Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Abdallah Saleh Possi (27 total)

MHE. MWANTUMU D. HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri aliyoyasema Mheshimiwa Waziri, naomba niongeze swali langu la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kuna Askari Polisi ambao kwa maksudi wanafumbia macho masuala ya biashara za madawa ya kulevya katika kuhakikisha mipango ya Serikali ya kudhibiti madawa ya kulevya inafikiwa. Je, kutakuwa na utaratibu gani wa kuwadhibiti Askari ambao hawaendi na kasi ya kupambana na biashara hiyo haramu ya madawa ya kulevya? (Makofi)
MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI - NAIBU WAZIRI, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU: Mheshimiwa Spika, labda niseme tu kutokuchukua hatua kuzuia uhalifu ni kosa la jinai kisheria. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge, Wabunge wote au mwananchi yeyote mwenye taarifa kuhusu Askari ambaye kwa maksudi kabisa hajatimiza wajibu wake, aviarifu vyombo husika na Askari huyo atachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake ya kweli. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kumekuwepo na malalamiko mengi sana kutoka kwa wananchi wa Mwakata walioathirika na hiyo mvua ya tarehe 3 mwaka jana kwamba usimamizi wa misaada mbalimbali nje ya ile iliyotoka Serikalini umekuwa na harufu mbaya, umekuwa na dalili za ufisadi. Nataka kujua Serikali iko tayari kufanya uchunguzi maalum wa Kiwizara ili kujua misaada yote iliyokusanywa na jinsi ambavyo ilitumika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, maafa haya yalikuwa na madhara makubwa sana kwa wananchi wanaoishi kwenye nyumba za tope. Serikali katika Ilani yake inayoitekeleza sasa hivi moja ya mkakati ni kujenga nyumba bora kwa maana nyumba za saruji. Nataka kujua Serikali imefikia wapi katika kupunguza ushuru wa vifaa vya ujenzi hasa simenti na kuweka standardization ya bei ili wananchi wanaoishi upande wa Magharibi mwa nchi yetu ambako hakuna viwanda na huipata bidhaa hiyo kwa gharama kubwa waweze kuipata kwa bei rahisi ili waweze kujenga nyumba bora na kuepuka majanga kama haya ambayo yanaweza yakawa yanajirudia endapo nyumba zitaendelea kutokuwa na ubora?
NAIBU WAZIRI WA SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI): Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ni kwamba Serikali ipo tayari siyo tu kufanya uchunguzi, lakini kuhakikisha kwamba kuna usimamizi wa karibu wa misaada yote inayotolewa kwa ajili ya kuwasaidia waathirika.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali kupitia Wizara husika na nafikiri Waziri yupo, zinatekeleza mikakati maalum ya kuhakikisha kwamba Watanzania wana uwezo wa kujenga nyumba kwa gharama nafuu.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wizara haijataja asilimia ngapi itakwenda kwa vijana wa kike na wa kiume; naomba Wizara ichukue ushauri wangu kwamba zile fedha zitakapopelekwa halmashauri waweze kusema asilimia kumi itakuwa kwa vijana wa kike na wa kiume na hii itapunguza mkanganyiko katika halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze katika maswali yangu mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
(a) Je, kwa nini Serikali isianzishe dhamana kwa vijana kukopa (credit guarantee scheme for youth)?
(b) Je, Serikali inaona kuna umuhimu wa kujenga mfumo madhubuti wa hifadhi ya jamii ili kuwezesha vijana kuweka akiba yao ya uzeeni, kupata bima ya afya na hata kuweza kupata mikopo katika biashara zao?
NAIBU WAZIRI WA SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Spika, katika eneo la kwanza la mikopo kwa ajili ya vijana, upo mpango wa muda mrefu na wa muda mfupi. Kwa sasa Serikali imeendelea kutoa mikopo kwa vikundi mbalimbali vya vijana kupitia katika SACCOS za Halmashauri lakini mpango wa muda mrefu ni kuja kuanzisha benki maalum ya vijana ambayo ndiyo itakuwa sehemu pekee ya vijana wengi kupata mikopo. Kwa hiyo, mpango wa muda mrefu ni uanzishwaji wa benki lakini tumeanza na SACCOS kwa ajili ya kuwajengea tabia vijana ya kufahamu masuala ya fedha kwa maana ya ukopaji na nidhamu ya urudishaji fedha.
Mheshimiwa Spika, la pili la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwashirikisha vijana, tayari katika programu mbalimbali za Mifuko ya Hifadhi za Jamii wamekuwa na eneo hili la kuwashirikisha vijana kupitia shughuli mbalimbali. Mojawapo ni Shirika la NSSF ambao tayari wameanzisha programu ambayo inaitwa AA Plus kwa maana ya Akiba na Afya kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, ambapo wanafunzi watachangia Sh. 20,000 kwa mwezi na watapata matibabu bure kwa muda wote ambao watakuwepo vyuoni lakini atakapohitimu mafunzo yake ya chuoni ile fedha anaweza kurejeshewa au akiamua ibaki kama akiba basi anaendelea kuitumia ikiwa ni sehemu yake pia kumsaidia baadaye kupata mikopo akiwa mwanachama wa shirika.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majawabu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
(a) Hoja ilikuwa ni kwa namna gani vyombo vya Kiserikali vinaweza kusaidia au kushirikiana na hawa watumiaji wa uraibu huu ili kuweza kuzifikia zile channel za waagizaji, wasambazaji na watumiaji. Je, kuna mlinganisho gani wa wale waliokamatwa pamoja na watumiaji wenyewe ambao wako mitaani? Serikali inaweza kutupa ulinganisho kwa sababu mitaani wako wengi lakini ambao wanakamatwa ni wachache?
(b) Ni kweli kuna baadhi ya watumiaji wako katika maeneo ambayo wanapatiwa huduma za kupata nafuu. Vijana hawa na watu wengine kwa jumla wanatumia dawa hizi na wakati mwingine kwa vishawishi lakini na wakati mwingine kwa kukata tamaa tu za maisha. Sasa mara baada ya kwisha kuwapa dawa hizi au nafuu hii wakitoka mitaani tumewaandalia mambo gani ambayo yanaweza kuwasaidia katika kujenga maisha yao huko mitaani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU - MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI): Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena.
(a) Serikali inatumia vyombo vyake na wakati mwingine nalazimika kupata taarifa kutoka kwa waraibu wa dawa hizi ili kuwakamata wafanyabiashara wakubwa na wadogo wa dawa hizi. Ndiyo maana tumefanikiwa sasa kukamata baadhi ya watu wenye majina makubwa katika biashara hii na ninavyozungumza wako vizuizini na kesi zinaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, limeulizwa swali kuhusu mlishanganisho; kuna mlinganisho gani kati ya wale wanaokamatwa na wale wanaotumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima niseme kweli, hakuna statistics lakini lazima tuweke wazi kwamba biashara hii tofauti na biashara ya nyanya au vitunguu ni biashara inayofanyika kwa kificho sana. Kwa hiyo, kusema kwamba utapata proper statistics itakuwa ni kudanganya watu. Wapo watu maofisini na katika maeneo mbalimbali wanatumia dawa hizo na huwezi ukajua moja kwa moja.
(b) Huduma za kupata nafuu. Kwanza naomba nirekebishe kitu kimoja ambacho kinaweza kikaonekana kama over generalization. Siyo kila mtumia dawa za kulevya anafanya hivyo kutokana na kukata tamaa ya maisha. Mifano ipo ndani na nje ya nchi. Akina Michael Jackson na wengine siyo kama walikuwa wamekata tamaa ya maisha. Vishawishi is fine!
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba juhudi za Serikali zinazochukuliwa za kukuza uchumi na kadhalika zina lengo la kuondoa ugumu wa maisha unaowaingiza vijana katika kutumia dawa za kulevya, kwa sababu sote tunafahamu kwamba vijana ndio nguvu kazi ya Taifa hili na nchi yeyote yenye nia thabiti ya kuendelea, ni lazima ichukue hatua madhubuti ya kuwalinda raia wake kutokana na kutumia dawa za kulevya.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo, niongezee tu kwamba juhudi za kuondoa watu kwenye vishawishi vya kutumia dawa za kulevya, siyo za Serikali peke yake, hili ni tatizo la kila mtu. Kwa hiyo, kila mtu awe ni kiongozi wa kisiasa, kiongozi wa familia na raia wote, wana jukumu la kuhakikisha kwamba wananchi wanaondokana na vishawishi vya kutumia dawa za kulevya mara baada ya kumaliza tiba inayohusika.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa naomba nipongeze juhudi za Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama kwa kutembelea vituo vyote vya utoaji wa madawa ya kulevya katika Mkoa wetu wa Dar es Salaam. Pia nipongeze juhudi za Madaktari na Wauguzi wa vituo hivi ambao wanafanya kazi kila siku bila kujali Jumapili, sikukuu, kila siku ya Mungu wanafanya kazi ya kuwasaidia vijana wetu. Sasa naomba niulize maswali mawili:-
Kwa kuwa, matumizi ya madawa ya kulevya yanazidi kuongeza katika Jiji la Dar es Salaam siku hadi siku, je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza vituo vya utoaji wa madawa hayo katika Jiji la Dar es Salaam kwa kuwa sasa hivi vituo vinavyotoa hayo madawa ni vitatu, Mwananyamala, Temeke na Muhimbili. Serikali ina utaratibu gani wa kuongeza vituo hivyo katika Jiji la Dar es Salaam?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa vijana wengi wameingia katika makundi ya madawa ya kulevya kwa sababu ya ukosefu wa kazi au shughuli mbalimbali za kujiajiri au ujasiriamali, je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kituo kikubwa cha walioathirika na madawa ya kulevya ambacho kitawasaidia hawa waathirika wapate mafunzo ya ujasiriamali?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI): Mheshimiwa Naibu Spika, moja, kuhusiana na mpango wa kuongeza vituo vingine. Serikali inatambua wingi wa wahitaji wa huduma ya kuondokana na urahibu wa madawa ya kulevya. Wazo la kujenga vituo hivyo ni zuri na pale uwezo utakaporuhusu, basi jambo hilo litafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusiana na uwezekano wa kujenga kituo ambacho kitawapa mafunzo. Katika swali la msingi nilishajibu kwamba tayari Serikali imeandaa mwongozo maalum utakaotumika na vituo mbalimbali vinavyowasaidia watu kuondokana na urahibu na mengineyo, mwongozo ambao bado utapitiwa na wadau, naamini kabisa hilo ni moja ya suala ambalo limezingatiwa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya nyongeza kutoka katika swali la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu hayo mazuri ambayo yametolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, tatizo hili la dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania, pamoja na kwamba siyo linaweza kujionyesha waziwazi lakini linaendelea kukua na tafiti zinatuambia mikoa ambayo iko katika maeneo ya mwambao mwa Bahari ya Hindi, Tanga, Mtwara, unakwenda mpaka Mwanza, yanaonekana kwamba ni maeneo ambayo tatizo la dawa za kulevya linaendelea kuwa kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pamoja na kuona umuhimu wa kuanza kutumia dawa ya methadone kuhakikisha inawatibu warahibu wa dawa hizi za kulevya, inaendelea kutoa wito kwa mashirika mbalimbali ili tuweze kuendelea kushirikiana na Watanzania wote kuhakikisha tunafanya kazi ya pamoja kuwaondoa watoto wetu katika tatizo hili la dawa za kulevya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, tatizo la dawa za kulevya bado linapambana na hali ya unyanyapaa kama tatizo la ugonjwa wa UKIMWI lililotangulia. Sasa ni wajibu wa kila Mtanzania tuanze kuondoa unyanyapaa, vijana wetu waweze kujitokeza kwa wingi, wapelekwe katika maeneo hayo yaliyopangwa kuwasaidia ili kwa pamoja tuweze kupambana na tatizo hili kwa vijana wetu na tusiendelee kuwaficha katika nyumba zetu, wale walioko mitaani, Serikali za Mitaa tushirikiane pamoja tuwalete ili waweze kupatiwa huduma hii na tuwarudishe katika hali yao ya kawaida.
MHE. STELLA IKUPA ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza:
(a) Je, ni lini Serikali itaziagiza Halmashauri na Manispaa, kutenga fungu maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu kama ilivyo ile asilimia 10 kwa wanawake na vijana?
(c) Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kufanya zoezi la utambuzi kwa watu wenye ulemavu, aina ya ulemavu walionao, pamoja na hali zao kiuchumi ili zinapotokea fursa iwe rahisi kuwafikia walengwa?
NAIBU WAZIRI WA SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI): Mheshimiwa Naibu Spika, moja, kuhusu kutenga asilimia ya mapato ya Halmashauri kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Kwanza niseme kabisa natambua utaratibu wa sasa wa kutenga asilimia 10 kwa maendeleo ya wanawake na vijana ulifanywa kutokana na kutambua tatizo la kuachwa nyuma kwa makundi haya muhimu. Falsafa hiyo hiyo inajengeka kwa watu wenye ulemavu. Hivyo basi, Serikali kwa kupitia taratibu zake za kiutawala na kisheria itaanza utaratibu wa kuutekeleza mpango huu pale hali itakaporuhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya mpango huo haujaanza kutekelezwa, nitoe wito kwamba katika asilimia hii 10 ya vijana na wanawake, basi kipaumbele maalum kitolewe kwa watu wenye ulemavu kwa mujibu wa Sheria Namba T isa (9) ya Mwaka 2010 kama nilivyoelezea kwa mujibu wa Kifungu cha tatu (3), pia kwa mujibu wa Kifungu namba 34(2), lakini pia kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inasema maana ya kubagua haitoizuia Serikali kuchukua hatua za makusudi ili kutatua matatizo mahsusi katika jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni wajibu wa Taasisi za Serikali kupitia Katiba na kupitia vifungu hivyo nilivyovitaja kutoa kipaumbele maalum kwa watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, namba mbili, kuhusu zoezi la utambuzi. Hapa kuna mawili; kwanza, tayari nilishazindua kazidata yenye taarifa za watu wenye ulemavu. Kazidata hiyo itatumika kufanya mambo mbalimbali ikiwemo utambuzi wa watu wenye ulemavu na mahitaji yao na inatarajiwa pale fedha itakapopatikana na hali ya teknolojia itakapoendelea, kazidata hii iunganishwe pia na kazidata nyingine zinazohusiana na taarifa ya hali ya watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niongeze kitu kimoja, kwamba tayari Serikali imeshatoa maagizo ya kuundwa kwa Kamati za Watu Wenye Ulemavu katika Halmashauri mbalimbali. Kamati hizi ndizo zitafanya kazi nzuri ya kuzishauri Halmashauri kuhusiana na mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu. Hivyo, kupitia Bunge hili nisisitize kutekelezwa kwa agizo hilo la Serikali la kuundwa kwa Kamati Maalum za Watu Wenye Ulemavu katika ngazi mbalimbali za Serikali za Mitaa.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri je, ni lini sasa Serikali itaanza kutoa mikopo hiyo?
Swali la pili, kwa kuwa wananchi wa Mkoa wa Manyara hasa Mbulu Vijijini wako tayari kabisa kwa elimu hiyo ya ujasiriamali, je, Mheshimiwa Waziri anaweza kusema anaweza kuanza na Mkoa huo kwa kuwa uko tayari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la lini fedha hizo zitaanza kugawanywa lazima tuangalie practical realities. Kwa sababu elimu inahitajika na ahadi haikuwa imewekewa time frame ni vizuri tuelewe kwamba fedha hiyo itatolewa ndani ya kipindi hiki, na mapema iwezekanavyo, mara baada ya taratibu zote za kuhakikisha matumizi salama na yenye tija ya kifedha yanakamilika. Kwa hiyo siwezi nikasema exactly ni lini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu whether kuanza na Mkoa upi, Manyara au mwingine na hili pia litategemea sana na hali halisi, lakini ninampongeza na ninawashukuru wananchi wa Manyara, kwa kuonesha utayari katika suala hilo.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo ahadi nyingi zilizotolewa na viongozi kuanzia Awamu ya Tatu, Awamu ya Nne na sasa Awamu ya Tano. Je, kwa nini Serikali isiweke utaratibu wa kuandaa ahadi hizo kwa kutengeneza kitabu cha mpango wa utekelezaji na sisi Wabunge tukagawiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Malocha kwa kifupi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ushauri mzuri na Serikali tunaupokea.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize
maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwanza
napenda niishukuru sana Serikali kwa kutupatia kiasi kidogo cha chakula katika Wilaya ya
Mpwapwa.
Kwa kuwa, Wilaya ya Mpwapwa ina Majimbo mawili, Jimbo la Mpwapwa na Jimbo la
Kibakwe, na kwa kuwa chakula hicho ambacho tumepatiwa ni kidogo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutuongezea chakula cha njaa Wilaya ya Mpwapwa?
Swali la pili, kwa kuwa hivi sasa baadhi ya wananchi wameacha kulima mashamba yao
wanalima vibarua ili wapate hela ya kununua chakula. Je, utakubaliana na mimi kwamba iko
haja sasa ulete chakula hicho haraka kwa Wilaya ya Mpwapwa na Wilaya ya Kongwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, VIJANA, AJIRA NA WALEMAVU -
(MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI): Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mbunge wa Jimbo
la Mpwapwa Mheshimiwa George Malima Lubeleje, kwamba Serikali inatambua jukumu lake la
kuwalinda na kuwasaidia wananchi wote wanaopatwa na matatizo mbali mbali, ikiwemo baa
la chakula.
Kuhusu swali lake la pili, tunafahamu umuhimu hiyo na tathmini itafanywa ili kuwezesha
upatikanaji wa chakula hicho kwa haraka.
MHE. DKT. ELLY M. MACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Sikuridhika sana na jibu lililotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri hasa katika kipengele (a). Kwa ajili hiyo basi, naomba kumuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ni lini basi mchakato wa mabadiliko ya sheria utafanyika ili kuhakikisha kwamba sheria inawapigania watu wenye ulemavu kwa kuwaongezea umri wa kustaafu kwa kuwa umri wao wa kuanza shule unakua umechelewa ili waweze kupata nafasi ya kufanya kazi zaidi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni mechanism gani ambayo Serikali imeweka katika kuhakikisha kwamba taasisi zake pamoja na sekta binafsi zinatenga asilimia tatu katika kila waajiriwa 20? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Elly Macha kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza la ni lini, lazima niseme kwamba siwezi nikatoa specific date kwa sababu ili kubadilisha umri wa kustaafu kuna watu wengine wanahusika kama waajiri, taasisi zinazohusiana na hifadhi za jamii na watu wenye ulemavu wenyewe. Tayari assignment ya kwanza kuifanya baada ya kushika nafasi hii ilikuwa ni kukutana na watu wenye ulemavu na moja ya mambo ambayo tulikubaliana ni kwamba walete maoni yao yote ambayo yatapelekea kubadilishwa kwa Sheria Na. 9 ya mwaka 2010 ili kuboresha baadhi ya mambo yakiwemo masuala yanayohusiana na ajira kwa watu wenye ulemavu kwa sababu tunaamini katika ile principle inayosema nothing for us without us ambayo ni muhimu sana kwa watu wenye ulemavu. Kwa sababu maoni yao yanafanyiwa kazi siwezi nikatangulia kabla ya kupata maoni yao kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme tu natambua kwamba wako baadhi ya watu wengine walianza kufanya hivyo mwaka 2003 nchini Kenya, umri wa kustaafu wakati huo ulikuwa ni miaka 55 kwa lazima kwa watu wenye ulemavu ilikuwa ni miaka 60 lakini mwaka 2009 ikabadilishwa. Serikali ya Kenya ilivyosema umri wa kustaafu kwa lazima ni miaka 60, mwaka 2013 ilipelekwa Bill ya kutaka kuongeza umri wa kustaafu kwa watumishi wenye ulemavu Kenya kufikia miaka 65 lakini mpaka navyozungumza Bill hii bado haijafanyiwa mabadiliko kutokana na sababu mbalimbali za kitaalamu zinazosababisha review ya sheria hiyo kuwa ngumu kidogo. Hata hivyo, hilo ni wazo zuri na tutalifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu mkakati uliowekwa, sheria imeonyesha wazi na tayari tumeshatoa maelekezo kwamba waajiri wote ni lazima watekeleze hili na Maafisa Kazi wanapokwenda kusimamia utekelezaji wa sheria baadhi ya mambo ambayo wanapaswa kuuliza ni utekelezwaji wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ikiwemo percentage na mambo mengine kama reasonable accommodation. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Elly Macha kwamba Serikali inafuatilia kwa makini usimamizi wa sheria hii kwa hiyo asiwe na wasiwasi wowote ule.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE WALEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana ambayo ameyaweka mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulihakikishia Bunge lako kwamba wakati tunatunga sheria hii kwa ajili ya kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanapata haki sawa katika nchi yetu, kifungu cha 12(1)(a) cha sheria hiyo kinalipa nguvu na mamlaka Baraza hili la Watu Wenye Ulemavu kuangalia matatizo na mambo mengine yote ambayo yamekuwa yakiwakumba watu wenye ulemavu nchini na kutoa mapendekezo na kuishauri Serikali nini cha kufanya. Kwa sababu tumeendelea kutenga fedha za kulifanya Baraza hili liwe linakutana, ningeshauri sana tufanye kazi kwa karibu na Baraza na yale ambayo wanayaona ni mambo ambayo yanatakiwa yafanyiwe mabadiliko ya kisheria, ya kikanuni na vitu vingine, basi wanaweza kulitumia lile Baraza tukashauriana na Serikali na tukaona lini na namna gani tunaweza tuka-consider hayo mambo ambayo ni ya msingi sana katika kuweka welfare ya walemavu nchini.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, disability is not inability. Kwa muda mrefu tumepiga kelele sana kwamba majengo hasa madarasa yawe disabaility friendly ili watoto wenye ulemavu waweze kusoma, lakini mpaka leo tunashuhudia madarasa yanajengwa hayana ngazi za kuwasaidia au ramps ili hawa watoto waweze kusoma kama wenzao na kwa kufanya hivyo suala la kwamba waongezewe muda wa kustaafu halitakuwepo. Serikali inatoa kauli gani kuhakikisha kwamba majengo yote ya Serikali yanakuwa disability friendly ili watoto waweze kuingia madarasani toka wakiwa na umri mdogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme tu wazi kwamba dhana ya elimu shirikishi au dhana ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za jamii kwa watu wenye ulemavu inaendana kabisa na kubadilisha mazingira ili kumfanya mtu mwenye ulemavu afike pale anapotaka bila vikwazo vyovyote vile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Ofisi ya Waziri Mkuu ilishatoa maagizo kwa Halmashauri mbalimbali ambazo zinahusika na ujenzi wa miundombinu mbalimbali kuhakikisha kwamba majengo yanayojengwa hasa ya shule yanakuwa ni shirikishi, yana hali ya kumfanya mtu mwenye ulemavu afike bila matatizo yoyote darasani. Siyo tu kwamba yalikuwa maagizo bali hilo ni takwa la Sheria Na. 9 ya mwaka 2010. Kwa hiyo, niseme tu kilichobakia ni kufuatilia utekelezaji wa sheria hiyo.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Meshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, je, Mswada huu wa Sheria ya Makao Makuu utaletwa Bungeni mwaka huu?
Swali la pili, je, bajeti kwa ajili ya mchakato huu imetengwa katika kipindi hiki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kama Muswada huu utaletwa mwaka huu au la kwa kweli itategemea hasa na majibu yatakayotokana na kikao cha wataalam. Kwa hiyo, kama maoni yao hayatokuwa na marekebisho mengi ni wazi kwamba muswada huu utaletwa mapema. Lakini kama maoni yao yatasababisha marekebisho makubwa katika muswada huu, basi muda unaweza ukahitajika zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili kuhusu suala la bajeti ni wazi kwamba bajeti haiwezi ikawa imepangwa kipindi hiki, kwa sababu sheria hiyo bado haijapita, na kwa vyovyote vile sheria itakapopitishwa Bungeni, itaweka wazi muda wa kuanza utekelezaji wake na kwa wakati huo ndio bajeti itapangwa.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Kwa kuwa dhamira inaonekana ni dhahiri ni mchakato tu unaendelea, je, ni lini Serikali itatoa maagizo kamili kwa Wizara zake zote ili pale panapotakiwa ujenzi wowote mpya au uendelezaji wa majengo au miundombinu ya Ofisi zake ifanyike Dodoma badala ya kuendelea kufanyika Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, labda nianze kwa ufafanuzi kwamba tofauti na nchi nyingine, kwa mfano kama vile Rwanda ambapo Makao Makuu yalitamkwa kabisa kisheria, Tanzania hatukuwa na Sheria inayotamkwa kwamba Makao Makuu ni Dodoma. Kilichotokea ni kwamba Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu yenyewe ndio iliyoanzishwa kisheria.
Sasa sheria hii ndio itatoa kwamba itakuwa binding, itailazimisha Serikali kuhamisha Makao Makuu Dodoma; kwa maana hiyo basi kuharakisha mchakato wa uendelezaji wa Makao Makuu na baadaya kufanyika hivyo ina maana kila kitu kitakuwa kinafanyika Dodoma kwa mujibu wa sheria.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa matatizo haya ya wafanyakazi wa migodini yamekuwa yakijirudia mara kwa mara katika Bunge hili, tumekuwa tukiyasikia, nataka kujua.
Je, ni lini sasa Serikali tafanya ukaguzi huo wa makampuni makubwa ya madini na kuwabaini wadanganyifu ambao wanakwepa kuwalipa wafanyakazi mafao yao ya NSSF na kodi nyingine?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa tumegundua kuna udanganyifu mkubwa sana katika migodi na makampuni makubwa ambayo yamekuwa yakihudumu katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, makampuni hayo wakati mwingine yamekuwa yakitoa salary slip mbili, moja ikionesha kiwango cha chini cha malipo ya mshahara na hicho ndicho kinachofanya contribution kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, lakini wana salary slip nyingine ambazo kodi za nchi hazikatwi inavyotakiwa wala mafao ya wafanyakazi hayapelekwi inavyotakiwa.
Naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu, tumegundua tatizo hilo na baada ya muda si mrefu mtasikia kikosi kazi kimeshaundwa kikiwa na wajumbe kutoka Wizara ya Fedha, TRA, Mwanasheria Mkuu, Ofisi ya kwangu - Ofisi ya Kazi, Kamishna Mkuu na watu wengine. Watafanya ukaguzi na kuwabaini hao wote na hatua kali zitachukuliwa na makato hayo yataanza kupelekwa kwa kuzingatia mshahara halisi wa mfanyakazi.
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ameelezea kwamba katika hivi viwanja vya ndege kuna wheel chairs na stretchers, lakini swali langu la msingi lilihoji kwa habari ya ambu-lift. Ukisema wheel chair inamsaidia tu yule mhitaji kumpeleka mpaka eneo la ndege, lakini anapofika pale inabidi abebwe juu juu na wale staff wa airport kitu ambacho kinakuwa ni very risk!
Mheshimiwa Naibu Waziri, kutokana na umuhimu wa ambu- lift, ni nini commitment ya Serikali kuhusiana na uwepo wa huduma hii katika viwanja vyote vya ndege nchini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme natambua majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Ujenzi. Niongezee tu mambo machache kuhusu huduma kwa watu wenye ulemavu katika viwanja vya ndege na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Sheria Na. 9 ya mwaka 2010 ilifuta sheria za zamani zilizokuwa zinazungumzia masuala ya watu wenye ulemavu, na moja ya mambo ambayo yameelezwa wazi katika sheria mpya hii ni kutambua suala la kufikika kirahisi na kupata huduma mbalimbali kirahisi kwa watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria hii ilianza kufanyakazi mwaka 2012 na ni wazi kwamba katika kipindi ambacho sheria hii imeanza kufanya kazi yapo, majengo na ipo miundombinu mingi sana ya Serikali ambayo kwa namna moja au kwa namna nyingine ilikuwa imejengwa kizamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, commitment ya Serikali kuyabadilisha ipo, lakini hili ni suala ambalo litachukuwa muda na Ofisi ya Waziri Mkuu itakuwa inawasiliana na Wizara nyingine kadri inavyowezekana kuhakikisha kwamba taasisi zote za Serikali katika nyanja mbalimbali, elimu, afya, miuondombinu na kadhalika, zinachukuwa hatua zinazofaa ili kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanapata huduma stahiki, kokote wanakokwenda.
MHE. MBAROUK SALIM ALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Lakini pamoja na majibu hayo nina maswali tena mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza katika awamu iliyopita kulikuwa na watu mashuhuri ambao walijilabu kwamba wanawajua watu ambao wanajishughulisha na biashara za dawa za kulevya. Je, Serikali inaonaje kuwaona watu hao au vingozi hao na kuwasihi ili wawapatie majina hayo ili Serikali ipate pa kuanzia? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, dawa za kulevya zinapiga vikali katika mishipa ya riyakh, na inaathiri sana nguvu za vijana ambao kwa kweli baada ya miaka 10, 15 nchi hii inaweza ikawa na mazezeta watupu. Sasa pamoja na Serikali kusema kwamba inabadilisha au ina muundo mpya wa mamlaka ya kudhibiti dawa za kulevya.
Je, Naibu Waziri anatuambiaje katika mamlaka hiyo mpya au katika mabadiliko hayo mapya kuna nini ambacho kinaweza kikakuhakikishia kwamba hali hii inapungua kwa kiasi kikubwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kwa kipengele cha kwanza kuhusiana na watu waliotoa taarifa kwamba wanawafahamu watu wanaojihusisha na dawa za kulevya, niseme tu kwamba Serikali iko tayari kushirikiana na mtu yeyote yule mwenye taraifa zinazohusu au zinaweza kupelekea kukamatwa kwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, japo sijalielewa vizuri niseme kwamba baada ya kupitishwa kwa sheria mpya ya mwaka 2015 kama nilivyoeleza awali Serikali itakuwa imepata nguvu katika maeneo yote ya kuchunguza kukamata na kuthibiti dawa za kulevya ikiwemo pia kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kwamba biashara ya dawa za kulevya inathibitiwa.
Mheshimiwa Spika, na jambo moja tu la uangalifu katika lugha hizi, watu wanaopata magonjwa ya akili kutokana na dawa za kulevya hatuwaiti mazezeta.
Mheshimiwa Spika, naomba Waheshimiwa Wabunge tuwe very sensitive katika lugha tunayotumia dhidi ya wagonjwa au watu wenye aina mojawapo au nyingine ya ulemavu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, inategemea na viwango, kuna wahanga au warahibu, kuna wagonjwa wa akili wa kawaida, lakini maneno kama mateja au mazezeta ni maneno ya unyanyapaa yaani stereo type. (Makofi).
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri niliyopewa, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Serikali imejipanga vipi kwa ajili ya kutoa elimu ili fedha zitakazotolewa zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa taasisi nyingi za fedha zimeonekana zinatoa mikopo kwa wanawake na vijana, Serikali imejipanga vipi katika kuinua uchumi au kuwawezesha kiuchumi wazee? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE WALEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga vizuri ili kuhakikisha kwamba elimu inatolewa kwa wajasiriamali wote hasa ukizingatia kwamba moja ya changamoto zilizopo kwa Mifuko ya mwanzo ilikuwa ni elimu ya ujasiriamali. Kwa hiyo, hilo tayari limeangaliwa na Serikali imejipanga vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wazee, bado Serikali inaangalia changamoto mbalimbali na tayari Ofisi ya Waziri Mkuu inaangalia kwa mfano namna ya kurasimisha pensheni ya wazee, lakini suala hili linafanyiwa kazi na pale litakapokamilika basi taarifa rasmi itatolewa na ikibidi sheria rasmi itatungwa.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba niulize maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa makazi haya ya watu wenye ulemavu yako ndani ya Halmashauri, je, Serikali sasa haioni haja Halmashauri ikatenga bajeti ndogo ili iweze kusaidia upatikanaji wa chakula ili wananchi hao wawe na uhakika wa kupata chakula badala ya kusubiri msaada kutoka kwa mwananchi mmoja mmoja? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na jitihada za Serikali za kupambana na mauaji haya. Je, sasa naomba Serikali inihakikishie ina mkakati gani wa haraka kuhakikisha watu hawa wanahudumiwa na vitendo hivi vinakoma ili wananchi hawa waweze kuungana na ndugu zao na jamii ili waweze kushirikiana katika shughuli mbalimbali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Halmashauri, ni kweli, kwa mujibu wa Sheria ya Watu wenye Ulemavu labda nifafanue kwanza; jukumu la kwanza la kumlinda mtu mwenye ulemavu linaanzia kwenye familia baadaye taasisi, Serikali kwa upande wa Halmashauri ni sehemu ya mwisho kwenye makazi kwa sababu msisitizo uko katika kuishi katika hali ya kuchangamana na wengine na kweli Halmashauri zinaagizwa kuhakikisha kwamba zinatenga bajeti kwa ajili ya kutoa misaada maalum hasa ya makazi na chakula kwa wale wanaohitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni jambo ambalo liko wazi kisheria, na tayari Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikitoa maagizo hayo na kwa kutumia fursa hii niwakumbushe wote wanaohusika na Wabunge pia kwa sababu ni Wajumbe katika Mabaraza ya Madiwani ambayo yanahusika kupanga bajeti ya Halmashauri mbalimbali kuhakikisha kwamba wanasimamia bajeti katika Halmashauri zao ili kuhakikisha kwa mba watu wenye ulemavu wanapewa kipaumbele katika masuala mbalimbali si tu ya makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu jitihada maalum, niseme tayari kumekuwa kuna jitihada mbalimbali na hata juzi tu nafikiri, siku ya Ijumaa kwa wale wanaosikiliza habari walisikia kuhusu hukumu nyingine ambayo ilitolewa na Mahakama Kuu - Kagera kwa watu waliofanya tukio mwaka 2008, majina yao siyakumbuki, lakini hizo hukumu zimetolewa na nafikiri katika mwaka huu kumekuwa kuna hukumu zaidi ya tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba makosa ya mauaji kwa sababu yana adhabu kubwa, kifo ushahidi wake inabidi uwe watertight kwa maana hiyo huwezi pia wakati mwingine ukaharakisha kutoa hukumu kwa sababu wengine wanasema kwa lugha ya kingereza justice rushed is justice buried na kuna changamoto zingine pia katika kesi hizi. Kuna baadhi ya watu hasa ukizingatia baadhi ya matukio yamekuwa yanafanywa na watu wa karibu katika familia, kumekuwa kuna ugumu wa kupata ushahidi kwa haraka, lakini niseme tu jitihada zinaendelea na zipo ambazo zimefanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa yote kama nilivyosema, suluhisho la kudumu ni katika kubadilisha tabia na ndio maana siku zilizopita chache katika wiki ya vijana Serikali ilianzisha mkakati maalum wa kuhakikisha kwamba elimu inatolewa ili tatizo hili liishe na nina imani hili tatizo litakwisha ndani ya muda mfupi.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa watoto wenye mtindio wa ubongo wamekuwa wakipata matatizo mbalimbali sawasawa na wale watoto wenye ulemavu wa ngozi, hususan suala la haki ya kupata elimu. Naomba nifahamu Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia watoto hawa ili wapate haki ya kupata elimu kwa kuanzisha madarasa maalum au shule maalum walau kwa kila Wilaya ili watoto hawa wapate haki hiyo ya elimu ikiwemo Wilaya yangu ya Babati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kusema kwamba wale watoto wenye learning difficulties nachelea kutumia jina mtindio wa ubongo sio wote wanaohitaji kwenda kwenye madarasa maalum. Tutofautishe normal learning difficulties na usonji yaani autism wako wengine ambao wanaweza wakaanzishwa katika shule za kawaida kabisa na wakafunguka, actually kuna taarifa za watu ambao walionekana kama wana learning difficulties wakasoma katika elimu shirikishi na wakafaulu mitihani ya darasa la saba na wako wengine depending on the level wanaweza wakaishi kwa kusoma na kufanya kazi katika mazingira mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo msisitizo upo katika elimu shirikishi isipokuwa kwa wale ambao kutokana na hali yao basi kuna madarasa maalum ninafahamu kuna shule maalum ambazo zimeanzishwa kwa ajili hiyo na Serikali inafanya jitihada za kutosha ili kuhakikisha kila mtoto anapata elimu kwa sababu tunaamini hali ya ulemavu ni sehemu tu ya mjumuiko wa binadamu kwa hiyo kila mwanadamu ana haki ya kupata fursa sawa na kila binadamu ana namna fulani ya kipaji chake ambacho hakipaswi tu kupuuzwa kwa ajili ya hali ya ulemavu.

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba niongezee majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusiana na eneo hili la wanafunzi wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi mpaka sasa hivi Serikali tayari kwa kushirikiana na Halmashauri kumeshakuwa na shule nyingi za watu wenye ulemavu lakini lazima nikiri kwamba kumekuwa na mapungufu katika shule nyingi nilizozitembelea, shule hizo zimekuwa hazipati rasilimali za kutosha pamoja na kuzipitia mara kwa mara, hata pia katika masula ya kibajeti. Lakini Wizara baada ya kutembea tumeshaona hayo mapungufu na sasa hivi mikakati tuliyonayo ni kwanza ni kuziboresha shule zenyewe ikiwemo kuziwekea miundombinu ikiwemo fensi pamoja na majengo, kwa sababu shule nyingi wanazokaa wanafunzi hawa wenye ulemavu ni zile za zamani kabisa. (Makofi)
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
8
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tayari Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya elimu tayari kuna vifaa maalum ambavyo vimeagizwa kwa ajili ya kusaidia hao wanafunzi wenye ulemavu. Lengo ni kuona kwamba wanafunzi hawa wasitengwe wala kubaguliwa lakini wakati huo huo wapewe haki zao za msingi za kusoma kadri inavyostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu hayo lakini niseme tu kwamba haitatosha kuwa na shule nyingi za watu wenye ulemavu kama hazitapewa huduma inayostahili, ahsante.
MHE. HAFIDH ALI TAHIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu yake lakini wakati akijibu swali langu alikuwa ameweka wazi kwamba sheria ya uchaguzi inaweza kufanyiwa marekebisho kulingana na wakati uliopo, swali langu kwamba hahisi kwamba sasa wakati wenyewe uliopo ndio huu, na tunapofika mwaka 2020 sheria hii tukaifanyia marekebisho, anasemaje?
Swali la pili, kwa sababu Waziri Mkuu yeye mwenyewe ni Mbunge wa kuchaguliwa na anahisi na anajua ugumu wa gharama katika jimbo, hivi Naibu Waziri si lazima anipe kwa ukamilifu lakini anachoweza kuliambia Bunge hili kiasi ambacho anafikiria hutumika katika kurudia uchaguzi katika majimbo yetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuhusu suala la kufanyia marekebisho swali hili lilikuwa lina vifungu (a) na (b) na nilijibu katika kile cha (b) kuhusiana na suala la kusimamisha uchaguzi pale anapofariki mgombea, of course hilo liko wazi lakini mwisho wa siku tunaobadilisha sheria ni sisi kama inaona inafaa na wadau watapendekeza basi hilo suala linaweza likaletwa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama mabadiliko hayo yalikuwa yanahusiana na kubadilisha ule mfumo wa uchaguzi kwamba akifariki mgombea ubunge basi yule aliyekuwa mshindi wa pili katika chama husika anachukua nafasi hiyo, hili si jambo rahisi sana na labda niseme tu ukiangalia system za uchaguzi duniani zipo takribani 23 sasa kwa nini nchi moja wakaamua kupigia chama, kwingine wakaamua kupigia mgombea, kwingine wakaamua kupigia orodha ya wagombea iliyofungwa ya chama, kwingine wakaamua kupigia orodha ya wagombea wa chama iliyokuwa wazi, kwingine wakaamua kuchanganya ni swali gumu kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme tu demokrasia yetu inakuwa na kubadilika kwa demokrasia, kubadilika kwa mifumo ya uchaguzi kwa namna moja au nyingine ni sehemu ya historia basi muda utakapofika utatoa majibu sahihi.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.
Maswali mengi kuhusu hizi milioni 50 tunaulizwa sisi Wabunge kwenye majimbo yetu. Wakati mwingine tunashindwa kutoa majawabu sahihi kwa sababu Serikali haijatoa taarifa rasmi kuhusu utoaji wa hizi shilingi milioni 50. Je, Mheshimiwa Waziri Serikali iko tayari sasa kwenda front na kutangaza kwamba wananchi wasubiri mpaka Baraza la Mawaziri likae ili liweze kutoa utaratibu wa kutoa hizi fedha ili sisi Wabunge tusipate wakati mgumu tunapokuwa Majimboni mwetu kuulizwa suala la shilingi milioni 50?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ambayo ndio iliwaahidi Watanzania kwamba itatoa shilingi milioni 50 katika kila kijiji, inatakiwa itekelezeke, ninaomba niwahakikishie Watanzania Serikali hii kwanza imeshatenga hiyo bajeti, pili Serikali hii imeshaona umuhimu wa kuanza haraka utekelezaji wa jambo hili, tatu Serikali hii ili kuhakikisha fedha hizo zinawafikia wanyonge sasa imeanza kuweka mfumo mzuri wa kuratibu zoezi hili na mara tu utakapokamilika Serikali hii itawaambia Watanzania ni mfumo gani utakaotumika. Na kwa sababu fedha zimetengwa katika bajeti ya mwaka huu, fedha hizo tutaanza kuzitoa katika mfumo rasmi utakaowafikia wanyonge ili kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa imekuwa ni tabia ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi kutoa ahadi ambazo zinaonekana tamu kwa wananchi wakati wa uchaguzi. Tukikumbuka kwamba katika Awamu ya Nne ulianzishwa mpango wa mabilioni ya Jakaya Kikwete ambao ulikufa bila kueleza Bunge au Watanzania kuwa umekufaje; na kwa sababu sasa hivi ni mwaka mmoja umepita tangu tumemaliza uchaguzi na Baraza la Mawaziri linajua kwamba hadi robo ya kwanza ya mwaka wa fedha ya mwaka 2016/2017 inakwisha kuna Wizara kadhaa hazijapata fedha za maendeleo.
Sasa namuuliza Waziri ni miujiza gani itakayotumiwa na Serikali hii ambayo leo imefilisika ambayo leo imeshindwa kutoa mikopo ya wanafunzi wa chuo kikuu kwa maelfu kwamba inaweza…
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nauliza ni miujiza gani Serikali iliyofilisika itakayotumia kutafuta fedha hizi shilingi bilioni 960 badala ya kuwadanganya wananchi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwanza kwamba Serikali hii haifanyi kazi kwa miujiza, Serikali hii inafanya kazi kwa mpangilio wa bajeti tuliojiwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na uthibitisho wa kwamba jambo hili litatekelezeka ni kama tulivyoweza kuwashangaza Watanzania kwa kutoa elimu bure kwa mabilioni ya fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulivyoweza kuwashangaza Watanzania kwa kutekeleza miradi mingine mikubwa na hata ununuaji wa ndege, tulivyoweza kuwashangaza Watanzania kwa utekelezeji wa Ilani yetu kwa mambo mengine mbalimbali ninaomba niwathibitishie Watanzania fedha hizi zitatolewa na Watanzania watazipata na Serikali hii haitafanya kazi kwa miujiza itafanya kazi kwa mpango wa utekelezaji wa bajeti ya wananchi tuliojiwekea. Na fedha hizo zitafika pia hata katika majimbo ya wapinzani katika nchi ya Tanzania.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza:-
Swali la kwanza; tarehe 3 Machi, 2015 kulitokea maafa ya mvua kwenye eneo la Mwakata kwenye Jimbo langu na watu 47 wakafa na misaada mingi ilikusanywa. Kwa bahati mbaya sana kumekuwepo usimamizi usioridhisha wa matumizi ya misaada ile na wananchi wamekuwa wakiwatuhumu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Bwana Ali Nassoro Lufunga na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, lakini pia Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya Bwana Benson Mpesya, aliyekuwa Mkuu wetu wa Wilaya kwamba, misaada ambayo ililenga kuwafikia waathirika wa Mwakata haikuwafikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua Serikali itasaidiaje kuhakikisha kwamba, taarifa sahihi ya fedha zilizokusanywa na misaada mingine kwa ajili ya maafa ya Mwakata inapatikana kutoka kwa watuhumiwa hao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa, Serikali inakiri kwamba, maafa ni jambo ambalo halitabiriki na pia inakiri kwamba Serikali ina wajibu wa kusaidia wananchi. Hatutaki Serikali ilipe fidia au kufanya chochote, lakini ni kwa nini isiangalie uwezekano wa kuwa na Mfuko, kama tulivyopendekeza kwenye swali la msingi, ambao unakuwa unachangiwa kwa njia endelevu ili likitokea janga hata mnapokwenda kusaidia angalau mna mahali pa kuanzia kuepuka aibu ambayo inajitokeza kwa sasa kwamba, zinafika mpaka nchi nyingine kuja kusaidia, sisi kama Serikali tunawaomba na kuitisha harambee sisi hata shilingi moja ya kuanzia hatuna. Hivi Serikali haioni kwamba, ni aibu katika mazingira ya namna hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na upatikanaji wa taarifa sahihi kutoka kwa watu wanaotuhumiwa. Niseme tu si kupata taarifa sahihi, Serikali itafanya yote yanayowezekana kwa mujibu wa Sheria ili kupata taarifa sahihi na kama hao watuhumiwa wamefanya makosa basi hatua mbalimbali zitachukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Maige ashirikiane na sisi, ili kuhakikisha kwamba, kweli kama kuna mtu ametumia fedha hizo vibaya, basi afikishwe katika mikono ya sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu Mfuko. Tayari Sheria imeanzisha Mfuko wa Maafa, ni tofauti na Sheria ile iliyotungwa mwaka 1990 ambayo Mfuko ulikuwa kwa ajili ya Kamati na haukuwa umeelezewa vizuri sana. Sheria hii imeanzisha Mfuko wa Maafa ambapo una vyanzo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala kwamba ni aibu kwa wananchi kuchangia, naomba niweke sawa; masuala kama ya tetemeko ni majanga makubwa sana na Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza kuchangiwa. Nitoe tu mfano, Iran lilipotokea lile tetemeko kubwa nafikiri mwaka 2013, lililofikia magnitude 7.7, mashirika mbalimbali yalisaidia ikiwemo National Federation of the Red Cross.
Mwaka 2015, Nepal kwa mfano, tunaona Wafaransa, Norway na nchi kadhaa yalisaidia, sitaki kusema nini kilitokea Japan na Indonesia na maeneo mengine ambayo matetemeko yamekuwa yanatokea mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi pia tumesikia kwa mfano Italy, ilikuwa inaomba msaada European Union ili kuangalia ni namna gani itaweza kurejesha hali baada ya kupata matetemeko kati ya Agosti na Oktoba. Kwa hiyo, kutokana na ukubwa wa matetemeko haya ni vigumu nchi kuwa haisaidiwi na ndio maana hata Umoja wa Mataifa ina wakala maalum wa kusaidia maafa kwa majanga kama haya, matetemeko, mafuriko na majanga mengine ambayo hayatabiriki. Kwa hiyo, niseme si aibu ila ni hali ya kawaida na Mfuko huu umeanzishwa kwa Sheria. Kwa hiyo, swali la pili kuhusu Mfuko nadhani limejibiwa.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kumekuwa na tatizo la Serikali kuwatishia Wakuu wa Wilaya ambao wilaya zao zitapata janga la njaa, kwamba watapoteza Ukuu wa Wilaya na hivyo kusababisha wasitoe takwimu halisi za upungufu wa chakula uliopo katika Wilaya zao. Wananchi wengi wamekuwa wakifa kutokana na njaa kwa kuficha wasijulikane kama kuna njaa wilayani kwao. Je, ni kwa nini chakula kinakuwepo wilaya nyingine au mikoa mingine kingi na wilaya nyingine hakipo, watu wanakufa njaa ndani ya nchi hii moja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nafikiri tutofautishe njaa inapotokea katika mkoa ambapo hakuna sababu, kwamba mvua zipo, ardhi yenye rutuba ipo, watu wa kufanya kazi wapo. Tutofauitishe na sehemu nyingine ambazo kuna baa la nzige, kweleakwelea, ukame, hivi ni vitu viwili tofauti. Kwa hiyo, niseme tu kwamba, Wakuu wa Wilaya hawatishiwi ila walikumbushwa kuwajibika pale ambapo rasilimali zipo.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa tatizo la ajira ni kubwa na kwa kuwa tuna miradi mingi ya kilimo; kwa mfano kilimo cha chai kule Njombe, miwa Kilombero, kahawa, pamba kule Kanda ya Ziwa na katika miradi hii kuna fursa ya kuweka programu ya outgrowers.
Mheshimiwa Spika, nilitaka kujua Serikali inatumia vipi hii fursa ya programu ya outgrowers kuwashirikisha vijana ili kuweza kutatua tatizo la ajira nchini?
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile tatizo hili la ajira nimekuwa nikilizungumzia mara kwa mara takribani miaka sita tangu nilipokuwa ndani ya Bunge hili, tangu nilipokuwa Mbunge wa Vijana. Nilitaka kujua, Serikali iniambie imeweza kutatua kwa kiasi gani tangu nianze kuzungumzia tatizo hili?
NAIBU WAZIRI OFISI YA WAZIRI MKUU KAZI AJIRA NA VIJANA: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ameuliza namna gani Serikali tunaweza tukawashirikisha vijana kwenye fursa mbalimbali hasa za kwenye kilimo.
Mheshimiwa Spika, tarehe 31 mwezi uliopita kupitia Wizara ya Kilimo pamoja na sisi Wizara chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu tumezindua mpango maalum wa kilimo ambao utawashirikisha vijana. Lengo lake ni kuwaweka vijana hawa katika makundi mbalimbali kutokana na mikoa yao waweze kushiriki katika kilimo cha nchi hii.
Mheshimiwa Spika, katika mpango huu tunakwenda pia sambamba na mpango ambao upo chini ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ambao ni mpango wanaouita ODOP (One District One Product) na lengo lake ni kufanya kitu kinachoitwa District branding ya kila sehemu kwa nchini nzima ambako shughuli za kilimo pamoja na shughuli nyingine za ujasiriamali zinafanyika. Kuwepo na kitu cha utambulisho katika Wilaya husika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali inatambua kabisa kilimo biashara ni kati ya eneo ambalo linaweza likachukua vijana wengi kwa wakati mmoja, na tumeweka msisitizo mkubwa kuhakikisha kwamba makundi makubwa ya vijana yanapata fursa ya kuweza kushiriki katika uchumi wa nchi yao.
Mheshimiwa Spika, lakini pili, katika swali lake ameuliza ni kwa kiwango gani sasa tumetatua changamoto hii. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba takwimu zinasema ukosefu wa ajira hasa kwa vijana nchini Tanzania umepungua kutoka asilimia 13.7 ya mwaka 2012 mpaka asilimia 11.7.
Mheshimiwa Spika, lakini ukilinganisha Tanzania na nchi nyingine za jirani kwa maana ya Kenya na Uganda; tatizo la ukosefu wa ajira kwa Kenya ni takribani asilimia 17.3, kwa Tanzania tumekwenda mpaka asilimia 11.7.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni dhahiri kwamba Serikali kupitia mipango yake mbalimbali imejaribu kutengeneza mazingira wezeshi kwa ajili ya vijana kutengeneza fursa mbalimbali na vijana wengi wameendelea kupata ajira.
Mheshimiwa Spika, nimuondoe hofu kwamba tunayo mipango madhubuti ya kuendelea kusaidia kundi kubwa hili la vijana waweze kupata ajira na kuondoka katika adha hii ya ukosefu wa ajira.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri ambayo sijayafurahia sana mimi kama mstaafu, napenda kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, pensheni hii ambayo tunalipwa kila mwezi kwa kadri miaka inavyokwenda gharama zinapanda na shilingi inashuka thamani. Nimemshuhudia hata baba yangu mzazi Mungu alimjalia umri wa miaka 90 lakini ile pensheni aliyokuwa anapata na alikuwa mtu mkubwa sana Serikalini ilikuwa kidogo sana kama asingekuwa na watoto wenye uwezo angekuwa ombaomba. Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba pensheni hizi za wastaafu zinawekewa hata percentage kidogo kusudi wasiwe ombaomba baada ya miaka kadhaa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, hifadhi hizi za jamii zimewekeza sana kwenye majengo, Mheshimiwa Rais juzi alisema wawekeze kwenye viwanda. Je, imefanyika actuarial study kuona kwamba hii mifuko haitafilisika na baadaye kuleta adha kwa wanachama?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na swali la kwanza la pensheni kidogo na kutaka kujua mkakati wa Serikali, katika utaratibu wa ulipaji wa mafao kipo kitu kinaitwa indexation ambacho ndiyo imekuwa ni nyongeza ya kiwango ambacho kimekuwa kikilipwa kila mara kwa wastaafu. Kwa takwimu zilizopo, wastaafu wengi walikuwa wakilipwa kima cha chini cha Sh.50,000 mpaka pale ambapo lilitoka tamko kupitia SSRA ambapo sasa hivi wastaafu wanaanza kulipwa kuanzia Sh.100,000 na kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko uliobaki ni mfuko wa LAPF tu lakini mifuko mingine yote sasa wataanza kuwalipa wastaafu kima kile cha malipo kuanzia Sh.100,000 na kuendelea na wamekwishaanza. Kwa hiyo, nimwondoe tu wasiwasi kwamba mifuko hii kadri inavyozidi kufanya uwekezaji wake na kadri ambavyo returns za investment zinaongezeka, watafanya kitu kinaitwa indexation kuweza kusaidia ili wastaafu wao waweze kukidhi maisha na mahitaji ya dunia ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili lilikuwa ni la wasiwasi ya kwamba, je, mifuko hii ikienda katika uwekezaji wa viwanda haitashindwa kweli kutimiza majukumu yake ya msingi? Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, katika utaratibu wa uendeshaji wa mifuko hii, kuna kitu kinaitwa actuarial valuation ambapo huwa inafanya tathmini ya afya ya mfuko. Mpaka maamuzi haya yanafanyika ni kwamba mifuko hii tayari inao uwezo wa kwenda kufanya uwekezaji huo pasipo kuathiri michango au mafao ambayo wanachama wanastahili. Kwa hiyo, nimwondoe hofu kwamba study ya uhakika imefanyika ya kuifanya mifuko hii iende kufanya uwekezaji katika uchumi wa viwanda.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika majibu ya swali la msingi, Mheshimiwa Waziri ameeleza kwamba mifuko hii iko imara. Kama kweli mifuko iko imara, kuna Walimu waliostaafu zaidi ya 6,000 hawajalipwa mafao yao zaidi ya shilingi bilioni 550. Walimu hawa wanateseka wakiwemo Walimu wangu wa Jimbo la Buyungu ambao kila wakati nahangaika kufuatilia mafao yao ya kustaafu. Ni kwa nini anayestaafu halipwi mafao yake kwa mujibu wa mkataba ndani ya miezi miwili baada ya kustaafu?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi ni kwamba mifuko hii imeanza kulipa mafao na kwa hivi sasa SSRA inawasimamia kuhakikisha kwamba wale wote ambao wanastahili kulipwa mafao wanalipwa. Zamani hapa lilikuwa linazungumzwa deni kubwa ambalo lilikuwepo hasa katika mfuko ambao unashughulika na watumishi wa umma ambao Serikali ilikuwa inadaiwa takribani shilingi trilioni 1.3.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka ninavyozungumza hivi sasa Serikali imeshalipa shilingi trilioni 1.2 na deni lililobaki ambalo Serikali inadaiwa ni shilingi bilioni 128 tu. Mfuko wa PSPF mpaka ninavyozungumza hivi sasa wameshalipwa takribani shilingi bilioni 720. Kwa hiyo, Mwalimu Kasuku kama bado kuna usumbufu huo, naomba uniletee nitazungumza na SSRA waweze kulifanyia kazi ili Walimu waweze kulipwa.