Answers to Primary Questions by Hon. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (24 total)
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-
Barabara ya Butengo Lumasa – Iparamasa – Mbogwe – Masumbwe ni barabara muhimu sana kwa maendeleo ya wananchi wa Wilaya ya Mbogwe na Mkoa wa Geita kwa ujumla:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuifanyia usanifu wa kina na upembuzi yakinifu barabara hii na hatimaye kuijenga kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Butengo Lumasa – Iparamasa – Mbogwe hadi Masumbwe yenye urefu wa kilometa 95 ni barabara ya mkoa inayounganisha barabara kuu za Isaka – Lusahunga na Usagara – Biharamulo na pia inaunganisha Wilaya za Mbogwe na Chato.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa sasa haijafikiria kuiingiza barabara hii katika mpango wa kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na hatimaye kuijenga kwa kiwango cha lami barabara hii. Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Geita inaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii kadri ya upatikanaji wa fedha ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2014/2015 jumla ya shilingi milioni 100 zilitumika katika matengenezo ya kawaida na katika mwaka 2015/2016 kiasi cha shilingi milioni 300 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya kawaida na shilingi milioni 345 zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa barabara hiyo na kazi zinaendelea.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR (K.n.y. MHE. BAHATI ALI ABEID) aliuliza:-
Simu fake zimezimwa kwa sababu ya madhara ya kiafya kwa Watanzania.
(a) Je, wananchi wanaoendelea kuzitumia kwa matumizi mengine hazitawaletea madhara ya kiafya?
(a) Kama zina madhara, je, Serikali haioni kuwa sasa ni wakati muafaka wa kutoa elimu kwa umma?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Ali Abeid, Mbunge wa Mahonda, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuwepo kwa Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010 na Kanuni za EPOCA za mwaka 2011 zimewezesha kutekelezwa kwa mfumo rajisi wa namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi ambayo ilipelekea kuzimwa kwa simu zenye namba tambulishi bandia ilipofika tarehe 17 Juni, 2016.
Mheshimiwa Spika, mfumo huu wa kielektroniki ulizinduliwa rasmi tarehe 17 Disemba, 2015 na unahifadhi kumbukumbi za namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano ya mkononi kwa lengo la kufuatilia namba tambulishi za vifaa vinavyoibiwa, kuharibika, kupotea au ambavyo havikidhi viwango (bandia) vya matumizi katika soko la mawasiliano. Namba tambulishi za vifaa vyote vya mawasiliano vya mkononi ambavyo vimeibiwa, vimeharibika, kupotea au visivyokidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano haviruhusiwi kuunganishwa kwenye mtandao wa watoa huduma tangu tarehe 16 Juni, 2016.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya utangulizi, naomba kujibu swali hili kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, wananchi wanaoendelea kutumia simu fake ama zisizokidhi viwango vya kulinda afya ya watumiaji ama zenye namba tambulishi bandia wanaweza kudhurika na matumizi yake kwani hazikutengenezwa kwa kupitia mfumo unaodhibiti simu hizo kutokuwa na kemikali hatari zinazoweza kudhuru binadamu na mazingira kwa mfano zebaki na kemikali nyinginezo.
(b) Mheshimiwa Spika, kabla na baada ya kuzima simu fake, Serikali imekuwa ikielimisha umma kuhusu tahadhari ya kutotumia simu hizo ili kuepuka madhara ambayo yanaweza kutokea kutokana na kutumia simu hizo zisizokidhi matakwa ya kulinda afya ya watumiaji. Aidha, Serikali inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu wananchi kujiepusha na matumizi ikiwa ni pamoja na kuzikusanya simu hizo na kuziteketeza kwa mujibu wa utaratibu uliopo.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA aliuliza:-
Kwa muda mrefu kumekuwepo ahadi ya kulipa fidia wananchi waliotoa maeneo yao kupisha ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Omukajunguti:-
(a) Je, ni lini wananchi wanaohusika watalipwa fidia walizoahidiwa?
(b) Je, ujenzi wa uwanja huo utaanza lini?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali ina mpango wa kujenga kiwanja kipya cha ndege katika Mkoa wa Kagera katika eneo la Omukajunguti kitakachokuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa kama Airbus 320 au Boeing 737 zenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 100 mpaka 200 kwa wakati mmoja. Eneo hilo lina ukubwa wa hekta zipatazo 2,400 linalojumuisha Vitongoji vya Mushasha, Bulembo na Bogorora. Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa uthamini wa mali za wakazi wa eneo hilo uliofanyika mwaka 2010 ulibainisha fidia ya shilingi bilioni 12.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa kutokana na fidia hizo kutolipwa kwa wakati italazimika kufanya marejeo ya uthamini wa awali kwa kuzingatia Sheria ya Ardhi husika. Hata hivyo, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetenga shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kuanza kulipa fidia kwa wananchi wa eneo hilo. Mara taratibu za marejeo ya uthamini zitakapokamilika zoezi la ulipaji fidia litaanza.
(b) Mheshimiwa Spika, ujenzi wa kiwanja cha ndege kipya katika eneo hilo upo katika mpango wa maendeleo wa muda mrefu. Ujenzi wake utategemea kuongezeka kwa mahitaji ya usafiri wa anga na kufikia ukomo wa uwezo wa kiwanga cha sasa cha Bukoba. Serikali itaendelea na maandalizi ya awali kwa ajili ya kiwanja cha ndege kipya yaani kwa kukamilisha ulipaji wa fidia, kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali ili kubaini makadirio ya gharama za uwekezaji katika kiwanja kipya.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO aliuliza:-
Kata za Wilaya ya Songwe zipo mbalimbali kwa zaidi ya kilometa 40 kutoka kata moja hadi nyingine. Iliyokuwa RCC ya Mkoa wa Mbeya ilisharidhia kupandisha hadhi barabaraya Kapalala hadi Gua na Kininga hadi Ngwala ziingie kwenye barabara za Mkoa lakini mpaka sasa hakuna utekelezaji.
Je, ni lini sasa Serikali itapandisha hadhi barabara hizo?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Phillipo Augustino Mulugo, Mbunge wa Songwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kupandisha hadhi barabaa unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Namba 13 ya mwaka 2007 na kanuni zake za mwaka 2009. Aidha, maombi ya kupandisha hadhi barabara ya Kapalala hadi Gua na Kininga hadi Ngwala kuwa za Mkoa yanaendelea kufanyiwa kazi na Wizara yangu sambamba na maombi kutoka Mikoa mingine. Mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo taarifa itatolewa na Serikali kupitia kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Songwe.
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:-
Barabara ya kutoka Kakuzi - Kapele mpaka Ilonga ina kilometa 50.6, pia inaunganisha Mkoa wa Songwe na Rukwa bado ipo chini ya Halmashauri pamoja na maombi ya kuipandisha hadhi kupitia vikao vyote ikiwemo Road Board kukubali.
Je, ni kwa nini Serikali inachelewa sana kuipandisha hadhi barabara hiyo ili ihudumiwe na TANROADS kutokana na umuhimu wake.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kupandishwa hadhi barabara unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007 na Kanuni zake za mwaka 2009. Aidha, maombi ya kupandisha hadhi barabara ya Wilaya ya Kakozi - Kapele hadi Ilonga kuwa ya Mkoa yamepokelewa na yatafanyiwa kazi na Wizara sambamba na maombi kutoka Mikoa mingine. Mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo taarifa itatolewa na Serikali kupitia kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Songwe.
MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:-
Eneo lote la Vijiji vya Delta na Mto Rufiji lina wakazi zaidi ya 30,000 na halina usikivu wa simu za mkononi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya utafiti na hatimaye kuweka minara ya simu katika Vijiji vya Ruma na Mbwera, Msala, Kiomboni, Kicheru na Kiasi?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji vya Mbwera, Msala na Kiasi vimeshapatiwa huduma ya mawasiliano kupitia utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi wa Kampuni ya Simu ya Viettel (Halotel).
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kwa kuzingatia umuhimu wa mawasiliano katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, Vijiji vya Ruma, Kiomboni na Kicheru vimeingizwa katika mpango wa pili wa mradi wa Kampuni ya Simu ya Hallotel ambao unategemea kuanza wakati wowote.
MHE. MPAKATE D. IDDI aliuliza:-
Sehemu kubwa ya Jimbo la Tunduru Kusini imepakana na Mto Ruvuma na vijiji vingi vipo pembezoni mwa mto huo, hivyo wananchi wake hupata baadhi ya bidhaa kutoka Msumbiji kwa kutumia mitumbwi ambayo siyo salama kwa maisha yao wanapovuka mto:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia kivuko wananchi wa Wenje na Makande ili waweze kuvuka Mto kwenda Msumbiji kwa usalama?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kupata mahitaji halisi ya kivuko kwa wananchi wa Wenje na Makande Wilayani Tunduru, Wizara yangu itatuma mtaalam kutafiti uwezekano wa kuweka kivuko eneo hilo. Utafiti huo utajumuisha upatikanaji wa eneo lenye kina cha maji cha kutosha kuwezesha kivuko kuelea wakati wowote wa mwaka, wakati wa masika na wakati wa kiangazi pamoja na kupata kibali cha kuweka maegesho ya kivuko upande wa Msumbiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo ya utafiti huo yatawezesha Wizara kuweka mpango wa kuweka kivuko hicho kwenye bajeti yake.
MHE. HALIMA A. BULEMBO aliuliza:-
Stesheni nyingi za reli hazina huduma nzuri kama maji, vyoo na sehemu za kukaa wakati wa mvua na hivyo abiria wengi hasa akina mama na watoto kupata shida.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuboresha huduma hizo ili kuwaondolea adha hiyo kubwa akina mama na watoto?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) ina jumla ya stesheni 124 katika mtandao wake wa reli. Aidha, kampuni ilishaanza ukarabati wa stesheni za treni ambao pamoja na mambo mengine umezingatia uboreshaji wa mifumo ya maji, vyoo na sehemu za kukaa abiria wakati wa mvua kwa kutumia vyanzo vya ndani ya mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, stesheni zilizokwisha kukarabatiwa ni Kigoma, Kaliua, Pugu, Malindi na Mwanza ambapo ukarabati kwa Mwanza bado unaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni inatambua changamoto ya ukosefu wa baadhi ya huduma katika stesheni chache za reli kutokana na kuwa na miundombinu chakavu na hivyo kuweka mpango mkakati wa kukarabati na kuboresha stesheni hizo kukidhi mahitaji ya sasa hatua kwa hatua kadiri hali ya kifedha itakavyokuwa inaruhusu.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-
Kwa muda mrefu sasa meli za mizigo za Zanzibar zimetengewa eneo maalum la kufunga gati linaloitwa Malindi Wharf (lighter key) kwenye bandari ya mizigo ya Dar es Salaam na kuna taarifa kuwa sehemu hiyo sasa inatarajia kujengwa katika upanuzi wa bandari, jambo ambalo ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu, ingawa sehemu hiyo ni muhimu sana katika kutoa huduma ya meli za upande wa pili wa Muungano (Zanzibar).
(a) Je, Serikali haioni kwamba ipo haja ya kutengwa eneo lingine maalum kwa ajili ya kufunga gati meli za mizigo za Zanzibar ili Wazanzibar waendelee kupata huduma kwenye bandari ya nchi yao?
(b) Endapo itaonekana ipo haja hiyo, je, ni sehemu gani kwenye bandari iliyopangwa kwa ajili ya meli za mizigo za Zanzibar endapo sehemu ya sasa itajengwa?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub, lenye Sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Bandari ya Dar es Salaam inafanyiwa marekebisho makubwa ikiwa ni pamoja na kujenga gati jipya katika eneo la Gerezani Creek, kupanua na kuongeza kina cha lango la meli, kupanua na kuongeza kina cha eneo la kugeuzia meli, kuimarisha na kuongeza kina cha gati kutoka Namba 1 mpaka Namba 7 na kuongeza eneo la kuhudumia shehena kwa kutumia vifaa vya kisasa.
Mheshimiwa Spika, kazi hizi zinafanywa katika sehemu ya awamu ya kwanza ya mpango wa kuboresha bandari yote ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub kwamba katika awamu hii ya kwanza maboresho yanayoendelea hayatahusisha miundombinu ya eneo la Kighter Quay, hivyo huduma zinazotolewa katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na zile za meli za mizigo za Zanzibar, zitaendelea kutolewa kama kawaida.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA aliuliza:-
Mradi wa ujenzi wa Barabara ya Singino/Kivinje maarufu kama Barabara ya Kwa Mkocho ni ahadi ya Serikali iliyotolewa na Rais Mstaafu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, karibu miaka 10 iliyopita. Aidha, kwa kipindi chote cha miaka 10 ujenzi wa barabara hiyo umekuwa wa kusuasua ingawa barabara hiyo ni kiunganishi kwa wananchi hasa wagonjwa wanaokwenda kutibiwa hospitali ya wilaya:-
(a) Je, ni nini kauli ya Serikali ya Awamu ya Tano juu ya ukamilishwaji wa ahadi hiyo?
(b) Je, Serikali inatoa maelezo gani kwa wananchi juu ya kuchelewa kukamilishwa kwa ujenzi wa barabara hiyo kwa kipindi cha miaka 10 sasa?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Said Bungara, Mbunge wa Kilwa Kusini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Singino/Kivinje – Kilwa ni barabara inayohudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa. Katika mwaka 2012, Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne aliahidi kutenga fedha kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ili barabara hiyo ijengwe kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ilisaini mkataba na kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi bilioni 1.478. Hata hivyo, mradi huo haujakamilika na mkandarasi amekimbia eneo la mradi. Wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, aliagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Lindi, kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini ya mahitaji ya fedha zinazotakiwa ili kuendelea kujenga kwa kiwango cha lami barabara hii yamefanyika na ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hii unatarajiwa kuanza pindi fedha zitakapopatikana.
MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-
Jimbo la Mlimba linakabiliwa na miundombinu mibovu ya barabara na kushindwa kupitika kipindi chote cha mwaka na hivyo kusababisha adha kubwa kwa wanawake, watoto, wagonjwa na pia wananchi kwa ujumla wanaosafirisha mazao kufuata wanunuzi na huduma za Serikali kama vile kwa Mkurugenzi wa Halmashauri, Mkuu wa Wilaya, Hospitali ya Wilaya, Mahakama na Polisi Wilayani Ifakara.
(a) Je, ni lini barabara ya Ifakara - Mlimba - Madeke - Njombe itajengwa kwa kiwango cha lami kwa kuwa upembuzi wa barabara hiyo ulishafanyika?
(b) Wakati tunasubiri barabara ya lami, je, Serikali ina mpango gani wa kuitengea fedha za kutosha barabara hiyo ili kuifanya ipitike kwa kipindi chote cha mvua na kiangazi?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Ifakara – Mlimba – Madeke yenye urefu wa kilometa 231.53 inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro. Barabara hii inaunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Njombe katika Kijiji cha Madeke. Barabara hii inapitika kwa kipindi kirefu cha mwaka ingawa kuna maeneo machache bado yanapitika kwa shida wakati wa majira ya mvua.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilishaanza maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami barabara hii ya Ifakara - Mlimba
- Madeke ambapo imeshakamilisha kazi ya usanifu wa kina wa sehemu ya barabara kati ya Ifakara na Kihansi yenye urefu wa kilometa 126 ili kuunganisha na kipande cha barabara ya lami chenye urefu kilometa 24 kilichojengwa kwa kiwango cha lami hapo awali kati ya Kihansi na Mlimba. Ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu hiyo iliyofanyiwa usanifu wa kina utaanza pindi fedha zitakapopatikana.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii kiuchumi na kijamii, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga shilingi bilioni 2.52 kwa ajili ya matengenezo ya aina mbalimbali ya barabara na madaraja ili barabara ipitike majira yote ya mwaka mpaka hapo itakapojengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI aliuliza:-
Usanifu wa Mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Miji ya Bisega, Bariadi, Itilima, Meatu na Maswa umekamilika kwa kiasi kikubwa lakini utanufaisha watu wa Maswa Mjini na baadhi ya vijiji katika Jimbo la Maswa Mashariki na kuliacha Jimbo la Maswa Magharibi bila ya maji ya uhakika:-
Je, kwa nini Serikali isichukue maji kutoka mji wa Algudu ambako tayari maji yameshafika na umbali ni mfupi ili Wananchi wa Kata za Malampaka, Mataba, Nyabubunza, Badi, Shishiyu, Masela, Sengwa, Jija, Kadoto, Mwanghondoli, Mwabayamla, Isanga, Busagi na Buchambi waweze kunufaika?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki Mbunge wa Maswa Mashariki kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali natekeleza mradi wa maji safi kutoka Ziwa Victoria kwenye Miji ya Busenga, Bariadi, Itilima, Mwanhuzi na Maswa na vijiji vilivyo kilometa 12 kutoka bomba kuu la maji. Serikali pia inatekeleza mradi wa maji safi kutoka Ziwa Victoria kwenda katika Miji ya Ngudu na vijiji vilivyo ndani ya kilometa 12 kutoka bomba kuu. Vijiji hivyo ni Runele, Ngatuli, Nyang’onge, Damhi na Chibuji. Mradi huu ulihusu ulazaji wa bomba kilometa 25 na sehemu nyingine ya bomba kuu ilitumika bomba la zamani la mrai wa visima uliojengwa miaka ya 70. Bomba hilo ni lenye kipenyo cha nchi nane na kulingana na usanifu halitoshi kupanua zaidi kwenda Malampaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikal kupitia programu ya maendeleo ya sekta ya maji imetekeleza miradi ya maji ya Malampaka, Sayusayu, Mwasayi, Njiapanda na Sangamwalugesha ambayo miradi hii imekamilika na wananchi wanapata maji safi na salama. Serikali pia imekamilisha usanifu na uandaaji wa wa makabrasha ya zabuni kwa miradi ya maji ya Mwabulindi, Mwamanege na Badi ambao utahudumia vijiji vitatu vya Muhiba Jihu na Badi yenyewe.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-
Mwezi Novemba, 2018, Waziri wa Maji alifanya ziara Wilayani Kakonko na Kibondo na kukagua miradi ya maji iliyokwisha tumia zaidi ya shilingi bilioni moja lakini haifanyi kazi:-
Je, ni lini miradi hiyo itakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII (K.n.y. WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika Miradi ya Maji ya Muhange, Kiduduye na Nyangwijima iliyopo Wilaya ya Kakonko baada ya kujengwa na kukamilika kulijitokeza changamoto zilizosababisha chanzo cha maji cha Mradi wa Muhange kujaa tope na kusababisha kazi ya kuondoa tope mara kwa mara. Aidha, katika Miradi ya Maji ya Kakonko, Nyabibuye na Gwanumpu sababu kubwa zilizosababisha miradi hiyo kutokamilika kwa wakati ni uwezo mdogo wa fedha kwa wakandarasi waliotekeleza ujenzi wa mradi huo.
Mheshimiwa Spika, katika kutatua changamoto zilizojitokeza katika Miradi ya Maji ya Muhange, Kiduduye na Nyagwijima, Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko kwa kushirikiana na Mkoa wa Kigoma imefanya mapitio ya usanifu wa miradi na kupendekeza namna ya kuboresha miundombinu na kutatua changamoto zilizopo ambapo gharama za kufanya marekebisho ya miundombinu ya vyanzo vya maji (intake structures) imekadiriwa kuwa shilingi milioni 373.99. Serikali itatoa fedha hizo ili kuhakikisha marekebisho hayo yanafanyika kwa upande wa Miradi ya Maji ya Kakonko, Gwanumpu na Nyabibuye. Halmashauri imechukua hatua kwa wakandarasi wanaochelewesha miradi kwa kuwaandikia barua ya kusudio la kuvunja mikataba endapo watashindwa kukamilisha miradi kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, miradi iliyotekelezwa kipindi cha miaka mitano, miradi hiyo imetekelezwa katika Vijiji vya Nyankwi, Nyabitaka, Kibingo, Kagezi na Minyima. Miradi ya Maji ya Nyankwi, Nyabitaka na Kibingo inafanya kazi na Jumuiya za Watumiaji Maji (COWSO) zimekabidhiwa kuendesha na kusimamia miradi hiyo. Serikali itaendelea na marekebisho yaliyojitokeza katika Miradi ya Kagenzi na Minyinya ili iweze kutoa maji kwa wakati.
MHE. ANTONY C. KOMU aliuliza:-
Serikali imetekelza mradi wa maji katika Kata ya Mbokomu lakini maji mengi yanavuja barabarani na kusababisha kukosekana kwa maji maeneo mengi ya mradi kama vile vijiji vya Korini Kusini, Kiwalaa na Korini Kaskazini.
Je, kwanini Serikali isihakiki ukamilifu wa mradi huo na kufanya marekebisho ikiwa ni pamoja na kubainisha waliohusika na kasoro zitakazobainika na kuwachukuliwa hatua stahiki?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Antony Komu, Mbunge wa Moshi Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mradi wa maji Korini ni moja ya miradi ya maji katika vijiji sita iliyotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi kupitia Awamu ya I ya program ya maendeleo ya sekta ya maji na ulikamilika tarehe 31 Julai, 2014 ukiwa unahudumia wananchi wapatao 10467 wa Vijiji vya Korini Juu, Korini Kati na Korini Kusini.
Mheshimiwa Spika, wakati mradi huu unaanza kutekelezwa kulikuwa na mradi wa maji wa zamani ambao ulikuwa unahudumia Kata hii ambayo ni mradi wa maji wa Mbokomu Mashariki na mradi wa maji wa Mbokomu Magharibi. Katika kipindi cha Septemba mwaka 2018 kulikuwa na ukarabati wa barabara kwenye Kata ya Mbokomu ambao ulisababisha bomba la maji la mradi wa zamani kuharibiwa na mtambo wa kutengeneza barabara na kusababisha maji kuanza kuvuja barabarani. Hata hivyo, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Moshi kwa kushirikiana na Mkandarasi wa barabara waliweza kukarabati na kumaliza tatizo la uvujaji maji barabarani kwa gharama ya shilingi milioni 1,437,000,000.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Wizara ya Maji ilikubali kurekebisha mchoro wa Mradi wa Maji kutoka Mto Ruvuma hadi Mtwara ili vijiji vingi vya Halmashauri ya Nanyamba vipate maji toka Mto Ruvuma:
(a) Je, marekebisho hayo yamefikia hatua gani?
(b) Je, ni vijiji vingapi vya Halmashauri ya Mji wa Nanyamba vitanufaika na mradi huo
(c) Je, ni lini mradi huo utaanza kutekelezwa?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, lenye sehemu (a), (b) na (c), kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali ilikubali kufanya marekebisho ya mchoro wa Mradi wa kutoa Maji kutoka Mto Ruvuma kwenye Manispaa ya Mtwara Mikindani ili kuongeza idadi ya vijiji zaidi vikwemo vya Halmashauri ya Nanyamba.
Mheshimiwa Spika, usanifu wa mradi huo ulishakamilika, hivyo, mabadiliko ya mchoro yatafanyika wakati wa utekelezaji wa mradi huo kabla ya kuanza kwa ujenzi wa kazi hiyo. Idadi ya vijiji vitakavyoongezwa itajulikana baada ya mabadiliko ya mchoro yatakayofanywa na Mtaalam Mshauri atakayesimamia ujenzi wa mradi huo.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa mradi huo unakadiriwa kugharimu kiasi cha Dola za Marekeni milioni 189.9. Kwa sasa Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha za utelekezaji wa mradi huo na unategemea zaidi upatikanaji wa fedha ili kazi iweze kuanza.
MHE. LUCY S. MAGERELI aliuliza:-
Ujenzi wa chujio la maji katika Bwawa la Manchira, ambalo ni chanzo pekee cha maji katika Mji wa Mugumu, Wilayani Serengeti umechukua muda mrefu sana na kusababisha wananchi kukosa amani na kupata maji yasiyokuwa na ubora kwa matumizi ya binadamu:-
(a) Je, Serikali ina kauli gani juu ya ujenzi wa chujio hilo na lini litakamilika?
(b) Je, ni lini Serikali itakamilisha mfumo wa usambazaji maji toka Bwawa la Manchira ili kuwafikishia wananchi wote wa Mji wa Mugumu na maeneo ya jirani huduma ya maji?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli ujenzi wa chujio katika Bwawa la Manchira umechukua muda mrefu, sababu kuu ikiwa ni upungufu uliojitokeza katika usanifu wa chujio na udhaifu katika uwezo wa kifedha wa mkandarasi aliyekuwa anatekeleza mradi huo. Kutokana na mwenendo usioridhisha wa utekelezaji, Wizara na kuzingatia ushauri wa kitaalam mnamo tarehe 8/1/2020 iliamua kuvunja mkataba wa ujenzi wa chujio hilo.
Mheshimiwa Spika, Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) na Mugumu (MUGUWASA), zimeelekezwa kutathimini na kupitia gharama zinazohitajika ili kukamilisha ujenzi wa chujio hilo kwa kutumia wataalam wa ndani (Force Account). Wizara itatoa fedha zitakazohitajika kukamilisha ujenzi wa chujio hilo linalohudumia Mji wa Mugumu.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wote wa Mji wa Mugumu na maeneo ya jirani, Serikali kupitia fedha za mkopo kutoka India, itakarabati na kupanua mtandao katika Mji wa Mugumu. Usanifu wa awali umefanyika ambapo kazi zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa matenki mawili ya kuhifadhia maji yenye ujazo wa mita 5,000 na 500, ulazaji wa bomba zenye vipenyo mbalimbali zenye urefu wa kilomita 200 na kutoka urefu wa sasa wa kilomita 42 na ukarabati mkubwa wa bomba za sasa na uboreshaji wa chujio.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Serikali ilishasema kwamba itatoa fedha ili maji yanayozalishwa na Mradi wa Maji BUWASA (Bukoba Water Supply and Sanitation Authority) yaweze kufika vijijini katika Kata za Maruku, Kanyangero, Kabaragaine, Katoma na Nyakato:-
Je, ni lini mradi huu utaanza kutekelezwa?
WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha wananchi wa Manispaa ya Mji wa Bukoba wanapata huduma ya majisafi na salama, mwaka 2016, Serikali ilikamilisha ujenzi wa mradi mkubwa wa maji. Aidha, baada ya kukamilisha mradi huo, Serikali imetoa fedha kwa ajili ya upanuzi wa mtandao wa maji ili wananchi wa maeneo ya Kata za Kibeta, Kagondo, Ijuganyundo na baadhi ya maeneo ya kata za Kahororo, Kashai, Nshambya na Nyaga waweze kunufaika kupitia mradi huo. Kwa sasa upanuzi huo umefikia asilimia 95. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kupeleka maji katika Kata za Maruku, Kanyangereko na Karabagaine.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Kata ya Katoma, Wizara kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) imefanya usanifu ili kutumia Mto Kyeiringisa kama chanzo cha maji katika eneo hilo na Kata ya Nyakato itanufaika kupitia upanuzi wa awamu ya pili ya mtandao wa maji wa mradi mkubwa wa Manispaa ya Bukoba.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: -
Wilaya ya Urambo inakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji hadi Serikali ikaingiza Wilaya hii katika mpango mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria, wakati wananchi wa Urambo wakisubiri mpango huo wa maji kutoka Ziwa Victoria:-
Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi ya kuchimba visima 30 katika Wilaya ya Urambo?
WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margareth Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na uhaba wa maji, Halmashauri ya Wilaya ya Urambo ilisaini Mkataba na uliokuwa Wakala wa Uchimbaji Visima (DDCA) tarehe 26 Machi, 2018 wa gharama ya Shilingi milioni 620.9 kwa ajili ya kuchimba visima 30 katika Vijiji vya Ussoke Mjini viwii; Itundu viwili; Kasisi viwili; Kiloleni viwili; Tulieni kimoja; Machinjioni kimoja; Ulassa B kimoja; Ifuta viwili; Ugalla viwili; Uyogo viwili; Nsenda viwili; Unzali viwili; Vumilia viwili; Kalembela viwili; Ussoke Mlimani viwili; Katunguru viwili; na Kapilula kimoja.
Mheshimiwa Spika, utafiti wa maeneo ya uchimbaji wa visima hivyo umekamilika na mradi huu utatekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ambapo unatarajiwa kufanyika mwezi Mei, 2020.
Mheshimiwa Spika, vilevile, Wilaya ya Urambo kupitia Mpango wa Matokeo (PforR) imepanga kuchimba visima virefu 18 ili kupunguza tatizo la uhaba wa maji katika Vijiji vya Isongwa, Kichangani, Milambo, Ulassa A, Kamalendi, Mtakuja, Sipungu, Tumaini, Ukwanga, Itegamatwi, MotoMoto, Kalembela, Usoke Mlimani, Usoke Mjini, Itebulanda, Tebela, Kasisi na Vumilia. Utekelezaji wa kazi hiyo unatarajiwa kuanza mwezi Aprili, 2020.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka maji katika Kata za Kwai, Kilole, Kwekanga na Makanya katika Jimbo la Lushoto?
WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Jimbo la Lushoto kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutatua tatizo la maji katika Wilaya ya Lushoto, Serikali tayari imekamilisha miradi ya Maji katika vijiji vya Mlalo/Mwangoi, Mlalo/Lwandai, Malibwi na Ngulu. Wananchi katika vijiji hivyo tayari wanapata huduma ya majisafi na salama na miradi mingine ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa, Kata ya Kwai kuna mradi wa maji unaotoa huduma katika Kijiji cha Kwai. Aidha, Kata ya Kwai na Makanya zipo kwenye mpango wa muda wa kati wa utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji utakaotoa huduma ya maji katika vijiji 16 ambapo usanifu wake ulikamilika na kupata kibali cha utekelezaji. Mradi huo, umepangwa kutekelezwa katika mwaka ujao wa fedha wa 2020/2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Kata ya Kilole, Kwekanga na Makanya Wizara imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 57 kwa ajili ya kufufua visima vifupi vilivyopo ambavyo havifanyi kazi. Kazi hii itafanyika kupitia mpango wa malipo kwa matokeo (Payment by Results). Tayari vifaa vya ujenzi wa miradi hiyo vimenunuliwa na utekelezaji wa mradi unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Aprili 2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa kuwaondolea adha ya upatikanaji wa maji wananchi, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.18 kwa Halmashauri ya Lushoto ili kukamilisha miradi inayoendelea kutekelezwa katika vijiji vya Shume, Manolo, Madala, Gologolo, Ngwelo ambayo itahudumia jumla ya watu 48,781.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wadau wote wanaotumia rasilimali ya maji katika shughuli zao wanashiriki pia kikamilifu kuhifadhi vyanzo vya maji ikiwemo misitu, mabonde na ardhi?
WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya, Mbunge wa Jimbo la Kaliua kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha vyanzo vya maji vinahifadhiwa, Wizara imeweka utaratibu mbalimbali ili kuhakikisha wadau wote wanaotumia rasilimali ya maji katika shughuli zao wanashiriki kikamilifu kuhifadhi vyanzo vya maji ikiwemo misitu, mabonde na ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu hizi ni pamoja na kuweka muundo wa kitaasisi wa usimamizi wa rasilimali za maji ambao unashirikisha watumia maji kupitia vyama vya watumia maji, utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na. 11 ya 2009 sambamba na sheria ya nyingine zinazohusika katika utunzaji wa vyanzo vya maji na kuandaa na kutekeleza mipango ya pamoja ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji nchini.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE Aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya kuanzia Matai kwenda Kasesya border inayounganisha nchi yetu na nchi ya Zambia?
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege Mbunge wa Kalambo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kazi ya Upembuzi yakinifu, Usanifu wa Kina na Uandaaji wa Nyaraka za Zabuni wa Barabara ya Matai - Kasesya yenye urefu wa kilomita 50 imekamilika. Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ipo katika hatua za mwisho za manunuzi kwa ajili ya kumpata Mkandarasi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa kilometa 25 sehemu ya Matai – Tatanda ambapo rasimu ya mkataba imepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali tarehe 27 mwaka huu kwa ajili ya kupata ridhaa (vetting) ili mkataba uweze kusainiwa. Aidha, Serikali kupitia TANROADS iko kwenye maandalizi ya kutangaza zabuni ya kazi ya ujenzi kwa sehemu iliyobaki ya kutoka Tatanda – Kasesya yenye urefu wa kilometa 25. Zabuni itakuwa imetangazwa kabla ya mwezi Juni mwaka huu.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza: -
(a) Je, ni lini Serikali itajenga air traffic control tower yenye urefu wa kutosha kumuwezesha muongoza ndege kuona miundombinu yote ya runway, taxiways na maegesho ya ndege katika Uwanja wa Ndege wa Mtwara?
(b) Je ni lini Serikali itajenga jengo la muda la abiria lenye ukubwa wa kutosha wingi wa abiria wanaoingia na kutoka katika uwanja huo?
(c) Je, ni lini parking shade ya mitambo ya zimamoto na uokoaji itajengwa katika eneo lililopangwa kwenye master plan?
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu: -
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mhe. Anastazia James Wambura wa Viti Maalum lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kiwanja cha Ndege cha Mtwara kilijengwa na kuanza kutoa huduma katika mwaka 1952/1953. Kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya kiwanja hiki yanayotokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii katika Mikoa ya Kusini, Kiwanja hiki kilihitaji kufanyiwa maboresho makubwa. Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), iliandaa Mpango Kabambe (Master Plan) uliopendekeza kupanua kiwanja hiki kutoka daraja Code 3C kwenda Code 4E (kwa mujibu wa ICAO). Kiwanja kitakapokamilika, kitakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa za ndani na nje ya nchi zenye ukubwa wa Boeing 787-8 (Dreamliner).
Mheshimiwa Spika, Uboreshaji wa Kiwanja hiki umegawanywa katika awamu mbili, ambapo kwa sasa ujenzi unaoendelea ni wa awamu ya kwanza unaohusisha baadhi ya kazi zikiwemo urefushaji wa njia ya kuruka na kutua ndege (runway), ujenzi wa maegesho mapya ya ndege (Apron) na barabara zake za maingilio (taxiway).
Mheshimiwa Spika, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Ujenzi wa mnara wa kuongozea ndege (Air Traffic Control Tower), Jengo la abiria (Airport Terminal Building) na kivuli kwa ajili ya maegesho ya mitambo ya zimamoto (Fire Fighting Equipment Shade) vitajengwa katika awamu ya pili mara baada ya kumalizika kwa awamu ya kwanza.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza:-
Je, lini Serikali itawalipa fidia Wananchi waliopisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege Nachingwea?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI K.n.y. WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea na jitihada mbalimbali katika kuhakikisha suala la ulipaji fidia kwa wananchi wanaopisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Nachingwea linakamilika. Aidha, hatua ya awali ya kutambua wafidiwa na mali zao imekamilika uwandani na tayari maombi ya fedha hizo za fidia yamewasilishwa Wizara ya Fedha, kwa ajili ya ulipaji. Vilevile, Serikali itahakikisha kuwa, wananchi wote wanaopisha maeneo yao, kwa ajili ya upanuzi wa Kiwanja hicho wanalipwa fidia zao stahiki. Ahsante.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua kipande cha Reli kuingia Uwanja wa Ndege wa KIA kwa ajili ya kusafirisha Mizigo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI K. n. y. WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TRC imeendelea kuboresha miundombinu ya reli iliyopo, ikiwa ni pamoja na kufufua njia za reli zilizokuwa zimefungwa. Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024, TRC imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 23 kwa ajili ya ukarabati wa njia ya Reli ya Kaskazini ikiwemo kipande cha njia ya Reli ya kuingia uwanja wa Ndege wa KIA na kwa sasa shirika linaendelea na taratibu za manunuzi ya reli nzito za ratili 80 kwa yadi kwa ajili ya matengenezo ya njia hiyo, ahsante.