Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Augustine Philip Mahiga (4 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie muda uliobakia kujibu baadhi ya maswali ambayo nimeyasikia kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, ni lile linalohusu haki za Wapalestina na watu wa Western Sahara. Katika hotuba yangu nimesema misingi ya Tanzania katika Jumuiya ya Kimatifa ni kuheshimika, kuthamini utu na kulinda uhuru. Kama hilo ndio letu inafuata kwamba wale ambao wamenyimwa uhuru, wamenyimwa utu, lazima washughulikiwe na wapate haki zao. Sasa sisi kama Tanzania lazima tufanye mambo matatu; la kwanza, tutambue kutokuwepo kwa haki hizo kwa watu huku duniani maana yake kama tunalitaka sisi na tunataka wenzetu wapate na hilo hatuwezi kuliacha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sisi wenyewe Tanzania tumesema ili hilo lipatikane lazima iwe ni diplomasia ya siasa na diplomasia ya siasa kusaidia nchi moja au nyingine inapatikana kwenye majukwaa ya kimataifa. Utazungumzia uhuru na haki na heshima ya Wapalestina au ya Western Sahara kwenye majukwaa muda umepita. Wakati ambapo kutetea haki za Afrika Kusini au Msumbiji au Namibia tulisema tutatumia silaha hatutumii silaha tena, tunasema tutaongea na moja ya silaha zetu ni kwamba tutashiriki kikamilifu katika mijadala ya kimataifa katika majukwaa mbalimbali kuhusu suala la Palestina na suala la POLISARIO. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati huo huo tuna diplomasia ya uchumi; wagomvi wa Palestina ni wa Israeli. Sasa hawa wa Israeli katika diplomasia ya uchumi kuna vitu pale tunaweza kuvipata na sisi tumesema hayo yanayozungumza kuhusu haki za wa Palestina tuyapeleke kwenye vikao, majukwaa ya kimataifa, Tanzania ni peke yake ilikuwa nchi ya kwanza kuipa Palestina diplomatic status hakuna nchi nyingine. Hiyo baada ya Mwalimu Arafati ondoa majeshi yako Uganda alipoondoa majeshi Uganda wakati wa vita akasema tutawapa diplomatic status. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ni watu wa kwanza na nilifanya makusudi kwamba Trump anapokwenda kufungua Jerusalem mimi nafungua Tel Aviv kwa sababu hilo ni kutambua kwamba Jerusalem ni mji wa utata. Nilipokwenda kule kwa makusudi nilisema nipelekeni Gaza Strip pale kwenye kivuko nikaona pale na nimewaambia Waisrael kimacho macho nikasema this is a time bomb lazima muishughulikie suala hili tulizungumze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika resolutions 12 za Umoja wa Mataifa kuhusu Palestina na kuhusu Israeli nimewaambia pande zote mbili na umoja wa Mataifa wanakubali kwamba tukae tutazame kwamba kuna resolution nyingine zimepitwa na wakati na tufanye zoezi hilo tutazame lakini hatutaweza kuacha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kabwe leo katika hotuba yangu nimeanza na aya inayosema POLISARIO na imeishia maneno ya POLISARIO sijawasahau. Ni kweli kwamba suala hili linazungumzwa mbele ya Umoja wa Mataifa, lakini maadam tumewaambia Morocco warudi ndani ya Afrika suala hili litaongezewa tija zaidi kama pia Afrika itachangia. Nadhani suala hili sio rahisi kihivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, wakati huo huo Morocco ni nchi yenye uchumi mkubwa ya tano ndani ya Afrika, sio uwanja tu wa ndege au uwanja wa mpira au stadium, lakini kuna maeneo hasa katika diplomasia ya kutengeneza mbolea na utalaam na mafunzo ambavyo tunaweza kupata. Hiyo haitatuzuia katika majukwaa yote Afrika and non-aligned countries au Umoja wa Mataifa kuwaambia jamani hili suala tulishughulikie kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la diplomasia ya uchumi uliojikita kwenye viwanda ili uwe na viwanda na vinavyofanya kazi kuna mambo manne muhimu. La kwanza, ni mtaji lazima kupata investors tupate pesa, kama zinatoka hapa au zinatoka nje. La pili, huwezi kuwa na viwanda kama huna energy, nishati ya kutosha, huwezi kuwa na viwanda kama huna miundombinu mizuri na huwezi kuwa na viwanda kama huna wataalam wanaoshika ule umeme na kufunga na kufungua wale watalii wataalam na hatimaye lazima uwe na soko. Sisi katika kuandaa vijana wetu tumesema hayo unapokwenda kule, hayo ndio uyafuate matano utafute pesa, mtafute wawekezaji, kwenye miundombinu, mtafute watakaoshiriki katika nishati, watakaoweza kutoa mafunzo na masoko ambayo lazima tuwe nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hili linaingia katika kutayarisha vijana wetu wanaokwenda nje kwa miaka miwili tumekuwa tunarudisha watu kuna wengine walikuwa wanakaa miezi na miezi, miaka na miaka hawarudi, tumehakikisha kwamba Balozi zote zinatazamwa na tunarudisha watu. Kurudisha watu ni fedha nyingi sana, tumerudisha 109 katika miaka miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaandaa kupeleka vijana ambao wanafanana na haya matano niliyoyasema. Tayari tumeshawatambua na sasa hivi tuko katika ngazi ya upekuzi, lazima wapekuliwe na vyombo vinavyohusika kabla hatujawapeleka. Natumaini hela nitakayopata kutoka bajeti hii ndio itakayotumika kuwapeleka vijana katika vituo vyote. Wote majina yao tumeshayaandaa na tunasubiri wapate kibali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Umoja wa Mataifa ulizaliwa mwaka 1945, leo una wanachama 193. Katika 193 chombo chenye nguvu kupita vyote ni Baraza la Usalama na Baraza la Usalama lina watu wa kudumu Mataifa matano Marekani, Uingereza, Ufaransa, Urusi na China. China isingeingia Security Council bila Tanzania, kabla ya mwaka 70 China ilikuwa inawakilishwa na Taiwan au Formosa au Sheing Tang Sheing lakini sisi Mwalimu akasema haiwezi kuwa Umoja wa Mataifa bila China. Hivyo ikarudi na ndio tuliiweka kule kwenye Security Council.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mageuzi ya mwisho yalifanyika mwaka 1963 kuongeza Baraza la Usalama kutoka tisa kufika 15, tangu mwaka 1963 hakujawa na mabadiliko. Sasa kuna aina nyingine ya mabadilko, kuna wale wanaosema tuingie na tupewe turufu na hao ni wakubwa Japan, Brazil, German. Ni kwamba hayo mageuzi Afrika nayo inadai ipewe haki kama hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa mchango wao. Maswali mengi nimeyapata na mengi tutayajibu kwa maandishi na haya yataleta tija sana katika kuboresha, kuna mengine ambayo lazima niseme wazi hatuwezi kuyafanya bila nyinyi kutusaidia kupitisha bajeti hii ili tuweze kuendeleza vizuri zaidi kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti naomba nichukue nafasi hii ya kuhitimisha mjadala huu wa hoja yangu kwa kutoa shukrani za pekee kwa Wabunge wote wa Bunge hili Tukufu kwa mchango wenu wa mawazo, kwa maandishi, lakini pia naamini kabisa kwamba Wizara yangu itaendelea kutegemea mawazo ya ujumla ya Bunge hili katika kutekeleza Sera zake na mipango yake ya kuendeleza uhusiano na nchi za nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa shukrani za pekee kwa Naibu Waziri wangu ambaye amemaliza tu kujibu baadhi ya maswali. Pia natoa shukrani za pekee kwa wafanyakazi katika Wizara yangu, Wakurugenzi, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu na wengine wote ambao tumeshirikiana katika kuandaa hotuba hii na kujibu maswali ambayo yamejitokeza ndani ya Bunge hili Tukufu
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru mke wangu Elizabeth Mahiga ambaye amekaa pale, ameniunga mkono na ameendelea kunifariji katika utendaji wangu wa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujibu maswali yote moja baada ya lingine lakini mengi ya maswali haya tutayajibu kwa maandishi. Nataka kusema yale ambayo ni ya msingi kuhusu Wizara hii ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni suala zima la Diplomacy ya jumla ya Tanzania, halafu nitakuja kuzungumzia Diplomacy ya uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa MWenyekiti, Diplomacy ya Tanzania ni urithi na tunu ya pekee kabisa katika Afrika; lazima tuienzi, tuidumishe na tuilinde. Ni kati ya vitu ambavyo tumerithi tangu kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wengine katika Awamu mbalimbali. Bara la Afrika na dunia inatambua hivyo. Nawaomba mkipata fursa mtembelee katika majukwaa ya Kimataifa. Kuna mikutano mingine haiwezi kuanza kama Tanzania haipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania inapotoa hotuba inasikilizwa na ulimwengu. Kama watu walikuwa wametoka kunywa chai katika mikutano ya Kimataifa, Tanzania inapoanza kuzungumza waliokuwa wanavuta sigara na kunywa chai wanarudi kwenye ukumbi. Hii ni baadhi tu ya heshima ambayo tunaipata Kimataifa na hapa katika Bara la Afrika na kwa kweli ni kitu ambacho lazima tujivunie na ni jukumu letu; na hakuna mahali pa kuenzi diplomasia ya Tanzania kama ndani ya Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa diplomasia yetu imekua na ni sahihi kabisa kwamba sasa lazima tujikite kwenye diplomasia ya kiuchumi. Diplomasia ya kiuchumi maana yake nini? Ni kweli tumekuwa na kama wimbo tunasema, diplomasia ya kiuchumi lakini ukimuuliza mtu maana yake nini na ukitoa kauli kwamba Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje haijatekeleza diplomasia ya kiuchumi si sahihi hata kidogo! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hutakuta viwanda kwenye Wizara yangu, hutakuta madini kwenye Wizara yangu, hutakuta mazao ya biashara kwenye Wizara yangu, lakini Wizara yangu ndiyo inayowezesha Wizara zote ziweze kuungana na ulimwengu katika kutekeleza Sera zao tofauti. Msione vinaelea, vimeundwa! Muundaji ni Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ndiyo inayofungua milango na madirisha ya mahusiano kati ya Serikali, sekta binafsi na Mashirika Yasiyo ya Serikali. Wizara hii ndiyo inayoratibu shughuli zote hizo. Kwa hivyo katika Economic Diplomacy Wizara inatakiwa kuleta mawasiliano kati ya Serikali nyingine, viwanda na Mashirika mengine. Kwa hivyo Economic Diplomacy ni kitu ambacho lazima kifuatiliwe kwa karibu na isiwe ni kitu cha mpito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima pia tuelewe na tufafanue na tuelewane, kwamba katika Economic Diplomacy unatengeneza framework ambayo itakuonesha dira ya wewe kama nchi kuhusiana na nchi nyingine na kama kuweka kitega uchumi ili uinufaishe nchi yako. Wizara ya Mambo ya Nje ndiyo inayofungua mlango halafu inaendelea kuratibu, hiyo ni kazi moja (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya pili ya Economic Diplomacy ni pale ambapo Tanzania inakwenda katika majukwaa ya Kimataifa na mahali kama pale unazungumza sio peke yako na wenzako. Kama ni suala la biashara, viwanda, au uwekezaji, vitu hivyo utavipata katika jukwaa na mtu wako anayekwenda pale kwenye jukwaa awe na uwezo wa kusema, kutetea na awe na uwezo wa kuwaletea nyumbani vitu kama hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuwahakikishia Wabunge kwamba diplomasia yetu hasa ya uchumi imejikita katika mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Tanzania inahesabika kama nchi ambayo uchumi wake unakua haraka kuliko nchi nyingine za Afrika, kwa asilimia saba. Sasa kama Tanzania inakua hivyo, hicho ndiyo kipimo cha Economic Diplomacy. Katika Afrika ya Mashariki, Tanzania ni ya kwanza katika uwekezaji ndani ya Afrika Mashariki lakini pia kutoka nje. Hivyo ndiyo vipimo vya Economic Diplomacy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kwa kifupi tu kuwaonesha baadhi ya masuala muhimu ya Economic Diplomacy ambayo tumeyavuna hivi karibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji ni mfano tu! Uwekezaji wa kiwanda cha cement cha Dangote. Uwekezaji ulioifanya Uchina ichague Tanzania kuwa moja ya nchi nne muhimu za uwekezaji. Wachina wenyewe wamesema, Balozi wenu pale Beijing ndiye aliyewashawishi vya kutosha kwamba Tanzania iwe moja ya nchi ambazo zitapewa kipaumbele katika uwekezaji wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipotoa hotuba yangu jana nimesema; sisi tutajikita kwenye diplomasia ya viwanda. Yaani hiyo diplomasia ya uchumi naipandisha safu. Tutajikita sasa kama Wizara kwenye diplomasia ya kushawishi na kuleta viwanda. Vile vile katika hotuba ile ile nimesema kukuza diplomasia ya viwanda haifiki popote peke yake, lazima iende sambamba na diplomasia ya kilimo kwa sababu hivi viwanda vitategemea kilimo. Lazima iende sambamba na diplomasia ya miundombinu kwasababu hivi viwanda vitahitaji umeme na uchukuaji na usafirishaji. Kwahivyo naweza kuwaelezeni ile safu ya Economic Diplomacy baada ya kuieleza kwamba ni ya pamoja na ya katika majukwaa sasa inapandishwa grade na Wizara yangu na itaitwa Economic Diplomacy of Industries. (Makofi) 0714197930
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini utekelezaji wake utakuwaje? Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli amesema; katika Wizara yako punguza watu na napunguza watu, nimepunguza wengi. Hata hivyo, anasema; unapopunguza hawa watu lazima upange na kupangua watu wako. Si tu kuwapeleka kwenye embassies, kwamba sasa mimi ni zamu yangu – posting, hapana! Nani aende wapi na kule aliko awe na nani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Economic Diplomacy si tu ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje, lazima tushirikiane na Wizara nyingine huko nje kama Utalii, Viwanda na Wizara nyingine ambazo zinahitaji wawekezaji lakini wanahitaji ushawishi wa pekee. Kwa hivyo, kutakuwa na kupanga na kupangua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia chuo chetu cha kule kurasini kitatoa mafunzo maalum ambayo yanaitwa The Economics of Economic Diplomacy. Lakini pia Economic Diplomacy tutaieneza na tutaifuata si tu kwa sababu ya mafunzo lakini pia ndani ya idara yetu tutatengeneza kitu kinaitwa Economic Unit ambayo itakuwa ni unit of economic intelligence na ambacho kitakuwa ni mtambuka, uchumi mtambuka wa sehemu zote za aina hiyo. Hiyo ndiyo aina ya diplomacy ambayo tunataka kuieneza, kuitetea na kuishuhudia katika Wizara yetu ya Mambo ya Nchi za Nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia nirudie tena lile suala la diaspora. Katika diaspora huwezi kuzungumzia diaspora bila kuitengenezea profile yake, nani yuko wapi na nani anafanya nini? Kuna Watanzania ambao ni wanafunzi, kuna Watanzania ambao ni wataalam wanafanya kazi zao huko, kuna Watanzania ambao ni wazamiaji; lazima tukubali hilo na kuna Watanzania kama nilivyosema ambao wako kwenye majela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni jukumu letu na tumeanzisha idara maalum katika Wizara yangu inayoitwa Idara ya diaspora. Tunashirikiana na wenzetu walio huko nje na pia na Serikali nyingine ili tuweze kuwatambua Watanzania wetu. Kuna wengine wanasema siji kwenye Ubalozi nitakamatwa, lakini hao hatimaye wanakuja wakipata shida na sisi tuko tayari kuwapokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunaweka mkakati maalum si tu kuwatambua lakini katika diaspora kuna wale wenye ujuzi wa pekee na wako tayari kuja huku nyumbani ama kwa miezi sita au mwaka mmoja wafanye kazi katika Wizara mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili nilizungumzie tena suala la uraia pacha au utaratibu mwingine wa kuwawezesha Watanzania walio nje washiriki katika mchakato wa uchumi. Hawa Watanzania walio nje ni wabunifu kweli kweli, wamekuwa na makongamano ya aina mbalimbali, mengine ya utalii, mengine uwekezaji, mengine ni ya kusaidiana tu kama jamii na lazima tuwaelewe zaidi ili tuweze kuwasaidia vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitafurahi kama ninyi wenyewe kwa umoja wenu au mmoja mmoja mnaweza kutupatia taarifa. Juzi hapa kuna Mbunge kutoka Upinzani amenifuata, anasema Balozi, sijui Waziri/Balozi; nina ndugu yangu alikamatwa na madawa, akatiwa ndani Nigeria, sasa amefunguliwa na lazima arudi nyumbani, Je, Wizara yako inaweza kutusaidia? Mara moja nilichukua hatua za kumrudisha yule kijana na juzi nimepata barua kutoka familia yake wanasema Waziri tunakushukuru. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tukumbushane kwamba hili suala la diaspora tumelizungumza mara kwa mara, lakini nina hakika tutafika mahali ambapo itabidi tukubaliane kwamba hawa diaspora wawe ni sehemu gani ya Watanzania walioko huko nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa sasa kuzungumzia suala la Mheshimiwa Rais, Dkt John Pombe Magufuli, kwamba haendi nje. Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ana sababu za kutokwenda nje, kwa sababu kuna mambo ambayo lazima afanye hapa nyumbani na wakati ule alikuwa anafanya uteuzi na kukamilisha Serikali yake. Hata hivyo, ningependa kuwaambia kama wengi hamjui, mimi kama Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje siwezi kwenda popote bila kutumwa na Mheshimiwa Rais! Kila ninakokwenda napata ridhaa ya Mheshimiwa Rais na maagizo ya Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia huyu Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa mkarimu sana kukutana na Mabalozi. Siwezi kusoma orodha yote hapa lakini amekutana na kila Balozi aliyepo Tanzania ambaye anataka kukutana naye na mazungumzo yanakuwa mazuri tu na baada ya hapo yanafuata maagizo ambayo mimi kama Waziri mwenye ridhaa nayatekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili nimwongeze pia Waziri wetu Mkuu. Juzi hapa nimesafiri naye, katika kile kipindi cha siku mbili cha kufanya kazi ameweza kuwashawishi wawekezaji wengi tu! Wengine wakiwa wamekubali kuleta kiwanda kizima cha matrekta hapa Tanzania. Kampuni ya Shell ambayo ndiyo mwekezaji mkuu kwenye gas yetu walikuwa wanasuasua, Waziri Mkuu aliwaita, tukakaa, tukazungumza nao. Wakasema; haa! Sasa tunaelewana na Tanzania na gesi tutaanza kuichimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nizungumzie suala la mjusi. Wiki mbili zilizopita nilikuwa Ujerumani kuangalia mjusi, hapana! Nikawauliza Wajerumani kwamba jamani yule mjusi vipi. (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajerumani nao wakaniambia vipi ninyi Watanzania. Nikawaambia kwa nini anasema kwa muda mrefu sasa, kumekuwa na Watanzania delegation after delegation inayokwenda Ujerumani kutazama mjusi. Delegation ya kwanza anasema ilikuwa na watu 19 kutoka Tanzania na ikiongozwa na National Museums, wakazungumza wakakubaliana kabisa jamani tufanye nini kuhusu huyu mjusi?. Wakawapa options anasema mnaweza kumchukua, lakini mkitaka kuchukua lazima kutafuta ndege maalum ambayo ni refrigerated na chemba nzima ambayo huyu mjusi atawekwa iwe katika temperature fulani na kila baada ya muda fulani huyu mjusi awe anapakwa vitu fulani, vinginevyo atayeyuka kama temperature ile haipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wao wakasema lakini kama mnataka sisi tutawasaidia. Baada ya hapo yule aliyeongoza ule ujumbe nasikia alifariki. Ukaenda ujumbe mwingine safari hii wakiwa Watanzania 24 kule Ujerumani, wakaenda pale kuzungumzia mjusi, wakasema sisi sasa tunarudi nyumbani na hili tutalipeleka kwa mamlaka husika tuanze kulitekeleza. Sasa mimi juzi nimeulizwa, jamani what is the problem with you, mnakuja tunazungumza tunakubaliana mnaondoka halafu mnakwenda tunaona tena delegation nyingine inarudi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukakubaliana hivi, tukasema ninyi Wajerumani pamoja na kuwa mnatupa misaada, juzi wametupa ndege za doria kwa ajili ya magaidi, ninyi mna pesa na mna uwezo na mnaweza kutusaidia pesa kama ni kumrudisha mjusi arudi au mnaweza kutusaidia fedha za maendeleo za ziada na zile ambazo mnatupatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamenipa changamoto, wanasema Waziri Mahiga rudi Tanzania, usiorodheshe tu mjusi maana pale alipogunduliwa huyu mjusi, wanasema kuna mijusi mingine ambayo inaweza ikachimbwa pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, wakasema pamoja na kuwa sisi tulikuwa pale kama wakoloni nawaombeni mwende mkaorodheshe maeneo yote ya kihistoria na urithi ambayo yanatokana na kuwepo kwa Wajerumani ndani ya nchi yenu. Tunaamini hii itakuwa ni kivutio maalum kwa watalii kutoka Ujerumani. Wakasema siyo mjusi tu, siyo liemba, siyo barabara ya Bismarck tu, bali ni shule, ni mahospitali hata maeneo mbalimbali ambayo yanatuunganisha sisi na Ujerumani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata taarifa kwamba pamoja na kuwa Wajerumani walirudisha fuvu la Mtwa Mkwawa, mwaka 1954 kumbe nasikia kuna mafuvu na mabaki ya Watanzania wengi tu kwenye museum zoo. Hii ni mojawapo ya maeneo ambayo tunaweza kwenda kuzungumza nao. Ukweli ni kwamba, wao wako tayari tukiongozana, tukishirikiana nao, kwamba tuweze kuhamasisha misaada ambayo italeta tija kwa Tanzania ambayo inatokana na kuwepo kwa Wajerumani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili la mjusi kwa kweli nadhani ni suala muhimu sana na lazima tulishughulikie. Nilipokutana na Deputy Minister wa Ujerumani, huyu ndiye alitoa ahadi kwamba maeneo alikotoka yule mjusi kuna barabara ambazo zinahitaji kujengwa. Ameeleza pia kwamba kuna maeneo ambayo Wajerumani waliishi, kuna barabara inaitwa sijui Bismarck road, nyingine inaitwa sijui Bismarck rock, sijui nyingine Bismarck nini; vyote hivi vinaashiria uhusiano fulani kati ya Wajerumani na Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajerumani wamesema hiyo timu iundwe, tuanze kutazama vile vitu ambavyo Serikali ya Ujerumani inaweza ikagharamia na inaweza ikafanya ni sehemu ya urithi wa historia kati ya Tanzania na Ujerumani, hilo wametoa kabisa kama blank cheque na sasa changamoto ni kwetu na nimeahidi kwamba hilo nitalifuatilia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Ujerumani inasema hakuna nchi ambayo kihistoria Afrika tuko karibu kama Tanzania, pamoja na tofauti zetu ambazo zimejitokeza hapa katikati nadhani suala la mjusi ni moja tu kati ya yale ambayo tunaweza kunufaika kutokana na uhusiano wetu na Ujerumani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuzungumzia juu ya majirani. Tulipokuwa Uingereza juzi na Waziri Mkuu, msaidizi wa John Kerry, Minister of Foreign Affairs au Minister of State wa Marekani, ambaye ni namba two wake aliomba kukutana na sisi na Waziri Mkuu. Wakasema Marekani inaamini kabisa kwamba katika ukanda wa maziwa makuu au hata katika Afrika, nchi ambayo inaweza ikazungumza na Kongo na ikasikilizwa ni Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, tunaombeni Watanzania mjenge uhusiano wa karibu na Kongo na pia muisaidie Kongo, kuwa na mtangamano wa kisiasa. Suala la kuanzisha Ubalozi mdogo Lubumbashi ni la siku nyingi sana. Sasa hivi, tunaitisha kikao kinachoitwa Joint Permanent Commission kati ya Tanzania na Kongo, kwa sababu inaelekea kwamba wanaweza kuanza kutafuta njia nyingine za kupitishia bidhaa zao. Tukiitisha kikao kile, tutazungumzia suala la consulate ya pale Lubumbashi lakini pia…
MWENYEKITI: Mheshimiwa naomba umalizie
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tutazungumzia masuala mengine ya uhusiano na hawa majirani zetu. Siwezi kuzungumza juu ya Burundi kwa sababu inajulikana lakini, ni kwamba nchi yetu imekuwa ikipokea wakimbizi. Hata kabla ya uhuru, wakimbizi wa kwanza kuja Tanzania ilikuwa mwaka 1959 walitoka Rwanda, hata uhuru hatujapata. Kwa hivyo, tuna jukumu la pekee na Jumuiya ya Mataifa nimewaambia lazima mtusaidie na lile suala la mazingira bora na mengineyo yashughulikiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa shukrani na nitaendelea kuzungumza nanyi, Upinzani nawashukuruni sana, Ndugu yangu Msigwa, tutazungumza mengi, tutasaidiana, tutabadilishana mawazo na tuendelee kuwa karibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapa, nadhani kuna kutoa hoja. Kutoa hoja baada ya Kamati ya Matumizi kupitisha vifungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa hoja
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Amani na Usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuhitimisha hoja, lakini kwa ruhusa yako, kabla sijahitimisha hoja, naomba niseme mambo mawili. La kwanza, kama ambavyo mmesikia Mbunge mwenzetu ameshambuliwa kwa shambulio baya na watu wasiojulikana, lakini taarifa rasmi mtapewa. Tutatoa kwa utaratibu kadiri tutakavyoongozwa na Bunge hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa tu za awali ni kwamba Madaktari wamejitahidi kwa kiwango cha hali ya juu kuweza kutoa huduma ya kwanza. Nimechelewa kuja hapa, nilikuwa pale na Mheshimiwa Spika, briefing ya mwisho tuliyopewa ni kwamba wamefanya vizuri wameweza kudhibiti damu zilizokuwa zinatoka. Kwa hiyo, wamesema hatua ya awali ya huduma ya kwanza waliyotoa imeenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la awali tu kwa upande wa Wizara ya Mambo ya Ndani, japo tutatoa tamko rasmi, lakini tunasema jambo hili lililotokea ni jambo ambalo halikubaliki; nasi kama Wizara ya Mambo ya Ndani na kama Serikali, hatutaruhusu na hatutaacha jambo hili lipite hivi hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeelekeza Polisi Mkoa wa Dodoma waweke vizuizi njia zote zinazotoka Dodoma na zinazoingia Dodoma na wasambae kuweza kuwasaka hao wote ambao wamehusika na tukio hili, tukio ambalo linapaka matope sura na heshima ya nchi yetu na tukio ambalo linapaka matope Serikali yetu ambayo inashughulikia masuala ya usalama wa raia.

Mheshimiwa Naibu Spika, iwe kwa sababu za kisiasa, iwe kwa sababu ya hujuma, iwe kwa sababu za ugomvi na iwe kwa sababu za za kijambazi, yote hayo tutasaka kuhakikisha kwamba wale wote ambao wamehusika na jambo hilo wanafikishwa katika mkono wa sheria ili kuweza kukomesha vitendo hivyo viovu ambavyo havijazoeleka katika nchi yetu. Watanzania wote tumwombee mwenzetu ili Mungu ampe afya njema na afya yake iimarike aweze kuendelea na kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, taarifa rasmi itatolewa kwa utaratibu ambao Kiti chenyewe kitatoa kwa masuala yote ya kiusalama pamoja na kiafya baada ya kuwa wenzetu wamefikia hatua ambayo wanaweza wakatoa taarifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia, nimeona wameunga mkono Azimio hili. Nami niendelee kusisitiza kwamba Azimio hili ni zuri, lina faida nyingi. Mambo mengi yalikuwa yakifanyika bila kuwa na misingi hii ambayo itakuwa imewekwa na Azimio na baadaye ambayo itapelekea uwepo wa sheria, kanuni na taratibu za kuweza kuyashughulikia mambo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilisema wakati wa kutoa hoja; na kama ambavyo wachangiaji wameelezea nikitoa na pongezi kwa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje aliyetoka kusema hivi punde, yatatusaidia katika kushughulikia masuala yaliyo ya kimipaka lakini na yaliyo ya kiujirani mwema hasa yanayohusiana na masuala ya kiusalama wa watu wetu pamoja na mali zao wa nchi hizi mbili na wageni wanaokuja katika nchi zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, itatusaidia hata kwenye maisha ya kila siku, masuala haya ambayo tumeyasemea yanayohusu mambo ya migogoro, shughuli za kiuchumi zinazoingiliana katika mipaka yetu. Kwa mfano, watu wetu wanaokaa jirani na mipaka ambao wana shughuli zinazoendana na zinazoingiliana, wao kwa asili zao hawatambui mipaka. Tunaamini uwepo wa Azimio na taratibu za kubadilishana taarifa na kubadilishana uzoefu wa kushughulikia uhalifu, itawasaidia watu wetu waweze kufanya shughuli hizo kwa njia ambayo ni salama na endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata kutimiza matakwa ya mikataba ambayo nchi yetu imeingia, nchi yetu ni nchi kiongozi katika uanzilishi wa jumuiya hii na katika uendeshaji wa jumuiya hii. Kwa hiyo, yale ambayo yanakubaliwa kama nchi wanachama ni wajibu wetu pia kama nchi kuweza kutekeleza na kuridhia na hasa baada ya kuwa tumeshajiridhisha na manufaa ambayo nchi yetu itapata kupitia jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, huku tukipokea hoja zote zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge, naomba sasa kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liridhie Azimio lake la Kuridhia Itifaki ya Amani na Usalama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (The East African Community Protocol on Peace and Security).

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kuhitimisha mjadala wa hoja yangu kwa kutoa shukrani za pekee kwa Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge hili Tukufu kwa mchango wenu wa maneno na maandishi. Pia naamini kabisa kwamba Wizara yangu itaendelea kutegemea mawazo ya ujumla ya Bunge hili katika kutekeleza sera na mipango yake ya kuendeleza uhusiano na nchi za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa shukrani za pekee kwa Naibu Waziri wangu ambaye amemaliza kujibu baadhi ya hoja zilizojitokeza. Pia natoa shukrani za pekee kwa wafanyakazi Wizarani kwangu, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, viongozi na wafanyakazi wote ambao tumeshirikiana katika kuandaa hotuba hii na kujibu maswali ambayo yamejitokeza ndani ya Bunge hili Tukufu ambapo jumla ya Waheshimiwa Wabunge zaidi ya 30 wamechangia katika hoja hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujibu hoja zote zilizowasilishwa ndani ya Bunge lako Tukufu, moja baada ya nyingine lakini kutokana na uchache wa muda hoja zote nitazijibu kwa maandishi kama yatakavyowafikieni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea pale alipoishia Naibu wangu. Je, Serikali haioni kuwa kutosafiri mara kwa mara kwa Mheshimiwa Rais nje ya nchi katika ziara rasmi au kushiriki Mikutano ya Kimataifa kwa kuzingatia kubana matumizi kunadhoofisha ushirikiano na ukuaji wa mahusiano ya kidiplomasia na mataifa mengine? Inapotokea kiongozi anasafiri kutafuta fursa na kujenga mahusiano ya nchi na Mashirika ya Kimataifa panakuwepo na kubezwa sana kwa safari hizi pamoja na maelezo mazuri sana ambayo yamekuwa yanatolewa mara kwa mara na Wizara yangu na Wizara nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande mwingine, inapotokea safari ya kwenda nje na kiongozi akaamua kutuma msaidizi wake kumwakilisha kwenye safari hizo kiongozi huyo anatuhumiwa kwamba anadhoofisha mahusiano. Hapo Wizara yangu inajiuliza, ni lipi jema hasa? Ukisafiri unaitwa mtalii na usiposafari unaua mahusiano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kama Mwanadiplomasia namba moja anatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na mafanikio makubwa. Kwa miaka mingi Tanzania inaheshimika katika medani ya kimataifa. Heshima hiyo imechangiwa sio tu kwa safari za viongozi na Serikali bali kwa kazi nzuri wanazofanya ndani ya nchi, Afrika Mashariki na Balozi zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Awamu hii ya Tano, Tanzania imeshatembelewa na viongozi wengi wa Mataifa makubwa yaliyoendelea na yale yanayoendelea na ambao walioambatana nao, ujumbe mkubwa wa wafanyabiashara hao, wamekuja na kufanya mazungumzo yenye tija kabisa kwa nchi yetu. Lazima ifahamike kwamba watu wanaokuja kututembelea wanaridhika kabisa na mazungumzo baada ya wao kuja kututembelea hapa na yameleta tija kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lingine ni kwa nini michago ya kifedha ya baadhi ya washirika ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki imekuwa haitolewi kwa ukamilifu? Jibu, michango yote ya Tanzania ndani ya Jumuiya hiyo imeshalipwa na hatudaiwi hata senti moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa za Gazeti la nchi ya Kenya la Daily Nation la tarehe 14 Mei, 2017 lilimnukuu Kiongozi wa Bunge katika Bunge la Kenya akitoa shutma kuwa Tanzania inapanga kuingilia mchakato wa uchaguzi wa nchi hiyo. Je, Serikali haioni kuwa taarifa hiyo itaathiri mahusiano kati yetu na nchi ya Kenya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati natoa hotuba yangu nilisema moja ya malengo ya Sera ya Mambo ya Nchi za Nje ya Tanzania ni kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine. Tanzania imekuwa nchi inayofuata na kuheshimu misingi ya demokrasia, utawala bora, ujirani mwema na uhuru wa nchi nyingine hasa majirani zetu. Tanzania inaheshimu maamuzi ya nchi nyingine ya kujiamulia mambo yao wenyewe na kuchagua viongozi wanaowataka kama ambavyo sisi tumefanya kwa awamu zote tano tangu ya Mwalimu Nyerere hadi ya sasa ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kusuluhisha migogoro kwenye Bara la Afrika na hasa nchi zinazotuzunguka ikiwemo Jamhuri ya Kenya mwaka 2007 ilipoingia kwenye machafuko ya kisiasa baada ya uchaguzi. Ni kwa misingi hiyo, Wizara inapenda kuweka bayana kuwa Tanzania haijaingilia na haitakaa iingilie masuala ya ndani ya nchi nyingine. Ni vema waandishi wa habari wakaandika habari za kweli na kuacha kuzichonganisha nchi majirani na ndugu kama vile sisi na ndugu zetu Wakenya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni upi msimamo wa Tanzania kuhusu nchi za Morocco na Sahara Magharibi. Tanzania ni mojawapo wa NchiWwanachama wa Umoja wa Afrika waliounga mkono ombi la Morocco kurejea katika Umoja wa Afrika ikiamini suluhu ya mgogoro uliopo wa Sahrawi ya Magharibi utazungumzwa. Nifafanue kwamba

katika sera yetu ya kutofungamana na nchi yoyote tumeamua kuwa na mahusiano na Morocco kwa sababu Morocco ikiwa ni nchi ya tano yenye uchumi mkubwa katika Afrika tutakuwa tunajinyima fursa ya kufanya biashara na uwekezaji na nchi hii. Kuisusa siyo suluhu ya mgogoro wa Sahrawi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kabisa kwamba ili kuisaidia Sahrawi, misingi yetu inayojulikana ya kulinda uhuru na heshima wa watu na makundi, suluhu inaweza kupatikana kwa mazungumzo. Baada ya miaka karibu 40 bila kupata suluhu tunaamini kwamba suluhu kati ya Morocco na Sahrawi itapatikana kwa mazungumzo ndani ya Umoja wa Nchi za Kiafrika ambapo Morocco imerudi na Tanzania itashiriki kikamilifu katika mijadala hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali kueleza msimamo wa nchi kuhusu mgogoro uliopo Syria, mgogoro kati ya India na Pakstan juu ya Kashmir pamoja na mgogoro kati ya nchi ya Marekani na washiriki wake dhidi ya nchi za Korea Kaskazini. Kwa misingi ile ile kwamba sisi hatufungamani na nchi zozote na suala hili la India na Pakstan ni la zaidi ya miaka 50 na wala halizungumzwi hata katika Umoja wa Mataifa. Nadhani hili ni suala ambalo nchi hizo mbili zinaweza kulizungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Syria itakumbukwa kwamba katika mageuzi ya Mashariki ya Kati yaliyoanzia Tunisia yakaenda Libya yakaikumba Misri yalifika Syria pale yakakwama. Sasa hivi ushindani kati ya upinzani na Serikali na vikundi mbalimbali vya upinzani imepelekea mataifa makubwa kuchukua nafasi tofauti zinazokingana. Katika hili, Tanzania inapendekeza kwamba suluhu ipatikane kwa mazungumzo. Kwa kuzingatia siasa yetu ya kutofungamana na upande wowote, sisi hatuwezi kuingilia mvutano huo wa ndani ya Syria na makundi yale ambayo yanaunga vikundi hivyo yakiongozwa na mataifa makubwa ya duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kugusia suala lingine ambalo limeulizwa na Mheshimiwa Profesa Anna Kajumulo Tibaijuka. Anasema mpaka baina ya Tanzania na Uganda haupo vizuri na Serikali imejipangaje kuliweka vizuri suala hili ili pawe na maelewano na mkataba kwenye mpaka huu pamoja na mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuwakumbusheni kwamba mipaka ya nchi za Kiafrika inatokana na maamuzi ya nchi za Kiafrika kwamba isibadilike na sisi nia yetu siyo kubadilisha mpaka huo lakini kuna wakati ambapo ni lazima tujaribu kufanya marekebisho kwa sababu wananchi wa pande zote mbili wanaoishi katika nchi hizi mara kwa mara wamekuwa hawaoni mstari ambao unatenganisha nchi hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baina yetu na Uganda tumeshafanya kikao huko Bukoba kuzungumzia suala hili ambapo katika pande mbili za mpaka kuna Waganda na Watanzania ambao wamevuka mpaka. Majadiliano haya yaliingia pia katika Tume ya Pamoja ya mazungumzo kati ya Uganda na Tanzania na tutaendelea kuyazungumza tena na tumepanga ndani ya mwezi ujao wa Juni tutaendelea kuzungumza. Nia siyo kubadilisha mpaka lakini ni kuwasaidia wananchi wa pande zote mbili kuelewa mpaka ulipo na kuleta tija zaidi katika ushirikiano na udugu wa nchi hizo. Nadhani hili linaeleweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka kumhakikishia Mheshimiwa Profesa Tibaijuka kwamba katika hotuba yangu nimeeleza kwamba Tanzania inachukua kila fursa ya majukwaa ya kimataifa kuzungumzia masuala ya uchumi. Kati ya majukwaa muhimu ya Umoja wa Mataifa ni Jukwaa la UNCTAD. Tumekuwa tukishiriki kikamilifu tangu mwaka 1964 na mazungumzo yanayoendelea pale ni ya tija kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ambayo yanajitokeza sasa tutaendelea kuyaweka katika ajenda ya UNCTAD. UNCTAD itaendelea kuwa ni chombo muhimu cha nchi zinazoendelea na hasa pale inapokuwa kati ya mahusiano ya sisi tunaoendelea na nchi za nje. Kama vile ilivyo WTO (World Trade Organization), Jukwaa la UNCTAD ni muhimu kwa Tanzania. Kama alivyogusia Mheshimiwa kwa kuleta ajenda zetu pale masuala mengi ya mahusiano ya kibiashara na uwekezaji yanaweza kutatuliwa kwa kutumia chombo kile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la EPA, napenda ifahamike kwamba huu ni mkataba ambao Ulaya walitaka nchi za Afrika Mashariki kwa umoja wao waweke saini lakini baada ya uchambuzi tumeona kwamba kuna upungufu katika mkataba huo. Tatizo linalokuja ni kwamba katika nchi za Afrika Mashariki, nchi tano zinaendelea kufanya biashara na Ulaya na kupeleka bidhaa bila vikwazo lakini nchi moja ambayo ni Kenya yenye uchumi wa wastani, Ulaya walisema ifikapo Oktoba mwaka jana wao hawatanufaika na kile kipengele cha kuondolewa ushuru kama sisi wengine. Wakasema Kenya haiwezi kuendelea lakini sisi wote kwa pamoja lazima tuweke saini ili kuinusuru Kenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukaiambia Kenya kwamba itakuwa vigumu kwa sisi kama mkataba huu ulivyo kwa sasa. Kuna haja ya kuchambua zaidi lakini tunaiambia Jumuiya ya Ulaya kwamba ivute subira na isiiwekee vikwazo Kenya kwa sababu Kenya ikisaini peke yake makubaliano hayakubaliki, hata ikisaini Kenya peke yake haikubaliki mpaka Kenya isaini pamoja na wenzake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye mkutano wa juzi wa nchi za Afrika Mashariki tumeamua kwamba kwa Umoja wetu wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wetu mpya Yoweri Museveni ataongoza ujumbe maalum kwenda Brussels mwezi ujao na kuiambia Jumuiya ya Ulaya kwamba wasubiri wasiweke vikwazo kwa Kenya mpaka hapo tutakapokubaliana sisi wanachama wa Jumuiya kutazama upya masuala ambayo yanatukera. Ndiyo maana Bunge hili Tukufu lilitoa ushauri ambao unaheshimika kabisa kwa Serikali yetu na kwa Mheshimiwa Rais kwamba tusiweke saini mkataba ule kwa sababu una upungufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na maamuzi ya juzi, Museveni atakwenda kufanya mambo matatu. La kwanza ni kuiambia Jumuiya ya Ulaya kwamba vuteni subira, msiiwekee vikwazo au msiifungie biashara Kenya. La pili, chini ya Uenyekiti wa President Museveni sisi Wanajumuiya ya Afrika Mashariki tutakaa tena kutazama upya kipengele kwa kipengele mahali ambapo panahitaji marekebisho na Ulaya watusubiri tukubaliane kwa sababu nchi moja hata ikisaini, haina tija, haina nguvu mpaka wote tusaini mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni kwamba endapo hiyo itashindikana kuna kipengele katika Mkataba wa East Africa ambacho kinaruhusu kitu kinaitwa variable-geometry. Variable-geometry ni kwamba ninyi wanachama mnamruhusu mwenzenu aendelee kuweka saini mkataba ninyi wengine mkiwa bado mnajipanga. Hata hivyo, dhamira ya nchi za Afrika Mashariki ni kwamba tuweke mkataba huu kwa pamoja na mpaka tufike kwenye variable- geometry itakuwa baada ya kwamba tumeshindwa kuwaambia Ulaya kwamba wavute subira ili tuweze kurekebisha mapatano hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndani ya mwezi ujao ni matarajio yetu kwamba Umoja wa Ulaya hautaiwekea Kenya vipingamizi vya biashara. Sisi tutaendelea kutazama mkataba ule na pale ambapo Kenya inaona umuhimu wa kuendelea sisi tutaridhia kwamba mwenzetu aendelee kwa kutumia kipengele kinachoitwa variable- geometry huku tukiendelea kuzungumza ili hatimaye sisi wote tuweze kuweka mkataba huo kwa pamoja. Nadhani hilo linaeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mengine Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq ameshauri Serikali iwe na majengo yake kwenye Ofisi za Balozi nje ya nchi ili kupunguza gharama za kulipia kodi za pango. Aidha, Wizara iwe na mkakati wa muda mrefu na mfupi, kuendeleza viwanja ambavyo Serikali imepewa nje ya nchi kupitia Balozi zetu na kutumia utaratibu wa mikopo ya benki ya hire purchase na mortgage finance ili iweze kuviendeleza viwanja hivyo kwa kujenga majengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuendeleza na kukarabati majengo ya ofisi na makazi ya watumishi Balozini na imekuwa ikitekeleza jukumu hilo kwa kutumia fedha za bajeti ya maendeleo zinazopangwa katika kila kipindi cha mwaka wa fedha. Mpango wa Wizara wa miaka 15 wa ujenzi, ununuzi na ukarabati wa majengo ya ofisi na makazi ya watumishi Ubalozini ulianza kutekelezwa mwaka wa fedha 2012/2013.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali kwenye Balozi zetu kama vile kufanikisha ujenzi wa jengo la Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania New Delhi India; ununuzi wa jengo la Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania Washington DC – Marekani; ununuzi wa jengo la Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania New York – Marekani; ununuzi wa Jengo la Ofisi na Makazi ya Balozi, Ubalozi wa Tanzania Paris – Ufaransa; ukarabati wa makazi ya Ubalozi wa Tanzania Nairobi – Kenya na ukarabati wa makazi ya Balozi wa Tanzania Tokyo – Japan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017, Wizara itakamilisha ukarabati wa jengo la ghorofa tisa la Ofisi na Makazi lililopo Ubalozi wa Tanzania Maputo – Msumbiji; ukarabati wa makazi ya Balozi na nyumba za watumishi zilizoko Ubalozi wa Tanzania Stockholm - Sweden na ukarabati wa Jengo la Ofisi na makazi ya Balozi yaliyoko Khartoum - Sudan. Hivi sasa Wizara inaandaa mpango mwingine wa miaka 15 wa ujenzi, ununuzi na ukarabati wa majengo ya Ofisi na Makazi ya watumishi Ubalozini utakaoanza kutekelezwa mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya miradi itakayotekelezwa ni ukarabati wa jengo la ofisi na makazi ya watumishi kwenye Balozi za Tanzania Harare – Zimbabwe; Kampala – Uganda; Beijing - China, Pretoria – Afrika Kusini na Cairo – Misri. Vilevile ukarabati wa nyumba za Ubalozi zilizoko kwenye Ubalozi wa Tanzania Lilongwe – Malawi na Kinshasa – DRC; ukarabati wa jengo la zamani la Ofisi ya Ubalozi ulioko Washington – DC; ukarabati wa miundombinu ya Chuo cha Diplomasia kilichopo Kurasini na ujenzi wa makazi ya Balozi, Ubalozi wa Tanzania Addis Ababa – Ethiopia na Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania Muscat, Oman.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati ya kutekeleza mpango huu ni kuendelea kutumia bajeti ya maendeleo ya Serikali, kuishirikisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kama vile Taasisi ya Miradi ya Maendeleo ya Miundombinu (UTT-PID) na kwa kutumia utaratibu wa karadha katika kutoa mikopo ya kutekeleza miradi ya maendeleo Ubalozini kwenye nchi za uwakilishi ambapo utaratibu huo unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kuwaonyesha kwamba tuna mkakati na kutoa mifano halisi ingawa ombi letu ni kwamba Bunge hili Tukufu litusaidie kupitisha maombi yetu ili tuweze kuanza kutekeleza haraka. Hii pia inajibu hoja kwamba tunachelewa kupeleka pesa kwenye Balozi zetu, kama Hazina ikitupatia pesa kwa wakati tutajitahidi kupeleka pesa hizo ili zikafanye kazi inayotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine linahusu upungufu wa wafanyakazi kwenye Ofisi za Balozi ambapo hakuna wataalam mbalimbali kama Wachumi, Wanasheria, wataalam wa utalii na Maafisa Uhamiaji ili kufanikisha Diplomasia ya Uchumi. Wizara imerejesha kiasi kikubwa cha watumishi waliomaliza muda wao katika Balozi zetu nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa tupo katika hatua ya kurejesha waliobaki ili kutekeleza hatua ya pili ya kupeleka watumishi nje kulingana na mahitaji. Tuko katikati ya mchakato huo, hatuwezi kupeleka watu kabla ya hatujarudisha watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara na taasisi zote zilizo chini ya Wizara zina tovuti na mtandao wa kijamii ambao una taarifa muhimu kuhusu huduma zinazotolewa na Wizara au taasisi husika zikiwemo taarifa za uwekezaji. Aidha, taarifa hizo zinapatikana kwa upana katika tovuti zinazohusika na taarifa zaidi kuhusu kazi zinazoendelea katika Balozi zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Cosato Chumi ameuliza na kwa kweli ametoa ushauri, Wizara kwa kushirikiana na mamlaka nyingine isimamie suala la makubaliano ya kutoza kodi mara mbili baina ya nchi yetu na nchi nyingine yaani double taxation na kulinda wawekezaji wa nje nchini (protection of investment). Wizara inapokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na tutalifanyia kazi pendekezo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia anashauri Wizara ijenge majengo yake yenyewe katika viwanja, nadhani hilo nimeshalijibu. Kuhusu upungufu wa wafanyakazi, hilo pia nimeshatoa majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeulizwa, ni lini Wizara itapeleka Balozi wa Heshima Lubumbashi, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo. Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na wawakilisha kamili wa Ubalozi wenye makazi katika nchi mbalimbali duniani na Konseli kuu katika maeneo ya kimkakati. Kutokana na mwingiliano mkubwa wa biashara baina ya wafanyabiashara wa Tanzania na Mashariki mwa Congo, Wizara imeanza utaratibu wa kupata Mwakilishi wa Heshima ambaye atakidhi mahitaji ya Watanzania wanaoishi Mashariki mwa Congo pamoja na wafanyabiashara watokao Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivi sasa Serikali imefungua Balozi sita mpya ambazo nilizitaja, lakini tutaendelea pia kutazama maeneo mengine ambayo ni muhimu na hasa kwa vile Mabalozi wanasimamia nchi nyingi na kuna umuhimu wa kuwa na Konseli Jenerali na hilo katika mwaka ujao tutalipa kipaumbele, siyo tu katika DRC lakini kuna nchi nyingine ambazo tumeona umuhimu wa kuwa na Konseli Jenerali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeulizwa kuhusu kunyanyaswa kwa Watanzania wanaokwenda kufanya kazi katika nchi za Uarabuni hususan Oman. Wameomba kupata taarifa juu ya kifo cha Mtanzania huyu anayesemekana kuwa aliuawa nchini humo. Aidha, wameshauri Wizara ishirikiane na Wizara ya Kazi na Ajira ili kuwepo na utaratibu ambao utaondoa unyanyasaji huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 14 Machi, 2017, Wizara ilipokea taarifa kutoka Ubalozi wetu nchini Oman kuhusu kifo cha kutatanisha cha Mtanzania Bi. Husna Issa Abdallah, mwenye umri wa miaka 28 aliyekuwa akifanya kazi za ndani. Taarifa hiyo imeeleza sababu za kifo hicho kwamba marehemu alijirusha na kuanguka kutoka ghorofa ya kwanza ya nyumba ya mwajiri wake huku mwajiri na familia yake wakiwa wameketi sebuleni. Aidha, taarifa ya Serikali ya Oman imeeleza kuwa kifo hicho kimetokana na yeye mwenyewe kujiua kwa kujirusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupokea taarifa hiyo, Ubalozi ulichukua hatua ya kuwasiliana na ndugu wa marehemu ili kupanga mipango ya kusafirisha mwili. Aidha, Ubalozi ulisaidia kushughulikia documentation zote zinazohusiana na usafirishaji wa mwili wa marehemu. Kwa upande wake, aliyekuwa mwajiri wa marehemu alijitolea kulipa gharama zote za kusafirisha mwili hadi kijijini kwao na pia kugharamia gharama za mazishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara ilipokea barua kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni ndugu wa marehemu kudai kuwa yeye ana nyaraka zinazoonyesha taarifa tofauti na ile tuliyonayo. Tulimwandikia barua ya kuomba nakala ya document hizo ili tuweze kufuatilia kupitia Ubalozi wetu mpaka sasa hatujapata jibu kutoka kwa ndugu huyu wa marehemu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ili kupata suluhu ya kudumu kuhusu changamoto zinazowakuta Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya Mashariki ya Kati, Wizara inaendelea kusisitiza Watanzania wanaoenda kufanya kazi nje ya nchi hususani katika eneo la Mashariki ya Kati, wafuate taratibu zilizowekwa na Wakala wa Ajira Tanzania (TaESA) kwa kutumia mawakala waliosajiliwa rasmi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa baadhi ya watumishi wanaotoka Balozini wamekuwa wakipelekwa na Serikali katika Ofisi mbalimbali ili kupata ujuzi katika sekta hizo lakini pia ili kupeleka ujuzi walionao. Suala hili pia limezungumzwa kwa kirefu katika hotuba yangu na lipo kwenye kitabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ni kutoka kwa Mheshimiwa Haji Khatib, ili kumaliza tatizo la kukamatwa na kufungwa kwa wavuvi wetu nchini Kenya, ni vema Serikali ya Tanzania na Kenya ikarudi kwenye mkataba uliosainiwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizi mbili mwaka 1975. Wizara kwa kutumia mahusiano yake mazuri na nchi rafiki imeingia makubaliano na Serikali na Wizara hii itahakikisha kwamba tunazungumza tena na kutazama mkataba huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuwa kule Pemba tukitoa mafunzo na semina, suala hili tulilipokea na tunaahidi kwamba tutaendelea kulifanyia kazi na hasa katika kuzingatia mahusiano ya biashara na usafiri kati ya wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani Tanzania na Kenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeambiwa pia kwamba Wizara ifanye maboresho katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha, hususani upande wa vyoo vya watu mashuhuri (VIP) na vyoo vingine vya kawaida. Tunachukua ushauri huo. Ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itoe maelezo juu ya uvumi kuhusu unyanyasaji wa Watanzania katika nchi nyingine ambazo tuna uhusiano nao. Majibu ni yaleyale tuhakikishe kwamba tunatoa elimu kwa vijana wetu ili wanapokwenda huko waweze kuwa wamepewa kibali na wanasimamiwa na agency ambazo zimewekwa za kupeleka watu kufanya kazi nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Maria Ndila Kangoye, Mbunge wa Viti Maalum, anasema kuwe na sera moja ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinazotumia Ziwa Victoria juu ya uvuvi na forodha. Kwa utaratibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, sheria inayoweza kutumiwa na nchi zote za Jumuiya hujadiliwa kwa pamoja na nchi wanachama zikachukua vipengele vinavyovitaka katika kila nchi. Hivyo, Sheria ya Uvuvi ya Tanzania ikirekebishwa haitakuwa kigezo cha kutumika katika nchi zote wanachama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa namna gani Zanzibar inanufaika na uwekezaji unaofanywa na Shirika la AICC kule Arusha. Ni kweli AICC ni Shirika la Muungano kwa kuwa liko chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambayo ni Wizara ya Muungano. Uwekezaji unaofanywa na AICC unanufaisha wananchi pande zote za Muungano. Hii ni kutokana na ukweli kuwa gawio linalopatikana linawasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango ambayo yenyewe ina mamlaka ya kutoa gawio Zanzibar kulingana na utaratibu uliopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mbunge wa Viti Maalum, alishauri Serikali ipeleke …

MWENYEKITI: Dakika moja.

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa wakati Balozini. Nadhani hili tumeshalizungumza na itategemea uhusiano wetu baada ya ninyi kutusaidia katika kuidhinisha pesa husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala kadhaa ambayo yameulizwa hapa, mengi tutayajibu kwa maandishi na tunatoa heshima ya pekee kwa mchango huu. Masuala mengi ni ya kuchangia kuboresha utendaji kazi wa Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani huu ndiyo mwisho, naomba kutoa hoja.