MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, asante sana. Nashukuru sana kupata fursa hii ya kipekee na ya heshima kubwa sana kwangu na kwa Serikali yangu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, utendaji na utekelezaji wa Ilani ya chetu cha CCM kwa kiasi kikubwa umekuwa na mafanikio. Mheshimiwa Waziri Mkuu utekelezaji wa ilani katika sekta ya kilimo, nishati, elimu, afya, madini, n.k. kumekuwa na hatua ya kuridhisha sana.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa karibu kipindi chetu kinakwisha tunakaribia uchaguzi Mkuu wa 2020 naomba kuuliza Serikali, lakini kabla sijauliza niseme kwamba, mafanikio haya tuliyoyafikia leo yamefikiwa kupitia na juhudi kubwa za Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na timu yake akiwemo Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia, Waziri Mkuu wewe mwenyewe Majaliwa na watendaji wote wa Serikali ambao wamefanya kazi nzuri kufikia maeneo hayo niliyoyataja hapo juu. Sasa hivi Serikali itakamilisha lini utaratibu wa kuwawezesha Watanzania wanaoishi nchi za nje kuweza kupata nafasi yao ya kidemokrasia kupiga kura?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha, Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa anataka kujua Serikali inaandaa utaratibu upi wa kuwezesha Watanzania walioko nje ya nchi kuja kupiga kura nchini wakati wa uchaguzi mkuu na chaguzi nyingine:-
Mheshimiwa Spika, jambo hili ni la kisera na Serikali imeendelea kuona utaratibu huo kama unaweza kufaa kwa sababu, lazima kwanza tupate kujua nani wako nje ya nchi, idadi yao, wanafanya shughuli gani na kama je, bado ni Watanzania au waliomba uraia nchi za nje. Na pindi sera hiyo itakapokamilika pale ambapo itaonekana inafaa tutakuja kulijulisha wote, Bunge na Tanzania nzima. Asante sana.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii leo kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu maswali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, nchi nyingi duniani zimeanza kuachana na mpango mzima wa kutumia pembejeo, viatilifu, madawa makali ya viwandani kwa kilimo na zinajikita zaidi katika kilimo hai.
Mheshimiwa Waziri Mkuu nchi yetu bado inakuwa soko la mbolea, viatilifu, dawa za viwandani ambazo si nzuri kwa afya na ubora wa ardhi yetu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kuna viatilifu 24 ambavyo vimeshapigwa marufuku duania kwamba vinasababisha kansa na kuharibu uzazi, lakini bado vinaendelea kutumika Tanzania yetu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, nchi kama Ufaransa tayari ina Wizara nzima inashughulikia kilimo hai na Uganda jirani yetu ana sera; je, Serikali haioni sasa kwamba ni muda muafaka wa kuanzisha walau idara maalum ya kushughulikia kilimo hai na kunusuru afya za wananchi wake na kuboresha ardhi yetu na vilevile kupanua soko la bidhaa za kilimo hai ambazo ina bei kubwa duniani na hasa kwa vile Tanzania tuna nchi ya kutosha na friendly kwa ajili ya shughuli hizo za kilimo hai na kuwapa msukumo vinara wa kilimo hai? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Mshua, Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua mpango wa Serikali wa kuanzisha idara maalum inayojikita na utafiti au kilimo hai. Ni kweli kwamba Serikali imeendelea kuhamasisha wakulima kwenda na kilimo hai. Kilimo hai hakihitaji mbolea za kemikali na tumeona mafanikio makubwa kwa wakulima ambao wanalima kilimo hai kwenye mazao kadhaa. Wiki mbili, tatu zilizopita nilikuwa mkoani Kagera ambako tulikuwa tunahamasisha kilimo cha kahawa na tulikuta wakulima wa makindi mawili wale ambao wanalima kilimo kinachohitaji pembejeo zilizotoka kwenye viwanda, lakini wako ambao wanalima kahawa wanatumia pembejeo ambazo zinatokana na mimea yetu ya asili ambayo bado tunaendelea nayo kama vile samadi, mboji na vitu kama hivyo.
Mheshimiwa Spika, Serikali tumeanza mpango wa kuimarisha kilimo hiki pale ambako tumeunda taasisi tunaita TPRI iko pale Arusha ambayo inapima viatilifu vyote vinavyoingia nchini kwa ubora wake kulingana na ardhi tuliyonayo ndani ya nchi. Kwa sababu matumizi ya mbolea yanategemea na ardhi tuliyonayo na hasa zile mbolea za kemikali ili kuzuia uharibifu wa ardhi tuliyonayo.
Kwa hiyo, tunaendelea na mkakati huo na kuwawezesha na kuwahamasisha wakulima kulima kilimo hai na tunawashauri ni aina gani ya mbolea inahitaji kutumia kilimo hicho na tunaweza kuona pia faida kwamba ukilima kilimo hai cha kahawa unapata bei kubwa zaidi kuliko kilimo kinachotumia mbolea za kemikali.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tumeendelea kuhamasisha hilo na taasisi yetu ya TPRI inaendelea kutoa mafunzo, lakini tunaanzisha kitengo maalum, kurugenzi maalum ndani ya Wizara ya Kilimo kusimamia hamasa ya kilimo hai kwenye mazao kadhaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niendelee kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote na wananchi ambao wanashughulika na kilimo kwamba wale wanaotaka kulima kilimo hai hii ni fursa sasa na tunaendelea kuwaambia aina gani ya mbolea inayotokana na mazao mbalimbali tukiozesha na kuweza kutumia mbolea hizo wakapata bei nzuri.
Nimepata nafasi ya kwenda Busokelo kwenye zao la Kokoa nako pia kuna wakulima wanalima kilimo hai na wanapata bei nzuri tu. Tumeenda pia hata kwenye chai tumeona watu wanalima kilimo hai wanapata bei nzuri tu. Kwa hiyo, kilimo hai kina tija zaidi kuliko kulima mazao yanayohitaji hizi mbolea za kemikali.
Kwa hiyo, hamasa hiyo inaendelea na tutaendelea kuwafikia wakulima na Wizara sasa imeimarisha kupeleka Maafisa Ugani mpaka Wilayani na moja ya jukumu lao ni kuhamasisha wakulima kulima kilimo hai lakini kuwaonyesha ni aina gani ya viatilifu ambavyo vinaweza kuwasaidia wao kukuza zao lao kwa kilimo hai, ahsante sana. (Makofi)