Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Asha Abdullah Juma (5 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi hii leo ya kuweza na mimi kuchangia.
Awali ya yote, nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu, Subhanahu Wataala, aliyenijalia uwezo na satwa ya leo kuwa mimi Asha Abdullah Juma kuwa Mbunge na kuweza kuchangia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi ya kwanza kabisa kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kuweza kuwa Rais na kuongoza kwa speed hii ambayo anakwenda nayo, kwa kweli anafanya kazi nzuri sana.
Vilevile nachukua nafasi ya kipekee kupongeza hatua iliyochukuliwa na chama chetu ya kuweza kumpendekeza Mheshimiwa Samia Sukuhu Hassan akawa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Napongeza pia uteuzi wa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, anao uwezo wa hali ya juu sana na anakubalika na tuna matumaini atafanya kazi nzuri sana. Niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote mliopata nafasi hii, nawapongeza pia wale waliopata nafasi ya Mawaziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nafasi ya kipekee kabisa nampongeza Mheshimi Dkt. Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa Zanzibar na kwa kushinda uchaguzi. Mheshimiwa Ally Saleh nakuona hapo, nakuambia kwamba Mheshimiwa Dkt. Shein ndiyo Rais wa Zanzibar na amechagua cabinet nzuri naamini itamsaidia kufanya kazi nzuri. (Makofi)
Kwa kupitia Bunge hili, nilaani kitendo alichofanyiwa Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein cha kuzomewa lakini lile halikumrudisha nyuma yeye ameendelea kuwa Rais wa Zanzibar kwa kura nyingi na sisi tunamuunga mkono kwa sababu ndiye tegemeo letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kitu kimoja, hii tabia ya kususasusa si nzuri, tabia ambayo inaoneshwa hapa kwa sababu inavunja demokrasia.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Anajijua mwenyewe aliyesusa. Inavunja demokrasia, watu wamewachagua mje hapa muwawakilishe, muisemee Serikali au muikosoe, mnakuja hapa kisingizio hiki, kile, mara kutoka nje, mara uzomee, mara unune, mara ugome, sasa ndiyo umechaguliwa kwa ajili hiyo? Ilimradi hakuna lililo zuri kwa upande wenu. Usichukue mshahara wa kutwa bila kufanya kazi ya kutwa.
Baniani mbaya ila kiatu chake dawa. Mshahara, posho yote mazuri mbona hamyakatai?
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Asha…
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya dibaji hiyo, sasa niende kwenye hoja.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Asha naomba ukae.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja ya Waziri Mkuu mia juu ya mia.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba pia unilindie muda wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuchangia kwanza kwa kupongeza safu nzima ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba niseme kwamba kwenye Ofisi yako ukianzia na Mheshimiwa Jenista Mhagama, Naibu Mawaziri Mheshimiwa Dkt. Abdallah Possi na Mheshimiwa Anthony Mavunde, hawa ni vifaa, tumewapima kupitia Kamati yetu ya Katiba, wanafanya kazi nzuri sana. Naamini watatusaidia sana kwa maendeleo husika katika Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nianze rasmi na naanza na eneo la Tume ya Uchaguzi. Naanza kwa kupongeza kazi nzuri iliyofanywa na Tume ya Uchaguzi kuanzia Mwenyekiti wake Jaji Lubuva…
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Kailima na Jecha pia. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tume hii ya Uchaguzi imethibitisha demokrasia, kama tulivyoona vyama 22 vimeshiriki na vimeshinda vingine na sasa hivi tupo hapa kuwawakilisha wenzetu. Hivyo, ukipata wapiga kura waliofikia 15,596,110 sawasawa na 67.3% ni hatua nzuri. Tuiombe Serikali iiongezee Tume ya Uchaguzi nguvu ili kudhibiti wizi wizi na vitendo vya kuivurugia kazi Tume hii ambayo inafanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo nataka kuligusia ni hili linalohusu vijana ambalo kwenye hotuba hii limezungumzwa vizuri la kuwapatia mafunzo. Tunajua vijana wanatuzidi kwa namba, ni wengi, kwa hiyo inahitajika mikakati na imara zaidi ya kuwahusisha ili wasitutoke wakawa kundi la wanaofanya vurugu na fujo. Kwa hiyo, mipango hii iliyopangwa nafikiri ingekuwa vizuri pia ikaelezwa waziwazi kila Wilaya watapata mafunzo kiasi gani na mafunzo gani ili kujua hawa watu wanashughulikiwa ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine nalotaka kuligusia ni hili la bandari. Tumeridhishwa na mpango ulioelezwa hapa lakini tuongeze kuoneshwa kwamba kunaongezwa vifaa vya kisasa zaidi ili kuharakisha upakizi na upakuaji na pia kudhibiti bila kutumia nguvu zaidi na pesa nyingi huu uvujaji na wizi katika bandari zetu. Pia nadhani kama ingekuwa vizuri kwenye eneo hili la bandari kukaimarishwa masuala ya uokoaji inapotekea disaster katika maeneo ya bandarini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jicho pia liongezwe katika kuimarisha bandari ya Mtwara na Tanga. Naona kama hii mipango iliyopangwa haijatosha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Serikali hii ione umuhimu huo na hasa kwa vile kule Mtwara tuna mategemeo ya kupata shughuli nyingi za kupokea na kusafirisha mizigo. Kwa hiyo, ni vyema jitihada ikaongezwa kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine la muhimu kabisa ambalo linatakiwa lipewe nguvu ya ziada ni elimu. Pongezi pia kwa Serikali kwa kuweza kuboresha elimu ya awali. Naomba tuendelee kuunga mkono juhudi hizi, kama tulivyofanya kwa kutenga pesa tukaziweka kwenye madawati hivyo na kila anavyofikiria mtu kuna namna nyingine ya kufanya ili kuweza kuiboresha elimu hii basi na tufanye.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hoja hii leo. Namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa nguvu kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu na kuweza kutoa mchango wangu kwa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi. Naanza kwa kuunga mkono hoja, napongeza juhudi na kazi nzuri inayofanywa na Profesa Joyce Ndalichako na timu yake akiwemo Engineer Stella Manyanya, pamoja na timu nzima ya Wizara na wakati huo huo nampa pole Mheshimiwa Stella Manyanya kwa kuondokewa na mama yake mzazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wizara hii ya Elimu ina umuhimu wake kipekee, hapo hapo naunganisha na kutoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kupitisha lile azimio la kupatia elimu bure kuanzia darasa la kwanza mpaka sekondari. Jambo hili lina maana sana, kwa sababu linatoa nafasi na fursa kwa wanyonge wengi kupata elimu kwa watoto wao. Wote tunajua umuhimu wa elimu, kwa hiyo zinahitajika juhudi zetu za pamoja kuunga mkono Wizara hii, ili vijana wetu wote wapate elimu stahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa elimu mpaka sekondari, ni bure kwa hivyo ningependekeza kwamba kidato cha tano na cha sita, vilevile tufanye jitihada, ili iweze kuwa bure vilevile. Kwa kuwa pale kuna watoto wa wanyonge wengi, ambao wameweza kupita kuanzia kutoka kwenye shule za kata mpaka wakafika pale.
Kwa hiyo, Serikali ifanye vile inavyoweza katika kuongeza ukusanyaji wake wa kodi au mbinu nyingine inakojua itapata pesa ili vijana hawa wasije wakakwazwa. Kwa kuwa vijana wa chuo kikuu wanapata mkopo, na hawa nao wapate, kwa kuwa form five na sixndio chimbuko la wataalam wetu, naamini juhudi za ukusanyaji wa kodi zitatuwezesha kufika hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara pia iangalie na ipitie ihakikishe kwamba angalau Wilaya zote zina shule za A-level za kutosha, kwa mfano Wilaya kubwa kama Rufiji ina shule moja tu yaA-level pale Mkongo na hii Wilaya ni kubwa kuliko Mkoa mzima wa Kilimanjaro, kwa hivyo Wizara ifanye ranking kuhakikisha kwamba Wilaya zote zina shule hizi la A-level.
kusimamia kujenga shule za sekondari za kata katika Kata zote, na maabara na madarasa. Hili jambo limefanikiwa kwa juhudi za wananchi na Serikali
pamoja.
Dhana ya elimu bure inapata mtikisiko kidogo, hii dhana imelenga kuondolea wazazi wanyonge, kuweza kuwasaidia vijana wao wapate elimu, maeneo mengi maabara zimesimama kujengwa, madarasa yamepungua kasi ya kujengwa, maeneo mengi wazazi wamepunguza kasi ya kujitolea kushiriki kwa kisingizio kwamba elimu ni ya bure, naomba sana tusiieleleze Serikali, tuendelee na spirit ile ile ya kuunga mkono jitihada za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuendelee kusisitiza wananchi waendelee kuelimishwa umuhimu wa kutimiza wajibu wao, tunakiri kwamba katika jambo hili la elimu bure ziko changamoto, na hilo ni jambo la kawaida kwa sababu jambo lolote la maendeleo huwa linavikwazo vikwazo, lakini tutashinda na tutafika tunakokwendea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijazungumza zaidi kuhusu masuala ya shule hizi za kata, naomba kwa ruhusa yako nizungumzie kidogo kuhusiana na sheria. Naomba nitanabaishe kuhusiana na Sheria za Shule za Kata, Sheria ya Elimu Namba 25 kama ilivyorekebishwa mwaka 1978, kwa Sheria Namba 10 ya mwaka 1995, imeweka utaratibu wa Kikanuni wa kuanzishwa shule za sekondari na msingi, kwa utaratibu wa sasa, tuna shule za kata ina maana sheria hii haizungumzii shule za kata, kwa hivyo kunahitajika marekebisho ya sheria, kujumiuisha shule ya kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile sheria na kanuni inayounda bodi za shule, inatoa maelekezo ya uteuzi wa wajumbe wa bodi katika mkoa; kwa kuwa sasa tuna shule za kata, tunahitaji malekebisho ya Kanuni ili tuweze kutoa wajumbe hao wa bodi kutoka kwenye kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilijitahidi sana kuanzisha Sekondari karibu 3,500 za kata kama sikosei, sasa niiulize Serikali hii inashindwaje kujenga vituo vya VETAkwa kila Wilaya ili hawa vijana wetu ambao ni wengi wakapate elimu ya amali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia ina vitu ambavyo tunategemea vijana wetu wafanye. Lakini tulifuta somo la elimu na elimu ya kujitegemea, kwa mfano kila Ijumaa iliku wakati wa mchana watu wanakwenda kufanya mambo ya bustani, kama ilivyokuwa setup ya Mwalimu Nyerere wakati ule. Sasa vijana hawa wanapomaliza, wanaishia kwenda kucheza pool kwa sababu ile elimu ya bustani haipo, kwa mfano siku hizi kuna elimu ya bustani katika sehemu ndogo inaitwa permaculture ingeweza ikaanzishwa kwenye shule mbalimbali kule, watu wakajipatia mboga, viazi na vitu vidogo vidogo. Kwa hiyo lazima tuchanganue zaidi kutafuta, utaalamu na teknolojia sasa wa kuweza kuzalisha katika sehemu ndogo zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijamaliziwa muda wangu, basi niombe Wizara ya hii ilekebishe curriculum,ili tuweze kupata masomo ya kilimo na biashara, michezo, ufundi, katika ngazi zote na masomo haya yatiliwe mkazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala kubwa sana la kupata mimba wasichana, hili ni suala linaleta matatizo, linaleta unyonge, kwa sababu Wizara ifikirie na izingatie kwa kina kwa uharaka ikiwezekana kuwarudisha watoto hawa kwenye madarasa. Hatusemi hivyo kama tunawatia washawasha ili wakapate mimba laa! Ilamimba nyingine zinakuja ni kwa accident, nyingine ni kwa kubwakwa, kwa hivyo tufikirie, unapomuadhibu kijana huyu asiendelee kusoma, umemuadhibu na mtoto atakayezaliwa, umeiathiri familia yake nzima, umeongeza umaskini, hujauondoa umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini uadhibu mtoto ambaye hana makosa, na yule ambaye mhusika mwingine mara nyingi anakwenda wanaposema wazungu anakwenda scot free, kwa sababu huwezi kumpata na hivyo anapata nafasi ya kwenda kufanya uharibifu, kuwawekea mimba watoto wengine.
Sasa tuone Wizara, sisi Wizara ya Elimu kule Zanzibar kwa mfano wameliona hili na wasichana wanaopata mimba kwa bahati mbaya, wanaendelea na masomo yao na imeonekana kwamba wengine hawa wanatokea kuwa wataalam wakubwa, wakatoa na mfano mzuri katika jamii, na mchango mzuri katika jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wizara yangu wakati nilipokuwa nahudumu kama Waziri, nilifika Bahamas. Nikatembelea darasa zima nikakuta watoto wote ambao wana miaka 16 hivi nakuendelea wote darasa zima wana mimba matumbo kiasi hiki. Lakini wameandaliwa darasa lao na wanafundishwa, kwa sababu huwezi kum-penalized huyu mtu, ile mimba inatokana na hali ya maumbile, saa nyingine huna nguvu za kumshinda mwanaume. Mimi baba yangu alisema usiende ukaa faragha na mwanaume itakuwa taabu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Fedha. Kwa dhati kabisa nakupongeza kwa umahiri na uhodari wako kwa jinsi unavyoliongoza Bunge hili na hivyo ndivyo tunavyotegemea, hutishwi wala hubabaishwi. Mimi ikiwezekana nataka ukae asubuhi na jioni uoneshe kama wewe uko fit kweli kweli. Maana hapa tuko katika sehemu ya kutunga sheria na kuondolea wananchi dhiki zao waliotutuma halafu tunakuja kufanya michezo ya kuigiza hapa kuingia na kutoka kama biharusi aliyekuwa hana kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo niseme kwanza naunga mkono hotuba hii ya Waziri wa Fedha kwa asilimia mia moja. Naamini kwa kupitisha bajeti hii basi yale mambo yote yaliyokuwa yanapata utatanishi au ugumu kidogo chini ya Mheshimiwa Dkt. Mpango yatakwenda sawa kwa sababu ni mchumi mahiri na anaweza kuongoza Wizara hii na naamini atafanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme katika kusimamia uchumi wa nchi yetu hii basi ni lazima uchumi huu uwe na udhibiti mkubwa, tutengeneze mikakati ya kudhibiti uchumi wetu. Kwa mfano, kwenye nchi hii sasa hivi mtu anatumia currency yoyote anayotaka na kwa sehemu yoyote anayotaka, hapa udhibiti unaonekana umekuwa hafifu. Unaenda sehemu saa nyingine unaambiwa ulipe kwa dola na wewe Mtanzania uko hapa, kwa nini? Kwa nini kule tunakokwenda kuwakilisha ukitaka kununua chochote kama kule South Africa, hata kama unayo hiyo dola au Euro unatakiwa ukanunue kwa pesa za kule ambazo ni rand. Sasa na sisi tuudhibiti uchumi wetu, Wizara ya Fedha ifanye kazi hiyo, shughuli ya kudhibiti currency yetu ifanywe kwa bidii zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mipango ya maendeleo inasema kwamba uchumi wetu kama sikosei umekua kwa 7% lakini ni kwa kiasi gani mtu wa kawaida anaweza kupata reflection hiyo? Unamfaidia vipi au mtu wa kawaida anaonekana vipi hali yake kunyanyuka kiuchumi? Kwa sababu haya maelezo tunayopewa hapa ni ya kisomi zaidi lakini tunataka aje chini hata yule mtu wa chini ajue anafaidika nini na ukuaji wa uchumi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nalotaka kuzungumzia ni hili la ukusanyaji wa kodi. Tunapongeza hatua zilizofikiwa za kuweka mashine za electronic sehemu nyingi lakini bado kuna uvujaji katika ukusanyaji huo, hii efficiency iko kwa kiasi gani? Kwa mfano, inawezekana na imeshatokea unakamatwa na traffic njiani anakwambia mashine ya kutolea risiti haifanyi kazi, sasa unamlipa nani au ile pesa ukiitoa inakwenda kwa nani? Hapa inaonekana ni vema udhibiti uzidishwe pamoja na kwamba tunakuwa na digital lakini udhibiti kwenye hivi vifaa vya kukusanyia kodi uwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la kukuza sekta binafsi. Sekta binafsi tumeambiwa inachangia uchumi kwa kiasi kikubwa na tunaunga mkono, jambo hili ni zuri. Hapa hapa inaonekana wadau wazalendo ambao wanashiriki kwenye hii sekta binafsi wanapata vikwazo kwa sababu wageni wanaleta bidhaa zao japokuwa hafifu, sisemi kama zote lakini nyingi ni hafifu, kwa bei ndogo ambayo wanaiuza hapa; mzawa na mwekezaji wa sekta binafsi anashindwa ku-compete. Hii binafsi na holela sana haifai, uwepo udhibiti wa bidhaa na tuwaunge mkono kweli kweli hawa wawekezaji wa binafsi ili waweze kushamiri. Kwa sababu nchi hii itajengwa na wenyewe wazawa, hao wengine wanakuja kuchuma kisha wanaenda zao. Itakuwa kama hii hadithi ya kudai mjusi, mjusi kachukuliwa tunadai hapa kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hali hiyo, naamini bado kuna kazi kubwa ambayo inatakiwa ifanywe na hii Wizara yetu ya Fedha na ninaamini itawezekana. Sina maneno zaidi kwa sababu mimi si mtaalamu wa fedha lakini kidogo mwanga ninao na naamini kwa kupitia Waziri wetu huyu kazi kubwa sana itafanyika. Nawapongeza wote na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii leo. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijaalia uzima na afya leo nikapata fursa hii ya kuweza kuchangia katika hotuba hii ya bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya kipekee nasisitiza na nakupongeza na nakuombea dua Mheshimiwa Naibu Spika, Tulia Ackson. Mungu akupe nguvu uendelee kuhudumu katika Bunge hili kwa umahiri kama hivi unavyofanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, umesimamia kanuni na taratibu bila kusita, hukubagua kama huyu mtu katoka chama gani wala nini. Mimi binafsi siku moja nilikatisha hapo ndivyo sivyo, ulivyomaliza kikao tu ukatoa mwongozo kwamba, siyo ruhusa kukatisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande mwingine nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Waziri wetu wa Fedha ambaye anapanga na anajua kupanga. Wizara hii amepewa kusudi kwa kuwa anajulikana anaimudu, uchumi wake unaonekana hapa na nimtie nguvu. Watu wengi humwita kaka yao, mdogo wao, sijui nani wao, mimi ni shemeji yangu na namwamini sana. Najua ataupeleka uchumi wetu kule tunakotaka kwenda kwenye uchumi wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa baada ya pongezi hizo na kutia nguvu huko, nianze kuzungumzia utaratibu wa kodi ya ongezeko la thamani. Hapa nataka kuhusisha ile section iliyozungumzia kuhusu bidhaa zitakazotoka kwenda pande mbili za nchi yetu za Muungano yaani Zanzibar na Tanzania Bara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nijue tu, je, kodi hii itahusisha vyakula? Nauliza kwa sababu kwenye ukurasa wa 48 wa hotuba, kifungu 67 namba moja mpaka mbili kimeondoa kodi kwa baadhi ya vyakula. Hali halisi ni kwamba Zanzibar inaagiza vyakula na mboga mboga kwa kiasi kikubwa sana. Sasa naendelea kutaka kujua kwa ufafanuzi, vyakula ambavyo havikutajwa kodi yake itakuwaje? Kama kuna uwezekano iandaliwe orodha ya vyakula ambavyo havitatozwa kodi ili kuepusha migongano.
Mheshimiwa Naibu Spika, wasiwasi mwingine juu ya kodi hii inayopendekezwa, kwamba je, pande hizi mbili zote zimeshirikishwa kupanga ili kuepuka kuwapa shida wananchi? Napendekeza pia kabla ya utaratibu huu yafanyike majadiliano ya kina kwa wadau wanaohusika na kwa kujua kiasi gani pande mbili hizi zimekutana na kutafakari mambo hayo ambayo kwa sehemu kubwa yasije yakasababisha kile kilichokuwa kinaitwa kero za muungano. Kwa sababu kwa spirit hiyo hiyo ya kuunganisha na kuboresha udugu wetu baina ya nchi yetu hii, kati yetu, basi ni lazima majadiliano ya kina yafanyike. Natambua kwamba Zanzibar ina bajeti yake na Bara ina bajeti yaken lakini ningeshauri hilo liwepo kwa spirit hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika sasa nataka kugusia uchumi wa viwanda ambalo ndilo tuliloambiwa na tulilotangaza kwenye ilani yetu na Mheshimiwa Rais wetu alisema kwamba Tanzania hii itakuwa kwenye uchumi wa viwanda na huko ndiko tutakopata manufaa. Naomba nijielekeze huko na naomba nilihusishe suala hilo na uwekezaji wa Kiwanda cha Sukari Bagamoyo ambacho kinajulikana kama Basic Bagamoyo Sugar Infrastructure and Sustainable Community Program. Hii ni program ambayo kwa bahati mbaya imepata mkwamo na imeanza siku nyingi sana, lakini ukichunguza kwa kina, mradi huu ni wa kipekee na unaendeshwa na mfadhili na Mwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mipango yote imepangwa. Mradi huu umeanza tangu 2005 na ungekuwa na faida kubwa kwa wananchi wetu kwa ujumla na hasa wananchi wa Bagamoyo. Wafadhili walikuwa tayari na washafanya study zao zote ni African Development Bank na IFAD na Mwekezaji ni ECO-ENERGY. ADB katika mradi huu ilivyojipanga ni kushughulikia miundombinu ya maji kuwafikia wakulima wadogo wadogo pamoja na barabara za mashambani. Pia kujenga bwawa la kuhifadhi maji litakalosaidia maji wakati wa kiangazi na kuzuia mafuriko.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwekezaji huu ambao umepatwa na vigingi vingi ungewasaidia sana. Kiwanda hiki kina uwezo wa kuzalisha tani 150,000 za sukari na tunajua sukari ni tatizo na tunajua pia kwamba Kiwanda hiki kinge-take off, kingeweza kuwa na 140,000 CDM za Ethanol na 90,000 megawatts za surplus ya electricity. Kiwanda kitazalisha ajira, na ndicho tunachopigania kwamba vijana wetu wengi hawana ajira; hapa zingetegemewa kupatikana ajira 2,500 hadi 3,000 za moja kwa moja na karibu ajira 13,000. IFAD inasaidia wakulima wadogo wadogo wa miwa na kusaidia vijiji 27 vitakavyozunguka na pia wananchi karibu 91,444 watafaidika na kujiendeleza na ukulima wa kisasa (smart agriculture). Halikadhalika pia wafanyabiashara wadogo wadogo watafaidika.
Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha sana kwamba mpango wa awamu ya nne wa BRN ulikusudia kuanzisha viwanda 10 ndani ya maeneo ya corridor ya kusini lakini mpaka sasa bado. Wafadhili wako tayari, gharama, project study zote zimeshafanywa, kitu gani kinachozuia?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kidogo nigusie ile pesa ambazo tunaweza kuzikosa mradi huu ukitutoka. Ni USD milioni 450 kwa ajili ya maandalizi, preparedness, USD milioni 10 kwa uhifadhi wa mazingira za kingo za Mto Ruvu na Wami, USD 350 kwa ajili ya monitoring na evaluation. Sasa sisi tunafikwa na nini? Nafasi hizi na fursa hizi tunazipoteza, wenzetu kwa mfano kule Swaziland wamefadhiliwa na watu hawa hawa, African Development Bank na IFAD na sasa hivi wanazalisha sukari nyingi na wanapata faida kubwa, humo humo wamepata kumwagilia maji, wanapata mahindi ya kutosha, sisi tunakwazwa na nini? Kwa nini fursa tunachelewa kuzishika? Kila kitu bureaucracy.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri afikirie sana tija itakayopatikana katika mradi huu. Inawezekana kuna watu ambao hawataki kwahivyo tutazame kwa kina faida inayopatikana….
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na afya, nikasimama mbele ya Bunge hili Tukufu ili kuweza kuchangia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati pamoja na pongezi kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa jinsi anavyosimamia, kuiendesha Serikali hii na kwa lengo la kuwapatia wananchi wote ustawi na maendeleo. Mheshimiwa Magufuli amefanya kazi nzuri na katika kazi yote hiyo iliyonifurahisha, moja inathibitisha kudumisha Muungano na inanifurahisha zaidi ni hii ya standard gauge nchini, Bombadia hewani, wabadhirifu, wafujaji na mafisadi kwapani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pongezi hizo za Dkt. Magufuli zinaenda pia kwa Mheshimiwa Makamu wa Rais kwa jinsi anavyoendeleza kazi zake, Mheshimwa Samia kwa kushirikiana na timu yake na vilevile Mheshimiwa Waziri Mkuu na Timu yote nzima ya Mawaziri na Watendaji, wanafanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nasimama kifua mbele hapa kutoa tena pongezi nyingine kwamba watu kule Uyui katika Uchaguzi Mdogo tumewabandika matokeo Chama cha Mapinduzi, katika Vijiji 14 tumepata na CHADEMA moja, Vitongoji 51 na kwa CHADEMA saba, CCM mbele kwa mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu hawa unaposema wewe wanakuwa wanaumia, wanakiherehere, lakini kila ukipigwa ngumi ndiyo unazidi kuwa imara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunajua umuhimu wa Muungano na ndiyo maana leo mimi niko hapa bila ya Muungano nisingekuwa na sauti hii ya kusimama hapa kusema. Umuhimu wa Muungano unajulikana, una tija, unaleta mshikamano, unaleta udugu. Sisi wengine tuna watoto mwisho wa reli huko, kwa sababu ya Muungano, hivyo hatuwezi kukubali Muungano huu ukatawanyika na Muungano huu una faida nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru mpaka sasa hivi kwenye ripoti hii tumeambiwa kero nyingi sana zimemalizika, zimebaki kama kero tatu hilo ni jambo la kupigiwa mfano, hongereni sana Wizara ya Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea sana lazima niseme hapa maana yake mimi bila ya kuletwa na Zanzibar haiwi. Natoa pongezi za dhati kwa Dkt. Shein kuendelea kuishikilia na kuiongoza Serikali ya Chama cha Mapinduzi bila wasiwasi, maendeleo yanaonekana, kazi nzuri inafanyika na wale wanaongoja zamu yao wangojee mpaka hapo 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la mazingira ambalo limeonekana kuwa ni tatizo kubwa sana. Mazingira yanaharibiwa vibaya sana, vyanzo vya maji, ukataji miti hovyo, ukataji mikoko ya baharini. Kwa mfano, kama sehemu za visiwa ile mikoko iko pale kwa kazi maalum ya biodiversity kulinda maji yasiingie zaidi, sasa inapokatwa maji yanasogea ardhi ambayo ingeweza kuwa ya kilimo inakuwa ya chumvi, kwa hivyo tija inapungua. Nafikiri iko haja ya kuendelea kuimarisha zaidi udhibiti wa maeneo haya au vilevile kutangaza maeneo ya hifadhi zaidi ya hayo yaliyopo ili kuzuia mambo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona kwamba kuna tabia ya watu kuchukua maji kutoka kwenye mito kupeleka kwenye sehemu zao wanazozitaka matokeo yake ni kuleta shida, kwa nini na sisi hatufanyi kama vile walivyotangaza wenzetu kule India ule Mto Ganges na mito yetu na sisi tukawa tunaiangalia kwamba mtu atakayechafua chafua
au atakayeharibu anakuwa sawa na ku-temper na uhai, kwa hivyo lazima kuwa na udhibiti muhimu, tuziimarishe hizo sheria zetu za kudhibiti kwa sababu tunajua mazingira yakiharibika ndiyo uhai unapotea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninalotaka niligusie kwa haraka haraka ni suala la ajira. Tunajua kwamba yalikuwepo makubaliano ya tutapata asilimia ishirini na moja ya share ya ajira kwa Zanzibar kwa nafasi za kutoka kwenye Taasisi za Muungano, sasa nimeambiwa nafasi hizo zipo lakini nataka Waziri akija hapa atuambie katika nafasi hizo wamepata Wazanzibari wangapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwamba kwa nafasi ya Majeshi na Polisi huko hatuna tabu vijana wetu wengi wanapata ajira. Kwa hivyo, tunaomba tufahamu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri kuhusu hizo nafasi kwa sababu katika kuzipata hizo nafasi kwa vijana wetu yako malalamiko ya kusuasua katika kupatikana nafasi hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuzungumzia ni hili la kuhusu makazi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais kule Zanzibar bado hayajawa katika hali nzuri sana yamechoka, nafikiri iko haja ya kufikiria kufanya ukarabati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee nataka nizungumzie ukiunganisha na hiyo kwamba bajeti inayotolewa kwa Ofisi hii naona haitoshelezi, iko haja ya kuongezwa. Kwa mfano, Ofisi binafsi ya Makamu wa Rais kupata 3.7 kwa mwaka mzima bado ni ndogo sana. Kwa mwaka jana Wizara hii ilipangiwa billioni nane lakini imeweza kupata millioni mia mbili, sasa inawakwaza watendaji wa Wizara hii, pamoja na Mawaziri ambao wanafanya kazi nzuri sana, lakini tusipowapatia pesa za kutosha inakuwa ni kikwazo. Tunawapa kazi lakini hatuwapi nyenzo za kufanyia kazi za kutosha, hivyo iko haja ya kufikiria ili kuongeza kipato chao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kusema, ni muhimu kuhakikisha Muungano huu unadumu na
unaendelea kudumu kwa sababu ziko tija tunazozipata na usalama tunao na tunaona faida zake. Kwa hivyo siyo Muungano wa kufanyia masihara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kuwa na maneno mengi, maneno yangu ni kwamba Muungano udumu na tunaona kazi inayofanywa na viongozi wetu kwa hivyo tuwape support. Wanawake kwa upande wetu tunashukuru viongozi wetu wametupa nafasi za kutosha, lakini tunataka zaidi lakini kila tukisema tunataka zaidi Mheshimiwa Rais anasikia na anatuongezea.