Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Constantine John Kanyasu (20 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza naomba kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha hapa lakini niwashukuru sana wapiga kura wangu kwa kunipa ridhaa hii ya kuwawakilisha. Niseme kwamba nitajitahidi kutimiza wajibu wangu kadri Mungu atakavyoniwezesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo vibaya nikasema kidogo kuhusu tukio lililotokea hapa kwamba limenisikitisha. Kwanza kwa namna ambavyo niliamini baada ya wewe kutoa amri kwamba sasa watu hawa washughulikiwe na baadaye nikaona watu hawashughulikiwi wanabembelezwa, haikunifurahisha sana. Mimi nilitarajia askari wakiwa nje wangepanga mkakati wao wa namna ya kuwashughulikia na wanapokuja ndani wanakuja straight wamekwishajua wanawashughulikia namna gani. Matokeo yake wameanza kutukanwa hapo, vyombo vya dola vinatukanwa na vyombo vya habari vinachukua. Nataka niseme, matukio haya hayawezi kukoma katika mfumo wa Jeshi legelege namna hii. Mwenyekiti anapotoa amri wanaoingia ndani kutimiza amri wanapaswa waache mjadala na wahalifu. Ipo siku watu watakuja hapa wamekamia kufanya maovu na watakuja kuchukua hatua tayari wamekwishaua mtu hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana wakati mchangiaji mmoja anachangia aliwashambulia sana Wakuu wa Wilaya akasema yeye angetamani kuona Wakuu wa Wilaya wanafutwa. Pengine inawezekana yeye katika Jimbo lake haoni umuhimu wao kwa sababu anatazama zaidi vyeo vyao vile vya kisiasa na namna wanavyoshughulikia wahalifu lakini wananchi wa kawaida nafasi ya Mkuu wa Wilaya ni ya muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimekuwa Mkuu wa Wilaya, kwa siku nilikuwa naweza kumaliza migogoro mingi ambayo ingeenda yote Mahakamani, Mahakama ile isingeweza kufanya kazi. Tuna migogoro mingi ya ardhi, kuna watu wanaonewa huko hawawezi hata kufika polisi wakajieleza, hawawezi kwenda mahakamani wakajieleza hata kama haki ni ya kwake akifika mahakamani hawezi kujieleza, kwa Mkuu wa Wilaya wanaongea kwa uhuru na matatizo yao yanasikilizwa.
Kwa hiyo, mimi nasema wananchi waache kupokea hizi propaganda ambazo zinaweza zikawafanya wakashawishika kufikiri kwamba Mkuu wa Wilaya siyo mtu muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumefika hapa watu wanaongea hovyo kwa sababu mwanzo watu wametumia sana vyombo vya habari kupata publicity. Mimi naunga mkono TBC isirushe live na sababu za msingi ziko kwamba watu wametumia vibaya sana nafasi hii na matokeo yake badala ya kuzungumzia vitu vyenye manufaa kwa wananchi, wamekuwa wakiitukana Serikali na wananchi. Kwa hiyo, naomba kusema kwamba msimamo huo ulikuwa sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nizungumzie sasa kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais ana vision ya kuona Tanzania inaelekea kwenye viwanda, mimi pia naunga mkono na nafikiri vision yake iko sahihi. Hata hivyo, yapi ni mahitaji muhimu ya kuwa na viwanda na viwe wapi. Tunachokitazama sasa hivi, ikitokea bahati mbaya likatokea tatizo, karibu 75% ya nchi itakuwa giza kwa sababu source ya umeme iko sehemu moja. Katika nchi hizi ambazo tunafikiri tunataka kuanzisha viwanda, kama viwanda vyote vitawekwa sehemu moja basi siyo ajabu siku moja Tanzania tukajikuta zaidi ya 30% ya watu walioko kwenye viwanda wamekosa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba tuanze kwanza kwa kutambua maeneo yapi tunataka kuweka viwanda. Ningetamani kuona tunaanzisha miji ya viwanda. Kwa mfano, kama tutasema tunafanya Singida kuwa mji wa viwanda na likatambuliwa eneo kubwa kuwa la viwanda, basi eneo hilo lipelekewe kila aina ya miundombinu ambayo itasababisha wawekezaji waweze kufika. Hatuwezi kuweka viwanda Singida tukategemea umeme unaotoka Dar es Salaam, ipo siku njia hii ya umeme wa kutoka Dar es Salaam itapata matatizo na viwanda vyote vitasimama. Lazima tuwe na alternative route ya umeme kutoka sehemu nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, pamoja na wingi wa gesi, tunavyo vyanzo vingine vya umeme. Pale Singida tuna upepo, hadithi hii imeongelewa kwa muda mrefu sana lakini kule Ngara tuna mto Ruvuvu, haukauki, una maji mengi sana. Tuna mradi wa umeme pale ambao Tanzania, Rwanda na Burundi wameamua kufanya kwa ubia, wamekadiria kutengeneza megawatts 70 peke yake lakini wataalamu walisema wangeweza kupata megawatts 300 kama wangewekeza vizuri. Mimi nafikiri ule mto kwa sababu ni source ya Mto Kagera na una maji mengi, badala ya Tanzania kulazimisha kutegemea mpaka kuingia ubia na nchi nyingine tungefikiria namna ya kupata umeme mwingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la viwanda inawezekana wawekezaji wakawa wanakuja lakini wanatukimbia kwa sababu hata waliopo wanalalamika uzalishaji gharama zake ni kubwa sana, tuna kodi nyingi na urasimu mwingi. Kama haya yote tutayarekebisha na tukapata maeneo ambayo ni industrial na yakawekewa kipaumbele cha kuwekewa kila aina ya miundombinu, vision ya Mheshimiwa Rais ya kuweka viwanda inaweza ikatimia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo langu ninalotoka tunachimba madini. Limekuwepo tatizo kubwa sana la wawekezaji wakubwa kuchukua maeneo yote mpaka ambayo walikuwa wanachimba wachimbaji wadogo wadogo. Ni kweli, tunaunga mkono wawekezaji wakubwa wapewe maeneo lakini kama Serikali itaendelea kupata pesa wananchi wanaendelea kuwa maskini tutaendelea kuona uchumi unakuwa kwenye Serikali lakini wananchi wanaendelea kuwa maskini kwa sababu hawana sehemu ya kuchimba. Kila wanapogundua madini anakuja mjanja anawahi Dar es Salaam analipia PL watu wanafukuzwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwangu Geita Mjini, Mgodi wa Geita umepewa kilometa za mraba 192 lakini hata katika maeneo ambayo walikuwa wanachimba wananchi kabla hawajapewa walifukuzwa wakapewa wao. Matokeo yake mji ule umedumaa na hauwezi kukua tena kwa sababu kazi ya asili ya watu wa pale ni kuchimba dhahabu. Naomba Serikali, wakati tunafikiria namna ya kuyafanya madini haya yawe na maana zaidi katika uchumi wa kwetu lazima tufikirie namna ya kuwafanya Watanzania waweze kupata maeneo ya kuchimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Rais alizungumzia suala la namna ambavyo Tanzania haifaidiki na mifugo na madini. Wakati miji hii ikiwa midogo wananchi wenye mifugo walikuwa wanaishi karibu na miji hii. Kadri miji inavyopanuka maeneo ya kuchungia mifugo yanazidi kupimwa na kujengwa nyumba, Serikali haijawahi kutenga eneo kwa ajili ya wafugaji ambao inawaondoa. Matokeo yake maeneo yote haya ambayo tunapima watu wanahamia ambayo zamani yalikuwa machungio ya mifugo sasa hivi kuna nyumba, sehemu zenye majosho kuna nyumba, hivi tunatarajia mifugo hii iende wapi? Hata kama tunasema mifugo hii ipunguzwe, huyo anayekuja kuweka kiwanda hapa Tanzania atapata wapi mifugo ya kulisha kiwanda chake? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri Serikali haijatimiza wajibu wake hapa. Tunayo mapori mengi ambayo hayana faida kwa nchi hii. Tukimuomba hapa Waziri wa Maliasili atuletee taarifa ya Pori la Biharamulo limeingiza shilingi ngapi, inawezekana tukachukua wazo la Mheshimiwa Waziri wa Mifugo la wafugaji kulipia wakawa na faida kuliko…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, nami naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwanza kwa kunipa afya na kunijalia kufika siku ya leo niweze kuchangia kwenye huu Mpango.
Mheshimiwa Spika, naanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwanza kwa kasi kubwa ambayo ameanza nayo. Kasi hii inawatisha watu wote. Ukiona maadui zako wanaendelea kukusifia, basi lazima ujue kuna tatizo. Kwa hiyo, wale ambao wanaona hawafanyi kazi, nadhani wanaogopa kivuli chake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nampongeza Rais kwa kurudisha nidhamu ya Watumishi wa Serikali. Nchi yetu ilikuwa inarudishwa nyuma na mambo mengi sana, likiwemo suala la Watumishi wa Serikali kutokuwa na nidhamu; nidhamu ya muda, lakini hata nidhamu ya utendaji. Hili kama litasimamiwa vizuri, tunaanza kujenga spirit ambayo mtu akiingia ofisini, anafahamu kwamba yuko pale kwa ajili ya kufanya kazi ya wananchi. Hili ni lazima lisimamiwe vizuri pamoja na viongozi wengine walioko ngazi ya chini.
Mheshimiwa Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kurudisha nidhamu ya matumizi. Naamini tulikuwa ni nchi ambayo tunaweza angalau kujitegemea kwa kiwango fulani lakini matumizi yetu yalikuwa yanakiuka baadhi ya mambo na kuonekana ni nchi maskini sana. Nampongeza pia kwa zoezi lake la kuhakikisha kwamba Watanzania wanalipa kodi.
Mheshimiwa Spika, suala la kodi ni suala ambalo Tanzania ilikuwa inaonekana anayelipa kodi ni mshamba. Watu wengi walikuwa wanajisifu kwa kutokulipa kodi. Sasa hivi utasikia malalamiko ya watu wengi kwamba wamebanwa. Watumishi wa Serikali tulikuwa tunalipa kodi kubwa zaidi kuliko wafanyabiashara.
Mheshimiwa Spika, ombi langu tu hapa ni kwamba, zipo lugha ambazo zinatuchonganisha; zinamchonganisha Mheshimiwa Rais. Wapo Watumishi wa Serikali wanakwenda kulazimisha watu walipe kodi kuliko ambayo inatakiwa kulipwa anasema na ni kwa sababu ya Serikali yenu. Naamini watu hawa wakifuatiliwa, kodi ni kwa manufaa ya umma.
Mheshimiwa Spika, nampongeza Waziri wa Fedha kwa kuja na Mpango wake huu. Naamini kwamba hivi vipaumbele ambavyo vimewekwa kwenye Mpango huu kama vitasimamiwa, tunaweza tukaifikisha Tanzania sehemu nyingine.
Mheshimiwa Spika, tunalo ongezeko la mapato ya TRA, mapato yetu ya kodi. Nawapongeza sana! Wasiwasi wangu ni mmoja tu hapa, yapo malalamiko sana kwa wafanyabiashara; hakuna uniformity pale bandarini. Leo atakuja mtu ana container, declaration inaonesha vifaa vilevile ataambiwa Shilingi milioni 20, lakini mtu yuleyule akirudi next time ataambiwa Shilingi milioni 50, lakini jana yake utaambiwa mtu mwingine amelipa Shilingi milioni tisa.
Mheshimiwa Spika, nadhani iko haja ya kuweka utaratibu, badala ya kuacha hii freelance ambayo mhusika anaweza aka-gamble nayo na kuhamasisha rushwa, uwekwe utaratibu ili kila mtu kabla ya kufanya importation, ajue kwamba mzigo huu nikiufikisha Tanzania anakwenda kulipa kodi ya shilingi ngapi.
Mheshimiwa Spika, bila kufanya hivyo, tutaendelea kuruhusu watu kukaa mezani na kujadili na matokeo yake yatakuwa kama aliyosema Mheshimiwa Keissy jana kwamba gari ile ile unanunua Dola 10,000, ukija pale, mtu wa TRA analazimisha iwe Dola 50,000, anakadiria kodi anayoitaka. Matokeo yake, watu wanakimbia gari pale bandarini, halafu Serikali inauza gari zile kwa bei rahisi zaidi kuliko ambayo alikuwa ameisema mhusika. Mimi nasema Serikali inafanya kazi nzuri, tunaipongeza, lakini ni lazima itoe macho zaidi katika suala hili.
Mheshimiwa Spika, niende kwenye Mpango ambao Mheshimiwa Waziri ameuleta. Kwanza nianze na suala hili la elimu. Nimekuwa napata tabu kidogo kuona Tanzania ina output ya wasomi wengi sana, lakini kila kona wasomi wanalalamika ajira. Tatizo ni kwamba hata anayemaliza Chuo Kikuu akimaliza hawezi kujitegemea, akimaliza hawezi kujiajiri, hata yule aliyesomea ufundi, ukimwingiza ukampa kiwanda leo, akifika mle ndani hawezi kufanya kazi aliyosomea. Nasema kwamba, katika kipindi hiki cha miaka mitano, ni lazima mfumo wetu wa output katika vyuo vyetu usimamiwe vizuri ili watu wanaotoka waweze kuwa ni material ambayo inakwenda kupata kazi kwenye soko.
Mheshimiwa Spika, niende mbali, tuna output kubwa sana ya darasa la saba na output kubwa sana ya form four na form six ambao hawapati bahati ya kwenda kwenda kwenye Vyuo. Nataka kushauri, katika nchi zote ambazo zimefanikiwa kupambana na tatizo la ajira hasa kwa vijana, wameimarisha sana kwenye Polytechnic Colleges ambazo ndiyo zinaweza zikasaidia kupunguza tatizo la ajira. Kama tunaweza tukaweka katika Mpango wetu huu wa miaka mitano, tuweke mpango kuhakikisha kila mtoto aliyemaliza kidato cha nne, anakwenda Chuo cha Ufundi na iwe ni lazima. Hawa watu wataweza kujiajiri.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa tumepeleka umeme katika kila kijiji, lakini mafundi wa umeme wanatoka Makao Makuu ya Wilaya. Hii sasa ilikuwa ni wajibu wa Serikali kuona kwamba tunaweka vyuo vya kutosha. Tunavyo Vyuo vya VETA, bado vyuo hivi ni gharama kubwa sana kwa wananchi wa kawaida. Chuo ambacho ulidhani angeenda mtu kusoma akapata ufundi, bado vyuo hivi vinachukua watu kwa kuchagua, wanakwenda watu 100 kati ya watu 10,000. Matokeo yake, bado kundi kubwa la vijana limezagaa mitaani, halina ujuzi wowote na Serikali nina uhakika hata tukizungumza kuwapa ajira, hawa sio sehemu ya kundi tunalofikiria.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kushauri, pamoja na kuzagaa kwa vyuo, pamoja na mpango mzuri wa Serikali, tuweke mpango kabambe wa kuwa na vyuo vya ufundi ambavyo vitamlazimisha kila mtoto anayemaliza kidato cha nne, aende Chuo cha Ufundi ili apate kazi mbadala.
Mheshimiwa Spika, huwa nawaambia rafiki zangu tunaokwenda China; kule China ziko simu watu wanatumia hapa, zinatengenezwa mitaani tu, kwenye nyumba ya mtu. Ziko nguo zinashonwa mitaani, viko vitu vinatengenezwa hata ukitafuta kiwanda, huwezi kukipata kwa sababu kuna msambao wa viwanda vidogo vidogo katika kila kona na ndiyo namna tunavyoweza kupambana na tatizo la ajira kwa vijana, lakini na tatizo la viwanda.
Mheshimiwa Spika, kwenye Mpango kuna suala la viwanda. Tatizo langu ni kubwa. Hivi tunazungumzia viwanda vya namna gani? Viwanda hivi vitapata raw material wapi? Sehemu kubwa ya viwanda tunavyozungumza ni viwanda vya kilimo. Wilayani kwangu tuna Kiwanda cha Pamba cha Ginnery, kipo pale Kasamwa. Kile kiwanda hakijafanya kazi karibu miaka 15 sasa. Ukitazama uzalishaji wa zao la pamba umeshuka kwa kiwango ambacho kinatisha. Tatizo, kwa nini uzalishaji unashuka? Productivity ya uzalishaji inapungua wakati gharama za kilimo zinaongezeka! Viwanda tunavyozungumzia vinakwenda kupata raw material wapi?
Mheshimiwa Spika, nataka kushauri kwenye suala la kilimo, kwanza tu- invest kiasi cha kutosha kuhakikisha kwamba uzalishaji unaongezeka maradufu ili watu watakaoanzisha viwanda wapate raw material. Leo watu wanalima pamba wanapelekewa mbegu feki, halafu mwisho wa siku kwenye uzalishaji mdogo waliopata, wanakwenda kudaiwa na kulazimisha walipe. Matokeo yake ni watu wote wameacha kulima pamba, wanahamia kwenye mazao mengine.
Mheshimiwa Spika, nataka kushauri katika Mpango huu tuwekeze kiasi cha kutosha kuhakikisha kwamba uzalishaji kwenye mashamba, uzalishaji wa mazao katika viwanda ambavyo tunafikiria tunakwenda kuvipeleka, lazima tufikirie namna ya kuongeza mazao yawe makubwa zaidi. Uzalishaji uwe mkubwa zaidi; na njia hapa ni rahisi tu!
Mheshimiwa Spika, cha kwanza ni kuwa na wataalam wetu katika kila kijiji na kuhakikisha wanafanya kazi; lakini kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa wakati. Tulikuwa na tatizo la pembejeo Mheshimiwa Waziri wa Kilimo anajua. Pembejeo zinafika kwa wakulima mwezi wa kwanza. Wakulima wamekwishalima, wameshapalilia ndiyo pembejeo zinafika. Hawa watu wanalipwa!
Mheshimiwa Spika, tumeiambia Serikali kwamba kuna watu wanadanganya kwenye pembejeo, Serikali inatumia pesa nyingi sana, lakini haziwafikii wakulima; zinachelewa kufika. Ndiyo maana mtu analima heka tano za pamba anapata kilo 300. Ni kwa sababu pembejeo zinachelewa kufika. Kwa hiyo, nasema suala la viwanda liangaliwe vizuri kwenye suala la kilimo. Vile vile twende pia kwenye namna ambavyo tunaweza tukawaimarisha wananchi wa kawaida
Mheshimiwa Spika, sina tatizo sana na masharti ambayo yanayowekwa na watu wa Mazingira na kadhalika, lakini nadhani tume-copy sana mambo kutoka Ulaya kiasi kwamba tunashindwa kufikiria katika mtazamo wa Kitanzania, ni viwanda gani vinaweza vikasaidia wananchi wetu? Unaona kila siku tunapambana na watu wanaotaka kujikwamua.
Mheshimiwa Spika, kule Ulaya ukienda, mtu mwenye ng‟ombe wanne anaweza kuanzisha Kiwanda cha Siagi nyumbani kwake na akapeleka mazao yake kwenye Supermarket. Sisi kila siku tukienda kwenye mtu aliyeanzisha kiwanda, tunamfungia, huyu tunamfungia. Badala ya kuwasaidia hawa watu waimarike na wakue, tunawapunguzia uwezo. Utaona Serikali inapambana na watu wapunguze ng‟ombe, lakini haiwambii hao ng‟ombe wanaowapunguza itawasidiaje wabadilike kuwa na maisha tofauti.
Mheshimiwa Spika, mfugaji wa ng‟ombe anafanana sana na mtu mwenye mabasi kumi. Siku zote mtu mwenye mabasi kumi anataka afikishe mabasi 20. Hivi tuliwahi kumfuata mtu mwenye mabasi 20 tukamwambia apunguze idadi ya mabasi? Kwa nini tunafikiria kumwambia mwenye ng‟ombe apunguze, lakini hatumwambii apeleke wapi hizo fedha zake?
Mheshimiwa Spika, naomba sana kwenye hili suala la viwanda, tutafute namna ya kuwasaidia wananchi wa kawaida kuimarisha viwanda vidogo vidogo. Haijulikani SIDO ilifia wapi? Haijulikani kama ipo, inafanya kazi gani?
Nilitarajia tuone Tanzania ina Viwanda vya Sabuni kila Mtaa, Viwanda vya Nguo kila Mtaa na Viwanda vya kila kitu kila Mtaa. Sasa haya mambo hayafanyiki kwa sababu ya masharti mengi yanayowabana Watanzania na kuwafanya waendelee kutegemea bidhaa za kutoka nje.
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze suala linguine. Kwenye Mpango naona kuna mpango wa kuongeza nishati. Nilisema wakati nachangia Hotuba ya Mheshimiwa Rais, nikasema naipongeza sana Serikali na mkakati wake wa kuimarisha njia ya umeme inayokwenda Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Spika, nimekuwa na wasiwasi sana ya kuwa na njia moja kuu ya umeme ya kupelekea robo tatu ya nchi. Napenda kushauri, katika Mpango huu, ile njia iliyotajwa katika Mpango; ya Nyakanazi, ni njia ya muhimu sana. Nchi nyingi zinapata majanga! Linaweza kutokea janga katikati hapa, nusu ya nchi ikawa giza na nchi hii inakwenda kuwa nchi ya viwanda. Ina maana tutasimama uchumi wetu siku hiyo hiyo. Ni lazima tutafute namna ya kuimarisha njia ya pili ya umeme.
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wangu wa Geita, bado umeme unazimika na kuwaka muda wowote kwa sababu njia iliyopo ni ile iliyokuwa inapelekea umeme Sengerema. Umeme ni mdogo sana. Wananchi pale kukatika kwa umeme kwao ni suala la kawaida, lakini umeme mzuri upo jirani tu Katoro pale.
Mheshimiwa Spika, nimezungumza na Waziri mara kadhaa na nimeomba sana katika mwaka huu wa fedha, umeme wa uhakika upelekwe Geita. Ni Mkoa mpya, Mkoa ambao tunatarajia utakuwa na viwanda vingi. Sisi katika Kanda ya Ziwa ni wakulima wakubwa sana wa nanasi, ingawa nanasi zile Mheshimiwa Mbunge mwenzangu alisema zinafaa kutengeneza madawa ya kienyeji, lakini tunapozungumzia viwanda, basi lazima wakulima waambiwe ni mananasi yapi yanayofaa kwa ajili ya kuuza kwenye viwanda, kwa sababu ardhi inakubali kulima nanasi, kahawa na mazao mengine. Ni lazima tukubaliane kwamba tunahitaji umeme ili huu umeme uweze kuwasaidia wananchi wa Geita.
Mheshimiwa Spika, katika Mpango huu, naomba sana, sisi Kanda ya Ziwa kama walivyosema wenzangu, tunalo tatizo la bidhaa zote zinazotoka Dar es Salaam kufika Kanda ya Ziwa zikiwa zimepanda bei. Ukifika Geita leo, utakuta bandali moja ya bati inauzwa Sh. 280,000/= wakati bandali hiyo hiyo Dar es Salaam inauzwa Sh.160,000/=. Ni kwa sababu ya matumizi ya barabara. Tunaomba sana reli, reli ikiimarika, itasaidia kupungua gharama za vifaa vya viwandani ambavyo vinapanda bei kila siku Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Spika, hata gharama ya mafuta iliyoko Geita ni kubwa kuliko iliyoko hapa, ni kwa sababu tatizo kubwa ni Usafirishaji. Hatuwezi kuendelea kujenga barabara zinazobomoka kila baada ya miaka miwili kwa sababu inabeba mizigo mikubwa. Tuwe wakweli! Kama barabara hizi zinatumia mamilioni ya shilingi, tunakopa, wenzetu wanakaa wanasema hawaoni faida ya mikopo na barabara hizo zinakufa, keshokutwa tutalazimika kuzijenga upya kabla ya kulipa madeni. Njia pekee ya kufanya suala hili ni kuimarisha sana mfumo wetu wa reli ili tuweze kuhakikisha kwamba tunakuwa na bidhaa zinazopungua bei.
Mheshimiwa Spika, nimeona kwenye Mpango, kuna mpango wa kujenga Uwanja wa Ndege Chato. Kutoka Geita kwenda Chato ni kilometa zaidi ya 150. Geita ni Makao Makuu ya Mkoa. Naomba sana Wizara hii itakapofika, tunataka kujua kama kutakuwa na mpango wowote kwa Geita kupata uwanja wake wa ndege. Watu hawawezi kutembea kilometa 160; tunakubali kwamba Mheshimiwa Rais anatoka Chato na sisi tunafurahi kuwa na Mheshimiwa Rais Chato, lakini Geita kama Makao Makuu ya Mkoa, tunataka uwanja wa ndege.
Mheshimiwa Spika, Geita tunayo machimbo mengi sana ya dhahabu. Kwa bahati mbaya Serikali imekuwa inapambana zaidi na maskini kuliko inavyopambana na umaskini.
SPIKA: Mheshimiwa Kanyasu, kama unaunga Mkono hoja, dakika zako zimekwisha.
MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOHN C. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba niseme kwa kifupi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba niwaombe wahusika Mfuko wa Jimbo bado unakwenda Halmashauri ya Wilaya hauji Halmashauri ya Mji walishughulikie.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la TASAF, tatizo lililosemwa na Wabunge wengine liko kwangu pia, naomba litazamwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Kamati yangu ya UKIMWI tulikutana na Group of Donors, wanasema ufadhili unaendelea kupungua na wanaitaka Serikali kuongeza uwezo wake kwenye mfuko wa AIDS Trust Fund. Kwa sababu kadri wanavyoonesha inaonekana mwaka huu itapungua zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliambiwa hapa kwamba jukumu la Ofisi za Wabunge liko chini ya TAMISEMI kwa maana ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Tunaomba watoe maelekezo tunapotoka hapa tupate ofisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme lingine, katika Hospitali yangu ya Wilaya ya Geita kuna madeni ya watumishi ya tangu mwaka 2007. Madeni hayo yamefanyiwa uhakiki zaidi ya mara tatu lakini fedha hizo haziendi na hawalipwi. Nilitaka kufahamu kwenye bajeti hii kama fedha hizo zimetengwa na wataanza kulipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika Hospitali yangu ya Wilaya ya Geita yalifanyika mazungumzo ya Serikali ya Mkoa pamoja na mfadhili COTECNA, ambaye walikubaliana kujenga diagnostic centre. Baada ya mabadiliko haya ya Mkuu wa Mkoa yule mfadhili amekwishaandaa fedha anakwenda pale anasema waliopo wote hawatoi ushirikiano. Naomba sana apewe ushirikiano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo tatizo la ukusanyaji wa service levy. GGM wanatoa orodha ya kampuni 1,000 wanazofanya nazo kazi lakini 90% ya hizo kampuni ziko nje ya nchi. Nilitaka kupata mwongozo hizo kampuni zilizoko nje ya nchi ambazo GGM hawataki ku-disclose kwamba zinatoaje service levy, tunazipataje hizo fedha Halmashauri ya Mji wa Geita? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yangu tulitembelea Buhangija, tukaenda kwenye kituo cha watoto albino. Tulipofika pale tulikuta kuna taarifa kwamba wake wa viongozi walifanya harambee kuchangia kituo kile miaka miwili iliyopita lakini fedha hizo hazijawahi kufika na tulikuwa na Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Possi. Tunaomba kujua waliofanya harambee hizo fedha zilikwenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kuchangia kwenye suala la ujenzi wa ofisi. Nchi hii kila Halmashauri ina ramani yake, nataka kushauri pawe na common ramani ya Halmashauri zote. Halmashauri yangu ina fedha za kujenga ofisi miaka minne sasa fedha ziko ndani, ofisi haijengwi na kwa taarifa zilizopo wamepunguza karibu shilingi milioni 300 kuchoresha ramani mpya. Mkuu wa Mkoa aliyekuwepo alikuwa amewaletea ramani ambayo tayari imechorwa na imejengwa sehemu zingine. Naomba Mheshimiwa Waziri afuatilie ili Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya iweze kujengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, kwa sababu ya muda nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kuhusu ada elekezi, Serikali iwaache wamiliki kupanga bei kwa kuwa gharama za uendeshaji wa shule hizo ni kubwa sana kutokana na michango mingi na kodi. Pia shule hizi hazifanani kutoka moja hadi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nizungumzie kuhusu vibali vya Walimu wa nje. Serikali iangalie namna ya kuondoa vizuizi vya Walimu wa kutoka nje kufundisha Tanzania hasa Walimu wa masomo ya hesabu na sayansi. Urasimu mkubwa wa Serikali wa kupata working permit na kodi kubwa inayotozwa na Serikali inakatisha tamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Chuo cha VETA Geita. Naiomba Serikali kunipatia majibu ni lini chuo cha VETA kitajengwa katika Mkoa wa Geita ambao ni mpya na eneo la kujenga chuo hicho lilitengwa toka mwaka 2014. Kwa mujibu wa VETA, ujenzi wa chuo hicho ulikuwa umefadhiliwa na ADB kwa thamani ya 6.7 billion, leo miaka miwili hakuna kinachoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne ni kuhusu utitiri wa vyuo binafsi. Serikali ichunguze sana viwango vya elimu vinavyotolewa na vyuo mbalimbali vilivyosajiliwa na NECTA. Mfano ni Chuo cha Elimu ya Utalii Musoma kimefungua matawi katika wilaya za Kanda nzima ya Ziwa, je, ubora wa certificate na diploma hizi unafanana? Hii ni pamoja na matawi ya vyuo vikubwa na vidogo Tanzania ikiwemo CBE, Mipango na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, madeni ya wazabuni mashuleni. Serikali itoe taarifa ni lini itawalipa wazabuni fedha zao walizotumia kutoa huduma mashuleni. Hivi sasa hali ya huduma katika shule zetu ni mbaya kutokana na madeni haya ya wazabuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, nyumba za Walimu vijijini. Naishauri Serikali kuanzia sasa itoe tamko la kuzuia kabisa halmashauri zote kujenga nyumba za watumishi wa mjini, kuacha kujenga ofisi za vijiji na kuacha kununua magari mapya na kuhamishia pesa yote kwa miaka mitatu kwenye nyumba za Walimu. Nashauri pia ramani ya nyumba simple iandaliwe kwa ajili ya nchi nzima mfano vyumba viwili vya kulala, sitting room na jiko.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Nyanza Cooperative Union wameshindwa kuendesha viwanda vya pamba kutokana na kuwa na madeni makubwa Benki. Pia kutokana na kupitwa na teknolojia ya viwanda walivyonavyo ambavyo sasa haviwezi kushindana katika soko kutokana na gharama za uzalishaji, kwa kuwa Serikali hivi sasa inataka kufufua viwanda vyote. Napenda kushauri Serikali kwanza kuwasaidia Nyanza kupata mbia ambaye atasaidia mitaji na teknolojia mpya katika ginneries.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Geita tunalima mananasi bora kabisa hapa Tanzania. Kwa muda mrefu zao la nanasi halijatumika kama kivutio cha uwekezaji na hivyo kupunguza uzalishaji kwa kuwa wakulima hawana soko la uhakika. Naiomba Serikali kupitia agenda ya Tanzania ya viwanda kutupatia mwekezajiwa Kiwanda cha Nanasi Geita na soko la nje la zao hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Tanzania inataka kuwa nchi ya viwanda, nashauri kila Mkoa upewe maelekezo ya kupima maeneo maalumu ya viwanda, yaani industrial area. Maeneo haya yatengenezewe hati na yamilikiwe na Halmashauri ili mwekezaji akifika usiwepo usumbufu wa kupata maeneo. Maeneo haya yapewe miundombinu ya umeme, barabara na maji ili kumfanya mwekezaji kuvutika na hali hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upatikanaji wa mitaji, naomba kushauri kwamba Serikali mara itakapokuwa imefanya utafiti katika eneo fulani na kuona panafaa kiwanda, lakini hakuna wawekezaji, utumike mtindo uliotumika Rwanda ambao ni kwamba watu wenye mitaji ya wastani wanaunganishwa kwa hisa na kupewa access ya kukopa kwa collateral kwenye Benki maalumu kama TIB na kuwafanya wazawa kadhaa kumiliki kwa pamoja kiwanda. Haya yamefanyika Rwanda na viwanda vingi vinafanya kazi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Nakushukuru sana Mwenyekiti, na naomba nimshukuru pia Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema, niwashukuru pia wapiga kura wangu wa Jimbo la Geita Mjini na wananchi wa Geita kwa ujumla wake kwa uvumilivu wao mkubwa wanaoupata kwenye matatizo ya umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwanza kwa kusoma kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 15 ambapo amesema Serikali iliajiri kampuni ya Shaka Consult Group ya Misri kuwa mshauri mwekezaji wa kusimamia utekelezaji wa mradi wa Bulyanhulu - Geita KV-220 kwenye urefu wa kilometa 55.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ameendelea kusema hapa lakini interest yangu ni kule chini; anasema gharama za mradi huu ni dola milioni 23 sawa na takriban bilioni 41. Jumla ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi huu ni shilingi bilioni sita, very interesting, na unatarajiwa kukamilika 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa mradi huu ambao ameukusudia kuupeleka Geita. Ninaamini kwamba una nia njema, lakini natazama fedha zilizotengwa sasa na pia natazama muda ambao umejiwekea kutekeleza nayaona matatizo makubwa ya umeme katika Mji wa Geita kwa sasa yataendelea kuwa kero kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anafahamu nimsumbua sana mara kwa mara, umeme wa Geita Mjini unazimika kila saa, umeme wa Geita Mjini ambao unatokea Sengerema kuja Geita ni mdogo, ulikuwa umefikiriwa kwa ajili ya Mji wa Sengerema na baadaye ukapelekwa Geita. Umeme ule inapofika saa moja jioni unawaka lakini taa haziwaki. Nimemueleza hili Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri analijua, sasa nilitarajia kwenye taarifa yake hii atakuwa angalau na mpango wa dharura kwa sababu Geita pale ni Mji mkubwa, lakini ni Mkoa ambao tungeweza kuweka mpango mzuri wa dharura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi ninayo mapendekezo, tunao umeme kilometa 22 tu kutoka Geita Mjini ambao uko Katolo ambao ni umeme wenye nguvu. Wakati unafikiria mradi mkubwa huu ambao utaisha 2018, na inawezekana ukaisha 2020. Umeme huu ambao uko kilometa 22 tu kutoka Katoro kuja Geita, na ambao gharama yake inakadiriwa haifiki bilioni moja kuuvuta kuufikisha Geita Mjini, ingelikuwa ni suluhisho la kwanza la kupeleka umeme katika Mji wa Geita. Hivi ninavyozungumza na wewe kata zinazotengeneza Mji wa Geita wenyewe, kata za Nyankumbu, Bombambili, Buhalahala, Mtakuja zote hazina umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani umeme upo pale pale kati kati ya Mji lakini Vitongoji vyote vya Geita Mjini havina umeme. Pamoja na huo uliopo kutokuwa hautoshi lakini havina umeme. Kuna sehemu wameweka transfoma ambayo kila inapofika jioni saa moja umeme unazimika. Nilikuwa nakuomba sana Mheshimiwa Waziri pamoja na nia njema ya mradi huu unaokwenda mpaka 2018 ambao pia naona fedha zake zimewekwa za kuanzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe suluhisho la sasa, kwa sababu umeme uliopo Katoro una nguvu, utolewe umeme upelekwe pale. Bahati nzuri sana Geita tuna Meneja mzuri wa TANESCO, ana-respond haraka, hana matatizo makubwa, kinachosumbua pale sasa ni kumwezesha ili aweze kufanya kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niende kwenye umeme wa REA. Katika Jimbo la Geita Mjini umeme wa REA bado katika kata zote 13 haujaenda, nimefanya mawasiliano na Meneja wa REA wa Kanda ile amesema ametuingiza kwenye awamu hii, lakini nilikuwa naomba sana, kwa sababu tatizo hili naliona hata katika Jimbo la Geita Vijijini, kazi ya mkandarasi imekamilika mpaka sehemu ya kutoka Nyamadoke tayari; pale panatakiwa tu kuunganishwa ule umeme, leo karibu miezi sita hapajaunganishwa. Nilikuwa naomba sana kwenye umeme wa REA Mheshimiwa Waziri suala hili lipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili ni suala la wachimbaji wadogo wadogo. Mheshimiwa Waziri alikuwepo Geita, na nashukuru kwamba tulifanya mkutano naye na akatoa takwimu nyingi sana. Lakini anakumba nilitoa ushauri wangu pale sikumpinga nilitoa ushauri, ana takwimu nyingi sana zinazoonesha wachimbaji wadogo wamepewa maeneo lakini wanaopewa ni wale wale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, anayepewa leo London – Singida, anayepewa leo Nyarugusu, anayepewa Kahama, majina ni yale yale. Nilimshauri atengeneze database, atagundua yako majina yale yale yanazunguka. Kila yanapogunduliwa madini wanakwenda wanafukuza wenyeji, wanaunda ka-SACCOS wananunua watu wanahamia pale. Nashauri kwamba wananchi wale wa kawaida bado hawapati maeneo, na ndio maana kelele za magwangala zitaendelea kuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakati tunazungumzia maeneo ya wachimbaji wadogowadogo lazima tuangalie watu wanaojirudiarudia, watu ambao kila mara yanapogundulika madini wanakwenda pale kwenda kutafuta maeneo mapya. Tulipokutana na Mheshimiwa Waziri kwenye ziara yetu Geita tulimgusia kuhusu milipuko. Mheshimiwa Naibu Waziri tulikuwa naye Geita, tulikwenda kwenye nyumba ambazo zimeathiriwa na milipuko, tulikwenda kwenye nyumba ambazo vigingi vya GGM viko ndani ya makazi yao, wale watu hawaruhusiwi kupima, hawaruhusiwi kuuza, wanaonekana eneo ni la mgodi lakini mgodi wanasema hawana kazi nalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishauriana na Mheshimiwa Naibu Waziri na akatoa muda, akawaambia wafanye declaration kama wanalihitaji lile eneo walipe fidia watu watoke na kama hawalihitaji, wawaruhusu watu waendelee na maisha yao mpaka leo hili suala halijafanyika, matatizo ya watu yanaendelea kuwa pale pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu niseme kwamba kuendelea kukaa katika vigingi watu hawa wanaendelea kuwa maskini. Hawawezi kupima, hawawezi kukopeshwa, hawawezi kujenga nyumba za kudumu. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutoa majibu atuambie anafanya nini kwa sababu hali hii inasababisha wananchi wangu wa Jimbo la Geita kuendelea kuwa maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kidogo kuhusu magwangala. Kama wanavyosema wenzangu magwangala inatokana na vijana wengi na wanotaka biashara za madini kukosa maeneo ya kuchimba; si suluhisho la matatizo ya wachimbaji wadogo wadogo kwa sababu nina uhakika magwangala yale hata yakitolewa leo baada ya miezi miwili, yatakwisha na yatakapokwisha yale magwangala tutatengeneza tatizo jingine kubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilitaka kusema pamoja na nia njema ya kutoa magwangala haya ambayo wananchi wanayapigia kelele, wananchi walikuwa na maeneo yao walikuwa wanachimba ya asili pale Geita, kama Nyamatagata, Samina wakaja wakatolewa, lakini maeneo yale dhahabu yake iko juu juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alipokuwa Geita akisema yeye hawezi kubadilisha hata mtu ampige risasi. Mimi nataka nimshawishi Mheshimiwa, sheria inasema kila baada ya muda, wanapofanya revision ya license kuna maeneo watu wanayaachia, ni vizuri sana Mheshimiwa Waziri maeneo ambayo wanayaachia yawe ni maeneo ambayo wananchi wanaweza wakachimba wakapata dhahabu ya juu juu.
Mheshimiwa Mwnyekiti, matatizo tuliyonayo sasa hivi Geita ni kwamba hata kama watu wa GGM wangejenga hospitali, shule na barabara kama jamii inayowazunguka pale inalala njaa, kama jamii inayowazunguka pale bado wanaishi katika mazingira kama wako utumwani bado wataendelea kuwachukia wawekezaji na tutaendelea kuuchukia mgodi.
Kwa hiyo, mimi nilitaka niwashauri kwamba ni lazima wananchi wapewe maeneo ya kuchimba, na hili liko ndani ya uwezo wako kwa sababu maeneo tunayo. Tatizo kubwa ni moja walipelekwa maeneo ya Isamilo, wakapewa license karibu 17 za SACCOS wamechimba watu wameweka karibu milioni 200 madini hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamechimba pale wanakutana na maji madini hakuna, kwa hiyo mara nyingi migodi inaachia maeneo ambayo imefanya utafiti imegundua kwamba dhahabu zilizopo pale ni ndogo na hazifai. Kwa hiyo nikuombe sana utakapotaka kutoa maeneo tuhakikishe kwamba maeneo haya yana madini ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni suala la service levy. Mheshimiwa Waziti alipokuwa Geita, tulimwambia hatuna mgogoro na Geita Gold Mine ingawa mchango wao wa service levy ni mdogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Geita ule ni mgodi wa pili Afrika kwa dhahabu nyingi, wanatupa bilioni nne. Tuliuliza swali, hizi ni asilimia ngapi ya mapato yao? Kwa sababu tunaamini mapato yao ni makubwa sana, lakini la pili, wanatoa orodha ya kampuni 1,000 wanazofanya nazo kazi. Katika hizo asilimia 80 kampuni zile ziko Ulaya, Australia, New Zealand na Marekani, wanafanya nazo electronic business. Kwa hiyo, anampa Mkurugenzi wa Halmashauri aende akakusanye service levy kwa kampuni ambayo haina license Tanzania, hailipi kodi Tanzania, haina address Tanzania. Tulimwambia Mheshimiwa Waziri, watu wa mgodi walazimishwe kufanya kazi na kampuni za Tanzania ambazo tunaweza kuzi-trace na kujua zinapatikana wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wanakupa kampuni iko New Zealand halafu wanakwambia ukusanye service levy kampuni hii haijulikani, haina leseni, hailipi kodi za Serikali, hata Tanzania haina address na Mheshimiwa hili niliwahi kufika mpaka ofisini kwako nikakutana na Katibu Mkuu wa Wizara, nikamshauri, nikazungumza naye na akasema atalishughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hawa watu pamoja na kuwaibia Halmashauri ya Geita, bado pia wanaiibia Serikali. Huwezi ukalipa mtu dola milioni moja kampuni yake iko South Africa, Tanzania haina leseni, hailipi kodi, haina ofisi na Serikali ipo inakubali hizo hesabu wakati wa kufanya Cooperate tax.
Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana hili liangaliwe vizuri. Na inawezekana kabisa haya yanafanyika kwenye makampuni yote katika nchi hii, kwa sababu visingizio ni kwamba kuna vipuri ambavyo vinaagizwa Ulaya na Watanzania wengi hawana uwezo wa kuviuza, yes tunakubali, lakini procedure za kufanya biashara Tanzania zinajulikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Watanzania hamuwaruhusu hata kufungua kibanda cha soda bila kupata TIN Number. Kwa nini huyo anayellipa mamilioni ya shilingi anaanza kufanya biashara na Mgodi na analipwa pesa na inakuwa declared kwenye hesabu wakati hana leseni Tanzania na halipi kodi? Ushauri wangu Mheshimiwa Waziri asaidie kupata hizi fedha kwa sababu ni fedha nyingi na tunazihiitaji kwa ajili ya maendeleo ya Mji wa Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kama unavyoitaza Geita sasa hivi, kuna mashimo makubwa, ambayo tayari dhahabu zimekwisha. Inawezekana kabisa miaka ishirini ijayo tukabaki na mashimo yale na wananchi wa Geita wakaendelea kubaki maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi letu ni kwamba wakati mgodi unafikiria kufanya CSR washirikiane na Halmashauri kuangalia miradi ambayo sisi tunadhani ina tija kwetu. Siyo wao wanabuni mradi wao halafu ule mradi wanaugeuza kuwa mradi wa wananchi wa Geita. Tunaunga mkono juhudi zao tunapenda waendelee kuwepo, tunataka wawekezaji zaidi lakini lazima waangalie mipango ya Halmashauri namna gani wataingia kwenye mipango hiyo kuliko kuja na mipango yao wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamekwenda wameanzisha, chuo cha kushona cherehani wameanza na watu 90 sasa hivi wako watu kumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naomba pia nitumie nafasi kukupongeza kwa namna ambavyo unaendesha Bunge letu na niwape pole wenzetu ambao wanasubiri siku ambapo utalegeza msimamo. Nadhani hii ndio namna bora ya watu kuheshimu taratibu na sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nianze kuchangia kwa hoja ya Mkoa wa Mwanza, Geita na Kagera kuonekana ni mikoa maskini zaidi Tanzania. Mwanzo ni kweli na nilikuwa napata shida, na nilikuwa sielewi mantiki ya suala hili linatoka wapi? Lakini nimekuja kugundua sababu za msingi ni kama ambazo wenzangu wamezieleza. Yapo mazao na kazi za msingi ambazo zilikuwa zinafanya maeneo haya yaonekane maeneo ambayo uchumi wake uko juu, yanaenda yanakufa polepole.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukizungumzia Mkoa wa Mwanza na Mkoa wa Geita, ambao miaka yote tulikuwa tunajivunia pamba, sasa hivi pamba imekufa hakuna dalili kuna mkakati maalum wa Serikali wa kurudisha zao hili kwenye chati na ukiangalia trend yake ya uzalishaji kwa miaka mitano, mwaka jana ilikuwa even worse. (Makofi)
Kwa hiyo, nadhani kwamba, hatuna sababu kwa nini tusiwe maskini. Mkoa wa Kagera walikuwa kahawa inakosa soko, walikuwa na migomba, migomba inaugua, ndivyo ilivyo katika mikoa mingine mingine ya Mwanza na Geita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaanza msimu wa pamba, lakini nataka kukuambia mpaka leo bei haijulikani na wananchi wana pamba iko ndani na ni haya haya ambayo mwakani zikija takwimu hapa itaonekana mikoa hii ni maskini sana. Kwa hiyo, nilikuwa nasema, Serikali pamoja na kutoa takwimu hizi bado ina kazi ya kufanya ili kuhakikisha kwamba, ina-coordinate mazao haya na kazi hizi za wananchi ziweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukiangalia katika Mkoa wa Geita, ambao una dhahabu katika kila Wilaya, haijulikani mpaka leo wale wachimbaji wenyewe wa dhahabu wanauza wapi? Wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu haijulikani wanauza wapi? Wanaojulikana ni wanunuzi wa dhahabu wakubwa wakubwa. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba uchumi huu mdogo katika level ya chini hauko coordinated, haujulikani. Lazima wananchi hawa waonekane ni maskini, lakini influx inayosababishwa na machimbo katika Mikoa ya Geita na Mwanza na wapi ni kubwa sana na watu wote hawa wako bize kwenye kazi za kiuchumi. Nilikuwa nadhani watu wa uchumi wanatakiwa wafanye kazi vizuri zaidi hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye pendekezo la kuondoa msamaha wa kodi kwenye bidhaa ambazo walikuwa wanauziwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Naweza nikaunga mkono suala hili, lakini naomba nitoe mapendekezo yangu kwamba bidhaa hizi zinaweza zikalipiwa kodi, lakini uwekwe utaratibu ambao utavifanya vyombo yetu vya ulinzi na usalama viwe na credit card wakati wa kufanya manunuzi. Kwa mfano kama askari hawa wataweza kwenda kwenye duka lolote bila kujali duka hili ni lile ambalo limetengwa, wakiwa na credit card au debit card na wakaweza kupata punguzo la kodi pale pale, mantiki ya maduka haya itaendelea kuwa ile ile na mantiki ya kuwapa huduma nyepesi wanajeshi watu itakuwa ile ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, unapoongeza mshahara au ukaongeza pesa kwenye mshahara wake haijulikani huyu mtu atanunua nini kwa mwezi, nina uhakika kwamba tutaendelea kufanya maisha ya vyombo hivi kuwa vigumu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, na naomba nichangie pia kwenye suala la kufutwa kwa misamaha kwenye taasisi mbalimbali. Ni kweli kwamba, Serikali ilikuwa inapoteza karibu shilingi trilioni mbili kwenye kodi kwa sababu ya misamaha, lakini ninataka tu kutoa hoja hapa kwamba kama vyombo hivi vitalipa kodi, urasimu wa namna ya kurejeshewa kodi hii lazima Serikali ijipange vizuri. Kwa sababu nitapa wasiwasi namna wanavyokwenda kugagua na kujiridhisha kwamba, bidhaa hizi zilizoingizwa zimetumika kwa mujibu wa malengo yaliokusudiwa na matokeo yake tuta-demoralize hawa waliokuwa wanasaidia. Maana yake ni lazima tukubaliane nchi yetu mpaka leo, sehemu kubwa ya Hospitali zilizo kwenye Wilaya, sehemu kubwa ya taasisi ziliko hapa, shule pamoja na nini zinamilikuwa na taasisi mbalimbali. Kama watu hawa watakatishwa tamaa na wataacha tutakuwa tunarudi nyuma badala ya kwenda mbele. Kwa hiyo, lazima Serikali iangalie namna ya kulifanya hili ili lisije likatela usumbufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, yamefanyika marekebisho mbalimbali kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri, nampongeza sana Waziri kwa kuondoa baadhi ya tozo kero kwenye maeneo mbalimbali. Lakini nilitaka kusema bado mazingira ya kufanya biashara kwenye nchi yetu ni magumu sana. Nitoe mfano sehemu moja tu. Sehemu ya hoteli, mtu akiwa na hoteli leo pamoja na kupata leseni, pamoja na kupata tax clearance kutoka TRA itaanza kulipa OSHA, atalipa Fire, atalipa hotel levy, ana aina ya tozo pale karibu kumi, ambazo zote hizi zinafanya mzunguko wa pesa kwa wananchi kuwa mdogo. Sasa inaonekana Serikali inajiaanda tu kukamata pesa kila kona na kuzirudisha kwake.
Mheshmiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa nadhani kwamba bado kuna haja ya kuangalia vizuri, kwenye hoteli hapo utakuna na mtu wa afya, utakutana na mtu wa TFDA, utakutana na kila aina ya ushuru na wote hawa ni vyanzo vya mapato, nilikuwa nadhani kuna haja nzuri ya kuliangalia vizuri upya hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kodi za majengo, naweza kusema kwamba nilikuwa naunga mkono watu wa Halmashauri waendelee kutoza hizi, lakini nitaunga mkono TRA iwapo Mheshimiwa Waziri, utatuambia ni kwa namna gani pesa zilizokadiriwa kwenye Halmashauri atahakikisha zinapatikana kama zilivyo kwenye bajeti, vinginevyo tutajikuta kwamba, wakishindwa kukusanya TRA madhara yakuwa makubwa sana kwenye Halmashauri zetu za Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu makato kwenye gratuity ya Mbunge; nilitaka tu nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, sisi Wabunge wa Bunge la Tanzania kwanza ni Wabunge tunaolipwa kidogo zaidi kuliko Mabunge yote Afrika Mashariki. Nataka nitoe takwimu hapa, ukichukua salary na allowance, Bunge la Kenya walipwa dola 11,000, Rwanda dola 9,000, Uganda dola 8,000, South Sudan dola 7,000, Burundi dola 6,000, Tanzania ni least pay dola 5,000, hii ni salary na allowance. Sasa atuambie baada ya kuingiza haya makato anakwenda kuboreha wapi ili tufanane na nchi zingine? Kama hilo halifanyiki nataka kumshawishi Mheshimiwa Waziri afikirie namna mpya ya kutanua hii tax base kwa sababu kinachomsumbua sasa ni kufikiri kwenye base ile ile wakati unaongeza projection. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na njia rahisi ya kutanua tax base, akumbuke kati mwaka 2007 na 2010, Serikali iliweka stimuli kwenye baadhi ya viwanda na mazao ili kuwa inalinda visife ili Serikali isipoteze walipa kodi. Sasa ushauri wangu hapa tunavyo viwanda vingi vimesimama, kama tunataka kuongeza kukusanya mapato tupeleke pesa huko viwanda vifufuke tuanze kukusanya kodi vinginevyo leo wataanza kukata kodi kwenye gratuity, kesho watakuja kwenye allowance, atakuja kwenye per diem baadaye pataisha pa kukata kodi wakati huo anaendelea kupanua projection. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa ninaomba pia suala la polisi ambao wamewekwa kwenye chanzo cha mapato. Unapo-commercial raise service ukawambia polisi wakae barabarani ukawapa malengo ya kukusanaya shilingi bilioni moja, maana yake unawambia wakamate sana watu barabarani na kwa tabia ya polisi hawa-negotiate na wateja tutaanza kupata migogoro mingi kwa sababu watajielekeza kwenye kufikia malengo ya kukusanya shilingi bilioni moja kwa mwezi. Nilikuwa nadhani hawa wangeachwa watoe huduma na inapotekea wanatoa faini iwe ni faini ya kawaida, lakini wanapowekwa kwenye kikapu cha kuanza kukusanya pesa na kwamba lazima walete shilingi bilioni fulani lazima tunatengeneza mgogoro mkubwa kati ya watumiaji wa barabara na poilisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na lingine ni kuhusu kodi kwenye withdraw mbalimbali M-pesa na benki. Nataka tu kufahamu kwamba Serikali imejiandaaje kuweka regulatory board ambayo ita-control sasa wasipandishe hovyo hovyo. Walizoea hizi pesa zote kuzichukua wao, sasa tumepeleka kodi pale matokeo yake wataongeza, tutajikuta watu wanaogopa kupeleka fedha benki.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nashukuru sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, namshauri Waziri aangalie upya ongezeko la kodi eneo la mapato ya ndani. Kila mwaka tunapoongeza budget projection ya nchi matokeo yake kila biashara inaongezewa kodi. Kuongezeka kwa kodi katika biashara ileile, mtaji uleule na mauzo yaleyale au yaliyopungua kwa zaidi ya asilimia 50, kunasababisha wafanyabiashara wengi kushindwa kulipa kodi, kufilisika na kufukuza wafanyakazi. Serikali iangalie vyanzo vipya kama kuanzisha malipo au tozo kwenye pikipiki zote kwa kuwa wanaoziendesha siyo wamiliki wake. Kuruhusu biashara hiyo kuwa bure maana yake wapo matajiri wengi hawalipi kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali iongeze uwekezaji katika kilimo cha mazao ya biashara na chakula. Kwa kuwa kama wananchi watawezeshwa vizuri katika kilimo tatizo la fedha litapungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iweke mpango mahsusi kuhusu maji. Mpango huo uhusishe ongezeko la Sh.50 kwenye lita ya mafuta ambayo yanaingia nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa ulipaji wa Road Licence uwe tofauti na sasa na nashauri kodi hiyo iunganishwe kwenye bei ya mafuta ambapo kila lita moja iwekewe ushuru maalum wa mafuta kulipia kodi hii. Mfano gari moja linatumia lita 20 kila siku zidisha kwa mwaka mmoja (20x360=7,200 lita). Ukichukua lita 7,200x50% tu ambayo itaongezwa kwa gari ndogo (tax) italipa ushuru wa Sh.360,000. Ushauri wangu hapa ni kwamba Road Licence fixed ikiondolewa na kuwekwa kwenye mafuta Serikali itapata pesa nyingi zaidi.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru. Kwanza naomba
kupongeza Kamati zote mbili kwa taarifa zao nzuri, lakini naomba nianze na tatizo la umeme
kwenye Mji wa Geita.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila siku umeme Geita unakatika kila siku zaidi ya mara nne.
Nimezungumza mara nyingi sana na Waziri, nimezungumza na Naibu Waziri na tatizo hili kwa
zaidi ya miezi nane halipatiwi majibu. Nafahamu kuna mradi ambao unaendelea lakini nadhani
speed ya mradi huo ni ndogo sana, kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Waheshimiwa Mawaziri
wanisikie kwamba kuna tatizo kubwa sana la umeme katika Mji wa Geita.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, mji wenyewe wa Geita ule, ni nusu peke yake ndiyo
unaowaka umeme, sehemu zingine umeme hakuna. Tunaambiwa tunasubiri umeme wa REA na
niliongea na Naibu Waziri nikamuomba basi atupe ratiba ya mradi wa REA wa nchi nzima tujue
kwamba Geita unakuja lini.
Mheshimiwa Naibu Spika, linguine pamekuwepo na malalamiko mengi sana kwamba
watu wanalalamika kwanini Geita uwanja wa ndege umejengwa Chato? Sisi watu wa Geita
ndiyo tunajua. Mheshimiwa Rais akitokea Geita kwenda Chato ni kilometa 160. Ili afike Chato,
magari yanayotangulia mbele yanasimamisha watu matokeo yake kwa saa sita watu
wamesimama Barabarani. Kwa hiyo, solution ni kumjengea uwanja karibu na nyumbani
kuondoa ule usumbufu. Kutoka Geita kwanda Chato ni kilometa 160 kwa hiyo, watu
wanaolalamika kujengwa uwanja Chato ni kwa sababu hawafahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hili, nilikuwa naiomba tu Wizara ya Mawasiliano isiondoe
sasa nafasi ya kutujengea uwanja wa Mkoa wa Geita kwa sababu hatuwezi kuzuia Mheshimiwa
Rais ule uwanja usijengwe kule. Hata usipojengwa kero yake ni kubwa sana kwa wananchi pale
barabarani.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la tatu, Mheshimiwa Rais Mgodi ule wa Geita karibu
miaka kumi ijayo utakuwa umeshachimba dhahabu. Geita hii tunayoizungumza ambayo kwa
Mgodi ule ndiyo the leading gold producer hapa Tanzania na karibu ya pili Afrika, wananchi
bado ni maskini. Na ukitazama, sioni dalili za namna ambavyo huu mgodi utabadilisha maisha
ya Wananchi sasa hivi kwa muda mfupi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali, wangeanzisha mfuko wa natural
resources rent extraction ambao unafanyika katika nchi nyingi sana. Kwa mfano, mfuko kama
huu upo Norway, mfuko kama huu upo Marekani. Wakati kazi za madini zinapokuwa
zinaendelea, mfuko maalum kwa ajili ya kuwafanya wananchi wa maeneo yale baada ya
shughuli za madini kuisha waweze kuendelea na mambo mengine unakuwa umeandaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyokwenda sasa hivi, kesho kutwa dhahabu zitakwisha
kama zinavyoisha Kahama, wananchi watabaki maskini, Geita hatuna hospitali, Geita hatuna
barabara, Geita hatuna maji, Geita hatuna kila kitu lakini dhahabu zipo nyingi. Kwa hiyo,
nilikuwa nafikiri kwamba kuna tatizo hapa, siyo suala la kwanza duniani ni tatizo ambalo watu
wengi wameshindwa kulisemea hili. Tukianzisha mfuko huu ambao utatusaidia watu wataweza
kusoma, utaweza ku-deal na humanitarian crisis lakini utaweza kushughulika pia na mambo
mengine ya development kwenye maeneo yale. Sasa hivi tunapata 0.7 CSR kwa miaka 17,
mgodi umejenga shule moja ya wasichana. Kila siku wanaonesha kwenye television, miaka 17
0.8 percent ya CSR wangeweza kuifanya Geita kuwa Ulaya, lakini kwa sababu wanaamua
wenyewe wafanye nini hakuna kinachooneka kimefanyika pale. Maisha ya wananchi wa Geita
inaendelea kuonekana kama vile hawapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda nashukuru kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba na mimi nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kunipa afya njema na kupata nafasi ya kusema machache kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini pia na Kamati ambazo ziliwasilisha maoni yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na kwenye hiki kitabu cha Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 21. Waziri Mkuu ametoa takwimu za upatikanaji wa chakula kwa mwaka uliopita na akagusia kwamba mwaka huu kuna maeneo ambapo hali ya hewa haikuwa nzuri sana. Nilichokuwa nakitegemea hapa kidogo na nitoe ushauri ni kwamba kutokana na hali hiyo kutokuwa nzuri, kwanza nilitarajia nione hapa kama kuna akiba kiasi gani sasa ya chakula lakini tunakitumia kwa namna gani ku-control bei inayoendelea kupanda kwenye soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza jana Mwanza gunia la mahindi lilikuwa shilingi 125,000 na wakati kelele za uhaba wa chakula zinaanza gunia la mahindi lilikuwa shilingi 80,000. Hii maana yake ni nini? Kadri tunavyokwenda kuja kufikia mwezi wa kumi kama hakuna
mechanism ya Serikali ku-control bei ya mahindi yatafika shilingi 160,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachozungumza hapa sio njaa, hatuzungumzi njaa tunazungumzia kwamba bei ya chakula inapanda kwa sababu Serikali ni kama haijachukua position yake ya ku-control bei ya chakula kwenye soko. Wakati tunazungumza wakati ule bei ya mchele ilikuwa
shilingi 1,200 leo ni shilingi 2,500, Mwanza ni shilingi 1,800. Maeneo yote haya ninayoyazungumzia hawakulima kwa sababu mvua hazikuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ombi langu Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama tunayo stock ya chakula kwenye godowns, Wizara ichukue position yake, chakula kingie kwenye masoko na bei elekezi itolewe ili kisiendelee kupanda, vinginevyo purchasing power ya wananchi
inapungua. Wananchi kipato ni kilekile, chakula kinapanda, matokeo yake watajikuta hata hiyo shilingi 2,000 ya kula kwa siku inakosekana. Hilo ndiyo lilikuwa ombi langu kwenye huu ukurasa wa 21.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 25 amezungumzia kuhusu hekta 38,567 za wachimbaji wa madini. Tatizo langu mimi sio utengaji wa maeneo, nilimwambia Waziri wa Nishati na Madini, alikuja Geita akazungumza takwimu kubwa za
kuwapa watu maeneo ya kuchimba. Nikamwambia tatizo kubwa lililoko hapa wanaopewa ni walewale. Ukiingia kwenye database utamkuta Kanyasu huyu ana-appear kwenye karibu kila eneo dhahabu inapotokea wale ambao wanatakiwa kabisa wapewe maeneo haya hawapewi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza na wewe tuna vikundi zaidi ya 100 Geita vimejiandikisha vinasubiri maeneo ya kuchimba havipewi, lakini ukienda kwenye takwimu za Wizara atakutajia kubwa ya watu ambao kimsingi ni walewale wachimbaji wakubwa ambao wanahama toka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana, ni ahadi yetu kwenye Ilani ya CCM, tutawapa watu maeneo ya kuchimba, lini? Huu ni mwaka wa pili sasa. Kama yapo tunaomba yaanze kutolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukurasa wa 28 limeongelewa suala la umeme. Geita kila siku umeme unakatika. Hivi ninavyozungumza na wewe umeme hakuna, unakatika zaidi ya mara nne. Nimezungumza na Waziri na Naibu Waziri, wana matengenezo ya kutoka Busisi kwenda
Geita karibu miaka miwili hayaishi. Nataka kufahamu hili tatizo la umeme Geita linakwisha lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hivyo, kuna maeneo tumepeleka umeme wa REA baada ya umeme wa REA kufika kazi imeisha, jirani akiomba umeme TANESCO hakuna vifaa. Ina maana REA peke yake ndiyo sasa inafanya kazi ya kusambaza umeme, TANESCO wenyewe hawana uwezo? Naomba sana eneo hili lifanyiwe kazi vizuri kwa sababu linakatisha tamaa, kama umeme umefika kijijini, kuna watu wanne wamepewa umeme, jirani hapewi umeme kwa sababu TANESCO hana vifaa, nadhani hapa kuna mipango mibovu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la fao la kujitoa. Mimi natoka Geita na naomba Waheshimiwa Wabunge wote wanisikilize vizuri sana. Geita pale karibu nusu ya watu wanaofanya kazi pale Geita Mjini ni watumishi wa mgodi. Kinachotokea kwenye mgodi pale ni kwamba
hakuna mwenye ajira ya kudumu. Kuna watu pale wanafanya kazi kwa mikataba ya miezi sita, miaka miwili, miaka mitatu. Anapofukuzwa kazi hawezi kupata kazi ya aina ile tena katika nchi hii, kuna wengi ni vibarua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa watu wanafukuzwa kazi, kwa sababu kandarasi iliyokuwa imempa kazi mkataba wake umekwisha, imeondoka imekwenda South Africa. Akienda kufuata pesa zake NSSF anaambiwa hizo pesa hawezi kupewa mpaka afike umri uliolezwa. Mtu leo ana
miaka 25 au 30 asubiri pesa hizi mpaka afikishe miaka 55 ndiyo aweze kulipwa na hana kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana kuna Mheshimiwa Mbunge mmoja ametoa hoja kwamba wapewe asilimia 25, hapana. Ziko kada ambazo wanaweza wakasubiri, ukimwambia mwalimu, polisi, daktari asubiri sawa. Pale mgodini kuna tabia supervisor akikuchukia anaku-blacklist,
akiku-blacklist huwezi kuajiriwa mgodi wowote duniani. Sasa unakaa unasubiri hiyo pesa mpaka utakapofikisha miaka 60 unaendelea kuwa maskini kwa misingi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kushauri, sekta ya madini iangaliwe kwa jicho tofauti. Kuna watu pale wanaacha kazi kwa sababu ni wagonjwa. Mgodi ule hauchukui watu wagonjwa, ukitibiwa mara mbili unaumwa kifua wanakufukuza, Mheshimiwa Jenista unafahamu nilikuletea watu wanaumwa, walipokuwa vilema walifukuzwa kwenye kazi, wana miaka 25, 30 halafu wananyimwa zile pesa wanaambiwa wasubiri mpaka watakapozeeka, anazeeka hizo pesa aje atumie nani? Ushauri wangu ni kwamba sekta ya madini ichukuliwe kwa namna tofauti, hatuwezi kuwa na jibu moja kwenye maswali yote magumu, lazima tuliangalie hili suala tofauti. Kama tuna nia ya kuwekeza NSSF wana mitaji mikubwa waangalie sehemu nyingine, lakini haya maisha ya watu kwa pale Geita tutawafanya kuwa maskini zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna gereza pale Geita Mjini, uwezo wake ni kuchukua watu 100 na zaidi, hivi sasa lina watu 800, sababu kubwa ni wachimbaji wadogo wadogo ambao wanatafuta pesa ndogo ndogo ya kula, akikamatwa anarundikwa pale. Kuna tatizo sasa hivi kwenye Jeshi la Polisi na watu wa Idara ya Sheria, kesi ya madai inageuzwa inakuwa jinai wanarundikwa mle, matokeo yake watu wanalala wamesimama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu Mheshimiwa Waziri Mkuu na nafikiri nilizungumza na wewe, pale kuna tatizo tuna OC-CID hafanyi kazi yake vizuri, kazi yake ni kukusanya pesa, anachokifanya yeye ni kuhakikisha kwamba kila anayetuhumiwa pale, iwe ni jinai, iwe ni civil lazima
abambikwe kesi ambayo itamuweka magereza zaidi ya miezi mitatu, gereza limejaa. Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe alikuja aliona, Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ulikuja uliona, tunaomba mtusaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna hizi kesi ndogo ndogo za kupita tu mgodini anakamatwa mtu anawekwa ndani miezi sita. Unapita tu na baiskeli unakamatwa unawekwa ndani miezi sita. Serikali ina pesa za kuchezea, kwa nini hizi pesa ambazo zinakwenda kulisha watu humo
wasipewe hawa wanasheria wakapeleka hizi kesi haraka? Mimi nadhani kuna haja ya kuisaidia Wilaya ya Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine ni uwepo wa migodi mingi sana kwenye Mkoa wa Geita na tatizo la huduma za afya. Wilaya ya Geita peke yake ina watu 800,000 kwa sensa ya mwaka 2012, lakini hospitali yetu iliyokuwa ya Wilaya tuliigeuza kuwa ya Mkoa, matokeo yake hatuna tena Hospitali ya Wilaya. Sasa ufikirie population ya watu 800,000 wa Wilaya moja na ile hospitali imegeuka kuwa ya mkoa, watu milioni mbili matokeo yake ile hospitali imezidiwa kabisa uwezo. Tuna vituo viwili vya afya tumeanza kuvitengeneza, tunaomba support yako Mheshimiwa Waziri wa Afya, tunakushukuru ulitupa gari lakini hatuna madaktari. Daktari aliyepo pale kuna specialist mmoja ambaye ni surgeon waliobaki wote ni AMO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishukuru sana Serikali, tulitaka kuleta muswada hapa wa kuwaondoa Madaktari Wasaidizi kwenye mfumo wa madaktari, lilikuwa ni kosa kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kule vijijini madaktari wetu ni ma-AMO na ndiyo wanaofanya kazi usiku na mchana. Ukiwaondoa wale kwenye mfumo wa madaktari waliobaki wengine wote ni mabosi wakienda kwenye wilaya kazi yao ni research, hawakai kwenye ofisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi namuomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu mtusaidie sana Hosptali yetu ya Mkoa wa Geita ianze ili Hospitali ya Wilaya irudishwe Wilayani ili gharama za matibabu ziweze kupungua. Hivi sasa navyozungumza na wewe gharama za matibabu ziko juu sana kwa sababu tunalipa… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ni desturi wawekezaji wa madini kupewa Mining License katika maeneo ya hifadhi ya misitu. Katika maeneo mengi wanayopewa hufyeka miti ovyo na kuchimba humo na kuharibu kabisa mazingira ya asili ya eneo hilo. Mfano katika Mkoa wa Geita maeneo ambayo yalikuwa na misitu mikubwa yote yamefyekwa na sasa ni jangwa. Aidha, sheria inawataka kufanya recovery (reforestation) baada ya kumaliza kazi (exit plan).
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba katika kipindi ambacho mgodi unaendelea kuleta madhara ya uharibifu huwapata wenyeji. Hivyo, madhara hayo huwezi kuyafidia baada ya mika 20 kwa kupanda miti. Maoni yangu ni kuwa:-
(i) Serikali ianzishe Sheria mpya ambapo mmiliki wa mgodi awajibike kutunza Maliasili zote katika eneo lake la license tangu siku ya kwanza ya kutoka, kwani kwa utaratibu hivi sasa mwenye license huangalia madini pekee (ardhini) na kutowajibika na uharibifu unaofanywa na wananchi katika eneo lake, isipokuwa kama watagusa madini. Mfano mzuri Geita Mjini msitu wote katika eneo la GGM umekwisha.
(ii) Serikali ianzishe mfumo maalum (Nature Resources Extract Fund) kama ulivyo Norway, USA na nchi za Kiarabu, maalum kwa ajili ya kuja kushughulika na rehabilitation kwenye maeneo yote yanayoathirika na miradi ya wawekezaji ambayo huvuruga kabisa mfumo wa maisha ya watu na wanyama wa eneo husika. Hivyo mfuko huo utasaidia kutoa elimu, majanga ya asili na kurudisha maisha yanayohusika kama kawaida baada ya miradi kukoma.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. KANYASU J. CONSTATINE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kunipatia Ambulance na pia mgawo na Madaktari wanne ambao tayari wamefika Geita. Kwa bahati mbaya mmoja bado yupo masomoni China mwaka mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba yafuatayo:-

(i) Hospitali yetu ya Wilaya imekuwa ya Rufaa ya Mkoa, kwa sasa imezidiwa sana na wagonjwa, gharama za dawa na huduma ziko juu kwa level ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Naomba sana juhudi za kujenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mheshimiwa Waziri aipe kipaumbele ili kupunguza gharama kwa wananchi.

(ii) Bado tuna uhaba mkubwa sana wa Madaktari Bingwa, Madaktari wa kati na wahudumu wa Afya, kama Nurses na watu wa Maabara. Naomba sana mwaka huu wakati wa mgao wa Watumishi wa Afya, Wizara isaidie kuitazama Hospitali ya Geita kwa jicho la huruma. Pamoja na suala hili kuwa la TAMISEMI bado Wizara ndiyo yenye jukumu.

(iii) Bado hospitali ya Rufaa ya Geita tunahitaji Duka la Dawa la MSD. Kosa kubwa limefanyika Geita ni kupeleka Duka la MSD Hospitali ya Wilaya Chato ambapo hakuna wagonjwa wengi, matokeo yake mahitaji ya msingi yamesahaulika au kupuuzwa. Ombi langu, Duka hili la Makao Makuu ya Mkoa lifunguliwe.

(iv) Ufanisi duni wa MSD, Halmashauri zetu zimekosa dawa muhimu kwenye bohari ya dawa, mafunzo yake, pesa hiyo inatumika kununua vifaa ambavyo siyo vya lazima na kuacha uhaba wa dawa ukiwa pale pale, matokeo yake MSD wanatoa O/S release kwenda kwa Private Vendor’s ambao huuza dawa na vifaa tiba kwa gharama kubwa, mara kumi zaidi ya bei ya soko ambalo watu wa kawaida wananunua. Hii maana yake ni kwamba pesa ya kutosha kutoa huduma mwezi mmoja kwa gharama za Private Vendor’s inatumika siku 10 tu.

Mheshimiwa Mwenyekti, naishauri Serikali kuhakikisha MSD wanazo dawa wakati wote kuepuka kupoteza fedha za umma.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami naomba nianze kwa kutoa pole sana kwa familia zote ambazo zimeguswa na msiba ambao umetokea mjini Arusha kwa kipekee kabisa. Kwa kweli msiba ule ni pigo kubwa kwa nchi yetu, na tunafahamu kwamba kuna tukio linaendelea pale Arusha tunawatakia kila la heri na kwa kweli tunawapa pole nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yupo rafiki yangu mmoja yuko Marekani jana alinipigia simu akaniuliza na nikashindwa kutoa jibu na nilikuwa nataka watu wa Kiswahili watusaidie kutafuta, inawezekana likawa ni neno jipya ambalo linaitwa “Bashite” kutafuta maana ya Kiswahili ili liwekwe kwenye Kamusi. Kwa sababu kuna wakati walioko nje wanashindwa kupata connection ya mazungumzo hayo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nianze kwanza kwa kutoa shukurani nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwanza kwa kuonesha kwamba anajali michezo, lakini pili kwa upendeleo kabisa wa kuleta uwanja mkubwa wa michezo hapa Dodoma. Mikoa mingi sana haina viwanja vizuri vya michezo na ni nafasi pekee hii katika Mkoa wa Dodoma kupata uwanja ambao unaweza ukawa ni uwanja wa pili wa Kimataifa baada ya uwanja wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, maoni yangu katika suala hili, naiomba Wizara ihakikishe kwamba uwanja huu unakuwa na vitu vingi vya lazima. Hapa tunapoongea Tanzania hata pamoja na mchango mkubwa wa wasanii wa muziki, wasanii wa ngumi na aina nyingine za michezo, tuna maeneo machache sana ya michezo ya aina hii ambayo yapo. Hatuna ukumbi wa kisasa wa muziki, hatuna ukumbi wa kisasa wa ngumi, tuna maeneo tu ambayo ni ma-hall ambayo ni ya kawaida hayawezi kuhamasisha michezo hii ya Kimataifa. Kwa hiyo kuja kwa uwanja huu niombe wale ambao wanasaidia kwenye mipango wahakikishe kwamba uwanja huu unakuwa na complex ili uweze ku-accommodate michezo mingi na ya aina mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapongeze sana wanamichezo wetu wengi, nianze na under 17 ambao kipekee sasa wanaelekea Gabon kwa ajili ya michezo hiyo ya Afrika; niwatakie sana mafanikio mema.

Vilevile niwapongeze sana wachezaji wetu wa Kimataifa walioko nje ambao wanacheza mpira wa kulipwa kama Samatta, Ulimwengu na wengine, niwapongeze sana Mwanariadha Simbu, Cecilia, Ginoka, Magdalena, Emmanuel, hawa wameendelea kuiuza Tanzania kwenye ramani ya Kimataifa. Wasiwasi wangu ni mmoja tu; ni mchango wa Serikali katika kuhakikisha kwamba mafanikio haya yanaendelea kuwepo.

Mheshimiwa Spika, ni bahati kubwa leo tunao akina Samatta, tunao hawa wanariadha wengine na kwa kweli kimsingi nchi hii kwa ukubwa wake na idadi yake ya watu, tungeterajia iwe na watu kama hawa zaidi ya 100.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kwa sasa kinachoendelea ni kwamba anajitokeza mmoja na yeye anakuwa kama wa dawa. Hii maana yake ni kwamba maandalizi ya kuwapata ha watu huku chini yamekuwa ni madogo na matokeo yake kila anayechomoza anachomoka kwa bahati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwenye eneo hili, miaka ya nyuma tulipata wanamichezo wengi sana walitokea kwenye Majeshi hasa JKT, Polisi na JWTZ. Nadhani sasa Serikali inapoelekeza kwenye kuchagua vijana hawa kutoka kwenye maeneo mbalimbali kwenye Wilaya iweke kipaumbele sana katika suala la michezo ili kuwapata vijana hawa wanaopelekwa kwenye maeneo haya waweze kuandaliwa vizuri waweze kuiwakilisha nchi yetu. Ni kwa sababu tu kwamba zamani pia tulikuwa na mashirika ya umma ambayo yalikuwa yanaweza kuwa na timu hizi za michezo. Baada ya mabadiliko ya sera, mashirika haya yakabadilisha mfumo matokeo yake ni kwamba hayana tena nafasi ya kuandaa wanamichezo wengi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nadhani kwamba vyombo hivi vya dola ambayo kimsingi bado vina uwezo mkubwa wa kuwa na bajeti ya kutosha lakini na nafasi ya kuwaandaa vingeendelea.

Mheshimiwa Spika, nimeisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri na kwa kweli niseme ni hotuba nzuri sana, nampongeza yeye pamoja na Naibu wake na Katibu wake Mkuu ambaye ni Mwalimu wangu, lakini napenda kusema upungufu kidogo ambao nimeuona hapa. Kwanza nilitarajia katika taarifa hii nione kwa kina inazungumzia uongozi mbovu na migogoro mingi iliyopo TFF. Kwa sababu ni kupitia mpira nchi yetu inaweza ikatengeneza wanamichezo wengine wapya kama Samatta.

Mheshimiwa Spika, juzi hapa kabla timu ya Taifa ya Vijana haijaondoka, tulishuhudia vijana wale wanateremshwa kwenye basi kwa deni kubwa la kodi ambalo wanadaiwa TFF pamoja na TRA. Nikatarajia kuona ni namna gani sasa Wizara inaondoa aibu hii.

Mheshimiwa Spika, tuliona mwaka 2016 vyombo hivi vya mpira kama FIFA, CAF na TFF vilikuwa haviingiliwi na chombo chochote cha uchunguzi cha Serikali, lakini mwaka 2016 FIFA, FBI waliingia ndani, miaka kama kumi huko nyuma chombo cha Italia cha Usalama kiliingia ndani kuchunguza.

Mheshimiwa Spika, nataka kufahamu sasa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, wakati nachangia katika ripoti yangu mwaka 2016 na hasa nilipogusia suala la rushwa katika Chama cha Mpira cha Tanzania, nilimtaka Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge na awaeleze Watanzania ni chombo gani independent ambacho kilifanya uchunguzi kama ilivyo FIFA, kama ilivyokuwa Italia na kama ilivyokuwa kwenye CAF hapa juzi, Rais mpya wa CAF alipochunguzwa kwa tuhuma za rushwa ambacho kiliihakikishia TFF kwamba sasa ilikuwa na uhalali wa kufanya maamuzi ya kuzishusha timu tatu za Majeshi ya Polisi na JWTZ, lakini pia na timu moja ya Geita Gold Sport ambayo ilishushwa daraja na kupandishwa timu nyingine kutoka nafasi ya tano kwa sababu za kuhisia.

Mheshimiwa Spika, mpaka leo tunazungumza na nimetazama sijawahi kupata hiyo taarifa, pamoja na uchunguzi huo mkubwa uliofanywa na PCCB.

Mheshimiwa Spika, niliahidiwa hapa na Mheshimiwa Waziri, kwamba baada ya uchunguzi huo wahusika watapelekwa mahakamani na hatua zitachukuliwa.

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe angalizo hapa kwa Serikali, mahakamani mara nyingi tunashindanisha maneno na inawezekana kabisa kwamba mwenye haki akakosa haki mahakamani kwa sababu ameshindwa kujenga kesi. Hii maana yake ni kwamba pamoja na uchunguzi mzuri wa PCCB na ushahidi wote waliopewa na wahusika kwamba palikuwa na harufu ya rushwa kubwa TFF, mpaka leo inavyoonekana wale watu ambao walituhumiwa na ushahidi wote wanaelekea kuokoka.

Mheshimiwa Spika, nataka tu nipate ushauri wa Mheshimiwa Waziri, ni kwa namna gani, ameitaja TFF, amezungumzia namna ambavyo anafikiria itaweza kusimamia michezo, lakini hajasema ni kwa namna gani anafikiria kuimarisha utawala bora kwenye TFF? Tunafahamu kwamba kwa mujibu wa sera, hizi ni taasisi ambazo zinajiendesha zenyewe, lakini kimsingi kama kuna rushwa, kama maamuzi yanayofanyika pale siyo ya haki, inakatisha tamaa wadau wa michezo.

Mheshimiwa Spika, hivi ninavyozungumza, leo ni mwaka mmoja na nusu tangu Geita Gold Sport walipoomba review ya kesi yao baada ya kukata rufaa, TFF hawajawahi kutoa maamuzi wala hawajawahi kusema rushwa alitoa nani? Alipewa nani? Shilingi ngapi? Wameishia kwenda kumfungia mchezaji miaka kumi, wamemfungia kocha miaka kumi ambaye haijulikani pesa alitoa wapi, kwa sababu viongozi wake wote wanaonekana hawana hatia.

Mheshimiwa Spika, nilitaka pia Mheshimiwa Waziri aje atuambie hapa, inapotokea suala kama hili, ni nini hasa nafasi ya Serikali? Kwa sababu tukiruhusu hali hii kuendelea tutafika mahali tutajikuta kwamba michezo ambayo inasemekana ni ajira haiwezi kuwa ajira tena. Wapo Watanzania wengi ambao sasa hivi wanafikiria wafike level ya Samatta, lakini kwa kukatishwa tamaa na matukio yanayoendelea katika TFF unaweza ukajikuta kwamba baadaye watu wote wanaona ni bora waachane na michezo wafanye kitu kingine.

Mheshimiwa Spika, nimelisema hili kwa muda mwingi kwa sababu ni suala ambalo linaigusa timu ya Geita Gold Sport ambayo ni timu inatoka Geita, ambapo wananchi wa Geita waliipandisha kwa gharama kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nilikuwa nataka kusema, pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Rais kuhusu kiwanja cha michezo, tumeona kwenye bajeti hii, lakini pia bajeti ya TAMISEMI, ni sehemu ndogo sana ya pesa ambayo inaelekezwa kwenye kuimarisha michezo. Kule kwetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na kwa sababu ya muda naomba nizungumze mambo machache tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba Geita Mjini tulipopata bahati ya kuwa Makao Makuu ya Mkoa wa Geita karibu nusu ya eneo la upande wa Mashariki miaka ya 1954 lilikuwa declared kwamba ni hifadhi, hakuna msitu wowote kuna bushes. Nilimwandikia barua na kumuomba kwamba wananchi wa Geita ule mkoa hauwezi kutanuka kuelekea Kaskazini wala kuelekea Magharibi kwa sababu ni eneo ambalo limepewa mgodi, eneo pekee la kutanuka ni kuelekea Kusini, na Mkoa kupitia RCC wameomba katika vikao tangu mwaka 2012 kuomba eneo la Msitu wa Usindakwe na eneo ambalo lilikuwa Msitu wa Geita (Usindakwe) liwe eneo ambalo Mkoa uruhusiwe kutoa maeneo ya makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza karibu nusu ya Mji wa Geita ni eneo ambalo zamani lilikuwa declared kwamba ni hifadhi, sasa nilikuomba Mheshimiwa Waziri kwa maandishi lakini sasa ni karibu miezi sita naomba leo uniambie ni hatua gani zimefikiwa? Sababu moja ni kwamba mpaka leo watu wa TFS wanazunguka, wanaweka alama kwenye nyumba, wana-disturb watu, lakini hakuna mti, hakuna chochote. Katika maeneo ya Nyakabale na Mgusu wananchi katikati ya kijiji kuna vigingi na katikati ya eneo la vijiji hivyo tayari mgodi umepewa eneo hilo, hivyo, wanashindwa kufanya chochote kwa sababu eneo hilo linaonekana kama ni hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni TFS katika Mkoa wa Geita, limetoka tangazo kupitia kwa Waziri kwamba ni marufuku kutumia pikipiki, baiskeli kubeba mkaa wala kubeba chochote. Vijiji vyetu vyote ambako wananchi wanakaa hakuna magari, hakuna chochote, kwa hiyo matokeo yake watu wa TFS wamerundika pikipiki na baiskeli Makao Makuu ya Ofisi zao na wanategemea kuzipiga mnada. Baiskeli ambayo imenunuliwa shilingi 150,000 inauzwa shilingi 10,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri jambo hili ni uonevu mkubwa kwa sababu wananchi katika maeneo hayo ya vijiji hawana usafiri mwingine wowote mbadala zaidi ya baiskeli. Sasa sheria inaposema kwamba ni lazima tutumie magari, kusafirisha mkaa, hivi wananchi kwenye vijiji wanapata wapi magari? Kwa sababu inavyonekana ni kama mkakati wa kuwadhulumu wananchi baiskeli zao, ananunua mtu baiskeli, anakamatwa anakimbizwa porini ananyanganywa na sasa hivi watu wa TFS wanakwenda kwenye masoko kusubiria watu. (Makofi)
Mimi nafikiri TFS wamesahau core function yao. Core function yao ni kulinda misitu, wanachokifanya sasa siyo kulinda misitu tena, ni kusubiri barabarani waendasha baiskeli na pikipiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuambie na tangaza leo hawa wananchi wanatumia nishati gani? Tuambie tu mimi niko tayari kuwaambia wananchi sasa acheni, ni nishati gani mbadala ambayo Wizara yako imeandaa kwamba sasa hii ndiyo itakuwa nishati mbadala? Kinachoendelea sasa hivi na kwa wananchi ni kwamba wananchi wanalazimishwa sasa waanze kulala njaa kwa sababu mkaa unakamatwa sokoni, unakamatwa barabarani, anakamatwa mwenye baiskeli, pikipiki, gari haijulikani utaratibu huu sasa unatupeleka wapi.

Mheshimiwa Waziri inawezekana wewe huna taarifa, nguvu inayotumika kwenye suala hili kule kwenye maeneo ya wananchi ni kubwa kuliko hata thamani ya kitu kinachoenda kuzuiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nikushauri Mheshimiwa Waziri, kwa nini unapata tatizo kubwa sana la kulinda misitu yako, unapata shida ya kulinda hifadhi? Kwa sababu ya mahusiano mabaya sana ya TFS na vijiji. Watu wa samaki walibuni kitu kinaitwa Beach Management Unit (BMU) kwa sababu wananchi wanatakiwa wajisimamie wenyewe. Ninyi mnatumia nguvu kubwa, amesema Mheshimiwa Mbunge asubuhi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii kuweza kuchangia na kwa niaba ya wapiga kura wangu wa Geita Mjini, naomba nitumie nafasi hii pia kuwataarifu kwamba lile tatizo lao la watu wa TFS kuweka alama kwenye nyumba ambazo zipo katikati ya Mji wa Geita wakidai ni hifadhi, nilishamjulisha Waziri wa Maliasili na kwamba tunachosubiri ni maombi ya RCC ili waweze kufikia maamuzi ya kuliachia eneo hilo. Maamuzi hayo yanachelewa sana na wananchi wanaendelea kusumbuliwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wananchi wa Geita wanaomba kuona unachukua hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema Mbunge, Mheshimiwa Doto Biteko, nimesomeshwa na pamba, lakini pia nimesomeshwa na uvuvi. Nimesomeshwa na uvuvi, natoka kilometa mbili kutoka Ziwani ndiko nilipozaliwa; na eneo letu tulilokuwa sisi tulikuwa na mashamba makubwa sana ya Nyanza wakati ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pamoja na pongezi nyingi sana ambazo nampatia Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwenye Wizara hii, hasa kwa kuondoa kero nyingi kwenye zao la pamba. Pia ninaomba kumkumbusha Mheshimiwa Waziri ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba Nyanza Cooperative Union, mali zake ambazo zilihujumiwa kinyemela, zinarudi na hatimaye Nyanza iweze kusimama imara. (Mkofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo cha mkataba inaoneka sasa hivi ni suala geni lakini sisi wakati tunakua wakati ule, pamba ndiyo lilikuwa zao la kujivunia kwenye Kanda ya Ziwa na umaskini wa wananchi wa Mkoa wa Geita na Mikoa ya Kanda ya Ziwa inaonekana kudorora kwa zao la pamba. Wakati huo mashamba yote ya pamba makubwa na mazuri uliyokuwa unayaona, wananchi walikuwa wanalima yalikuwa aidha ni ya Nyanza au ni ya watu walikuwa wanakopa pembejeo. Mfumo wa kukopa pembejeo ulikuwepo tangu zamani wala siyo mgeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wananchi walikuwa wanapewa mbegu bora, walikuwa wanapewa madawa na baadaye vyama vya ushirika kwa sababu vilikuwa vina nguvu, vilikuwa vinaweza kununua yale mazao kwa wakati na kuwalipa kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri kuona namna ya kuimarisha vyama vya ushirika kwa sababu ndiyo reliable vinaweza kuwakopesha wakulima. Kama hilo haliwezekani, ni kuona namna ya kuwafanya hawa private buyers ambao mnawapa usajili waweze kuwa engaged namna ya kuwasaidia wakulima. Bila kutatua tatizo la kuwapatia pembejeo na mbegu bora wakulima, hatuwezi kulifanya zao la pamba likarudi kwenye nafasi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namna ambayo naiona hapa, kwanza wakulima sasa hivi wamekata tamaa kwa sababu ukiacha wastani wa heka moja kuzalisha tani mbili na kilo 200 wengi wanazalisha kilo 100 au kilo 200. Sasa kilo 200 hata kama ungempa kilo moja Sh.2,000/= bado hawezi kulipa gharama za kilimo, productivity imeshuka sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, huyu mkulima kama ataweza kuzalisha tani moja kwenye heka, hata ukimpa kilo Sh.1,000/= utakuwa umemsaidia. Tatizo kubwa liko wapi? Tunao Maafisa Ugani wengi sana kwenye Halmashauri za Wilaya, lakini nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri hawa watu hawapewi target. Ameajiriwa, amepewa ofisi, amepewa Kata, hakuna mtu anayemsimamia. Nataka nimshauri Mheshimiwa Waziri, hebu aweke utaratibu wa kuhakikisha kwamba hawa watu wanakaguliwa, wanapimwa kwa kitu fulani ambacho wamekifanya kwa mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watu wanaamka asubuhi, anakwenda anasaini, anarudi, analala, hata katika kijiji ambacho anakaa wakulima hawafahamu. Hata katika kijiji ambacho wanakaa hajawahi kutoa utaalam wa aina yoyote. Kwa hiyo, matokeo yake wakulima wameligeuza zao la pamba kuwa zao la pili na wengi wamehama. Wengi wanakwenda kwenye mazao mengine kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano Geita watu wengi wanalima mpunga; na mpunga kwa sababu pia hata utaalam wa watu wengi wanalima kutokana na ulimaji wa asili, wamehamia huko kwa sababu ni zao la chakula na zao la biashara. Kwa hiyo, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri Maafisa Kilimo, hata angeajiri wengi namna gani, kama waliopo hawasimamiwi, bado zao la pamba litaendelea kuwa chini kwa sababu hakuna uzalishaji ambao unaendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema kwamba nilisomeshwa na samaki. Naomba hapa Mheshimiwa Waziri anisikilize vizuri. Ipo sheria ambayo ilitungwa mwaka 2003 na kanuni yake ya mwaka 2009. Sheria ambayo inasema “it is illegal to manufacture, possess, store, sell and use or cause another person to use for a fishing gear of more than 26 mesh deep in the Lake Victoria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa lugha ya kawaida wanasema ni makosa kuzalisha au kukutwa una nyavu ambayo ina macho 26. Sasa macho 26 nikifanya mikono yangu miwili hapa, tayari ni macho 26 ya mtego.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anatoka kisiwani, tumevua wote samaki. Naomba nimkumbushe, ukitoka Mwanza South pale ukaenda Nautical Mile 15, chini ni mita 70, hebu aende na hiyo nyavu ya macho 26 akavue samaki kama atapata kilo tano. Kinachofanyika sasa, imetungwa sheria, hiyo sheria imeipitishwa lakini inahamasisha watu waende kuvua samaki kwenye breeding areas. Wanakwenda kwenye zile breeding areas ambazo tungetarajia ziwe hifadhi, samaki wazaliane kwa sababu nyavu wanayopendekeza ambayo wanaiita illegal, ni nyavu fupi. Ni mikono yangu miwili hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Gozba ni mita 100 chini. Nataka nimpe challenge Mheshimiwa Waziri, nimefanya kazi ya samaki miaka 25. Kama ana wataalam wake wa uvuvi awaambie waweke nyavu 100 twende Gozba, wakirudi na kilo kumi naacha Ubunge. Naacha Ubunge kwa sababu wanachokifanya ni kuwaonea kabisa wavuvi. Wanaenda wanachukua zile nyavu, wanaita illegal wanazichoma moto.

Mheshimiwa Naibu Spika, mvuvi gani anatengeneza nyavu? Nyavu zimepita bandarini, zimelipiwa ushuru, mvuvi amekopa pesa benki, amekwenda kuweka kwenye mtumbwi, size ya nyavu anayotaka ni ile ile nchi tano au sita ambazo wameruhusu; lakini wanasema ikishazidi macho 26 ni illegal. Sasa wakati inapita bandarini watu wake walikuwa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hilo tu. Yeye kama ni mvuvi na anafahamu mambo ya uvuvi twende ziwani. Wavuvi wetu wengi ni local, wanafanya traditional fishing, hakuna mwenye fish finder; hakuna mwenye chochote. Kwa hiyo, hakuna anayeona samaki chini. Tuchukue hizo nyavu tuende nautical mile 50 tukatege, halafu turudi kesho tukavue; tukipata samaki kilo 50, mimi naacha Ubunge. Kwa sababu nimefanya kazi hii kwa miaka 20 na nimekimbia huko kwa sababu ya masharti mengi yasiyo na maana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachomaliza samaki Ziwa Victoria ni matumizi ya monofilament na matumizi ya makokoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, Mheshimiwa Waziri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua kuna maeneo ya wananchi katika Wilaya ya Ilemela ambayo Jeshi liliyapima ili kuyachukua kwa miaka mingi bila kulipa fidia na kuwaondoa wananchi katika maeneo hayo, Mheshimiwa Waziri naomba kufahamu uthamini uliofanyika maeneo ya Nyagunguku - Ilemela, Nyanguku, Lukobe kwa miaka miwili sasa umefutwa au bado upo valid?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama lengo la JWTZ lilikuwa kufanya uthamini na baadaye kuwaacha wananchi katika maeneo yao kwa muda mrefu bila kujua hatima yao, naomba kujua watalipwa lini au Jeshi limejiondoa kwenye nia ya kumiliki maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatana na timu za Orjoro JKT na Kanembwa JKT kushushwa daraja kwa tuhuma za rushwa ambazo zimeshindwa kuthibitishwa na chombo cha kisheria cha uchunguzi wa makosa hayo (PCCB). Je, ni hatua gani Wizara yako imechukua kupigania haki ya vijana wako na heshima ya vyombo hivyo nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kudorora sana kwa michezo ya aina mbalimbali, mfano, riadha, sarakasi, ngumi, mitupo, volleyball, nimetaja kwa uchache tu kwa nini kuanzia sasa kipaumbele cha kijana kujiunga na JWTZ na JKT au vyombo vingine isiwe ni kipaji kimojawapo cha michezo ili kuufanya umma wa Watanzania kupenda michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili vijana hao wawe competent ni vizuri Wizara yako ikatafuta wabia (marafiki) kutoka nje ya nchi kusaidia kuongeza taaluma, mfano, China, Cuba, Urusi na Korea, ambapo vijana wetu waweze kupata ujuzi mpya au nyongeza ya ujuzi walionao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Wizara yako ina mpango mkakati upi wa kusaidia kuimarisha michezo nchini?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kushauri yafuatayo; Serikali iongeze bajeti kwenye fungu la maendeleo na pesa hii ipo kwenye mafuta, umeme na maji yenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mingi ya umwagiliaji inakumbana na pingamizi kwa kuwa ujenzi wa miundombinu umejielekeza kujenga mabwawa kukinga maji. Hapa wananchi wanaogopa kupoteza ardhi zao, kwa nini tusitumie mfumo wa visima virefu na wind wheels kuweka maji kwenye matanki na kusambaza kwa gravity kwa kuwa gharama ni nafuu na eneo linalopotea ni dogo. Mradi kama huu upo kata ya Kanyalla Ibada na umepingwa na wananchi kwa sababu hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu tatizo la maji Mjini Geita, hivi sasa Mradi wa Maji wa LV-Watsan unasuasua sana mpaka leo miezi minne imepita, mkandarasi ameshindwa kumaliza kazi, nashauri mtu huyu afutwe kwenye orodha ya wakandarasi kwa kuwa hana uwezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uhaba wa maji katika Mji wa Kasamwe, naishauri Serikali kuunganisha mradi mpya wa maji wa fedha za India kwa Mji wa Geita ili maji yake yafike Kasamwa, kwa sababu kwa mujibu wa wataalamu hivi sasa kuna tanki kubwa la maji Buhalanda ambalo lipo kilometa 10 tu kutoka Kasamwa na ambapo maji yatafika kwa gravity na kwa kuanzia ziwekwe DP’s tu kwenye mitaa ili wananchi wapate maji, badala ya sasa kutumia bwawa ambalo gharama yake ni kubwa

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kunipa majibu maji katika Kata za Shiloleli, Bulela, Ihanamilo, Nyanguku, Mgusu na Bung’wangoko yatafika kupitia mradi huu wa fedha za India? Kwa sababu hizi kata ni sehemu ya kata za Mji wa Geita Jimbo la Geita.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
The Finance Bill, 2016
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami naunga mkono sehemu kubwa ya mapendekezo ya sheria hii lakini naomba tu nitoe ushauri kwenye maeneo machache.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza nilitaka Mheshimiwa Waziri wa Fedha akija atuambie, benki na taasisi nyingi zina riba kubwa sana ya mikopo, ni kodi kiasi gani ambayo Serikali inaweza kukusanya kutoka kwenye riba kubwa hizi ambazo wanatozwa wananchi na zina mchango gani? Kwa sababu naona kama hawa watu wanatengeneza faida kubwa na hatupati mapato yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwenye Muswada huu wa Sheria kifungu cha 65E mpaka 65N, yapo mapendekezo kwamba hesabu za mtu anayetafiti na ambaye yupo kwenye full operations zinabebana, anapoanza operations akija kwenye uchimbaji gharama zile zinachukuliwa zinahamishiwa huku, matokeo yake huyu mtu halipi kodi. Hapa nina mfano mzuri na kama tukiruhusu suala hili makampuni yataendelea kutokulipa kodi katika nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano nilikuwa Ngara kule kuna kampuni moja inaitwa Kabanga Nickle, kwa miaka 45 wao wanafanya utafiti na kila mwaka kuna watu pale wako kwenye operations, matokeo yake hizi gharama zote siku moja akija mwekezaji zitaingizwa kwenye kampuni itakayokuja, hii kampuni haitalipa kodi milele. Kwa hiyo, nashauri gharama za utafutaji ziwe tofauti na gharama halisi wakati huu mgodi unaanza operations kwa ajili ya kulinda maslahi mapana ya nchi. Tunao watu katika maeneo kama Geita pale, wameshikilia maeneo wana miaka 20, hawachimbi, hawafanyi chochote kila mwaka wana-renew licence. Matokeo yake gharama hizi za kusimamia maeneo haya watakuja kuiwekea Serikali halafu hawatalipa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ambalo nataka kusema ni kwamba halmashauri zetu zina migogoro mingi sana kwa sababu ya wafugaji na maeneo mengi ambayo yalikuwa yanafaa kwa ajili ya kilimo ili halmashauri zikusanye kodi yanatumika kwa ajili ya mifugo lakini mifugo hii ilisamehewa kodi. Naomba kuishauri Serikali iziruhusu halmashauri zitoze kodi kwenye mifugo ili mifugo hii iwe na faida kwa halmashauri. Tunaendelea kuiona mifugo haina thamani, haina maana yoyote kwa sababu tuliisamehe kodi sisi wenyewe. Mtu ana ng‟ombe 5,000 anaonekana ni masikini lakini mtu mwenye nyumba moja anakwenda kulipa kodi. Kwa hiyo, mimi sioni kama hapa kuna proportionality. Naomba sana Serikali ifanye mabadiliko kwenye hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, napendekeza kwamba tumesamehe kodi kwenye taasisi za umma hasa hospitali na Mashirika ya Dini, tukasahau kidogo kwamba Waraka wa Elimu wa mwaka 1978 unasema elimu ni huduma. Nataka kushauri Serikali kwenye property tax hapa kwamba shule zingewekewa badala ya kuacha hiki kiwango kikawa kinayumbayumba, kuwaachia TRA na Halmashauri waamue wenyewe, tutafute flat rate kwa ajili ya shule kwa sababu hivi vyombo ambavyo vinatoa huduma, ni taasisi za huduma ili tuepuke watoto na wazazi kuja kulipia gharama hizi kwenye Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na nakushukuru sana.
The Written Laws (Miscellaneous Amendment) (No.2) Bill, 2016
MHE. CONSTATINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kufika siku ya leo, pia niwape pole wananchi wa Wilaya ya Biharamulo ambao Mheshimiwa Mbunge wao wa Bunge lililopita Mheshimiwa Anthony Mbassa jana tulipata taarifa kwamba amefariki na niwatakie moyo wa subira kwa familia, ni majirani zetu Geita kwa hiyo tunafahamiana vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa mabadiliko makubwa aliyoyafanya jana ya Wakuu wa Wilaya na kwa kweli naomba nimpongeze kwa sababu ameendelea kuimarisha safu yake ya uongozi. Ninawapongeza walioteuliwa na niwatakie kila la kheri, pia niwapongeze ambao uteuzi wao umetenguliwa au hawakuteuliwa na niwatakie kila la kheri huko uraiani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka tu nitoe mapendekezo mawili kwenye sheria hii. Ukiangalia vizuri nia njema ya Mheshimiwa Rais ya kuwateua vijana kuwa Wakuu wa Wilaya ni kwa ajili ya kuwaingiza katika Mfumo wa Uongozi wa Nchi ni nia njema sana na wengine wanateuliwa wakitoka kazini. Nafahamu Serikali iliyopita wakati wa Mheshimiwa Jakaya Kikwete, wapo baadhi ya ma-DC wakiwa Maafisa Tarafa, Maafisa Mipango, wakiwa na miaka 20 mpaka 30, wamehudumia miaka mitano na uteuzi huu wameachwa, ukitazama vizuri sheria hii sasa hawa walipoteza ajira yao huko nyuma na sasa hivi siyo tena watumishi, unaona kabisa kwamba vijana hawa baada ya miaka miwili watakuwa ni watu ambao ni mzigo kwa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kusema sheria ukishateuliwa kuwa DC ajira yako ya kwanza inapotea, akija Rais mwingine baada ya miaka 10 akikuacha na ajira yako bado una miaka 38 unapoteza kila kitu. Kwa hiyo, ni sheria ambayo ninaiona kama siyo nzuri. Kwa sababu wapo waliotoka kwenye Utumishi wa Umma sasa zaidi ya 20 ambao wanakwenda kuwa Wakuu Wilaya, baada ya miaka 10 ya Mheshimiwa Rais Magufuli, anaweza akuja Rais mwingine akasema nao hawahitaji, hawawezi kurudi Serikalini umri wao ni miaka 35, ninadhani Sheria hii siyo nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Rais, lakini niwatakie kila la kheri walioteuliwa na niwape pole vijana wenzangu ambao tulikuwa nao na wengi wako chini ya miaka 40 ambao wameachwa, wajipange upya huko uraiani. Nakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda sasa kwenye marekebisho ya sheria nianze na Sheria ya Elimu ambayo kwa kiasi kikubwa imependekeza adhabu kali ya miaka 30, kwa mtu atakayepatikana na hatia ya kumpa ujauzito mwanafunzi. Nazungumzia wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niipongeze Serikali sheria ni nzuri, ingawa kwa mtazamo wangu kuna mambo mengi ya kufanya. Mimi niko katika Kamati ya UKIMWI; tumeangalia kwenye taarifa tulizoletewa, tumeona watoto wanaanza kufanya mapenzi wengine wakiwa na miaka kumi na kuendelea. Maana yake ni kwamba waanza kufanya mapenzi na wanapata maambukizi ya UKIMWI chini ya miaka 15; na hawa ni wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari. Upo uwezekano huyu ambaye ameanza kufanya mapenzi katika umri mdogo anaporudi shuleni huyu binti wa miaka 12, miaka 13 akam-convince kijana awa kiume wa miaka 15, miaka 16 na matokeo yake huyu wa miaka 13 hadi miaka 14 akipata mimba unaweza kufikiri ni ya mwanafunzi kumbe amepata uraiani huko. Kwa sababu taarifa zinaonesha kwamba hawa wanapoanza kufanya mapenzi wanafanya na watu wazima wala hawafanyi na watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo maana yake ni nini? Sheria hii upo uwezekano wa kumfunga mtu miaka 30 mwisho ukagundua kwamba mimba hii haikuwa ya yule aliyefungwa na unagudua haikuwa ya yule aliyefungwa tayari mtu huyu alishatumikia kifungo cha miaka 30, unatoka jela mtoto siyo wa kwako, mtoto ni wa mtu mwingine kwa sababu watoto wetu siku hizi wanaanza kujifunza mambo haya wakiwa na umri mdogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri Serikali iende mbali zaidi kwa kuleta vipimo vya DNA ikiwezekana kwenye level ya kila Wilaya, kwa sababu kwenye ushauri uliotolewa juzi kila Kata haiwezekani, kwenye level ya kila Wilaya, au kwenye level ambayo itakuwa ni rahisi kugundua kwamba ujauzito huu siyo wa mwanafunzi. Ninazungumzia hapa kwa sababu vijana wetu hawa kwenye maeneo mengi ya shule anaweza akatafuta mnyonge wa kumkimbilia, akafuata mwanafunzi mwenzake, lakini kwa sababu mambo haya wanaanza mapema, inawezekana ujauzito huu ameupata uraiani huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimezungumza hii kwa mifano sahihi kabisa ambayo tumepata kutoka kwenye Kamati yetu na inaonesha kabisa wazi kwa mba vijana wetu wana wanaanza matendo haya mapema zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, tuangalie namna ya kutengeneza adhabu nyingine zaidi, unapomfunga mtu miaka 30 anakwenda jela, halafu baada ya mwaka mmoja anakuwa kama vile amezoea maisha ya jela, inakuwa tena siyo adhabu, ninafikiri pamoja na miaka 30, kila mwezi huyu mtu awe anapata viboko 12, kwa miaka yote 30 mpaka atakapotoka. Hii itamfanya mtu asizoee kile kifungo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekutana na watu wengi sana jela huko, akishafungwa miaka mitatu inakuwa kama vile ni nyumbani, ukienda mtaani unakutana nao, hata Askari Magereza hana tena muda wa kuwachunga wanawaacha tu wanatembea wenyewe kwa sababu walishazoea maisha ni mazuri, anakula vizuri, ameshakuwa mnyampara mle, anapata sabuni mafuta. Kwa hiyo, unamkuta mtu yule huku aliacha ameharibu mtoto wa mtu lakini kule anaendelea na maisha yake kama kawaida. Kwa hiyo, nafikiri kila mwezi akipata viboko 12 mpaka miaka yote 30 itakapoisha itatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine huyu binti ambaye sasa amekwishajifungua tunamfanyaje? Kwa vile atajifungua Baba amefungwa, atafukuzwa shule na hatasoma tena. Ushauri wangu ni kwamba baada ya kujifungua binti huyu, uangaliwe uwezekanano wa kubadilisha sheria ili aendelee na masomo, kwa sababu baadaye mtoto huyu atajikuta ana mama hakusoma, ana baba ambaye alifungwa akiwa mwanafunzi naye hakusoma tutakuwa tumetengeneza mtoto ambaye atakosa msaada kwa baba na atakosa msaada kwa mama.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia sheria itazame vizuri, kuna wakati mwingine unakuta kwenye darasa moja binti ni umri mkubwa kuliko kijana. Labda binti ana miaka 23 alichelewa kusoma. Kule usukumani watu wanaanza shule wakiwa na umri mkubwa, anaweza kuanza kusoma akiwa na miaka 15 ndiyo anakwenda darasa la kwanza, kwa hiyo anajikuta amefika sekondari ana miaka 24; halafu huyu binti anapewa mimba na kijana wa miaka 15; sasa hapa mwenye kosa ni nani, kwa sababu inaonekana kama vile binti atakuwa ndiye aliyemtongoza kijana, halafu unakwenda kumfunga huyu kijana ana miaka 15 unamwacha huyu binti wa miaka 24 uraiani, ni kama vile tunaleta uonezi hapa. Nafirikiri sheria itazame vizuri ili kuangalia namna ambavyo sheria hii inaweza kwenda ikafanya kazi sehemu zote mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono marekebisho ya sheria nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kifupi sana kwanza niseme naunga mkono muswada huu na labda tu nitoe mapendekezo yangu machache, nilikuwa nimetarajia ningeweza kuchangia kesho, lakini naweza kusema haya machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza naungana na ambao wangependa tutofautishe Ibara ya 18, kuna tatizo la tafsiri kwamba haki ya kupata taarifa na haki ya kupata habari, lakini haki ya kupata habari palepale inalazimishwa ionekane iko sawa na haki ya kupata taarifa. Katika mazingira ya kawaida, taarifa hii inaweza kutolewa katika muda wowote ule ili mradi mlengwa aliyekuwa anataka taarifa anatakiwa apate hii taarifa kadri alivyokuwa anaihitaji. Kwa hiyo, pamekuwa na tatizo la kuichanganya hii kuonekana kwamba mtu asipopata taarifa pale pale Katiba imekiukwa. Siyo kweli kwamba Katiba inakiukwa kwa mtu kutokupewa taarifa pale pale lakini inatakiwa mtu apewe taarifa sahihi wakati wowote baada ya tukio hilo kutokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la msingi katika hili ni kama walivyosema wenzangu, ni vizuri sana sheria yetu ikatofautisha ni maeneo gani tunaamanisha taarifa za siri. Zipo taarifa za intelijensia ambazo zikiachwa wazi zinahatarisha usalama wa nchi yetu, lakini ziko zingine ni taarifa ambazo zimekuwa tu zikibanwa na walengwa kwa nia ya kuficha baadhi ya siri kwenye taasisi na wengi wamezitumia hizi vibaya. Watu wengi wanasema kwamba kwenye Halmashauri zetu ni rahisi sana kupata taarifa, lakini mimi ambaye ninaamini nimekuwa kwenye Halmashauri kwa muda mrefu kuna wakati hata Mheshimiwa Mbunge kama taarifa unayotaka ina madhara kwa walengwa walioko kwenye Halmashauri ile unaweza ukasubiri taarifa ile kwa muda mrefu na usiipate.
Kwa hiyo, sheria hii ni ya muhimu, ni sheria ambayo kimsingi inawalazimisha wahusika kutoa taarifa sahihi hata kama taarifa ile haitatolewa pale pale lakini taarifa hii itatolewa kwa mtu ambaye anaihitaji na itakwenda kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la msingi hapa ningependa Mheshimiwa Waziri atakapokuja atusaidie tunatunga sheria hii kwa ajili ya Serikali peke yake au pia kwa ajili ya makampuni binafsi. Kwa mfano, kama ni Serikali peke yake ieleweke lakini tunayo makampuni ambayo yanatuzunguka kwenye maeneo yetu, makampuni yanayofanya biashara na makampuni yanayochimba madini ambayo ni wadau wakubwa wa Serikali. Kuna wakati makampuni haya yanaweza yakalipa service levy bila wadau kujua yanalipa kutokana na mauzo yapi, yanalipa kutokana na mapato gani na unapokwenda kufuata hizi taarifa inaonekana ni taarifa za siri za hizo kampuni.
Kwa hiyo, ni vizuri pia kueleweka kwamba sheria hii inakwenda kugusa kila eneo, kila idara, kila taasisi au ni sheria ambayo inalenga kugusa Serikali peke yake au ni sheria ambayo inalenga kugusa kila sehemu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona ndugu zetu wengi wana wasiwasi sana na baadhi ya matumizi ya sheria hii unapofanya makosa. Mimi sijawahi kuona mtu anaadhibiwa bila kufanya makosa na ametusaidia hapa Mheshimiwa Bashe kwamba wadau wa habari wameshirikishwa kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira ya kawaida tunaamini lengo la sheria ni kujenga nidhamu. Kama watu wanatumia vibaya haki yao ya msingi ya kutoa taarifa na kupotosha umma lazima watu waadhibiwe. Hili lisije likaonekana kama ni suala baya kwa sababu bila kufanya hivyo tutakuwa tunajenga nchi ya watu wanaofanya makusudi, wanaopotosha umma na matokeo yake mtu anapata sifa kwa sababu ya kuharibu sifa ya mtu mwingine. Tumeshuhudia huko nyuma mtu anasimama hapa anatengeneza uongo, huko nje wanamsifu, halafu kesho yake hana hata data moja inayoonyesha kwamba taarifa hiyo ni ya ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema Mheshimiwa mmoja hapa kwamba ni vizuri sana source ya information pia tujiridhishe nayo. Kwa mfano, kama mtu anayetoa taarifa hana uhakika na taarifa ile halafu aliyepewa taarifa ndiye anayekwenda kuadhibiwa nadhani sio sahihi. Ni vizuri sana yule anayetoa taarifa ajiridhishe na taarifa ile kabla ya kuitoa na iwapo taarifa hiyo itakuwa na mapungufu yule aliyepewa taarifa pia asije akaadhibiwa kwa makosa ya taarifa ambayo aliiipata kimakosa kutoka kwa mtu ambaye alikosea. Vinginevyo adhabu hizi ziwekwe kwa watu wote wawili au watu wote wawili wasamehe na adhabu ambayo itakuja kufuatia kwenye sheria yenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, naomba kuunga mkono hoja, nakushukuru sana.