Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Seif Khamis Said Gulamali (7 total)

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tumekuwa tunapata taarifa za Serikali juu ya kuanza kwa mradi huu kila mwaka na hata mwaka 2014 tulipata taarifa hiyo, je, Serikali inaweza kutuambia katika bajeti hii ya mwaka 2016/2017 imetenga kiasi gani cha fedha kwa ajili ya kuanza kwa mradi huo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa ilikuwa ni ahadi ya Makamu wa Rais kutupatia maji ya Ziwa Victoria katika maeneo ya Choma na Tarafa ya Simbo na iliombwa kwa madhumuni ya kuwa, moja tunakwenda kupata Wilaya mpya, lakini pili katika maeneo hayo tuna hospitali ya rufaa ya Nkinga ambayo inahudumia karibu mikoa mitano, je, Serikali haijaona haja ya kupeleka maji katika maeneo hayo yaliyoombwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato wa ujenzi wa mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda maeneo ya Nzega, Tabora na Igunga ulianza mwaka 2012 na inatarajiwa sasa katika mwaka mpya wa fedha unaokuja 2016/2017 taratibu zile za manunuzi zitakuwa zimekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri mradi huu unafadhiliwa na tayari mfadhili amesha-commit dola milioni 268.35. Kwa hiyo, uhakika wa fedha tunao. Kama nilivyojibu katika hoja ya msingi kwamba sasa hivi tumeshamaliza kutambua Makandarasi na tumepeleka kwa mfadhili Benki ya India kwa jili ya kupata no objection ili tuweze kuendelea na hatua nyingine ili ifikapo mwezi Julai mwaka huu tuwe tumeanza kazi ya ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kweli taarifa ipo, kwamba Mheshimiwa Makamu wa Rais aliahidi kupeleka maji Manonga, lakini kama nilivyosema kwamba mchakato huu ulianza mwaka 2012 na tukaanza kufanya usanifu na kipindi hicho wakati tunatengeneza memorandum tulikubaliana kwamba kwa maana ya mradi huu utakwenda kilomita 12 kila upande wa bomba litakapopita lile bomba kuu. Kwa hiyo, ahadi imekuja wakati taratibu hii iko nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, namuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, huu siyo mwisho, ahadi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais tunayo, kwa hiyo, asubiri tuanze ujenzi. Wakati wa ujenzi tutaangalia tutakachofanya ili kuhakikisha kwamba, tunatimiza ahadi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa Naibu Waziri. Kwa kuwa tatizo la umeme lililopo Zanzibar linafanana sana na tatizo la umeme lililopo Igunga, sasa kwa sababu Naibu Waziri anatambua vizuri sana: Je, nini kauli ya Serikali juu malipo ya fidia kwa Kata za Chabutwa, Simbo pamoja na Mwisi ili waweze hasa kujua watapata lini hiyo fidia yao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Niabu Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Gulamali, jana na juzi tumehangaikia sana suala la fidia ya wananchi wako. Kama ambavyo tumelifikisha, kwanza nikupongeze. Sasa hivi mthamini wa ardhi wa Mkoa anapitia viwango vya fidia vya wananchi wa Manonga na hasa katika vijiji vya Chabutwa Simbo na maeneo ya jirani ambapo umetaja, ni kweli kabisa kuna wananchi 722 ambao hawajafidiwa na malipo hayo yako katika hatua za mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba jana wakati tunapitia, tulipoongea na Mkuu wa Mkoa wa Tabora nadhani alikwambia kwamba kabla ya mwezi ujao na miezi miwili ijayo wananchi wako watalipwa fidia. Kwa hiyo, nakuomba sana wafikishie taarifa waendelee kuwa na subira jambo la fidia yao linafanyiwa kazi.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali fupi kwa Naibu Waziri.
Ni lini sasa maeneo ya kata za Mwashiku, Ngulu, Uswaya na Igoweko yataweza kupata mawasiliano kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri ameweza kujibu swali la Mheshimiwa Mgimwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Gulamali ni mfuatiliaji sana, siyo wa masuala ya mawasiliano peke yake, bali ni pamoja na barabara zake zile mbili ambazo viongozi wetu wakuu walitoa ahadi, na nyakati zote wakati akifuatilia hiyo miradi nimekuwa nikimhakikishia kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano inatenda inachoahidi. Mheshimiwa Gulamali nikuahidi katika yale uliyoyafuatilia vijiji hivi sikumbuki kama ulinitajia. Kwa hiyo, nitafuatilia ratiba ya utekelezaji wa makapuni yote yanayotuletea mawasiliano nchini kuona kama hivi vimeshaingizwa katika ratiba na kama vitakuwa havijaingizwa namhakikishia tutaviingiza.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza na swali langu napenda kulielekeza kwa Waziri, Wizara ya ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Swali langu linafanana sana na swali lililoulizwa hivi punde; ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Ziba kwenda Ikinga, Simbo mpaka Tabora na Ziba, Choma mpaka Shinyanga hasa ukizingatia hizi ni ahadi za Mheshimiwa Rais na huu ni mwaka wa 2017? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Seif Gulamali na wananchi wote wa Manonga na Wilaya ya Igunga kwa ujumla, kwamba ahadi zote ambazo viongozi wetu wamezitoa katika kipindi hiki cha miaka mitano tutazitekeleza. Lazima twende hatua kwa hatua, hatuwezi kutekeleza ahadi zote kwa mwaka mmoja wa fedha. Na nimhakikishie tu kwamba kabla ya kipindi hiki cha miaka mitano barabara hii tutakuwa tumeitendea haki kama ambavyo viongozi wetu wakubwa wa kitaifa walitolea ahadi.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Napenda sasa katika majibu yake angeweza kufafanua kwa jinsi ambavyo barua ilivyokuwa imeelekeza, kwa sababu tunavyojua katika kikao chetu cha RCC pamoja na uanzishwaji wa Wilaya mpya ya Bukene pia kulikuwa na maombi ya Wilaya mpya ya Manonga.
Kwa hiyo, nilikuwa nafikiria MheshimiwaWaziri atuambie; je, mchakato huo utaenda sambamba pamoja lakini turahisishiwe katika kuanzishiwa Mkoa wetu wa Tabora kwa sababu Mkoa wa Tabora ni mkubwa katika mikoa yote iliyobakia kwa sasa, una kilometa zaidi ya 75,000 na tumeshaona baadhi ya mikoa mingine imegawanywa kama Mkoa wa Mbeya, Arusha na Shinyanga. Naomba sasa Mheshimiwa Waziri atuhakikishie uharakishaji wa kugawa huu mkoa ili kurahisisha kupeleka maendeleo kwa wananchi. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, alichosema Mheshimiwa Mbunge ni kweli, kwa sababu maombi haya yalivyokuja, lengo kubwa lilikuwa ni kuanzisha Mkoa mpya wa Nzega ambao uliainisha mkoa huo utakuwa na Wilaya nne. Ilipendekezwa kwamba kutakuwa na Wilaya hii mpya ya Bukene, Wilaya kongwe ya Nzega, Wilaya ya Igunga, halikadhalika na Wilaya mpya ya Manonga. Kwa hiyo, huo ndiyo mchakato wenyewe ulivyokuwa katika pendekezo lile. Ndiyo maana nimesema kwamba kulikuwa na mapungufu kadhaa, baadaye sasa ofisi yetu ikapeleka mrejesho kwa Katibu Tawala wa Mkoa na wameshafanyia kazi hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nimesema kwamba physical verification imeshaenda kufanyika, sasa kilichobakia ni kwamba iko katika mchakato wa kupelekwa kwa Mheshimiwa Rais naye atafanya maamuzi, lakini tukiwa na angalizo kwamba na Mheshimiwa Rais alifika pale Tabora, kuna mazungumzo aliyazungumza. Kwa hiyo, yeye mwenyewe atapima ataona nini kifanyike kuhakikisha kwamba jambo linafanikiwa kwa kadri yeye mwenyewe atakavyoona inafaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya hayo yote ili mradi kufanya jambo hili kwa matakwa yenu na Mheshimiwa Rais aweze kufanya maamuzi.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swlai dogo la nyongeza. Kwa kuwa kukua kwa soko huria katika utoaji wa huduma ya anga nchini, hivyohivyo naweza nikaambatanisha na kukua kwa elimu yetu kuwa huria na nilikuwa nataka tu kupata maelekezo ya Wizara juu ya huria hii ya kutokana na elimu yetu ya Tanzania kuwa huria, hali iliyosababisha baada ya kutoka kwa uhakiki wa vyeti feki imepelekea baadhi ya Madaktari, Walimu, Watumishi, taarifa zao kuonekana ni incomplete. Hii ni kwa sababu ya elimu yetu kuwa huria. Sasa naiomba Serikali itoe maelekezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninapozungumza,
kuna watumishi sasa wanaelekea Dar es Salaam kwenda kuhakiki incomplete zao…
Mheshimiwa Mwenyekiti,
swali langu ni kwamba nakata kujua: Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya wafanyakazi ambao taarifa iliyotoka juzi ya uhakiki wa vyeti vyao, hasa wale wote walioandikiwa incomplete? Serikali hasa Wizara hii ya Elimu ituelekeze, maana leo hii watu wanasafiri wengi kwenda kuhakiki vyeti vyao vya Form Four. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni hilo nalielekeza kwa Mheshimiwa Waziri kwa sababu hapa ni mada huria na elimu yetu ni huria, naomba Wizara ya Elimu itoe tamko juu ya kadhia hii ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni kweli kwamba tumekuwa tukitoa elimu huria ili kuwezesha maeneo mbalimbali ya ajira kuweza kupata wataalam wanaohitajika. Katika suala hili la watu kusafiri kuhusiana na kuhakiki vyeti vyao, napenda tu kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna makundi makuu matatu ambayo yameendana na uhakiki uliofanyika. Kuna kundi la kwanza la vyeti feki au vyeti vya kugushi, kundi hili kama kuna yeyote anayeona kwamba hajaridhika, anachotakiwa kufanya siyo kusafiri, bali ni kukusanya vyeti vyake halali na kumwona mwajiri wake ambaye ni DED (Mkurugenzi wa Halmashauri) au Katibu Tawala wa Mkoa ili apeleke huo ushahidi wake na viweze kuwasilishwa. Vitawasilishwa kwa Katibu Mkuu, Utumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna kundi lingine,
hili analolizungumza la incomplete (vyeti visivyokamilika). Yawezekana wakati wa kuwasilisha, mtu aliwasilisha labda vyeti vya Chuoni, vyeti vya Kidato cha nne au cha sita hakuwasilisha; au vyeti vingine vinavyohusiana. Kwa hiyo, anachotakiwa kufanya ni vilevile, kupeleka vile vyeti ambavyo vilikuwa havijawasilishwa kwa hao waajiri wake ambao ni Mkurugenzi wa Halmashauri au RAS (Katibu Tawala wa Mkoa).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kundi la tatu la vyeti vyenye utata. Vyeti vyenye utata unakuta kwamba cheti kimoja kimetumika na watu zaidi ya mmoja. Kwa hali hiyo inabidi lazima kumfahamu ni yupi mwenye cheti halisi. Wanachotakiwa kufanya ni kila mtu anayeamini ndiye mwenye cheti hicho, hao ndio wanaotakiwa kusafiri, waende NECTA ili sasa wakahakikiwe na kujulikana mwenye cheti chake ni yupi kwa sababu haiwezekani cheti kimoja kikatumika na mtu zaidi ya mmoja. Huo ndiyo ufafanuzi wangu. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kufahamu, je, Serikali ina mpango gani ya kusambaza huduma hii nchi nzima hasa katika Wilaya ya Igunga na Mkoa wa Tabora na ukifuatilia kwamba katika Wilaya ya Igunga na Mkoa wa Tabora hivi karibuni tutaweza kupata maji ya Ziwa Victoria?
Mheshimiwa, la pili, nilikuwa nataka kujua juu ya Wizara hii ya Maji, inatoa tamko gani kwa baadhi ya Mamlaka za Maji nchini ambazo zinatoa bili kubwa kwa watumiaji wa maji kuwabambikiza bili kubwa watumiaji wa maji kuliko matumizi halisi ya wananchi wanaotumia kwenye maji? Nataka kujua tamko la Serikali juu ya ubambikizaji wa gharama za maji, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyopigania wananchi wake. Lakini kikubwa napenda kujibu maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni kuhusu suala zima la usambazaji mkakati wetu kama Serikali. Safari ni hatua na hatua tumeshaianza ya kutekeleza mamlaka saba na kwa kuwa safari moja huanzisha nyingine sisi kama Serikali kwa kupata nafasi ya kuweza kutekeleza mamlaka saba tunaziagiza mamlaka zote zenye uwezo wa kujitosheleza kigharama kutenga bajeti kuhakikisha kwamba wanatengeneza mifumo hii ili kuweza kuyafikia maeneo ya mbali katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, katika baadhi ya mamlaka kuwabambikia wananchi ama wateja gharama ambazo si halisia haipendezi, wala haifurahishi, kuona baadhi ya mamlaka zinawabambikia bei wananchi. Mimi nataka niziagize mamlaka zote nchini kwamba watoe bei halisia ambazo zimeidhinishwa na EWURA. Kama kuna mtu au mamlaka itakayokaidi hata kama ana mapembe marefu kiwango gani tutayakata ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata huduma bila usumbufu wowote.