake inayo hasa baada ya kumegwamegwa, tumepata hapo Kibiti na Mafia na tunaelewa kabisa kwamba miundombinu ya Mahakama katika Jimbo lake ni mbaya. Naomba nimhakikishie katika mpango wa Mahakama wa miaka mitano, suala la miundombinu ya Mahakama ya Rufiji tutalitilia maanani sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu tofauti ya mishahara ya Mahakimu na Majaji, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba tunaangalia pia mishahara ya maafisa ya Mahakama walioko chini. La msingi tu ni kwamba ili kukidhi matakwa ya Kimataifa na pia matakwa yetu ya kikatiba, ni lazima tufikie vigezo vya kuwalipa Majaji vizuri wasiwe na vishawishi vya kuweza kuchukua rushwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri katika hili kwa upande wa Majaji Tanzania tumefanikiwa sana. Kazi yetu kubwa ni kuangalia Mahakama za chini siyo tu Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama ya Wilaya lakini mpaka Mahakama za Mwanzo kwani kwa upande wa Mahakama za juu tumejitahidi. Nafikiri sisi ni moja ya nchi chache duniani ambazo kwa kweli tumefikia viwango stahili katika kujali maslahi ya Mahakama zetu za juu.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza Mheshimiwa Waziri atambue kwamba mimi siyo aina ya Wabunge ambao atawajibu rejareja nikamwachia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Mheshimiwa Waziri atambue kwamba mwaka 1955 Mwalimu Nyerere aliahidi ujenzi wa barabara hii akiwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya TANU, Tarafa ya Mkongo. Pia tarehe 9/9/2015, Mama Samia Suluhu aliahidi ujenzi wa barabara hii kiwango cha lami alipokuwa katika harakati za kampeni pamoja na Rais, Mheshimiwa Magufuli. Vilevile Rais wa Awamu ya Nne na Awamu ya Tatu wote waliahidi ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Mheshimiwa Waziri ametudanganya hapa kwamba barabara hii inapitika kirahisi, naomba atuambie kwamba ahadi hizi za Marais hawa zilikuwa ni ahadi hewa? Hiyo ni moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, terehe 5 Juni, 2016, Rais Magufuli akiwa Ubungo aliahidi ujenzi wa barabara ya Ubungo kwa kiwango cha lami ambapo suala hili wananchi wa Jimbo la Rufiji waliliona kwamba ni neema kwa kuwa Mheshimiwa Rais atakuja pia kuweka ahadi za namna hiyo katika Jimbo la Rufiji hususani barabara hii ya Nyamwage - Utete ambayo inategemewa na wananchi hususani akina mama. Naomba kufahamu kwamba Wizara hii ipo tayari kukiuka Ibara ya 13 ya mgawanyo sawa wa pato la taifa kwa kuwasaidia na kuhakikisha kwamba inawatendea haki maskini na wanyonge wa Jimbo langu la Rufiji? Ahsante
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, viongozi wanapotoa ahadi wanaonesha dhamira. Mimi nimhakikishie Serikali hii ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli nayo ina dhamira ya dhati ya kuwajengea Watanzania miundombinu ikiwa ni pamoja na wananchi hawa wa Rufiji kwa barabara hii anayoiongelea. Naomba nimhakikishie kwamba hiki tulichokisema humu ni cha dhati na hatudanganyi na hakuna viongozi wanaodanganya. Dhamira huwa haidanganywi, dhamira ni dhamira, kinachofuatia baada ya dhamira ni uwezo wa kuikamilisha ile dhamira ambapo inategemea na upatikanaji wa fedha pamoja mipango mbalimbali ya taifa zima kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mchengerwa kwamba barabara hii tuna dhamira ya kuijenga na namhakikishia tutaijenga katika awamu hii ya miaka ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli 10. Mimi namhakikishia kwamba hii miaka 10 ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli tutaijenga mapema sana hii barabara kama ambavyo sasa tumeitaka TANROAD Mkoa wa Pwani ianze kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa kujenga kwa lami barabara hii kama ilivyoahidiwa na Marehemu Mwalimu Nyerere kama ambavyo yeye alisema.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru huku nyuma hatuonekani inatubidi tuanze kunywa maji ya kutosha.
Swali langu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, Rufiji tunabeba asilimia 49.8 la eneo la hifadhi na misitu nikimaanisha square kilometer 6,300 ziko ndani ya hifadhi na misitu, na kati ya hizo square kilomita 13,000 ndiyo eneo kubwa la Jimbo langu la Rufiji. Wananchi wa Jimbo la Rufiji wana masikitiko makubwa katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii ambapo hatujaingiwa katika mgao wa madawati.

Waziri, umetumia kigezo gani kugawa madawati katika maeneo ambayo wanatunza hifadhi ya misitu yetu naomba kufahamu hilo kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Rufiji?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani inawezekana anazungumzia suala la mgao wa madawati uliofanywa hivi karibuni na Wizara kupitia TANAPA na kama hivyo ndivyo ningependa tu nimueleweshe tu kwamba TANAPA ni wasimamizi au wanashughulikia masuala ya uhifadhi, lakini kwenye hifadhi za wanyamapori siyo misitu. Na kigezo kilichotumika kwa kipaumbele ni kuangalia cha kwanza kuangalia maeneo yanayopakana na hifadhi hizo za wanyamapori tena zile ambazo ziko chini ya TANAPA hilo ni kuhusu swali hilo la mgao wa juzi. Lakini kwa upana wake ni kwamba kila wakati tutakapokwenda kuangalia sasa namna ambavyo jamii zinazoishi jirani na maeneo ya hifadhi au ya wanyamapori ni ilani ya Chama cha Mapinduzi, ni content ya ilani ya Chama cha Mapinduzi kwamba hawa wanaoishi jirani ndiyo wawe wanufaika wa kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama kwenye eneo hili la misitu anakokuzungumzia kule Rufiji hali ilivyo ni hivyo alivyosema basi nakwenda kutizama kama hivi karibu tumefanya uvunaji wa aina yoyote au kama hivi karibuni limejitokeza jambo lolote ambalo lina maslahi kwa wananchi niende kuangalia kama kulitokea kasoro ya kuweza kutowahusisha wananchi ambao amewazungumzia kwenye eneo lake. Na ikiwa hivyo ndivyo basi Serikali itachukua hatua za mara moja kurekebisha.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, nina maswali mawili ya nyongeza, lakini nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo yamenipa faraja kuliko majibu ya juzi yaliyotolewa na Waziri wa Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza la nyongeza, katika kuwasaidia wakulima hao hao, bajeti ya Wizara hii ya Kilimo na Mifugo kwa mwaka huu wa fedha 2016/2017 imetenga maeneo ya kipaumbele na katika maeneo hayo ya kipaumbele Rufiji si maeneo ya kipaumbele kwa mujibu wa bajeti hii ya mwaka 2016/2017. Kama Wizara hii ingeweza kutoa kipaumbele kwa Rufiji inamaanisha kwamba tatizo la sukari hapa nchini lingeweza kwisha kabisa kwa Serikali kuwekeza na kutengeneza viwanda vikubwa vya sukari. Nataka nifahamu hawa wataalam waliomsaidia Mheshimiwa Waziri kuandaa bajeti hii wana elimu gani, darasa la saba au ni form four? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, Serikali kupitia Wizara hii ya Kilimo ilituletea sera ya kutuletea RUBADA. RUBADAhii wamekuwa wabadhirifu wakubwa wa fedha za umma ambao pia ni madalali wa viwanja na mashamba, wamesababisha anguko kubwa la uchumi Rufiji kwa kushindwa kusaidia kuleta wawekezaji katika kilimo lakini pia kushindwa kusimamia Bonde la Mto Rufiji? Nataka nisikie kauli ya Mheshimiwa Waziri hapa ni lini ataifuta hii RUBADAna kutuletea mradi mkubwa wa kilimo kwa ajili ya Wanarufiji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu elimu ya watendaji walionisaidia kutayarisha majibu haya, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kama zilivyo Wizara nyingi za Serikali zina wataalam waliobobea katika fani mbalimbali. Kwa hiyo, kuhusu uwezo wao hatujawahi kuutilia maanani. Kuna changamoto ndiyo katika utekelezaji tunadiriki kusema hivyo lakini haitokani na uwezo wa wataalam wetu. (Kicheko)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri unamaanisha hamjawahi kuutilia mashaka na siyo maanani? (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile nijibu swali lake kuhusu RUBADA. Ni kweli kabisa kama alivyosema Mheshimiwa Mchengerwa kwamba kumekuwepo na changamoto nyingi kuhusiana na RUBADA lakini Serikali imeifanyia marekebisho makubwa RUBADA. Mnafahamu kwamba tayari tumeshabadilisha uongozi na tunaendelea kufanyia marekebisho na bado tunaamini kwamba RUBADA itaendelea kuwa ni chombo muhimu katika lengo la Serikali la kutumia Rufiji kama sehemu muhimu sana kwa ajili ya kilimo.
Vilevile nimfahamishe Mheshimiwa Mchengerwa kwamba hatujaitenga Rufiji katika vipaumbele vyetu na ndiyo maana katika nchi nzima sehemu ya pekee ambayo imepata fedha katika bajeti yetu kwa ajili ya kilimo kwa ajili ya vijana ni Rufiji. Kwa hiyo, nimfahamishe tu kwamba Rufiji ni sehemu muhimu sana, ni bonde ambalo ni muhimu sana kwa kilimo katika nchi yetu na tutaendelea kulitumia kwa ajili ya kilimo cha mazao mbalimbali ikiwa ni pamoja na namna ya kutatua changamoto tulionayo ya sukari, tunafahamu ni bonde muhimu sana. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hatujaisahau Rufiji, hatujaisahau RUBADA tutaendelea kufanyia kazi changamoto zilizopo ili tuweze kutumia eneo hilo vizuri.

WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na majibu sahihi. Nilitaka tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu mara kwa mara amekuwa akija hata ofisini kufuatilia jambo hili pamoja na mambo mengine ya wapiga kura na mimi niwapongeze wapiga kura wake kwa kumpigia kura na kwa kweli anastahili kuwa mwakilishi wao. Nimhakikishie kwamba mimi binafsi baada ya Bunge la Bajeti nitapanga ziara na nitaongozana naye kwenda kupita haya maeneo yote ambayo amekuwa akiyalalamikia na ambayo amekuwa akiyaleta ili Serikali iweze kuchukua uamuzi tukiwa kwenye eneo la tukio.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona swali langu ni dogo tu ambalo linafanana na swali la msingi la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, utamaduni uliokuwepo wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa miaka ya nyuma uliruhusu wananchi wanaoishi kando kando mwa maeneo ya hifadhi waliruhusiwa kuvua samaki kwenye mabwawa hususan wananchi wa Jimbo langu la Rufiji wa maeneo ya Luwingo na utaratibu huu ulienda sambamba na kata zote; kata ya Mwasenimloka, kata ya Ngolongo pamoja Kagira, naomba kufahamu Wizara ya Maliasili na Utalii inaweka utaratibu gani sasa ili kuweza kuwasaidia wananchi wa maeneo haya katika kuchimba mabwawa ya samaki ili wananchi hawa wawekeza kuuza samaki hizo kuwasaidia kwa ajili ya kuwapeleka watoto wao shuleni? Ahsante.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu ya msingi ya Mheshimiwa Naibu Waziri alielezea kuhusu masuala ya kimkakati ambayo ni lazima tuyashughulikie katika kuendesha hifadhi hizi na kutokana na mabadiliko ambayo yametokea katika maeneo ya mipaka ya hifadhi zetu zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, suala hili ni moja ya masuala ya mkakati na tutajadiliana na wananchi na hasa kwenda kabisa katika maeneo hayo ili tukubaliane na wananchi namna ya kutumia maeneo hayo ya kuvua na pale inapowezekana tuwasaidie wananchi kuwa na mabwawa yao wenyewe ili kusiwe na sababu yao kwenda ndani ya hifadhi.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo ya maji katika Jimbo langu la Rufiji ni makubwa na hatuwezi kuyafananisha na Morogoro. Eneo dogo la Rufiji ambalo linapata maji safi ni Tarafa ya Ikwiriri, lakini tumeharibikiwa motor pump huu sasa mwezi wa Nane. Tuliwasilisha maombi kwa Mheshimiwa Waziri lakini mpaka leo hii hatujapata motor pump hiyo au kupata fedha kwa ajili ya ununuzi wa motor pump ili kuweza kuwasaidia wananchi wa Jimbo langu la Rufiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipate taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, ni lini sasa fedha hizi zitatoka kwa ajili ya ununuzi wa motor pump ili kuweza kuwasaidia wananchi wa Jimbo langu la Rufiji hususan Tarafa ya Ikwiriri? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa ni mwezi wa Sita na mmepitisha bajeti ya Wizara ya Maji ambayo utekelezaji wa bajeti unaanza Julai. Sasa naomba tusubiri fedha za Mwaka wa Fedha wa 2016/2017 itakapotoka ndipo tuweze kumpatia Mheshimiwa Mbunge.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli anasema kwamba msema kweli ndiyo mpenzi wa Mungu na mimi naomba niulize maswali ya kiukweli ukweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la umeme Rufiji ni takribani mwaka mmoja sasa tunapata umeme kwa saa nne tu kwa siku. Hali hii imesababisha vijana wa pale Ikwiriri kufunga viwanda vyao vidogo vya furniture kwa kuwa umeme wakati mwingine unakuja usiku. Naomba kufahamu kauli ya Serikali waliyoitoa kwamba nchi hii hakuna mgawo wa umeme, je, Rufiji siyo sehemu ya Tanzania? Hilo ni moja.
Swali la pili, wananchi hawa wa Rufiji hawana barabara hata robo kilometa, hawana maji, hawana hospitali hata X-ray machine hawana japokuwa wilaya hii ni ya zamani sana. Mchango wa Rufiji kwa Pato la Taifa ni asilimia 19 kutokana na hifadhi ya Taifa pamoja na misitu. Naomba kufahamu kwa nini Serikali inawachonganisha wananchi wa Jimbo la Rufiji na Chama chao cha Mapinduzi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza sana Mheshimiwa Mchengerwa kwa maswali yake mazuri, lakini kwa jinsi anavyowawakilisha wananchi wa Rufiji. Mheshimiwa Mchengerwa hongera sana na wananchi wako nadhani watapata maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijielekeze kwenye maswali mazuri ya nyongeza ya Mheshimiwa Mchengerwa. Suala la kukatikakatika kwa umeme, maeneo yanayopatiwa umeme kutoka Somanga Funga ambao ni mtambo unaosambaza umeme maeneo ya Rufiji pamoja na Kilwa, ni kweli kabisa kuna tatizo hilo. Kama nilivyowaeleza juzi mtambo wetu wa Somanga Funga ulikuwa na matatizo. Mtambo huu una vituo vitatu na mashine tatu za kuzalisha umeme, lakini mashine zilikuwa na matatizo ya uchakavu jambo ambalo tunalifanyia kazi na Serikali imetenga shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ukarabati. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mchengerwa pamoja na wananchi wa Rufiji mtambo huo utarekebika na kukatika umeme kutaisha kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata ule mtambo wa tatu ambao pia ulikuwa na hitilafu tunafunga sasa mtambo mwingine kwa ajili ya kuboresha uzalishaji wa umeme kwenye Mji wa Rufiji ambao unagharimu shilingi bilioni mbili. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mchengerwa na wananchi wake watapata umeme wa uhakika hivi karibuni. Nimhakikishie vijiji vyake vyote vya Luwe, Ngarambe, Ngombani, Kilimani A na B na Mashariki vyote vitapata umeme. Kwa hiyo, wananchi watapata umeme wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikiri kwamba Rufiji ni sehemu ya Tanzania kama vijiji vingine. Sasa nijibu swali la pili kwa nini Serikali inawachonganisha wananchi wa Rufiji na maeneo mengine, sidhani na sina uhakika Mheshimiwa Mchengerwa. Nikiri kwamba Serikali haiwachonganishi wananchi wa Rufiji na maeneo mengine. Japo swali lako linahusiana na masuala ya barabara, maji, umeme lakini kwa vile Serikali ni moja nimhakikishie kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haiwachonganishi wananchi na Rufiji na maeneo mengine. Ahsante sana.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wananchi waliokuwa na umri wa kuelewa mambo, mwaka 1956 Mwalimu Nyerere aliahidi ujenzi wa Bwawa la Stiegler‟s Gorge ili kuweza kutatua tatizo la umeme. Bwawa hili lingejengwa pale katika Kata ya Mwaseni. Ahadi hii ina miaka 61.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kufahamu kama ahadi hii ya Mheshimiwa Waziri aliyotuahidi hapa ujenzi wa mabwawa katika Kata za Mwaseni, Kipugira, Kilimani pamoja na Mkongo itachukua pia miaka 61 au itakuwa muda mfupi kidogo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Wizara ya Maliasili na Utalii inachangia pato la Taifa asilimia 19 na Rufiji yetu iko ndani ya hifadhi kwa zaidi ya nusu ya Rufiji, yaani square kilometer 6,500 ipo ndani ya hifadhi ya Maliasili na Utalii. Naomba kufahamu, mchakato wa ujenzi wa vyoo katika eneo la Selous pale Rufiji, leo hii watalii wanajisaidia katika maeneo ya hifadhi bila kuwa na vyoo. Naomba kufahamu, hili pato la Taifa mgawanyo wake ukoje katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii ili kuweza kusaidia wanyama hawa ambao wapo ndani ya hifadhi ikizingatia kwamba watalii wetu leo hii wanajisaidia sehemu ambazo ni za wazi bila kujisaidia eneo la vyoo.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza la wasiwasi au mashaka ya kwamba pengine hata ahadi hii tuliyoitoa hapa inaweza ikachukua muda mrefu ule alioutaja zaidi ya miaka 60 akifananisha na suala la mradi wa Stiegler‟s Gorge; kwanza nataka tu nimpe taarifa kwamba mradi wa Stiegler‟s Gorge akileta swali ambalo ni mahsusi kwa mujibu wa Kanuni za Bunge litajibiwa vizuri sana na Wizara ya Maji kwa sababu lina majibu sahihi kabisa na mahsusi ya kwa nini imechukua muda mrefu kiasi hicho kutekeleza mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na majibu haya ya utekelezaji wa ujenzi wa mabwawa matano; kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, kwamba hivi ninavyozungumza, kutokana na jitihada zake, wananchi wa Jimbo lake wanaelekea kupata majawabu ya changamoto kubwa hii ya kupata maeneo ya uvuvi hivi karibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi karibuni kwa sababu ninavyozungumza sasa hivi tayari mawasiliano yameshafanyika kati ya Wizara yangu na Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji. Tumeshabadilishana uzoefu na taarifa na tayari tuna makisio ya awali ya gharama za ujenzi wa mabwawa hayo matano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kutokana na kiwango cha fedha kile ambacho tumekiona katika hatua za awali, tunafanya mapitio ili tujue ukubwa wa mabwawa yale lakini pia tujue namna ya kuyajenga ili kuweza kutumia gharama ambazo zitakuwa zina unafuu, lakini bado tufikie malengo ya kuweza kuwapatia mabwawa hayo wananchi.
Kwa hiyo, wananchi wa Rufiji wasiwe na wasiwasi, Mheshimiwa Mchengerwa anawapigania na watapata maeneo ya kuvua samaki mbadala nje ya Hifadhi ya Selous. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili; ni kweli utalii unachangia asilimia zaidi ya 17 katika pato la Taifa; lakini pia niongeze kwamba robo ya upatikanaji wa fedha za kigeni katika muda wa miaka mitatu mfululizo lilitokana na pato linalotokana na utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu changamoto aliyoisema ya eneo la maingilio ndani ya hifadhi, changamoto ambayo inaleta usumbufu kwa watalii, nataka kusema kwamba changamoto hii imeshamalizika kwa sababu tayari ni miongoni mwa mambo ambayo tumeyapa kipaumbele hivi karibuni, yale ambayo tunatakiwa kuyashughulikia kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua unapokuwa na changamoto kuna nyingine ni kubwa sana zinahitaji labda jitihada kubwa na rasilimali nyingi, lakini hizi nyingine ndogo ndogo kama hii, hizi ni quick wins, kwa hiyo, tunazifanyia utaratibu wa haraka. Nataka nimhakikishie kwamba kabla mwaka huu haujakwisha, tutakuwa tumetatua tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sekunde moja naomba niendelee kutoa pole kwa wananchi wangu wa Rufiji hususan tukio la jana ambapo Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambuju alitaka kuuawa lakini alisalimika baada ya kukimbia kugundua majambazi wale wameshaingia nyumbani kwake,
taarifa ambazo nimezipokea muda huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili tu ya nyongeza; la kwanza nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri migogoro baina ya wananchi na wahifadhi imechangiwa na kuondolewa kwa mipaka ya awali iliyokuwepo hususan katika Kata ya Mwaseni na wananchi kuzuiliwa kuvua samaki
wale ambao wapo katika vijiji vinavyopakana na hifadhi. Naomba kufahamu Serikali ina mpango gani sasa ili yale mabwawa matano niliyoyaomba kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii yaweze kuchimbwa haraka katika Kata ya Mwaseni, Kata ya Kipugira hususan maeneo ya Nyaminywili, Kipo na Kipugila pia katika Kata ya Ngorongo? Naomba kufahamu Serikali inaharakisha vipi
mchakato wa uchimbwaji wa mabwawa ya samaki kwa wananchi wangu wa maeneo hayo?
Mheshimiwa naibu Spika, lakini pili……
Mheshimiwa Naibu Spika, ninafuta hilo swali la samaki, naomba la mgogoro wa mipaka libaki. Swali la pili, watumishi wa hifadhi wamekuwa
wakiweka beacons na alama kadhaa katika baadhi ya nyumba hususani katika maeneo ya Kipugila maeneo ya Nyaminywili na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato wa uwekaji wa beacons unakiuka Ibara ya 13 ya Katiba, pia unakiuka Ibara ya 16 ya Katiba ambayo inazungumzia haki za msingi za wananchi ubinafsi wao, ufamilia wao pamoja na uhifadhi wa maskani zao. Ninaomba kufahamu je, Wizara hii ya Maliasili na Utalii imedhamiria kabisa kukiuka Katiba ya haki za msingi ya Ibara ya 13 na Ibara ya 16, katika kuweka beacons na kusababisha uhuru wa wananchi wa mnaeneo husika kukosa haki zao za msingi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuanza na swali lake la pili. Uchukuaji wa hatua wa wawekaji mipaka kwenye maeneo yote ya hifadhi unafanyika hivyo kwa mujibu wa sheria. Kama tunavyofahamu zimetungwa na Bunge lako Tukufu jambo ambalo limefanyika pia kwa mujibu wa Katiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ule ni utekelezaji wa sheria ambazo zipo kwa mujibu wa Katiba, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba hata mara moja Serikali kupitia Wizara ya Maliasili haiwezi kuvunja Katiba. Iwapo kuna jambo lolote mahususi ambalo anadhani kwamba linaweza kufanana na hicho anachokisema basi namkaribisha aweze kuja kuniona tuweze kulijadili na kuweza kulipatia ufumbuzi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili ambalo lilikuwa la kwanza la uwekaji wa mipaka au uwekaji wa alama. Uwekaji wa alama ni hatua inayochukuliwa baada ya kuwa tayari mipaka ilikuwepo miaka mingi iliyopita. Wakati wa utekelezaji wa zoezi la uwekaji wa alama Wizara
inafanya mazoezi haya kwa kushirikisha wananchi katika maeneo yanayohusika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini katika maeneo
ambayo ameyataja Mheshimiwa Mchengerwa zoezi hili limefanyika kwa utaratibu huo wa kushirikisha wananchi, iwapo kuna hoja mahsusi zinazohusiana na alama hizo basi anaweza kuzileta kwa kutaja vijiji vyenyewe hasa ili tuweze
kuona namna ambavyo tunaweza kwenda kuona namna bora zaidi ya kwenda kuweka alama hizo. Nisisitize kwamba zoezi hili kwamba zoezi hili ni agizo la Serikali kupitia maagizo ya Viongozi Wakuu wa Serikali akiwemo Mheshimiwa Waziri
Mkuu na kwa hiyo litaendelea lakini jambo la msingi tutaendelea kushirikisha wananchi ili liweze kuwa zoezi rafiki.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na kilio kikubwa sana cha mahitaji ya umeme Kata ya Mkange pale Chalinze ukizingatia kuwa sehemu hii inachangia kwenye uchumi wetu wa Taifa hususan katika Wilaya ya Bagamoyo, pia na Halmashauri ya Chalinze na Tanzania kwa ujumla hususan katika viwanda pamoja na utalii.
Je, Serikali inajipangaje kusaidia wananchi pamoja na wawekezaji wa viwanda umeme ili kupunguza ukali wa maisha wa eneo hili la Kata ya Mkange? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mkubwa wa Stiglers Gorge unadhamiria kuikomboa nchi yetu katika umeme hususan katika viwanda vinavyojengwa pamoja na treni hii ya umeme.
Je, Serikali inawaachaje wananchi wa Jimbo la Rufiji ambao wametunza bwawa hili pamoja na Mto Rufiji kwa miaka mingi sana hususan wakazi wa Kata ya Mwaseni, Kipugira, Ngorongo na Mkongwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge Mchengerwa na naomba nimpongeze kwa jitihada zake za kufuatilia changamoto mbalimbali za nishati katika jimbo lake pamoja na muuliza swali la msingi. Ameuliza swali juu ya mahitaji ya umeme kwenye Kata ya Mkange iliyoko Jimbo la Chalinze na ni kweli Kata hii ya Mkange imepakana na Mbuga ya Saadani.
Naomba nimtaarifu kwamba katika mradi ambao unaendelea waUrban Peri Urban Edification Project of Coast Region na Kigamboni – Kata ya Mkange itapata umeme kupitia Miono. Kwa hiyo, naomba nimtaarifu kwamba Serikali imezingatia na kwa kuwa ina dhamira kwamba kila kijiji ifikapo 2020/2021 kipate umeme kwa hiyo Kata ya Mkange itapata umeme kupitia Miono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameulizia suala la Stiglers Gorge. Naomba nilitaarifu Bunge lako Tukufu ni kweli Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kwa dhati kuongeza upatikanaji wa nishati nchini kwetu na imedhamiria kwa dhati kutekeleza mradi huu ambao utaongeza megawati 2100, tender imeshatangazwa na zaidi ya makampuni…
Mheshimiwa Mwenyekiti, na nimtaarifu tu Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa mradi huu unatekelezwa katika maeneo ya Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Pwani eneo la Rufiji Kata alizotaja Mwaseni na Ngorongo ni Kata ambazo ni kweli zimetunza bwawa hili na zitafaidika kwanza kupitia upatikanaji wa nishati hii ya umeme lakini pia kupitia ajira ambazo zitapatikana kipindi cha ujenzi wa bwawa hili, lakini tatu, Wilaya hii ya Rufiji imekuwa ikikumbwa na mafuriko ya mara kwa mara. Kupitia ujenzi wa bwawa hili ni dhahiri kwamba ule uhifadhi wa maji utasaidia kuzuia masuala ya mafuriko katika maeneo haya.
…lakini langu lingine pia ujenzi wa bwawa hili litasaidia shughuli za kilimo cha umwagiliaji kwa maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba Watanzania muamini mradi huu unatekelezwa kwa pesa za ndani za nchi yetu. (Makofi/Vigelegele)
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Swali langu la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri, nataka kufahamu; je, Serikali iliafiki mwekezaji huyu kukopa na kwenda kuwekeza kiwanda kikubwa nchini Congo wakati hapa nchini bado kuna uhaba mkubwa wa sukari? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili la nyongeza ni kwamba majuzi Kiwanda cha Sukari cha Mahonda kimefungwa kutokana na uhaba wa miwa. Hali hii itapelekea Zanzibar kukosa sukari. Naomba kufahamu; je, Serikali ni lini sasa itatekeleza ujenzi wa Kiwanda cha Sukari kule Rufiji kwa kutumia bonde la Mto Rufiji katika ardhi iliyotengwa katika Kata ya Muhoro, Chumbi, Mkongo pamoja na Kata ya Mbwara ili kuweza kuwatosheleza Watanzania kwa upatikanaji wa sukari ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Kagera Sugar mpaka leo kimeshawekeza zaidi ya dola za Kimarekani milioni 250 na kiasi kilichokopwa kwa guarantee ya Serikali ni dola za Kimarekani milioni 65; kwa hiyo kusema wamewekeza dola milioni 250, halafu wamekopa milioni 65 na kupeleka Congo, naona siyo jambo la kawaida. Na mimi nimefika mwenyewe Kiwanda cha Kagera Sugar nimejionea uwekezaji mkubwa uliowekezwa.
Mheshimiwa Spika, ni imani ya Serikali na tunatambua hivyo kwamba pesa yote iliyokopwa kupitia guarantee ya Serikali hii dola za Kimarekani milioni 65 imewekezwa yote ndani ya Taifa letu na ni moja ya viwanda vinavyofanya vizuri sana ndani ya Taifa letu, kimeajiri Watanzania wengi, kinatoa huduma za afya bure katika ukanda wote unaozunguka Kiwanda cha Kagera Sugar, kinatoa huduma za elimu bure kwa watoto wote wa wafanyakazi ndani ya Kagera Sugar na ndani ya wananchi wanaozunguka kiwanda hicho.
Mheshimiwa Spika, tuendelee kuwapa moyo Kiwanda cha Kagera Sugar kwamba wanafanya vizuri waendelee kuwekeza kwa ajili ya manufaa ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, napenda tu kuliarifu Bunge lako Tukufu, Serikali ipo kwenye mchakato wa kuendelea kukiwezesha Kiwanda cha Kagera Sugar ili kiendelee kuwa cha mfano ndani ya Taifa letu, kiwanda kinachomilikiwa na Watanzania halisi wenye uchungu na Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, napenda kusema kuwa Serikali ilifanya jambo jema kurejesha bonde lile lilokuwa linamilikiwa na RUBADA. Sasa hivi Serikali ya Magufuli, Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali ya viwanda, tunafahamu na ndiyo maana juzi tuliwaambia ndugu zetu wa Zanzibar, Zanzibar kuna upungufu wa sukari, miwa haitoshi. Leo kiwanda kimefungwa kwa sababu miwa haitoshi kwa ajili ya Kiwanda cha Mahonda; na Serikali yetu iko tayari kabisa Mheshimiwa Mchengerwa kwenda kuwawezesha wananchi wa Rufiji kuwekeza kwenye mashamba yale tuweze kupata outgrowers wengi na kiwanda kitawekezwa. (Makofi) Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza majibu mazuri ya dada yangu Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, mchapa kazi na ninaona kabisa anakwenda kuchukua Jimbo la mtu huko Mbeya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza; kwanza kabisa Rufiji tunatambua jitihada anazofanya Mheshimiwa Rais za ujenzi wa bwawa la Stiegler’s Gorge kama ambavyo amelisema Mheshimiwa Naibu Waziri na kwamba tunatambua Serikali inapelekea zaidi ya shilingi trilioni mbili kwenye mradi huu na kuifanya Rufiji kuwa moto moto kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu wa Stiegler’s Gorge una zaidi ya ekari 150,000 ambazo zimetengwa kwa ajili ya kilimo. Swali langu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo: Je, Serikali inawaandaaje Warufiji sasa ili kuweza kupokea fursa hizi za eneo hili la kilimo zaidi ya ekari 150,000 katika kuweka miradi mbalimbali ikiwemo na ule mradi wa kiwanda kikubwa cha sukari kule Rufiji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, Watanzania wa Rufiji kwa asilimia 90 wanategemea kilimo na RUBADA ilikuwa katika Kata ya Mkongo pale Rufiji; na hii ndiyo kata iliyoathirika sana kwa wafugaji kuingiza mifugo yao eneo la wakulima; je, Serikali inajipangaje kuwasaidia wakulima hususan katika vijiji vya Mbunju, Ruwe pamoja na Mkongo Kusini ambao wameathirika sana kwa mazao yao kuliwa na wafugaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza kipekee kabisa naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji kwa dhati kabisa kwa maana yeye alikuwa ni sehemu mojawapo ya watu ambao walishatueleza na wakatuambia kabisa kwamba mradi huu wa RUBADA ni non-starter na yeye alikuwa ni sehemu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria, kuleta na kupendekeza kwamba mradi huu wa RUBADA haufanyi kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, sasa naomba naiende moja kwa moja kumjibu maswali yake madogo sana ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba sisi kama Serikali katika Bonde hili la Rufiji ni hekta 1,350 kwa ajili ya mradi wa Stiegler’s Gorge. Naomba niseme kwamba eneo la hekta 300,000 limetengwa kwa ajili ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hizo hekta 300,000 zilizotengwa kwa ajili ya kilimo, ni kwa ajili ya irrigation scheme. Kwa maana hiyo, naomba nimhakikishie kwamba wananchi wa Rufiji na maeneo mengine yote watanufaika kwenye kilimo kupitia mradi huu ambao unaitwa irrigation scheme.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine lile la (b) ni kuhusu suala zima la migogoro aliyoizungumzia kuhusu ardhi. Ni kwamba Serikali tumejipanga na mpaka sasa hivi sheria inaandaliwa; tunaangalia suala zima la migogoro hii ya ardhi na maandalizi tayari yameshafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, Serikali inaandaa suala zima la ardhi kwa sababu tumegundua kwamba kuna migogoro mingi sana kati ya wakulima na wafugaji. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Rufiji ni Wilaya kongwe sana iliyozaa zaidi ya Wilaya tano lakini pia imezaa Taifa la Fiji kama ambavyo wewe mwenyewe unafahamu. Lakini pia eneo la Rufiji, Kibiti na Kilwa hakuna benki yoyote ya biashara na Serikali sasa inapeleka zaidi ya trilioni saba za ujenzi wa uzalishaji wa umeme katika Bwala la Mto Rufiji ambapo tunategemea kuwepo kwa watumishi, wafanyakazi zaidi ya 6,000 mpaka 7,000.

Je, Serikali haioni umuhimu sasa kwamba tawi la benki katika Wilaya yetu ya Rufiji haliepukiki? Hilo swali la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, eneo la Rufiji lina ukubwa wa zaidi ya hekari 500,000 ambao lipo ndani ya Bonde la Mto Rufiji, lakini pia kwa kuwa Serikali inatekeleza Mradi wa Umeme wa Rufiji, Serikali pamoja na Wilaya ya Rufiji imetenga zaidi ya hekari 150,000 kwa ajili ya kwenye kilimo cha kisasa cha umwagiliaji.

Je, Serikali haioni umuhimu sasa kwamba Benki ya Maendeleo ya Kilimo ni muhimu sasa kuwepo Rufiji ili kuweza kuwasaidia wananchi wa Rufiji kuchangamkia fursa za maendeleo, fursa za kilimo, fursa za biashara katika Mradi wetu wa Umeme wa Rufiji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza kuhusu kwamba Serikali haioni kwamba haiepukiki sasa kufungua tawi Rufiji, kama nilivyosema benki nyingi zinaendeshwa kibiashara na benki nyingi huwa zinaangalia commercial viability ya eneo husika kabla hawajaweza kupeleka tawi la benki husika kwenye eneo husika. Kwa hiyo, kama ambavyo nimesema kwenye jibu la msingi, mabenki yetu yanafanya utafiti huo na tathmini kujiridhisha na nini kinatakiwa kufanyika kwenye maeneo husika. Hata hivyo, nimwambie Mheshimiwa Mchengerwa kwamba baada ya swali lake hili kama Serikali tumeanza kuifanyia kazi na tumeongea na Mkurugenzi wa TPB PLC na Mkurugenzi ameomba yafanyike yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza anaomba apate maombi mahsusi ili kuweza sasa kutuma timu yake kwenda kufanya kufanya feasibility study na kujiridhisha na commercial viability ya eneo la Rufiji ili kwenda kufungua tawi la Benki ya TPB kutokana na potentials zote kama zilivyoelezwa na Mheshimiwa Mchengerwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili kuhusu Benki ya Kilimo, kama alivyosema yeye mwenyewe Benki ya Kilimo ni benki ya maendeleo, hivyo lazima kila inapokwenda kufunguliwa ielewe kabisa wanakwenda kuhudumia aina gani ya wananchi ambao wako kwenye miradi mikubwa ya kimaendeleo. Pia Rufiji hawako mbali sana na Dar es Salaam ambako Benki yetu ya Kilimo ya Maendeleo ndipo Makao Makuu yake yalipo ambapo inahudumia maeneo yote ya Pwani, maeneo ya Morogoro. Kwa hiyo, niwaombe sana wakulima wetu wakubwa ambao wanahitaji mikopo ya maendeleo wafike Dar es Salaam na watahudumia na Benki yetu ya Kilimo ya Maendeleo. (Makofi)
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme sikuwa na hakika kwamba, swali hili lilikwenda TAMISEMI na binafsi swali hili tulilielekeza Wizara ya Ardhi kwa kutambua agizo la Mheshimiwa Rais la ujenzi wa Kiwanda cha Sukari kule maeneo yetu ya Rufiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri pengine atuambie Serikali imeandaa mpango gani kwa ajili ya matumizi ya ekari 150,000 ambazo zinaandaliwa baada ya ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Mheshimiwa Mchengerwa anajenga hoja, amesema alitarajia kwamba swali hili lingejibiwa na Wizara ya Ardhi, lakini wanufaika ni vile vijiji ambavyo amevitaja ambapo sisi kama TAMISEMI tuna maslahi na vijiji vile. Katika swali lake la nyongeza anataka kujua mpango wa Serikali wa matumizi ya ekari 50,000 baada ya ujenzi wa bwawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii imekuwa makini, imekuwa ikifuata taratibu zote na kuona namna gani tufanye kulingana na wakati husika. Tutaainisha baada ya kujiridhisha kwamba eneo hilo litafaa kwa ajili ya shughuli gani na Mheshimiwa Mbunge naye atapata taarifa pamoja na wananchi wanaozunguka eneo la bwawa hilo.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuongezea kidogo katika suala hilo la kuendeleza Bonde la Mto Rufiji hekta 150,000 zilizokuwa downstream baada ya Bwawa la Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari tumeshaielekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na imeshaanza kuainisha na kwenda huko kufanya utafiti kuonesha namna gani tutaanza kutumia kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji baada ya bwawa lile kumalizika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge aendelee kushirikiana na Serikali yake hii na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na sasa hivi tumeweka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji mpaka ngazi ya Wilaya. Kwa hiyo, kuna Afisa wa Tume ya Umwagiliaji kwenye Wilaya ya Rufiji, Mkoa wa Pwani, Kanda ya Mashariki pamoja na Taifa. Kwa timu hiyo, tutaenda kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ambacho ni kilimo cha uhakika.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la maji kwenye Wilaya ya Rufiji ni kubwa sana hali iliyopelekea nguvu kazi kubwa ya vijana na akina mama kupotea wakijaribu kutembea umbali mrefu, pia wakidiriki kuchota maji kwenye maeneo ya Mto Rufiji na kupelekea wananchi wengi kuchukuliwa na Mamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango gani wa kuja kufanya tathmini ikizingatiwa kwamba Rufiji ni kanda maalum, pia Rufiji tunatekeleza mradi wa uzalishaji wa umeme wa Stiegler’s Gorge. Je, ni lini Serikali itakuja kufanya tathmini halisi kabisa ya tatizo la maji Wilaya yetu ya Rufiji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tatizo la maji kwenye Kata ya Mbwala ambayo Mheshimiwa Waziri amejibia ni kubwa sana tofauti kabisa na majibu ambayo wenzetu wa Halmashauri walimwandalia. Eneo kubwa la Kata ya Mbwala wananchi wanalazamika kusafiri umbali wa kilometa saba mpaka 10 kufuata maji katika maeneo ya Kikobo na maeneo mengine.

Je, ni lini Serikali itadhamiria kabisa kuchimba visima virefu karibu na kwa wananchi hali ambayo hivi sasa imepelekea vijiji vingi wananchi kuhama kutafuta maji kwa sababu wanadiriki kusafiri umbali mpaka wa kiklometa 7 - 10?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. Nataka niwahakikishie Wandengereko wote, wamechagua jembe wembe na anafanya kazi kubwa sana katika Bunge letu Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa anataka kujua jitihada za Serikali. Tunatambua kwamba maji ni uhai na ni moja ya changamoto kubwa, lakini sisi kama Wizara ya Maji tumefanya jitihada kubwa ya uchimbaji visima 13 pale yenye thamani zaidi ya shilingi milioni 400, tumeshachimba visima 10. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, baada ya ukamilikishaji ule wa visima tutafanya usanifu katika kuhakikisha tunatekeleza miradi mikubwa ili wananchi wako waweze kupata huduma hii ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nataka nikuhakikishie kutokana na Kata hiyo ya Mbwala, mimi kama Naibu Waziri nitapata nafasi ya kuja katika Jimbo lako na nitafika katika Kata ya Mbwala ili tuweze kushauriana na kuangalia namna gani tunaweza tukatatua tatizo la maji katika kata yako. Ahsante sana.