Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Abdallah Saleh Possi (20 total)

MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-

Wananchi wa Wilaya ya Mpwapwa wanakabiliwa na tatizo kubwa la njaa, na katika msimu wa mwaka 2014/2015 mvua hazikunyesha kabisa na kusababisha wananchi wengi kukosa chakula kutokana na ukame; na Serikali imekwisha tamka kwamba hakuna mwananchi atakayekufa kwa njaa.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kugawa chakula cha njaa Wilaya ya Mpwapwa?
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwanza napenda niishukuru sana Serikali kwa kutupatia kiasi kidogo cha chakula katika Wilaya ya Mpwapwa.

Kwa kuwa, Wilaya ya Mpwapwa ina Majimbo mawili, Jimbo la Mpwapwa na Jimbo la Kibakwe, na kwa kuwa chakula hicho ambacho tumepatiwa ni kidogo.

Je, Serikali ina mpango gani wa kutuongezea chakula cha njaa Wilaya ya Mpwapwa?

Swali la pili, kwa kuwa hivi sasa baadhi ya wananchi wameacha kulima mashamba yao wanalima vibarua ili wapate hela ya kununua chakula. Je, utakubaliana na mimi kwamba iko haja sasa ulete chakula hicho haraka kwa Wilaya ya Mpwapwa na Wilaya ya Kongwa?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, VIJANA, AJIRA NA WALEMAVU - (MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa hakuna mwananchi anayekufa kwa njaa kutokana na ukosefu wa chakula, Serikali imekuwa ikifanya tathmini ya hali ya chakula na lishe katika maeneo mbalimbali nchini na kutoa chakula cha msaada kwenye Halmashauri zilizoonekana kuwa na upungufu wa chakula ikiwemo Mpwapwa.
Mheshimiwa Spika, tarehe 15 Disemba, 2015 Serikali ilitoa chakula cha msaada tani 200 za mahindi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa. Aidha, kati ya tarehe 4 na 7 Januari, 2016 Serikali imepeleka Wilayani Mpwapwa chakula cha msaada tani 1,619 na shilingi milioni 35 kwa ajili ya kununua mbegu za mtama na mihogo. Hivyo jumla ya chakula cha msaada kilichopelekwa Wilayani Mpwapwa mwezi Disemba, 2015 na Januari, 2016 ni tani 1,819.
Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa chakula cha kupunguza makali ya bei ya soko tani 6,000 kwa Mkoa wa Dodoma kupitia wafanyabiashara wa Mkoa huo ili kuwezesha upatikanaji wa chakula chenye bei nafuu kwa wananchi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma ikiwemo Wilaya ya Mpwapwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa wito kwa wananchi waliopo kwenye maeneo yenye ukame wakiwemo wananchi wa Wilaya ya Mpwapwa kuhakikisha kuwa wanalima mazao yanayostahimili ukame na kufuata kanuni bora za kilimo ili kupunguza tatizo la upungufu wa chakula.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, VIJANA, AJIRA NA WALEMAVU - (MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI): Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa Mheshimiwa George Malima Lubeleje, kwamba Serikali inatambua jukumu lake la kuwalinda na kuwasaidia wananchi wote wanaopatwa na matatizo mbali mbali, ikiwemo baa la chakula.
Kuhusu swali lake la pili, tunafahamu umuhimu hiyo na tathmini itafanywa ili kuwezesha upatikanaji wa chakula hicho kwa haraka.
MHE. MWANTUMU D. HAJI aliuliza:-
Vijana ndiyo nguvu kazi ya kutegemea katika Taifa hili na ulimwenguni
kote. Kwa bahati mbaya, vijana wetu wengi wameathirika sana na madawa ya
kulevya kiasi kwamba, badala ya kuwa nguvu kazi, imekuwa ni mzigo mkubwa
kwa familia zao na Taifa kwa ujumla.
Je, Serikali imejipanga vipi kuona inawanusuru vijana katika janga hili?
MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI - NAIBU WAZIRI, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA,
VIJANA NA WALEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu napenda kujibu swali la
Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa, matumizi ya dawa za
kulevya yana madhara mengi kwa watumiaji, familia na jamii kwa ujumla. Ili
kuwanusuru vijana wetu na madhara hayo Serikali imechukua hatua zifuatazo:-
1. Kuongeza juhudi za dhati za kimkakati za kuhakikisha za kuhakikisha wale
wote wanaojihusisha na biashara hii haramu wanakamatwa na
kuadhibiwa vikali kupitia Sheria Na. 5 ya mwaka 2015.
2. Kuendeleza huduma njema na endelevu ya Serikali ya kutoa matibabu
kwa watumiaji wa dawa za kulevya katika hospitali na vituo vya
wagonjwa wa akili nchini, ili kuwasaidia watumiaji wa madawa hayo
kuacha.
3. Kuendelea kuratibu na kusaidia kusambazwa kwa nyumba za ushauri
nasaha na upataji nafuu (Sober Houses) na huduma za kuwafikia
watumiaji katika miji mbalimbali nchini.
4. Kuanzisha huduma ya tiba kwa kutumia dawa ya methodone katika
hospitali zetu.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE aliuliza:-
Mvua ya theluji ilionyesha terehe 3 Machi, 2015 ilisababisha maafa makubwa ambapo familia zilikosa makazi na Mheshimiwa Rais wakati huo aliwaahidi wahanga wa maafa hayo kuwa Serikali itasaidia kujenga nyumba 343:-
(a) Je, ni nyumba ngapi hadi sasa zimejengwa katika kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais?
(b) Je, ni kiasi gani cha pesa kinahitajika kwa ajili ya utekelezaji wa ahadi hiyo?
(c) Je, ni kiasi gani cha fedha na misaada ya kibinadamu ya aina nyingine iliyotolewa na Serikali katika kukabiliana na janga hilo?
NAIBU WAZIRI WA SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolya Maige, Mbunge wa Msalala, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha ujenzi wa nyumba mbili za mfano kwa lengo la kujua gharama halisi za ujenzi wa nyumba zilizoahidiwa na Serikali.
(b) Mheshimiwa Spika, jumla ya Sh.2,500,000,000 zinahitajika kugharamia ujenzi wa nyumba hizo. Gharama hizi zimepatikana baada ya kukamilika kwa tathmini ya gharama za ujenzi wa nyumba moja moja.
(c) Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na maafa haya Serikali ilitoa huduma za dharura za malazi, makazi ya muda na matibabu. Misaada mingine iliyotolewa na Serikali ni pamoja na mahindi tani 100.4, Sh.45,290,045 kwa ajili ya ununuzi wa maharage, mafuta ya kupikia na usafirishaji wa mahindi. Aidha, Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Mfuko wa Maafa ilitoa Sh.10,000,000 kwa ajili ya mahitaji mbalimbali.
MHE. HALIMA A. BULEMBO aliuliza:-
Nchi ya Tanzania ni moja kati ya nchi zenye vijana wengi, asilimia 72 ya Watanzania wapo kwenye umri chini ya miaka 29 kwa mujibu wa taarifa ya Taifa ya Takwimu ya 2013 na ajira kwa vijana hao ndiyo suluhisho la kuhakikisha kuwa vijana wanalihudumia Taifa lao:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha vijana wawe wajasiriamali kwa kuwapa mitaji, mikopo na ni vigezo gani vitakavyosimamia na kuwalinda na kuweka usawa wa upatikanaji wa ushiriki wao katika fursa hizo?
(b) Je, ni lini ahadi ya Sh. 50,000,000 kwa kila kijiji itatekelezwa na vijana watapata mgao wao wa asilimia ngapi?
NAIBU WAZIRI WA SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa vijana wanakuwa wajasiriamali na wanaweza kupatiwa mikopo na mitaji, Serikali imejiwekea mikakati ifuatayo:-
(i) Kutambua vijana na mahitaji yao katika ngazi mbalimbali;
(ii) Kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa makundi mbalimbali ya vijana; na
(iii) Kutekeleza mkakati wa Kitaifa wa kukuza ujuzi nchini ambao umelenga kutoa mafunzo ya vitendo maeneo ya kazi kwa wahitimu hususani wa vyuo vya elimu ya juu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mikakati hiyo yote, vigezo ambavyo vimekuwa vikitumika katika kutoa mikopo na mitaji kwa vijana ni umri usiozidi miaka 35; kujiunga katika SACCOS za Vijana za Wilaya na kuunda vikundi na kuvisajili kisheria.
(b) Mheshimiwa Spika, ahadi ya Mheshimiwa Rais ya Sh.50,000,000 kwa kila kijiji itaanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha ujao yaani 2016/2017. Utaratibu wa kugawa fedha hizi unaandaliwa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kushirikiana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza:-
Dawa za kulevya nchini zimekuwa na athari kubwa sana kwa wananchi wetu hususan kundi la vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa:-
(a) Je, Serikali haioni kuwa kwa kutumia vyombo vyake inaweza kubaini watumiaji, wauzaji mpaka vigogo wanaoingiza na kusambaza dawa nchini?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa dhati wa kuwaweka waathirika wa dawa za kulevya katika makambi maalum ya kuwatibu na hatimaye kurudi katika hali yao ya kawaida?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU - MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khalifa Mohamed Issa, Mbunge wa Mtambwe lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali siku zote hutumia vyombo vyake kuwabaini, kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria wafanyabiashara wadogo na wakubwa wa dawa za kulevya nchini kwa kushirikiana na wananchi wakiwemo watumiaji wa dawa za kulevya. Juhudi hizi zimefanikisha kuwakamata wauzaji wadogo na wakubwa na kuwafikisha kwenye vyombo vya kisheria. Baadhi ya watuhumiwa wakubwa wa biashara hiyo waliokamatwa ni Ali Khatibu Haji (maarufu kwa jina la Shkuba), Mohammed Mwarami (maarufu kwa jina la Chonji na Mwanaidi Mfundo maarufu kwa jina la Mama Leila).
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Asasi za Kiraia inaendelea na progamu maalum ya kutoa huduma za upataji nafuu katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, Serikali imetoa mwongozo wa uendeshaji wa huduma hizo na inaendelea na ujenzi wa kituo kikubwa cha huduma za matibabu na utengemano katika eneo la Itega, Mjini Dodoma na inaratibu ujenzi wa kituo kama hicho Mjini Tanga.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-
Tatizo la matumizi ya dawa za kulevya linazidi kuongezeka siku hadi siku:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia vijana wetu walioathirika na dawa za kulevya?
NAIBU WAZIRI WA SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inalitambua tatizo la matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini na athari wanazozipata watumiaji, hasa vijana ambao ni nguvu kazi muhimu, ambao huathirika kiafya, kiuchumi na kijamii. Ili kuwasaidia vijana walioathirika kwa kutumia dawa za kulevya, Serikali imekuwa ikitekeleza mikakati ifuatayo:-
(i) Serikali kupitia hospitali na vituo vya afya imekuwa ikitoa huduma mbalimbali ya kuwaondoa katika urahibu watumiaji wa dawa za kulevya. Baadhi ya hospitali ambazo zimekuwa zikitoa huduma hizo ni pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Magonjwa ya Akili Mirembe - Dodoma, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali za Temeke na Mwananyamala za Mkoa wa Dar es Salaam na Hospitali ya Afya ya Akili Lulindi - Korogwe. Huduma zinazotolewa katika hospitali hizo ni pamoja na ushauri nasaha, kuondoa sumu mwilini na matibabu ya methadone.
(ii) Serikali kwa kushirikiana na Asasi za Kiraia inaendelea na programu maalum ya kutoa huduma za upataji nafuu katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, Serikali imetoa mwongozo wa uendeshaji wa huduma hizo na inaendelea na ujenzi wa kituo kikubwa cha huduma za matibabu ya utengemao katika eneo la Itega mjini Dodoma na inaratibu ujenzi wa kituo kama hicho mjini Tanga.
MHE. STELLA IKUPA ALEX aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko la ombaomba au utegemezi kwa watu wenye ulemavu nchini:-
Je, ni kwa nini Serikali isiwawezeshe kiuchumi watu wenye ulemavu kwa kuwapa upendeleo wa zabuni za kazi mbalimbali, kama vile kuzoa takataka, usafi wa vyoo, ushonaji na kadhalika kwenye Halmashauri?
NAIBU WAZIRI WA SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu, napenda kujibu swali namba 61 la Mheshimiwa Stella Alex, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua haki za watu wenye ulemavu kufanya kazi kwa misingi sawa na wengine, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kiuchumi, fursa za ajira na kuwaandalia mazingira wezeshi. Serikali pia inatambua uwepo wa watu wenye ulemavu waliojiajiri wenyewe kupitia makampuni au vikundi mbalimbali ambao wanahitaji kuungwa mkono ili kupambana na utegemezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha upatikanaji wa fursa sawa kwa watu wenye ulemavu katika fursa mbalimbali, zikiwemo fursa za ajira na za kiuchumi, Serikali itaendeleza kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, Sheria Namba Tisa (9) ya Mwaka 2010 inayoelekeza hatua za makusudi za msingi na wajibu wa kutambua haki za watu wenye ulemavu. Kifungu 34(2) cha Sheria tajwa kinaipa nguvu Serikali kuchagiza upatikanaji wa fursa za ajira kwa watu wenye ulemavu kwa kufuata utaratibu wa kutoa kipaumbele maalum (affirmative action).
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa umuhimu wa pekee Serikali inawasisitiza Watendaji wote kwamba kwa mujibu wa Kifungu cha tatu (3) cha Sheria Namba Tisa (9) ya Mwaka 2010, maana ya neno kubagua inajumuisha, kukataa bila sababu maalum kutoa kipaumbele maalum kwa watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirudie, kwa mujibu wa Kifungu cha tatu (3) cha Sheria Namba Tisa (9) ya Mwaka 2010, maana ya neno kubagua inajumuisha, kukataa bila sababu yoyote kutoa kipaumbele maalum kwa watu wenye ulemavu. Hivyo basi, Watendaji wa Serikali wanawajibika kutoa kipaumbele maalum kwa watu wenye ulemavu katika masuala na fursa mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi Ibara ya 58(2) imeelekeza kutengea asilimia 30 ya tenda zote za utoaji huduma kwenye Halmashauri zote nchini kwa makundi maalum wakiwemo watu wenye ulemavu.
MHE. FLATEI G. MASSAY (K.n.y MHE. ESTER A. MAHAWE) aliuliza:-
Serikali kupitia mpango mkakati wa kuwawezesha wananchi wa vijijini iliahidi kutoa shilingi 50,000,000 kwa kila kijiji na mtaa:-
(a) Je, ni lini fedha hizo zitatolewa?
(b) Je, Serikali imejipanga vipi kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wananchi juu ya njia bora ya kutumia fedha hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga shilingi bilioni 59.5 katika Bajeti ya mwaka 2016/2017 chini ya Fungu 21 kwa ajili ya kuwawezesha wananchi vijijini kwa kutoa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Fedha hizo zitatolewa mara baada ya kuidhinishwa na Bunge lako Tukufu na baada ya kukamilisha taratibu mbalimbali zinazolenga kuhakikisha uwepo wa tija katika matumizi ya fedha hizo.
(b) Mheshimiwa Spika, kuhusu mpango bora wa elimu ya ujasiriamali kwa wananchi, ili kuhakikisha matumizi bora ya fedha hizo Serikali inaendelea kukamilisha maandalizi ya utaratibu maalumu wa utoaji wa fedha hizo, ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu ya ujasiriamali. Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI imepewa kazi ya kuratibu utekelezaji wa mpango huo.
MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:-
Pamoja na juhudi kubwa ya Serikali ya Awamu ya Nne katika kutekeleza
ahadi ya miradi katika Ilani ya Uchaguzi bado haikuweza kukamilisha ahadi
zote ilizotoa:-
Je, Serikali ya Awamu ya Tano ina mpango gani wa kukamilisha ahadi za
miradi iliyoachwa na Serikali ya Awamu ya Nne bila kukamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba uniwie radhi huenda sauti
yangu leo ikaonekana nene kuliko kawaida lakini sina haja ya kumtisha mtu
yeyote. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu,
napenda kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge wa Viti
Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Nne kupitia Ilani yake ya
Uchaguzi ya mwaka 2010-2015, iliahidi kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta
za uzalishaji, miundombinu na huduma za kiuchumi, huduma za jamii na
uendelezaji wa wananchi kiuchumi. Miradi iliyopangwa kutekelezwa katika
sekta hizo ilijumuisha miradi ya muda mfupi na muda mrefu. Kulingana na aina
ya miradi, muda unaotumika kukamilisha miradi umekuwa ukivuka awamu moja
kwenda awamu nyingine ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha ahadi za utekelezaji wa miradi ya
uchaguzi ya mwaka 2010 inakamilika na kuendelea na miradi ya Ilani ya
Uchaguzi ya mwaka 2015, Serikali ya Awamu ya Tano tayari imezindua Mpango
wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Pia kupitia Bunge imekamilisha kupitisha
Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/2017 ambayo asilimia 40 itaelekezwa katika
miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali kupitia mipango na sera
mbalimbali za utekelezaji wa kibajeti itahakikisha kuwa miradi iliyoachwa na
Serikali ya Awamu ya Nne inaendelea kutekelezwa, na miradi ya Kiilani ya
Uchaguzi ya Awamu ya Tano nayo itatekelezwa.
MHE. DKT. ELLY M. MACHA aliuliza:-
Elimu kwa watoto wenye ulemavu hupatikana kwa vikwazo na matatizo mengi kiasi kwamba wengi huanza shule katika umri mkubwa ukilinganisha na watoto wasio na ulemavu:-
(a) Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuongeza umri wa kustaafu kwa lazima kuwa miaka 65 kwa watu wenye ulemavu?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kutoa upendeleo maalum wa ajira kwa watu wenye ulemavu katika Wizara na Taasisi zake pale ambapo mtu mwenye ulemavu atakuwa na sifa stahiki wakati wa zoezi la ajira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye ulemavu kuhusiana na mambo mbalimbali kama vile upatikanaji wa elimu na ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba elimu na ajira ni baadhi ya mambo muhimu kabisa yenye uwezo wa kumtoa mtu mwenye ulemavu kutoka katika hali ya unyonge na utegemezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, napenda kujibu swali namba199 lenye sehemu (a) na (b) lililoulizwa na Mheshimiwa Dkt. Elly Macha, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya Mwaka 2002, umri wa kustaafu kwa lazima kwa mtumishi ni miaka 60. Hata hivyo, suala la kuongeza umri wa kustaafu kwa watumishi wenye ulemavu litategemea mabadiliko ya sera na hasa kwa kuzingatia maoni ya wadau na ushauri mwingine utakaotolewa kulingana na uhalisia wa suala hilo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetoa upendeleo maalum wa ajira kwa watu wenye ulemavu katika Wizara, Taasisi zake na Mashirika yasiyo ya Kiserikali pale ambapo mtu mwenye ulemavu anakuwa na sifa stahiki za ajira wakati wa zoezi la ajira. Kwa mujibu wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010, kifungu cha 31(2) kinaeleza wazi kwamba kila taasisi au sekta binafsi yenye watumishi wapatao 20 basi asilimia tatu wawe ni watu wenye ulemavu.
Aidha, kifungu cha 32 cha Sheria hii kinaeleza kuwa kwa madhumuni ya kuendeleza na kulinda ajira ya watu wenye ulemavu, kila mwajiri anatakiwa kufanya bidii ya kuendeleza ajira ya watu wenye ulemavu katika eneo lake la kazi. Serikali itaendelea na inaendelea kufuatilia utekelezaji wa sheria hii ili ajira za watu wenye ulemavu ziweze kupatikana kwa kuzingatia sheria na taratibu za ajira nchini.
Suala la Makao Makuu ya Serikali kuhamia Dodoma kwa muda mrefu limekuwa na kigugumizi na Ofisi za Wizara nyingi bado hazijahamia Dodoma, kutokana na kutokuwepo Sheria inayotamka kuwa Dodoma ndio Makao Makuu ya Nchi.
Je, ni lini Sheria hiyo itatungwa ili kuwezesha mchakato huo wa kuhamia Dodoma?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeishaanza mchakato wa kutunga Sheria ya Makao Makuu ya Nchi. Tayari Waraka wa Baraza la Mawaziri wa kutunga Sheria hiyo umekamilika, na sasa unasubiri kupangiwa tarehe ya kujadiliwa katika kikao cha wataalam cha Makatibu Wakuu (IMTC) na kisha kuwasilishwa ngazi ya Baraza la Mawaziri kwa uamuzi na hatimaye kuandaliwa Muswada wa Sheria, utakaowekwa Bungeni kujadiliwa na kupitishwa na Bunge kuwa sheria.
MHE. MBAROUK SALUM ALI aliuliza:-
Pamoja na sheria kali ya udhibiti na usimamizi wa dawa za kulevya, bado biashara hiyo ni tatizo kubwa kwa Tanzania.
Je, nini mkakati mahususi wa Serikali wa kupambana na kadhia hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbarouk Salim Ali, Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa dhamira ya dhati, inaendelea kuhakikisha kuwa inafanya udhibiti wa kutosha wa kupambana na kadhia ya dawa za kulevya nchini.
Mheshimiwa Spika, ili dhamira ya Serikali ya kudhibiti dawa za kulevya nchini itimie serikali kupitia Sheria Namba Tano ya mwaka 2015 imeanza kutekeleza maeneo yafuatayo ya kimkakati katika vita ya dawa za kulevya nchini:-
(i) Kukamilisha muundo mpya wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ili kuongeza nguvu ya kisheria ya kuchunguza, kupeleleza na kukamata watuhumiwa wa dawa za kulevya.
(ii) Kupunguza urasimu katika utendaji kwa kuwa na watendaji wa mamlaka wanaoshiriki moja kwa moja katika kutekeleza majukumu yao.
(iii) Kuharakisha kesi za dawa za kulevya kwa kuongeza nguvu katika maeneo ya uchunguzi, upelelezi na ukamataji.
(iv) Kuongeza nguvu katika huduma za matibabu na utengamao pamoja na kuzuia matumizi haramu ya dawa za kulevya, maabara na vifaa vya kuzalisha dawa za kulevya nchini.
Mheshimiwa Spika, nilihakikishie Bunge lako tukufu kwamba baada ya kuanza kutumika kwa Sheria Namba Tano ya mwaka 2015, shughuli za udhibiti wa dawa za kulevya nchini zitasimamiwa vyema na Serikali.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA aliuliza:-
Uwezeshwaji wa wananchi ni suala muhimu sana ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo hususani vijana na wanawake na Mifuko iliyopita kama ule wa Mabilioni ya Kikwete, Mfuko wa Wanawake na Vijana na kadhalika haikuwafikia walengwa:-
(a) Je, Serikali ya Awamu ya Tano ina mkakati gani wa kuboresha Mifuko hii na kuibua mingine?
(b) Je, ni kiasi gani cha fedha kilichorejeshwa na wananchi kwenye Mifuko hiyo ili na wengine waweze kufaidika nayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE WALEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inakusudia kufanya tathmini ya Mifuko yote ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi inayosimamiwa na Serikali ili kutambua ni kwa kiasi gani Mifuko hiyo inafikia malengo yake ya kuwawezesha wananchi kiuchumi na pia kufanya maboresho kwenye utendaji wa Mifuko. Tathmini hiyo ndiyo itakayotoa uelekeo wa namna bora ya kuratibu utendaji wa Mifuko hiyo kwa kuzingatia tija katika kila Mfuko. Kwa maana hiyo, suala la kuanzisha au kupunguza Mifuko mingine litategemeana na matokeo ya tathmini itakayofanyika.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo unaotumika kukopesha wananchi mikopo hii ni wa mzunguko (revolving fund), hivyo bado fedha hizo zinaendelea kuzunguka miongoni mwa wananchi na hivyo kutoa fursa kwa wengi kunufaika nayo. Kwa mfano, Mfuko wa Mabilioni ya JK ulikopesha shilingi bilioni 50.6 na zilirejeshwa shilingi bilioni 41.533 sawa na asilimia 82; Mfuko wa Wajasiriliamali wa Wananchi (NEDF) ulikopesha shilingi bilioni 36.387 na zimerejeshwa shilingi bilioni 32.748 sawa na asilimia 90; na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ulikopesha shilingi bilioni 5.789 na kurejesha shilingi bilioni 3.473 sawa na asilimia 60.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Kumekuwa na mauaji ya Watanzania wenye ulemavu wa ngozi kwa muda mrefu sasa ambapo hali hiyo imesababisha wananchi wasamaria wema kuanzisha makazi maalum kwa ajili ya kuwahifadhi.
Je, Serikali inashiriki vipi katika kutoa huduma muhimu ikiwemo kuhakikisha wanapata elimu, matibabu pamoja na lotion?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha takriban miaka kumi, kumekuwa na matukio ya vitendo vya kikatili dhidi ya watu wenye ualbino ambavyo vimesababisha baadhi ya wasamaria wema kuanzisha makazi maalum ya kuwahifadhi watu wenye ualbino. Licha ya matukio hayo kupungua, bado kuna makazi yanayotumika kuwatunza watu wenye ualbino kwa sababu mbalimbali zikiwemo sababu za unyanyapaa na taarifa za baadhi ya matukio ya mashambulio japo si mara kwa mara kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita. Makazi hayo yanajumuisha yale yaliyoanzishwa na Serikali na yale yaliyoanzishwa na wasamaria wema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika makazi haya, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inawajibika kuhakikisha kuwa watoto wenye ualbino wanapata elimu katika mazingira salama na kadri inavyowezekana kwa kuzingatia hali halisi Serikali itahakikisha watoto hawa wanapata elimu katika mazingira shirikishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa matibabu na mafuta maalum ya ngozi, Serikali kwa kushirikiana na Taasisi za Tiba za Ocean Road, KCMC, Bugando na wadau wengine imekuwa ikitoa matibabu na mafuta maalum ya kuzuia athari za mionzi ya jua katika ngozi, yaani sun screen lotion, kwa watu wenye ualbino. Aidha, Serikali kupitia Bohari Kuu ya Madawa (MSD) imeandaa mkakati wa kusambaza mafuta maalum katika hospitali zote za Wilaya ili kuwasaidia watu wenye ualbino ambapo mafuta hayo yameingizwa katika kundi la dawa kwa lengo la kurahisisha upatikanaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali ikishirikiana na wadau wengine imeandaa utaratibu wa kuwapima macho na ngozi watu wenye ualbino na kuwapatia tiba pamoja na ushauri ili wasiathirike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaamini kuwa suluhisho la kudumu la kuondoa vitendo vya ukatili na unyanyapaa dhidi ya watu wenye ualbino nchini ni kutoa elimu ili kubadili fikra potofu kwa jamiii kuliko kunzisha makazi na vituo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufanikisha azma hii, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana mamlaka ya Serikali za Mitaa na wadau wengine imeanzisha kampeni ya kupinga unyanyapaa na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino kwa lengo la kutoa uelewa na kutokomeza imani potofu iliyojengeka miongoni mwa jamii kuhusu watu wenye ualbino.
MHE. HAFIDH ALI TAHIR aliuliza:-
Chaguzi zetu zimekuwa zikikumbwa na matatizo mengi yanayosababisha upotevu wa fedha nyingi za Taifa jambo linaloweza kuepukika kwa faida ya Watanzania mathalani inapotokea mshindi wa uchaguzi wa Jimbo wa chama fulani amefariki hurudiwa badala ya nafasi hiyo kuchukuliwa na mshindi wa pili ndani ya chama hicho.
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka utaratibu kuwa pindi mshindi wa jimbo kupitia chama fulani anapofariki mshindi wa pili ndani ya chama apewe nafasi aliyoiacha marehemu badala ya kurudia uchaguzi?
(b) Je, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka kuondoa utaratibu wa kusimamisha uchaguzi mkuu wakati mgombea anapofariki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hafidh Ali Tahir, Mbunge wa Dimani lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria za uchaguzi pamoja na mfumo wa uchaguzi tulionao unamwelekeza mpiga kura kumpigia mtu (mgombea) na siyo chama kama ilivyo katika mifumo mingine ya uchaguzi ya kupigia chama. Hivyo, kwa sasa Serikali itaendelea kutumia utaratibu uliopo, kwa sababu mshindi wa pili atakayechukuliwa kujaza nafasi ya wazi, atakuwa hajachaguliwa na wananchi wote nchini au jimbo au kata husika, bali wanachama wachache wa chama hicho.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya sasa ya Uchaguzi, Sura ya 343 inaelekeza kusimamisha uchaguzi mkuu nchi nzima anapofariki mgombea Urais au Makamu wa Rais. Anapofariki mgombea Ubunge au Udiwani, uchaguzi mkuu nchi nzima huendelea, isipokuwa katika jimbo au kata husika ambayo mgombea amefariki. Hata hivyo, sheria ya uchaguzi inaweza kufanyiwa marekebisho kwa kuzingatia wakati uliopo, mazingira halisi ya nchi, tafiti na tathmini za uchaguzi zinazofanyika na jambo hili linaweza kujadiliwa pia.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y MHE. GRACE V. TENDEGA) aliuliza:-
Mojawapo ya jukumu la Serikali katika kupambana na ugonjwa wa UKIMWI ni kuhakikisha wanatoa elimu kwa umma na waathirika kupatiwa huduma za matibabu kulingana na masharti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo ndiyo hufadhili huduma hizo kwa takribani 100%.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba huduma hizo zinaendelea kutolewa hata kama msaada kutoka Shirika la Afya Duniani utatetereka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Grace Tendega, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha kwamba huduma za elimu kwa umma na matibabu kwa waathirika wa UKIMWI zinaendelea kutolewa hata pale misaada ya hisani itakapopungua, Serikali tayari imeanzisha Mfuko wa UKIMWI kupitia marekebisho ya Sheria ya UKIMWI Namba 6 ya mwaka 2015 kwa madhumuni ya kuratibu ukusanyaji fedha za kudhibiti UKIMWI nchini. Hata hivyo, Serikali kupitia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021) na bajeti za kila mwaka inaendelea kuhakikisha huduma kwa waishio na VVU na elimu kwa wananchi kuhusu UKIMWI inakuwa ajenda muhimu katika nchi yetu.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA (K.n.y. MHE. EZEKIEL M. MAIGE) aliuliza:-
Kutokana na mabadiliko ya tabia nchi matukio ya majanga na maafa kama mvua za mawe pamoja na matetemeko ya ardhi yameanza kutokea mara kwa mara na mara zote Serikali imekuwa haina maandalizi ya kifedha na vifaa vya kusaidia wahanga kwa muda mfupi na muda mrefu na badala yake imekuwa ikitegemea zaidi wasamaria wema wa Mataifa mengine:-
(a) Je, ni kwa nini Serikali imekuwa haisaidii kifedha na vifaa zaidi ya kuhamasisha wasamaria wema wasaidie na wenyewe kubaki na jukumu la kupeleka wataalam kama Madaktari na kuratibu misaada pekee?
(b) Je, ni kwa nini Serikali isianzishe Mfuko wa Maafa Kitaifa ambao utakuwa unachangiwa wakati wote kwa njia endelevu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Msalala, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali inatambua kuwa ni wajibu wake kusaidia wananchi pindi wanapokumbwa na maafa yanayoharibu mfumo wa maisha ya kila siku. Katika kutekeleza wajibu huo Serikali imekuwa ikitoa misaada ya aina mbalimbali kwa waathirika wa maafa ikiwemo vyakula, malazi, vifaa vya kibinadamu na huduma za afya.
Vilevile Serikali imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kununua mahitaji ya dharura ya kibinadamu pamoja na kurejesha miundombinu iliyoharibika. Aidha, katika jitihada za kuhakikisha kuwa misaada inawafikia wananchi kwa haraka Serikali tayari ina maghala ya maafa yenye vifaa mbalimbali vya kukabiliana na maafa katika Kanda sita nchini.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema ifahamike kuwa suala la kukabiliana na maafa ni mtambuka na haliwezi kuachwa mikononi mwa Serikali peke yake kwani wakati mwingine maafa yanakuwa ni makubwa sana hivyo kuhitaji juhudi za pamoja baina ya Serikali, wadau wa maendeleo na wananchi katika kuyakabili na kurejesha hali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua hilo Serikali ilileta Muswada wa Sheria ya Maafa uliopitishwa na Bunge lako Tukufu na kuwa Sheria Namba 7 ya mwaka 2015 ambayo pamoja na mambo mengine inaelekeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Maafa na pia, Kifungu 31 kinaainisha vyanzo vya mapato vya Mfuko huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa wadau wa maendeleo pamoja na wananchi kwa ujumla kuendelea kushirikiana na Serikali katika harakati zake za kujiandaa, kukabili na kurejesha hali, ili kuhakikisha jamii yetu inakuwa salama zaidi dhidi ya majanga mbalimbali.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Vijana wengi nchini wanakabiliwa na tatizo kubwa sana la ukosefu wa ajira.
Je, Serikali imejipanga vipi kutatua tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA: alijibu:-
Mheshiwa Spika, kwa niaba wa Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa utafiti wa nguvukazi wa mwaka 2014, kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana ni asilimia 11.7. Ili kukabiliana na tatizo hilo, Serikali imejipanga kutekeleza yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, moja, ni kuendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Ujuzi Nchini ambao umelenga kutoa mafunzo ya vitendo yatakayofanyika maeneo ya kazi. Aidha, ili kuwapa vijana wengi fursa za mafunzo Serikali imeanzisha programu maalum ya kutambua ujuzi uliopatikana kupitia mfumo usio rasmi na kuurasimisha kwa kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wale watakaobainika kuhitaji na kuwapa vyeti.
Mheshimiwa Spika, ili kuthibitisha hilo kwa sasa Serikali inaendelea kufundisha vijana 400 katika kiwanda cha Took Garment Company Ltd. lengo ni kufundisha vijana 1000. Mafunzo mengine yataanza mwezi Novemba, 2016 katika kiwanda cha Mazava Fabrics, Morogoro pamoja na DIT Mwanza ambayo ni kwa ajili ya kutengeneza viatu na bidhaa za Ngozi. VETA nchi nzima watafundishwa vijana 4000. Serikali inaendelea kujadiliana na taasisi nyingine zikiwemo kiwanda cha Karanga Moshi na nyinginezo.
Mheshimiwa Spika, pili, ni kuwezesha vijana kuwa wajasiriamali kwa kuwatambua vijana na mahitaji yao katika ngazi mbalimbali na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa makundi mbalimbali ya vijana.
Mheshimiwa Spika, tatu, ni kuhamasisha vijana wenye utaalamu mbalimbali kushiriki katika shughuli za kiuchumi kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika sekta zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira hususani kilimo na biashara.
Aidha, Serikali itajikita zaidi kuhamasisha vijana na kuwawezesha kuwekeza kwenye viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili kufikisha lengo la asilimia 40 ya nguvu za kazi nchini kuwa katika sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2020 kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
Mheshimiwa Spika, nne ni kuendelea kuimarisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao kupitia mfuko huo vikundi vya vijana 6,076 vyenye wanachama 30,380 vimepata mikopo yenye masharti nafuu ya kiasi cha shilingi takribani bilioni moja na milioni mia sita kupitia kwenye SACCOS zao za Halmashauri za Wilaya ili ziweze kuwakopesha vijana mikopo ya masharti nafuu na hivyo vijana waweze kujiajiri.
MHE. CAPT. ABBAS ALI MWINYI (K.n.y. MHE. KHAMIS MTUMWA ALI) aliuliza:-

Serikali ilizuia sherehe za kuadhimisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuelekeza kusheherekea kwa kufanya usafi wa mazingira. Wakati zuio hilo linatolewa maandalizi ya sherehe hizo yalikwishaanza na gharama mbalimbali zilitumika ikiwemo mafunzo ya halaiki ya watoto:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwafidia wale waliotumia gharama binafsi wakiwemo wakufunzi wa maandalizi ya sherehe hizo?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khamis Mtumwa Ali, Mbunge wa Kiwengwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, maadhimisho ya sherehe za miaka 52 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 2016 yalifanyika kwa wananchi kupumzika siku hiyo na kuendelea kutafakari umuhimu wa Muungano wetu ambao unazidi kuimarika na hivyo kufanya shughuli mbalimbali kama vile usafi wa mazingira, kujitolea katika shughuli mbalimbali za maendeleo na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali haina kumbukumbu zozote za watu binafsi waliotumia rasilimali zao kwa maandalizi ya sherehe hizo. Maandalizi hufanyika baada ya idhini kutolewa na viongozi wakuu hivyo hakuna mtu, kikundi au taasisi itakayofidiwa kwa namna yoyote ile.
MHE. RUTH H. MOLLEL aliuliza:-

Mashirika ya Hifadhi ya Jamii yamewekeza katika miradi mbalimbali kwa kutumia michango ya wanachama:-
Je, wanachama wamepata gawio kiasi gani na faida ya uwekezaji?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ruth Hiyob Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifuko ya hifadhi ya jamii imegawanyika katika makundi makuu mawili. Mifuko inayoendeshwa kwa mfumo wa pensheni yaani defined benefits schemes na mifuko inayoendeshwa kwa mfumo wa akiba yaani defined contribution schemes. Mfumo unaotumika Tanzania ni mfumo bayana wa pensheni (defined benefits schemes).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa mfumo huu, malipo ya mafao ni ahadi ambayo mfuko huahidi kumlipa mwanachama pindi anapojiunga na mfuko kupitia vikokotoo maalum vya mafao vilivyowekwa kisheria. Hivyo, katika mfumo huu hakuna utaratibu wa kumlipa mwanachama gawio badala yake ukokotoaji wa mafao ya mwanachama huzingatia mshahara wa mwanachama na muda wa uchangiaji. Kwa mwanachama aliyechangia kwa kipindi kinachostahili (vesting period) na ambaye mshahara wake ulikuwa ukiongezeka katika kipindi cha ajira yake kiasi cha mafao anacholipwa wakati wa kustaafu ni kikubwa zaidi kuliko kiasi alichochangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiasi cha pensheni wanacholipwa wastaafu nchini ni asilimia 72 ya mishahara yao ya mwisho. Kiasi hiki hulipwa kila mwezi kwa muda wote wa uhai wa mwanachama. Hivyo, uwekezaji na faida yote inayopatikana katika uwekezaji unaofanywa na mifuko ya hifadhi ya jamii husaidia mfuko husika kuweza kulipa mafao kama ulivyoahidi pamoja na mafao mengine ya muda mfupi kama vile mafao ya uzazi, matibabu na mazishi.