Contributions by Hon. Prof. Joyce Lazaro Ndalichako (31 total)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi na mimi nichangie hoja hii iliyoko mble yetu.
Kwanza kabisa, napenda kuanza kutoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Joseph Pombe Magufuli kwa imani kubwa kabisa aliyoonyesha kwangu kwa kuniteua kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania na kuniteua kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Rais kwamba nitaifanya kazi aliyonipa kwa moyo wa dhati kabisa na nitawatumikia wananchi, Watanzania wenzangu katika sekta hii ya elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingi zimezungumzwa katika Wizara yangu, lakini kwa sababu ya muda nitazungumzia tu chache. Napenda kuanza kuzungumzia suala la elimu bila malipo ambalo mwenzangu wa TAMISEMI amelizungumzia, lakini ningependa kuongezea tu jambo dogo katika kutoa ufafanuzi kwa sababu umejitokeza mkanganyiko kwamba Serikali inabagua baadhi ya watoto; wengine wanapewa chakula na wengine hawapewi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kusema kwamba usajili wa shule uko wa aina mbili na Wizara yangu ndiyo inayofanya usajili wa shule. Tuna shule za kutwa na shule za bweni. Shule za bweni zina vigezo vyake. Tunatambua kama alivyosema Waziri wa TAMISEMI kwamba kuna baadhi ya shule za kutwa ambazo zimewekewa hostel kwa sababu maalumu. Sasa zile haziko katika utaratibu wa sasa wa wanafunzi kupatiwa chakula kwa sababu usajili wake ni shule za kutwa na sio shule za bweni. (Makofi)
Kwa hiyo, nami narudia kuwaomba Wakurugenzi wote wa Halmashauri, kama kuna shule ambayo ilisajiliwa kama shule ya kutwa lakini inakidhi vigezo; kwa sababu vigezo vipo ili shule iweze kuwa ya bweni. Ina vitu vingi ambavyo wanapaswa kuzingatia. Basi kama wamekidhi vile vigezo, waje Wizarani tuwabadilishie usajili. Ili waweze kupata chakula, lazima iwe ni shule ya bweni na siyo vinginevyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa shule ya kutwa kwa sababu inahesabika kwamba mwanafuni anakuja shuleni na kurudi nyumbani, kwa hiyo, lile jukumu la chakula bado ni jukumu la mzazi kwa sababu mwanafunzi anaishi nyumbani kwa mujibu wa usajili shule husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimeona hilo jambo pamoja na maelezo mazuri ambayo aliyasema, nizungumzie kwa sababu ni suala la kisera.
Kwa hiyo, shule iliyosajiliwa kama shule ya bweni inapata chakula, shule iliyosajiliwa kama ya kutwa katika mwongozo ambao tumeutoa mzazi ataendelea kuchangia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuzungumzia kidogo suala ambalo limejitokeza kuhusiana na malalamiko kwamba ada kubwa. Hii imejitokeza hata katika hotuba ya Mheshimiwa Rais kwamba mojawapo ya kero ni ada kubwa zinazotozwa na shule binafsi. Naomba tu niseme kwamba Wizara yangu tayari inalifanyia kazi suala hilo na tunajaribu kuja na ada elekezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba hili suala la ada elekezi linahitaji kufanyiwa kazi kwa kina na kuangalia vizuri shule zetu, kwa sababu shule ziko katika makundi mbalimbali. Unaweza kukuta zile huduma au facilities ambazo zinapatikana shuleni zinatofautiana sana. Kuna shule nyingine mpaka zina swimming pool, zimejengwa kwa terazo, nyingine zimejengwa kwa tiles au kwa marble, sasa unapokuwa unatoa ada elekezi, ni lazima pia uzingatie kwamba mwanafunzi anasoma katika aina gani ya shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo shule nyingine za binafsi ambazo hazina hata sakafu. Kwa hiyo, huwezi kuja na ada elekezi ukasema tu kwamba ni shilingi kadhaa. Ni lazima haya mambo yote uyaangalie. Hata chakula wanachopewa wanafunzi kinatofautiana. Baadhi ya shule wanapewa mpaka sausage, wanakula pilau na wengine wanakula ugali na maharage kila siku. Huwezi ukaja na ada elekezi ambayo ni uniform. (Makofi)
Kwa hiyo, Wizara yangu lazima iliangalie hili jambo kwa umakini mkubwa sana. Tutaangalia mpaka mishahara wanayolipwa walimu. Kuna baadhi ya shule zinawaonea walimu inawapa mishahara kidogo.
Kwa hiyo, naomba Watanzania tuwe na subira, Wizara yangu inalifanyia kazi hili jambo, lakini siyo jambo ambalo linahitaji kufanya kazi kwa haraka. Tutakapokuwa tayari, tutakuja kuwapa majibu. Tutakapokubaliana, kwa sababu tunafanya kwa kina na tuna mtaalam mshauri, tutaweka class za shule kwa vigezo mbalimbali ambavyo tutavitambua, basi tutakapokuwa tumekamilisha, naomba tukubaliane na hiyo ada. Nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu ili niweze kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge zilizotolewa wakati wa kujadili Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yangu kwa mwaka wa fedha 2016/2017. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Eng. Stella Manyanya ambaye kwa kweli tumekuwa tunafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na hata katika kuandaa hii hoja, tumekuwa naye bega kwa bega hadi tarehe 21 ambapo bahati mbaya alipata taarifa za msiba wa mama yake.
Kwa hiyo, nafahamu sasa hivi atakuwa na majonzi mara mbili; anasikitikia kuondokewa na mama yake, lakini anasikitika kwamba hajaweza kuwa pamoja na mimi katika kuhitimisha hoja hii. Naendelea kumpa pole sana na ninamwombea Mwenyezi Mungu aendelee kumtia nguvu katika kipindi hiki kigumu alichonacho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nitumie fursa hii kumshukuru kwa dhati kabisa Katibu Mkuu wa Wizara yangu, Bibi Maimuna Tarishi kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Kwa kweli ananipa ushirikiano mkubwa sana katika sekta hii ya elimu ambayo wote mnakubali kuna changamoto. Nawashukuru sana Manaibu Katibu Wakuu, Watendaji wa Taasisi, Wakuu wa Vyuo na Watendaji wote katika Wizara ya Elimu kwa ushirikiano wao mkubwa ambao umeniwezesha hata kusimama kuhitimisha hoja hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mheshimiwa Peter Serukamba pamoja na Wajumbe wote wa Kamati hii kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuchambua kwa kina bajeti ya Wizara yangu. Kwa hakika niseme kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu kwamba nimefarijika na nimefurahishwa sana na maoni na ushauri wa Kamati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yao yanaonyesha jinsi gani Kamati yangu imejaa Wajumbe ambao wana weledi mkubwa katika sekta hii ya elimu na wana dhamira ya dhati kabisa ya kuona mabadiliko katika Sekta ya Elimu. Nawashukuru sana na niwaambie tu kwamba mambo yote mliyoyasema tutayazingitia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nichukue fursa hii kumshukuru kwa dhati kabisa classmate wangu Mheshimiwa Suzan Anselim Lyimo, Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani, kwa kuwasilisha vyema maoni ya Kambi ya Upinzani, lakini vile vile kwa ushauri na mapendekezo yake ambayo kama nilivyosema, tunachoangalia ni kuwatumikia Watanzania na kujenga nchi yetu. Kwa hiyo, mapendekezo yote ambayo yana tija kwa Tanzania tutayafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee kabisa nirudie tena kutoa shukrani za dhati kabisa kwa familia yangu, mume wangu amekuja kuniunga mkono; lakini pia nashukuru kwamba yupo pamoja na mwanangu, tangu jana wamekuwa na mimi hadi leo ninavyohitimisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naishukuru familia yangu yote kwa ujumla, wamekuwa wakinivumlia na wananipa ushirikiano mkubwa. Haya majukumu huwezi kuyafanya vizuri bila ushirikiano wa familia. Naomba mwendelee kunivumilia, kazi iliyopo mbele yangu ni kubwa ili niweze kuwatumikia Watanzania. (Makofi
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa majadiliano ya hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Waheshimiwa Wabunge 16 walitoa hoja zao kuhusiana na Sekta ya Elimu. Aidha, baada ya kuwasilisha hotuba yangu Waheshimiwa Wabunge 60 wamechangia hoja kwa kuongea na Wabunge 61 wamechangia kwa maandishi, ninawashukuru sana Waheshimiwa wote ambao mmechangia katika hoja yangu ama kwa maandishi ama kwa kuzungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niwashukuru niwashukuru pia hata wale ambao hawakuweza kupata nafasi ya kuchangia nikiamini kwamba yale yaliyochangiwa na wengine yamewakilisha mawazo yao pia. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, Wizara yangu itazingatia ushauri uliotolea na Wabunge wote na itafanyia kazi pia mapendekezo yaliyotolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikisikiliza kwa makini sana michango ambayo imekuwa ikitolewa, kuanzia kwenye Kamati yangu ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, upande wa Upinzani na kwa Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamezungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kujali itikadi zetu, bila kujali upande gani tumekaa nadhani wote katika hoja yangu tumezungumza lugha moja, tumezungumza lugha moja kwamba, tunataka kuona elimu katika nchi hii inatoa wahitimu wenye ubora, tunataka kuona mazingira ya kujifunzia yako vizuri, tunataka kuona ukaguzi wa shule unafanyika vizuri ili kudhibiti ubora wa elimu.
Tunataka kuona maslahi ya Walimu na stahiki zao zinaboreshwa, tunataka mamlaka za udhibiti wa ubora hizi tunazozipigia kelele TCU, NACTE na ukaguzi zifanye kazi zao vizuri ndicho tunachokitaka, tunataka wanafunzi wenye uhitaji maalum wafanye kazi vizuri na mambo mengine ambayo ziwezi kuyaorodhesha lakini wote kwa kauli moja tumeonesha kwamba, haya ndiyo mambo ambayo Watanzania wanayataka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema ni kuwa Waheshimiwa Wabunge wamekuwa na mambo mengi mazuri ambayo wameyachangia, labda niseme tu pengine kuna sehemu nyingine tofauti tu ni ile aina ya uwasilishaji na lugha inayotumika lakini mimi kimsingi naangalia hoja ile ambayo inawasilishwa na kama nilivyosema yote yatazingatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulialifu Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kwa dhati kabisa katika kuboresha na kuinua ubora wa elimu katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimenukuu katika kitabu changu cha bajeti, na hii haikuwa ni bahati mbaya. Nimemnukuu Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania maneno yake ambayo aliyatoa katika Bunge hili siku ya tarehe 22 mwezi wa Novemba, wakati alipokuwa analizindua Bunge rasmi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alisema na ninaomba kunukuu “Serikali ya Awamu ya Tano itajielekeza katika kuongeza ubora wa elimu inayotolewa ikiwa ni pamoja na kuongeza mkazo kwenye masomo ya sayansi” mwisho wa kunukuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wameongea kwa uchungu sana, tena sana wakielezea masikitiko yao makubwa kuhusiana na hali ya elimu ilivyo sasa hivi nchini kila mmoja wetu hapa anasikitika. Waheshimiwa Wabunge, wanaonekana kutoridhishwa kabisa na ubora wa elimu inayotolewa katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie kwamba, sasa hilo ndilo jukumu ambalo Mheshimiwa Rais amenikabidhi na nina nia ya dhati, ninao uwezo wa kuweza kuhakikisha kwamba elimu yetu inakwenda vizuri. Kwa hiyo tu nianze kwa kusema kwamba, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge wote mniunge mkono katika bajeti yangu ili sasa nikaanze kufanya ile kazi ambayo wote mnahamu kuona ikiwa inafanyika katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekii, ninawahikishia tu kwamba tunayo dhamira ya dhati na nimefarijika kabisa na michango yenu ambayo inaendana na ile kipaumbele chetu ambacho maneno yake nimeyatoa, siyo kama ninasema tu kwa sababu mmechangia lakini hiyo ndiyo kauli na ahadi ya Mheshimiwa Rais. Ninachoweza kusema tu kumbe katika Sekta ya Elimu tulipoweka kipaumbele cha kuinua ubora wa elimu hakika tumelengesha kwa sababu ndipo Tanzania wanapopahitaji. Ningependa tu niseme kwamba, tunaposema kuboresha elimu maana hiyo ndiyo msingi ya hoja zote ilikuwa katika hali halisi ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaposema kuboresha elimu maana yake ni nini? Maana yake lazima tujitazame tulipo, tuangalie changamoto tulizonazo na mahali ambapo tunataka kuenda. Niwakumbushe tu maneno aliyekuwa anasema Mheshimiwa Rais wetu katika kampeni zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alikuwa anawaambia wananchi kwamba, akichaguliwa anakuja kuleta mabadiliko ya kweli katika nchi hii. Na mimi naomba Bunge lako Tukufu liniruhusu nifanye mabadiliko ya kweli katika Sekta ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana mturuhusu kufanya mabadiliko ya kweli, kwanini ninasema hivyo. Tumekuwa na utamaduni wa kuwa tunatoa mapendekezo na Serikali inakwenda kufanyiakazi mapendekezo lakini baada ya kufanyiakazi mapendekezo wakati mwingine inakuwa inaonekana kwamba, kunakuwa pengine na maoni tofauti.
Mabadiliko ya kweli yanahitaji mabadiliko ya mfumo, huwezi ukawa na mabadiliko ya kweli wakati mfumo ni uleule na hatuwezi kuwa tayari hapa tulipo kama kweli hatuna dhamira ya dhati ya kufanya mabadiliko katika mfumo wetu wa elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika michango kumekuwa na hoja inayojitokeza kwamba kila Waziri anayekuja, anakuja na mitaala yake anakuja na mabadilikoyake. Kwa hiyo niseme tu kwamba, kama hayo ndiyo yatakuwa maoni kwamba, labda sasa katika sekta yetu ya elimu tubaki kama tulivyo inamaana tukubali kubaki na elimu ambayo wote tunailalamikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, pale inapohitajika mabadiliko tutayafanya lakini tutahakikisha kwamba, tunashirikisha wadau wote muhimu ili kufahamu misingi ya mabadiliko, nafikiri hilo ndilo jambo la msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapofanya mabadiliko, mabadiliko hata wanataaluma kuna mtaaluma mmoja ambaye amekuwa anaandika sana mambo ya masuala ya mabadiliko, Profesa Fulani amekuwa anasema kwamba kunakuwa na uwoga wa mabadiliko hilo ni jambo la kawaida, mtu anapotaka kufanya mabadiliko kunakuwa na uwoga. Mabadiliko lazima yawaguse watu, mabadiliko lazima yaguse sehemu ambazo pengine niseme kwamba, zinaweza zikaleta maumivu labda kwa lugha ambayo ni nyepesi. Kwahiyo tukubali tunapokuwa tunayafanya hivyo kwa sababu haiwezekani tukatoka hapa tulipo kama tutabaki kama tulivyo.
Mhesimiwa Mwenyekiti, labda nikitolea tu mfano sasa labda kwanini nimeanza na utangulizi huu mrefu, nimeyasema haya yote kwa sababu ninatambua umuhimu wa kufanya mabadiliko katika sekta ya elimu na kwakweli ndiomana nasema nimefurahishwa sana na michango yote ya Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia katika Wizara hii, michango yote ni mizuri sana yenye afya na yenye tija katika sekta ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kuwakumbusha tu kwamba, sasa tunaposema tunafanya mabadiliko tunakubali wote kwamba kuna changamoto, kama kuna changamoto lazima tuwe na mahali pa kuanzia na tunaposema mahali pa kuanzia kwa mfano, nikianza sasa kutoa mifano, tunaposema walimu wawe bora ni dhahiri kwamba, kuna baadhi ya Walimu pengine inawawezekana wakawa wamepita wasiokuwa na sifa ambazo ni stahiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itakapokuwa inachukua hatua za kukagua na kuhakikisha kwamba walimu waliopo wanasifa mtuunge mkono maana kunakuwa na ile ku-symphasize kupita kiasi kwa hiyo mara nyingi tunaonea huruma watu badala ya kuionea huruma nchi na ndiyo matatizo yanakuwa yako mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la wanafunzi wa St. Joseph ambalo limejitokeza sana katika michango ya Waheshimiwa Wabunge wengi walipokuwa wanachangia hoja yangu. Hili suala nimeliongea kwa kirefu katika hotuba yangu na nirudie tu kusema kwa kifupi ni kwamba, hawa wanafunzi nimesikia michango mingine wanasema kwamba walikuwa wanasifa za wakati huo, mimi kwa kweli sijafahamu ni lini Serikali hii kulikuwa na sifa ya mwanafunzi kwenda kusoma digrii akiwa amemaliza kidato cha Nne akiwa na ufaulu wa D nne. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kuna wengine humu ndani wanafahamu kwa heshima kabisa ili tuweze kwenda vizuri, wanisaidie kwa sababu kuwa Waziri haina maana unafahamu kila kitu, sipuuzi kabisa naheshimu michango ya watu, lakini pengine tuwe tunasaidiana kwa kuonyeshana na lini Tanzania hii tulishawahi kuwa na sifa za mwanafunzi kujiunga na Chuo Kikuu akiwa na ufaulu wa Kidato cha Nne na „D‟ mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo majibu niliyoyatoa na maelezo niliyoyatoa mbele ya Bunge lako yanazingatia hali halisi ya elimu na kumekuwa na kuchanganya kati ya sifa ya kujiunga na Chuo Kikuu na sifa ya kujiunga na Cheti cha Ualimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwamba, hata katika kujiunga na cheti cha uwalimu hawa wanafunzi walipokuwa wanadahiliwa mwaka 2013/2014 ilikuwa ni ufaulu wa point 27 ambazo ni sawa mtu awe na angalau D 6 na C moja ndiyo ilikuwa kiwango cha chini. Kwa hiyo, wale ambao walikuwa wanajua kwamba zilikuwepo sifa za namna hiyo, nikizipokea Wizara yangu itapitia kwa kuzingatia pia na hizo taarifa ambazo mpaka sasa hivi hazipo mezani kwangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa nataka kusema sasahii ndiyo mfano ambao tunakuwa tunasema tunataka mabadiliko lakini pale ambapo hatua mahsusi zinapochukuliwa za kuonesha kwamba, tunataka kuwa na elimu iliyo bora pia sasa tunakuwa tunapata pingamizi au tunakuwa tunapata malalamiko. Ninawaomba sana Waheshimiwa mtuunge mkono katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ni sawa na kiwanda bahati mbaya ndugu yangu Mheshimiwa Mwijage ana shughuli hayupo hapa maana kila siku ndiyo eneo lake kila akisimama anazungumzia masuala ya viwanda na ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu mambo ya kilimo. Nataka tu kusema kwamba, elimu ni sawa na kiwanda, haiwezekani kama wewe unataka kutengeneza nguo kiwandani ukaanza na pamba iliyo mbovu ukategemea utoe nguo iliyo bora, haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kupata products nzuri kiwandani lazima na malighafi ziwe na ubora ulio mzuri. Kwa hiyo, hii inakwenda hivyo hivyo hata katika sekta ya elimu. Haiwezekani uwe na wahitimu wazuri wanaoweza kuchangia katika kuleta maendeleo katika nchi hii wakati unaowadahili wana viwango vya chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi mwanafunzi amefeli katika somo, katika level ya Kidato cha Nne unampeleka akachukue digrii na kwa miongozo ya Wizara ya Elimu, mwanafunzi mwenye digrii ya uwalimu anatakiwa afundishe A-Level. Yeye mwenyewe hajafika, yeye mwenyewe hakufaulu halafu anatakiwa akafundisha A-Level hivi kweli itawezekana! (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge, naomba katika hili mtuunge mkono na kwamba, mturuhusu tuendelee kufanyakazi ambayo wote kwa siku mbili mmekuwa mkichangia kwamba mnataka kuona elimu hii inakwenda vizuri. mtuunge mkono kwamba, huo ni mwanzo tu tutaendelea kusafisha katika elimu, tutaendelea kusafisha katika vyuo vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kama wapo ambao wamekwisha maliza wako katika soko la ajira tutafika hata huko. Tusipofanya hivyo tutakuwa tunayasema haya kila siku. Kwa hiyo, ninachotaka kusema ni kwamba, hilo suala tutalifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sioni utofauti unapozungumzia mtumishi hewa sioni tofauti na mfanyakazi asiyekuwa na sifa akikaa mahali. Tofauti tu ni kwamba, mmoja, ni mtumishi hewa haonekani kabisa, lakini mwingine ni mtumishi hewa amekaa mahali ambapo hastahili na hawezi kuleta tija katika Taifa hili. Kwa hiyo, kwasababu mmekuwa mnachangia kwa siku mbili mfululizo ninaamini kwamba, michango yenu ilikuwa inatoka moyoni na mlikuwa mnachangia kwa dhati kabisa na ndiyo maana nimesema bila kujali mchango umetoka upande gani, kwa sababu haya ndiyo malengo ya Serikali ya Awamu Tano katika sekta ya elimu. Nashukuru kwamba, wote tuna-share vision moja na Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii tuliyoifanya St. Joseph haitaishia hapo, kazi ndiyo imeanza na kwa heshima tu labda ya wale ambao wako kwenye utumishi wanatumi vyeti feki, wanatumia qualification feki. Mimi niseme kwamba, mjitoe katika Utumishi wenu kwa heshima yenu, vinginevyo tutawafikia, wajitoe wenyewe, wajisafishe wenyewe kwa sababu tunaposema mnataka mabadiliko basi mkubali mabadiliko ya kweli ni mabadiliko ya kweli ni kuthubutu kuchukua hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nguvu na ujasiri wa kuthubutu tunao na hatua tutazichukua. Kwa hiyo, hili suala la St. Joseph ni mwanzo tutaendelea kama nilivyosema tutavikagua Vyuo kama vina watu ambao hawana sifa tutawaondoa. Pia kama mlivyoshauri na ninaungana na ninyi kabisa kwamba, tutaangalia na hatua za ziada za kuchukua kwa sababu haiwezekani kufanya utapeli, unawapotezea muda vijana kwa kitu ambacho unajua kabisa mwisho wa siku hawatafika popote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kwa kweli ndugu yangu Mwanasheria Mkuu wa Serikali atanisaidia tuangalie hatua gani za ziada zitachukuliwa lakini suala la wale wanafunzi kurudi pale halipo, isipokuwa tutaangalia kuwashauri kulingana na sifa zao, kwa sababu kuna nafasi mbalimbali katika elimu basi wanaweza wakaenda katika nafasi nyingine ambazo zipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata humu ndani kama kuna watu wembe ni huo huo. Ni lazima tukubali kwamba Kiongozi ni kuwa mfano, kwa sababu haiwezekani tu tuwe tunakemea. Haiwezekani sisi tuwe wa kwanza kupaza sauti halafu sisi wenyewe tunakuwa na matendo hayo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie eneo lingine ambalo limechangiwa kwa nguvu sana, suala la ada elekezi; Kwanza nimefurahi kuona kwamba humu ndani hata nikiamua kufanya kikao cha kutoa maelekezo kuhusu shule nitapata tu column ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa wengi ambao wamechangia wamekuwa wanasema ni wamiliki wa shule, wengi humu ndani wameonyesha ni wamiliki wa shule, ni jambo jema. Lakini tu niseme kwamba ni kwa nini Serikali ilianza huu mchakato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la ada elekezi lilianzia humu ndani ya Bunge lako Tukufu, ambapo Waheshimiwa Wabunge mmekuwa mkitumwa na Wawakilishi wenu muihoji Serikali kwamba, ni kwa nini Serikali inaziachia shule zipandishe ada kiholela? Huu ndiyo msingi na chimbuko la ada elekezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyokuwa nafuatilia mjadala kidogo nikawa nasema ndiyo hivyo, wanasema kila wakati kingereza every day is a new beginning kwamba, kila siku inakuwa na mambo yake, sina maana kama napinga maoni yaliyotolewa lakini tu nilikuwa nataka tukumbuke historia ambapo tumetoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo katika hili suala la ada elekezi tumekuwa na hoja nyingi zimekuwa zinatolewa na wananchi mbalimbali wakilalamika kwamba, viwango vinapandishwa kiholela, humu ndani katika Bunge lako kukawa na ombi au maelekezo kwa Serikali kwamba ije na ada elekezi ili kutoruhusu shule kupandisha ada kiholela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii inaendelea kufanyika ambapo kulikuwa na mtaalam elekezi ambaye anatoka Chuo Kikuu Huria aliyekuwa amepewa kuifanya kazi hii. Hii kazi ilikuwa inafanyika kwa ushirikishwaji wa wamiliki wa shule binafsi na mpaka mwezi Februari kulikuwa tayari na majadiliano yanaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuifanya kazi hii ni kweli kumekuwa na changamoto hilo lazima nikiri, haikuwa rahisi sana kuweza kufikia viwango kutokana na kwamba shule ziko katika madaraja tofauti tofauti, kwa hiyo mwezi Februari tulikaa kikao cha pamoja na wamiliki wa shule binafsi kwa sababu wao ni wadau tulikuwa tunataka kitu cha ushirikishwaji ambacho tukikitoa wote tunakuwa tunaelewa kwamba misingi na sababu ya kufika tulipofika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kikao kile tulifikia hatua ya wote tulikubaliana hizi shule tulizozikagua viwango viko tofauti. Kwa hiyo, tukawa tumefikia hatua ya kwamba, tuweke madaraja lakini kabla hili zoezi halijakamilika wenzetu ambao tumekuwa tunafanya nao kazi upande wa pili, wamiliki wa shule binafsi wakawa wameona ni vema labda hili suala walifikishe huku. Kamati yangu ya Kudumu ya Huduma za Jamii tulifanya kikao cha pamoja kujadili suala la ada elekezi nafikiri ilikuwa tarehe 15 Aprili na katika kikao hicho hoja za pande zote zilizingatiwa na tukawa tumefikia muafaka kwamba, kwa sasa hivi hilo suala kwa sababu limechukua muda kulikamilisha na kumekuwa na changamoto, Kamati ikawa imetushauri kwamba kwa sasa Wizara tuna changamoto nyingi, hebu hilo tuendele kulitafakari na kuliangalia labda namna bora zaidi ya kuli-approach na Serikali ikawa imekubaliana na ushauri wa Kamati, tukawa tumesema kwamba kwa sasa hili suala la ada elekezi tutaendelea kulifanyia utafiti kwa kuzingatia changamoto ambazo zimejitokeza.
Kwa hiyo, mimi nilikuwa nasikiliza michango tu lakini kimsingi tulikuwa tunajadili suala ambalo ukurasa huo ulikuwa umeshafungwa tarahe 15 mwezi Aprili mbele ya Kamati. Ninashukuru hiyo michango mliyochangia tutaizingatia lakini hili suala lilikuwa limeshahitimishwa tarahe 15 mwezi Aprili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nimalizie kwamba suala hili la ada elekezi limehitimishwa kivipi, maana hilo ndiyo jambo la msingi. Kwamba kumekuwa na malalamiko ya shule za binafsi kupandisha ada na pia kumekuwa na michango ya kiholela. Kwa sasa hivi tulipofika makubaliano tuliyofika tutatumia taratibu zetu na ukiangalia katika hata Sera ya Elimu kabla ya hii mpya ambayo ilikuwa 1995, imeonyesha kabisa kwamba, shule binafsi zitaweka ada kwa kupata kibali cha Kamishna wa Elimu, kwa sasa hivi ofisi ya Kamishna wa Elimu itaendelea pamoja na Wakaguzi wa Shule kuendelea kuangalia uhalali wa ada zinazotozwa katika utaratibu ambao umeainishwa katika Sera ya Elimu na taratibu za elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado Serikali haiwezi ikajitoa kabisa katika hili jambo, kwa sababu humu ndani tunapozungumza tumegawanyika pande mbili. Wengine humu wanaochangia wanasema ni huduma wengine wanasema ni biashara, kwa hiyo tutakachokifanya hatuweki ada elekezi lakini ni ile tu kuangalia uhalali kwa sababu kuna shule nyingine Mwanafunzi anaambiwa kila mmoja mchango wa majengo sasa kama shule ilikuwa haina majengo ilisajiliwa vipi? Kuna michango mingine ambayo haina uhalali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kigezo kimojawapo ili uweze kupata usajili wa shule lazima uwe na majengo na je, unapowachangisha wazazi wachangie majengo yako ya shule na wao watakuwa wabia katika shule yako? Kwa sabaabu shule ni ya kwako mwenyewe. Kwa hiyo kuna mambo ambayo lazima kama Serikali tutayaangalia na kamwe hatuwezi kuyafumbia macho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shule zingine zinamtoza kila Mwanafunzi shilingi 100,000 kwa ajili ya Ulinzi, hiyo shule ina Walinzi wangapi? Je, kila Mwanafunzi ana mlinzi wake? Kwa hiyo ninachotaka kusema kwamba, katika msafara wa kenge na mamba wanakuwemo! Kwa hiyo hata katika shule binafsi katika msafara wa kenge…..hivyo hivyo! (Makofi na Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoendeleza maana ya ada elekezi haina maana Serikali itaacha tu mtu atumie kivuli cha shule, akilala, akiamka anawaambia wazazi kesho mje na kitu fulani. Tutaangalia, tutaenda katika utaratibu ambao tutakuwa tumekubaliana ambao utazingatia kanuni na taratibu zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie kuhusiana na suala la VETA kwasababu hili suala limekuwa linajitokeza kwa wachangiaji wengi. Ni kweli kumekuwa na ahadi ya Ujenzi wa VETA ambao labda kasi yake haijaenda kwa kiwango ambacho Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla walikuwa wanatarajia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaliarifu Bunge lako Tukufu kwamba katika hati idhini ya Serikali ya Awamu ya Tano, Vyuo vyote vya Maendeleo ya Jamii vimewekwa chini ya Wizara yangu, kwa hiyo niwaombe kwa dhati kabisa Waheshimiwa Wabunge mnipitishie bajeti yangu ili sasa niende nikaviangalie vile Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, mmekuwa mnaomba sana mpate VETA tutafanya ukaguzi tuangalie vina hali gani ili tuweze kuanza mara moja kuvitumia hivyo kwa sababu mtaji wa kuanzia utakuwa ni mdogo kuliko kuanza kujenga upya. Ninaamini kabisa hatua hiyo ya Serikali ya kuleta Vyuo vya Maendeleo katika Wizara ya Elimu itaweza kutatua kwa kasi kubwa suala hili la VETA ambalo kwa kweli ni muhimu sana.
Waheshimiwa Wabunge ningeomba tu niwasihi na kuwaomba sana, tunapozungumzia VETA tusizungumzie kwamba ni kwa sababu ya Watoto waliofeli, hapana! VETA ni kwa ajili ya kujenga uwezo, VETA ni kwa ajili ya kujenga ujuzi ili Watoto waweze kuleta tija, tusiichukulie kwamba ni chuo cha wale ambao wameshindwa kwa sababu inaweza ikatufanya tusipate watu ambao ni wazuri ambao wanaweza wakalisaidia Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie ndugu yangu alikuwa anaulizia kuhusu suala la VETA ya Ludewa na akawa anasema kwamba atashika shilingi yangu. Mheshimiwa Mbunge wa Ludewa wala huna haja ya kushika shilingi yangu, mimi na Serikali ni waaminifu, Serikali haiwezi kusema uwongo, tuliahidi tutajenga VETA Ludewa tutaijenga na pengine huioni katika kitabu kwa sababu inasomeka kama Chuo cha VETA cha Mkoa wa Njombe. Hiki Chuo cha VETA Mkoa wa Njombe kitajengwa katika Kijiji cha Shaurimoyo ambayo iko Ludewa, kwa hiyo utakuwa na bahati kwamba ni Chuo cha Mkoa lakini kinajengwa sehemu ya Ludewa, inapatikana katika ukurasa wa 59 wa kitabu changu cha bajeti.
Hivyo, Waheshimiwa Wabunge wamechangia na nikubaliane na ninyi kwamba kasi ya ujenzi wa VETA haijaenda kwa namna ambavyo tulikuwa tunatarajia, lakini naomba tu kwamba sasa kwa kuwa tumepewa hivi Vyuo vya Maendeleo ya Jamii mniruhusu kwamba nikalifanyie kazi, nikaviangalie vile ambavyo vitakuwa vinaweza kutumika mara moja na mdogo wangu Mheshimiwa Esther Matiko asubuhi alichomekea wakati Mheshimiwa Grace anachangia, kwa hiyo vyuo vyote katika Nchi nzima tutavitazama ili viweze kutumika mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo limechangiwa ni suala la Bodi ya Mikopo, suala la urejeshwaji wa mikopo pamoja na ule uhalali wa Bodi ya Mikopo ku-charge zile tozo zinazotolewa kwa Wahitimu. Kwanza kabisa nishukuru kwa michango yenu kuhusiana na suala hili la Bodi ya Mikopo na vilevile Waheshimiwa Wabunge walisema kwamba wana mambo ya ziada ambayo wanaweza wakanipatia ili niweze kuyafanyia kazi. Naomba sana, niko tayari kupokea michango hiyo na niwahakikishie kabisa nikiipata nitaifanyia kazi kwa sababu hizi fedha ni kwa ajili ya Watanzania na kwa ajili ya kuwakopesha watoto wa Kitanzania ambao hawana uwezo, kwa hiyo ni jukumu letu sote kusaidiana ili ziweze kurejeshwa kwa kasi inayotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie tu kwamba ni kwanini kumekuwa na hii retention fee katika Bodi ya Mikopo. Suala la retention fee linawekwa ili ile thamani ya fedha iweze kubaki pale pale. Nitasema viwango. Inawezekana ikaonekana 60 percent kwa sababu mtu amekaa nayo muda mrefu, kadri unavyochelewa kulipa ni wazi kwamba ile fedha itaongezeka, lakini kiwango ambacho kinatozwa cha value retention fee ni asilimia sita ya mkopo wa mwanafunzi lakini vilevile kunakuwa na administration fee ambayo inakuwa ni one pecent ya mkopo anaouchukua mwanafunzi. Hivyo, kadri mtu anavyochelewa retention fee inakuwa ni kubwa kwa sababu kuna wengine ambao walikopa tangu Bodi ya Mikopo inaanza lakini bado hawajarejesha mikopo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haina nia ya kukusanya mapato ya ziada kwa watu, kinachotakiwa, madam watu wanafahamu kwamba kunakuwa na retention fee, basi turejeshe mapema ili tusichajiwe kwa sababu ni hiari ya mtu ukirejesha mapema hautachajiwa, lakini wale ambao watachelewa ili thamani ya shilingi yetu iweze kubaki pale pale, ni lazima tuchaji hiyo retention fee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la urejeshwaji mikopo, changamoto zake zimezungumzwa kwa kirefu na mimi nikiri kwamba kama nilivyokuwa nimekiri kwenye hotuba yangu natambua kwamba kuna changamoto lakini kuna hatua ambazo tayari tunazichukua na vilevile kuna changamoto pia za kisheria. Baadhi ya maeneo katika Sheria ya Bodi ya Mikopo itakuwa vema kama ikifanyiwa marekebisho ili kuweza kuongeza kasi ya urejeshwaji ili kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kunufaika na mikopo inayotolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine lililozungumziwa ni suala la utekelezaji wa sera, kwamba kumekuwa na maswali hii elimu ya lazima ya miaka kumi inaanza kutekelezwa lini na kadhalika. Niseme tu kwamba, ukisoma Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, imeainisha wazi kwamba ili utekelezaji wa sera hiyo uwe fanisi, kuna sheria ambazo zinahitaji kufanyiwa marekebisho. Sasa hivi tuko katika hatua ya kupitia sheria mbalimbali, kwanza kuna Sheria ya Elimu sura ya 353, kuna Sheria ya Serikali za Mitaa sura ya 287 na sura ya 288 na sheria nyingine ambazo zitawezesha sasa hii Sera ya Elimu iweze kutekelezwa kwa ufanisi. Hivyo, tupo tunafanya kazi na nategemea katika Bunge lijalo, baadhi ya sheria tutazileta na natarajia pia hata katika Bunge hili, Sheria ya Marekebisho ya Bodi ya Mikopo nitaiwasilisha kwenu, kwa hiyo itakapokamilika na taratibu zake zikawa zimewekwa na mikakati ya kuangalia madarasa na walimu, basi hiyo Elimu ya Msingi ya miaka 10 ndipo itakapoanza rasmi, sasa hivi bado tunaendelea na mikakati ya kuhakiksha kwamba tunakamilisha maandalizi ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imezungumziwa ni kuhusiana na suala la kutokuwepo kwa mtaala wa elimu ya awali na kutokuwepo na walimu wa kutosha. Ningependa tu kusema kwamba, mtaala wa elimu ya awali unaounganishwa na muhtasari wake umeshaandaliwa. Nikiri tu kwamba mtaala ambao ulikuwa unatumika zamani sasa hivi umerekebishwa na wako katika hatua sasa ya kuandaa vitabu. Pia kuhusiana na idadi ya Walimu kuwa pungufu ni kwamba katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu iliongeza idadi ya Vyuo vinavyotoa mafunzo kwa ajili ya walimu wa elimu ya awali kutoka vyuo tisa hadi vyuo 13.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi tuna wananfunzi 3,200 ambao wanasoma ili wawe walimu wa elimu ya awali, kwa hiyo ninaamini kabisa kwamba jambo hili ni changamoto ambayo tunaikabili lakini tayari kuna hatua ambazo zinachukuliwa na ninaamini kwamba hawa watakapomaliza mwakani hili suala litatatuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika mafunzo ya walimu kunakuwa na somo la elimu ya awali ambalo ni somo la lazima kwa kila mwalimu na hivyo basi, pamoja na kwamba wale wanakuwa hawajabobea kwa maana ya specialization katika elimu ya awali lakini katika mafunzo yao ya Ualimu wamepata course ya elimu ya awali, kwa hiyo naamini kabisa kwa kutumia ujuzi huo wanakuwa wanaweza kuwafundisha vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango mwingine ambao umechangiwa kwa wingi sana na Waheshimiwa Wabunge ni kuhusiana na suala la ununuzi wa vifaa vya maabara. Ni kweli juhudi kubwa sana ilifanyika ya ujenzi wa maabara, na nichukue nafasi hii kuwapongeza sana wananchi wote, Halmashauri zote na watu wote walioshiriki katika ujenzi wa maabara hizi ambazo kwa sasa zimekamilika. Tunatambua kwamba maabara zilijengwa ili zitumike na ninaomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba Wizara yangu inafanyia kazi suala hilo kupitia mpango wa program yetu ya lipa kulingana na matokeo ambayo hii ni sehemu ya BRN.
Katika BRN kulikuwa na makubaliano na washirika wetu wa maendeleo kwamba, Wizara tunapokuwa tunatekeleza vigezo ambavyo tumekuwa tumewekewa, tunakuwa tunapata fedha ambazo kwa kweli zinakuwa na msaada mkubwa sana na hizo fedha tunazozipata katika Wizara yangu tunakuwa tunaachiwa uhuru tofauti na fedha nyingine za wafadhili ambazo wanakuwa wamekupangia, hizo ndiyo fedha pekee ambazo wanakupa halafu wanasema panga unavyotaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo pamoja na kwamba jukumu la kununua vifaa vya maabara liko katika ofisi ya Rais - TAMISEMI lakini niseme tu kwamba Wizara yangu imetenga kiasi cha shilingi bilioni 12 kwa ajili ya kununua vifaa vya maabara na tayari hizi ni katika fedha za mwaka unaokwisha, sasa tunavyoongea ni kwamba tumeelezea hata katika kitabu chetu iko katika ukurasa wa 75, kwa hiyo niwahakikishie kabisa kwamba hilo suala tunalitambua, tunataka wanafunzi wajifunze Sayansi kwa vitendo na siyo kwa nadharia kwahiyo shule zote ambazo zimejenga maabara na imekamilika kabisa, naomba niseme vizuri, shule ambazo zimejenga maabara na zimekamilika kabisa mpaka mwezi Februari tulikuwa tumezitambua shule 1,536 hizi zote zitapata vifaa. (Makofi)
Kwa hiyo, nichukue fursa hii pia kuzihamasisha Halmashauri nyingine ambazo hazijakamilisha ujenzi wa maabara basi nazo zikamilishe na niseme tu kwamba kwasababu hii program ya pay for results bado inaendela na kwa kutambua kwamba kipaumbele chetu ni kuboresha elimu yetu inayotolewa, niwahakikishie tu kwamba hizi fedha kila tunapozipata tutakuwa tunazitumia katika kuboresha elimu na tunatambua kwamba hatuwezi kuwa na elimu bora kama hatuna vifaa vya kufundishia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala la elimu maalum. Limechangiwa vizuri na Dada yangu Mheshimiwa Dkt. Elly Macha amezungumzia suala la kiwanda cha kuchapa vitabu na ile lugha ya alama na kadhalika kuhusiana na elimu maalum.
Naomba tu niseme kwamba, kama ambavyo nilikuwa nimesema katika hotuba yangu, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, elimu maalum itakuwa ni kipaumbele. Tutahakikisha tunanunua vifaa, tayari kuna fedha ambazo tumezitenga kwa ajili ya elimu maalum na ni fedha nyingi takribani bilioni 5 siyo hela kidogo hizo, tunataka kuhakikisha zile kero za msingi katika hii elimu maalum tunaziondoa. Kwa hiyo nirudie kuwahakikishia kwamba umuhimu wa elimu maalum tunautambua na katika bajeti yetu tumezingatia. Tumeweka fedha za kutosha na tutaendelea kuimarisha kadri uwezo wa kifedha unavyojitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Kiwanda cha kuchapa vitabu vya wasiiona pia nacho tutakifanyia maboresho na vilevile suala la lugha za alama nililipata nilivyoenda kutembelea Kilimanjaro, kuna changamoto kule kwamba kuna shule ya wanafunzi wanafundishwa lakini wanakuwa wengi wanashindwa kwenda sekondari kwa sababu hakuna wataalamu, tayari tumeshaanza kulifanyia kazi na tunashirikiana na kitengo cha elimu maalum katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Wameniandikia andiko la mapendekezo ya jinsi gani ambavyo tunaweza tukatatua hilo suala la lugha za alama ili kuwawezesha wanafunzi hao kuendelea na elimu ya sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala ambalo limeongelewa kwa kirefu pia sana humu ndani, suala la watoto wa kike wanaopata mimba kuweza kurejea masomo yao. Hili suala la kuwarejesha wanafunzi ni suala ambalo najua limeanza muda mrefu kidogo na nakumbuka nilikuwa na Kamati, Mheshimiwa Zaynab Vullu nakumbuka alikuwa ni Mjumbe wa hiyo Kamati, tulishafanya hata na presentation muda, lakini na Mheshimiwa Suzan Lyimo na Margret Sitta wote walikuwa kwenye hiyo Kamati Maalum ilikuwa imeundwa ajili ya kuangalia ni kitu gani cha kufanya na pia walienda hata kutembela hata katika Nchi nyingine kuona, kimsingi pendekezo ambalo lilikuja ni kwamba, hawa wanafunzi wapewe nafasi ya kuweza kurudi shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Waziri mwenye dhamana ya elimu ambaye pia nina dhamana ya kuangalia elimu nje ya mfumo rasmi, elimu ndani ya mfumo rasmi sina pingamizi kabisa na hawa wanafunzi kurudi shuleni. Kitu ambacho tutafanya katika Wizara yangu ni kukaa na wadau ambao ni muhimu katika jambo hili hasa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, ili tuhakikishe kwamba tunapomuangalia binti arudi shuleni, lakini pia tusimsahau mtoto wake, kwa sababu binti ana haki ya kupata elimu lakini na huyu mtoto ana haki ya kupata malezi. Kwa hiyo, hicho kikao cha kuangalia utaratibu gani utawekwa ili hizi pande zote mbili ziweze kunufaika bila ya kuwa na madhara, tukiweza kuwa na utaratibu mzuri sioni kama kuna tatizo lolote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema michango ni mingi na nimejitahidi kuongea mengi lakini naona kengele ya kwanza imeshagongwa, siwezi kuyamaliza yote lakini niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba hoja zenu zote tutazijibu na tayari tuna rasimu hii hapa – tumeshaanza kuzijibu, tutamalizia na tutawakabidhi. Kwa hiyo wale ambao pengine hoja zao sijazijibu naomba tu msione labda pengine siyo za muhimu ni kwa sababu ya muda, michango yote kama nilivyosema ni muhimu, michango yote ina tija na mtapata majibu kwa maandishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa nigongewe kengele ya pili, nihitimishe hoja yangu kwa kukushukuru sana wewe Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kutuongozea majadiliano, nashukuru sana pia Naibu Spika ambaye tulianza naye jana na Wenyeviti wote ambao wameshiriki katika kuongoza majadiliano ya hoja hii. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu na sasa ninaomba sana kwa heshima kubwa mniunge mkono ili nikafanye kazi ambayo mnataka tuifanye. Naomba muunge mkono hoja yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 3 wa Mwaka 2017
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa fursa hii.
Kwanza nianze kwa kusema kwamba naunga mkono hoja ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu Marekebisho ya Sheria ambayo imewasilishwa mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa nitumie fursa hii moja kwa moja kutoa ufafanuzi katika baadhi ya mambo ambayo yamesemwa kuhusu sekta ya elimu na suala ambalo limezungumziwa hapa ni kuhusiana na usajili wa shule binafsi na kwamba wamiliki wa shule wamekuwa na changamoto mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusema kwamba Serikali ina utaratibu wa kupokea malalamiko na tumekuwa tunayafanyia kazi kadri ambavyo yanajitokeza. Kwa hiyo, kupitia fursa hii niwaambie wamiliki wa shule za binafsi kama kuna malalamiko yoyote wayawasilishe na nawahakikishia kwamba tutachukua hatua stahiki, kwa sababu moja ya jambo ambalo limesemwa kwamba kuna urasimu na kuna dalili za rushwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wote na wananchi wa Tanzania wote ni mashahidi jinsi Serikali ya Awamu ya Tano inavyopambana na rushwa. Kama kuna rushwa katika sekta ya elimu basi wahusika hawatasalimika. Tunachohitaji ni kupata taarifa ili tuweze kuzifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, imesemwa kwamba Serikali iache kuangalia shule binafsi ijikite katika kushughulikia Serikali yake. Niliambie Bunge lako Tukufu kwamba Serikali haiwezi kuacha kuangalia zile shule binafsi kwa sababu zinapaswa kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu na ni jukumu la Wizara yangu ni kuhakikisha kwamba wamiliki wote wa shule wanazingatia sheria, taratibu na kanuni ambazo tunajiwekea. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kuzisimamia na kwa wale ambao wanakiuka taratibu hatua dhidi yao zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa fursa hii
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuhitimisha hoja yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ningependa kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha kujadili hoja hii tangu jana nilipoiweka hapa mezani na hata sasahivi ambapo tunahitimisha. Nakushukuru wewe kwa kutuongozea vema mjadala wetu na ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao hakika niseme kwamba hoja hii imepokelewa vizuri sana na Wabunge wote na kimsingi Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia wameiunga mkono hoja hii, lakini wamekuwa tu maeneo machache ambayo wametoa mapendekezo ili Serikali iweze kuangalia na kuweza kuboresha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee niishukuru tena Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Peter Serukamba kwa ushirikiano mkubwa ambao ameutoa tangu Serikali ilipowasilisha muswada huu. Hakika Kamati imefanya kazi kubwa, wamechambua Taarifa ya Kamati iligawiwa Bungeni jana, mmeona ni jinsi gani Kamati kwa kweli imeutendea haki huu muswada, sisi Serikali tunasema tunashukuru sana, asilimia kubwa ya maoni ambayo yametolewa na Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Serikali imeyapokea na mtayaona tutakapokuwa tunapitia kifungu kwa kifungu tumeweza kuyafanyia kazi. (Makofi)
Pia nashukuru upande wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pia kwa maoni yao ambayo wameyatoa na mengine Serikali imeweza kuyazingatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja hii ilichangiwa na jumla ya Waheshimiwa Wabunge 20 ambao walionga na Wabunge kumi ambao wamechangia kwa maandishi.
Napenda kuchukua nafasi hii kutoa shukrani za dhati kabisa kwa Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao ambayo kwa kweli michango yote ilikuwa inalenga katika kuhakikisha kwamba tunatengeneza chombo ambacho kitaenda kuisaidia nchi yetu kuhakikisha kwamba mwalimu anakuwa na hadhi, pia upande mwingine kitahakikisha kwamba hakuna suala ambalo labda litakuwa linaongeza gharama na michango kwa walimu ambayo itakuwa inawapa mzigo. (Makofi)
Kwa kuwa kanuni haziniruhusu kutaja majina ya Waheshimiwa Wabunge waliochangia, basi niseme tu kwamba, orodha yao ya majina ninayo hapa na nitaomba iingie kwenye Hansard.
Orodha ya Majina ya Waheshimiwa Wabunge waliochangia Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania, 2018 kwa kuzungumza na maandishi kama yalivyowasilishwa Mezani:-
Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwa kuzungumza ni Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest, Mheshimiwa Othman Omary Haji, Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba, Mheshimiwa Jumanne Abdallah Maghembe, Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe, Mheshimiwa Joram Ismael Hongoli, Mheshimiwa Allan Joseph Kiula, Mheshimiwa Richard Phillip Mbogo, Mheshimiwa Balozi Dkt. Deodoriou B. Kamala, MheshimiwaEdward F. Mwalongo, Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mheshimiwa Seif Khamis Said Gulamali, Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mheshimiwa Susan Anselm Lyimo, Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya, Mheshimiwa Pascal Yohana Haonga, Mheshimiwa Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, Mheshimiwa Almas Athuman Maige na Mheshimiwa Salum Mwinyi Rehani.
Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwa maandishi ni Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mheshimiwa Zainabu Mndolwa Amir, Mheshimiwa Zainabu Mussa Bakar, Mheshimiwa Omar Abdallah Kigoda, Mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola na Mheshimiwa Omar Mohamed Kigua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo ya utangulizi sasa naomba kwanza niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri ambao wametangulia na wameweza kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja na vipengele ambavyo vilizungumziwa na wachangiaji ambao wamezungumzia muswada huu. Kwa hiyo, nashukuru kwa michango yao na ningependa kujikita katika kuzidi kuweka msisitizo wa madhumuni ya kuanzisha Bodi ya Utaalamu wa Walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na mkanganyiko kwamba sasa hii inakuwa inasababisha walimu wanakuwa na vyombo vingi vya kuwahudumia na kwamba Bodi ya Utaalam wa Walimu inaenda kuchukua kazi za Tume ya Utumishi wa Walimu. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba hakuna muingliano wowote wa kimajukumu kwa sababu Tume ya Utumishi wa Walimu iko chini ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na jukumu lake ni kuangalia utumishi wa walimu katika sekta ya umma. Kwa hiyo, wao wanajikita katika kuangalia masuala ya kiutumishi na katika Tume ya Utumishi wa Walimu walimu wanakuwa kuna kumbukumbu kama ambavyo hata hapa Bungeni bila shaka kunakuwa na kumbukumbu ya kuonesha kwamba, Bunge lina Wabunge wangapi, kutoka Jimbo lipi na kadhalika. Kwa hiyo, ile register ambayo inatunzwa na Tume ya Utumishi wa Walimu ni kwa ajili ya taarifa za kumbukumbu za kiutumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bodi ya Utumishi wa Walimu tutaweka register ambayo itatuwezesha kutambua walimu walioko nchini katika sekta ya umma, katika sekta binafsi, pia itakuwa inatambua hata walimu ambao ni wageni kutoka nje ya nchi. Tume ya Utumishi wa Walimu inasimamia nidhamu ya walimu kiutumishi. Ukiangalia hata Kanuni za Tume ya Utumishi wa Walimu kwenye masuala ya nidhamu inasema kwamba masuala ya nidhamu ya kiualimu yatazingatia taratibu za utumishi wa umma. Sasa katika Bodi ya Utaalam wa Walimu tunataka kuangalia zaidi katika maadili na miiko ya walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hakuna mtu ambaye hafahamu umuhimu na thamani ya mwalimu. Mwalimu ni kioo cha jamii, mwalimu ni mtu ambaye anakaa muda mwingi na watoto wanapokua katika umri wa kwenda shule kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne. Ukiangalia saa ambazo watoto wanakaa shuleni ni nyingi zaidi kuliko hata yale ambayo wanakaa na wazazi. Kwa hiyo, ni lazima tuhakikishe kwamba tunalinda maadili, haiba ya mwalimu, utendaji wake na muonekano wake katika jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hii Bodi ya Utaalam wa Walimu ambayo tunaiunda itakuwa pia inaangalia miiko na maadili ya walimu. Kwa hiyo, hata masuala ya mavazi, nafahamu kwamba hata masuala ya mavazi kwenye utumishi wa umma yameainishwa, lakini hapa tunataka kuweka msisitizo zaidi ili hata zile adhabu zinazotolewa kwa sababu makosa katika utumishi wa umma yameweka pamoja na adhabu, lakini pengine kutokana na umuhimu wa walimu kuna makosa mengine ambayo yanadhalilisha taaluma ya walimu. Tunataka kuhakikisha kwamba yale makosa ambayo yanashusha hadhi ya ualimu yanakuwa yanashughulikiwa na bodi ambayo imeundwa mahususi katika kuangalia utaalamu wa ualimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo wamezungumza waliokuwa wanajibu hoja waliotangulia ni kwamba, hata taaluma nyingine zinazo bodi zao ambao zinasimamia. Kwa hiyo, mimi niseme kwamba tumechelewa sana kuanzisha Bodi ya Utaalamu ya Walimu kwa sababu wenzetu wahandisi jana walikuwa wanasherehekea miaka 50 ya Bodi ya Makandarasi, lakini leo hii walimu ambao ndiyo fani ambayo ni muhimu, hata hao makandarasi wasingeweza kufika hapo bila kuwa na mwalimu. Kwa hiyo, ualimu ni fani ambayo kwa kweli, ndyo taaluma mama kwa sababu, walimu ndiyo wanazalisha hata hizi profession nyingine ambazo tayari zimekuwa na bodi.
Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge kama ambavyo mmekuwa mkiunga mkono wakati wa uchangiaji naomba kabisa hata tutakapokaa katika session ya kupitia kifungu kwa kifungu muendelee kuunga mkono ili hatimaye hili jambo ambalo kwa kweli lilikuwa limechelewa basi liweze kupitishwa na tuweze kuanza kufanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge katika michango kuna jambo ambalo wengi waliokuwa wanazungumza walionesha wasiwasi wa tozo zinazotolewa na kwamba kutakuwa na ada ya usajili, kwamba Serikali inakwenda kumbebesha mzigo mwalimu, ukiangalia kipato chake na hali halisi ya maisha.
Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba suala la tozo, suala la ada kwa kweli, Serikali haikusudii hata kidogo kumpa mwalimu mzigo wa ziada. Baada ya kusikiliza maoni na mapendekezo mtaona katika jedwali letu hata zile tozo za adhabu kwa kweli, tumezipunguza kwa kiasi kikubwa. Niwahakikishie kwamba baada ya huu muswada kupitishwa ni kwamba tutatunga kanuni na kanuni zitakapokuwa zinaandaliwa zoezi la uandaaji wa kanuni litakuwa ni shirikishi. Kwa hiyo, ada itakuwepo, lakini itakuwa ni kiasi kidogo sana ambacho hakuna mwalimu ambaye ataweza kushindwa, lakini pia haitakuwa ni suala ambalo litakuwa ni mzigo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaona katika marekebisho ambayo tumeyaleta kwa kweli, hili suala tumelizingatia sana, lakini niwahakikishie kwamba hata katika hatua ya kutengeneza kanuni tutahakikisha kwamba suala la gharama linazingatiwa kwa sababu si lengo la Serikali kumpa mzigo mwalimu kwa sababu tunathamini kazi ya ualimu na tungependa kwa kweli walimu waendelee kulitumikia Taifa hili kwa moyo wao wote. Kwa hiyo, kwa namna yoyote ile Serikali isingependa kuwapa mzigo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limezungumzwa ni kwamba uwakilishi wa Vyama vya Walimu katika Bodi na kwamba kuwe na uwakilishi katika muundo wa bodi na kadhalika. Niseme kwamba suala hili limezingatiwa na imekuwa ni vigumu kwa Serikali kuweza kutaja kwamba labda ni chama gani cha walimu kitaingia kwa sababu hata walimu wenyewe hawana chama kimoja, kuna Chama cha Walimu Tanzania, kuna chama kinachotetea haki na maslahi ya walimu. Kwa hiyo, hata walimu kama wao hawana umbrella moja au hawana chama kimoja ambacho kinatetea maslahi yao. Sisi kama Serikali kwa sababu vyama vyote vimeanzishwa kisheria tutakachokifanya vyama vyote vitakuwa vinatambuliwa na unaweza hata ukawekwa utaratibu kama itakuwa ni kwa rotation, lakini kitu kikubwa ambacho tutazingatia ni sifa za mtu ambaye anateuliwa kuingia katika bodi. Jambo la msingi kwa sababu ni suala la uwakilishi na ni suala la majukumu kwamba anakuja kutekeleza jukumu fulani, kwa hiyo, uwakilishi katika vyama vya walimu utazingatiwa, lakini kubwa zaidi itakuwa ni weledi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie pia hata katika suala la uteuzi wa Wajumbe wa Bodi na pia suala la uadilifu na suala la weledi na utaalam kwa sababu anakuja kusimamia utaalam wa walimu. Ni dhahiri kwamba mtu ambaye anapaswa kufanya hivyo lazima kwanza yeye mwenyewe awe amethibitika bila shaka kwamba amefuzu na ana vigezo vinavyotakiwa lakini pia hata na uadilifu wake usiwe unatia shaka, kwa sababu wewe huwezi ukasimamia maadili ya wenzako wakati na wewe uadilifu wako unatiliwa shaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie kwamba suala la uteuzi wa Wajumbe wa Bodi ni kuhakikisha kwamba wanateuliwa kwa kuwakilisha zile taasisi zote ambazo zinamhusu mwalimu utaona katika ile composition tumependekeza hata hii Tume ya Utumishi wa Walimu wawepo ndani ya Bodi na kama kutakuwa na kujitokeza jambo lolote huko mbele ambalo labda litakuwa na muingiliano basi yule Mjumbe kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu anaweza akawa analiona na kuliratibu vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwa kusema kwamba naomba sana Waheshimiwa Wabunge wote tuunge mkono muswada huu ambao madhumuni yake makubwa ni kuweka utaratibu wa kisheria wa kusimamia hadhi na viwango vya ubora wa walimu katika nchi yetu na kutoa leseni kwa walimu wote walio katika sekta ya umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida nyingine ambayo tutaipata kutokana na muswada huu, muswada huu unaweza ukamzuia mwalimu ambaye anafukuzwa kazi kwa makosa ya kuiuka maadili katika utaratibu wa sasa Tume ya Utumishi wa Walimu inamuondoa kwenye register, lakini mwalimu huyu anaweza akaenda akafundisha shule binafsi wakati anawafundisha watoto wa Kitanzania.
Kwa hiyo, sasa hivi kupitia Bodi ya Utaalam wa Walimu mwalimu ambaye ataonekana kwa kweli hana maadili ambayo yanaendana na fani ya ualimu akiondolewa kwenye bodi hataweza kufundisha mahali popote kwenye Serikali au binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bodi itaandaa code of professional conduct yaani itakuwa inasimamia maadili ya utaalam wa walimu wakati Tume ya Utumishi wa Walimu inasimamia maadili ya walimu kama watumishi wa umma na imejikita tu kwa watumishi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hakuna mtu asiyefahamu changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza katika shule binafsi. Hakukuwa na sheria ambayo inabana moja kwa moja viwango na maadili ya walimu ambao wanaajiriwa katika shule binafsi.
Kwa hiyo, kupitia sheria hii sasa walimu pia wanaoajiriwa katika shule binafsi, walimu wa shule za awali, shule za msingi, sekondari, vyuo vya ualimu na taasisi ambazo zinatoa mafunzo ya elimu ya watu wazima wataweza kudhibitiwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo ya ufafanuzi huo sasa kwa heshima kubwa kabisa naomba Waheshimiwa Wabunge wote tutakapokaa kama Kamati kwa pamoja tuunge mkono na kupitisha Muswada huu wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa mwaka 2018 (The Tanzania Teachers’ Professional Board Bill, 2018).
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili nichangie hoja iliyoko mbele yetu.
Kwanza nianze kwa kusema kwamba, naunga mkono hoja hii na nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa mapendekezo mazuri katika sekta ya elimu. Vilevile nipende kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wameleta michango mizuri kwenye elimu na kwa sababu ya muda sitaweza kugusia maeneo yote mliyoyazungumzia, lakini niseme tu kwamba michango yenu ni mizuri, tunashukuru sana na tutaizingatia tunapokuwa tunafanya mapitio na kutengeneza ule Mpango wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa tu kuzungumzia masuala machache na ningependa nianze na suala la elimu bila malipo kwa sababu limezungumziwa kwa nyanja tofauti, katika sura ya pongezi na katika sura ya kutoa changamoto na yote tumeyapokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa tu kuweka wazi jambo moja kwamba, suala la elimu bila malipo linaongozwa na Waraka wa Elimu Na. 6 wa mwaka 2015. Waraka huu umebainisha wazi majukumu ya Serikali, majukumu ya wazazi na wadau wengine wote. Kwa hiyo, kuna wengine wanakuja na dhana kuwa Serikali inafanya utapeli, kwamba imewaahidi wananchi kwamba itakuwa ni elimu bure lakini inachangisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni dhana potofu ambayo ningependa Watanzania waifahamu kwamba waraka umebainisha wazi kabisa, kuna majukumu ya mzazi ambayo bado mzazi atawajibika kumnunulia mtoto wake uniform, mzazi atawajibika kugharamia matibabu ya mtoto wake na kumnunulia vifaa vinavyotakiwa kwenda navyo shuleni. Serikali inatoa capitation grant kwa ajili ya wanafunzi, Serikali imeondoa ile ada ambayo mwanafunzi alikuwa analipa ambayo ni shilingi 20,000/= kwa mwanafunzi wa kutwa na shilingi 70,000/= kwa mwanafunzi wa bweni. Vilevile Serikali imeondoa gharama za mitihani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashindwa kuelewa kwa nini baadhi ya watu wanabeza, wakati nikiwa Baraza la Mitihani tulivyokuwa tunatangaza matokeo, wanafunzi wa Tanzania wengi kwa maelfu walikuwa wanazuiliwa matokeo yao ya mitihani kwa sababu ya kushindwa kulipa ada, leo hii Serikali imewaondolea, badala ya kushukuru, tunaibeza. Kwa hiyo, naomba tu niseme kwamba majukumu yameaninishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ningependa kuliweka wazi, Serikali haijakataza wananchi kuchangia katika maendeleo ya elimu. Imeweka wazi kabisa kwamba bado jamiii ina wajibu wa kutoa ushirikiano katika shughuli za kuleta maendeleo katika maeneo yao. Bado imeeleza wazi kwamba jamii ina wajibu wa kuendelea kujitolea nguvu kazi na mali ili kuleta maendeleo katika shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na Mbunge ambaye amechangia asubuhi, akasema kwamba kuna matatizo katika Jimbo lake na kwamba anatoa mifuko 1,500, Waheshimiwa Wabunge wengine wote ruksa fedha zenu za Mifuko ya Majimbo msije mkaacha kuchangia katika sekta ya elimu eti kwamba Serikali imekataza, hakuna hicho kitu. Nimeona nitoe huo ufafanuzi kwa sababu naona labda hii dhana inaweza ikapotoshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuzungumzia kwa kifupi pia suala la ubora wa elimu ambalo limezungumziwa. Naomba niwahakikishie Watanzania kwamba Wizara yangu imejipanga na tuna nia thabiti kabisa ya kuhakikisha ubora wa elimu katika nyanja zote, kuanzia elimu ya awali mpaka elimu ya juu. Tutafanya hivyo kwa kuhakikisha kwanza kwenye elimu ya msingi mpaka sekondari tunafanya ufuatiliaji wa karibu, Wakaguzi wetu tayari wameshaelekezwa kufanya ufuatiliaji kwa kuangalia kile kinachofundishwa darasani, kwa sababu maarifa na stadi zinapatikana ndani ya darasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile mamlaka zetu ambazo zina wajibu wa kudhibiti elimu ya kati na elimu ya juu, tutahakikisha kwamba zinafanya kazi zao kwa weledi na vigezo vyao wanavyovitumia katika kuangalia kwamba chuo kinafaa, chuo kina sifa, ni lazima viwe ni vigezo ambavyo kweli vitatutolea wahitimu ambao wana ubora ambao tunauhitaji katika kuipeleka nchi yetu katika uchumi wa kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuzungumzia pia kidogo kuhusu elimu kwa watu wenye ulemavu. Nashukuru sana kwa michango iliyotolewa na niseme tu kwamba ni suala ambalo mimi kama mama, kama Waziri mwenye dhamana ya elimu linanigusa sana. Niseme kwamba Watanzania wenye ulemavu ni asilimia ndogo ukilinganisha na Watanzania ambao hawana mahitaji maalum. Hivyo basi Wizara yangu itahakikisha kwamba wana…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Nashukuru sana Mwenyekiti naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 – Wizara ya Fedha na Mipango
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa kunipatia nafasi na mimi nichangie hoja hii iliyoko mbele yetu na nianze kutoa pongezi za dhati kabisa kwa Waziri wa Fedha, Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa bajeti nzuri ambayo wameiwasilisha mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii na nitatoa sababu kwa nini naiunga mkono hoja hii. Bajeti hii imeandaliwa kwa umakini mkubwa na ina dhamira ya dhati kabisa ya kuondoa matatizo ya wananchi na kuleta maendeleo. Ukiangalia sekta ya elimu, sekta ya elimu imetengewa kiasi cha shilingi trilioni 4.77 ambayo ni sawa sawa na asilimia 22.1 ya bajeti yote hii na mgawanyo huu wa fedha unaonesha bayana, jinsi gani ambavyo Serikali ina dhamira ya dhati ya kuwahudumia wananchi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa elimu katika maendeleo ya nchi hii na ndio maana fedha zimetengwa za kiasi kikubwa na fedha hizi nyingi zitaelezwa katika miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naipongeza Wizara ya Fedha,kwa kuja na vyanzo vipya vya mapato ambavyo vitaiwezesha Serikali kupata fedha, za kutekeleza mpango ambayo imeahinishwa na kama walivyozungumza wachangiaji wengine, hii ni bajeti ya mwaka mmoja tu.
Mheshimiwa Naibu Spika,hii bajeti imetokana na Mpango wetu wa Maendeleo wa Miaka Mitano na imezingatia katika kutufikisha kule ambako tunatarajia kufika ukizingatia Ilani yetu ya uchaguzi na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, kwa hiyo niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuiunge mkono tukitambua kwamba hii ni bajeti ya mwaka mmoja, haiwezi kumaliza matatizo yote kwa sababu Serikali inakwenda hatua kwa hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kuunga mkono bajeti hii ya mwaka mmoja, kutaiwezesha Serikali kuanza hatua yake ya kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo, katika maeneo ambayo yameainishwa. Vilevile napongeza kwa dhati kabisa, hatua za Serikali za kubana matumizi na kudhibiti matumizi yasiyokuwa ya lazima, hii yote inaonesha jinsi gani ambavyo Serikali ina dhamira ya dhati kabisa kuwatumikia wananchi wake hivyo tuna kila sababu ya kuunga mkono bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba sasa nizungumzie kidogo masuala ambayo yalielekezwa katika sekta ya elimu na kutokana na muda nitazungumzia mambo machache na mengine tutayajibu kwa maandishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, limejitokeza suala la fedha za utafiti,na Waheshimiwa Wabunge wameonesha wasiwasi wao kwamba kiasi cha fedha kilichotengwa ni kidogo na kwamba msisitizo katika utafiti wa kilimo, haupewi kipaumbele kinachotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kusema kwamba Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya utafiti, kupitia kwenye Tume ya Taifa ya Utafiti yaani COSTECH; na kuna kazi nyingi ambazo zimekuwa zikifanyika na utaratibu tu ambao umekuwa ukitumika ni utaratibu wa ushindani. Kumekuwa na hoja kwamba kwa nini utumike utaratibu wa ushindani kutoa fedha za utafiti?
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa ushindani kwanza unaihakikishia Serikali kwamba yule anayeomba fedha yuko tayari, kwa maana ya kwamba tayari atakuwa na mpango kazi wake. Anajua anataka kufanya nini kwa hiyo inaihakikishia kwamba yule anayepata fedha kwa ushindani anakuwa anazitumia fedha hizo vizuri, badala ya kuzigawa hata kwa mtu ambaye hajawa yuko tayari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia suala la ushindani jumla ya miradi 102 imeweza kufadhiliwa,na ambapo kuna masuala mengi tu yamefanyika ikiwa ni pamoja na kujenga rasilimali watu kuwajengea uwezo wa kuweza kufanya utafiti; na katika hilo jumla ya watafiti 517 wamepatiwa mafunzo na jumla ya watu 130 wamepata mafunzo katika ngazi ya uzamili na uzamivu. Vilevile fedha za utafiti zimewezesha kujenga miundombinu ya kufanyia utafiti ambapo kwa mfano Serikali imeweza kujenga mabwawa 42 ya zege na kukarabati maabara za uzalishaji wa vifaranga vya samaki katika Chuo Kikuu cha Sokoine.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika bajeti ya mwaka 2016/2017 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 12.8 kwa ajili ya suala la utafiti. Lakini pamoja na fedha hizi, bado Serikali itaendelea kupata fedha kupitia kwa wafadhili mbalimbali ambao wamekuwa wakipeleka fedha hizo moja kwa moja katika vyuo vyetu vya elimu ya juu.
Suala lingine ambalo limezungumzwa katika Wizara yangu ni suala la kuitaka Serikali iangalie kozi zinazoanzishwa katika vyuo vya elimu ya juu, kujiridhisha kama kuna walimu wa kutosha. Niwahakikishie Watanzania kwamba katika kuhakikisha ubora wa elimu hiyo ndio kipaumbele chetu katika Awamu ya Tano. Hivyo basi hakuna kozi yoyote ambayo itaanzishwa kama Serikali haijaridhika na miundombinu, kama Serikali haijaridhika na uwepo wa elimu ambao wana sifa stahiki. Pamoja na kuangalia kozi mpya lakini niseme kwamba hata kozi ambazo zipo Serikali inafanya mapitio kuona kwamba kozi zote zinazotolewa katika elimu ya juu zina wataalam wa kutosha na ziko katika mazingira ambayo yanastahiki. Kwa hiyo, tutachukua hatua zinazostahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo limezungumziwa ni suala la ukarabati wa vyuo vikuu, pamoja na miundombinu ya kutolea elimu. Ukiangaliwa kitabu cha hotuba ya bajeti ya Waziri wa Fedha na kitabu cha hotuba cha Wizara yangu, tumebainisha wazi mikakati ya Serikali katika kuhakikisha kwamba tunakarabati miundombinu ya shule na vyuo vikuu ili kuhakikisha kwamba Watanzania na wananchi wanapata elimu katika mazingira ambayo ni rafiki na kama nilivyosema tunafanya hatua kwa hatua, kwa mfano katika mwaka huu wa fedha, tutaweza kufanya ukarabari kwenye shule kongwe 40. Lakini vilevile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambacho ni Chuo Kikuu kongwe tumekitengea kiasi cha shilingi bilioni tisa kwa ajili ya kufanya ukarabati na hili zoezi ni endelevu. Kama nilivyosema hii ni hatua tu, lakini ahadi zetu zitatekelezwa katika miaka mitano. Kwa hiyo tutaendelea kukarabati na kuhakikisha kwamba mazingira ya kujifunzia yanakuwa ni rafiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo limezungumziwa ni suala la elimu bure, kwamba hii sera iende mpaka kidato cha sita. Ninachoweza kusema ni kwamba kama Serikali, tumepokea huo ushauri lakini tungeomba kwamba kama tunavyosema tunataka utekelezaji wetu wa ahadi kwa wananchi uende hatua kwa hatua. Kwa hiyo tumeanza na mpaka kidato cha nne tungeomba kwanza tuendelee kuimarisha utekelezaji wa sera ya elimu bila malipo kwa kidato cha nne na kutatua changamoto ambazo zipo kabla hatujafikiria kuongeza wigo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine lililozungumziwa katika eneo langu ni suala la VETA kuwa na vifaa vya kisasa na hilo tutalifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama tena mbele yako ili niweze kutoa ufafanuzi wa hoja ambayo niliiwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu tarehe 13 Mei, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekito, Waheshimiwa Wabunge wametoa hoja mbalimbali, wakati wakijadili makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yangu kwa mwaka 2016/ 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumshukuru kwa dhati Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba na wajumbe wake kwa kuchambua na kujadili kwa kina bajeti ya Wizara yangu. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Hussein Bashe kwa kuwasilisha vyema Maoni ya Kamati hapa mbele ya Bunge lako Tukufu. Niseme kwamba Wizara yangu imepokea maoni na ushauri ambao umetolewa na Kamati yangu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na tutaufanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumshukuru Mheshimiwa Susan Anselm Lyimo, Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani na Naibu Waziri Kivuli wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani, na niseme kwamba ushauri ambao wameutoa utazingatiwa na Wizara yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuchukua fursa hii, kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa maoni mazuri na kwa michango yao ambayo wameitoa katika sekta ya elimu lakini pia ambayo waliitoa wakati wakijadili hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo jumla ya Wabunge 85 walichangia kuhusu sekta ya elimu. Katika hoja hii ambayo nimeiwasilisha tarehe 13 Mei; jumla ya Wabunge 53 walichangia hoja kwa kuongea na Waheshimwa Wabunge 57 walichangia kwa maandishi. Ninawashukuru sana Waheshimiwa wote kwa michango yao mizuri ambayo hakika itachangia kuimarisha sekta ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mjadala ulikuwa umeletwa kwa hisia na umekuwa ni mjadala ambao umeibua mambo mengi, lakini niseme tu kwamba Wizara yangu inapenda kulihakikishia kabisa Bunge lako Tukufu kwamba ushauri wote ambao umetolewa na Waheshimiwa Wabunge ambao unalenga kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata elimu iliyo bora inayoendana na mahitaji ya sasa, Serikali itauchukulia ushauri wao kwa uzito wa hali ya juu na itafanyia kazi mapendekezo yote na maoni ambayo Waheshimiwa Wabunge wametoa wakiwa na lengo la kuhakikisha kwamba azma ya Serikali yetu ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda inaweza kutekelezwa; na wakitambua kwamba elimu ndio nguzo pekee ya kutufikisha hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu imejipanga kutoa ufafanuzi wa hoja zilizotolewa na kwa kweli kutokana na umuhimu na michango mizuri ya Waheshimiwa Wabunge ningetamani kila ambaye alisimama hapa kuongea au aliyechangia kwa maandishi niweze kumpa fafanuzi. Hata hivyo kutokana na muda nilio nao sitaweza kutoa fafanuzi wa hoja zote. Naomba Waheshimiwa Wabunge mkubali kwamba nitatoa fafanuzi kwa yale ambayo nitaweza kujaliwa kulingana na muda, lakini ninawahakikishia kwamba hoja zenu zote ambazo mmezitoa nitawapa ufafanuzi kwa maandishi na nitaziwasilisha kwenu kabla hatujamaliza kikao hiki cha Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo sasa naomba kujibu hoja za Waheshimiwa na kwa sababu ya muda na kwa sababu pia siwezi kuwataja Waheshimiwa wote basi nitataja tu hoja bila kueleza nani ameisema, lakini nitakapotoa katika maandishi nitawatambua wote ambao wamezitoa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na suala la elimu maalum. Suala la elimu maalum limezungumzwa kwa hisia kali sana kuhusu changamoto ambazo watoto wetu wa Kitanzania ambao wana mahitaji maalum wamekuwa wakizipata katika jitihada zao za kupata haki yao ya msingi ya elimu. Kwa kweli mambo mengi yamezungumzwa kuhusiana na mazingira ambayo si rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, kuhusiana na vifaa vyao vya kujifunzia na changamoto nyingine ambazo wanazipata ambapo wengine wanalazimika kukaa shuleni hata hawaendi likizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba kama kuna kitu ambacho Wizara yangu inaipa kipaumbele ni hawa watoto wenye mahitaji maalum. Kwa kweli wakati hoja hizo zilipokuwa zinawasilishwa ziligusa sana hisia yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, itoshe tu kusema kwamba suala la watoto wenye mahitaji maalum ni kipaumbele katika Serikali ya Awamu ya Tano, na niseme kwamba kwa kuzingatia uzito wa hoja ambazo zimetolewa hata katika vitabu kama kuna mambo ambayo tunaweza tukayafanya tutajitazama upya hata kama ni kufanya re-allocation lakini kwa kweli tutahakikisha kwamba tunaweka kasi ya nguvu ya kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto ambazo zinawakabili wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Kwa hiyo, niseme kwamba yote mliyoyazungumza kuhusu wanafunzi wenye mahitaji maalum Waheshimiwa Wabunge nimeyapokea na ninawaahidi kwa moyo mkunjufu nitayafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limezungumzwa na ninaona katika michango ya maandishi Waheshimiwa Wabunge wengi wamelizungumza ni kuhusiana na suala la ukarabati wa shule kongwe. Kumekuwa na michango mingi ambayo wanaiuliza kwamba mbona hapa hakuna na mpaka nimeulizwa kwamba Waziri hukumbuki ulikotoka, hata shule yako ya Tabora Girls haipo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ufafanuzi kwamba shule hizi kongwe zinakarabatiwa zote, na tulizo hesabu kwa vigezo ambavyo tulitumia ni zile shule ambazo zimeanza miaka ya zamani miaka ya 60 kwenda mbele, yaani kati ya 60 na 70 ambazo zilikuwa ni shule za Kitaifa. Tunazifahamu shule kama Malangali, Ungwe, Tabora Girls, Tabora Boys, Kwiro kwa hiyo niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba zote zitakarabatiwa; na kuna mpango wa ukarabati ambao nimewasilisha karatasi kwenu ukionyesha kila shule iko katika mpango gani. Shule ya Tabora Girls, Tabora Boys zipo katika awamu ya kwanza na zinafadhiliwa na TEA kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge muondoe wasiwasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limeulizwa sana hasa katika michango ya maandishi, ni kuhusu vigezo vya kuanzisha kidato cha tano. Waheshimiwa Wabunge ni kwamba Wizara yangu itagawa kwa sababu ya muda mwongozo ambao mnapaswa kuzingatia katika kuanzisha kidato cha tano. Naahidi kwamba mpaka wiki ijayo nitawapa muongozo kwa utaratibu ambao mnatakiwa muufuate. Hata hivyo Waheshimiwa Wabunge ningependa kuwaambia kwamba shule zote za A-Level ni shule za kitaifa. Ipo dhana kwamba ukibadilisha shule ikawa ya A-Level basi watakaochaguliwa watakuwa ni wale ambao wanatoka katika jumuiya yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu iko tayari na itafurahi kupokea maombi na itayafanyia kazi. Hata hivyo tutambue kwamba tunapozibadilisha kuwa shule za A-Level zinakuwa ni shule za kitaifa. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge sina haja ya kuusoma muongozo hapa kwa sababu ya muda lakini ninawahakikishia kwamba wote nitawagawia ili muweze kuufahamu na muweze kutekeleza jukumu lenu la msingi la kuhakikisha kwamba mnapeleka elimu si tu elimu ya sekondari ya chini lakini hata na A-Level ziweze kuwa nyingi katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limezungumziwa na wachangiaji wengi ni suala la ukaguzi wa shule. Wachangiaji wameonyesha kutoridhishwa, kutofurahishwa na mazingira ya ukaguzi shule ambayo yako katika maeneo yetu. Waheshimiwa Wabunge na mimi nikiri kwamba kweli Idara yetu ya Ukaguzi inakabiliwa na changamoto, na ndiyo maana katika bajeti hii Wizara yangu imetenga fedha hata za kuwawezesha kupata ofisi, kwa sababu wengi wanakaa katika sehemu za kupanga, na sote tunafahamu mambo ya kupanga yana adha yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Wizara yangu itaendelea kuimaridha mazingira ya wakaguzi wa shule kwa kutambua kwamba wathibiti wa ubora wa shule, wana mchango wa pekee, wao ndilo jicho letu la kutuambia kitu gani kitaendelea katika sekta ya elimu. Kama Wizara lazima tutahakikisha kwamba tunawapa vitendea kazi, tunawapa mazingira mazuri ya kufanyia kazi ili waweze kutuangalizia vizuri elimu yetu katika ngazi zote kwa sababu wao wako katika sehemu zote kuanzia huko kwenye vijiji mpaka kwenye ngazi ya Taifa; wanaweza wakaona kwa urahisi kama tutawezesha vizuri. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge napokea ushauri wenu na Serikali itaendelea kufanyia kazi suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo limechangiwa na Waheshimiwa Wabunge ni kuhusiana na suala la makato ya asilimia 15 kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu. Niseme kwamba suala hili kuna kesi ambayo imefunguliwa mahakamani miscellaneous case course namba 6/2017, kwa hiyo kwa mujibu wa kanuni ya 64(1)(c) cha kanuni za kudumu za Bunge sitaweza kutolea ufafanuzi suala hili kwa sababu kifungu hiki kinazuia kujadili mambo ambayo yako mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie hoja na mapendekezo ambayo yametolewa na yamekuwa yakitolewa pia hata na Kamati yetu ya kuweza kupitia na kuangalia upya mfumo wetu wa elimu kwa lengo la kuweka misingi imara ili Taifa liweze kupata kasi ya maendeleo hasa sasa hivi ambapo tunatekeleza sera ya viwanda katika awamu hii ya tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba Serikali imekuwa ikifanya mapitio ya mfumo wake wa elimu na itaendelea kufanya mapitio ya mfumo wake wa elimu. Hata hivyo kwa kuzingatia kwamba suala hili limekuwa likijitokeza mara kwa mara mimi ninaomba kwa dhati kabisa, kama kuna maeneo, kama kuna hadidu za rejea ambazo inaonekana ni vema Serikali ikazingatia inapokuwa inafanya mapitio, Wizara yangu iko tayari kupokea. Kama nilivyosema tutaendelea kufanya mapitio kwa sababu lengo letu ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata elimu iliyo bora. Kwa hiyo, maoni yoyote, ushauri wowote ambao unalenga kumpatia mtoto wa Kitanzania elimu iliyo bora Wizara yangu itaupokea kwa mikono miwili kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumziwa pia suala la uhaba wa wahadhili katika vyuo vyetu vya elimu ya juu.
Mimi nikiri kwamba hiyo ni changamoto ambayo ipo na Serikali imekua ikitatua changamoto hiyo kwa kutafuta ufadhili kutoka kwenye nchi mbalimbali kwa sababu kumekuwa na baadhi ya nchi ambazo waekuwa wakitoa scholarship kama vile China, Uingereza, Misri, kuna wanaosoma Ujerumani kupitia DAAD scholarship.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema charity begins at home, katika bajeti hii ambayo Waheshimiwa Wabunge ninaomba sana mnipitishie tumetenga kiasi cha shilingi bilioni nane za kwetu wenyewe kwa ajili ya kuongezea nguvu ambayo wahadhili wetu waliokuwa wakifundisha watoka nje zaidi. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge naomba mniunge mkono ili tuendelee kutatua hiyo changamoto ya uhaba wa walimu katika vyuo vyetu vikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumziwa suala la hospitali yetu ya kisasa ya Mloganzila. Kwanza nipokee pongezi za dhati ambapo Waheshimiwa Wabunge wengi wamepongeza kwa hospitali ya kisasa na yenye vifaa tiba vya kisasa. Serikali imepokea pongezi zenu na tunawashukuru sana. Waheshiniwa Wabunge niwahakikishie kwamba kama mnavyoona hiyo ni hospitali ya kisasa imejengwa kwa gharama kubwa na dhamira ya Serikali ya kuanzisha hiyo hospitali iko pale pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Utumishi amenisaidia kutoa ufafanuzi kuhusu ajira za watumishi na Kamati ya Bunge ilisema kwemba nilikuwa nimeahidi nilipokutana nao tarehe 27 Machi, kwamba Serikali itatoa kiasi cha shilingi bilioni tano. Nafurahi kulialifu Bunge lako Tukufu tayari Serikali imekwisha ipatia hospitali ile ya Mloganzila shilingi bilioni tano ili kuiwezesha hospitali hiyo kukamilisha maandalizi muhimu ili tuweze kuifungua rasmi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaamini kwamba ndani ya muda mfupi nitakuja na habari njema na nitawakaribisha Waheshimiwa Wabunge tutakapokuwa tunazindua rasmi huduma katika hospitali hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limeongelewa nalo ntaliongea kwa kifupi kwa sababu ya muda ni suala la wamiliki wa shule binafsi na kwa maoni yangu na kwa michango ambayo imekuwa ikisemwa kama kumekuwa na dhana kama vile sasa wamekuwa ni watu ambao hawakubaliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Waziri mwenye dhamana ya elimu naomba niwatoe wasiwasi na niwahakikishie kabisa kwamba Serikali bado inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na sekta binafsi katika sekta ya elimu. Hivyo basi niombe hata Waswahili wanasema vikombe viwili vikaa pamoja havikosi kugongana. kama kuna mambo ni changamoto za kawaida, mimi sioni kama kuna jambo ambalo mkikaa mkiwa na dhamira, kwa sababu cha kwanza ni dhamira na kukiwa na dhamira hakuna jambo ambalo linashindikana.
Kwa hiyo, naomba sana hizi changamoto ambazo zimezungumzwa nadhani hapa hatuwezi kuzimaliza, lakini niwaambie wamiliki wa shule binafsi tuko pamoja na ninyi na mimi nitaomba tuwe na kikao ili tuweze kukaa kwa pamoja tuangalie kwa kina na tupate ufumbuzi wa moja kwa moja kwa sababu haipendezi kila siku jambo linakuwa linasemwa hilo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende kwenye suala ambalo limezungumzwa sana na Waheshimiwa Wabunge na limezungumzwa kwa hisia kubwa sana; suala la wasichana ambao wanapata ujauzito wanapokuwa shuleni. Nimesimama hapa nikiwa kama mama, kama mzazi na kama Waziri mwenye dhamana ya elimu. Hili suala ukitazama michango ambayo imetolewa ni suala ambalo kwa kweli inabidi tuliangalie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kwanza inasikitika sana inapoona watoto wa kike wanakatisha ndoto zao za elimu kutokana na sababu yoyote ile ikiwemo ya mimba. Ninafahamu kwamba mimba kabla ya ndoa inaathiri sana hata kisaikolojia kwa sababu unakuwa kama vile hata ukubaliki na kadhalika. Kwa hiyo, kunakuwa na madhara makubwa ambayo yanakuwa yanajitokeza. Pamoja na tatizo kubwa la mimba za utotoni kwa watoto wa shule ambao wanakuwa wanakosa fursa ya kuendelea lakini lipo tatizo pia kubwa la utoro shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ningeomba nitoe takwimu, ukiangalia takwimu za kitabu cha elimu Basic Education Statistics cha mwaka 2016, ambacho nitaomba Waheshimiwa Wabunge wote wapatiwe nakala mapema iwezekanavyo. Takwimu zinatuonesha kwamba katika mwaka 2015 wanafunzi wa kike ambao waliacha shule ya msingi kwa ajili ya ujauzito walikuwa 251, na watoto wa kike walioacha shule kwa sababu ya kupata ujauzito walikuwa 37,658. Ukienda kwa watoto wa kiume walioacha shule kwa utoro ni 44,930.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, tatizo la mimba ni kweli ni tatizo kubwa na linawatesa hata watoto wetu kisaikolojia, lakini naomba niseme kwamba tatizo la utoro ni kubwa zaidi kuliko hata la mimba. Tunapoteza wanafunzi wa kike peke yake 37,658, na hawa ni wa msingi peke yake, ukienda sekondari watoto wa kike walioacha shule kwa utoro walikuwa 26,069 na watoto wa kiume walikuwa 31,209. Ukijumlisha wote wa msingi na wa sekondari jumla yao walioacha shule kwa utoro ilikuwa ni 139,886 na walioacha shule kwa mimba walikuwa 3,637. (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge, kama ninavyosema Serikali yetu imesaini makubaliano ya kutekeleza mpango wa maendeleo endelevu mwaka 2030 ambapo tunawajibika kuhakikisha watoto wote wa Kitanzania wanaenda shule mpaka sekondari. Kama Waziri mwenye dhamana ninatambua hivyo na ninapoona kwamba unakuwa na wanafunzi 139,000 ambao hawaendi shule kwa sababu ya utoro, Waheshimiwa Wabunge ninaomba sote tuungane kwa kuhakikisha kwamba kwanza tunashughulikia tatizo la utoro shuleni. Kwa sababu tatizo la utoro shuleni ndilo ambalo linapoteza vijana wengi zaidi kuliko hata mimba. Tukianza na tatizo la utoro tutakuwa tumeokoa vijana wengi zaidi.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie suala la wanafunzi ambao wanapata mimba shuleni. Nchi yetu inaongozwa kwa sheria, kanuni na taratibu na bahati nzuri Waheshimiwa Wabunge sisi wenyewe ndio ambao tunatunga sheria. Ninashukuru sana watu ambao wamegusia sheria ambayo Bunge hili lilipitisha mwaka 2016, ambayo ilifanya marekebisho ya Sheria ya Elimu na kuweka kifungu ambacho kinatoa adhabu kwa mtu yoyote ambaye anatoa ujauzito kwa mtoto wa kike akafungwe jela miaka
30. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia naomba sambamba na kuzungumzia na mimba shuleni naomba nilifahamishe Bunge lako Tukufu kwamba zipo sababu nyingine ambazo zinapelekea pia wanafunzi kukosa haki yao ya msingi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, katika Sheria ya Elimu Sura ya 353 (61)(o) kinatoa utaratibu wa kuandaa kanuni za kuainisha vigezo vitakavyotumika kufukuza mwanafunzi shuleni kutokana na masuala mbalimbali. Kanuni ya nne ya elimu ya mwaka 214 inatoa mwogozo kuhusu mambo ambayo yanaweza yakasababisha mwanafunzi akafukuzwa shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niyasome kwa ridhaa yako, kwanza, utovu wa nidhamu wa makusudi unaojirudiarudia na unaohatarisha nidhamu ya wanafunzi shuleni au kuharibu hadhi ya shule kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ya pili, kufanya makosa ya jinai kama vile wizi, kuharibu mali za umma na mali za shule; tatu, uasherati; ya nne dawa za kulevya; ya tano kosa lolote jingine ambalo litaenda kinyume na maadili bila kujali kama aliwahi kutumikia kosa hilo au hapana. Nchi yetu imekuwa ikiwajengea vijana malezi ambayo yanazingatia maadili na utamaduni wa kitanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua feelings ambazo zimeonyeshwa katika hili suala na kama ninavyosema mimi linanigusa moja kwa moja kwa sababu sitakiwi kumwacha mtoto hata mmoja katika sekta ya elimu, awe mtoto wa kike au awe mtoto wa kiume ni jukumu langu kuhakikisha kwamba anapata elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hayo niliyoyaeleza na kwa kuzingatia kwamba pia zipo sababu nyingine ambazo zinasababisha mtu kufukuzwa shule; kutokana na hii sheria mwanafunzi anapobainika anabusiana shuleni anafukuzwa shule, kitendo cha kubusiana tu. Kwa hiyo, ninachotaka kusema kwa nini ninayasema haya yote, niseme nimepokea hoja na hisia za Wabunge wote, lakini kwa kuzingatia haya ambayo ninaelekeza ambayo ninaeleza ninaona pia bado upo umuhimu wa kuliangalia hili jambo kwa mapana yake. Kama tunaangalia basi tuangalie vipengele vyote vinavyosababisha mwanafunzi kufukuzwa shule na kadhalika lakini pia tuzingatie mila na desturi na vitu vingine ambavyo vinatunza kama kielelezo cha maadili ya utu wa Mtanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelizungumza na mimi hili linanitia hasira sana, ni suala la vitabu kuwa na makosa. Mheshimiwa Naibu Waziri wangu ameomba hapa msamaha lakini mimi siwezi kuomba msamaha kwa ajili ya uzembe wa watu, ila nasema nitawawajibisha, siwezi kuomba msamaha kwa ajili ya uzembe wa watu ambao wanalipwa mshahara kwa kodi za Watanzania kufanya kazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kama nilivyozungumza katika hotuba yangu, nilipokea taarifa kuhusu hivyo vitabu na nikiri kwamba sijapata muda binafsi wa kuviangalia; lakini kile kitabu cha kiingereza darasa la tatu binafsi nilikiangalia, ni aibu nilikiangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwamba kitabu cha darasa la tatu cha kiingereza watu walioandika ni aibu, watu wanaoajiriwa Taasisi ya Elimu kigezo cha chini kabisa cha elimu ili mtu aweze kuwa Mkuza Mitaala ni degree. Hivi mtu ambaye amesoma mpaka akapata degree, na elimu yetu sekondari ni kwa kiingereza, hata kama amepita diploma akaenda mpaka akapata degree kwa kiingereza, kiingereza cha namna ilie, hili jambo haliwezi kukubalika hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba wote tunafahamu makali ya Serikali ya Awamu ya Tano, kama tumethubutu watumishi wasiokuwa na vyeti 9,900 kwa mkupuo wakaondoka, hawa wanaotaka kuhujumu elimu yetu ni nani? Hili ni jambo ambalo Serikali inalichukulia kwa uzito wa hali ya juu sana na kila mmoja ambaye amehusika na kadhia hii kila mtu atabeba msalaba wake mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema tayari kuna kamati ambayo imeundwa na Wizara yangu ya kuchambua; kwa sababu nimesema kwamba binafsi nimeona kitabu kimoja na kama Waziri mwenye dhamana siwezi kufanya maamuzi bila kuwa na taarifa inayochambua vitabu vyote tayari wataalam wapo kazini wanachambua kitabu kimoja baada ya kingine ili tuweze kubaini ukubwa wa tatito hili na hivyo basi Serikali iweze kuchukua hatua stahiki.
Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge katika suala hili la vitabu ni kwamba binafsi naungana na ninyi na hata kama mnaweza mkatusaidia kutuonyesha makosa ambayo ninyi mmeyabaini zaidi, Serikali itafanyia kazi kwa sababu hatuwezi kucheza na elimu yetu na vitabu ndio chanzo cha maarifa kwa watoto wetu hatuwezi ku-afford kama Serikali tukawa na vitabu ambavyo vina makosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona umeshanipigia kengele na nisingependa ukanipigia kengele ya mwisho, lakini labda tu nizumgumzie jambo moja la mwisho kuhusiana na mabweni ya chuo kikuu cha Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala haya yameainishwa na ndugu yangu msemaji kambi ya upinzani kuhusiana na gharama za ujenzi na kwamba hata katika mchango wake wa maandishi amekuwa na wasiwasi kwamba hivi shilingi bilioni 10 zinaweza zikajenga majengo yale yanayoonekana. Niseme kwamba Serikali imetumia force account ambayo ni utaratibu ambao uliidhinishwa na Bunge lenyewe ambao unawezesha vifaa kununuliwa moja kwa moja na kazi ikasimamiwa na wakala au Taasisi ya Serikali.
Majengo yamejengwa na Wakala wa Majengo Tanzania, na niseme kwamba Wizara yangu imelipa kiasi cha shilingi bilioni 10 kwa ajili ya majengo na mimi nilikuwa nategemea kwamba mngetupongeza kwamba tumeweza kujenga mabweni kwa bei ambayo ni ya nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na suala la kwamba hizi fedha hazikupitishwa na Bunge naomba niweke sawa. Ahadi ya kujenga mabweni aliitoa Mheshimiwa Rais wetu tarehe 4/06/2016 alipokuwa Chuo Kikuu cha Dar essalaam na alipokuwa ametoa hata mkiangalia katika vitabu vyenu vya volume estimates mtaona kwamba katika mwaka huu wa fedha kulikuwa na shilingi bilioni tano, ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya Chuo Kikuu kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa chuo kikuu cha Dar e salaam. Mara baada ya ahadi hiyo hicho kiasi cha shilingi bilioni tano za mwaka wa fedha 2015/2016 zilipelekwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na katika bajeti ya mwaka 2016/2017 ukiangalia hata katika vitabu utaona kwamba walikuwa wametengewa shilingi bilioni tisa ambapo tayari bilioni tano zilitolewa kwa ajili ya mabweni na bilioni nne nyingine zitakuwa kwa ajili ya ukarabati kwa sababu mwaka wa fedha haujaisha. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge niwahakikishie kwamba hakuna kitu ambacho kimekiukwa, na niombe tu kwamba tumpongeze Rais wetu kwa uamuzi mzuri na kweli ametatua tatizo kubwa kwa wanafunzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo ya ufafanuzi wa hoja ambazo nimeweza kuzifafanua kutokana na muda, kama nilivyosema hapo awali naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba hoja zenu zote ambazo mmezitoa tutawapa ufafanuzi kwa maandishi kabla hatujaondoka katika kikao hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na baada ya maelezo hayo niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge wote tunapoenda sasa kwenye kupitia mafungu ili kupitisha bajeti yangu naomba wote kwa umoja wenu mniunge mkono ili niweze kuendelea kutumikia katika sekta hii ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kutoa hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa kunipatia nafasi na mimi nichangie hoja hii iliyoko mbele yetu na nianze kutoa pongezi za dhati kabisa kwa Waziri wa Fedha, Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa bajeti nzuri ambayo wameiwasilisha mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii na nitatoa sababu kwa nini naiunga mkono hoja hii. Bajeti hii imeandaliwa kwa umakini mkubwa na ina dhamira ya dhati kabisa ya kuondoa matatizo ya wananchi na kuleta maendeleo. Ukiangalia sekta ya elimu, sekta ya elimu imetengewa kiasi cha shilingi trilioni 4.77 ambayo ni sawa sawa na asilimia 22.1 ya bajeti yote hii na mgawanyo huu wa fedha unaonesha bayana, jinsi gani ambavyo Serikali ina dhamira ya dhati ya kuwahudumia wananchi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa elimu katika maendeleo ya nchi hii na ndio maana fedha zimetengwa za kiasi kikubwa na fedha hizi nyingi zitaelezwa katika miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naipongeza Wizara ya Fedha,kwa kuja na vyanzo vipya vya mapato ambavyo vitaiwezesha Serikali kupata fedha, za kutekeleza mpango ambayo imeahinishwa na kama walivyozungumza wachangiaji wengine, hii ni bajeti ya mwaka mmoja tu.
Mheshimiwa Naibu Spika,hii bajeti imetokana na Mpango wetu wa Maendeleo wa Miaka Mitano na imezingatia katika kutufikisha kule ambako tunatarajia kufika ukizingatia Ilani yetu ya uchaguzi na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, kwa hiyo niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuiunge mkono tukitambua kwamba hii ni bajeti ya mwaka mmoja, haiwezi kumaliza matatizo yote kwa sababu Serikali inakwenda hatua kwa hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kuunga mkono bajeti hii ya mwaka mmoja, kutaiwezesha Serikali kuanza hatua yake ya kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo, katika maeneo ambayo yameainishwa. Vilevile napongeza kwa dhati kabisa, hatua za Serikali za kubana matumizi na kudhibiti matumizi yasiyokuwa ya lazima, hii yote inaonesha jinsi gani ambavyo Serikali ina dhamira ya dhati kabisa kuwatumikia wananchi wake hivyo tuna kila sababu ya kuunga mkono bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba sasa nizungumzie kidogo masuala ambayo yalielekezwa katika sekta ya elimu na kutokana na muda nitazungumzia mambo machache na mengine tutayajibu kwa maandishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, limejitokeza suala la fedha za utafiti,na Waheshimiwa Wabunge wameonesha wasiwasi wao kwamba kiasi cha fedha kilichotengwa ni kidogo na kwamba msisitizo katika utafiti wa kilimo, haupewi kipaumbele kinachotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kusema kwamba Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya utafiti, kupitia kwenye Tume ya Taifa ya Utafiti yaani COSTECH; na kuna kazi nyingi ambazo zimekuwa zikifanyika na utaratibu tu ambao umekuwa ukitumika ni utaratibu wa ushindani. Kumekuwa na hoja kwamba kwa nini utumike utaratibu wa ushindani kutoa fedha za utafiti?
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa ushindani kwanza unaihakikishia Serikali kwamba yule anayeomba fedha yuko tayari, kwa maana ya kwamba tayari atakuwa na mpango kazi wake. Anajua anataka kufanya nini kwa hiyo inaihakikishia kwamba yule anayepata fedha kwa ushindani anakuwa anazitumia fedha hizo vizuri, badala ya kuzigawa hata kwa mtu ambaye hajawa yuko tayari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia suala la ushindani jumla ya miradi 102 imeweza kufadhiliwa,na ambapo kuna masuala mengi tu yamefanyika ikiwa ni pamoja na kujenga rasilimali watu kuwajengea uwezo wa kuweza kufanya utafiti; na katika hilo jumla ya watafiti 517 wamepatiwa mafunzo na jumla ya watu 130 wamepata mafunzo katika ngazi ya uzamili na uzamivu. Vilevile fedha za utafiti zimewezesha kujenga miundombinu ya kufanyia utafiti ambapo kwa mfano Serikali imeweza kujenga mabwawa 42 ya zege na kukarabati maabara za uzalishaji wa vifaranga vya samaki katika Chuo Kikuu cha Sokoine.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika bajeti ya mwaka 2016/2017 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 12.8 kwa ajili ya suala la utafiti. Lakini pamoja na fedha hizi, bado Serikali itaendelea kupata fedha kupitia kwa wafadhili mbalimbali ambao wamekuwa wakipeleka fedha hizo moja kwa moja katika vyuo vyetu vya elimu ya juu.
Suala lingine ambalo limezungumzwa katika Wizara yangu ni suala la kuitaka Serikali iangalie kozi zinazoanzishwa katika vyuo vya elimu ya juu, kujiridhisha kama kuna walimu wa kutosha. Niwahakikishie Watanzania kwamba katika kuhakikisha ubora wa elimu hiyo ndio kipaumbele chetu katika Awamu ya Tano. Hivyo basi hakuna kozi yoyote ambayo itaanzishwa kama Serikali haijaridhika na miundombinu, kama Serikali haijaridhika na uwepo wa elimu ambao wana sifa stahiki. Pamoja na kuangalia kozi mpya lakini niseme kwamba hata kozi ambazo zipo Serikali inafanya mapitio kuona kwamba kozi zote zinazotolewa katika elimu ya juu zina wataalam wa kutosha na ziko katika mazingira ambayo yanastahiki. Kwa hiyo, tutachukua hatua zinazostahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo limezungumziwa ni suala la ukarabati wa vyuo vikuu, pamoja na miundombinu ya kutolea elimu. Ukiangaliwa kitabu cha hotuba ya bajeti ya Waziri wa Fedha na kitabu cha hotuba cha Wizara yangu, tumebainisha wazi mikakati ya Serikali katika kuhakikisha kwamba tunakarabati miundombinu ya shule na vyuo vikuu ili kuhakikisha kwamba Watanzania na wananchi wanapata elimu katika mazingira ambayo ni rafiki na kama nilivyosema tunafanya hatua kwa hatua, kwa mfano katika mwaka huu wa fedha, tutaweza kufanya ukarabari kwenye shule kongwe 40. Lakini vilevile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambacho ni Chuo Kikuu kongwe tumekitengea kiasi cha shilingi bilioni tisa kwa ajili ya kufanya ukarabati na hili zoezi ni endelevu. Kama nilivyosema hii ni hatua tu, lakini ahadi zetu zitatekelezwa katika miaka mitano. Kwa hiyo tutaendelea kukarabati na kuhakikisha kwamba mazingira ya kujifunzia yanakuwa ni rafiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo limezungumziwa ni suala la elimu bure, kwamba hii sera iende mpaka kidato cha sita. Ninachoweza kusema ni kwamba kama Serikali, tumepokea huo ushauri lakini tungeomba kwamba kama tunavyosema tunataka utekelezaji wetu wa ahadi kwa wananchi uende hatua kwa hatua. Kwa hiyo tumeanza na mpaka kidato cha nne tungeomba kwanza tuendelee kuimarisha utekelezaji wa sera ya elimu bila malipo kwa kidato cha nne na kutatua changamoto ambazo zipo kabla hatujafikiria kuongeza wigo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine lililozungumziwa katika eneo langu ni suala la VETA kuwa na vifaa vya kisasa na hilo tutalifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii nami nichangie hoja ambayo iko mezani kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuanza kwa kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniamini na kuniteua tena niendelee kutumikia katika sekta hii ya elimu. Nimhakikishie Mheshimiwa Rais na Watanzania kwa ujumla kwamba nitafanya kazi yangu kwa uadilifu na kamwe sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuanza mchango wangu kwa hoja iliyoko mbele yetu ambayo ni Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2018/2019 pamoja na Mwongozo wa Bajeti kwa kuanza kusema kwamba ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja hii kwa sababu imeandaliwa vizuri na imeangalia maeneo ambayo ni muhimu katika kusukuma maendeleo kwa Taifa letu. Napenda kumpongeza kwa dhati Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na Naibu wake kwa kazi nzuri ambayo wameifanya katika kuandaa hoja hizi pamoja na watendaji wote katika Wizara ya Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza Mpango huu, Wizara yangu inayo mchango muhimu kwa sababu elimu ndiyo nguzo muhimu katika kuleta maendeleo ya Taifa letu. Kama ambavyo tunafahamu, Mpango wetu wa maendeleo umejikita katika kujenga uchumi wa viwanda na ili tuweze kujenga uchumi wa viwanda ni lazima kuangalia kwa umakini ujuzi wa Watanzania ambao ndiyo nguzo kuu ya maendeleo katika Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu katika kuhakikisha kwamba tunaweka mchango unaotakiwa katika kukuza ujuzi nchini, tumeweza kufanya mambo mbalimbali, Waheshimiwa Wabunge wamekuwa katika michango yao wanaulizia na kuonesha wasiwasi wao kama kweli hii Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba kunakuwa na ujuzi wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme katika mpango wetu tumeonyesha kwamba ili tuweze kwenda na kasi inayotakiwa tunatakiwa tuwe na asilimia 55 ya Watanzania wenye ujuzi wa chini, asilimia 33 ya ujuzi wa kati na asilimia 12 ya ujuzi wa juu.
Kwa hiyo, Serikali inao Mpango Mkakati wa Kukuza Ujuzi (National Skills Development Strategy) ambao katika kutekeleza mpango huo, Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kuna mpango ambao tunazo dola milioni 120 ambazo ni sawa na fedha za Kitanzania bilioni 250 ambazo zinalenga kukuza ujuzi
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi zitawezesha kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi kwa kuimarisha miundombinu katika taasisi zetu zinazotoa mafunzo ya ufundi stadi hususan VETA, Arusha Technical, Dar es Salaam Institute of Technology pamoja na taasisi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia huu mpango wa elimu na ujuzi kwa kazi zenye tija (education and skills for productive jobs) umejikita katika kuangalia maeneo ambayo ni ya kipaumbele katika mpango wetu wa maendeleo ambao ni pamoja na sekta ya kilimo, utalii, usafirishaji, ujenzi, nishati pamoja na TEHAMA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namna mojawapo ya kupata fedha hizi ambazo nimezisema bilioni 250 ambazo Serikali tayari inazo kwa ajili ya kutekeleza mradi huu itakuwa ni pamoja na kuandika maandiko ambayo ni shindani. Kwa hiyo, nitumie fursa hii kuwataka Waheshimiwa Wabunge tushirikiane katika kuhakikisha kwamba fedha hizi ambazo tunategemea kutangaza kwa mara ya kwanza maombi kwa ajili ya kupaya ufadhili (skills development fund) mwishoni mwa mwezi huu tushirikiane kuhamasisha taasisi za ufundi zilizoko katika maeneo yetu kwa sababu fedha zitakuwa zinatolewa katika mfumo wa ushindani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ningependa kuchangia ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelizungumza katika michango yao ni suala la utoaji wa elimu bure na suala la changamoto zilizopo katika utoaji elimu.
Kwanza niseme kwamba suala la utaoji wa elimu bure katika Nchi hii limekua na mafanikio makubwa sana. Kila mwezi Serikali inatoa kiasi cha shilingi bilioni 20.8 kwa ajili ya elimu bure na mojawapo ya vigezo ambavyo tunaweza tukavitumia kusema kwamba kumekuwa na mafanikio makubwa, ukiangalia takwimu za wanafunzi ambao wanafanya mtihani wa kidato cha pili ambao wameanza leo hii wameongezeka kutoka wanafunzi 435,075 mwaka 2016 hadi kufukia wanafunzi 521,855 ambalo ni ongezeko la wanafunzi 87,730.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mpango wa elimu bure ulianza kutekelezwa mwaka 2016, hii ina maana kwamba, wale wazazi ambao walikuwa wanashindwa kuwapeleka watoto wao sekondari kwa sababu ya ada, Serikali imefungulia na ndiyo maana leo hii tunaona hata idadi ya watahiniwa wanaofanya mtihani wa kidato cha pili imeongezeka sana. Niwahakikishie Watanzania kwamba, Serikali imejipanga vizuri katika kuimarisha miundombinu katika ngazi zote za elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na changamoto za ongezeko la wanafunzi tumekwishajenga madarasa 1,409 tumeshajenga matundu ya vyoo 3,394 lakini vilevile tumeongeza mabweni kwa ajili ya kuhakikisha kwamba watoto wa kike wanaotoka umbali mrefu wanaweza kusoma katika mazingira ambayo ni tulivu zaidi kwa hiyo, tumejenga mabweni 261.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua kwamba mazingira ni muhimu kwa wananfunzi kujifunza vizuri tunafanya ukarabati wa shule zetu kongwe na mpaka sasa tumekwishaanza ukarabati katika shule 42 kati ya shule kongwe 88 katika nchi hii, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba shule zote kongwe nchini zitafanyiwa ukarabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeboresha miundombinu katika vyuo vyetu vya ualimu na tunaendelea kufanya hivi. Sasa hivi ninavyozungumza Vyuo vya Ualimu vya Kitangali, Mpuguso, Ndala na Shinyanga miundiombinu yake inaimarishwa kwa kiwango kikubwa, majengo ya kisasa yanajengwa, hii yote ni katika kutekeleza mpango wa Serikali ambao unalenga kufungamanisha maendeleo na rasilimali watu, ili kufanya hivyo lazima tuhakikishe kwamba tunayo rasilimali iliyobobea katika ujuzi katika kutekeleza mpango wetu wa maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo Wizara imekuwa ikifanya katika kutekeleza mpango huu ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na msingi ulio imara. Kwa sababu tunafahamu kwamba nyumba bora inajengwa katika msingi ulio imara, Serikali imekuwa ikiweka kipaumbele katika elimu ya awali kuhakikisha kwamba vijana wanapata utayari wa kuanza elimu ya msingi, tumeendelea kutekeleza Programu ya Kukuza Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu ili kuwajengea vijana wetu msingi mzuri wa kuweza kupata maarifa wanapokuwa wanaanza darasa la kwaza, la tatu hadi la nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufanya hivyo tumekuwa tukitoa mafunzo kwa walimu wa darasa la kwanza, la pili, walimu wa darasa la tatu na la nne pamoja na walimu ambao wanafundisha wananfunzi wenye mahitaji maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum ambapo tumewanunulia vifaa vya kujifunzia vyenye thamani ya shilingi bilioni 3.6 lakini pia Serikali inaendelea kuimarisha ufundishaji wa sayansi kwa sababu tukipata Wanasayansi wazuri ndiyo chachu muhimu ya kuweza kupata wataalam ambao wanahitajika katika fani mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeendelea pia kuhakikisha kwamba tunakwenda sambamba na utoaji wa elimu ya juu kwa kuimarisha miundominu katika elimu ya juu. Ninapende kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba pamoja na taarifa ya Serikali ambayo niliisoma hapa Bungeni tarehe Tisa pia Bodi ya Mikopo imeendelea kutoa mikopo na wananfunzi zaidi ya 1,775 wamepangiwa mikopo na hivyo kufanya sasa jumla ya wananfunzi ambao wameshapangiwa mikopo kufikia 31,353.
Mheshsimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kwa Wanafunzi ambao hawajapata mikopo lakini wanaona bado wana uhitaji, dirisha la kukata rufaa limefunguliwa leo na litafungwa tarehe 19 Novemba, 2017. Niwaombe na niwaelekeze wanafunzi wote ambao hawajapata mikopo lakini wanaona wana uhitaji mkubwa, watumie fursa hiyo kukata rufaa na Serikali inaendelea kujiridhisha kama Je, kweli wanafunzi wale waliopangiwa mikopo ndiyo wale ambao wana uhitaji ukilinganisha na wale ambao hawajapata ili kuhakikisha kwamba dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba mikopo ya elimu ya juu inatolewa kwa wanafunzi tu wenye uhitaji kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa inazingatiwa, kwa sababu hiyo tayari nimeagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya mikopo kupitia jina moja baada ya lingine ili kujiridhisha kwamba je, wale waliopangiwa mikopo ndiyo wenye uhitaji kuliko wale ambao hawajapangiwa, lakini pia kupitia majina yote ya wanafunzi ambao hawajapata mikopo ili kujiridhisha kama kweli hawana vigezo kwa mujibu wa vigezo mbavyo vimewekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie kama nilivyosema, wanafunzi wa elimu ya juu kwamba Serikali inatekeleza sera ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wenye uhitaji tu na hapo Waheshimiwa Wabunge tuelewane kwamba sera yetu ya elimu ya juu ni sera ya uchangiaji. Hatujafikia mahali ambapo Serikali inatoa mikopo kwa wanafunzi wote na ndiyo maana hata Sheria ya Bodi ya Mikopo imeainisha wazi kwamba mikopo itatolewa kwa wanafunzi wenye uhitaji, kazi ya Wizara yangu ni kusimamia na kuhakikisha kwamba wale ambao wanapangiwa mikopo ni wale tu wenye uhitaji na siyo vinginevyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kushukuru kwa nafasi na kama nilivyosema tangu mwanzo wakati naanza ninaunga mkono hoja hii na ningeomba Wabunge wote tuiunge mkono kwa sababu ni Mpango ambao ni mzuri sana. Ahsante sana.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nina dakika ngapi?
MWENYEKITI: Una dakika saba.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia fursa ya kuchangia kuhusu hoja iliyoko mbele yetu. Kwanza kabisa napenda nianze kwa kuishukuru Kamati yangu ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa ushauri na mapendekezo ambayo imeyatoa katika Wizara yangu. Niseme tu kwamba kwa sababu ya muda niliopewa, haitakuwa rahisi kujibu hoja zote zilizojitokeza, kwa hiyo, naomba nijielekeze kwenye masuala machache, kadri ya muda utakavyoruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na suala la mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, ambalo limezungumzwa na Kamati, lakini pia limezungumzwa na wachangiaji wengi. Kuna vipengele vingi ambavyo vimezungumzwa kuhusiana na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. Kwanza ni suala la vigezo vya utoaji mikopo ambavyo kwa sasa tunaangalia uyatima, uhitaji, ulemavu, pamoja na vipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kwamba hivi vigezo vina matatizo na ninafurahi kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba tayari Wizara yangu imeshaunda Kamati ambayo imepitia hivi vigezo na kuleta mapendekezo ambapo tarehe 28 tulikaa na Kamati yangu ya Kudumu na kuvipitia, nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba tunapoanza mwaka 2017/2018 katika bajeti hii, tutakuja na vigezo ambavyo vitakuwa vimeboreshwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la utoaji wa mikopo na kwamba kuna baadhi ya wanafunzi ambao walikuwa wanapata mikopo lakini mikopo yao imefutwa, niseme kwamba Wizara yangu imekuwa ikihakiki wanafunzi wa elimu ya juu ambao wana sifa za kupata mikopo. Wale wote ambao hawana sifa, bila kujali kwamba yuko mwaka wa ngapi, tunawafutia mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nililisema hata katika Bunge la mwezi Novemba. Nasisitiza kwamba huo ndiyo msimamo wa Serikali. Kuna wengine ambao walikuwa wamepata mikopo kwa sababu walidai kwamba wao ni yatima; tumepeleka vile vyeti vya vifo vya wazazi RITA na tukabaini kwamba ni vyeti vya kughushi. Kwa hiyo, tumefuta na tutaendelea kuhakiki na wale wote ambao wamepata mikopo kwa njia ya udanganyifu, hao tutaendelea kuwaondoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la urejeshaji mikopo. Ninakubaliana na Kamati kwamba kwa kweli kasi ya urejeshaji mikopo hairidhishi kabisa. Napokea ushauri wa Kamati kwamba kama Serikali kwa kweli tunapaswa kuimarisha urejeshaji wa mikopo kwa sababu hadi kufikia Juni, 2016 Serikali ilitoa jumla ya shilingi trilioni 2.5 lakini ambazo zimekwisharejeshwa ni shilingi bilioni 147.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utaratibu huu hatuwezi kutegemea kwamba Serikali iendelee kuongeza wigo wa utoaji mikopo wakati urejeshwaji hauko imara. Kwa hiyo, hatua ambazo Serikali tunazichukua, kwanza tumeongeza kato badala ya 8% kuanzia mwezi huu ni 15%. Nitumie fursa hii kuwataka waajiri wahakikishe kwamba wanafanya makato ya mikopo na kuyawasilisha kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nihamie katika eneo lingine ambalo limezungumzwa ambalo ni suala la udahili wa wanafunzi katika elimu ya juu. Hili suala limezungumzwa sana kwamba TCU amegeuka kuwa dalali wa udahili katika vyuo vya binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Serikali inaliangalia suala hilo. Katika udahili wa mwaka 2017/2018 Serikali itafanya mapitio na kuja na mfumo ambao utakuwa na tija zaidi ili vyuo binafsi navyo vijione kwamba vina jukumu la kuboresha elimu yao na kuhakikisha kwamba vinajitangaza kutokana na ubora wa elimu na siyo kutegemea kupata wanafunzi kupitia mgongo wa TCU. Ushauri umepokelewa na utafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo limezungumzwa ni suala la upatikanaji wa vitabu. Nikiri kwamba kumekuwa na uchelewaji wa usambazaji wa vitabu kutokana na changamoto ambazo zilijitokeza katika suala zima la manunuzi. Nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba leo Wizara yangu imeanza kusambaza vitabu 2,426,135 kwa ajili ya kidato cha nne mpaka cha sita. Tunategemea kusambaza vitabu takribani milioni 5.5 kuanzia wiki mbili zijazo. Kwa hiyo, hilo suala la upatikanaji wa vitabu, changamoto ambazo ni za manunuzi zilizochelewesha tutazifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala moja tu kuhusu elimu ya msingi kwa sababu limezungumzwa sana. Kuna suala ambalo limeulizwa kwamba, je, hii Sera ya Elimu Msingi ya kwamba wanafunzi wanamaliza mpaka kidato cha nne imeanza kutekelezwa au la?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine wamekuwa na maoni tofauti, napenda kutoa ufafanuzi kwamba suala la elimu ya msingi kwamba mwanafunzi atasoma kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne limeainishwa katika Sera ya Elimu ya mwaka 2014. Ili matamko ya sera yaanze kutekelezwa, inahitaji kutungwa sheria, kanuni na taratibu. Kwa sasa sheria inayoongoza jambo hilo bado. Nawahikishia Watanzania kwamba jambo hili litakapoanza kutekelezwa mtajulishwa, lakini kwa sasa hivi bado halijaanza kutekelezwa, elimu yetu bado ni miaka saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nichangie katika hoja iliyoko mbele yetu. Kwanza nianze kwa kuipongeza Kamati kwa taarifa nzuri ambayo wameiwasilisha, lakini pia nimpongeze sana Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Peter Serukamba, kwa uwasilishaji mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia fursa hii kuishukuru sana Kamati kwa namna ambavyo tumekuwa tunafanya kazi na kwa ushauri na maelekezo yao. Katika misingi hiyo, nianze tu kwa kusema kwamba Serikali imepokea ushauri ambao umetolewa na Kamati na itaufanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza katika mambo machache ambayo yamezungumzwa na Kamati na mengine ambayo yamechangiwa na Waheshimiwa Wabunge ambao wamepata nafasi ya kuchangia hoja hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ningependa kuzungumzia suala la Hospitali ya Taaluma ya Kufundishia Mloganzila. Niseme kwamba Serikali imejenga Hospitali ya kufundishia ya Mloganzila kwa lengo la kuimarisha mafunzo ya fani za afya na tiba katika nchi yetu. Hii ilitokana na dira na malengo ya chuo hicho pamoja na malengo ya Serikali ya kuhakikisha kwamba inakuwa na wataalam wa kutosha, na utaratibu wa kuwa na hospitali ya kufundishia ni utaratibu ambao upo hata katika Mataifa na nchi nyingine za Afrika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilihakikishie Bunge lako kwamba dhamira ya Serikali ya kuwa na Hospitali ya Taaluma ya Kufundishia ya Mloganzila bado iko palepale na Serikali kwa sasa haina mpango wowote kwa sababu ndiyo kwanza hospitali hiyo imekamilika, ni hospitali nzuri ya kisasa na ina uwezo wa kutoa mafunzo na tiba katika fani zote. Kwa hiyo, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili kitaendelea na kusimamia hospitali hiyo kama ambavyo kimesimamia katika mchakato wote wa ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuzungumzia suala la vitabu ambalo limezungumziwa. Ni kweli kama ambavyo nilisema tarehe 15, Mei wakati nahitimisha hotuba, kulikuwa na changamoto ya vitabu na nikaahidi katika Bunge hili kwamba Serikali itaenda kuvifanyia kazi, kuvifanyia mapitio na kuchukua hatua kwa wale waliosababisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kazi ya kufanya mapitio ya vitabu imekamilika na baadhi ya vitabu vilivyorekebishwa viko hapa na viko katika hatua ya uchapaji ili viweze kusambazwa. Pia niwahakikishie Wabunge kwamba Serikali itaendelea kuimarisha Taasisi yetu ya Elimu Tanzania ili iweze kutekeleza vizuri majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba vitabu vyote shuleni vinapatikana vikiwa na ubora unaotakiwa na kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na suala ambalo limezungumziwa la kuhusiana na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, kwamba hii taasisi ifutwe kwa sababu inaonekana kwamba haina tija. Ningependa kusema kwamba Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ilianzishwa kwa Sheria Na. 139 ya Mwaka 1989 na lengo lake kubwa ilikuwa ni kutoa elimu kwa watu ambao hawakuweza kupata mafunzo katika mfumo ambao uko rasmi, lakini pia ina lengo la kutoa mafunzo endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu kwamba bado madhumuni ya kuanzisha taasisi hiyo yapo na Serikali itaangalia namna ya kuimarisha na tupo tayari kupokea ushauri na mapendekezo kwa namna ambavyo taasisi hii inaweza ikaimarishwa zaidi ili iendane na mahitaji ya sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo mdogo wangu, Mheshimiwa Rehema alilizungumzia, kuhusiana na suala la Waraka wa Elimu Bila Malipo na kwamba Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo ambayo yanapingana na Waraka wa Elimu bila malipo. Ningependa tu kumwambia ndugu yangu, Mheshimiwa Rehema, Mwalimu mwenzangu Migila kwamba Serikali hii, kwanza niseme kwamba Waraka Namba Tatu wa Elimu Bila Malipo ni waraka wa Serikali na Kiongozi wa Serikali hii ya Awamu ya Tano ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli na ni Rais ambaye ni mfuatiliaji, anajua kila kitu kinachoendelea katika Serikali yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo yote ambayo Mheshimiwa Rais aliyatoa kuhusiana na elimu bila malipo, tarehe 17, Januari, 2018, hakuna hata jambo moja ambalo Mheshimiwa Rais amelisema ambalo linakinzana na Waraka wa Elimu Bila Malipo ambao ni waraka wa Serikali ambayo Kiongozi wake mkubwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, ningependa kumshauri tu dada yangu atafute ile clip aisikilize kwa umakini kwa sababu hakuna jambo ambalo Mheshimiwa Rais alilosema ambalo ni kinyume na huo waraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuzungumzia suala la Chuo Kikuu Huria. Chuo hiki kilianzishwa kwa Sura 344, Sheria Na. 346 na kupata hati idhini mwaka 2007 na madhumuni ya kuanzisha Chuo Kikuu Huria ilikuwa ni kutoa fursa kwa watu ambao hawawezi kwenda kukaa darasani kutokana na majukumu mbalimbali kwenda kusoma kwa kutumia huo mfumo wa masafa au open and distance learning bado kuna mahitaji hata sasa ya watu kupata mafunzo kwa kupitia mfumo huo huria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Sheria ya Chuo Kikuu Huria iko hapa na majukumu ya Chuo Kikuu Huria yameainishwa vizuri na Serikali haina mpango wowote wa kufuta hicho Chuo Kikuu Huria kwa sababu inaona kwamba yale majukumu bado yanahitajika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Serikali imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kuimarisha miundombinu katika Sekta ya Elimu. Tumeendelea kuboresha shule zetu kongwe, nafikiri Waheshimiwa Wabunge mnaona katika maeneo yenu shule mbalimbali tumezifanyia ukarabati. Ukienda Ifakara, ukienda Musoma Technical, ukienda Ifunda, ukienda Kondoa, Masasi, Tabora Girls, Ihungo huko watani wangu hawa akina Mheshimiwa Mwijage wananiambia Mheshimiwa hii sio sekondari, wananiambia hii ni University of Ihungo kwa sababu imejengwa kwa uimara ambao uko vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea pia kuimarisha miundombinu katika vyuo vya ualimu, tunafanya ukarabati katika Chuo cha Ualimu Tandala, Chuo cha Ualimu Nachingwea, Tarime, Kinampanda, Mandaka, Patandi na Ilonga.
Hata Tarime kwako tumefika tu, sisi hatuna ubaguzi, Serikali hii inawatumikia wananchi wote hata kama ni jimbo la Upinzani tunatumikia. Kwa hiyo tupo Tarime tunafanya hiyo kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niseme kwamba tunaendelea na ujenzi katika vyuo vyetu vya ualimu ambavyo ni pamoja na Chuo cha Ualimu cha Ndala, Chuo cha Ualimu cha Mpuguso pamoja na Chuo cha Ualimu cha Shinyanga ambapo majengo ya kisasa; madarasa, mabweni, maabara, kumbi za mihadhara, inaendelea kufanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia katika vyuo vikuu tunafahamu kwamba bweni namba mbili na namba tano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lilikuwa limekuwa na uchakavu mkubwa mpaka lilikuwa haliwezi kutumika, Serikali hii ya Awamu ya Tano tayari imekwishaanza kulifanyia ukarabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Chuo cha Elimu cha Mkwawa tunaendelea na ujenzi, tunakamilisha ujenzi wa ukumbi wa mihadhara ambao utaweza kuweka wanafunzi 1,200 kwa wakati mmoja, lakini pia tumewapatia shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kujenga maabara ya chemistry. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunaendelea na ujenzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Maktaba ambayo ina uwezo wa kuweka wanafunzi 2,500 kwa wakati mmoja. Kwa hiyo, nataka kusema tu kwamba Serikali inaendelea na jitihada katika kuboresha miundombinu katika Sekta ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la shule binafsi, wachangiaji mbalimbali wamezungumza na kuna wengine wamesema kwamba Serikali inaziingilia hizi shule. Naomba niseme tu kwamba hizi shule zipo kwa mujibu wa sheria na Wizara ya Elimu ndiyo msimamizi wa sheria za elimu, kwa hiyo, niombe tu kwamba wamiliki wa shule binafsi wanafahamu sheria na walipewa nyaraka, walipewa miongozo wakati wanasajili shule zao wahakikishe kwamba wanaendesha shule kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitakuwa ni kitu cha ajabu kwamba Serikali iache tu, kwamba kwa sababu ni shule binafsi wakati Serikali ndiyo imepewa dhamana ya kusimamia elimu ikiwa ni pamoja na shule binafsi. Kwa hiyo niseme kwenye suala la kukaririsha na suala la kufukuza wanafunzi kimsingi hivi vitu vinaongozwa na nyaraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waraka wa Elimu Na. 7 wa Mwaka 2004 ulikataza suala la kukaririsha wanafunzi au kuwafukuza wanafunzi kwa sababu hawajafikisha alama ambazo zimewekwa na shule na mitihani inayotungwa hakuna mtu ambaye anaikagua kuona kwamba ina kiwango gani lakini pia hata usahihishaji hakuna mtu ambaye anauangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Waraka Na. 12 wa Mwaka 2011 ukawa umeweka utaratibu kama kuna haja ya wanafunzi kukariri basi kuna utaratibu ambao unatakiwa kufuatwa. Kilichojitokeza, wakati shule zimeanza mwaka huu, 2018, kulikuwepo na wimbi kubwa la wanafunzi ambao walikuwa wanafukuzwa shuleni kwa sababu shule zinadai kwamba hawajafikisha zile alama na hawa wanafunzi waliokuwa wanafukuzwa ni wanafunzi ambao wako katika miaka ya mitihani; wanafunzi wa primary wa dasara la saba na wanafunzi wa sekondari wa kidato cha nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo shule ambazo shule moja ilikuwa imediriki kufukuza wanafunzi 114, shule moja inafukuza wanafunzi 35, shule moja inafukuza wanafunzi 25, hawa wanafunzi wanapokuwa wanafukuzwa kwa wingi namna hiyo wanajua kwamba wana Serikali yao na wazazi wamekuwa wanakuja kulalamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukianza kuangalia, hivi shule moja inafukuza wanafunzi 114 kwa mkupuo kwa kigezo kwamba hawajafikisha alama. Je, tatizo ni wanafunzi au Walimu? Kwa hiyo Serikali inaliangalia hilo jambo na tunashirikiana na shule binafsi, na wenyewe wameelewa na tutaendelea kuangalia kama kuna haja ya kupitia huu waraka wa kukariri basi tutafanya katika njia shirikishi, lakini suala la kuwafukuza wanafunzi nadhani ni suala ambalo halikubaliki. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako tukufu ili niweze kuhitimisha hoja yangu ambayo niliwasilisha tarehe 30 Aprili, 2018. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuendelea kuniunga mkono katika kazi yangu na kwa uongozi wake ambao umetukuka. Kwa dhati kabisa napenda kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye yeye ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za Serikali na hakika yeye ni kiranja kweli kweli, anatusimamia kweli kweli. Mheshimiwa Waziri Mkuu tunakushukuru sana kwa uongozi wako mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati kabisa napenda kukushukuru wewe wa kuniongozea mjadala wa hoja yangu tangu nilipoiweka mezani na mpaka sasa tunapohitimisha. Nakushukuru sana umeongoza hoja hii vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa shukrani za dhati kabisa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Peter Serukamba na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Juma Nkamia kwa ushirikiano mkubwa sana ambao ninaupata kutoka kwa Kamati hii. Nawashukuru sana kwa mchango mzuri ambao wameutoa katika hoja yangu na ninaahidi kwamba nitaendelea kuwapa ushirikiano na kuendelea kufanyia kazi maoni na ushauri mzuri ambao wananipatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe shukrani za dhati kwa Naibu Waziri wangu kwa ushirikiano mzuri anaonipatia, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu na watendaji wote ambao tumeshirikiana katika kuhakikisha kwamba tunafaikisha hoja hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwashukuru washirika wa maendeleo lakini kipekee naomba nimshukuru Bi. Alice Birnbaum ambaye ni Mwenyekiti wa Washirika wa Maendeleo kutoka Canada lakini yeye ndiye Mwenyekiti wa Wadau wa Maendeleo ya Elimu; Ndugu Pantaleo Kapich kutoka UNICEF; Ndugu John Lusingu kutoka DFID, Ndugu Helen Reutersward kutoka SIDA; Ndugu Faith Shayo kutoka UNESCO na Ndugu Mwanahamisi Singano kutoka Sekretarieti ya Development Partners. Hao wamekuwa na mimi tangu nilipowasilisha hoja hii na mpaka sasa hivi wapo wanaangalia ninavyohitimisha, nasema ahsanteni sana, thank you very much. Naamini kukaa kwenu hapa mmesikia hoja za Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, nikija kwenu kuomba ili…
KUHUSU UTARATIBU . . .
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hata maandiko matakatifu yanatufundisha kwamba tushukuru Mungu kwa kila jambo. Hawa watu wametusaidia tumejenga madarasa, kwa hiyo, mimi nawashukuru, naomba niendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niwashukuru sasa Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia hoja hii. Naomba nimalizie kwa kumshukuru mama yangu mzazi pamoja na mdogo wangu ambao wapo hapa kwa kuendelea kuniunga mkono, ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, naomba niseme kwamba hoja yangu imepata michango mingi ya Waheshimiwa Wabunge ambapo jumla ya Wabunge 117 wamechangia hotuba. Waheshimiwa Wabunge 77 wamechangia kwa maandishi na Waheshimiwa Wabunge 46 ambao wamechangia kwa kuongea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kanuni haziniruhusu kuwataja Waheshimiwa Wabunge waliozungumza, majina yao ninayo hapa na nitaomba orodha yao iingie kwenye Hansard. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa unyenyekevu kabisa naomba nitoe shukrani za dhati kabisa kwa Waheshimiwa Wabunge wote ambao mmechangia. Kwa kweli michango yenu imekuwa ni mizuri sana na inaonesha ni jinsi gani ambavyo mnaithamini elimu. Kuonesha jinsi ambavyo michango imekuwa mizuri, leo tumepata mpaka na pambio kutoka kwa Mheshimiwa Mbatia, ametuimbia na wimbo wa chekechea. Waheshimiwa Wabunge nawashukuru sana na ninawaahidi kwamba michango yenu yote nimeipokea na nitaizingatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda sitaweza kujibu hoja zote, lakini naomba nizungumzie mambo machache ambayo yamezungumziwa na Waheshimiwa wengi, lakini pia nitajikita kujibu hoja ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati yangu. Kwa bahati nzuri hoja ambazo zimetolewa na Kamati pia zimekuwa ni hoja ambazo zimezungumziwa na Waheshimiwa Wabunge wengi. Kwa hiyo, napotoa maelezo nitakuwa sitaji hoja imetoka kwa nani lakini nitakuwa najikita kwenye hoja moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ulikuwa unawahisha shughuli kaka yangu hapa wewe tulia tu hakuna shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie hali ya elimu, ni suala ambalo limezungumzwa sana, limezungumza na Kamati yangu, lakini pia limezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wengi sana ambao wamechangia. Katika hoja hii wamesema kwamba hali ya elimu katika nchi yetu inashuka na kuna changamoto nyingi katika utoaji wa elimu katika nchi yetu, miundombinu, upatikanaji wa walimu na vifaa toshelezi vya kufundishia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuelezea kwamba elimu katika nchi yetu imekuwa ikipita katika vipindi mbalimbali. Tumekuwa na kipindi ambacho tulikuwa na changamoto sana ya uandikishaji katika shule za msingi na sekondari, tukaja na Progamu ya Maendeleo ya Elimu ya Msingi almaarufu kama PEDP ambayo iliongeza udahili wa wanafunzi katika shule za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tulikuwa na changamoto ya udahili mdogo katika shule za sekondari na tukawa na Programu ya Mpango wa Maendeleo ya Sekondari. Vilevile kulikuwa na mkakati wa dhati kabisa wa kujenga shule ya sekondari katika kila kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango hii imekuwa na mafanikio makubwa sana. Ukiangalia idadi ya shule za sekondari zilizokuwepo, mwaka 2005 zilikuwa 1,202 na kutokana na mikakati hii hadi kufikia mwaka 2010 jumla ya sekondari zilizokuwepo nchini zilikuwa 3,508. Mafanikio haya yalienda sambamba na ongezeko kubwa la wanafunzi ambao waliongezeka kutoka wanafunzi 524,324 hadi kufikia 1,401,330 kutoka mwaka 2005 hadi 2010.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio haya ya ongezeko kubwa la wanafunzi ni dhahiri kwamba yaliambatana na changamoto kama vile miundombinu ambayo sasa haitoshelezi kama vile madarasa, ofisi za walimu, mabweni na maabara lakini pia ilileta uhaba mkubwa wa walimu. Sote tunafahamu tulipokuwa tunatekeleza mpango wa PEDP na SEDP kulikuwa na upungufu mkubwa wa walimu. Serikali ilifanya jitihada za kukabiliana na changamoto ya walimu kwa kuwa na mikakati mbalimbali ambapo bado utoshelezi haujafikiwa hasa katika masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua haya, Rais wetu wa Awamu ya Tano, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli alipokuwa ameingia madarakani alikuwa anatambua fika kwamba amekabidhiwa nchi ikiwa na changamoto ambazo zilitokana na mafanikio ya kuongeza upatikanaji wa nafasi za elimu kwa watoto wa Kitanzania kwenye elimu ya msingi na elimu ya sekondari. Kwa kutambua hayo, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuwa analizindua Bunge hili tarehe 22 Novemba 2015, alizungumza na naomba kunukuu; “Natambua juhudi kubwa zimefanyika katika upanuzi wa elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vikuu. Serikali ya Awamu ya Tano itajielekeza katika kuongeza ubora wa elimu inayotolewa ikiwa ni pamoja na kuongeza mkazo katika masomo ya sayansi.” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hayo ili kukumbusha kwamba elimu imekuwa ikipitia katika vipindi mbalimbali na Mheshimiwa Rais alitambua changamoto zilizokuwepo na alizungumza ndani ya Bunge lako Tukufu. Nimpongeze sana Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu ametekeleza ahadi yake kwa vitendo. Ndani ya kipindi chake cha uongozi tumeona akitekeleza kwa vitendo uboreshaji wa elimu na nitaeleza kwa uchache mambo ambayo yamefanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na uboreshaji wa elimu, Mheshimiwa Rais akaanzisha utoaji wa elimu bila malipo. Kwa kweli hiyo ni commitment kubwa huku unaboresha elimu na wakati huo unatoa elimu bila malipo. Utoaji wa elimu bila malipo nao umekuja na mafanikio makubwa sana, idadi ya wanafunzi waliojiandikisha darasa la kwanza iliongezeka kutoka 1,386,592 hadi kufikia 1,896,584. Kwa hiyo, kwa maneno mengine changamoto ya madarasa ikazidi kuongezeka kutokana na ongezeko la wanafunzi ambao wanakwenda shuleni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika sekta ya elimu ni kazi ambayo inaonekana wazi kabisa, haijajificha. Nenda katika Halmashauri yoyote utaona kazi nzuri ambayo imefanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika sekta ya elimu. Kuna miundombinu ambayo inajengwa, lakini vilevile kumekuwa na kuhakikisha kwamba tunapeleka vifaa vya maabara. Kwa kweli, niseme tu kwamba Waheshimiwa Wabunge suala la kuboresha elimu ni commitment ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano na analitekeleza kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwa uchache mambo ambayo yamekwishafanyika kutoka Serikali Kuu, tukumbuke kwamba ujenzi wa miundombinu ni jukumu la TAMISEMI, hizo kazi zinafanywa na Halmashauri zetu, lakini kwa kutambua uzito na mzigo ambao halmashauri zilikuwa zinaelemewa Serikali ya Awamu ya Tano imeona pia nayo ishiriki katika kuangalia yale maeneo ambayo yana changamoto kubwa tumekuwa tukipeleka kuwaunga mkono. Kwa hiyo, tayari jumla ya madarasa 1,947 na mabweni 338 yamekwishajengwa. Tumekuwa tukizungumzia hapa adha ambayo mtoto wa kike anaipata kutembea umbali mrefu kwenda shuleni. Serikali ya Awamu ya Tano inaliona hilo na kwa kupitia Serikali Kuu tayari tumekwishajenga mabweni 338 sambamba na yale ambayo yanajengwa na Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile matundu ya vyoo tumekwishajenga 4,501; nyumba za walimu 95; maktaba nne, majengo ya utawala 21 na mabwalo 14. Haya ni yale ambayo yamefanywa na Serikali Kuu, lakini hayajajumuisha idadi ya vyoo ambavyo vimejengwa katika Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tumeshuhudia jinsi ambavyo shule zetu kongwe zilikuwa zipo katika hali mbaya, zilikuwa zipo choka mbaya kweli kweli, lakini Serikali ya Awamu ya Tano inakarabati shule kongwe na tayari tumeanza na shule 46 na mpaka sasa hivi tumekwishakamilisha shule 20 na ukarabati wa hizi shule nyingine unaendelea na shule zote kongwe 88 zitakarabatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, hata vyuo vyetu vya ualimu vilikuwa katika hali ya uchakavu. Tumekwishafanya ukarabati katika vyuo vya walimu 22 na dada yangu Mheshimiwa Esther Matiko hata kwake Tarime tumefika tunafanya ukarabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali inaendelea na uboreshaji wa miundombinu katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na vyuo vikuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuonyesha dhamira ya Mheshimiwa Rais wetu muungwana, akiahidi anatekeleza, hata bajeti ya mwaka huu ambayo nimesimama Waheshimiwa Wabunge na naomba wote kwa pamoja muiunge mkono kwa sababu elimu ndiyo uti wa mgongo wa maendeleo ya nchi yetu na kwa hiyo elimu haina itikadi, naomba mtuunge mkono bajeti yetu ya maendeleo imeongezeka kutoka shilingi 916,841,822 hadi shilingi 929,969,402. Kwa hiyo, hiyo, inaonesha dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika kuboresha elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaambie tu Waheshimiwa Wabunge hata Roma haikujengwa kwa siku moja, lakini jitihada kubwa zinafanyika, muendelee kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu na nina hakika kwa hapa tulipoanzia tutafika na elimu yetu itakaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya pia usambazaji wa vifaa, tumekuwa tukinunua vifaa vya maabara na tumepeleka katika shule 1,696. Kama mnakumbuka ahadi ya Mheshimiwa Rais ilikuwa pia kuboresha mambo ya ufundishaji wa sayansi. Tunatambua pia kwamba ili elimu iweze kwenda vizuri lazima kuwe na mwalimu bora. Kwa hiyo, Serikali imekuwa ikiwekeza pia katika mafunzo kwa walimu kazini. Katika hili tumefanya sana, tumeweza kutoa mafunzo kwa walimu wa awali 16,129; tumetoa mafunzo kwa walimu wanaofundisha stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu ambazo Mheshimiwa Mbatia naona naye atakuja kuungana nao ili aweze kufundisha kwa nyimbo zake zile nzuri walimu 65,232; tumetoa mafunzo kwa walimu wenye mahitaji maalum 800 na vilevile tumetoa mafunzo kwa walimu wa sekondari 12,726 kati ya hao walimu wa sayansi 10,614 na walimu wa lugha 2,112. Hayo ni kwa uchache tu kwa sababu ya muda siwezi kuelezea mambo ambayo Serikali ya Awamu ya Tano inafanya kuboresha elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge tuungane na tuhakikishe kwamba ule upungufu ambao tunaweza tukaenda kwa kasi zaidi, ushauri wenu tunaupokea, tutaufanyia kazi lakini tunatambua kwamba tumetoka mbali katika historia ya elimu yetu. Tusiangalie tu Awamu ya Tano, lakini kama nchi historia ya elimu yetu imekuwa katika mapito mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala ambalo limezungumzwa sana hapa la wahitimu kumaliza bila kuwa na umahiri unaotakiwa. Wamezungumzia watu wanamaliza elimu ya msingi, hawajui kusoma na kuandika, watu wanamaliza vyuo vikuu, mtu anachukua sheria lakini hawezi kuandika hukumu na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili naomba niseme kwamba Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji katika sekta ya elimu. Niungane mkono na Kamati yangu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, wamenukuu Taarifa ya Benki ya Dunia kuhusu viashiria vya utoaji huduma (service delivery indicators) ambazo zinaonesha kwamba walimu wanakuwa shuleni, lakini hawaingii madarasani au wakati mwingine hawafiki shuleni kabisa. Hali hii inaonesha kutowajibika kwa viongozi ambao wamepewa dhamana ya kusimamia elimu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba hapa katika sekta ya elimu tuna bahati kwa sababu tuna usimamizi mpaka kwenye ngazi ya kata, tuna Afisa Elimu Kata.
Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kutoa maagizo kwa Maafisa Elimu wote nchini kuhakikisha wanafanya kazi yao ipasavyo, wasimamie kwa karibu elimu na kuhakikisha kwamba walimu wanafundisha kama inavyotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaase waache mtindo wa kumchukulia mwalimu sasa kama ndio mtu wa kulaumiwa yanapotokea matatizo, mwalimu ndiyo anaachishwa kazi. Kwa nini usubiri matokeo ya mtihani shule yake ikifanya vibaya ndiyo umuachishe kazi, ulikuwa wapi mwaka mzima kumfuatilia, kuangalia anafanya nini, unasubiri matokeo ya mtihani yeye ndiyo umfukuze kazi. Hiyo sio sawa, ni uonevu kwa wakuu wa shule kwa sababu na wenyewe wana viongozi juu yao, kwa nini wao ambao wanatakiwa kuwasimamia wasiwajibishwe? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaagiza Maafisa Elimu wafanye kazi yao vizuri. Maafisa Elimu wa ngazi ya Kata unakuta mtu ana shule tano tu, utashindwaje kuzisimamia au utashindwaje kuona matatizo. Kwa hiyo, katika hili Serikali itahakikisha tunaimarisha usimamizi ikiwa ni pamoja na kuwaondoa viongozi ambao ni mzigo, ambao ndiyo wanaotufikisha hapa. Serikali inafanya kazi kubwa ya kuwekeza, lakini kama hakuna usimamizi imara katika sekta ya elimu tutakuwa kama vile tunatwanga maji kwenye kinu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa taasisi za elimu ya juu na vyuo vya kati, wahitimu wanamaliza hawawezi hata kuandika hukumu, tunavyo vyombo ambavyo vimepewa mamlaka kisheria vya kuhakikisha vinadhibiti ubora katika elimu ya kati na elimu ya juu. Tunalo Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na tuna Tume ya Vyuo Vikuu nchini. Kwa hiyo, hii nayo inadhihirisha kwamba pengine zana wanazozitumia katika kufanya ukaguzi zinahitaji kufanyiwa mapitio. Kwa sababu tumekuwa tukiona hapa Tume ya Vyuo Vikuu imekuwa ikifungia vyuo kwa sababu havina sifa, tumeona hapa Baraza la Taifa la Ufundi limekuwa likifungia vyuo lakini nadhani ipo haja ya kukaa chini kwa taasisi hizi kupitia upya zana wanazozitumia kukagua vyuo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, natoa maagizo kwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi, wakae chini wapitie upya vigezo ambavyo wanatumia kuangalia ubora wa vyuo vyetu vikuu. Angalieni mitaala inayotumika, angalieni sifa za walimu ambao wako katika vyuo vikuu, angalieni mpaka na aina ya mitihani ambayo inatolewa, namna inavyosahihishwa ili muangalie vigezo vyote kwa ujumla wake. Kwa sababu haiwezekani tuwe tunafungia vyuo halafu bado hata vyuo ambavyo tunaviona vinafaa vinatoa wahitimu ambao hawahitajiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kutoa wahitimu ambao hawana sifa zinazotakiwa halikubaliki. Naviagiza hivi vyombo kufanya kazi yao bila kumuogopa mtu yeyote. Chuo chochote ambacho kitabainika hakina sifa, iwe ni cha Serikali, iwe ni cha binafsi, kama hakina sifa kifungiwe. Hatuwezi tukaendelea kuangamiza Taifa hili kwa kuzalisha watu ambao hawana sifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la hali ya ufaulu nchini. Suala hili pia limeongelewa sana na hata Kamati yetu imetoa takwimu kubwa na mimi nikiri kwamba hali ya ufaulu ilivyo hata na mimi natamani kwamba wanafunzi wangeweza kufaulu kwa wingi zaidi kuliko wanavyofaulu sasa. Kama nilivyotangulia kusema Waheshimiwa Wabunge ni kwamba maendeleo na hasa katika sekta ya elimu ni hatua kwa hatua. Kwa hiyo, tumekuwa kwa kweli na ufaulu ambao ukiangalia asilimia kubwa ya wanafunzi wanakuwa katika daraja la nne na daraja la sifuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kwamba mtu anayefaulu kwa daraja la kwanza amefaulu zaidi kuliko wa daraja la nne lakini niombe tu tusije tukaweka dhana kwamba mtu aliyepata daraja la nne hafai kabisa, kwa sababu kwa vigezo tulivyonavyo sasa daraja la nne amefaulu. Suala ambalo tunaweza tukazungumza ni kama labda pengine tunaona viwango viko chini tunaweza tukafikiria hata kuviongeza lakini kwa sababu kwa viwango tulivyojiwekea daraja la nne mtu amefaulu, tusiongee katika lugha ambayo ni kukatisha tamaa. Kwa hiyo, nimesema kwamba kupata division one amefaulu vizuri zaidi, lakini kwa utaratibu uliopo sasa hivi hata aliyepata division four amefaulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme pia kwamba suala la idadi ya ambao wamepata division one mpaka three kama nilivyosema si ya kuridhisha kwa kiwango ambacho hata Serikali ingetamani. Sisi hatuwezi kuchakachua matokeo, tunatoa matokeo kadri ambavyo yapo, lakini Serikali inachokifanya ni kutekeleza wajibu wake, kuweka miundombinu na kuhakikisha walimu wanapatikana. Kwa hiyo, pia nitumie nafasi hii kuwaomba wanafunzi nao watekeleze wajibu wao kwa sababu hata mwanafunzi naye pia ana wajibu katika kuweza kufanya vizuri katika mitihani yake, lakini hata mzazi naye ana wajibu kwa mwanafunzi kufanya vizuri. Serikali itaendelea kutekeleza wajibu wake lakini suala la ufaulu mzuri ni collective responsibility kati ya mzazi, walimu, wanafunzi na jamii kwa ujumla. Kwa hiyo, naomba kwa kweli tushirikiane na Serikali kwa sababu Serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha kwamba wanaopata daraja la kwanza mpaka la tatu wanakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufaulu umekuwa ukiongezeka kama ninavyosema, japo siyo kwa kasi kubwa, lakini ukiangalia mwaka 2015 waliopata daraja la kwanza mpaka la tatu walikuwa asilimia 25.34; mwaka 2016 walikuwa asilimia 27.60 na mwaka 2017 walikuwa asilimia 30.15. Kwa hiyo, kuna ongezeko dogo lakini tukishirikiana na usimamizi ukawa mzuri naamini hata hii kasi ya ongezeko inaweza ikaenda vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii pia kuwaomba Waheshimiwa Wabunge tuiangalie elimu katika mapana yake kwa ujumla. Hata sisi Waheshimiwa Wabunge ulipoingia humu Bungeni siku ya kwanza na ulivyo leo, sasa hivi tuna miaka miwili na nusu uko tofauti kabisa, hakuna chaki, hakuna ubao lakini hata interaction ambayo unaipata pia ni elimu tosha. Kwa hiyo, tunapopima mafanikio ya elimu tuangalie pia katika ujumla wake hata mwamko wa wananchi kupeleka wanafunzi shule pia ni mafanikio katika sekta ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani Serikali ilikuwa inatumia nguvu kubwa sana kupita katika kijiji na katika kaya kuwatoa watoto ili waende shuleni lakini sasa hivi tunashuhudia mafuriko ya wanafunzi shuleni. Mimi nasema kwamba haya ni mafanikio katika elimu na mafanikio haya ndiyo yameendelea kuleta changamoto ambazo Serikali inazifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie mwamko wa wananchi katika shughuli za kijamii, unakuta hata mzee anakwenda kushiriki katika kujenga shule na zahanati. Mimi nasema haya ni mafanikio kwa sababu wangekuwa hawaoni umuhimu wa elimu wasingejitokeza kujitolea nguvu zao. Pia hata ukiona mwitikio katika masuala ya kijamii kwa ujumla, masuala ya afya, idadi ya wanawake ambao wanakwenda kliniki, yote ni mafanikio ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nielekee kwenye suala lingine ambalo limeongelewa kweli kweli, suala la usimamizi wa shule binafsi, lakini pia nitaliunganisha na suala la wanafunzi kukariri. Waheshimiwa Wabunge wameongea sana na wengine wameongea kwa hisia na wengine wameenda mbali kabisa wanasema kwamba Serikali inaonea wivu sekta binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na suala la kukariri na naomba nilizungumze tu vizuri, nami najua Waheshimiwa Wabunge ni waelewa, wakati mwingine pengine inawezekana hamkuwa na taarifa kamili ya jambo hili. Kimsingi niseme kwamba suala la wanafunzi kukariri ni suala ambalo lipo kwa mujibu wa taratibu na kukariri hata wanafunzi wa shule za Serikali wanaruhusiwa kukariri kwa mujibu wa utaratibu ambao umewekwa.
Kuna mitihani ambayo inatolewa, kuna mtihani wa darasa la nne mwanafunzi ambaye hafikishi alama anatakiwa kukariri na kuna mtihani wa kidato cha pili mwanafunzi anaruhusiwa kukariri. Mbali na mitihani hiyo bado kuna utaratibu ambao mwanafunzi anaweza kukariri ikiwa mzazi wake anaona kwamba uwezo wa mtoto wake ni mdogo kama ataendelea na hatua aliyofikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaratibu huo upo na nizishukuru sana shule binafsi kwa sababu asilimia kubwa wanatekeleza kikamilifu miongozo na taratibu za elimu. Hata hivyo, wapo wachache, tena wachache sana ambao wanakwenda kinyume na utaratibu na nitatoa mifano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Waheshimiwa Wabunge walikuwa wanazungumzia suala la wanafunzi kukariri, lakini tatizo ni zaidi ya hapo, sio tu kukariri, shule zimekuwa zikiwafukuza wanafunzi na kufukuza huko kwa kweli mimi nasema kwingine kumepitiliza. Kwa mfano, tulipokuwa tunaanza mwaka huu 2018, shule ambazo zimetoa taarifa, tulikuwa na wanafunzi 1,029 ambao wengine wako katika mwaka wa mtihani amefukuzwa tu kwa sababu hajafikia alama, siyo kwamba anakariri, hapana, anaambiwa ondoka, aende nyumbani, mzazi amelipa mamilioni ya fedha na kwa sababu mwanafunzi hakufikisha alama anaambiwa aondoke. Kwani kazi ya shule ni nini, si ndiyo kutoa elimu? Kama mwanafunzi hawezi si umwambie akae hapo umfundishe? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli suala la kuwafukuza wanafunzi si halali. Suala hili linakwenda kinyume na sheria ya elimu kwa sababu hizi shule binafsi nazo zinatakiwa zizingatie sharia hii kwa sababu sheria tunapozitunga hapa Bungeni wote tunawajibika kuzizingatia ikiwemo Serikali na kila mmoja ambaye sheria hiyo inamhusu. Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 inasema wazi kwamba; primary school shall be compulsory for every child who has reached the age of seven years to be enrolled for primary school. Sheria hiyo inaonesha kabisa kwamba mtoto lazima asome, ahudhurie mpaka amalize, ndivyo sheria inavyosema, haisemi akifika darasa la sita kwa sababu unamuona hajafikisha alama umfukuze aende mitaani, tutazalisha watoto wa mitaani bila sababu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni kutokana na changamoto hiyo ambayo nikitoa mfano shule ya Panda Hill iliyoko Mbeya peke yake ilikuwa imefukuza wanafunzi 114, shule moja wanafunzi 114, eti hawajafikisha alama ambayo imewekwa na shule. Hivi shule moja wanafunzi 114 wakishindwa kufanya vizuri ni tatizo la wanafunzi au inawezekana ni tatizo la walimu wao hawakuwafundisha vizuri? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule hizi zinachukua wanafunzi ambao ni cream, leo wanafunzi 114 unawafukuza? Ni kutokana na sababu hizo za watu kufukuza ndiyo Serikali ikawa hata imetoa na maelekezo kwamba wale waliofukuzwa warudi shuleni, suala la kukaririsha halina matatizo yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kutokana na changamoto hizo mimi mwenyewe binafsi nilikutana na wamiliki wa shule binafsi. Mwanzoni walikuwa wanaona kama vile Serikali imewaonea, lakini baada ya kuwapa takwimu kwa kweli na wenyewe walikiri kwamba suala hili shule moja kama hiyo Panda Hill imefukuza wanafunzi 114, Shule ya Sekondari ya St. Pius ya Dar es Salaam wanafunzi 89 kwa mwaka mmoja wanafukuzwa. Kwa hiyo, wao wenyewe shule binafsi mimi nawashukuru sana, hata na wao ni wazalendo sana, walisema Mheshimiwa Waziri, hili jambo ungetuambia sisi wenyewe, tuna chama chetu tungewashughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kweli suala hili wala siyo tatizo kubwa sana ni suala tu sasa la baada ya hayo kutokea tulichokubaliana na wamiliki wa shule binafsi ni kwamba tukae kwa pamoja kwamba pamoja na nia njema ya kuhakikisha kwamba kabla mtoto hajaendelea anakuwa na viwango vizuri, lakini tuweke na utaratibu wa kulinda watoto wa wanyonge wa Kitanzania ambao wanakuwa milioni za fedha halafu mtu mmoja tu kwa mtihani ambao hakuna anayejua ameutunga kwa vigezo gani, kwa mtihani ambao hakuna anayejua ameusahihisha kwa vigezo gani, analala anaamka anawaambiwa watoto 114 kwenye shule moja waondoke. Jambo hili halikubaliki na Waheshimiwa Wabunge naomba katika hili la kufukuza kwa utaratibu huo mniunge mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna Kamati ya Majadiliano ambayo kuna wajumbe kutoka Wizara ya Elimu na wajumbe kutoka sekta binafsi ambao kwenye sekta binafsi kuna Bwana Laurent Gama wa TAPIE ambaye ni Katibu, kuna Bi. Stella Rweikiza wa TAPIE na Bwana Moses Kyando kutoka TAMONGSCO ambapo majadiliano yanakwenda vizuri. Wenyewe wamesema pia wataisaidia Serikali katika kuhakikisha hakuna shule za binafsi ambazo zinawachafua kwa sababu wanatambua kwamba samaki mmoja akioza wote wameoza. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge hili suala halina tatizo lolote na baada ya muda mfupi tutafikia mwafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihitimishe hoja hii kwa kulieleza Bunge lako tukufu kwamba Serikali inaheshimu na kuthamini sana mchango wa sekta binafsi katika utoaji elimu. Kwa taarifa tu ya Bunge hili, sekta binafsi kwenye elimu ni wadau wakubwa sana ambao Serikali kwa namna yoyote ile haiwezi ikawachezea au kutothamini mchango wao kwa sababu shule za msingi za binafsi zilizoko nchini ni 1,247; shule za sekondari za binafsi ni 1,192 na wanaosoma hapo ni watoto wa Kitanzania. Sasa ina maana Serikali ikinyanyasa shule binafsi inanyanyasa watoto wa Kitanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie kwamba hakuna mgogoro wowote, hakuna wivu wala chuki kwa shule binafsi. Labda tu kinachoweza kujitokeza ni mawasiliano, pengine inawezekana kuna watendaji ndani ya Wizara yangu wakiona wamiliki wa shule binafsi wanakuwa wanawapa majibu ambayo siyo mazuri. Sasa hilo ni suala la kiutendaji na naomba kama wapo watendaji wa namna hiyo niambiwe, nitawashughulikia kikweli kweli, wasituharibie ushirikiano wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imezungumzwa ni suala la udhibiti ubora wa shule na Waheshimiwa Wabunge wengi kwa ujumla wao wameizungumza sana lakini hata na Kamati yangu wamezungumza na kumetolewa ushauri wa kuundwa chombo cha kudhibiti ubora yaani uanzishwaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Elimu katika nchi yetu. Kwanza nianze kusema kwamba napokea ushauri huu kwa heshima kubwa na niseme kwamba kama nilivyotangulia kusema katika maelezo yangu ya utangulizi, nimefaidika sana na michango ambayo Waheshimiwa Wabunge mmeitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala hili nalipokea lakini nizungumzie jitihada ambazo kwa sasa Serikali ilikuwa imeanza kuzifanya katika kuboresha hii sekta ya udhibiti ubora wa shule. Kwanza, nimeelezea ile changamoto ya wanafunzi kuwa wengi katika shule zetu, lakini nimeeleza pia na jitihada ambazo Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikifanya katika kukabiliana na changamoto hizo. Ni ukweli kwamba katika baadhi ya shule ile idadi ya ongezeko la wanafunzi halijaenda sawia na idadi ya walimu ambao wanatakiwa kuwepo shuleni. Kwa kutambua hilo, Wizara imekuwa ikiendelea kuimarisha mafunzo kazini na uhaba wa walimu wa sayansi pamoja na mkakati wa wanafunzi wale ambao walikuwa wako UDOM ambao mwaka huu kuna bunch ambayo imemaliza lakini pia hata katika bajeti yangu mwaka huu tutatenga fedha kwa ajili ya waafunzi ambao wamesoma Bachelor of Science, ile general, ili wakafanye Postgraduate Diploma in Education kuweza kuendelea kutatua changamoto za elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika udhibiti ubora wa shule, kwa kutambua umuhimu mkubwa wa ufuatiliaji na ujifunzaji kwa sababu Wadhibiti Ubora wa Shule ndiyo jicho letu, ni sawa ambavyo CAG ndio jicho la Serikali katika matumizi ya fedha za umma.
Kwa hiyo, Wizara kwanza tumebadilisha mfumo wa ukaguzi, nimeeleza katika hotuba yangu kwamba tumeandaa kiunzi cha udhibiti ubora wa shule ambacho kitaboresha usimamizi wa masuala ya elimu.
Pia tumetoa mafunzo kuanzia ngazi ya shule na Kamati za shule. Kwa mara ya kwanza tumeshirikisha pia Kamati za Shule, kwa sababu ni kweli tunaona kwamba tuwe na chombo cha kuangalia hii elimu yetu lakini niseme kwamba tuna shule za msingi 17,000, tuna shule za sekondari kama 5,500, kwa hiyo, kwa namna yoyote ile chombo ambacho kitakuwa kipo kitaifa bado kitakuwa na changamoto. Mkakati wa Wizara pia ni pamoja na kuimarisha Bodi za Shule abazo ndizo zinazowajibika katika usimamizi wa moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu udhibiti ubora wa shule tunauboresha na nashukuru katika michango kuna Waheshimiwa Wabunge waliona kwamba tunajenga ofisi 50 za udhibiti ubora wa shule. Pia nimesema tumenunua magari 54, pikipiki 2,894 kwa ajili ya kuimarisha ufuatiliaji ngazi ya kata. Waheshimiwa Wabunge pikipiki hizi tutazigawa kabla hatujamaliza Bunge. Kwa hiyo, mkirudi majimboni mtapata pikipiki ili kuimarisha usimamizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tushirikiane katika kuwabana watu wasimamie elimu ipasavyo, hii ndiyo jitihada ya Serikali. Kama nilivyosema, elimu ni juhudi za Serikali, wazazi, wanafunzi, wote kwa ujumla wetu tukishikana mkono, nina uhakika kwamba elimu ya Tanzania itasimama. Niwatoe hofu kabisa wale ambao mnasema kwamba elimu ya nchi yetu iko vibaya; niwaambie elimu ya nchi yetu iko vizuri kabisa, ina afya njema na Rais wetu ana utashi, amekwishafanya mambo makubwa, kitu kikubwa ni ushirikiano ambao unatakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata suala la kuwa na mjadala wa elimu limezungumzwa sana. Niseme tu kwamba mjadala katika sekta ya elimu ni mjadala ambao utatuwezesha sisi kubaini matatizo. Niseme kwamba kuna matatizo ambayo tayari tunayafahamu, tunafahamu kwamba kuna shule ambazo zina mrundikano na ndiyo maana tumejikita katika miundombinu; tunafahamu kuna shule zina uhaba wa walimu, namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Utumishi ameahidi kwamba ataendelea kulitatua; tunafahamu kwamba kuna shule ambazo watoto wanatembea umbali mrefu, ndiyo maana tumekuwa tunajenga mabweni.
Kwa hiyo, kipaumbele cha Serikali kwa sasa ilikuwa ni kujikita katika kutatua changamoto ambazo tayari tunazifahamu lakini hii haizuii wadau ambao wana mapenzi mema na nchi yetu kuendelea kuibua changamoto nyingine na kuipa changamoto Serikali yao ili sambamba na changamoto ambazo Serikali imeamua inafanyia kazi, kama zipo nyingine zitafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mjadala ji suala ambalo lina afya kwa sababu linalenga katika kuibua changamoto zilizopo ili Serikali, Serikali hii sikivu iweze kuzifanyia kazi na tumekuwa tukishuhudia mijadala kwa mfano tulikuwa na Kigoda cha Mwalimu kilikuwa kinazungumzia masuala ya uporaji wa rushwa na rasilimali za nchi yetu; tumeshuhudia Kibweta cha Mwalimu ambacho kilikuwa kinazungumzia kuelekea uchumi wa kati. Kwa hiyo, tumekuwa na mijadala mbalimbali ambayo ikitokea katika nchi na hivyo basi mjadala kwenye elimu ni suala ambalo niseme kama Waziri mwenye dhamana linapokelewa kwa mikono miwili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshapigiwa kengele na nisingependa kupigiwa kengele ya pili kama nilivyosema michango ya Waheshimiwa Wabunge ilikuwa ni mingi ni mizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na moja tu ambalo nalo lilizungumzwa sana kuhusiana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na kwamba hakuna mpango mkakati wa sera na kwamba tunatumia sheria ya mwaka 1978, nikiri kwamba kweli ile sera yetu ya elimu bado haijawekewa zile sheria na niseme kwamba tayari ile sera ya elimu kwa namna ambavyo iliandikwa kwa bahati mbaya iliandikwa katika namna ambayo inakuwa ni nyaraka au document ambayo haiishi, wanasema a living document kwamba mle ndani kwa mfano imesema Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa sasa hivi haipo mle ndani inazungumzia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ile pale Wizara sasa hivi haipo na mambo mengine nimetoa kwa uchache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaona kwamba ni vema hata hiyo uandishi wa sera yetu uandikwe katika namna ambayo itakuwa ni document ambayo inaweza ikakaa miaka mingi bila kuhitaji kubadilisha badilisha na Mheshimiwa Mbatia naona ameishilikia, lakini tu kwa uchache ni kwamba hii suala la sera ya elimu pia kuna suala kwa mfano na umri wa kwenda shuleni kutoka miaka saba kwenda miaka mitano ilibadilishwa kabla ya hata kubadilisha sheria kwa sababu miaka saba umri wa kwenda shuleni umewekwa ndani ya sheria. Kwa hiyo, tayari hata kuna mkingano katika sheria zilizopo. Niombe katika hii sera ya elimu tunakusudia kufanya mapitio vile vitu ambavyo vinaukinzani tuvibadilishe kwanza kabla hatujaenda kwenye kutengeneza sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maelezo hayo na kwa sababu kwamba muda wa kwenda shuleni miaka saba umetajwa kwenye sheria ya elimu na katika Bunge lako tukufu hamjafanya mapitio ya marekebisho ya Sheria ya Elimu miaka ya elimu ya msingi itaendele kuwa miaka saba hadi pale marekebisho ya sheria yatakapofanyika. Kwa hiyo, suala la kusema kwamba kutakuwa na wanafunzi ambao wanamaliza wengine darasa la sita, wengine ni darasa la saba kwa sasa halipo mpaka hii sheria ambayo tunaitumia itakapofanyiwa marekebisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo na ufafanuzi huu wa hoja naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge ambao sikuweza kupata muda wa kujibu hoja zao kwamba hoja zote tutazijibu kwa maandishi na baada ya ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizotolewa ambazo nimeweza kuzielezea pamoja na zile ambazo ninazileta kwa maandishi, sasa kwa unyenyekevu mkubwa kabisa ninawaomba Waheshimiwa Wabunge wote tutakapokaa kama Kamati naomba wote kwa pamoja muunge mkono hoja yangu mnipitishie Makadirio ya Mapato na Matumizi ili sasa haya ambayo nimewahaidi niweze kwenda kutekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo naomba kutoa hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyopo mbele yetu. Kwanza kabisa, napenda kuanza kwa kusema kwamba ninaunga mkono hoja za Kamati tatu ambazo zimewasilishwa.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee kabisa, nami nichukue nafasi hii kuishukuru na kuipongeza kwa dhati kabisa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendelo ya Jamii kwa namna ambavyo wamekuwa wakitushauri kwa maoni na mchango mzuri. Hakika nikupongeze na wewe kwa namna ambavyo uliisuka hiyo Kamati, ina watu ambao wanajali kabisa na wana michango mizuri. Niseme mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba Kamati hii ni tofauti kabisa na namna ambavyo watu walikuwa wanai-perceive wakati unaiunda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kweli tunafanya nao kazi vizuri, wamekuwa wakitupa maoni mazuri na tumekuwa tukisonga mbele kwa sababu kuna ushirikiano mzuri na maoni mazuri kutoka kwa Kamati. Kwa hiyo, baada ya shukrani hizo niseme tu kwamba tumepokea maoni na ushauri wa Kamati na Serikali itayafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kutolea ufafanuzi baadhi ya hoja ambazo zimejitokeza katika mjadala wa hoja iliyopo mezani leo hii. Kwanza kabisa, kuna suala ambalo limezungumzwa la upungufu wa Wahadhiri hasa wale wenye kiwango cha Shahada ya Uzamivu pamoja na Maprofesa na hasa katika Chuo Kikuu cha Dodoma.
Mheshimiwa Spika, niseme kweli kuna upungufu wa Wahadhiri katika vyuo hivyo na ndiyo maana Chuo Kikuu cha Dodoma hakijaweza kudahili wanafunzi capacity yake ni 40,000 lakini tunafahamu kwamba chuo kikuu siyo majengo tu ni pamoja na kuwa na Wahadhiri wenye sifa. Nilihakikishie Bunge lako kwamba Serikali inafanyia kazi suala hili kwa nguvu zote na katika bajeti ya mwaka 2018/2019, Serikali ilitenga shilingi bilioni 4 ambapo tayari kuna Wahadhiri 68 ambao wanafadhiliwa na ufadhili wa Serikali kwa ajili ya Shahada za Uzamivu na kati yao 14 wanatoka Chuo Kikuu Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na juhudi za Serikali kutoa fedha zake kusomesha Wahadhiri lakini pia Serikali imeendelea kutafuta scholarship mbalimbali. Tuna scholarship 77 ambapo wameenda kusoma China, 30 wameenda kusoma Hungary, 26 wameenda kwa utaratibu wa Commonwealth pamoja na scholarship nyingine.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nimshukuru Mheshimiwa Rais, pamoja hizi scholarship 77 za China lakini kwa juhudi yake aliongea na Serikali ya China akaomba tuongezewe kwenye fani ya udaktari ambako tuna upungufu mkubwa. Serikali ya China ikaongeza scholarship nyingine zaidi kufuatia ombi la Rais. Kwa hiyo, nilihakikishie Bunge lako kwamba Serikali inafanyia kazi uhaba wa watumishi wa vyuo vikuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo limezungumziwa ni umuhimu wa kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi na kuhakikisha kwamba tunakuwa na watu ambao wamebobea na ambao wanaweza hata kujiajiri. Naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inaona umuhimu wa kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi na tumekuwa tukiendelea kuwekeza katika vyuo vya ufundi stadi. Kwa mfano, sasa hivi tunaendelea na ujenzi wa VETA za Mikoa katika Mikoa ya Rukwa na Geita lakini taratibu za kumpata mkandarasi Simiyu zinakamilika na kwa watani wangu Kagera nilikuwa huko juzi kuangalia maandalizi ya kiwanja ambacho kimeshakamilika na mkandarasi anaweza akaanza kazi wakati wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeendelea pia kuimarisha VETA za Wilaya na hata hivi karibuni mwezi Januari Serikali imetoa kiasi cha fedha shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kuimarisha majengo ambayo Halmashauri imeipatia Serikali ili yaendelezwe kama vituo vya ufundi stadi. Tumepeleka fedha Ileje, Palamawe kule Nkasi, Kamachumu, Urambo, Cherekeni pamoja na Kitangali kwa ndugu yangu Mheshimiwa Mkuchika. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba tunaendelea kuimarisha vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi. Sasa hivi pia tunaendelea na ukarabati wa vyuo 20 vya maendeleo ya jamii. Yote hii lengo lake ni kuongeza ujuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo napenda kulitolea ufafanuzi ni mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. Waheshimiwa Wabunge wengi wamelizungumzia lakini pia hata katika taarifa ya Kamati wamezungumzia suala la vigezo vya mikopo na mambo mengine na kama nilivyosema ushauri wa Kamati tumeupokea. Hata hivyo, napenda kutoa ufafanuzi wa mambo machache, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, vigezo vya mikopo vimekuwa vikiboreshwa kila mwaka ili kuangalia changamoto zilizojitokeza na kutoa fursa kwa mwaka ujao. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge, kama wana maeneo mahsusi ambayo wangefikiri ni muhimu Serikali iyazingatie katika utoaji wa mikopo, iko tayari kuyapokea na kufanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni la wanafunzi wanaohama kutoka chuo kimoja kwenda kingine. Utaratibu ni kwamba mwanafunzi anapohama anahama na masomo aliyokuwa anasoma na mkopo wake kama alivyokuwa anapata. Kama nilivyotoa taarifa wakati Mheshimiwa Ester Mmasi alivyokuwa anazungumza, iwapo kuna wanafunzi wanakwenda na kusoma kitu ambacho ni tofauti hilo ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna wanafunzi 208 kati ya 1,699 ambao walihama na mpaka leo bado hawajapata mkopo. Hii inatokana na changamoto za taarifa zao kwa sababu kuna baadhi ya wanafunzi ambao unakuta taarifa zile za kozi aliyokuwa anasoma awali inatofautiana na kozi aliyokuwa anakwenda, ikitokea hivyo kwetu inakuwa ni tatizo mpaka hizo taarifa tuzihakiki lakini pia kuna ambao wana tatizo la masuala ya mitihani.
Mheshimiwa Spika, niseme kwamba huu ni uzembe wa baadhi ya vyuo na hatuwezi kuendelea kuwaumiza wanafunzi kwa masuala ambayo wao siyo wanaopeleka taarifa. Tayari Bodi ya Mikopo ilishaviandikia vyuo barua tangu tarehe 17 Januari wahakikishe huu utata wa taarifa unaondolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimesimama hapa nasema hivi, ikifika tarehe 15 Februari, kusiwepo na mwanafunzi hata mmoja ambaye amehamishwa na bado hajapata mkopo wake kwa sababu kumekuwa na mvutano. Napendekeza Tume ya Vyuo Vikuu ingeangalia katika sheria yake namna ya kuviadhibu vyuo ambavyo vinashindwa kutoa taarifa za wanafunzi kwa wakati na matokeo yake wanafunzi wanaumia wakati hawana tatizo lolote. Hilo nadhani ni eneo ambalo tungeangalia kuvibana zaidi vyuo katika sheria zetu ili viache huo mfumo ambao wakati mwingine kutokana na taarifa hizo wanafunzi wanakuwa wanacheleweshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna suala limezungumzwa la usajili wa shule kwamba kutokana kazi nzuri ya Mheshimiwa Rais wetu ya kutoa elimu bila malipo mwitikio wa wananchi umekuwa ni mkubwa, sasa ifike mahali Serikali iruhusu wanafunzi wakasome maturubai au madarasa ya nyasi. Mimi sioni kama tumefika hapo, kwanza Serikali inafanya kazi kubwa sana ya kukabiliana na ongezeko la wanafunzi ambao wanajiandikisha shuleni kutokana na elimu bila malipo na Serikali imekuwa ikijenga miundombinu lakini pia Halmashauri zetu tumeona kazi kubwa inafanyika. Niseme hapa elimu ni haki ya kila mtoto lakini pia ni jukumu la Serikali kuhakikisha ulinzi na usalama wa watoto.
Mheshimiwa Spika, leo hii tulivyokuwa tunatoka mvua ilikuwa inanyesha, Waheshimiwa Wabunge wote hakuna aliyekuwa anakwenda, walikuwa wamekaa wanasubiri kwanza mvua iondoke. Hatuwezi tukaruhusu miundombinu ambayo ni hatarishi kwa maisha ya watoto wetu. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba kabla ya kuruhusu shule isajiliwe, itakaguliwa kuhakikisha kwamba miundombinu yote ambayo shule imeiandaa iko salama kwa ajili ya watoto wetu, waweze kupata elimu lakini tuna jukumu pia la kulinda usalama wa watoto wanapokuwa shuleni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo limezungumziwa ni kuhusu kuboresha mfumo wa elimu yetu lakini pia lugha ya kufundishia. Nashukuru hili suala kila linapojitokeza kunakuwa na mjadala ambao upande mmoja unaona tutumie Lugha ya Kiswahili lakini pia kuna hoja ya kwamba lugha peke yake siyo jawabu, suala ni kuangalia changamoto kwa nini wanafunzi hawafanyi vizuri. Nafurahi kwamba katika mjadala tumeonesha kwamba hesabu kwenye shule za msingi wanafundishwa kwa Kiswahili lakini hawafanyi vizuri. Kwa hiyo, ushauri nimeupokea, jambo la msingi ni kuangalia zile changamoto zinazosababisha wanafunzi wasifanye vizuri na Serikali izifanyie kazi.
Mheshimiwa Spika, la mwisho kwa ridhaa yako nizungumzie suala la uhaba wa walimu. Ni kweli kuna baadhi ya maeneo kuna uhaba wa walimu, kwa hiyo, tutaendelea kuomba Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuangalia pale ambapo kuna walimu ambao wamezidi kuwe na mgawanyo sawia. Mheshimiwa Kapteni Mkuchika ameshazungumzia suala la kuajiri kuziba zile nafasi za wastaafu ili zile shule ambazo kweli hazina walimu kabisa tuweze kuzipatia walimu kwa haraka. Pia Serikali itaendelea kuwasimamia walimu wafanye kazi yao vizuri na kuwapatia mafunzo kazini ili wawe na weledi wa kutosha na hivyo basi tuongeze ubora wa ufaulu.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na kwa mara nyingine naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza kabisa sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kuhitimisha hoja ambayo niliiwasilisha mbele ya Bunge lako mnamo tarehe 29 Aprili, 2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa naomba nikushukuru wewe kwa kuuongoza vyema mjadala wa hoja yangu, lakini pia niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wametoa michango mizuri katika bajeti ambayo nimewasilisha leo kuhusu Fungu Namba 46 pamoja na Fungu Namba 18.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe shukurani za kipekee kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa ushirikiano mkubwa ambao wameendelea kuutoa katika Wizara yangu na kwa kweli kwa mara nyingine nishukuru sana Uongozi wa Bunge kwa kuisuka vyema Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ambayo hakika imesheheni Wajumbe ambao wanaifahamu vyema sekta ya elimu. Kwa hiyo wamekuwa na michango mizuri ambayo hakika inachangia sana katika kuboresha elimu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nishukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia hoja hii. Tumepokea michango mingi sana na michango mizuri ambayo yote ilikuwa na lengo moja na kuhakikisha tunaimarisha na kuboresha elimu katika nchi yetu na kuweka mazingira rafiki kwa vijana wa Kitanzania ili waweze kujifunza vizuri. Kwa hiyo, nianze kusema tu kwamba kwa moyo mkunjufu, Wizara imepokea michango yote ambayo imetolewa na Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya Waheshimiwa Wabunge 114 walichangia hoja yangu na kati yao, Waheshimiwa Wabunge 63 wamechangia kwa maandishi na Wabunge 51 wamechangia kwa kuongea. Naomba kwa sababu ya muda siwezi kuwataja lakini naomba orodha yao iingie kwenye Hansard waweze kutambulika.
Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwa maandishi ni pamoja na Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mheshimiwa Omari M. Kigua, Mheshimiwa Amina N. Makilagi, Mheshimiwa Husna S. K. Mwilima, Mheshimiwa Richard M. Ndassa, Mheshimiwa George M. Lubeleje, Mheshimiwa Rhoda E. Kunchela, Mheshimiwa Joseph L. Haule, Mheshimiwa Joseph M. Mkundi, Mheshimiwa Aida Joseph Kheneni, Mheshimiwa Nuru A. Bafadhili, Mheshimiwa Mbaraka Kitwana, Mheshimiwa Shaabani O. Shekilindi, Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mheshimiwa Zuberi M. Kuchauka, Mheshimiwa Engineer Gerson H. Lwenge, Mheshimiwa Hamidu H. Bobali, Mheshimiwa Ally M. Kessy, Mheshimiwa Margaret Sitta, Mheshimiwa Ruth H. Mollel, Mheshimiwa Esther N. Matiko, Mheshimiwa Dkt Chrestine G. Ishengoma, Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa, Mheshimiwa Suzana C. Mgonukulima, Mheshimiwa Ignas A. Malocha, Mheshimiwa Flatei G. Massay, Mheshimiwa Engineer Edwin A. Ngonyani, Mheshimiwa Lucia U. M. Mlowe, Mheshimiwa Zainabu M. Amiri, Mheshimiwa Lucy S. Magereli, Mheshimiwa Ritta E. Kabati, Mheshimiwa William V. Lukuvi, Mheshimiwa Mgeni J. Kadika, Mheshimiwa Abdallah D. Chikota, Mheshimiwa Kiza
H. Mayeye, Mheshimiwa Mary D. Muro, Mheshimiwa Anatropia L. Theonest, Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Kikwembe, Mheshimiwa Sonia J. Magogo, Mheshimiwa Zainab M. Bakar, Mheshimiwa Silafu J. Maufi, Mheshimiwa Mussa B. Mbarouk, Mheshimiwa Cosato D. Chumi, Mheshimiwa Timotheo P. Mnzava, Mheshimiwa Joyce B. Sokombi, Mheshimiwa Lolesia J. Bukwimba, Mheshimiwa Shally J. Raymond, Mheshimiwa Marwa R. Chacha, Mheshimiwa Juma O. Hija, Mheshimiwa Omari A. Kigoda, Mheshimiwa Mashimba M. Ndaki, Mheshimiwa Qambalo W. Qulwi, Mheshimiwa Mahmoud H. Mgimwa, Mheshimiwa Elibariki I. Kingu, Mheshimiwa Jitu V. Soni, Mheshimiwa Devotha M. Minja, Mheshimiwa Rev. Dkt. Getrude P. Rwakatare, Mheshimiwa Maria N. Kangoye, Mheshimiwa Salma R. Kikwete, Mheshimiwa Catherine N. Ruge, Mheshimiwa Zainabu N. Mwamwindi, Mheshimiwa Khadija N. Ali, Mheshimiwa Dkt. Dalaly P. Kafumu na Mheshimiwa Richard P. Mbogo.
Aidha, Waheshimiwa Wabunge waliochangangia hotuba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya mwaka wa fedha 2019/2020 kwa kuzungumza ni pamoja na Mheshimiwa Yosepher F. Komba, Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mheshimiwa Mendrad L. Kigola, Mheshimiwa Joram I. Hongoli, Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mheshimiwa Joseph Leonard Haule, Mheshimiwa Pascal Y. Haonga, Mheshimiwa Hasna Mwilima, Mheshimiwa Phillipo A. Mulugo, Mheshimiwa Joseph M. Mkundi, Mheshimiwa Sikudhani Y. Chikambo, Mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola, Mheshimiwa Abdallah D. Chikota, Mheshimiwa Amina N. Makilagi, Mheshimiwa Edward F. Mwalongo, Mheshimiwa Shaaban O. Shekilindi, Mheshimiwa Daimu I. Mpakate, Mheshimiwa Esther N. Matiko, Mheshimiwa Engineer Edwin A. Ngonyani, Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mheshimiwa Angelina A. Malembeka, Mheshimiwa Vedasto E. Ngombale, Mheshimiwa Salma R. Kikwete, Mheshimiwa Jumanne K. Kishimba, Mheshimiwa Sixtus R Mapunda, Mheshimiwa Zainab
M. Bakar, Mheshimiwa Dkt. Immaculate S. Semesi, Mheshimiwa Profesa Jumanne A. Maghembe, Mheshimiwa Dkt. Jasmine T. Bunga, Mheshimiwa Rashid M. Chuachua, Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus B. Kamala, Mheshimiwa Joseph K. Mhagama, Mheshimiwa Tauhida C. G. Nyimbo, Mheshimiwa James F. Mbatia, Mheshimiwa Hamidu H. Bobali, Mheshimiwa Susan A. J. Lyimo, Mheshimiwa Marwa R. Chacha, Mheshimiwa Maria N. Kangoye, Mheshimiwa Fatma H. Toufiq, Mheshimiwa Kemilembe J. Lwota, Mheshimiwa Dkt. Charles J. Tizeba, Mheshimiwa Masoud A. Salim, Mheshimiwa Khadija N. Ali, Mheshimiwa Sebastian S. Kapufi, Mheshimiwa Goodluck A. Mlinga na Mheshimiwa Mwita M. Waitara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri ambao wamechangia hoja yangu. Kwa namna ya kipekee nimshukuru sana Kaka yangu Waziri wa Fedha amejibu vizuri na kitaalam hoja zinazohusu masuala ya fedha lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, TAMISEMI na yeye kwa ufafanuzi wa hoja ambao ameutoa. Kwa ujumla kwa kweli Wabunge wote kwa umoja wenu michango yenu imekuwa ni mizuri na kipekee kabisa nimshukuru Waziri Kivuli Mheshimiwa Susana Lyimo hakika safari hii umekuja kivingine na hotuba yako imesheheni ushauri. Kwa hiyo tunashukuru sana na kwa mara ya kwanza, Mheshimiwa Susan Lyimo ameipongeza Taasisi ya Elimu Tanzania, nashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli niwaahidi Waheshimiwa Wabunge kwamba sitaweza kwa muda niliopewa kujibu hoja zao zote lakini hoja zote zitajibiwa kwa maandishi na tutahakikisha kwamba kabla ya kumaliza Bunge hili basi tutaweza kukabidhi majibu yetu kwa Waheshimiwa Wabunge wote. Kwa hiyo, naomba sasa nizungumzie tu hoja ambazo nitaweza kuzizungumza kutokana na muda nilionao na nitaanza na masuala ambayo yamezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuanza na suala la uchapaji wa vitabu; suala la uchapaji wa vitabu limejitokeza na hii ninaamini ni kwa sababu Waheshimiwa Wabunge wanatambua kwamba vitabu na Taasisi ya Elimu ndiyo moyo wa sekta ya elimu. Kwa hiyo Taasisi ya Elimu ispofanya vizuri ni dhahiri kwamba elimu yetu itakuwa haiko vizuri. Baadhi ya hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezizungumzia ni kutokuwepo kwa vitabu vya baadhi ya masomo na kutokuwepo kwa vitabu vya elimu ya msingi, vya darasa la Tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza kabisa nianze kuwashukuru Wabunge wote waliochangia kuhusiana na suala la vitabu kwa sababu suala la ufundishaji na ujifunzaji haliwezi kwenda vizuri kama hatuna vitabu ambavyo ni vizuri kwa hiyo maoni yao na msisitizo ambao wanauweka unaendana pia na namna ambavyo Serikali imekuwa ikiisimamia Taasisi hii ya Elimu na ndiyo maana hata katika Bunge hili nadhani ni kwa mara ya kwanza ambapo tunazungumzia Bajeti ya Wizara ya Elimu na hakuna vitabu vibovu ambavyo vimeletwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka ilikuwa mwaka 2013 Mheshimiwa Mbatia aliingia na sanduku la vitabu ambavyo vimejaa makosa na ndiyo maana Serikali ikaamua, wakati huo hivyo vitabu vilikuwa vinachapwa na Kampuni binafsi Serikali ikaamua sasa hilo jukumu kurudisha Taasisi ya Elimu Tanzania. Lakini bahati mbaya Taasisi ya Elimu Tanzania na yenyewe ilipoanza wanasema Waswahili “mwanzo ni mgumu” haikufanya vizuri katika baadhi ya maeneo lakini, Serikali tulikuwa wakali kweli kweli na vile vitabu vyote vyenye makosa tuliviondoa shuleni na sasa hivi Taasisi ya Elimu imesimama vizuri na kazi yao imetukuka kwa hiyo tunakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu vitabu vya darasa la Tano vilishasambazwa shuleni nakala milioni 2,867,400 waliochelewa kupata walipata Mwezi Februari, na kwa sababu kuna tabia ya baadhi ya watu kufungia vitabu, tunapeleka shuleni lakini havifiki kwa walengwa, kwa hiyo, nilivyosikia tu Waheshimiwa Wabunge wanachangia nilifuatilia hata kwenye hizo halmashauri kuuliza kulikoni wakati tunajua vitabu vimepelekwa inakuaje Waheshimiwa Wabunge wanakuja kuuliza huku Bungeni? Kwa hiyo, nimejiridhisha na hata sehemu ambazo waliuliza maswali vitabu vilivyochelewa kufika vilikuwa ni Mwezi wa Pili kwa hiyo vitabu viko shuleni na wanafunzi wanavisoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ilihusu kutokuwepo kwa mtaala na mihtasari kwa shule zinazotumia lugha ya Kingereza; naomba niliarifu Bunge lako Tukufu, mitaala kwa lugha ya Kingereza ilishaandaliwa tangu Mwaka 2016 na inapatikana katika duka la vitabu la Taasisi ya Elimu Tanzania na Maduka ya Mawakala wa Taasisi ya Elimu Tanzania ambayo yanapatikana katika Mikoa yote nchi nzima.
Mheshimiwa Mweyekiti, aidha, Wizara kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania imekamilisha kazi ya kuandaa vitabu vya kiada kwa shule zinazotumia lugha ya Kingereza kama lugha ya kufundishia kwa Darasa la Kwanza, la Pili na la Tatu na vitabu hivyo nilisema katika hotuba yangu, kwamba tumeanzisha Maktaba ya Mtandao. Kwa hiyo, vitabu hivi ambavyo nimekuja na sampuli kuwaonyesha Waheshimiwa Wabunge vinapatikana katika Maktaba mtandao kwa hiyo vitabu vya lugha ya Kingereza vipo hivi hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge watembelee tovuti yetu kama inavyoonekana pale ambayo ni www.tie.go.tz ili waweze kujipatia kwa urahisi vitabu ambavyo tayari Serikali imekwisha viandaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo ilizungumzwa na Mheshimiwa Ndugu yangu na rafiki yangu kabisa Mheshimiwa Phillipo Mulugo kuhusiana na suala la vitabu ambavyo vilikuwa na dosari. Baada ya marekebisho ambayo Serikali imefanya, amesema kwamba kuna baadhi ya wadau wetu ambao walikuwa wamevinunua na hivyo wamepata hasara kubwa sana kwa sababu vitabu vilivyokuwa Serikalini vimeondolewa lakini wale wadau wengine ambao walikuwa wamenunua nje ya mfumo wa Serikali wao wamepata hasara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa ambazo tunazo, Serikali haikuwa imeuza kitabu chochote kwa mtu yoyote kwa sababu makosa yalibainika mara tu baada ya kusambaza hivyo vitabu. Kwa hiyo, naomba niseme mbele ya Bunge lako tukufu, kama kuna mtu wa yoyote ambaye alikuwa amenunua vitabu ambavyo vina makosa ninaomba awasilishe vilelezo (receipt) yake na vitabu ambavyo vina makosa na Serikali itambadilishia kwa sababu tayari Serikali imetoa tamko la kuviondoa vitabu hivyo shuleni na havitakiwi kutumika mahali popote na havitakiwi kuwa kwenye circulation kwa sababu watoto wadogo wanaweza wakakutana nacho wakakitumia. Kwa hiyo, ni msimamo wa Serikali vile vitabu ni marufuku kutumika mahali popote. Kwa hiyo, kama kuna mtu ana kitabu na alikuwa amekinunua akirudishe na atapewa kitabu kingine ambacho ni kizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine limezungumzwa na Ndugu yangu Mheshimiwa Esther Mahawe ambaye ni Rais wa TAPIE (Wamiliki wa Shule Binafsi) na alikuwa anazungumzia suala la gharama za mafunzo kwa ajili ya walimu wa shule binafsi. Nimesikia hapa lugha zinazungumzwa kwamba utoaji wa elimu bure kwamba kunakuwa na ubaguzi kwenye shule za Serikali wanafanya mitihani bure au wanakuwa wanafanya mafunzo bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hakuna kitu cha bure, shule za Serikali zinalipiwa na Serikali ndiyo maana Waziri wa Fedha kila mwezi anatoa bilioni 23.8 kwa hiyo hakuna cha bure, inategemea tu kwamba gharama inalipwa na nani. Kwa hiyo, Serikali inalipia Walimu wanapokuwa wanakwenda mafunzo kazini, Serikali inawalipia wanafunzi wanapokuwa wanafanya mitihani. Na shule binafsi tungeziomba zichangie katika grarama za mafunzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala la gharama ya mafunzo ambayo iliwekwa, kwa taarifa nilizonazo ni kwamba walikaa kikao wakawa wameshauriana Wamiliki wa Shule Binafsi na Taasisi ya Elimu Tanzania na niwaombe kwa sababu kwa kweli tunafanyakazi vizuri na shule binafsi, kama hizo fedha ambazo mlikuwa mmekubaliana baadaye mmeziona kwamba ni kubwa, rudini tu mkakae kwenye mazungumzo. Nia yetu ni moja kuhakikisha kwamba tunaendeleza elimu yetu, sidhani kama tunaweza tukashindwa kuelewana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limezungumzwa sana na Waheshimiwa Wabunge wengi ni malalamiko kuhusiana na kubadilika kwa mtaala mara kwa mara. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba tangu tumepata uhuru mwaka 1961 mtaala umebadilika mara nne tu. Tangu tumepata uhuru mwaka 1961 mitaala ya elimu imebadilika mara nne tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya kwanza ni mara baada ya kupata uhuru, mara ya pili ni baada ya Azimio la Arusha mwaka 1967, mara ya tatu ulibadilika mwaka 1979 kuingiza masomo ya michepuo na mara ya nne ulibadilika mwaka 1997 baada ya mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa hiyo kulikuwa na context ambazo zilibadilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine tunakuwa tunafanya maboresho ya mtaala. Nitatoa mfano, kwa mfano, mwaka 2005 kumezaliwa Nchi ya Sudan Kusini ni lazima tufanye maboresho haya siyo mabadiliko. Ni maboresho katika mtaala kuonyesha kwamba nchi za Afrika idadi imeongezeka kwa sababu kuna nchi mpya imezaliwa, haya hauwezi ukasema ni mabadiliko. Kwa hiyo, kumekuwa na maboresho ambayo yanafanyika madogo madogo ya kawaida, maboresho yanayozingatia mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia, lakini mabadiliko makubwa yamefanyika mara nne tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na suala hilo, watu wamezungumzia sana mfumo wa elimu yetu na vilevile wamzungumzia sana hata suala la kwamba sasa hivi elimu yetu inakuwa inakwenda ndivyo sivyo na nilikuwa natafuta hapa quotation ya Mheshimiwa Susan Lyimo aliyoanzanayo. Katika kitabu chake alianza na quotation ya kuonyesha kwamba “ukitaka kuangamiza nchi yetu basi uchezee mfumo wa elimu na kwamba ukiwa na watu wenye vyeti feki, ukiwa na watu ambao wamekaa wanafanya kazi mahali ambapo sipo basi itakuwa ni silaha kubwa ya kuangamiza nchi yetu”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie kwamba Serikali ya Awamu ya Tano iko makini sana na inatambua kwamba bila mfumo imara wa elimu basi mambo hayawezi kwenda vizuri na ndiyo maana Serikali ilifanya uhakiki wa watu wenye vyeti feki. Jumla ya watumishi 15336 wameondolewa kwenye Utumishi lakini pia Serikali kwa kutambua kwamba ukimuweka mtu mahali ambapo hana sifa nazo hawezi kufanya vizuri. Zaidi ya watumishi 5300 ambao walikuwa wameajiriwa katika fani ambazo hawana ujuzi nazo wameondolewa. Wanataka Serikali ifanye nini zaidi ya hapo kuonyesha kwamba inatambua na kujali umuhimu wa elimu katika nchi yetu ya Tanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limezungumziwa, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango amejibu vizuri na kitaalam masuala ambayo yanahusiana na masuala ya fedha. Lakini naomba tu nifafanue moja. Kuna suala moja ambalo kwa kweli niseme hapa na Ndugu zetu Washirika wa maendeleo wako pamoja na mimi walikuja hapa jana na Kiti kiliwatambulisha na hata sasa wanafuatilia mjadala wetu. Haipendezi hata kidogo kwa mtu ambaye ni mstaarabu, mtu ambae ni muungwana, mtu ambae anashirikiana na wewe katika maendeleo tunatumia maneno ya ajabu ajabu kuwasema Washirika wetu wa maendeleo, siyo jambo jema hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwanza hii dhana ya kusema kwamba Serikali imekuwa tegemezi sana siyo sawa. Ukiangalia bajeti ya Wizara kwa miaka mitatu iliyopita; Mwaka 2017/2018, mchango wa Serikali ulikuwa ni asilimia 66.2 na mchango wa Wafadhili ulikuwa ni asilimia 33.8 lakini katika Mwaka huu wa fedha wa Bajeti hii ambayo Waheshimiwa Wabunge, ninawaomba kwa unyenyekevu kabisa muidhinishe mchango wa Serikali ni asilimia 67.6 na mchango wa Wafadhili ni asilimia 32.4, kwa hiyo, Serikali imeendelea kuwa inapunguza utegemezi. Lakini Waheshimiwa Wabunge naomba niwaulize swali; hivi kama Serikali ina mahusiano mazuri na wafadhili, ina marafiki kutokana na Utawala Bora, wako tayari kuja kutoa misaada katika nchi yetu, kuna kosa gani Ndugu zangu? Kwa sababu inakuwa kama vile ni dhambi. Kwa nini inakuwa kama vile ni dhambi Serikali ikipata misaada kutoka nje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nafikiri mngeipongeza Serikali, haiwezekani mtu aje akuletee fedha zake kama wewe huna usimamizi mzuri, kama wewe huna Utawala Bora, kama wewe husimamii vizuri zile fedha ambazo zinaletwa. Kwa hiyo, Ndugu zangu sioni kama kuna sababu yoyote ya kuhangaika na nitoe tu taarifa kwamba hata sasa hivi tunapoongea Serikali ya Uswisi imetoa msaada wa jumla ya shilingi bilioni 14,900,000,000 kwa ajili ya kuendeleza ujuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hizi hata kwenye kitabu chako hazionekani kwa sababu ni makubaliano ambayo tumeingia hivi karibuni na tarehe 31 Mei tutazindua rasmi huu mpango. Lakini nitoe taarifa zaidi kwamba kupitia Global Partnership in Education, mfuko huu umetoa Dola milioni 90 kwa Tanzania mwanzoni mwa Mwezi huu wa Nne ambao ni sawa na bilioni 200 za Kitanzania na huo ni msaada kutokana na Utawala Bora katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kuhusiana na fedha maana mengi Mheshimiwa Waziri ameyajibu; kumekuwa pia na dhana kwamba bajeti ya Wizara imepungua, mwaka uliopita ilikuwa trilioni 1,407,000,000,000 na Mwaka huu ni trilioni 1,388,000,000,000. Waheshimiwa Wabunge naomba niwahakikishie Serikali hii ya Awamu ya Tano iko makini sana na Bajeti ya Wizara ya Elimu ndiyo maana mmeona kuna mambo mengi mazuri yamefanyika. Naomba niwaambie kwamba fedha za elimu hazijapungua isipokuwa tumekuwa na mabadiliko kidogo katika program yetu ya lipa kulingana na matokeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiasi cha shilingi bilioni 90,088,000,340 za Lipa Kulingana na Matokeo tumezipeleka katika Fungu Namba 56-Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwa hiyo, kama zingebaki katika Fungu Namba 46 kama ambavyo ilikuwa katika bajeti ya 2018/2019, bajeti yetu ingesomeka trilioni 1,478,000,000,000. Kwa hiyo, endeleeni kumuamini Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli yuko makini sana katika maeneo ambayo ni muhimu katika Taifa hili, na kamwe hawezi kuchezea mfumo wa elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie suala ambalo limekuwa likijitokeza ambalo Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati yetu wamekuwa wakitushauri kama Serikali. Kwa kweli kama nilivyosema tunaheshimu sana na kuthamini michango ambayo inatolewa na Kamati yetu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii lakini nikiri tu kwamba wakati mwingine siyo kila ushauri unaweza ukafanyika au ukatekelezeka kwa mara moja na haina maana kwamba usipotekeleza umepuuza. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge tunaposema Serikali imepokea ushauri mtuelewe hivyo kwamba kuna mambo mengine ambayo tunapaswa kama Serikali kuyazingatia na kujiridhisha kabla ya kutekeleza moja kwa moja ushauri ambao umetolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ushauri ambao umetolewa kwamba tuvipange Vyuo vyetu Vikuu katika madaraja mbalimbali. Mifano imetolewa kwamba tuangalie nchi kama Marekani; ukiangalia Nchi ya Marekani, ukiangalia Nchi za Ulaya zenyewe zimeendelea sana katika mifumo yao ya elimu. Sisi katika Elimu ya Juu vyuo vyetu vingi bado ni vichanga na kwa maana hiyo Serikali ina wajibu wa kuvilea na kuhakikisha kwamba vinakuwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tukianza kuweka madaraja ukasema kwamba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Daraja la Kwanza, ukasema labda kwa mfano, Chuo Kikuu cha Mzumbe sijui Daraja la Tatu, tayari utakuwa unawapa picha Watanzania kwamba hapa siyo mahali pazuri pakwenda; na ukianza kuangalia kwamba Serikali ina vyuo, sasa Serikali yenyewe ikianza kupanga vyuo na ni ukweli usiofichika kwamba tukipanga vyuo vya Seriakli ndiyo vitakuwa katika madaraja mazuri. Sasa kesho mtarudi hapa na kusema kwamba Serikali inanyanyapaa vyuo binafsi. Tuache Watanzania wenyewe wataamua kwamba waende wapi na ndiyo maana Serikali imetoa uhuru, hatuwapangii wanafunzi mahali pakwenda kusoma. Kila mwanafunzi yuko huru kuchangua Chuo anachotaka kwenda kusoma mwenyewe. Lakini tumeshuhudia vipo vyuo ambavyo vinapata tabu sana kupata Wanafunzi. Kwa hiyo tayari madaraja yamejipanga miongoni mwa Watanzania wanafahamu wapi wakienda watapata elimu iliyo bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tumejaribu kuangalia uzoefu katika Nchi za wenzetu ambao wanapanga hayo madaraja. Kunakuwa na changamoto kwa sababu unapoweka madaraja kunakuwa na changamoto kama vile kuwepo kwa malengo na vigezo tofauti na vinavyotumika katika ushindani au kunakuwa na vyuo vinajikita zaidi katika yale maeneo ambayo yanajua kwamba ndiyo haya yanayotumika katika kuwapanga katika madaraja. Lakini pia katika Nchi za wenzetu, jukumu la kuvipanga vyuo katika ubora halifanywi na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika nchi za wenzetu jukumu la kuvipanga vyuo katika ubora halifanywi na Serikali. Kwa hiyo, pia nishauri kwamba Kamati ya Makamu Wakuu wa Vyuo na Wakuu wa Vyuo Vishiriki hapa nchini wanaweza wakalichukua hilo jambo wakaliangalia lisiwe jambo la Serikali. Kama wataona inafaa, sisi Serikali hatuna tatizo lolote, lakini upande wa Serikali tukianza kupanga Vyuo vya Serikali vipo daraja la juu, vyuo vingine vinaweza vikafa ikaonekana kama vile kuna namna ambayo Serikali inasema kwamba huku hakufai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu la Serikali, tutaendelea kuhakikisha kwamba tunakagua na kujiridhisha kwamba vyuo vyote nchini vinazo sifa stahiki ambazo zinaruhusiwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia ni suala la Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambacho Mheshimiwa Amina Makilagi alizungumzia, lakini na ndugu yangu Mheshimiwa Getere akampa taarifa ambayo alikuwa anachomekea, kweli ali shindilia, kwa hiyo, nimepokea maoni yenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na mwaka huu tunatimiza miaka 20 tangu ameondoka duniani, Serikali inamthamini sana na Serikali ina dhamira ya kumuenzi kwa kuanzisha Chuo cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo kama ambavyo hata imeonesha katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu sasa kwa sababu limeulizwa hapa Bungeni, ni bahati mbaya kwamba hiki chuo pamoja na kwamba kuna majengo ambayo yalitolewa, lakini yalitolewa kwa maneno, kama Serikali hatujapata hati za kukabidhi na Serikali imekuwa ikifanya kazi kubwa sana kufuatailia, lakini mpaka leo ninavyozungumza, hati miliki hazijapatikana. Kwa hiyo, nisingependa kulizungumza sana, lakini naomba wanaohusika nitoe wito wakamilishe taratibu haraka kwa sababu dhamira ya Serikali ya kuanzisha chuo hiki iko pale pale kama ambavyo imeainishwa katika ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa noamba nizungumzie uimarishaji wa mazingira ya wanafunzi wenye mahitaji maalum. Suala la wanafunzi wenye mahitaji maalum Serikali inalichukulia kwa uzito mkubwa sana. Kwa kutambua matatizo makubwa ambayo yapo katika shule hizi na Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamelizungumzia, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 11.2 katika bajeti hii kwa ajili ya kununua vifaa visaidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa kutambua changamoto za ufundishaji, Serikali katika mwaka wa fedha 2018/2019 imeanzisha kozi ya stashahada katika Chuo cha Ualimu Patandi kwa ajili ya walimu wanafunzi wenye mahitaji maalum. Pia Serikali imejenga Shule Maalum ya Sekondari katika Chuo cha Walimu Patandi ambayo inaweza kuchukua wanafunzi 640.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la kuhusiana na Wanafunzi Wenye Mahitaji Maalum ni kuhusu muda wa kufanya mtihani, kwamba ule muda wanaopewa hautoshelezi. Naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Baraza la Mitihani la Tanzania huwa linatoa muda wa nyongeza kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na huwa linatoa dakika 10 za ziada kwa mitihani ya sanaa za jamii na dakika 20 za ziada kwa kila saa kwa somo la hisabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ina maana kama ni mtihani wa masaa matatu, mwanafunzi mwenye mahitaji maalum atapewa masaa manne ya kuyafanya kwa sababu anaongezewa dakika 20 kwa kila saa ya mtihani na kwa masomo ya Arts anaongezewa dakika 10 kwa kila saa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba Serikali inawathamini sana watoto wenye mahitaji maalum. Kama muda huu ambao tunaongeza dakika 20 kwa kila saa, utaonekana hautoshi, sisi tuko tayari kufanya review, lakini kwa sasa naomba tutambue kwamba Serikali inaongeza muda kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, lakini hata mwaka 2017 Baraza la Mitihani lilifanya mapitio ya muundo wa mitihani kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kuzingatia namna ya maswali ambayo yanaweza yakaulizwa kulingana na mahitaji maalum waliyonayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Sera ya Elimu na Mafunzo ambalo pia limezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wengi; na hususan ni suala la muda wa elimu kwamba je, elimu yetu ni miaka sita au saba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba nilishawahi kujibu katika Bunge lako Tukufu, naomba nirudie kusema tena. Muda wa Elimu ya Msingi ni miaka saba, haujabadilika. Kwa sasa hivi Serikali haina mpango wowote wa kubadilisha muda huo kwa sababu Serikali imejikita zaidi katika kutatua changamoto ambazo Waheshimiwa Wabunge mmezizungumzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba mitaala yetu inaishia Darasa la Sita, siyo kweli. Mtaala wa Elimu ya Msingi ambao taasisi ya elimu imeutoa uko mpaka Darasa la Saba. Kwa hiyo, niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba watoto mwaka ule wa saba wataenda kucheza. Hakuna muda wa mchezo, hii ni Serikali ya kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu; na kazi ya mwanafunzi ni kusoma. Kwa hiyo, hata wanafunzi nao watasoma darasa la saba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA). Nikiri kwamba katika vyuo hivi kumekuwa na ahadi za muda mrefu na hata imekuwa kero kwa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kila siku wanakuja kuuliza maswali Bungeni kuhusiana na vyuo vyao. Wanahoji kwamba sasa je, Serikali ina dhamira kweli ya kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba dhamira ya Serikali iko pale pale na sasa hivi dhamira iko kubwa zaidi kwa sababu tunajenga uchumi wa viwanda. Tunapojenga uchumi wa viwanda tunahitaji mafundi stadi na mafundi mchundo wengi zaidi. Kwa hiyo, dhamira ya Serikali ya kutekeleza sera ya kujenga VETA katika mikoa na Wilaya iko pale pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimesema, kupitia fedha ambazo nasikitika sana kwamba wengine wanatumia maneno mabaya ya kuzungumzia kwa Washirika wetu wa Maendeleo, Serikali imeamua na inakwenda kufanya. Kwanza sasa hivi tunaendelea na ujenzi wa VETA Mkoa wa Rukwa na Geita, tunakamilisha maandalizi ya ujenzi wa VETA kwa Mikoa ya Njombe, Simiyu na Kagera. Pia Serikali imekamilisha VETA ya Wilaya ya Namtumbo; na sasa hivi tuko katika hatua za ukamilishaji na usimikaji wa vifaa katika Wilaya ya Ileje, Nkasi, Urambo, Newala, Muleba na Simanjiro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali inaendelea kukamilisha matayarisho ya VETA Wilaya ya Itilima, Kasulu Halmashauri ya Wilaya, Babati na Ngorongoro. Pia Serikali inakamilisha kupata wataalam elekezi kwa ajili ya kujenga VETA katika Wilaya ya Ruwangwa, Kongwa, Halmashauri ya Mji wa Kasulu na Nyasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumaeamua katika bajeti yetu ya mwaka 2019/2020 Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 40 na tunakwenda kujenga VETA katika Wilaya zifuatazo: Chunya, Kilindi, Korogwe, Ukerewe, Chemba, Igunga, Pangani, Kishapu, Rufiji, Uyui, Kwimba, Bahi, Mafia, Longido, Mkinga, Uvinza, Ikungi, Iringa Vijijini, Lushoto, Mbarali, Monduli, Buhigwe, Ulanga, Masasi na Butiama.
Waheshimiwa Wabunge, mnataka nini tena ndugu zangu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu kwa kweli kwa sababu ya muda kama nilivyosema, nisingependa unifukuze kwa kengele, lakini niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote kwamba sisi tumepokea maoni yenu lakini labda sambamba na hili la Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi kumekuwa na maombi ya Waheshimiwa Wabunge kubadilisha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi kuzifanya ziwe VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge kwamba Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vimeanzishwa kwa malengo mahususi, kwa hiyo, Serikali isingependa kuvibadilisha. Tutashirikiana na Wajumbe katika maeneo husika, kama kutakuwa na fedha, kwa sababu hata hizi Wilaya ni kwa kuanzia, lakini zoezi la kuendelea kujenga VETA katika Wilaya litakuwa endelevu. Kwa hiyo, tutaweza kuwasiliana na katika maeneo ambayo tutakuwa tumeyafanyia tathimini kwa kuangalia taratibu ambazo tunazitumia, basi hakuna dhambi yoyote ukiwa na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi na ukawa pia na vhuo cha VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutakarabati Vyuo vyote vya Maendeleo ya Wananchi na pia tutaboresha mafunzo yake lakini suala la VETA na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi ningeomba sana Waheshimiwa Wabunge tuache kama vitu viwili tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie tena kwa kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa kweli kwa michango mizuri ambayo wameitoa. Niwahakikishie kwamba Serikali hii katika mambo ya elimu, kama kuna vitu ambavyo Mheshimiwa Rais ameviweka katika kipaumbele, ni elimu. Mumsikilize, mahali popote anapoongea, hawezi akamaliza kuzungumza bila kuzungumzia masuala ya elimu. Hazungumzi maneno tu, lakini hata fedha tunapata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika mwaka kwa fedha ulioisha 2017/2018, mpaka kufika Juni, 2018 tulipata bajeti ya maendeleo kwa asilimia 86 na tulipata bajeti ya matumizi mengineyo kwa asilimia 107, yaani tulipata zaidi ya kile kiasi ambacho kimetengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama alivyosema Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, ninayo imani kubwa sana na Serikali kwamba katika kipindi hiki cha miezi miwili iliyobaki, Wizara ya Fedha itaendelea kutoa fedha kwa miradi ambayo ilitengewa fedha lakini mpaka sasa haijapata ili kuhakikisha kwamba tunaweza kufikia malengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimalizie pia kwa kuishukuru familia yangu kwa kuendelea kuniunga mkono; nimshukuru mwanangu Dajosi ambaye yuko hapa pamoja na mdogo wangu Benjamini Ndalichako. Nawashukuru sana Washirika wetu wa Maendeleo ambao wamekuwa nasi katika Bunge hili tangu jana tulipowasilisha hoja hii. Naomba tu waelewe kwamba kuna lugha za Kibunge. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge wote wanathamini michango yao na ninaomba waendelee kushirikiana na Serikali kuiunga mkono nchi yetu katika sekta ya elimu ili iweze kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe shukurani za dhati sana kwa Watanzania wote wenye mapenzi na mema na Sekta ya Elimu ambao wamekuwa wakinipa maoni na ushauri mbalimbali ambayo yamekuwa chachu ya kuboresha elimu yetu. Niwahakikishie kwamba nitaendelea kuwa napokea maoni yenu na mnivumile wakati mwingine unakuta una message zaidi ya 350, siyo rahisi kuyapokea kwa wakati mmoja, lakini huwa najitahidi kusoma na kufanyia kazi kile ambacho mnanishauri kwa maslahi ya nchi yetu. Kwa hiyo, naomba msichoke kutoa ushauri na Wizara yangu itaendelea kulipokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia sana suala la mfumo wa elimu na kuwa na mjadala. Kama ambavyo wenzetu wa madini wamefanya kwa kukutana na wadau wao, naomba nimwagize Katibu Mkuu wangu aangalie uwezekano wa kuwa na mkutano mkubwa wa wadau wa Sekta ya Elimu ili tuweze kupata mawazo yao. Hakuna tatizo lolote. Serikali ipo tayari kusikiliza na iko tayari kufanyia kazi mawazo ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawashukuru sana ndugu zangu wa Mkoa wa Kigoma, ndugu zangu wa Wilaya ya Kasulu ambao wamekuwa wakinitia moyo katika jukumu langu la Kitaifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wote waunge mkono bajeti hii ili tuweze kwenda mbele, tuweze kuchapa kazi, tuweze kuendeleza elimu katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, naamini kwamba Waheshimiwa Wabunge wote wataunga mkono bajeti hii kwa sababu elimu haina itikadi, watoto wote wa Kitanzania wanastahili kupata elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuhitimisha hoja yangu.
Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama tena hapa mbele ya Bunge lako Tukufu kuhitimisha hoja hii ambayo tuliiwasilisha jana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumshukuru Mheshimiwa Spika, Job Yustino Ndugai, kwa kuongoza mjadala wa hoja yangu jana, lakini pia nakushukuru sana wewe ambaye umekaa katika Kiti hiki tangu asubuhi na mpaka sasa ninapohitimisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote, nawashukuru sana kwa michango mizuri sana ambayo mmeitoa, hakika mmekuwa na michango mizuri ambayo inaonesha dhamira yenu ya kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto zilizopo katika sekta ya elimu na kuhakikisha kwamba elimu ambayo inatolewa katika nchi yetu inakidhi mahitaji katika Taifa letu na kimataifa. Ahsante sana Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishukuru Kamati ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii. Ukiangalia taarifa ya Kamati imesheheni uchambuzi wa kitaalam, imesheheni maoni na mapendekezo ambayo wote kwa pamoja, niwaambie tu Wajumbe wa Kamati, Serikali tumepokea mapendekezo yenu na tutakwenda kufanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda sitaweza kujibu hoja moja baada ya nyingine, lakini niwahakikishie kwamba maoni yote ya Kamati tumeyachukua kwa uzito kama ambavyo nao wameyafanyia kazi kwa uzito mkubwa. Kwa hiyo, tunawashukuru sana Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na si vibaya nikisema tu kwamba Kamati ile ukienda pale lazima uwe umejipanga, wanachambua kwelikweli. Kwa hiyo, Kamati ya Huduma za Jamii iko vizuri, tunawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya Waheshimiwa Wabunge 63 wamechangia hoja yangu ambapo Wabunge 58 wamechangia kwa kuzungumza na Wabunge watano wamechangia kwa maandishi. Michango yote ililenga kuhakikisha kuwa elimu yetu inaendelea kuboreshwa kwa kiwango stahiki na kuhakikisha kwamba tunatoa wahitimu ambao wameiva vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote sitaweza kuzijibu hoja zote, wengine walikuwa na dakika na tano na wengine saba lakini anachangia mambo mengi. Kwa kweli naona walikuwa wamejipanga vizuri kwenye Wizara yangu ya Elimu naendelea kuwashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa pongezi ambazo wamezitoa katika Wizara yetu ya Elimu. Hakika tumefarijika sana kuona kwamba mnatambua kazi ambayo tunafanya kama Wizara ya Elimu. Kwa hiyo, niwahakikishie kwamba pongezi ambazo mmezitoa kwa Wizara zitakuwa chachu kwetu ya kwenda kufanya Zaidi. Pongezi ambazo mmezitoa zitakuwa chachu kwetu ya kwenda kufanyia kazi maoni na mapendekezo ambayo mmetupatia. Kwa hiyo, tunawashukuru sana na tunaahidi kwamba tutajituma zaidi ili kuhakikisha kwamba tunatekeleza majukumu yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa unyenyekevu mkubwa, naomba pia niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa pongezi ambazo wamezitoa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Hakika tunashukuru sana kwa namna ambavyo mmepokea uamuzi wake wa kuondoa tozo ya asilimia 6 katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuwahakikishie kwamba Mheshimiwa Rais ameonyesha njia, yupo tayari kusikiliza na kufanya maamuzi. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge tumuunge mkono ili adhma yake ya kuweza kuwatumikia Watanzania na kutuletea yaliyo mema zaidi iweze kutekelezwa. Kwa hiyo, nimepokea kwa unyenyekevu mkubwa salamu na pongezi kutoka kwa Waheshimiwa kwa niaba ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo sasa, naomba niende kwenye hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezisema na nitakuwa sitaji majina kwa sababu muda hautoshi kuwataja wote isije ikaonekana kwamba nyingine nimeziacha, lakini nimejaribu kuchukua hoja ambazo zilichangiwa na watu wengi na ndiyo nimeona nianze kuzitolea ufafanuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, ni kuhusiana na mfumo wa elimu. Waheshimiwa Wabunge wengi ambao wamezungumza, wamezungumzia mfumo wa elimu na wamezungumzia haja ya mfumo wa elimu kujikita katika falsafa ya elimu ya kujitegemea. Waheshimiwa Wabunge wameonyesha kwamba wangependa elimu yetu iweze kumjengea mwanafunzi uwezo wa kujiamini, imjengee uwezo wa kujifunza zaidi kwa wengine lakini pia, iwajengee uwezo wa kufanya kazi za uzalishaji mali mara baada wanapohitimu masomo yao. Pia suala la mitaala limezungumzwa na Wabunge wameomba kuwe na Mjadala wa Taifa wa kujadili mitaala na kuangalia ni namna gani tunakwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na mfumo wa elimu yetu, Wizara imepokea maoni ambayo yametolewa na Waheshimiwa Wabunge na hatuoni tatizo lolote la kuwa na mjadala kuhusiana na suala la elimu. Kwa hiyo, tutafanya utaratibu, tutafanya mjadala na tutaomba Waheshimiwa Wabunge nao wawe ni sehemu ya kuchangia kwamba tunataka kwenda wapi. Mtaona changamoto ambayo inajitokeza kwa sababu hata katika michango huyu anasema tufanye hiki, huyu anasema tufanye kile, kwa hiyo, tutasikiliza na mwisho wa siku tutaona kile ambacho kweli kikitekelezwa kinakwenda kufanya vijana wetu watoke wakiwa wameiva vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali kukubaliana na hoja ya kufanya mjadala kwa sababu ukiangalia ile Sera ya Elimu ni ya tangu mwaka 2014, muda haujapita mrefu sana lakini tangu imeanza kulikuwa na changamoto za hapa na pale. Ndiyo maana kuna baadhi ya matamko ambayo yapo kwenye sera lakini hayajaanza kutekelezwa. Kwa hiyo, Serikali imekubaliana tutafanya mapitio.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia na mimi niungane na baadhi ya wachangiaji waliosema pamoja na kufanya mapitio isionekane kwamba sasa elimu ya Tanzania si mali kitu, si kweli ndugu zangu, elimu yetu ni nzuri, ina changamoto za hapa na pale na hayo ndiyo tunaenda kuyarekebisha. Tusije tukajenga dhana kwamba yaani elimu ya Tanzania haifai na inafika mahali labda mtu anaona kwamba hakuna sababu ya kumpeleka mtoto shule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi huwa nasikiliza michango humu, bahati nzuri wanaosema kwamba hakuna haja ya kuendelea na masomo zaidi ya darasa saba, wengine hata nimewasaidia kuwatafutia watoto wao vyuo vikuu. Kwa hiyo, najua ni maneno tu ambayo wanayasema kwa sababu nawafahamu wengine ni darasa la saba na wanafanya vizuri lakini wanawasomesha watoto wao tena kwa wivu wote na wanasomesha katika shule nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, isije ikatafsiriwa kwamba wanachokisema ndicho wanachokiamini. Naomba mimi nisimame kuwaambia Watanzania elimu ni ufunguo wa maisha, ni mwanga na ni tochi inakuonyesha uende wapi. Tusifike mahali kama taifa tukaanza kubeza kwamba elimu haina maana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niwapongeze sana wale ambao pengine hawakwenda shule kwa sababu moja au nyingine lakini wakafanikiwa lakini tujiulize wapo wangapi? Tunapochukulia kama hicho ni kigezo tujiulize wapo wangapi? Kwa hiyo, kweli kuna watu ambao wamefanikiwa sana lakini pia si wengi kama ambavyo tunataka kuwaaminisha Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi kama Waziri nimepewa dhamana ya elimu naomba watoto wote waende shule, elimu ni haki ya kila mtoto wa Kitanzania. Tuhakikishe watoto wanasoma shule na Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya watoto kusoma shule lakini yule ambaye anakipaji, ndiyo maana tunayo pia section ya ubunifu ambapo tunawaendeleza vijana wetu ili yule ambaye Mwenyezi Mungu amemjalia kipaji na kipawa kama kuna njia nyingine ambayo anaweza akafanikiwa kwa haraka zaidi mifumo yote hiyo katika elimu yetu ipo; tuna elimu rasmi na elimu nje ya mfumo rasmi. Kwa hiyo, niliona ni muhimu hilo suala nilizungumzie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili la kupitia mfumo wa elimu litaenda sambamba na kupitia Sera yetu ya Elimu, mitaala na Sheria ya Elimu. Ombi langu, naomba Wizara tupewe nasafi ya kufanya kazi, mambo mazuri hayataki haraka. Suala la kupitia Mfumo wa Elimu inabidi ufanye utafiti, tuangalie na washindani wetu, mazingira yetu na resource zetu, kwa hiyo, tusitegemee kwamba tukirudi mwakani tuna mfumo mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niwahahakishie Waheshimiwa Wabunge kazi hii inakwenda kuanza kabla hata ya Julai. Tumeshakaa na Katibu Mkuu, fedha kidogo ambazo zipo wazitumie ili huu mjadala uanze kabla hata ya Julai. Kwa hiyo, nachotaka kusema ni kwamba kazi ya kufanya mapitio tutaianza. Hata hivyo, naomba niwaandae kisaikolojia, tunataka tuifanye kisawasawa, kwa sababu kama tumebadilisha sera mwaka 2014 leo hii tunasema tubadilishe tena, tutakuwa ni nchi ambayo kila siku tunabadilisha mambo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi ya Marekani mwaka 1983 ilifanya mapitio makubwa ya sekta ya elimu kama ambayo sasa tunataka kuyafanya katika nchi yetu. Utafiti wenyewe ulichukua mwaka mmoja na nusu lakini sisi mtu anategemea mwakani tumekuja na mitaala mipya. Jambo hili tutalifanya lakini tutalifanya kwa weledi, kwa umakini na kuna mengine ambayo tutaanza kuyatekeleza wakati tunafanya mapitio makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa niwahahakikishe kwamba tuna dhamira ya dhati kwa sababu hata sisi tunaosimamia elimu hatupendi kila siku kusikia elimu yetu ikilalamikiwa, tunafanya vizuri lakini kuna mambo ambayo tunatakiwa kuyarekebisha. Tuko tayari kusikiliza maoni ya wadau, tupo tayari kuyafanyia kazi na naamini tutatoka vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wakati tunaendelea na huu mchakato ambao nimeuzungumzia kidogo mtupe muda tufanye kitu cha uhakika. Kuna mambo mengine ambayo tutaanza kuyafanya, kwa mfano, kuimarisha mafunzo ya ufundi, tayari tuna shule zetu za ufundi, kwa hiyo, niwahahakishie kwamba suala la kuimarisha mafunzo kwa vitendo hilo tayari tumelianza. Shule zetu zote za ufundi zile tisa nilizozitaja, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge aliyesema kwamba ni chache ni kweli, lakini nasema ukweli ndiyo zilizopo. Kwa hiyo, tutaanza na hizo tisa zilizopo, tayari tumezinunulia vifaa, tumezipelekea walimu wa kutosha na sasa hivi tuna fedha nyingine milioni mia moja katika kila shule ya kuendelea kuziimarisha. Kwa hiyo, hilo ni suala ambalo tumelianza na tutaendelea kulifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia katika vyuo vyetu vya VETA tutahakikisha tunaimarisha mafunzo kwa vitendo. Wanafunzi waende viwandani na kwenye makampuni kujifunza. Niwapongeze VETA wameanza ushirikiano huo, Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam nao wameanza, wana kitu ambacho wanaita dhana ya mafunzo viwandani. Kuna mabasi yao mnaweza kuyaona yameandikwa Teaching Factory, hayo ni mabasi ambayo yanakuwa yanawachukua wanafunzi kuwapeleka kwenye viwanda na tutaendelea kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tutaendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo imekasimiwa jukumu la kuendeleza ujuzi na tunashirikiana vizuri na dada yangu Chief Whip, Mheshimiwa Jenista Mhagama.
Kwa hiyo, niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge, kama mnavyofahamu akina mama tukisamama, tunasimama kweli kweli, kwa hiyo, suala la ujuzi dada yangu Jenista Mhagama nadhani umesikia vizuri michango ya Wabunge, bajeti yangu ikipita hapa naomba kama tulivyokubaliana tukae kikao wataalam wa Ofisi ya Waziri Mkuu na wataalam wa Ofisi ya Wizara ya Elimu kuangalia masuala ya kujenga ujuzi yanayotekelezwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na yale ambayo tunayatekeleza Wizara ya Elimu ili kama nchi tuwe na mfumo ambao utakuwa umeunganishwa kwa pamoja. Kwa hiyo, hilo tunakwenda kulifanyia kazi mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kutoa wito kwa taasisi za elimu kuhakikisha zinazingatia mafunzo kwa vitendo. Nchi yetu inajenga uchumi wa viwanda, naomba Vice Chancellors (Makamu Wakuu wa Vyuo) wajitafakari hivi ni wangapi ambao wanatembelea viwanda vilivyopo Tanzania ili kuhakikisha kwamba ujuzi unaotakiwa kwenye viwanda ndiyo ule ambao wanautoa katika taasisi zao. Kwa hiyo, niwasihi sana Makamu Wakuu wote wa Vyuo na taasisi zote zinazotoa elimu kuhakikisha kwamba suala hili la kufanya mafunzo kwa vitendo linaanza kutekelezwa mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo limezungumzwa ni eneo la kilimo na ujasiriamali. Naomba tu niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba masomo haya ya kilimo na ujasiarimali kwa sasa yanafundishwa katika somo la Stadi za Kazi. Hata hivyo, tumepokea michango yenu, tutaangalia namna ya kuyaboresha zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefurahi kwamba Waheshimiwa Wabunge wanazungumzia suala la elimu ya kujitegemea (suala la kilimo) kwa sababu wapo baadhi ya wazazi ambao mtoto wake akiambiwa kwenda shamba anapiga simu kwa Waziri analalamika kwamba sasa hivi watoto wetu wanalimishwa. Kwa hiyo, nimefurahi kwamba ni mtazamo wa nchi kwamba elimu ya kujitegemea ni muhimu, elimu ni kazi na watoto shuleni wawe tayari kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia ambalo linahusiana na hili suala la kazi ni utoaji wa chakula shuleni. Waheshimiwa Wabunge wamezungumza na mimi kwa kweli niwashukuru sana kwa kuwajali watoto kwa sababu wakiwa na njaa ni ukweli kwamba hawawezi wakasoma. Kwa hiyo, suala hilo ni la muhimu sana na Wizara tayari imetoa mwongozo (kitabu hiki hapa) cha namna ya kutoa chakula na lishe shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Waraka wetu Na. 1 wa mwaka 2016 wa Utoaji Elimu Bila Malipo tulisisitiza pia suala la utoaji wa chakula shuleni. Kwa sababu Bunge hili ni jipya niahidi kwamba nitagawa kwa Waheshimiwa Wabunge ili watusaidie kuwa mabalozi kwa sababu imeainishwa vizuri na kwa sababu ya muda siwezi kwenda ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia ni suala la uwepo wa chombo kimoja kinachosimamia elimu ya juu. Ni kweli kwamba sheria iliyoanzishwa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi imeipa mamlaka ya kusimamia elimu kuanzia ngazi ya cheti, degree mpaka na ngazi ya udhamivu lakini pia Tume ya Vyuo Vikuu imepewa mamlaka hayo, kwa hiyo, kuna mwingiliano wa kimajukumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mapendekezo pia kwamba hii vyuo vya kati ambavyo vinatoa degree vijikite katika kutoa utaalamu katika fani ambazo walianzishwa. Kwa sababu mmetupa kazi ya kufanya mapitio na kuwa na mjadala, naomba niwahakikishie katika kufanya mapitio suala hilo tutalizingatia kuhakikisha kwamba tunapunguza vyuo ambavyo vinatoa degree. Kwa sababu sasa hivi kila chuo cha kati na chenyewe kinatoa degree. Kwa hiyo, tumepokea michango yenu na tutalifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusiana na vyuo vikuu kuchelewa kuwasimamia wanafunzi na kusababisha wanafunzi kuchelewa kumaliza na kulazimika kulipa tena ada, jambo hili halipendezi hata kidogo. Nichukue nafasi hii kuviagiza vyuo vikuu hasa Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu vyote vya umma na vya binafsi kuweka mfumo mzuri wa kufuatilia wanafunzi wanaoenda kusoma hasa katika ngazi za uzamili na uzamivu na kuweka utaratibu wa kuwafualia walimu ili kujua kulikoni na waanze na kufanya tathmini, je, ni katika faculty zote au kuna baadhi ya shule ambazo zinachelewa na wachukue hatua mahsusi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vyuo vikuu naviheshimu sana kwa sababu na mimi nimetoka huko, ni vyuo ambavyo wanafanya kazi kwa misingi na taratibu na ndiyo maana hamuwezi mkaniona naenda kukagua ufundishaji katika vyuo vikuu. Hata hivyo, kwa malalamiko yaliyopo sasa hivi, naomba niwahahakishe kwamba sasa mimi mwenyewe nitafanya kazi ya kufuatilia katika kila chuo kuangalia tatizo nini ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa lakini jambo hili halikubaliki hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo limezungumzwa tena kwa uchungu sana ni suala la kuanzisha Chuo Kikuu cha Kilimo cha Teknolojia cha Mwalimu Nyerere Butiama. Mwalimu Nyerere Baba wa Taifa kwa kweli alituwekea misingi mizuri, tunamheshimu sana na tunamuenzi. Kwa hiyo, Wizara ya Elimu haiwezi kufanya utapeli katika eneo ambalo anatoka Muasisi wa Taifa hili, Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sitaki kutumia muda kueleza lakini najua tu ni kwa sababu wanataka kutoa pressure kwa Serikali lakini hata Waheshimiwa Wabunge wanaouliza wanafahamu changomoto zilizokuwepo ambazo zimechelewesha kuanzishwa kwa chuo hiki na nyingine zinatokana na mahali wanakotoka. Waswahili wanasema yaliyopita si ndwele, bahati nzuri leo hii wameuliza swali hili Bungeni tukiwa tumeshakamilisha changamoto zote zilizokuwepo, kwa hiyo, sasa tupo tayari kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kitabu changu cha hotuba katika miradi ya Wizara ya Elimu, tuna Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Juu ambapo tumetenga Dola za Kimarekani milioni 42 kwa ajili ya kuanzisha Chuo cha Mwalimu Nyerere. Niseme tu kwamba majengo ya sekondari hayawezi kuwa majengo ya chuo kikuu maana walikuwa wanasema majengo yapo lakini wenyewe wamesema ile ilikuwa ni sekondari. Hadhi ya chuo kikuu na hadhi ya sekondari ni vitu viwili tofauti. Kwa hiyo, niwatoe hofu, jambo hilo Serikali tunalifuatilia vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine dada yangu Mheshimiwa Jacqueline Msongozi alizungumzia suala la Chuo cha JUCO na akawa amesema kwamba leo shilingi yangu ataishika, dakika moja tu asinishikie shilingi. Suala la Chuo cha JUCO ni kweli kilianzishwa mwezi Julai 2013, lakini kutokana na changamoto za uendeshaji katika kikao cha 37 cha Bodi ya Wadhamini ya Vyuo Vikuu cha Kikatoliki Tanzania maana kinamilikiwa na Wakatoliki, walikaa tarehe 12 na tarehe 13 Februari, 2019 wakaazimia kwamba wasitishe kuendesha chuo kwa sababu walikuwa na vyuo karibu kila mkoa, kwa hiyo, gharama za uendeshaji zikawa kubwa. Kwa hiyo, tumekisitisha kutokana na ombi kutoka kwenye Bodi ya Wadhamini ya Chuo Kikuu hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hoja yake kwamba kwa nini Serikali haiviungi mkono vyuo binafsi, Serikali inaviunga mkono vyuo binafsi. Tunapotoa mafunzo namna ya kuendesha hivi vyuo tunawakaribisha kwa gharama ya Serikali Wahadhiri kutoka vyuo vikuu binafsi. Nimhakikishie tu dada yangu Mheshimiwa Jacqueline Msongozi kwamba Serikali inathamini elimu ya juu na tunathamini pia viongozi wa dini hatuwezi kuwafanyia uharamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu niwaambie Waheshimiwa Wabunge wamesikia kengele lakini mambo ya kuwajibu yalikuwa mengi, michango ilikuwa ni mizuri lakini sasa siwezi kuomba muda wa ziada nitakuwa nimevunja Kanuni. Naomba tu mridhike kwamba hoja zenu zote tutazijibu kwa maandishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, kwa heshima kubwa naomba sana mtuidhinishie mafungu yetu ili tukatendee kazi maoni na mapendekezo ambayo mmeyatoa. Naomba sana Waheshimiwa Wabunge wote muunge mkono bajeti ya Wizara ya Elimu ili kazi iendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni sana, naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia bajeti ya Serikali. Kwanza kabisa nianze kusema ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na ninaunga mkono hoja kwa sababu bajeti hii imeitendea haki sekta ya elimu, na bajeti hii inalenga katika kuondoa kero ambazo zimekuwa zikiwasumbua Watanzania kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, naomba nipongeze hatua ya Serikali ya kuanzisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato (e- government payment gateway) ambayo kwa kweli inalenga kuondoa upotevu wa mapato ambao unasababisha Serikali isiweze kuwahudumia wananchi wake ipasavyo. Vilevile napongeza kodi ambazo zimeondolea katika sekta ya elimu katika katarasi za kujibia maswali, lakini vilevile napongeza hatua ya kuondoa kodi kwa ajili ya vifaa vya wanafunzi wenye ulemavu.
Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo, sasa naomba nijikite katika kujibu hoja ambazo zilihusu sekta ya elimu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kumekuwa na hoja ambayo imejitokeza kuhusu namna ambavyo Serikali imejipanga katika kuhakikisha kwamba inatatua kero za wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Mheshimiwa Spika, nilihakikishie tena Bunge lako Tukufu kwamba utatuaji wa kero za wanafunzi wenye mahitaji maalum ni kipaumbele namba moja cha Serikali ya Awamu ya Tano, na tayari hatua za kutatua matatizo hayo zimekwisha chukuliwa.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti iliyopita tulinunua vifaa ambavyo vimesambazwa katika shule na Waheshimiwa Wabunge wanaweza wakaangalia katika kitabu changu cha bajeti kielelezo namba 8 hadi10 kimeonyesha mgao wa vifaa vilivyonunua na kwa Waheshimiwa Wabunge ambao hamkuapa katika awamu hii ni wahakikishie kwamba katika bajeti hii ambayo leo tunaipigia kura zimetengwa fedha kwa ajili yakuhakikisha kwamba ile mikoa na shule ambazo hazijapata zitapatiwa vifaa.
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala la Ukaguzi. Limezungumziwa hapa suala la kuboresha ukaguzi ili kuwa na ufanisi zaidi. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali inatambua kwamba Idara ya Udhibiti Ubora ndiyo jicho la Serikali katika sekta ya elimu; kwa hiyo kwa namna yoyote ile Serikali itahakikisha kwamba inaboresha. Hatua ambazo tumezichukua ni pamoja na kuhakikisha kwamba tunanunua vitendea kazi, tunafahamu kwamba mazingira ya Wadhibiti Ubora hayakuwa mazuri. Katika bajeti ya sekta ya elimu tumetenga fedha kwa ajili ya kujenga ofisi 50 pamoja na kununua vitendea kazi.
Mheshimiwa Spika, vifaa peke yake haviwezi kuleta ufanisi inatakiwa pia na watu ambao ni mahiri katika kufanya kazi. Mfumo mzima wa Ukaguzi katika sekta ya elimu tutaungalia kwa kuhakikisha kwamba tunakuwa na ufanisi zaidi. Kwa sababu mfumo wa sasa ambapo Mkaguzi wa Shule za Msingi hawezi kukagua shule za sekondari umepitwa na wakati kwa sababu kila ilipo shule ya msingi jirani yake kuna shule ya sekondari. Kwa hiyo, tunaangalia mfumo mzima na tumetengeza kihunzi cha ukaguzi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na mfumo ambao ni fanisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo imezungumziwa katika sekta ya elimu ilikuwa inahusiana na mazingira ya miundombinu katika sekta ya elimu. Nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ya awamu ya tano imeweka dhamira ya dhati na katika bajeti hii tumeweka mikakati ya kuhakikisha kwamba tunaendelea kuboresha mazingira katika sekta ya elimu kuanzia vyuo vya ualimu pamoja na vyuo vyetu vikuu. Kama tulivyofanya katika kujenga mabweni katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam tutaendelea na katika taasisi zetu nyingine za elimu ya juu ili kuhakikisha kwamba vijana wa Kitanzania wanapata elimu yao katika mazingira ambayo ni mazingira tulivu na ni rafiki katika kujifunza.
Mheshimiwa Spika, vile vile kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tutaendelea kuimarisha mazingira katika sekta ya elimu. Niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge wanaozungumzia mazingira ya wanafunzi wenye mahitaji maalum kwamba tuna mpango wa kujenga shule maalum ya kisasa katika Chuo chetu cha Walimu cha Patandi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum ili chuo kiwe karibu na mahali ambapo mafunzo ya walimu yanatolewa kwa lengo la kuhakikisha kwamba mafunzo ya walimu ambao wanahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum yatolewa kwa vitendo.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo limeongelewa ni suala la kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi. Niseme kwamba jirani yangu hapa Mwijage ambaye anajenga viwanda hawezi akafanikiwa kama sijampa raslimaliwatu ya kutosha. Wizara yangu inalitambua hilo na tumeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kamba tunakwenda sambamba na dhamira ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Spika, hivi tunavyo ongea Chuo cha Ufundi Arusha kimesha andaa kozi mahususi kuhakikisha kwamba Watanzania wananufaika na fursa ya kujenga bomba la mafuta ambazo nchi yetu imepata katika mazingira ya ushindani mkali. Kwa hiyo, tunaanda kozi ya kuwezesha vijana wetu kuwamahiri katika ujenzi wa bomba na vilevile katika nyanja nyingine zozote ambazo zinahusiana na viwanda vinavyoanzishwa. Tunafanya kazi kwa karibu na Wizara ya Viwanda na Biashara wanatupatia mahitaji na Wizara yangu hatulali tunahakikisha kwamba tunaweka mazingira fanisi ya kuweza kuhakikisha kwamba tunatoa mafunzo yanayoendana mahitaji.
Mheshimiwa Spika, suala la ujenzi wa VETA katika wilaya na katika maeneo yetu limekuwa likuzungumzwa, sana na niseme kwamba zile VETA ambazo zilikuwa zijengwe kwa ufadhili wa ADB tangu mwaka 2015 kulikuwa na changamoto ambazo Wizara yangu ilikuwa inapatia uvumbuzi na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba zile VETA zote ambazo ziko katika mchakato wa kujengwa tutahakikisha kwamba katika mwaka huu wa fedha 2017/2018 tunazikamilisha ili tuweze kupata fursa ya kuweza kujenga maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, kwa uchache hayo ndiyo ambayo yalizungumziwa katika sekta ya elimu. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja kama nilivyosema ni bajeti nzuri ni bajeti ambayo inaenda kuondoa kero katika sekta ya elimu lakini pia ni bajeti ambayo itawezesha kuimarisha mifumo ya elimu. Nakushukuru.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja hii ya Serikali ambayo ni bajeti ya Serikali. Kwanza nianze kwa kusema naunga mkono hoja hii, kwa sababu bajeti hii ya Serikali, ni bajeti ambayo inakwenda kuimarisha Sekta ya Elimu, ni bajeti ambayo inakwenda kutatua changamoto zilizopo katika Sekta ya Elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefurahishwa sana na hatua ya Serikali kuongeza vyanzo vya kuboresha barabara vijijini, kwa sababu barabara zinapokuwa mbovu hata Wizara ya Elimu tunapata shida kupeleka mitihani. Kwa hiyo barabara zikiwa nzuri hata Walimu wanapokuwa wanakwenda kwenye shughuli za kufanya kazi mjini kama wana shida au wanaenda kikazi itawarahishia ili kurudi mapema kufundisha. Pia suala la maji na umeme, ni muhimu ili elimu iende vizuri. Kwa hiyo naunga mkono hoja kwa asilimia mia kwa sababu mambo haya yamekwenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii pia kwa sababu kwanza imeimarisha hata mikopo, naona hata vijana wangu wapo hapa, mikopo kwa fedha zilizotengwa mwaka 2020/2021ilikuwa ni shilingi bilioni 464, lakini katika bajeti ya Wizara yangu iliyopita zipo bilioni 500, zilizopita zilikuwa bilioni 464 na mwaka unaokuja ni bilioni 500.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wakipitisha mapendekezo haya ambayo Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameyaleta, tutaweza pia kupata fedha nyingine za nyongeza katika Bodi ya Mikopo. Haya ndiyo yamenifanya niweze kuunga mkono hoja hii na nawasihi Waheshimiwa Wabunge waiunge mkono ili vijana wetu waendelee kusoma. Pia kwa wale ambao hawana uwezo wa kujikimu, basi Serikali iweze kuongeza wigo na tupunguze zile kelele za wanafunzi ambao wanakuwa na sifa wanadahiliwa na wakati mwingine wanakuwa wanakosa mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitapenda kuchangia baadhi tu ya maeneo machache ambayo yamezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge katika hoja hii. Kwanza niongelee suala la ujuzi, Waheshimiwa Wabunge wameendelea kusisitiza kwamba elimu yetu iwe kwa vitendo zaidi, ijenge ujuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nikwambie kwamba suala hilo tayari, hata kwenye hotuba ya bajeti yangu nimeshaliweka, lakini ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ameshatoa maelekezo kwa Wizara ya Elimu na tayari tumeanza mapitio, mlituona Mlimani City tarehe 18 Juni, tulikaribisha wadau wa elimu ambao wametupa maoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunapokea maoni kwa kupitia njia ya kimtandao google drive ambayo mpaka jana mchana tulikuwa na wananchi 1,152 ambao walikuwa wametoa maoni kwa njia ya mtandao. Kwa hiyo tutaendelea maoni na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, tutafanyia kazi na wasikose kuendelea kutupatia maoni na tutapanga muda mahsusi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tumepanga tuwe na mjadala Dodoma tarehe 26 Jumamosi, lakini Wizara ya Uwekezaji na Ofisi ya Waziri Mkuu tayari wana jambo lao, Kongamano la Vijana. Kwa hiyo tutaangalia kwa sababu yote ni mambo Serikali, hatuwezi tukaweka mambo mawili kwa wakati mmoja ili kuweza kuruhusu ushiriki kikamilifu kwa sababu masuala yote ni muhimu, lakini niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tutaendelea kuwashirikisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo lingine ambalo limezungumziwa kuhusiana na suala la watoto kubaki shuleni wakati wa likizo. Huwa ni msikivu sana na huwa najizuia kumpa Mheshimiwa Mbunge mwenzangu taarifa anapoongea, lakini leo kidogo jinsi lilivyoletwa na nikasikia kama mama, nasikia hata kauchungu fulani, Mheshimiwa anavyosema kwamba kuna baadhi ya shule wanawacha watoto shuleni, hakuna mabweni, wanafunzi wanalazwa kwenye sakafu kwenye majani. Hiyo hapana, hiyo sio sawa na Serikali haiwezi kuruhusu jambo kama hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka mfumo wa kwenda likizo kwa sababu tunaamini kwamba akili ya binadamu inachoka. Wanafunzi wanahitaji kupumzika, kukaa na familia zao na kufanya shughuli za nyumbani, maana akikaa shuleni tu kila wakati, mazingira pia mengine wanakuwa hawawezi kuyafanya. Nikitoa mfano wa wanafunzi wa kidato cha nne, wamefungua shule January, 13. Wataanza mitihani yao ya kumaliza kidato cha nne, tarehe 14 mwezi Novemba. Sasa mtoto yupo tangu January unamwambia mwezi Juni asiende nyumbani akae shuleni mpaka Disemba ndio anamaliza mitihani tarehe 13 Desemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama Serikali tunaona kwamba likizo kwa wanafunzi ni muhimu. Kwa sababu suala la mjadala wa elimu lipo mezani, tumeshafungua pazia, tunapokea maoni ya wadau na hili suala la likizo ya wanafunzi ambao wapo kwenye mitihani, tulipitie ili tuone kama kweli tumefika mahali ambapo tunaona kwamba Serikali itoe waraka ili ifute hizo likizo. Kwa sasa tunatekeleza nyaraka ambazo zipo na nyaraka ambazo zipo ndio zinavyoelekeza, wanafunzi wapate na muda wa kupumzika.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba, utaratibu pia unaowekwa na shule ambazo zinawabakiza watoto shuleni unakuwa pia mwingine siyo sawa, kwa sababu inakuwa kama ni dharura, wazazi inakuwa kamata kamata, lazima walete hela na mzazi asipoleta mtoto inakuwa ni shida. Sasa kipindi cha likizo ni kipindi cha kupumzika, isiwe ni lazima kwa mzazi ambaye labda anaenda likizo anataka mtoto wake aende naye, anaambiwa lazima abaki shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kuzikumbusha shule za Serikali, Serikali inatoa elimu bila malipo, sasa hili la kuwabakisha wanafunzi wakati wa likizo limekuwa ni uchochoro wa kuongeza gharama. Gharama zinazotozwa wakati wa likizo zinaanzia Sh.5,000 mpaka Sh.250,000 kwa mwezi mmoja. Kwa hiyo sasa ni namna ambavyo gharama za elimu zinarudishwa kwa njia nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwakumbushe Maafisa Elimu wa Mikoa wote na Maafisa Elimu Wilaya kuzingatia waraka wa elimu namba tatu wa mwaka 2016, ambapo umeelekeza bayana kwamba Serikali inatoa elimu bila malipo na kama kuna ulazima wa kuwachangisha wanafunzi michango ya aina yoyote, Waraka Na.3 wa mwaka 2016 unaelekeza utaratibu unaopaswa kufuatwa. Kwa hiyo wazingatie utaratibu huo, vinginevyo Maafisa Elimu, kwa sababu sehemu tumefuatilia sehemu nyingi shule zinafungwa kwa maelekezo ya Afisa Elimu, Waziri wa TAMISEMI ambaye ndiye anasimamia shule hana taarifa, Waziri wa Elimu hana taarifa, kwa hivyo Maafisa Elimu acheni kupoka mamlaka ya kuweka sera.
Mheshimiwa Naibu Spika, shule nyingi za Serikali zimeanza huu mtindo, hata madarasa mengine yasiyokuwa ya mitihani wanaambiwa wasiende shule. Leo nimepata malalamiko kwa mfano Kagera, kuna shule moja, mpaka wanafunzi wa elimu ya awali wanaambiwa wasiende likizo. Hiyo hapana, inakuwa too much sio tu masuala ya mitihani, yaani wanasema mafunzo rekebishi na kila mwanafunzi anayekwenda shule hata huyo mwanafunzi wa elimu wa awali, anatakiwa alipe. Kwa hiyo ukilitafakari kwa undani, kuna baadhi ya shule, Serikali inatoa elimu bila malipo, lakini wao wameamua kurudisha gharama kwa kivuli cha kwamba wanaandaa wanafunzi. Tumetunga mtaala wetu, tunaamini kwamba siku 194 za masomo zinatosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu ng’ombe hanenepeshwi siku ya mnada, mwanafunzi amekuwa shuleni miaka saba, darasa la kwanza, la pili kwa nini nguvu anayotumia mwanafunzi akiwa kwenye darasa la mitihani wasitumie miaka yote mwanafunzi anapokuwa shuleni? Kama hakuandaliwa vizuri kwa miaka saba jinsi mitaala yetu ilivyoandaliwa, haiwezekani kwa mwaka mmoja ukamshindilia mtoto, mambo ambayo alipaswa kusoma kwa miaka saba, huyu mtoto akaweza kuelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo cha kuwashindilia watoto mwaka wa mwisho, unataka mambo ambayo walitakiwa kuwafundisha miaka saba, ayasome kwa mwaka mmoja, wengine ndio maana wakiingia kwenye vyumba vya mitihani wanwakuwa wamechanganikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, naomba sana Waheshimiwa Wabunge, Serikali imelipokea suala hili na kwa sababu linaonekana ni tatizo tuna malalamiko mengi sana kutoka kwa wazazi. Shule binafsi nyingine zina utaratibu mzuri tangu kwenye joining instruction wanakuwa wameonesha na inakuwa ni sehemu ya ada zao, lakini kuna shule nyingine zinakuwa zinawashtukiza wazazi tu dakika ya mwisho mwanafunzi anatakiwa kuja, inakuwa kama dharura kwamba hawatakuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nadhani suala hili kama Serikali kwa sababu tumeshaiona hiyo changamoto, Waheshimiwa Wabunge tunapokea maoni kuhusiana na mitaala. Hata hivyo, suala hili lenyewe, tutalichukua na kwenda kulifanyia kazi na hasa hizi shule za Serikali, tutakwenda kufanya ukaguzi kwa sababu kuna shule za msingi kwenda mwanafunzi kusoma wiki tatu anatakiwa alipe Sh. 85,000/= shule ya Serikali. Hii sio sawa, msimamo wa Serikali kutoa elimu bila malipo upo pale pale, tutaendelea kutoa elimu bila malipo bila ya kuingiza gharama kwa kutumia kivuli kingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa elimu ya juu, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba bajeti hii inakwenda kuimarisha miundombinu katika elimu ya juu, inakwenda kuhakikisha kwamba tunaongeza idadi ya wanafunzi ambao wanajiunga na elimu ya juu kwa sababu kutokana na elimu bila malipo, ongezeko la wanafunzi Shule za Msingi na Sekondari ni kubwa. Kwa hiyo, tunaandaa mazingira sasa ya kuwapokea watakapokwenda Vyuo Vikuu. Kwa hiyo, tutakuwa na ujenzi wa miundombinu, kutakuwa na kutoa ufadhili wa wahadhiri wetu ili waweze kupata shahada za uzamivu na tuweze kuandaa walimu wengi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tutaimarisha sana mafunzo kwa vitendo. Hapa niendelee kuwasishi Wakuu wa Vyuo, Taasisi za Elimu ya Juu kuweka ushirikiano mzuri na sekta binafsi pamoja na viwanda ili kuweza kupata sehemu za kufanya mafunzo kwa wanafunzi wetu wa elimu ya juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja hii kwa sababu hakika inakwenda kuimarisha elimu yetu. Nashukuru sana kwa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, nianze tu kusema kwamba naunga mkono hoja hii ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameiwasilisha kwa umahiri mkubwa sana.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kuchangia nikiwa kama Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, naomba niruhusu nimshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini na kuniteua katika nafasi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia nimshukuru Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, kwa miongozo ambayo amekuwa akinipatia ambayo imekuwa chachu ya ufanisi katika kazi zangu. Nampongeza Mheshimiwa Dkt. Hussein Ally Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kazi kubwa ambayo anaifanya.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba nishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa maoni na ushauri waliotupatia na niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia katika eneo la kazi, vijana na ajira na wenye ulemavu naomba nitoe sasa ufufanuzi katika hoja chache ambazo wamezichangia.
Mheshimiwa Spika, nitaanza na hoja ya Kamati na Waheshimiwa Wabunge wengine walichangia kuhusiana na program ya kukuza ujuzi nchi ambayo program hii inalenga katika kujenga ujuzi na kuondoa changamoto ya ajira kwa vijana. Waheshimiwa Wabunge wameona kuna changamoto ya watu wanaopata ujuzi, kwanza wanakubali kwamba program hii inatoa ujuzi ambao ni mzuri na muhimu kwa vijana lakini changamoto inakuwa namna ya kutumia ujuzi kwa sababu ya mitaji.
Mheshimiwa Spika Serikali inafanyia kazi jambo hili na kwa hatua ya kwanza tumewatambua vijana wote ambao wamepata ujuzi huu na orodha hiyo tumeikabidhi Ofisi ya Rais - TAMISEMI ili katika ile mikopo ya asilimia 10 wapewe kipaumbele, vilevile tunawapa kipaumbele katika fursa za uwekezaji ambazo zinajitokeza. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali itaendelea kutafuta fursa zinazopatikana ili iendelee kuwawezesha vijana ambao wanapata mafunzo haya.
Mheshimiwa Spika, niliambie Bunge lako Tukufu baadhi ya vijana ambao wamepitia katika program hizi wameweza kupata kazi katika miradi ya kimkakati kama ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, ujenzi wa reli ya kisasa, pia alishiriki katika miradil ile ambayo ilikuwa inafadhiliwa na Mfuko wa UVIKO-19. Tutaendelea kutoa ujuzi na tutaendelea kutafuta fursa kwa vijana ili waendelee kunufaika na ujuzi unaoupata.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine imetolewa ya kuhusiana na gharama za vitalu nyumba kwa wale vijana ambao wanapata mafunzo ya kujenga vitalu nyumba na kilimo kwa kutumia vitalu nyumba. Tumepokea ushauri wa Waheshimiwa Wabunge na tutaendelea kufanya tafiti kuangalia namna ya kupata vifaa vyenye gharama nafuu ili ujuzi wanaoupata waweze kuenda kuuendeleza.
Mheshimiwa Spika, vilevile tutaendelea kutoa vifaa na mikopo kadri fedha zinapopatikana za kufanya hivyo ili ujuzi wanaoupata waweze kuutumia.
Mheshimiwa Spika, kuna hoja ambayo imetolewa kuhusiana na ufanisi wa mafunzo kwa vitendo. Kamati imependekeza kwamba tushirikiane na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kuhakikisha kwamba mitaala inaboreshwa na inakuwa inawajengea ujuzi ili kupunguza gharama ya kuwa na program baada ya wahitimu.
Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie Wizara yangu inafanya kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na hata program hizi ambazo tunaziendesha mitaala yake imeandaliwa kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na tunatoa msisitizo wa mafunzo kwa vitendo kwenye program ya wanagenzi kwa mfano; asilimia 60 ya muda wa mafunzo unaelekeza kwenye mafunzo kwa vitendao na asilimia 40 inakuwa ndio nadharia.
Mheshimiwa Spika, pia tunashirikiana na waajiri katika kuhakikisha kwamba wanatoa fursa kwa vijana kwenda kufanya mafunzo kwa vitendo. Kupitia Bunge lako Tukufu naomba nitoe wito kwa waajiri nchini, kuwapa fursa vijana, yakufanya mafunzo kwa vitendo kwa sababu yale ni muhimu katika kuhakikisha kwamba ujuzi wanaoupata katika mafunzo yao unaendana na soko la ajira.
Mheshimiwa Spika, na wanapokuwa katika mafunzo kwa vitendo kuna kuwa na mwanya wa kurekebisha kama kuna mapungufu ambayo yanajitokeza katika mafunzo yao. Kwa hiyo, niwasihi sana, waajiri hapa nchini wenye viwanda, waendelee kutoa fursa kwa vijana wetu kwenda kufanya mafunzo kwa vitendo.
Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie kwamba tutashirikiana kikamilifu na Wizara ya Elimu katika jukumu hili ambalo wamepewa sasa hivi na Serikali ya kuhakikisha wanapitia mitaala, kuhakikisha mitaala yote nchini kuanzia elimu ya awali mpaka vyuo vikuu inajikita katika kujenga ujuzi. Kwa hiyo, kwa sababu Wizara yetu pia imekuwa na program za kukuza ujuzi tutafanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha kwamba yale ambayo tumekuwa tunawafundisha vijana baada ya kuhitimu yaingie katika mitaala ili wanapomaliza shule au vyuo wawe na ujuzi stahiki.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo Waheshimiwa Wabunge wameizungumzia ni kuhusiana na Serikali ina mpango gani wa kuboresha kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi. Nikuhakikishie Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inatuambua umuhimu wa maslahi kwa wafanyakazi na kwa kutambua hilo, tayari Serikali imeshaunda Bodi ya Kima cha Chini cha Mishahara kwenye sekta binafsi na Bodi hiyo nimeizindua jana tarehe 12 Aprili, 2022. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Bodi hiyo inapaswa kufanya utafiti ili iweze kuishauri Serikali kuhusiana na kima cha chini cha mshahara. Nitumie nafasi hii kuwasihii waajiri wote nchini pamoja na wafanyakazi kutoa ushirikiano unaotakiwa kwenye bodi hii ili iweze kufanya kazi yake ya utafiti na hatimae iweze kutoa mapendekezo kwa Serikali kuhusiana na kima cha chini cha mishahara katika sekta binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo limezungumziwa ni kuhusiana na Mabaraza ya Wafanyakazi kwamba Mabaraza haya kwanza katika kuna baadhi ya taasisi na waajiri wengine hawaundi Mabaraza ya Wafanyakazi na hata wengine ambao wameyaunda Mabaraza haya hayafanyi kazi kwa kuzingatia vikao ambavyo vimewekwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, naomba niwakumbushe waajiri hapa nchini kwamba Mabaraza ya wafanyakazi yapo kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo niwasihi ninawataka waajiri wote nchini kuhakikisha kwamba Mabaraza ya Wafanyakazi yanaundwa na wanafanya vikao vyao kwa mujibu wa sheria. Mabaraza haya ni muhimu katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na maelewano katika maeneo ya kazi na kutatua migogoro ambayo inaweza ikajitokeza.
Mheshimiwa Spika, kunapokuwa na utulivu mahali pa kazi kunapokuwa na mahusiano mazuri kuna kuwa na tija zaidi na ufanisi. Kwa hiyo, ninawasihi waajiri kuhakikisha kwamba Mabaraza yanaundwa na yanafanya kazi kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, tumepokea pia maoni kuhusiana na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na hapa maoni yamejikita katika maeneo tofauti, kwanza kuna maoni kwamba baadhi ya Wastaafu wanapostaafu wanachelewa kulipwa mafao yao na wanapata usumbufu wa kutakiwa kupeleka barua na nyaraka mbalimbali au wakati mwingine wanaambiwa kwamba hawawezi kulipwa kwa sababu mwajiri hakupeleka michango yao kwa miezi kadhaa.
Mheshimiwa Spika, ni kweli jambo hili limekuwa usumbufu kwa wastaafu lakini nikuhakikishie kwamba Serikali inalifanyia kazi kikamilifu na katika hatua ya kuanzia tunaboresha mifumo ya TEHAMA, changamoto inayokuja ni kwamba watu walioajiriwa miaka ya nyuma kabla ya mifumo ya TEHAMA haijawa imara kumbukumbu zao zilikuwa zinatunzwa katika nakala ngumu, kwa hiyo wakati mwingine Watumishi hasa wale ameajiriwa kabla ya miaka 1999 ambao waliingizwa kwenye mifuko baada ya kuwa ameshaajiriwa baadhi yao kumekuwa na changamoto ya kupata taarifa zao.
Mheshimiwa Spika, jambo hili linafanyiwa kazi kikamilifu na tutahakikisha kwamba tunaondoa hiyo kero. Mimi mwenyewe nimejiwekea dhamira ya kufuatilia kwa ukaribu ili nipande kwa undani malalamiko hayo ya Wastaafu kwa sababu ni jambo ambalo halipendezi hata kidogo.
Mheshimiwa Spika, hao Wastaafu wameitumikia nchi yetu kwa moja mkunjufu, wamejituma kwa nafasi yao wamelijenga Taifa letu, kwa hiyo wanapomaliza utumishi wao ni lazima wapate stahiki zao kwa wakati na bila usumbufu wowote. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu suala hili na kuchukua hatua kuhakikisha usumbufu kwa wastaafu unaondolewa.
Mheshimiwa Spika, jambo jingine ambalo limezungumzwa ni kuhusiana na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Kuna fedha ambazo Serikali imetoa kiasi cha Shilingi Bilioni Moja kwa ajili ya kuwawezesha vijana na mpaka kufikia Februari fedha hizo zilikuwa zimetumika kwa takribani Shilingi Milioni 245.
Mheshimiwa Spika, naomba uchelewaji wa kutoa fedha kwa mwaka huu wa fedha umetokana na kwamba kulikuwa na uboreshaji wa mwongozo wa utoaji wa mikopo ambao ulitokana na maoni ya Waheshimiwa Wabunge. Nikuhakikishie kwamba tunatambua kilio cha vijana, tunatambua kwamba vijana wengi kama nilivyosema wanapata ujuzi lakini hawana mitaji, vijana wengi wanaomaliza vyuo vikuu wengine wameanzisha startup zao lakini hawana mitaji. Kwa hiyo nikuhakikishie kwamba tutafanyia kazi suala hili kuhakikisha kwamba fedha zinapopatikana zinatoka ziende kuwanufaisha wanufaika.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo mimi ninakushukuru sana kwa nafasi hii na ninaunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia katika hoja hii. Kwanza nianze kwa kusema naunga mkono hoja ambayo kwa kweli imesheheni namna ambavyo Serikali imetekeleza mipango ya maendeleo kwa ajili ya kuimarisha uchumi wetu na ustawi wa Watanzania. Pia hoja hii imeweza kuonesha Watanzania namna ambavyo Serikali imeendelea kujipanga na kuweka mipango ya mbele katika kuendelea kuimarisha uchumi na maendeleo ya Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii nimshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini na kunipa nafasi ya kuwa msaidizi wake katika nafasi hii ya Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye ulemavu. Kipekee nimpongeze kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ametimiza miaka miwili ya uongozi wake na ni hakika ni miaka miwili ya mafanikio makubwa.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge ambao wamesimama kuchangia hapa kila mmoja ameelezea namna ambavyo katika maeneo yake katika jimbo lake ameguswa. Tanzania yote hii imeshuhudia uongozi uliotukuka wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ni kiongozi bora, kiongozi imara, kiongozi shupavu na tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya njema na maono zaidi ili aendelee kulitumikia Taifa letu na tuendelee kupata mafanikio. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Viongozi hawa wawili pia wamekuwa wakinipa miongozo na maelekezo ambayo yameniwezesha kutekeleza majukumu yangu. Naomba niwaahidi viongozi wangu nitaendelea kuwa mtumishi mwaminifu na nitafanya kazi zangu kwa weledi kwa maslahi mapana ya Taifa letu la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipekee naomba nikupongeze wewe, Spika wetu mahiri, Spika wa viwango kwa hakika unatuheshimisha sana Wabunge. Nakupongeza wewe pamoja na Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wetu wa Bunge kwa kazi nzuri wanazofanya na Wenyeviti wote wa Kamati kwa kweli pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote ambao kwa hakika mnatupa ushauri na maoni na mapendekezo yenu yameendelea kuwa chachu ya sisi kujituma zaidi kwa sababu mnawakilisha wananchi. kwa hiyo, lazima tuwasikilize, lazima tufanyie kazi mapendekezo yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nishukuru kipekee Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii chini ya uongozi wa Mwenyekiti, Dada yangu Mheshimiwa Fatma Toufiq kwa namna ambavyo wanatupa ushirikiano, ushauri na maelekezo. Wakati wa kuchambua bajeti hii kuna mambo mengi walitushauri na tuliyazingatia wakati tunaandaa bajeti yetu.
Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze dada yangu, pacha wangu Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama kwa kuteuliwa kuwa Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu na nimwahidi kwamba tutafanya kazi kama ilivyo kawaida yetu, kwa weledi wa hali ya juu. Namshukuru kaka yangu Mheshimiwa Boniface Simbachawene ambaye tumefanya naye kazi vizuri mpaka hapo Mheshimiwa Rais alipomteua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipekee namshukuru Naibu Waziri wangu, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa, bila kuwaacha wadau wangu wa utatu; Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania pamoja na Chama cha Waajiri Tanzania kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa, pamoja na washirika wa maendeleo; ILO, UNICEF, UNDFPA pamoja GIZ. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipekee niwashukuru pia wapiga kura wangu Jimbo la Kasulu Mjini ambao ndio wamenipa heshima ya kuwa katika Bunge hili, na niwaahidi kwamba nitaendelea kuwatumikia kwa moyo wangu wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo, naomba sasa nijibu baadhi ya hoja za Wabunge. Naomba nianze na suala ambalo Waheshimiwa Wabunge wamechangia kuhusu maslahi ya wafanyakazi na hususan wakazungumzia maslahi ya wafanyakazi katika sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, niwaambie katika pongezi ambazo nimempa Mheshimiwa Rais katika miaka miwili ya uongozi, kama kuna eneo ambalo Mheshimiwa Rais ameligusa na ameweka alama ni kwenye suala la watumishi wa umma na kwenye sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, Serikali inawathamini wafanyakazi na mchango wao na kupitia Bodi ya Kima cha Chini cha Mishahara tumeweza kutoa amri kupitia Gazeti la Serikali Na. 687 ambalo lilichapishwa tarehe 25 mwezi wa 11 ambapo kima cha chini cha mishahara kwenye sekta binafsi kimeongezwa na utekelezaji umeanza tarehe 1 Januari, 2023.
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuendelea kusisitiza waajiri ambao bado wana uzito wa kutekeleza amri hii ni kuwaambia kwamba ni haki ya wafanyakazi kupata mshahara kama ambavyo imeainishwa katika amri ya kima cha chini cha mishahara. Kwa hiyo, katika kaguzi zetu tutaendelea kufuatilia ili kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanalipwa kama ambavyo Bodi ya Kima cha Chini cha Mishahara imependekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo jingine ambalo limezungumziwa ni masuala ya malipo ya mafao ya wastaafu na hata mchangiaji ambaye amezungumza asubuhi hii ya leo amezungumza pia kwamba kuna wastaafu ambao hawalipwi kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba ulipaji wa mafao kwa wastaafu umeimarishwa kwa kiwango kikubwa na changamoto zilizokuwepo ambazo zilikuwa zinasababisha wastaafu wasilipwe kwa wakati, Serikali hii ya Awamu ya Sita tayari imezifanyia kazi na changamoto kubwa iliyokuwepo ilikuwa ni ukwasi.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na deni la wafanyakazi waliorithiwa kutoka kwenye mfuko uliokuwa PSPF ambao wafanyakazi kabla ya mwaka 1999 walikuwa hawachangii. Kwa hiyo, Serikali ilivyowaingiza kwenye mfuko ikawa imeahidi kwamba itawalipia michango kiasi cha shilingi trilioni 4.6 na ninaomba niliambie Bunge lako tukufu. Serikali ya Awamu ya Sita tayari ukiangalia katika Hotuba ya Waziri Mkuu ukurasa wa 67 aya ya 124; Serikali imeeleza kwamba tayari kiasi cha shilingi trilioni 2.17 kimelipwa. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu hoja ni ya Waziri Mkuu kwa hiyo Mawaziri chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu wanajikuta na wao wako katika mazingira ya kuchangia lakini hoja inapokuwa inahitimishwa na Waziri kikanuni haiwezi kupewa taarifa. Kwa hiyo, tuwe tumeelewana vizuri. Mheshimiwa Ndalichako kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ester Bulaya.
T A A R I F A
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Ndalichako kwamba suala la ukwasi kwenye PSSF bado lipo na kama anasema limeisha niko tayari ku-resign Ubunge na mpaka sasa hivi kwa mujibu wa sheria ukwasi inatakiwa iwe 40%. Mpaka sasa hivi kwa taarifa latest bado 22% na suala la fedha ambazo unasema zimelipwa, ile ni hatifungani na bado mifuko iko kwenye hali mbaya.
SPIKA: Mheshimiwa Ester Bulaya, ukwasi huo wa kiasi ulichotaja wewe mwenyewe kabla sijarudi kwa unayempa taarifa unatosheleza kulipa watu mafao ama hautoshelezi, ukwasi huo huo wa asilimia ishirini na ulizozisema wewe.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ukwasi huo kwenye hii mifuko hautoshelezi na ndiyo maana mifuko inaenda kuchukua mpaka kwenye fedha za michango. Mpaka fedha za michango unakwenda kukopa kwenye maeneo mengine. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Ndalichako unaipokea taarifa hiyo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, siipokei taarifa yake kwa sababu kwanza kazi ya michango ndiyo pamoja na kulipa mafao. Wanakusanya ili pia waweze kulipa mafao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia nimeeleza deni ambalo Serikali imelipa kupitia hatifungani shilingi trilioni 2.16. Taarifa ya ukwasi anayoizungumzia Mheshimiwa Ester Bulaya ilifanyika mwaka 2020. Leo hii tuko mwaka 2023, kabla ya hapo deni lilikuwa halijalipwa na pamoja na hizi fedha hatifungani ya shilingi trilioni 2.17 lakini pia kulikuwa na madeni mengine ambayo yanatokana na uwekezaji Serikali imelipa shilingi bilioni 500 katika mifuko ya hifadhi ya jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba niendelee.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la ucheleweshwaji wa malipo kwa wastaafu, naomba nilihakikishie Bunge lako kwamba mifuko ya hifadhi ya jamii imeimarisha mifumo yake ya ulipaji wa mafao kwa wastaafu na inalipwa kwa wakati. Kama kuna ucheleweshwaji wowote, basi naomba tupate taarifa lakini niwahakikishie Bunge kwamba sasa hivi Mfuko wa NSSF, Mfuko wa PSSF unalipa mafao ya wastaafu ndani ya muda ambao umewekwa kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, inawezekana ikatokea kuna tatizo la michango ya mtumishi ambaye anastaafu, hiyo itakuwa ni case tofauti. Nazungumzia mtu ambaye amestaafu, michango yake iliwasilishwa na taarifa zake zimekuja kwenye mfuko analipwa mafao yake ndani ya muda ambao umewekwa kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, naomba nichukue nafasi hii kutoa wito kama kuna mtu yeyote ana changamoto zozote za kulipwa kwa wakati atoe taarifa ili tuweze kuifanyia kazi lakini kwa maana ya mifuko, mifumo iko imara na wastaafu wanalipwa mafao yao ndani ya muda ambao umewekwa kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna suala ambalo lilizungumziwa la kuimarisha mahusiano kazini na kuhakikisha kwamba mabaraza ya wafanyakazi yana fanya kazi vizuri. Kwanza niliambie Bunge lako tukufu sasa hivi tumeimarisha usimamizi kuhakikisha kwamba mabaraza ya wafanyakazi yanaundwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nitoe wito kwa waajiri kuhakikisha kwamba mabaraza haya ya wafanyakazi ambayo yameundwa yanafanya kazi kwa mujibu wa sheria. Watoe nafasi kwa wafanyakazi kufanya vikao kama ambavyo inatakiwa kwa mujibu wa sheria na ofisi yangu kupitia kwa Kamishna wa Kazi tutaendelea kufuatilia ili kuhakikisha kwamba wanafanya kazi kama inavyotakiwa.
Mheshimiwa Spika, pia umetolewa ushauri kwamba tuendelee kuimarisha Baraza letu la Ushauri na Masuala ya Kazi, Uchumi na Kijamii LESCO ili liweze kufanya majukumu yake ipasavyo. Nikuhakikishie kwamba Serikali imejikita katika kuhakikisha kwamba inashughulikia masuala ya wafanyakazi kwenye Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baadhi ya mambo ambayo yamefanyika kupitia LESCO katika kipindi cha mwaka wa fedha huu ambao tunauzungumzia. Kwanza ni kutoa ushauri kuhusiana na kima cha chini cha mishahara ambacho kimeshatangazwa kwenye Gazeti la Serikali cha mwezi Novemba na kimeanza kutekelezwa mwezi Januari.
Mheshimiwa Spika, pia LESCO imetoa ushauri katika kanuni za sheria ya usalama na afya mahali pa kazi ambazo nazo zinaanza kutumika. LESCO imetoa ushauri kuhusu viwango vya posho kwa madereva ambao wanasafirisha shehena za mizigo kwenda nje ya nchi. Waheshimiwa Wabunge mnafahamu kwamba kuna kipindi hali ya upande wa usafirishaji ilikuwa inakuwa tete kutokana na changamoto za madereva kutopata maslahi yao vizuri lakini kupitia LESCO tumeweza kufikia mahali ambapo kumekuwa na viwango ambavyo vimependekezwa na tayari vinatumika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie jambo jingine kuhusiana na kanuni ya mafao kwa watumishi wa umma almaarufu kama kikotoo. Kumekuwa na upotoshaji mkubwa kuhusiana na hii kanuni ya mafao kwa watumishi na labda hapa nitatumia muda kidogo ili tuweze kwenda vizuri na nitumie fursa hii pia kutoa elimu hata kwa wafanyakazi ambao watakuwa wanatufuatilia kwenye Bunge hili.
Mheshimiwa Spika, kanuni hii ya kukokotoa mafao kwa watumishi wa umma ambayo imeanza kutumika tarehe 1 Julai, 2022 imetokana na sheria Na. 2 ya mwaka 2018 ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ambayo ndiyo ilianzisha Mfuko wa Watumishi wa Umma PSSSF na iliunganisha mifuko minne; Mfuko wa GEPF, LAPF, PPF na PSPF. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kabla ya kuunganisha mifuko hii, mifuko hii ilikuwa na kanuni tofauti za ulipaji wa mafao. Mfuko wa GEPF na PPF ulikuwa unalipa mafao ya mkupuo ya 25% na mfuko wa LAPF pamoja na Mfuko wa PSPF ulikuwa unalipa mafao ya mkupuo ya 50%.
Mheshimiwa Spika, vile vile tulikuwa na mfuko kwa ajili ya watumishi kwenye sekta binafsi, NSSF ambao ulikuwa unatoa mafao ya mkupuo ya 25%. Baada ya kuunganisha mifuko kulikuwa na ulazima wa kuiainisha kanuni. Huwezi ukawa na mfuko mmoja ambao unalipa wanachama wake kwa kutumia kanuni tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mwaka 2018 ziliundwa kanuni kwa ajili ya kutekeleza sheria hii ambazo ziliweka watumishi wote walipwe mafao ya mkupuo ya 25%. Sasa baada ya kutunga kanuni hizo waliokuwa wanapata mafao ya 50%.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Profesa Ndalichako kuna taarifa. Waheshimiwa Wabunge, kwa kutazama muda wetu taarifa hiyo itakuwa ya mwisho.
T A A R I F A
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nadhani Mheshimiwa Waziri kwanza anatakiwa akiri hapa, mifuko iliunganishwa kwa sababu Mfuko Mkubwa wa PSSF ulikuwa kwenye hali mbaya na ulikuwa unakufa. Huo ndiyo ukweli wa kwanza ambao aukiri kwa sababu anafahamu kabla mifuko haijaunganishwa, deni la PSSF kwa Serikali ya pre 1999 and past 1999 ilikuwa zaidi ya shilingi trilioni saba. Kwa hiyo, wakaenda kufanya uhakiki wakaja na shilingi trilioni 4.5 waliokuwa wanataka kuisema? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hilo la kwanza lakini la pili.
SPIKA: Haya ahsante sasa taarifa ni moja Mheshimiwa.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo akiri siyo anaongea vitu ambavyo havipo.
SPIKA: Mheshimiwa sasa wewe unampa taarifa au unamuuliza swali?
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nampa taarifa na ushauri.
SPIKA: Wewe umempa taarifa kwa hiyo ana uamuzi wa kupokea taarifa yako au hapana. Sasa ukimwambia akiri maana yake umemuuliza swali. Mheshimiwa Prof. Ndalichako unipokea taarifa hiyo au hapana?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, siwezi kuipokea taarifa kwa sababu hata yeye mwenyewe mtoa taarifa naona hata haelewi anazungumza anataka sijui. Kwa hiyo, siipokei taarifa yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kwa sababu nilikuwa naeleza na Waheshimiwa Wabunge naomba tuwe na utulivu tusikilize kwa sababu nilichokuwa naeleza na yeye anachoingilia sasa ilikuwa ni kitu tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mifuko hiyo baada ya kuunganishwa na kanuni zikatengenezwa zilikuwa zinalipa watumishi wote mkupuo wa 25%. Sasa baada ya kanuni hii kuanza kutumika ni dhahiri kwamba wale waliokuwa wanalipwa 50% kutoka 50% mpaka 25% walikuwa wanaona wameshushwa mahali pakubwa. Kwa hiyo, kukawa na malalamiko na Serikali hii ni Sikivu, Serikali ikasema kwamba isitishe kuendelea kutumia na hizo kanuni tukae chini tukutane na wafanyakazi na wadau wanaohusika tuje na kanuni ambayo…
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, kuna taarifa.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: …itawakutanisha watumishi katikati. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, baada ya majadiliano na kushirikishana, taasisi ambazo zinahusika na wafanyakazi ndiyo tumekuja na kanuni ya 33%. Kwa hiyo, kanuni hii lengo lake ilikuwa inataka kuwakutanisha katikati waliokuwa wanapata 50% na waliokuwa wanapata 25%. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niliambie Bunge lako tukufu, kanuni hii ambayo ya 33% imeongeza mafao ya mkupuo kwa wanachama 1,364,050 sawa na 81% ya wanachama wote, waliokuwa wanapata 25%. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, watumishi kwenye taasisi zote za umma mafao yenu yameongezeka kutoka 25% mpaka 33%. Watumishi kwenye sekta binafsi kupitia kanuni hii, mafao yenu ya mkupuo yameongezeka.
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kanuni hii kuna wafanyakazi 326,137 sawa na 19% ndiyo hao ambao walikuwa wana 50% wamekuja kwenye 33% lakini mafao yao ya pensheni kwa mwezi yameongezeka. Walikuwa wanlipwa 50% sasa wanalipwa 67%. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimeona nitoe ufafanuzi huo kwa sababu jambo hili linakuwa linaongelewa kana kwamba yaani wafanyakazi wote wameshushiwa. Wafanyakazi 81% mafao yao ya mkupuo yameongezeka. Wote waliokuwa wanachama wa PPF waliokuwa wanachama wa GEPF, NSSF mafao yao yameongezeka kutoka mkupuo wa 25% kwenda kwenye mkupuo wa 33%. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimalizie kwa kushukuru tena kwa nafasi hii ambayo nimeipata ya kuchangia na naomba niseme naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia bajeti ya Serikali. Kwanza kabisa nianze kusema ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na ninaunga mkono hoja kwa sababu bajeti hii imeitendea haki sekta ya elimu, na bajeti hii inalenga katika kuondoa kero ambazo zimekuwa zikiwasumbua Watanzania kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, naomba nipongeze hatua ya Serikali ya kuanzisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato (e- government payment gateway) ambayo kwa kweli inalenga kuondoa upotevu wa mapato ambao unasababisha Serikali isiweze kuwahudumia wananchi wake ipasavyo. Vilevile napongeza kodi ambazo zimeondolea katika sekta ya elimu katika katarasi za kujibia maswali, lakini vilevile napongeza hatua ya kuondoa kodi kwa ajili ya vifaa vya wanafunzi wenye ulemavu.
Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo, sasa naomba nijikite katika kujibu hoja ambazo zilihusu sekta ya elimu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kumekuwa na hoja ambayo imejitokeza kuhusu namna ambavyo Serikali imejipanga katika kuhakikisha kwamba inatatua kero za wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Mheshimiwa Spika, nilihakikishie tena Bunge lako Tukufu kwamba utatuaji wa kero za wanafunzi wenye mahitaji maalum ni kipaumbele namba moja cha Serikali ya Awamu ya Tano, na tayari hatua za kutatua matatizo hayo zimekwisha chukuliwa.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti iliyopita tulinunua vifaa ambavyo vimesambazwa katika shule na Waheshimiwa Wabunge wanaweza wakaangalia katika kitabu changu cha bajeti kielelezo namba 8 hadi10 kimeonyesha mgao wa vifaa vilivyonunua na kwa Waheshimiwa Wabunge ambao hamkuapa katika awamu hii ni wahakikishie kwamba katika bajeti hii ambayo leo tunaipigia kura zimetengwa fedha kwa ajili yakuhakikisha kwamba ile mikoa na shule ambazo hazijapata zitapatiwa vifaa.
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala la Ukaguzi. Limezungumziwa hapa suala la kuboresha ukaguzi ili kuwa na ufanisi zaidi. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali inatambua kwamba Idara ya Udhibiti Ubora ndiyo jicho la Serikali katika sekta ya elimu; kwa hiyo kwa namna yoyote ile Serikali itahakikisha kwamba inaboresha. Hatua ambazo tumezichukua ni pamoja na kuhakikisha kwamba tunanunua vitendea kazi, tunafahamu kwamba mazingira ya Wadhibiti Ubora hayakuwa mazuri. Katika bajeti ya sekta ya elimu tumetenga fedha kwa ajili ya kujenga ofisi 50 pamoja na kununua vitendea kazi.
Mheshimiwa Spika, vifaa peke yake haviwezi kuleta ufanisi inatakiwa pia na watu ambao ni mahiri katika kufanya kazi. Mfumo mzima wa Ukaguzi katika sekta ya elimu tutaungalia kwa kuhakikisha kwamba tunakuwa na ufanisi zaidi. Kwa sababu mfumo wa sasa ambapo Mkaguzi wa Shule za Msingi hawezi kukagua shule za sekondari umepitwa na wakati kwa sababu kila ilipo shule ya msingi jirani yake kuna shule ya sekondari. Kwa hiyo, tunaangalia mfumo mzima na tumetengeza kihunzi cha ukaguzi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na mfumo ambao ni fanisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo imezungumziwa katika sekta ya elimu ilikuwa inahusiana na mazingira ya miundombinu katika sekta ya elimu. Nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ya awamu ya tano imeweka dhamira ya dhati na katika bajeti hii tumeweka mikakati ya kuhakikisha kwamba tunaendelea kuboresha mazingira katika sekta ya elimu kuanzia vyuo vya ualimu pamoja na vyuo vyetu vikuu. Kama tulivyofanya katika kujenga mabweni katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam tutaendelea na katika taasisi zetu nyingine za elimu ya juu ili kuhakikisha kwamba vijana wa Kitanzania wanapata elimu yao katika mazingira ambayo ni mazingira tulivu na ni rafiki katika kujifunza.
Mheshimiwa Spika, vile vile kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa tutaendelea kuimarisha mazingira katika sekta ya elimu. Niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge wanaozungumzia mazingira ya wanafunzi wenye mahitaji maalum kwamba tuna mpango wa kujenga shule maalum ya kisasa katika Chuo chetu cha Walimu cha Patandi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum ili chuo kiwe karibu na mahali ambapo mafunzo ya walimu yanatolewa kwa lengo la kuhakikisha kwamba mafunzo ya walimu ambao wanahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum yatolewa kwa vitendo.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo limeongelewa ni suala la kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi. Niseme kwamba jirani yangu hapa Mwijage ambaye anajenga viwanda hawezi akafanikiwa kama sijampa raslimaliwatu ya kutosha. Wizara yangu inalitambua hilo na tumeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kamba tunakwenda sambamba na dhamira ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Spika, hivi tunavyo ongea Chuo cha Ufundi Arusha kimesha andaa kozi mahususi kuhakikisha kwamba Watanzania wananufaika na fursa ya kujenga bomba la mafuta ambazo nchi yetu imepata katika mazingira ya ushindani mkali. Kwa hiyo, tunaanda kozi ya kuwezesha vijana wetu kuwamahiri katika ujenzi wa bomba na vilevile katika nyanja nyingine zozote ambazo zinahusiana na viwanda vinavyoanzishwa. Tunafanya kazi kwa karibu na Wizara ya Viwanda na Biashara wanatupatia mahitaji na Wizara yangu hatulali tunahakikisha kwamba tunaweka mazingira fanisi ya kuweza kuhakikisha kwamba tunatoa mafunzo yanayoendana mahitaji.
Mheshimiwa Spika, suala la ujenzi wa VETA katika wilaya na katika maeneo yetu limekuwa likuzungumzwa, sana na niseme kwamba zile VETA ambazo zilikuwa zijengwe kwa ufadhili wa ADB tangu mwaka 2015 kulikuwa na changamoto ambazo Wizara yangu ilikuwa inapatia uvumbuzi na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba zile VETA zote ambazo ziko katika mchakato wa kujengwa tutahakikisha kwamba katika mwaka huu wa fedha 2017/2018 tunazikamilisha ili tuweze kupata fursa ya kuweza kujenga maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, kwa uchache hayo ndiyo ambayo yalizungumziwa katika sekta ya elimu. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja kama nilivyosema ni bajeti nzuri ni bajeti ambayo inaenda kuondoa kero katika sekta ya elimu lakini pia ni bajeti ambayo itawezesha kuimarisha mifumo ya elimu. Nakushukuru.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia hoja za Kamati zetu tatu ambazo zimewasilishwa mbele yetu.
Mheshimiwa Spika, niwapongeze sana Wajumbe wote wa Kamati hizi tatu kwa uchanbuzi wao wa makini na niseme kwamba Wizara yetu imepokea mapendekezo, maoni na ushauri ambayo yametolewa na Kamati na tutaufanyia kazi ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea na kuchangia hoja hii naomba nimpongeze kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiongoza Nchi yetu kwa weledi, kwa kuchukua hatua mahususi za kuhakikisha kwamba analeta ustawi kwa Watanzania za kuhakikisha kwamba anatatua kero za muda mrefu katika baadhi ya maeneo ambayo yameguswa na taarifa ambazo zimewasilishwa na kamati zetu makini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, moja ya maeneo ambayo Kamati zimezungumzia ni madeni ya muda mrefu ya kwenye mifuko. Mfuko wa PSSF ulikuwa na deni la trilioni 4.600 ambalo lilitokana na deni la tangu mwaka 1999 ambapo Serikali ilipoanzisha mifuko iliamua kuchukua jukumu la kulipia wafanyakazi wote waliokuwa wameajiriwa kabla ya Julai 1999.
Mheshimiwa Spika, tangu Serikali imechukua uamuzi huo mwaka 1999 fedha hizo zilikuwa hazijawahi kulipwa mpaka Disemba 2021chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Nampongeza kwa dhati kwa kweli kwa sababu hatua hiyo imeimaarisha sana mfuko wetu wa PSSF. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, alikuta deni la mfuko wa PSSF la bilioni 731 na tayari Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekwishalipa kiasi cha shilingi bilioni 500. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alikuta pia kuna kero kubwa ya baadhi ya waajiri kutopeleka michango ya wastaafu ambayo imesababisha Wabunge kwa vipindi tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata Kiti chako umeshakuwa ukizungumzia suala hili la madeni marefu ya waajiri kwenye mifuko ambayo yanasababisha wazee wetu ambao wamefanya kazi wa weledi kulitumikia Taifa hili wanapata usumbufu wa kupata mafao yao. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo na aliyarudia maelekezo yake hata wakati wa Mei Mosi kwamba Wizara yetu ichukue hatua mahususi za kufuatilia madeni hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maelekezo hayo, lakini kama ambavyo hata Ripoti ya CAG kwenye Taarifa ya PAC imebainisha kwamba NSSF walikuwa na michango ya kiasi cha shilingi bilioni 408 ambazo zilikuwa bado hazijakusanywa kutoka kwa waajiri mbali mbali.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelekezo ya Mheshimiwa Rais na kwa kuzingatia kwamba hizi ni hoja za muda mrefu kwa kweli niseme kwamba CAG pamoja na Mheshimiwa Rais ametusaidia kufikiri nje ya box, ametuwezesha tumeunda Kamati Maalumu ya kufatilia fedha hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba nilijulishe Bunge lako Tukufu tangu tumepokea Ripoti ya CAG kutokana na kazi kubwa na nzuri ambayo imefanywa na timu mahususi ambayo tumeiunda tumefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 200.6 kati ya bilioni 408 zilizobaki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nafurahi kwamba Bunge lako kwa kweli linazungumza kwa hisia kwa uchungu kwa sababu haya ni maisha ya watu, haya ni maisha ya wazee wetu ambao ndiyo walituwekea misingi sisi leo tunajivuna katika Taifa hili ni kwa sababu kazi kubwa ya hawa wazee wetu mbao ni wastaafu waliifanya kwa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa namna yoyote ile ni lamiza Serikali tutahakikisha kupata fedha zilizobaki ambazo bado hatujakusanya tutahakikisha tunazifanyia kazi…
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Profesa Ndalichako kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jesca Msambatavangu.
TAARIFA
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa maelezo mazuri ya Mheshimiwa Waziri na task force aliyoiunda. Tunafahamu kwamba wamekaa kikao cha Mock LAAC kati ya Septemba na Oktoba ambacho kina-clear out zile hja zote za CAG kwa maelezo haya anayosema kwa task force waliyoiunda. Nataka kujua hiyo task force yake anasema imefanya kazi kubwa.
Mheshimiwa Spika, mpaka tunakuja sasa hivi kwa Taarifa hii CAG ametuambia wapo wafanyakazi wa Jiji la Tanga walichangishana milioni 8 wakailipa PSSSF ili wapate mafao yao. Kwanza nataka kujua hiyo task force yake inajua kwamba hilo linafanyika, na wamechukua hatua gani, na je? … (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Msambatavangu Taarifa ni moja. Ahsante sana
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, naomba hiyo task force yake imefanya nini kwenye masuala, na wanakusanya hiyo michango kwa Sheria ipi unakwenda kuchukua mchango kwa mtumishi au mstaafu na sio kwa mwajiri.
SPIKA: Mheshimiwa Profesa Ndalichako. Ameuliza swali kwa hiyo hulazimiki kujibu.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, sawa lakini kwa faida ya Wabunge taarifa hii ya Kamati bahati nzuri ime-acknowledge haya ambayo tunayasema. Mafanikio haya yaliyopatikana tungeyaripoti kwenye kamati na Kamati imeonyesha kwamba kulikuwa na deni la milioni 407 na ikasema kwamba wakati Kamati inafanya kazi yake jumla ya bilioni 194 zilikuwa zimekusanywa.
Mheshimiwa Spika, hatulali. Tangu kipindi cha Oktoba tulipotoka kwenye Kamati tumeshakusanya bilioni 6 nyingine. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kwenye eneo lingine.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Profesa Ndalichako kuna Taarifa nyingine kutoka kwa Mheshimiwa Ester Bulaya.
TAARIFA
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa LAAC, ni jeshi ulilonihamishia hivi karibuni nilikuwana napenda kumpa Taarifa Mheshimiwa Waziri kwamba mpaka juzi kwenye halmashauri michango ambayo haijapelekwa kwenye mfuko bilioni 260 ya watumishi wa Taifa hili. (Makofi)
SPIKA: Haya Waziri Mheshimiwa Profesa Ndalichako.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, dada yangu Ester Bulaya anawaisha shughuli. Anachokisema ndiyo ilikuwa sehemu ambayo naendelea na mchango wangu. Ni kweli kwamba katika halmashauri zetu kumekuwa na michango ambayo haijawasilishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama navyosema tupo kazini kuhakikisha kwamba hii kero ya muda mrefu tunaifanyia kazi. Katika michango ya halmashauri tuliunda na yenyewe hiki kikosi kazi kilikuwa kinashughulikia mfuko wa NSSF lakini na PSSSF tulikuwa na task force nyingine kwa sababu hawa ni watumishi wa umma ambao ilijumuisha Makatibu Wakuu wanaohusikia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika TAMISEMI naomba niripoti kwenye Bunge lako kwamba tayari…
SPIKA: Ngoja amalizie.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, tayari tumeingia makubaliano na halmashauri 81 ambazo zina madai ya muda mrefu na halmashauri hizi 81 zimetuwezesha kuwakomboa wastaafu 1425 ambao walikuwa na madeni ya muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia kwa faida ya Watanzania na kwa sababu hili jambo limekuwa ni kero ya muda mrefu nichukue nafasi hii kumwagiza Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF kuzifuatilia halmashauri ya 103 ambazo hazijaweka makubaliano ya namna gani wataleta michango yao. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, taarifa.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, nimuombe kaka yangu Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI Mchengerwa mchapakazi mtu bingwa nitakukabidhi orodha ya hawa watu wa TAMISEMI ili waweze kuleta fedha tuweze kulipa mafao wastaafu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Waziri umemaliza mchango wako kuna Mbunge alikuwa anataka kutoa Taarifa, itabidi, maana dakika yake ya mwisho ilikuwa imeshaisha lakini namna unavyosisitiza ni kama vile una jambo la dharura.
TAARIFA
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa mawasilisho ya Waziri. Kuna wastaafu ambao walishastaafu na wakaamua kwenda kukopa fedha kwengine ili waende walipe yale malimbikizo ambapo hawajapeleka pamoja na penati sasa wakishalipa ina maana wanalipwa fedha zao kutoka kwenye mfumo tayari unakuta hawasomeki.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa nampa Taarifa kwamba hiyo task force aliyoiunda ihakikishe kwamba inawafatilia wale wote ambao wameshatoa hela zao wakalipa yale malimbikizo kwa hela zao zingine kwa sasa walizopata na penati ili wawatafute wahakikishe kama wanalipa zile fedha zao kihalali warudishiwe zile hela ambazo walikopa kwa…
SPIKA: Haya ahsante sana. Mheshimiwa Waziri Ndalichako.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kwa faida ya Watanzania kwa sababu suala la wastaafu linaguza wazee wetu na wazee ni nuru ya Taifa. Kwa faida ya wazee wetu niseme kwamba utaratibu ambao upo Kisheria control number ya kulipa michango inapelekwa kwa mwajiri.
Mheshimiwa Spika, sasa kama kuna mwajiri ambaye anampa mtumishi ile control number ili akalipie tupate taarifa tutashughulikia kwa sababu utaratibu wa Kisheria upo kwa hiyo, tumepokea ushauri wake.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kama wanafahamu waniletee tutafanyia kazi, ni hilo tu. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia dakika tano nina mambo mengi lakini nitajitahidi kuongea kwa muda niliopatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuishukuru Kamati kwa taarifa lakini pia niwashukuru Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia na hususani maeneo ambayo yanahusu sekta ya elimu. Kwa hiyo, nitaanza moja kwa moja kuzungumzia suala la Mlimani City ambalo limezungumzwa sana kwenye Kamati lakini pia limechangiwa na Waheshimiwa Wajumbe wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba Serikali inatambua kwamba katika utekelezaji wa mkataba huu wa Mlimani City yapo maeneo ambayo kuna ukakasi katika utekelezaji, na tayari Serikali ilikwishaanza kuchukua hatua. Kama ambavyo Kamati imeeleza kwamba imekuwa hairidhishwi na mazungumzo kati ya mwekezaji na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ni kweli kulikuwa na ugumu hata wa hawa watu kukaa mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba tarai Serikali imekwishamlazimisha yule mwekezaji kufanya mazungumzo na mwekezaji amekiwshakubali na sasa hivi Serikali inaangalia ni nani awe kwenye timu ya majadiliano ili kuangalia vipengele vya mkataba ambavyo havitekelezwi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilihakikishie Bunge kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ina dhamira ya dhati ya kulinda rasilimali na ndiyo maana tulileta hapa Bungeni Sheria ya kulinda rasilimali yetu. Kwa hiyo, hili halina mjadala lazima Watanzania wanufaike na rasilimali yao, pale mwekezaji amechukua ardhi, kwa hiyo, lazima Serikali ihakikishe tunanufaika kama ambavyo imekusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kwamba miaka 13 sasa mradi wa hoteli ya nyota tatu bado haujaanza. Ni kweli kwamba bado haijaanza kujengwa, lakini niseme kwamba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam bado kinamkomalia mwekezaji na kwa sababu muda wa kumaliza uwekezaji ni Disemba, 2019. Tutahakikisha kwamba hilo suala tunaendelea kulisimamia kama ambavyo liko kwenye mkataba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme tu kwamba baadhi ya wachangiaji wamekuwa wakionesha kwamba huu mradi hauna manufaa kabisa. Naomba tu kwa ajili ya kuweka records vizuri; niseme tu kwamba hwa wa Mlimani city wamekuwa wakikilipa Chuo Kikuu cha Dar es salaam takribani bilioni mbili kwa mwezi na hata zile samani zilizowekwa katika hosteli mpya za Chuo Kikuu cha Dar es salaam zimenunuliwa kwa kutumia fedha ambazo zinalipwa na mwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile pia huu mradi umeweza kutengeneza ajira kwa Watanzania zaidi ya 1,600 ajira za moja kwa moja na ajira ambazo tunasema ni indirect employment. Pia hili eneo limekuwa sehemu ambayo watu wengi wamekuwa wakienda pale kupumzika na kupata burudani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa nataka kusema kwamba si kwamba hakuna manufaa kabisa, lakini kuna vipengele vya mkataba ambavyo havitekelezwi vizuri na hivyo Serikali tayari imeshamlazimisha yule mwekezaji ambaye alikuwa na ugumu wa kuzungumza na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nikuhakikishie kwamba chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano hakuna mtu yoyote ambaye anataka kuhujumu rasilimali yetu atakaebaki salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala ambalo kaka yangu Paroko Selasini alizungumzia kuhusiana na utekelezaji wa elimu bila malipo. Kwanza nimshukuru sana kwa sababu naona anaelewa vizuri waraka huu ambao ndio unatoa mwongozo wa namna ya kutekeleza elimu bila malipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda niseme tu suala ambalo amelizungumzia ambalo limeleta ukakasi. Baada ya sisi kukemea wale ambao walikuwa wanatoa michango ambayo ni kinyume na maelekezo hayo; sasa kuna watu wengine wanataka kupotosha, wanasema kwamba hata vyakula kwa wanafunzi wa kutwa hawaruhusiwi kuchangia hii si kweli, huu waraka umebainisha bayana majukumu ya wadau mbalimbali; na kwa ridhaa yako na kwasababu hili jambo ni muhimu kwa Taifa naomba uniruhusu nitolee ufafanuzi ili mkanganyiko unaondelea usiendelee kujitokeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, waraka unasema wazi kabisa, wajibu wa Mkuu wa Shule ni kuwapa maelekezo wazazi kuhusu aina na vifaa vinavyohitajika. mfano rangi ya kitambaa cha sare ya shule, idadi ya madaftari, vitabu na kadhalika. Kilichokuwa kinajitokeza baadhi ya walimu walikuwa wanalazimisha wazazi kununua sare shuleni kwa bei ambayo ilikuwa ni kubwa ukilinganisha na vile ambavyo mzazi angeweza kununua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye suala la chakula ambalo limeleta sintofahamu; huu waraka unasema wazi kabisa kwamba ni jukumu la mkuu wa shule kushirikiana na jamii katika kuweka utaratibu wa kutoa huduma ya chakula cha mchana kwa wanafunzi wa kutwa au kutoa chakula na husuma nyingine kwa wanafunzi wa bweni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye Kamati ya Shule pia inasema ni jukumu la Kamati ya Shule kushirikiana na jamii katika kuweka utaratibu wa kutoa huduma ya chakula kwa wanafunzi wa bweni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu ka kusema kwamba, hakuna mahali ambapo ama Serikali kwa kupitia waraka ama ufafanuzi wowote ambao umetolewa na viongozi umekataza wazazi kwa hiari yao kuweka utaratibu wa chakula na michango mingine shuleni. Kwa hiyo niwatake wakurugenzi na watu wote ambao wanasimamia utaratibu huu kuhakikisha kwamba wanazingatia huu waraka kama ambavyo umeainishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2016
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nianze moja kwa moja kwa kusema kwamba naunga mkono hoja hii ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.3 wa mwaka 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajielekeza zaidi katika sehemu ya marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Niseme tu kwanza haya mapendekezo ya marekebisho yamekuja kwa kuchelewa. Nitumie fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia pamoja na Kamati ya Sheria na Katiba kwa mchango mzuri ambao kimsingi umelenga katika kuboresha hoja hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ya kuleta marekebisho haya ni kuongeza ufanisi katika urudishaji wa mikopo na kufanya Mfuko wa Mikopo kuwa himilivu na endelevu ili kuwawezesha Watanzania wengi ambao wana uhitaji wa mikopo waweze kuendelea kunufaika na mikopo ambayo imewekwa kwa lengo la kuwasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia vipengele ambavyo vimechangiwa na wazungumzaji wengi. Kwanza kabisa, jambo ambalo limezungumziwa sana ni suala la muundo wa Bodi ya Elimu ya Juu. Niseme tu kwamba kazi ya Bodi ni kuiongoza na kuisimamia ile taasisi. Kwa hiyo, tukielekeza zaidi uchaguzi wa Bodi katika uwakilishi wakati mwingine kuna mambo mengine ya msingi ambayo yanaweza yasitekelezeke kwa sababu kazi na majukumu ya Bodi yameainishwa katika sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali imezingatia maoni na mapendekezo ya wadau na katika Schedule of Amendment ambayo tunaileta tumekubaliana na pendekezo la kuongeza Mjumbe kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar na vilevile tunaongeza mjumbe kutoka NACTE. Kwa hiyo, suala hilo limezingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kulikuwa na suala la kuzingatia uwiano wa gender. Mimi Waziri ambaye pia ni mwanamke siwezi kuwaangusha akinamama wenzangu, lakini pia hiyo tumeilinda katika kuiweka kwenye sheria ili anapokuja Waziri mwingine yeyote ahakikishe kwamba uteuzi wa Bodi unazingatia gender. Kwa hiyo, hilo suala tumelizingatia na lipo katika Schedule of Amendment ambayo tunaleta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo limezungumzwa sana ni muda wa marejesho ya fedha baada ya mwanafunzi ama kuhitimu mafunzo yake au kusitisha mafunzo kwa sababu mbalimbali. Serikali ilikuwa imependekeza kwamba mwanafunzi aanze kurudisha mkopo wake mara moja kwa sababu tunatambua kwamba pamoja na tatizo la ajira lililopo, lakini wapo wanafunzi wengine ambao mara baada ya kumaliza mafunzo yao huwa wanapata ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusikiliza mapendekezo na maoni kutoka kwa Kamati, kwa waliochangia kwa maandishi na waliozungumza, Serikali imekubaliana na pendezo la kuweka muda wa mwaka mmoja tangu kumaliza lakini haimnyimi fursa yule ambaye atakuwa na uwezo wa kurejesha moja aweze kurejesha. Kwa hiyo, muda wa marejesho utakuwa ni mwaka mmoja lakini kwa yule ambaye atabahatika kupata kazi mapema arejeshe hata kabla ya huo muda wa mwaka mmoja.
Mheshimiwa mwenyekiti, eneo lingine lililokuwa linazungumziwa ni eneo la kuwapa adhabu waajiri kwa kutowasilisha makato. Naomba itambuliwe kwamba makato ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ni sehemu ya makato kama yalivyo makato mengine ya kisheria. Hivyo basi tunavyosema kwamba mtu ambaye hatarejesha atapewa adhabu ni kama ambavyo inakuwa kwenye mfuko wa NSSF na LAPF. Kwenye hii mifuko ya kijamii mtu ambaye hapeleki makato kwa wakati anapewa adhabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo siyo kuwakomoa waajiri ni kuwakumbusha wajibu wao. Kwa kuzingatia hilo hata ile adhabu tuliyokuwa tumependekeza tumeipunguza, tumeiacha kama ambavyo ilikuwa kwenye sheria hii. Kwa hiyo, katika Schedule of Amendment tunasema kwamba adhabu lazima iwepo ili kuwakumbusha waajiri kwamba nao wana wajibu wa kushirikiana na Serikali kuhakikisha kwamba hii mikopo inarejeshwa. Kwa hiyo, katika Schedule of Amendment, Ndugu yangu Mheshimiwa Riziki tumebadilisha, adhabu itakuwa ni shilingi milioni moja tu. Kwa hiyo, tunaomba waajiri nao wajione kwamba wana wajibu wa kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumzwa na ndugu zetu Kambi Rasmi ya Upinzani linahusu suala la Mheshimiwa Rais kutoa takwimu za fedha ambazo zinatofautiana na zile ambazo nilizitoa. Mheshimiwa Rais alizungumzia shilingi bilioni 80 kama fedha ambazo zimetolewa na Serikali kwa ajili ya posho ya kujikimu wanafunzi mimi nilizungumzia shilingi bilioni 120 nikiwa nimejumuisha kiasi cha shilingi bilioni 40 ambazo zimetolewa katika financial year hii kwa ajili ya tuition fees za vyuo. Hata katika taarifa yao wanazungumzia kwamba kuna madeni kwa vyuo ya shilingi bilioni 60, tunayalipa na ndizo hizi shilingi bilioni 40 ambazo tayari Serikali imekwishatoa kwa vyuo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, taarifa yangu ilikuwa inajumuisha kiasi cha shilingi bilioni 80 ambazo tumezitoa mahsusi kwa ajili ya wanafunzi pamoja na shilingi bilioni 40 ambazo tumezitoa kwa ajili ya tuition fee. Kwa hiyo, hakuna kugongana kwa taarifa, inategemea mtu anarejea kitu lakini hakuna kupishana kwa taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia suala ambalo limezungumzwa hapa kwamba Serikali inakuwa kama inafanya biashara kwenye mikopo. Serikali haifanyi biashara. Mikopo imetolewa kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wenye uhitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata mapendekezo ya kiasi ambacho tumeleta mbele ya Bunge lako cha 15% ni kidogo tu kwa sababu katika utumishi wa umma, mtumishi anaweza akakatwa mpaka abaki na moja ya tatu (1/3) ya kipato chake. Serikali hatukutaka kwenda huko, tunakata 15% tu anabaki na asilimia 85. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna dhana kwamba tunafanya biashara, tunatengeneza faida kwa kuwakata wanafunzi. Hakuna riba inayotozwa kwenye mikopo isipokuwa kuna tozo la kuchelewesha. Sasa kama hutaki kukatwa hiyo tozo lipa kwa wakati hakuna mtu atakayekudai, lipa kwa wakati ili watoto wengine waendelee kunufaika. Kwa hiyo, Serikali haifanyi biashara ila tunawakumbusha vijana wanaopata hii siyo ruzuku, ukikopa mkopo lazima urejeshe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna dhana hapa kwamba mwanafunzi mwingine anaweza akaacha masomo kwa sababu ameugua. Hayo yote yameelezwa wazi kwenye kanuni kwamba mwanafunzi akifariki au akiugua nini kifanyike. Kwa hiyo, ni masuala ambayo Serikali inatambua kwamba kila mtu anaweza akawa na matatizo na yote hayo yamekwishazingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ufafanuzi huo, niseme tu kwamba, naomba Waheshimiwa Wabunge wote tuunge mkono mapendekezo haya ambayo kwa kweli yana lengo jema kabisa la kuhakikisha kwamba vijana wengi wananufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo suala alilozungumzia Mheshimiwa Ester Mmasi kuhusiana na vyuo ambavyo havina sifa. Nitumie fursa hii kutangaza rasmi kwamba kama kuna vyuo vinaendesha programu zozote ambazo ama hazitambuliki na Professional Bodies mwaka huu wa fedha itakuwa ndiyo mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunavyozungumza ziko timu za wataalam zinakagua vyuo vyote. Kwa hiyo, kama kuna programu zozote ambazo zinaendeshwa kinyume na taratibu tutazifungia. Pia kama kuna chuo kikuu ambacho kilianzishwa na hakina wataalam mwaka huu wa fedha ndiyo mwisho, hii hadithi hatutaisikia tena. Tunaomba Waheshimiwa Wabunge mtuunge mkono katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuongeza udahili katika vyuo vya umma hilo tutalizingatia na hasa katika fani ya afya ambapo Chuo Kikuu cha Mloganzila tumeshakamilisha teaching hospital. Serikali itafanya jitihada kuhakikisha kwamba angalau katika mwaka wa masomo unaokuja 2017/2018, wawepo wanafunzi angalau ile hospitali inapotumika na mafunzo yawe yanaendelea ili tuongeze wigo wa kufundisha madaktari kwa sababu vyuo vya madaktari vimekuwa vichache. Kwa hiyo, ushauri huo utazingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo limezungumziwa ni kwamba, Serikali bado haijapanga mikopo kwa wanafunzi wengi na kwamba mpaka sasa hivi ni wanafunzi 21,000 tu ndiyo wamepata mikopo. Naomba niseme kwamba tangu nilipotoa ile taarifa yangu zoezi hili la kuendelea kupanga mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza limekuwa likiendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi jumla ya wanafunzi 25,228 wa mwaka wa kwanza wamekwishapangiwa mikopo. Tofauti na nilivyokuwa nimetoa taarifa wiki iliyopita hadi leo kiasi cha Sh. 73,153,910,172 zimekwishatumwa na zoezi bado linaendelea kwa sababu kulikuwa na wanafunzi wengine ambao wanadahiliwa kupitia NACTE ambapo majina yao hayakufika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hakika kabisa baada ya ufafanuzi huu, Waheshimiwa Wabunge wote wataunga mkono hoja hii ili tuongeze tija katika makusanyo ya mikopo ili vijana wetu wasiendelee kutaabika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019; na Mapendekezo ya Serikali Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza katika siku ya leo. Napenda kuanza kwa kutoa pongezi za dhati kwa Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mpango, pamoja na Naibu Waziri, Mheshimiwa Kijaji pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu Dkt James Doto.
Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa nimpongeze kaka yangu Dkt. Philip Mpango, kwa uwasilishaji wa umahiri kabisa wa bajeti hii, alitumia saa moja na dakika arobaini na tano lakini hatukuchoka. Tunampongeza sana na naunga mkono hoja hii kwa sababu bajeti hii imeandaliwa kwa lengo la kutatua kero za Watanzania.
Mheshimiwa Spika, katika mchango wangu nitapenda kuzungumzia masuala machache kwa sababu ya muda na ningeanza na suala ambalo wachangiaji wengi walikuwa wakilizungumzia kwamba Serikali haipeleki fedha kwamba tunakuwa tunapitisha hapa bajeti lakini mwisho wa siku Serikali haipeleki fedha. Pia wengine walienda mbali na wakawa wanasema kwamba hii Serikali inaleta bajeti hewa.
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze kwa dhati Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ambaye kwa kweli ni Raisi shupavu, ni Rais ambaye anafanya vitu kwa vitendo, akiahidi anatekeleza.
Mheshimiwa Spika, pongezi hizi nazitoa kwa sababu kwenye sekta ya elimu fedha zimekuwa zikija kama ambavyo zimepangwa. Wizara ya Elimu ilipangiwa jumla ya trilioni moja na bilioni mia tatu thelathini na sita na mpaka sasa Serikali imeshatoa trilioni moja na bilioni mia moja ishirini na tisa.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imekuwa ikitekeleza ahadi yake ya elimu bila malipo kila mwezi bila kukosa, fedha kwa ajili ya elimu bila malipo zimekuwa zikienda bilioni ishirini kwa wakati. Pia Serikali ilikuwa imetenga bilioni 427.54 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na mpaka sasa ninapozungumza tayari Serikali imekwisha pokea shilingi bilioni 427.44 sawa na asilimia mia moja ya fedha zote ambazo zilitengwa.
Mheshimiwa Spika, kutokana na upatikanaji huu wa fedha katika sekta ya elimu Serikali imeweza kufanya mambo mengi. Tumeweza kujenga madarasa kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa nafasi za elimu pamoja na kuboresha mazingira ya elimu ambapo jumla ya madarasa 1907 yamejengwa lakini na matundu ya vyoo elfu nne mia tano na moja.
Mheshimiwa Spika, na nichukue nafsi hii kuwapongeza kwa dhati, umoja wa Wanawake Wabunge kwa uchangishaji wa vyoo bora kwa mtoto wa kike ambao kwa kweli inaungana na juhudi za Serikali katika utoaji wa elimu bora tunashukuru sana.
Mheshimiwa Spika, pia tumeweza kujenga mabweni 338, tumefanya ukarabati wa shule kongwe 45 na vilevile ukarabati wa vyoo vya walimu 17. Vile vile kutokana na upatikanaji wa fedha hizi Serikali imeweza kuendelea kuimarisha tafiti katika nchi hii. Serikali ilitoa shilingi bilioni 3.2 kwa ajili ya miradi nane ya tafiti na hii miradi imelenga katika kuimarisha viwanda pamoja na kilimo.
Mheshimiwa Spika, jana tulikuwa tunazungumzia masuala ya kilimo, tunajua kwamba kilimo ndio kinabeba Watanzania na kwa hiyo Serikali imetoa bilioni 3.2 ambazo ni kwa ajili ya miradi minane ya utafiti. Kwa mfano na taasisi inayoshughulika na magonjwa ya binadam, (NIMR) imepata fedha kwa ajili ya kutengeneza maabara kwa ajili ya dawa, pia Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) kimepata fedha pia kwa ajili ya masuala ya dawa.
Mheshimiwa Spika, hatujasahau na hapa Mkoa wa Dodoma Makao Makuu tumetoa fedha kwa ajili ya kuimarisha utafiti wa zao la zabibu. Kwa hiyo tumetoa fedha kwenye hii Taasisi ya Utafiti wa Mifugo ya TALIRI kwa ajili ya kuzalisha mifugo.
Mheshimiwa Spika, vile vile tumetoa fedha kwa ajlili ya utafiti wa kuboresha mitambo ya kuzalisha mvinyo katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Makutupora. Haya yote nayazungumza kwa uchache tu kuonesha kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali ambayo inatenda kwa vitendo na hii yote imetokana na bajeti ambayo imetengwa.
Mheshimiwa Spika, nizungumzie kwenye Taasisi za Elimu ya Juu, Serikali hii imefanya mambo makubwa sana kwenye hizi Taasisi za Elimu ya Juu. Ukienda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sasa hivi inajengwa maktaba ya kisasa na ya kipekee katika Bara la Afrika, ambayo itakuwa na uwezo wa kuweka wanafunzi 2,500 kwa wakati.
Mheshimiwa Spika,ile vile Tume ya Mionzi ya Taifa inajenga Maabara kwa ajili ya kupima mionzi na maabara hiyo ikikamilika kwa kweli itakuwa ni maabara ya kipekee katika Ukanda wa Afrika. Tayari vifaa kwa ajili ya maabara hizo vimekamilika. Nashukuru kwamba Serikali imeshatoa fedha ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya hii Tume na zinaendelea kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, katika suala la kusema kwamba Serikali inatenga fedha haizitoi; kwa sababu ya muda siwezi kumaliza taasisi, lakini niseme kwamba ukienda Mzumbe, ukienda Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, ukienda Mbeya Chuo cha Utafiti, ukienda Arusha Technical utakuta mambo mengi yanafanyika.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo lilikuwa linazungumziwa katika michango ni namna gani Serikali inaimarisha elimu ya ufundi. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kama ambavyo imeainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano na ambao umekuwa
ukitekelezwa mwaka hadi mwaka, Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuhakikisha kwamba inaongeza ujuzi kwa wananchi katika nyanja mbalimbali, maana kuna ujuzi wa chini, kuna ujuzi wa kati na ujuzi wa juu.
Mheshimiwa Spika, hivi tunavyoongea katika Chuo cha Ufundi Arusha Karakana zote zinabadilishiwa vifaa ili ziweze kutoa mafunzo ya kisasa. Kuna kontena kumi na sita ambazo zimefungwa, tayari vifaa vile vipo kwa ajili ya kufungwa, kwa hiyo Serikali inaendelea kuimarisha.
Mheshimiwa Spika, kuna suala la Walimu, kwa sababu elimu si majengo tu, ni pamoja na Walimu. Serikali imekuwa ikiendelea kuimarisha utoaji wa mafunzo ya ualimu. Sasa hivi tunafanya upanuzi wa vyuo vyetu vya ualimu; ukienda kule Kitangali utakuta Chuo cha Ualimu cha kisasa kimejengwa, nenda Mkuguso, nenda Ndala, nenda Shinyanga utaona kazi nzuri ambayo inafanywa na Serikali ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Spika, Serikali hii ambayo Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ni Rais ambaye anaangalia wanyonge hajasahau wanafunzi wenye mahitaji wenye mahitaji maalum. Kwa hiyo katika mambo ambayo tunafanya tumeendelea pia kuimarisha utoaji wa elimu kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maaalum.
Mheshimiwa Spika, hivi ninavyozungumza ujenzi wa shule maalum kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum inaendelea katika Chuo cha Ualimu Patandi. Sambamba na ujenzi huo lakini Serikali pia imepanga kununua vifaa kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum; na tayari tumeshatoa maelekezo kwamba katika shule zote katika miundombinu yote ya kielimu inayojengwa lazima tuzingatie mahitaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niseme tu kwamba niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuiunge mkono bajeti ya Serikali kwa sababu ni bajeti ambayo italeta maendeleo, ni bajeti ambayo inakwenda kutatua kero za wananchi na ni bajeti ambayo inatusaidia hata sisi
Waheshimiwa Wabunge kutekeleza ahadi ambazo tumezitoa kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nategemea kwamba jioni kama ulivyoelekeza Wabunge wote watajitokeza wapige Kura ya Ndiyo katika bajeti hii ili wanafunzi wa elimu ya juu waendelee kupata mikopo ambapo tunategemea kutoa mikopo kwa wanafunzi 123,000.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naunga mkono hoja, lakini kwa heshima kubwa nawaomba Waheshimiwa Wabunge wote tupige Kura ya ndio. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Ningependa kuanza kwanza kabisa kwa kusema naunga mkono hoja hii na napenda kuipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo wanafanya katika kuratibu shughuli za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchangia katika maeneo machache. Kwanza kuna suala la mafunzo ya ufundi stadi ambalo limeongelewa na Waheshimiwa Wabunge wameonesha dhamira au nia ya kuona elimu ya mafunzo ya ufundi stadi inaendelea kuimarishwa katika maeneo yao. Niseme tu kuwa Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba inaongeza fursa na nafasi za mafunzo ya ufundi stadi na kama ambavyo wiki iliyopita tulikuwa na Mheshimiwa Rais kule Namtumbo tunazindua Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi Namtumbo. Pia kuna chuo vingine vya ufundi stadi ambavyo tunaendelea na ujenzi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Wilaya ya Ileje, Chato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunaendelea na ujenzi wa VETA za Mikoa; Mkoa wa Kagera, Simiyu, Mkoa wa Njombe pamoja na Mkoa wa Geita. Pia Serikali imefanya ukarabati wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) na mpaka sasa tumeshafikia vyuo 20 kati 34 na katika bajeti ya mwaka huu ambapo naamini Waheshimiwa Wabunge wataiunga mkono, tunategemea kufikia vyuo 34 vilivyobaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limezungumziwa ni suala la udhibiti ubora wa shule. Ningependa kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali iko makini sana katika suala la udhibiti ubora kwa sababu tunaamini kwamba Wadhibiti Ubora wa Shule ndio jicho la Serikali katika kutuhakikishia kwamba tunafikia malengo yetu katika sekta ya elimu. Kwa hiyo Serikali inaendelea kuiangalia idara hiyo kwa makini zaidi na vile vile tumeendelea kuiimarisha katika kuhakikisha kwamba inapata vitendea kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha uliopita, Serikali ilitoa magari 45 kwa ajili ya ofisi mbalimbali za udhibiti ubora wa shule, lakini tumeendelea kuiimarisha katika vitendea kazi kama kompyuta. Pia tumeangalia namna Wadhibiti Ubora wanavyofanya kazi kwa sababu zamani Wadhibiti Ubora walikuwa wamekaa kipolisi polisi zaidi. Wanaenda kuwatisha Walimu badala ya kwenda kuwapa support yaani kwa maana kwamba kuwaonesha upungufu wao na kufanya kazi. Tumebadilisha mfumo na tumetengeneza kiuzi cha udhibiti ubora ambacho lengo ni kwenda kuboresha mifumo ambayo inajitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile limezungumziwa suala la vifaa vya kufundisha hasa katika shule za sekondari. Serikali ya Awamu ya Tano imefanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba maabara ambazo zilikuwa zimeanzishwa na wananchi zinapata vifaa. Kwa hiyo jumla ya shule za sekondari 1,696 zimeweza kupata vifaa vya kufundishia masomo ya sayansi ambayo yapo kwenye muhtasari kuanzia kidato cha kwanza mpaka kidato cha sita, ni vifaa ambavyo vinajitosheleza. Niendelee kuwahakikishia Wabunge kwamba kwenye sekta ya elimu na hasa kwenye masuala ya Mafunzo ya Ufundi stadi ambayo tunafanya na Ofisi ya Waziri Mkuu, tunakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, ningependa kuzungumzia suala la elimu maalum ambalo pia nalo tunalifanya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu. Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaendelea kupata elimu yao katika mazingira rafiki zaidi. Kwa hiyo, tuna progamu ya kusambaza vifaa na visaidizi kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum na tutaendelea kufanya hivyo kwa sababu tunaamini kwamba elimu ni haki ya kila mtoto na hata yule ambaye ana changamoto anastahili kupata elimu katika mazingira mazuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nianze kwa kusema naunga mkono hoja kwa sababu hotuba hii imeeleza kwa ufasaha mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano na imeainisha kazi ambayo inakwenda kufanyika katika mwaka 2020/2021. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya katika Serikali hii.
Pia napenda kuwapongeza Mawaziri katika Ofisi yake, Dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama na Mheshimiwa Angellah Kairuki, hakika wanaonyesha mfano namna ambavyo wanawake wanafanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia katika Sekta ya Elimu na niseme kwamba michango yote tumeipokea. Kwa sababu ya muda na kwa kuzingatia kwamba ndiyo mara yangu ya kwanza kuongea Bungeni tangu Benki ya Dunia ilipopitisha mkopo wa shilingi milioni 500, nitumie nafasi hii kutoa shukurani za dhati kwa Benki ya Dunia kwa kuidhinisha mkopo huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, unafahamu namna ambavyo mkopo huu ulileta sintofahamu na hata kuna kipindi ambapo katika Bunge lako kulikuwa na mjadala kuhusu suala hili. Tunashukuru kwamba baada ya majadiliano wameweza kuzipitisha. Niseme kwamba fedha hizi zinakwenda kuimarisha elimu ya sekondari, zinakwenda kuondoa vikwazo na hasa kwa watoto wa kike kuhakikisha kwamba wanapata elimu iliyo bora. Mradi huu utakwenda kunufaisha watoto wasiopungua 6,500,000 na utatoa kwa elimu kwa watoto wote wa kike na wa kiume bila ubaguzi wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mradi huu utasimamiwa na Wizara ya Elimu ambayo ndiyo ina dhamana ya kusimamia elimu hapa nchini na tutahakikisha kwamba tunasimamia mradi huu kwa kushirikiana na wadau wote muhimu.
Kwa hiyo, niwahakikishie Watanzania kwamba Serikali iliomba huu mkopo kwa sababu ina dhamira ya dhati ya kuboresha elimu. Kwa sababu sasa mkopo umeidhinishwa, Serikali inakwenda kuutekeleza kama ambavyo tumekubaliana na Benki ya Dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu na wakati mwingine huwa unakemea hizi tabia; yapo mambo ambayo yameshaanza kuleta majadiliano kuhusiana na huu mkopo na ndiyo maana nimeona mimi mchango wangu niutumie katika kuleta ufafanuzi. Mradi huu unatekelezwa katika mfumo wa “Lipa Kulingana na Matokeo” kama ambavyo Wabunge wote mnafahamu mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo tulionao. Tunao uzoefu, tunayo dhamira, tunao uwezo wa kuhakikisha kwamba tutatekeleza mradi huu kulingana na mipango ambayo tumeiweka ili tuweze kufikia malengo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwahakikishie Watanzania, nia yetu iko pale pale, uwezo wetu uko pale pale, tunakwenda kuimarisha elimu yetu na tutahakikisha kwamba tunawashirikisha wadau wote katika hatua zote ili kuhakikisha tunafanikiwa.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuzungumzia mradi huu ambao utakuwa na mazingira ambayo ni jumuishi na rafiki kwa watoto wetu wote, nizungumzie na mimi janga ambalo liko kwenye nchi yetu na dunia kwa ujumla, suala la virusi vya Corona.
Mheshimiwa Spika, tunafahamu shule zetu zimefungwa, wanafunzi wako nyumbani. Hivyo basi, imekuwa kwa kweli ni jambo ambalo kidogo linaathiri hali yetu ya elimu kama ambavyo linaathiri sekta nyingine. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuendelea kusisitiza na katika mchango wa Wabunge, kuna suala ambalo lilijitokeza kwamba kuna baadhi ya wazazi ambao watoto wao wanaendelea kwenda tuition.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekataza mikusanyiko isiyokuwa ya lazima na Serikali ilifunga shule kwa sababu ya kuwaweka watoto katika mazingira salama ili wasiwe na mikusanyiko. Kwa hiyo, natumia nafasi hii kusema kwamba tuition zote zinazofanyika sasa hivi ni batili. Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya wahakikishe kwamba wanasimamia maelekezo ya Serikali. Mtu yeyote anayeendesha tuition, ni batili, achukuliwe hatua inayotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kwa kutambua kwamba Wanafunzi wako nyumbani na wanahitaji kuendelea kuwa wanapata elimu hata wakiwa nyumbani, tunayo huduma ya maktaba ambayo inatolewa na Taasisi ya Elimu Tanzania ambayo kiutaratibu ili uweze kupata vitabu katika huduma hiyo ilikuwa unapaswa kulipa. Sasa kwa kutambua kwamba wanafunzi wamefunga shule, Serikali inatoa huduma ya upatikanaji wa vitabu vyote kuanzia Elimu ya Awali, vya Shule ya Msingi, Shule ya Sekondari kuanzia O- level na A-level bila malipo yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwasihi sana wanafunzi wote, huko waliko majumbani kwao watumie muda wao kusoma vitabu ambavyo Serikali inawapa access bila gharama yoyote badala ya kwenda kuzurura mitaani na kujiweka katika hatari ya kuweza kupata maambukizi ya virusi vya corona. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, narudia kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja za kamati mbili ambazo ziko mezani.
Kwanza nianze kwa kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini na kuniteua kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, inayoshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Rais kwamba nitafanya kazi yangu kwa bidii yote na kwa uadilifu wa hali ya juu ili kuhakikisha kwamba malengo ya Wizara hii yanatekelezwa kwa ufanisi wa hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kupongeza Mheshimiwa Spika na Naibu Spika kwa kuchaguliwa kuongoza muhimili huu muhimu lakini pia niwapongeze wenyeviti wa kamati hizi mbili kwa sababu nao wamechaguliwa hivi karibuni nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo naomba niishukuru kamati zote mbili kwa taarifa zao nzuri ambazo kwa hakika zimesheheni maoni na mapendekezo mazuri ambayo yanaonyesha jinsi gani wajumbe wa kamati hizi wana uweledi wa hali ya juu na wamechambua kwa kina masuala ambayo yanahusiana na kamati na mimi nazungumzia hususan yanayohusiana na eneo la Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana na kama alivyosema jirani hapa kimsingi yote ambayo wameyashauri ni mambo ambayo yanakwenda kujenga kuongeza tija katika utendaji wetu wa kazi kwa hiyo niseme kwamba tumeyapokea na tuwahakikishie kwamba yote tutayafanyia kazi kwa ukamilifu na tutatoa taarifa ya namna ambavyo tumefanyia kazi maoni na mapendekezo ya kamati nawashukuru sana wajumbe kwa kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nizungumzie baadhi ya maeneo kwa uchache katika taarifa ya kamati ya Katiba na Sheria wamezungumzia suala la kiwanda cha viatu kule Kilimanjaro na kiwanda hiki ni muhimu kwa sababu kinachochea upatikanaji wa soko la ngozi kwa wafugaji wetu ina maana kwamba kadri kitakavyofanya vizuri basi tutaongeza na kipato kwa wafugaji wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali inaona umuhimu wa kiwanda hicho na tunashukuru kwamba wametushauri tuendelee kuongeza masoko jambo hilo tunalifanyia kuhakikisha kwamba tuna masoko endelevu na kwa kuanzia kiwanda tayari kimetangaza nafasi za mawakala watanzania ambao wako tayari kuwa mawakala wa kuuza bidhaa zinazotengenezwa na kiwanda hicho viatu pamoja na bidhaa nyingine za Ngozi. Kwa hiyo. niwahamasishe kwamba wachangamkie hiyo fursa kwa sasa hivi tunafanya uchambuzi wa maombi yaliyopokelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile tumeshauriwa tuhakikishe kwamba tunajitangaza kupitia maonyesho hilo Ofisi ya Waziri Mkuu itasimamia kuhakikisha kiwanda kinatumia fursa zote za maonyesho zinazokuwepo lakini hata kuja hapa kwa Waheshimiwa Wabunge kwa sababu Waheshimiwa Wabunge ni jeshi kubwa wanawakilisha watanzania. Kwa hiyo, akifahamu vizuri bidhaa hizi watakuwa mabalozi wazuri wa kusaidia kututangazia, kwa hiyo, hilo tutalizingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini eneo ambalo limezungumziwa pia sana ni kuhusiana na hii 4% inayokwenda kwa vijana fedha za halmashauri pamoja na mfuko wa maendeleo ya vijana kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imeshauri kwamba Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na TAMISEMI tufanye ufuatiliaji wa hizi fedha zinazoenda kwa vijana. Hilo nalipokea na niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba hili lilikuwa ni agizo la Mheshimiwa Rais alipoongea na vijana kwenye uwanja wa Nyamagana siku ya tarehe 15 Juni, 2021 kule Jijini Mwanza alizungumzia suala hili fedha zinazotolewa kwa vijana kwamba Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa vijana lakini wakati mwingine vijana wanakuwa hawana taarifa sahihi za hizi fedha kwa hiyo wanakuwa hawanufaiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia alihoji kwamba wale wanaonufaika wanafanyaje kufanya marejesho ili vijana wenzao waweze kunufaika. Ni dhahiri kwamba kauli ya Mheshimiwa Rais inatutaka sisi ambao tunahusika moja kwa moja na kusimamia vijana pamoja na TAMISEMI ambao inahusika na kutoa hizi fedha tufanye ufuatiliaji na kutoa miongozo na hata kutoa elimu kwa wale wanaopata hizi fedha tutoe elimu ya ujasiriamali na mafunzo ili kuhakikisha kwamba zinakuwa na tija na zinazunguka ili ziweze kwenda kuwakopesha vijana wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo jingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelizungumzia ni changamoto ambazo baadhi ya vijana wanapata kuhusiana na fursa ambazo zinatolewa za kukuza ujuzi. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametupatia bilioni 9 kwa ajili ya kukuza ujuzi na kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge baadhi ya vijana wanapata changamoto kwa sababu wako mbali niwaambie kwamba Serikali ni sikivu jambo hilo tumeshaanza kulichukulia hatua wale wanaofanya mafunzo ya kilimo kitalu nyumba tunawalipa shilingi elfu 10 kwa siku kuwawezesha kwenda kuhudhuria na wale ambao wanapata mafunzo ya uzoefu kazini tunawalipa 150,000 kwa mwezi na tutaendelea kufanyia kazi changamoto hii na kuangalia namna bora zaidi ya kuhakikisha tunafanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimalizie kwa kuunga mkono hoja kwa kamati zote mbili nashukuru sana kwa ushauri tutaufanyia kazi. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja iliyoko mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuipongeza Kamati kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya na niseme kwamba naunga mkono hoja za Kamati zote mbili, Kamati ya Katiba na Sheria pamoja na Kamati ya Sheria Ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imetoa ushauri katika maeneo mbalimbali, lakini na Waheshimiwa Wabunge pia ambao wamechangia nao wametoa maoni yao. Kimsingi kama nilivyosema Serikali imepokea maoni yote na tunaunga mkono maazimio ambayo yametolewa na hizi Kamati na tunapenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali itayafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze kwa kifupi katika baadhi ya maeneo; nianze na kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Taarifa inaonesha kwamba hadi kufikia mwezi Februari, 2022 Serikali ilikuwa imetoa kiasi cha shilingi milioni 205 kati ya shilingi bilioni moja ambazo zilikuwa zimetengwa. Naomba nichukue nafasi hi kuriarifu Bunge lako tukufu hadi kufikia Juni, 2022 fedha zote shilingi bilioni moja ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii zilikuwa tayari zimekopeshwa kwa walengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la utoaji wa elimu, hilo tutalizingatia na nichukue nafasi hii kuwafahamisha Vijana kwamba mwongozo wa namna ya kupata mikopo unapatikana katika halmashauri zote nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwongozo huu tumeuboresha; kwanza, tumeongeza kiwango cha juu cha kutoa mkopo kutoka shilingi milioni 10 hadi shilingi milioni 50; lakini pia tumelegeza masharti kwamba mtu anaweza kukopa kama kikundi au anaweza kukopa kama mtu mmoja, mmoja. Kwa hiuyo, yote hiyo ni kuwawezesha vijana ambao ni wabunifu, mwingine anaweza akawa na ubunifu wa peke yake ambapo ukimlazimisha mpaka awe na kikundi inakuwa ni vigumu kukidhi hayo masharti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge pamoja na Kamati wamelizungumzia ni suala la mwongozo wa utekelezaji wa ujumuishaji na uimarishwaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu. Serikali imepokea maoni kwamba upo umuhimu wa kutoa elimu na kuhakikisha kwamba taasisi zote za Serikali na zisizo za Serikali zinatekeleza kikamilifu mwongozo wa utoaji wa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la upatikanaji wa takwimu, ni suala la msingi na Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwaka 2022 iliweka kipengele mahususi kwa ajili ya kupata takwimu za watu wenye ulemavu hapa nchini. Tunaamini kwamba Taasisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) ikikamilisha uchakati wa takwimu za sensa tutapata idadi kamili ya watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tunashirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tunaandaa mfumo ambao utakuwa ni endelevu ambao tutakuwa tunaweka taarifa za watu wenye ulemavu kama Kamati ilivyoshauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni Sera ya Taifa ya Vijana. Kama nilivyosema maoni yote tumeyapitia lakini kwa taarifa tu, napenda niliarifu Bunge lako kwamba mchakato wa kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Vijana unaendelea vizuri na tumefikia sasa hatua ya kupokea maoni kutoka kwa wadau. Kwa hiyo, tutasimamia na kuhakikisha kwamba hadi kufikia Disemba yaani mpaka tutakapokuwa tunakuja kutoa utekelezaji wa maazimio haya itakuwa imetekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda naomba nikushukuru tena kwa nafasi na niseme kwamba naunga mkono maazimio na kuhakikisha kwamba tutayasimamia kuhakikisha utekelezaji wake, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyoko mezani, kwanza nianze kwa kusema kwamba naunga mkono hoja hotuba ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambayo imewasilishwa hapa mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuchangia tu jambo moja ambalo limejitokeza katika michango ya Waheshimiwa Wabunge kuhusiana na suala la wastaafu. Kwanza wamezungumzia suala la wastaafu kuchelewa kupata malipo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niliambie Bunge lako tukufu kwamba, mifuko yetu imeweza kulipa mafao kwa wastaafu kati ya kipindi cha mwaka 2018 ambapo Mfuko wa PSSF ulianzishwa hadi Machi 2022 tumeweza kulipa mafao yenye thamani ya Shilingi Trilioni Sita na Bilioni Tisini na Moja na kila mwezi Serikali inalipa fedha Shilingi Bilioni 58.75 kwa wastaafu 148,868 kwa mwezi tarehe 25 bila kukosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakiri kwamba kulikuwa na changamoto hasa kwa wastaafu ambao walikuwa wameanza kazi kabla ya mwaka 1999 ambao walikuwa hawachangii lakini wakaingia kwenye mfuko. Kwa hiyo hao walisababisha Mfuko kuelemewa kwa sababu walikuwa hawachangii lakini walikuwa wanatakiwa kulipwa na ndiyo hiyo hela ambayo mdogo wangu Ester Bulaya anaizungumzia ya Shilingi Trilioni 4.62 ambayo ilitokana na watumishi ambao walikuwa hawachangii katika mifuko lakini Serikali iliona na wenyewe wapate mafao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imetoa fedha Trilioni 2.17 ambayo imewezesha mifuko kupata nguvu na watu wote ambao malimbikizo yao yaliyokuwepo ya mifuko kwa wastaafu wamelipwa na sasa hivi watumishi wanaostaafu wanapata mafao yao ndani ya siku 60 tangu walipoleta taarifa zao za kustaafu yaani tangu tarehe ya kustaafu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna changamoto inawezekana kuna wachache ambao taarifa kama ambavyo kuna Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia mwingine anakuwa hana barua ya ajira kama nilivyosema, wale ambao walikuwepo kabla ya mwaka 1999 kweli kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshafuatilia kundi hili waliobaki ni wachache na tunaendelea kuweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba hata hao ambao waliingia kwenye mfuko wakati tayari wako kwenye utumishi na taarifa zao hazikuwa zimekuja rasmi, kwa kiasi kikubwa tumeshakamilisha kwa hiyo usumbufu huo hautakuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uhakiki wa wastaafu, hili suala la uhakiki wa wastaafu niseme kwamba wastaafu wetu ni watu ambao wameitumikia nchi yetu kwa uadilifu na Serikali inawathamini wafanyakazi wanapokuwa kazini, na hata wanapostaafu Serikali inaendelea kuwathamini. Tayari Serikali imeshatoa maelekezo zoezi hili la wastaafu lisilete usumbufu kwa wazee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo napenda kuchukua nafasi hii kuwaelekeza PSSSF pamoja na NSSF zoezi la kuhakiki wastaafu lifanyike katika namna ambayo haitawalazimu wazee wetu kusafiri muda mrefu kwenda kwenye Makao Makuu ya Mikoa.
Kwa hiyo, hilo ni suala la usimamizi, tayari Serikali imetoa maelekezo kuhakikisha kwamba uhakiki wa wastaafu unafanyika katika namna ambayo haileti usumbufu kwa wazee wetu, lazima wazee waheshimiwe na lazima wazee walindwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo Waheshimiwa wanalizungumzia ni uhimilivu wa mifuko. Naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba mifuko hii bado ni himilivu bado itaendelea kulipa mafao kwa wastaafu na deni ambalo lilikuwepo la...
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa kutoka wapi?
MHE. ESTER A. BULAYA: Hapa
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester Bulaya taarifa.
T A A R I F A
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpe taarifa Mheshimiwa Waziri. Taarifa za Serikali ya Machi 2022 ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali amesema mifuko ina hali mbaya, siyo himilivu na iko kinyume na taratibu wa ukwasi wa asilimia 40, mlipolipa ile pre 99 Trilioni Mbili walau imefika asilimia 30 lakini ….
MWENYEKITI: Taarifa ya Serikali au taarifa ya CAG?
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni taarifa ya CAG na ndiyo Serikali yenyewe.
MWENYEKITI: Basi rekebisha vizuri.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakupa pia taarifa kwamba PSSSF kwa miaka hii ya karibuni mapato yake ya michango ni madogo kuliko mahitaji ya wazee wastaafu wanaotakiwa kulipwa, iko himilivu wapi?
MWENYEKITI: Mheshimiwa Prof. Ndalichako unapokea taarifa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Ofisi ya Waziri Mkuu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siipokei hiyo taarifa kwa sababu taarifa ya CAG ni ya mpaka Juni, 2021.
(Hapa Mhe. Ester A. Bulaya alizungumza bila kutumia kipaza sauti)
MWENYEKITI: Nani amekuruhusu uzungumze Mheshimiwa Bulaya? Hili ni Bunge endelea Mheshimiwa Profesa.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU KAZI AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimeeleza kwamba tayari Serikali imetoa fedha shilingi trilioni mbili na bilioni mia moja sabini kwa ajii ya kulipia fedha za mifuko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali imetoa fedha hizo ni dhahiri kwamba hata hizi ambazo zimebaki kiasi cha shilingi bilioni 2.45 Serikali itazitoa tu Serikali yetu ni sikivu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hili ni deni la muda mrefu ambalo tangu mwaka 1999 lakini Serikali imeshalipia trilioni 2.17 na zilizobaki ni suala la muda tu. Kwa hiyo, suala hili litalipwa na wastaafu wataendelea kupata mafao yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PROF. JOYCE L. NDALICHAKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nichangie hoja ambayo iko mbele yetu. Naomba nianze kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake uliotukuka ambao sote tunashuhudia mafanikio makubwa katika sekta zote muhimu za ustawi wa jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nampongeza kwa kutoa dira ya mwelekeo wa mageuzi katika Sekta ya Elimu. Alitoa dira hiyo katika Bunge lako Tukufu wakati alipolihutubia tarehe 22 Aprili, 2021. Hotuba hiyo ndiyo ambayo imezaa Sera Mpya ya Elimu, Toleo la Mwaka 2023 na mitaala mipya ambayo imeanza kutekelezwa mwaka 2024.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa nampongeza Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa hakika anafanya kazi nzuri, msaidizi wake Mheshimiwa Kipanga, Katibu Mkuu Profesa Nombo pamoja na watendaji wote. Hakika wanafanya kazi nzuri ya kusimamia Sekta ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Taasisi ya Elimu ambayo ndiyo imefanya kazi ya kusimamia mabadiliko haya ya mitaala ambayo yameanza kutekelezwa ambapo wameanzisha na mkondo wa elimu ya amali. Ufanisi katika utekelezaji wa mitaala unahitaji mambo mengi ikiwa ni pamoja na mwanafunzi mwenyewe, mwalimu, mazingira ya shule, vifaa vya kujifundishia pamoja na mfumo wa ufuatiliaji na udhibiti wa elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nielekeze mchango wangu upande wa walimu kwa sababu, natambua kwamba, mwalimu ndiyo nguzo na nyenzo muhimu katika ufanisi wa utekelezaji wa mitaala. Naipongeza Serikali kwa hatua ambazo imezichukua kuwapitisha walimu na kuwapa mafunzo kuhusu mtaala mpya, lakini mafunzo hayo bado hayajatosheleza. Naomba mafunzo hayo yawe endelevu kwa sababu, mtaala huu mzunguko wake ni wa miaka 10. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi elimu msingi ya lazima imekuwa ni miaka 10, ambapo ni miaka sita ya elimu msingi na miaka minne ya sekondari. Kwa hiyo, ufanisi wa utekelezaji utategemea uimara na umahiri wa walimu katika utekelezaji wa mitaala, kwa hiyo, mafunzo kazini yawe ni endelevu kwa upande wa walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia iangalie shule ambazo zina uhaba wa walimu, lakini naipongeza imekuwa ikiajiri walimu na tayari kuna tangazo la kuajiri walimu wengine. Kwa hiyo, Serikali iendelee kuajiri walimu wengi zaidi na kufanya msawazo wa walimu ili shule zile ambazo zina uhaba wa walimu ziweze kupata walimu wa kutosha na hasa ukizingatia hapo alipomalizia Profesa aliyekuwa anachangia, Mheshimiwa Muhongo kwamba, elimu inataka mafunzo kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili uweze kufanya mafunzo kwa vitendo ni lazima uwe na walimu wa kutosha, uwe na vifaa vya kutosha na uwe na rasilimali za kutosha katika kutekeleza mtaala katika mkondo wa amali. Kwa hiyo, ufanisi katika utekelezaji wa mtaala huu unategemea sana umahiri wa walimu na uwepo wa vifaa vitakavyowawezesha wanafunzi kufanya mafunzo yao kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa elimu pia, tuangalie suala la udhibiti ubora. Wadhibiti ubora ndiyo jicho la Serikali katika kuhakikisha kwamba, elimu inatolewa kwa viwango ambavyo vimewekwa. Kwa hiyo, ni muhimu sana wadhibiti ubora waangaliwe kwa jicho la kipekee. Natambua na napongeza jitihada ambazo Serikali imezifanya katika kuwawezesha wadhibiti ubora, kuwajengea ofisi wale ambao walikuwa hawana ofisi, karibu halmashauri zote wamejengewa, kuwanunulia magari na kuwanunulia pia, vitendea kazi, vifaa vya ofisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana wawezeshwe kufika katika shule ili waweze kufanya ukaguzi na kujiridhisha kama mitaala hii mipya ambayo imeanza kutekelezwa Januari, 2024, inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mageuzi haya ni makubwa kwa hiyo kusipokuwepo na usimamizi na ufuatiliaji wa makini malengo yaliyokusudiwa yanaweza yasifikiwe. Kwa hiyo, niombe sana Idara ya Udhibiti wa Elimu iwezeshwe ili iweze kufanya kazi zake kwa kuzingatia mpango kazi uliowekwa, lakini kubwa niombe ushauri unaotolewa na wadhibiti ubora wa shule ufanyiwe kazi, maana mara nyingi wamekuwa wakikagua, wakiandika report zao, lakini zinakuwa tu ni kama kitu cha kawaida ambacho hakipewi uzito ambao unastahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kwenye huu mtaala kuna mkondo wa elimu ya amali. Tunatambua kuna changamoto kubwa ya uhaba wa walimu wa mafunzo ya amali. Kwa hiyo, niombe sana Serikali iwe na mpango mahsusi wa kuandaa walimu kwa ajili ya mkondo wa elimu ya amali kwa sababu tunafahamu kwamba shule za ufundi hapa katikati kulikuwa na utaratibu ambao ulizifanya zikawa hazifanyi kazi. Kwa hiyo, walimu wengi walikuwa wameshaondoka wamekwenda kufanya shughuli nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iweke mipango madhubuti na hasa ukizingatia hotuba ya Waziri inaonesha kwamba katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 wana mpango wa kujenga shule 100 za ufundi na Mheshimiwa Waziri ametuambia kwamba anategemea shule 26 zitaanza kufanya kazi mwaka 2025. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri awe na mipango thabiti ya kupata walimu kwa sababu kama nilivyosema walimu ndio nyenzo na nguzo muhimu katika kuhakikisha ufanisi wa mitaala ambayo imewekwa na hii pia inaenda katika vyuo vya ufundi stadi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Mheshimiwa Waziri inaonesha kwamba chuo pekee kinachotoa mafunzo ya ufundi stadi cha Morogoro katika Mwaka wa Fedha 2023/2024, kimedahili wanafunzi takribani 352 ambayo ni sawa na 53% ya lengo. Sasa kama tunaongeza VETA, tumekamilisha kujenga VETA 29, ambapo 25 ni za wilaya na nne za mkoa. Pia tunaendelea na ujenzi wa VETA 65. Ni dhahiri kwamba kama udahili hatufiki hata lile lengo lililokusudiwa kuna kazi ya ziada ambayo inapaswa kufanyika ili kuhakikisha kwamba tunakuwa na walimu wa kutosha ili lengo la kuwa na wahitimu ambao wana ujuzi, wana umahiri liweze kufikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kidogo kuhusiana na elimu maalum. Elimu maalum katika nchi yetu imekuwa ikifanyika vizuri sana na tumekuwa ni mfano kwa sababu mazingira yetu ya kutolea elimu tumeendelea kuyaboresha na tumeendelea kuhakikisha kwamba tunaweka bajeti ya kutosha kwa ajili ya kununua vifaa visaidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum. Kwa hiyo, lengo la Serikali ni kuendelea kuhakikisha kwamba inatoa elimu bora kwa wote ambayo inazingatia usawa kwa watoto wote hata wale wenye mahitaji maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefurahishwa sana na hatua ambayo Serikali imechukua ya kuandaa mwongozo wa shule ya nyumbani wa mwaka 2023 ambao mwongozo huo unatoa fursa kwa watoto wenye mahitaji maalum ya kiwango cha juu kuweza kupata elimu wakiwa nyumbani. Kwa hiyo, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, wataona ni namna gani ambavyo Serikali imejizatiti kuhakikisha kwamba hakuna mtoto anayeachwa kwenye elimu hata yule mwenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana Wizara iendelee kuhakikisha kwamba inatangaza huduma hii ya kuweza kutoa elimu mtoto anapokuwa nyumbani kwani bado kuna tabia ya baadhi ya wazazi kuwaficha nyumbani watoto ambao wana mahitaji maalum. Hivyo basi pamoja na mipango mizuri ya Serikali bado kunakuwa na watoto ambao wanaachwa. Tuendelee kutoa elimu, tuendelee kuhakikisha kwamba watoto wote wanaenda shule na kupata elimu iliyo bora. Pia tuboreshe mafunzo kwa ajili ya walimu wenye mahitaji maalum na kuhakikisha kwamba wanapomaliza mafunzo yao wanapangiwa katika shule ambazo zina wanafunzi wenye mahitaji maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii na naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 5) wa Mwaka 2017
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hoja iliyoko mezani. Kwanza nianze kwa kusema naunga mkono hoja hii ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali na naunga mkono mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma ambayo inapendekeza kuongeza umri wa kustaafu kwa maprofesa na wahadhiri waandamizi pamoja na madaktari bingwa kutoka umri wa miaka 60 hadi miaka 65.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii kama walivyozungumza Waheshimiwa Wabunge ambao nashukuru sana wachangiaji karibu wote wameunga mkono hoja hii. Uhitaji wa maprofesa na madaktari ni mkubwa sana na ndiyo maana kati ya mwaka 2012 mpaka 2016 maprofesa na wahadhiri waandamizi ambao walistaafu walikuwa ni 395; lakini kati yao walioajiriwa kwa mkataba walikuwa ni 324. Kwa hiyo inaonesha ni jinsi gani bado wanakuwa wanahitajika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kumwambia Mheshimiwa dada yangu Magdalena Sakaya kwamba ukiangalia hizi takwimu hawa maprofesa wanaoendelea; ni kwamba hii mikataba inakuwa ni ya hiari. Kwa hiyo ukiangalia idadi ya wanaomaliza lakini bado wanaendelea ni kubwa. Niseme kwamba Serikali inayo mikakati ya kuhakikisha kwamba suala hili la uhaba wa maprofesa linafanyiwa kazi. Niseme tu kwamba maprofesa hawapatikani kwa kusomeshwa, kuna Mbunge mmoja alikuwa anasema kwamba kuna kipindi tumekaa bila kusomesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwa profesa ni juhudi binafsi na inatokana na kuandika, kufanya machapisho. Serikali inapoajiri ngazi ya chini katika vyuo vikuu ni mkufunzi msaidizi (tutorial assistant) ambaye anakuwa na degree ya kwanza; baada ya hapo sasa anapanda kulingana na mchapisho. Ngazi inayofuata ni Mhadhiri Msaidizi ambaye ni Assistant Lecture anatakiwa awe na shahada ya uzamili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo anaweza akapanda kuwa Mhadhiri kwa kuandika machapisho matatu. Kutoka Mhadhiri kwenda Mhadhiri mwandamizi yaani Senior Lecture lazima awe na shahada ya uzamivu. Kwa hiyo unaweza ukaona kwamba kuna vigezo vingine ambavyo ni juhudi binafsi ya mkufunzi au mwalimu kuweza kufika hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunatambua kwamba baadhi ya wahadhiri wameshindwa kupata shahada za uzamivu kutokana na ufadhili. Mkakati wa Serikali katika mwaka huu wa fedha tumetenga shilingi bilioni nane kwa ajili ya kutoa ufadhili katika fani ambazo zina uhaba mkubwa wa wahadhiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutatua tatizo la madaktari ambalo lipo nchini tayari Serikali kupitia chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi MUHAS; tunayo hospitali ya Mloganzila ambayo ni hususan kwa ajili ya kufundishia madaktari pamoja na watoa huduma mbalimbali wa afya. Tayari Serikali imekwishatenga fedha shilingi bilioni 13.1 kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hili ambapo tumewapa kazi Wakala wa Majengo Tanzania kuweza kujenga baadhi ya majengo ambayo yatawezesha kuongeza udahili wa wanafunzi 1,500 katika mwaka wa masomo 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Serikali imekwishatoa fedha za awali kwa TBA bilioni 3.9. Pia Wizara ya Fedha katika bajeti yake kuna fedha ambazo zimetengwa na kuna madaktari 290 ambao wanasoma kwa ajili ya ufadhili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda Serikali pamoja na kuomba Muswada wa kuongeza umri wa madaktari na maprofesa lakini tuna mikakati. Niseme tu kwamba uhaba wa madaktari pia umechangiwa na kuongezeka kwa vyuo vikuu, jambo ambalo lina afya kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ningeomba Waheshimiwa Wabunge wote waunge mkono hoja hii kwa sababu ina maslahi mapana kwa Taifa letu, ina maslahi kwa maprofesa wetu ambao kadri wanavyokuwa wanaendelea na umri wao pia uzoefu katika fani zao unakuwa ni mkubwa na ndiyo maana katika nchi nyingine maprofesa hawawekewi umri wa kustaafu. Naamini kwa kufanya hivyo tutaendelea kuongeza pia vyuo vikuu na tutaendelea kuwahitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.