Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Asha Abdullah Juma (66 total)

MHE. ASHA A JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa mwingiliano baina ya wananchi na kambi ni mkubwa, sasa pamoja na hatua za miti na kuta, ni kwa kiasi gani au ni tahadhari gani ya ziada zilizochukuliwa kukabili matokeo ambayo hayatarajiwi ya bahati mbaya kama yale yaliyotokea Gongolamboto na Mbagala? Na nataka nithibitishiwe hapa kwamba wahanga wote wa Gongolamboto na Mbagala kama walishapata fidia?
Swali la pili, ni kwamba Jeshi linapopanua sehemu zake hizo huwa linatoa fidia. Je, katika suala hili limejipanga kiasi gani katika mpango wa kulipa fidia kwa wananchi ambao inawahamisha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (Kn.y WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA): Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya Serikali kwa swali lake la kwanza ni kwamba mpaka hivi tunavyoongea hapa tayari ndani ya Jeshi kuna mikakati ya kujenga maghala mapya na kwa kiasi kikubwa maghala mapya ya kuhifadhia ilaha yamekwisha kamilika kwenye vikosi mbalimbali, kambi mbalimbali. Japakuwa sitovitaja ni vikosi gani kwa sababu za kiusalama, lakini tayari mabomu na vifaa vyote vya milipuko vya Jeshi vimekwishahamishwa kwenye kambi ambazo zipo karibu zaidi na wananchi na kuwekwa kwenye maghala hayo mapya ili kuondoa uwezekano wa matatizo kama yale yaliyojitokeza pale Mbagala na kule Gongolamboto.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa fidia tayari naamini utakuwa ulishaanza na pengine ulishamalizika sina uhakika sana na hilo, naomba nisiseme lolote.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali lake la pili, kuhusiana na wananchi kupatiwa fidia kwenye maeneo ambayo Jeshi linaonekana limevamia. Kiukweli ni kinyume chake. Jeshi limekuwepo katika maeneo haya ya makambi kwa kiasi kikubwa lakini wananchi ndiyo wamekuwa wakivamia maeneo ya majeshi. Lakini kwa kuwa Jeshi hili ni la wananchi na ni rafiki kwa wananchi, japokuwa wananchi wanavamia Jeshi mara kadhaa limekuwa hata likilazimika kuhamisha mipaka yake kutoka kule waliko wananchi na kuingiza ndani zaidi kwenye maeneo yake. Pamoja na kwamba wanayahitaji hayo maeneo lakini Jeshi kwa sababu ni la wananchi na ni rafiki kwa wananchi limekuwa likifanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niwasihi wananchi wote ambao wapo karibu na maeneo ya Jeshi wasiendelee kuwa na tabia ya kuvamia maeneo ya majeshi na tayari sasa hivi Serikali imeshaanza kubaini mipaka yote ya kambi za majeshi na kupanda miti kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi na kwenye kambi hizi ndogo ndogo kuweka fence aidha ya wavu ya ukuta. Ninaamini tunapoelekea matatizo kama haya ya mwingiliano baina ya wananchi na Jeshi hayatojitokeza.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu na kwa kuwa mimi ni msema kweli daima napenda niseme sijaridhika na majibu hayo; na kwa kuwa, Serikali yetu hii ya Awamu ya Tano imejikita zaidi kuwaondolea dhiki wanyonge na wanyonge wa Zanzibar pamoja na Tanzania Bara bado wanapata dhiki katika suala hili, nipende kusema na kumwambia Waziri kwamba ni kwa kiasi gani Serikali itaongeza udhibiti wa mamlaka husika kwa kuhakikisha kwamba bei hizi zinapungua na wananchi wanapata nafuu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa haiingii akilini Mhesimiwa Waziri anaposema kwamba mtu anayetaka kufanya safari afanye booking siku nne au siku ngapi hizo zote anazoziona yeye; kwa kuwa safari nyingine ni za dharura sana. Kwa mfano, watu wanapokuja huku Bara ni kwa ajili ya kupata tiba katika Hospitali ya Rufaa, pengine Muhimbili, pengine Kituo cha Cancer Ocean Road na mambo mengine ya dharura mtu anapoumwa unapomwambia akafanye booking ya siku nne ili apate nafuu ya ndege nafikiri hiyo siyo sahihi.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, Mheshimiwa Waziri bado atilie mkazo katika mamlaka hizi pamoja na hivyo vyombo vya pwani, bado nauli hii bado ni kubwa sana kwa wanyonge…
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nataka majibu ya maswali yangu hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kukubaliana na maelezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Asha Abdullah Juma na ninamhakikishia kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwamba tutafute muda twende wote Zanzibar tukakutane na Zanzibar Maritime Authority, ili tukalijadili hilo kwa undani, hatimaye mamlaka hizo mbili za Muungano, mamlaka iliyoko upande wa Zanzibar na mamlaka iliyoko upande wa Tanzania Bara ziweze kutekeleza majukumu yake kama ambavyo Mheshimiwa Asha Abdullah Juma amependekeza. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa mashaka ya vijana wetu yamekuwa yakizidi siku kwa siku, vijana wanajihusisha katika michezo hii ambapo muda mwingi unapotea hata muda wa masomo, muda wa kufanya kazi …

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Maadili yamepotea, kuna masuala ya betting ambayo yanachukua muda mwingi wa vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Waziri kuniambia kwamba kuna Sheria Namba 4 inayoruhusu mambo hayo lakini udhibiti wake ukoje? Je, mpaka sasa ni wafanyabiashara wangapi wamekamatwa na maduka yao kufungwa ambao hawakuzingatia taratibu za kuzuia vijana wenye umri mdogo kuingia sehemu hizo na je, wamepelekwa kwenye vyombo husika na kuchukuliwa hatua?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza aliuliza udhibiti wake ukoje, kama nilivyosema sheria yetu imeweka wazi na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha iko makini kusimamia michezo hii yote ndani ya nchi yetu ili kuhakikisha sheria hii iliyotungwa na Bunge letu Tukufu inafuatwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, ni watu wangapi na maduka mangapi yamefungwa, naomba nilichukue swali hili tuweze kulifanyia kazi kwa sababu linahitaji data mahsusi ili tuweze kumjulisha Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako Tukufu.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ila nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, kwa kuwa nyendo zimekuwa nyingi, watu wanakwenda sana kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa ajili ya kiuchumi na mengineyo, kwa hiyo ajali za majini, baharini na kwenye maziwa yawezekana zikatokea. Serikali imejipanga hivi ilivyojipanga; Je, Serikali inaonesha vipi shughuli zinazofanywa na SUMATRA na kule Zanzibar, kwa sababu bado ajali zitakuwa zinatokea tunafanyaje?
Swali la pili; Serikali ina mpango gani kwa wale waliopatwa na msiba na kupoteza ndugu zao wakati ilipopata tatizo MV Bukoba, MV Spice Islander iliyozama kule Nungwi na ajali nyingine. Je, watu wote hawa wameshalipwa fidia zao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mahusiano ya MRCC na upande wa Zanzibar, naomba nimhakikishie kwamba MRCC ni ya masuala ya Muungano na yanasimamiwa na SUMATRA, kwa hiyo Zanzibar Maritime Authority watashirikiana na taasisi yetu katika kusimamia hii MRCC iweze kuhudumia pande zote za Muungano mara ajali inapotekea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la pili nimuombe tu Mheshimiwa Asha Juma kwamba ajali ya MV Bukoba na ajali nyingine zote zimeshughulikiwa na Serikali kwa kiwango kikubwa sana, maadam sina takwimu hapa nisingeweza kumpa undani wa nini kilifanyika, lakini ni masula ambayo yalishughulikiwa na Idara yetu ya maafa iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ukamilifu kabisa.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza nashukuru kwa majibu, nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa pamoja na mikataba na vipengele vingi vilivyoratibiwa vizuri hali bado kwenye eneo hili siyo nzuri. Bado wananchi wetu wengi wanaendelea kupata matatizo hasa wanawake wanaokwenda kufanya kazi nchi za Urabuni. Serikali kupitia Ubalozi wetu inalazimika kutumia gharama nyingi za kifedha ambazo zingeweza kutumika katika shughuli za maendeleo, kwa mfano, miundombinu, standard gauge na kutununulia ndege nyingine ya Bombadier. Je, Serikali haijaona kwamba sasa wakati umefika wa kuwakatibisha hawa ma-agent, wafanya mikataba ili kuweza kuweka deposit ya fedha ambazo zitatumika kuwashughulikia wananchi wetu hawa inapobidi kurudishwa wanapokuwa wagonjwa wakati wanapokuwa wametelekezwa na waajiri wao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa zipo taarifa na malalamiko kwamba baadhi ya wananchi wetu hawa wanaokwenda kufanya kazi huko huambiwa, kwa mfano, wanakwenda kuuza duka wakafika kule wakafanyishwa kazi nyingine kinyume na hilo duka na kinyume na ridhaa yao na pengine kusababisha hatari kwenye afya zao. Je, Serikali inalisaidiaje jambo hili katika kudhibiti na kuhakikisha kama wananchi wetu hawaendi kuongezewa udhalilishaji huko nchi za Kiarabu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI): Mheshimiwa Spika, la kwanza, Mheshimiwa Mbunge alitaka kujua namna ambavyo Serikali tutaweka mfumo mzuri wa kuweza kuwabana mawakala hawa. Kazi hii ya kuwapeleka Watanzania kufanya kazi nje ya nchi inaratibiwa kwa mujibu wa sheria zetu na mawakala hawa wanasajiliwa katika utaratibu ambao umewekwa. Wakala yeyote ambaye anavunja masharti na matakwa ya sheria hizi tumekuwa tukimchukulia hatua kwa kufuta pia usajili wake ili kumtaka ufuate taratibu za nchi ambazo tumeziweka katika kupeleka wafanyakazi nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, lakini pia katika eneo hili nitoe rai tu kwa wafanyakazi wote ambao wanafanya kazi nje ya Tanzania hasa katika nchi za Kiarabu hususani Oman kufuata taratibu tulizoziweka kupitia Ofisi ya Wakala wetu wa Huduma za Ajira (TAESA) ambapo tumeweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba kabla ya mfanyakazi wa Tanzania hajatoka nje ya nchi tunafanya kwanza mawasiliano kufahamu kazi anayokwenda kufanya lakini na mkataba na malipo yake. Matatizo mengi yanakuja kwa sababu asilimia kubwa ya wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi hawapitii katika utaratibu ambao tumeuweka na ndiyo maana wakipata matatizo huwa inakuwa ngumu sana kuweza kushughulikia kwa sababu hawajapitia katika mfumo wetu na hawapo katika kanzidata yetu ya watumishi ambao wanafanyakazi nje ya nchi. Nitoe rai kwa Watanzania wote wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi kufuata taratibu ili wapatapo matatizo iwe rahisi kuweza kuwasaidia.
Mheshimiwa Spika, la mwisho, katika hili eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge amelizungumza kuhusu kwenda kufanyishwa kazi kinyume na utaratibu uliowekwa, haya yote yanatokana na iwapo tu wafanyakazi hawa hawatakuwa wamepitia katika ofisi zetu. Sisi tunawabana mawakala ili waje na mikataba ambayo tutaipitia wote kwa pamoja na Ubalozi utabaki na nakala yake ili kuweza kufuatilia. Inapotokea Mtanzania anafanya kazi tofauti na ile ambayo ilisemwa katika mkataba ni rahisi kwenda kuripoti katika Balozi zetu na sisi kuweza kuchukua hatua.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi, napenda niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mashaka, matatizo, huzuni na gharama kubwa za matibabu zinaendelea kuwakabili vijana wetu hawa kutokana na hizi ajali za bodaboda. Je, ni lini Serikali itaongeza usimamizi na udhibiti wa kuhakikisha kwamba helmet na reflector zinavaliwa na vilevile kudhibiti upakianaji wa kimishikaki ambao unasababisha watu wengi zaidi kuumia kwa wakati mmoja? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu maelekezo tulishatoa na tunachukua hatua kwa maswali yote mawili aliyoyauliza. Moja likiwepo hili la kuvaa kofia ngumu, tumeweka hiyo ni sheria na tumeenda mbali zaidi tunataka si tu mwendesha bodaboda tunataka hata abiria naye atimize wajibu huo wa kuvaa kofia ngumu. Pamoja na hilo, hili lingine la ubebaji wa mishikaki kama alivyoita, abiria zaidi ya moja na lenyewe tumeelekeza popote pale yanapotokea lichukuliwe kuwa ni kosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema mwanzo kwamba jambo hili ni vema likaongelewa kwa ngazi ya kijamii na familia kwamba tuendelee kuwaelekeza vijana wetu. Mara nyingi vijana wetu wakielekezwa kwa mkono wa Serikali wanaona kama wanaonewa lakini wakielekezwa kuanzia ngazi ya familia, tunapokaa tuwaambie vijana wetu tunawapenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe niliwahi kuwapa vijana bodaboda kule Jimboni, niliwahi kuwapa wadogo zangu, watoto wa dada zangu lakini jambo la kwanza nililowaambia, niliwaambia nawapa chombo hiki cha moto lakini chombo hiki kinauwa. Wakiambiwa mkono ambao usio wa kisheria ambao ni wa kifamilia linawakaa zaidi kutambua kwamba ukikosea masharti ya uendeshaji ukaenda kasi, ukakosea sheria za uendeshaji barabarani, gharama yake ni kupoteza maisha ya mwendeshaji mwenyewe na abiria aliyebebwa kutoka kwenye hicho chombo.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa mashaka na madhila yatokanayo na matumizi ya vipodozi hatarishi yanazidi kuwaathiri wananchi wetu waliokuwa wengi, japokuwa Mheshimiwa Waziri umegusia kama mtatoa elimu, lakini nataka kujua kuna mkakati gani madhubuti kwa elimu hii ya umma ili wananchi hawa wafahamu na wasiweze kutumia vipodozi hivi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali iwe na mkakati wa kuwawajibisha na kuwalazimisha kulipa gharama za tiba kwa maradhi yanayosababishwa na matumizi ya vipodozi hivi kwa vile kila siku tunaambiwa tusitumie na wao hawasikii. Kwa hiyo, sehemu ile ya tiba walipe wale kwa sababu Serikali ina maradhi mengi sana ya kushughulikia, lakini bado…
inashughulikia maradhi ya makusudi ya kutafuta weupe. Kwa hivyo, Serikali ina kauli juu ya hilo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Asha Mshua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumeanza mkakati wa kutoa taarifa na elimu katika vyombo vya habari, mihadhara, matangazo ya redio, mafunzo kwa njia ya mada, maonyesho pamoja na huduma kwa wateja.
Katika mwaka wa fedha 2016/2017 tumeweza kutoa elimu kwa wanafuzi 73,323 katika vyuo saba na shule za sekondari 170 katika mikoa yote 21 nchini. Nitaendelea kusisitiza kwamba tunapokea ushauri wako Bi. Mshua na tutajaribu kuzingatia wakati tunafikiria kuongeza adhabu zinazohusiana na uingizaji na matumizi ya vipodozi haramu.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri yaliyotolewa na Mheshimiwa Anthony Mavunde, Naibu Waziri anayehusika na masuala haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, kutokana na kwamba bado hakujawa na udhibiti wa kutosha wa kuzuia madawa ya kulevya yasipenye na kutokana na tulivyomsikia Mkuu anayeshughulika na udhibiti wa madawa ya kulevya kwamba kule Zanzibar bado kunatumika kama kipenyo cha kupitisha madawa haya ya kulevya. Je, Serikali imejipangaje kuongeza ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi ili kudhibiti na kuhakikisha kwamba kule Zanzibar hakuwi mlango wa kupitisha madawa haya ya kulevya? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli baada ya jitihada na juhudi kuwa kubwa sana Tanzania Bara, hasa kazi kubwa sana ambayo ilifanywa na Mamlaka ambayo imewafanya wafanyabiashara wengi sana wa dawa za kulevya nchini na wengine kukimbilia Zanzibar, ni kweli sasa Zanzibar imeanza kutumika kama sehemu ya uchochoro wa wafanyabiashara ambao wanakimbia kutoka Tanzania Bara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi inayofanyika hivi sasa ni kuhakikisha kwamba tunaanza kufanya kazi kwa pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kwanza kutengeneza mfumo mzuri wa kusaidia katika kuhakikisha kwamba tunawabaini wafanyabiashara hata hao wanaokwenda nje Tanzania Bara ambao wanakwenda Zanzibar. Pia vimekuwepo vikao vya mara kwa mara kati ya Mamlaka na wataalam kutoka kule Zanzibar, lengo lake kubwa ni kuhakikisha kwamba tunatengeneza mfumo mzuri wa udhibiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimwondolee hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hiyo inaendelea na tayari tatizo hilo limebainika, naamini muda siyo mrefu sana maridhiano yakikamilika basi tutafanya kazi pia kuhakikisha kwamba tunazuia na upande wa Zanzibar.(Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa bado hali ya upatikanaji maji katika baadhi ya mabweni hasa vyooni haujarekebishwa pamoja na kutengewa hizo shilingi bilioni mbili na kupatikana hizo zilizopatikana. Je, ni lini Serikali itafanya zoezi la dharura kuhakikisha maji yanapatikana hasa hizi sehemu za vyooni wakati ukarabati mkubwa ukiendelea?
Swali la pili, nilitaka kufahamu katika ukarabati huo, je, Serikali ina huo mpango wa kuyabomoa kabisa yale majengo yaliyochoka na kuyaweka mengine yenye sifa na haiba ya Chuo hiki Kikuu cha Mzumbe na lini jambo hili litatekelezwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. la kwanza; katika kufanya marekebisho ya dharura tayari tumeshawaelekeza na hatua zinachukuliwa kuhakikisha kwa kutumia fedha zao za ndani Chuo cha Mzumbe kitaanza mara moja katika ukarabati wa miundombinu hiyo ya maji.
Lakini vilevile katika mpango wa kudumu kuhusiana pia na majengo ambayo yana hali mbaya, kwa mwaka huu wa fedha unaoanza Wizara yetu imejipanga vizuri sana na kwamba tuna fedha taslimu takribani shilingi bilioni 56 hizo tunazo mkononi kwa ajili ya kuboresha vyuo vyetu mbalimbali ikiwemo Mzumbe ambayo itapatiwa mabweni ya kutosha wanafunzi 3,000 pamoja na kumbi za mihadhara na majengo mengine ya utawala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo vingine ni pamoja na Chuo Kikuu Huria ambacho kitapata jengo hapa Dodoma, Chuo cha Ushirika-Moshi lakini pia mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na pale DUCE.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyeki, ahsante kwa majibu mazuri. Nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa usumbufu umekuwepo kwa watumiaji wa hizi cable hasa hii Cable ya Dodoma, mtu ushaharibikiwa inabidi uende trip mara mbili, mara tatu kuripoti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa majibu aliyonijibu Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba inabidi uende tena Ofisi ya Mamlaka ya Mawasiliano ukatoe ripoti, hizo ni gharama na ni usumbufu. Kwa nini Serikali isiweke kitu kama hotline ikiwa mtu unaposumbuliwa na mambo kama hayo unapiga ukapata ripoti ili kuhakikisha kwamba mtumiaji anapata haki kwa ile pesa yake aliyoitoa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyeki, swali langu lingine ni vile unavyokwenda kutaka kujiunga na hizi cable unaahidiwa utapata channel kama 200 au 300. Inapokuja kwenye hali halisi ukijaribu kutafuta channel nyingi unaambiwa access denied, sasa huu kweli si wizi wa kiwaziwazi? Je, Serikali inadhibiti vipi kuhakikisha kwamba mtumiaji anapata haki yake kwa pesa aliyoilipia? Nahisi bado Mamlaka ya Mawasiliano inatakiwa izidishe udhibiti kwenye vyombo hivi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyeki, napenda kumtaarifu tu Mheshimiwa Asha kwamba huwa zipo hotline lakini kwa kweli sasa hivi sipo nazo kichwani. Baada ya muda tukikuta tu hata pale canteen nitakuwa nimeshazipata kutoka kwa watu wa TCRA CCC na kumpatia ili kuweza kuwasiliana na watu ambao wako pale kwa ajili kuhudumia wateja.
Mheshimiwa Mwenyeki, swali lake la pili ni kuhusu channel chache kuliko zinavyopaswa, hiyo inahusika na masuala ya ving’amuzi. Nipende tu kumhakikishia Mheshimiwa Asha kwamba Serikali kupia TCRA tunaendelea kuwahakiki hawa wanaotoa huduma za TV. Kuna leseni mbalimbali, leseni kama DSTV wale wako wazi kabisa kwamba channel za bure ni mbili au tatu lakini kwa mfano hivi ving’amuzi vingine kama Dodoma Cable, sijapata uhakika Mheshimiwa Asha wana channel za bure ngapi na kwa zipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakapopata uhakika nitakuwa na nafasi nzuri sana ya kukujibu lakini tuna uhakika na kama Serikali tunafahamu kwamba kuna baadhi ya cables ambazo zinatakiwa zitoe channel za bure na zile ambazo hazitoi channel za bure tunazifuatilia kwa karibu ili tuweze kuzifungia kama zinakiuka masharti.
MHE. ASHA ABDALLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, bado vijana wengi wanaomaliza darasa la saba wanakuwa hawajapata nafasi kwenye vyuo vya ufundi au kuendelea na masomo ya sekondari. Ni lini Serikali itaboresha elimu ya msingi kuhusisha mafunzo ya ufundi ndani yake ili kuwaasaidia wale wanaobaki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mtaala wa VETA ni mmoja nchi nzima wakati mahitaji yanatofautiana sehemu na sehemu. Kwa mfano, mikoa yenye gesi wangefundishwa mambo yanayotokana na gesi, mikoa ya uvuvi wangefundishwa taaluma za uvuvi na mikoa ya madini vivyo hivyo. Sasa Serikali ina utaratibu gani kuhusu kuingiza component hiyo katika mitaala yake?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuhusu suala la wanafunzi ambao wanamaliza darasa la saba lakini hawapati nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari, kama ambavyo nimesema kwenye majibu yangu ya msingi, Serikali inafanya kazi kubwa ya kuongeza nafasi za udahili kwenye vyuo vya ufundi kwa kujenga vyuo vipya vya ufundi pamoja na kuboresha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niseme kwamba katika mtaala wa elimu ya msingi kuna somo la stadi za kazi ambalo limewekwa mahsusi kwa ajili ya kuwapatia vijana wetu angalau ujuzi ili hata yule anayemaliza elimu yake ya msingi awe tayari ana uwezo wa kufanya jambo katika mazingira yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu mtaala wa VETA kwamba unafanana, kimsingi masuala ya ufundi yanatakiwa yaangalie mazingira halisi ya mahali ufundi unapofanyika. Kwa hiyo, suala la kuangalia masuala ya gesi au masuala ya uvuvi ndiyo jambo ambalo limekuwa likifanyika. Kwa hiyo, niendelee kutoa wito kwa wote wanaotoa mafunzo ya ufundi stadi wahakikishe kwamba mitaala yao inazingatia mazingira halisi ya pale ambapo wanatoa mafunzo ili kuwawezesha wananchi wa eneo husika kuongeza tija katika shughuli wanazozifanya.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi, na mimi nina maswali mawili ya nyongeza.
Moja kumbe, haya. (Kicheko)..... Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ziko sababu kadhaa ambazo nyingine hazizuiliki zinazosababisha watoto hawa kuzaliwa mapema, je, Serikali ina utaratibu gani wa kuziimarisha na kuziboresha hizi special care intensive nurseries zilizopo na zipo ngapi katika mikoa yetu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali la msingi huduma kwa mtoto yeyote ambaye anatarajiwa kuzaliwa inaanza katika mahudhurio ya kliniki. Ninaendelea kusisitiza na kutoa rai kwamba wanawake wajawazito na baada ya kubaini wameshapata ujauzito ni muhimu sana kwenda kliniki mara nne, kwa sababu katika mahudhurio haya ya kliniki ndipo hapo ambapo tunaweza tukabaini changamoto kama hizo na uwezekano wa mtoto kuzaliwa akiwa njiti. Sambamba na hilo nimesema kwamba tumetoa elimu kwa watoa huduma wetu wote katika ngazi zote kuhusiana na jinsi gani wanaweza wakawahudumia watoto njiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali sasa hivi katika bajeti ambayo mmetupitishia katika moja ya kipaumbele ambacho tumesema tutaweza kuweka katika hospitali za rufaa za mikoa ni pamoja na huduma za Neonatal ICU. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru sana kupata majibu hayo ya kina ambayo yameelezea vizuri sana juu ya miradi muhimu kama hiyo REA, Standard Gauge na bomba la mafuta lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, ni kwa nini Serikali isije na utaratibu wa kuwachukua vijana hawa moja kwa moja kutoka kwenye vyuo ili kuwapunguzia mihangaiko ya kuzunguka na barua za maombi na kushinda mitandaoni kama ilivyokuwa kwenye sekta nyingine, mfano, afya na elimu ambapo watu hupata ajira kwa wepesi zaidi kutokana na taaluma zao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, Wizara hii na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ina mikakati gani kutengeneza mazingira wezeshi ikiwemo Incubation Centres za uhakika za kutosha, mitaji, vitendea kazi kwa wahitimu hawa ili waweze kupata wepesi wa kujiajiri na vilevile kwenda na Sera yetu ya Tanzania ya Viwanda, Inawezekana? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza la kuwachukua vijana hawa wahitimu wa vyuo vya ufundi moja kwa moja, tunachokifanya kama Serikali kwanza kabisa kwa kushirikiana na sekta binafsi ambazo pindi nafasi zinapopatikana huwa tunawaunganisha moja kwa moja na vyuo vyetu vya ufundi ili vijana hawa waweze kupata nafasi za ajira za moja kwa moja. Pia baadhi ya vyuo, kwa mfano, Chuo cha Don Bosco kimekuwa kina utaratibu wa kila mwaka kuandaa Kongamano la Waajiri ambapo wamekuwa wakiunganisha wahitimu hawa moja kwa moja na waajiri na vijana wengi wameajiriwa kwa kupitia mfumo huo. Kwa hiyo, naamini kabisa wazo la Mheshimiwa Mbunge ni jema, nasi kama Serikali tutaona namna ya kuweza kuviunganisha vyuo vyetu vya ufundi pamoja na waajiri ili vijana hawa wapate nafasi za ajira za moja kwa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, suala la incubation kwa ajili ya kuwandaa vijana hawa, kuwalea na kuwapatia mitaji, sisi Ofisi ya Waziri Mkuu tunavyo Vituo vya Vijana. Kipo Kituo cha Vijana Sasanda-Mbozi, Ilonga pale Kilosa na Kilimanjaro. Vituo hivi viko kwa ajili ya kuwalea vijana na kuwandaa kuwa na sifa za kuajiriwa. Pia vijana hawa wanawezeshwa kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Vijana ambao umekuwa ukitoa mikopo kwa vikundi vya vijana lakini vilevile na asilimia 5 za mapato ya ndani ya Halmashauri yamekuwa yakisaidia katika kuwakomboa vijana kwa kuwapatia mitaji.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pia nashukuru kwa majibu hayo yaliyotolewa na Serikali na kwa kuwa bado stesheni zetu nyingi hasa ikiwemo hii ya Makao Makuu bado hazina sura ya kuvutia na kwa kuwa huduma za vyoo na maji ni muhimu sana kwa afya, majibu ya Serikali yameeleza kwamba itategemea upatikanaji na vyanzo vya ndani, ambavyo vinaweza vipatikane au visipatikane au vitengwe au visitengwe. Je, ni kwa nini Serikali isitenge ikahaulisha kwenye mafungu mengine kufanyia matengenezo huduma hizi muhimu kwa afya ya wananchi wengi hasa wenye uwezo mdogo ambao wanatumia reli hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa watoaji wa huduma wengi kwenye reli hii ni wajasiriamali wadogo akinababa lishe, akinamama lishe na vijana. Kwa nini Serikali isiwafanyie utaratibu wa kujenga sheds au miavuli iliyopangika kwa utaratibu unaolekeweka wakafanya shughuli zao kuliko kutawanya masufuria, majungu, majiko, kuni along the railway lane? Na kwa nini Serikali…
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO – (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba hali ya Shirika la Reli Tanzania halijaimarika sana; lakini tukumbuke tu kwamba Shirika la Reli nalo linafanya biashara na linao wajibu na jukumu la kuhudumia wateja wake. Pale watakapoona kwamba wameshindwa tutataarifiana ndani ya Wizara halafu tutajua namna ya kuwasaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la pili, ni kweli kwamba wajasiriamali wapo wengi kwenye station zetu mbalimbali hapa nchini na wamekuwa wakifanya shughuli pamoja na Shirika letu la Reli. Ni jukumu sasa la Shirika la Reli wakae na hao wajasiriamali waweze kuwatengenezea mazingira wezeshi ya kufanya shughuli zao.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali na napongeza juhudi kubwa za Serikali kwa kujenga Kituo kipya huko Chukwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Chukwani ni nyuma kidogo, Mazizini ni barabarani na ni centre na karibu na Shehia nyingi kama vile Shakani, Kombeni, Maungani na kadhalika. Sasa kile Kituo cha Wilaya kwa nini hiki cha Mazizini mnataka kukiua?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, kwa nini msifanye taratibu kama hivyo mnavyoshirikiana na wadau kufanya kampeni ya kuboresha vyoo na vyumba vya mahabusu kwa nchi zima mkianzia na hapo Mazizini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, hatutarajii kukiua Kituo cha Mazizini, kitu ambacho tunafanya ni kuhamisha kuwa Kituo cha Wilaya, kuhamishia Chukwani. Kwa hiyo Kituo cha Mazizini kitaendelea kutumika tu, tutafanya jitahada ya kukikarabati na kwa kuwa kiko barabarani kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema, tunaamini kwamba kinahitajika kuendelea kutoa kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, kuhusu ukarabati wa vituo vyetu kwa ujumla wake ikiwemo mahabusu, ni jambo ambalo tunakwenda nalo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wake kuhusu kuwatumia wadau ndiyo tumekuwa tukiufanya kazi, wako wadau ambao wamekuwa wakishirikiana nasi kwa dhamira ya kurekebisha mazingira ya Vituo vyetu vya Polisi ikiwemo mahabusu.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi. Naomba kuuliza swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itaandaa jedwali la kuonyesha miradi mikubwa ya barabara zinazounganisha miji mikuu ya mikoa ili kuonyesha hali ilivyo na hivyo kuweza kuwaanika wakandarasi wanaochelewesha kazi hiyo kwa makusudi na kuwapa wananchi dhiki mfano barabara ya Nyakanazi – Kabingo - Kidahwe - Kasulu ambazo kwa muda mrefu hazikamiliki?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko miradi mingi sana ya ujenzi wa barabara inatekelezwa kote nchini. Nawaona Waheshimiwa wa Kigoma wanatabasamu kwa sababu wanafahamu fika kwamba miradi hii ambayo ilikuwa inatekelezwa katika Mkoa wa Kigoma ukianzia Nyakanazi – Kibondo - Kidahwe – Kasulu inaendelea vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie wananchi wa Kigoma kwa ujumla kwamba ipo miradi mingi sana ambayo kwa hapa siwezi kuitaja inaendelea vizuri. Mheshimiwa Nsanzugwanko na Mheshimiwa Zitto wanafahamu kwamba sasa appetite ya matengenezo ya barabara kwenye Mkoa wa Kigoma ipo juu sana na barabara karibu zote zina fedha kwa ajili ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Asha asiwe na wasiwasi. Hata eneo hili lililokuwa linasuasua kutoka Nyakanazi - Kakonko tumeendelea kulisimamia. Mimi mwenyewe nimekwenda mara kadhaa na tumezungumza na mkandarasi na zile changamoto zilizokuwa zinamkabili kama Serikali tumezitatua. Tunaendelea kusukuma na nitahakikisha barabara hii inakamilika ili wananchi wa Kigoma nao wapate faraja ya kuwa na miundombinu kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya mkoa wao.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa majibu niliyopatiwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko la watoto wetu wanaoendelea kupata mimba bado limeshika kasi. Ni juzi tu tumepata habari kwamba kuna mwalimu amewafanya wake zake watoto wa primary karibu 10. Wako wanaopata mimba kwa kubakwa, wako wanaopata mimba kwa kushawishiwa na wako wanaopata mimba kwa bahati mbaya yoyote ambayo inatokezea lakini huwa siyo dhamira, dhamira hasa ni watu hawa wapate haki ya kielimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni zito sana…

MWENYEKITI: Swali sasa.

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Sheria Na. 5 imetoa adhabu ya miaka 30 kwa yule mharibifu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Abdullah, nipe maswali.

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, nataka niiulize Serikali ni lini hasa itakaa chini itizame upya kadhia hii inayowakuta watoto wa wanyonge, wafanyakazi na wakulima, wasichana ambao wanakosa haki yao kielimu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, lini Serikali itatafuta mbinu mbadala ya kuwasaidia watoto hawa ambao wanakosa haki yao ya kimsingi? Hili jambo linauma sana, lazima Serikali itazame upya.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu langu kwenye swali la msingi, Serikali inachukua hatua kadhaa kuhakikisha inadhibiti tatizo hili. Kubwa ambalo limezungumziwa ni mabadiliko ya sheria ambapo imekuwa ni kosa la jinai kwa mtu yeyote kumpa mimba mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari. Tunachoomba na Waheshimiwa Wabunge ni mabalozi wazuri katika hili, Serikali ina dhamira ya kuhakikisha kwamba wale wote wanaokutwa na makosa haya wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sharia na kama tulivyosema tumeweka kifungo cha miaka 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi kinachotokea ni kwamba ushirikiano kutoka kwa wazazi wa wanafunzi ambao wameathirika unakuwa siyo mkubwa. Pindi tutakapopata ushirikiano na ushahidi ukiwepo, Serikali itaendelea kuchukua hatua kuhakikisha kwamba wale wahusika wote wanachukuliwa hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili tunachukua hatua zipi kuhakikisha kwamba wale wanafunzi wanaoathirika wanaendelea na safari ya masomo? Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba mwanafunzi kupata mimba haimaanishi kwamba ndiyo mwisho wa safari yake ya masomo. Serikali imeweka taratibu kadha wa kadha ili kuhakikisha wanafunzi wale bado wanapata fursa nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fursa hiyo ipo katika maeneo matatu makubwa; moja Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ina utaratibu wa kutoa elimu nje ya mfumo rasmi. Napenda kutoa taarifa kwamba kwa mwaka jana kuna wanafunzi 10,000 ambao wamehitimu kidato cha nne kupitia utaratibu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na 6,000 ni wasichana. Tunaamini kwamba baadhi yao ni wanafunzi wale ambao walikatisha masomo kwa sababu ya mimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na UNICEF tunaendesha Mradi wa Elimu Changamani kwa wanafunzi ambao wameshindwa kuendelea na shule kwa sababu ya kupata ujauzito. Pia, Serikali imeendelea kuimarisha elimu ya ufundi, kwa hiyo, wanafunzi ambao hawajaweza kwenda sekondari au ambao wameshindwa kuendelea kwa sababu ya kupata ujauzito kuna fursa vilevile ya kupata elimu ya ufundi na tumeendelea kuimarisha na elimu hiyo sasa hivi ni bora.

Kwa hiyo, tunachosema kimsingi, hata kama mwanafunzi amepata ujauzito sio mwisho wa safari yake ya masomo kuna fursa nyingine na kuna wengi ambao wamenufaika. Nina hakika hata baadhi ya Wabunge kwenye Bunge hili wamenufaika na mipango hii ya Serikali.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa hali ya maumbile ya mwanadamu, hasa mwanamke yanapelekea kujifungua au kupata watoto: Je, Serikali inachukua hatua gani kudhibiti utungwaji mimba ndani ya Magereza ili kupunguza shida ambazo watoto hao watapata katika kulelewa katika mazingira ambayo siyo rafiki kama Magereza; kwa kuwa bado inasemekana kwamba kuna mchanganyiko wa wanawake na wanaume na wanapata access ya kukutana? Sasa Mheshimiwa Waziri atuambie atadhibiti vipi utungwaji mimba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilieleza wakati najibu swali la msingi kuhusiana na uwezekano wa mwanamke kupata mimba ndani ya Magereza. Nimezungumza hivyo kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba Magereza yametenganishwa, hakuna mchanganyiko kati ya Magereza upande wa wanawake na wanaume; hata Askari ambao wanahudumia wafungwa na mahabusu wa kike basi wanakuwa ni Askari wa kike. Kwa hiyo, mara nyingi tunapozungumzia upataji mimba wa Magereza inakuwa ni kwa wafungwa ama mahabusu ambao wameingia tayari Magerezani ikiwa mimba zimeshaanza kutungwa.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi napongeza sana Serikali kwa hatua zake za kusambaza na kusimamia mawasiliano pamoja na kujenga minara sehemu zote. Pamoja na hayo nataka niulize Serikali ina mikakati gani na ya haraka kwa kiasi gani katika kudhibiti au kuimarisha kikosi kazi cha kupambana na hawa wahuni kila siku wanaosumbua wananchi katika kuwaibia pesa zao kupitia mtandaoni kwa kuwaambia tuma hela hii kwa namba hi, tuma hela hii kwa namba hii, Serikali inafanya nini kuwadhibiti wahuni hawa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, ipo mikakati mingi ya kupambana na hali hii ambayo inajitokeza kwa sababu ya ukuwaji wa teknolojia pia changamoto nazo zinakuwa zipo nyingi, tunao mkakati kwanza wa kuelimisha wananchi ili kuwaokoa na hii hali ambayo inajitokeza lakini pia mara kwa mara mnaona tunaendelea kuboresha Sheria na Kanuni hata hili zoezi la uandikishaji wananchi kwa kupitia alama za vidole kufanya usajili wa simu ni hatua hizo madhubuti za kuhakikisha tutaendelea kumbambana nah ii changamoto ambayo ipo. Kwa hiyo, ni kuahakikishie tu kwamba kila wakati changamoto inapojitokeza kama sisi Serikali tunachukuwa hatua hii kuwafanya wananchi wetu kuwa salama.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Nashukuru sana kwa majibu mazuri, ya kina na yenye maelezo ya kutosha na kwa kiasi kikubwa suala langu limepata ufafanuzi kwa swali la aliyeuliza kabla yangu lakini nitakuwa na maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti baadhi ya utawala wa shule ambao huwa unawazuia watoto wenye uwezo mdogo au uwezo wastani kufanya mitihani yao ya mwisho na kuwalazimisha waende wakajiandikishe kama private candidates kwenye vituo vingine wakati wakijua kufanya hivyo ni kuwapunguzia moral na kuwavuruga kiasi kwamba wanawazidishia kutofanya vizuri lakini pia ni kuwabagua watoto hawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kwa kiasi gani Serikali imejipanga kushirikiana na wazazi na walezi kuona kwamba Kamati za Ahule zinasaidia kupunguza kadhia hii kwa watoto hao wenye uwezo pungufu katika masomo yao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asha Abdulla Juma kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaeleze Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watazania kwa ujumla kwamba ni kosa kumbagua mtoto yeyote kwa sababu yoyote. Wote ni watoto wa Kitanzania na tena Serikali inatoa msisitizo zaidi kwa wale ambao wana changamoto mbalimbali za ujifunzaji. Kwa hiyo, ikibainika kwamba kuna mwalimu au kiongozi yeyote wa elimu ambaye anawabagua watoto wenye changamoto ya uzito katika kujifunza kwa kweli ni kosa na atachukuliwa hatua za kisheria. Naomba nimtake Mhshimiwa Mbunge kama ana ushahidi kuhusu hili alete kwetu na sisi hatutasita kuchukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuhusu nafasi ya Kamati na Bodi za shule katika kutatua changamoto hii, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni kwamba lengo zima la kuanzisha Kamati za shule katika Shule za Msingi na Bodi katika Shule za Sekondari ni pamoja na kuangalia changamoto kama hizi ili kuhakikisha kwamba sheria, taratibu na miongozo ya Serikali inatiliwa mkazo katika usimamizi wa elimu. Kwa hiyo, tuendelee kuwaunga mkono kwa sababu ndiyo kazi yao hasa.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Nashukuru kwa majibu hayo yaliyotolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako wananchi wengi waliofanya mambo ya muhimu na ya kuandika historia. Mfano Meja Jenerali Mrisho Sarakikya aliyepandisha bendera ya siku ya Tanganyika ilivyopata uhuru. Hivi Serikali haioni umuhimu wa kuandaa sera ya kushughulikia viongozi kama hawa ikasaidia kuamsha ari ya uzalendo kwa nchi yetu ya Tanzania kuliko kusema kwamba tutawaonea huruma, tutawatazama wako hawa na hawa? Serikali inasemaje kuhusiana na suala hili?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Naibu Waziri, naomba nijibu swali la nyongeza lililoulizwa nikijumuisha pamoja na majibu yaliyotolewa kwa swali lililopita kwamba nchi hii inayo watu wengi sana waliofanya mambo makubwa katika historia ya nchi yetu na Serikali imekuwa ikitambua michango yao kwa namna mbalimbali. Hawa wanne tunaowazungumzia waliochanganya udongo wa Tanzania Zanzibar na Tanganyika na kufanya alama ya Muungano ni moja tu ya wazee wengi ambao wengine hata kuwatambua bado hatujawatambua. Wako wazee waliopigana vita ya Kagera, wako watu waliofanya shughuli mbalimbvali zilizofanya Tanzania hii ya leo tunayoiona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo hili ni lazima tujipe tahadhari kuhusu ukubwa wake lakini pia hatuwezi tukaliacha hivi hivi ni lazima tutafakari kwamba je, tunapotaka kuchukua tuchukue kada ya namna gani au watu wa namna gani. Naomba tu niseme kwa niaba ya Serikali kwamba kwanza tunatambua na kuheshimu na kuenzi michango ya wazee waliofanya mambo makubwa hapa nchini lakini tunahitaji muda wa kutafakari sana mwisho wake yaani limitation na scope yake iwe wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. ASHA ABDULLA JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri yaliyosheheni vigezo.

Mheshimiwa Spika, askari wa Jeshi letu la Polisi wanafanyakazi nzuri sana ikiwepo usalama barabarani, usalama wa raia na mali zao na kutuelimisha kutii sheria bila shuruti.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wako baadhi ya askari ambao hawakupandishwa cheo mpaka wamefikia kustaafu, na kwa kuwa kutokupandishwa huko si kosa lao, ni kosa la mfumo; je, Serikali ina mpango gani wa kuwafidia ili wasiwe wamepoteza haki zao na hasa kwa vile sasa hivi wako wastaafu wanahitaji sana fedha hizo?

Mheshimiwa Spika, swali langu lingine; Je, Serikali haioni umuhimu wa kuandaa mfumo na utaratibu uliowazi kabisa unaoonyesha namna gani na vigezo gani vya kuweka nafasi ya kwenda course ili uweze kupandishwa cheo na utaratibu huo uwe wazi na haki kabisa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Asha Abdalla Juma, Mbunge wa Viti Maalum kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mfumo ambao tunao sasa hivi wa upandishwaji askari vyeo uko vizuri; na nimeeleza katika jibu la msingi vigezo ambavyo vinatumika. Hata hivyo kulingana na wingi wa askari tuliokuwanao na uchache na ufinyu wa nafasi hizo inasabbaisha wakati mwingine askari wengine kutumia muda mrefu zaidi katika kupata vyeo.

Hata hivyo tumekuwa tukifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha kwamba wale askari ambao wanatimiza vigezo wanapata fursa ya kupandishwa vyeo; kwa hiyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Asha Abdalla Juma kuhusiana na hilo.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na hoja yake, kama nitakuwa nimemuelewa vizuri, ya kuwafidia, nadhani hilo halipo katika utaratibu. Kimsingi tu ni kwamba tutaendelea kuhakikisha tu kwamba askari ambao wenye sifa wanapandishwa vyeo. Katika kipindi cha mwaka huu mmoja, hivi karibuni tulipandisha vyeo askari kwa upande wa Jeshi la Polisi pekee kwa haraka haraka nadhani ni zaidi ya askari 9000 ukiachilia mbali majeshi mengine yaliyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Utaona kwamba tunafanya jitihada kama Serikali kuona askari hawa ambao wanafanyakazi vizuri wanapata fursa ya kupandishwa vyeo kadri ya hali na uwezo wa Serikali unavyoruhusu.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nina maswali mawili: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kupongeza Serikali kwa jitihada kubwa za maboresho kwenye magereza na pia tumeona juhudi za Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli pale alipo tembelea Gereza na Butimba na maelekezo aliyotoa na hatua zinazochukuliwa na Serikali nzima katika kupunguza kadhia ya magereza. Kama tunavyofahamu kwamba gerezani siyo kuzuri. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka takwimu, data ya wakosaji makosa na adhabu wanazozipata wakiwa magerezani na kuziweka wazi takwimu hizi ili kuona kwamba udhibiti upo na kwamba haya makosa yanaendelea yamedhibitiwa au yanapungua?

Swali la pili, Je, Serikali haioni kwamba sasa ni wakati muafaka wa kufikiria kuweka wigo wa kutoa adhabu za kutumikia ndani ya jamii kwa wale ambao wanamakosa ambayo si ya kuleta dhara kwenye jamii zaidi, kuliko kuwarundika kwenye magereza kwa kuwa kufanya hivyo itaweza kupunguza mzigo mkubwa wa mkusanyiko magerezani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yake ya kwanza ilikuwa ni ushauri ambao tunaupokea kuhusiana na takwimu kuziweka wazi. Lakini swali la pili ambalo aliuliza kimsingi jambo hilo tunalo tuna utaratibu ambao unaitwa kwa lugha ya kiingereza extramurally labor ambao utaratibu huu kwa kawaida unatumika kutoa adhabu kwa maana ya adhabu za vifungo vya nje kwa baadhi ya watuhumiwa kulingana na masharti na vigezo vilivyowekwa. Kwa hiyo, utaratibu huo tunao na tunaendelea nao. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kupata nafasi hii, nashukuru sana Mheshimiwa Waziri wa majibu yako mazuri lakini nitakuwa na suala moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa muingiliano umekuwa mkubwa na watu wamekuwa wengi, kwanini hiki kituo kisitafutiwe sehemu nyingine, kikajengwa huko, kikawa na nafasi kubwa kikaelekea kama kituo kweli cha polisi kuliko pale kilivyokaa, hakijapendeza wala haifai. Huku kituo, huku soko, nafikiri Serikali ifikirie kukihamisha kikapate nafasi kubwa zaidi na majengo ya kisasa yaliyokuwa bora zaidi. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja ya kuhamisha kituo hiki kwa sababu ya ufinyu wa nafasi kiusahihi ni kwamba eneo la kituo lile ni kubwa mno, labda Mheshimiwa Mbunge tukipata nafasi tukatembelee ili nimuoneshe. Ni juzi tu hapa kuna eneo ambalo liliwahi hata kupewa mwekezaji na kutokana na maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kwamba maeneo ya vyombo vya usalama yabakie kwa matumizi ya vyombo hivi tulitoa maelekezo na kuhakikisha kwamba tumemhamisha yule mwekezaji.

Mheshimiwa Spika, lakini utakumbuka pia hata eneo ambalo liko pembeni ya kituo cha polisi ambacho kimetumika kama soko kama alivyozungumza kwenye swali la msingi ni eneo pia la polisi ukiachia mbali eneo la nyuma ambalo ni kubwa. Kwa hiyo, kimsingi kuhamisha kituo hiki kwa sababu ya ufinyu wa eneo nadhani haitakuwa sahihi kwa sababu kuna eneo la kutosha. Cha msingi ni kuendelea kutoa wito kwa wananchi kutumia nafasi yao yoyote ya kuvamia maeneo ya polisi kuacha maeneo ya polisi yaendelee kutumika kwa ajili ya shughuli za kiusalama.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, jambo hili ni zito linalowakuta wasichana wetu hawa, linavuruga maisha yao utaratibu wao na kuleta simanzi na huzuni katika familia japokuwa kaja kiumbe lakini kaja vipi na atahudumiwa namna gani. Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka wa kuwarudisha wasichana hawa wakaendelea na masomo yao baada ya kujifungua kuliko kuwapeleka kwenye vituo nje ya mfumo rasmi. Kwa kuwa mimba siyo maradhi ya kuambukiza wao walikuwa wakazane kuleta mitaala juu ya ngono, uzazi. (Makofi)

Swali la pili Je, Serikali haioni kwamba kuzuia watoto wa kike waliopata mimba kuendelea na masomo yao na kuwaachia watoto wa kiume waliohusika kuendelea kama vile hawajafanya chochote siyo ubaguzi wa kijinsia?(Makofi)

Mheshimiwa Spika, waliofanya makosa watu wawili, bakora anapigwa mtu mmoja kweli hiyo ni haki? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asha.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri amelizungumza ni kweli tumeweka huo utaratibu na kama unakumbuka kupitia mradi wetu wa SEQUIP ambao karibu tunaanza kuutekeleza tumeweka pia kipengele cha kuangalia Watoto wanaopata ujazito wakiwa shuleni na tutaenda kuimarisha vituo vyao ambavyo tumevieleza katika jibu la msingi.

Mheshimiwa Spika, jambo hili limekuwa linazungumzwa kwa muda mrefu na kwa sababu sasa ndiyo tunaanza kutekeleza mpango mahsusi ambao tumeuweka ningeomba tutekeleze angalau kwa kipindi cha mwaka huku Serikali ikiendelea kutafakari maoni ambayo yamekuwa yanatolewa na wadau ili tuone namna bora zaidi ya kutekeleza hayo maoni ambayo yamekuwa yakitolewa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili kwamba kwanini anayehusika asichukuliwe hatua. Utakumbuka kwamba mwaka 2016 Bunge lako Tukufu lilitunga sheria ambayo inatoa adhabu kali kwa mtu yeyote ambaye anajihusisha na masuala ya mapenzi shuleni kwa wanafunzi au mtu ambaye anakatiza ndoto ya watoto wa kike ya kupata elimu. Yeyote ambaye anabainika kwa mujibu wa sheria hiyo iliyotungwa mwaka 2016 anapata adhabu ya kifungo cha miaka 30. Nashukuru kwa nafasi.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante na nashukuru kwa majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa nafasi za kufanya mazoezi kwa vitendo kwa wanafunzi bado imekuwa shida sana, inakuwa kama hisani, upendeleo au kujuana kwa mara kadhaa.

Je, ni lini Serikali itaweka muongozo na kanuni ya kuelekeza taasisi za umma na za binafsi na waajiri kuweka utaratibu mzuri wa kuwapokea wanafunzi hawa bila kuhangaika sana? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa vile majibu ya Serikali yameashiria kama hakuna tatizo kubwa kwenye zoezi hili; je, ni kwa nini Serikali isifanye utafiti wa kina wa kubaini changamoto na matatizo yanayowakumba wanafunzi hawa na kuweka utaratibu rahisi wa kupata nafasi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba sasa kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asha Abdullah Juma yenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu kwenye programu hizi za mafunzo kwa vitendo na katika programu hizo tunajua kwamba tunapambana au tunakabiliana na changamoto mbalimbali.

Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa changamoto hizi tutaendelea kuzifanyia kazi na kuzitatua, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa vile ametoa ushauri, kwa nini tusifanye utafiti, basi naomba sasa tulichukue wazo hili twende tukafanye utafiti ili kwa pamoja kuweza kukabiliana na changamoto hizi. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili. Kwanza nashukuru kwa majibu.

Je, ni lini zoezi hili litakamilika ukizingatia umuhimu wa kukusanya kodi na kwa vile ni muda tangu Mheshimiwa Rais alipotoa agizo hili?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali na TRA ina mkakati gani rafiki wa kufanya makadirio ya kodi kwa wafanyabiashara yanayoendana na mapato halisi ili kuzuia wafanyabiashara wasishindwe kulipa kodi hizi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali kwanza, inategemea ushirikiano ya mteja wakati wa kufanya majadiliano. Kama mteja atakuwa na ushirikiano mzuri basi suala hili linamalizika kwa kipindi kifupi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili; mikakati ambayo tumechukua sisi Serikali ni kutoa fursa kwa wateja, yaani wafanyabiashara, kufanya self assessment, yaani kujifanyia tathmini wenyewe halafu na sisi tunajiridhisha. Mkakati wa pili ni kutoa elimu kwa wafanyabiashara wote ili wafate taratibu za kulipa kodi.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Msheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kumekuwa na malalamiko na changamoto kadhaa kwa upatikanaji wa mbolea na bei kuwa juu. Je, Serikali ina mpango gani wa kushajihisha kilimo hai ambacho kinatumia mbolea asilia na kina gharama nafuu ambazo pia hakitumiii kemikali na vilevile ina uwezo wa kuhuisha afya ya udongo na afya zetu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asha Juma, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara tumekuwa tukifanya jitihada mbalimbali za kuwakaribisha wadau mbalimbali wanaozalisha mbolea ambao ni organic na habari njema tu ni kwamba nilipata nafasi ya kwenda katika maonesho ya kilimo hai Ujerumani na tukakutana na wawekezaji wengi ambao wameonesha nia ya kuja uwekeza hasa katika Mkoa wa Lindi na Mtwara. Hivyo, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba mbolea hii pia inazalishwa ili kupunguza gharama hii kwa wakulima.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu ya Serikali.

Kwa kuwa mchakato wa bima ya afya kwa wote umo mbioni kukamilishwa, na kwa kuwa miaka ya nyuma kulikuwa na utaratibu mzuri wa kwenda kuchunguza afya za watoto mashuleni kwa vipindi kadhaa kwa mwaka. Je, Serikali haioni umuhimu wa kurudisha mpango huu wa kuchunguza afya za vijana wetu shuleni walau mara mbili kwa mwaka, katika jitihada za kupunguza gharama kwa kugundua maradhi mapema ili kukinga na kuwapunguzia wanafunzi hawa shida au wazazi wao kupeleka hospitali wanapokutwa maradhi yameshawatokea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ni muhimu sana kuwa na utaratibu wa ku-check afya za wanafunzi shuleni angalau mara mbili kwa mwaka, utaratibu huo uko kwenye miongozo yetu, ni kweli kwamba hapa katikati ufanisi wake umepungua kidogo. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwanza tumepokea ushauri wake tutakwenda kutekeleza, pia nitoe maelekezo kwa Wakuu wa Shule na Halmshauri zetu kuhakikisha wanaweka utaratibu kwa kutumia Waratibu wa Elimu, pia na Waratibu wa Huduma za Afya katika shule ili watoto wetu wachekiwe mara kwa mara afya zao na kupewa matibabu mapema. Ahsante. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafsi. Kwa kuwa mabadiliko ya tabianchi yana madhara makubwa na huweza kusababisha majanga.

Je Serikali inaimarishaje kuwapa taaluma kisasa zaidi ya uokozi na uhifadhi watu wengi zaidi badala ya kutegemea JWTZ na Zima Moto pekee?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO
NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Zanzibar, najibu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, athari za mabadiliko ya tabianchi siku zote zinasababishwa na zinachangiwa kiasi kikubwa na shughuli za kibinandamu ambazo binadamu wanafanya katika maisha yao ya kila siku. Zikiwemo shughuli za ukataji wa miti, shughuli za uharibifu wa vyanzo vya maji, shughuli za uchomaji wa misitu, shughuli za ufanyaji wa shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya hifadhi na shughuli nyingine. Kwa hiyo hatua moja ambayo tumeichukua kwanza ni kuwaelemisha wananchi, kuwaeleza athari ambazo zinapatikana baada ya wao kufanya hizo shughuli za kiubinadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili amabalo tunalifanya ni kusimamia sheria. Kwa sababu mbali na kuwaelimisha lakini kwa vile sheria zipo ni kuzisimamia sheria. Tatu ni kuchukua hatua za kisheria kwa wale wote wanaochafua ili lengo na madhumnuni tusiwape mzigo wengine wakina Zima Moto na watu wanaoshirikiana maafa na watu wengine.

Mhehsimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa uharibifu huu unaofanyika kwenye milima, uko vilevile kwenye fukwe za bahari na zile sehemu ambazo bahari inaungana na mito. Mikoko inazidi kukatwa, kila kukicha na hivyo kuharibu mazingira na sehemu za kuzalia viumbe vya majini.

Je, Serikali sasa itakuja na program gani ya kuongeza hamasa katika kupanda mikoko katika sehemu hizo ili kunusuru mazingira hayo.(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS - MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha maarufu kwa jina la ‘Mshua’ kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango mkakati ambao wananchi wote ambao wanasaidia kupanda mikoko kando kando ya bahari, wanakuwa na taaluma maalum lakini wanapewa motisha. Kwa mfano, Bagamoyo, Zanzibar, ziko sehemu ambazo tayari wameshapanda mikoko na wale ambao wamepanda mikoko well na ikawa inahuika, basi Serikali tunawapa motisha na kufuatilia siku hadi siku. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Pamoja na vibali na eneo lililotengwa, lakini bado kadhia ya magari makubwa hupaki, kupakua na kupakia mizigo katika Barabara kama za Nyati, Faru, Tembo na kadhalika inaendelea.

Je, Serikali inaelewa kwamba wafanyabiashara hawa wa mizigo wanawakosesha haki ya kimsingi wanye makazi ya kulala, pia kuharibu utaratibu mzima wa afya ya akili?

Je, ukitokea moto, wakati barabara zote zimezibwa na magari makubwa haya ya mizigo, Serikali haioni kama hilo janga in the make, ina mpango gani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, cha kwanza tunatambua haki za msingi za wananchi wa maeneo hayo wanayokaa na kero wanayoipata. Kwa hiyo, kutokana na umuhimu wake, sisi kama ofisi ya Rais TAMISEMI, tunaomba tulipokee na tuangalie namna bora ambayo tunaweza tukaifanya kuchukua hatua za haraka.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la msingi, kuhusu majanga ya moto, tumesema moja ya mkakati wetu na mkakati wa Jiji la Dar es Salaam ni kujenga eneo jipya katika eneo la Mnazi Mmoja kwaajili ya maegesho ya magari. Kwa hiyo, kwa kuuliza hili swali la msingi maana yake sasa tutaiharakisha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ianze huo mkakati hara iwezekavyo ili muondokane na hiyo kero. Ahsante.

Mheshimiwa Naibu Waziri tunakushukuru sana kwa majibu yako kwa maswali ya Waheshimiwa Wabunge. Wizara ya Maji, Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya sasa ulize swali lake.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.

Kwa kuwa, Serikali yetu na nchi yetu inajikita zaidi katika matumizi ya teknolojia na TEHAMA. Je, Serikali ni lini itaona ni wakati muafaka wa kuongeza masomo haya ya sayansi ikiwemo hisabati kwa wanafunzi wanaofanya masomo ya HGKL. Ni ni lini ili kuwafanya watu hawa wawe tayari katika soko la ulimwengu na Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Asha Mshua kama ifuatavyo: -

Mhehsimiwa Mwenyekiti, masomo ya hisabati pamoja na teknolojia tayari yapo kwenye mitaala yetu lakini naomba tu nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, hivi sasa tunafanya mapitio ya mitaala katika ngazi zote za elimu ambapo tutazingatia hasahasa kwenye maeneo haya ya sayansi pamoja na teknolojia na tunaamini kabisa kwa mwendo huo tunaokwenda nao swali lake litakuwa limepata majibu ya jumla na ya moja kwa moja.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Nashukuru sana kwa majibu ya Serikali; pamoja na kitu kizito alichopigwa nacho Mheshimiwa Naibu Waziri jana Mkapa, lakini anaweza kutoa majibu ya kina. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali imefanya uhakiki kwamba viuatilifu hivi 44 vilivyobainishwa vimeweza kutokomezwa na kwamba notice ya katazo au ya ku- deregister au zuio inabainika kwa uwazi na kwa ufasaha kabisa kwa wanunuzi, watumiaji na wanaohusika wote? (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, swali lingine: Je kuna mpango gani wa Serikali kupima mboga mboga zinazoingia sokoni na kuwajulisha watumijai na walaji kama vile tunavyofanya kwa mazao yanayouzwa nchi za nje? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza kwa mujibu wa Sheria Na. 4 ya Afya ya Mimea ya Mwaka 2020, ni wajibu wa kimsingi wa mamlaka kuhakikisha kwamba inafanya kaguzi za mara kwa mara ili kuweza kubaini viuatilifu ambavyo vimesitishwa na kuweza kuchukua hatua sambamba na kutoa taarifa kwa watumiaji ili isiweze kuleta madhara zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili la kuhusu upimaji wa mazao ya mboga mboga, Serikali inapima uwepo wa masalia ya viuatilifu vilivyotokomezwa katika mazao yote. Hivi sasa tumenunua Rapid Test Kit ambayo pia itasaidia kupima masalia ya viuatilifu katika mazao ya mboga mboga ili kuweza kumlinda mtumiaji. Kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo pia tunahamasisha na kilimo hai, kuondokana na changamoto hizi ambazo zinajitokeza na matumizi ya viuatilifu.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Tauhida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa mpango huu wa Serikali umekuwepo kwa siku kidogo lakini bado ulipaji wa madeni umesuasua. Je, ni mikakati gani ya dharura ambayo Serikali itachukua kuhakikisha kwamba ulipaji unafanyika kwa uharaka na kwa ufanisi zaidi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa bilioni 244 ni pesa nyingi sana inazodai Serikali, je, Serikali ina mikakati gani ya kisheria ambayo itachukua kuhakikisha kwamba hizi pesa zinalipwa kwa kuwapeleka hawa watu Mahakamani au kwa njia nyingine yeyote, lakini pesa hizi zilipwe ambazo ni muhimu sana kwa maendeleo ya shirika na nchi yetu kwa jumla?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asha Abdullah Juma kwa pamoja, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme hizi pesa bilioni
244 kwa sehemu kubwa ni deni la nyuma na ni deni la siku nyingi. Ni deni ambalo lilikuwepo kipindi kile ambacho bado tulikuwa hatujaanza kutumia LUKU na tulikuwa hatujaweza kukusanya vizuri. Kwa hiyo ni madeni ya siku nyingi na tunaendelea kuhangaika nayo kama ambavyo Mheshimiwa amesema tuna mkakati gani wa kuhakikisha kwamba tunayakusanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mikakati iliyopo ya kukusanya pesa hizi kwanza ya dharura kabisa tayari TANESCO imeshakamilisha taratibu za kuwapata madalali wa kukusanya madeni wawili ambao taratibu zinakamilishwa na siku siyo nyingi wataanza kuingia mtaani na kukusanya fedha hizi ambazo ziko kwa watu mbalimbali ili kuweza kuzipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili upande wa Serikali, Wizara na TANESCO tumeshirikiana na kuiomba Serikali kupitia Hazina ilipe pesa hii yote inayodaiwa kwa TANESCO ili TANESCO iweze kupata fedha ya kuweza kujiendesha. Sasa kwenye mikakati inayokuja ya nini kinafanyika pamoja na hizi LUKU ambazo tumeshaweka, lakini zinawekwa LUKU zinaitwa boundaries meters ambazo zitawekwa kwenye ngazi ya Mkoa ili kila Mkoa tujue inatumia umeme kiasi gani. Pia tunakwenda kwenye kuweka smart meters ambazo zitatusaidia kujua mtu anapogusa meter yetu moja kwa moja tukiwa ofisini tutaiona na kuhakikisha kwamba tunashughulikia suala hilo mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mahakama, tusingependa tufike huko mapema kwa sababu Mahakama inachukua muda mrefu na process nyingi, lakini wale wateja ambao tunashindwana kabisa hata zile hatua za kukata umeme, basi tunapelekana Mahakamani. Zipo kesi kadhaa ambazo tumeenda Mahakamani na tumeshinda na tuna uhakika kwamba deni hili tutalikusanya lote ndani ya muda mfupi.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa nyumba kadhaa zilizo chini ya mamlaka ya TBA hasa hapa Dodoma ni chakavu, miundombinu ya maji taka imechoka, maji ya karo na vyoo yanafurika hovyo na hivyo kuwa tishio kwa afya.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuisimamia mamlaka hii ya TBA ili kuhakikisha nyumba hizi ziko katika hali ya usalama na si tishio kwa wakazi, na hasa kwa vile wanalipwa kodi na hawakai bure?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Asha kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli badhi ya nyumba za TBA hapa Dodoma ni chakavu, na nikushukuru Mheshimiwa Spika, kwamba baadhi ya watumishi wa Serikali wanadaiwa. Na kwa kuwa wanadaiwa wanakila sababu ya kulipa ili tukarabati nyumba hizi ambazo ni chakavu, ukizingatia kwamba TBA fedha zake zinakata kutoka ruzuku za Serikali lakini pia na kodi za mpangaji, inapokusanywa ndipo inapokarabati nyumba hizi za TBA, ahsante.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Serikali ina mpango gani wa kuwanyanyua vijana hawa wa skauti walioiva kimaadili na kizalendo, kuwatengea mgao maalum wa kupata ajira zinapotokea kama vile kwa Jeshi la Wananchi na taasisi nyingine?

Mheshimwia Mwenyekiti, swali la pili: Serikali ina mpango gani wa kutenga ruzuku malalum kwa ajili ya shughuli za Skauti Tanzania?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kwa vijana walioiva kiuzalendo ambao wanatoka skauti, na mara nyingi tumekuwa tukiwaangalia sana kwenye suala la ajira, na ajira hizi pindi zinapotokea ziwe za Serikali na pia kwenye taasisi na vyombo vyetu vya usalama, imekuwa ni moja ya sifa ama kigezo, kama wale walioenda Mgambo na JKT kuangaliwa kama sifa ya ziada. Kwa hiyo, tumekuwa tukiwaingiza kwenye vyombo vyetu vya ulinzi na usalama na pia katika majukumu mengine ambayo yanatokana, au ajira zinazotoka upande wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu ruzuku; Skauti Tanzania imeanzishwa kwa mujibu wa sheria, na bahati nzuri kabisa, Skauti Mkuu Tanzania ni Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa hiyo, katika utaratibu wa masuala ya kuwawezesha, kama jinsi sheria ya kuwaanzisha wao inavyoeleza, ndivyo hivyo hivyo wanaweza kupata pia fedha kupitia mifuko mbalimbali ambayo inasaidia kama sehemu ya chombo ambacho ni kama Jeshi, yaani inafanana na ile ambayo ipo katika Jeshi la Mgambo. Kwa hiyo, msaada, na pia iko fedha inayotoka Serikalini na kuna fedha ambazo ni kutoka kwa wadau mbalimbali huzitoa kupitia mifuko hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutazidi kuangalia kuweza kuboresha zaidi maslahi ya Skauti wetu kwa sababu wamekuwa wakifanya kazi kubwa na hasa kwenye masuala ya uokoaji pale yanapotokea majanga, sherehe za kitaifa na majukumu mengine, ahsante.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wazee wengi ambao walikuwa wafanyakazi wa Shirika la Posta na Simu na ATCL na Mashirika mengine kama Reli, mpaka sasa hivi wanahangaika kupata vipensheni vyao. Je, ni lini Serikali itamalizana na wazee hawa ili wakifa wakapumzike kwa amani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kifo ni mpango wa Mungu lakini hatuombei itokee hivyo kwa wazee wetu, waishi na waendelee kudumu.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali hilo la Mheshimiwa Asha kuhusiana na wazee hawa waliokuwa watumishi wa Shirika la Posta pamoja na Reli kupata pensheni zao; itakumbukwa vizuri kwamba tayari kulikuwa na mashauri mbalimbali ya wazee ambao walikuwa wanafanya kazi kwenye mashirika hayo. Wapo tayari ambao wamekwishalipwa pensheni zao lakini pia wapo ambao wameendelea kuwa na madai. Hii imetokana zaidi na kutokuwepo kwa taarifa sahihi za madai yale lakini Serikali imeendelea kufanya ufuatiliaji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimwombe pia Mheshimiwa Mbunge, mama yangu Asha, baada ya hapa pia nipate taarifa ya madai hayo, kama kuna watu specific au mahususi tuweze kwenda kufanya ufuatiliaji kwamba wamekwama wapi katika kulipwa kama walikuwa kweli wafanyakazi halali, ahsante.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Dkt. Charles Kimei. Je, lini Serikali itakarabati kituo cha Mwika Kaskanzini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika maeneo ambayo kuna zahanati, lakini maeneo ni madogo: Je, Serikali ipo tayari kupandisha zahanati za Rombo kuwa vituo vya afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza; la kwanza kuhusu lini Serikali itafanya ukarabati wa katika Kituo cha Afya cha Mwika, Serikali itafanya ukarabati katika kituo hiki cha afya kadiri ya upatikanaji wa fedha. Tutaangalia katika mwaka wa fedha 2023/2024 kama kimetengewa fedha ya ukarabati, basi tutahakikisha fedha inaenda mara moja. Kama hakijatengewa fedha kwenye mwaka huu wa fedha, tutahakikisha katika mwaka wa fedha 2024/2025 Kituo cha Afya cha Mwika kinatengewa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali la pili la kupandisha hadhi zahanati kuwa kituo cha afya katika eneo la Rombo, tunalipokea hili kama Serikali. Nichukue nafasi hii kumwelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kufika katika zahanati hizi ambazo zimetajwa na kuangalia kama zinakidhi vigezo vya kupandishwa kuwa vituo vya afya na kuwasilisha taarifa hii katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili tuweze kuona ni namna gani tunawasaidia wananchi wa maeneo haya kupata vituo vya afya.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Naipongeza sana Serikali kwa jitihada zake za kupanga mipango ya umwagiliaji. Kwa kuwa Serikali ndiyo yenye wataalam, wabobezi katika masuala haya ya umwagiliaji.

Je, ni lini Serikali itapanga mipango ya kuwasaidia wakulima kufanya levelling kufikisha maji kwenye mashamba yao badala ya kuwaachia kazi mkulima mmoja mmoja afanye jambo hilo ambapo hawana utaalamu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inge-copy mambo yanayofanyika Egypt. Egypt wanafanyakazi zote mpaka kuwapeleka watu mashambani, kwa sababu ninyi ndio mna kamera, ninyi ndio mna vifaa vya kupimia: Sasa Serikali mna mpango gani wa kushughulikia wakilima ili maji yaende kwa watu wote?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni mawazo mazuri kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ndiYo yenye dhamana ya kuhakikisha skimu za umwagiliaji na kuhakikisha maji yanaenda katika mashamba na maeneo mbalimbali ambako wananchi wanafanya shughuli za kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mipango ya Serikali tumesema moja ya maeneo ambayo yameongezwa sana fedha ni kwenye maeneo haya ya umwagiliaji. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mipango ya Serikali ni thabiti na itaendelea kutekelezwa kulingana na fedha ambazo tunazipanga na kuhakikisha tunaenda na vipaumbele katika maeneo ambayo kuna mahitaji haya ya skimu za umwagiliaji. Hivyo, tuwaondoe hofu Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwamba Serikali itatekeleza miradi yake na mipango yake kwa kadri ambavyo tunapanga kwenye mipango ya kila mwaka wa fedha wa bajeti, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA : Mheshimiwa Spika, ahsante sana na nashukuru kwa majibu mazuri ila nina maswali mawili.

Je, ni kwa nini Serikali haifanyi utafiti wa suala la bei wa safari za ndege za ndani ya nchi kutokana na bei hizo kuwa kubwa sana, kwa mfano Dodoma - Dar es Salaam 200,000 na zaidi mpaka 500,000 kwa safari ya mara moja?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Serikali haioni hatari ya kupoteza soko la ndani endapo yakajitokeza mashirika mengine yakafanya biashara hii kwa mfano Flight-Link inafanya safari hiyo kwa dola 180 sawa na shilingi 450,000 kwa safari ya kwenda na kurudi Dodoma - Dar es Salaam na ni fixed. Kwa nini hamuoni mfanye bidii ili kuliokoa Shirika la Ndege Tanzania lisije likazama? Kwa nini hamjiongezi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asha Abdullah Juma kama alivyoeleza.

Mheshimiwa Spika, moja kuhusu tafiti, Shirika letu kwanza, mashirika ya ndege sio moja yako mengi kama alivyosema Mheshimiwa Spika, lakini kwa kuwa amegusia kwenye ATCL specific, ni kwamba tafiti zinafanyika lakini kwa kuwa jukumu la Bunge ni kushauri Serikali tutaongeza pengine utafiti zaidi ili kwenda sambamba na hoja yake.

Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja namba mbili ya kwamba je, hatuoni hatari ya kupoteza soko, nadhani ni jambo ambalo pia linazungumzika kupitia utafiti huo ambao tunaenda nao ambao ameusema kama alivyoshauri tutaendelea kujipima, lakini kwa sasa hivi ATCL haijapoteza soko kwa sababu ipo kwenye ushindani na viwango vilivyowekwa ni kwa mujibu wa ushindani kama nilivyosema kwenye jibu la msingi. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa juhudi kubwa za Serikali zimefanyika kujenga hospitali vituo vya afya vya kileo;

Je, Serikali ina mpango gani kuhimarisha huduma ya kinywa na meno katika vituo vya afya na zahanati zote nchini, kwa sababu sehemu hiyo inaonekana kusahaulika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuhakikisha inaboresha afya za Watanzania ikiwemo afya ya kinywa na meno. Na ndio maana Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga fedha nyingi sana katika ununuzi wa vifaa tiba vikiwemo hivi vya kinywa na meno. Tayari tuna timu ya Ofisi ya Rais TAMISEMI ambayo inazunguka kwenye maeneo yote yaliyopatiwa vifaa tiba kutoa mafunzo kwa wataalam wetu kuona ni namna gani wanaweza kuanza kutumia vifaa hivi kutoa huduma ya kinywa na meno kwenye hospitali zetu za wilaya na kwenye vituo vyetu vya afya vya kimkakati.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi kuuliza swali;

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga benki ya kuhifadhi mbegu asilia zisije kupotea kabisa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mamlaka ya afya mimea na viuatilifu pale Arusha tayari tunayo benki ya uhifadhi wa mbegu za asili, na tunaendelea kufanya utafiti. Lengo letu ni kuzitunza na kuhakikisha kwamba zinaendelea kutumika na kuwaletea tija wakulima wetu wa nchi ya Tanzania.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, ni lini Serikali itahakikisha alama zote muhimu katika barabara kuu za nchi yetu zinawekwa na zinasomeka vizuri?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara zote zinazojengwa kisheria ni lazima ziwekewe alama zote za barabarani kwa sababu hizo ndizo zinazoongoza watembea kwa miguu, lakini pia wanaotumia magari na vyombo vyote vya moto, na kila tunapojenga barabara hizo kwa kweli huwa tunajitahidi kuweka alama.

Mheshimiwa Spika, changamoto ni kwamba kuna maeneo ambayo tukishaweka hizo alama, na hasa zile za vyuma inatokea baadhi ya wananchi huziharibu, hiyo ndiyo changamoto. Lakini pengine nitumie nafasi hii kuwaomba wananchi kwamba alama zote za barabarani zina umuhimu sana kwa maisha yetu na wale watumia barabara zetu muda wote.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, aah! Sorry, ahsante sana kwa kunipa nafasi.

Je, Serikali imewaandaje Askari wa Jeshi la Zimamoto katika uokoaji kwenye uvamizi wa nyuki katika makazi ya watu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kama ambavyo jukumu lake limebainishwa linashirikiana na mamlaka za misitu kila inapotokea janga kama hilo la nyuki kama ilivyotea siku tatu zilizopita hapa Dodoma, wameshirikiana vizuri sana wenzetu wa idara ya misitu kukabiliana na janga lile na kuwahamisha kabisa nyuki kutoka eneo lile. Nadhani ni jambo ambalo tunaomba wananchi inapotokea makundi ya nyuki kwenye maeneo yao wapige namba ya dharura inayoonyesha always 114 ili vyombo vyetu viweze kukabiliana nayo kabla haijaleta madhara kwa jamii zetu, nashukuru.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa baadhi ya watumiaji wenye mahitaji maalum baadhi huwa wanasota kwenda kupata huduma: Je, Serikali inaweza kuhakikisha kwamba vyuo na mashule vilivyojengwa hivi karibuni vimewekewa visaidizi maalum kwa watumiaji hawa kufika vyooni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Asha Abdullah Juma, almaarufu Bi. Mshua, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika taratibu za Serikali, katika kila Halmashauri wako watu wanaitwa Wakaguzi wa Ubora wa Shule zetu. Maelekezo yetu Serikali ni kwamba wakaguzi wote wa ubora wa shule, wapite katika kila shule iliyopo ndani ya Halmashauri zetu kuhakikisha kama hili hitaji au changamoto iliyoelezwa na Mheshimiwa Bi. Asha (Mshua), inafanyiwa kazi, kuhakikisha kwamba walemavu wote au wenye mahitaji maalum wote mahitaji yao yameangaliwa. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Je ni lini Serikali itaweka bayana mpango mzima wa ukarabati au ujenzi wa Vituo vya Polisi pamoja na nyumba za kuishi kwa nchi nzima ili kuepuka kudaiwa huduma hii kila kukicha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nataka nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumeshaanza kufanya tathmini ya kuona namna ambavyo tunaweza tukauandaa huo mpango. Kwa hiyo nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutajitahidi kadiri iwezekanavyo tuone namna ambavyo tunauhangaikia huo na kuweza kuanza kuufanyia kazi kama ambavyo Mheshimiwa ametaka. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Je, Serikali imejipangaje kushajihisha, kuongeza uzalishaji wa mazao ya nafaka asilia kama fiwi, mtama, uwele, ufuta, dengu,choroko na mbaazi kwa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya kilimo hiki?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejipanga kuanzisha kanda za kilimo Tanzania Agricultural Growth Corridor ambalo lengo lake kubwa ni kulima mazao kutokana na afya ya udongo itakavyoruhusu. Kwa hiyo, tunaendelea na kazi ya upimaji wa afya ya udongo, yale maeneo ambayo mazao uliyosema yanastawi tutayapa kipaumbele na tutatenga maeneo ili wakulima wapate maeneo ya kutosha na waweze kunufaika zaidi kupitia mazao hayo.

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu ya Serikali. Kwa kuwa ajali ni jambo ambalo sometimes haliepukiki, linaweza likatokea wakati wowote. Swali la kwanza; ili kuhakikisha usalama na kuepuka ajali za majini, je, TASAC inachukua hatua gani za kila siku za kuimarisha uokozi kwa ajili ya ajali za majini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Serikali ina mpango gani katika kuwekeza kwenye dhana kama vile boti za mwendokasi, vifaa na kuwawezesha kwa kuwapa utaalam wa uokozi wakati wa ajali za majini?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asha Abdallah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Shirika letu la TASAC Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali hususani katika uokozi maeneo ya majini, ziwani pamoja na baharini kwa kuchukua hatua mbalimbali. Hatua ya kwanza, huwa tunatoa elimu kwa wadau wote wanajishughulisha na masuala ya uvuvi baharini ama baharia. Hatua ya pili, kupitia TMA (Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini) ambako tunatoa taarifa ya hali ya hewa kila siku kwa Maziwa yote Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa pamoja na Baharini ili kujua mwenendo wa upepo pamoja na hali ya Maziwa hayo na Bahari kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua nyingine, tunafanya uchunguzi wa ajali ili kubaini vyanzo vya ajali hizo na itatusaidia katika ajali nyinginezo zitakazojitokeza na kuzuia zisitokee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tumefanya mafunzo kwa Mabaharia kupitia International Maritime Organization na kupewa vyeti (Ithibati) kwa Mabaharia wote ambao wako katika maeneo hayo ya maziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu vifaa, kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi kwamba Serikali katika mwaka wa fedha ujao imetenga takribani bilioni 1.74 kwa ajili ya ununuzi wa boti mbili kwa ajili ya uokozi ambapo boti moja itakuwa kama ambulance katika kutatua changamoto zote ndani ya maziwa na baharini, ahsante.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Liko soko kubwa sana la mazao ya kilimohai, kwa mfano pamba yetu ya Tanzania iko namba tatu: Je, ni lini Serikali itaweka angalau kitengo mahususi cha kushughulikia kilimohai katika Wizara ya Kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, mazao mengi ya kilimohai yana soko kubwa na yana uhakika sana wa masoko nje ya mipaka ya Tanzania. Kama Serikali, tumekuwa ni sehemu ya washiriki katika kuhakikisha kwamba tunafanikisha wakulima wetu kuweza kuyafikia masoko hayo makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Wizara ya Kilimo pia tunaweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba tunashirikiana na wadau wakubwa wa kilimohai kwa kuweka kitengo maalum ambacho tutakuwa tunashirikiananao ili mwisho wa siku tufanye kazi kwa pamoja, maana wadau wakubwa wa kilimohai ni taasisi nyingi za binafsi ambazo zimekuwa zina mchango mkubwa. Nasi kama Serikali lazima tuhakikishe pia tunashirikiananao. Kwa hiyo, tunao watu ambao ni focal person katika Wizara ya Kilimo. Tutaendelea kuwaimarisha ili wafanye kazi kwa pamoja na sekta binafsi kwenye kilimohai.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, asante sana.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali kupitia Mahakama zake imejenga Mahakama za Wilaya kwa kiwango safi kabisa. Je, ni lini Serikali itakamilisha kujenga Mahakama za Wilaya zote Tanzania kwa kiwango kama kile ambacho wameshajenga? ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma (Mshua) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza sehemu zote zenye Mahakama, zenye majengo ambayo yanaendelea kutumika hatuna mpango wa kwenda kuvunja na kuanza upya. Tuna mpango wa kujenga mahakama katika maeneo ambayo hayana mahakama kabisa lakini tutakarabati kwa kiwango bora zaidi kwenye yale majengo ambayo sasa yameendelea kutumika asante.

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria ameendelea kuyatoa kuhusiana na miundombinu ya Mahakama. Ningependa kuongeza taarifa ya uhakika kwamba Mahakama ya Tanzania ilishafanya utafiti wa hali ya miundombinu ya Mahakama nchi nzima kwa ngazi ya Mahakama za Wilaya, Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama Kuu. Kwa hiyo, upo mpango wa miaka mitano unaohusu ujenzi wa miundombinu ya Mahakama. Mpango ambao unaendana na mpango mkakati wa Mahakama ambao unaendana na kiasi cha fedha kilichotengwa kwa mahala ambako hakuna jengo la Mahakama kabisa, vilevile fedha iliyotengwa kwa Mahakama zinazohitaji ukarabati.

Mheshimiwa Spika, nitaomba labda Wizara ya Katiba na Sheria inachoweza kufanya ni kuwasilisha ule mpango ofisini kwako ili baadae mpango huo uweze kufikika kwa Waheshimiwa Wabunge wote. Pia tutaangalia uwezekano vilevile nakala kwa njia laini kama itawezekana ukaweza kuwa accessible na kila Mbunge. Nashukuru. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi; kwa kuwa stand nyingi inakuwa unaingia tu kwa kuwa huna la kufanya lakini hazina mwelekeo wa stand; kwa nini Serikali haiji na model stand kwa Makao Makuu ya Mikoa zikafanana zote kama vile ilivyo vituo vya polisi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asha Juma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimpongeze kwa kazi kubwa anayoifanya kuwasemea Watanzania kwa ujumla wake, lakini Serikali tulishatoa maelekezo na standard drawings za stand za ngazi ya Halmashauri, Mikoa lakini na majengo mengine. Kwa hiyo suala hili tunaendelea kuliboresha, kumekuwa na utofauti, kati ya mikoa na mikoa, lakini tumeshatoa sasa utaratibu ambayo ile michoro yote itakuwa inafanana. Ahsante.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara kadhaa Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakisimama na kuomba kujengewa vituo au kukarabatiwa.

Sasa ni lini Serikali itaandaa mpango mzima utakoonyesha orodha wa vituo vinanavyotaka kujengwa au kukarabatiwa kwa nchi nzima ili kuwapunguzia waheshimiwa kusimama kuomba vituo mwaka nenda mwaka rudi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Asha Juma Mshua kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokea ushauri wako na kwa kweli Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeandaa mpango mkakati wa kuboresha sekta ya usalama wa raia ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa majengo. Kwa hiyo, ushauri wa kuleta mwongozo hapa unaoonyesha kituo gani kitajengwa lini au kitakarabatiwa lini tutauandaa tuweze kuuleta kwa Waheshimiwa Wabunge ili kwa kweli kupunguza maswali mengi ya nyongeza ambalo jibu lake linakuwa kama vile linafanana. Nashukuru.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri; sote tunatambua umuhimu wa eneo hili la Jangwani barabara ya Morogoro kama kiunganishi.

Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili (a) na (b); kwa sababu mvua zitaendelea kunyesha, tope, takataka, magugu, mafuriko yataendelea kuwepo na usumbufu upo kwa watumiaji wa pale.

Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wakati tukisubiri huo mpango ambao utaratibu wake unaonekana kuchukua muda mrefu?

Swali la pili, hapo siku za nyuma Serikali ilitueleza mpango mzuri wa kuendeleza eneo lile la Jangwani ikiwemo kuunganisha na kupitia pembezoni mwa mto mpaka Salender Bridge pamoja na kuwekwa viwokwe. Naomba kuuliza Serikali mpango ule mzuri wa kuendeleza eneo lile la Jangwani umefikia wapi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tuna mpango wa dharura ambao unatumika kuhakikisha kwamba daraja lile linapitika na ndiyo maana utaona pamoja na kwamba mvua zinanyesha, lakini bado daraja linaendelea kupitika. Tumemuweka mkandarasi kwa lile daraja ambaye kila baada ya mvua kunyesha anaondoa mchanga, udongo na taka ngumu mita 500 juu na mita 500 chini ili kuruhusu maji yaweze kupita na changamoto hii inasababisha tu na watu kufnayakazi karibu na mto ule. Kwa hiyo, nitoe pia rai kwa wanaofanyakazi wasifanye kazi karibu na kingo za mto ambazo zinasababisha kushindwa kupitika kwa maji kwenye daraja.

Mheshimiwa Spika, suala la pili alilouliza mpango wa kuendeleza Bonde la Jangwani ni kweli upo kupitia mpango wa DMDP, lakini pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wa Dar es Salaam ambao walikaa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, TAMISEMI pamoja Hazina kwamba Serikali imeamua kwamba itajenga flyover ambayo itakuwa inaunganisha makutano ya fire na makutano ya Magomeni, ahsante.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, asante sana.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali kupitia Mahakama zake imejenga Mahakama za Wilaya kwa kiwango safi kabisa. Je, ni lini Serikali itakamilisha kujenga Mahakama za Wilaya zote Tanzania kwa kiwango kama kile ambacho wameshajenga? ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma (Mshua) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza sehemu zote zenye Mahakama, zenye majengo ambayo yanaendelea kutumika hatuna mpango wa kwenda kuvunja na kuanza upya. Tuna mpango wa kujenga mahakama katika maeneo ambayo hayana mahakama kabisa lakini tutakarabati kwa kiwango bora zaidi kwenye yale majengo ambayo sasa yameendelea kutumika asante.

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria ameendelea kuyatoa kuhusiana na miundombinu ya Mahakama. Ningependa kuongeza taarifa ya uhakika kwamba Mahakama ya Tanzania ilishafanya utafiti wa hali ya miundombinu ya Mahakama nchi nzima kwa ngazi ya Mahakama za Wilaya, Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama Kuu. Kwa hiyo, upo mpango wa miaka mitano unaohusu ujenzi wa miundombinu ya Mahakama. Mpango ambao unaendana na mpango mkakati wa Mahakama ambao unaendana na kiasi cha fedha kilichotengwa kwa mahala ambako hakuna jengo la Mahakama kabisa, vilevile fedha iliyotengwa kwa Mahakama zinazohitaji ukarabati.

Mheshimiwa Spika, nitaomba labda Wizara ya Katiba na Sheria inachoweza kufanya ni kuwasilisha ule mpango ofisini kwako ili baadae mpango huo uweze kufikika kwa Waheshimiwa Wabunge wote. Pia tutaangalia uwezekano vilevile nakala kwa njia laini kama itawezekana ukaweza kuwa accessible na kila Mbunge. Nashukuru. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Benki Kuu ya Tanzania ndio custodian wa waendesha biashara za benki nchini Tanzania.

Je, ni lini Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania itachukua hatua ya kuwafidia waliokuwa wateja wa SBNE pamoja na wafanyakazi kuwalipa haki zao kama vile inavyofanya SMZ - Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imewalipa wateja wa Master Life waliopata kadhia kama hiyo? Sasa Serikali hii yetu ya Tanzanzania itafanya nini na kwa nini haiwapi taarifa wananchi kuhusu kadhia hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Mshua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imechukua hatua mbalimbali kutoa fidia kwa wale waathirika wa benki kama zilivyotokea wakati huo na bado Serikali ipo inafanya upembuzi, fedha itakapojitosheleza na kujiridhisha Serikali itatoa fidia kwa wananchi wake. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Kwa kuwa, uhitaji wa ujenzi wa vituo vya Polisi umekuwa mkubwa nchini; je, Serikali haioni umuhimu wa kuimarisha kikosi cha ujenzi cha Jeshi la Polisi na kuiga mfano kama wa Jeshi la Kujenga Taifa na Magereza katika ujenzi wa majengo yao, ambao pia utaokoa fedha nyingi za Serikali? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdallah Juma kama ifuatavyo:-

Swali zuri la Mheshimiwa Mbunge, ni kweli kuna umuhimu huo lakini umuhimu huo tumeshaanza kuuona na kuufanyia kazi, kwa maana ya kwamba kupitia Shirika letu la Uzalishaji Mali la Jeshi la Polisi tumeanza jitihada za kuweza kufanya mageuzi makubwa ya shirika hili ili kuhakikisha linatoa mchango wake mkubwa katika kuendeleza miradi mbalimbali ya Jeshi la Polisi ikiwemo ya ujenzi.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kwamba moja katika mikakati hiyo ni kuimarisha kikosi chetu cha ujenzi ambacho hata hivyo hakiko katika hali mbaya sana, kwa sababu ziko shughuli ambazo zinafanywa na kikosi cha ujenzi cha Jeshi la Polisi, lakini nakubaliana na yeye kwamba kuna haja ya kufanyakazi ya ziada zaidi kukiimarisha kiwe bora Zaidi. Hilo jambo tunaendelea nalo na wazo lake tutaendelea kulifanyia kazi.(Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa magereza mengi yana mwonekano wa kuchoka sana, kwa mfano Gereza la Mjini Lushoto.

Je, ni lini Serikali itafanya utaratibu wa kuyakarabati magereza yote yakawa na sura ya matumaini ndani na nje haidhuru kwa kuwatumia wafungwa hao hao kwa kufanya kazi za ujenzi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la msingi lilikuwa kutwaa eneo na kutumiwa na magereza, lakini ninaweza nikamjibu kwa sababu nina background kidogo ya eneo hilo. Ninafahamu mpango wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni kujenga upya magereza kwenye maeneo ambayo hayana magereza, lakini pia kukarabati magereza ambayo yamechakaa na ukarabati huo umeenza katika maeneo mbalimbali ili kuboresha hali ya magereza hizo.

Kwa hiyo, nimpe uhakika Mheshimiwa Mbunge kwamba kadiri hali ya fedha itakavyoruhusu kwa maana ya bajeti magereza kama alivyorejea hilo la Lushoto, litakarabatiwa ili lilingane na hadhi kama ambavyo ameshauri, nashukuru.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na nakushukuru sana wewe na Bunge zima kwa jinsi mlivyonichukulia na mlivyonipenda na mlivyonihifadhi mpaka leo Mshua nimeingia ndani ya Bunge lako. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, majengo ya Mahakama yapo ya kutosha tunashukuru, lakini kuna wananchi wengi bado wanapata shida na usumbufu kufuatilia kesi zao ambazo zinapigwa danadana kwa muda mrefu. Je, ni lini Serikali itatengeneza hotline au kitengo maalum kwa watu wanaopata shida, wanaofuatilia kesi zao indefinitely kesi ndogo ndogo kama za upangaji, mtu kapanga nyumba halafu hataki kuhama, wala hataki kulipa? Lini Serikali itawasaidia wananchi hawa kuondoa kero yao hiyo? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, wanasema a.k.a Mshua. Suala la kuwa na hotline kama alivyosema ni jambo la muhimu, na tayari Mahakama ina hotline. Wale ambao wanadhani kesi zao zimecheleweshwa, wanaweza kupiga simu na kuweza kujua taarifa zao.

Mheshimiwa Spika, wakati unatembelea Mahakama walikuonesha hiyo namba ambayo wananchi wanaweza kupiga kuulizia kuhusu kesi. Kwa hiyo, tayari kama anavyosema, hotline tunayo. Pia Mahakama hivi sasa tumepunguza backlog hadi kufikia asilimia nne. Tunaendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais, ameteua Majaji. Hivi sasa Majaji wameongezeka na Mahakama zetu zimejitahidi kutekeleza kesi kwa haraka sana kwa sababu hivi sasa tunatumia teknolojia (e-Case Management) ili kuhakikisha kesi haziendi muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, suala la Mheshimiwa ni la msingi na hivi sasa tuna-fast track kesi zisichukue muda mrefu. Tukichukulia Mahakama za Mwanzo huwa hazizidi miezi sita. Ndani ya miezi sita Mahakama za Mwanzo nyingi wanakuwa wameshamaliza shauri, inabaki zile ambazo zinaenda kwa appeal, Mahakama za Wilaya au Mahakama Kuu na Mahakama za Rufaa. Kwa hiyo, mkakati wa kupunguza backlog unaendelea.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu ya Serikali. Kwa kuwa bado kuna ukiukwaji wa utaratibu huu na kwamba bado wananchi wanaosafiri kwa kutumia mabasi ya mbali wanaendelea kupata usumbufu mkubwa barabarani, swali la kwanza; je, ni lini Serikali itaweka vifaa mtandao vya kidijitali kwenye stesheni zote ili kuhakikisha kwamba jambo hili linadhibitiwa kijumla?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, ni lini Serikali itaweka ripoti walau ya mwezi ya kuonesha waliohalifu amri hii na faini au adhabu walizopata ili kuwa fundisho kwa wengine?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi. Magari na mabasi makubwa hayafungwi wala kulazimishwa kushusha abiria au kusimama kwenye stendi za wilaya isipokuwa za mkoa. Kwa maana ya stendi za mkoa yale ambayo hayasimami na kwa maana ya hoja ya Mheshimiwa Mbunge, kwamba tuweke mfumo wa kidijitali, tayari Serikali imeshaanza na hivi ninavyozungumza tumeshaanza majaribio katika stendi mbili. Stendi ya Nanenane Jijini Dodoma pamoja na Stendi ya Magufuli Jijini Dar es Salaam. Tunataka tufike wapi? Tunataka tufike mahali msafiri wa basi awe anaona kwenye screen kama inavyokuwa kwenye airport, kwamba basi langu lipo wapi, litafika saa ngapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa swali lake la pili, kwamba ni lini tutaweka ripoti za wahalifu na faini tulizowapiga hadharani. Kwa sasa Serikali haijaanza mchakato huo au mfumo huo. Tutapokea kama ushauri, tuchakate na kupima kama je, tuko tayari kwa sasa kuanza kuainisha wahalifu wote kwenye nchi yetu, kwamba wamekosa wapi na wamepigwa faini kiasi gani. Tukiona ina tija tutaanza kutekeleza pia.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; je, ni lini Serikali itaongeza viti mwendo vya umeme katika viwanja vyetu vya ndege na stesheni zetu, hasa SGR kwa kuwahudumia watu wenye mahitaji maalum?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa tumeshuhudia watu wenye mahitaji maalum wanapata shida sana wakisafiri hasa kwenye stesheni zetu za SGR. Je, ni lini Serikali itatoa mafunzo maalum kwa wahudumiaji wa watu hawa wanaposafiri katika stesheni zetu za SGR na viwanja vya ndege na vituo vya mabasi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi anavyopigania haki ya watu wenye mahitaji maalumu katika viwanja vyetu katika SGR, treni na usafiri mwingine wa mabasi. Serikali inayo nia na imekuwa ikifanya hivyo. Kama ambavyo nimesema kwenye swali la msingi, ujenzi wowote unaojengwa katika viwanja vyote unazingatia watu wenye mahitaji maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, tayari tuna vitimwendo vya umeme ambavyo vinasimamiwa na watoa huduma katika maeneo mbalimbali ikiwemo Swissport na wengine. Pia, hata kwenye upande wa SGR au hata kwenye ndege unapokwenda kupanda usafiri huu wako watu wenye mafunzo, si tu pale unapokuwa unapanda lakini pia wapo na madaktari pamoja na fani mbalimbali katika afya ambao kama kutakuwa na changamoto yoyote wako tayari kwa ajili ya kuja kuhudumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, tunapokea ushauri wake. Tutaendelea kuongeza ubora katika viwanja vyetu kulingana na mahitaji ya watu wenye mahitaji maalum hatua kwa hatua.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nimepokea majibu ya Serikali; imekuwa mashaka na mtihani mzito, mazingira yanachafuka kwa vifungashio na plastiki mbalimbali ambapo ardhi pia inaharibika na wanyama wanakufa kwa kumeza. Je, Serikali ina mpango gani wa kuiongezea meno sheria ambayo ipo ili kuwabana waharibifu hawa na kuwapa adhabu kali? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni hatua gani Serikali itawachukulia wenye viwanda ambao bado wanaendelea kutengeneza mifuko myepesi na mifuko iliyopigwa marufuku ambavyo inachangia kuharibu mazingira yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Asha kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimeeleza kwenye jibu letu la msingi kwamba sheria ipo, ambayo inasimamia matumizi mabaya ya mifuko ya plastiki, na Sheria hii tayari tumeiundia timu maalum na inasimamiwa na inatekelezwa vizuri, tayari sheria hii imetuelekeza tuwe tunafanya doria na hivyo tunafanya. Pia, sheria hii imeelekeza tuwe tunachukua hatua na tunachukua. Sheria hii imetuelekeza tuwe tunasimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria hii na sheria ipo na inafanya kazi.

Mheshimiwa Spika, sasa hapa nataka kuchukua fursa hii kuwapongeza sana wenzetu wa NEMC ambao wanafanya kazi kubwa katika utekelezaji na usimamizi wa sheria hii. Sasa kama Mheshimiwa anahisi kuna haja ya kuiongezea meno basi wazo tumelichukua ili tuone namna ambavyo tunaweza tukaongeza baadhi ya vitu vya kuongeza usimamizi wa mifuko ya plastiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa viwanda tunafanya kazi kubwa, tayari viko viwanda tumeshavifanyia doria kwa ajili ya kuona namna ambavyo wanatengeneza hiyo mifuko. Lakini tumeshaanza hatua nyingi sana za misako na hatua nyingine zikiwemo za kutoa faini, kufunga kabisa, kutoa onyo, pamoja na kuwapa elimu wamiliki wa viwanda na tayari viko viwanda ambavyo tumeshavichukulia hatua. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nimuambie tu kwamba tutaendelea kufanya kazi hii ili kupunguza hii athari kubwa ya ongezeko la mifuko ya plastiki katika jamii. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa magereza mengi yana mwonekano wa kuchoka sana, kwa mfano Gereza la Mjini Lushoto.

Je, ni lini Serikali itafanya utaratibu wa kuyakarabati magereza yote yakawa na sura ya matumaini ndani na nje haidhuru kwa kuwatumia wafungwa hao hao kwa kufanya kazi za ujenzi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la msingi lilikuwa kutwaa eneo na kutumiwa na magereza, lakini ninaweza nikamjibu kwa sababu nina background kidogo ya eneo hilo. Ninafahamu mpango wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni kujenga upya magereza kwenye maeneo ambayo hayana magereza, lakini pia kukarabati magereza ambayo yamechakaa na ukarabati huo umeenza katika maeneo mbalimbali ili kuboresha hali ya magereza hizo.

Kwa hiyo, nimpe uhakika Mheshimiwa Mbunge kwamba kadiri hali ya fedha itakavyoruhusu kwa maana ya bajeti magereza kama alivyorejea hilo la Lushoto, litakarabatiwa ili lilingane na hadhi kama ambavyo ameshauri, nashukuru.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Je, Serikali ni lini itawasaidia wastaafu ambao wameambiwa bima zao zimesitishwa ambapo na wao wanaendelea kuumwa hawapati dawa huko kwenye sehemu zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni haki ya wastaafu kuendelea kupata huduma za afya kupitia bima. Naomba tulichukue jambo hili, tuweze kufuatilia ni wastaafu gani ambao wamepata changamoto hiyo. Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya tutalifanyia kazi ili wazee hawa wapate haki yao ya matibabu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ninashukuru sana kwa majibu ya kina kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; tumeshuhudia mvua kubwa hivi karibuni na siku za nyuma na upotevu wa maji mengi ya mvua ambayo ni muhimu kwa kilimo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuainisha maeneo yale ambayo maji yanaendelea kupotea na kujenga mabwawa ya wastani na madogo madogo kwa ajili ya kilimo ambacho ndiyo uti wa mgongo wa nchi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; mara kadhaa tumeshuhudia mafuriko katika maeneo ya Rufiji, ambayo yameharibu kilimo makazi, miundombinu hata maisha ya watu. Je, ni lini Serikali itafanya utafiti mahsusi wa kujua ni aina gani ya mabwawa yajengwe kwenye maeneo hayo ili kugema haya maji kwa maendeleo ya kilimo nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nimthibitishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tuna mpango madhubuti; ambapo tulishapata maelekezo kutoka kwa Mheshimiwa Rais; wa kujenga mabwawa makubwa 100 nchi nzima. Mpango huo ambao tunao katika hatua ya sasa tumewakabidhi washauri waelekezi kwa ajili ya kuandaa usanifu wa maeneo hayo yote.

Mheshimiwa Spika, kazi hii itafanyika ndani ya kipindi cha miezi sita na baada ya hapo tutakuwa na taarifa kamili na tutaanza sasa kujua tunatafuta pesa wapi na kuanza kutangaza tender ili tupate wakandarasi. Kwa hiyo, hatua hiyo ipo kwa sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu Bonde la Mto Rufiji ambako kumekuwa na mafuriko makubwa na yenyewe ni kwamba msanifu mkubwa kampuni ya SABA ipo kule site sasa hivi. Wakishamaliza maana yake tutatangaza tender haraka kwa sababu haya yalikuwa ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais wakati ule mafuriko yametokea. Kwa hiyo tender hizi zitafanyika katika mwaka huu wa fedha, ahsante.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza sana hatua ya Serikali kwa kupitisha mkakati wa kilimo hai ekolojia wa mwaka 2023 mpaka 2030 hii ni component muhimu sana. Swali la kwanza; je, Serikali katika bajeti hii ya kilimo iliyosheheni fedha imetenga kiasi gani kwa ajili ya kuendeleza mkakati wa kilimo hai ekolojia ambao una mwelekeo wa kuwanufaisha wakulima wetu na kuwatajirisha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, vipi lile dawati la kilimo hai kwenye Wizara bado lipo hai? Kwa isivyo bahati aliyekuwa anashughulika na dawati hili Mwenyezi Mungu alimpenda tangu hapo hatujasikia mwingine. Sasa kwa kuwa tunataka shughuli za kilimo hai ziendelee, tunataka uhakika huyu mtu ameshakuwa-replaced? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimthibitishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumetenga bajeti kwa ajili ya kusimamia kilimo hai na ukiangalia pale, tuna kifungu kabisa kime-state amount ambayo itatumika kwa ajili ya kusimamia zao hili ambayo siyo chini ya shilingi milioni 200 na katika moja ya mkakati mkubwa tulionao tumeiteua Bihawana kuwa moja ya centre of excellence kwa mazao haya ya kilimo hai ekolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu dawati, dawati lipo hai na tayari tumeshamteua msimamizi tarehe 6 Juni, 2024, tayari mtu ambaye anasimamia dawati la kilimo hai pale Wizarani amepatikana kupitia katika ule mkutano na nimthibitishie tumepata vilevile wawekezaji ambao wapo tayari kutu-support katika uendelezaji wa kilimo hai ekolojia. Ahsante.