MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ahsante; ni dhahiri kwamba Watanzania wengi ambao unakuta wamemaliza kidato cha sita na wengine ambao wanasifa za kwenda vyuo vikuu wanatamani sana kupata mikopo ya elimu ya juu ili tuweze kuwa na wataalam wa fani mbalimbali. Mikopo hii inapotolewa tumeweka riba kubwa sana ya asilimia kumi na tano ambayo ipo katika sheria ya 2016 na penati ya asilimia sita. Hivyo, tunakuta wanufaika wengi ambao ni watoto wa familia maskini wanashindwa kulipa au kubeba huu mzigo. Je, ni lini sasa Serikali italeta mabadiliko ya sheria hii angalau tupeleke kwenye singledigit kwa maana ya asilimia nane au tano ili tuwe na lengo la kutoa wajuzi na siyo kugeuza kama chanzo cha mapato? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Matiko kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza swali lake la nyongeza ukiangalia kwa kiasi kikubwa haliendani na swali la msingi, lakini kwa sababu ya umuhimu wa masuala ya Bodi ya Mikopo, ningependa kwanza kuonesha kwamba mwombaji wa kwanza anasema wanafunzi wote wapate mikopo, lakini mwombaji wa pili anasema makusanyo wapunguze.
Mheshimiwa Spika, lengo la kuanzisha Mfuko huu wa mikopo ilikuwa ni kwamba watu wafanye marejesho, mikopo ijiendeshe yenyewe kama vile revolving fund yaani yale marejesho yakikusanywa yatosheleze kuwapatia wanafunzi wengine. Kwa hiyo, ukiangalia hata sasa makusanyo ya mikopo yanachangia asilimia 46 ya bajeti ya mikopo. Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba umuhimu wa kurejesha mikopo upo na asilimia 15 ambayo mwanafunzi anakatwa, anabaki na asilimia 85 ya mkopo wake, tukumbuke kwamba mkopo wa Bodi ya Mikopo ndiyo uliotangulia kabla ya mikopo mingine na Kanuni za Utumishi makato ni kwamba mtumishi anatakiwa abaki na theluthi moja ya mshahara.
Mheshimiwa Spika, nawasihi wanaochukua mikopo, waone umuhimu wa kulipa na wale wenye fedha wasisubiri kukatwa hiyo asilimia kumi na tano, kumi na tano ili wanafunzi wengine waweze kunufaika kama wao walivyonufaika, wakaweza kupata ajira. Kwa hiyo naomba sana Waheshimiwa Wabunge watusaidie kutoa elimu kuonesha umuhimu wa kurejesha mikopo kwa sababu marejesho hayo ndiyo yanawasaidia wengine kupata mikopo.