Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kasuku Samson Bilago (32 total)

MHE. KASUKU S. BILAGO: Hii nafasi ni ya Mwalimu.
Mheshimiwa Spika, nina swali dogo kuhusiana na fedha hizi zinazotarajiwa kutolewa vijijini za Sh. 50,000,000 kwa kila kijiji. Sasa hivi imeanza mizengwe kwamba fedha hizi zitatolewa kwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi. Naomba Serikali itoe kauli fedha hizi zitatolewa kwa utaratibu gani ili kuepuka kwenda kwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi peke yao?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza niseme fedha hizi za Sh. 50,000,000 ilikuwa ni ahadi ya Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kupitia kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini Watanzania ambao walichagua Serikali ya Chama cha Mapinduzi na Serikali hii iliamua kuwatumikia Watanzania wote bila kujali itikadi ya vyama vyao wala jambo lingine lolote. Katika majibu yetu ya msingi tumesema Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Tanzania wameshaanza kutengeneza utaratibu wa namna ambavyo fedha hiyo ya Sh. 50,000,000 itaweza kuwafaidisha wananchi wetu kule vijijini wakiwemo vijana, wanawake lakini vilevile na Watanzania wengine wote. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mbunge jambo hilo analolisema ni hofu tu, lakini Serikali ipo imara na itazingatia utaratibu wa kisheria wa kuhakikisha fedha hizi zinawafikia Watanzania.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu yaliyotolewa na Wizara ambayo hayakidhi viwango.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wastaafu zaidi ya idadi iliyotolewa na hasa walimu, hata Jimboni kwangu Buyungu idadi kubwa ya walimu waliostaafu inaweza ikaakisi idadi ya watumishi walistaafu katika nchi hii. Sababu zilizotolewa za wastaafu hao kutolipwa moja kubwa ni kukosa fedha kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambayo Serikali haijataja.
Swali la kwanza, naomba Serikali ikiri ni lini italipa wastaafu wote kwa kupeleka fedha kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili wasiendelee kuteseka sambamba na kuwarudisha nyumbani kwao mara baada ya kustaafu? (Makofi)
Swali la pili, wapo wastaafu wa aina mbili, wapo wanaolipwa pensheni na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na wapo wanaolipwa pensheni na Hazina. Wale wa Mifuko wa Hifadhi ya Jamii wanapata monthly pension wale wahazina wanalipwa kwa miezi mitatu (quaterly pension) hali hii inawasumbua na kuwatesa wastaafu wetu. Naomba wastaafu wote walipwe monthly pension kama ilivyo kwenye mkataba wa kazi. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naomba uulize swali, naona unaleta ombi.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Swali la pili dogo, ni lini Serikali itaanza kuwalipa wastaafu wote pensheni ya kila mwezi badala ya miezi mitatu? Ahsante!
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumhakikishia data nilizompatia ni za kweli na za uhakika, kwa hiyo naomba aamini hao ndiyo wastaafu ambao tunajua wamestaafu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili sababu nilizozitaja ndizo zinazosababisha wastaafu hao wachelewe kulipwa siyo upelekaji wa fedha. Serikali imekuwa ikipeleka fedha kwenye Mifuko hii ili waweze kulipwa wastaafu hawa na hizi sababu nilizozileta ndizo ambazo tunazifahamu kama Serikali na Mifuko yote imeendelea kupokea fedha kutoka Serikalini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, wastaafu wanaolipwa Hazina kulipwa kwa miezi mitatu mitatu. Naomba nilieleze Bunge lako Tukufu kwamba uamuzi wa Serikali kuelekea kulipa miezi mitatu mitatu lilifikiwa baada ya maombi ya wastaafu hawa kuomba walipwe miezi mitatu mitatu. Kama itaonekana sasa wataomba tena walipwe mwezi moja moja, Serikali haioni ugumu wowote kurejea kule tulikotoka.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii niulize swali fupi. Kwa kuwa, suala la Katavi linafanana sana na la Mkoa wa Kigoma ambao hatuna kiwanda hata kimoja na rasilimali ziko za kutosha, hususan katika Jimbo la Buyungu ambako kuna rasilimali kama mihogo, mpunga na kadhalika. Je, Waziri yuko tayari kuja kujenga viwanda katika Wilaya ya Kakonko? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haijengi viwanda! Serikali inahamasisha Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi waje kujenga viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwape habari nzuri Kigoma; kuna kampuni inaitwa Kigoma Sugar, tumewapa hekta 47,000 watajenga Kiwanda cha Sukari kinachozalisha tani 120,000 watakapoanza kazi, nimewaambia ifikapo Septemba matrekta yote yaende kulima kwetu Kigoma ili kusudi tuzalishe sukari. Mambo mazuri yanakuja Kigoma.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii.
Kwa kuwa, hili suala la Geita linafanana sana na tatizo lililoko Wilaya ya Kakonko, Jimbo la Buyungu kutokuwa na sekondari kabisa ya A-level na tunayo shule moja ya sekondari Kakonko ambayo ikiwekewa miundombinu mizuri yafaa kuwa na A-level.
Je, Waziri yuko tayari kuweka kipaumbele katika shule ya sekondari Kakonko ili ipewe hadhi ya kuwa na A-level itakayokuwa ya kwanza katika Wilaya ya Kakonko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba Serikali kutoa kipaumbele, nadhani hili tumetoa maagizo katika maeneo mbalimbali, kwa sababu tuna shule nyingi sana za kata. Shule hizi za kata watoto wakifaulu lazima waende Advance Level. Tunapokuwa na shule za kata wanafunzi wanishia form four maana yake wakikosa nafasi za kwenda advance, shule zikiwa chache vijana inawezekana wakafaulu lakini wakakosa nafasi.
Kwa hiyo, haya ni maelelekezo ya maeneo yote, ndiyo maana mwaka huu hata ukiangalia bajeti yetu tumezungumza, tunakarabati zile shule kongwe, hali kadhalika kuhamasisha maeneo mbalimbali kujenga shule. Kwa sababu tunajua eneo lile jiografia yake ni ngumu tutaangalia jinsi gani ya kufanya maeneo ambayo hayana shule za Kata tuyape msukumo shule za advance level ili kwamba watoto wakifaulu katika shule a O level waende advance level katika maeneo husika.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, asante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa Waziri mwenyewe amekiri katika majibu yake ya swali la msingi kwamba ajira ya walimu imekasimiwa kwenye mamlaka zingine, na mamlaka zilizokasimiwa ajira za walimu ndizo zimesababisha matatizo makubwa ya walimu, walimu kutopanda madaraja kwa wakati, walimu kutolipwa mishahara mizuri na walimu kutolipwa madai yao kwa muda mrefu sana.
Je, Waziri yuko tayari hii Tume iliyoundwa namba 25 ya mwaka 2015 iwe na mamlaka kamili ya kuwaajiri na kulipa mishahara bila kukasimiwa kwenye mlolongo wa vyombo vingine?
Swali la pili, kwa kuwa matatizo yaliyosababishwa ya walimu nchini yametokana na mfumo kwa kukasimu mamlaka ya ajira ya walimu kwa vyombo vingine vingi kuanzia Katibu Kata, Mratibu, TSD, Utumishi, Hazina na kadhalika, vyote vinavyoleta usumbufu kwa ajira ya mwalimu na maslahi yake kupotea.
Je, Serikali iko tayari kuwahudumia walimu kwa dharura kabisa kulipa madai yao yanazidi shilingi bilioni 20 kwa dharura ya haraka ili walimu hao waweze kufanyakazi kwa moyo? Asante
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwalimu Bilago ametaka kujua kama Serikali iko tayari kuipa Tume ya Utumishi ya Ualimu mamlaka kamili ya kulipa mishahara. Niseme tu kwamba ukiangalia katika kifungu cha 5 kinachoanzisha Tume hii ya Utumishi wa Walimu, Mamlaka kwa Tume hii ni Mamlaka ya ajira. Bado suala zima la kulipa mishahara kama ilivyo Kanuni ya Utumishi wa Umma na kama wanavyolipwa watumishi wote wa umma itabaki katika Serikali. Lakini ukiangalia kama Mamlaka ya Usimamizi kwenye Serikali za Mitaa, ambao ndio wanaendesha na wenye shule uko chini, wao wanachokifanya ni kulipa tu mishahara kwa kuwa wao ndiyo mamlaka ya usimamizi, kwa hiyo tutaendelea hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba pamekuwa na changanmoto ambazo tunazitambua kwa kuanzisha Tume hii tunaamini sasa kwa kuwa ni Tume ambayo inajitegemea, maana ukiaangalia huko awali Idara ya Walimu ilikuwa chini ya Utumishi wa Umma, lakini Tume hii mpya ambayo tunayoianzisha itakuwa ni Tume inayojitegemea na tunaamini sisi kama Serikali kwa kuwa tumejipanga kuiwezesha kwa rasilimali fedha, kuiwezesha kwa rasilimali watu na vitendeakazi mbalimbali tunaamini changamoto mbalimbali ambazo zilijitokeza basi zitaweza kutatuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge aweze kuwa na imani, tuweze kuanza Tume hii halafu tuone mambo yatakavyojitokeza lakini sisi kama Serikali tuko tayari kuiwezesha Tume hii kwa hali na mali. Ukiangalia katika mahitaji ya kibajeti yaliyobainishwa ni takribani shilingi bilioni 75, wakati ukiangalia ni ilipokuwa ni Idara ya Utumishi wa Walimu walikuwa wanategemea bajeti yao kutoka katika Tume ya Utumishi wa Walimu, ndiyo maana changamoto mbalimbali za kupandishiwa mishahara, changamoto za kupandishwa madaraja na mambo mengine yalikuwa zinajitokeza. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge aiamini Serikali, tuipe nafasi Tume iweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili kuhusiana na madeni ya walimu, kama nilivyoeleza jana. Ni kweli madeni ya walimu yako katika kiwango cha juu, takribani shilingi bilioni 42, lakini hivi sasa tunachokifanya ni kuhakiki madeni haya. Nilitoa angalizo, yako madeni au madai yanayowasilishwa ambayo unajikuta yana mapugufu fulani, yako ambayo unajikuta hayana nyaraka mbalimbali za kiutumishi. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama Serikali tutajitahidi kuhakikisha kwamba tunalipa madeni haya haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sasa kupitia Bunge lako Tukufu, kwa kuwa mfumo wetu wa Human Capital Management System uko katika Halmashauri mbalimbali, niwaombe Waheshimiwa Wabunge ambao nao ni Madiwani katika Halmashauri husika waweze kufuatilia madeni haya, yako kiasi gani kwa mwezi husika, mwezi unaofuata unatarajiwa kulipa kiasi gani, lakini vilevile endapo kuna madai ambayo yamerudishwa changamoto ni nini, waweze kutusaidia.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii adimu. Pamoja na majibu yaliyotolewa na Naibu Waziri, ipo nguvu kazi nzuri sana katika nchi hii iliyotafuta ajira binafsi; vijana wa bodaboda. Hawa vijana wa bodaboda tunawatumia vizuri wakati wa uchaguzi, baada ya uchaguzi, wanapata misukosuko ya kufa mtu. Wanasumbuliwa na Polisi. Bodaboda wangu waliopo Kakonko na nchi nzima, hawa bodaboda tunawalindaje katika ajira zao hizi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, hata mimi nataka nikiri kwamba kundi hili ni kundi ambalo kwa kiwango kikubwa sana, asilimia kubwa tuliopo hapa tuliwatumia katika kampeni zetu na ndio wametufanya tumefika katika jengo hili. Vile vile nataka nikiri tu kwamba, bodaboda ni biashara ambayo sisi tunaamini kwa kiwango kikubwa sana kwamba inasaidia katika kutatua changamoto za ukosefu wa ajira kwa vijana wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika eneo hili imefanyaje? Kwanza kabisa, Serikali kwa kushirikiana na mamlaka zile husika hasa mamlaka za Halmashauri ya Manispaa na Majiji, kwanza kabisa kutenga maeneo maalum na kuwatambua na kazi yao iheshimiwe. Pili, tuna program maalum kupitia Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi pamoja na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya ukopeshaji wa pikipiki, hizi bodaboda ili vijana wetu hawa ambao asilimia kubwa sana wanafanya kazi kwa watu wapate fursa ya kukopa wenyewe moja kwa moja na pikipiki zile ziwe mali zao na ziwasaidie katika kuinua uchumi wao.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mgogoro uliopo Kasulu - Kagera Nkanda unafanana kabisa na mgogoro ambao upo Wilaya ya Kakonko ambako tunayo mbuga ya wanayama ya Moyowosi na Kigosi inayozungumzwa. Vijiji vya Mganza, Itumbiko, Kabingo na Kanyonza vinapakana na maeneo hayo na; kwa hiyo vimekosa ardhi kabisa ya kutumia kwasababu ya ongezeko la watu. Kwa hiyo, nauliza swali; ni lini mchakato huo wa Wizara ya Maliasili na Utalii itaiona hoja ya wananchi kuongezewa ardhi kutoka kwenye hifadhi badala ya hifadhi kuwa na ardhi kubwa kuliko wananchi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi maswali yote yanayohusiana na migogoro ya mipaka ambayo unaweza ukaiita migogoro ya ardhi, lakini inayohusiana na hifadhi yanakuwa yanahusiana na maliasili na utalii. Ukizungumzia migogoro ya ardhi hiyo hoja ni pana zaidi kuliko hivi sasa.
Kwa hiyo, suala ni lini tutashugulikia mgogoro wa Kakonko kule jibu ni lile lile, kwamba tuvute subira tusubiri twende tufike kwenye maeneo haya tufanye utafiti, tufanye ukaguzi ili twende tukafanye team work.
Mheshimiwa Naibu Spika, bila kwenda kukagua kwa pamoja tukaangalia pengine tunaweza tukakurupuka na majawabu ambayo si sahihi. Ipeni nafasi Serikali tufike kule, Wizara zote sita kwa ujumla wetu tukishirikisha TAMISEMI lakini pia tukishirikisha hata wananchi wenyewe ambao ndio wanaguswa na matatizo na changamoto hizi. Zoezi zima litakuwa ni shirikishi, kwa hiyo tutapata majawabu ambayo yatakuwa ni ya kudumu.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii.
Kwa kuwa suala la wakimbizi ambalo linaathiri Wilaya ya Kibondo, vilevile limeathiri Wilaya ya Kakonko, Jimbo la Buyungu.
Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuwashauri watu wa UNHCR kutoa huduma za afya katika Kituo cha Afya Wilaya ya Kakonko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kuzungumza wazi kwamba tuwashukuru wenzetu wa UNHCR katika maeneo mbalimbali. Kwa mfano mwezi uliopita nilikuwa katika Mkoa wa Katavi. Miongoni mwa kazi kubwa sana waliyoifanya kule licha ya kusaidia katika miundombinu, lakini nimeona wamesaidia ambulance katika maeneo yale.
Kwa hiyo, ni imani yangu kwamba kwa suala analolizungumza Mheshimiwa Mbunge, nadhani hili ni wadau wetu wa karibu sana, ofisi yetu ya Mkoa kule itafanya utaratibu kuangalia ni jinsi gani tutafanya; na kwa Mkoa wa Kigoma kwenda kutoa juhudi hizo especially katika sehemu ya afya. Mwisho wa siku tunahitaji wananchi wetu katika eneo lile waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazo zuri sana, nadhani katika Serikali tunalichukua hili kwa ajili ya kuleta ule msisitizo tu wa makubaliano ya karibu kwamba lile linalowezekana basi liweze kufanyika, wananchi wa eneo lile waweze kupata huduma vizuri.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kumekuwa na tatizo la Serikali kuwatishia Wakuu wa Wilaya ambao wilaya zao zitapata janga la njaa, kwamba watapoteza Ukuu wa Wilaya na hivyo kusababisha wasitoe takwimu halisi za upungufu wa chakula uliopo katika Wilaya zao. Wananchi wengi wamekuwa wakifa kutokana na njaa kwa kuficha wasijulikane kama kuna njaa wilayani kwao. Je, ni kwa nini chakula kinakuwepo wilaya nyingine au mikoa mingine kingi na wilaya nyingine hakipo, watu wanakufa njaa ndani ya nchi hii moja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nafikiri tutofautishe njaa inapotokea katika mkoa ambapo hakuna sababu, kwamba mvua zipo, ardhi yenye rutuba ipo, watu wa kufanya kazi wapo. Tutofauitishe na sehemu nyingine ambazo kuna baa la nzige, kweleakwelea, ukame, hivi ni vitu viwili tofauti. Kwa hiyo, niseme tu kwamba, Wakuu wa Wilaya hawatishiwi ila walikumbushwa kuwajibika pale ambapo rasilimali zipo.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii. Pamoja na maelezo mazuri ya Naibu Waziri juu ya Workers Compensation na sheria inayohusika, kuna tatizo moja kutoka chombo kilichokuwa kinashughulikia compensation ambacho kimekwisha na kikachukuliwa hiki cha sasa ambacho ni Compensation Act ambayo imeanza Julai, 2016. Naomba anihakikishie kwamba wale wafanyakazi walioumia kwa sheria ya zamani ambayo ilikuwa inalipa viwango vidogo kama sh. 100,000/= watachukuliwa walipwe na Mfuko huu mpya kwa malipo ya Mfuko huu wa sasa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, Mfuko huu unaanza kulipa fidia kuanzia tarehe 1 Julai, 2016, hasa baada ya kuwa na kipindi cha mpito cha mwaka mmoja kuanzia mwaka 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimkumbushe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa mujibu wa taratibu za kisheria; sheria huwa haiendi retrospectively; kwa sababu hii sheria imeshatungwa katika mazingira haya na kuainisha wale ambao watapata madhara kuanzia kipindi hicho, basi Mfuko huu na sheria hii itahudumia wale tu ambao wanaguswa na sheria kuanzia pale ambapo ilitungwa lakini pia tarehe ya utekelezaji ambayo imetamkwa kwa maana ya kuanzia tarehe 1 Julai, 2016.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Suala la ufaulu wa watoto wa kike elimu ya juu inategemea na ufaulu wa watoto haohao wa kike kwenye shule za chini (O-Level na A-level), sasa kumekuwa na tatizo la watoto wa kike wanaobeba mimba wakiwa shuleni kuachishwa masomo, na hili tumekuwa tukilizungumza muda mrefu; ni lini Serikai italeta utaratibu hapa Bungeni, sheria itungwe ili watoto wa kike wanaobeba mimba shuleni wakishajifungua waruhusiwe kuendelea na shule?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hilo limezungumziwa katika nyakati tofauti tofauti, hivi karibuni pia tulipitisha mpango wa kushughulikia masuala yoyote yanayohusika na unyanyasaji kwa watoto wa kike na suala hilo limekuwa likishughulikiwa mia na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na tayari rasimu ya mwanzo ya mwongozo imeshatoka namna gani tufanye na pia niliweza kwenda kutembelea Zanzibar kuongea na Mheshimiwa Waziri kule kuweza kujua wenzetu wamekuwa wakifanya vipi katika eneo hilo, tukajifunza changamoto ambazo zilikuwa zinajitokeza kwa upande wao kwa mfano mwingine anaweza akasema anapata mimba na aliyempa mimba akasema anataka kumuoa katika mazingira kama hayo. Lakini mwisho wa yote tunaamini kwamba tutaweza kutekeleza kuona kwamba fursa zinatolewa kwa mtoto wa kike aliyepata mimba kuweza kurudi shuleni.
Changamoto tu ni namna gani, je arudi kwenye shule ileile, je unyanyapaaji utakuwepo au apewe shule maalum, ndiyo hayo ambayo wadau mbalimbali wanaendelea kutoa mawazo lakini mwisho wa yote tutatekeleza mapema iwezekanavyo.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika majibu ya swali la msingi, Mheshimiwa Waziri ameeleza kwamba mifuko hii iko imara. Kama kweli mifuko iko imara, kuna Walimu waliostaafu zaidi ya 6,000 hawajalipwa mafao yao zaidi ya shilingi bilioni 550. Walimu hawa wanateseka wakiwemo Walimu wangu wa Jimbo la Buyungu ambao kila wakati nahangaika kufuatilia mafao yao ya kustaafu. Ni kwa nini anayestaafu halipwi mafao yake kwa mujibu wa mkataba ndani ya miezi miwili baada ya kustaafu?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi ni kwamba mifuko hii imeanza kulipa mafao na kwa hivi sasa SSRA inawasimamia kuhakikisha kwamba wale wote ambao wanastahili kulipwa mafao wanalipwa. Zamani hapa lilikuwa linazungumzwa deni kubwa ambalo lilikuwepo hasa katika mfuko ambao unashughulika na watumishi wa umma ambao Serikali ilikuwa inadaiwa takribani shilingi trilioni 1.3.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka ninavyozungumza hivi sasa Serikali imeshalipa shilingi trilioni 1.2 na deni lililobaki ambalo Serikali inadaiwa ni shilingi bilioni 128 tu. Mfuko wa PSPF mpaka ninavyozungumza hivi sasa wameshalipwa takribani shilingi bilioni 720. Kwa hiyo, Mwalimu Kasuku kama bado kuna usumbufu huo, naomba uniletee nitazungumza na SSRA waweze kulifanyia kazi ili Walimu waweze kulipwa.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nisikitike kwa majibu yaliyotolewa na Wizara juu ya swali hili, haya siyo majibu sahihi kwa swali hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza. Mji wa Kakonko nyumba zinazozungumziwa zilikuwepo kabla ya mwaka 1967 kwa sheria iliyotungwa. Haiwezekani survey inayofanyika ikafanyika na kukuta hakuna nyumba hata moja inayokidhi
vigezo vya kulipwa. Kwa maelezo hayo, Serikali ya Chama cha Mapinduzi imepanga kuwatia umaskini wananchi katika Mji wa Kakonko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, survey ile inaonesha tangu miaka tisa iliyopita hakuna aliyekuja kuzungumzia kwamba nyumba zile hazitalipwa. Wananchi wamekuwa wakipigwa picha wanapewa matumaini ya kulipwa leo taarifa inakuja hawawezi kulipwa. Sasa nauliza, je, ana uhakika kwamba
hakuna nyumba iliyokuwepo kwa sheria iliyokuwepo kabla ya mwaka 1967?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa majibu
hayajakidhi vigezo vya nyumba zilizopo katika eneo hilo ambazo zitabomolewa na zote hazina vigezo, Serikali iko tayari kwenda kufanya survey upya katika Mji wa Kakonko na kujiridhisha kwamba zipo nyumba ambazo zinakidhi vigezo na hivyo wananchi wake waweze kulipwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA
MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, hizi sheria tunatunga wenyewe humu ndani ya Bunge. Sheria ya siku za nyuma toka mwaka 1932 mpaka ilipokuja kurekebishwa mwaka 1967 na
sasa tunayo ya mwaka 2007 zote zilitungwa ndani ya Bunge. Naomba sana ndugu zangu tuheshimu kile ambacho tulikubaliana wote ndani ya Bunge hili.
Mheshimiwa Spika, naomba kurudia jibu langu la
msingi kwamba katika barabara hiyo survey imefanyika na hakuna nyumba ambayo ipo nje ya mita 22.5 kwa sheria ya 1967 na nje ya mita 7.5 ya nyongeza kwa sheria ya mwaka 2007. Kwa hiyo, kurudia survey wakati mwingine tunapoteza
fedha lakini kama kutakuwa na tatizo mahsusi, naomba Mheshimiwa Bilago awasiliane na meneja TANROAD Mkoa halafu tutaanzia hapo.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tatizo lililopo Manyara linafanana kabisa na tatizo lililopo Wilaya ya Kakonko. Tatizo ambalo lipo Hospitali ya Wilaya ya Kakonko ambayo ni kituo cha afya haijapata hadhi ya Wilaya ni kupata dawa zenye hadhi ya kituo cha
afya lakini zinatumiwa na wananchi wa Wilaya nzima kama Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri alitembelea Kakonko akaona hali ya kituo cha afya ilivyo…
MHE. KASUKU S. BILAGO: Ndiyo nauliza hivyo; ni lini sasa Kituo cha Afya Kakonko kitabakia kuwa kituo cha Afya ili iweze kujengwa Hospitali ya Wilaya ya Kakonko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kweli nikiri kwamba, nimefika pale Kakonko na nimetembelea kile kituo cha afya tukiwa pamoja na Mbunge ni kweli kuna changamoto hizo kubwa lakini tubaini kwamba vipaumbele hivi mchakato wake unaanza kiwilaya. Hata hivyo, Mheshimiwa Bilago anafahamu kwamba pale alikuwa hana ambulance; Serikali imepeleka tayari ambulance kipindi hiki kifupi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika mpango wa bajeti katika Basket Fund yake ana milioni 395, fedha ambayo nimpe taarifa mpaka mwezi wa Saba Halmashauri yake zaidi ya shilingi 197 zilikuwa hazijatumika zimevuka mwaka wakati
wananchi wana matatizo. Kwa hiyo, naomba niseme sisi kama Serikali tutaangalia jinsi gani tutafanya katika mchakato huu ili kwenda pamoja na wenzetu wa Halmashauri, lakini jambo la msingi ni lazima tuwasimamie watendaji wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine kuna
baadhi ya wengine wanafanya mambo ya hovyo na wananchi wanaendelea kupata shida wakati fedha zipo; Mbunge na watu wengine wanapata matatizo kumbe fedha zipo watendaji wetu wameshindwa kutimiza wajibu wao. Kwa hiyo, tupo pamoja kuhakikisha mambo yanaenda vizuri
katika Halmashauri zetu.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii adimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililoko Madaba linafanana sana na tatizo lililoko Jimbo la Buyungu. Wilaya ya Kakonko ina miradi ya maji ya Mradi wa World Bank katika vijiji vya Muhange, Katanga na Nyagwijima kata ya Mgunzu. Miradi ile inaendelea kusuasua na wananchi hawanufaiki na miradi ile wakati fedha zilitolewa na fedha hizo ni za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Kauli ya Serikali ni lini miradi hiyo itakamilishwa ili wananchi wa Muhange, Katanga na Nyagwijima waweze kupata maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Bilago mwenyewe ni shahidi, Serikali imetoa fedha. Utekelezaji wa miradi unafanywa na Halmashauri. Katika hiyo Halmashauri, Mheshimiwa Mbunge wewe ni Diwani kule, hebu naomba tusaidiane kusimamia hao Wakandarasi waweze kukamilisha hii miradi. Tatizo la hela halipo, hela tunayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Halmashauri ya Kakonko na sisi Madiwani na Mheshimiwa Mbunge, tuwasimamie Wakandarasi ipasavyo ili miradi iweze kukamilika.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Tatizo lililopo Mbulu Vijijini linafanana kabisa na tatizo lililopo Wilaya ya Kakonko. Wilaya ya Kakonko Kata za Nyamtukuza, Nyabibuye, Warama, Muhange, Kasuga na mwambao wote wa Burundi, simu zinaingiliana na mitambo ya Burundi na hivyo wananchi wa Wilaya ya Kakonko maeneo hayo yanayopakana na Burundi wanapata hasara kubwa sana kwa kuongeza vocha ambazo zinaliwa na mitandao ya Burundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba commitment ya Serikali hapa; Serikali inafanya jitihada gani kuhakikisha kwamba wananchi hawa hawapati hasara katika matumizi yao ya simu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo aliyoyataja, kama alivyosema, yako mpakani na tuna mipango maalum ya kushughulikia maeneo ya mipakani. Nitakwenda kuangalia ni kwa nini hasa eneo lake bado halijaboreshwa kwa namna ambavyo ameeleza?
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Suala la Teaching Allowance huwa halieleweki vizuri ndiyo maana linachanganywa na kada zingine. Teaching Allowance lengo lake ni ku-offset zile saa nyingi ambazo mwalimu anatumia kusahihisha madaftari au kazi za wanafunzi mpaka nyumbani kazi ambayo haifanywi na sekta zingine. Hakuna Bwana Kilimo anakwenda kusimamia…
Najenga hoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali lazima iangalie Teaching Allowance kwa walimu kama kitu pekee kabisa. Je, ni lini sasa Serikali itakuja na mkakati rasmi wa kuwasaidia walimu hawa kupata hiyo Teaching Allowance? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Wazir wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bilago, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nimueleze tu Mheshimiwa Bilago kwamba kama Serikali tunatambua umuhimu na thamani ya mwalimu na uzito na ugumu wa kazi wanayofanya na ndiyo maana ukiangalia katika kada za utumishi wa umma walimu wamepewa kipaumbele cha hali ya juu na bado hatutasita kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika,nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge, tumeanza zoezi la tathmini ya kazi, tunaangalia uzito, majukumu na aina za kazi kwa ujumla wake katika Utumishi wa Umma na posho zipi zitatakiwa kuwepo katika kada gani.
Nimuombe Mheshimiwa Mbunge aendelee kuvuta subira, zoezi hilo la tathmini ya kazi litakamilika katika mwaka huu wa fedha na baada ya hapo tutaweza kuainisha na kupitia na kuhuisha miundo mbalimbali ya kiutumishi vilevile kuangalia ni posho zipi ambazo zinahitajika kuwepo ikiwemo na hiyo ya Teaching Allowance kwa mapana yake. (Makofi)
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika jibu alilotoa Waziri kuhusu usalama uliosababisha kufungwa kwa Ofisi ya Uhamiaji Muhange miaka ya 1990 si la kweli. Miaka zaidi ya 20 Muhange ni salama na hakuna ofisi pale, wananchi wako pale, ofisi nyingine zote za Serikali zipo, inakuwaje Ofisi ya Uhamiaji ndiyo ishindikane kuwepo Muhange kwa sababu za kiusalama?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Burundi ni miongoni mwa Nchi za Afrika Mashariki kama zilivyo Kenya, Rwanda na kadhalika. Mipaka inayopakana na nchi hizi wananchi wake wananufaika kwa kubadilishana biashara kama mipaka ya Tunduma, Sirari, Namanga na kadhalika, pale kwetu, Jimbo la Buyungu wapo Warundi wanaokuja asubuhi kulima mashamba na kurudi nyumbani au sokoni na kurudi jioni, lakini Warundi hao wamekuwa wakikamatwa, mbona wale wa Sirari, Namanga na kadhalika hawakamatwi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, nilipojibu swali langu la msingi nilieleza sababu zilizosababisha kituo kile kufungwa ni hali ya usalama Burundi, sio Tanzania. Kwa hiyo, hoja yake kwamba Muhange ni salama sio hoja ambayo nimeijibu katika swali la msingi, ni kwa sababu ya hali ya machafuko Burundi ilivyoanza, ndiyo sababu ambayo nilijibu katika swali la msingi.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili, ni kweli wananchi waliopo mipakani katika nchi yetu na nchi jirani, zikiwemo Burundi, Uganda, Rwanda na kadhalika, tumekuwa na mahusiano ya muda mrefu na ndiyo maana kuna utaratibu ambao upo kwa mujibu wa sheria zetu. Kuna utaratibu ambao upo kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiaji wa jinsi gani raia wa kigeni wanapaswa kuingia nchini na nini wafanye na ni aina gani ya viza wawe nayo. Na tunaendelea kusisitiza kwamba sheria hizi ambazo zimetungwa kwa maslahi ya Taifa letu wananchi wa nchi jirani waendelee kuzitii.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kumekuwa kuna utaratibu wa utoaji wa vibali maalum kwa wananchi ambao wanaishi mipakani kwa masafa yasioyozidi kilometa kumi ambavyo vinaitwa vibali vya ujirani mwema. Vibali hivi vinatolewa bila ya malipo ili kuweza kuhamasisha na kusaidia wananchi ambao wamekuwa wakiishi mipakani kuendelea kutekeleza shughuli zao wanapokuwa wanavuka mipaka kwa shughuli za kawaida.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili mfanyakazi aliyemaliza kazi kwa kustaafu au kupoteza kazi aweze kulipwa mafao yake katika mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ni pamoja na kupata barua yake ya mwisho. Wafanyakazi waliopatikana na vyeti fake hawajapata mafao yao kutoka kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa sababu hawana barua za kumaliza huo ufanyakazi fake.
Je, Serikali iko tayari kuwapa barua zao ili wakahangaike kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na majibu fasaha na huo ndiyo utaratibu wa Serikali katika kushughulikia yale ya awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jibu la Mheshimiwa Bilago, swali hili la mafao ya watumishi ambao wameonekana kwamba ni watumishi wenye vyeti fake na ambao wamepatikana na masuala kadha wa kadha katika utumishi wao, limekuwa likijibiwa na Serikali mara kadhaa ndani ya Bunge lako Tukufu na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma. Ninaomba Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine wote waendelee kuvuta subira, yale ambayo yamekuwa yakijibiwa na Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma hayo ndiyo ambayo yatakuja kutekelezwa baada ya Serikali kufikia maamuzi yale ambayo Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma amekuwa akieleza humu ndani ya Bunge lako Tukufu kila siku.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ulitaka kupanua goli. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri aliyotoa kwa swali hili, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, katika eneo hili ambalo lina chokaa linaloitwa Bumuli maarufu Ngongogwa liko katika Hifadhi ya Moyowosi - Kigosi. Wafanyabiashara wanaotaka kuchimba hiyo chokaa wamekuwa wakikwamishwa na shughuli zinazofanyika katika hifadhi na Mamlaka ya Hifadhi kuwazuia kufanya shughuli hiyo. Je, Serikali inaweza ikatoa utaratibu mahsusi watakaofuata wananchi wa Kaknoko ili waweze kuchimba chokaa hiyo ambayo ni grade two? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo dhahabu ambayo imepatikana sehemu za Nyamwilonge na Nyakayenze na maeneo ya Ruhuli inayoendelea kuchimbwa na wachimbaji wadogo wadogo kwa kutumia zana hafifu. Je, Serikali iko tayari kutoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo wadogo katika maeneo hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Bilago lakini pia namshukuru kwa sababu anafuatilia sana maeneo ya wachimbaji katika maeneo yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imechukua hatua nyingi sana, lakini kulingana na Sheria ya Madini na Sheria ya Hifadhi ya Mazingira, kifungu cha 95 cha Sheria ya Madini kinatoa utaratibu na utaratibu unaotumika hivi sasa kuchimba madini katika maeneo mengine kwanza kabisa mtu anaruhusiwa kupata leseni lakini akishapata leseni ya uchimbaji anawaona watu wa maliasili ili apate kibali cha maandishi na huo ndiyo utaratibu unaotumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshatoa leseni 70 katika maeneo karibu na Hifadhi ya Moyowosi na hizo leseni wananchi wanachimba na kuna vikundi viwili vya ushirika ambapo wanafanya kazi hiyo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Bilago utaratibu upo lakini ni vizuri tukaa zaidi ili nikueleweshe ili wananchi wa Jimbo lako wanufaike zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la nyongeza la pili, maeneo ya Nyamwilonge na Nyakayenze pamoja na Makele na maeneo ya mbali, maeneo haya tumeshatoa leseni kwa sababu kuna uchimbaji mzuri wa dhahabu. Mwaka 2012 kuligunduliwa dhahabu na tukalitenga eneo hilo na hivi sasa kuna leseni 76 katika maeneo hayo. Nimuombe Mheshimiwa Bilago awahamasishe wananchi wa Jimbo lake ili eneo lililobaki tulilolitenga pia walitumie kwa manufaa ya maisha yao.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii. Fursa ambazo Tanzania imezipata kupitia SADC ni sawa na ambavyo tunapata fursa kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sambamba na mikoa mingine ambayo inazunguka nchi za Afrika Mashariki, Mkoa wa Kigoma na hususan Wilaya ya Kakonko, hatuna fursa ambazo tunazipata kwa kupakana na Burundi, matokeo yake Warundi wanateswa na kusumbuliwa katika Wilaya ya Kakonko na mwambao wote unaoambaa Wilaya zote za Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kupata maelezo ya Serikali, Burundi siyo sehemu ya Afrika Mashariki? Kama ni hivyo, kwa nini waendelee kuteswa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya mwisho, wiki iliyopita pia alisema kwamba kuna raia wa Burundi kama 300 wamepigwa sana, lakini mimi nimefuatilia suala hilo sijaliona. Kama kuna sababu zozote zinazoonesha kwamba labda Burundi wanawafanyia ndivyo sivyo Watanzania, ningepata tu ushahidi na tutafuatilia, kwa sababu, katika vikao vyetu vya Mabaraza ya Mawaziri yanapotokea mambo ambayo hayaendani na utaratibu wa kisheria, huwa tunakaa na kuyatatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Mbunge aniletee taarifa hiyo, ili sisi kama Wizara tufuatilie. (Makofi)
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu aliyotoa kwa swali hili, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, wavuvi wa Ziwa Tanganyika katika Manispaa ya Kigoma Ujiji maisha yao yote yanategemea uvuvi na vyombo vile kama mitumbwi inatumika kwa ajili ya uvuvi siyo kusafirisha abiria. Sasa ni lini Serikali itaondoa tozo hii ili kuondoa manyanyaso kwa wavuvi wa Kigoma Ujiji?
Swali la pili, sambamba na vyombo vya majini, bodaboda walioko Wilaya ya Kakonko na Wilaya zingine hapa nchini nao wanatozwa SUMATRA. SUMATRA ya bodaboda ni shilingi 22,000 sawa na kiti kimoja mwenye basi angelipa kwa kiti basi lenye abiria...
Mheshimiwa Mwenyekiti ndio nakuja. Basi lenye abiria 60 lingelipa shilingi 1,320,000. Ni lini sasa Serikali itaondoa tozo ya SUMATRA kwa bodaboda katika Wilaya ya Kakonko na Wilaya zingine nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali yote mawili kwa pamoja kwamba kimsingi hatutozi tozo kama ambavyo nilisema katika jibu la msingi, kinachotozwa na SUMATRA ni ada ya ukaguzi. SUMATRA wanahitajika kukagua iwe hizo meli au hizo boti zinazotumika kwenye uvuvi au pikipiki zote hizi zinatakiwa zikaguliwe ili tuwe na uhakika zinapotoa huduma au zinapofanya shughuli za uvuvi zipo salama. Sasa kazi hiyo inayofanywa na SUMATRA inahitaji kulipiwa ada kidogo.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaruhusu nyavu zisizotakiwa zinaingia nchini na Serikali hiyo hiyo inachukua kodi kwa waingizaji wa nyavu ambazo hazifai, nyavu zikishauzwa anayepata hasara ni mwananchi aliyenunua nyavu zile ambazo kumbe Serikali inafahamu hazihitajiki na ilichukua kodi. Sasa kama Serikali inaweza ikazuia madawa ya kulevya yasiingie nchini inashindwaje kuzuia nyavu zisizofaa kwa wavuvi zisiingie nchini na hivyo kuwatia hasara baada ya kuwa wameshazinunua? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi jambo hili la nyavu lina mkinzano. Zipo nyavu ambazo zinaruhusiwa katika bahari lakini size hiyo hiyo ya nyavu inaweza isiruhusiwe katika maziwa yetu; wapo wafanyabiasara ambao wanaweza kuagiza nyavu kwa nia ya kusema wanazipeleka katika bahari lakini wakishafika na kuzitoa bandarini wakazipeleka kwenye maziwa pasiporuhusiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hila hii wataalam wetu na sisi kama Wizara tunaendelea kukabiliana nayo na hata sasa tunazo kesi mahakamani za jambo la namna hii. Sisi tunaomba uungwaji mkono wa kuhakikisha kwamba mkanganyiko huu tunautatua ilimradi tuhakikishe kwamba wafanyabiashara wetu, wazalishaji wetu wa nyavu, wote wanakwenda kwa matakwa ya sheria, kanuni na taratibu zetu zinazo-guide shughuli nzima hii ya uvuvi. Uvuvi ni maisha yetu, lakini ni lazima tuhakikishe tunalinda mazingira kwa ajili ya vizazi vya leo na vya kesho. Nashukuru sana.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Maagizo yaliyotolewa na Serikali ya kuhamishia watoto wenye uhitaji wa elimu maalum ifikapo Desemba 31 mwaka huu hayatekelezeki; kwa sababu hata kwangu Wilaya ya Kakonko hakuna shule hiyo. Swali la kwanza, Serikali iko tayari kujenga shule ya watoto wenye uhitaji wa elimu maalum katika Wilaya ya Kakonko ikizingatiwa kwamba kuna watoto zaidi ya 200, Walimu wako watano tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa maelezo hayo hayo ambayo nchi nzima itaathiriwa na agizo hili la Serikali, je, Serikali inaweza ikajiridhisha kwamba kila wilaya inapata shule ya watoto wenye vipaji maalum yenye mabweni ili kuwaokoa katika usumbufu wanaoupata? Ahsante.
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Kasuku Samson Bilago, hajasahau taaluma yake licha ya kuwa Mbunge. Sasa naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kasuku kama ifuatavyo:-
Serikali imeshatoa maagizo tangu mwaka jana kwamba kila halmashauri iteue shule angalau moja ili watoto wenye mahitaji maalum waweze kusomeshwa vizuri kwa mujibu wa mazingira ya mahitaji yao. Sasa kama kwenye wilaya yake hakuna hata shule moja, natoa agizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ili aweze kutekeleza agizo la Serikali lililotolewa tangu mwaka jana mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, amezungumza kwamba kwenye eneo lake la Ubunge wapo Walimu watano tu ambao wana taaluma ya elimu maalum. Namhakikishia kwa agizo ambalo limetolewa na Serikali leo; mimi nimesisitiza tu lilishatolewa siku nyingi, nasisitiza na kuwapa muda kwamba ifikapo Desemba 31, 2018 agizo hili linatekelezeka. Ndiyo maana tumewapa muda mrefu vinginevyo tungeweza kuwapa mwisho tarehe 30 mwezi wa Juni, lakini tumewapa muda mrefu hadi Desemba ya 2018 ili Halmashauri ziweze kujipanga vizuri kuhakikisha agizo linatekelezeka. (Makofi)
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii nyeti. Wilaya ya Kakonko ni miongoni mwa Wilaya zenye matatizo ya usikivu wa TBC. Kule tunasikiliza Redio Burundi, ndugu yangu Mheshimiwa Mwamoto ni shahidi amekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibondo kule. Maeneo ya Kibondo na Kokonko hakuna usikivu wa TBC. Katika swali la msingi imetajwa Wilaya ya Kakonko. Naomba kujua na nipewe time frame na Serikali ni lini, ni tarehe ngapi TBC itaanza kusikika Kakonko?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni kweli kwamba Kakonko ni moja ya zile Wilaya tano za mipakani ambazo zimetengewa fedha katika bajeti ya mwaka huu 2016/2017, ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwamba amekuwa akipambania usikivu katika Wilaya yake na ni kweli kwamba matangazo mengi wanayapata kutoka nchi jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utaratibu ambao tumeanza, tulianza na kufanya tathmini kwamba ni wapi minara iwekwe tayari tulishaomba masafa kutoka TCRA na tumepata, tayari mzabuni ameshapata zabuni ya kufanya kazi hii, lakini time frame tuliyopanga ni mwisho wa mwaka huu wa fedha usikivu utakuwa umeimarika katika Wilaya ya Kakonko na maeneo mengine ambayo ameyataja. Ahsante.(Makofi)
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii nyeti. Wilaya ya Kakonko ni miongoni mwa Wilaya zenye matatizo ya usikivu wa TBC. Kule tunasikiliza Redio Burundi, ndugu yangu Mheshimiwa Mwamoto ni shahidi amekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibondo kule. Maeneo ya Kibondo na Kokonko hakuna usikivu wa TBC. Katika swali la msingi imetajwa Wilaya ya Kakonko. Naomba kujua na nipewe time frame na Serikali ni lini, ni tarehe ngapi TBC itaanza kusikika Kakonko?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni kweli kwamba Kakonko ni moja ya zile Wilaya tano za mipakani ambazo zimetengewa fedha katika bajeti ya mwaka huu 2016/2017, ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwamba amekuwa akipambania usikivu katika Wilaya yake na ni kweli kwamba matangazo mengi wanayapata kutoka nchi jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utaratibu ambao tumeanza, tulianza na kufanya tathmini kwamba ni wapi minara iwekwe tayari tulishaomba masafa kutoka TCRA na tumepata, tayari mzabuni ameshapata zabuni ya kufanya kazi hii, lakini time frame tuliyopanga ni mwisho wa mwaka huu wa fedha usikivu utakuwa umeimarika katika Wilaya ya Kakonko na maeneo mengine ambayo ameyataja. Ahsante. (Makofi)
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Jimbo la Buyungu, Wilaya ya Kakonko tumepata ufadhili wa kujengewa vituo vya kisasa vya baba, mama na mtoto kutoka Bloomberg, USA. Ni vituo vya kisasa kabisa. Sasa nataka commitment ya Serikali, vituo vile vinawekewa vifaa vya kisasa na vinahitaji wataalam wa kisasa. Je, Serikali iko tayari kuleta wataalam baada ya vituo hivyo kukamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli Kakonko ni eneo ambalo linapata changamoto kubwa sana. Ndiyo maana siku ile nilivyokuwa naongea na watumishi wetu pale Kakonko mpaka kama binadamu unajisikia huzuni kwa cost load waliyokuwa nayo, ni kubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie, kwa sababu Serikali ipo katika mpango wa kuajiri watumishi wengi; na najua katika Mkoa wa Kigoma tumepeleka watumishi wapatao takribani tisa au 12, kati ya hapo tu kwa Mkoa mzima wa Kigoma, lakini mahitaji ni makubwa zaidi. Ngoja mchakato huu sasa wa ajira hizi mpya utakapotoka tutaangalia jinsi gani tusaidie wananchi wa Kakonko pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili siyo kwa Kakonko peke yake na Mkoa wa Kigoma wote kwa ujumla kwa sababu kuna changamoto kubwa ya wakimbizi, kwa hiyo, huduma inakuwa ni tight sana. Kwa hiyo, lazima tutalichukua jambo hilo; Kasulu, Kakonko, Kibondo, Uvinza na sehemu nyingine, kutoa kipaumbele kwa Mkoa wa Kigoma. (Makofi)
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante Mtemi. Wilaya ya Kakonko mwaka jana ilipata shida kubwa ya mbolea mpaka nikadiriki kumpigia Waziri wa Kilimo juu ya ukosefu wa mbolea katika Wilaya ya Kakonko. Tatizo hili lilitokana na wale suppliers ambao hawakuwa na uwezo kabisa wa kununua mbolea na kuiuza kwa bei elekezi kwa sababu ilikuwa inatoka mbali. Nataka Waziri, tena bila kumumunya maneno, anihakikishie kama wananchi wa Kakonko watapata mbolea mwaka huu bila usumbufu? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na kwa niaba ya Waziri Wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba tu nimhakikishie rafiki yangu Mheshimiwa Kasuku Bilago kwamba mfumo huu ambao tunataka kuwasiminisha Wabunge wote utampa huo uhakika anaoutaka. Naomba nimhakikishie kwamba mbolea itapatikana kwa wakati wote nchini.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu yaliyotolewa kwa swali hili, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kumekuwa na upotoshaji mkubwa sana kuhusu TASAF kwamba ni fedha zinazotolewa na Chama cha Mapinduzi. Hata Ndugu Polepole alipokuja jimboni kwangu aliwaambia wanufaika wa TASAF ni kwamba ni fedha zinazotolewa na Chama cha Mapinduzi. Naomba kauli ya Serikali kuhusu kuzuia upotoshaji huu unaofanywa na Ndugu Polepole pamoja na wenzake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna vijiji 12 katika Jimbo la Buyungu havinufaiki na TASAF kama Vijiji vya Juhudi, Kewe, Rusenga, Kikulazo, Kihomoka, Ruhuru, Njomlole, Yakiobe, Kiniha, Muhange ya Juu, Nyanzige na Nkuba. Ni lini vijiji hivi vitaingia kwenye mfumo wa TASAF? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, la kwanza, sikuwepo Buyungu wala Kigoma kusikia nini alisema Katibu Mwenezi wa CCM, lakini ametaka kujua fedha hizi zinatolewa na CCM au zinatolewa na Serikali? Majibu dhahiri wazi kwamba fedha hizi ni mkopo umekopwa na Serikali ya Tanzania utalipwa na Serikali ya Tanzania unachangiwa na Serikali ya Tanzania, lakini muhimu hiyo Serikali ya Tanzania iliyoweka mipango yote hii inaongozwa na CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kwamba viko vijiji 12 katika jimbo lake ambavyo haviko katika mpango. Napenda kuchukua nafasi hii kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba mpango wa TASAF mpaka sasa kwa Tanzania nzima tumefikia maeneo na watu asilimia 70, hatujafika maeneo yaliyobaki asilimia 30. Maandalizi tunayofanya sasa awamu itakayokuja kuhakikisha kwamba tunamaliza asilimia 30 iliyobaki na tukifanya hivyo hapa shaka vijiji vyake 12 vilivyobaki vitakuwa vimeingia katika mpango wa TASAF.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kituo cha Afya Kakonko kimeelemewa sana na wagonjwa. Kituo hiki cha Afya Kakonko Waziri wa TAMISEMI akiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Jafo, aliwahi kukitembelea akaona ukubwa wa kazi inayofanyika katika kituo kile. Kinapata mgao wa dawa sawa na Kituo cha Afya, kinatoa huduma kama Hospitali ya Wilaya. Sasa ni lini Serikali kwa makusudi kabisa itajenga Hospitali ya Wilaya ya Kakonko ili kuondoa mzigo kwenye Kituo cha Afya cha Kakonko? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba maeneo yote ambayo kuna Vituo vya Afya na hakuna Hospitali za Wilaya, hivyo Vituo vya Afya ndivyo ambavyo vimekuwa huduma kama Hospitali za Wilaya. Ni ukweli usiopingika kwamba sifa ya kituo cha afya na sifa ya Hospitali ya Wilaya ni tofauti. Ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo hakuna Hospitali ya Wilaya tunajenga na ndio maana tumeanza na hizo hospitali 67. Ni azma kuhakikisha Wilaya zote Tanzania zinakuwa na Hospitali za Wilaya.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana nilileta swali hapa Bungeni ili kujua maeneo yenye madini katika Wilaya ya Kakonko. Maeneo yaliyoanishwa na Serikali katika majibu yake ni pamoja na chokaa iliyoko eneo la Nkogongwa, dhahabu iliyoko Ruhuru Nyakayenzi na Nyamwilonge. Baada ya kuwa maeneo hayo yametambulika wananchi walichangamkia wakataka kuchimba madini lakini ghafla Serikali ikasitisha leseni za uchimbaji.
Ninachotaka kujua ni lini Serikali itafungua utoaji wa leseni kwa wachimbaji wadogo wadogo wa Wilaya ya Kakonko ili waweze kuanza uchimbaji? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na mabadiliko yake ya mwaka 2017 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2018, ni kwamba sasa hivi Tume ya Madini ambayo imeundwa ndiyo itakuwa na wajibu wa kutoa leseni kwa wachimbaji wakubwa, wadogo na wachimbaji wote wa kati. Ni juzi tu Mheshimiwa Rais ndiyo ameteua Mwenyekiti wa Tume ya Madini ambayo sasa ndiyo inaendelea na michakato ya kuchakata kwa maana ya kutoa leseni kwa watu wote walioomba leseni za kuchimba madini. Kwa hiyo, nimueleze Mheshimiwa Mbunge aendelee kuhamasisha wachimbaji wake waombe leseni na sasa Tume imeanza kufanya kazi, watapata leseni walizoomba na wataendelea na uchimbaji. Ahsante sana.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Wilaya ya Kakonko ina wafugaji wa samaki waliojiunga kwenye vikundi katika Vijiji vya Nagwijima, Kasanda na Nyabibuye. Swali langu, Waziri yuko tayari kuwasaidia mikopo, ruzuku au chochote kile watu hawa ambao wametumia nguvu yao na nguvu ya Mbunge kutokana na Mfuko wa Jimbo ili waweze kuendeleza ufugaji wa samaki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko tayari kama Serikali kuwasaidia wafugaji wa samaki na ndiyo maana katika mapendekezo ya sheria na bajeti mwaka huu atakuja kuona kwamba tumependekeza kuhakikisha kodi na tozo mbalimbali zinazofanya tasnia hii ya ufugaji wa samaki isisonge mbele ziweze kupunguzwa ama kufutwa ili kusudi tuweze kuwasaidia wafugaji wa samaki.