Contributions by Hon. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (32 total)
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kunipa fursa hii kuweza kuzungumza machache mbele ya hoja hii iliyoko mbele yetu. Pili, nasema kwamba naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, toka mjadala huu ulipoanza, Wabunge wote hasa Wabunge wa Kanda ya Ziwa walikuwa wanasimama mbele yetu na kila mmoja kwa hisia tofauti, kwa ukali na kwa uchungu sana wanazungumzia kuhusu reli ya kati. (Makofi)
Mimi Mwenyewe kama Waziri imenigusa sana na inaniuma sana jinsi gani ambavyo tunasimamia mpango wa ujenzi wa reli ya kati. Serikali vilevile inaliona kwamba hili ni jambo muhimu na tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba tutajenga reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtandao wa reli ya kati unaotarajiwa kujengwa kwa kiwango cha standard gauge utakuwa na kilometa 2,560. Mtandao huu utajumuisha reli kati ya Dar es Salaam - Tabora - Isaka, reli kati ya Tabora - Kigoma kilometa 411; reli kati ya Uvinza - Msongati, kilometa 200; reli kati ya Isaka - Mwanza, kilometa 249; reli kati ya Kaliua - Mpanda - Kalema, kilometa 360; na reli kati ya Isaka - Keiza, kilometa 381; pia itakwenda reli kati ya Keiza - Rusumo na mwisho tumalizia kuunganisha na wenzetu wa Kigali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, reli kati ya Tabora - Kigoma, kilometa 411, zilifanyiwa feasibility study mwaka 2015 mwezi Februari na sasa hivi zimekamilika. Reli kati ya Kaliua - Mpanda vilevile zimefanyiwa feasibility study katika kipindi hicho. Reli kati ya Isaka - Mwanza, kilometa 249 zilifanyiwa feasibility study na kampuni ya Denmark na kazi ilikamilika mwezi Mei mwaka 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, reli kati ya Mpanda - Kalema na Uvinza - Msongati inafanyiwa feasibility study na kampuni ya HP-Gulf ya Ujerumani. Kazi hiyo ilianza mwezi Machi, 2015 na ikamalizika mwezi Desemba, 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali iko katika mpango wa kutafuta pesa kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kati katika kiwango cha standard gauge ambapo reli hiyo kama nilivyosema itaunganisha matawi niliyoyataja hapo juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na maoni kwamba tutumie Mfuko wa Reli kwa ajili ya kujenga reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge. Kwa taarifa tu, Mfuko wa Reli kwa mwaka tunapata shilingi bilioni 50. Ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge, kwa kilometa 2,561 itagharimu takribani dola za Kimarekani bilioni 7.5, sawa na shilingi trilioni 15. Hii inaweza kupungua ama inaongezeka, itategemea kama tutaamua tutajenga tuta jipya, pesa itakuja hii na tukiamua kuchanganya reli baina ya meter gage na standard gauge inaweza kushuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kutumia Mfuko huu wa Reli, itachukua muda mrefu si chini ya miaka 300 kwa shilingi bilioni 50 ndiyo tuweze kupata trilioni 15. Kwa hivyo, Serikali sasa inaweka kipaumbele chake cha kwanza katika kujenga reli ya kati kupitia utaratibu wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu mwingine utakaoweza kutumika ni utaratibu wa ushirikiano baina ya nchi na nchi yaani Bilateral agreement ili kupata mkopo wenye masharti nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu. Serikali imeona mradi huu ni muhimu na tutasimamia kwa nguvu zetu zote ili tuhakikishe kwamba reli hiyo ambayo ina manufaa makubwa sana kwa nchi yetu hasa upande wa Congo kule na upande wa Burundi iweze kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki Nyongeza ya Tano ya Mwaka 1994, Itifaki Nyongeza ya Sita ya Mwaka 1999, Itifaki Nyongeza ya Saba ya Mwaka 2004, Itifaki Nyongeza ya Nane ya Mwaka 2008 na Itifaki Nyongeza ya Tisa ya Mwaka 2016 ya Katiba ya Umoja wa Posta Duniani
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nawashukuru sana Wabunge wote kwa kuelewa umuhimu wa Itifaki hizi kwa maslahi ya Shirika la Posta Tanzania vilevile kwa maslahi ya nchi yetu. Kama tunavyojua sasa kwamba kumekuwa na mabadiliko makubwa ya teknolojia na utandawazi kwa hivyo ni muhimu sana kuwa tunaendana na mabadiliko haya kuhakikisha kwamba nchi yetu haiachwi nyuma katika maendeleo vilevile nchi yetu inaendelea vizuri na kuhakikisha tunatoa huduma nzuri za posta ambazo tunahitaji sana hasa katika kipindi hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepokea baadhi ya mapendekezo ya Kamati ya Miundombinu ambayo ndiyo Kamati Mama kwenye sekta yetu hii na tunawahakikishia tu Wajumbe wote wa Kamati hii kwamba maoni yao yote waliyotoa hasa kwenye upande wa anuani za makazi na
misimbo ya posta tutazifanyia kazi kwa maslahi ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini kabisa kama nchi yetu itaweza kuweka mifumo ya anuani za makazi na misimbo ya posta, bila shaka tutaweza kupeleka uchumi wetu mbele hasa ukiangalia kwamba tutakuwa na uwezo mkubwa wa kuweza kumtambua mtu kila alipo na tukifanya hivyo tutaweza kulipa kodi vizuri, tutaweza kuokoa wananchi pale tunapokuwa na majanga na tunaweza kuutumia mfumo huo ukatusaidia kwa kiasi kikubwa kuleta maendeleo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru tena kwa kukubali kupitisha Maazimio yetu ya Itifaki kuanzia ya Tano ya mwaka 1994, Itifaki Nyongeza ya Sita ya mwaka 1999, Itifaki Nyongeza ya Saba ya mwaka 2004, Itifaki Nyongeza ya Nane ya mwaka 2008 na Itifaki Nyongeza ya Tisa ya mwaka 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia kukutana hapa leo tukiwa na afya njema. Pili, na mimi nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii kuchangia hoja iliyoko mbele yetu, ambayo ni hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanzia ninaunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitachangia kupitia hoja mbalimbali ambazo zimewasilishwa na Waheshimiwa Wabunge kwa muda wa kipindi chote cha hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utagawanyika katika sehemu tatu muhimu; kwanza nitajikita zaidi kwenye usafiri wa anga, halafu nitakwenda kwenye usafiri wa majini, halafu nitazungumzia mwisho usafiri wa nchi kavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa usafiri wa anga kama unavyojua nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba, anga letu linakuwa salama ili Watanzania na wageni wetu mbalimbali waweze kusafiri kwa njia salama. Katika kutekeleza jambo hili kama mnavyojua, wiki moja iliyopita tulizindua mradi wa ujenzi wa rada nne za kisasa ambapo rada ya kwanza itajengwa pale Dar es Salaam, ya pili itajengwa Mwanza, ya tatu itajengwa huko Songwe na ya nne itajengwa huko KIA. Mradi ule utakuwa na gharama ya takribani dola za Kimarekani bilioni 67.3 na kazi inaenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mnavyojua mwaka jana peke yake katika viwanja vyetu vya ndege takribani wasafiri milioni 4.13 waliweza kusafiri, hiyo ikiwa ni Watanzania pia na watu wengine kutoka nje ambao wanakuja nchini kwetu kwa ajili ya utalii. Ili kuhakikisha kwamba tunajenga miundombinu ya kisasa kuvutia watu watumie kwa kiwango kikubwa usafiri wa anga pamoja na wageni wetu, tumeanzisha miradi takribani 11 sasa nchini ambayo tunafanya ukarabati wa viwanja vya ndege.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukianzia pale Dar es Salaam tunajenga jengo la kisasa ambalo litakuwa na uwezo wa kuchukua abiria milioni 6.5 kwa mwaka na gharama yake ni shilingi bilioni 560 ukilinganisha na jengo lililoko sasa hivi ambalo lina uwezo wa kuchukua abiria milioni 2.5 kwa mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa huko Mtwara tunakarabati uwanja wa Mtwara ambao tunaujenga sasa uwe na urefu wa kilometa 2.8 ambao ndege kubwa sasa kwa mfano Airbus A320, Airbus A330 ziweze kutua bila matatizo. Tayari mkandarasi tumeshampata ambaye ni Engineering Construction Engineering Company ambaye atafanya kazi hiyo kwa gharama ya takribani shilingi bilioni
53. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mwanza tunaendele na ukarabati wa uwanja wa Mwanza ambao tayari sasa hivi tumeongeza eneo la kutua ndege ambalo sasa hivi limekuwa na urefu wa kilometa 3.5 na gharama ya kazi hiyo yote ni takribani bilioni 85. Kazi inayoendelea sasa hivi ni ujenzi wa jengo la control tower pamoja na maegesho ya ndege za abiria na ndege za mizigo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa hivi mradi huo umefikia asilimia 68. Kazi tunayojipanga sasa ni kuhakikisha tunatafuta fedha kwa ajili ya kujenga jengo la abiria za kisasa lenye uwezo wa kuchukua takribani abiria milioni 2.5 kwa mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mambo ya viwanja vya ndege tumeenda huko Sumbawanga ambako tayari tunataka kujenga uwanja wa ndege ambao una urefu wa kilometa 1.75 na utajengwa kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 55.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hiyo vilevile inafanyika huko Shinyanga ambako sasa tutatanua uwanja wetu kufikia kilometa mbili ambayo itagharimu takribani bilioni 49.5 na kazi hiyo tayari mkandarasi tumeshampata. Pia huko Shinyanga tutajenga jengo la abiria.
Aidha, kazi kama hiyo itafanyika Kigoma na Tabora ambako kwa maeneo hayo mawili tutajenga mjengo ya abiria na pesa zipo. Sasa hivi tunatafuta mkandarasi kwa upande wa Kigoma, lakini kwa upande wa Tabora tayari mkandarasi wa kazi hiyo ameshapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma tayari mkandarasi tumempata na sasa hivi tuko katika mazungumzo ya kuweza kufikia mapatano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kiwanja cha ndege cha huko Songwe kazi ya ujenzi wa jengo la abiria unaendelea na vilevile tunajaribu kutafuta au tayari tumeshampata mkandarasi kwa ajili ya kuweka taa sasa za kuongozea ndege ambapo ndege sasa zitaweza kutua saa 24 kwa siku, siku saba kwa wiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama ya kazi hiyo ni takribani shilingi bilioni 4.8. Tayari mkandarasi yupo na tunaendelea na mazungumzo yake kuona lini tutasaini mkataba ili kazi hiyo ianze mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna kazi ambayo inaendelea vile vile huko Songea pamoja na kiwanja cha ndege cha Iringa. Tunaamini hivi karibuni na huko tutaweza kupata mkandarasi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama unavyoelewa kwamba, unaweza kuwa na viwanja vya ndege vizuri, lakini kama huna ndege zako inakuwa si jambo zuri sana. Kwa kulijua hilo Serikali imenunua ndege sita kama wote mnavyojua, ndege tatu sasa hivi ziko mjini hapa Tanzania na zinafanya safari zake za kwenda Dar es Salaam, Dodoma, Tabora, Kigoma, Mwanza, Bukoba, Kilimanjaro, Zanzibar na Songea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni tutaanza safari za Mpanda pamoja na Tanga. Vilevile tutaanza safari za kwenda Entebe huko Uganda, Bujumbura, Burundi na Nairobi, Kenya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo kwa ufupi ndiyo kuhusu usafiri wa anga. Sasa naomba kwa ufupi niende kwenye usafiri wa majini...
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri Mbarawa, muda wako umekwisha, lakini naona Wabunge wote wanataka kuendelea kukusikiliza hapa, kwa hiyo, ngoja nikuongezee dakika chache umalizie hayo maeneo mawili yaliyobaki. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa muda huo na fursa hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa eneo la usafiri wa majini tuna maziwa makubwa, Ziwa Tanganyika na vilevile tuna Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Ziwa Tanganyika tayari tuna utaratibu tumeshaanzisha wa kununua meli ya abiria ambayo itachukua abiria 600 na mizigo tani 400 ambapo tunaendelea kumtafuta Mkandarasi. Vilevile tunafanya ukarabati wa MV Liemba ambapo tayari tumeshapata kampuni ya kutoka Denmark na tumetenga takribani bilioni 3.4 kwa kuanzia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Lake Vicktoria, kama mnavyojua tunataka kujenga meli ya kisasa. Bado tunaendelea na mazungumzo kutoka Korea. Meli hii itakuwa na uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na mizigo tani 200 na magari 25 kwa vile itakuwa ni meli ya kisasa. Tunaamini hivi karibuni tutafikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikigusia kidogo kuhusu usafiri wa Kisiwa cha Mafia, najua muda mrefu wananchi kule wamelalamika. Sasa hivi tunataka kujenga land craft ambayo ni boti ya kisasa yenye uwezo wa kupeleka abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Mafia. Bajeti inayokuja tutatenga takriban shilingi bilioni tatu kwa kuanzia tunaamini baadaye huko mbele tunaweza kumalizia ili wananchi wale sasa na wao tuweze kuendelea au kuwatatulia changamoto inayowakabili kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho kama nilivyosema ni kuhusu usafiri wa nchi kavu. Hapa kuna Wabunge wengi walitoa hoja zao, nikianzia kwa Mheshimiwa Mbunge hapa ambaye yeye alikuwa anazungumzia barabara yake kutoka Kidahwe - Kasulu yenye urefu wa kilomita 63. Kazi inaendelea na tunatafuta hela ili mkandarasi sasa asiweze kusimama kuhakikisha kazi ile inamalizika kwa muda unaostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna mradi ambao unaendelea sasa hivi wa ujenzi wa barabara ya kutoka Mafinga - Igawa yenye urefu wa kilomita 137.9, kazi inaendelea vizuri. Pia huko Njombe tunaenda mpaka Makete kwa ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 107.4 na kazi inaendelea vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna miradi mingi lakini kwa vile bajeti yetu inakuja, naomba niishie hapa na wakati wa bajeti tutazungumza mengi, Mungu akitujalia. Ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia tena hapa leo kuendelea na kikao chetu hiki na mimi kupata fursa ya kuchangia au kutoa mchango wangu kwenye hoja iliyoko mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimshukuru Mheshimiwa Spika wewe mwenyewe na Wenyeviti wote wa Bunge kwa uwezo na umahiri mkubwa mnaoonesha katika kuliendesha Bunge letu. Nachukua fursa hii kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu kwa umakini wake kwa kusimamia shughuli za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, napenda nimshukuru sana au niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliopata fursa ya kuchangia hoja yangu niliyowasilisha hapa Bungeni kwa michango yao mizuri na yenye lengo la kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Wizara yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingi zimetolewa na hii ni dalili ya dhati inayoonesha kwamba Waheshimiwa Wabunge wana maono makubwa kwenye kuendeleza Sekta hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ili sekta hizi ziweze kuchangia katika maendeleo ya nchi yetu. Aidha, katika michango yao, imedhihirika wazi juu ya mahitaji makubwa ya miundombinu bora na ya kisasa kwenye huduma za usafiri wa anga, nchi kavu na majini ambazo ni muhimu sana kwa nchi yetu katika uchumi wa viwanda na uchumi wa kati ufikapo mwaka 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba yangu imechangiwa na wachangiaji wengi ambapo wachangiaji 82 wamechangia kwa maandishi na 100 wamechangia kwa kuzungumza. Michango ya Waheshimiwa Wabunge wote ilikuwa mizuri sana na iliyosheheni mapendekezo, ushauri na busara namna bora ya kuendeleza sekta hizi za ujenzi, uchukuzi na mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, siyo rahisi kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge wote kwa kina na kutosheleza kwa muda huu mfupi nilionao ninaahidi kwamba hoja zote tutazijibu kwa maandishi na kuwapatia Waheshimiwa Wabunge wote majibu ya hoja hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri na Kamati ya Bunge ya Miundombinu umezingatiwa, hivyo napenda nitumie muda huu mfupi nilionao kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya hoja tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, michango yangu itajikita kwenye sehemu tatu; kwanza, kwenye Sekta ya Anga, Sekta ya Usafiri wa Nchi Kavu halafu Sekta ya Usafiri wa Majini.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo asubuhi kwenye kuchangia, Mheshimiwa Mlinga hapa amezungumzia kuhusu ujio wa ndege kubwa iliyokuja jana kwenye kiwanja cha Dar es Salaam, lakini yeye amezungumza Kibunge, mimi leo kwa sababu nasimamia sekta, nitazungumzia zaidi kiupande wa sekta ya anga.
Mheshimiwa Naibu Spika, jana kulikuwa na ndege ambayo ilikuwa inatoka Dubai kwenda Mauritius. Ni ndege ya Airbus 380 – 800, ndege ambayo ilkuwa ni Flight No. AK 700 01E. Ndege hii baada ya kufika kwenye kisiwa cha Madagaska walipata taarifa kwamba hali ya hewa Mauritius ni mbaya. Kwa kawaida ukipata taarifa hiyo unakwenda kwenye uwanja wa ndege ulio karibu nao.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa marubani baada ya kupima viwanja vya ndege vyote vilivyopo karibu, ukiwa Madagascar kiwanja chake cha kwanza cha karibu inakuwa ni Madagascar wenyewe, cha pili pale ni Zimbabwe. Zimbabwe pale kuna Mozambique, vilevile kuna Namibia kuna South Africa. Baada ya kuangalia yote wakaamua waje watue kiwanja cha ndege cha Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndege hii inachukua abiria 868, ni ndege kubwa duniani. Kwa jana ilikuwa na abiria 503. Ndege ile ilikuja Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam na ikatua vizuri na historia katika nchi yetu ama nchi nyingi za Afrika kutua Airbus 380; kwa niaba ya Serikali kwanza nawashukuru sana wafanyakazi wa kiwanja cha ndege cha JNIA, wafanyakazi wa TCA kwa kazi nzuri waliyoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii haikuja bure, isipokuwa sasa ulimwengu unatambua kwamba viwanja vyetu vya ndege hasa vya kimataifa ina vigezo vya kisasa, vigezo bora na vigezo vya kimataifa. Vinginevyo kama ingekuwa hatuna vigezo hivyo, ndege ile isingekuja Dar es Salaam na wafanyakazi walifanya kazi kubwa kwa sababu kipindi cha saa saba mpaka saa 11 inakuwa ni peak hours, panajaa sana pale, lakini wafanyakazi wale walifanya vizuri, immigration ilifanya vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawapongeza sana kwa kazi hii nzuri, tuendelee kushirikiana ili tuhakikishe kwamba tunajenga sekta hizi kwa maslahi ya Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niende kwenye sekta moja kwa moja. Kama tunavyojua, mwaka 2017/2018 tulipata takribani abiria milioni 4,950 waliotumia usafiri wa anga. Usafiri wa anga ni muhimu sana kwanza kwenye sekta yenyewe ya anga, pili kwenye sekta ya biashara na tatu, sekta ya utalii. Sekta ya utalii kwenye usafiri wa anga ni muhimu sana. Ndege hizi zikija Tanzania zinachukua Watanzania, ama zinasafirisha Watanzania, lakini pia tunasafirisha watalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya utalii ni sekta ambayo inachangia sana kwenye pesa za kigeni na ni sekta ambayo inachangia sana ajira hapa Tanzania. Kwa vile ni dhamira ya Serikali na sekta yetu kuhakikisha kwamba tunatoa huduma kwenye usafiri wa anga, lakini wakati huo huo tunahakikisha kwamba sekta ya utalii tunaiboresha zaidi. Kwa kuangalia hivyo, kuna baadhi ya maeneo ya nchi yetu bado sekta ya utalii haijaendelea sana, kwa mfano, upande wa nyanda za juu, tuna mbuga nzuri za wanyama lakini watalii bado kule hawajawa wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye kanda ya Magharibi kule, tuna Game Reserve nzuri sana. Kwa mfano tuna ile tunaita BBK, Biharamulo Game Reserve, tuna Burigi Game Reserve, tuna Ibada Game Reserve na nyinginezo, lakini bado watalii wengi wameshindwa kwenda kwa sababu kule hakuna viwanja vya ndege au barabara nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kulijua hilo, sasa tumekuja na mpango mkakati ambapo kila kwenye maeneo haya ya uvutiaji wa utalii tutajenga kiwanja cha ndege, tutajenga barabara na ndiyo mmeona sasa mwaka huu tumepanga pesa kwa ajili ya kiwanja cha ndege cha Iringa pamoja na barabara yenyewe ya kutoka Iringa mpaka Ruaha National Park, tunaijenga kwa kiwango cha lami barabara yenye urefu wa kilometa 104. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo huo tunajenga Kiwanja cha Geita ili kuhakikisha sasa tunatoa au tunakuza sekta ya utalii hasa kwenye Kanda ya Magharibi. Ili kuhakikisha kwamba anga letu liko salama, Serikali kupitia TCA tumeamua kununua rada nne za kisasa kwa ajili ya ndege za abiria. Rada hizo zitagharimu takriban shilingi bilioni 67.3, rada hizo zitajengwa moja pale Dar es Salaam JNIA; ya pili, itajengwa Songwe; ya tatu, itajengwa KIA; na ya nne, itajengwa huko Mwanza. Hatukusimamia hapo tu kwa sababu kuna baadhi ya viwanja vya ndege sasa hivi ndege zimekuwa nyingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Zanzibar Kiwanja cha Abeid Amani Karume traffic imekuwa kubwa. Kwa kawaida ikishafikia hatua hiyo, tunaweka vifaa vya kisasa ambavyo tunaita instrument landing system kama alivyosema Mheshimiwa Zungu juzi, kwa vile Zanzibar tunajenga vifaa hivyo na tutatumia takribani shilingi bilioni 3.6. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimezungumzia usalama wa anga yetu, tukiweka rada hizi tunazozizungumza, kwanza anga yetu kwa upande wa ndege za abiria itakuwa salama sana. Pili, kuna eneo kula ya Mashariki chini ya Pemba kule na Zanzibar, ndege zilizokuwa zinapita pale zilikuwa zinaangaliwa na anga ya Kenya. Sasa baada ya kuweka rada hizi, ndege zile tutakuwa tunaziangalia sisi wenyewe na kuziongoza sisi wenyewe na tutaweza kupata mapato yanayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, kwenye viwanja vyetu huko kwenye madini na kwenye mbuga za wanyama, kuna airport ndogo ndogo nyingi. Sasa hivi hatuna uwezo wa kuziona, lakini baada ya kukamilika rada hizi nne, tutaweza kuona anga lote Tanzania na tutaweza kuangalia mali zetu inavyostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ni kwa upande wa usalama wa anga, lakini unaweza kuwa na usalama wa anga huko mzuri lakini kama viwanja vyako haviko vizuri, hiyo siyo sahihi. Kwa kulijua hilo sasa, Serikali tumeamua kwanza kujenga jengo la abiria pale kwenye Uwanja wa Dar es Salaam, JNIA, jengo namba tatu ambalo lenyewe litakuwa na uwezo wa kuchukua abiria milioni sita kwa mwaka. Jengo lenyewe litakuwa na uwezo wa kupaki ndege 21 kwa wakati mmoja, ndege aina ya Airbus 320. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jengo la abiria namba mbili tulililonalo sasa hivi lina uwezo wa kuchukua abiria milioni mbili tu na ndiyo ukienda Dar es Salaam kuanzia saa 7.00 mpaka saa 11.00, peak hours pale watu wamejaa; lakini mwisho wa mwaka huu, jengo la abiria namba tatu likikamilika, tunaamini tatizo hilo litaisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Mtwara tunataka kuifanya hub ya upande wa Kusini, tunapanua Uwanja wa Ndege wa Mtwara ambapo sasa ndege ya Airbus 320 inaweza kutua. Gharama ya ujenzi huo itakuwa takribani shilingi bilioni 53.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zitakazofanyika pale ni kutanua uwanja wa ndege na kuwa na urefu wa kilometa 2.8, kujenga jengo la kuegeshea ndege, kujenga vifaa vya kuongozea ndege, pia kujenga parking kwa ajili ya magari na barabara ya kuingilia kwenye kiwanja cha ndege. Hivi tunavyozungumza, mkandarasi wa kazi hiyo tumempata ambaye ni Beijing Construction Engineering Group. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kiwanja cha Ndege cha Mwanza, nia ya Serikali kufanya kiwanja hiki kiwe kiwanja cha kimataifa sasa. Tunatanua Uwanja wa Ndege wa Mwanza na umefikia kilometa 3.5. Ndege kama iliyotua Dar es Salaam jana, ninaamini na Mwanza inaweza kutua yaani ndege ya Airbus 380.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Mwanza kazi zinazofanyika, tunajenga jengo la kuongozea ndege, tunajenga eneo la maegesho ya ndege, tunakarabati taa za kuongozea ndege na tunaongeza ndege kwa ajili ya ndege na kuengesha ndege za abiria, mwisho tutahakikisha kwamba tunajenga jengo la abiria. Kwa sababu huwezi kuwa na kiwanja cha ndege kizuri kama kile bila kuwa na jengo la abiria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi inayoendelea sasa hivi inagharimu takriban shilingi bilioni 85. Tuna kazi vile vile huko Sumbawanga, tunaongeza urefu wa Kiwanja cha Ndege Sumbawanga ambapo tunaongeza kiwe na urefu wa kilometa 1.75 ambapo gharama huko itatumia shilingi bilioni 55.6. Pale tunajenga jengo la abiria, tunajenga eneo la kugeuzia ndege au maegesho ya ndege. Pia tutajenga taa za kuongozea ndege na huko vilevile Mkandarasi tumeshampata. Kazi tunayofanya sasa hivi ni kulipa fidia kwa wananchi wale wanaostahili fidia kama sheria inavyoelekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafanya kazi hiyo ya kujenga uwanja wa ndege Shinyanga ambao kazi inayofanyika ni kutanua uwanja wa ndege mpaka kufikia kilomita mbili na Mkandarasi yupo na pale tutajenga jengo la abiria. Vilevile gharama ya kiwanja hicho ni shilingi bilioni 49.
Mheshimiwa Naibu Spika, huko Songwe kazi inayoendelea sasa hivi ni kujenga jengo la abiria na gharama ni shilingi bilioni 11.5, lakini tunajua kilio cha muda mrefu cha watu wa huko Songwe ambao wanahitaji taa za kuongozea ndege, kwa vile sasa hivi tumempata mkandarasi ambaye atajenga taa ama ataweka taa kwenye kiwanja kile na taa hizo zitatumika kuongoza ndege saa 24 kwa siku, siku saba kwa wiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mradi kama huo huko Musoma wa kuhakikisha na kiwanja cha Musoma sasa ndege yetu ya Bombardier inaweza kutua na Mkandarasi tayari tumeshampata, isipokuwa sasa hivi tuko kwenye mazungumzo na tunaamini kwamba hivi karibuni tutamaliza kuhakikisha kazi hiyo inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna kazi vilevile ya kujenga Kiwanja cha Ndege cha Iringa kama nilivyosema, kwa sababu nia ya Serikali sasa ni kuboresha utalii kwenye Ruaha National Park na tunajenga barabara kutoka Iringa mpaka huko kwenye park ambayo ina urefu wa kilometa 104. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya uwanja wa ndege inandelea huko mkoa wa Geita na kama nilivyosema, nia kubwa ya Serikali ni kuhakiksha sasa tunaanzisha ule utalii kwenye Kanda ya Magharibi. Kama nilivyosema, kule kuna game reserve kubwa na utalii wa kule hasa sasa hivi ni utalii wa picha ambao ni utalii umechukua nguvu sasa duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimezungumzia viwanja vya ndege kwa ufupi, naomba nijikite kidogo kwenye Shirika la Air Tanzania. Nia ya Serikali kama nilivyosema huwezi ukawa na viwanja vya ndege, huwezi ukawa na anga lililokuwa salama kama huna shirika lako la ndege. Kwa kulijua hilo, Serikali imenunua ndege sita ambapo ndege tatu zimefika nchini na zinafanya kazi. Mwaka huu tunategemea vilevile ndege tatu ambazo zitawasili. Ndege ya kwanza ni Boeing 787 yenye uwezo wa kuchukua abiria 262 ambapo ndege hii itakwenda masafa marefu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndege nyingine mbili zenye uwezo wa kila moja kuchukua abiria 132 ni Bombardier CSeries 300 zitawasili ndege mbili hizi na tunaamini zitaanza kufanya kazi nzuri. Kwa kawaida huwezi kuwa na ndege moja ya masafa marefu na ikafanya kazi vizuri. Kwa vile kwenye bajeti hii tumeshapanga kununua ndege nyingine ya Boeing 787 ili tuwe na ndege mbili. Kwa mfano, tukiamua tunaenda Guangzhou, ndege moja inatoka Guangzhou inakuja Dar es Salaam na nyingine zinapishana, inatoka Dar es Salaam inaenda Guangzhou. Hivyo ndivyo utaratibu unavyokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, shirika letu la ndege limeanza kufanya kazi na linafanya kazi vizuri. Hivi tunavyozungumza, Shirika letu la Ndege linakwenda Dar es Salaam, hapa Dodoma na Wabunge wengi mnapanda ndege ya shirika letu la ndege, ni jambo zuri sana. Tabora, Kigoma, Mwanza, Bukoba, Kilimanjro, Zanzibar, Songwe na huko Hayahaya, Comoro. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni tutaanza safari za kwenda Mpanda, Tanga, Entebe huko Uganda na Bujumbura, Burundi. Kuanzia mwaka 2017 Shirikala la Air Tanzania Julai mpaka Machi, 2018 tumeweza kusafirisha abiria 150,518 ikilinganishwa na mwaka 2017 kwa kipindi kama hicho ambacho tulisafirisha abiria 104,207. Hili ni ongezeko la asilimia 46. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kumekuwa na kuongezeka kwa mapato ghafi ambayo tumeongeza kutoka shilingi bilioni 34.4 mpaka shilingi bilioni 43.8. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja hapa Wabunge wengi walipiga kelele kwamba Shirika la Air Tanzania halina business plan. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla Air Tanzania tunazo business plan ndiyo hizi hapa tunazotumia. Naomba mhakikishe kwamba tunakwenda kwa mipango na tunayo business plan. Business plan siyo msahafu, kila baada ya muda lazima ibadilishwe, kwa vile tutaendelea kuboresha business plan yetu hii kutokana na mahitaji ya soko na mahitaji ya Watanzania na wateja wetuwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja moja ilitokea juzi hapa; je, kwa nini ATCL isikodi ndege (leasing)? Kwa nini tunanunua ndege mpya?
Mheshimiwa Naibu Spika, kununua ndege mpya ni rahisi kama ndege hizo zinakuwa zinatumika kwa muda mrefu. Kampuni nyingi za ndege kwa mfano Kenya Airways, RwandAir, Ethiopia Airways, Emirates, zote zinanunua ndege mpya. Wana-lease ndege ama wanakodi ndege tu kwa sababu maalum ya msingi. Kama imetokea route mpya wanataka kwenda, ndiyo wananunua ndege mpya, lakini kawaida, wana-lease.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukinunua ndege mpya unapata faida kubwa kwa sababu discount ni kubwa. Hii inakupa faida kwenye uendeshaji wako wa ndege yako kwa sababu ndege mpya gharama zake za matengenezo ni ndogo ukilinganisha na ndege iliyozeeka. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge hili tulielewe.
Waheshimiwa Wabunge, nitatoa mfano mmoja, nita- compare ku-lease ndege na kununua ndege mpya na nitaangalia mfano kama nitakodi ndege ya Bombardier Q400 na nitaangalia ndege mpya ita-cost kiasi gani? Kuna njia mbili za kukodi ndege. Aina ya kwanza tunaita dry lease, maana yake unakodi ndege bila marubani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Njia ya pili tunaita wet lease. Ukichukua wet Lease maana yake unakodi ndege pamoja na marubani. Kitaalam, njia rahisi ya kukodi ndege ni dry lease ambapo unakodi ndege yako bila ya marubani, bila wahudumu na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bei ya wastani ya kukodi ndege kwa mwezi ni dola 200,000 mpaka 250,000 hiyo ya kwanza; ya pili, gharama ya matengenezo kwa mwezi, dola za Kimarekani 18,000. Kuna withholding tax ya TRA, ukikodi ndege unatakiwa ulipe dola 25,000 kwa mwezi. Jumla kwa mwezi mmoja unatakiwa angalau uwe na dola 300,000 ukikodi ndege. Kwa mwaka unatakiwa uwe na dola milioni tatu na nusu ukikodi ndege.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukichukua na bima unatakiwa uwe na dola milioni nne kwa mwaka mmoja. Sasa ndege za Air Tanzania kipindi chake cha kuishi (life cycle) ni miaka 35. Sasa kwa muda wa miaka 35 huo, ukiendelea kukodi ndege utatumia takriban dola milioni 140, lakini sisi tunanunua ndege moja ambayo list price yake ni kama dola milioni 35. List price nasema, ile price ambayo iko kwenye mtandao. Kwa vile kukodi ndege ni rahisi kuliko kununua; samahani kukodi ndege ni gharama kubwa kuliko kununua, ndiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tena, kukodi ndege ni gharama kubwa kuliko kununua kwa sababu gani? Narejea, kwa sababu ndege moja ya Air Tanzania ambayo tumenunua itaishi miaka 35. Ukikodi kwa muda huo utatumia dola za Kimarekani milioni 140, wakati ukinunua ndege mpya itakuwa gharama yako ni dola milioni 35. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa dola milioni 35 umenunua, dola milioni 140 umekodi, ipi faida? Mnataka Serikali iende wapi? Ikanunue au ikakodi? Waheshimiwa Wabunge, ninyi ndiyo mnawakilisha Watanzania, mnataka tukanunue au tukakodi ndege? Watanzania wametusikia na majibu wanayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sitazungumzia wet lease kwa sababu bei yake ni mbaya zaidi. Nitazungumzia hiyo tu, nafikiri hiyo hapo imetosha, tuendelee mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kawaida mashirika yanakodi ndege tu kama kuna matumizi ya muda mrefu kama nilivyosema. Kama leo imetokea route kwa mfano Dar es Salaam – Bombay na hatuna ndege, pale ndiyo unakodi ndege, lakini wakati huo huo unaagiza ndege yako. Ndivyo yanavyofanya mashirika ya ndege yote. Huwezi kwenda kukodi ndege kama unataka kutumia ndege muda mrefu. Kama nilivyosema Rwanda wana ndege nane, zote wamenunua. Sasa sisi tutafanya nini? Lazima tununue ndege na ndege kununua ni rahisi kuliko kukodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, niwaulize ninyi ni mashahidi, mmeshakuwa Bungeni huu ni mwaka wa saba sasa. Kila Mbunge akianza kuja Bungeni anafikiria kununua nyumba. Kwa nini hamfikirii kukodi nyumba kule mnakotoka? Kwa sababu kukodi nyumba ni bei ghai kuliko kununua. Ukizungumza kununua na kukodi huwezi ukalinganisha hata siku moja. (Makofi)
Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge, hili jambo liko hivyo, Serikali tumefanya maamuzi sahihi ya kununua ndege na tutaendele akufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja nyingine wanasema kwa nini tunanunua ndege kutoka makampuni mbalimbali? Hali hii itasababisha kuwa na gharama nyingi za matengenezo. Tukinunua ndege, tunaangalia ndege ambayo italeta faida kwa Shirika la Ndege, italeta faida kwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vigezo maalum vinatumika katika kununua ndege. Kigezo cha kwanza, unaangalia hiyo ndege yako inakwenda wapi? Yaani runway, kiwanja chako cha ndege kina urefu gani? Huwezi kwa mfano, leo unataka kwenda pengine Kiwanja cha Ndege cha Tabora ukasema upeleke jet engine, haiwezekani! Kile kiwanja kimetengenezwa kwa urefu wa kilometa 1.8, ni ndege ya turbo propeller engine ndiyo itakayokwenda tu, hiyo ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kigezo cha pili, unanunua ndege kutokana na hali ya hewa ya eneo lako. Hiyo ni muhimu sana na temperature ya kiwanja cha ndege, ndege yako inakokwenda. Eneo la tatu unaloliangalia ni mwinuko wa kiwanja cha ndege kule unakokwenda. Watu wengi tunakuwa na historia, tunapata simu au tunaambiwa kwamba Fastjet leo imekwenda Songwe na imeacha abiria.
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wengi hawajui kwa sababu gani inaacha abiria? Kiwanja cha Ndege cha Songwe kile wakati mwingine hali ya hewa inabadilika sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Fastjet haina uwezo wa kuchukua mzigo ule na abiria wale kwa wakati ule, ndiyo unakuta baadhi ya abiria wanaachwa na baadhi ya mizigo inaachwa. Ni kwa sababu kiwanja cha ndege kile wakati mwingine hasa mchana hivi hakiwezi kuchukua ndege ya Fastjet na mzigo wote. Kwa hiyo, ukichagua ndege yako lazima hiyo uiweke kwenye akili vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu unaangalia ndege yako, je, ndege hiyo inataka kwenda sekta gani? Kwa mfano, kama unataka kwenda Mumbai – India, inabidi utafute ndege ambayo itakupa faida kwa kwenda Mumbai. Huwezi kuchukua ndege ambayo ukienda Mumbai unapata hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, tunanunua ndege kutokana na kule tunakokwenda. Mfano mzuri, ni Ethiopian Airlines today.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri leo Ethiopian Airways, ni shirika kubwa lakini wana Airbus, Boeing na Bombardier. Wana ndege zote hizi. Wakija Dar es Salaam wale wanaosafiri na Ethiopian Airways, usiku inakuja Bombardier hapa. Kwa sababu wanaona need ya kuja Dar es Salaam au mahitaji ya Dar es Salaam ni Bombardier, siyo ndege nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kununua ndege tu kama unavyonunua njugu za aina moja, hapana. Unanunua ndege kutokana na soko lako na mahitaji. Hiyo ni muhimu sana Waheshimiwa Wabunge na Watanzania tuelewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunalofanya sisi Serikali au wanalofanya Air Tanzania ni jambo sahihi na hatukurupuki tu. Tunatumia utaalam wa kutosha na tunafanya maamuzi sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakupa mifano mizuri, Kenya Airways wana Airbus, Boeing, Embria halafu wana Fokker 50, kwa sababu huwezi kununua ndege za aina moja. Unanunua ndege kutokana na mahitaji na sekta kuhakikisha kwamba unapata faida. Otherwise, ukinunua ndege za aina moja, unataka Airbus, utafanya nini? Bukoba haiwezi kwenda Airbus kwa sababu Airbus hawana ndege ya propeller. Pemba, Tanga haiwezi kwenda Airbus. Tutawafanya nini Watanzania hawa sasa? Hatuendi hivyo bwana! Au Pemba naambiwa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja je, tumepata taarifa kuwa ATCL imeondolewa kwenye IATA kwa sababu ya madeni?
Waheshimiwa Wabunge, ATCL kweli iliondolewa kwenye IATA lakini siyo leo, ni mwaka 2008. Kazi tunayofanya sasa hivi Serikali ni kuirudisha ATCL kwenye IATA ambayo itawezesha kufanya booking popote pale duniani. Tunategemea kabla ya mwisho wa mwaka huu tutakuwa tumeingia kwenye mfumo, kwa sababu Serikali imejipanga na ninaamini Waheshimiwa Wabunge mtapitisha bajeti yetu tuhakikishe kwamba tunaingia kwenye mfumo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, kuna hoja nyingine inasema, Taarifa ya Ukaguzi wa CAG juu ya ATCL haijawasilishwa Bungeni ili ichambuliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika jitihada zake za kufufua ATCL ilibaini kuwa hesabu za ATCL zilikuwa hazijakaguliwa toka mwaka 2007 mpaka 2015. Kazi tuliyoifanya Serikali ilimuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu kufanya ukaguzi wa hesabu ya ATCL kuanzia mwaka 2007/2008 mpaka 2014/2015. Kazi hiyo imekamilika na ripoti imepelekwa kwenye Bodi ya ATCL. Kazi inayoendelea sasa hivi ni kufanya ukaguzi wa mwaka 2015/2016 na 2016/2017. Nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba ATCL inasimama. Lazima tuhakikishe kila senti tunayoingiza kwenye ATCL inatumika vizuri. Tukiweka shilingi tano tuhakikishe kwamba shilingi tano inatumika kwa maslahi ya ATCL na Watanzania. Kwa hiyo, naomba niwahakikishe Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali tumejipanga na tutalisimamia jambo hili vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo sasa kwenye sekta ya anga naomba niingie kidogo nizungumzie kwenye sekta ya usafiri wa nchi kavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote ni mashahidi kwamba Serikali ya Awamu ya Tano tunajenga reli ya kisasa ya kiwango cha standard gauge kutoka Dar es Salaam – Makutupora – Tabora – Isaka – Mwanza; Tabora – Kigoma; Tabora – Mpanda. Hiyo ndiyo central line ambayo ninaijua na Serikali tunaijua hiyo na tunaifanya hiyo kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanzia, tumeanza Dar es Salaam – Morogoro kilometa 300; Morogoro - Makutupora kilometa 422. Tunajenga treni ambayo katika nchi zetu hizi za East Africa ndiyo treni ya kwanza kwa sababu treni hii itakuwa inatembea na umeme, itakuwa na uwezo wa kwenda speed ya kilometa 160 kwa saa. Maana yake nini? Ni kwamba unatoka Dar es Salaam leo mpaka Dodoma kwa masaa yako mawili na nusu au matatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi zote za jirani, ukienda Kenya wanajenga treni yenye speed ya 120, ukienda Ethiopia 120; speed kama hii unaiona South Africa kwenye Gautrain speed 160 lakini wana kilometa 80 tu wao pale mjini tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumejipanga na gharama ya ujenzi huu kutoka Dar es Salaam mpaka Makutupora ni shilingi trilioni 7.016. Pesa ipo na wakandarasi wanafanya kazi. Awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro itamalizika mwezi Novemba mwakani. Awamu ya Pili itamalizika mwaka 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Sera na msukumo wa Serikali ya Awamu ya Tano ni kujenga reli ya kati na matawi yake yote kama nilivyosema. Tabora kwa upande wa Tabora – Kigoma tayari sasa hivi tunamalizia upembuzi yakinifu ambao unafanywa na kampuni ya COY kutoka Denmark. Tunahakikisha kwamba tunatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi huo. Hatuwezi kuanza ujenzi bila ya kuwa na feasibility study. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema kwa upande wa Tabora – Kigoma upembuzi wa kina, sehemu utakamilika mwezi Juni, 2018, miezi miwili inayokuja. Baada ya hapo ndiyo tutaanza kujipanga kuweza kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi. Huwezi kuanza ujenzi kama huna feasibility study. Utajua shilingi ngapi? Si utakwenda kupigwa tu? Waheshimiwa Wabunge, tumejipanga na tutaifanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna reli ya Dar es Salaam – Isaka – Rusumo – Kigali ambapo tunaanzia Isaka – Rusumo – Kigali kilometa 572. Reli hii imegawanyika sehemu mbili. Kuna Isaka – Rusumo ambapo Serikali ya Tanzania itajenga na Rusumo - Kigali Serikali ya Rwanda itajenga. Reli hii ina faida kubwa sana kwa sababu itahudumia mzigo wa Kigali
yenyewe, pia itahudumia mzigo wa Congo Kaskazini ambayo ni maeneo ya Goma na Bukavu.
Mhesimiwa Naibu Spika, kutoka Dar es Salaam leo mpaka Kigali ni masaa au ni kilometa 1,491. Kwa mwendo wa standard gauge au kwa kutumia standard gauge utatumia masaa 15, lakini mzigo ukitoka Mombasa, Malaba ambao unaenda Uganda mpaka Kigali ni kilometa 1,792 utatumia masaa 24 hasa ukiangalia reli ya Kenya ya mzigo ni kilometa 80 kwa saa. Sasa itakuwa jambo la kichekesho kwamba mtu wa Rwanda ambaye ana mzigo wake kutoka Dar es Salaam mpaka Kigali ambaye anaweza kutumia masaa kama 15 aende akapitie Mombasa ambako atatumia masaa 24, hiyo kwa biashara haiingii akilini hata siku moja. Mfanyabiashara yeyote anahakikisha kwamba anatumia njia fupi kusafirisha mzigo wake ambayo itampatia faida zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nimesema tutapata mzigo wa Congo hasa kule sehemu ya Kaskazini? Ni kwa sababu kutoka Kigali mpaka Bukavu ni kilometa 225 na barabara iko nzuri sana unaenda masaa matatu umefika, kwa vile mzigo ukitoka Dar es Salaam mpaka Bukavu utatumia masaa 18. Mzigo huo huo ukitoka Mombasa mpaka Bukavu utatumia masaa 27 kwa reli ya Kenya. Mfanyabiashara wa Congo especially eneo la Kaskazini hataweza kutumia reli ya Kenya, atatumia reli ya Tanzania kwa sababu ndiyo njia rahisi. Hii hata huhitaji tochi wala huitaji rocket science, ni simple, one plus one inakupa mbili. Wala haina mjadala hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa hivi Rwanda wanatumia Bandari ya Dar es Salaam na kuna zaidi ya tani milioni 1.1, asilimia 98 ya mzigo huu unapita barabarani, lakini unatumia bandari ya Dar es Salaam. Kule Bukavu Kongo kule kuna mzigo tani 772,000. Sasa ukichukua maeneo haya mawili, Rwanda na Kaskazini Kongo kuna takriban tani milioni mbili za mzigo ambazo zitapita Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, hii reli tunayoijenga itafika kwenye machimbo ya Nickel kule Kabanga ambapo kwenye machimbo yale kuna tani milioni 36.3, inahitaji reli hii inayotoka Dar es Salaam ikapita Isaka, Isaka ikaenda Rusumo, Rusumo - Kigali. Kabla hujafika Rusumo, unachepuka unakwenda Kabanga kwenye machimbo. Kwa hiyo, plan ya Serikali ni hiyo lakini wakati huo reli ya kati tunaijenga, hasa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, hii ya Kigoma nataka nayo niizungumze kidogo. Kutoka Kigoma tukijenga standard gauge mpaka Dar es Salaam, utatumia masaa kumi. Ni karibu Kigoma, lakini kutoka Kigoma mpaka Kalemie ni kilometa kama 120 kuvuka lile ziwa pale, lakini kwa meli ya mzigo utatumia masaa matano. Hii ni uzoevu kutoka Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukitoka Pemba kwenda Zanzibar ni distance hii tu, lakini kwa meli ya mizigo unatumia masaa manne au matano, wale mashahidi si ndio; kwa meli ya mzigo siyo meli ya abiria. Ukienda ukishusha na kupakia mzigo wako utatumia kama masaa manane kupakia na kuteremsha mzigo. Halafu kutoka Kigoma au Kalemie unaenda Lubumbashi kwa sababu mzigo mkubwa pale uko kwenye Kasanga kule, sehemu ya kule Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutoka Kigoma mpaka Lubumbashi ni kilometa 664 na bahati mbaya sana reli ya pale imekufa. Hii ya Tanzania ni nzuri kuliko ya pale, inaenda kilometa 25 kwa saa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mzigo ukipitia njia ya kule utachukua karibu masaa 41. Kule kuna tani milioni tatu sasa hivi ambapo Tanzania sisi tunapata tani 764,000. Mzigo mwingine unaenda Afrika Kusini, mzigo mwingine unaenda Durban, mwingine unaenda Namibia na mwingine unaenda Angola.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyosema, mahesabu siyo tatizo, tuko tayari kujenga reli ya kutoka Tabora mpaka Kigoma. Tunalosubiri ni hiyo feasibility study ifanyike ili tujue mahesabu kiasi gani, tuanze kutafuta fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na maoni kwamba Serikali tujenge reli kwa kutumia mfumo wa PPP. Ni kweli Serikali tunapenda sana mfumo wa PPP, ni mfumo mzuri, lakini katika historia ya ujenzi wa reli katika Afrika, hasa reli za standard gauge haijawahi kujengwa kwa kutumia mfumo wa PPP.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kenya wamechukua mkopo kutoka China; Ethiopia wamechukua mkopo kutoka China; Nigeria wanajenga standard gauge, wamechukua mkopo kutoka China; Morocco wamechukua mkopo na wao kutoka mabenki na Serikali. Kwenye miradi mikubwa kama hii, siyo rahisi kupata PPP kama watu wanavyofikiria. Serikali tuko tayari kushirikiana na mtu yeyote yule tuweze kufanya PPP lakini siyo rahisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niongelee sekta ya bandari, usafiri wa nchi kavu. Bandari yetu inafanya kazi vizuri, mzigo umeongezeka. Kama nilivyosema, kutoka mwezi Julai, 2017 mpaka mwezi Machi, 2018 tumesafirisha takriban tani milioni 9.822 ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2016/2017. Hili ni ongezeko la asilimia 14.6. Mizigo ya nchi za jirani mwaka huu tumesafirisha mizigo tani milioni 3.9 ikilinganishwa na tani milioni 3.1 mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mapato mwaka 2017 kuanzia mwezi Julai mpaka mwezi Desemba bandari wameweza kupata mapato ya shilingi bilioni 14.79 wakati matumizi yamekuwa shilingi bilioni 139, salio takriban shilingi bilioni 280. Kwa kipindi kama hicho mwaka uliopita kulikuwa na salio la shilingi bilioni 83 tu. Kwa vile bandari inafanya kazi vizuri na naomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wenzangu tuendelee kui-support Bandari ya Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo miradi mingi sasa hivi tunatekeleza Bandari ya Dar es Salaam tukianzia pale Dar es Salaam penyewe. Kwanza sasa hivi tunafanya ukarabati na kuongeza kina cha maji kutoka Gati Namba Moja mpaka Namba Saba. Vilevile tunajenga gati maalum sasa kwa ajili ya kupakilia na kupakulia magari ambapo kasi inaenda vizuri. Hivi karibuni tutaanza kutekeleza mradi mwingine kwa ajili ya kujenga eneo la kugeuzia meli na kuongeza gango la Bandari ya Dar es Salaam. Mradi unaoendelea hivi sasa unagharimu takriban shilingi za Kitanzania shilingi bilioni 377.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna kazi tunaendelea nayo huko Mtwara, tunajenga gati jipya watu wa Mtwara wanajua. Gati hilo lina urefu wa mita 300 na tutatumia takriban shilingi bilioni 137 kwa kazi ile. Kasi inaenda vizuri na tunategemea kazi itamalizika vizuri. Tuna kazi huko Lindi tunajenga gati la Lindi na limefiki asilimia 70. Tuna kazi huko Kigoma tunajenga Bandari za Kigoma tatu; Kigoma wenyewe, Ujiji na Tiberizi, zote tunazijenga. Tumetenga pesa bajeti ya mwaka huu na kazi nzuri inaendelea. Tuna kazi hivyo hivyo huko Mwanza inaendelea kuboresha gati yetu ya Mwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa usafiri wa majini, tunajenga meli mpya sasa huko Ziwa Tanganyika yenye uwezo wa kuchukua abiria 600 na tani za mzigo tani 400. Tunafanya kazi hiyo hiyo huko Lake Victoria ambapo tunajenga meli ya kuchukua abiria 1,200 na itachukua mzigo wa tani 200 na magari 25.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafanya kazi kama hiyo huko Lake Nyasa, tunajenga meli ya kuchukua abiria 200 halafu na tani 200 za mzigo. Vilevile tunafanya ukarabati wa MV. Liemba, MV. Victoria na Meli nyingine zote tunazifanyia ukarabati tuhakikishe kwamba sasa hivi zinafanya vizuri. (Makofi)
Mhshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kuboresha usafiri wa majini tunataka kujenga kivuko kwa ajili ya ndugu zetu wa huko Nyamisati na Mafia. Tayari tumetenga kwenye bajeti hii shilingi bilioni tatu kwa kujenga landing craft mpya ambayo itatumika kwa watu wa Mafia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hayo ndiyo maelezo machache kuhusu usafiri wa majini. Naomba nizungumzie kidogo kuhusu usafiri wa nchi kavu. Tokea juzi kulikuwa na mazungumzo mengi hapa kuhusu TARURA na maoni ya Waheshimiwa Wabunge tumeyapokea, tunaheshimu na tutayafanyia kazi. Naomba nitoe maelezo kidogo na ninyi mpate picha ya Mfuko wa Barabara unafanya kazi vipi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Fedha za Barabara kwa kawaida unagharamia miradi ya barabara kuu na barabara za mikoa ambazo zinasimamiwa TANROADS halafu barabara za Wilaya ambazo zinasimamiwa na TARURA. Inatoa fedha kwenye TARURA na TANROADS huku asilimia nafikiri 70 huku 30. Vilevile kuna vigezo maalum vinatumika katika kutoa pesa. Kigezo cha kwanza tunachotumia, tunaangalia urefu wa mtandao wa barabara; kigezo cha pili, tunaangalia je, barabara hizo ni za lami, changarawe au udongo? Kigezo cha tatu tunachoangalia, tunatumia hali ya barabara yenyewe ikoje (conditions)? Kigezo cha nne, tunatumia wastani wa idadi ya magari na uzito wa magari yanayopita kwenye barabara hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, TANROARD au mtandao wa barabara unaosimamiwa na TANROAD una jumla kilometa 36,257.97. Kati ya kilometa hizo, kilometa 9,264.57 ni za lami, kilometa 25,303.4 ni za changarawe na kilometa 1,690 ni za udongo. Mtandao wa barabara unaosimamiwa na TARURA una jumla ya kilomita 108,946.19. Kati ya kilometa hizo, kilomita 1,449.55 ndizo za lami ukilinganisha na TANROADS wenye kilometa 9,000 za mahitaji kwa kutengeneza au matengenezo ya barabara ya TANROADS ni makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA vilevile inahudumia kilometa 24,405 za changarawe pamoja na kilometa 85,091.24 za udongo. Kwa vile ukilinganisha tu mtandao TANROADS wanasimamia barabara kubwa sana za lami kuliko TARURA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, matengenezo ya barabara za lami ni gharama zaidi kuliko matengenezo aina nyingine ya barabara. TANROADS yenye kilometa 9,264 za lami inahitaji fedha nyingi kuliko TARURA yenye urefu wa kilometa 1,449.55 za lami kwa sasa. Aidha, upana wa barabara zinazosimamiwa na TANROADS ni mita 8.5 mpaka mita 9.5. Upana wa barabara unaosimamiwa na TARURA ni mita 4.5 mpaka mita 6.0. Hii inafanya TANROADS ihitaji fedha nyingi kwa ajili ya matengenezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, idadi ya magari yanayotumia barabara kila siku, barabara kuu za mikoa idadi ya magari ni kati ya 300 mpaka 52,000. Ukichukua barabara ya New Bagamoyo Road ndiyo hayo. Wakati barabara za Wilaya nyingine ni kati ya magari matano mpaka 50 kwa siku. Kwa hiyo, wingi wa magari husababisha barabara kuharibika zaidi na kuhitaji zaidi fedha za matengenezo zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, uzito wa magari yanayopita katika barabara zinazotumika na TANROADS ni tani 55 wakati barabara za Wilaya zote ni tani 10. Uzito wa magari husababisha barabara kuharibika haraka kwa vile barabara inayosimamiwa na TANROADS zinahitaji pesa nyingi. Tumetoa ushauri ambao tunasema, tumejaribu kuangalia ushauri wa kuongeza tozo la mafuta kuangalia kama tutapata pesa zaidi kwa ajili ya TARURA.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunasema tutafute vianzo vipya ikiwa ni pamoja na tozo ya maegesho ya magari mjini, ukaguzi wa magari, tozo ya magari mazito, tozo ya barabara na tozo ya matumizi ya barabara kulingana na uzito na umbali wa magari. Hivi ndiyo baadhi ya vyanzo vyote ambavyo tunapendekeza tuone jinsi gani tutaweza kuongeza pesa za TANROADS na pesa kwa ajili ya kukarabati barabara za TARURA.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema leo asubuhi Mheshimiwa Naibu Waziri, tunazo barabara nyingi tunazijenga kwa kiwango cha lami hivi sasa. Barabara tunazojenga kwa kiwango cha lami ambazo nyingi zinaunganisha mikoa na mikoa kwa mfano sasa hivi tunajenga barabara kutoka Sumbawanga – Matai – Kasanga Port yenye urefu wa kilometa 112; tunajenga barabara ya Ushirombo - Lusahunga yenye urefu wa kilometa 110; barabara kutoka Kidatu - Ifakara yenye urefu wa kilometa 65; barabara kutoka Tabora - Sikonge yenye urefu kilometa 30; tunajenga barabara kutoka Usesula - Komanga yenye urefu wa kilometa 115.5; barabara kutoka Komanga mpaka Kasinde yenye urefu wa kilometa 112.8; barabara ya kutoka Kasinde - Mpanda kilometa 111.7.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunajenga barabara inayotoka Mara kwenda Arusha - Makutano - Sanzate kilometa 50; barabara kutoka Waso mpaka Sare Junction kilometa 50; barabara ambayo inatoka Mpanda mpaka kuelekea huko Kigoma ambayo tumeanzia kwanza Mpanda - Vikonge kilometa 35; barabara kutoka Kisole - Bulamba kilometa 50, barabara kutoka Maswa - Bariadi kilometa 49.5; barabara kutoka Kidahwe - Kasulu kilometa 63; barabara kutoka Nyakanazi - Kakonko kilometa 50; barabara kutoka Nduta – Kibondo - Kabingo inayojumuisha barabara ya kupita Kibondo Mjini kilometa 87.7 na tunajenga barabara ya Uvinza - Malagarasi yenye kilometa 51.1.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara vilevile itaanza maandalizi ya ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara kutoka Tanga mpaka Pangani yenye urefu wa kilometa 50; huko Geita- Bulyanhulu Junction kilometa 58.3; barabara kutoka Bulyanhulu Junction mpaka Kahama kilometa 61.7; tunatayarisha ujenzi wa barabara kutoka Kazilambwa mpaka Chagu kilometa 42; tuna mpango wa kujenga barabara ya kutoka Ludewa – Kilosa kilometa 24; tuna mpango wa kujenga barabara kutoka Norangi – Itigi - Mkiwa kilometa 56.9; na tunajenga barabara kutoka Lusaunga - Lusaumo kilometa 91.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna mpango wa kujenga barabara ya Kibaoni - Stalike kilometa 71; tuna mpango wa kujenga barabara kutoka Vikonge - Mangunga mpaka Uvinza kilometa 159; tunafanya upanuzi wa barabara ya kwenda Kiwanja cha Ndege Mwanza na tuna mpango wa kujenga barabara ya kutoka Nyangunge mpaka Simiyu - Mara - Boda yenye urefu wa kilometa 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna miradi mingi siwezi kuitaja yote, lakini tuna kazi kubwa tunahakikisha kwamba mikoa yote ya Tanzania tunaifungua ili kuhakikisha Watanzania wanapata miundombinu hii ya kisasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mnavyojua pia tunajenga huko Dar es Salaam TAZARA flyover ambayo tutatumia takribani shilingi bilioni 99. Tunajenga Ubungo interchanges ambayo tunatumia takriban shilingi bilioni 177; tunajenga daraja huko Momba, tunajenga daraja huko Magara, Sibiti, Lukuledi, Wami Juu, Simiyu, Sukuma mkoani Mwanza na daraja la Salenda Dar es Salaam; tunafanya feasibility study kwa ajili ya daraja la Mtera, Kigogo Busisi na Malagarasi Chini huko Kigoma.
Mheshimiwa naibu Spika, tuna miradi mingi sana ya barabara ambayo yote mnaweza kuiona kwenye kitabu changu cha hotuba ya bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya mawasiliano muhimu sana kwa nchi yetu. Sekta ya mawasiliano ndiyo uchumi wa nchi yetu, ni maendeleo na ndiyo maisha ya Watanzania. Bila mawasiliano kwa kweli maisha kidogo yanaweza kuleta shida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia Desemba, 2017 tulikuwa na wateja wa simu takribani milioni 50; watumiaji wa internet takriban milioni 23. Watanzania ambao wanatuma pesa kwenye mitandao mbalimbali takribani kuna akaunti milioni 22. Pesa zilizotumwa kwenye mtandao mwaka 2017 ni takriban shilingi trilioni 104.3. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kama nilivyosema, sekta ya mawasiliano ni muhimu sana na ni sekta ambayo inapeleka uchumi wetu kwenye hali ya juu. Kwa upande wa mawsiliano vijijini kama Naibu Waziri alivyosema leo, kwa kipindi tulichopita tumejenga Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umepeleka mawasiliano kwenye Kata 551, vijijini 1,954.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepeleka mawasiliano vijijini pamoja na makampuni yote takribani vijiji 5,751. Mwaka 2018/2019 utakuwa ni mwaka ambao utaleta maendeleo makubwa kwenye sekta ya mawasiliano. Naomba tu Watanzania waitumie miundombinu hii kwa maslahi ya maendeleo, wasiitumie mindombinu ya mawasiliano kwa kupeleka message za uchochezi, kupeleka picha chafu na kufanya ulaghai na mambo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mbele yenu tena na kutoa mchango wangu katika hoja hii iliyopo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukushukuru wewe mwenyewe binafsi, Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wote wa Bunge kwa uwezo na umahiri mkubwa mnaoonesha katika kuliendesha Bunge letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwa umakini wake wa kusimamia shughuli za Serikali. Aidha, napenda kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliopata fursa ya kuchangia hoja yetu iliyowasilishwa hapa Bungeni. Kwa kweli michango ni mizuri na imejaa hekima kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, michango na changamoto nyingi zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge kuhusu Sekta ya Maji. Hii ni kwa sababu Sekta ya Maji kama tunavyofahamu maji ni uhai, maji ni afya, maji ni kilimo, maji ni uchumi, maji ni viwanda, maji ni ustaarabu na maji ni kila kitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba yangu imechangiwa na wachangiaji 173 ambapo wachangiaji 59 wamechangia kwa maandishi na wachangiaji 88 wamechangia kwa kuzungumza. Kama nilivyosema hapo mwanzoni, michango ya Waheshimiwa Wabunge wote ilikuwa ni mizuri sana na ilivyosheheni mapendekezo, ushauri, busara na namna bora ya kuendeleza Sekta ya Maji. Aidha, siyo rahisi kujibu hoja zote za Waheshimiwa Wabunge kwa kina na kutosheleza kwa muda huu mfupi nilionao. Naahidi kwamba hoja zote tutazichukua, tutazifanyia na tutazijibu kwa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite kwenye maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ambalo nitaanza kujikita ni usimamizi wa miradi. Naamini kwamba changamoto namba moja sasa hivi ya Wizara ya Maji ni usimamizi wa miradi. Tumekuwa na changamoto kubwa ya usimamizi wa miradi ya maji na changamoto hii imeanzia Halmashauri kwa Engineer wa maji, ikaja kwa Engineer wa Mkoa mpaka ikafika Wizarani, ni changamoto kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hii kuna maeneo mawili; eneo la mwanzo la usimamizi linahusiana na viwango na ubora wa miradi. Changamoto hii ni kihistoria, ilianzia toka mwaka 2010; miradi mingi iliyojengwa kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ilijengwa kwa viwango vya chini. Miradi hiyo ilitekelezwa kati ya mwaka 2010 – 2015, tume nyingi zimeenda kuchunguza miradi hii na imethibitisha kwamba miradi hiyo ilijengwa chini ya viwango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingi ya kipindi hicho ndiyo yenye changamoto ambazo sasa tunapambana nazo na ni lazima tuna jukumu na tumepewa jukumu la Tanzania lazima tutatue tatizo hili na tuwapelekee Watanzania maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi iliyoanza kujengwa mwaka 2017 kwa kiasi kikubwa changamoto hizi zimepungua. Hii imetokana na ufuatiliaji wa karibu sana wa viongozi wa Wizara ya Maji, ninyi nyote mmekuwa mashahidi, kila leo mnaona viongozi wa Wizara ya Maji wanatembelea maeneo mbalimbali ya nchi yetu kuangalia miradi ya maji. Nawashukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na viongozi wote kwa kufanya kazi hii ya kuhakikisha kwamba miradi ya maji tunayojenga inaenda kwa viwango vinavyokubaliwa ili Watanzania waweze kupata maji safi na salama, hilo eneo la mwanzo ambalo kwa kiasi kikubwa sasa hivi wakandarasi wameanza kuogopa na tumeweza kwenda nao vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo ni tatizo na bado ilikuwa ni changamoto ni gharama halisi ya miradi ya maji. Gharama ya miradi ya maji iko juu sana, huku ndiko wakandarasi wengi wanakojificha na kupiga pesa za Serikali. Hii inafanywa kwa ushirikiano mkubwa kati ya wakandarasi wetu, Halmashauri, Wakurugenzi, Wahandisi wa Maji Mikoani, Wahandisi wa Maji wa Wizara ya Maji yenyewe, Idara ya Manunuzi, Wizara ya Maji pamoja na Mfuko wa Maji. Kumekuwa na mtandao mkubwa sana ambao unaanzia kule kwenye Halmashauri, Mkoani hadi Wizarani, hili jambo halikubaliki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mtandao huu, Wahandisi wetu wa Maji wa Wilaya wanatengeneza engineering estimation au makisio ya kihandisi ambayo si sahihi, wanaweka gharama za juu. Ubaya zaidi wanajaribu kuwapa wakandarasi wazijue kabla ya tenda. Hili ni jambo baya, siyo uadilifu na halikubaliki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mifano miwili ambayo ipo ambayo inaonesha jinsi gani pesa za Serikali zinaliwa kwa mtindo huu. Sitataja jina la mradi lakini kuna Project A (Mradi A), mradi huu ulitangazwa, mkandarasi akaomba na akatoa bei yake ni shilingi bilioni 4.5. Sisi baada ya kupitia mradi huu vizuri tukaona unaweza kujengwa kwa bilioni shilingi 2.4.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuchambua vizuri, nikiwaonyesha hapa, hii ndiyo bei ya mkandarasi nah ii ndiyo bei tuliyofanya uchambuzi wetu, baada ya kupitia tuliona kwanza kwenye mabomba alisema bei ya mabomba ni shilingi bilioni 2.77, sisi baada ya kufanya utafiti tukaona bei ya bomba ni shilingi bilioni 1.13, karibuni mara mbili. La pili, tumeenda tena tukaangalia baadhi ya maeneo kwa mfano ujenzi wa tenki yeye ame-quote milioni 488, sisi tuka-quote milioni 771. Sasa huku ndiko wakandarasi wengi wanakopiga pesa na mtandao huu unaanzia Halmashauri mpaka Wizarani. Watu wengi wanapiga hela kwa kutumia utaratibu huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumaliza hapo mkandarasi huyu tukasema hatufai. Tulilofanya tukasema sasa pesa ile ambayo tulikuwa tumpe mkandarasi huyu tutumie utaratibu wetu sisi tukajenge kazi hiyohiyo kwa shilingi bilioni 2.5 ama 2.6 lakini pesa nyingine tupeleke kwenye miradi mingine, kwa mfano tujenge mradi wa Kamwanda kule kwa Mheshimiwa Serukamba ambao ni shilingi milioni 811. Pesa iliyobaki tunaweza pia kujenga mradi wa Horohoro ambao ni takribani shilingi milioni 350. Pesa ambayo tume-save kwenye mradi huu kwa kutokumpa kazi mkandarasi yule tunaweza kujenga mradi wa Tunduma kwa shilingi milioni 500. Kwa kweli watu wengi wanapiga pesa kwenye miradi ya maji kwa njia hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukusimama hapo, tulikwenda kuchukua mradi wa pili, mkandarasi huyu aliomba kazi hii kwa shilingi bilioni 1.6, baada ya kufanya mahesabu vizuri tukaona kazi ile inaweza kujengwa kwa shilingi takribani milioni 800 mpaka bilioni 1, hapa kuna takribani shilingi milioni 600 zingeliwa na mkandarasi. Pesa hizo tukizitumia tunaweza kuchimba takribani visima virefu 30 ambapo Wabunge wengi hapa wana shida ya visima hivyo. Kwa kweli kuna changamoto kubwa Wizara ya Maji na tumejipanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuona tatizo hilo, tukaenda tena mbali tukaangalia miradi kama mitatu, minne tukaona tatizo ndiyo hilohilo. Sasa tulifanya nini kama Wizara. Kuna mambo ya msingi tulifanya, hatua ya mwanzo tuliyochukua, tulifuta vibali vya miradi yote husika na tukaja na utaratibu mpya wa kutafuta mkandarasi na mkandarasi huyu tutatumia Mamlaka yetu ya Maji ambayo itafanya kazi nzuri na kwa bei nafuu na kwa muda mfupi kuliko mkandarasi yule aliyekuwa amependekezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya pili tuliyochukua ni kuondoa watumishi 14 ndani ya Wizara ya Maji kwa muda wa wiki mbili. Watumishi watano (5) tumewaondoa Idara ya Maji Vijijini; watumishi watatu (3) Idara ya Manunuzi au Sekta ya Manunuzi; tumemuondoa Mkurugenzi wa Manunuzi, Msaidizi wake na mtumishi mmoja; tumeondoa watumishi watatu kwenye Mfuko wa Maji na Bodi yote ya Mfuko wa Maji tumeiondoa kwa sababu hivi ndivyo vilikuwa vichochoro vya kupigia pesa za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kuwa tumejipanga kusafisha. Ni lazima wafanyakazi wote wa Wizara ya Maji wabadilike, lazima wafanye kazi kwa uadilifu na weledi mkubwa. Wakati wa kupiga Serikali sasa imetosha, haikubaliki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo tumefanya ni kuimarisha idara mbalimbali za Wizara ya Maji. Tumeimarisha Idara ya Maji yenyewe kwa kuunganisha maji vijijini na mjini; tumeboresha Kitengo cha Manunuzi, tunaboresha Mfuko wa Maji na tunaboresha Kitengo cha Usanifu ambapo penyewe pana matatizo makubwa. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla kuwa Wizara ya Maji itabadilika, lazima ibadilike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kila siku watu wanakaa ofisini wanapiga pesa lakini Watanzania wetu wanapata taabu ya maji safi na salama, hii haiwezekani. Imetosha, lazima tujipange, aliyekuwa hawezi kufanya kazi hii anaondoka. Kama ni Mkurugenzi, kama ni nani, wote wanaondoka, lazima Wizara ya Maji inyooke. (Makofi/ Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuboresha hilo, tumesema sasa Wizara ya Maji lazima tuje na mpango wa kujua gharama za miradi ya maji. Kwa mfano, tunalofanya sasa hivi tunataka kujua unit cost kwa kila mradi, ukijenga tenki pengine la lita milioni mia moja itatumia shilingi ngapi, tunataka kuleta kitabu ambacho kitaonesha bei halisi za mradi wa maji ambapo Wahandisi wetu wa RUWASA na wengine wote watatumia kitabu hicho kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapata thamani ya pesa tunayoingiza kwenye miradi ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo tunafanya maboresho makubwa ni uanzishwaji wa RUWASA (Wakala wa Maji Vijijini. Kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyosema, kama Waheshimiwa Wabunge walivyosema kwamba Wahandisi wa Halmashauri ni tatizo, sasa tunakuja na RUWASA, wafanye kazi pale, tuhakikishe kwamba tunapata thamani ya miradi tunayotekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo kila Mhandisi anayetoka Halmashauri tutampeleka RUWASA. Kazi tutakayoifanya tutahakikisha tunafanya upekuzi wa kina kwa Wahandisi wote wanaotoka Halmashauri, hatutaki kupeleka watu wapigaji kwenye RUWASA hii mpya tunayoianzisha. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, tatizo la maji litamalizika na tumejipanga kuhakikisha kwamba tatizo la maji linakwisha na wananchi wetu wanapata maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine nalotaka kuchangia ni kuhusu upatikanaji wa fedha. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, Fungu Na.49 - Wizara ya Maji, iliidhinishiwa bajeti ya maendeleo shilingi bilioni 673.214. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2019, jumla ya shilingi bilioni 343.486 zilipokelewa. Tarehe 30 Aprili, 2019, Wizara ilipokea tena shilingi bilioni 56.26 ambapo shilingi bilioni 12 ni za Mfuko wa Maji na shilingi bilioni 44 ni pesa kutoka Serikali Kuu ama Hazina. Mpaka kufikia tarehe 30 Aprili, 2019, Wizara ilipokea shilingi takribani bilioni 400.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenendo wa madeni ya wakandarasi. Kama alivyoongea Naibu Waziri, hadi kufikia mwezi Aprili, Wizara ilikuwa na certificates za miradi mbalimbali yenye thamani ya shilingi bilioni 78.67. Baada ya kupokea fedha hizo, shilingi bilioni 56.256 ambazo kwa sasa tunaendelea kuwalipa wakandarasi hao, deni la certificates limepungua kwa asilimia kubwa sana na certificates tunazozipata sasa hivi tunazifanyia uhakiki ili tuhakikishe nazo zimeenda sawa baadaye tuanze kuzilipa mwezi Juni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kukuhakikishia wewe na Bunge lako Tukufu itakapofika mwezi Juni wakandarasi wote watakuwa hawatudai. Hata hivyo, naomba muelewe kwamba kila siku wakandarasi wanazalisha certificates kwa sababu kazi zinaendelea site, lakini tumejipanga tuhakikishe kwamba kila certificate inayokuja tunailipa lakini baada ya kuhakiki kwa sababu Wizara ya Maji kuna historia ya upigaji, lazima tujipange tuhakikishe kwamba tunakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine nalotaka kulizungumza, Mheshimiwa Naibu Waziri ameligusia kidogo, ni tozo kwa watumiaji maji chini ya ardhi (tozo ya uchimbaji visima). Kupitia Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji, Na. 11 ya mwaka 2003, kifungu cha 96 na Kanuni zake kinanipa mamlaka ya kusimamia tozo za uchimbaji visima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Mheshimiwa Spika alizungumza hili kwa masikitiko makubwa na sisi kama Serikali tulilisikia. Waheshimiwa Wabunge mlilizungumza jambo hili la tozo ya uchimbaji wa visima kwa masikitiko makubwa, tulilisikia. Watanzania wanyonge wamelalamikia jambo hili tumelisikia. Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, imesikia kilio cha wanyonge, cha Watanzania kuhusu tozo ya watumiaji wa visima vya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia leo Serikali imefuta tozo ya visima vya maji kwa watumiaji binafsi kwa matumizi ya nyumbani. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena; kuanzia leo Serikali imefuta tozo ya visima vya maji kwa watumiaji binafsi kwa matumizi ya nyumbani. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania hawa lazima wapate maji safi na salama. Hhatuwezi kuona Watanzania wetu wanalalamika na wanapata shida, Serikali tunafanya kila tunaloweza kuhakikisha kwamba matatizo haya tunayaondoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni huduma za usambazaji wa maji vijijini. Sera ya Taifa ya 2002 inasema waziwazi Watanzania wapate huduma ya maji si zaidi ya mita 500 kutoka maeneo wanayoishi. Vilevile Ilani ya Chama cha Mapinduzi inasema kwamba itakapofika mwaka 2020, Watanzania waishio vijijini wapate maji asilimia 85.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tumejipanga, tunaendelea kutekeleza miradi mbalimbali. Hadi hivi sasa jumla ya miradi 1,659 yenye vituo vya kuchotea maji 131,370 imejengwa. Kati ya vituo hivyo, vituo 86,780 vinafanya kazi na vina uwezo wa kuwahudumia wananchi milioni 25.359. Aidha, miradi 653 yenye gharama ya takribani shilingi bilioni 501 inatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kujipanga hivyo, Serikali inatekeleza miradi mingine kwa mfano tuna mradi wa maji vijijini ambao unagharimu takribani shilingi bilioni 46.47 ambapo mradi huu tunaita payment by result. Tuna mradi mwingine ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia ambapo gharama yake ni takribani shiligi bilioni 806 na kazi yake kubwa ni kupeleka huduma ya maji vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ya miradi ya vijijini ni kama ifuatavyo. Kama nilivyosema mwanzo, miradi mingi iliyojengwa kati ya 2010 - 2015 imejengwa chini ya viwango. Kazi yetu sisi kama Serikali na kama Wizara ni kuendelea kuhakikisha kwamba miradi hii tunaisawazisha ili wananchi wapate huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo lina changamoto ni uharibifu wa mazingira. Hali ya tabianchi inabadilika kila siku na baadhi ya maeneo yana changamoto sana. Tunachimba kisima leo baada ya miaka kumi kisima hicho kimekauka. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kuwaomba Watanzania wenzangu tupambane na hali hii ili kuhakikisha kwamba miundombinu tunayojenga hii inakuwa endelevu ili tuweze kutumia sisi wenyewe pamoja na vizazi vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine iko kwenye usimamizi wa Jumuiya za Maji. Utakumbuka Bunge lako Tukufu hapa lilipitisha Sheria ya Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira, Na. 5 ya mwaka 2019, ambayo yenyewe imeeleza kwa kina uboreshaji wa jumuiya hizi za watumia maji. Tunaamini tukiweka mambo haya vizuri, miradi ya maji kwa kiasi kikubwa itafanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite kwenye eneo la huduma ya maji mijini. Kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi imeeleza waziwazi ifikapo mwaka 2020 wananchi watakaopata maji kwenye miji mikuu ya mikoa lazima iwe asilimia 95. Hali ikoje leo hii? Hivi tunavyozungumza kuna baadhi ya maeneo watu wanapata maji asilimia 97, 90, 86, lakini kwa wastani watu wanaopata maji kwenye miji mikuu ya mikoa ni asilimia 87. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejipanga kuhakikisha kwamba tutafikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2020. Katika kujipanga huko kazi ya mwanzo tuliyoifanya ni kuhakikisha tunaboresha utendaji kazi wa Mamlaka zetu za Maji, hilo la kwanza, kwa sababu kama mamlaka za maji zitalegalega hatutaweza kufikia malengo tuliyojiwekea. Kwa hiyo, kazi ya kwanza tuliyojiwekea ni uboreshaji wa utendaji kazi wa Mamlaka zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo jambo la kwanza tulilofanya ni kuweka performance contract (mikataba ya kazi) baina ya Waziri na Mwenyekiti wa Bodi, baina ya Katibu Mkuu na Mtendaji wa Mamlaka, lazima tuwapime kutokana na utendaji wao wa kazi. Hatuwezi kuendelea biashara kama kawaida, watu wanafanya wanavyotaka, watu wanakaa hawafanyi kazi, hili tutalisimamia na mimi ntalisimamia kwa nguvu zangu zote. Mtendaji Mkuu yeyote ambaye hatafanya kazi kama tulivyokubaliana, tutamuondoa. Lazima Mamlaka za Maji zibadilike, lazima Wizara ya Maji ibadilike, lazima Watanzania sasa waone matokeo makubwa ya Serikali yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumefanya maboresho kwenye ulipaji wa bili za maji. Kuna changamoto kubwa kwa baadhi ya maeneo ya watu kutokulipa bili za maji. Tumeamua sasa tulete prepaid meters, mita za kielektroniki ambazo tumezifunga watu waweze kupata huduma nzuri na walipe maji kutokana na matumizi wanayotumia. Kwa sababu kulikuwa na mchezo kwa baadhi ya Mamlaka kuibia wananchi lakini ukitumia prepaid meter sasa utalipa kutokana na matumizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili tutalisimamia na tutahakikisha kwamba tunafunga prepaid meters maeneo mengi. Bado prepaid meter bei yake iko juu lakini tutajitahidi kama tunavyoweza tuhakikishe kwamba tunawafungia wananchi wengi ili waweze kupata huduma nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeamua kwenye Mamlaka hizi kuboresha miundombinu ili kupunguza kwa kiasi kikubwa upotevu wa maji. Kuna upotevu wa maji kwenye maeneo mengi sana na tumeamua kujipanga kuhakikisha kwamba upotevu wa maji unapungua kwa asilimia kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo tumekubaliana na Mamlaka za Maji, kwenye mapato yao lazima kila mwezi watenge asilimia 35 ili waende kujenga miundombinu ya maji. Utaratibu uliokuwepo zamani Mamlaka zote za Maji zikitaka kujenga mradi zinakuja Wizarani kuomba pesa kwenye Mfuko wa Maji. Baada ya kuingia Wizarani nikawaambia hii haiwezekani, ninyi mnafanya biashara, mnauza maji, lazima muanze kujenga miundombinu ya maji na tumejipanga na hii tunaisimamia kwelikweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoa mfano, DAWASA (Mamlaka ya Maji ya Dar es Salaam) tayari wanajenga miradi mbalimbali kwa kutumia pesa zao za ndani. Mradi wa kwanza ni ule wa Chalinze – Mboga – Bagamoyo ambao unatumia takribani shilingi bilioni 10.7. Mradi wa pili ni Kibamba – Kisarawe ambao vilevile unajengwa kwa pesa za ndani za Mamlaka ya Maji DAWASA na tunatumia takribani shilingi bilioni 10.67. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi mingine kwa mfano usambazaji wa maji maeneo ya Kiwalani, Madale, Usukumani na mengine mengi, kote huko tunapeleka huduma ya maji kwa kutumia pesa za Mamlaka zenyewe. Pia tuna mradi ule wa visima Kimbiji, tayari tumeshatangaza tenda ambapo tutatoa maji kutoka visima vyetu vya Kimbiji kuleta pale Kigamboni na tunajenga matenki na kazi hii itafanywa kwa kutumia pesa za ndani za DAWASA. Hatuwezi kuendelea tena kuanza kuzibeba Mamlaka hizi za maji wakati zinafanya biashara, zinafanya kazi, lazima tubadilike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo jingine ambalo nataka kulizungumzia ni miradi ambayo tunaitekeleza ili kufikia malengo tuliyopewa na ilani ya Chama cha Mapinduzi. Hivi ninavyozungumza, tunatekeleza mradi wa maji kutoka ziwa Victoria kwenda Nzega Igunga, Tabora, Uyuwi, ambao unagharimu takribani shilingi bilioni 605. Tunatekeleza vile vile, mradi wa maji wa Arusha ambao unagharimu takribani shilingi bilioni 525.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatekeleza mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda kwako wewe Mheshimiwa Mwenyekiti Bariadi, Busega, Itilima, ambao utagharimu takribani shilingi bilioni 300 na mkataba ulisainiwa hivi juzi. Tuna changamoto kwenye miji mingi hapa Tanzania Serikali kwa kulitambua hilo, Serikali kwa mapenzi makubwa yaliyonayo kwa wananchi wake inatekeleza mradi wa miji 29 ambao unafadhiliwa kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka Indi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu utagharimu takribani shilingi tirion moja nukta mbili, miji ambayo itanufaika na mradi huu kwanza ni muheza, Wanging’ombe, Makambako, Kianga, Songea, HTM, Korongwe na handeni, Njombe Mugumu Kilwa Masoko, Geita, Chunya, Makonde, Manyoni, Sikonge, Kasulu, Lujewa, Chato, Singida Mjini, Kiamboi, Mpanda, Chemba, Mafinga, Urambo, Kaliuwa, Pangani, Ifakara Rorya, Tarime, Chamwino na Nanyumbu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi inaendelea vizuri na tunategemea wiki inayokuja tutasaini na mkandarasi ambaye atapitia usanifu na kutayarisha makabrasha ya zabuni nitawaalika Wabunge wote ambao wanapitiwa na mradi huu waje washuhudie sherehe hii kwa sababu ni jambo muhimu katika maisha ya watanzania wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kulifuatilia hili, tutampa mkandarasi huyu au mtaalam mshauri huyu miezi miwili aweze kumaliza usanifu na kutupatia makabrasha ya zabuni na tunategemea mambo yote yatakwenda vizuri mkandarasi atakuwa kwenye site bayana ya mwezi Septemba na mwezi Oktoba ili aanze kazi ya kujenga miundombinu kwenye maeneo mbalimbali hapa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunao mradi wa kupeleka maji miji sita ambayo ni Mwanza, Musoma, Bukoba, Misungwi na Lamadi ambao unagharibu takribani shilingi bilioni 276. Tunao mradi wa kiistoria, mradi wa Mugango Kiabakari Butiama, ambao utagharibu takribani shilingi bilioni 30.69. Mradi huu umezungumzwa kwa muda mrefu, lakini sasa tulishafikia mahala pazuri tulishapata mkandarasi tumeshaandika BADEA kwa no objection BADEA imeshatoa un objection Kuwait fund imeshatoa un objection sasa tuna subiri no objection kutoka Saudi fund na tunategemea hivi karibuni watatuletea na mkandarasi ataanza kufanya mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwahakikishie ndugu zangu wa Mugango, Kiabakari, Butiama, na Musoma kwa ujumla kwamba itakapofika mwisho wa mwezi wa sita tunategemea mkandarasi awekwe site tutatuwe tatizo la maji ambalo linawakabili. Pia tunayo miradi mingi sana tuna mradi pale Dar es Salaam, mradi wa wasambaji maji ambao unagharimu takribani shilingi bilioni 197.8.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijikite kidogo na eneo ambalo ya miradi ambayo imejengwa kutoka mwaka 2010 mpaka 2015 lakini hayatoi maji. Kuna miradi takribani 88 ambayo ilijengwa mwaka 2010 mpaka 2015 lakini haitoi maji miradi hiyo kwa mfano; kuanzia mradi wa masoko kule Rungwe Mbeya, mradi wa Mwanza Shirima kule Kwimba, mradi wa Tunduru kuna mradi wa Mbesa, kuna mradi wa maji kule Matimira, kuna mradi wa maji kule Singida ambayo ni Ikole Miginga, Kuna mradi wa maji kule maeneo Kigoma Kankoko, ambayo kuna miradi sita haifanyi kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuja na mpango wa kuhakikisha kwamba miradi hii yote inafanya kazi na wala hatutaleta mkandarasi tutatumia wataalam wetu wa Mamlaka za Maji, hivi tunavyozungumza mradi wa masoko wako watu tumenunua mabomba na wako vibarua takribani 80 wanachimba mtaro kuhakikisha kwamba kazi ya mradi huo inamalizika mara moja. Vilevile, kwa mradi wa Kakonko huko Kigoma tumepeleka wataalamu wetu kutoka Moshi, Mamlaka ya Maji Moshi ambayo wanauwezo mzuri wa kujenga vyazo vya maji kwenda kufanya kazi hiyo huko Kakonko Kigoma ili kutatua matatizo ya maji ya huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa miradi kwa mfano ya kule Kwimba tumepeleka Mamlaka ya Maji ya Mwanza kuhakikisha pia wanamaliza tatizo la mradi huu naomba niwahakikishie ndugu zangu watanzania, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na wengine wametuona kule Mbeya vijijini matatizo ya maji kwenye maeneo mengi tutayamaliza ili kuhakikisha watanzania watapata maji safi na salama. Kama mradi umejengwa 2010 mpaka 2015 lazima tuukarabati kwa sababu wataanzania wanalotaka wao ni kusikia habari ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na mazungumzo kuhusu wataalam wa maji ni kweli wataalam wa maji wengine wanachangamoto kubwa, wataalam wa maji wengine weledi wao ni mdogo, wataalam maji wengine hasa wa halmashauri uwezo wao ni mdogo, wataalamu wengine wa halmashauri siyo waadilifu, lakini pia nina amini wapo baadhi ya wataalamu ni wazuri sana na wataalam hawa wanategemea kuangalia kiongozi wao kama kiongozi wao anaonyesha njia kama kiongozi wao unasimamia vizuri na wao watajifunza kutoka kwako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba niwahakikishie kwamba tutafanya kila tutakaloweza tuchukuwe wataalam ambao ni waadilifu na tutasimamia kwa uwadilifu mkubwa. Kama nilivyosema mwanzo mtaalam yoyote kama yupo halmashauri, kama yupo kwenye mkoa, kama yupo wizarani, akifanya uzembe kama si mhadilifu nitamfukuza hapo hapo bila kupoteza hata muda. Nia yetu lazima tujenge Wizara ya maji mpya, Wizara ya maji ambayo itakwenda kujibu matatizo ya watanzania watanzania wamechoka wanahitaji maji Safi na Salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na issue nyingine wa uvunaji wa maji tumesikia maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge ili tumelichukuwa na tulizielekeza halmashauri zitengeneze sheria ndogo ndogo kwa ajili ya kuvuna maji hasa kwenye majengo na taasisi za Serikali kwa vile hili naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge tutaendelea kulisimamia kuhakikisha kwamba tutafanya kazi hiyo vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utunzaji wa vyanzo vya maji, Mheshimiwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira amelizungumza sana hili kwa kweli utunzaji wa vyanzo vya maji ni muhimu sana kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri mwaka, tunazungumzia mwaka 1962 wakati watanzania wapo milioni 10 upatikanaji wa maji kwa mto mmoja ilikuwa mita za ujazo 7862, leo hii tuko watu karibuni milioni 54 upatikanaji wa maji takribani au upatikanaji kwa maji kwa mtu mmoja ni lita za ujazo 2300.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tujipange kwa sababu tulipoangalia vizuri tunaelekea chini ambako baadaye nchi yetu itakuwa na shida kubwa ya maji hili, jambo linaweza kutokea popote nyote Waheshimiwa Wabunge mlikuwa mashahidi South Africa Cap town siku zake zilizopita kulikuwa na changamoto kubwa ya maji, sisi tumejipanga kuhakikisha kwamba tunatunza vyanzo vya maji tunapanda miti na tunafanya kilimo ambacho kinaenda na vyanzo vya maji hasa kwenye maeneo ya vyanzo vya maji, hiyo ni muhimu sana kuhakikisha kwamba vyanzo vya maji hivi tulivyonavyo vinakuwa endelevu tuvitumie sisi pamoja na watoto wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunajaribu kuweka mipaka tunapima mipaka kwenye vyanzo vya maji ili visianze kuvamiwa vamiwa, tumejipanga vizuri tukishirikiana na wadau wote kuhakikisha kwamba vyanzo vya maji vyote tunavilinda na vinakuwa salama sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na Waheshimiwa Wabunge Wabunge wengi wamezungumza kwenye michango yao kwamba na mahitaji ya visima, na Waheshimiwa Wabunge tutatoa karatasi kila Mbunge aandike mahitaji yake ya visima ili tuanze kuhifanya kazi hiyo kwa uharaka sana kwa sababu wananchi wetu hatutaki wapate tabu hii ni muhimu sana tutatumia resources zetu zote, tutatumia nguvu zetu zote, tutatumia utaalam wetu tuhakikishe visima hivyo vimechimbwa haraka iwezekanavyo. Yule ambaye atashindwa kwenda na speed yetu tutamwambia imetosha kaa pembeni, tumejipanga kuhakikisha kwamba nchi yetu sasa kwenye sekta ya maji tunaenda mbele tumechoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Bwawa la Kidunda ni kweli imekuwa muda mrefu lakini tunajipanga sasa Serikali kuanza kufanya kazi ya ujenzi wa Bwawa hilo ili tuwe na maji ya uhakika kwa ajili ya Dar es Salaam, Bagamoyo na Kibaha, tutafanya kazi hiyo hiyo kwa bwawa la Farkwa, ambalo linategemiea sana na chemba na hapa Wilaya ya Chemba pamoja na jiji hili la Dodoma ambalo Serikali iko hapa makao Makuu yake, tumejipanga kwa ufupi kuhakikisha kwamba sekta ya maji matatizo yote tunamaliza ili watanzania wapate maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa sasa ninaomba kutoa hoja.
WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia hoja hizi tatu zilizoko mbele yetu. Niwapongeze sana Wenyeviti kwa kuwasilisha hoja nzuri ambazo tunazichangia leo hii. Nitajikita kwenye maeneo mawili; eneo la kwanza nitaanzia na KADCO, Kiwanja cha Ndege cha KIA.
Mheshimiwa Spika, Kiwanja cha Ndege cha KIA ni kiwanja cha ndege cha Serikali kwa asilimia 100. Kabla ya mwaka 2009 Kiwanja cha Ndege cha KIA kilikuwa na wanahisa wanne, mwanahisa wa kwanza alikuwa ni Serikali ambaye alikuwa anamiliki asilimia 24, mwanahisa wa pili alikuwa ni McDonald kutoka Uingereza ambaye alikuwa anamiliki asilimia 41.4, mwanahisa wa tatu alikuwa South Africa Infrastructure Fund ambaye alikuwa anamiliki asilimia 30 na mwanahisa wa mwisho alikuwa Inter Consult Limited ya Tanzania ambayo ilikuwa inamiliki asilimia 4.6.
Mheshimiwa Spika, kati ya mwaka 2009 mpaka 2010 Serikali ilifanya maamuzi ya kununua wanahisa wengine ambapo Serikali ilinunua wanahisa hao kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Kampuni ya McDonald ambayo ilikuwa na asilimia 41.4 ilinunuliwa kwa dola za kimarekeni milioni 2.752.
(b) Mheshimiwa Spika, Kampuni ya South Afrika, South Africa Infrastructure Fund ambayo ilikuwa na asilimia 30 ilinunuliwa kwa dola za kimarekani milioni 1.994
(c) Mheshimiwa Spika, na kampuni ya Kitanzania Inter Consult Limited iliyokuwa na asilimia 4.6 ilinunuliwa kwa dola za kimarekani 839,737.
Mheshimiwa Spika, kwa maelezo hayo kuanzia mwaka 2011 au mwisho wa 2010 KADCO ilikuwa ni kampuni ya Serikali kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Spika, Kampuni ya KADCO inaendeshwa au imeundwa kwa mujibu wa Sheria ya Kampuni, Sura Namba 212 ya Mwaka 1978. Kwa sasa Kampuni ya KADCO inasimamiwa na Wizara, lakini iko chini ya Msajili wa Hazina na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya KADCO pamoja na Bodi ya Kampuni ya KADCO wanateuliwa na Serikali, wote wanateuliwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika, Kampuni ya KADCO inalipa kodi. Inalipa kodi Corporate Tax na inalipa Service Levy kwenye Halmashauri ya Hai, pia, Kampuni ya KADCO inalipa dividend. Kwa mfano, mwaka 2016/2017 ililipa shilingi milioni 555; mwaka 2017/2018 ililipa milioni 583; mwaka 2018/2019 ililipa shilingi bilioni moja; mwaka 2019/2020 haikulipa kwa sababu, kulikuwa hakuna wasafiri kutokana na ugonjwa wa Covid; mwaka 2020/2021 vilevile haikulipa dividend kwa sababu ilikuwa kuna ugonjwa wa Covid-19 na wasafiri walipungua sana. Na hizi dividends zote zililipwa kwenye Serikali.
Mheshimiwa Spika, wafanyakazi wote wa KADCO ni Watanzania, hakuna mtu mgeni wote ni wafanyakazi wa Tanzania na karibuni ni vijana wadogo tu. Kwa vile mtu akisema kama ni kampuni ya wageni, Hapana, haelezi ukweli na sio sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Kampuni ya KADCO, kama nilivyosema, inaendeshwa kwa mujibu wa Sheria za Makampuni, haiko chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kwa sababu, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege iko chini ya Sheria ya Uwakala wa Serikali (Agencies). Hivi tulivyo tuko katika mpango wa kuibadilisha sheria hiyo na kuifanya iwe mamlaka au authority, pengine huko mbele ndio tunaweza tukaziunganisha taasisi hizi mbili, lakini kwa sasa ni taasisi ambazo zinaendeshwa kwa sheria tofauti.
Mheshimiwa Spika, nafikiri hili lilikuwa ni jambo muhimu kulieleza kwa sababu, leo limezungumzwa sana kwamba, Kampuni ya KADCO ni kampuni ambayo inamilikiwa na watu wa nje wakati si kweli. Kwa asilimia 100 inamilikiwa na Watanzania, yaani ni Serikali.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri, Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam unaendeshwa na kampuni gani?
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam unaendeshwa na Kampuni ya TAA… (Makofi)
SPIKA: Ngoja kidogo Waheshimiwa Wabunge.
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, unaendeshwa na Kampuni ta Tanzania Airport Agency (TAA).
SPIKA: Wakati Serikali ikilipa pesa 2009 na kununua zile hisa na kurejesha uwanja kwenye umiliki wa asilimia 100, ule mkataba unazungumziwa sasa hivi ni mkataba gani? Baada ya kuwa Serikali imeshalipa pesa zote?
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ni mkataba ambao ni wa Serikali kwa asilimia 100, lakini kwa jina unaendeshwa na Kampuni ya KADCO. Ni jina tu, lakini kampuni yenyewe ni ya Serikali kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Spika, naweza kuitwa Peter ama nikaitwa Mbarawa, lakini hakutakuwa na tofauti yoyote ndio nitakuwa ni mimi tu.
(Hapa, baadhi ya Wabunge walipaza sauti)
SPIKA: Unajua tunapata hii changamoto kwa sababu, sasa hivi Waheshimiwa Wabunge hatuamshi jambo jipya, tunatazama Taarifa za Mkaguzi wa Hesabu za Serikali amesemaje. Mkaguzi wa Hesabu hicho alichokisema, Kamati wamepata nafasi ya kuonana na Wizara na hao watu wa KADCO na TAA, bado inaonekana kuna changamoto.
Ukisoma taarifa ya Kamati yetu wanazungumzia mkataba kwamba, mkataba unaisha Juni, 2023. Ni mkataba gani kwa sababu, KADCO kimsingi ile iliyokuwepo awali ni kwamba, haipo, ndio msingi, kisheria ni kwamba ile kampuni iliyokuwepo awali sasa haipo kabisa. Kama haipo haya mazungumzo ya mkataba yanatokana na nini? Hilo moja. (Makofi)
La pili, kwa nini hiyo KADCO wakati Serikali iliponunua haikurejesha TAA kama ambavyo TAA inafanya Dar-es- Salaam ifanye na huko kwa sababu, haya yote yasingejitokeza kama CAG hakuonesha kuna shida? (Makofi)
La tatu, pesa umeeleza hapa na niwapongeze sana Serikali kwamba, mnafuatilia kwamba, KADCO inalipa pesa. Sasa hata wewe unaona ni KADCO inalipa pesa, sio Serikali inajilipa pesa. Hii KADCO imezishikilia wapi hizi pesa ambazo kwa kawaida zinashikiliwa sehemu nyingine halafu yenyewe ndio inailipa Serikali? (Makofi)
Hayo tu Mheshimiwa Waziri, halafu tuendelee na michango mingine.
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, hili la kwanza kama ulivyosema, mkataba unaisha tutalifanyia kazi, hilo sitaki kulizungumza sana naomba tulichukue tukalifanyie kazi tuone mkataba unaishaje na tunafanyaje, lakini kuna mpango wa Serikali ambao sisi wenyewe tunataka kuhakikisha kwamba, KADCO inarejea kwenye TAA hiyo tunao mpango, lakini kwa sasa kwanza tubadilishe Sheria ya TAA ambayo inasimamia Kiwanja cha Dar-es-Salaam, kiwanja cha Mwanza na viwanja vingine.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu kama nilivyosema TAA sasa hivi inasimamiwa na Sheria ya Uwakala (agencies), kwa vile tunachotaka kufanya ni kuhakikisha kwamba TAA inakuwa mamlaka na baada ya hapo mchakato wa kuhamisha KADCO utaendelea. Mazungumzo yameanza muda mrefu ya jambo hili kwamba KADCO lazima iwe chini ya TAA, hilo tunaendelea kulifanyia kazi, hilo ni la kwanza.
Mheshimiwa Spika, pesa zinawekwa wapi, pesa kama kuna akaunti mbalimbali zinawekwa. Katika Mashiriki yote ya Serikali mengi yanaweka pesa zao katika akaunti zao BOT na ikifika wakati wakulipa dividend inatoa BOT inaipelekea Serikali, kama taasisi zingine zilivyo kama TPA na nyingine zote ambazo huwa kunakuwa na akaunti maalum ambayo inawekwa BOT, wakitaka kutumia kawaida wanaomba kibali kama taratibu zinavyoelekeza.
Mheshimiwa Spika, naomba hilo kwa ufafanuzi wa jambo hilo, lakini kwa ufupi tutalichukua na tutalifanyia kazi kuhakikisha kwamba mwisho wa siku KADCO inarudi chini ya TAA.
Mheshimiwa Spika…
SPIKA: Mheshimiwa Waziri, mimi nitakupa tena nafasi, siyo leo ili hayo mengine ukayafanyie kazi. Nitakupa nafasi tena Jumamosi wakati wanahitimisha Wenyeviti wetu, Mawaziri mtapata nafasi ya kufafanua mambo mbalimbali na wewe Mheshimiwa Waziri pia utapewa.
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, sawa.
SPIKA: Itaturahisishia ili Bunge liweze kufanya maazimio ambayo kwanza yanatekelezeka, pili yana uhalisia wa huko nje. Mheshimiwa Waziri utatusaidia kufafanua hii KADCO akaunti yake ipo pia BOT? Kwa sababu ni ya Serikali asilimia mia moja, halafu ulisema unayo mambo mawili kwa hiyo hili la KADCO umeshatoa maelezo, haya mengine ambayo nimeuliza kama ulivyosema unalichukua utalitolea ufafanuzi Jumamosi. Hilo la pili sasa nakupa fursa, maana ulisema una mambo mawili, karibu sana.
WAZIRI WA UJENZI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, nina mambo mawili, jambo la pili lilizungumzwa kuhusu viwanja vya ndege sasa hivi vinasimamiwa ujenzi na TANROADS kwa nini visisimamiwe na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA). Ni kweli jambo hili uamuzi ulifanyika mwaka 2017 ambapo instrument ilibadilishwa na viwanja vya ndege kupelekwa TANROADS, vilipelekwa kwa kipindi hicho kukiwa na sababu za msingi lakini baada ya muda mrefu tukaona hizo sababu hazipo na sasa tuko kwenye mchakato wa kurejesha baadhi ya ujenzi chini ya TAA. Kuna ujenzi ambao umeanza mfano, hapa Msalato tumepata pesa za ADB itakuwa ni vigumu sasa kuanza kutoa uwanja wa Msalato chini ya TANROADs kwenda TAA kwa sababu mchakato wenyewe unakuwa mrefu na kazi imeanza. Kwa vile, viwanja ambavyo vitaanza kujengwa sasa hivi ujenzi utasimamiwa na TAA kama Sheria ya ICAO inavyosema.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba kuwasilisha. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 – Wizara ya Fedha na Mipango
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nami napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutupa fursa ya kuchangia kwenye hoja muhimu ya Serikali iliyoko mbele yetu. Kabla ya yote, napenda kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Wabunge wengi wamechangia, hasa kuhusu miundombinu, kwani Wabunge wengi wanafahamu bila miundombinu nchi yetu haiwezi kuingia katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianzia na Mheshimiwa Hawa Ghasia, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Miundombinu, ametoa hoja ifuatayo: katika Mpango wa Maendeleo wa Mwaka Mmoja Serikali imeainisha miradi saba ya kielelezo itakayohitaji mtaji mkubwa wa uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Miradi hiyo ni ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge, ununuzi na ukarabati wa meli kwenye Maziwa Makuu, kuboresha Shirika la Ndege Tanzania, ujenzi wa Barabara ya Kidahwa – Kanyani, Kasulu – Kibondo – Nyakanazi na Barabara ya Masasi – Songea – Mbaba Bay pamoja na mradi wa makaa yam awe na Mchuchuma na mradi wa chuma wa Liganga.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati inataka Serikali kuainisha miradi itakayotekelezwa kwa mfumo wa Public Private Partnership, muda wa kukamilisha na gharama za mradi husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu hoja hiyo, kama ifiuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kutekeleza miradi ya barabara kwa kushirikisha sekta binafsi kwa utaratibu wa PPP.
Kwa sasa mradi pekee wa barabara ambao umepangwa kutekelezwa kwa utaratibu huu ni ujenzi wa Barabara ya Dar es Salaam – Chalinze Express Way. Barabara hii inatarajiwa kuwa na urefu wa kilometa 140 itakapokamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu wa mradi huu upo katika hatua za mwisho za kukamilishwa. Mara baada ya hatua hii kukamilika gharama za awali na muda wa utekelezaji wa mradi huo utajulikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Ghasia alikuwa na hoja ifuatayo; ushauri kwa Serikali kuhakikisha inahusisha Sekta binafsi kwa kugharamia mradi kwa njia ya ushirikishi yaani PPP pamoja na kutumia fedha zake za ndani ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo. Ushauri umepokelewa, Serikali imepanga kutekeleza miradi mingi iwezekanavyo ya miundombinu ya usafiri kwa njia ya PPP kila inapowezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge kama ifuatavyo; kwanza ushauri kwa Serikali kuhakikisha sekta wezeshi zinatekeleza miradi kikamilifu kwa bajeti iliyotengwa kwa miradi hiyo. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Chunya hadi Itigi, na barabara ya Ipole hadi Ikoga. Ushauri umepokelewa kwa barabara ya Chunya hadi Itigi upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umekamilika kwa barabara yote yenye urefu wa kilometa 413 na barabara hii itajengwa kwa awamu. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa shilingi bilioni 5.84 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kiwango cha lami wa sehemu ya Itigi - Mkiwa yenye kilometa 35. Kwa sehemu iliyobaki Serikali itaendelea kujadiliana na washiriki wa maendeleo ili zipatikane fedha kwa ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa barabara ya Ipole, Koga hadi Mpanda hatua za ununuzi wa Wahandisi Washauri watakapofanya mapitio ya usanifu na usimamizi, pamoja na mkandarasi atakayejenga barabara hiyo zinaendelea. Ujenzi umepangwa kuanza katika mwaka wa fedha 2016/2017, jumla ya shilingi bilioni 103.93 zimetengwa kama inavyooneshwa kwenye kitabu changu cha bajeti ukurasa 223.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna hoja kutoka kwa Mheshimiwa Josephat Kandege, Mbunge wa Kalambo kama ifuatavyo; kwanza anatoa pongezi kwa Serikali, pongezi hizo zimepokelewa, pia anatoa ushauri kwa Serikali kuwathibitishia au kuondoa wataalam wanaokaimu nafasi mbalimbali za uongozi katika taasisi na Serikali Kuu ili kuboresha uwajibikaji wa watumishi husika.
Kwanza ushauri huo umepokelewa, pili Serikali inaendelea na utaratibu wa kuhakikisha kuwa wataalam wote ambao sasa hivi wanakaimu wanafanyiwa confirmation ili wawe na muda wa kutosha wa kufanya kazi hiyo. Kwa kuanzia tu wiki iliyopita tulitangaza Bodi ya TPA ambayo sasa imeanza kufanya kazi, hatua inayofuata sasa hivi ni kumchangua Mtendaji Mkuu wa Bandari au Mamlaka ya Bandari ili aweze kuendelea na kazi hiyo ya kuendesha bandari zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna hoja ya Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau wa Jimbo la Mafia ambapo hoja yake inasema kama ifuatavyoa; Serikali itoe mchanganuo wa muda wa utekelezaji yaani timeframe ya miradi yote ya maendeleo pamoja na gharama zake na siyo tu kwa ujumla kwa mfano ujenzi wa kiwango cha express way wa barabara ya Dar es Salaam hadi Chalinze.
Kwanza ushauri umepokelewa Mheshimiwa Mbunge, muda halisi wa ujenzi wa barabara ya Chalinze express way utajulikana baada zabuni kutangazwa na mwekezaji kujulikana. Kwa sasa mtaalam elekezi anakamilisha upembuzi yakinifu wa mradi huo na wakati huo utakapofika muda maalum utaelezwa kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia alikuwa anahoja Serikali ijengwe….
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha naomba umalizie.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, narejea tena naomba kuunga mkono hoja asilimia moa moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote na mimi ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuwepo hapa leo kukamilisha kazi ambayo niliianza toka siku jana tarehe 17 Mei, ambapo niliwasilisha hoja hii. Katika siku hizi mbili Waheshimiwa Wabunge 209 wametoa michango yao kwa njia ya maswali, mapendekezo na maoni kuhusu namna bora ya kusimamia, kuendesha, kuboresha na kuendeleza miundombinu ya Sekta ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kwako wewe binafsi, Wenyeviti wote na Makatibu wa Bunge kwa umakini wa hali ya juu mliotuonesha kwa kusimamia kwa ufanisi mkubwa majadiliano yote kwenye Mkutano huu wa Tatu wa Bunge letu hili Tukufu. Aidha, napenda pia kumpongeza Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa utendaji kazi wake wenye ufanisi na tija ya hali ya juu ambao umetufanya sisi wasaidizi wake kuwa na kazi rahisi kutekeleza majukumu yetu. Ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mwisho, lakini si kwa umuhimu, napenda pia kuwapongeza Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu na Kamati ya Bunge ya Bajeti kwa kufanya kazi kwa karibu sana na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Kamati hizi zimetuonesha upeo mkubwa wa ufahamu kuhusu wajibu wa sekta, kuwezesha sekta nyingine kufikia malengo yao. Ahadi yangu kwa Wajumbe wote wa Kamati hizi ambao waliwawakilisha Waheshimiwa Wabunge wote wengine ni kuwa yote tuliyokubaliana kwenye vikao mbalimbali kati ya Wizara na Kamati tutayatekeleza. Wizara itaendelea kufanya kazi kwa karibu na kamati hizi, ili kufikia malengo yake. (Makofi)
Mheshmiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wizara ninayoisimamia ina sekta kuu tatu (sekta ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano), nitajibu kisekta hoja kuu za Waheshimiwa Wabunge. Mheshimiwa Naibu Waziri tayari amejibu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge, kazi yangu itakuwa ni kujibu hoja kuu zilizojitokeza ambazo ndio msingi wa utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza na sekta ya ujenzi ikifuatiwa na sekta ya uchukuzi na hatimaye sekta ya mawasiliano. Kitakwimu Waheshimiwa Wabunge 209 walichangia wakati wa majadiliano ya hoja ya Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasilino ambapo Waheshimiwa Wabunge 89 walichangia kwa kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge 120 walichangia kwa maandishi. Ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukuhakikishia kuwa tutajibu hoja zote za Wabunge kwa maandishi na kuwapatia Waheshimiwa Wabunge wote majibu ya hoja hizo kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Kumi na Nne wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo kwa yale yote ambayo hatutoweza kuyajibu hapa leo kwa sababu ya muda, majibu yatapatika kupita maandishi ambayo Wizara yangu itaandaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nianze na sekta ya ujenzi na ukarabati wa barabara. Barabara ni moja ya miundombinu muhimu kwa ajili ya kuchochea maendeleo. Serikali itaenda kutenga fedha ili kujenga na kukarabati barabara ikiwa ni pamoja na kutekeleza sera ya kuunganisha mikoa kwa mikoa pamoja na nchi jirani kwa barabara za lami kama walivyoshauri Waheshimiwa Wabunge wengi waliochangia hoja hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Fungu 98 - Ujenzi kwa ajili ya miradi ya maendeleo imepangiwa shilingi trilioni 2.176. Kulikuwa na hoja kwamba je, kati ya fedha hizo, fedha ngapi au shilingi ngapi zitakwenda kwenye kulipa madeni?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 400, zitatumika kukamilisha malipo ya madeni ya nyuma ya Makandarasi na Wahandisi Washauri wa miradi ya barabara itakayobakia, yaani shilingi trilioni 1.776 zitatumika kwa kujenga barabara. Kama unavyojua, Wizara yangu imepewa takribani shilingi trilioni 4.895, hii ni historia kwa nchi yetu, haijawahi kutokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wenzangu kwamba, tutasimamia wajibu wetu kwa uadilifu mkubwa na hatutawaangusha. Waheshimiwa uwezo tunao, nia tunayo ya kuhakikisha kwamba tunawajengea Watanzania miundombinu ya kisasa ili waweze kuingia kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020/2025. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila miundombinu bora hakuna nchi yoyote iliongia uchumi wa kati. Kwa kulitambua hili, tutalifanyia kazi na tutajipanga inavyopaswa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea katika maoni ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni, kumetolewa hoja inayohusu upotevu wa shilingi bilioni 5.616 ya riba inayotokana na TANROAD kutokulipa madai ya Makandarasi kwa wakati, katika kipindi cha mwaka 2012 hadi 2015 ambayo imetoka na Ripoti ya CAG iliyotolewa mwezi Machi, mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuweka kumbukumbu sawa napenda kunukuu mapaendekezo ya CAG kwenye ripoti ya mwaka 2014/2015 kuhusu taarifa ya fedha za Serikali kwa mwaka unaoishia tarehe 30 Juni, 2015 iliyotolewa Machi mwaka huu, ukurasa wa 143 kama ifuatavyo; “Napendekeza Wakala wa Barabara yaani TANROADS ifuatilie fedha ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati, pia napendekeza mikataba itolewe kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Hii itasababisha Serikali kuepuka gharama zisizo za lazima yaani riba zinazotokana na ucheleweshaji wa malipo ya wakandarasi.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ya hoja hiyo ni kwamba madai ya riba kwenye madeni ya wakandarasi kumetokana na ukosefu wa fedha za kulipa madeni ya makandarasi na wahandisi washauri wa miradi ya barabara kwa wakati. Serikali kwa sasa inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kulipa madeni ya makandarasi na wahandisi washauri wa miradi ya barabara na madaraja, kwa hivyo kupunguza madeni hayo na kupunguza riba inayotokana na malimbikizo hayo. Nyote mmekuwa mashahidi mara baada ya Mheshimiwa Magufuli kuingia madarakani, kuanzia mwezi wa Novemba mpaka sasa hivi, Wizara yetu imepelekewa takribani shilingi trilioni moja, hili ni jambo kubwa na tunamshukuru sana Mheshimiwa Magufuli. Tunaamini huko tunakokwenda hakutokuwa na malimbikizo tena kwa vile tunaamini tukipata ukaguzi wetu utakuwa uko safi na hautokuwa una matatizo tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja nyingine inayosema kwamba barabara zilizotengewa fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami katika Mkoa wa Mara ilikuwa ni kilometa 0.8, ukweli wenyewe ambao uko katika bajeti yetu kwa mkoa wa Mara tumetenga zaidi ya kilometa 58 katika mwaka wa fedha 2016/2017 ambazo zimetengewa jumla ya shilingi bilioni 64.88 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa kwanza ni Makutano- Nata- Mugumu shilingi bilioni 12, mradi wa pili ni Simiyu - Mara Border - Mosoma, shilingi bilioni 16.4, mradi wa tatu, Makutano - Sirari shilingi bilioni mbili, mradi wa nne ni Nansio - Bulamba shilingi bilioni 20.697. Mradi mwingine Nyamuswa – Bunda - Bulamba shilingi bilioni 8.435, mradi mwingine ni Musoma- Makojo- Besekela shilingi bilioni 2 na mradi wa mwisho ni daraja la Kirumi na daraja la Mara zote daraja mbili zimetengewa shilingi bilioni 3.8. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa kurejea, Waheshimiwa Wabunge, nendeni kwenye kitabu changu cha bajeti na tembeleeni ukurasa wa 218, 219 na 225 wa kitabu hicho mtaona maelezo hayo ambayo nimeyaweka hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, jumla ya shilingi bilioni 31 zimetengwa kwa ajili ya miradi mingine ya ujenzi na ukarabati wa barabara kwa kiwango cha lami na changarawe pamoja na matengenezo ya barabara katika Mkoa wa Mara. Fedha zote zilizotengwa kwa Mkoa wa Mara ni shilingi bilioni 96.38, ninaomba, Waheshimiwa Wabunge rejeeni kwenye kitabu changu cha bajeti, ukurasa 218, 219, 244, 262, 273, 275, 279, 284, 289, 293, 305, 319, 329, 337 na ukurasa wa 345. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja nyingine ambayo inasema, mkandarasi wa barabara ya Makutano - Nata - Mugumu, sehemu ya makutano Sanzate amelipwa fedha kama ifuatavyo; kulikuwa na hoja kwamba amelipwa fedha zaidi, lakini tulilofanya kwanza tumelipa malipo ya awali (advance payment) ambayo ni shilingi bilioni 6.7 halafu tumelipa ya kazi zilizofanywa ambayo ni shilingi bilioni 8.2, jumla shilingi bilioni 14.9 zimelipwa. Kati ya fedha ya advance payment ya shilingi bilioni 6.7 zilizorejeshwa ni shilingi bilioni 1.4. Kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa daraja ambalo limekamilika kwa asilimia 80, mkandarasi ameunda tuta la barabara la kilometa 40 baada ya kukamilika ujenzi wa tuta la kilometa 40, mkandarasi amefanya maandalizi ya ujenzi wa matabaka ya msingi, yaani sub base na base course na hatimaye tabaka la lami.
Waheshimiwa Wabunge naomba muelewe kwamba katika ujenzi wa barabara, sehemu ndogo ya fedha inatumika kwa kuweka lami, lakini asilimia kubwa ya fedha inatumika kwa ile kazi ya msingi. Kwanza ile civil work, halafu course work, halafu base work, sasa tumemlipa huyu mkandarasi kutokana kazi aliyoifanya sivyo hivyo ilivyoelezwa. Mradi huu unahusisha makandarasi 11, una lengo la kuwajengea uwezo makandarasi wazalendo. Makandarasi hawa walimaliza mradi mkubwa wa ujenzi wa daraja la Mbutu, mkoani Tabora kwa ufanisi mkubwa. kwa hivyo, tuna wajibu sana wa kuwezesha Watanzania, Serikali hii ina jukumu kubwa la kuwa-empower Watanzania, Wizara tuna wajibu mkubwa wa kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja inayohusu kivuko cha Mv Dar es Salaam, nikirejea tena kwenye hoja ya CAG, kwenye ripoti yake CAG alisema kuna mapungufu yafuatayo; mapungufu ya ununuzi wa kivuko shilingi bilioni 7.9, naomba nisome hoja hiyo kama ilivyoelekezwa na Mheshimiwa CAG:
Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Umeme, Mitambo na ufundi yaani TEMESA iliingia mkataba na Ms Jones Gram Hansen DK Copenhagen ya Denmark kwa ununuzi wa kivuko cha Dar es Salaam - Bagamoyo chenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 4.98 bila Kodi ya Ongezekoo la Thamani. Mapungufu yafuatayo yalibainika katika manunuzi hayo:-
Kwanza, kasi ya kivuko haikukidhi matakwa ya ununuzi. Ripoti maalum ya mkaguzi ilibainisha kwamba kiwango cha juu na cha chini cha kasi ya kivuko wakati wa majaribio kilikuwa ni kati ya notes 19.45 na 17.25 kinyume na makubaliano yalioainishwa kwenye mkataba ya kasi ya note 20, maana yake haikufikiwa ile speed ambayo ilikubalika kwenye mkataba.
Pili, ilikuwa Hati ya makabidhiano haikutolewa, kivuko kilikabidhiwa bila hati ya makubaliano (good acceptance certificate) mwezi Novemba, 2014, baada ya ucheleweshwaji wa siku 16. Naomba niwachukue Waheshimiwa Wabunge kwenye utaratibu wote ambao tuliweza kununua kivuko hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Ufundi na Umeme ulitangaza zabuni ya ununuzi wa kivuko hiki kwa kupitia njia ya International Competitive Bidding ambayo ilifanyika tarehe 29 Oktoba, 2012 kupitia gazeti la Daily News. Kampuni tano ziliomba na kampuni ya Jones Gram Hansen ambayo ilikuwa na bei ya chini ndiyo ilikubaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, thamani za zabuni baada ya thamani kufanyika ilionekana kwamba kampuni ya Jones Gram Hansen ya Denmark ndiyo ilikuwa imetuma zabuni hiyo lowest evaluated bidder kwa gharama ya dola za Kimarekani milioni 4.98 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 7.968.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Zabuni kuridhia; Bodi ya Zabuni ya TEMESA kupitia kikao kilichofanyika tarehe 20 mwezi wa Pili mwaka 2013, ililidhia zabuni hiyo kupewa kampuni ya Ms Jones Gram Hansen ya Denmark kwa gharama iliyotajwa hapo juu yaani dola za Kimarekani milioni 4.98 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 7.968 kama ilivyopendekezwa na Kamati ya Thamini ya Zabuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusaini mkataba; mkataba wa zabuni ya ujenzi wa kivuko cha Mv Dar es Salaam ulisainiwa kati ya TEMESA na kampuni ya Ms Jones Gram Hansen ya Denmark tarehe 25 Aprili, 2013.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa kivuko; ujenzi wa kivuko ulianza kutekelezwa baada ya mkataba kusainiwa na wakati wa ujenzi wa kivuko hiki ukaguzi ulifanyika hatua kwa hatua na ulihusisha watalaam wa SUMATRA. Picha zilizoambatanishwa ambazo ziko hapa zinaonyesha watalaam mbalimbali ambao walikwenda kuangalia kivuko hicho hatua kwa hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni ya Ms Jones Gram Hansen ilikamilisha ujenzi wa kivuko cha Mv Dar es Salaam mwezi Septemba, 2014 na ilisafirisha kivuko hicho kuja nchini Tanzania mwezi Novemba, 2014.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kivuko kuwasili kulingana na matakwa ya mkataba, mzabuni alitakiwa kufanya ukaguzi wa pamoja na Kamati ya mapokezi na majaribio ya kivuko hicho kabla ya kukikabidhi kivuko hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa ukaguzi wa Kivuko, vifaa vyake na majaribio kitu kikubwa kilichoonekana ni kivuko kutofikia kasi uliyotakiwa ya note 20 badala yake ilifikia note 15.7. Mzabuni Jones Hansen alifahamishwa juu ya upungufu huu na alikubali kufanya marekebisho hayo kabla kivuko kupokelewa na kulipwa asilimia 10 ya malipo ya mwisho kwa gharama zake, kwa sababu alitakiwa alipwe ten percent lakini kutokana na matatizo haya alitakiwa afanye kazi hii aimalize ndiyo alipwe fedha zake na hii kazi aifanye kwa gharama zake. Hadi sasa mzabuni hajalipwa kiasi hicho cha fedha hadi atakapo kamilisha marekebisho hayo. Kwa sasa mzabuni ameleta mpango wa marekebisho anayotarajiwa kuyafanya ili kufikia mwendo kasi uliokusudiwa yaani note 20. Wakala wa Ufundi na Umeme utapitia mpango huo ili kujiridhisha marekebisho hayo kufanywa kwa mzabuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ndiyo maelezo kuhusu utaratibu mzima wa kununua Mv Dar es Salaam na kulikuwa hakuna ukiukwaji wowote uliyofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee na hoja nyingine. Kuna hoja ambayo imewasilishwa juu ya suala la uuzwaji wa nyumba za Serikali. Ni kweli kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Azimio kuhusu Uuzwaji wa Nyumba za Serikali tarehe 24 Aprili, 2008 katika Mkutano wa Kumi na Moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia Azimio hilo, Serikali kupitia iliyokuwa Wizara ya Ujenzi iliwasilisha taarifa ya mwisho ya utekelezaji wa Azimio hilo tarehe 01 Julai, 2009. Taarifa ambayo ilipokelewa na kupitiwa kwa kina na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu. Baada ya Kamati hiyo kuridhika na hatua za utekelezaji zilizochukuliwa, Serikali iliwasilisha taarifa yake mbele ya Bunge ambalo liliipokea na kukubali, kwa mantiki hiyo hoja hii ilikuwa imeshafungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kulinda miundombinu ya barabara ambayo inagharamu fedha nyingi. Tuna mizani 60 kwa ajili ya kupima uzito wa magari ili kudhibiti uzidishaji wa uzito ambao unaharibu barabara zetu. Pamoja na kuwepo kwa mizani hizo bado baadhi ya barabara zinaharibika kutokana na uzito wa magari yanayopita katika barabara hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na utafiti uliyofanywa na Wizara hivi karibuni kwenye magari yenye matairi ya super single imebainika kuwa asilimia 70 ya magari yote yanayotumia matairi ya super single ambayo hayana viwango vinavyokubalika kisheria. Aidha, imebainika kuwa magari yenyewe hayana viwango vya air suspension vinavyokubalika. Kutokana na matokeo hayo ya utafiti, Wizara inafanya utaratibu wa kuzuia matumizi ya matairi ya aina ya super single yasiyo na viwango vinavyokubalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya ujenzi; hoja ya mwisho ilikuwa athari zilizojitokeza kutokana na kujitoa kwa MCC katika ufadhili wa miradi. Kwa upande wa miradi ya barabara na viwanja vya ndege hakuna athari zilizojitokeza kutokana na kujitoa kwa MCC katika ufadhili wa miradi. Miradi ifuatayo ya barabara na kiwanja cha ndege imejengwa kwa kiwango cha lami na kukamilika kwa ufanisi mkubwa wakati wa awamu ya kwanza ya MCC. Tanga - Horohoro kilometa 65, Tunduma - Sumbawanga kilometa 223.1, Peramiho - Mbinga kilometa 78, Songea - Namtumbo kilometa 72 na uwanja wa ndege wa Mafia umejengwa na hakuna tatizo lolote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwenye sekta ya uchukuzi. Hoja ambayo imevuta mvuto mkubwa sana kwenye Bunge lako leo ni hoja ya ujenzi wa reli ya kati. (Makofi)
Kwanza kabisa kwenye kitabu changu cha hotuba ya bajeti kuna baadhi ya Wabunge kidogo hawakunielewa. Kwenye kitabu changu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 72, tunazungumzia utekelezaji wa miradi, hatuzungumzii utekelezaji wa miradi kwa mwaka 2016/2017. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua hata kama tutatumia pesa gani kujenga barabara, lakini barabara zetu hazitaweza kudumu kama hatutawekeza kwenye reli. Bila reli hatutaweza kujenga uchumi wa kati kama tunavyosema. Kwa kulitambua hilo, Serikali ya Awamu ya Tano imesimama kidete kuhakikisha kwamba tunajenga reli ya kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba reli ya kati ina urefu takribani wa kilometa 2,527 ambao unaanzia Dar es Salaam – Tabora – Isaka - Mwanza kilometa 1,219. Tabora - Kigoma kilometa 411, Uvinza - Msongati kilometa 200, Kaliua – Mpanda - Karema kilometa 360 na Isaka - Rusumo kilometa 337. Kama tunataka kujenga mradi huu wote kwa pamoja tunahitaji tuwe na takribani dola za Kimarekani bilioni nane ambazo ni takribani trilioni 16. Hizi ni pesa nyingi, hakuna nchi yoyote inayoweza kuipa Tanzania mkopo wa dola bilioni nane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kulitambua hilo mimi nilipata fursa ya kufuatana na Mheshimiwa Rais Mstaafu kwenda China kuzungumzia jinsi ya kupata mkopo kwa ajili ya reli ya kati. Serikali ya China ilitoa ushauri kwamba huu mradi ni mkubwa ni lazima tuugawe kwa awamu. Kwa busara tukaona tuchukue tawi kubwa ambalo ndilo litakuwa backbone ya mradi huu ambayo itakuwa kuanzia Dar es Salaam - Tabora - Isaka - Mwanza yenye kilometa 1,219, kwa vile awamu ya kwanza ya mradi huu tunataka tuanze Dar es Salaam - Tabora - Isaka - Mwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kawaida ulimwenguni kilometa moja ya reli inajengwa kwa takribani dola za Kimarekani kuanzia milioni 3.5 mpaka dola za Kimarekani milioni 4.5, kwa mahesabu ya haraka ukichukua kilometa 1,219 tunatakiwa tupate angalau dola za Kimarekani, kwa bei ya chini bilioni 4.256 na pengine ya juu inaweza kwenda bilioni 4.876, itategemea geology ya eneo ambalo unajenga, itategemea miamba ya eneo ambalo unajenga, itategemea, kama eneo hilo lina matetemeko bei itabadilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya China ilitukubalia tunaweza tukachukua mkopo kwa ajili ya mradi huo na kawaida ukichukua mkopo China, kuna mikopo ya aina tatu. Mkopo kwanza kabisa kuna 100 percent loan ambayo ni concession loan unapata asilimia 100 mkopo. Kikawaida katika Tanzania ni miradi michache imepata mkopo asilimia 100, mradi ninaojua mimi ni mradi wa National ICT Backbone, ule umepata mkopo wa asilimia 100 kutoka China. Mikopo mingine ambayo unaweza kupata, unapata mkopo wa asilimia 85 na wewe mwenyewe unatakiwa uwe na asilimia 15. Mkopo wa mwisho ni mkopo wa commercial.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile sisi tunataka kuchukua mkopo, lazima tujipange tuwe na mtaji wa kuanzia, ndiyo Serikali ikaweka trilioni moja kwenye bajeti ya mwaka huu. Trilioni moja maana yake nini, maana yake kama umechukua mkopo wa dola za Kimarekani bilioni 4.2, 10 percent ya hiyo ni dola milioni 420 za Kimarekani. Sasa tukichukua trilioni moja tunapata kama dola milioni 400, ina maana tuna uwezo wa kuchukua mkopo hata kama tukiambiwa tulipe asilimia 85.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tumefanya nini kwenye jambo hili.
Kwanza tumeanzisha technical team, pili tumeanzisha National Steering Committee kwa ajili ya mchakato huu. Step inayofuata ni kutangaza tender ili kupata kampuni za Kichina ziweze kujenga reli hiyo. Kwa nini tumeamua kufanya hivyo, Waheshimiwa Wabunge nitawapa tu kidogo. Wenzetu wa Kenya wamejenga reli kutoka Mombasa - Nairobi kwa standard gauge ambayo ni kilometa 485, kwa kilometa moja wametumia dola za Kimarekani milioni 7.84. Nigeria wamejenga reli yao inaitwa Nigeria Railway Modernisation Project wametumia dola za Kimarekani milioni 6.31. Chad wamejenga reli yao wametumia dola za Kimarekani milioni 5.58. Tunafikiria lazima tuitangaze tender, watu waombe, tunaamini tukifanya hivyo tutapata bei nzuri kuliko kwenda kwa bei ya Kenya na nchi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi lakini muda umeisha. Mwisho kabisa sasa na mimi naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
AZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuwepo hapa kukamilisha kazi ambayo niliianza wiki iliyopita.
Aidha, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwako wewe binafsi Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wengine wote na Katibu wa Bunge kwa kusimamia kwa ufanisi mkubwa majadiliano yote kwenye Mkutano huu wa Saba wa Bunge letu Tukufu. Kwa namna ya kipekee, napenda pia kumpongeza Kiongozi wa Shughuli za Bunge, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa umahiri wa hali ya juu anaoendelea kuuonyesha na kutuongoza sisi wasaidizi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii pia kuwashukuru Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Kamati ya Bajeti kwa kufanya kazi kwa karibu na Wizara yangu. Naahidi kwamba Wizara ninayoingoza itayafanyia kazi yote yaliyoshauriwa na Kamati hizi ya kusimamia, kuendedesha, kuboresha na kuendeleza miundombinu na huduma za sekta ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano kwa weledi wa hali ya juu.
Napenda kumshukuru Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa maoni na mapendekezo yake kuhusu bajeti hii. Mwisho lakini si kwa umuhimu, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii kwa kuzungumza na kwa maandishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu limejipanga kuwa nchi ya kipato cha uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020/2025. Katika kufikia lengo hili, Taifa limelipa kipaumbele sekta ya viwanda na uendelezaji rasilimali watu ili kuwezesha kufikia lengo tunalokusudia. Wizara yangu itafanya jitihada kubwa kuweka mazingira wezeshi kwa kujenga miundombinu bora ili kurahisisha uendelezaji wa viwanda hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalihakikishia Bunge lako hili Tukufu kwamba mimi na Mheshimiwa Naibu Waziri wangu pamoja na watendaji wote wa Wizara tutasimamia ujenzi wa miundombinu muhimu ya usafirishaji na ya uunganishaji maeneo ya uzalishaji wa viwanda hivyo na maeneo ya mahitaji yaani masoko ya ndani na ya nje ya nchi. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge wote tuunganishe nguvu zetu ili pamoja na Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuwezeshe Taifa letu kufikia ndoto hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya masuala hayo ya jumla, sasa noamba nijikite kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge kwa kuzingatia sekta tatu yaani sekta za ujenzi, uchukuzi na mawasiliano. Mheshimiwa Naibu Waziri tayari amejibu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge kwa kuzingatia makundi ya Wabunge na maeneo ya kisekta. Kazi yangu kubwa itakuwa ni kujibu hoja kuu zilizojitokeza ambazo zitakuwa msingi wa utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitakwimu Waheshimiwa 29 walichangia wakati wa majadiliano ya hoja ya Waziri Mkuu na wakati wa majadiliano ya Wizara yangu tumepokea michango ya Waheshimiwa Wabunge 68 waliotoa maoni yao kwa kuzungumza na michango kwa maandishi 98. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba Wizara itajibu hoja zote za Waheshimiwa Wabunge kwa maandishi na kuwapatia majibu ya maandishi kwa njia ya kitabu kitakachoandaliwa kabla ya kuanza Mkutano wa Nane wa Bunge letu Tukufu. Hivyo kwa yale ambayo hatutaweza kuyajibu hapa leo kwa sababu ya muda kutotosha, majibu yatapatikana kupitia kitabu kitakachoandaliwa na Wizara yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijikite kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge nikianzia na sekta ya mawasiliano, uchukuzi na mwisho sekta ya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeamua kuanzia sekta ya mawasiliano kwa sababu wewe leo ni Mwenyekiti na ulikuwa mchangiaji wa kwanza kwenye sekta hii na hasa ulijikita kwenye suala la TTMS. Ulisema kwamba iko haja ya Serikali kuangalia upya mfumo wa TTMS.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilieleze Bunge lako Tukufu pamoja na Watanzania wote kwamba mfumo wa TTMS umejengwa kwa utaratibu wa jenga, endesha na kabidhi (Build, Operate and Transfer - BOT) na hivyo hakuna malipo yoyote ya awali yaliyolipwa na Serikali kwa mkandarasi wakati wa utekelezaji wa mradi huo. Mkataba wa uendeshaji ni miaka mitano na mkandarasi atakabidhi mfumo huo wa TTMS kwa Serikali kupitia TCRA mwezi Oktoba, 2018 na kuwezesha Serikali kumiliki mtambo huo kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za ujenzi wa mtambo huo kwa mkandarasi yanatokana na malipo yanayotokana na termination fee ya senti 25 kwa simu zinazoingia ndani ya nchi (international incoming calls), mgawanyo ni kama ifuatavyo:-
Mkandarasi analipwa senti nne za dola kwa ajili ya mtambo ule, senti 12 zinakwenda kwa mtoa huduma yaani makampuni ya simu, senti 8 zinakwenda Serikalini na senti moja ya dola inakwenda kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kwa ajili ya kusimamia mtambo huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma zinazotolewa kwa sasa ni kama ifuatavyo; kusimamia simu za kimataifa (international incoming calls); kusimamia simu za ndani (local off network monitoring); Kusimamia ubora wa huduma (quality of service platform) na kusimamia au kutambua simu za ulaghai (anti-fraud management system).
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu toka mtambo huo kufungwa mpaka sasa hivi tuna kesi 22 mahakamani na Serikali imepoteza pesa nyingi kupitia wizi huo wa njia za panya. Kwa mfano, mpaka sasa hivi Serikali imepoteza takribani shilingi bilioni 15.2 kupitia wizi wa mawasiliano kwa njia za panya. Kama ingekuwa hakuna mfumo wa TTMS tunaamini wizi ungekuwa mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mtambo huo sasa hivi unaweza kuona miamala ya fedha zote zinazopita hapa nchini kupitia kwenye mitandao ya mawasiliano. Taarifa na takwimu za miamala ya fedha hutumiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania na huwasilishwa BoT. BoT na Mamlaka ya Mapato Tanzania zote zimepewa uwezo wa kuweza kuona takwimu mbalimbali zinazopita kwenye mtambo huu hasa za fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mtambo huu una uwezo wa kutambua rajisi ya namba za utambulisho wa simu za kiganjani (Central Equipment Identification Register). Kwa sasa mtambo huu hauna uwezo wa kutambua revenue assurance kwa maana ya kutambua mapato ingawa kumefungwa kifaa kwa kila NOC ya mtoa huduma. Network Operative Centre ya Vodacom, Airtel, Tigo kumefungwa sensor kwa ajili ya kupata information hizo lakini bahati mbaya mtambo huu mpaka sasa haujaweza kutambua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini mtambo huu haujaweza kutambua code hiyo ni kwa sababu kulikuwa na mvutano mkubwa baina ya sisi Serikali kwa upande wa TCRA na mkandarasi yule kwa sababu alikuwa anasema hiyo huduma ya revenue assurance ilikuwa haipo kwenye mkataba. Tumevutana nao kwa zaidi ya miezi tisa na mwisho tumekubaliana kwamba aweke platform hiyo ya revenue assurance bure bila ya malipo yoyote na kazi hiyo imeanza.
Tunaamini kwamba itakapofika mwezi Agosti, mkandarasi yule ataweza kuweka mfumo huo na hapo tutaweza kupata malipo sahihi ya simu zetu kupitia kwenye mtambo ule. Naomba nieleze kwamba maoni yako tumeyachukua na tutazidi kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine uliyozungumza ni ya TTCL kwamba Serikali ifanye kila inavyoweza ili kuiwezesha TTCL kwa sababu TTCL ni kampuni ambayo kama itawezeshwa vizuri itakuwa na uwezo wa kuchangia sana pato la Serikali. Serikali tunakubaliana na wewe na tuko kwenye mpango madhubuti wa kuhakikisha kwamba sasa TTCL tunaiwezesha na kuhakikisha kwamba inachangia inavyowezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ya msingi ambayo Serikali tumeyafanya kuiwezesha TTCL. La kwanza kabisa tumeiruhusu TTCL kutumia rasilimali zake zenyewe. TTCL ina rasilimali nyingi ili kuweza kukopa shilingi bilioni 96. Jambo la pili ambalo tumelifanya kwa TTCL kwa sababu kwenye sekta ya mawasiliano issue siyo pesa ni masafa, TTCL tumewapa masafa ya Mhz 1800 kwa ajili ya teknolojia ya 4G LTG. Mpaka sasa hivi TTCL wameweza kufika mikoa kumi na mingine itaendelea mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia TTCL tuna mpango wa kuwapa tena masafa mengine mapya ya 800Mhz itakapofika mwezi wa Juni, 2017. Kwa kuiwezesha TTCL tumeipa Data Center kwa ajili ya uendeshaji na inapata malipo kwa uendeshaji huo. Pia TTCL tumeipa kuendesha Mkongo wa Taifa na inapata malipo kupitia mkongo huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ulizungumzia kuhusu technology ya internet of things, tumejipanga. TTCL ni kampuni ambayo itaweza kujiingiza kwenye biashara hii ya Internet of things ambayo naamini ikienda kwenye biashara hii na kwa vile ina Mkongo wa Taifa itafanya vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza machache kuhusu sekta ya mawasiliano, naomba sasa nijikite kwenye sekta ya Uchukuzi. Wakati wa majadiliano ya hoja ya Waziri Mkuu pamoja na hoja niliyotoa tokea wiki iliyopita, michango mingi ya Waheshimiwa Wabunge imegusa miundombinu ya reli, huduma za uchukuzi kwa njia ya anga, miundombinu ya bandari na miundombinu ya viwanja vya ndege.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianzie na miundombinu ya reli. Reli tunayotumia sasa ya meter gauge imejengwa mwaka 1905 kwa ajili ya mizigo isiyozidi tani milioni tano kwa mwaka. Kwa reli hiyo treni ilikuwa inaenda mwendo kasi mdogo na ilikuwa na uwezo wa kutumia uzani wa tani 11 kwa excel. Mtawala wa Uingereza alipokuja yeye aliibadilisha kidogo treni hiyo badala ya kwenda kwa kutumia
mvuke akaifanya iweze kwenda kwa kutumia kwa diesel na ikawa na uwezo wa tani 14 kwa excel.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, miundombinu ya treni hii kwa sasa imechakaa sana na mwendo wake mkubwa sasa inakuwa kilometa 30 kwa saa. Kwa uchumi tunaotaka kwa viwanda kwa treni hii haiwezekani. Serikali ya Awamu ya Tano imeamua sasa kujenga reli mpya ya standard gauge yenye uwezo wa kubeba mizigo ya tani milioni 17 kwa mwaka. Treni hii itatumia umeme, ni treni ambayo itakwenda mwendo kasi wa kilometa 160 kwa saa kwa treni ya abiria. Reli hii itahimili mzigo mkubwa wa tani 35 kwa excel. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnavyofahamu Mheshimiwa Rais aliweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa reli hii kutoka Dar es Salaam - Morogoro. Gharama ya ujenzi wa reli hii ilikuwa ni dola bilioni 1.212 za Kimarekani sawa na shilingi trilioni 2.2. Urefu wa njia ambao tumeweka jiwe la msingi ni kilometa 300 ambapo kutoka Dar es Salaam - Morogoro ni kilometa 205 na kilomita 95 ni za mapishano ya reli hiyo. Kwa ujumla itakuwa ni kilometa 300. Katika kujenga reli hii kwa kila kilomita moja tutatumiwa dola za kimarekani milioni nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nifanye kidogo comparison na wenzetu wa Kenya. Gharama ya ujenzi wa reli ya Kenya ya standard gauge kutoka Mombasa - Nairobi ni dola za kimarekani bilioni 3.8. Urefu wa njia ya reli ya kutoka Mombasa - Nairobi pamoja na maeneo ya kupishana ni kilometa 609. Kwa hiyo, kwa upande wa Kenya kilometa moja imegharimu dola za kimarekani milioni 6.23 wakati ya Tanzania kila kilometa moja imegharimu dola za kimarekani milioni nne. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza tumeanza kufanya evaluation kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ujenzi wa kipande cha Morogoro - Makutupora chenye urefu wa kilometa 336. Tunaamini mapema Juni, tutaweza kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa reli kutoka Morogoro - Makutupora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Makutupora - Tabora, Tabora - Isaka na Isaka - Mwanza zabuni zitafunguliwa mwisho wa mwezi huu. Aidha, kwa upande wa matawi ya Kaliua – Mpanda - Karema, Tabora – Kigoma, Uvinza – Msongati zabuni kwa matawi hayo zitatangazwa mara baada ya kukamilika usanifu wa kina ambao utamalizika hivi karibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, safari ya treni ya abiria kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro kwa kutumia reli ya standard gauge itachukua saa 1.30. Kutoka Dar es Salaam - Dodoma itatumia saa 2.45. Kutoka Dar es Salaam - Mwanza itachukua saa 7.40. Kutoka Dar es Salaam - Kigoma itachukua saa 7.45. Bado tunaangalia uwezo wa kupunguza muda huo kwa kuongeza speed. Tunaamini baada ya Singida tunaweza kuongeza speed kutoka 160 tukaenda mpaka 200 kwa sababu eneo lile lipo tambarale na tunaamini tunaweza kufanya hivyo ili Watanzania hawa sasa waweze kufika maeneo yao kwa muda mfupi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa treni ya mizigo kwa kutumia reli hii tunayojenga itakuwa na uwezo kwa kusafirisha mizigo ya tani 10,000 kwa mara moja sawa na makontena 400 ya futi ishirini, ishirini. Hii ni sawa na semi- trailer 500 zenye uwezo wa kubeba tani 20 kwa kila semi- trailer moja. Treni hii itakuwa na mwendo kasi wa kilometa 120 kwa saa. Treni ya mizigo inakuwa tofauti na treni ya abiria, treni ya abiria inakwenda kwa kasi kuliko treni ya mizigo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge vilevile walizungumzia kidogo kuhusu Northern Corridor huko Kenya. Nikilinganisha na wenzetu wa Northern Corridor, treni ya mizigo ya wenzetu itakuwa inachukua makontena 216 kwa wakati mmoja wakati ya Tanzania itakuwa inachukua makontena 400 kwa wakati mmoja. Treni ya mizigo ya wenzetu itakuwa inakwenda mwendo wa kilometa 80 kwa saa wakati ya Tanzania itakuwa inakwenda kilometa 120 kwa saa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kutoka Dar es Salaam - Kigali ambapo urefu ni kilometa 1,461, mzigo kutoka bandari ya Dar es Salaam mpaka Kigali itachukua saa 13 kwa kutumia treni yetu. Kutoka Mombasa - Kigali (Rwanda) ni kilometa 1,659.3. Kwa hiyo, treni ya mizigo kutoka bandari ya Mombasa - Kigali itachukua saa 21, mara mbili ya muda ambao itachukua treni yetu. Naamini kabisa ndani ya moyo wangu kwa kasi tunayokwenda nayo treni hii itamalizika haraka na naamini kabisa mizigo ya Rwanda, Burundi, DRC na hata ya Uganda hapo baadaye itapita kwenye bandari yetu ya Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja juu ya fedha za ujenzi wa reli. Lengo la Serikali ni kujenga mtandao wa reli kwa kutumia fedha za ndani na za mkopo wenye masharti nafuu. Kipande cha Dar es Salaam - Morogoro katika mwaka wa fedha 2016/2017 tulitenga shilingi trilioni moja na bajeti hii ambayo tutaipitisha leo tumetenga shilingi bilioni 900. Kutokana na mahitaji makubwa ya fedha za ujenzi wa reli, Serikali imeendelea kufanya mazungumzo na wafadhili mbalimbali ikiwemo Serikali ya Uturuki, China na wengine ili kupata mikopo yenye masharti nafuu. Kwa mfano, wiki iliyopita Serikali kupitia RAHCO ilikuwa na mazungumzo na mabenki matano kutoka nje kuhusu kupata mkopo wa bei nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja kuhusu ujenzi wa reli ya Mtwara – Mbamba Bay na matawi yake ya kwenda Liganga na Mchuchuma yenye urefu wa kilometa 1,000. Mwaka wa fedha 2017/2018 tunategemea kutangaza zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi, lakini reli hii tutaijenga kwa mfumo wa PPP.
Kuhusu ujenzi wa reli ya Tanga – Arusha - Musoma, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kazi ya upembuzi na usanifu wa kina wa ujenzi wa reli hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa na hoja kuhusu TAZARA kwamba Serikali ina mikakati gani ya kuifanya TAZARA iweze kujiendesha kwa faida. Reli ya TAZARA iliyosanifiwa kubeba tani milioni 5 za mzigo kwa mwaka ili kusafirisha tani hizo unahitaji injini au locomotives 174. Kwa hivi sasa TAZARA inasafirisha tani 128,105 kwa mwaka. Sasa hivi TAZARA ina wastani wa vichwa 13 tu ambavyo vinatumika kwa mwaka. Ili TAZARA kuweza kusafirisha mzigo tani 1,273,000 zilizoweza kusafirishwa mwaka 1977/1978 inahitaji vichwa vya treni 48. Injini hizi 13 zilizopo sasa ni asilimia 27 ya vichwa vyote vinavyohitajika ambavyo vilitumika mwaka 1977/1978.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuisaidia TAZARA, Serikali tumejipanga kama ifuatavyo; kwanza, Serikali ya Tanzania kupitia bajeti hii tumepanga kuweka shilingi bilioni 26 kwa ajili ya kusaidia TAZARA. Tunaamini na wenzetu wa Zambia watatenga kiasi kama hicho ili kuweza kuisaidia TAZARA. Pili, tayari Serikali zetu mbili zimefanya mabadiliko makubwa ya viongozi wa ngazi za juu ikiwa ni pamoja na kuajiri Mtendaji Mkuu mpya, Naibu Mkurugenzi Mtendaji Mkuu mpya na Meneja wa Mkoa wa Tanzania mpya na kinachoendelea sasa ni uajiri wa Meneja wa Mkoa wa Zambia ambao uko katika hatua za mwisho za kiutawala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuisaidia TAZARA iweze kufanya biashara sasa hivi tupo kwenye mpango wa kufanya marekebisho ya Sheria Na.4 ya mwaka 1995. Wataalam wa nchi zote mbili wapo kwenye hatua ya mwisho kukamilisha marekebisho hayo. Baada ya hapo marekebisho hayo yatapelekwa kwenye Baraza la Mawaziri na mwisho yatakuja kwenye Bunge lako Tukufu ambalo tunaamini litaweza kupitisha marekebisho hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijikite kwenye huduma za uchukuzi kwa njia ya anga. Mwaka jana niliahidi kuanza kuchukua hatua za kulibadilisha Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ili hatimaye liweze kujiendesha kibiashara. Tayari tumeunda Bodi mpya na Menejimenti yenye weledi na uzalendo wa hali ya juu kuiendesha kampuni hii ambapo mpaka sasa hivi tunajua itakapofika mwaka 2018 itakuwa na ndege mpya sita. Bodi na Menejimenti ya ATCL zinaendelea na taratibu za kuirudisha kampuni hii kwenye Chama cha Watoa Huduma za Usafiri wa Anga Duniani Ili mtu akiwa eneo lolote lile duniani aweze kununua tikiti bila usumbufu wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2016/2017 zilitengwa shilingi bilioni 500 fedha za ndani kwa ajili ya ununuzi wa ndege. Tayari Serikali imenunua ndege tatu za Bombadier Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila mmoja na kulipa malipo ya awali ya ndege mbili ya aina ya CS Series 300 zenye uwezo wa kubeba abiria 127 kila moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali imelipa pesa za awali za ndege ya masafa marefu ya aina ya Boeing 787-8 dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262. Katika kipindi cha bajeti 2017/2018 zimetengwa shilingi bilioni 500 kwa ajili ya kukamilisha malipo ya ndege zilizotajwa hapo juu pamoja na malipo ya ndege nyingine mpya ya masafa marefu ya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie ndege 12 za terrible teens. Siku tatu zilizopita tumesikia maneno mengi hapa Bungeni na kwenye mitandao kuhusu ndege 12 za terrible teens ambazo zimeundwa na Boeing. Terrible teens ni ndege za mwanzo aina ya Dreamliner 787 zilizotengenezwa na Boeing miaka sita, saba iliyopita huko nyuma. Ndege hizo ni nzito kidogo ikilinganishwa na ndege za kisasa za Dreamliner 787-8, zina uzito wa zaidi ya tani nne mpaka sita ukilinganisha na ndege za kisasa za dreamliner. Ndege hizi zina upungufu, kwa sababu ndege hizi ni nzito kwa hiyo zinakula mafuta zaidi ukilinganisha na ndege za kisasa. Pia ndege hizi hazina uwezo wa kwenda masafa ya mbali kwa mfano kutoka Dar es Salaam mpaka New York inabidi ziende mpaka sehemu zijaze mafuta ili ziweze kuendelea. Ndege za kisasa za Dreamliner zinaweza kutoka Dar es Salaam mpaka New York bila kunywa mafuta na ikafika New York na ikaanza safari kwa kunywa mafuta huko New York.
Mheshimiwa Mwenyekiti, terrible teens zinazozungumzwa hapa, kawaida ndege tunaitaja kwa line number kwa hiyo mimi nitataja line number. Terrible teens zinazozungumzwa hapa ni line number 4 na ya pili ni line number 5. Ndege hizi mbili sasa hivi zinatumiwa na Boeing as a test aircraft. Ndege nyingine inayozungumzwa hapa ni line number 10 ambayo Ethiopian Airways wameshaonesha nia ya kuinunua. Ndege nyingine inayozungumzwa ni line number 11 ambayo inatumiwa na Boeing Bussiness Jet. Ndege nyingine inayozungumzwa ambazo zina uzito mkubwa Line number 12 ambayo Ethiopian Airways imeonyesha interest ya kuichukua. Ndege nyingine ni Line 13 na 14 ambazo vilevile Ethiopian Airways imeonyesha interest ya kuichukua. Ndege nyingine ni line 15 ambayo kuna kampuni moja ya Air Australia imeichukua; Line 16 Ethiopian Airways imeonyesha nia ya kuichukua; Line 17 Ethiopian Airways imeonyesha nia ya kuichukua; Line 18 Ethiopian Airways imeonyesha nia ya kuichukua na Line 19 kulikuwa na maneno kwamba Rwanda Air inaweza kuichukua lakini mpaka sasa hivi haijawekwa vizuri na Line 22 kuna kampuni ya Air Australia imeonyesha kuichukua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, si kweli kwamba ndege iliyonunuliwa na Serikali kwa Shirika la Ndege la Air Tanzania Boeing 787-8 Dreamliner ni miongoni mwa ndege 12 za terrible teens dreamliners ambazo zilikosa soko. Tuna ushahidi wa kutosha kuhusu jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeingia mkataba na Boeing wa kutengeneza ndege mpya yenye line number 719. Ndege inayozungumzwa hapa kwamba tumeichukua ilikuwa iende Rwanda ina line number 19, yetu sisi ni line number 719, ni tofauti. Pia Serikali imeweka ratiba ambayo tutaifuatilia ndege hiyo hatua kwa hatua. Kinachoendelea sasa hivi tunachagua injini ya ndege. Dreamliner inatumia injini za aina mbili, inatumia Rolls-Royce na General Electric (GE). Kabla ya ndege kumalizika mnapewa uhuru wa kuchagua, tunalolifanya sasa hivi ATCL ni kuchagua injini gani tuweke kwenye ndege ile kwa vile ndege hii ni mpya sio kama maneno yaliyoletwa kwenye mitandao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge wakiwa na jambo kama hili ambalo linahitaji maelezo ya kitaalam wawasiliane na sisi Serikalini. Tupo saa 24, siku saba kwa wiki, siku 365 kwa mwaka, Serikali ipo. Waheshimiwa Wabunge, elimu haina mwisho naomba tujifunze. Pia naomba sana Waheshimiwa Wabunge tushirikiane kujenga Shirika letu la Ndege la ATCL, tushirikiane kujenga nchi yetu, hatuna nchi nyingine Waheshimiwa Wabunge, maendeleo hayana chama sisi sote tunahitaji maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maelezo yaliyoelezwa katika tovuti ya Boeing ni sahihi katika mantiki ya kisoko maana bei iliyowekwa katika tovuti hiyo ambayo walisema Tanzania wamenunua ndege kwa pesa hizo ni sahihi. Ile bei iliyowekwa pale ni list price, ni bei ya ndege, lakini wakati wa kununua ndege kunakuwa na mazungumzo marefu. Pamoja na kuwekwa bei hiyo kwenye tovuti, mazungumzo marefu yalifanyika na tulipewa punguzo kubwa sana, Serikali ilipata bei nzuri. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wenzangu Serikali imenunua ndege mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner, ndege ya kisasa na kwa bei nafuu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemaliza hilo la ndege, naomba sasa nijikite kwenye hoja ya Mheshimiwa ambaye alitaka kujua Air Tanzania kama tumeuza route zetu kwa South Afrika. Route za ndege haziuzwi ni mali ya nchi. Route za ndege zinapatikana kwa kuweka makubaliano ya nchi na nchi. Kwa hiyo, route zote za Air Tanzania bado ni mali ya Tanzania na wakati wowote tutaweza kuipa Air Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi navyozungumza na ninyi Air Tanzania inafanya tathmini ya njia zitakazoweza kuhudumiwa na ndege za masafa ya kati na masafa marefu. Njia hizo zitajumuisha zile zilizokuwa zikihudumiwa hapo zamani yaani njia ya kuendea Oman, Dubai, London, Entebe, Nairobi, Johannesburg, Lusaka na Bujumbura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Mbunge alisema wenzetu wa Kenya Airways wameuza route yao kutoka Nairobi kwenda London sijui kwa dola milioni 20. Narudia tena route haiuzwi ni makubaliano ya nchi na nchi. Ninavyofikiria Kenya Airways walichowauzia Oman Air ni slot ya kuingia pale Heathrow Airport kwa sababu kuingia Heathrow Airport ni very expensive. Kwa kila sekunde tano Heathrow Airport kunaruka ndege. Walilolifanya wao ni kuzungumza na Kenya Airways wapate ile slot, lakini si kuwauzi route, si sahihi. Sisi tukitaka kwenda London, London kuna Airport tatu; Heathrow Airport, City Airport na Luton Airport. Hizi mbili kwa maana ya City Airport na Luton ni rahisi, bei yake sio kama Heathrow. Naomba kuwaambia Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwamba ATCL hawajauza routes na imejipanga kwenda route zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua muda unanikimbia lakini nizungumze tu lingine, Mheshimiwa Mbunge aliuliza kwa miaka kumi Mamlaka ya Usafiri wa Anga imekusanya kiasi gani na Zanzibar imepeleka kiasi gani? Mamlaka ya Usafiri wa Anga haikusanyi mapato, kazi yake kubwa ni kuangalia usalama wa nchi ya Tanzania. Mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Anga yanatumiwa kwa ajili ya kununua vifaa mbalimbali vya kuangalia usalama wa anga letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2008 Serikali ya Zanzibar kwa bahati mbaya sana iliamua kuchukua mapato yanayotokana na tozo za abiria kwa upande wa Airport ya Zanzibar, lakini Mamlaka ya Usafiri wa Anga haitakiwi kuipa Serikali ya Muungano wala Serikali ya Zanzibar. Jambo hili lipo kwenye sheria ya kuunda mamlaka hii kwa hiyo hakuna pesa yoyote kwa kipindi cha miaka kumi ambayo tumeipeleka Zanzibar sababu sheria hairuhusu hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa haraka haraka nijikite na hoja ya bandari. Kulikuwa na hoja kwamba taasisi zilizopo pale bandarini ziweze kufanya kazi saa 24. Tunavyozungumza taasisi mbalimbali zilizopo pale bandarini zinafanya kazi saa 24. Nachukua fursa hii kuwaomba wateja wetu na mawakala wetu wa forodha kupata huduma bandarini wakati wowote ndani ya saa 24.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la gharama kuongezeka kutokana na VAT kwa huduma zinazotolewa kwa wakala wa mizigo inayosafirishwa kwenda nchi za jirani. Ushauri huu tumeuchukua, tunaufanyia kazi na tutaupeleka Wizara ya Fedha ili uweze kufanyiwa kazi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya kupunguza tozo ya dola 23 ya Kimarekani kwa tani kwa mzigo wa shaba ambapo bandari nyingine shindani kwa mfano Durban zinatoza dola za Kimarekani 17.86. Ni kweli mzigo wa shaba hutozwa dola 23 kwa tani, hata hivyo tozo za Bandari za Dar es Salaam hufanyika kwa dola za Kimarekani wakati bandari ya Durban mzigo hutozwa kwa rand yaani currency ya South Africa. Hali hii husababisha gharama za bandari za Durban kuwa ndogo wakati sarafu hiyo inapokuwa dhaifu ikilinganishwa na dola hasa sasa hivi ambapo exchange rate dola moja ni rand 13.41.
Aidha, tozo kwa upande wa Bandari ya Dar es Salaam hupungua hadi kufikia dola 17 kutegemeana na kiasi cha mzigo na hali ya ushindani. Kwa vile hatuko fixed tunajaribu kuwa flexible na tunabadilika sana.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Nakuongezea dakika mbili lakini vilevile tujibu kuhusu share za Serikali ambazo ziko Airtel.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavoyojua Bandari ya Dar es Salaam ina changamoto kubwa kuhusu miundombinu, lakini tuna mradi ambao sasa tumejipanga kuhakikisha kwamba tunaboresha kina cha maji cha Bandari ya Dar es Salaam na pia kujenga gati mpya kwa ajili ya kuteremshia magari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitakuwa na muda wa kwenda kwenye barabara lakini Mheshimiwa Naibu Waziri amezitaja nyingi. Waheshimiwa Wabunge hatutaweza kujibu kila kitu hapa muda hauwezi kuturuhusu lakini mjue tu kwamba maelezo na ushauri wenu hasa kwenye kuangalia sera ya barabara ya kuunganisha mikoa mbalimbali tumeichukua na tutaifanyia kazi kuhakikisha kwamba mikoa yote ya Tanzania inaunganishwa kwa barabara. Hatuwezi kuingia kwenye uchumi wa kati bila kuunganisha mikoa yetu yote na barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kusema kuwa bajeti ya Wizara yangu mwaka 2017/2018 ni bajeti ya kuanza kuweka mazingira ya uwekezaji kwenye sekta ya viwanda na kuinua uchumi wa nchi yetu kijumla ili uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2020/2025 uweze kufikiwa. Kama nilivyoliomba Bunge lako Tukufu mwanzo wa hotuba yangu ndivyo ninavyomalizia kwa kuwaomba tuunganishe nguvu zetu kwa kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge katika kutekeleza malengo ya Wizara yangu. Kwa kufanya hivyo, nchi yetu itafikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020/2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo sasa...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri subiri kwanza, share za Serikali ziko Airtel zinafanya nini? Airtel mpaka leo haijatoa faida kwa nini msizichukue mkazipeleka TTCL? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni Mwenyekiti ukiuliza swali lazima nilijibu. Kwa heshima yako, tumelichukua wazo lako kuhusu share za Serikali ndani ya Airtel na tunalifanyia kazi. Ni jambo ambalo tunatakiwa tufanye utafiti wa kina, tufanye mambo mengi ya kitaalam, siyo jambo ambalo naweza kutoa jawabu hapa kwa sababu jambo la shares watu ile ni business yao. Hata hivyo, tumelichukua na tutalifanyia kazi tu haina shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, sasa naomba kutoa hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nami napenda kuchukua fursa hii, kama walivyoanza wenzangu, kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia kukutana hapa leo tukiwa na afya njema. Kipekee kabisa napenda nikushukuru wewe mwenyewe kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia hoja za kamati tatu zilizoko mbele yetu.
Mheshimiwa Spika, ninaomba niwashukuru sana Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati pamoja na Wenyeviti wa Kamati zote tatu na Waheshimiwa Wabunge wote waliopata fursa ya kuchangia kwenye hoja hizi. Naomba niwahakikishie Wajumbe wa Kamati kwamba michango yao ni mizuri na tunaendelea kuithamini.
Mheshimiwa Spika, kwa muda wa siku tatu kulikuwa na mchango uliendelea kwa muda mrefu kuhusu KADCO. Ninaomba nami nianze kuzungumzia KADCO.
Mheshimiwa Spika, mwaka 1998 Serikali iliagiza ukodishaji na uendelezaji wa Kiwanja cha Ndege cha KIA (Kilimanjaro International Airport) utekelezwe na kampuni ya binafsi. Hii ilikuwa ni moja kati ya uendelezaji wa Sera ya Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma yaliyofanywa kwa kipindi hicho.
Mheshimiwa Spika, baada ya mchakato wa ubinafsishaji kukamilika, Kiwanja cha Ndege cha KIA ilianzishwa kampuni binafsi ambayo ni KADCO tarehe 11, Machi 1998 chini ya Sheria ya Makampuni sura 212, wakati huo kampuni hiyo ikiwa na wanahisa wawili. Mwanahisa wa kwanza alikuwa ni Motor Mc Donald International ya Uingereza na mwanahisa alikuwa ni Inter- consult Tanzania limited. Baadaye waliongezwa wanahisa wawili ambapo mwanahisa mwingine alikuwa ni Serikali na mwanahisa mwingine wa nne alikuwa ni South African Infrastructure Fund.
Mheshimiwa Spika, wanahisa hao walikuwa na mgawanyo wa hisa kama ifuatavyo: -
(a) Motor Mc Donald International ya Uingereza ilikuwa na hisa 41.40%,
(b) South African Infrastructure Fund ilikuwa na hisa 30%,
(c) Inter Consult Tanzania Limited ya Tanzania ilikuwa na hisa 4.6%, na
(d) Serikali ilikuwa na hisa 24%.
Mheshimiwa Spika, katika ubinafsishaji huu kulikuwa na changamoto kubwa zilizojitokeza. Changamoto ya kwanza iliyojitokeza ni kuwa wanahisa walishindwa kuwekeza kwenye Kiwanja cha Ndege cha KIA, changamoto ya pili ilyojitokeza ni Serikali kutonufaika na mkataba wa uendeshaji wa Kiwanja cha Ndege cha KIA, na Changamoto ya tatu iliyojitokeza ni kukosa kipengele cha kuitaka KADCO kulipa ada ya uendeshaji (concession fee), na changamoto ya nne iliyojitokeza, kulikuwa na exclusive right ya kuzuia uwekezaji au ujenzi wa kiwanja cha ndege ndani ya usawa wa mzunguko (radius) ya kilomita 240. Yaani ndani ya radius ya kilomita 240 hakukutakiwa mwekezaji yeyote awezekujenga kiwanja cha kimataifa.
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hizi Serikali iliona mkataba huo unamaslahi machache. Kwa hivyo Serikali ikaamua kwamba sasa iko haja ya kuvunja mkataba huo. hata hivyo kabla ya hapo kulikuwa na mikataba mitatu ambayo ilisainiwa. Mkataba wa kwanza ilikuwa ni sharehold agreement, mkataba wa pili ulikuwa ni uendeshaji (concession fee) na mkataba wa tatu ni wa ukodishaji (lease agreement) ambao uliwekwa kati ya Serikali na KADCO.
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto zilizojitokeza Serikali ilifanya maamuzi ya kuamua kuwanunua wanahisa. Ambapo Kampuni ya Motor Mc Donald International ya Uingereza ililipwa dola za Marekani 2,752,540.6, hizi ni Dola za Kimarekani, South African Infrastructure Fund ililipwa dola za Marekani 1,994,593.52 na Inter Consult Tanzania Limited ya Tanzania ililipwa dola za Marekani 339,373.01.
Mheshimiwa Spika, baada ya kulipwa fedha hizo na Serikali, Kampuni ya KADCO ikawa asilimia 100 ni Kampuni ya Serikali na share zake zote zipo chini ya Msajili wa Hazina kama ilivyo kampuni nyingine za Serikali. Haya yote yanathibitishwa kupitia hati ya usajili namba 33,616 ya BRELA kuhusu usajili wa KADCO.
Mheshimiwa Spika, baada ya Serikali kununua share hizo, shareholding agreement automatically ilikufa yenyewe kwa sababu wana-share hawapo. Mikataba miwili iliyobaki, concession agreement pamoja na lease agreement zilikuwepo lakini hazikufanyiwa mabadiliko yoyote. Tulitegemea pengine zingefanyiwa mabadiliko na kukawa na agreement back kati ya TAA na KADCO lakini haikufanywa hivyo. Nitaeleza huko mbele hatua ambazo Serikali itazichukua kwa ajili ya kufanya mabadiliko hayo.
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie kidogo kuhusu wafanyakazi wa KADCO. Kama nilivyosema, KADCO ni kampuni ya Serikali kwa asilimia 100 na bodi ya KADCO pamoja na wanabodi wa KADCO na Mwenyekiti wa bodi wanachaguliwa na Serikali na hivi ninavyosema kwamba bodi hii iko na inaenda vizuri.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kuna taarifa kuktoka kwa Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere.
T A A R I F A
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa Waziri, alikuwa ametupeleka vizuri, ametuonesha njia na dola zilivyolipwa na mikataba ile mitatu, sasa angetumaliza kwenye hiyo hoja halafu akaenda ya wafanyakazi ili tukawa na mtiririko mzuri wa mambo hayo. Kwa sababu akiturudisha huku tena tutakuwa tumesahau, atupeleke huko huko alikokuwa anatupeleka tumalizie. Ahsante.
SPIKA: Mheshimiwa Getere yeye ndiyo alilvyopanga mtiririko wa mchango wake sasa tusimchanganye ila tusikilize kama unalo kwenye hili analosema unaruhusiwa kutoa taarifa, lakini yeye amepanga mtiririko ambao yeye anauelewa maana yeye ndiyo anatoa maelezo. Mheshimiwa Waziri.
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, nitakwenda hivyo anavyotaka kwa sababu kila kitu kiko hapa, hakuna tofauti yoyote. Kama nilivyosema KADCO ilianzishwa kama kampuni kwa sura ya 212. Lakini TAA (Tanzania Airport Authority) ilianzishwa kupitia tangazo la Serikali Namba 404 la mwaka 1999 chini ya kifungu namba tatu cha Sheria ya Uwakala wa Serikali. Kwa vile Tanzania Airport Authority si mamlaka, inaitwa tu jina hilo kwa sababu sheria iliyoanzisha ilikuwa ni Sheria ya Uwakala wa Serikali Sura Namba 244 ya mwaka 1997.
Mheshimiwa Spika, katika kutatua tatizo la KADCO na kuweka utaratibu mzuri wa kuendesha viwanja vya ndege, Serikali tumeanza mchakato wa kutengeneza Sheria ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kama mamlaka, na kwenye sheria hiyo tutahakikisha kwamba KADCO inaelekezwa vizuri. Kwenye sheria hiyo, tutahakikisha kwamba KADCO inaelekezwa vizuri, aidha imilikiwe moja kwa moja; sasa hivi inamilikiwa na TAA, lakini imilikiwe ndani ya sheria au alternative ifanyike kwamba, ianzishwe kampuni tanzu ambayo yenyewe ndiyo itaendesha Kiwanja cha Ndege cha KIA. Suala la KADCO linaweza kuwepo ama linaweza kufa moja kwa moja, itategemea sheria itakavyoelekeza. Hayo tutayafanya sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, siyo hilo tu, kwenye sheria hiyo tunaangalia utaratibu ambao utavifanya viwanja vyetu vya ndege viwe salama na ulinzi ukamilike kwa sababu kuna changamoto kubwa sana kwenye viwanja vya ndege. Sheria iliyopo sasa hivi haikidhi uendeshaji wa viwanja vya ndege.
Mheshimiwa Spika, ninaamini kwamba sheria hii itakapokuja kupitishwa hapa Bungeni tatizo la KADCO litamalizwa maisha, litakuwa limeisha. Inaweza kuendeshwa moja kwa moja kupitia TAA yenyewe au inaweza kuanzishwa kampuni nyingine ambayo itasimamia Kiwanja cha Ndege cha KIA.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Saashisha Mafuwe.
T A A R I F A
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa kwamba wananchi wa Hai sasa hivi wako kwenye TV wanasubiri maagizo ya Serikali kwenye jambo hili. Ameeleza historia vizuri, akaja akatuambia KADCO ni ya Serikali, katikati hapa anasema inaweza ikawepo au isiwepo. Kwa hiyo, nataka tu kumwambia, leo tunategemea kupata majibu ya Serikali thabiti kwamba KADCO ni ya Serikali au siyo ya Serikali; na hatma yake ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, natoa taarifa yangu kwa sababu kule kuna jambo linaendelea na hizi taarifa kule zinachanganya wananchi. Sasa hapa tunaambiwa ni ya Serikali asilimia 100, lakini inaweza ikaondolewa au isiondolewe. Serikali inasemaje kuhusu jambo hili ili sisi wananchi wa Hai tunaosikiliza Serikali hapa tujue hatma ya jambo hili? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kikanuni unapotoa taarifa ni kwamba unamwongezea yule mchangiaji jambo fulani, siyo unamwuliza maswali. Sijui tunaelewana! Eeh, yaani siyo umwulize maswali, sasa inakuwa kimegeuka kuwa kipindi cha maswali na majibu. Hapa anayeruhusiwa kuuliza maswali ni mimi hapa. Mimi ndio naruhusiwa kuuliza maswali, lakini ninyi toeni tu taarifa kwa mujibu wa kanuni zetu.
Mheshimiwa Waziri, malizia mchango wako.
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, tutaleta sheria hapa kama nilivyosema ambayo itaeleza mfumo mzima wa uendeshaji wa viwanja vya ndege, ikiwemo Kiwanja cha Ndege cha KIA. Wakati utafika Waheshimiwa Wabunge nyote mtapata hiyo fursa, mtalichambua jambo hili kwa kina na ushauri wenu sisi tutaupokea.
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla.
T A A R I F A
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, napenda kumpa taarifa Mheshimiwa Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kwamba Serikali kupitia Kikao cha Baraza la Mawaziri namba 15 cha mwaka 2009 kilichofanyika Mei 14 mwaka huo, kilielekeza kwamba Wizara ya Uchukuzi iache majadiliano na Kampuni ya Omniport ambayo ilikuwa inataka ikabidhiwe Uwanja wa Ndege wa KIA badala ya KADCO kwa kuwa KADCO alishindwa kuwekeza. Taarifa zilizoletwa zilionesha kwamba hata huyo Omniport ambaye alikuwa apewe huo uwanja, naye hakuwa na uwezo wa kuwekeza, ilikuwa ni usanii. Hatua ya kwanza.
Mheshimiwa Spika, hatua ya pili, Serikali…
SPIKA: Mheshimiwa taarifa ni moja.
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, inaendana na hiyo tu. Ni kwamba katika maamuzi hayo ya Serikali, ikaelekezwa kwamba KADCO, huyo Omniport wote watolewe, Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro urudishwe chini ya mikono ya TAA. Sasa ni kwa nini haukurudishwa na mpaka leo hii tunajadili KADCO wakati maelekezo ya Serikali yalikuwa upelekwe chini ya mikono ya TAA? (Makofi)
SPIKA: Sawa ahsante. Mheshimiwa Waziri unaipokea taarifa hiyo?
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, inanipa taabu kwa sababu kujibu kwa nini haikurejeshwa, hilo swali siwezi kulitolea ufafanuzi hapa.
SPIKA: Nami nimekusaidia. Yaani mtu akitoa taarifa, ni ile taarifa ambayo haina swali, kwa sababu wewe siyo kazi yako kujibizana na Mbunge. Au umeshamaliza mchango wako? Wewe malizia mchango wako, kama taarifa yake unaona imeuliza swali, wewe endelea na mchango. Maswali ni mimi hapa ndio naruhusiwa kuuliza.
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, kuhusu wafanyakazi wa KADCO, kama nilivyosema, KADCO ni kampuni ya Serikali na Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Mwenyekiti wanachaguliwa na Serikali. Hivi ninavyozungumza, tuna bodi pamoja na wajumbe wote na wanafanya kazi. Wafanyakazi wote wa KADCO ni Watanzania. Pia KADCO inayo mwanasheria ambaye anaitwa Winfrey Komba ambaye yeye alihamishwa KADCO mwezi Januari, 2021.
Mheshimiwa Spika, pia KADCO inaendelea kulipa kodi mbalimbali, kwa mfano tu imelipa gawio mwaka 2016/2017 Shilingi milioni 555; mwaka 2017/2018 ililipa Shilingi milioni 583; mwaka 2018/2019 ililipa Shilingi bilioni moja; miaka miwili iliyofuatia 2019/2020 na 2021 haikulipa kutokana na ugonjwa wa Covid na sekta ya anga iliathiriwa kwa asilimia kubwa. Pia KADCO inayo akaunti Benki Kuu ya Tanzania na malipo yote yanayofanywa na makampuni ya ndege yanawasilishwa kule. Hiyo ni hoja kuhusu KADCO.
Mheshimiwa Spika, pia naomba niongelee hoja kuhusu maingiliano kati ya TANROADS na TAA kuhusu ujenzi wa viwanja vya ndege. Ni kweli yalifanyika maamuzi mwaka 2018 kuhamisha ujenzi wa viwanja vya ndege kwenda TANROADS. Kulikuwa na changamoto ambazo zilisababisha kufanya hivyo na ilifanya hivyo kupitia GN namba 293 ya mwaka 2000 ya TANROADS ambayo ilifanyiwa mabadiliko ili kazi hiyo iweze kufanyika ndani ya TANROADS.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Dakika moja malizia mchango wako.
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea, sasa hivi tumeshafanya mchakato na ujenzi wa viwanja vya ndege sasa vitaanza kurejeshwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA). Ila kwa ile miradi ambayo inaendelea, kwa mfano Kiwanja cha Ndege cha Shinyanga, Sumbawanga, Kigoma na Tabora, mchakato utaendelea chini ya TANROADS kwa sababu tukiurejesha tena utachukua muda mrefu na viwanja vya ndege hivyo havitajengwa.
Mheshimiwa Spika, pia kuhusu Kiwanja cha Ndege cha Msalato ambacho kinajengwa chini ya ufadhili wa ADB nacho kitaendelea kutekelezwa na TANROADS kwa sababu mchakato wenyewe kuurejesha tena utatuchukua muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, suala la mwisho ambalo nilitaka kuligusia ni kuhusu suala la Bandari ya Tanga. Mheshimiwa Kapinga alilizungumza kwa hisia kali suala hili, lakini naomba kumwambia tu na Wabunge wote na Watanzania kwa ujumla kwamba Bandari ya Tanga ni muhimu sana kwetu sisi na tunaendelea na ujenzi na mkandarasi yuko site. Kuhusu kwamba kuna Mkandarasi alipewa subcontract kwa bei ndogo, hili linafanyiwa kazi na CAG na naliomba Bunge lako Tukufu, utupe muda CAG afanye uchunguzi maalum, halafu tutapata ripoti na tutaifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. (Makofi)
SPIKA: Naamini Mwenyekiti ameshasikia. Sasa katika ufafanuzi wako Mheshimiwa Waziri; kwanza Waheshimiwa Wabunge mtakumbuka ile siku nadhani ni juzi, nilisema ningempa nafasi Mheshimiwa Waziri leo na amepewa. Nilisema katika majibu yake, mojawapo ya mambo anatakiwa atuambie ni akaunti za KADCO ziko wapi? Leo amejibu hapa, nadhani mmemsikia, amesema akaunti za KADCO ziko Benki Kuu. Nimesikia vizuri Mheshimiwa Waziri au sijasikia vizuri?
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ndiyo akaunti ya KADCO iko BOT.
SPIKA: Sawa. Sasa Mheshimiwa Waziri ili tuongozane vizuri kwenye haya maazimio ya Kamati na Wenyeviti wanasikiliza hapa kwa sababu kuna maeneo watafanya marekebisho kwa kuwasikiliza na kama watakuwa wameelewa. Wakati hii KADCO ilikuwa ni kampuni binafsi; na natumia neno “ilikuwa kampuni binafsi”, Serikali ikanunua shares zote, ikalipa pesa wale watu binafsi; ikahamia kuwa kwenye umiliki wa Serikali kwa asilimia 100. Mkataba ambao umesema kwamba ulikufa, ni mkataba mmoja tu kati ya mitatu uliyoitaja, kwamba ni ule mkataba wa hisa ndiyo uliokufa. Mkataba wa upangishaji (lease agreement) bado upo, kwa maelezo uliyotoa. Mkataba wa concession ambao ulikuwa unaipa kampuni binafsi mamlaka ya kuendesha pale na kufanya hivi, bado upo. Huu mkataba wa upangaji, nani ni mpangaji sasa na nani mpangishaji? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, kama ulivyosema kuna mikataba miwili ambayo ipo concession agreement na lease agreement na mikataba hii ilikuwa kati ya Serikali na KADCO. Kwa hiyo,…
SPIKA: Ilikuwa kati ya Serikali na KADCO wakati KADCO ni binafsi.
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ni wakati huo. Wakati huo KADCO ilikuwa ni Kampuni ya binafsi, lakini baadaye KADCO ilibadilika kuwa kampuni ya Serikali kwa asilimia 100.
SPIKA: Hapo tuko wote, pamoja kabisa. Hoja ni kwamba, huu mkataba wa upangishaji, kabla hata sijaenda kwenye concession, mkataba wa upangishaji ni kati ya nani na nani kwa sasa? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, mikataba hii ilikuwa ifanyiwe mabadiliko, lakini ilivyo sasa hivi…
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, siyo hoja yake binafsi ni hoja ya Serikali, wala siyo yeye aliyekuwa ofisini. Kwa hiyo, msiwe mnamtaza kama vile…
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, mkataba ulivyo sasa hivi hata ukichukua mkataba ule unaona ni kati ya KADCO na Serikali…
SPIKA: KADCO binafsi?
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, KADCO binafsi, lakini ilibadilika kuwa ya Serikali.
SPIKA: Sawa, ahsante. Ngoja, hapo tumeshaelewa. Mkataba wa upangishaji ni kati ya KADCO binafsi ambaye alishakufa, lakini kwenye mkataba huu anaishi. Sawa. (Makofi)
Halafu concession agreement pia ilikuwa kati ya KADCO binafsi na Serikali. Niko sahihi?
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ndiyo, lakini KADCO mpaka sasa hivi ipo, isipokuwa zile shares zilibadilika kutoka watu binafsi kuja kwenye Serikali.
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, nilitaka kuyaelewa haya ili tunapoelekea kwenye maazimio tujue tunaazimia nini? Maana ni jambo la muda mrefu. Haiwezekani kila siku inazungumziwa KADCO, KADCO, KADCO! Lazima tufike mahali. (Makofi)
Jambo la mwisho Mheshimiwa Waziri, huu mkopo ambao TAA iliagizwa kukopa na Serikali, kwamba kwa kuwa wewe ndio unashughulika na viwanja vya ndege, kopa kalipe. Huu mkopo analipa nani? TAA au KADCO ya Serikali?
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, kama ulivyosema kwamba mkopo huu Serikali iliagiza TAA ikope na imelipa TAA kutoka Benki…
SPIKA: Imelipa TAA na siyo KADCO?
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, siyo KADCO.
SPIKA: Haya, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nami napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutupa fursa ya kuchangia kwenye hoja muhimu ya Serikali iliyoko mbele yetu. Kabla ya yote, napenda kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Wabunge wengi wamechangia, hasa kuhusu miundombinu, kwani Wabunge wengi wanafahamu bila miundombinu nchi yetu haiwezi kuingia katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianzia na Mheshimiwa Hawa Ghasia, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Miundombinu, ametoa hoja ifuatayo: katika Mpango wa Maendeleo wa Mwaka Mmoja Serikali imeainisha miradi saba ya kielelezo itakayohitaji mtaji mkubwa wa uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Miradi hiyo ni ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge, ununuzi na ukarabati wa meli kwenye Maziwa Makuu, kuboresha Shirika la Ndege Tanzania, ujenzi wa Barabara ya Kidahwa – Kanyani, Kasulu – Kibondo – Nyakanazi na Barabara ya Masasi – Songea – Mbaba Bay pamoja na mradi wa makaa yam awe na Mchuchuma na mradi wa chuma wa Liganga.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati inataka Serikali kuainisha miradi itakayotekelezwa kwa mfumo wa Public Private Partnership, muda wa kukamilisha na gharama za mradi husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu hoja hiyo, kama ifiuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kutekeleza miradi ya barabara kwa kushirikisha sekta binafsi kwa utaratibu wa PPP.
Kwa sasa mradi pekee wa barabara ambao umepangwa kutekelezwa kwa utaratibu huu ni ujenzi wa Barabara ya Dar es Salaam – Chalinze Express Way. Barabara hii inatarajiwa kuwa na urefu wa kilometa 140 itakapokamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu wa mradi huu upo katika hatua za mwisho za kukamilishwa. Mara baada ya hatua hii kukamilika gharama za awali na muda wa utekelezaji wa mradi huo utajulikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Ghasia alikuwa na hoja ifuatayo; ushauri kwa Serikali kuhakikisha inahusisha Sekta binafsi kwa kugharamia mradi kwa njia ya ushirikishi yaani PPP pamoja na kutumia fedha zake za ndani ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo. Ushauri umepokelewa, Serikali imepanga kutekeleza miradi mingi iwezekanavyo ya miundombinu ya usafiri kwa njia ya PPP kila inapowezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge kama ifuatavyo; kwanza ushauri kwa Serikali kuhakikisha sekta wezeshi zinatekeleza miradi kikamilifu kwa bajeti iliyotengwa kwa miradi hiyo. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Chunya hadi Itigi, na barabara ya Ipole hadi Ikoga. Ushauri umepokelewa kwa barabara ya Chunya hadi Itigi upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umekamilika kwa barabara yote yenye urefu wa kilometa 413 na barabara hii itajengwa kwa awamu. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa shilingi bilioni 5.84 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kiwango cha lami wa sehemu ya Itigi - Mkiwa yenye kilometa 35. Kwa sehemu iliyobaki Serikali itaendelea kujadiliana na washiriki wa maendeleo ili zipatikane fedha kwa ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa barabara ya Ipole, Koga hadi Mpanda hatua za ununuzi wa Wahandisi Washauri watakapofanya mapitio ya usanifu na usimamizi, pamoja na mkandarasi atakayejenga barabara hiyo zinaendelea. Ujenzi umepangwa kuanza katika mwaka wa fedha 2016/2017, jumla ya shilingi bilioni 103.93 zimetengwa kama inavyooneshwa kwenye kitabu changu cha bajeti ukurasa 223.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna hoja kutoka kwa Mheshimiwa Josephat Kandege, Mbunge wa Kalambo kama ifuatavyo; kwanza anatoa pongezi kwa Serikali, pongezi hizo zimepokelewa, pia anatoa ushauri kwa Serikali kuwathibitishia au kuondoa wataalam wanaokaimu nafasi mbalimbali za uongozi katika taasisi na Serikali Kuu ili kuboresha uwajibikaji wa watumishi husika.
Kwanza ushauri huo umepokelewa, pili Serikali inaendelea na utaratibu wa kuhakikisha kuwa wataalam wote ambao sasa hivi wanakaimu wanafanyiwa confirmation ili wawe na muda wa kutosha wa kufanya kazi hiyo. Kwa kuanzia tu wiki iliyopita tulitangaza Bodi ya TPA ambayo sasa imeanza kufanya kazi, hatua inayofuata sasa hivi ni kumchangua Mtendaji Mkuu wa Bandari au Mamlaka ya Bandari ili aweze kuendelea na kazi hiyo ya kuendesha bandari zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna hoja ya Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau wa Jimbo la Mafia ambapo hoja yake inasema kama ifuatavyoa; Serikali itoe mchanganuo wa muda wa utekelezaji yaani timeframe ya miradi yote ya maendeleo pamoja na gharama zake na siyo tu kwa ujumla kwa mfano ujenzi wa kiwango cha express way wa barabara ya Dar es Salaam hadi Chalinze.
Kwanza ushauri umepokelewa Mheshimiwa Mbunge, muda halisi wa ujenzi wa barabara ya Chalinze express way utajulikana baada zabuni kutangazwa na mwekezaji kujulikana. Kwa sasa mtaalam elekezi anakamilisha upembuzi yakinifu wa mradi huo na wakati huo utakapofika muda maalum utaelezwa kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia alikuwa anahoja Serikali ijengwe….
Mheshimiwa Naibu Spika, narejea tena naomba kuunga mkono hoja asilimia moa moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana katika Bunge hili tukufu la bajeti hii kukamilisha kazi tuliyoianza jana tarehe 22 Mei, 2023 ambapo niliwasilisha hoja hii.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kukushukuru wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wenyeviti wote wa Bunge kwa jinsi mlivyoliongoza na kusimamia majadiliano ya hoja hii. Aidha, nachukua fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge letu Tukufu kwa kuwa wazi na kutoa maoni na michango yao ya kina wakati wa majadiliano haya. Ninawathibitishia kwamba michango yenu yote tumeichukua kwa uzito mkubwa na kwenda kuifanyia kazi ili kuendelea kuleta ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
Mheshimiwa Spika, kipekee naomba nimshukuru Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Selemani Moshi Kakoso na Waheshimiwa Wajumbe wote wa Kamati kwa hoja nzuri zilizotolewa na Kamati yake. Nakiri kwamba hoja hizo ni muhimu sana kwa maendeleo na ukuaji wa sekta ya ujenzi na uchukuzi hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliyochangia katika bajeti yangu. Waheshimiwa Wabunge 75 wamechangia wakati wa majadiliano ya hoja hii ambapo Waheshimiwa 67 wamechangia kwa kuongea na Waheshimiwa nane wamechangia kwa maandishi. Waheshimiwa Wabunge, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja kuu zilizowasilishwa katika majadiliano haya ni kama ifuatavyo:- Kwanza kabisa ni ujenzi na ukarabati wa barabara mbalimbali nchini ambayo imezungumzwa kwa kina Mheshimiwa Naibu Waziri anayesimimia Sekta ya Ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la pili lilikuwa ni utekelezaji wa miradi kwa utaratibu wa EPC + Finance ambao leo ndiyo mpango mzima katika Bunge letu. Hii imezungumzwa kwa kina na Mheshimiwa Naibu Waziri anayesimamia sekta ya ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, masuala ya fidia kwa wananchi waliyoathirika na ongezeko la upana wa eneo la hifadhi ya Barabara. Kuna suala la ongezeko la gharama ya miradi ya barabara (variation) kwenye miradi ya barabara, kuna suala la ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uendeshaji na uendelezaji wa bandari zetu hasa Bandari ya Dar es Salaam. Pia kuna suala la marekebisho ya Sheria ya Reli ya TAZARA na Reli ya TRC ambalo limezunguzwa kwa kina na Mheshimiwa Naibu Waziri anayesimamia sekta ya uchukuzi.
Mheshimiwa Spika, la saba usimamizi, uendeshaji na uendelezaji wa viwanja vya ndege ambayo imezungumzwa kwa kina na Mheshimiwa Naibu Waziri anayesimamia sekta ya uchukuzi. Kuna hoja nyingine ya ukamilishaji wa ujenzi wa Reli ya SGR na kuanza kutoa huduma kwa vipande vilivyokamilika; na hii imeshazungumzwa; na kuna umiliki wa Shirika letu la Ndege la Air Tanzania; na mwisho, kuna suala la ujenzi na ukarabati wa meli katika Ziwa Tanganyika ambapo na yenyewe imeshazungmzwa na Mheshimiwa Naibu Waziri anayesimamia sekta ya uchukuzi.
Mheshimiwa Spika, muda mchache uliopita kama nilivyosema Waheshimiwa Naibu Mawaziri wa Wizara yangu wamemaliza kujibu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge kwa kuzingatia maeneo ya kisekta kwa ufasaha na weledi mkubwa, ahsanteni sana Waheshimiwa Naibu Mawaziri, ninashukuru sana kwa jinsi ambavyo mmejibu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge na mimi nitajaribu kujibu hoja chache zilizobakia. Aidha, naomba kulihakikishia Bunge lako tukufu kwamba Wizara itajibu hoja zote za Waheshimiwa Wabunge kwa maandishi na kuziwasilisha Bungeni kabla kuhitimisha kwa Mkutano wa Bunge hili la Bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nianze kuhitimisha hoja yangu kwa kutoa ufafanuzi wa kiujumla kwa baadhi ya hoja zilizojitokeza kwenye maeneo makubwa yaliyojitokeza. Kwanza kwenye sekta ya uchukuzi; hoja kubwa ambayo imejitokeza kwenye mjadala wetu huu ni ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uendeshaji na uendelezaji wa bandari nchini.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge takribani 80% waliochangia sekta ya uchukuzi wamejikita zaidi kwenye ushirikishwaji wa sekta binafsi kwenye uendeshaji na uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam. Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia wamekubaliana na hoja hii na wengine wamechangia kwa hisia kali sana na wamesema tumechelewa kuleta sekta binafsi kwenye uendeshaji na uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam. (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge tumewasikia, Serikali tumewasikia tunaenda kulifanyia kazi mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa wamefanya hivyo kwa sababu wanajua Bandari ya Dar es Salaam ndio lango kuu la uchumi wa nchi yetu. Asilimia 37 takribani trilioni 7.78 ya makusanyo ya mapato ya kiforodha ya TRA yanakusanywa kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Hili ni jambo kubwa na hili ni jambo muhimu na lazima tulisimamie kwa nguvu zetu zote. Aidha, mara nyingi Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kwamba bandari inaweza kuchangia asilimia kubwa sana ya bajeti ya nchi yetu kama tutaisimamia vizuri na kwa uadilifu mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niwapitishe haraka kwa utendaji usioridhisha wa Bandari ya Dar es Salaam; TPA mwaka 2015/2016 ilihudumia mizigo tani 15,670,000; na mwaka 2020/2022 ilihudumia takribani mizigo tani 20,730,000 sawa na ongezeko la asilimia 30.5. Kiwango hiki kinaonekana ni kikubwa ambacho ni wastani wa ongezeko la asilimia 4.3 lakini ni kidogo kutokana na mpango mkakati wa TPA ambayo ilisema kwamba lazima ongezeko la bandari la mizigo liwe kati ya asilimia 10 mpaka asilimia 12.9 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, kuna sababu ambazo zimechangia kutofikia lengo hili; sababu ya kwanza ni changamoto ya uendeshaji. Sababu ya pili kubwa ni changamoto ya ucheleweshaji wa mizigo pale nangani Bandari ya Dar es Salaam. Meli inakuwa-charged demurrange charge ya takribani dola 25,000 kwa siku ikichelewa na gharama hizi zote zinakwenda kwa mlaji yaani mimi na wewe.
Mheshimiwa Spika, changamoto ya tatu ni changamoto ya uwekezaji mdogo kwenye ununuzi wa mitambo, bandari zozote ni lazima uwe na mitambo ya kisasa na mitambo mikubwa sana.
Mheshimiwa Spika, changamoto ya nne ni usimikaji wa mifumo ya TEHAMA ambayo imesababisha ucheleweshaji mkubwa wa utoaji wa mizigo bandarini;na changamoto ya tano ni ukarabati na ujenzi wa magati mapya. Bandari ya Dar es Saalam ina magati kumi na mbili tu, lakini bandari nyingine mtaona zina magati karibuni hamsini. Pia mwisho kulikuwa hakuna ufumbuzi katika mnyororo mzima wa usafirishaji wa mizigo kuanzia kwenye meli mpaka kwa mdau ambaye unampelekea huduma hiyo.
Mheshimiwa Spika, Bandari ya Dar es Salaam ina ushindani mkubwa kwenye bandari nne duniani hasa kwenye mizigo ya Zambia, Malawi, Rwanda, Uganda na DRC. Bandari ya kwanza ambayo inatupa pressure kubwa na ushindani mkubwa ni Bandari ya Mombasa. Bandari ya Mombasa inamilikiwa na Mamlaka ya Bandari ya Kenya. Bandari hii ina gati kumi na saba, Dar es Salaam tuna gati kumi na mbili. Magati kumi na tatu ni ya mizigo ya kawaida, magati sita ni kwa ajili ya kuhudumia makasha na kati hiyo bandari ya kuhudumia makasha, Container Terminal Two inaendeshwa na private sector, haiendeshwi na Kenya Port Authority, private sector. Inaendeshwa na Mediterranean Shipping Company hii ni kampuni ya Kiitaliano, hakuna suala la usalama, hakuna suala la nini, inaendesha hiyo kazi.
Mheshimiwa Spika, bandari ya pili ni gati maalum kwa ajili ya kushushia nafaka (Grain Terminal) ambayo inaendeshwa na private sector, Grain Bulk Handler Limited ya Kenya ndio inaendesha, ni private sector. Kwa hiyo, tusiogope private sector kwenye kuendesha bandari. Tusiwe waoga, ni aibu kuona mtu anasimama anasema anaogopa private sector, inaonekana mtu wa ajabu kwenye kuendesha bandari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bandari nyingine ambayo inatupa pressure kubwa ni bandari ya Durban. Bandari ya Durban inamilikiwa na Transnet National Port Authority ya South Africa. Bandari hii ina magati 50. Magati 31 ni ya kawaida, magati ya kuhudumia makasha ni kumi na magati kwa ajili ya mafuta, makaa ya mawe na chuma ni tisa. Magati 31 ya kawaida na magati kumi ya kuhudumia makasha inaendeshwa na Transnet Port Terminal siyo Transnet National Port Authority, hii ni kampuni tofauti. Magati tisa ya mafuta na makaa ya mawe na biashara au bidhaa za chuma na saruji yanaendeshwa na private sector, Durban Bulk Spring Company inaendeshwa na Spring Leaf na Total Bad Freight ni private sector.
Mheshimiwa Spika, kwa vile duniani kote unapokwenda ni private sector inaendesha bandari hasa maeneo ya kontena.
Mheshimiwa Spika, Bandari ya Beira, Msumbiji; hii ni bandari inayotupa ushindani mkubwa. Bandari hii inamilikiwa na Shirika la Bandari na Reli la Msumbiji na ina magati kumi na moja. Magati ya shehena za mchanganyiko na magati ya kushushia kontena. Gati hizi zote za shehena ya mchanganyiko na magati ya kushushia makontena au makasha inaendeshwa na kampuni ya Gold Elder Mozambique ambayo yenyewe ni private sector.
Mheshimiwa Spika, ukienda bandari inayotupa pressure tena ya Namibia Bandari ya Walvis Bay ya Namibia. Bandari hii inamilikiwa na Mamlaka ya Bandari Namibia na gati ya kushushia makontena au makasha inaendeshwa na kampuni ya Terminal Investment Limited ni private sector na hakuna issue ya security, watu wanaogopa; tunaogopa nini Watanzania? Ni aibu kuwa tunaogopa ogopa, ni aibu sana.
Mheshimiwa Spika, natoa mifano ya bandari mbili za mwisho; Bandari ya Tanger Med Port ya Morocco. Bandari hii inamilikiwa na Mamlaka ya Bandari ya Tanger Med ya Morocco, ina magati manne ambayo yanafanya kazi ya kushusha makontena ambayo yana uwezo wa kushusha kontena 9,900,000 kwa mwaka, wakati bandari ya Dar es Salaam inashusha makontena 760,000; hii inashusha 9,900,000 na ina terminal nne au ina magati manne makubwa. Gati ya kwanza inaendeshwa na private sector ambaye anaitwa MPM Terminals, gati ya pili inaendeshwa na private sector inaitwa Euro Gate ya Europe; gati ya tatu inaendeshwa na private sector na gati ya nne inaendeshwa na private sector. Zote zinaendeshwa na private sector.
Mheshimiwa Spika, naweza kutaja yaani bandari nyingi duniani zinaendeshwa na private sector na hatujawahi kusikia issue ya security na hizi kampuni zinafanya vizuri lazima Watanzania tubadilike.
Mheshimiwa Spika, tuna uzoefu sisi wa kuendesha TICTS katika endeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam. Itakumbukwa kuwa kwa mara ya kwanza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliingia mkataba na TICTS mnamo mwaka 2000 wa kukodisha Kitengo cha Makasha cha Bandari ya Dar es Salaam, kuanzia gati namba nane mpaka namba kumi na moja. Mkataba ule kwanza ulikuwa na shida, lakini mwaka 2017 tulikaa sisi na timu ya wataalam, tulibadilisha mkataba ule na ndiyo iliyotusaidia tukaweza kumalizana nao mwezi Desemba mwaka huu.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na mapungufu mengi kwenye utendeshaji wa TICTS. TICTS haikuweza kuleta ufumbuzi katika mnyororo mzima wa usafirishaji wa mizigo na matokeo yake kwanza ilitokea alishindwa kufikia viwango vya kimataifa vya ushushaji wa mizigo na matokeo yake meli zilikaa nangani kati ya siku kumi mpaka siku kumi na nne. Kulikuwa na ucheleweshwaji mkubwa wa mizigo kutoa bandarini na tukalazimika tusiendelee tena na ule mkataba wa TICTS.
Mheshimiwa Spika, tunahitaji wawekezaji mahiri kwenye Bandari za Dar es Salaam. Tunahitaji au Serikali inahitaji waendeshaji na wawekezji wa bandari ambao wana ujuzi wa kimataifa ambao tunawaita Global Port Operators wenye uwezo na sifa zifuatazo; kwanza wawe na uwezo wa kufikia viwango vya kimataifa pamoja wawe na ufanisi utakaowezesha Bandari ya Dar es Salaam kuwa washindani na bandari nyingine; hiyo ni condition ya kwanza.
Pili, wawe na uwezo wa kutoa ufumbuzi katika mnyororo mzima wa usafirishaji (end to end total logistic chain solution) kutoka toka mzigo unaingizwa kwenye meli mpaka unafika kwa mteja.
Tatu, wawe na mtandao mpana wa kupata mizigo kwenye soko la usafirishaji mali duniani. Hatutaki mtu ambaye hata kutafuta mzigo hawezi, hapana tupate kampuni kubwa ya kimataifa amabyo inajulikana duniani; na nne, wawe na uwezo wa kimataifa katika kuendeleza na kuendesha shughuli za kibandari.
Mheshimiwa Spika, kama tutapata wawekezaji kama hao matokeo yake ni kama ifuatavyo; kwanza kupunguza muda wa meli kukaa nagani kutoka siku tano za sasa mpaka kufikia saa 24 au siku moja. Hii itaongeza idadi ya meli zinazokuja bandari ya Dar es Salaam.
Pili, kupunguza muda wa ushushaji wa makasha kutoka siku nne za sasa mpaka kufikia siku moja na nusu; tatu kupunguza muda wa uendeshaji mizigo (truck turn around) kutoka saa mbili za sasa hadi kufikia dakika thelathini. Gari inaingia within thirty minutes inatoka bandarini. Huyo ndiyo mtu tunayemtaka.
Mheshimiwa Spika, nne, kuongeza shehena ya mzigo kutoka tani 20,108,000 za sasa mpaka kufikia tani 47,570,000 mwaka 2033; tano, kuongeza mapato yanayotokana na kodi ya forodha kutoka shilingi trilioni 7.756 mwaka 2022/2023 mpaka kufikia trilioni 26.709 mwaka 2030, tunamtaka mtu kama huyo. Tukifikia hapa 70% au 80% ya bajeti itakuwa inatoka bandarini; na sita, kulinda ajira zilizopo na kuongeza mnyororo wa ajira mpya mpaka kufikia 28,990 tunataka mtu kama huyo.
Saba, kushusha kwa gharama ya usafirishaji kupitia bandari ya Dar es Salaam ambapo itachangia kupunguza gharama za bidhaa zinazoingia nchini; na nane, tunataka mtu ambaye kuchagiza ukuaji wa sekta nyingine za usafiri kama vile reli, mnajua tumetumia pesa nyingi kujenga reli, tunataka mtu atakayeleta mzigo wa kutosha ili kuipa reli yetu mzigo wa kutosha, huyo ndio muwekezaji tunayemtaka.
Mheshimiwa Spika, suala la uwekezaji halina mjadala, Serikali imeamua inakwenda mbele lazima Bandari ya Dar es Salaam tuweke wawekezaji ambao wataleta maslahi mapana ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo; Bandari ya Dar es Salaam ina limitations zake na limitations za Bandari ya Dar es Salaam inakuja kwa sababu kila siku kuna meli mpya za teknolojia mpya. Kwa mfano, meli ambayo inaweza kubeba makontena 18,000 yenyewe kwenye entrance channel inatakiwa mita 250, Bandari ya Dar es Salaam sasa hivi entrance channel pale inapovuka ferry ni mita 170, hatuwezi ku-extend tena itafika wakati.
Mheshimiwa Spika, sasa tukitaka meli kubwa zenye urefu wa mita 370 lazima twende Bandari ya Bagamoyo na ndugu zangu Serikali imeshaamua mwaka huu wa fedha kwenye bajeti tumezungumza ukienda kwenye ukurasa wa 117 kifungu cha 11 tumesema tunaenda kuanza Bandari ya Bagamoyo. Bandari ya Dar es Salaam itafanya kazi, lakini kwa zile meli kubwa ambazo zitashindwa kuingia kwenye Bandari ya Dar es Salaam itakwenda Bandari ya Bagamoyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri alilizungumzia hili la reli ya Mchuchuma, hili jambo limezungumzwa mara nyingi na Mheshimiwa Kingu amelizungumza leo hapa na amelizungumza kwa uchungu mkali na hisia kali na kwa kweli feasibility study imeshafanyika. Lakini Waheshimiwa Wabunge ninaomba sana Sheria yetu ya PPP sasa hivi ni ngumu sana kuleta mwekezaji, lakini tumepata fursa nimeshasema mara ya kwanza, mara ya pili nategemea itakuja, ninaomba sana tufanye maboresho makubwa ili tuweze kufungua nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tutasema, tutazungumza lakini bila ya kufanya mabadiliko kwenye Sheria yetu ya PPP hatutoweza kuwafanyia watanzania haki. Waheshimiwa Wabunge tuna jukumu kubwa na sheria hiyo itakuja ninaomba tuifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna suala la umiliki wa ndege, tumekubaliana na Wabunge wote kwa kweli suala la umiliki wa ndege ni sahihi liende Air Tanzania na Serikali imeunda timu ya wataalam, inajumuisha wataalam hapa nchini na kutoka nje wenye uelewa wa masuala ya usafiri wa anga na uendeshaji wa mashirika ya ndege ili kupitia muundo wa sasa wa Air Tanzania ikiwa ni pamoja na suala la umiliki wa ndege. Timu hiyo tayari imekamilisha kazi yake na itawasilisha taarifa yake kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri wakati wowote na uamuzi utatoka. Naomba niwahakikishie tu kwamba tutafanya maamuzi sahihi kwa maslahi ya Air Tanzania na kwa maslahi ya Watanzania kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende kwenye sekta ya ujenzi; kupanda kwa gharama kwneye miradi ya maendeleo TANROADS; kuna mambo ya msingi ambayo yanasababisha kupandisha gharama za miradi. Jambo la kwanza kabisa ni mabadiliko ya usanifu (poor design), miradi mingi inapandisha hela ama miradi mingi inaongezeka hela kwa sababu ya poor design, hili tumelijua ndani ya TANROADS tumejipanga sasa kwamba tuhakikishe kuwa design tunazozifanya zinaenda na viwango vinavyotakiwa.
Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo linasababisha kupanda kwa gharama za ujenzi ni mabadiliko kwenye site. Unaweza ukaanza site yako ya ujenzi, ukafika pahala ukakutana na mwamba, hiyo lazima itabadilisha gharama za ujenzi.
Mheshimiwa Spika, ya tatu ni mpangilio mbovu wa kazi; kama unaenda kufanya kazi, lakini mpangilio wako siyo sahihi hiyo definitely itabadilisha gharama za ujenzi na hili tumelijua TANROADS tunajipanga vizuri.
Suala la nne ni ucheleweshwaji wa kutoa maamuzi; utoaji wa maamuzi ni muhimu kwenye kujenga, unaweza kufanya kazi mara TANROADS hajatoa, mara Meneja hajatoa, hiyo pia inasababisha ucheleweshwaji au uongezaji wa gharama ya kazi.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni hali ya hewa, kwa mfano pale Makete. Makete ukikosea muda wa kujenga karibuni miezi sita pale ni mvua. Usipokuwa makini hii italeta shida, sasa wakandarasi na wataalam wetu wa TANROADS hilo walijue na la mwisho linalosababisha ni mawasiliano mabovu kati ya mtaalamu yaani mshauri elekezi na mkandarasi na client yaani sisi TANROADS, hili tunalifahamu na yote haya tunayafahamu. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge mtuamini, tunaenda kuyafanyia kazi ili kuhakikisha kwamba tunaenda ku–control hizi variation za miradi ya ujenzi wa barabara.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ni taa za barabarani; tunafahamu kwamba taa za barabarani ni muhimu sana kwenye usalama wa watumiaji wa barabara, pia zinatoa fursa wananchi kufanya kazi zao usiku na mchana. Serikali tumeamua kwamba barabara zote zitakazojengwa na TANROADS sasa tutafunga taa za barabarani na zile ambazo zilishajengwa tutakwenda kufunga taa za barabarani. Hatuwezi kuendelea tunatumia hela nyingi kujenga barabara lakini tunaacha giza, hilo halikubaliki. Tumeamua na tumeshatoa maelekezo kwamba barabara zote sasa zitafungwa taa ili wananchi wetu waweze kufanya kazi usiku na mchana.
Mheshimiwa Spika, kuna hoja ya EPC lakini sitaki niizungumze kwa sababu EPC ndio my baby, ndio kwa mara ya kwanza Serikalini Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tumeanzisha EPC+Finance. Mwaka jana wote mlikuwa hamtuamini hapa, wengine mlisema tunasema tu lakini haitekelezeki, lakini leo mambo mmeyaona wenyewe. Baada ya miaka minne tutaandika historia ya nchi yetu. Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumza sana, sitaki kulizungumza jambo hili naomba hili jambo ni kubwa sasa sisi malengo yetu ni kuangalia Dar es Salaam Express Way kutoka Dar es Salaam, kutoka Kibaha - Chalinze na Morogoro. Hilo ndio lengo letu kubwa. EPC tumemaliza sasa tunaangalia Dar es Salaam Express Way.
Mheshimiwa Spika, kuna barabara za Waheshimiwa Wabunge hapa kwa mfano Mheshimiwa Ramadhani jana alisema kwa masikitiko makubwa mpaka alikuwa kidogo anataka kulia anasema Kinyaturu anasema kila lugha, kwa vile tumeamua kwamba tunaenda kujenga barabara hiyo kwanza tutaanza kwa kilometa 10. (Makofi)
Mheshimiwa Mbunge wa Nansio vilevile kuna changamoto kubwa kule kwake, hasa kwenye kupata material ya ujenzi. Kila siku kujengea changarawe inakuwa ni shida. Tumeamua kwenda kuijenga ile barabara kutoka Rugezi mpaka Nansio yenye urefu wa kilometa 12 kwa kiwango cha lami na tutaitangaza mapema mwakani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna Mheshimiwa Mbunge wa Sumve ambaye na yeye ana changamoto pale wilayani kwake, kwamba hakuna barabara yoyote ya lami. Tumeamua sasa nayo tunaenda kuijenga kwa lami. Mheshimiwa Gulamali vilevile na yeye kuna barabara yake tumesema kwamba tunaenda kujenga angalao kilometa 10, Puge – Ziba mpaka Chomo, lakini tunaanza kwa kilometa 10 tunahakikisha kwamba tunaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamesema barabara zao nyingi, zote tumezichukua na tunaenda kuzifanyia kazi kuhakikisha kwamba, tunazijenga kwa kiwango cha lami kwa asilimia 100. Mwisho kabisa napenda kuchukua fursa hii tena kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupa fedha nyingi kwenye Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Tunaomba kumwambia tu kwamba, hatutamuangusha, kazi iendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, kwanza ninaomba kuchukua fursa hii kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maono yake na jinsi anavyojitoa katika kuwahudumia Watanzania. (Makofi)
Napenda pia kutoa pongezi na shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Phillip Isdor Mpango, Makamu wa Rais kwa namna anavyomsaidia Mheshimiwa Rais. Pia napenda kuchukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba kukushukuru sana kwa kunipa tena nafasi hii na mimi kuchangia kwenye hoja hii iliyopo mbele yetu. Kwanza kabisa ninaomba kuunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba pia kipekee nimshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mheshimiwa Selemani Moshi Kakoso na Waheshimiwa Wabunge wote, Wajumbe wote wa Kamati kwa hoja nzuri walizozitoa za Kamati. Aidha, ninamshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mitaji ya Umma - Mheshimiwa Jerry Silaa na Waheshimiwa Wajumbe wote wa Kamati ya PIC kwa michango yao mizuri. Kamati hizi mbili zilifanya kazi kubwa ya kuchambua azimio hili, ninaomba kuwahakikishia maoni yao yote pamoja na maoni ya wadau wote waliopitisha maoni yao kwenye Kamati hizo mbili tumeyapokea na tunakwenda kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bado muda tunao, fursa kubwa ya kuyafanyia kazi ipo na tunawahakikishia kwamba tutayafanyia kazi maoni yote na ya Watanzania wote kwenye mikataba ya miradi na mkataba wa nchi mwenyeji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninapenda kutumia fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika hoja hii. Naomba sasa nianze kuhitimisha hoja yangu kwa kutoa ufafanuzi wa kijumla kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamechangia kwa hisia kali kuhusu azimio la makubaliano haya kuhusu uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi katika bandari Tanzania na Waheshimiwa Wabunge wanakubaliana wote na azimio la makubaliano lililoko mbele yetu. Ninaomba kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa maoni yenu na maelezo yenu na tunawaambia kwamba tunaenda kuyafanyia kazi, tunao muda na tutayafanyia kazi kama mlivyoelekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamefanya hivyo kwa kuchangia kwa hisia kali kwa sababu wanafahamu kwamba Bandari ya Dar es Salaam ndiyo lango kuu la uchumi wetu kwa sasa. Kama walivyosema wengi 37% sawa na shilingi trilioni 7.78 ya makusanyo ya mapato ya kiforodha ya TRA yanakusanywa kwenye bandari zetu hasa Bandari ya Dar es Salaam. Kwa hiyo, bandari zetu ni muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye hotuba yangu mikataba kwa kila mradi itakayoandaliwa itapewa bayana kipindi cha utekelezaji wake na ukomo kila mradi tukianzia mradi wa uendeshaji utapewa muda wake, tukianzia kama kuna mradi wa ujenzi pengine gati la abiria tutaupa muda wake na ninaomba nichukue fursa hii hili jambo la muda tuwaachie wataalam. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, mwekezaji anayendesha bandari na mwekezaji anayejenga bandari wanapewa muda tofauti. Huwezi mtu anayeendesha bandari ukampa miaka kumi, anayejenga bandari ukampe miaka kumi; siyo sahihi hata kidogo, kwa sababu mmoja anawekeza sana, mmoja anafanya operation, kwa kweli naomba hili ni jambo la kitaalamu, sisi tutalichukua na tuna wataalamu wazuri ambao watalifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla kwamba tutaweka muda wa marejeo. Tutaweka time ya kufanya review kwa kila mradi. Miradi mingine tutafanya review kila baada ya mwaka mmoja, na miradi mingine tutafanya review kila baada ya miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia tutaweka viashiria muhimu vya ufanisi wa kiutendaji yaani key performance indicators kwa kila mradi na ninaomba Waheshimiwa Wabunge niwaeleze key performance indicators hizi ndiyo zilizomtoa TICTS. TICTS alikuwa asitoke, lakini TICTS alishindwa kufikia vigezo tulivyomuwekea na ikawa hana njia lazima aondoke tu. (Makofi)
Kwa hiyo, naomba sana muwaamini wataalamu wetu tunaamini wataalamu wazuri na ninaamini kwa kila mradi wataweka hizo key performance indicators na mkandarasi yoyote ama muwekezaji yoyote kama atashindwa kutekeleza tutaachana naye. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba tuwahakikishie kwamba uandaaji wa mikataba ya miradi utafanywa na timu chini ya usimamizi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, narejea tena, tuna vijana wazuri ambao wana uwezo mkubwa wa kutengeneza miradi kama hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, waliopata kuona ule mkataba wa TICTS, ule mkataba ulikuwa non-starter, ilikuwa hatuwezi kutoka lakini vijana wale wale tuliokuwa nao jana waliupitia mradi ule na TICTS mwezi wa Desemba aliondoka bila matatizo yoyote, bila mgogoro wowote kwa vile tunao vijana wazuri wana uwezo mkubwa na watafanya hiyo kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nijielekeze kwenye utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam. Wabunge wengi wameongea hapa kwamba Tanzania imeelekeza au Tanzania imewekeza takribani shilingi trilioni moja. Serikali imeelekeza ama iliwekeza karibuni shilingi trilioni moja kwenye Bandari ya Dar es Salaam, lakini ufanisi kwenye bandari yetu bado ni changamoto kubwa. Nitawapa mfano, kwa mfano kitengo chetu cha makasha kuanzia gati namba tano mpaka namba saba ambayo inahudumiwa na TICTS mwaka uliopita iliweza kuhudumia makasha 150,000 tu wakati pale malengo ilikuwa tuhudumia takribani makasha 600,000. Hii haiwezekani, hatuwezi tukafanya hivyo kuwaachia watu ambao uwezo wao siyo mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna sababu za msingi ambazo zimefanya utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam hasa kwenye kitengo kama cha makasha uwe ni dhaifu. Sababu ya kwanza kabisa tumeshindwa kuwekeza kwenye mitambo mikubwa ya kushushia makontena au makasha kwenye meli. Mheshimiwa Ezra amesema hapa ukitaka kununua ship to shore crane moja unahitaji takribani shilingi za Kitanzania bilioni 45 mpaka 50 na kwa meli moja unahitaji ship to shore cranes nne kwa wakati mmoja ndiyo utaweza kufanya hiyo kazi vizuri.
Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine tuliyonayo pale sote tunafahamu, tumekuwa na changamoto kubwa sana la mifumo ya TEHAMA na kila Mheshimiwa Mbunge aliyesimama hapa amezungumzia mambo ya TEHAMA. Sasa tunakwenda kupata mwarobaini kwa ajili ya changamoto hizi.
Mheshimiwa Spika, pia Bandari yetu ya Dar es Salaam tumekuwa na changamoto kubwa ya utafutaji masoko. Haya makontena hayaji tu hivi hivi kama watu wanavyofikiria, lazima uwe na mtu ambaye ana uwezo mkubwa, ana network kubwa aweze kwenda nje kuleta mizigo mingi zaidi. Kwa vile tuna amini kwa mtazamo tunaokwenda nao wa DP World, sasa tunaweza kwena kupata mwekezaji ambaye atatutoa hapa tulipo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema majibu ya changamoto hii ni kuleta mwekezaji mahiri na sisi tunaamini kwamba DP World ni mwekezaji mahiri na anaweza kututoa hapa tulipo. (Makofi)
Ninaomba nieleze machache tu kuhusu bandari tunazoshindana nazo. Sisi sote katika ukanda huu tunapambania soko la Zambia, Malawi, Rwanda na Uganda pamoja na DRC. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mshindani wetu mkubwa namba moja kwa sasa kwa hapa karibu ni port au Bandari ya Mombasa. Bandari ya Mombasa ina gati 19 wakati sisi Dar es Salaam tuna gati 12 tu. Magati ya kawaida wanayo 13 na magati sita ni kwa kuhudumia makasha. Sisi tunazo gati sita, lakini zote ni ndogo kulinganisha na Mombasa.
Mheshimiwa Spika, lakini wenzetu Mombasa sasa na wao wameshaanza kwenda kutafuta private sector kuendesha bandari hiyo hasa sehemu ya makasha. Container Terminal Number Two kwa sasa ambao wameijenga kwa mkopo na wao kutoka JICA kwa gharama ya dola za Kimarekani 280 tayari sasa hivi inaendeshwa na Kampuni ya Mediterranean Shipping Company ya Italy. Kampuni hii inamilikiwa na familia tajiri ya Kiitaliano Bwana Aponte ambaye yeye ni tajiri mkubwa kwenye mambo ya meli.
Mheshimiwa Spika, bandari hii vilevile ina gati ambayo inaendeshwa na private sector ambayo kazi yake kubwa ni kuhudumia nafaka.
Mheshimiwa Spika, Bandari ya Durban; Bandari ya Durban inamilikiwa na Transnet National Port ya South Africa ina magati 50; magati 31 ni ya kawaida ya kuhudumia makontena ni magati 10 na magati ya mafuta na chuma ni magati tisa. Magati 31 ya kawaida na magati 10 yanahudumiwa na Transnet Port Terminal siyo Transnet National Port Authority ni mtu tofauti ni kampuni ya South Africa lakini tofauti. Magati tisa yaliyobaki ya mafuta na mawe na chuma yanahudumiwa na private sector.
Mheshimiwa Spika, mshindani wetu mwingine ni Beira kutoka Msumbiji. Bandari ya Beira yenyewe ina magati 11; magati ya shehena za mchanganyiko pamoja na magati ya kuhudumia makontena yanahudumiwa na private sector (Conal Eda Mozambique) ni kampuni ambayo inatoka huko Uholanzi.
Mheshimiwa Spika, mshindani wetu mwingine ni Bandari ya Vizag...
SPIKA: Mheshimiwa Waziri dakika tatu malizia.
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, kwa ufupi tu niseme bandari zote sasa hivi hasa kwenye maeneo ya kontena zinahudumiwa kwa asilimia mia moja na private sector. Ukichukua Angola, ukichukua Egypt, ukichukua Ghana, ukichukua Nigeria kila mahali wanafanya private sector kwa sababu wanafahamu private sector ina uwezo mkubwa wa kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Spika, tuliamua kuleta private sector na tukaamua tulete private sector ambaye ana uwezo wa kufikia viwango vya kimataifa pamoja na awe na ufanisi katika utekelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, sifa ya pili ambayo private sector tunataka tumlete awe na uwezo wa kutoa ufumbuzi katika mnyororo mzima wa usafirishaji; sifa ya tatu awe na mtandao mpana wa kupata mizigo kutoka soko la usafirishaji duniani; na sifa ya nne awe na uwezo wa kimataifa katika kuendeleza na kuendesha shughuli za kibandari.
Mheshimiwa Spika, majibu yote yako kwa DP World. Kampuni ya DP World ina uwezo mkubwa katika uendeshaji wa shughuli za bandari duniani kuanzia Afrika, Asia, Ulaya, Marekani ya Kaskazini na Kusini, kwa ufupi anao mtandao mkubwa sana duniani.
Pili, DP World ina uzoefu na utaalamu wa kuchagiza mnyororo mzima wa usafirishaji kutoka maeneo ambayo bidhaa zinatoka mpaka kufikia kwa walaji. Kampuni ya DP World inamiliki kampuni kubwa ya meli (P&O) ambayo ina takribani meli 100 na zinafanya kazi biashara duniani kote. Tunaamini kwa kwenda na DP World tutaweza kufanikiwa kwa asilimia kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Kampuni ya DP World inaendesha maeneo mengi maalum ya kiuchumi karibu na bandari, inasafirisha usafirishaji baharini na inafanya kazi kwenye nchi kavu nyingi na hivi sasa tunavyozungumza kule Rwanda wana logistic park kubwa ambayo tunaamini DP World ikija Tanzania mizigo yote ya Rwanda itakuja au itapitia Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema leo kwamba baada ya kazi hii ya kumleta DP World kuna matokeo makubwa tutayapata kwenye Bandari yetu ya Dar es Salaam. Ninaomba nimalizie haya mawili.
Kwanza tunaamini tutapunguza muda wa meli kukaa nangani kutoka masaa manne mpaka matano mpaka kufikia saa 24 kwa siku. Meli inaingia sasa hivi jioni, kesho inaondoka.
SPIKA: Ngoja, ngoja, hapo mwanzoni nadhani ulikusudia kusema siku umesema masaa sasa nadhani tutakuwa tuna…
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimesema siku nne mpaka tano za sasa mpaka masaa 24 kwa siku. (Makofi)
Pili, kama tutafanikiwa, na naamini tutafanikiwa kumleta DP World tutapunguza muda wa ushushaji wa makasha yaani kutoka siku nne kwa sasa mpaka kufikia siku moja na nusu yaani meli itaingia pale baada ya siku mbili inaondoka. Pia tunasema kama tutamleta DP World tunaweza kuongeza mzigo kutoka tani milioni 20.8 za sasa mpaka kufikia tani milioni 47.57 ifikapo mwaka 2032/2033.
Mheshimiwa Spika, jambo muhimu ambalo tutafanikiwa nalo ni kuweza kuongeza mapato yanayotokana na kodi ya forodha. Kwa sasa tunakusanya takribani shilingi trilioni 7.756 kupitia TRA kama tutaweza kumleta mwekezaji DP World tutaweza kwenda mpaka shilingi trilioni 26.709 sawa na 62% ya bajeti ya nchi yetu, pia tutaweza kuongeza kwa kiasi kikubwa ujaji wa meli katika bandari yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niaomba mwisho kabisa niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Wabunge mtuamini sana kama tunaenda kuifanya kazi hii kwa uadilifu mkubwa na ninyi wenyewe matokeo mtayaona. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo sasa ninaomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nami napenda kuanza kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kutujalia kukutana hapa leo tukiwa na afya njema ili kukamilisha kazi tuliyoianza jana tarehe 23 Mei ambapo niliwasilisha hoja hii.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kukushukuru wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa jinsi ulivyoongoza wakati wa majadiliano ya hoja hii. Aidha, nichukue fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa wawazi na kutoa michango yao ya kina wakati wa majadiliano haya. Ninawathibitishia kwamba michango hiyo tunaichukua kwa uzito mkubwa ili kuendelea kuleta ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
Mheshimiwa Spika, naomba kipekee nimshukuru Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mheshimiwa Sulemani Moshi Kakoso kwa hoja zilizotolewa na Kamati yake. Nikiri kwamba hoja hizo ni muhimu na Wizara itazifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Waheshimwia Wabunge wote waliochangia katika bajeti yangu. Waheshimiwa Wabunge 79 wamechangia wakati wa majadiliano ya hoja hii ambapo Waheshimiwa 70 wamechangia kwa kuongea na Waheshimiwa tisa wamechangia kwa maandishi.
Mheshimiwa Spika, muda mchache uliopita Waheshimiwa Manaibu Waziri wa Wizara yangu wamemaliza kujibu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge kwa kuzingatia maeneo ya kisekta, ninawashukuru sana kwa jinsi ambavyo wamejibu baadhi ya hoja. Nitajaribu kujibu hoja chache zilizobakia.
Mheshimiwa Spika, aidha, naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Wizara itajibu hoja zote za Waheshimiwa Wabunge kwa maandishi na kuziwasilisha Bungeni kabla ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Bunge hili la bajeti unaoendelea.
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nianze kuhitimisha hoja yangu kwa kutoa ufafanuzi wa ujumla kwa baadhi ya hoja zilizojitokeza. Maeneo muhimu yaliyojitokeza katika hoja nyingi za Waheshimiwa Wabunge, hoja tuliyoijadili ndani ya siku mbili ilihusu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ambayo imegusa masuala mbalimbali yaliyojikita katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa ujenzi na ukarabati wa barabara mbalimbali nchini ikiwemo masuala ya ulipaji fidia kwa barabara na viwanja vya ndege. Waheshimiwa Wabunge wengi karibu asilimia 96 wamezungumzia mambo ya barabara. Hii inaonesha kwamba barabara ni njia moja muhimu ya usafiri na lazima Serikali tujipange kuhakikisha kwamba tunatatua matatizo ya barabara nchini.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine lililozungumziwa ni changamoto ya huduma za vivuko nchini. Mheshimiwa Naibu Waziri amelizungumzia hili lakini nami nikipata muda nitalizungumzia baadaye.
Mheshimiwa Spika, eneo la tatu lililozungumziwa ni changamoto mbalimbali kuhusu usafiri wa anga na utekelezaji wa miradi ya viwanja vya ndege likiwemo suala la fidia. Hapa tena Naibu Waziri anayesimamia Sekta ya Uchukuzi amezungumiza suala la usafiri wa anga na Mheshimiwa Naibu Waziri anayesimamia Sekta ya Ujenzi amezungumzia suala la ujenzi wa viwanja vya ndege.
Mheshimiwa Spika, suala jingine lililojitokeza ni ukamilishaji wa ujezi wa Reli ya Kisasa ya SGR na ukarabati wa Reli iliyopita. Eneo la SGR nitalizungumza sasa hivi nitalitolea ufafanuzi baadhi ya maeneo. Eneo jingine ambalo limezungumziwa ni uboreshaji wa huduma za usafiri wa majini hususan ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli za zamani hili nitalizungumzia mimi kwa undani kidogo.
Mheshimiwa Spika, eneo jingine lilojitokeza ni masuala ya uboreshaji wa huduma za hali ya hewa hususan maslahi ya watumishi. Pamoja na kwamba Manaibu wangu wametoa ufafanuzi wa kina kwenye maeneo mbalimbali kwa kuzingatia hoja zilizotolewa, naomba sasa nitoe ufafanuzi kwa baadhi ya hoja kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu zilizowasilishwa na Mheshimiwa Mwenyekiti wetu. Hoja ya kwanza ilikuwa ni kama ifuatavyo, utekelezaji wa miradi ya barabara kuu, barabara za Mikoa na ujenzi wa madaraja upo chini ya kiwango. Kamati imeona kuwa hali hii hairidhishi majibu ya hoja hiyo ni kama ifuatavyo;
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa miradi uko chini kutokana ya miradi mingi kuchelewa kuanza kwa sababu ya kuchelewa kutolewa kwa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani yaani VAT. Miradi mingi ilipata misamaha wakati wa kipindi cha mvua kwa vile ikashindwa kuanza kutokana na hali hiyo. Lakini sasa miradi mingi imeshapata msamaha wa VAT naamini speed ya kufanya miradi hiyo itaongezeka kwa kasi kikubwa.
Mheshimiwa Spika, hoja ya pili, iliyowasilishwa na Mheshimiwa Mwenyekiti ni fedha ya Bajeti iliyoidhinishwa mwaka 2021/2022 zilitumika kulipa madeni badala ya kutekeleza miradi iliyokusudiwa. Majibu ya hoja hiyo ni kama ifuatavyo, hadi mwisho wa Julai mwaka huu jumla ya shilingi bilioni 418.92 zililipwa kwa ajili ya kazi za miradi ya barabara zilizofanyika katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2021/2022. Aidha, bajeti ya ujenzi wa barabara na madaraja katika Mwaka wa Fedha 2021/2022 ilikuwa ni bilioni 491.7, shilingi bilioni 314.11 zililipwa kwa ajili ya madeni ya kuanzia mwezi Julai, 2021 hadi huko nyuma na hizi zilitolewa pesa tofauti siyo pesa za bajeti ya mwaka huu. Baadhi ya fedha za bajeti kama utaratibu ulivyo zilipelekwa kwenda kufanya matengenezo ya barabara ambazo sasa hizi zinatoka kwenye mfuko wa barabara.
Mheshimiwa Spika, hoja ya tatu, kutowepo kwa mpango unaoruhusu ujenzi wa barabara kwa kupitia ubia hii hoja iliwasilishwa na kamati yetu. Majibu ya hoja hiyo ni kama ifuatavyo, katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 Serikali inapanga kuanza kushirikisha Sekta Binafsi katika ujenzi wa barabara na madaraja kwa kutumia utaratibu wa EPC plus Financing.
Mheshimiwa Spika, jumla mtandao wa barabara nchini ambao unasimamiwa na TANROADS kilomita 36,362 kati ya kilomita hizi kilomita 11,513 ni barabara za lami. Kwa upande mwingine hadi kufikia mwezi Mei mwaka huu jumla ya kilomita 1,206.5 zinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami ambayo gharama yake ni takribani shilingi trioni 2.9.
Mheshimiwa Spika, gharama za kujenga barabara zote ambazo hazina lami ambazo ni kilomita 24,849.05 inahitajika takribani shilingi trioni 37 kuweza kukamilisha mtandao wote wa lami ambazo unasimamiwa na TANROAD. Mwarobaini wa tatizo hili kuamua sasa kuanza utaratibu mpya wa kutumia EPC plus Finance maana yake nini, maana yake mtu mwenye uwezo wake, ataleta fedha, akileta fedha sisi tutaendelea kumlipa kidogokidogo lakini tunaendelea kujenga barabara. Utaratibu huu unatumika duniani kote na ndiyo utaratibu pekee tutakaoweza kutupelekea kujenga barabara kwa haraka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ziko barabara ambazo tunaamini ukizijenga leo na ukiweka tollgate utapata hela, kwa mfano barabara ya Kibaha, Mlandizi, Chalinze, Morogoro express way yenye urefu wa kilomita 205 tukijenga barabara hii kwa kutumia EPC plus Finance na tukaweka tollgate tunaamini kwamba tutaweza kupata fedha na fedha hizo zitakwenda kwenye miradi mingine. Watu wale ambao hawataki kutumia tollgate kutakuwa na njia mbadala wataweza kutumia bila matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa vile hapa tunatoa option kwa watu ambao wanauwezo watalipa pengine shilingi 3,000 shilingi 4,000 kwa trip waliyokuwa hawana uwezo watatumia barabara ya kawaida. Nafikiri hili ni jambo zuri na lazima tuendeleze. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika utaratibu huu vilevile tutafanya ukarabati wa barabara ya Igawa, Tunduma yenye urefu wa kilomita 218 na Uyole, Songwe by pass yenye urefu wa kilomita 48.9. Kuna barabara kwa mfano Handeni, Kiberashi, Kwamtoro, Singida yenye urefu kwa kilomita 411 hii tutaijenga kwa EPC plus Finance lakini hatutaweka tollgate kwa sababu wananchi wetu wa maeneo ya kule hawana uwezo wa kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna barabara kwa mfano Kidatu, Ifakara, Lupilo, Malinyi, Kilosa, Kwampepo, Londo, Kitanda, Lumecha, yenye urefu wa kilomita 486 na hii tutaijenga kwa utaratibu wa EPC plus Finance lakini hatutaweka tollgate kwa sababu wananchi wetu uwezo wao siyo mkubwa na wananchi wetu hawana njia mbadala ya kuweza kupitia. Kwa vile, tutakwenda na utaratibu huu na tunaamini tukianza utaratibu huu tutafungua kwa kiasi kikubwa mtandao wa barabara nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine iliyowasilishwa na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati na wajumbe wengine, inasema kutokuwepo kwa bajeti ya ukarabati wa barabara zilizopandishwa hadhi. Jibu la hoja hii ni kama ifuatavyo, barabara inapopandishwa hadhi Meneja wa Mkoa husika huingiza katika mpango wake ili izingatiwe katika bajeti ya mwaka husika kupitia mfuko wa barabara. Kwa vile barabara tunapoipandisha moja kwa moja Meneja wa Mkoa anaichukua na anatoa hela kwa ajili ya ukarabati. Kwa vile kazi kubwa tunayotakiwa kama kuna changamoto ya barabara zileteni Wizarani tutazipandisha kama zimezidi vigezo then tutaweka fedha kwa ajili ya ukarabati kama taratibu na Sheria zinavyoelekeza.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine iliyotolewa na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati na wajumbe wengine, athari za mikataba kwa Wakandarasi kwa kuchelewa kulipwa madeni. Majibu ya hoja hii ni kama ifuatavyo, katika Mwaka wa Fedha 2021/2022 Serikali ililipa madeni ya Wakandarasi kupitia hati za madai zilizowasilishwa kwa kila mwezi hivyo kupunguza athari za ucheleweshaji. Kwa muda wa mwaka huu kwa kipindi hichi tumekuwa kila ikiletwa certificate tunailipa, leo ukienda daraja la Kigongo, Busisi hatuna deni, leo ukienda daraja la Wami hakuna deni, na miradi mingi mingi ambao hakuna deni, certificate ikiingia tunalipa. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kulijua hili kwa sababu athari ya deni ni jambo kubwa sana. Na sisi tutahakikisha mchakato ukifika Wizarani haucheleweshwi unakwenda Wizara ya Fedha naamini na Wizara ya Fedha Waziri yupo mchakato utaenda mapema ili tusicheleweshe ku-create interest rate ambayo haina faida yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna hoja nyingine inasema miradi mipya ya barabara kushindwa kuanza kutekelezwa wakati wake kwa mwaka 2021/2022 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo fedha zake kutumika kulipa miradi ya nyuma. Majibu ya hoja suala hili ni kama ifuatavyo, hadi kufika mwezi Aprili mwaka huu mikataba ya miradi ifuatayo ilisainiwa.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa kwanza ni barabara ya Ntendo, Muze, Kilyamatundu yenye urefu wa kilomita 179 sehemu ya Ntendo, Kizungu yenye kilomita 25 ilisainiwa. Karatu, Mbulu, Haydom, Sibiti, River, Lalago, Maswa yenye urefu wa kilomita 389 sehemu ya Mbulu, Garibabi ilisainiwa yenye urefu wa kilomita 25. Matai, Kasesya yenye urefu wa kilomita 50 sehemu ya Matai, Tatanda ulisainiwa. Mradi wa Tarime, Mugumu wenye urefu wa kilomita 87.14 sehemu ya Tarime, Nyamanga ulisainiwa. Na miradi mingi ilisainiwa na sasa hizi kazi imeanza lakini utaratibu unachukua muda kwa sababu mkisaini Mkataba hatua inayofuata kwanza ni Mkandarasi kuleta performance bond baada ya kuleta performance bond kuna kipindi cha miezi kama mitatu ya mobilization kwa vile ndiyo unaona Mkataba ukishasainiwa kazi inachelewa kuanza. Lakini na Waheshimiwa wabunge naomba niwahakikishie kwamba Wizara tunajipanga na hakuna sababu ya kuchelewesha miradi.
Mheshimiwa Spika, kuna hoja ya Mheshimiwa Jerry na jana alilia bahati mbaya sana, Mkandarasi Sino Hydro Cooperation Limited anayejenga barabara BRT Phase II utendaji kazi wake ni mbovu kwa nini kapewa tena kazi ya BRT III. Majibu ni kama ifuatavyo, Kampuni ya Sino Hydro Cooperation Limited ilipatikana kwa njia ya ushindani competitive bidding ambapo alionyesha kukidhi vigezo vyote vya zabuni ikiwa ni pamoja na kuwa na gharama ya chini takribani bilioni tano ikilinganishwa na Kampuni iliyofuata, alikuwa na bei ya chini bilioni tano. Aidha, Wizara kupitia TANROADS itasimamia kikamilifu ujenzi kwa mujibu wa Mkataba.
Mheshimiwa Spika, nilifanya ziara kwenye Mradi wa BRT mara tatu na niligundua kuna mapungufu katika utendaji wa kazi na kama kawaida tulimtaka Mkandarasi arejee kazi hiyo kwa gharama yake mwenyewe. Na hivyo anavyoendelea au tunavyoendelea Mkandarasi huyo anarejea kazi hiyo kwa fedha yake mwenyewe.
Mheshimiwa Spika, katika ziara ya mwisho ambayo niliifanya mwezi Aprili mwaka huu tulikubalina na Mkandarasi fly over ya makutano ya Kilwa Road na Mandela pale Uhasibu upande mmoja uweze kufunguliwa tarehe 30 na vilevile fly over ya makutano ya Chang’ombe na Nyerere tutaruhusu kupita magari tarehe 30 mwezi huu ule upande mmoja. Hii tunafanya yote kuhakikisha kwamba wananchi wa Dar es Salaam hawapati shida ya usafiri.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Mradi wa BRT umefikia actually performance actually 58.8 wakati planned performance ile iliyotarajiwa working plan ilikuwa iwe 57.5 Mkandarasi yuko nyuma ya asilimia 1.7, hii tutambana Mkandarasi na tunaendelea kumbana kuhakikisha kwamba anafanya kazi kwa speed inayotakiwa.
Mheshimiwa Spika, naomba nijikite kwenye hoja ya pili, ujenzi wa reli ya kati ya kiwango cha standard gauge. Ujenzi wa reli ya kisasa ulianza rasmi mwaka 2017 kwa Awamu ya Kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza yenye urefu wa kilomita 1,219. Ujenzi huu umegawika katika vipande vitano or lot tano, lot ya kwanza ni kutoka Dar es Salaam, Morogoro yenye urefu wa kilomita 300 gharama ya Mradi huu ni takribani dola za Kimarekani bilioni 1.215 sawa na shilingi trioni 2.7.
Mheshimiwa Spika, Mkataba ulisainiwa mwezi Februari mwaka 2017 maendeleo ya ujenzi mpaka sasa hivi Mkandarasi amefikia asilimia 96.5. Malipo yaliyolipwa kwa Mkandarasi takribani dola bilioni 1.004 gharama kwa kilomita moja ni dola za Kimarekani milioni 4.05 kwa kilomita hii pamoja na VAT. Mwendokasi wa reli hii utakuwa ni kilomita 160 itatumia umeme na uwezo wake wa kubeba mzigo itakuwa ni excel tan ya tani 35. Mkandarasi Yapi, na naomba tu niwaambie Waheshimiwa Wabunge wakati wa mchakato wa Mradi huu ilikuwa ni shida kubwa kwa sababu walichukua bidding document Makandarasi karibuni 30 lakini akarejesha Mkandarasi tu mmoja tu Yapi.
Mheshimiwa Spika, tukazungumza na Mkandarasi na kukubaliana na tukaendelea kulikuwa na maneno mengi lakini watu walikuwa hawasemi kama wanavyosema leo. Watu leo jambo kidogo linaenda huku na huku lakini na hapo kulikuwa na changamoto na tuliweza kusimamia mradi huu na kazi inaendelea vizuri.
Mheshimiwa Spika, kipande cha pili ni kutoka Morogoro, Makutupora chenye urefu wa kilomita 422 chenye gharama takribani dola za Kimarekani bilioni 1.923 sawa na shilingi trioni 4.4 za Kitanzania. Mkataba ulisainiwa Septemba mwaka 2017 na umefikia asilimia 82.68, gharama kwa kilomita moja ni dola za Kimarekani milioni 4.55, malipo yaliyofanywa mpaka sasa hivi ni dola za Kimarekani bilioni 1.2154 Mkandarasi ni Yapi Merkezi.
Mheshimiwa Spika, kipande cha tatu ni kutoka Makutupora, Tabora chenye urefu wa kilomita 368 gharama ya ujenzi wa kipande hichi ni dola za Kimarekani bilioni 1.908 sawa na shilingi trioni 4.4, malipo ya awali ni dola za Kimarekani milioni 263.9 ambazo Mkandarasi ameshalipwa. Mkandarasi ameanza maandalizi ya utekelezaji, gharama kwa kilomita moja hapa ni dola za Kimarekani milioni 5.18 bei imepanda kwa sababu reli hapa inapita kwenye maeneo ya Rift Valley kwa vile ujenzi wake huwezi ukalinganisha na maeneo kama Dar es Salaam kwa vile gharama itapanda na mambo mengine yanaongezeka kidogo.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri, dakika tatu, malizia.
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, kipande kinachofuata ni kipande cha Isaka, Mwanza chenye urefu wa kilomita 341, Mkataba ulisainiwa tarehe 15 Mei, 2021 mpaka sasa hivi Mkandarasi amefikia kazi ya utekelezaji ni asilimia 6.8 actually lakini aliyotakiwa kufanya iwe asilimia 6.85 kuna kuna tofauti ya asilimia 0.1 huwezi ukasema kwamba Mkandarasi huyu haja-perform. Kitu kinachokusababisha kufahamu mkandarasi ame-perform ni working plan siyo kwenda kuona, ukiona haikusababishi kusema Mkandarasi ame-perform ama haja-perform tunavyoamini sisi kutokana na namba hizi Mkandarasi ame-perform. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa tuta Mkandarasi amefikia asilimia 13.7 mbele ya mpango kazi amekwenda zaidi asilimia mbili. Gharama ya kipande hichi ni bilioni 1.32 na Mkandarasi mpaka sasa hivi amelipwa dola milioni 201.012. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipande kinachofuata Tabora, Isaka kina urefu wa kilomita 165, kipande hichi kilitangazwa zamani na wazabuni, lakini mzabuni aliyejitokeza ali-quote price ya dola za Kimarekani bilioni 1.4987 na Mkandarasi huyu alikuwa ni Motor Angelo kutoka Ureno na Transnet ya South Africa. Tenda hiyo ilifutwa na tukaamua tuje na utaratibu wa single source kama sheria inavyoelekeza. Sasa baada ya kufanya mchakato huo bei sasa imeshuka kutoka dola za Kimarekani bilioni 1.498 mpaka dola za Kimarekani milioni 712.8 bila VAT ukichukua na VAT unapata dola za Kimareka milioni 900.1, sasa ukilinganisha wewe unakuta kwamba single source hapa imeleta faida kuliko competitive bidding. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Waziri sasa omba fedha, toa hoja.
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hoja zetu tatu zilizopo mbele yetu. Mchango wangu kwanza utajikita kwenye Azimio la Bunge ambalo lilitolewa mwaka jana kuhusu kuhamisha KADCO kwenda TAA.
Mheshimiwa Spika, hakuna mtu yeyote kwenye Serikali ambaye anapingana na maagizo ya Bunge na sisi kama Serikali tunathamini sana maagizo yanayotolewa na Waheshimiwa Wabunge pamoja na Bunge lako Tukufu. Mara baada ya kikao kile tulianza kujipanga kwenda kuangalia jinsi gani tutaweza kutekeleza agizo hili, lakini kulitokea changamoto kubwa kuhusu Sheria ya TAA ambayo ni sheria ya Executive Agency, Act No.3 ya mwaka 1977 hairuhusu utaratibu wa kutoa hizo fursa moja kwa moja.
Mheshimiwa Spika, baada ya kushauriana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, tuliamua kutengeneza sheria mahususi ya TAA ambayo itaruhusu uendeshaji na uendelezaji kupewa Taasisi za Serikali na Private Sector. Sheria hiyo imepita katika maeneo mbalimbali na ngazi mbalimbali na wadau mbalimbali wametoa maoni. Tarehe 20 mwezi uliopita, Serikali ilitoa maamuzi kwamba sheria hiyo iundwe ambayo itatoa fursa mahususi sasa kwa ajili ya mpango huo wa kuhamisha KADCO kwenda TAA, pamoja na kuipa fursa TAA kuingia mikataba na kampuni za private, pia kuipa fursa TAA kushirikiana na Taasisi mbalimbali za Serikali.
Mheshimiwa Spika, hatua tuliyofikia sasa sheria inaendelea kutungwa na Bunge letu linalokuja la Februari, sheria hiyo itawasilishwa hapa Bungeni ili Waheshimiwa Wabunge waijadili. Naamini kwa hamu waliyonayo sheria hiyo itapita na tutaendelea kufanya mchakato wa kuhamisha KADCO kwenda TAA bila matatizo
Mheshimiwa Spika, tulilazimika kwenda na utaratibu huo kwa sababu tulitaka na sisi tusivunje sheria. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, KADCO ni Kampuni ya Serikali ambayo ipo chini ya Msimamizi wa Msajili wa Hazina na itaendelea kuwa hivyo hata ikienda huko TAA, kwa sababu, kampuni zote hizi za Serikali zipo chini ya Msajili wa Hazina.
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nijikite kwenye hoja za CAG…
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Mbarawa kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mtemvu.
TAARIFA
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri anazungumza vizuri juu ya jambo la KADCO, kwamba, sasa hivi wanatengeneza sheria ili TAA iweze kuimiliki na hii private company. Tukiwa tunatambua TAA inamiliki viwanja vingine Tanzania hapa ambayo tungeamini na KIA kingekuwa ndani. Kama Kamati, nikiwa Mjumbe wa PAC tunatambua KADCO imemaliza mkataba wake uliokuwepo Tarehe 16 Mwezi Julai, 2023. Sasa, Mheshimiwa Waziri atuambie sasa hivi KADCO inaendelea kuwepo pale kama nani? Ikiwa haina mkataba wowote na mkataba wake umeisha?
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, pengine hii hoja ya KADCO inaleta ugumu kidogo kwa sababu nakumbuka mwaka jana na ninayo Hansard hapa, Bunge lilikuwa kali sana kuhusu jambo hili. Serikali ilikuwa imeshatoa maelezo inaenda kufanyia kazi Maazimio ya Bunge. Hili ni Azimio mojawapo ambalo ni kati ya yale ambayo Bunge limeazimia, Serikali ikaleta taarifa Juni, ikasema jambo hili wameshafikia hatua nzuri kufikia sijui mwezi wa ngapi litakuwa tayari na sasa tena tunaambiwa bado. Sasa naambiwa huko na Wajumbe wa Kamati kwamba mkataba ukwisha. Mkataba umekwisha lakini KADCO bado wapo.
Waheshimiwa Wabunge, wakati huo huo KADCO ni ya Serikali, wakati huo huo haiwezi kukabidhi kiwanja TAA ambayo nayo ni ya Serikali. Sasa, mazingira hayo Mheshimiwa Waziri, leo nitakupa muda wa kutosha tuelewe vizuri hili jambo la KADCO, kwa sababu, lina Azimio maalum la tangu mwaka jana.
Mengine yote najua huko mwishoni nitapata nafasi ya kuzungumza lakini hili la KADCO kelele zilikuwa nyingi na Mheshimiwa AG upo hapa, nitawapa nafasi wewe na Mhehishimiwa Waziri mtueleze vizuri hilo jambo. Kwamba, viwanja vingine vyote vimewezekana kwenda TAA, isipokuwa kiwanja cha KIA kimeshindikana kwa sababu KADCO yupo pale na ni wa Serikali. Sijui ugumu unatokea wapi mpaka mnahitaji sheria mpya ili TAA akabidhiwe KADCO. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, halafu Mheshimiwa AG.
WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, TAA inaendesha viwanja 54 vya Serikali, KADCO hakipo. Vilevile TAA ni taasisi ambayo ipo chini ya Msajili wa Hazina. KADCO sasa ipo chini ya Msajili wa Hazina. Sasa, kwa Sheria ya TAA ilivyo sasa kama nilivyosema na Sheria ya KADCO ilivyo, hatuwezi kuihamisha KADCO moja kwa moja kuipeleka TAA kwa sasa.
SPIKA: Malizia, nawasha najiandaa.
WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, tuliomba ushauri kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuhusu jambo hili na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ikatwambia kwa jambo lilivyo kwa kuwa kampuni hizi ni tofauti, ile moja ni kampuni ambayo imenzishwa kwa Executive Agency, nyingine imeanzishwa kwa utaratibu mwingine, inabidi muanzishe sheria maalum ambayo itaifanya TAA kuchukua viwanja kwa mfano cha KADCO na viwanja vingine vya private.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala hili ni kweli KADCO muda wake wa uendeshaji umemalizika, lakini na hilo tulilipeleka kwa Mwanasheria Mkuu akasema, hili lazima tuandike waraka kupeleka kwenye mamlaka na tumefanya hivyo, tupo katika hatua za kutolewa maamuzi.
SPIKA: Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, kwanza niunge mkono sehemu ya maelezo iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana na Uchukuzi. Suala la KADCO lina historia ambapo uamuzi wa awali kabisa ulikuwa ni Serikali kuichukua hisa zote kwenye kampuni hiyo. Hilo likakamilika.
Mheshimiwa Spika, hatua ya pili, katika hatua ya kuhamishia TAA kukajitokeza kulikuwa na liabilities za KADCO ambazo hazikuwa sahihi, TAA izirithi. Kwa hiyo, pamoja na Azimio la Bunge hili, vilevile kulikuwa na maamuzi ya Baraza la Mawaziri. Waziri alilazimika kurejesha suala hili kwa kutoa taarifa kwenye mamlaka zinazohusika na baadaye sasa maamuzi yamekwishafanyika kama alivyosema Mheshimiwa Waziri. Kwa sasa, concessional agreement imemaliza muda wake mwezi Julai, lease agreement muda wake utaisha mwezi wa kumi na moja.
Mheshimiwa Spika, kipindi hiki hapa katikati, kabla Bunge hili halijafikia mwisho wiki ijayo, naamini mchakato wa kuletwa Bungeni kusomwa mara ya kwanza kwa Sheria ya TAA ambayo sasa itakuwa imewekea mawanda makubwa ya kuendesha viwanja vyote vya ndege nchini, nafikiri sasa tutakuwa tumefikia kwenye ukamilifu wa Azimio la Bunge la mwaka jana.
Mheshimiwa Spika, nashukuru.
SPIKA: Mwanasheria Mkuu wa Serikali tusaidie, hii KADCO mkataba umeisha, inafanya kazi. Unasema liabilities za KADCO ambazo hamkutaka ziende TAA ndiyo zilizozuia kumalizika huu mkataba. Hizi liability, maelezo ya ukweli kabisa ni kwamba asilimia mia moja KADCO inamilikiwa na Serikali, nipo sahihi? Kama hivyo ndivyo, maana yake Serikali si inamiliki na na hizo liability ama liabilities ameachiwa yule aliyekuwa mmiliki wa KADCO kabla Serikali haijachukua umiliki? (Makofi)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, kwa sababu KADCO kama kampuni iliyosajiliwa chini ya Sheria ya Makampuni ilikuwa ina hadhi za kisheria. Kwa hiyo, transition iliyofanyika baada ya Serikali kuwa na hisa zote ilikuwa ni kuiweka sasa chini ya muundo wa Serikali ambapo sasa mambo ambayo yanafanyika sasa, nafikiri ni yale ninayosema, hatua mojawapo ni kisheria. Hii ni baada ya ile lease agreement, moja, haitakuwa na mkataba wowote; lakini pili TR ambaye kwa sasa ndiye msimamizi mkuu, nafikiri chini ya Wizara husika, kwa sababu kufikia Februari sheria itakuwa imepita, naamini…
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa AG endelea au ulikuwa umemaliza?
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilikuwa naamini kwamba kwa sababu kuna utaratibu..
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, baada ya ule Muswada, wiki ijayo unaposomwa kwa mara ya kwanza, utakuwa umeshawekwa tayari, utakuwa umeshakuwa umeshakuwa gazetted.
SPIKA: Kwa sasa nani anaendesha kiwanda cha KIA?
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, ni KADCO chini ya usimamizi wa Serikali.
SPIKA: KADCO ambaye mkataba wake umekwisha. (Makofi)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, Lease agreement haijafikia ukomo.
SPIKA: Hii ndiyo Novemba unayoitaja au ni Novemba mwakani? Maana umesema mwenyewe hapa, Mwezi wa Kumi na Moja na ndiyo leo hapa tupo Tarehe 4 Mwezi wa Kumi na Moja. Ni mwezi huu au ni Mwezi wa Kumi na Moja mwakani?
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, no ni Mwezi wa Kumi na Moja, mwaka huu.
SPIKA: Mwaka huu?
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, ndiyo.
SPIKA: Sasa, kwa kweli kwenye jambo hili mnalipa Bunge wakati mgumu. Kwa sababu kama kampuni hiyo ya KADCO ambayo umiliki asilimia 100 ni wa Serikali na iko chini ya Msajili wa Hazina, Mkataba wake umeisha bado iko site inafanya kazi. Masharti yake ya uendeshaji wa kiwanja, huo mkataba ulishaisha. Uliobaki sasa hivi ni wa lease pekee. Sasa ule wa lease unawaruhusu kweli kuendesha uwanja? Mheshimiwa AG, hii Lease Agreement inawapa wao mamlaka ya kuendesha uwanja baada ya mkataba kuisha? Kwa sababu kisheria mseme hivi, tumewaongeza muda kwa sababu tunataka tubadili sheria. Ukisema mkataba umeisha bado wako pale wanafanya nini? (Makofi)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, nafikiri tunaongea lugha moja. Kwa sababu ninaposema TR ndiye anayesimamia kama makampuni mengine ambayo yako chini ya Serikali, maana yake Katibu Mkuu mwenye dhamana na Waziri mwenye dhamana wana usimamizi wa moja kwa moja. Hii transition ninayoisema ya kuletwa sheria, maana yake lengo lake kubwa itakuwa ni kuipa ile comprehensive mandate TAA kuweza kuendesha operations za viwanja vyote nchini.
SPIKA: Yaani mimi nakuelewa sana. Aweze huyo TAA kuendesha viwanja vyote, isipokuwa KADCO mpaka anahitaji sheria? Sheria mpya inahitajika kwa ajili tu ya KADCO? Haya Mheshimiwa Waziri malizia mchango wako. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, Mwongozo wa Spika.
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, nimewasikia lakini sasa Mheshimiwa Waziri alikuwa ameshasimama na mwongozo unaombwa akiwa hajasimama. Kwa hiyo, nimewaona wacha Mheshimiwa Waziri amalizie halafu nitawapa nafasi. Mheshimiwa Waziri.
WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, kwa ufupi tu kama Mheshimiwa AG alivyosema, sisi tumeshaandika kuomba Serikali ili kwa kipindi hicho tupate angalau hicho kibali tuweze kumpa mpaka hapo sheria mpya itakapotungwa.
MHE. CHRISTOPER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, hiyo Serikalini linaendelea.
MHE. CHRISTOPER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: KADCO, KADCO, KADCO!
MHE. CHRISTOPER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Saashisha Mafuwe.
MWONGOZO WA SPIKA
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, jambo hili hapa ndani linaleta mkanganyiko mkubwa sana. Kule site kwa wananchi lina mkanganyiko mkubwa zaidi. Sasa hivi kuna zoezi linaendelea, kulipa fidia, Mheshimiwa Rais ametoa bilioni 11, wananchi wameelimishwa wameelewa na haikuwa kazi rahisi. Nilikuwa naenda site mimi kuzungumza nao, wakiwa na hasira kubwa mno, wameelewa jambo hili. Sasa, sasa hivi wanasikia tena wanapisha uwanja wao kwa mapenzi kwamba uwanja ni mali ya Serikali, hapa ukisikiliza hii sentensi maana yake ni kwamba KADCO sasa haijulikani ni ya nani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba Mwongozo wako, ikiwezekana Serikali ipewe muda ndani ya wiki hii, Jumatatu au Jumanne walete tamko ili kuondoa confusion, kwa sababu tukiliacha hivi kule site litatuletea vurugu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukisikiliza maelezo ya Mheshimiwa Waziri pamoja na Mwanasheria ni dhahiri kwamba KADCO inaelea mahali, haina mwenyewe. Sasa ili tupate sentensi tusichanganye wananchi. Kama sisi humu ndani vinatuchanganya kule site itakuwaje? Mtatupa kazi kubwa na zoezi lile linaloendela kule.
Mheshimiwa Spika, naomba sana utupe Mwongozo wako lifikie mwisho, tupate sentensi ya Serikali itakayoeleweka kwa wananchi, kwamba KADCO ni nani?
SPIKA: Haya ahsante sana. Mheshimiwa Ole-Sendeka.
TAARIFA
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kutoa taarifa. Bunge hili ni Bunge lililopo kwa mujibu wa Katiba na Maazimio ya Bunge yanapaswa kuheshimiwa, kwa sababu Bunge linapofanya maazimio na sehemu ya pili Serikali ipo, kwa maana ya Waziri Mkuu, Mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri, maelezo yote yaliyotolewa na Attorney General ambae ninamheshimu sana, pamoja na Profesa ambaye ninamheshimu sana, kwa kweli hayana sababu yoyote (hayatoi sura nyingine) isipokuwa Serikali kupuuza kutekeleza Azimio la Bunge. Hakuna lugha nyingine ya kistaarabu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine lililo kubwa zaidi, nchi hii tuna uzoefu, kuna taasisi nyingi za Serikali ambazo shughuli zake zimetoka kutoka taasisi hii kwenda taasisi nyingine, taasisi zote hizi mbili ziko chini ya TR, mnashindwa nini leo kuihamisha, ili kama mnataka kubinafsisha tena TAA au viwanja vinavyosimamiwa na TAA, mje muuze tu kwa bei ya jumla, kama ndiyo mmeamua kuelekea huko, kwa sababu kuna hatari, nami nataka niwaambieni…
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
SPIKA: Sekunde 30, malizia.
MHE. CHRISTOPER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, haya, namalizia. Jamani naomba muone hali ni mbaya sana. Tumesomesha vijana wengi, darasa alilokuweko Dkt. Tulia Ackson na alilokuwepo Prof. Mbarawa kuna wenzenu mlisoma nao, kama ninyi mmeweza kuongoza taasisi hizi kubwa, hivi kweli hamna Watanzania wanaoweza kumudu kuendesha hivyo viwanja vya ndege mpaka muwe na mawazo yote ya kukabidhi kila kitu ughaibuni? Naomba niwaambie hayawafurahishi wapiga kura wetu na haifurahishi Taifa. KADCO iondoke, ikabidhiwe TAA na viwanja vya ndege viongozwe na Watanzania wenyewe. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, Mwongozo wa Spika.
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tutulie kidogo, tutulie kidogo. Mheshimiwa AG hebu nisaidie, nani alikuwa anamiliki hicho kiwanja kabla KADCO hawajaja? Maana siyo KADCO waliojenga, ama ni KADCO wamejenga? Nani alikuwa anamiliki hicho kiwanja kabla ya KADCO? Waziri au nani anataka kujibu?
SPIKA: Waheshimiwa Waziri.
WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, Kiwanja cha KADCO kwanza kilikuwa Kiwanja cha Serikali, I mean Kiwanja cha KIA.
SPIKA: KADCO haina kiwanja ni kiwanja cha KIA.
WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika ni kiwanja cha KIA…
SPIKA: Kiwanja cha KIA.
WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, Kiwanja cha KIA kilikuwa Kiwanja cha Serikali, halafu wakati wa ubinafsishaji, ikaundwa kampuni ambayo kuna baadhi ya watu wa private sector waliingia. Mwingereza nafikiri kampuni ya Kiingereza MacDonald pamoja na Kampuni ya South Africa. Baada ya kuona ule utaratibu uliowekwa siyo wa kuridhisha, Serikali ikaamua kuununua na wakalipa hiyo hela na ikatoa maelekezo huku nyuma kwamba kiwanja hicho kirejeshwe kwa TAA lakini kwa nini hakikuweza kurejeshwa kwa wakati huo wote.
Mheshimiwa Spika, sasa, KADCO sasa hivi ilivyo ni kampuni ya Serikali chini ya asilimia 100 na KADCO sasa hivi inaendeshwa na Mtanzania, haiendeshwi na watu wa nje na wafanyakazi wale wote ni Watanzania.
SPIKA: Sasa, nisaidie jambo jambo moja halafu tuendelee mbele Waheshimiwa Wabunge. Hii KADCO, maelezo yanayotoka ndiyo yanayotupa wasiwasi kama Bunge. KADCO asilimia 100 ni ya Serikali, kwa nini hii mijadala huwa inakuja na kwenda? KADCO asilimia 100 ni ya Serikali, TAA asilimia 100 ni ya Serikali, shida iko wapi ili Bunge tusaidie kwenye hiyo shida, tukwamue huo mkwamo ambao unatokea kati ya KADCO na TAA. (Makofi/Kicheko)
WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, tunakoelekea sasa hakuna mkwamo, kwa sababu kama alivyosema Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wiki hii italetwa sheria ya kusomwa mara ya kwanza ambayo itaweka mawanda yote kwa ujumla ya kuondoa KADCO kwenye TAA.
MJUMBE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Sasa unajua hizi taarifa zimetukutia katikati kwamba na mkataba umeisha na hapa tuko Bungeni na sisi tutakuwa sehemu ya huu mchakato, tutakuwa sehemu, Serikali hebu itufafanulie huyu KADCO atafanyaje kazi, anaendeleaje kufanya kazi wakati mkataba haupo? Mwanasheria Mkuu wa Serikali, tufafanulie hilo tutoke hapa tukijua kwamba huo uwanja wa Watanzania uko salama pamoja na KADCO kuendelea kuendesha wakati mkataba haupo.
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, nafikiri ufafanuzi wa kwanza ni kuomba subira kama ilivyo subira yavuta kheri kwa sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Spika, hakuna ubishi juu ya umiliki wa uwanja kwa Serikali, vilevile, hakuna ubishi juu ya uamuzi wa Serikali ku-take over. Pia, hakuna ubishi juu ya Azimio la Bunge hili la mwaka jana la shughuli zote za KADCO kuhamishiwa TAA. Sasa Taarifa ya Serikali kwamba, Baraza limekwishaamua na Serikali inaleta hapa Muswada, Muswada ambao kwa mujibu wa taratibu mnajua kwamba Bunge hili ndiyo litakuwa na dhamana ya kuujadili na kuupitisha.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Spika, taarifa.
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kinachoweza kufanyika labda wiki ijayo Serikali iweze kuleta maelezo ya kuelezea hiyo transitional arrangements zilizosalia.
SPIKA: Sawa. Sasa Waheshimiwa Wabunge, nitamruhusu Mheshimiwa Mgungusi halafu kwenye hoja hii tutafanya maamuzi sasa halafu tusonge mbele. Mheshimiwa Mgungusi.
TAARIFA
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nafikiri kwa kifupi, mimi sijaona nia ya dhati, tuseme Wizara ya Uchukuzi, kama siyo Serikali juu ya sakata hili la KADCO na KIA. Maelezo ya Mheshimiwa Waziri na AG, yanazungumzia mchakato ulivyokuwa mgumu kuhamisha KADCO kwenda TAA ambazo zote zinasimamiwa na TR. Hatukuazimia kwamba KADCO iende TAA, hoja yetu ni ule Uwanja wa KIA ndiyo wakwetu, Uwanja wa KIA uende TAA, hauhitaji sheria na mchakato. Kwa hiyo, mchakatao ufuatwe namna ya ku-dissolve KADCO au KADCO kampuni tanzu ya TAA, hilo ni jambo la kisheria la baadae. Issue yetu ilikuwa siyo KADCO kama lilivyo, Uwanja wa KIA mara moja uende TAA ndiyo ilikuwa ajenda hata mwaka jana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la nyongeza tu, nasema nia ya dhati haipo kwa maana ya kwamba, Menejimenti ya KADCO wanaendelea kuongea kwamba, Azimio la mwaka jana la Bunge limetolewa lakini bado wao hawatofanya kama vile ambavyo inapaswa, kwa maana KADCO itaendelea ku-run uwanja. Kwa hiyo, kilichopo sasa hivi wanapambana huko uvunguni, wanafanya lobbying kwamba Azimio la Bunge lisitekelezeke. Hicho ndicho kinachoendelea KADCO sasa hivi. (Makofi)
SPIKA: Mwanasheria Mkuu wa Serikali, naona ulisimama.
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, nilisimama kumpatia taarifa Mheshimiwa Mbunge, ninaemheshimu sana kwamba siyo taarifa yangu wala siyo taarifa ya Mheshimiwa Waziri iliyotolewa hapa kwamba Serikali ina mpango wa kuihamishia KADCO, TAA.
WABUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, mwongozo wa Spika.
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tutulie kidogo. Mheshimiwa Waziri wa Nchi, naona umesimama.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hoja ambayo iko mezani kwetu ni hoja ya CAG na hoja hii ya CAG ni hoja ambayo inashirikisha pande zote mbili katika kufanya majadiliano. Serikali lakini ni hoja ya Bunge kwa maana ni hoja inayomilikiwa na Kamati za Bunge.
Mheshimiwa Spika, kama itakupendeza, kwa kuwa bado Kanuni zinaturuhusu ambazo hazizuii mjadala huu kuendelea na kuhitimishwa kwa mujibu wa utaratibu. Kama Bunge lako itakupendeza, Mheshimiwa Waziri ametoa maelezo na Mwanasheria Mkuu amatoa maelezo na kwa kuwa tayari Serikali inaonesha kwamba ina hatua ambazo zimekwishachukuliwa.
Mheshimiwa Spika, kama itakupendeza basi katika Bunge, Mkutano huu Serikali tupate nafasi ya kuja kutoa kauli yetu ya Serikali kuonesha hali halisi ya mahali tulikotoka, mahali tulipofikia na hasa katika katika kutekeleza agizo la Bunge na kutekeleza maagizo yote ambayo yalitolewa pia na Baraza la Mawaziri ili tuweze kupata uelewa mzuri wa pamoja, ikikupendeza. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI ZA MITAA (LAAC): Mheshimiwa Spika, Mwongozo wa Spika.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, Mwongozo wa Spika.
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, amesimama hapo Mheshimiwa Waziri, pia nafikiri tulimsikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali akiomba pengine wiki ijayo wapewe muda waje watoe maelezo, lakini changamoto iliyopo ni kwamba, kauli za Serikali huwa hazijadiliwi, unasema halafu tunakuwa tumeelewa kwenye hoja hiyo.
Hoja ya msingi iliyopo mezani sasa, ni kwamba Bunge liliazimia, Serikali ikatoa majibu kuashiria kwamba hilo jambo limeshafika mahali, sehemu. Sasa leo tena imekuja na maelezo ya ziada. Kwa sababu hii Taarifa ya CAG ambayo inajadiliwa leo ni ya tangu Machi na hapo majibu yalishatokea, yalishatokea yalishatokea. (Makofi)
Februari mwakani siyo muda mrefu, lakini hoja iko pale pale. Hii KADCO ni ya Serikali na TAA ni ya Serikali, yaani KADCO inataka kulisimamisha Bunge? Yaani KADCO kama kampuni inataka kulisimamisha Bunge? Sawa, tuendelee na michango. Tutafanya uamuzi, sisi ndiyo Bunge tuko hapa na ndiyo kazi yetu kuisimamia Serikali. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza na mimi naunga mkono hoja ya Dkt. Mpango. Mimi nina maeneo matatu nataka nijielekeze, la kwanza ni kutoa ufafanuzi kuhusu landing fees kwenye viwanja vyetu vya ndege, la pili nitajielekeza kwenye bandari ya Dar es salaam na tatu nitajielekeza kwenye ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya Wabunge wamezungumza kwamba landing fees ya viwanja vyetu vya ndege iko juu sana, lakini ukweli wenyewe ni kwamba landing fees ya viwanja vya ndege vyetu vya Tanzania iko chini ukilinganisha na ya viwanja vyote katika region yetu. Hapa Dar es Salaam sasa hivi au Tanzania landing fees inakuwa ni kati ya dola tano mpaka dola tatu kwa ndege yenye uzito wa kilogramu 1,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Kenya hasa kiwanja cha Nairobi, Mombasa na Moi, wao kwa ndege yenye uzito wa kilogramu moja mpaka kilogramu 1,500 wanachaji dola 10. Kwa upande wa South Africa hasa kiwanja cha Johannesburg, Capetown na Durban kwa ndege yenye uzito wa kilogramu 1,000 wanachaji dola 7.52. Kwa upande wa Msumbiji viwanja vya Maputo, Bella na Nampula wanachaji dola 11.5. Kwa hiyo, viwanja vyetu hapa landing fees ni ya chini kabisa huwezi ukalinganisha na viwanja vyoyote katika nchi zetu za jirani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa ambayo sasa hivi Serikali inafanya ni ujenzi wa viwanja vyetu, sasa hivi tunajenga jengo la terminal three pale uwanja wa Dar es Salaam, tunajenga jengo la abiria huko Mbeya, tunajenga uwanja wa Mwanza na wiki inayokuja tutafungua tender au tutapata mkandarasi kwa ajili ya kiwanja cha Sumbawanga, Shinyanga, pia tutajenga jengo la abiria kwa ajili ya uwanja wa Kigoma na Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko mbioni sasa kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Musoma, Iringa, pamoja na Songea. Tunaamini kazi yote hii tunayoifanya tuna hakika kwamba viwanja vyetu hivi vitachangia sana na nchi yetu itakua hub kwa ajili ya ndege kubwa za kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa bandari. Ni kweli usiopingika kwamba mizigo kwenye bandari yetu ya Dar es Salaam imepungua lakini siyo bandari ya Dar es Salaam tu. Kwa mfano bandari ya Durban - South Africa mizigo imepungua kwa asilimia 10, bandari ya Mombasa imepungua kwa asilimia 1.5 na bandari ya Dar es Salaam kwa ujumla imepungua kwa asilima 5.47.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sababu za msingi ambazo zilisababisha mizigo kwenye bandari ya Dar es Salaam kupungua. Ya kwanza wafanyabiashara wengi zamani walikuwa hawapendi kulipa kodi, sasa tumeendelea kuwabana na kila mtu analipa kodi na hivyo wafanyabiashara wengi sasa wamekimbia. Pili iliyosababisha hivyo ni kudorora kwa bei ya shaba duniani. Hiyo imesababisha mzigo kutoka Zambia kutokupita kwa wingi kwenye bandari ya Dar es Salaam na kusababisha mzigo wa bandari Dar es Salaam kushuka. Pia kuna matatizo kwenye uchumi wa dunia hasa China ambapo mizigo yetu mingi inatoka huko imesababisha mizigo vile vile kupungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande mwingine kuna changamoto kwenye miundombinu ya reli ambayo haiko vizuri na hii imechangia sana katika kupungua mizigo yetu katika bandari ya Dar es Salaam kwani inachukua muda mrefu kusafirisha mizigo kutoka hapa kupeleka nchi za jirani. Pia kuna changamoto nyingine ambayo bandari yetu ya Dar es Salaam inayo. Miundombinu ya bandari ya Dar es Salaam si mizuri hasa kina cha maji, kuanzia bandari ya namba moja mpaka namba saba sasa hivi ina kina cha maji takribani mita 10 na kwa meli kubwa za kisasa inatakiwa takribani iwe na kina cha maji ambacho ni mita 14. Sasa tuna mpango kabambe wa kuhakikisha kwamba tunaboresha bandari yetu ya Dar es Salaam kuhakikisha kwamba meli kubwa za kisasa zinaingia na zinaleta mizigo kwa wingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ya mwisho kuhusu reli, mchakato wa ujenzi wa reli ya kati unaenda, vizuri tumetangaza tender kwa lot ya kwanza, ambayo inatoka Dar es Salaam mpaka Morogoro, wakandarasi kama 39 mpaka sasa hivi wameomba, tunaamini tutakapofungua tender hiyo tarehe 6 Desemba watafikia wakandarasi kama 50 hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya pili tutaanzia Morogoro mpaka Makutopora alafu na lot ya tatu itaanzia Makutopora mpaka Tabora, lot ya nne itaanzia Tabora mpaka Isaka na lot ya tano itaanzia Isaka mpaka Mwanza ambayo kazi za tender kwa ajili ya kazi hiyo zitatangazwa wiki inayokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa, naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya SADC ya Usimamizi wa Mazingira kwa ajili ya Maendeleo Endelevu (The Southern African Development Community SADC – Protocol on Environmental Management for Sustainable Development)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote tena napenda kuchukua fursa hii kwanza kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kupata fursa hii nami kuja kuhitimisha hoja zetu hizi mbili za Maazimio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishukuru sana Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira kwa michango mizuri na maekelezo mazuri ambayo wanatupatia hasa kwenye Maazimio haya mawili. Naomba niwahakikishie tu kwamba maoni yao, mawazo yao na fikra zao zote tumezichukua na tutakwenda kuzifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia, wameonesha kwa dhati umuhimu mkubwa wa kupambana na emission hizi ili kuhakikisha kwamba na sisi Taifa letu na ulimwengu kwa ujumla unakuwa salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe wote wamechangia vizuri Maazimio yote mawili; kwanza, Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya SADC ya Usimamizi wa Mazingira kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu. Kama tunavyojua kwamba emission hazina mipaka kwa vile ni juhudi za pamoja, zinahitajika kwa nchi zote za SADC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kuchangia na kutoa msisitizo mkubwa kuhusu Azimio la Kuridhia Marekebisho ya Kigali ya Kupunguza hizi Emissions za HFCs ambazo zina athari kubwa kama alivyosema Mheshimiwa Juma Hamad.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi tu, nakubaliana na Bunge kwamba, kwa pamoja hatunabudi kupitisha maazimio haya kwa sababu zina faidi kubwa ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezieleza hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana katika Bunge letu hili Tukufu la bajeti ili kukamilisha kazi tuliyoanza leo asubuhi ambapo niliwasilisha hoja hii ya Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kukushukuru wewe mwenyewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wenyeviti wote wa Bunge kwa jinsi walivyotuongoza na kusimamia majadiliano ya hoja hii pamoja na hoja nyingine zilizotangulia. Aidha, nichukue fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa wawazi na kutoa michango yao ya kina wakati wa majadiliano haya. Niwathibitishie kwamba michango yao yote tumeichukua kwa uzito mkubwa na kwenda kuyafanyia kazi ili kuendelea kuleta ufanisi na utekelezaji mzuri kwenye sekta ya uchukuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia kipekee nimshukuru Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Selemani Moshi Kakoso na Waheshimiwa Wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwa hoja nzuri walizozitoa kwenye Kamati yetu. Nikiri kwamba hoja zao ni muhimu sana kwa maendeleo na ukuaji wa miundombinu na huduma za usafiri na usafirishaji hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Wabunge wote waliochangia katika bajeti hii. Waheshimiwa Wabunge 26 wamechangia wakati wa majadiliano ya hoja hii ambapo Wabunge 20 wamechangia kwa kuongea na Waheshimiwa Wabunge sita wamechangia kwa maandishi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, muda mchache uliopita Mheshimiwa Naibu Waziri amemalizia kuchangia na kujibu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge kwa ufasaha na weledi mkubwa. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa jinsi ambavyo amejibu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge na nitajibu baadhi ya hoja zilizobaki. Aidha, naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Wizara itajibu hoja zote za Waheshimiwa Wabunge kwa maandishi na kuziwasilisha hapa Bungeni kabla ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Bunge hili la bajeti unaoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nianze kuhitimisha hoja yangu kwa kutoa ufafanuzi wa kijumla wa baadhi ya hoja zilizojitokeza kwenye maeneo makubwa yaliyojitokeza.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema asubuhi hii leo kwamba Sekta ya Uchukuzi imeendelea kutoa mchango mkubwa wa ukuaji wa uchumi wetu na Taifa kwa ujumla na kuwa sekta hii ni sekta wezeshi hasa kwa Sekta ya Kilimo, Madini, Utalii, Viwanda na Biashara. Kama nilivyosema mwaka 2022, Sekta hii ya Uchukuzi ilikua kwa 3.8% na ilichangia pato la Taifa kwa takribani 6.7%. Kwa upande wa fedha za kigeni kama nilivyosema asubuhi, pato la kigeni ambalo linachangiwa na sekta hii limeongezeka kutoka Dola za Kimarekani bilioni 1.6 mwaka 2022 hadi kufikia Dola za Kimarekani bilioni 2.4 mwaka 2024 ambayo limeongezeka kwa 50% na mchango huu mkubwa kwa kiasi kikubwa umetokana na Sekta ya Uchukuzi hasa eneo la bandari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukweli huo ndiyo uliosababisha au uliosukuma Waheshimiwa Wabunge takribani 85% leo wamejikita zaidi kwenye eneo la bandari wengine wamejikita kwenye wharfage.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamechangia na wamefanya hivyo pia kwa sababu bandari ndio lango kuu la uchumi wa nchi yetu na takribani 37% ya makusanyo ya kiforodha ya TRA yanakusanywa kupitia hasa kwenye Bandari yetu ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, tunafahamu changamoto mbalimbali za Bandari ya Dar es Salaam, kama tulivyojua kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa la meli kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Leo ukipita na ndege ama ukipita na boti kwenda Zanzibar au kwenda maeneo mengine kwenye nanga, utakuta takribani meli kati ya 20 mpaka 25. Kuna baadhi ya siku zinafika mpaka meli 30 na meli hizi zinakaa pale nangani kwa siku kuanzia kumi mpaka siku 15 na kila siku mwenye mzigo analipa takribani dola 25 ambayo hiyo kwa ufupi ni takribani shilingi milioni 50, 52 au 53.
Mheshimiwa Spika, tunazo changamoto kubwa hasa kwenye eneo la gati. Gati tulizonazo Bandari ya Dar es Salaam hazitoshi, hivi leo ninavyozungumza Bandari ya Dar es Salaam kuna gati 13. Tuna gati namba zero mpaka gati namba 11, halafu tuna gati namba 12 kwa ajili ya mafuta - KOJ, tuna gati 13. Wakati bandari za wenzetu hasa tunazoshindana nazo kwa mfano Bandari ya Mombasa wana gati 19. Gati 13 ni gati za kawaida na gati 6 ni kwa ajili ya kontena. Pia, wana gati maalumu kwa ajili ya kushushia nafaka.
Mheshimiwa Spika, mshindani wetu mkubwa mwingine ni Bandari ya Durban. Bandari ya Durban ina gati 50, gati 31 ni za mizigo ya kawaida na gati 10 ni kwa ajili ya makontena na magati 9 ni kwa ajili ya bidhaa chafu. Hivyo, lazima tufanye maamuzi sahihi ya kujenga bandari wakati huu, lazima tujenge gati mpya kuanzia leo otherwise tukifanya kesho tutakuwa tumechelewa. Tunao ushindani mkubwa hasa kwa wateja wetu wa kutoka Zambia, DRC, Malawi, Zimbabwe pamoja na Kenya. Kwa hivyo, Serikali tumeamua kuanza uwekezaji mkubwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam kuhakikisha kwamba hatuendi kuwapoteza wateja wetu.
Mheshimiwa Spika, Serikali tumeamua sasa kama nilivyosema asubuhi, tunajenga matanki 15 ya mafuta kwa ajili ya kuhifadhia mafuta mita za ujazo 420,000 kwa siku kwa wakati mmoja ambapo mradi huo una gharama ya shilingi bilioni 578.6. Serikali imeanza kutoa pesa hizo.
Mheshimiwa Spika, pia tunajenga Bandari ya Mbamba Bay ambayo gharama yake ni takribani shilingi bilioni 75, bandari hii ni muhimu sana hasa kwa ndugu zetu wa Malawi na Zambia. Pia, tunafanya ukarabati wa Bandari ya Kemondo na Bukoba Mjini kwa gharama takribani shilingi bilioni 40. Tumenunua vifaa vya kisasa SSG (Ship to Shore Gantry Cranes) ambazo zimegharimu takribani shilingi bilioni 250.
Mheshimiwa Spika, tunaendelea na uwekezaji wa ujenzi wa Bandari Chafu huko Mtwara ambayo itajengwa kule Kisiwa Mgao, tayari Mkandarasi ameshapatikana. Tunaendelea na ujenzi wa gati pale Dar es Salaam ambayo itakuwa na urefu wa mita 500 ambapo kwa ufupi hizo zitakuwa ni gati mbili, pale tunapopaita marine wharf, sasa hivi tuko kwenye hatua ya mwisho ya kumpata mkandarasi. Tunaendelea kufanya ukarabati wa Bandari ya Mwanza South kwa shilingi bilioni 20.
Mheshimiwa Spika, haya yote yanafanywa kupitia Serikali pia tunaendelea kuhimiza sekta binafsi kuwekeza na kufanya kazi na Serikali kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Kama nyote mnavyojua bandari namba nne mpaka namba saba tayari sasa hivi iko private sector, gati namba nane mpaka 11 tuko katika hatua ya mwisho ya kumpata mwekezaji mwingine. Vilevile, Serikali tuko katika hatua nyingine ya kutafuta mjenzi kwa njia ya private sector au kwa kutumia taratibu yoyote kwa ajili ya gati namba 13 mpaka namba 15.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema Waheshimiwa Wabunge wengi 85% leo wamechangia kuhusu wharfage, kwamba malipo ya wharfage yanayokusanywa yabaki TPA, suala hili ni muhimu; tumelipokea na tutalifanyia kazi. Tunaenda kulifanyia kazi kwa sababu ni muhimu kwa maslahi ya bandari na Taifa kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kulikuwa pia na suala lingine la Air Tanzania kuja Dodoma, kutoka Dodoma kwenda Mbeya, kutoka Dodoma kwenda Mtwara na maeneo mengine. Tunatamani kwamba Air Tanzania isambae Tanzania nzima, lakini changamoto inayotukabili hatuna ndege za kutosha. Kila mwaka Serikali tunaendelea kununua ndege, kama nilivyosema mwaka huu tumepokea ndege tatu na mwakani naamini tutaanza kupokea ndege nyingine. Naomba niwapatie habari njema kuhusu hapa Dodoma, kuanzia mwezi Oktoba tutaleta ndege kubwa ya Max 737 ambayo itaanza kuja Dodoma, kwa sababu Dodoma wasafiri ni wengi na ukweli wenyewe ndege tuliyonayo haiwezi kutimiza mahitaji ya Dodoma. Kwa hiyo uwanja wetu wa Dodoma sasa hivi hauwezi kuruhusu ndege kubwa ya Boeing 737 Max.
Mheshimiwa Spika, tunategemea mwezi Oktoba na Novemba uwanja wetu wa Msalato utakuwa tayati na tutaanza kufanya kazi hiyo, ingawaje jengo la abiria na control tower itakuwa havijakamilika lakini ndege ile itaweza kutua kwa sababu tutajenga temporary pale kama alivyosema Mheshimiwa Ezra na tutairuhusu ndege ile ku-control kwa kutumia temporary control tower ambayo tutaijenga pale kwa muda mfupi, lakini ni muhimu kwa sasa na wakati umefika kuleta ndege kubwa.
Mheshimiwa Spika, kwa siku moja hapa tunaleta ndege nne, hazitoshi lakini tunaamini tukileta ndege kubwa mbili zitaweza kuhimili mahitaji ya Dodoma. Vilevile, tutaleta ndege nyingine itaanzia Dar es Salaam hapa Dodoma mpaka Mwanza, hii ni habari njema sana kwa wananchi wa Mwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaendelea kuangalia soko linasemaje, tunaamini huko mbele pengine tutatoka hapa kwenda Mbeya, Kilimanjaro na maeneo mengine, safari ni hatua tumejipanga na tunaamini tutafika vizuri.
Mheshimiwa Spika, suala la Air Tanzania kwenda Pemba. Mimi natoka Pemba nitahakikisha kwamba ndege ya Air Tanzania itakwenda Pemba bila matatizo yoyote.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ambayo pia imechangiwa kwa mtazamo au kwa hisia kali ya malipo ya passenger service charges yabaki TAA. Hili suala ni muhimu na tunalijua na sisi kama Serikali tumelichukua tunakwenda kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, kuna hoja ambayo Wabunge wa Kigoma, Rukwa na Katavi wamelichangia sana suala hili, nakubaliana na hawa Waheshimiwa Wabunge, ni kweli wananchi wa mikoa ile wanapata tabu sana kwa ajili ya usafiri wa majini. Jana tulikaa sana kulizungumza jambo hili na sisi kama Serikali tumeamua kufanya yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mtazamo wa muda mfupi au kwa kutatua tatizo hili kwa muda mfupi kwanza tumeamua kuikarabati meli ya MV Liemba. Tayari tumeshampata mkandarasi na mkataba ulisainiwa tarehe 11 Novemba, 2023 na tayari Serikali imeshatoa shilingi bilioni tano za advance payment kwa ajili ya malipo ya kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hatukuangalia hivyo, kama tulivyokubaliana na wananchi wa kule kupitia Wabunge wao, tumekubaliana tufanye ukarabati wa MV Mwongozo. MV Mwongozo ni meli ambayo ilikuwa inafanya kazi zamani, ni meli nzuri, lakini baada ya kutokea ajali ya MV Victoria meli hiyo ilisimamishwa kwa sababu wataalam walisema kulikuwa na shida ya stability ya meli hiyo. Sasa tumepeleka timu ya wataalam wamefanya uchunguzi wa kutosha na wametushauri nini cha kufanya ili meli ile iweze kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Spika, tayari wametupa gharama za meli hiyo ambayo kuitengeneza ili iweze kufanya kazi vizuri itagharimu dola za Kimarekani milioni 2.77 ambapo Serikali nayo imetoa shilingi bilioni tano kwa ajili ya ukarabati wa meli hiyo. Huu ni mpango wa muda mfupi, tunaamini meli ya MV Mwongozo itakapofika mwisho wa mwaka huu itakuwa tayari. Ni kazi ambayo naamini kunako baina ya miezi sita mpaka saba itakuwa imekamilika.
Mheshimiwa Spika, tuna mpango pia wa muda mrefu. Kwanza, tunakwenda kujenga meli mpya ya mizigo ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukua tani 3,500 ambayo itagharimu shilingi bilioni 158 na mkandarasi tumeshampata. Kitu cha muhimu tunachokwenda kukifanya kule kwanza ni kujenga shipyard, kiwanda cha kutengenezea meli kwa ajili ya Ziwa Tanganyika. Ni mara ya kwanza katika nchi yetu katika maziwa yote haya tuliyonayo Tanzania hakuna kiwanda cha kutengenezea meli.
Mheshimiwa Spika, gharama ya kiwanda hicho ni takribani shilingi bilioni 313 na mkandarasi tumeshampata. Mwisho wa mwezi huu tutamlipa mkandarasi huyo pesa za advance payment hasa kwa utengenezaji wa kiwanda hicho, kwa sababu kwanza unatakiwa utengeneze kiwanda halafu ndiyo unaenda kutengeneza meli. Tunaamini mipango hii ya Serikali kuanzia ya muda mfupi na ya muda mrefu itaweza kutatua tatizo lote la usafiri wa Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2024/2025, tumepanga takribani shilingi bilioni 190 kwa ajili ya ujenzi wa meli. Kati ya pesa hizo shilingi bilioni 116 tumeelekeza Ziwa Tanganyika, ambazo hizi ni pesa nyingi ukilinganisha na eneo hilo lote, shilingi bilioni 100 tumeelekeza katika maeneo mengine kwa vile hili ni jambo kubwa sana na nawaomba Waheshimiwa Wabunge wa Katavi, Kigoma na Rukwa watuamini, tunakwenda kufanya kazi hii. Watuamini tutahakikisha kwamba kazi hii itafanyika kwa umakini mkubwa na kwa wakati tuliopanga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya hoja ambazo zimewasilishwa hapa na Kamati ya Kudumu ya Miundombinu. Hoja ya kwanza inasema, hakikisha kwamba Wizara inasimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi yake yote ili iweze kukidhi viwango bora endelevu (sustainability) na kuwepo kwa thamani ya fedha. Majibu ya hoja hiyo ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza ushauri umepokelewa, Serikali imeendelea kuweka mifumo mbalimbali ya kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuanzisha kitengo maalumu kinachojitegemea cha kufuatilia na kufanya tathmini ya miradi mbalimbali yote inayosimamiwa na Wizara ili kuangalia value for money. Tunaamini Mradi wa SGR tulioutekeleza una viwango vya juu, watu wengi wamekuja kujifunza kwenye Mradi wetu huu wa SGR. Watu wametoka Uganda, DRC, Burundi na nchi nyingine nyingi wamekuja kujifunza.
Mheshimiwa Spika, kuna hoja ya pili kutoka Kamati inasema kwamba, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na uendeshaji wa TRC, Kamati imetoa pongezi kwanza kwa kazi hiyo, kufanya majaribio ni jambo jema, lakini kazi hiyo imalizike kwa haraka. Kwa niaba ya TRC na wadau wote tumepokea pongezi na ushauri uliotolewa na Kamati. Wizara inapenda kujibu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TRC inaendelea na maandalizi ya uendeshaji ili kuanza kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria ifikapo Julai, 2024, kama ilivyoelekezwa na Mheshimiwa Rais. Kwa kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma. Kuhusu ujenzi wa kipande hicho kutoka Dar es Salaam - Morogoro kama nilivyosema asubuhi, umekamilika kwa asilimia 98.93, kazi zilizobaki ni kukamilisha ujenzi wa reli kuelekea bandarini ambako mradi umefikia asilimia 46.12.
Mheshimiwa Spika, vivuko vya juu vya Vingunguti, Airport na Njia panda ya Segerea umefikia asilimia 99.3. Mheshimiwa Mbunge hapa amesema kwamba barabara zake zimefungwa kwa muda mrefu, lakini tunamwambia itakapofika mwezi Juni tutakuwa tumemaliza kuweka lami barabara hizo na tutazifungua rasmi.
Mheshimiwa Spika, hali kadhalika ujenzi wa kipande cha kutoka Morogoro – Makutupora, kilometa 422 umekamilika kwa kiasi cha asilimia 96.61. Kazi zilizobaki ni kukamilisha ujenzi wa vivuko vya juu ambao umefikia asilimia 98.52 na kazi ya uzio imefikia asilimia 86.02. Reli yetu yote ina uzio wa kuzuia wanyama na watu wengine kukatiza wakati reli hii itakapokuwa inafanya kazi. Aidha, TRC inaendelea na majaribio ya njia pamoja na vitendea kazi ikiwemo mabehewa na vichwa vya treni kabla ya kuanza kazi rasmi. Naomba niwahakikishie Watanzania kwamba itakapofika mwezi Julai wataweza kufaidika na reli hiyo na bei za reli hiyo zitakuwa ni bei nzuri hasa kwa lile daraja la tatu.
Mheshimiwa Spika, hoja ya tatu ya Kamati inaishauri Serikali kufanya tathmini ya kuboresha makusanyo katika reli ya MGR, mkakati huu unapaswa kwenda sambamba na juhudi za makusudi za kuboresha miundombinu ikiwemo kutenga bajeti ya matengenezo ya mara kwa mara na ya haraka pale miundombinu ya reli hiyo inapoathiriwa na majanga kama vile mvua.
Mheshimiwa Spika, kwanza, tumeupokea ushauri, lakini Serikali inaendelea na mpango wa ukarabati wa reli hii ya meter gauge ambayo ina urefu wa kilometa 2,707. Mradi huu umegawanyika kwa awamu mbili, awamu ya kwanza ulianza kutoka Dar es Salaam mpaka Tabora, kwa kuongeza uwezo wa kubeba mizigo kwa reli hiyo kutoka tani 13 kwa excel hadi kufikia tani 18.5 kwa excel pamoja na kuweka reli nzito za ratili 80 kwa yadi.
Mheshimiwa Spika, hali kadhalika TRC imesaini mikataba ya ukarabati wa njia ya reli kati ya Tabora na Kigoma yenye urefu wa kilometa 411 na Kaliua – Mpanda yenye urefu wa kilometa 210 na kazi za ukarabati zinaendelea. Sambamba na hilo, TRC imesaini mkataba wa ununuzi wa malighafi ya ukarabati kwa ajili ya ukarabati wa njia ya reli ya kaskazini ikijumuisha kipande cha Ruvu na Mruazi Junction, kazi hii itaanza mara moja. Aidha, kupitia bajeti ya mwaka huu ambao tumeiomba 2024/2025, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 312.0 kugharamia matengenezo ya miundombinu ya reli, MGR.
Mheshimiwa Spika, hoja namba nne iliyowasilishwa na Kamati yetu ni uendeshwaji wa Shirika la Ndege, Kamati imeendelea kuipongeza Serikali kwa ununuzi wa ndege za abiria na mizigo. Hata hivyo, katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 Kamati inaishauri Serikali kuhakikisha inakuwa na ubunifu wa kuboresha usafiri wa anga kupitia ATCL na hatimaye kuzalisha faida ili kuongeza mapato au pato la Serikali. Tunaomba kujibu hoja hiyo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kusimamia na kuiwezesha ATCL katika ufunguzi wa vituo vipya ikiwemo kituo cha Dubai kilichofunguliwa tarehe 29 Machi, 2024, kuendelea na taratibu za kurejeshwa kwa Kituo cha Johannesburg huko South Afrika na maandalizi ya kufungua Kituo cha London. Kama nilivyosema na kwa vituo vya ndani tutaanza na kituo cha kutoka hapa Dodoma kwenda Mwanza na maeneo mengine kuhakikisha kwamba tunaweka network yetu vizuri na hata hapa ndani.
Mheshimiwa Spika, kuna hoja namba tano kuhusu maboresho ya uendeshaji wa reli ya TAZARA. Kamati inatambua juhudi za Serikali katika kuhakikisha kwamba wabia wa uendeshaji wa reli ya TAZARA kwa maana ya Tanzania na Nchi ya Zambia wanakaa meza moja kwa majdiliano kuhusu TAZARA. Serikali zetu mbili Serikali ya Zambia na Serikali ya Tanzania zimeamua kutafuta mbia wa kuwekeza kwenye reli ya TAZARA, hivi tunavyozungumza mazungumzo yanaendelea vizuri kati ya Zambia, Tanzania na Serikali ya China kwa ajili ya kumpata mwekezaji kutoka China.
Mheshimiwa Spika, timu hiyo ambayo inafanya majadiliano inaongozwa na ndugu Mussa Mbura, Mkurugenzi Mkuu wa TAA ambaye ndiye Mwenyekiti wa timu upande wa Tanzania na Zambia. Tunaamini utakapofika mwezi Juni, jambo hili litakuwa limeshafika mwisho na tutahakikisha kwamba TAZARA inasimama vizuri na inaenda vizuri.
Mheshimiwa Spika, tunafanya haya yote kwa ajili ya kuifungua Bandari yetu ya Dar es Salaam, huko Zambia na DRC kuna mzigo mkubwa wa madini na makampuni yote yanayochimba madini huko ni Makampuni ya Kichina, tunaamini tukimpa TAZARA Kampuni ya Kichina tunavutia makampuni mengi ya madini kuitumia TAZARA na tukiitumia TAZARA maana yake tunaitumia Bandari yetu ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, kuna hoja nyingine kuhusu usafiri wa majini kama ilivyoulizwa na Kamati yetu. Kamati inapenda kuikumbusha Serikali kwamba isimamie kwa bidii miradi ile ya kusimamia utafutaji na uokoaji kwenye kituo cha Mwanza. Hili tumelichukua na tunaenda kulisimamia kuhakikisha kwamba mradi huo unamalizika kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna suala la LATRA. Utendaji wa LATRA, Kamati inaendelea kuisisitiza Serikali kuhakikisha kwamba inashughulikia changamoto zote za mgongano wa kiuratibu na kisheria kuhusu masuala ya usalama barabarani ili LATRA iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo bila kuingiliana na majukumu ya Jeshi la Polisi. Majibu ya hoja hii ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha utendaji wa LATRA unaratibiwa bila mgongano hususan na Jeshi la Polisi, LATRA ilikutana na Tume ya Haki Jinai na Jeshi la Polisi na kujadiliana kwa kina namna ya kuondoa changamoto hiyo. Sasa inaandaa rasimu ya mapendekezo ya mabadiliko ya kisheria kwa ajili ya kupata maoni ya wadau kwa hatua zaidi.
Mheshimiwa Spika, kuna suala la mwisho kuhusu Uwanja wa Ndege wa Serengeti. Uwanja wa Ndege wa Serengeti ni muhimu hasa kwa Sekta ya Utalii. Serikali tumeamua, tunakwenda kuujenga uwanja huo kwa kushirikiana na Sekta Binafsi. Uwanja huo ni muhimu sana kwa sababu kwa sasa wakati wa peak season kunakuwa na ndege ndogo nyingi zinaingia kwenye mbuga kule ambapo siyo jambo zuri. Tunaamini tukijenga uwanja huu utachangia sana kwenye Sekta ya Utalii pamoja na uchumi wa nchi yetu kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kabla sijamaliza, naomba kuzungumzia suala moja hapa la mwisho ambalo Mheshimiwa Bonnah amezungumza sana kuhusu kulipa fidia. Tunajua kwamba wananchi wake wanadai Serikali fidia takriban shilingi bilioni 129. Kwenye bajeti hii ambayo tumeomba leo tumeweka fedha kwa ajili ya kuwalipa wananchi hao. Naomba Mheshimiwa Mbunge awe mvumilivu, kuanzia mapema mwezi Julai fedha hizo zitatolewa kwa ajili ya kuwalipa wananchi hao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia hoja hii iliyopo mbele yetu. Mwisho kabisa naomba kutoa hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Reli wa Mwaka 2017
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote ninapenda kuchukua fursa hii kukushukuru sana, pamoja na kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia kwenye Muswada huu. Pia napenda kuishukuru sana Kamati yetu ya Kudumu ya Miundombinu, ni Kamati ambayo nafikiri leo wamefurahia sana kwa sababu kwa kipindi chote hicho walikuwa wamesimamia kwa makini kwamba TRL na RAHCO lazima iwe kampuni moja. Nafikiri walikuwa wanafanya hivyo kwa sababu walikuwa wanajua hasa changamoto zilizopo katika kampuni yetu ya TRL. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sababu za msingi ambazo zimesababisha tuweze kuunganisha TRL na RAHCO. Kwanza kabisa kiutendaji, TRL ina wafanyakazi takribani 1,900 wakati RAHCO ina wafanyakazi 38. TRL kazi yake kubwa ni kuendesha usafiri wa treni, RAHCO kazi yake kubwa ilikuwa ni kujenga miundombinu. Sasa hizi kazi kikawaida zinatakiwa zifanywe pamoja lakini kulikuwa na changamoto kubwa hapo zamani. Kwa mfano, kukitokea tatizo kwenye barabara na RAHCO kama hawako tayari kwenda kutengeneza barabara hiyo au reli ina maana TRL wanashindwa kufanya kazi. Kwa vile ilikuwa siku zote TRL inategemea sana RAHCO na RAHCO wakati mwingine hawako tayari kufanya kazi yao ya kufanya ukarabati wa njia za reli.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ilisababisha kwanza kushuka kwa kiasi kikubwa cha mapato ya TRL pia kwa upande mwingine ilisababisha vilevile utendaji wa bandari yetu. Pia ilisababisha vilevile uharibifu wa barabara kwa sababu mizigo mingi sana ilianza kuhamia kwenye barabara. Kwa bahati nzuri tuliliona kama Serikali na Kamati yetu ya Bunge waliliona wakalisimamia na leo hii tumefanikiwa kuleta Muswada huo. Tunawashukuru sana wale ambao walisimamia jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipekee vile vile napenda nimshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amesimamia sana sana utengenezaji wa muswada huu kwa ajili ya sheria hii ambayo leo tunataka tuipitishe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli muswada huu umekuja wakati muafaka kwa sababu sasa hivi nchi yetu iko katika ujenzi wa standard gauge. Tuna mpango ambao tunajenga standard gauge kwa awamu, sasa tumeanza awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro ambayo ni takribani kilometa 215 ujenzi umeanza, ukijumlisha na zile barabara za kupishana, takribani kilometa 300. Ujenzi huu umegharimu takribani dola za Kimarekani bilioni 1.219.
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya pili itaanza Morogoro mpaka Makutupora. Sasa hivi tumeshampata
Mkandarasi na mazungumzo yanaendelea baina ya Serikali na Mkandarasi huyo kuhakikisha kwamba kazi hiyo inaanza kujengwa mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya pili itakuwa ni Makutupora mpaka Tabora, Tabora – Isaka – Mwanza. Vilevile kutoka Tabora kwenda Kigoma halafu kutoka Tabora kwenda Mpanda – kazi hiyo inafanywa na tunajipanga na tunafanya kila linalowezekana ili kazi hiyo ianze mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na mambo mengi Waheshimiwa Wabunge wamechangia. Kwanza tunashukuru sana kwa sababu Waheshimiwa Wabunge wote wameukubali muswada huu asilimia mia moja. Tunawashukuru sana kwa sababu wanajua muswada huu una manufaa makubwa kwa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na maoni mawili, matatu ambayo nitajaribu kuyagusia moja baada ya lingine. Kwanza kulikuwa na suala la ticket kwamba faini kubwa kwa ajili ya tiketi wale waliokuwa hawana tiketi tumeweka faini asilimia moa moja. Ni kweli tumeweka faini hii kwa sababu tunataka watu sasa wachukue dhamana, wawe na responsibility. Mtu hawezi tu kupanda treni bila ya kulipia tiketi, haiwezekani! Lazima Watanzania sasa tubadilike.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna changamoto. Kuna baadhi ya maeneo ambayo kweli hayana vituo vya kukatia tiketi. Kwenye sheria hii ukienda kwenye kifungu cha 47(3) imezungumzia kuhusu maeneo ambayo hayana vituo vya kukatia tiketi. Sasa hili limeangaliwa vizuri kwenye sheria hii na katika maeneo hayo mtu ataruhusiwa kupanda kwenye treni na atakata tiketi mle ndani ya treni. Lakini maeneo yote ambayo mtu anapanda treni bila tiketi atalipa faini asilimia moa moja. Otherwise lazima tubadilike na tuhakikishe kwamba tunasimamia sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyokwenda utaratibu mwingi sasa tutakwenda kwenye electronic ticket. Hutahitajika hata kwenda kwenye kituo cha kukata tiketi, kwenye simu yako, kama unaponunua vocha, unapolipia maji, kama unapolipia umeme wa luku na tiketi itakuwa hivyo hivyo.
Kwa hiyo, nawaomba Watanzania wenzangu, nawaomba Waheshimiwa Wabunge muelewe sasa lazima kwa wale ambao hawatalipa tiketi au hawatanunua tiketi lazima walipe faini asilimia mia moja, vinginevyo tukifanya hivyo hii biashara haitaenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala la magenge. Ni kweli magenge ni muhimu sana katika uendeshaji wa reli na hapo katikati tulipokuwa na TRL mambo ya magenge yamekufa lakini sasa tunaanza upya na tutahakikisha kwamba tunaimarisha magenge sehemu zote ambazo njia za reli zinapita. Tukifanya hivyo tunaamini hata utendaji, usalama wa reli sasa utaimarika zaidi kwa vile hili ni jambo zuri na tunaendelea kulisimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala ambalo limezungumzwa sana na kila Mheshimiwa Mbunge aliyesimama hapa kuhusu wafanyakazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyakazi waliokuwa TRC ambao walihamia TRL ajira zao ziliendelezwa kwa masharti ya ajira waliyokuwa nayo. Wote ambao walitokea TRC tuliwapeleka TRL na RAHCO na ajira zao ziliendelezwa kama mikataba yao ilivyosema na malimbikizo yao ya madeni yote yalilipwa.
Kwa vile Waheshimiwa Wabunge, wale wote ambao walikuwepo TRC (Tanzania Railway Corporation) ya zamani wote tumewalipa na maslahi yao na haki zao zote za utaratibu wa kazi tulizizingatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyakazi waliokuwa East African Railways Corporation nao vilevile stahili zao zote walilipwa. Ni utaratibu wa Serikali unapomhamisha mtu kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine stahili zake na haki zake zote zinalipwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa wafanyakazi wa TRL na RAHCO watakaohamishiwa kwenye shirika jipya hili, stahili zao zitalipwa. Ukienda kwenye muswada huu, kuanzia kwenye kifungu cha 115 mpaka 118 tunazungumza haki za wafanyakazi wa RAHCO na TRL. Wote ambao watahamishwa haki zao zitaangaliwa na wale ambao watapelekwa Serikali, haki zao zitaangaliwa; na wale ambao watapelekwa kwenye taasisi mbalimbali, haki zao zitaangaliwa; na wale ambao wataachishwa kazi haki zao zitaangaliwa na watalipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwahakikishie Wabunge kwamba sheria hii imeangalia mambo yote hayo, na sisi kama Serikali tumejipanga vizuri. Kulikuwa na suala lingine kuhusu utaratibu wa ufanyaji kazi kwenye sehemu za reli kuhusu survey and inspection. Ukienda kwenye kifungu cha 26 - Surveys and Inspection, tumesema pale; “an authorized officer of the Corporation may, on the production of evidence of such authorization if required to do so enter on any land or a dwelling house,” anaweza kuingia popote. Hicho ni cha kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda tena kifungu cha 26(2) inasema;“Before an authorized officer enters any land or a dwelling house he shall obtain consent of the owner or occupier of the land or dwelling house.” Kwa hiyo, hawawezi tu kwenda kuingia isipokuwa lazima wafuate utaratibu huo ambao tumeueleza na hiyo tumeeleza vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la fidia. Serikalini tunapomhamisha mtu, kwa mfano kama barabara imemfuata mwananchi, Serikali inalipa fidia, lakini kama mwananchi au raia yeyote amevamia barabara, hatuwezi kulipa fidia, na sisi tunasimamia sheria. Ukiangalia kwenye muswada huu tumeeleza very clearly kuhusu mambo ya fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye kifungu cha 34(4); “Acquisition of land and property right during the railway works,” tumeongea very clear. “A railway order should contain such provision as a Corporation considered necessary or experience for the purpose of the order.” Then ukienda zaidi ukisoma mwisho pale namba nne; “the Corporation should pay compansation equivalent to the value of the land or the other property rights acquired.” Kwa vile iko very clear kwenye Muswada huu tutalipa kutokana na mali iliyoko pale na ndiyo tunavyofanya siku zote Serikalini. Kwenye barabara tunafanya hivyo hivyo na kwenye reli tunafanya hivyo hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, kwamba tukiandika hizi sheria tunaangalia zaidi maslahi ya nchi. Hatuangalii leo tu, lakini tunaangalia hata miaka kumi mbele kwa sababu technology inabadilika na kila kitu kinabadilika, ndiyo maana tunaenda mbele. Kwa hiyo, hilo jambo limeangaliwa vizuri na ninaomba ndugu wananchi na Waheshimiwa Wabunge msiwe na wasiwasi na jambo hilo, liko vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na swali kwamba tuweke kwenye madhumuni ya shirika kwamba ionekane kama ni shirika la kufanya biashara. Wakati wote ukitengeneza shirika, madhumuni makubwa ya shirika ni kufanya biashara. Kufanya biashara maana yake ni faida, vinginevyo hakuna maana ya kutengeneza shirika lolote. Madhumuni yaliyoandikwa kwenye muswada huu tunamini kabisa italifanya TRA kutengeneza faida. Jambo tunalotakiwa sisi kama Serikali ni kulisimamia lifanye kazi kutokana na sheria ambayo tunaipendekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile muswada huu umetoa maelezo au vifungu mbalimbali vinazungumzia jinsi ya kulipa uwezo shirika linalokuja kuchukua mkopo. Shirika ambalo lilikuwepo zamani ilikuwa haliwezi kufanya mkopo, lakini shirika jipya hili leo litakuwa na uwezo wa kuchukua mkopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye kifungu cha 6(1)(n) imeeleza very clear na kinasema: “enter into any arrangement with any person or any relevant entity which, in opinion of the Board, shall promote or secure the provision, or improved provision or any service or facility which may separate provide and without prejudice to the generality any of the other function.” Ninazungumza kwamba wanaweza kuingia mkopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ukienda section 14, iko very clear zaidi. Section 14(b) ya muswada huu; “subject to any other directions which may be given by the Minister the Board may: (b) approve the proposal to borrow money for the purpose of the Corporation.” Limeruhusiwa au litaruhusiwa kuchukua mkopo kwa ajili ya uendeshaji, kwa ajili ya ujenzi wa miundmbinu. Kwa vile mambo haya yote tumeangalia vizuri na kama Serikali, na yako vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kuhusu jina TRC. Kwa nini tuliamua tuite Tanzania Railway Corporation (TRC)? Zamani kulikuwa na TRC na watu wote ambao wanakaa Kanda ya Ziwa walikuwa wanasafiri na Shirika hilo la Reli.
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika hilo lilifanya kazi vizuri sana na kila Mtanzania alikuwa ameona kazi iliyokuwa ikifanywa na TRC. Baadaye katikati hapo tukaunganisha baina ya TRC na kampuni ile ya Wahindi. Bahati mbaya sana ndiyo tukapata TRL, lakini kazi iliyofanywa na TRL ilikuwa mbaya sana, hairidhishi. Kila mtu siku zote aliyekuwa anakumbuka TRC; sisi kama Serikali kwa kuangalia brand name nzuri, tukaona hili shirika letu Watanzania wengi bado wanatamani TRC, tukaamua tuite TRC as brand name. Hii ni brand name, tunafanya marketing. Tunaamini Watanzania wengi leo wakisikia TRC watakupa TRC ya zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya hivyo, tunaamini TRC yetu mpya itaweza kufanya kazi kwa ufanisi na itafanya kazi vizuri zaidi kuliko TRC ya zamani. Kwa vile TRC hii ni mpya kabisa, ina mambo mapya, inakuja na standard gauge, inakuja na treni ambayo itakwenda kwa kilometa 160 kwa saa, Watanzania hawajawahi kuiona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo machache, sasa naomba kutoa hoja.
Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli Tanzania wa Mwaka 2017
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mbele yako na kutoa mchango wangu katika hoja hii.
Mheshimiwa Spika, napenda nikushukuru wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kwa uwezo na umahiri mkubwa mnaoonesha katika kuliendesha Bunge letu Tukufu.
Aidha, napenda kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge waliopata fursa ya kuchangia hoja yangu niliyowasilisha hapa Bungeni leo asubuhi kwa michango mizuri na yenye kina na lengo la kuboresha Sheria hii ya Shirika la Wakala wa Meli wa Taifa ya Mwaka 2007.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na wachangiaji 12 waliochangia kwa kuzungumza na wachangiaji sita (6) waliochangia kwa maandishi. Michango yote ya Waheshimiwa Wabunge ilikuwa ni mizuri sana na iliyosheheni mapendekezo, ushauri na hasa namna bora ya kuendeleza shirika letu hili ambalo tutaliunda hivi karibuni.
Mheshimiwa Spika, ushauri wa Bunge na maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imezingatia na tutaendelea kuifanyia kazi. Vile vile maoni ya Kambi ya Upinzani tumeyapokea na tutayazingatia. Hata hivyo, ningependa nitumie muda wangu mchache kidogo kufafanua baadhi ya hoja zilizotolewa na viongozi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, kwanza kama tunavyojua Bandari ya Dar es Salaam imekuwa ni lango kubwa sana la biashara kwa nchi yetu. Sio tu kwa nchi yetu, isipokuwa hasa pia kwa nchi za Malawi, Zambia, Rwanda, Burundi, Uganda na Mashariki mwa Jamhuri ya Congo. Nchi zote hizi zinaitegemea Bandari ya Dar es Salaam. Kwa mfano; mwaka 2016/2017, hali ya utendaji wa Mamlaka ya Bandari Dar es Salaam imepata mafanikio makubwa kwani kwa kipindi hiko takriban tani milioni 14.6 zimepitia kwenye Bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Tanga na Bandari ya Mtwara.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya mikakati mikubwa kwa ajili ya kuiboresha Bandari ya Dar es Salaam na tunaamini kila mwaka Bandari ya Dar es Salaam itaendelea kuimarika. Kwa muda mrefu sana kumekuwa na changamoto kubwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Changamoto ya kwanza ni udanganyifu wa nyaraka mbalimbali. Nyaraka zinakuja hizi lakini at the end of the day sio nyaraka zenyewe. Pia kumekuwa na upotevu mkubwa wa mizigo hasa makontena.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano mwaka 2015 takriban makontena 600 yalipotea kwenye Bandari ya Dar es Salaam na yamepotea kwa sababu hakuna kumbukumbu sahihi. Kama mnavyokumbuka, Mheshimiwa Rais alitembelea pale
na tukaona udanganyifu mkubwa hasa kwenye makontena ya makinikia. Kwenye documents unasema kuna makontena 200, lakini ukiangalia kuna makontena 500. Hii ndiyo changamoto kubwa ambayo imetufanya leo hii tuje na Muswada huu. Kuna maeneo mawili ambayo ni muhimu sana katika usafirishaji wa mali. Eneo la kwanza ni documents zenyewe na eneo la pili ni uhakiki.
Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano mdogo tu jinsi gani mzigo unavyosafirishwa kutoka kwa mteja mpaka unapoingia melini. Kwa mfano, msafirishaji wa shehena inayotoka yaani shipper or exporter kawaida anawasiliana kwanza na clearing and forwarding agent kumwambia kwamba nina mzigo wangu nataka kusafirisha pengine kwenda Dubai. Anaomba nafasi kwenye meli kupitia kwa wakala wa meli. Wakala wa Meli anatoa nyaraka kuthibitisha nafasi ya kusafirisha shehena kama maelezo yanavyoeleza. Clearing and forwarding agent anajaza fomu hiyo, akishajaza fomu hiyo anaiwasilisha kwa customs ambaye na yeye anajiridhisha kwamba kwenye fomu ile imejazwa mizigo yote.
Mheshimiwa Spika, kabla meli haijaingia bandarini tayari wameshaambiwa kwamba meli fulani itafika siku fulani na nafasi yenu iko sehemu fulani na kabla ya kupakia mzigo kwanza mzigo unatakiwa uhakikiwe kama ni kontena zinatakiwa zifunguliwe, kama ni mizigo mingine inabidi ihakikiwe. Wanaohakiki sasa hivi kwa Bandari ya Dar es Salaam ni watu binafsi, hapo ndiyo shida inaanzia.
Mheshimiwa Spika, watu binafsi wanachukua makontena wanayafungua, wanayahakiki, wanajiridhisha halafu wao ndiyo wanapeleka ripoti TRA, TPA na maeneo mengine. Sasa udanganyifu unaanzia hapo! Wakishamaliza kuhakiki makampuni haya, yanachukua mzigo, unapelekwa melini Kapteni wa Meli anasaini kwamba amepata mzigo huo halafu anatayarisha manifest. Kama tutaweza kuzuia lile eneo la uhakiki, hapo tutahakikisha kwamba mizigo haipotei tena na hii ndiyo kazi kubwa ambayo hili shirika tunalolitengeneza tunataka likahakiki hiyo mizigo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nikitoa maelezo hapa au nikieleza kidogo kuna kampuni saba ambazo zenyewe zinafanya kazi ya uhakiki. Kampuni ya kwanza ni CGS Collateral Control ambayo ni Private Sector; kampuni ya pili ni Mehemba Marines Surveyor and Consultant; kampuni ya tatu ni Rob Marine Pandi Service Limited; kampuni ya nne, Luchi impex Limited; kampuni ya tano ni Tanzania Ships Contractors Limited; kampuni ya sita, Toplass and Handling Tanzania Limited; na kampuni ya saba, Vision Control and Superintendence Limited.
Mheshimiwa Spika kampuni zote hizi zinakuwa na uhusiano wa karibu kwanza na Wakala wa Meli, zinakuwa na uhusiano wa karibu sana na watu wenye meli. Sasa hapa kunakuwa na udanganyifu. Sasa kwa kulitambua hilo, ndiyo sasa Serikali tunataka kabla mizigo haijaingizwa kwenye meli pale NASAC ianze kufanya haki ya uhakiki. Tunaamini tukilisimamia hilo, tatizo la uhakiki wa mizigo litaisha.
Mheshimiwa Spika, mizigo ikija hapa Tanzania tunataka documents zote kwanza zipelekwe kwa NASAC zikishatoka kwa NASAC ndiyo zipelekwe kwa Wakala wa Meli kwa sababu kinachotokea sasa, documents zikija hapa Tanzania, Wakala wa Meli na wengine wanazichakachua na hii imeoneshwa wakati vilipoingia vichwa vya treni. Bill of lading ya mwanzo iliyoleta vichwa vya treni ilionesha Engineer Kisamvu. Baada ya kubanwa wakabadilisha hapa hapa Tanzania ambapo kiutaratibu wa meli jambo hilo halitakiwi kufanyika. Kwa hiyo, hayo ndiyo madhumuni makubwa ya kutaka kuanzisha hii kampuni ya NASAC.
Mheshimiwa Spika, kwa nini kampuni isiitwe authority, kwa nini tunaita NASAC? Kama alivyosema Mwanasheria Mkuu, hapa tutakuwa na kazi mbili; kazi ya kwanza ni ku- regulate, kudhibiti. Kazi ya pili ni kufanya biashara ya uwakala kwenye maeneo maalum.
Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza litakuwa ni kuweka documentation, kufanya talling, halafu vilevile kufanya uwakala kwenye maeneo ya madini, petroli, kwenye silaha, kwenye wanyama na maeneo mengine. Hatutakwenda kwenye maeneo mengine, sasa vifungu hivi kwenye sheria vimewekwa kwa mfano Kifungu cha sita (6), saba (7), 10, 11 na 12 kimeeleza majukumu ya Muswada huu.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, naomba niwatoe wasiwasi wafanyabiashara wengine kwamba, NASAC haitafanya biashara ya uwakala kwa kila eneo. Itafanya hivyo, pale tu itakapotokea mambo matatu, kama alivyosema Mwanasheria Mkuu; jambo la kwanza kama mfanyabiashara huyo atashindwa kufuata masharti ya kanuni za leseni. Jambo la pili kama kampuni hiyo ya uwakala itafilisika then hapo ataingia. Jambo la tatu kama mwenye meli ataitaka NASAC kufanya kazi hiyo, hapo ndio wataanza kujikita kwenye kazi hiyo, lakini kwa msingi kabisa itafanya katika maeneo matatu ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kuna suala ambalo limekuja kwa nini DG tumempa mamlaka makubwa. Tumeweka kifungu ambacho kitasimamia utoaji wa leseni na kwenye kifungu hicho tuna Kamati Maalum ambayo ina watu watatu. Kazi yao ni kumshauri DG kuhakikisha kwamba, anatoa leseni bila upendeleo, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, la pili, kulikuwa na malalamiko vilevile kwamba, Waheshimiwa Wabunge wamesema anaweza kuamua kumtolea ama kufuta leseni wakati wowote. Mimi nina bahati sana, ninasimamia sasa hivi mamlaka tatu; nina TCRA, nina TCAA na SUMATRA na utaratibu wa kufuta leseni uko sawasawa.
Mheshimiwa Spika, ukichukua TCRA kama mtu ameshindwa kutimiza masharti ya leseni Mkurugenzi Mkuu anaanza kumpa notice, akishindwa anampa notice ya pili kumwambia sasa nafuta leseni yako. Hatua ya tatu kama atashindwa kuthibitisha kwa nini leseni yake isifutwe, mambo hayo yanapelekwa kwenye bodi, bodi inatoa kibali cha kufuta. Baada ya bodi kutoa kibali cha kufuta, inakuja kwangu mimi Waziri naifuta leseni hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, toka nimeingia Wizara hii sasa hivi nina miaka saba, nimefuta leseni sita tu. Leseni za TCRA ni leseni ukizifuta inabidi ufikirie siku kumi kumi kwa sababu, masafa yenyewe tu yale ukiyauza yanafika kama dola milioni 10, lakini utaratibu ndio huohuo na tunafanya bila ya kupendelea mtu.
Mheshimiwa Spika, ukija kwa upande wa SUMATRA kuna leseni za aina mbili; kuna leseni ya muda mfupi na leseni ya muda mrefu, yani miaka mitano. Leseni ya muda mfupi inafutwa na DG, definitely kwanza anatoa notice, anamwambia kwa nini tusifute leseni yako, anatoa maelezo, kama hana leseni inafutwa. Leseni ya muda mrefu kwanza DG anatoa notice, halafu inaenda kwenye bodi, kama yule jamaa atashindwa kuonesha kwa nini leseni yake isifutwe, inakuja kwa Waziri na Waziri nafuta na TCAA, utaratibu ni huohuo.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba tu walielewe watu hili kwamba, hili tunalolifanya hivi kwa authorities zote tunafanya hivihivi. Sio kwa sababu hii tu, lakini ukienda TCAA, TCRA na ukija SUMATRA tunafanya hivihivi. Leseni ya TCRA ni leseni ambayo thamani yake ni kubwa zaidi na tunaifuta kwa utaratibu kama huu na mpaka sasa hivi hatujapata malalamiko yoyote.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba tu wadau wote na Waheshimiwa Wabunge waelewe, hizi kazi tulizompa DG, DG atafanya na kuna utaratibu kwamba, ipo bodi ambayo itasimamia mchakato wote. Kama mtu akiona hakuridhika na maamuzi yake anakuja kwa Waziri, kama hakuridhika na maamuzi ya Waziri anakwenda Mahakama Kuu. Iko very clear kwenye sheria na tutaisimamia hiyo.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ambayo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wameleta, pia na Kamati yetu imeleta, kwa nini tusiende FCC – Fair Competition Commission? Nina bahati kama nilivyosema nasimamia mamlaka tatu na mamlaka mbili zinakwenda FCC, lakini hivi ninavyoongea FCC kuna kesi nyingi. Tumepeleka sisi kesi toka
mwezi Mei mwaka huu, tuna kesi pale ya DSTV, kuna kesi ya Star TV na kesi nyingine nyingi tu, zinachukua muda mrefu, kwa sababu, tatizo lililoko pale kwa kipindi kirefu kulikuwa hakuna Makamishna wa kutosha. Sasa ninavyoamini rufaa kwa Waziri inaweza kuchukua muda mfupi zaidi kuliko kwenda FCC na kwa kuliona hilo ndio tukafanya hivi.
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kuwahakikishia wadau wote wa sekta ya usafiri wa majini kwamba, utaratibu huu ni wa haraka zaidi kuliko wa FCC. FCC wanaweza kuchukua hata mwaka mmoja kesi haijahukumiwa. Kwa hiyo, naomba tu watuamini kwamba, tutalisimamia vizuri na halina utata wowote.
Mheshimiwa Spika, kuna suala kwa nini hamuoni Serikali kutenganisha masuala ya udhibiti na masuala ya biashara? Kama nilivyosema sekta ya usafiri majini bado hatujaitendea haki. Miaka yote ilikuwa chini ya SUMATRA wakati SUMATRA yenyewe ina mambo mengi sana, kwa hiyo, sasa tukaona kuitendea haki sekta hii ambayo ni kubwa kuanzia usafiri wa baharini mpaka usafiri kwenye maziwa, tuweke mdhibiti ambaye atakuwa chini ya NASAC mwenyewe ndio NASAC afanye kazi hiyo. Hilo ya kwanza.
Mheshimiwa Spika, la pili, tukisema kwamba, tutengeneze agency, hiyo agency itakuwa haina kazi kwa sababu, makinikia hayatokei kila siku, mwaka mmoja yanaweza kutokea makinikia miezi mitatu. Je, tutaajiri watu 60 hapa wamekaa na hawana kazi yoyote? Nafikiri hili halitakuwa jambo zuri na hatutaifanyia haki nchi yetu. Bado naendelea kusema hii kama tutaisimamia itafanya kazi vizuri. Kuna maeneo mengi na watu wengi wanafanya hivyo na inafanya kazi vizuri, kitu muhimu hapa ni kusimamia na kila mtu ajue wajibu wake ni nini na tunafanya nini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nikuhakikishie na tuwatoe wasiwasi wadau wetu kwamba, hapa hakutakuwa na ubabaishaji. Tukisema tuendelee kama watu wengine wamesema tutengeneze agency; ukitengeneza agency, kama nilivyosema una makinikia, una mafuta yanakuja mwaka mara tano, halafu una wanyama pengine hawasafirishwi hata siku moja ama kuna silaha, pengine inakuja miaka miwili mara moja, ukitengeneza agency kwa muda wote huo, nafikiri tutakuwa hatuifanyii haki nchi yetu na tutapoteza pesa nyingi. Naamini na bado naendelea kuamini mfumo huu utatufikisha pazuri.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja kwa nini SUMATRA hasimamii jambo hili? SUMATRA sasa hivi anafanya kazi mbili; kwanza anasimamia udhibiti njia ya majini, halafu anasimamia udhibiti kwenye nchi kavu, yaani barabara, lakini ukiangalia nchi yetu hii ya Tanzania, asilimia kubwa kabisa ya Watanzania wanatumia usafiri wa barabarani na usafiri wa reli. Kwa hiyo, sehemu kubwa ya SUMATRA au kazi kubwa ya SUMATRA inajikita zaidi kwenye usimamizi wa nchi kavu, kwa kiwango kidogo kabisa wanajikita kwenye sehemu ya usafiri wa majini. Sasa ndiyo utaona mambo ya udhibiti kwenye usafiri wa majini hayaendi vizuri.
Mheshimiwa Spika, vilevile Sheria iliyopo sasa hivi ya SUMATRA haiipi nguvu ya kuchukua documents pamoja na kufanya uhakiki. Ndio sababu kubwa SUMATRA imeshindwa kusimamia hasa kwenye ubadhirifu, hasa kwenye upotevu wa nyaraka bandarini. Baada ya kuona changamoto hizi tukaona sasa iko haja ya kuanzisha NASAC ambayo itasimamia shughuli hizi kwa pamoja. Kwanza itasimamia shughuli ya udhibiti halafu itasimamia shughuli ya uwakala wa madini, hasa kwenye maeneo yale nyeti ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile nchi zote ambazo zina bahari, ukienda Kenya, South Africa, Singapore, wenzetu wana mdhibiti ambaye anasimamia usafiri wa baharini kama tunavyoanzisha sisi NASAC, lakini hapa petu tu SUMATRA ndio anasimamia sehemu zote mbili, ambapo nafikiri hatutendi haki. Hata ukienda Kenya leo kuna mtu anasimamia usafiri wa nchi kavu na kuna mtu anasimamia usafiri wa baharini. Sasa na sisi tukaona tuiondoe sehemu ile tuipeleke kwenye NASAC ili mambo yaende vizuri.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja kwa nini NASACO ilifeli? Mheshimiwa Naibu Waziri alizungumza sana. NASACO ilianzishwa mwaka 1973, jukumu kubwa lilikuwa ni kufanya biashara ya wakala wa meli, lakini wakati huo kulikuwa na monopoly kubwa kwa NASACO na baadhi ya watoa huduma wa meli au wenye meli walianza kulalamika kwamba, NASACO ina monopoly kubwa, pia NASACO inatoa siri zao kwa makampuni mengine. Sasa Serikali ikaona ifanye utafiti wa kina kuangalia jinsi gani tunaweza kuiboresha NASACO.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilichokifanya mwaka 1998 NASACO iligawika kwenye kampuni nne; Kampuni ya kwanza ni Azania Shipping Agency Company Limited; Kampuni ya pili ni Victoria Shipping Agency Company Limited; Kampuni ya tatu ni Worldwide Shipping Agency Company Limited; na Kampuni ya nne ni Oceania Shipping Company Limited. Hiyo ilikuwa hatua ya kwanza.
Mheshimiwa Spika, hatua ya pili Serikali ilisema baada ya hapo itabidi sasa Watanzania wanunue hisa za makampuni haya na walitakiwa Watanzania wanunue hisa 25, wamiliki wa meli wawe na hisa 35 na Serikali iwe na hisa 40, lakini hili halikufanyika. Badala yake ilifanyika hatua ambayo ndiyo imesababisha matatizo haya, walitoa leseni kwa makampuni ya meli kufanya kazi ya uwakala wa meli na hapo ndio tatizo likaanza. Baada ya hapo kila mwenye kampuni ya meli alianzisha wakala wake wa meli, matokeo yake NASACO ikafilisika. NASACO ilifilisika kwa njama, kwanza haukuwekwa utaratibu, mzuri matokeo yake watu wajanja wajanja wakachukua fursa hiyo, NASACO ndio ikaambiwa bye-bye.
Mheshimiwa Spika, sasa sisi tunaloanzisha hatuendi kufanya uwakala kwenye baadhi ya maeneo kwa vile hatuendi kushindana na makampuni ya uwakala mengine. Sisi tutasimamia eneo moja tu kwenye mambo ya uwakala, kuangalia madini na kuangalia nyaraka na uhakiki, ndio hayo tu. Vilevile tutasimamia mambo ya udhibiti kwa vile sioni sababu ya msingi kwa nini Watanzania na wadau wengine wawe na wasiwasi kuhusu NASAC. Naamini NASAC itafanya kazi vizuri na itaendelea vizuri.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo machache sasa, naomba niende nikajikite kwenye hoja mojamoja za Waheshimiwa, nikianzia kwanza na Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu. Kuna hoja ya kwanza kutenganisha udhibiti na biashara kwa nia ya kuondoa mgongano wa kimaslahi na kuimarisha ushindani wa haki.
Mheshimiwa Spika, kwa utaratibu tuliouweka na kwa sheria hii hakutakuwa na mgongano wowote. Kama nilivyosema kwenye maelezo yangu, kama kutakuwa na mgongano kuna hatua mbalimbali zinatakiwa mdau anaweza ku-appeal. Kwanza anaanza kwa Waziri, kama hakuridhika kwa Waziri then anakwenda Mahakama Kuu. Kwa hiyo, naomba tu niwahakikishie kwamba, hapa hakuna mgongano wowote na tumeweka Kifungu Namba 10(2) ambacho kitasimamia jambo hili.
Mheshimiwa Spika, kuna hoja nyingine, kufuta Kifungu cha (2) ambacho kilikuwa kinataka sheria hii itumike Zanzibar:-
Mheshimiwa Spika, kama tulivyosema asubuhi hii kwamba, kifungu hiki kimefutwa. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Balozi kwa uongozi wao makini ambao umetuwezesha kutatua tatizo hili kwa maslahi ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kuna jina. Kwa nini jina la Muswada libadilike, ili kuwa na neno Maritime Authority. Kama nilivyosema Serikali yetu ni sikivu na tumelisikia, lakini mimi kwa kuanzia kwa sababu, shirika hili litafanya kazi mbili; kazi ya kwanza itakuwa ni uwakala kwa maeneo maalum na kazi ya pili kwa udhibiti, naomba sana Bunge lako Tukufu na Waheshimiwa Wabunge kwanza twende hivi, kama itaonekana huko mbele iko haja, Sheria sio msahafu wala sio Biblia, tunaweza tukabadilisha wakati wowote, lakini bado nawaomba Waheshimiwa Wabunge twende katika mtazamo huu.
Mheshimiwa Spika, kuna hoja, masharti nya leseni yalegezwe ili kuruhusu wenye meli kupewa leseni za uwakala. Tatizo kubwa tunalolipata ni kwa sababu, tuliwapa wamiliki wa meli, kama tutalegeza masharti itakuwa hatujatatua tatizo. Naomba Waheshimiwa Wabunge mwelewe kwamba, tunatengeneza Muswada huu au sheria hii kwa maslahi ya nchi yetu. Kwa hiyo, naomba tuendelee na utaratibu kama kawaida.
Mheshimiwa Spika, kuna hoja inasema Muswada uainishe masharti na utaratibu wa utoaji leseni na udhibiti wa wakala wa meli. Hii imefanyika na hili liko kwenye sheria.
Mheshimiwa Spika, kuna hoja inasema ushiriki wa Watanzania katika biashara ya wakala wa meli iainishwe katika Muswada. Hii tumefanya hivyo na tumeweka asilimia 60 sasa kwa Watanzania. Kampuni yoyote itakayokuja Tanzania ambayo itafanya kazi ya uwakala lazima iwe na asilimia 60 ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika, kuna hoja ya rufaa dhidi ya maamuzi ya shirika zifuate utaratibu wa Tume ya Ushindani. Ni jambo zuri, lakini kama nilivyosema kwenye Tume kunachukua muda mrefu na hatutawatendea haki Watanzania ambao wana malalamiko. Kwa utaratibu tuliouweka naamini matatizo yao yataamuliwa kwa muda mfupi sana.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasema jina haliakisi maudhui ya Muswada. Naamini kama tutasoma kwa kina maudhui ya Muswada huu utaona jina hili ni jina halisi kwa ajili ya Muswada huu.
Mheshimiwa Spika, kuna Wabunge ambao wamechangia mmoja mmoja; kuna Mheshimiwa Omary Mgumba ambaye yeye ametoa pongezi kwa Serikali kwa ajili ya Muswada wa Sheria kuanzisha NASAC. Pongezi zimepokelewa.
Mheshimiwa Spika, pia kuna hoja ya kwamba kazi ya udhibiti na mtoa huduma zitenganishwe kwa nia ya kuondoa mgongano wa kimaslahi na kuimarisha ushindani wa haki. Kama nilivyosema kwa sasa hivi kama tutatenganisha, hili halitaleta maslahi mapana kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kuna Mheshimiwa Mbunge Janeth Massaburi, yeye ameunga mkono hoja na kuainisha kwamba, Serikali yoyote makini duniani haiwezi kuacha lango kuu la uchumi bila kuweka mkono wake kwa ukaribu. Tumekubaliana na yeye na maoni yamechukuliwa.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rukia ameipongeza Serikali kwa muswada huu. Pongezi zimepokelewa.
Mheshimiwa Spika, halafu amekwenda hoja ya pili, kwa nini NASACO ilikufa na NASAC itasaidiaje? Kama nilivyosema niliweka sababu za msingi kwa nini NASACO ilikufa, basically kwa sababu ya makampuni ya meli yalianzisha kampuni zao na ikawa hakuna kazi inayokwenda kwa NASACO na ndio bila shaka NASACO ilifariki, lakini sasa hivi haitakuwa hivyo, kwa sababu hatuendi kushindana na wao. Sisi tunafanya udhibiti na vilevile tunafanya shughuli maalum ya uwakala katika eneo maalum, kwa hiyo, hakuna sababu kwa nini NASAC iweze kufa.
Mheshimiwa Spika, kuna Mheshimiwa Emmanuel Mwakasaka ambaye ameipongeza Serikali kwa Muswada na kuunga mkono hoja. Pongezi zimepokelewa.
Mheshimiwa Spika, kuna hoja nyingine inasema Serikali iwe inatoa muda wa kutosha kwa Kamati kupitia Muswada. Hili tumelipokea na tutalifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo machache sasa naomba kutoa hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote
na mimi napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu na naunga mkono hoja kwa
asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitajielekeza kwanza kwenye Reli ya Kati. Kama
tunavyojua reli hii ya kati imejengwa mwaka 1905 na imechoka sana kwa sasa; na ina uwezo a
kuchukua tani milioni tano tu; na kutoka Da r es Salaam kwa mfano kwenda mwanza
unachukua takribani masaa 30. Serikali ya Awamu ya Tano chini ya kiongozi wetu Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli aliamua sasa tujenge reli ya kisasa, reli ambayo itakuwa na uwezo wa
kuchukua mizigo tani milioni 17. Pia itakuwa na uwezo wa kukimbia kwa speed ya kilometa 160
kwa saa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ina maana kuwa kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro
tutatumia saa moja na dakika kumi na sita, kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma tutatumia
masaa mawili na nusu na kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza tutatumia masaa saba na
nusu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Afrika kuna nchi tatu zilizojenga standard gauge, ya
kwanza Kenya, Ethiopia na Nigeria; lakini zote hizo treni zake zinakwenda speed ya 120 si 160
kama Tanzania. Na katika nchi hizo ni Ethiopia tu ndiyo inatumia umeme na sisi Tanzania. Katika
Bara la Afrika ni treni moja tu sasa hivi inayokwenda kilometa 160 ambayo ni Gautrain, ni ile
iliyopo pale Johannesburg na ile ni treni ya mjini inakwenda kilometa 80 tu; lakini ya Tanzania
itakwenda kilometa takribani 1,600. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mlivyosikia tarehe tatu tulisaini mkataba kati ya RAHCO
kwa niaba ya Serikali na kampuni ya Kituruki ambayo tunaita Yapi Merkezi na Kampuni ya Mota-
Engil ya huko Ureno kwa gharama ya dola za Kimarekani bilioni 1.2 sawa na kila kilometa moja
tutajenga kwa dola za Kimarekani milioni nne, hiyo ni pamoja na VAT. Ukiondoa ushuru kwa kila
kilometa moja tutajenga kwa dola milioni 3.4.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba niwachukue Waheshimiwa Wabunge kwa
wenzetu majirani. Kenya wanajenga reli yenye urefu wa kilometa 605, wao wanatumia dola za
Kimarekani bilioni 3.1 sawa na kwa kila kilometa dola za Kimarekani milioni 5.3 wakati Tanzania
tunatumia dola za Kimarekani milioni 4. Ethiopia na wao wanajenga treni kama hii, wao
wanatumia kwa kila kilometa moja dola za Kimarekani milioni 4.5. Kwa hiyo, Tanzania tumeweza
kufanya wajibu wetu vizuri na tumepata kwa bei nzuri kuliko wenzetu wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kukawia kwingine ni kuzuri sana, unaweza kuwahi mwisho
wake ukaenda ukaangukia pabaya. Tunaamini Tanzania na timu yetu iliyofanya kazi hii ilifanya kwa uadilifu mkubwa na tumepata good deal tunasema. Na kazi hii ya ujenzi itaanza mwisho
wa mwezi Machi na itachukua takribani miezi 30. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo huo tumetangaza tender kwa ajili ya Morogoro -
Makutupora; tumetangaza tender nyingine kwa ajili ya Makutupora hadi Tabora, kutoka Tabora
hadi Isaka na tender ya mwisho kutoka Isaka hadi Mwanza. Nia yetu ni kuwapata wakandarasi
mbalimbali ili kazi hii iende haraka na Tabora - Kigoma inakuja. Lakini kama kazi hii tutampa
mkandarasi mmoja anaweza kuchukua hata miaka minne ama mitano. Kwa vile Serikali
tumefanya uamuzi sahihi kwa watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijikite haraka haraka kwenye Mamlaka ya
Bandari. Ni kweli Mamlaka ya Bandari katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha mizigo
ilipungua wala hakuna mjadala kuhusu hilo. Lakini kuanzia mwezi Oktoba, Novemba na
Disemba meli ziliongezeka na mzigo ulianza kuimarika. Ni kweli sasa hali ya bandari inaendelea
vizuri kuhusu mizigo na tunategemea hali hiyo itaendelea vizuri kila tunapoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa ujenzi wa miundombinu, tayari tumemepata
mkandarasi kwa ajili ya ujenzi au ukarabati wa Bandari ya Dar es Salaam gati namba moja
mpaka namba saba; na tunategemea baada ya mwezi mmoja na nusu kazi ya ujenzi itaanza.
World Bank wanataka kutoa pesa, lakini kama watachelewa tayari tumejipanga, tunazo pesa
bandari na tutaanza kufanya kazi hiyo mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Bandari ya Mtwara tayari vile vile
tumeshampata mkandarasi na sasa hivi tunaanza kujipanga ili kazi ianze. Tumepeleka
document Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kwa ajili ya vetting na tunafanya due diligence ya
mkandarasi huyo ili aweze kuanza kazi mara moja na gharama kwa ajili ya ujenzi wa gati hiyo
italipwa na Mamlaka ya Bandari kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu flow meter. Tulitangaza tender lakini kwa bahati
mbaya sana tulipata wakandarasi wawili lakini wote hawakukidhi vigezo, kwa hiyo, tukaamua
tuanze mchakato upya na mchakato unaendelea vizuri kama alivyosema Mwenyekiti wa
Kamati yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa scanner bandarini tayari tumetoa order ya
scanner kama tano kwa ajili ya kuimarisha ulinzi kwenye bandari zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita kidogo kwenye shirika la ndege. Kama mnavyojua
shirika letu la ndege linaimarika vizuri na Wabunge wengi sasa mmefaidi matunda ya
Bombardier Q400, si kibajaji tena, sasa zimekuwa ndege. Serikali tunaamini tunaendelea
kujipanga kuleta ndege nyingine mpya nne ambayo Bombardier moja itakuja mwezi wa tano;
C series ambayo ni jet engine itakuja mwakani; kila moja itakuwa na uwezo wa kubeba abiria
150. Mwakani vile tutaleta ndege nyingine Boeing Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria
262. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mpango wa kuibadilisha au ku-trade in ndege yetu
Bombardier Q300 ile ambayo ni mzee tuweze kupata ndege mpya Bombardier
Q400. Itakapofika mwisho wa mwaka 2018 shirika la ndege la Air Tanzania litakuwa na ndege
saba mpya. (Makofi)
Katika kuboresha utendaji kazi na utoaji huduma wa Air Tanzania wamenunua progamu
mpya sasa kwa ajili ya kufanya reservation na booking kwa wateja wake. Sasa wateja wote wa Air Tanzania wanaweza ku-book kupitia kwenye computer au hata kwenye smartphone.
Tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba tunatoa huduma iliyotukuka. (Makofi)
(Hapa kengele ya kwanza ililia)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu marubani tunajipanga tulete marubani na kila sehemu
ya Tanzania tunataka kuhakikisha kwamba Bombardier Q400 inatua. Mheshimiwa Hawa Ghasia
tumekusikia na tutakuletea ndege hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge
tumesikia malalamiko yao kuhusu barabara, Serikali ya Awamu ya Tano tumejipanga sana na
tunataka kuibadilisha nchi yetu kupitia miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa kuhusu sekta ya mawasiliano; tumebadilisha
kanuni za Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kuhakikisha kwamba tunapeleka huduma ya
mawasiliano kila eneo la Tanzania hasa yale maeneo ya mpakani ambayo hayana mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wa kuhusu TAZARA umepokelewa na mwisho kabisa kama nilivyoanza mwanzo ninaomba kuunga mkono hoja hii asilimia mia moja, ahsanteni sana.
Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania wa Mwaka 2017
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia kukutana hapa tukiwa na afya njema.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza nikushukuru wewe mwenyewe binafsi na Wenyeviti wote wa Bunge kwa uwezo na umahiri mkubwa mnaoonesha katika kuliendesha Bunge letu Tukufu. Aidha, napenda kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliopata fursa ya kuchangia hoja yangu niliyowasilisha hapa Bungeni leo asubuhi na wametoa michango mizuri sana ambayo tumeichukua na tumeifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Waheshimiwa Wabunge 14 waliochangia katika Muswada huu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania wa Mwaka 2017 (The Tanzania Telecommunications Corporation Bill, 2017). Michango ya Waheshimiwa Wabunge wote ilikuwa ni mizuri sana na ilisheheni mapendekezo, ushauri na hasa namna bora ya kuendeleza Shirika la Mawasiliano Tanzania ili liweze kuchangia zaidi katika maendeleo ya Watanzania wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri na maoni ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu yamezingatiwa. Vilevile maoni na ushauri kutoka Kambi Rasmi ya Upinzani utazingatiwa. Hata hivyo, ningependa nitumie muda wangu mfupi sana kujibu baadhi ya hoja zilizowasilishwa mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nia ya Serikali yetu ni kuweka mikakati mizuri ya kuliimarisha Shirika la Simu Tanzania (TTCL) ili nalo liweze kuleta ushindani mkubwa kwenye soko la mawasiliano. Kuna baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamelalamika sana kwa nini tunafanya corporation au ushirika, hili sio jambo geni, kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyosema, nchi mbalimbali duniani zina utaratibu huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri ambao nyote mnauona ni wa Viettel ya Vietnam. Hii ni kampuni ya Serikali, na si tu kampuni ya Serikali, ni kampuni ya jeshi na inafanya kazi kubwa na hapa Tanzania kwa muda mfupi tumeona wana takribani subscribers au wateja milioni 3.5. Ukienda China, China Telecom ni kampuni ya Serikali na ni kampuni ambayo inakuwa kwa kasi kubwa duniani, China Mobile ni kampuni ya Serikali ambayo inafanya kazi vizuri sana. Ukienda Singapore kuna Singtel, ni kampuni ya Serikali inafanya vizuri sana. Naweza kutaja kampuni nyingi za mawasiliano za simu za Serikali ambazo zinafanya vizuri; jambo muhimu ni usimamizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu, Serikali yetu na Serikali ya Awamu ya Tano, Awamu ya Nne, tumefanya kazi kubwa sana kuimarisha Shirika la Simu la Tanzania. Kuanzia mwaka 2009 Serikali ilikabidhi Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa Shirika la Simu la TTCL. Mkongo ule unagharimu takribani Dola za Kimarekani milioni mia mbili na wamekabidhiwa TTCL na TTCL inautumia na inauza huduma hizo za mkongo kwa kampuni zote Tanzania. Kwa ufupi, kampuni zote za Tanzania zinazonunua huduma ya mkongo kutoka Kampuni ya TTCL zimeridhika sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2014, Serikali iliipa Kampuni ya TTCL masafa ya megahertz 1,800 kwa ajili ya kupeleka huduma ya simu za mkononi na TTCL sasa hivi imeanza kufanya kazi hiyo. Mwaka 2014 kampuni ya Serikali iliipa Kampuni ya TTCL bandwidth ya Serikali kwa ajili ya taasisi mbalimbali za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015, Serikali ilifuta deni la TTCL takribani bilioni 25 ambazo ilikuwa ikidaiwa na TCRA. Mwaka 2015 tena Serikali ilifuta deni la TTCL takribani bilioni 76, hii yote tunaifanya TTCL iweze kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha Kampuni ya TTCL mwaka 2016, Serikali iliipa TTCL data center ambayo leo hii ina wateja 28. Kati ya wateja hao, wateja 19 ni taasisi za Serikali na tisa ni kutoka Sekta Binafsi. Mwaka 2016, katika kuiimarisha TTCL Serikali ilinunua shares za Bharti Airtel kwa shilingi takribani bilioni 14.7 ili kuifanya TTCL kuwa kampuni ya Serikali kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2017, ili TTCL iweze kuendelea na huduma ya 4G, Serikali tumeipa Kampuni ya TTCL masafa ya megahertz 800; ni kampuni pekee sasa hivi tuliyoipa masafa hayo ambayo inaweza kutoa huduma bora za 4G. Mwaka 2017, TTCL ilianzisha Kampuni ya TTCL Pesa ambayo iko chini ya TTCL wenyewe na leo hii tunatayarisha sheria hii ili kuiwezesha zaidi Kampuni yetu ya TTCL.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ufupi, katika huduma za data hapa Tanzania, kampuni bora ya huduma hizo ni TTCL. Huwezi ukailinganisha na Vodacom, Airtel, Tigo wala Halotel kwenye huduma ya data. Kwa hiyo kama tutaipitisha sheria hii na kuiwezesha TTCL tunaamini kwamba itakuwa kampuni kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto nne muhimu ambazo zimetufanya tuweze kutengeneza sheria hii. Changamoto ya kwanza kabisa ni ukuaji wa Sekta ya Mawasiliano. Sekta hii inakua kila siku na ni muhimu kuiwezesha kampuni yako ili iweze kushindana. Kwa hiyo, tumeona tuitengeneze sheria hii ili kampuni ya TTCL iweze kushindana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya pili ya msingi, miundombinu ya TTCL sasa hivi imezeeka, kwa hiyo iko haja ya kuwezesha TTCL ili iweze kuendana na huduma za mawasiliano na ushindani kwa kuwekeza kwenye mitambo
mipya. Sababu ya tatu ya msingi, Watanzania wengi wako vijijini na kwenye vijiji vyetu kuna changamoto kubwa ya mawasiliano. Kwa kuiwezesha Kampuni yetu ya Mawasiliano tunaamini sasa vijiji vingi vya Tanzania vitapata huduma ya mawasiliano ambayo ni bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Waheshimiwa Wabunge wengi walivyosema, suala la usalama halina mjadala. TTCL kiusalama ni kampuni moja nzuri. Kwa kuwafahamisha tu; wakati Rais wa Marekani alipotembelea Tanzania, kampuni ambayo alitumia kwenye huduma za mawasiliano ni TTCL, hakwenda kutumia Vodacom, Airtel wala nini, mawasiliano yote yaliunganishwa kwenye mtandao wa TTCL kwa vile TTCL ni kampuni muhimu na ipo haja ya kuiimarisha kwenye mambo ya kiusalama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na Mbunge mmoja, Mheshimiwa Saada, alizungumzia kuhusu utaratibu wa utendaji kazi wa TTCL. Naomba nimfahamishe tu; TTCL inafanya kazi kiutaratibu wa ukanda. Kuna kanda ya kwanza tunaita Kanda ya Dar es Salaam, kuna Kanda ya Pwani ambayo yenyewe inachukua Zanzibar, Pemba, Mtwara na Lindi; kuna Kanda ya Kaskazini, kuna Kanda ya Ziwa na kuna Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, Kanda ya Pwani inachukua Zanzibar, Pemba, Mtwara na Lindi na utaratibu wa ajira wa TTCL Mtanzania yeyote anafanya kazi kwenye TTCL. Tunachoangalia sisi muhimu ni uwezo wa mtu na sifa za mtu. Ni jambo ambalo limenishtua sana na sikutegemea Mheshimiwa Saada angesema vile, kwamba anataka TTCL Zanzibar ifanywe na Wazanzibari wenyewe tu, hicho kitu sikutegemea, hasa kutoka kwa kiongozi kama Mheshimiwa Saada ambaye amekuwepo Serikalini; hasa kutoka kwa kiongozi kama Mheshimiwa Saada ambaye ana uzoefu mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitegemea Mheshimiwa Saada asilete mawazo na maoni kama hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitegemea mawazo au maoni kama yale wazungumze watu wa kijijini kule Pemba, nilitegemea mawazo kama yale wazungumze watu wa vijiweni pale Darajani, sikutegemea kabisa. Nilitegemea yeye kama kiongozi na sisi kama Watanzania katika kujenga umoja wetu tuseme kila Mtanzania aweze kufanya mahali popote pa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tunavyoongea leo Meneja wa TTCL Zanzibar ni Mzanzibari anaitwa Mohamed Mohamed, Meneja wa TTCL Pemba ni Mzanzibari, anaitwa Ngwali Hamis. Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Saada, hazijui kiutendaji; Mtendaji Mkuu wa TTCL mwaka 2010 mpaka 2012 alikuwa Engineer Said Ameir ambaye mimi ni mwalimu wangu, ni Mzanzibari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sikutegemea; nasema tena, ni kitu ambacho kimeniuma sana, hasa kwa mimi kwa sababu haya mambo siyajui; nilitegemea kama Mtanzania unatoka Lindi kama kuna fursa Zanzibar kwenye TTCL uende, kama Mzanzibari anatoka Zanzibar kuna fursa Kibondo ama wapi, anywhere, aende; hii ndiyo Tanzania tunayoitaka, hii ndiyo Tanzania Watanzania kule nje wanayoitaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda zaidi; tuna TTCL Pesa, ina watendaji watano, senior management positions kuna Watanzania watano, watatu ni Wazanzibari. Mkuu wa Head of Compliance anaitwa ndugu Lulu, ni kutoka Zanzibar, bwana Hamis Rashid anatoka Zanzibar, ni mkuu pale, ndugu Nasra Mulher, pengine ni ndugu yetu, anatoka Zanzibar. Sasa leo tunapeleka message kwamba hawa wote tuwatoe tuwapeleke Zanzibar ama Pemba, sio sahihi, hatuwatendei haki Watanzania. Sisi viongozi tuoneshe mfano, hasa sisi tuliopo Serikalini na wengine waliokaa Serikalini, wanajua utaratibu; Watanzania wote ni wamoja, lazima tujenge umoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Saada, Serikali ya SMZ itam-support kiongozi yeyote ambaye anafanya kazi TTCL Zanzibar au Tanzania nzima, haitambagua Mtanzania yeyote; naomba alifahamu hilo na Waheshimiwa Wabunge wote naomba mlijue hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi walizungumzia suala la kuchagua Wajumbe wa Bodi kutoka mmoja kuwa wawili; mwezi wa Tisa sisi tulikwenda Zanzibar, kama kawaida yetu ikiwa jambo la Muungano tunashauriana na wenzetu wa Zanzibar na wenzetu, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikasema kwamba tuongeze Mjumbe mwingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kujua umuhimu wetu na kwa kujua ushirikiano baina ya Serikali hizo mbili, tulilipokea na tumeleta mabadiliko kwenye Muswada huu, Wajumbe kutoka Zanzibar sasa watakuwa wawili. Naomba niwahakikishie Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar maoni mtakayotupatia wakati wowote tutayachukua, si kwa Muswada huu tu lakini Miswada yote inayohusu mambo ya Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na issue ya uzoefu wa Mtendaji Mkuu. Sisi tumependekeza kwenye Muswada tuweke miaka minane na miaka minane ni sahihi kwa Mtendaji Mkuu wa shirika kama lile. Huwezi kumchukua mtu wa mwaka mmoja ukaenda kumjaribu. Ntawapa mifano; Mtendaji Mkuu wa Vodacom, Ian Forare, ana umri wa miaka 34 lakini ana experience ya miaka zaidi ya 12 ya senior management. Mtendaji Mkuu wa Airtel ni kijana mdogo, ana miaka 40, lakini ana zaidi ya miaka kumi ya experience kwenye senior management.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi tu kufanya mtu wa miaka miwili au mwaka mmoja tumpeleke, si sahihi, lazima tuweke utaratibu wa kisheria ambao tunaweka muda wa kutosha (experience). Tusichanganye hapa baina ya CEO na entrepreneur, ni vitu tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, entrepreneurs au mjasiriamali anaweza kuvumbua pengine akatengeneza software yeye ni mvumbuaji anaweza kutengeneza pesa nyingi lakini kiutendaji kama Kampuni hawezi kufanya. Lazima kwenye suala la Kampuni tuheshimu uzoefu kwa vile sisi Serikali tumeona hili ni jambo sahihi na tutaendelea nalo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine ambao nyote mnajua, mtendaji mkuu wa National housing, Mchechu yeye ni CEO mzuri sana na ana uzoefu mkubwa wa zaidi ya miaka 10 ya senior management position. Mwaka 2002 alikuwa ni director kwenye Benki ya Standard Bank, ana uzoefu mkubwa. Sasa hatuwezi kujaribu kuchukua tu mtu wa mwaka mmoja, miaka miwili tukampeleka kwenye position ile. (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge, naomba hii nafasi ni kubwa tusicheze na makampuni yetu. Kama tunataka makampuni haya yasimame lazima tuweke watu wenye uzoefu. Tunaweza kupata kijana tofauti ambaye ana uzoefu mdogo tukamweka lakini tuweke utaratibu. Nakutolea mfano mzuri wa Ian, Ian miaka 34 ana uzoefu wa miaka 12, CEO wa Vodacom. Si kwamba mtu akiwa kijana mdogo hana uzoefu mnakosea, kwa hiyo naomba muelewe pale sisi tumeweka huo umri kwa sababu tunaamini tukiweka mtu mwenye umri huo atasimamia Shirika letu vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la mkongo, kuna mkongo wa Zanzibar na mkongo wa Taifa. TTCL wanasimamia mkono wa Taifa ambao wenyewe una kilometa 7,560, umeunganisha mikoa yote ya Tanzania, tumewapa TTCL ndio wanaosimamia hili. TTCL tumewapa vile vile kuendesha data center; lakini mkongo za Zanzibar unasimamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wenyewe ni kilometa nafikiri 400 tu kwa vile iko huko Zanzibar na inafanya kazi Zanzibar na hatuna mpango wa kwenda kuuchukua, kwa hiyo naomba mlijue. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mkongo tena unazungumzwa, mkongo wa Halotel; Halotel imejenga mkongo takribani kilometa 18,000. Kila unapopita Mkongo ule zimeweka pair sita kwa ajili ya matumizi ya Serikali. Mkongo wa Halotel haushindani na mkongo wa Taifa. wamekwenda kwenye Wilaya, na condition ama sharti ambalo tuliwapa Halotel katika kuweka mkongo lazima wasishindane na mkongo wa Taifa, na ndivyo hivyo tulivyo. Kwa hiyo, naomba tu niwahakikishie Watanzania na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba Serikali inasimamia miundombinu yote ya mawasiliano hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa njikite kwenye hoja kwa haraka haraka. Kwanza kuna hoja ya Kamati ambapo Kamati inasema Shirika linaloanzishwa liondokane na mfumo wa utendaji wa urasimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge na Watanzania nataka niwahakikishie kwamba Shirika hili tunalolianzisha sasa litakuwa ni Shirika la mfano. Tutalisimamia kwa nguvu zetu zote ili kuhakikisha kwamba linafanya kazi ile ambayo ilikusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la Mtendaji Mkuu nimeshalizungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja, ili Shirika liweze kufanya vizuri, Bodi na Mtendaji Mkuu wa Shirika wapewe madaraka kamili. Taasisi zote za Serikali, Bodi pamoja na watendaji tunawapa mamlaka kamili na wasipotekeleza mamlaka hayo tuwafukuza. Kwa hiyo, naomba waelewe Watanzania ama watendaji wenyewe waelewe, tunawapa madaraka kamili na wanafanya hivyo na pale wanapoharibu tunawaambia the door is open bye bye.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati imeendelea na kusema kuna kipengele namba 7(7) kuhusu Waziri ku-consult Mwenyekiti. Hili tumelichukua na tumelifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwa haraka haraka kwenye hoja za Mbunge mmoja mmoja. Kuna hoja ya Mheshimiwa Zuberi, anauliza kwa nini Serikali ilibinafsisha Kampuni na sasa tumeamua kuirejesha? Ni kweli Serikali iliamua kuibinafsisha kampuni kwa kuzingatia sera zilizokuwepo wakati huo na tumeona sasa sera hizo haziwezi kuleta tija kwa Shirika, kwa sababu hii tumeamua kubadilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hija nyingine ya Mheshimiwa Zuberi anasema, namna gani Serikali imejipanga ili Shirika liweze kushiriki katika ushindani kwa maslahi ya Taifa? Majibu ya hoja hiyo ni kama ifuatavyo. Serikali imejipanga kwa kutayarisha Mpango wa Biashara wa miaka mitano wenye lengo la kuboresha utendaji kazi wa Shirika la Simu la TTCL ili iweze kushindana. Baada ya mpango huo tutakuwa tunafuatilia kila baada ya muda ili kuona kwamba mpango huo unakwenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja nyingine ya Mheshimiwa Zuberi, anasema namna gani data center itatumika kikamilifu. Kama nilivyosema kwenye majibu yangu, Serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya data center ambapo sasa kuna taasisi 28 ambapo taasisi 19 ni za Serikali na taasisi tisa ni za watu binafsi. Tunaendelea kuhamasisha watu wengi waweze kuitumia data center hiyo na nchi za jirani kwa mfano Burundi, Rwanda zote tunataka wahifadhie data zao hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna hoja kwamba, je, Serikali imepanga kuwekeza mtaji kiasi gani katika shirika. Kama nilivyosema, Serikali imeandaa Mpango Mkakati wa Biashara wa miaka mitano ambao huanzia mwaka wa fedha 2017/2018 hadi mwaka 2021/2022, ambao tunaamini baada ya makadirio haya yatakapoletwa ndipo tutaweza kutenga mtaji kwa ajili ya Shirika letu la TTCL.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ya Mheshimiwa Cecilia Pareso, kwamba kwa nini tunatoka kuwa kampuni na kuwa shirika? Hiyo ndiyo hoja yake na majibu ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, shirika lililopo kwa sasa, kampuni ya TTCL inatoa fursa kwa kampuni kubinafsishwa ilhali nia ya Serikali kwa sasa ni kulifanya shirika liwe madhubuti. Kwa hivyo iko haja ya kubadilisha sheria hii iliyopo. Pia sheria iliyopo haijaainisha masuala ya usimamizi wa miundombinu ya kimkakati, hivyo Muswada huu unapendekeza kuainisha miundombinu ya kimkakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, anaendelea kuuliza, je, shirika linaweza kulinda usalama? Muswada unaopendekezwa unaainisha ulinzi wa usalama wa miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia amezungumza kuhusu suala la bodi ambalo tayari tumeshalizungumza, kwamba tumeweka wajumbe wawili kwenye Bodi yetu sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lingine Mheshimiwa Said Kubenea aliuliza je, Serikali ilikosea wakati wa ubinafsishaji wa TTCL? Mazingira ya wakati huo yalilazimu Serikali kuchukua hatua hizo ambapo kwa sasa mazingira yamebadilika na ndiyo tumeamua kuleta Muswada huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ameuliza tena, kwa nini muwekezaji ameng’oa mitambo, hakuja na mtaji na Serikali ikanunua hisa? Katika kuiandaa TTCL kuingia ubia na mwekezaji mitambo yote ambayo haikuwa na uhusiano na masuala ya utoaji wa huduma za simu ilichukuliwa na Serikali, lakini si kwamba mwekezaji aling’oa mitambo hiyo. Katika makubaliano na mwekezaji kuingia ubia na Serikali, mwekezaji alipaswa kununua hisa asilimia 35 kama sehemu yake ya uwekezaji ndani ya Kampuni. Serikali ilinunua hisa hizo za mwekezaji asilimia 35 kwa shilingi bilioni 14.7 kwa ajili ya kuifanya kampuni ya simu iwe asilimia 100 ya Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, masuala ya Mheshimiwa Saada Mkuya nilishayajibu sipendi nirejee tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbaraka dau kulikuwa na hoja Shirika hili ni la kimkakati. Ni kweli Sheria inayopendekeza imezingatia suala hili kwamba Shirika hili ni la mkakati. Kuna suala je, ni kampuni ngapi na benki ngapi zinatumia data center tangu ilipoanzishwa? Kama nilivyosema, mpaka sasa hivi kuna Taasisi 28 zinatumia data center. Taasisi 19 ni za Serikali na Taasisi tisa ni za sekta binafsi. Nia yetu ni kuhakikisha kwamba taasisi zote za Serikali zinatumia data center. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, iko hoja tena inasema Serikali iongeze mtaji kwa TTCL na iuze hisa kwenye soko la hisa ili kutunisha mtaji wa TTCL. Mpango Mkakati wa Kibiashara wa TTCL utaainisha mahitaji ya mtaji na hivyo Serikali tutajipanga kutokana na mpango mkakati huo. Aidha, kwa sasa Serikali imejikita zaidi katika kumiliki Kampuni ya TTCL kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, anaendelea Mheshimiwa Dau kuuliza Serikali impe mamlaka Bodi na CEO kufanyakazi bila kuingiliwa. Siku zote Serikali inaipa Bodi mamlaka na Mtendaji Mkuu wakati wote ili kuhakikisha wanaweza kufanya kazi iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchangiaji wetu wa mwisho ni Mheshimiwa Deo ambaye katika hoja yake ya kwanza anasema kwamba TTCL ipatiwe mtaji wa kutosha ili iweze kujiendesha kwa faida na kupeleka gawio Serikalini. Ushauri huo umepokelewa
Mheshimiwa Naibu Spika, TTCL ipewe Mkongo wa Taifa ili iweze kujiimarisha. Kwa sasa Serikali imeipa mkongo wa Taifa na data center TTCL ili iweze kujiendesha.
Mheshimiwa Naibu Spika, anaendelea na hoja yake kuhusu Sheria ya PPRA kwa TTCL iangaliwe kwa baadhi ya maeneo ili iweze kujiendesha kibiashara. Sheria ya Manunuzi iliyopo kwa sasa inajitosheleza na inatoa mwanya kwa kila aina ya manunuzi yanayohitajika kulingana na mazingira ya manunuzi husika
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba kutoa hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
WAZIRI WA MAJI NA UMWANGILIAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda kuchukuwa fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mbele yako na kuchangia kwenye hoja hii ya Kamati iliyowasilishwa mbele yetu. Napenda kushukuru sana Kamati yetu kwa kazi nzuri wanayofanya ya kutushauri na kwa kiasi kikubwa Kamati hii imetusaidia sana na tutaendelea kushirikiana nayo kwa maslahi ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama tulivyosikia michango mingi imezungumzwa hapa kuhusu sekta ya maji kwa sababu maji ni jambo muhimu sana na sote tunafahamu maji ni uhai, maji ni afya, kama nilivyosema juzi maji kilimo, maji ni viwanda, maji ni ustaarabu, maji ni kila kitu, bila maji huwezi kufanya jambo lolote.
Mheshimiwa Spika, nitazungumzia kama mambo matano. Jambo la kwanza ambalo Kamati limezungumzia, ni kuhusu huduma ya maji mjini na vijini. Jambo la pili nitazungumzia kuhusu Mfuko wa Maji nitazungumzia na majitaka halafu mwisho nitazungumzia. Miji 25 ambayo inapata wafadhili kutoka Serikali ya India. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama tulivyoelewa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, imesema waziwazi itapofika mwaka 2020, wananchi wanaokaa kwenye mikoa lazima wapate maji kwa asilimia 95, wanaokaa kwenye miji ya Wilaya lazima wapate maji kwa asilimia 90 na kwenye vijiji lazima wapate maji asilimia 85.
Mheshimiwa Spika, hivi tunavyozungumza, kwa wananchi wanaokaa kwenye vijiji, wanapata maji asilimia 64.8; na hivi tunavyozungumza, miradi takriban 1,652 imekamilika na miradi 500 sasa inaendelea kutekelezwa. Miradi inayotekelezwa sasa hivi, kwa mfano, Mkoa wa Arusha tuna mradi mkubwa pale ambao unagharimu takriban shilingi bilioni 520. Longido tuna mradi mkubwa unagharimu shilingi bilioni 15.
Mheshimiwa Spika, naendelea kwa upande wa Mkoa wa Tabora, Nzega, Igunga, tuna mradi unaogharimu takriban shilingi bilioni 604. Kwa upande Magu, Misungwi na Lamadi, tuna mradi unaogharimu takribani shilingi bilioni 42.6. Mwanza kule maeneo ya milimani tuna mradi unaogharimu shilingi bilioni 39.2. Kama nilivyosema juzi, huko Bariadi tuna mradi unaogharimu takribani shilingi bilioni 491.9; na hapa Dodoma tuna mradi wa maji unaogharimu shilingi takriban bilioni 7.288.
Mheshimiwa Spika, nikitaja miradi ni mingi na sitaweza kuitaja yote, lakini kwa ufupi tu, Serikali tunatumia matrilioni ya pesa kuhakikisha kwamba tunamaliza tatizo la maji katika nchi yetu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na issue ya majitaka. Kweli majitaka miaka ya nyuma ilikuwa siyo kipaumbele, lakini sasa Wizara ya Maji tumeamua kwamba lazima tupambane na tupeleke huduma ya majitaka, kwa sababu ni muhimu na kama tunavyojua majitaka yanaweza kupunguza matatizo mengi kwa mfano, maradhi na mambo mengine.
Mheshimiwa Spika, Dar es Salaam pale tunavyozungumza, tuna miradi miwili ya majitaka, mmoja unagharimu takribani shilingi bilioni 239.3 na mradi mwingine unagharimu shilingi bilioni 149.4; kule Arusha tuna mradi wa maji unagharimu takribani shilingi bilioni 116.99 ambao unaendelea; huko Musoma tuna mradi wa majitaka unagharimu takribani shilingi bilioni 30.
Mheshimiwa Spika, kwa ufupi, katika miradi yetu yote ya maji sasa hivi tunahakikisha component ya majitaka inaingizwa ili kuhakikisha tunaendana na Sera yetu ya maji safi na majitaka.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja nyingine kuhusu Mfuko wa Maji. Tumetengeneza kanuni ambazo zimesema wazi wazi angalau asilimia 65 ya fedha za Mfuko wa Maji lazima ziende vijijini. Kwa sababu vijijini ndiyo kwenye changamoto kubwa sana ya maji. Bila kutatua tatizo la maji huko vijijini, itakuwa hatukuwasaidia Watanzania hasa wanaokaa vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuanzia mwezi Julai, 2018 mpaka mwezi Desemba, 2018 tumepokea takribani shilingi bilioni 88 za Mfuko wa Maji. Kati ya pesa hizo, shilingi bilioni 61.6 zimekwenda vijijini, yaani asilimia 70; na shilingi bilioni 26.4 asilimia 30 zimekwenda mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile tumepokea shilingi bilioni 4.73 kutoka pesa za nje kwa ajili ya miradi ya maji. Kwa ujumla, kutoka Julai mpaka Desemba mwaka 2018 tumepokea takribani shilingi bilioni 92.7. Kati ya pesa hizo, Mheshimiwa Pascal aliyosema, kule Jimboni kwake kuna mradi wa maji wa Mloo ambao unajengwa kwa shilingi takribani milioni 465 ambao hivi tunavyozungumza wananchi wanapata maji na Mkandarasi tumemlipa shilingi takriban 265. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna mradi mwingine wa maji kwenye Jimbo lake vilevile, mradi wa Isaka, Itewe unagharimu takribani shilingi bilioni 1.6 na kila akitoa mgao tunampelekea Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa sisi hatuchagui Chama, Watanzania wote ni wamoja na nia yetu ni kuwapelekea Watanzania wote huduma majisafi na salama; kama wako mjini kama wako vijijini, kama wako Chadema au CCM, wote tutawapelekea majisafi na salama.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na issue iliyozungumzwa pia kuhusu madeni makubwa ya Taasisi za Serikali kwa mamlaka. Hili kweli ni changamoto, lakini tumepanga kuanzia sasa hivi, kila tunapopeleka kwenye huduma za maji hizi tunafuatia bili zetu na vile vile tumeamua sasa tuingize vifaa vya kisasa, yaani Pre-paid meter kuhakikisha kwamba kama hukulipa, inapofika mwisho wa mwezi maji yanakatika. Tunaamini tukiweka mfumo huu wa pre-paid meters Wizara zote na Taasisi zote zitaweza kulipa maji au bili za maji bila matatizo.
Mheshimiwa Spika, tunataka kuwekeza kwenye Wizara zote za Serikali; kwenye Mji wa Serikali, Ofisi zote tutaweka pre-paid meters ili tuhakikishe kwamba kama Waziri au Wizara haikulipia maji inakatiwa. Tunaamini tukifanya hivi, kila Wizara italipa bili zake kwa wakati bila kuchelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na suala lingine kuhusu taarifa ya mchakato wa kupeleka huduma ya maji miji 26 ambao unafadhiliwa na Benki ya Exim Bank ya India, ambao unagharimu takribani dola za Kimarekani milioni 500 sawa na shilingi za Kitanzania trilioni 1.2. Miji 26 hiyo ni Muheza, Korogwe, Makonda, Pangani, Ifakara, Kilwa Masoko, Makambako, Njombe, Songea, Chunya, Rujewa, Mafinga, Manyoni, Sikonge, Singida, Mpanda, Urambo, Kaliua, na mingineyo.
Mheshimiwa Spika, hatua tuliyofikia sasa hivi, kwanza mchakato ulianza tarehe 17 mwezi wa Nane mwaka 2018; na wakati huo tulitangaza tender. Tender hiyo ilitangazwa huko India na makampuni 10 ya India yaliomba kwa sababu huu ni mradi ambao unafadhiliwa kwa mkopo kutoka India. Mchakato ulifanyika na tukapata makampuni manne; na hivi sasa tumeshafungua zabuni kwa ajili ya kumpata Mkandarasi mmoja. Kesho wataendelea na mchakato wa kupitia Financia Bill kwa ajili ya finally ya kumpata Mkandarasi ambaye ataanza kufanya usanifu na kutengeneza Tender Document kwa ajili ya miji hiyo 26. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wajumbe wote hawa ama Wabunge wote…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante Profesa.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, la mwisho, Waheshimiwa Wabunge wote ambao wana miradi hii ya miji 26 tumetayarisha group la WhatsApp, kila tunalofanya tunawapa taarifa na ninaamini Wabunge wote hawa wanajua nini Serikali inafanya kuhusu miradi hii na tutaendelea kuwafahamisha mpaka pale ambapo miradi hii utakapokamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja, ninai-support sana hoja ya Kamati yangu. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. PROF. MAKAME M. MBARAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia kwenye Wizara hii ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Awali ya yote, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujaalia kukutana hapa tukiwa na afya njema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita hasa kwenye eneo la miundombinu kwa sababu kubwa kama tunazungumzia digital economy, kama tunazungumzia maudhui, kama tunazungumzia chochote kile kwenye sekta hii ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano jambo muhimu ni miundombinu sahihi. Ndio sababu Serikali yetu iliamua kujenga miundombinu sahihi, miundombinu mahiri, miundombinu ya uhakika kwa kuhakikisha kwamba Watanzania hawa wanapata huduma safi na salama ya mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia kwanza kwenye sekta hii eneo la Mkongo wa Taifa. Kama unavyofahamu na Watanzania wote wanavyoelewa kwamba Serikali yetu imewekeza kwenye Mkongo wa Taifa mabilioni ya fedha. Mpaka sasa hivi tumejenga takriban kilometa 7,450 ambazo zimeunganisha mikoa yote ya Tanzania pamoja na nchi jirani, kwa maana inaunganisha nchi yetu na nchi za nje. Tunafanya vizuri na nchi yetu sasa imekuwa kituo mahiri kwa ajili ya muunganisho wa sekta ya mawasiliano. Pia tumeona taasisi nyingi za Serikali tunatumia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, kuna eneo ambalo bado hatujafanya vizuri. Eneo hili ni eneo la elimu mtandao, matibabu mtandao, biashara mtandao, kilimo mtandao na kadhalika. Watu wengi hapa wanazungumzia kuhusu maudhui, maudhui yanapatikana hasa kama tunakwenda kwenye elimu mtandao kwa sababu tunasomesha vijana wengi, tunawapa nafasi nyingi, matokeo yake vijana hawa wanaweza kufanya vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini hatujafanya vizuri kwenye maeneo haya, kwanza, ni kwa sababu bundle yenye kasi kubwa high speed internet bandwith ipo bei juu. Pili, kumekuwa na shida ya excess network, last mail connectivity. Maeneo mengi ya mjini yanayo internet lakini ukitoka nje ya miji kuna shida, tumefika kwenye wilaya lakini bado kuna shida ya connectivity. Tatu, kunatakiwa taasisi maalum ambayo itasimamia mkongo kwa uwezo mzuri zaidi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi tunaishauri TTCL ambayo ndiyo shirika letu la mawasiliano likishiriana na Wizara iweze kutoa bandwith hasa kwa Vyuo Vikuu na hospitali kwa bei nafuu ili kuwawezesha watu hao kufanya elimu mtandao, waweze kufanya matibabu mtandao na kadhalika. Naamini tukifanya hivyo tutaweza kutumia mkongo wetu vizuri na utaleta faida kubwa zaidi kuliko ilivyo sasa hivi. Sasa hivi wakati mwingi tunatuma mkongo kwa ajili ya simu, kupeleka meseji huku na kule, kupeleka picha huku na kule lakini hatujautumia ipasavyo hasa katika kuleta maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ninalotaka kuchangia ni kuhusu miundombinu ya data center. Pale Kijitonyama tumejenga mfumo wa kisasa wa data center. Data center ile ni ya kisasa, nathubutu kusema kwamba katika Afrika ya Mashariki ndio data center kubwa na ndiyo yenye uwezo wa kisasa. Ina kiwango kinachoitwa tier-3 ambayo inatambulika kimataifa. Hata hivyo, bahati mbaya sana, taasisi chache hasa sekta binafsi zimejiunga na mfumo ule. Nachukua fursa hii kuiomba Wizara itumie muda mwingi kuhamasisha watu wengi waweze kujiunga na taasisi ile au data center ile. Kwa sababu watu wengi wakijiunga na data center ile tutapata fedha zaidi, tutaweza kupata hub grade, tutaweza kufanya mambo mengi na Watanzania watafaidika zaidi na mfumo ule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ya data ni biashara muhimu sana duniani na kila nchi inafanya biashara ya data, lakini hapa kwetu bado hatujachangamkia sana fursa ile na Serikali imewekeza shilingi nyingi karibuni, kama sikosei Dola za Kimarekani milioni 91 zimewekezwa pale kwa ajili ya kujenga data center. Kwa hiyo naomba sana Wizara, naomba sana TTCL na wadau wote waitumie fursa ile kwa maslahi mapana ya nchi yetu. Pia ile data center iko pale tu Kijitonyama lakini ipo haja ya kujenga na maeneo mengine kwa mfano hapa Dodoma na Zanzibar kwa sababu lazima tuwe na backup. Ikitokea la kutokea leo pale Kijitonyama tutapoteza data nyingi ambalo hilo litakuwa siyo jambo zuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mweyekiti, kwa hiyo naomba wizara ifanye jambo hili na iweze kuchangamkia, waweze kujenga data center moja hapa Dodoma, nafikiri mpango huo ulikuwepo na vile vile waweze kujenga data center nyingine huko Zanzibar. Tukifanya hivyo data zitakuwa salama na nchi yetu inaweza kufanya biashara kubwa ya data. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni suala la PKI - Public Infrastructure, hili ni jambo kubwa sana na Wizara wanalifahamu na wamejipanga, naomba waongeze kasi ya kutengeza jambo, kwa sababu mfumo huu ni muhimu sana hasa kwenye usalama wa miala tunayofanya. Kama unavyojua sasa kila mtu sasa hivi ananunua vitu kupitia kwenye mitandao, ananunua vitu kupitia kwenye simu, lakini usalama wa miamala hiyo bado ni shida. Kwa hiyo, tukianzisha mfumo huu wa PKI, naamini kwamba sasa tutajipanga vizuri na tutaweza kufanya kazi vizuri na nchi yetu itafaidika katika teknolojia hii ya habari na utangazaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo machache, sasa naomba kuunga mkono hoja na nafikiri tunaendelea vizuri. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira wa Mwaka 2018
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nichukue fura hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kusimama mbele yenu tena na kutoa mchango wangu katika hoja hii niliyoiwasilisha leo asubuhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nikushukuru wewe binafsi. Pia napenda niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliopata nafasi ya kuchangia hoja yangu niliyoiwasilisha hapa Bungeni leo asubuhi na michango yao
ni mizuri na ya kina yenye lengo la kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Wizara yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingi zimetolewa na hii ni dalili ya dhati inayoonyesha mwamko mkubwa walionao Waheshimiwa Wabunge kwa upande wa kuendeleza sekta ya maji. Kama tunavyofahamu maji ni uhai, afya, kilimo, viwanda, ustaarabu na kila kitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba yangu imechangiwa na wachangiaji 21 ambapo wachangiaji sita wamechangia kwa maandishi na wachangiaji 15 wamechangia kwa kuzungumza. Michango ya Waheshimiwa Wabunge wote ilikuwa ni mizuri sana na iliyosheheni mapendekezo, ushauri na busara ya namna bora ya kuendeleza sekta ya maji. Aidha, siyo rahisi kujibu hoja zote za Waheshimiwa Wabunge kwa kina na kutosheleza kwa muda mfupi huu tulio nao lakini naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba hoja zao zote tumezichukua na tutazifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma ya maji vijijini. Kwanza Sera ya Taifa ya mwaka 2002 inaeleza waziwazi kwamba wananchi wa vijijini lazima wapate majisafi na salama siyo umbali wa mita 400 kutoka kwenye makazi yao. Pia Ilani ya Chama cha Mapinduzi imeeleza waziwazi kwamba ifikapo mwaka 2020 Watanzania wote wanaoishi vijijini ni lazima wapate maji asilimia 85, wale wanaoishi Miji Mikuu ya Wilaya lazima wapate maji asilimia 90 na wale wanaoishi Miji Mikuu ya Mikoa lazima wapate maji asilimia 95. Je, hali ikoje sasa hivi kwa vijijini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vijijini sasa miundombinu ya maji iliyojengwa ina jumla ya vituo vya kuchotea maji 123,888 ambavyo vina uwezo wa kuhudumia Watanzania takribani milioni 30.72 sawa na asilimia 85.2 ya wananchi wanaoishi vijijini ambao ni asilimia 35.344. Hata hivyo, katika vituo hivyo, ni vituo 85,286 tu ndivyo vinavyofanya kazi na kutoa huduma kwa Watanzania wapatao 21,321,500 sawa na asilimia 59 ya wananchi wanaoishi vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni changamoto kubwa na sisi tumeahidi ifikapo mwaka 2020 Watanzania watakaopata maji vijijini ni asilimia 85 na tumejipanga kuhakikisha kwamba asilimia 85 hiyo tutaifikia na njia moja ambayo tumejipanga ni kuleta Muswada huu hapa Bungeni. Hali hii yote imechangiwa na changamoto ya mfumo uliopo wa usimamizi na uendeshaji wa miradi ya maji, miundombinu ambayo imejengwa kwa chini ya kiwango na uharibifu wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo hayo yote kwa pamoja ndiyo yamesababisha tuweze kufikia asilimia hii ya
59. Uzoefu na uchambuzi wa mazingira ya sasa wa utoaji wa huduma za maji nchini umeonesha kuna haja ya kuangalia upya mfumo wa utoaji wa huduma ya maji hapa nchini hasa maeneo ya vijijini na ndiyo sababu ya msingi kubwa kuleta Muswada huu uliopo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya usimamizi wa uendeshaji wa jumuiya ya watumiaji maji pia ndiyo sababu kuwa iliyosababisha kuleta Muswada huu. Pia usimamizi wa miradi ya maji, wataalamu wote wa maji kuwajibika kwenye Wizara ya Maji; sasa hivi walivyo wanawajibika kwenye Wizara ya TAMISEMI ambayo hii inaleta shida katika usimamizi na hii imeleta changamoto na miradi mingi kutokukamilika kwa viwango vinavyostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja kuhusu Mfuko wa Maji. Wengi walilalamika na walitaka kufahamu asilimia ngapi ya pesa hizi zinakwenda huko vijijini. Tumeandika kanuni ambayo inasema mapato ya Mfuko wa Maji angalau asilimia 95 lazima yaende kupeleka huduma za maji huko vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia Julai mpaka Desemba, 2019, pesa tulizopokea ni shilingi bilioni 67.8, pesa zilizopelewa vijijini ilikuwa shilin bilioni 46.2 sawa na asilimia 7.8; tunaenda juu sasa. Zilizopelekwa mjini takribani shilingi bilioni 21.6 sawa na asilimia 31.9 na miji yenyewe siyo ile miji mikubwa, ni ile miji midogo ambayo yenyewe miundombinu yake ni hafifu kwa mfano Longido lazima kule utaona kama ni mjini lakini kwa kweli kule ni kama vijijini kwa upande wa maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizarani tumejipanga sasa, Mamlaka zote za Maji Mikuu ya Mikoa hasa zile zilipo katika grade A sasa hawatopata hela kwenye Mfuko wa Maji. Tumeanzia na DAWASA, miradi yote inayotekelezwa DAWASA sasa hivi pale Dar es Salaam wanajitegemea wenyewe kwenye pesa zao wenyewe (own source) na kila mwezi wanatenga takribani asilimia 34 ya mapato yao. Matokeo yake hivi tunavyozungumza DAWASA wana mradi mkubwa wa kutoa maji Chalinze ambao unapeleka maji Chalinze, Mboga na Bagamoyo wenye thamani shilingi bilioni 10.7 unatekelezwa kwa pesa za DAWASA kwa asilimia 100 na hawapati pesa kwenye Mfuko wa Maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi mwingine wa kutoa maji kutoka Kibamba – Kisarawe unatekelezwa na DAWASA kwa shilingi bilioni 10.7. Pesa hizi ni kutoka kwenye Mfuko wa DAWASA, hawapati pesa kutoka kwenye Mfuko wa Maji hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi mingi kwa mfano tunapeleka maji Kiwalani, Madale, Usukumani na maeneo mengi Dar es Salaam ambayo pesa zote hizi za miradi hii ni asilimia 100 kutoka DAWASA hawategemei hata senti tano kutoka kwenye Mfuko wa Maji. Tuna mradi mwingine wa kupeleka maji kule Kigamboni kutoka kwenye visima vyetu 12 vilivyopo pale Mpiji; tumetangaza siku tatu zilizopita na mradi huu vilevile utasimamiwa kwa asilimia 100 na DAWASA, hawatochukua pesa kwenye Mfuko wa Maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwahakikishie Wabunge kwamba tumekuja na mpango sasa, Mamlaka zote za Maji kwa mfano ya Arusha, Moshi, Mwanza lazima zijitegemee kwa asilimia 100 hasa hii miradi ya usambazaji. Hawawezi tena wao wakategemea Mfuko wa Maji kwa ajili ya kupeleka maji. Hii tumejipanga na tunatekeleza kwa
vitendo na tumeweka makubalino (performance contract) baina ya Wizara na Mamlaka zote za Maji kuhakikisha kwamba sasa wanabadilika na wanajitegemea kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja kwamba sasa wakati umefika lazima tuchukue miradi ya maji kutoka Ziwa Victoria. Hivi tunavyozungumza kuna mradi mkubwa wa maji unatoka Lake Victoria kupitia Shinyanga, Tabora, Nzega na Igunga ambao unagharimu takribani shilingi bilioni 605. Hata kwenye Jimbo lako tuna mradi mkubwa ambao utaanza mwezi Septemba ambao wenyewe utachukua maji Lake Victoria utapeleka Mjini Bariadi, Busega, Itilima na vijiji vingine kama 70. Mradi huu utagharimu takribani shilingi bilioni
491.9 na mkataba umeshasainiwa baina ya Green Fund na KfW au Shirika la Maendeleo la Ujerumani. Tumejipanga kuhakikisha kwamba Watanzania popote walipo kama upande wa Victoria, Mwanza na Kigoma wote wanapata majisafi na salama na tunahakikisha kwamba hili tunatekeleza kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja ya VAT kwenye miradi ya maji. Ni kweli kulikuwa na changamoto kubwa kupata VAT kwa ajili ya miradi ya maji ama miradi yote ya miundombinu lakini tumekaa na tumeshakubaliana baina ya mimi mwenyewe, Waziri wa Miundombinu, Waziri wa Fedha, Mwanasheria Mkuu na wadau wote wanaohusika kwamba sasa vibali vya VAT au maombi ya VAT yasichukue zaidi ya wiki moja kwa ajili ya miradi yote ili miradi iweze kutekelezwa haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya vyanzo vya maji. Vyanzo vya maji ni muhimu sana. Kwenye Sheria yetu ya Usimamizi wa Maji, Na.11 ya mwaka 2009 ni lazima tusimamie sheria hii. Nitakupa mfano, mwaka 1962 kiwango cha maji kwa mtu mmoja hapa Tanzania kilikuwa wastani wa mita za ujazo 7,861 kwa mwaka wakati huo tulikuwa na watu takribani milioni 10.6. Leo hii tunavyozungumza kiwango cha wastani kwa mtu mmoja kimeshuka mpaka kufikia mita za ujazo 1,800 mwaka 2018 wakati huu sasa tuna watu takribani milioni 54.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imesababishwa kwanza na ongezeko la watu; uharibifu wa mazingira ambao husababisha vyanzo vya maji kukauka; mabadiliko ya tabianchi na uchafuzi unaoharibu vyanzo vya maji. Iko haja ya kusimamia vyanzo hivi ili kuhakikisha kwamba sasa tunalinda vyanzo vyetu kwa maslahi ya Watanzania wa leo, wa kesho na vizazi vinavyokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna sheria ya kulinda mito kwenye vyanzo vya maji ya mita 60, sheria ya kulinda mabwawa ya mita 500; hizi zote tunazipitia upya. Tunajaribu kujiuliza, je, kama tutapunguza mpaka mita 55 itakuwaje? Je, kutoka mita 60 kama tutapunguza mpaka mita 45 itakuwaje? Nia yetu kwanza ni kutoa fursa kwa Watanzania walioko maeneo yale lakini vilevile kulinda vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mabwawa, tuna mita 500 sasa hivi zimewekwa kisheria, tunajaribu kuuliza, je, kwa nini zimewekwa mita 500? Mita 500 hizi zimewekwa kulinda usalama wa wananchi waliopo pale. Wote Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, mwaka jana kule Count ya Kenya watu karibuni 14 walikufa baada ya bwawa moja kupasuka. Wiki iliyopita tu Brazil nyote ni mashahidi hapa, watu wengi wamekufa baada ya bwawa moja kupasuka kule. Kwa hiyo, tutaangalia mambo yote hao kwa ujumla, tunafanya utafiti kuangalia hivi vigezo kama ni sahihi lakini wakati huo huo tunaangalia mazingira yetu, usalama wa wananchi wetu, vyanzo vya maji na kila kitu kwa maslahi mapana ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuja suala vilevile la uchimbaji wa visima, hili vilevile tunapitia kanuni. Tunajua miaka kumi iliyopita ukichimba kisima mita tano ama 15 unapata maji lakini hali ilivyo leo pengine mpaka uende mita
25. Hili tunaliangalia upya na tutaleta mwongozo kuhakikisha kwamba miongozo, kanuni na taratibu hizi zitaleta maslahi mapana kwa Watanzania wote kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja nyingine kuhusu uwakilishi wa wanawake kwenye Bodi. Hili tumeliangalia kwa kina; kama utakwenda kwenye Jedwali la 1-5 tumeeleza waziwazi wanawake ambao watakuwa kwenye Bodi hizi itakuwa angalau one third. Hii ina maana kama una Wajumbe kumi unaweza kwenda wajumbe 3, 5 hata wajumbe 10 unaweza kuwapata wanawake. Nia yetu ni kuwawezesha wanawake kwa sababu tunajua wanawake ndiyo wanapata changamoto kubwa za maji. Hili tumelijua na tunalifanyia kazi na mimi kama Waziri nitahakikisha kwamba Bodi zote zina angalau asilimia 50 wanawake na kuendelea mbele. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja nyingine kuhusu fedha za kuendeshea RUWASA. Kwanza tutapata fedha kutoka kwenye Mfuko wa Maji. Vilevile tuna fedha ambazo zinatoka kwenye Benki ya Dunia. Tumepata mkopo wa shilingi bilioni 804 kutoka Benki ya Dunia ambapo baadhi ya pesa hizi zitakwenda kuendeshea mamlaka (agency) hii ya RUWASA ili kuhakikisha kwamba agency hii itaweza kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na maneno mengi kwa mfano misuse water, definition tumetoa ili kuhakikisha kwamba kila tunalofanya sheria hii iweze kuwasaidia Watanzania kwa ujumla. Hatutaki sheria hii iwe pingamizi kwa ajili ya kuwapatia Watanzania huduma ya maji. Nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba sheria hii inawezesha Watanzania kupata majisafi na salama popote pale walipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja kwamba madeni mengi ya wakandarasi hatuyalipi. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tumejipanga sana kuhakikisha kwamba madeni yote tunayalipa kwa wakati ili wakandarasi wale waweze kufanya kazi kwa uadilifu na kwa viwango tulivyokubaliana.
Natoa wito kwamba wahandisi wote lazima wasimamie miradi hii kwa uadilifu kwa sababu changamoto kubwa kabisa tunayopata kwenye miradi ya maji kama alivyosema Naibu Waziri ni usimamizi mbovu na matokeo yake tunajenga miradi kwa pesa nyingi lakini mwisho wa siku miradi ile inashindwa kufanya kazi inavyostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini sasa dawa ya jambo hili tumelipata, sheria hii itatatua kwa kiasi kikubwa tatizo hili. Tunaamini baada ya sheria hii mabadiliko makubwa sana yatatokea hasa upatikanaji wa maji kwenye maeneo ya vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, napenda sana kuwashukuru sana wafanyakazi wote wa Wizara ya Maji kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kusimamia Muswada huu mpaka leo tukaweza kuuleta hapa mbele yenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa sasa naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. PROF. MAKAME MNYAA MBARAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninaomba kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha na mimi kutoa mchango wangu kwa maandishi kwenye hoja hii iliyopo mbele yetu ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2021/2022.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipongeza sana Serikali yetu kwa kuondoa Kodi ya Ongezeko kwenye maeneo mbalimbali kwenye simu janja za mkononi (smart phones) HS Code 8517.12.00, vishikwambi (Tablets) HS Code 8471.30.00 au 8517.12.00 na modemu (modems) HS Code 8517.62.00 au 8517.69.00.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango alivyosema kwenye kitabu chake cha hotuba ya bajeti (ukurasa wa 29 mpaka 30) lengo kubwa la hatua hii ni kuhamasisha matumizi ya huduma za mawasiliano ili kufikia lengo la asilimia 80 ya watumiaji wa intaneti ifikapo mwaka 2025 kutoka asilimia 46 iliyopo sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, upenyaji (penetration) mkubwa wa simu janja, vishikwambi na modem ni muhimu sana kwa sababu zifuatazo; kwanza, wastani wa mapato kwa mtumiaji (avarage revenue per user (ARPU)) huongezeka kutokana na matumizi ya data kupitia vifaa tajwa hapo juu. Motokeo yake mapato ya makampuni ya simu huongezeka zaidi kutokana na utumiaji mkubwa wa data. Makampuni hayo yanaweza kupata faida zaidi na kulipa ushuru zaidi kwa Serikali. Aidha, simu janja na vifaa vingine tajwa hapo juu kwa ujumla hufanya maisha ya watumiaji katika Taifa lolote duniani iwe rahisi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, upenyaji mkubwa wa simu janja, vishikwambi, na modem huhamasisha uanzishwaji biashara mtando, huongeza utoaji wa huduma za jamii kama vile elimu mtandao, matibabu mtando na kadhalika. Kuongezeka biashara mbalimbali kupitia mtandao huongeza ushuru na mapato kwa Serikali. Aidha kuimarika kwa huduma za jamii kutapunguza umaskini nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, tafiti mbalimbali duniani zinaonesha ya kuwa ongezeko la matumizi ya simu janja na matumizi ya Mkongo wa Mawasiliano kwa asilimia 10 hukuza Pato la Taifa kwa asilimia 1.2, huongeza ubunifu, tija katika maeneo ya kazi na ajira. Kwa hiyo hatua hii ya Serikali ya kuondoa kodi ya ongezeko kwenye vifaa hivyo ni ya kupongezwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kuwa Serikali yetu kwa miaka mingi imekuwa ikifanya jitihada za makusudi kupunguza bei ya bando (gigabit kwa sekunde (GB)) kwa dhamira ya ujumuishaji wa kidijiti na kukuza uchumi wa kidijiti nchini. Kwa bahati mbaya matokeo chanya hasa wananchi wa kipato cha chini na wananchi wa vijijini hayajafikiwa. Ninaendelea kuishauri Serikali yetu sikivu iendelee kupunguza bei ya bundle ili wananchi wote wa mijini na vijijini na wenye vipato vya chini waweze kufaidika na TEHAMA na uchumi wa kidijiti. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iendelee kuwekeza kwenye mindombinu hasa maeneo ya vijijini ambako ndio kwenye Watanzania wenye kipato cha chini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia. Mwisho ninaunga mkono hoja hii iliopo mbele yetu.
Azimio la Bunge Kuhusu Mapendekezo ya Kurejea Katiba ya Tume ya Usafiri wa Anga ya Afrika ya Mwaka 2009
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijafanya hitimisho la hoja iliyoko mbele, naomba kufanya masahihisho kidogo tu. Wakati natoa hoja yangu nilisema Mkutano wa Kumi na Moja, lakini huu ni Mkutano wa Kumi na Mbili, naomba isomeke hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote tena, napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana hapa kwenye Bunge letu Tukufu na kujadili hoja hii iliyo muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kukushukuru wewe binafsi, kwa jinsi ulivyoongoza majadiliano kwenye hoja hii ya Katiba ya Tume ya Usafiri wa Anga wa Afrika ya Mwaka 2009.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kipekee nimshukuru Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Selemani Moshi Kakoso pamoja na Waheshimiwa wote, Wajumbe wa Kamati ya Miundombinu kwa jinsi ambavyo walichangia hoja hii na jinsi ambavyo walichambua hoja hii kwanza kuanzia kwenye Kamati mpaka walipokuja hapa Mwenyekiti amechangia vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri kwamba hoja hii ni muhimu sana kwa maendeleo na ukuaji wa Sekta ya Anga hapa nchini. Pia, nawashukuru Waheshimiwa wote Wabunge waliochangia hoja hii, tumezichukua hoja zao na tunaenda kuzifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hoja za Kamati ya Bunge ya Kudumu zilikuwa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ya kwanza ilikuwa ni kutoa fursa kwa lugha ya Kiswahili itangazwe. Pili, fursa za soko la ajira pamoja na za anga pia, wadau wengine washirikishwe. Yote haya tumeyachukua tunaenda kuyafanyia kazi, tutaboresha zaidi au tutaitangaza zaidi Lugha ya Kiswahili, pamoja tutatangaza zaidi soko la anga hapa Tanzania pamoja na kuwashirikisha wadau.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Chamuriho yeye ana wasiwasi tu ambao ameonyesha kuhusu Mkataba wa Yamoussoukro. Ukweli wenyewe kama alivyosema Naibu Waziri, kwamba mkataba wa nchi na nchi unaongozwa na Bilateral Air Service Agreement. Kwa mfano, leo Kenya wamesaini Katiba hii, Rwanda wamesaini Katiba hii, lakini Rwanda yeye haiwezi kutoka ikaenda Nairobi ikachukua abiria kupeleka Mombasa, haiwezi. Kwa sababu inaongozwa baina ya Kenya na Rwanda ni Bi-Service Agreement au Bilateral Service Agreement baina ya Kenya na Rwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunayo na nchi mbalimbali, tuna na Kenya, tuna na Rwanda na nchi nyingine mbalimbali, tunayo mikataba hiyo. Hiyo ndio inaongoza utaratibu wa kutoa abiria kutoka eneo moja kwenda la pili. Leo kwa mfano, KLM inafika Kilimanjaro lakini haiwezi kuchukua abiria wa ndani kutoka KIA kuwaleta Dar es Salaam. Kwa hiyo, tumepokea maoni ya Mheshimiwa Dkt. Chamuriho, tunayaheshimu na tunaenda kuyafanyia kazi, lakini nimhakikishie tu kwamba usaifiri wa anga nchini upo salama na Air Tanzania tutaendelea kuilinda ili iweze kufanya kazi iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo mafupi, sasa naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyoanza wenzangu naomba kuchukua fursa hii, kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kutujalia/kunipa fursa hii. Napenda kwanza kuipongeza sana Kamati yetu ya Miundombinu kwa ripoti nzuri na kubwa na sisi, kwenye Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ripoti hiyo tumeikubali na tunakwenda kuifanyia kazi kama walivyoelekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nijikite kwenye ujenzi wa reli. Ujenzi wa reli unakwenda vizuri na mpaka sasa hivi ninavyoongea kipande cha Dar es Salaam mpaka Morogoro, chenye urefu wa kilomita 300 umefikia asilimia 95. Tarehe 18 Februari treni ya mwanzo ya umeme itaingia nchini na itafanya majaribio kwenye line ile, pamoja na kuwafundisha madereva wetu jinsi ya kuendesha treni ya umeme. Kipande cha pili cha kutoka Morogoro mpaka Makutupora chenye urefu wa kilometa 422 nacho kimefikia asilimia 81. Kipande cha tatu kutoka Mwanza Isaka chenye urefu wa kilometa 130 umefikia asilimia nnena kipande cha Makutupora mpaka Tabora yenye urefu wa kilomita 368, ambayo imegharimu takribani shilingi trilioni 4.4 tulisaini mbele ya Mheshimiwa Rais tarehe 28 mwezi Disemba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na tayari ameshatupatia fedha kwa ajili ya kulipa advance payment/malipo ya awali kwa makandarasi hao. Mpaka hivi sasa tunavyoongea Serikali yetu imewekeza takribani shilingi trilioni 14.7 kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa. Kujenga reli ni jambo lingine lakini la msingi pia ni kuwa na miundombinu/vifaa vya kutumia reli hiyo. Wiki mbili zilizopita Serikali ilitoa kibali na tulisaini mkataba wa manunuzi, wa mabehewa 1,430 wenye gharama takribani Shilingi bilioni 301. Vile vile, tumesaini mikataba mingine kwa ajili ya vichwa vya treni vya umeme 17 EMU 10 na Simulator kwa takribani dola za Kimarekani 294.7. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi vichwa vya umeme pamoja na vifaa vingine tayari Serikali imeshaendelea kutoa takribani shilingi trilioni 1.2 tunawaambia watanzania kwamba, reli hii itakuwa ni reli ya kisasa na itakuwa na uwezo mkubwa na Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi tumejipanga vizuri mambo yatakuwa vizuri na itakuwa ni reli ya mfano ya kuigwa katika Bara la Afrika. Kwa upande wa viwanja vya ndege kweli tunakubaliana na Kamati kwamba, ipo haja sasa ujenzi wa viwanja vya ndege uhamishiwe kutoka TANROADS kupelekwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege. Hilo tunalifanyia kazi na tutalikamilisha hivi karibuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Kamati yetu imeongea kwamba kuna changamoto kubwa ya mifumo ya TEHAMA pale bandari ni kweli, hilo tunalijua na tunaendelea kuhakikisha tunaiboresha ili sasa mapato yasiweze kupotea. Kila fedha inayoingia pale tuweze kuijua imekwenda wapi na imefanya nini. Kuhusu mizani kuna Mbunge mmoja ameongelea kuhusu mizani hili ni jambo kubwa na tunalijua na tumekuja na utaratibu mpya sasa wa kupunguza mizani. Kwa mfano, magari ya mafuta yanayotoka bandarini kwenda Kigali sasa yanapima kwenye mizani tatu tu na tunaendelea, nafikiri huko baada ya mwezi mmoja tunafanya utafiti tutapunguza na itakuwa inapima mizani moja tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nia yetu ni kuhakikisha kwamba tunaifungua Bandari ya Dar es Salaam na kila mtu aweze kutumia Bandari ya Dar es Salaam. Mwisho kuhusu mradi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) tayari tumefanya awamu ya kwanza (BRT I) tayari imekamilika. Tuko (BRT II) sasa inaendelea vizuri na hivi karibuni tutaanza kufungua baadhi ya maeneo na (BRT III) tutaanza kusaini wiki mbili zinazokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, kwanza nami ninakushukuru kwa kunipa fursa hii kuchangia kwenye hotuba yetu hii iliyoko mbele yetu. Pili, napenda kusema kwanza ninaunga mkono hotuba hii kwa asilimia 100. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna hoja tatu ambazo zimewasilishwa kwa upande wa Wizara yetu. Hoja ya kwanza ni kuhusu ujenzi wa reli ya kisasa -Standard Gauge. Kama tunavyokumbuka reli ya kisasa Standard Gauge ilianza mwaka 2017 na ina urefu wa takribani kilomita 1,219 kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza. Reli hii imegawanyika katika vipande vitano. Kipande cha kwanza ni kutoka Dar es Saalam mpaka Morogoro chenye urefu wa kilomita 300, kati ya kilomita 300 kilometa 205 ni za njia kuu na kilometa 95 ni za kupishana. Kipande hiki kinajengwa kwa gharama ya takribani dola za Kimarekani bilioni 1.215 sawa na Shilingi Trilioni 2.7 za Kitanzania. Maendeleo ya ujenzi wa kipande hiki umefikia asilimi 95.72. Bei kwa kilomita moja ni takribani Dola Milioni 4.05 hii gharama inajumlisha na VAT.
Mheshimiwa Spika, wakati tunaweka mchakato wa ununuzi kwa ajili ya kipande hiki Wakandarasi wengi walichukua tender document lakini mwisho wa siku ni mkandarasi mmoja tu aliyerudisha hiyo tender document ambaye ni Yepi. Tulimpa kazi hiyo kwa kutumia kigezo chetu tulichojiwekea ambayo ni engineering estimation. Kwa vile kazi hiyo inaenda vizuri na tumefikia asilimia hiyo nategemea mwezi Mei tutaanza kufanya majaribio kwa ajili ya treni ya kwanza ya umeme itaanza kupita.
Mheshimiwa Spika, kipande cha pili ni kutoka Morogoro mpaka Makutupola chenye jumla ya kilomita 422. Kati ya kilomita hizo kilomita 336 ni za njia kuu na kilomita 86 ni njia za kupishana. Gharama ya mradi huo ni Dola Bilioni 1.923 sawa na shilingi trilioni 4.4 za Kitanzania. Ujenzi wake unaendelea na umefikia asilimia 82.68. Gharama kwa kila kilomita moja ni takribani dola za Kimarekani milioni 4.55 na gharama inaongezeka kwa sababu inategemea eneo gani tunapita.
Mheshimiwa Spika, kwa Dar es Salaam ilikuwa hali ni nzuri yaani tambarale lakini kila ukienda baadhi ya maeneo mengine kuna mito, kuna milima hiyo madaraja yanaongezeka, kuna maeneo lazima ujenge mahandaki ili kuhakikisha kwamba reli yako inakuwa salama vizuri.
Mheshimiwa Spika, lot nyingine ni lot ya tatu na rote ya nne. Lot hizi mbili tulizitangaza lakini hatukuweza kupata Mkandarasi. Kwa hiyo, tukawajibika kuja na utaratibu mwingine wa single source ambao unakubalika kisheria. Kigezo cha kwanza cha single source lazima yule Mkandarasi unaemchukua awe na uwezo na uzoefu mkubwa. Pili Mkandarasi huyo awepo kwenye eneo la site yenyewe, yaani anafanya kazi kama hiyo kwenye site hiyo. Kwa vile, katika kipande cha tatu, kipande cha Makutupora mpaka Tabora chenye urefu wa kilomita 368 tulitumia utaratibu huo na gharama ilikuwa Dola za Kimarekani Bilioni 1.908 sawa na Shilingi Trilioni 4.41.
Mheshimiwa Spika, jana tumeweka jiwe la msingi kwa ajili ya kipande hicho na sasa tumeshamlipa Mkandarasi takribani Shilingi Bilioni 609.36. Mkandarasi hapa ni Yepi na ndiyo anaanza sasa hivi kuweka vifaa, gharama kwa kilomita Moja ni takribani dola za Kimarekani Milioni 5.14. Hapa mnaona gharama inaanza kuongezeka kwa sababu tunapita kwenye milima, tunapita kwenye maeneo yenye tetemeko. Kwa vile reli yetu lazima ijengwe imara zaidi kuliko maeneo mengine ambayo hayana changamoto hizi za kijiografia.
Mheshimiwa Spika, kipande kingine ni kutoka Tabora – Isaka chenyewe kina urefu wa kilomita 168. Tumefanya utaratibu kama huu wa single source lakini mpaka sasa hatujakubaliana na Mkandarasi kwa sababu Mkandarasi ameleta bei ya juu ukilinganisha na bei tuliyojiwekea yaani engineering estimation. Bado mazungumzo yanaendelea na tunaamini Mkandarasi atashuka vizuri ili bei tutakayoipata hapa iendane na engineering estimation ambayo tuliiweka hapo zamani.
Mheshimiwa Spika, kipande cha tano ambacho kinaendelea ni kipande cha kutoka Isaka mpaka Mwanza chenye urefu wa kilomita 341. Kipande hiki kina urefu wa kilomita 249 njia kuu na kilomita 92 njia za kupishana. Kazi inaendelea na mobilization inaendelea na Mkandarasi amefika asilimia 4.46.
Mheshimiwa Spika, Mkandarasi hapa ni...
SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, maelezo mengi nitatoa wakati tutakapoleta bajeti yetu. Naomba tu kuunga mkono hoja kama nilivyosema kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Spika, ahsanteni sana kwa kunisikiliza. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninakushukuru sana kwa kunipa fursa hii kusimama mbele yako kuchangia kwenye hoja iliyoko mbele yetu. Naendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia kukutana hapa leo tukiwa na afya njema.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kutuwezesha na kutupa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali. Serikali inatambua kwamba, miundombinu ndiyo inakuza uchumi wa nchi yeyote duniani. Ninapenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika Sekta ya Uchukuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo matano ambayo nitayatolea ufafanuzi. Eneo la kwanza, ni kuhusu bandari; wachangiaji wote kwa ujumla wamezungumzia bandari. Tunafahamu kwamba, Bandari ya Dar es Salaam ndiyo lango kubwa la uchumi na imekuwa ikitegemewa na Tanzania na nchi mbalimbali za Jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni tumekuwa na ongezeko kubwa la meli pale Bandari ya Dar es Salaam. Hii ni baraka kubwa kwa nchi yetu lakini pia imetupa changamoto kubwa ya kujipanga jinsi gani tutaweza kutatua changamoto hii ili isiweze kujitokeza tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza mpango huo, Serikali imeamua kujenga gati kubwa, lenye urefu wa mita 590 pale Malindi wharf ambayo itakuwa na uwezo wa kuwekeza meli mbili kwa wakati mmoja. Hivi ninavyozungumza, tunatafuta Mkandarasi kwa ajili ya kazi hiyo na pesa ipo. Mkakati wa pili ambao tumejipangia, ni kujenga bandari ya kisasa kwa ajili ya ushushaji wa mafuta pamoja na matenki ya kuhifadhia mafuta. Mradi huu unaendelea. Hivi sasa ninavyozungumza, tayari Mkandarasi tumeshampata kwa ajili ya kazi hiyo na tutatumia takribani shilingi bilioni 560 kwa ajili ya kujenga matenki hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya pili itakayofuata ni kujenga bandari hiyo huko Bagamoyo kwa ajili ya kuteremshia mafuta ili kupunguza msongamano wa meli za mafuta ambao sasa hivi upo. Hatua ya tatu ambayo tumeendelea nayo kupunguza msongamano unaoendelea, ni kujenga bandari Gati namba 13 mpaka 15. Sasa hivi tuko katika hatua ya kupitia design ya mradi huo ili tuweze kuitangaza, tupate mkandarasi kwa ajili ya kazi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haikuishia hapo tu, lakini huko Mtwara, tunajua hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la meli na tumeamua sasa kujenga Bandari Maalum kwa ajili ya mizigo michafu yaani dirty cargos.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyozungumza tayari tuko katika hatua ya mwisho ya kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa gati hilo. Hatukusimama hapo tu lakini karibu kila sehemu ya nchi yetu tunajenga Bandari ili kuifungua Bandari ya Dar es Salaam na kuongeza biashara kati ya nchi yetu na nchi za Jirani. Kwa mfano, huko Mwanza, pale Mwanza south, tunajenga Bandari ambayo itakuwa na uwezo wa kuhudumia meli mbalimbali na gharama yake takribani shilingi milioni 24. Huko Kemondo, Kagera tunajenga Bandari ambayo itakuwa na uwezo wa kuhudumia meli mbalimbali za mizigo na za abiria na inagharimu takribani shilingi bilioni 19.6
Mheshimiwa Naibu Spika, huko vilevile Bukoba pale Mjini tunajenga bandari nyingine ambayo itakuwa na uwezo wa kuhudumia meli mbalimbali. Huko Ziwa Nyasa, Mbamba Bay pia tunajenga bandari ya kisasa ambayo inagharimu takribani shilingi bilioni 75 kwa ajili ya abiria na mizigo ambayo Bandari hiyo wataitumia watu wa Malawi pamoja na watu wa Zambia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuipa TPA na Taasisi zote za Serikali pesa ya kutosha kuhakikisha kwamba tunaijengea Miundombinu ya kisasa kuhakikisha, inakabiliana na ongezeko kubwa la mizigo inayotokea kwenye bandari zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huo kwa upande wa Miundombinu lakini Serikali tunajua unaweza kujenga miundombinu ya kisasa lakini bila kuboresha utendaji, haitosaidia sana. Kwa vile Serikali tumejipanga kuhakikisha kuwa tunaboresha utendaji kazi wa bandari zetu na hivi tunavyozungumza, tumeona ufanisi mkubwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ninalotaka kulizungumzia ni sehemu ya marine service. Kwa kweli kama Kamati walivyosema, kuna miradi mingi ya zamani ambayo bado haijamalizika kwa sababu mbalimbali lakini tunahakikisha kwamba tunaendelea kuimaliza ili imalizike kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano hivi majuzi tu tumesaini mradi wa kwanza kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha ujenzi wa meli huko Kigoma ambacho kitakuwa kina uwezo wa kujenga meli mbalimbali. Pia tumesaini mradi wa meli ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukua mizigo tani 3,500 ambayo itahudunmia eneo la Kigoma, Congo pamoja na Zambia kwa ajili ya kupeleka mizigo. Tunafanya mambo haya yote ili kuhakikisha Bandari ya Dar es Salaam, inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaendelea na ukarabati wa meli ya MV. Sangara ambayo inagharimu takribani shilingi bilioni 9.016, pia mefikia asilimia 92 na tunategemea itamalizika mwezi Mei, 2024.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaifanyia utafiti ili tuweze kuitengeneza meli ya MV. Mwongozo. Ilikuwa na tatizo la stability ambayo hivi sasa wataalam wanajaribu kuifanyia utafiti kuona jinsi gani ambavyo tutaweza kuitengeneza ili na yenyewe iweze kufanya kazi ya kupeleka mafuta kutoka Tanzania kwenda DRC pamoja na Nchi ya Zambia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia huko Kigoma tunaendelea, tumefunga saini mkataba kwa ajili ya ukarabati wa meli ya MV. Liemba ambayo ni meli ya siku nyingi na ukarabati huo utagharimu takribani shilingi bilioni 33.38. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huko Mwanza vilevile kama mnavyojua tunajenga meli ya kisasa MV. Mwanza. Tunategemea itamalizika mwezi Mei, 2024 na itagharimu kakribani shilingi bilioni 127.27 na imefikia asilimia 93, kazi inaendelea vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la LATRA, tunakubaliana na Kamati kwamba tupitie kanuni mbalimbali zilizopo ili tuweze kuboresha ufanisi wa utendaji wa LATRA na hii tutaifanyia kazi. Pia kuna changamoto ya wafanyakazi, tutaendelea kuajiri wafanyakazi wengi na wenye ujuzi ambao utaongeza ufanisi wa LATRA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TAA tunajipanga kuboresha au kutengeneza Sheria Mpya ya Uendeshaji wa Viwanja vya Ndege. Tunaamini Sheria hii italeta mabadiliko makubwa kwenye Sekta ya Uendeshaji wa Viwanja vya Ndege.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kuhusu Air Tanzania, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, Air Tanzania itakwenda maeneo yote ya nchi yetu. Tunajenga viwanja vya ndege vya kisasa na tunahakikisha Viwanja vyote vya ndege vya kisasa vinavyojengwa, vitakuwa na taa ili ndege ziweze kwenda masaa 24 kwa siku. Hivi tunavyotegemea, mwisho wa mwezi huu tutapata ndege moja ambayo itaongeza ndege tulizonazo na tutaongeza ufanisi wa Air Tanzania katika maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi wa nne Mungu akitujaalia tutapata ndege nyingine ya Dream Liner ambayo pia itaongeza ufanisi na usafiri katika maeneo mbalimbali hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2016
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii kuchangia Muswada ulioko mbele yetu. Kwanza kabisa, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu kwa kuwasilisha vizuri na naunga mkono hoja iliyoko mbele yetu kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mawili nataka kuchangia. La kwanza, ni kuhusu Marekebisho katika Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Sura ya 413 kwa kuongeza kifungu kipya cha 40A ili kuweka masharti yanayohusu ulipwaji wa faini pale mkosaji anapokiri kosa badala ya kumpeleka Mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu huu una faida kubwa, kwanza unaondoa tatizo la kwenda Mahakamani ambapo baadhi ya wakati kesi zinachukua muda mrefu. Pili, utaratibu huu unapunguza sana gharama za kuendesha kesi huko Mahakamani. Utaratibu huu unatumiwa na wadhibiti wengi, kwa mfano TCRA na EWURA na unafanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka kuzungumzia machache kuhusu Ibara ya 35 ya Muswada inayopendekeza kurekebisha kifungu cha 11(6) kwa kuainisha kuwa adhabu ya kosa la leseni za usafirishaji chini ya kifungu hicho sasa itakuwa shilingi laki mbili kwa kosa la kwanza na utakaporejea kosa kiwango hicho sasa kiwe si zaidi ya shilingi laki tano. Sheria ya zamani ya Leseni ya mwaka 1973 ilikuwa inatoa faini ya shilingi elfu kumi kiwango cha chini na kiwango cha juu ilikuwa ni shilingi elfu hamsini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili lina faida kubwa sana, kwanza ni kuweka viwango vya faini vinavyoendana na wakati. Viwango vya mwaka 1973 vimedumu kwa muda wa miongo minne na hivyo vimepitwa na wakati. Kwa mfano, shilingi elfu kumi mwaka 1973 ilikuwa sawa na dola za Kimarekani 1,400/= kwa exchange rate ya Dola moja shilingi saba. Kama utachukua faini hiyo leo itakuwa sawa na shilingi milioni 3. Hata hivyo, kwa kutambua changamoto zilizopo sisi tumeweka kiwango cha chini kuwa ni shilingi laki mbili na cha juu kisizidi shilingi laki tano ambapo tunaamini kabisa kiwango kama hiki kitapunguza sana ajali za mabasi barabarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzoefu unaonesha nchi ambazo wana faini kali pamoja na kutoa elimu na kutumia teknolojia ya kisasa hasa TEHAMA kwa kiasi kikubwa zimefanikiwa kupunguza ajali za barabarani. Kwa hiyo, nasi kwa kuweka faini hizi pamoja na kutumia teknolojia ya kisasa ya TEHAMA na kuendelea kutoa elimu kwa watu wanaotumia vyombo hivyo tutapunguza kwa asilimia kubwa sana ajali za barabarani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, marekebisho haya yanayopendekezwa yanalenga kuhuisha adhabu ambazo zitatolewa kwa watoa huduma watakaofanya biashara bila ya kuwa na leseni au wale watakaokiuka masharti ya leseni. Kwa mfano, gari la abiria lenye leseni linatakiwa liwe na hali ya usalama na ubora, kama gari haliko kwenye hali ya usalama itabidi walipe faini hiyo. Mfano mwingine, dereva wa gari la abiria anayeajiriwa anatakiwa awe na sifa zinazostahili kwa ajili ya kuendesha gari hilo, kama dereva huyo hana leseni sheria hii itatumika na mengine mengineyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naomba niongelee mabadiliko ya sheria kuhusu usafiri wa anga. Kwenye usafiri wa anga tunataka kufanya mabadiliko hayo, ili kuleta usalama.
MWENYEKITI: Ahsante.
Muswada wa Sheria ya Viwanja vya Ndege Tanzania ya Mwaka 2024
WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru tena Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujalia afya na kutuwezesha kukutana tena na kujadili hoja hii iliyowasilishwa muda mfupi uliopita.
Mheshimiwa Spika, natumia fursa hii pia kukushukuru wewe binafsi. Aidha, nachukua fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa wawazi na kutoa michango yao ya kina wakati wa kujadili hoja hii. Nithibitishe kwamba michango yao yote tumeichukua kwa uzito mkubwa na tunakwenda kuifanyia kazi ili kuhakikisha kwamba sekta ya anga inakua kwa mujibu wa mipango tuliyoiweka.
Mheshimiwa Spika, naomba pia kipekee nimshukuru Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mheshimiwa Suleiman Moshi Kakoso na Waheshimiwa Wabunge wote wa Kamati ya Kudumu ya Miundombinu kwa hoja nzuri zilizotolewa na Kamati yao. Nakiri kwamba hoja hizi ni muhimu sana kwa maendeleo na ukuaji wa miundombinu na huduma za usafiri wa anga hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya na uongozi wote wa Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya pamoja na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege.
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nianze kuhitimisha hoja yangu kwa kutoa ufafanuzi wa kijumla na mfupi kuhusu hoja mbalimbali zilizowasilishwa. Kama nilivyosema wakati nawasilisha hoja hii, lengo la kutungwa kwa sheria hii ni kuweka mfumo madhubuti na thabiti wa kisheria wa usimamizi, uendeshaji na uendelezaji wa viwanja vya ndege hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, aidha, Muswada huu unakusudia kutatua changamoto mbalimbali za usimamizi, uendelezaji na uendeshaji wa viwanja vya ndege ambapo hapo zamani ilipokuwa Wakala wa Viwanja vya Ndege ilikuwa TAA inakumbana nazo. Pia kuna changamoto nyingi ambazo leo zinaukabili usafiri wa anga. Kwa mfano, kumekuwepo na changamoto kwenye usimamizi wa viwanja vya ndege, kumekuwa na ubadilikaji wa kila mara wa Kanuni na usafiri wa anga na itifaki za usalama duniani.
Mheshimiwa Spika, leo ukienda kwenye viwanja vya ndege, kama alivyosema, unaambiwa uvue viatu, ufanye nini, ni kwa vile kulikuwa na hayo mabadiliko na yataendelea kuwepo kulingana na jinsi teknolojia inavyokua. Tunaamini kwamba changamoto hizi zote zitaweza kutatuliwa na sheria hii. Sheria hii inayopendekezwa pamoja kanuni na miongozo, itawezesha usimamizi mzuri wa viwanja vya ndege hapa nchini pamoja na uboreshaji wa usalama katika viwanja vyetu vya ndege.
Mheshimiwa Spika, pia kuna changamoto, kuna matarajio makubwa ya abiria wanaotumia huduma za ndege, kuanzia wanapoingia kwenye viwanja vya ndege, wanapopanda ndege na mpaka wanapopokea mizigo yao. Sasa hivi abiria anataka akishuka tu kwenye ndege, mzigo wake aukute pale. Haya yote yanaweza kukamilika au kutatuliwa kama tutakuwa na sheria, kanuni, na miongozo mizuri.
Mheshimiwa Spika, kama tutaweka mifumo mizuri ya kigitali, tunaamini kwamba abiria watapata huduma bora na huduma ambayo imetukuka. Kwa hiyo, sheria hii ni muhimu, na tunaamini kwamba sheria hii itaweza kutatua changamoto hizo.
Mheshimiwa Spika, pia kuna tatizo kubwa la miundombinu. Kama tunavyofahamu, upanuzi au uboreshaji wa miundombinu ya viwanja vya ndege kunahitaji uwekezaji mkubwa. Changamoto hii ya kupata fedha na ujenzi wakati wa utumiaji wa viwanja vya ndege, iko haja ya kupata sheria ambayo itashirikisha kwa kiasi kikubwa sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, tunaamini kwamba ushirikishwaji wa sekta binafsi ambao sheria hii inapendekeza, utaweza kuboresha huduma za usafiri wa anga hapa nchini, utaweza kuboresha utendaji wa sekta ya anga hapa nchini, na utaweza kuboresha huduma ya uendeshaji wa viwanja vya ndege. Tunaamini kwamba baadhi ya viwanja vya ndege tukishirikiana na sekta binafsi, huduma zitakuwa nzuri na wananchi watapata huduma ambayo ni bora zaidi.
Mheshimiwa Spika, naomba nijikite kwenye maeneo mawili ambayo Kamati pamoja na wachangiaji wote wamewasilisha hapa. Eneo la kwanza ni eneo la kitengo cha zimamoto. Tunakubaliana na Kamati na Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kuhusu jambo hili. Kama Kamati ilivyosema, tutakaa sisi Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Ulinzi halafu tutafanya upembuzi yakinifu kuona jinsi gani jambo hili tutaweza kulisimamia
Mheshimiwa Spika, lakini tunaomba Waheshimiwa Wabunge wasisahau kwamba maoni ya Tume ya Hakijinai ilielekeza kwamba Idara ya Zimamoto sasa ipelekwe huko halmashauri, kwa vile tutakaa pamoja sote tuone tutalifanyaje jambo hili kwa maslahi mapana ya usalama wa viwanja vya ndege hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo limezungumzwa sana ni kuhusu Passenger Service Charges. Kama Kamati ilivyoeleza na Waheshimiwa walivyozungumza, Wizara ya Fedha, Wizara ya Uchukuzi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu tutakaa pamoja, tuzungumze jambo hili tuone jinsi gani ambavyo tutaweza kulitatua ili service charge hiyo iweze kubaki kwenye viwanja vya ndege. Ninavyozungumza sasa hivi, service charge kwa mwaka ni takribani shilingi bilioni 70.
Mheshimiwa Spika, wakati huo huo Serikali tumewekeza fedha nyingi kwenye kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege hapa nchini. Kwa mfano, Uwanja wa Msalato ambao kuna Phase I na Phase II; Phase 1 ni ujenzi wa runway, na Phase II ni ujenzi wa jengo la abiria. Tunatumia takribani shilingi bilioni 360, na uwanja huo hasa ile runway tunategemea mwezi Oktoba utakamilika na tutaanza kufanya safari za ndege kupitia Kiwanja cha Ndege cha Msalato. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa fedha, kwa mfano Uwanja wa Ndege wa Musoma tumetumia au tunaendelea kutumia takribani shilingi bilioni 36.63; Shinyanga tunatumia takribani shilingi bilioni 49.197; Iringa kama alivyosema Mheshimiwa Ritta, pale tumetumia takribani shilingi bilioni 63. Huko Songwe tumejenga jengo zuri la abiria na tumetumia takribani shilingi bilioni 28.87; huko Mtwara, uwanja wa ndege tayari Phase I tumeshatumia taribani shilingi bilioni 56.993.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunaenda kujenga jengo la abiria ambapo tutatumia takribani shilingi bilioni 70 na mkandarasi tumeshampata. Huko Lindi kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunakwenda kujenga runway pamoja na jengo la abiria ambapo tutatumia takribani shilingi bilioni 130.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, Serikali tunatumia takribani shilingi trilioni 1.1 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya viwanja vya ndege hapa nchini. Niendelee kusema tena kwamba tumepokea maoni ya Waheshimiwa Wabunge pamoja na Kamati yetu na tutakwenda kukaa ili tuweze kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, naomba tena kutoa hoja.