Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Philip Isdor Mpango (6 total)

MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA aliuliza:-
Je, Serikali imeshalipa stahiki za wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Suzana, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshalipa stahili za wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki iliyovunjika Juni, 1977.
Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya 2005 na 2010, Serikali iliwalipa wastaafu 31,519 kati ya wastaafu 31,831 wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Serikali ililipa jumla ya shilingi bilioni 115.3. Wastaafu waliolipwa stahili zao ni wale ambao walijitokeza na kuthibitishwa na waliokuwa waajiri wao yaani mashirika waliyokuwa wakiyafanyia kazi. Aidha, katika kipindi cha 2011 mpaka 2013, Serikali iliendelea kuwalipa wale ambao walikuwa hawajalipwa (on a case by case basis) ambapo wastaafu 269 walilipwa kiasi cha shilingi bilioni 1.58 na kufanya jumla ya wastaafu waliolipwa kufikia 31,788 na kiasi kilicholipwa kufikia shilingi bilioni 116. 88.
Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi la kupokea madai mapya lilisitishwa tarehe 13 Desemba, 2013 kwa mujibu wa makubaliano kati ya wawakilishi wa wastaafu wakiwa na Wanasheria wao kwa upande mmoja na Serikali kwa upande mwingine.
MHE. JAMAL KASSIM ALI aliuliza:- Je, Dar es Salaam Stock Exchange Market (DSE) na Capital Markets and Securities Authority (CMSA) mpaka sasa zimetoa mchango gani kwa wafanyabiashara wazalendo?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jamal Kassim Ali, Mbunge wa Magomeni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi yetu Soko la Mitaji (Capital Market) linahudumiwa na taasisi mbili ambazo ni: Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ambaye ni msimamizi wa soko (regulator) na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ambaye ni mwendeshaji (operator) kwa kuuza hisa na dhamana kwa taasisi na watu binafsi kwa niaba ya makampuni ambayo yanayohitaji kuongeza mitaji baada ya kupata kibali kutoka CMSA. Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya kampuni zilizoorodhesha hisa zao katika Soko la Hisa, baada ya kubinafsishwa ni pamoja na TBL, TOLGases, TCC, Swissport, Tanga Cement, Twiga Cement na NMB Bank. Makampuni haya yamekuwa yakitoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi ikiwemo ajira, gawio kwa Serikali na wanahisa, lakini pia ni miongoni mwa walipa kodi wakubwa. Kwa mfano mwaka 2015 NMB iliweza kutoa gawio la shilingi bilioni 16.5 na TCC gawio la shilingi bilioni 1.4 kwa hisa zinazimilikiwa na Serikali. Mheshimiwa Mwenyekiti, wanahisa wengineyo walipata gawio la shilingi bilioni 35. 4 kutoka NMB na shilingi bilioni 58.6 kutoka TCC. Mapato yanayotokana na kodi pamoja na gawio, vinatumiwa katika kutoa huduma mbalimbali ambazo jamii ikijumuisha wafanyabiashara wadogo ambao wananufaika nazo. Vilevile Serikali imekuwa ikitumia masoko ya mitaji kama chanzo cha upatikanaji wa fedha za bajeti kwa miradi ya maendeleo, kwa kutoa hatifungani za Serikali (treasury bonds). Miradi inayotekelezwa na fedha hizi pamoja na mambo mengine imekuwa ikitoa ajira na fursa za kibiashara kwa wafanyabiashara wazalendo wadogo na wa kati. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua mchango mkubwa wa makampuni madogo katika kukuza uchumi wa nchi, mwaka 2013 Soko la Hisa Dar es Salaam lilianzisha dirisha la makampuni madogo na ya kati (enterprises growth market) kwa lengo la kutoa nafasi kwa makampuni za wazawa zilizokidhi vigezo vya dirisha kuu la soko (main investment market) kuweza kutumia soko la hisa katika kupata mitaji na kuorodheshwa kupitia soko la hisa. Dirisha hili linatoa fursa kwa makampuni madogo na yanayoanza kulitumia soko kikamilifu kupata mitaji kutoka kwa umma wa Watanzania. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa njia hii Watanzania wengi wananufaika na uwepo wa soko la hisa na kushiriki moja kwa moja katika umiliki wa uchumi wa nchi. Baadhi ya wanufaika na dirisha hili dogo ni pamoja na Mwalimu Commercial Bank, Swala Oil and GasTanzania, Maendeleo Bank PLC, Yetu Microfinance na Mkombozi Commercial Bank. Makampuni haya mpaka sasa yana jumla ya mitaji isiyopungua bilioni 120. Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge kuwahamasisha wananchi na hasa wafanyabiashara wazawa kutumia fursa hii ya dirisha dogo kwa ajili ya kujiongezea mtaji.
MHE. LUCY S. MAGERELI aliluliza:-
Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano kumekuwa na mabadiliko makubwa ya uendeshaji wa shughuli za Bunge kwa kupunguza muda. Bunge sasa hukaa kwa siku 10 hadi 12 tu jambo ambalo linasababisha muda wa kuchangia na Mawaziri kujibu hoja kuendelea kupunguzwa hadi kufika dakika tano tu kitu ambacho kimepunguza kabisa ufanisi wa chombo hiki muhimu chenye majukumu muhimu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuliwezesha Bunge
kufanya shughuli zake kwa ufanisi kwa kuliongezea bajeti?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Simon Magereli, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Serikali kuliwezesha Bunge kufanya shughuli zake kwa ufanisi ni kwa kutoa fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali kwenda kwenye Mfuko wa Bunge Fungu namba 42 kwa kuzingatia bajeti iliyoidhinishwa na Bunge, taarifa ya utekelezaji ya Mfuko wa Bunge na hali ya upatikanaji wa fedha. Kifungu cha 45(b) cha Sheria ya Bajeti kinatuelekeza tufanye hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa msingi huo, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Mfuko wa Bunge uliidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 99 na hadi Februari, 2017 jumla ya shilingi bilioni 62.6 sawa na asilimia 68 ya bajeti ya mfuko huo zilitolewa. Serikali inaahidi kutoa fedha zote zilizobaki kwenye bajeti ya fungu hili yaani shilingi bilioni 8.3 kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi bilioni 6.7 kwa ajili ya miradi ya maendeleo kabla ya tarehe 30 Juni, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka ujao wa fedha, Serikali imeongeza bajeti ya Mfuko wa Bunge kutoka shilingi bilioni 99 mwaka 2016/2017 mpaka shilingi bilioni 121 mwaka ujao wa fedha.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA aliuliza:-
Hapa nchini pamekuwepo na ongezeko kubwa la Taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za kifedha kama vile Benki, Vikundi mbalimbali kama VICOBA, Taasisi za Kukopesha Watumishi, Taasisi za kukopesha wafanyabiashara na wakati mwingine watu na mitaji yao wanakopesha watumishi (kienyeji) kwa kificho ficho:-
(a) Je, ni chombo kipi hasa chenye wajibu wa kufuatia kodi zinazotozwa na wananchi?
(b) Je, kodi zinazotozwa ni halali?
(c) Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha wananchi
wake hawaibiwi kwa njia hiyo?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la
Mheshimiwa Desderius John Mipata, Mbunge wa Nkasi Kusini,
kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, Toleo la 2005, Ibara ya 138(1) inaelekeza kuwa, hakuna kodi ya aina yoyote itakayotozwa isipokuwa kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge au kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa Kisheria na uliotiwa nguvu Kisheria na Sheria iliyotungwa na Bunge
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, Sura ya 399(5) imeipatia Mamlaka ya mapato wajibu wa kukadiria, kutoza na kutoa hesabu za mapato yote ya umma. Aidha, Sheria ya bajeti kifungu cha 58(b) inaelekeza kuwa mtu yeyote aliyepewa Mamlaka ya kukusanya mapato ya Serikali atawajibika kukusanya kwa ufanisi, kutoa hesabu za mapato, kuyawasilisha na kuyatolea taarifa kwa kuzingatia Sheria husika na kuchukua tahadhari kuzuia usimamizi mbovu wa mapato na pale inapolazimu, mfano; katika operesheni maalum dhidi ya wakwepa kodi sugu au mazingira hatarishi, TRA inaweza kuomba msaada wa vyombo vingine vya dola.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kodi halali zinazotozwa kwenye huduma za kifedha kwa mujibu wa Sheria ni zifuatazo:- Kodi ya zuio kwenye faida inayolipwa kwa Mwekezaji ambayo ni pamoja na amana za Benki, dhamana za Makampuni au Serikali na hisa; Kodi za ongezeko la thamani kwenye ada zinazotozwa kwenye huduma za kifedha na ushuru wa bidhaa kwenye ada inayotolewa kwenye kutuma au kupokea fedha kwa njia za kielektroniki na hususani simu za mkononi.
Mheshimiwa Naibu Spika, endapo mtu binafsi ama
Taasisi itatoza ama kukusanya kodi yoyote kinyume na matakwa ya Sheria, anakuwa ametenda kosa na hatua stahiki zinapaswa kuchukuliwa mara moja dhidi yake.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-
Jumuiya za kiuchumi za Kikanda zimekuwa sehemu ya mkakati mkubwa katika kuratibu masuala ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kimazingira. Ileje ni Wilaya ya mpakani mwa Nchi za Malawi na Zambia lakini haina kituo cha forodha. Hakuna miundombinu ya soko la Kimataifa, hakuna kituo cha uhamiaji, hakuna kituo cha kudhibiti mazao, mifugo wala silaha. Hii inasababisha wahamiaji haramu na wahalifu kutumia mipaka kinyume cha sheria na taratibu:-
Je, ni lini Serikali itajenga kituo cha forodha, kituo cha uhamiaji, soko la Kimataifa na kituo cha kukagua mifugo na silaha kwa ufanisi na maendeleo ya Ileje?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Ileje kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kabisa kuwa katika Wilaya ya Ileje hakuna kituo cha forodha na uhamiaji wala soko la Kimataifa na vituo vya kukagua mifugo na silaha. Namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge ambaye ameendelea kufuatilia jambo hili kwa nguvu sana na kwa kutambua umuhimu huo, Mamlaka ya Mapato na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tayari tumefanya jitihada tumepata kiwanja kwa ajili hiyo lakini bado tunafanya mashauriano na nchi jirani na hususani Zambia na Malawi kwa sababu ya utaratibu wa kujenga kituo cha pamoja lakini pia tutahitaji maandalizi kwa ajili ya kuamua jengo lenyewe hilo la kituo cha pamoja liweje.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kazi hizo kukamilika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaanza utekelezaji wa ujenzi wa kituo hicho mara baada ya kuwa shughuli hiyo imekamilika, lakini kwa sasa natoa rai kwa niaba ya Serikali kwa wananchi wa Wilaya ya Ileje na Wilaya zinazofanana na hizo kuendelea kutumia huduma zilizo katika Wilaya na Mikoa jirani wakati tunafanya utaratibu wa kujenga vituo hivyo.
MHE. SAED A. KUBENEA aliuliza:-

Kuna taarifa kwamba ubadhirifu bado unaendelea katika Shirika la NIC; vilevile taarifa zinaonesha kuwa Shirika hilo halina mipango thabiti ya kukabiliana na washindani wake kibiashara:-

(a) Je, ukweli juu ya taarifa hizo ni upi?

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuisaidia NIC kifedha na kitaalam ili kuliwezesha shirika hilo kukabiliana na ushindani wa kibiashara?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, hakuna ubadhirifu wowote unaoendelea katika Shirika la Bima la Taifa (NIC) na Shirika limeendelea kuboresha mifumo yake ya udhibiti wa mapato na matumizi ili kukabiliana na washindani wake kibiashara katika sekta ya bima. Katika kujiimarisha kibiashara, Shirika limechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mapato yote yanakusanywa kwa kutumia Mfumo wa Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali (GePG) ambao ulianza kutumiwa na Shirika mwezi Novemba 2019 na kuondoa ukusanyaji wa mapato kwa fedha taslimu (cash); kuongeza udhibiti katika ulipaji wa madai ikiwepo kufanya ukaguzi maalum wa madai yote ya Bima za Maisha ili kujiridhisha juu ya uhalali wa madai haya; Shirika lipo katika hatua za mwisho za kuunganishwa na Mfumo wa Usimamizi wa Shughuli za Kihasibu na Malipo katika Taasisi za Umma (MUSE) ambao utaongeza udhibiti katika malipo yote yanayofanyika; kusitisha matumizi ya hundi (cheque) ambapo kuanzia mwezi Desemba 2019, Shirika lilisitisha matumizi ya hundi (cheque) katika malipo yake yote na kuanza kutumia mfumo wa malipo wa kielektroniki hivyo kuongeza uthibiti wa matumizi na kuzuia uwezekano wa matumizi ya hundi feki (forged cheques).

(b) Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imechukua hatua mbalimbali kuliimarisha Shirika la Bima la Taifa (NIC) kitaalam kwa kufanya yafuatayo: Kuliondoa Shirika kutoka kwenye mashirika yaliyotakiwa kubinafsishwa na kuliwezesha kushiriki katika biashara ya bima kwa ushindani; imelifanyia mabadiliko ya kiuongozi Shirika ili kuongeza tija na kuleta mabadiliko chanya kwenye utendaji na usimamizi wa shughuli zake; na imelisaidia Shirika kwa kuwapatia wataalamu mbalimbali katika nyanja za mifumo ya TEHAMA, mifumo ya utendaji kazi na mifumo ya utunzaji kumbukumbu (e-Office) ili kuweza kuongeza ufanisi wa Shirika na kuweza kukabiliana na ushindani wa kibiashara.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeliimarisha Shirika kifedha kwa kuchukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kupata biashara za Serikali na kushinikiza malipo ya hapo kwa hapo ya premium ambayo yamesaidia kupunguza malimbikizo ya premium kutoka kwa Taasisi za Serikali kutoka zaidi ya shilingi bilioni 20 hadi milioni 500 kwa kipindi cha Julai 2019 hadi Februari 2020.

Mheshimiwa Spika, pamoja na maendeleo mazuri ya Shirika, Serikali inaendelea kuliimarisha Shirika hili la kimkakati kwa kulisaidia katika kupitia upya Mpango Mkakati wake ili uendane na mahitaji halisi ya biashara ya ushindani; kuongeza uwekezaji katika mifumo ya TEHAMA ili kuwafikia wateja wengi zaidi; kuongeza ubora wa huduma zake na kulipa madai haraka na kwa urahisi; kujitangaza zaidi na kuongeza uwekezaji wenye tija ili kutoa gawio kubwa kwa Serikali na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya Taifa.