Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli (27 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naitwa Bonnah Kaluwa Mbunge wa Jimbo la Segerea. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kunileta hapa katika Bunge lako Tukufu na kuweza kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba pia niwashukuru wananchi wangu au wanachama wenzangu wa Jimbo la Segerea wa Chama cha Mapinduzi ambao waliweza kunipa tiketi ya kuja hapa bila kuwasahau wananchi wa vyama vya siasa kwa jina maarufu vyama vya UKAWA lakini pia wananchi wote wa Jimbo la Segerea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kwa dhati kumuunga mkono Mheshimiwa Rais John Joseph Pombe Magufuli kwa hotuba yake aliyoitoa siku ya tarehe 20 Novemba, 2015 ilikuwa hotuba nzuri ambayo ililenga kuwatatulia matatizo wananchi wetu.
Napenda nianze kwa kuchaangia katika suala la elimu. Napenda nitoe shukrani zangu za dhati na kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Segerea, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuondoa michango mbalimbali ambayo ilikuwepo kwenye shule zetu, kuanzaia shule za msingi mpaka shule za sekondari. Ninaongea hivyo kwa sababu nimekuwa ni mdau wa elimu kwa muda mrefu, tangu nikiwa Diwani nilikuwa nina mfuko ambao ulikuwa unahusika na kulipia watoto ambao wamefaulu lakini hawana uwezo wa kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wengi wameweza kufaidika na hii kauli ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa kwamba watoto wote waende shule na ikiwa shule ni bure na michango mbalimbali kwa sababu walikuwa wanapata shida na watoto wengi waliuwa hawawezi kwenda shuleni au kujiandikisha au wanachelewa kuanza shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kusema hayo naomba sasa nijikite kwenye masuala ya miundombinu ya elimu. Pamoja na Mheshimiwa Rais kutangaza kwamba elimu itakuwa bure lakini pia kuna changamoto nilikuwa nataka nizishauri kama Mbunge wa Jimbo la Segerea, kwa Jimbo langu ambalo lina shule za msingi 37 ambazo zina matatizo. Pamoja na kwamba shule zetu ni bure kwa sasa, lakini tulikuwa tunamuomba Mheshimiwa Rais aangalie au Mawaziri na watendaji waangalie shule zetu za Jimbo la Segerea zina matatizo makubwa.
Kwanza miundombinu yake siyo mizuri nikiwa na maana kwamba mazingira siyo rafiki kwa watoto ambao wanakwenda shule. Madawati hakuna, watoto wengi wanakaa chini, lakini mifumo mibovu ya vyoo, vyoo ni vibovu, unakuta shule ina watoto 2000 lakini ina matundu ya vyoo mawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba shule ni bure lakini tuangalie na matatizo haya ya miundombinu, tunajua ndiyo kwanza tumeanza, changamoto ni nyingi, lakini ninaomba katika bajeti hii ambayo inayokuja, kama tunataka shule zetu ziwe bure na tuweze kutoa viwango vizuri na watoto wetu waweze kufaulu vizuri watoto wa kuanzia shule za msingi, basi tunaomba watutengenezee mazingira rafiki ambayo kwa kawaida watoto wanatakiwa wakae 45 kwenye darasa moja, lakini sasa hivi wanakaa watoto150 kwa hiyo watoto wanarundikana wengi, hata hivyo madarasa yemekuwa ni machakavu sana. Kwa Jiji maarufu kama Dar es salaam, itakuwa ni aibu sana kukuta watoto wanakaa chini. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri aangalie katika Bajeti inayokuja miundombinu ya elimu aiangalie sana katika Jimbo langu ambayo kuna shule nyingi na kuna sehemu zingine kwa sabau sasa hivi tumegawanisha Kata, kuna sehemu zingine hazina hata shule za msingi kwa sasa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata kama ya Buguruni ambayo ina wananchi wengi karibia 70,000 lakini hawana hata shule ya sekondari wanakwenda kusoma Kata za jirani. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, tunaomba utuangalie sana katika bajeti yako katika miundombinu ya elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuchangia katika miundombinu ya elimu, naomba nichangie katika masuala ya afya. Jimbo langu la Segerea, kwanza ni Jimbo lenye changamoto nyingi, lina watu wengi, kwa sensa iliyopita tulikuwa tuna watu karibu laki 5 na Jimbo langu la Segrea lina Kata 13, lakini katika Kata 13 tuna zahanati saba, hizi zahanati zote hazina vitendea kazi. Kuna zahanati zingine ambazo hazina hata umeme, wananchi wanakuwa wanapata shida kwa sababu itakapofika saa 12 jioni inabidi ifungwe. Wananchi wengi hawawezi kutibiwa maeneo hayo. Kwa hiyo kutakuwa na mrundikano wa watu wengi ambao wanatoka kwenye Jimbo la Segerea kuelekea hospitali ya Amana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Afya ya mwaka 2010 ilisema kwamba kila Kata inatakiwa kuwa na kituo cha afya na kuangalia kwenye Jimbo langu kwa sababu ya umuhimu wa watu wengi, tunaomba Mheshimiwa Waziri wa afya, atuangalie tupate kituo cha afya kwa sababu mpaka sasa hivi pamoja na kwamba tulikuwa tuna watu 375,000 ambao walijiandikisha kupiga kura lakini Jimbo lenye Kata 13 na lenye watu 375,000 hatuna kituo cha afya. Pamoja na kutokuwa na kituo cha afya, huduma zetu za afya kwenye hizo zahanati ambazo zipo hazikidhi viwango vinavyotolewa. Hakuna madawa, tumesema kwamba watoto kuanzia 0 mpaka miaka mitano wanapata huduma bure lakini wale watoto wakienda wanachokipata pale ni kuandkiwa dawa na kuambiwa muende mkanunue kwa sababu dawa hazipatikani.
Mheshiwa Waziri wa afya, tunaomba utuangalie lakini sambamba na hilo, tunajua kabisa Kata ya Mnyamani tuna mrundikano wa watu wengi lakini pia tuna hospitali moja ambayo pia katika Kata yetu ya Mnyamani kuna Mabwawa ambayo wanayotunzia maji machafu, Mheshimiwa Waziri tunaomba yale mabwawa yaweze kuondoka pale Mnyamani kwa sababu yanaleta hali ya hewa ambayo siyo nzuri kwa sababu yapo karibu na zahanati au na hospitali ambayo ipo kwa wakazi wa Mnyamani na magonjwa mengi ya mlipuko yanatokea Mnyamani kwa sababu mazingira siyo mazuri.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bonnah muda wako umekwisha!
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kwanza kukushukuru kwa kunipa hii nafasi ili niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa bajeti yake ambayo imekuja inaleta matumaini kwa wananchi, pia nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumteua Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Naibu wake kwa sababu hii kazi wanaiweza vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii pia kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutoa milioni 500 kwa kila Jimbo kwa ajili ya barabara zetu na mimi nimekuwa nikichangia hapa siku zote sisi ambao tunatoka Mkoa wa Dar es Salaam au na Mikoa mingine ambayo inafanya biashara au inatumia sana miundombinu, tunamshukuru sana kwa sababu ndiyo kitu kikubwa ambacho tunakipigania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilitaka niongelee mradi wa DMDP na Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Mwigulu pamoja na Mheshimiwa Ummy tumesha wafuata sana kuhusiana na mradi wa DMDP. Mradi wa DMDP kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni muhimu sana na hata Mheshimiwa Waziri alivyoongea kwenye bajeti yake kwamba wapo kwenye mazungumzo tulitaka tujue haya mazungumzo yataisha lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kama unavyojua baada ya Bunge hapa Wabunge wote tunaenda kufanya mikutano na wananchi wetu na maswali ambayo tutakayoulizwa ni maswali ya barabara na tuna ahadi ya kama Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, mradi wa DMDP pamoja na Bonde la Mto Msimbazi. Wakati tukiwa kwenye kampeni tuliahidi kwamba tutakapomaliza kampeni Bonde la Mto wa Msimbazi litaanza kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tukaahidi kwamba mradi wa DMDP Phase II utaanza na tayari wananchi wameshaanza kuuliza na tumekaa hapa Mheshimiwa Waziri miezi mitatu tukijadili maendeleo ya wananchi, tukirudi kule inabidi twende tukawaambie, hatuwezi kwenda kuwaambia kwamba Mheshimiwa Waziri katika kusoma bajeti yake amesoma mradi wa DMDP utakuwepo Phase II, utakuwepo lini? mwaka gani wa fedha unaanza? na utaanza lini? ili tuweze kujua tuweze kuwaambia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu huu mradi siyo kwamba tu upo Dar es Salaam, Dar es Salaam tunaita DMDP, lakini sehemu nyingine wanaita TACTIC kwa hiyo huu mradi upo Miji 45 nani miradi ya muhimu sana, sana Mheshimiwa Waziri tunaomba hayo maongezi ambayo yanaendelea sasa hivi yaweze kumalizika haraka ili hii miradi iweze kuanza, itatusaidia sana wananchi wa Dar es Salaam na ukizingatia Mkoa wa Dar es Salaam kama nilivyosema hapa nilisimama wakati wa bajeti ya TAMISEMI nikasema hatuhitaji mbolea, hatuhitaji sijui stakabadhi ghalani, sijui vitu gani, sisi tunachohitaji ni barabara na maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Dar es Salaam ndiyo unaolipatia mapato makubwa Taifa letu, kwa hiyo ni Mkoa ambao unatakiwa kulelewa, kuangaliwa, kutengenezewa miundombinu mizuri ambayo wananchi au wawekezaji waweze kuwekeza vizuri wakiona mazingira ni mazuri pamoja na miundombinu yetu ni mizuri tutaweza kupata wawekezaji waje kuwekeza katika Mkoa wa Dar es Salaam, lakini kwa sasa hivi Mkoa ule haufai kabisa, barabara ni mbovu kwa sababu hata master plan ya Dar es Salaam ni mbovu, sasa hivi mvua ikinyesha saa moja mvua ikinyesha Dar es Salaam, kwa sababu hata stendi ya mwendokasi wamejenga kwenye mto, kwa hiyo mvua inavyonyesha tu inabidi kwanza yale mabasi ya mwendokasi wayaondoe yaani mji wote unasimama kwa mvua ya saa moja Mji unasimama kwa siku nzima hakuna biashara inayofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikisimama hapa siku zote nikisema Mkoa wa Dar es Salaam tunahitaji sana miundombinu kwa sababu hiyo na sasa hivi Mheshimiwa Waziri Mkoa wa Dar es Salaam mvua yaani inanyesha kila siku na watalaam wetu mvua ikianza kunyesha…

MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Ridhiwani.

T A A R I F A

MHE. RIDHIWANI J. M. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mchangiaji kwamba hilo jambo lilishajadiliwa humu ndani arudi kwenye Hansard za mwaka 2014 kama sikosei mchango mzuri wa Waziri kipindi kile Mheshimiwa Professor Anna Tibajiuka unaweza kumuelezea nini ambacho kilipangwa katika mradi huo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Bonnah Kamoli.

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa naipokea, lakini mpango wenyewe ulikamilika? Haujakamilika kwa hiyo mimi ninachoongea hapa huu mpango ukamilike, kama ni suala la kujadili hata mimi hapa katika miaka yangu mitano nimeongea sana kuhusu master plan ya Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam sasa hivi ndiyo inatuingizia mapato, ndiyo inatuingizia uchumi, yaani kila kitu kinafanyika Dar es Salaam, hakuna mtu anayeingia kutoka nchi tofauti bila kupita Dar es Salaam, lakini Dar es Salaam yenyewe ukifika tu pale airport ambayo ipo Kipawa, barabara yake ni mbovu, ukija kama ninavyokwambia hayo mabasi ya mwendokasi kama mgeni anakuja siku mvua inanyesha magari yenyewe yamepaki kwa sababu hata huyo mtu ambaye alienda kujenga hiyo stendi akaijenga kwenye Bonde la Mto Msimbazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ndiyo maana tunasema kwamba watu wa Dar es Salaam tunaomba sana ili uchumi wetu uweze kukua ni lazima muilee Dar es Salaam nani lazima muitengenezee mazingira mazuri ili barabara zake ziweze kuwa nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zingine, kwa mfano kama kwenye Jimbo la Segerea, unakuta barabara ya kilometa tano inajengwa kwa miaka mitano. Sasa hapo utaona kweli kuna uchumi gani hapo. Mtu anachukua mzigo wake bandarini mpaka kuufikisha Chalinze masaa 10. Kwa hiyo hayo yote yanaifanya Serikali iweze kupoteza uchumi. Kwa hiyo kama wataweza kutengeneza hiyo miundombinu basi inaweza kuwapatia uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho nilikuwa nataka niongee ni kuhusiana na kauli ya Mheshimiwa Rais Mama Samia. Mama Samia katika mikutano yake au events zake ambazo alizifanya aliongea kwamba, Manispaa ambazo zinakusanya mapato mengi au mapato kwa wingi inabidi ziangalie barabara zake, yaani pesa zibaki kwa ajili ya kutengeneza barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kauli hii tangu Mheshimiwa Rais ameisema, tunaomba basi Mheshimiwa Waziri utakapokuja kuongea uende waraka wa Mkurugenzi. Pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais amesema, lakini tunataka tujue, ni asilimia ngapi ndiyo itabaki kwa ajili ya barabara, ili Madiwani waweze kujua ni jinsi ya kuweza kufanya mipango yao, wakakaa kwa ajili ya ku-budget fedha hizo za barabara, kwa sababu tangu tumelisema hapa halijafanyiwa kazi. Kwa hiyo nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri pamoja na DMDP na hili ni mambo muhimu kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilikuwa nataka kuliongelea ni kuhusiana na diaspora. Ili kukuza diplomasia ya uchumi, ni lazima hawa diaspora tuwaingize kwenye bajeti zetu. Tuwatengenezee mazingira mazuri ili waweze kuja kuwekeza. Kwa sababu hawa watu wako nje na wana uwezo wa kukutana na watu wengi kule kwa ajili ya kuja kuwekeza huku, lakini tatizo huku mazingira sio mazuri. Nilikuwa nashauri dawati la uwekezaji wawe na special package ya hawa watu wa diaspora ili waweze kuja kuwekeza kwenye nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliongea hapa kwenye Wizara ya Mambo ya Nje, tukasema, kwamba hawa watu pamoja na kwamba wako kule bado ni Watanzania; na kule wanafanya shughuli nyingi ambazo sisi wanaweza wakaja huku Tanzania na wakatuingizia mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa sababu Serikali mnatafuta fedha na mnatafuta uchumi lazima hawa watu waingie, yaani muwatengenezee mazingira waje kuwekeza. Kwasababu, kwa sasa hawa watu wanataka kuja lakini hawawezi kuja kutokana na mazingira kutokuwa mazuri. Kwa hiyo nilikuwa nakuomba Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara ya Uwekezaji kwamba litengenezwe dawati special kwa ajili ya watu wa diaspora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nililokuwa nataka…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda umeisha, Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nami naomba nichangie hii Bajeti ya Wizara ya Fedha. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo ameifanya katika hii bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa niaba ya Wananchi wa Jimbo la Segerea Kata ya Kipunguni kwa Mheshimiwa Waziri kuiweka Bajeti ya Malipo ya Fidia ya Kipunguni Kata ya Kipawa kwenye hii Bajeti, tunashukuru sana sana kwa sababu hawa wananchi wamekaa muda mrefu bila kupata malipo yao takribani miaka 30. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunakushukuru lakini tunaomba ulisema utapeleka wakaguzi ambao wanatoka Wizara ya Fedha tulikuwa tunaomba uwapeleke kwa haraka ili hawa wananchi waweze kupata fedha zao na ikiwezekana mwezi wa, huu tuko mwezi wa sita basi mwezi wa saba waweze kuanza kulipwa Mheshimiwa Waziri tutashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nililokuwa nataka kuongelea ni kuhusiana na barabara. Barabara za DMDP ambazo nimekusikia Mheshimiwa Waziri umeziingiza kwenye Bajeti ya mwaka huu tunashukuru sana. Nimekuwa nikichangia hapa kwa muda wa miaka karibuni mitano kuhusiana na Barabara za DMDP. Mkoa wetu wa Dar es Salaam Mheshimiwa Waziri unategemea sana miundombinu na tunapata wawekezaji wengi kuja kuwekeza kwenye nchi yetu lakini lango kubwa ambalo wanatumia ni kwanza wanaingia Dar es Salaam na wanapitia katika Airport yetu, Airport ya Dar es Salaam International Airport. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia mazingira ya Mkoa wa Dar es Salaam kuhusiana na miundombinu kwa kweli imekuwa hairidhishi. Kwa hiyo, kitu ambacho tunaomba pamoja na kwamba umeweka barabara kwenye hii Bajeti basi tunaomba ianze haraka kwa sababu kumekuwa kuna ucheleweshaji sana. Mfano kama mkitangaza hizi miundombinu au mkitangaza Bajeti kwamba kuna barabara zitajengwa hazianzi wakati huo huo zinakuwa zinachukua hata miezi sita Mheshimiwa Waziri au hata mwaka. Kwa hiyo, kwa sababu sasa hivi wananchi wetu wengi wamesikia kwamba kuna barabara sasa zinaenda kutengenezwa, barabara za DMDP. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba kwa kuwa Mheshimiwa Waziri mmetangaza na mmesaini, na kupongeze sana pia nimpongeze Waziri wa TAMISEMI. Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Angellah Kairuki alikuja kufanya ziara katika Jimbo langu la Segerea. Unaweza ukaona Mheshimiwa Waziri kwamba Jimbo la Segerea lipo mjini lakini ukitembelea maeneo yake mengi ni barabara kama ziko vijijini. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri ameziona na ameona jinsi gani wananchi wanahangaika kutokana na barabara kuwa mbovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunamuomba sana Mheshimiwa Waziri hii bajeti ambayo ameisoma na ameweka miundombinu tunaomba hiyo miundombinu iende ikatengenezwe kwenye Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuongelea ni kuhusiana na wakandarasi wetu. Mkoa wetu wa Dar es Salaam miundombinu yake au jiografia yake ni kama unavyoiona. Inakuwaje barabara inatengenezwa na inakuwa mpya lakini mvua ikinyesha masaa mawili unashangaa maji yamejaa Dar es Saalam nzima na inaweza ikasababisha masaa matatu hakuna kitu chochote kinachofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo tunaomba hata hawa wakandarasi ambao wanaenda kututengenezea sasa hizi barabara wazingatie jiografia ya Mkoa wa Dar es Salaam. Kwa sababu kuna sehemu nyingine kwa mfano Jimbo la Segerea kuna miinuko na milima mingi. Sasa tunaomba wakandarasi wawe wanaangalia sehemu ambazo wanaenda kutengeneza barabara ili sasa kuondoa yale matatizo, kwamba barabara ikishatengenezwa basi hayo maji yasijae.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuliongelea ni kuhusiana na taasisi hizi mbili ambazo zote ni za Serikali; maji pamoja na miundombinu. Unaweza ukashangaa barabara imejengwa haina hata miezi miwili nao watu wa DAWASA wanakuja wanchimba kwenye ile ile barabara ambayo imejengwa haina hata miezi miwili. Kwa hiyo mimi napendekeza; hizi taasisi zote mbili ni taasisi za Serikali, kwa hiyo kwa nini zisiwe zina mawasiliano ya karibu? Kwamba sisi sasa hivi tunataka kujenga hapa barabara je, kuna bomba lolote la maji ambalo linaweza kupita, kwa sababu linaleta usumbufu mkubwa sana. Na yale mashimo ambayo wanachimba watu wa DAWASA yanakaa muda mrefu sana na yanasababisha watu wanapata ajali. Kwa hiyo tunaomba barabara kama inajengwa watu wa DAWASA wawe wameshapita na kuweka mabomba yao, tunaomba sana. Hilo pia litasaidia hata Serikali kutokupata hasara kwa sababu barabara inapojengwa halafu tena inaenda inabomolewa ina maana kuna hasara ambayo inaongezeka hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuliongelea ni kuhusiana na TARURA. Tunashukuru sana TARURA kwa kipindi kirefu imekuwa ikipata hela bajeti ambayo si kubwa lakini sasa hivi naona mmeongeza bajeti. Kwa hiyo tunaomba hiyo bajeti ambayo imewekwa kwenye TARURA iende ikafanye kazi kwa haraka. Jambo lingine ni kuhusiana na fedha ambazo zinakusanywa na halmashauri, zile asilimia 10, tulisema kwamba kuna fedha ambazo zinaenda kwenye barabara. Sasa kumekuwa katika kipindi hiki cha kama miezi sita kuna hela ambazo zimepelekwa kwa mkurugenzi kwa ajili ya kutengeneza barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hizi fedha ambazo zinapelekwa kwa Mkurugenzi, sasa hivi tangu imeanzishwa Taasisi ya TARURA mkurugenzi hana mainjinia, kwa hiyo kumekuwa kuna tatizo la ucheleweshaji wa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kwenye Jimbo langu la Segerea kuna barabara ambazo tulikuwa tumezitembelea tangu mwaka jana ambazo zilikuwa zimewekwa ili zitengenezwe na halmashauri kutokana na ile asilimia, lakini mpaka sasa hivi ninavyoongea hizo barabara hazijatengenezwa kwa sababu kumekuwa kuna ucheleweshaji kati ya TARURA na halmashauri. Halmashauri sasa hivi hawana mainjinia, kwa hiyo tunaomba hizi fedha ziendelee kupelekwa TARURA. Kwa sababu jambo hili unafuatilia halmashauri halafu ukifika Mkurugenzi anakwambia mimi sina injinia, kwa iyo inabidi urudi TARURA. Kwa hiyo kumekuwa na ucheleweshwaji sana. Kama mlikuwa mnapeleka hizi fedha TARURA basi tunaomba tu muendelee kupeleka TARURA hizi fedha ili watu waweze kuendelea kupata barabara kwa haraka pia TARURA waweze kufanya kazi yao vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuongelea ni mifumo ya halmashauri. Sasa hivi mwezi mzima hakuna kitu kinafanyika shughuli zimelala, mifumo yote haisomi. Kwa hiyo tulikuwa tunaomba, sijui ni jambo gani Mheshimiwa Waziri, naomba ulishughulikie. Kwa sababu kama mwezi mzima mifumo ikiwa haisomi ina maana hata itakapofunguliwa unaweza ukakuta kuna mapato yamepotea au kuna wizi umetokea mpaka mje mgundue inakuwa ni imechukua muda. Kwa hiyo tunaomba ulishughulikie jambo hilo ili mifumo iweze kusoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na sheria za kodi. Nafikiri hizi sheria za kodi kama zingepitiwa upya hata kusingekuwa na migogoro ambayo inaenda kutokea, kwa mfano kama mgogoro uliotokea Kariakoo kuhusiana na wafanyabiashara, na Iringa. Napendekeza, kama inawezekana hizi sheria ziletwe Bungeni ili tuweze kuzipitia upya ili ziweze kuwa sheria rafiki. Hii ni kwa sababu hii migogoro itakuwa inaendelea kila siku. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenda kumaliza huu mgogoro ambao ulitokea Kariakoo. Kwa hiyo tunaomba sana sheria hizi uangalie Mheshimiwa Waziri ili ziweze kuwa ni sheria rafiki ili tuweze kuendelea na mambo mengine ambayo yanaweza yakatuingizia kipato kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu elimu. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa fedha ambazo zimekuja katika Jimbo letu la Segerea pia Mkoa wa Dar es Salaam mzima. Katika Jimbo langu la Segerea tumepata fedha nyingi sana kwa mwaka ambao umepita na tumejenga miundombinu mingi sana ya elimu. Na mpaka sasa hivi tunajenga maghorofa matatu kwa ajili ya sekondari. Pia tunajenga madarasa mengi kwa kutumia fedha ambazo zimekuja kwa ajili ya elimu. Kwa hiyo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. BONNAH L. KAMOLI: …tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais pia tunakushukuru Mheshimiwa Waziri naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu kama ilivyoelezwa kwenye Taarifa ya Kamati yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninapenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika kuhakikisha kuwa wananchi wake wa Tanzania tunaweza kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Taarifa ya PAC Mwenyekiti wangu ameongelea kuhusiana na DAWASA. DAWASA kumekuwa kuna Taasisi nyingi za Serikali ambazo zinadaiwa na DAWASA. Kama unavyojua, kuna sehemu nyingi kwenye majimbo mengi bado watu hawajaunganishiwa maji kutokana na uchache wa fedha. Hizi fedha shilingi bilioni 13.5 zipo katika Taasisi za Serikali, kwa hiyo, nilikuwa ninaomba nichukue nafasi hii kuziomba hizi taasisi ziweze kuwalipa DAWASA ili wananchi waweze kuunganishiwa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua, mwananchi wa kawaida asipolipa maji tu kwa miezi miwili anakatiwa maji lakini hizi taasisi zimekaa muda mrefu sana hazijawahi kulipa bili zao wala hazijawahi kukatiwa. Tunajua kwamba hizi ni taasisi muhimu na tunajua hawapati asilimia 100 ya bajeti lakini wajaribu kuangalia. Katika bajeti ambayo wanaipata waweze kuwalipa DAWASA ili na wao waweze kufanya shughuli zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilikuwa ninataka kuliongelea ni jambo la kumuomba Mheshimiwa Waziri wa Maji aweze kuangalia bili. Bili zetu ambazo tunazipata au wananchi wanazozipata hazina uwiano na matumizi ya maji. Unakuta mwananchi ambaye ana familia ya watu watatu anapata bili sawa na mwenye familia ya watu 10 na hizi bili zinakuja, kila bili zinapokuja unaweza ukuta kwa muda wa miezi mitatu iliyoongozana mtu anapata bili ambazo, mfano kama alipata shilingi 220,000 mwezi uliopita basi atapata shilingi 220,000 kwa muda wa miezi mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuangalie ni jinsi gani usomaji wa bili unaonekana kuna tatizo kidogo. Waangalie ni jinsi gani wanaweza kutofautisha familia ya watu wengi na familia ya watu wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na miundombinu mibovu ya maji. Maji ambayo yanatoka DAWASA ambayo tayari yameshatengenezwa asilimia 37 maji yote yanapotelea njiani na ni kwa sababu ya miundombinu mibovu. Kingine, mfano bomba limepasuka, unaweza ukawaita watu wa DAWASA waje kutengeneza lile bomba kwa sababu bomba linapopasuka maji yanatoka inawezekana hata kwa siku tano mfululizo lakini hawa watu hawaji na ndiyo maana hawa watu wa DAWASA wanaendelea kupata hasara kwa sababu miundombinu yao mingi ni mibovu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana wananchi wengi mfano Mkoa wa Dar es Salaam, Jimbo la Segerea kuna kata zangu, Kata ya Kinyerezi, Kata ya Bunyokwa, lakini pia na Kata ya Segerea, maji yanatoka kwa mgao kwa sababu maji mengi ambayo yanakuja ili yaende kwa wananchi yanaishia njiani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tulikuwa tunawaomba. Pamoja na kazi kubwa ambayo anaifanya Mheshimiwa Rais, pamoja na kazi kubwa anayoifanya Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri lakini kama huku chini kutakuwa hakuna watu ambao wanaweza kufanya kazi kuziba haya mapengo basi wananchi wataendelea kukosa maji muda wote kwa sababu maji ambayo yanakuja yanaishia njiani. Na haya maji yamekuwa yakileta hasara kubwa kwenye barabara, watu wametengeneza barabara, bomba likipasuka barabara yote inaharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyoy, tulikuwa tunaomba watu wa DAWASA, kwa kweli watu wa DAWASA wamekuwa ni wavivu sana hawa watu wa chini kuja kushughulikia haya mabomba machakavu. Na haya mabomba kama ninavyosema yanaleta usumbufu katika barabara lakini pia kwa wananchi. Unaweza ukakuta bomba limepasuka maji yanaingia kwa wananchi. Nilikuwa ninaomba haya mambo yaweze kufuatiliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nililokuwa ninataka kumuomba Mheshimiwa Waziri ni kuhusiana na jumuiya ya watumia maji. Tulikuwa na visima ambavyo vilikuwa vinaendeshwa na jumuiya ya watumia maji, DAWASA wakavichukua hivi visima, lakini sasa hivi hawavihudumii. Visima vyenyewe pampu zilishakufa siku nyingi. Kwa hiyo, nilikuwa ninaomba kama wenyewe wameshindwa kuviendeleza au kuvifanyia service ili viendelee kutoa maji, basi wawarudishie watumia maji kwa sababu kwa muda mrefu hivi visima vimekuwa vikiangaliwa na jumuiya ya watumia maji na vilikuwa vizuri tu. Tangu walivyovichukua DAWASA, visima vimekuwa havitoi maji, vingine vimekufa, vingine havifanyi kazi. Yaani tuna shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi kata zangu ambazo nimekuambia kata tatu au tano zina visima vya watumia maji lakini kwa sababu pampu zake zimekufa na DAWASA hawajaenda kutengeneza, inabidi wanunue maji na wakati vile visima vipo pale. Kwa hiyo, tunamuomba sana Mhehimiwa Waziri aangalie ni jinsi gani anaweza akavirudisha hivi visima kwa wananchi ili waweze kufanya kazi ya kuviendeleza na wananchi waweze kupata maji. Kwa sababu, kwa kawaida sisi tunapata maji ya mgao, Bonyokwa, Segerea, Kimanga pamoja na Kinyerezi wanapata maji ya mgao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama wanapata maji ya mgao, hivi visima ndiyo vingekuwa vinatusaidia lakini DAWASA visima wanavyo, lakini pia maji hayatoki. Waturudishie hivi visima vya watumia maji ili wananchi waweze kutumia hivi visima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nililokuwa ninataka kuongelea ni kuhusiana na vyanzo vya maji. Vyanzo vya maji vimekuwa ni tatizo kubwa kwa sababu kwenye vyanzo vya maji kumekuwa kuna shughuli za kibinadamu na ndiyo maana sisi tunapata maji ya mgao. Pamoja na kwamba, Mheshimiwa Rais anaanzisha miradi mingi na tunamshukuru pamoja na Mheshimiwa waziri, tunamshukuru hasa kwa miradi hii ya kimkakati ambayo imeanzishwa katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa jina la Dar es Salaam ya Kusini, tunashukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana sana viangaliwe hivi vyanzo vya maji. Kwa sababu, kwenye hivi vyanzo vya maji kama kutaendelea kuwa na shughuli za kibinadamu maji hayatakuwa yanatoka. Tutaendelea kupata mgao wa maji na tutaendelea kupata mgao wa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwapunguzie wananchi wetu ili waweze kupata mgao mmoja, wapate tu hata huo mgao wa maji, lakini visima hivi ambavyo tulikuwa tunaviendesha wenyewe tuweze kuvitumia. Visima hivyo wanavyo, pamoja na maji yao yanatoka kwa mgao. Tunaomba sana, tunajua Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri wanafanya kazi kubwa sana, Mkurugenzi wangu wa DAWASA Dar es Salaam, anafanya kazi kubwa sana lakini wasipoangalia huku chini maji yanakopotea itakuwa ni shida sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetoka Mwaka 2015 mpaka Mwaka 2020, tulikuwa hatuna tatizo la maji mpaka Mwaka 2021, lakini sasa hivi linaanza kurudi tatizo la maji. Ukiangalia tatizo kubwa la maji linasababishwa na miundombinu. Mabomba yanapasuka. Hata hapa hapa Dodoma ukiangalia mabomba yanapasuka lakini ukiwapigia simu wahusika hawaji kwa wakati. Maji yanaendelea kupotea na wakija kwenye taarifa wanasema kwamba wana hasara, upotevu wa maji asilimia 37 na haya maji yanayopotea tayari yameshawekewa dawa kwa hiyo, wanaendelea kupata hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba hawa watu wanatakiwa wawalipe, DAWASA kutokana na hizi kazi zao pamoja na changamoto zao lakini pia waweze kurekebisha miundombinu yao ya maji. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Bonnah Kamoli.

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami nitoe mchango wangu katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais (Sera, Bunge, Vijana, Kazi na Walemavu).
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu. Pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli; vile vile napongeza Baraza zima la Mawaziri kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya, lakini pia kuwapongeza kwa juhudi wanazotusaidia kwa kushirikiana na sisi Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati kabisa napenda kuwapongeza Mawaziri ambao wamekuwa wakija katika Jimbo langu la Segerea kutatua changamoto mbalimbali ambazo zinatukabili; Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Mheshimiwa Jafo na Waheshimiwa wengine ambao walifika kama Mheshimiwa Angelina Mabula. Nawapongeza sana, ahsanteni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/2017, zimezungumziwa program mbili. Program ya kwanza ni program ya kukuza ujuzi wa vijana na program ya pili ni kwa ajili ya kuwasaidia vijana ili kuweza kupata ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015/2016 iliandaliwa program na Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana ya wakati huo, ambayo ilitenga shilingi bilioni 4.1 ambayo iliweza kuwasaidia vijana waliohitimu mafunzo ya Chuo Kikuu au wahitimu wa juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hizo fedha zilizotolewa hazikuweza kukidhi au kuwasaidia vijana wote ambao waliweza kumaliza; kwa sababu tukiangalia takwimu ya vijana wetu wanaomaliza Chuo Kikuu na pesa inayotengwa, inakuwa ni ndogo sana.
Kwa hiyo, naomba Serikali pamoja na kwamba inatenga hizi fedha kwa ajili ya wahitimu wetu wa Vyuo Vikuu, naomba waangalie hili suala kwa kuangalia mifumo mingine ya taasisi za kifedha ambazo zinaweza zikashirikiana na taasisi za kijamii kuona ni jinsi gani wanaweza wakaungana nao ili kuhakikisha wanawasaidia vijana wetu ambao wanamaliza kwa wingi sana Vyuo Vikuu lakini pesa za kuwasaidia kupata ujuzi au ajira au kujiajiri wenyewe zinakuwa ni ndogo. Kwa hiyo, naomba suala hilo waliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sura ya nne, kipengele cha nne, ukurasa wa 48 - Kazi na Ajira. Katika Mpango wa Maendeleo 2016/2017, zimezungumziwa program mbili kama nilivyosema; program moja ya ajira ambayo imeweza kutolewa shilingi bilioni moja, lakini program nyingine ya kukuza ujuzi ni shilingi bilioni 15.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa hiki walichokifanya kwa ajili ya vijana wetu, kwa sababu tuna vijana wengi ambao wanahitaji kusaidiwa pamoja na kuandaliwa vizuri. Hizi fedha hazikidhi viwango vya vijana ambao wanamaliza Chuo Kikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuongelea suala la vijana wetu ambao wapo kwenye matabaka ya kati, ambao wamemaliza kidato cha nne au darasa la saba. Vijana wamekuwa wakijiajiri wenyewe. Sasa naomba Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi, iwaangalie hawa vijana kwa sababu wamekuwa wakijiajiri wenyewe, lakini pia mbali na kujiajiri wenyewe, kuna vijana wengine wana vipaji; lakini hawajawekwa kwenye huu mfumo wa kupata pesa kwa ajili ya kusaidiwa, kwa sababu huu mpango umeelezea kusaidia vijana tu ambao wamehitimu elimu ya juu. Sasa hawa vijana wa kati hatujawatengenezea mpango ni jinsi gani wanaweza wakasaidika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali ije na mpango maalum kwa ajili ya hawa vijana ambao wengine ni wasanii na wana vipaji. Kama Serikali ikiwatambua inawezekana ikawa ndiyo ajira yao ya kudumu. Pia pamoja na kuwa ajira ya kudumu, hao vijana wataweza kulipa kodi kwenye Serikali yetu. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi ambayo inaangalia watu wote kuanzia wenye elimu ya kati, lakini pia na wenye elimu ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napenda kuzungumzia suala la bomoa bomoa katika Jimbo langu la Segerea. Kwanza nachukua nafasi hii kumshukuru Waziri ambaye aliweza kusimamisha hiyo bomoa bomoa isiendelee wakati walipokuwa wanabomoa, lakini kwa sasa hivi wananchi hawajui kinachoendelea. Tunajua kwamba kulikuwa kuna kesi sijui imetupiliwa mbali! Kwa hiyo, tunajua wananchi wengi wamejenga sehemu ambazo siyo salama, lakini wakati wanajenga, tuna Serikali ya Mtaa, pia tuna Serikali ya Kata. Hawa watu wamekuwa wakijenga, watu wanaangalia, kuna Watendaji wetu wapo kule wamekuwa wanawaruhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wenyewe, wanasiasa, tumekuwa tukifanya mikutano katika hayo maeneo, tukienda kwenye mikutano wanatuomba barabara, sisi tunakuja kwenye Manispaa zetu tunaomba barabara na wale watu wanapelekewa barabara. Pia wamepelekewa huduma nyingi za kijamii za kuwaonyesha kwamba sisi Serikali tunaunga mkono wenyewe waendelee kuishi pale. Sasa hivi tukisema kwamba tunawabomolea au tunawapa siku kadhaa ili waweze kutoka pale itakuwa hatujawatendea wananchi haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie, ni kitu gani kitafanyika kuhusu bomoa bomoa? Watu wengi hawana elimu ya kujua kwamba mimi natakiwa nijenge mita 60 kutokea wapi? Kwa hiyo, Sheria ya Mazingira iliyokuja kwa sasa hivi, imekuja tu kuongea wananchi wengi ambao wanakaa sehemu ambazo mimi nipo, hawajui Sheria ya Mazingira. Sasa hivi ndiyo wameanza kuambiwa kwamba unatakiwa ujenge mita 60. Wananchi haelewi.
Kwa hiyo, naomba Serikali kabla hamjawabomolea inabidi kwanza mwende mkawape elimu. Pamoja na kuwapa elimu, hawa wananchi hawana kitu chochote. Kuna wengine walijengewa na watoto wao, watoto wao walishakufa, wamebaki wazee. Sasa hivi unavyokwenda unambomolea nyumba mwananchi kama yule, anakuwa hana sehemu ya kukimbilia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa mhusika aende akaangalie ni jinsi gani tunaweza tukawasaidia. Tuna Manispaa tatu Dar es Salaam, tuna viwanja ambavyo vipo waangaliwe wananchi watasaidiwaje kupata viwanja ili tutokane na hili tatizo la bomoa bomoa. Najua Serikali ya Chama cha Mapinduzi siku zote imekuwa mstari wa mbele kuwaangalia wananchi wake na hasa wananchi wa hali ya chini.
MWENYEKITI: Mheshimiwa, umemaliza muda wako, naomba ukae.
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kushukuru kupata nafasi hii, ili na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara nyeti ambayo inaongoza mustakabali wa elimu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kuchangia katika Sera yetu ambayo iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo inazungumzia elimu bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bure tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutuletea elimu bure kwa watoto wetu, lakini hii elimu bure imekuwa na changamoto kubwa. Jimbo la Segerea tuna shule 37 na tuna wanafunzi ambao wamejiandikisha kwa sasa ni 8,949. Katika Jimbo la Segerea ukitembelea hizi shule Mheshimiwa Waziri wewe mwenyewe utaona huruma na utashangaa. Najua wewe utasema kwamba, unasimamia sera na hii iko kwa TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama ni sera Mheshimiwa Waziri naomba usimamie hizi shule zipate miundombinu ambayo tunaihitaji kwa sababu mwaka 2013 mlikuja na programu ya kila kata kuweka maabara, lakini kabla hamjamaliza maabara zile kuweka vifaa tumekuja na programu nyingine ambayo ni elimu bure, lakini katika hiyo elimu bure tunaanza sasa kutafuta madawati, tunatafuta miundombinu, tunatafuta mambo ambayo sisi wenyewe inaonekana tulikuwa hatujajipanga vizuri. Na hii inasababisha na inaweza ikatuletea matatizo katika elimu yetu na baadaye kuleta matabaka katika elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Segerea kama nilivyosema lina shule 37, lakini kuna madarasa mengine watoto wa darasa la kwanza wako A, B, C, D yaani ina maana kuna wengine wanaingia asubuhi, wengine wanaingia saa 07.00 mchana, wengine wanaingia saa 10.00 jioni, sasa hii yote ni kuwatesa watoto! Mheshimiwa Waziri tunaomba Waziri wa TAMISEMI hili jambo la elimu bure alishughulikie kwa makini sana kwa sababu, tunapoliachia hili jambo tuna miaka tisa na baadaye tutaona madhara yake. Baadaye mtoto atakayemaliza form four atakuwa hawezi kusoma au kuandika jina lake, lakini sisi tutaanza kushangaa kusema kwamba pengine ni wazazi au ni walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu tunawapa mzigo mkubwa. Unakuta mwalimu amesimama anafundisha hana hata nafasi ya kufundishia. Amesimama hapa wanafunzi wameanzia hapa kukaa chini. Mtoto amekaa chini anaandika, hawezi hata kuona anaandika kitu gani. Halafu baadaye tunasema kwamba elimu yetu imeshuka. Elimu yetu inashuka, sisi wenyewe hatuna msingi, hatujajenga msingi mzuri wa kuboresha elimu ya Tanzania.
Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri kwanza uangalie zile maabara ambazo tumejenga mwaka 2013 mpaka sasa hivi ziko kama mapambo, hakuna kitu chochote kinachoendelea katika maabara zetu. Naomba usimamie hilo ili hizo maabara ziweze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine Mheshimiwa Waziri naomba niongelee wanafunzi wahitimu wanaohitimu wanaomaliza shule kutoka vyuo vikuu. Hapa tuna wahitimu wa aina nyingi, lakini wahitimu ambao wamepata mafunzo ya vitendo ni madaktari, wauguzi na walimu. Hatuwezi kufikia uchumi wa kati wakati sisi hatujawaandaa wahitimu wanaotoka vyuo vikuu waje kupambana na kutengeneza ajira na kuajiri watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ningeomba sana, pamoja na mkakati wako wa kusema kwamba unaboresha miundombinu ya vyuo na mambo mengine, ningeomba pia uwaangalie na hawa vijana wahitimu wanafanyaje kupata ajira au kujitengenezea ajira kutokana na hiyo elimu yao ambayo wameisoma na sio tu kwamba ni elimu wakimaliza wanakuja huku mtaani, na mtaani tunajua kabisa kwamba, Serikali uwezo wake wa kuajiri hatuwezi kuajiri wahitimu wote, lakini kama mhitimu atakuwa ametengenezewa uwezo wa kujiajiri na kuajiri yeye mwenyewe, basi tunaweza tukapunguza matatizo ya ajira za kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho ninataka niongelee ni kuhusiana na changamoto ambazo zinawapata walimu. Walimu sasa hivi ambao wanafundisha shule za msingi, lakini pia na shule za sekondari; kuna walimu wengine wanashindwa kuingia kwenye vipindi kufundisha kwa sababu ya kudai madai yao. Kuna walimu wengine ambao unakutana nao Manispaa hawaelewi wanaenda kumdai nani na kama tunavyosema sasa hivi tunasema Hapa Kazi Tu, lakini mwalimu kama hajapata mshahara wake hawezi kukaa akamfundisha mtoto, inabidi afuatilie pesa zake, ili aweze kula na familia yake.
Kwa hiyo, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri uangalie kwanza masuala ya walimu, lakini pia, uangalie miundombinu ya shule pamoja na kwamba inasimamiwa na TAMISEMI, lakini cha tatu uangalie mitaala ya vyuo vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hawa wahitimu wanavyohitimu vyuo vikuu, lakini pia, muwaandae waweze kupambana na soko la ajira kwa sababu sasa hivi huwezi kumlinganisha mhitimu aliyemaliza chuo kikuu cha Tanzania na mhitimu wa chuo kikuu cha nje, obvious huyu wa kwetu hapa atashindwa kwa sababu hajafundishwa kwa vitendo.
Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, najua wewe ni mtaalam na ni mfanyakazi mzuri unaweza ukayasimamia haya mambo na sio mwanasiasa, unaweza ukasimamia vizuri haya mambo yakakaa vizuri ili kesho na keshokutwa tusije tukapata tabaka la watu ambao wamesoma vizuri na watu ambao hawajasoma vizuri ikawa ni matatizo kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kwanza kukushukuru wewe mwenyewe kwa kunipa nafasi na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia kuwa hapa leo na kuweza kuchangia Wizara. Kwanza nianze kumpongeza Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi wanazozifanya, lakini pia kwa kutusaidia katika Majimbo yetu tunapokuwa tuna shida.
Mheshimiwa Spika, lakini umeongelea kwamba tusichangie zahanati na mambo mengine kwa sababu yako TAMISEMI. Tunaomba tuendelee kuchangia kwa sababu tunajua kabisa Wizara ya Afya inasimamia sera. Kwenye Jimbo la Segerea kuna watu 500,000 na katika Jimbo la Segerea kuna kata moja ambayo ni Kata ya Vingunguti ndiyo inayoongoza kuwa na watu wengi Tanzania nzima. Kata hii ya Vingunguti haina zahanati wala haina Kituo cha afya. Juzi Mheshimiwa Naibu Waziri alisema kwamba wanategemea kukipandisha kuwa kituo cha afya hospitali ya Kata ya Segerea na Segerea ni mbali.
Mheshimiwa Spika, pia akazungumzia zahanati ya Plan International ambayo iko Mnyamani. Zahanati hii kwanza imebanwa na nyumba nyingi na hawa watu wameomba kuondoka, lakini mpaka sasa hivi hawajapewa fidia ili waweze kuondoka. Hapa kwenye hii Kata ya Mnyamani, kwanza kuna mabwawa ya maji taka na mlipuko wa magonjwa ukianza tu tunaanza na hii Kata ambayo tayari ina watu wengi, lakini pia kuna mabwawa ambayo yanasababisha watoto kuanzia zero mpaka miaka mitano waweze kuugua kwa wingi.
Mheshimiwa Spika, tumeshafanya research kwenye hii zahanati kwa kupita kwenye hii Kata ya Mnyamani, tumegundua wagonjwa wengi wanaopelekwa kwenye hiyo Plan International ni watoto wadogo wa kuanzia mwaka mmoja mpaka miaka mitano.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaomba pamoja na kwamba tusizungumzie sana suala la zahanati na mambo mengine katika hii Wizara, lakini tunaomba Waziri dada yangu Ummy pamoja na Naibu Waziri msimamie sera inayosema kwamba kila Mtaa uwe na zahanati, lakini kila kata iwe ina kituo cha afya, ambapo Jimbo la Segerea lina mitaa 60 na lina zahanati kumi. Kwa hiyo, unaweza kuona kabisa kwamba Watanzania ambao wanaishi Jimbo la Segerea wanateseka kiasi gani kwa kukosa huduma za afya.
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Spika, naomba tu nielezee kidogo kwamba mimi nimekuwa Diwani kuanzia mwaka 2010 mpaka mwaka 2015.
Mheshimiwa Spika, Manispaa ya Ilala ina mambo mengi ambayo yanajitokeza, tunayaita mambo ya zimamoto, kwa hiyo, bajeti nyingi ambazo zinatengwa katika Manispaa ya Ilala zinakwenda kwenye shughuli nyingine ambazo zinakuja, haziko kwenye programu na hii ndiyo imekuwa kila wakati inatufanya sisi tusiweze kujenga zahanati.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2014 tulipanga tujenge zahanati, lakini ikashindikana kwa sababu pesa tulizopanga kujenga zahanati Serikali ilielekeza tukajenge maabara na ndiyo maana tumeshindwa kujenga zahanati mpaka sasa hivi. Sasa hivi nimekuwa Mbunge, nimeona haya matatizo tuliyokuwa nayo kama Diwani niyalete kwenye Bunge ili Mheshimiwa Waziri aweze kuyatatua.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo Mheshimiwa Waziri ameongelea udhibiti wa ukatili wa kijinsia…
SPIKA: Suala moja tu la eneo, mmeshatenga eneo pia?
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Spika, eneo lipo lakini kila mwaka Manispaa ya Ilala inaweka kwenye programu kwamba itajenga, lakini hizo zahanati hazijengwi mpaka sasa hivi na ndiyo maana tunaomba Waziri akishirikiana na Waziri wa TAMISEMI waweze kututatulia hili tatizo na hela zinakwenda kwenye mambo niliyokwambia, mambo ya zimamoto na mambo mengine ya madeni.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri amesema atashirikiana na wadau mbalimbali ili kuweza kutatua tatizo la ukatili wa kijinsia. Naomba Waziri aweke mikakati kwa sababu suala la ukatili wa kijinsia limekuwa kubwa, akisema atashirikiana pengine inaweza isitoshe. Kuna wasichana ambao, sisi tulitembelea Gereza la Segerea, tumekuta wasichana wadogo ambao wana miaka 14, miaka 13 ambao walikuwa ni ma-house girl wa watu, wamewaweka ndani. Cha kushangaza au cha kusikitisha au cha kuchekesha wale watoto wamefungwa miaka miwili kwa kosa la kwamba amechana dera la bosi wake. Kwa hiyo hii tunaita ni ukatili wa kijinsia.
Mheshimiwa Spika, wengine wamepoteza shilingi 30,000, anasema alitumwa mboga, bosi wake kaamua kumpeleka polisi na hatimaye kumpeleka mahakamani, hatimaye yule mtoto mdogo na innocent anakwenda kufungwa. Sasa tusipolifanyia mkakati hili jambo la ukatili wa kijinsia. Hawa watoto wako innocent, wanakwenda kule gerezani, Gereza la Segerea wanakutana na watu wengine ambao ndiyo wahalifu wa kweli, kwa hiyo, wanapokaa ile miaka miwili wakitoka kule ndani wanakuwa wameshajifunza kuwa wahalifu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaomba Mheshimiwa Waziri, watoto kama hawa kwanza napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru Chama cha Wanasheria Wanawake ambao hili jambo baada ya kuliona waliamua kulifuatilia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri pamoja na kwamba umesema utashirikiana na wadau, lakini pia tunaomba uweke mikakati ambayo inaweza ikasaidia. Tunajua kabisa kwamba unapochukua mfanyakazi wa ndani, unapoamua kukaa naye, anakuwa ni part ya familia, kwa hiyo hawezi kutendewa mambo mabaya.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia mi Benki ya Wanawake. Naishukuru sana Serikali iliamua kuanzisha Benki ya Wanawake mwaka 2009, lakini cha kushangaza hii Benki ya Wanawake haisaidii wanawake walengwa, inasaidia wanawake ambao tayari wana pesa zao kwa sababu hawa wanawake walengwa wako ndani kwenye kata ambao wanafanya biashara ndogo ndogo, lakini hawawezi kufika huku na hawajui process za kufika katika hiyo Benki ya Wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna Bibi Maendeleo au Maafisa Maendeleo wako kwenye kata zetu. Wale Maafisa Maendeleo kazi zao ni kuangalia kata na kuhakikisha kwamba akinamama wanakuwa na maendeleo, lakini wale Maafisa Maendeleo hawafanyi hizo kazi. Kwa hiyo, kuna akinamama ambao wanahitaji wapate tu shilingi 50,000 ya mtaji ili aweze kupika vitumbua au kupika chapati hajui pa kuzipata. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri ili aweze kuliangalia hili jambo na kushirikiana na Mkurugenzi wa Benki ya Wanawake, waangalie watawafuata vipi akinamama ambao wako mitaani ili waweze kusaidika.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine la mwisho, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kumteua mwanamke aongoze hii Wizara. Tunaomba Mheshimiwa Waziri, akinamama wanaokwenda kujifungua hasa wa vijijini, mtu anaumwa uchungu, hivi mtu ukiwa unaumwa uchungu utabebaje mafuta ya taa au taa uende nayo ili uweze kujifungua? Tunaomba ushirikiane na Waziri wa Nishati ili hizi zahanati zipate umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Waziri tunaomba hawa akinamama ambao wanaambiwa waende na gloves, waende sijui na pamba. Naomba ukisimama katika majumuisho yako utoe tamko hii iwe mwisho, mama anakwenda kujifungua aende bila kitu chochote na kila siku sisi tunasema akinamama jeshi kubwa, ushindi ni lazima, kwa hiyo, lazima tuwakumbuke akinamama wetu ambao tumewaacha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuongea. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri ambayo ameitoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri sijaona bajeti ya wakazi wa Kipunguni ambao wapo Kata ya Kipawa. Wakazi hawa wa Kipunguni kama Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999 inavyosema watu wanaweza wakaiachia sehemu kama Serikali inaiihitaji lakini kwa kupata fidia. Wananchi wa Kipunguni wa Kata ya Kipawa, mtaa wa Kipunguni na wa Mashariki, wamefanyiwa tathmini mwaka 1995 lakini mpaka leo hawajawahi kupewa hiyo fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wananchi hawa wengine sasa hivi wamekuwa ni wazee na wengine ni wastaafu wana maisha magumu sana. Kwanza, zile nyumba zao hawawezi kuendeleza kitu chochote kwa sababu hizo leseni zao za makazi hawawezi hata wakawapa benki au mtu yeyote ili waweze kupata kitu chochote ambacho kinaweza kikawasaidia kwa miradi yao maendeleo. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anafanya majumuisho ya hotuba yake atueleze ni lini sasa Serikali itawalipa fidia hawa wananchi wa Kipunguni pamoja na Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nataka Waziri aje kutueleza kwamba hawa wakazi waliofanyiwa tathmini mwaka 1995 watakapowapa sasa hivi hiyo fidia watawapa fidia ya aina gani. Kwa sababu mwaka 1995 hata mfuko wa simenti ulikuwa unauzwa bei ndogo, lakini kwa sasa hivi bei zimeshapanda na hawa wakazi ndio kama hivyo bado wanasubiri wapewe fedha zao au hiyo fidia ambayo walifanyiwa tathmini 1995. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri akija anipe hayo majibu mawili, kwanza aniambie atawalipa lini na pili aniambie atatumia sheria gani ya kuwalipa hawa watu waliofanyiwa tathmini mwaka1995. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine nataka niongelee Bodi ya Wakandarasi kwa sababu Dar es Salaam, Manispaa ya Ilala barabara zetu zimekuwa zikitengenezwa kwa kiwango duni sana. Mfano kama barabara ya St. Mary’s, Vingunguti ambayo inatokea Barakuda na Kimanga zimetengenezwa lakini sasa hivi haziwezi kupitika kwa sababu waliotengeneza wametengeneza kwa kiwango duni na magari yanayopita hapo ni makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atuambie Bodi ya Wakandarasi wanashughulikia kitu gani kwa sababu tumekuwa kila mwaka tunarudia kutengeneza barabara na hii inatufanya wakazi wa Manispaa ya Ilala hasa Jimbo la Segerea wasiweze kwenda mbele kwa sababu ya barabara. Hizi barabara nazoziongelea ni barabara ambazo kama zingetengenezwa vizuri na kama zingeweza kupitia vizuri basi kungekuwa hakuna foleni pale TAZARA au Ubungo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba kwenye hii Bodi ya Wakandarasi pamoja na kwamba unasema sasa hivi tunasaidia wakandarasi wazawa, lakini tuwasaidie wakandarasi wazawa wenye uwezo. Tumeangalia wakandarasi wengi ambao wanasema kwamba wanasaidiwa na sisi tunashukuru kwa sababu wakandarasi wazawa watakaposaidiwa ndiyo na nchi yetu inapiga hatua lakini sasa hawa wakandarasi hawana vifaa vya kufanyia kazi. Mfano mimi nilimtembelea mkandarasi ambaye anajenga daraja Boyonkwa, nimekuta mchanga anabebea kwenye matoroli, hana vifaa vya kufanyia kazi na nilivyouliza sana wanasema mkandarasi huyo hana vifaa vya kufanyia kazi lakini bado wanaendelea kupewa tender na Manispaa ya Ilala. Hiyo inatukwaza sisi watu wa Manispaa ya Ilala lakini pia inatukwaza watu wa Dar es Salaam kwa sababu hawa ndiyo ambao wanaendeleza foleni inakuwa kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho nataka niongelee ni kuhusu daraja ambalo linaunganisha Kipawa na Kata ya Segerea na kuja daraja lingine ambalo linaunganisha Kipawa na Kata ya Kinyerezi. Najua kwamba TANROADS wamejenga daraja ambalo linaunganisha Kata ya Kipawa na Segerea lakini hili daraja lingine ambalo ni la Kata ya Kipawa linalounganisha Segerea na lenyewe ni kubwa kama linalounganisha Kipawa na Kinyerezi. Nimesikia daraja lile linajengwa na Manispaa ya Ilala kwa maana kwamba linajengwa na TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu mwaka 2011 hili daraja lilipochukuliwa na mafuriko halijawahi kujengwa mpaka leo 2016 kila mwaka wanalipangia bajeti lakini hakuna kitu chochote kinachoendelea. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri aangalie ni jinsi gani anaweza akafanya hili daraja walichukue wenyewe la si hivyo wananchi wanaendelea kupata matatizo, mvua ikinyesha wananchi wa Segera wanabaki Segerea, wananchi wa Kipawa wanabaki Kipawa. Cha ajabu daraja ambalo lina vigezo kama hivyo ambalo linaunganisha Kinyerezi na Kipawa limejengwa. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja aweze kutuambia atafanya kitu gani katika mambo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nalotaka kuongelea ni bandari kavu. Mji wetu wa Dar es Salaam sasa hivi una foleni kubwa kutokana na kwamba hakuna bandari kavu, magari yote yanarundikana sehemu moja. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri asimamie tupate bandari kavu pale Kibaha ili magari yaweze kuwa yanakusanyikia hapo, lakini pia tuondoe hizo conjunction za Dar es Salaam, kwa sababu sasa hivi Dar es Salaam magari ni mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia katika Wizara hii nyeti. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniweka salama na kunipa nguvu za kuweza kuchangia siku hii ya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo, napenda kutoa pongezi zangu kwa Mawaziri wote wawili ambao wameweza kutoa hotuba zao ambazo zimeonekana zina mashiko. Pia napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Serikali yangu kwa miradi ambayo inaendelea kuzinduliwa katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo, sasa naomba nianze mchango wangu kwa huduma za afya na ustawi wa jamii.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wizara hii ndiyo inayosimamia na kuratibu utoaji wa huduma za afya katika nchi yetu na ni Sera ya ya Wizara ya Afya kwamba kila Kata itakuwa na kituo cha afya. Pamoja na Jimbo la Segerea kuwa mjini na mpaka sasa lina watu 700,000 lakini Jimbo hili bado halina kituo cha afya.
Mheshimiwa Spika, miezi mitatu iliyopita tulifanya ziara na Naibu Waziri wa Afya na kugundua kwamba tuna zahanati ambazo zingeweza kupandishwa kutoka level ya zahanati kwenda kituo cha afya, lakini mpaka sasa hivi hazijapandishwa kuwa kituo cha afya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kumalizia kusoma hotuba yake kwenye ku-wind up aweze kutuambia je, atatumia njia gani kutujengea kituo cha afya au atupandishie vituo vya afya ambavyo tunavyo viwili; kimoja kipo Tabata ‘A’ na kingine
kipo Mnyamani ambacho ni Plan International? Hizi zahanati zote zina vigezo vya kuitwa vituo vya afya, lakini mpaka sasa hivi ni vitu vidogo vidogo tu ambavyo havijafanyika ili waweze kupandisha na kuwa vituo vya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa namwomba Mheshimiwa Waziri, atakapokuja kumalizia kwenye hotuba yake aangalie ni jinsi gani kama wanaweza kutujengea kituo cha afya au waweze kutupandishia kituo cha afya au waweze kupandisha hivi ambavyo vipo na vyenye upungufu
mchache. Kwa hiyo, nilikua naomba hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kitu kingine ambacho nachopenda kuongelea ni kuhusu miundombinu ya elimu hususan Mkoa wa Dar es Salaam lakini katika Jimbo langu la Segerea. Mkoa wa Dar es Salaam, naomba kwa niaba ya wananchi wa Segerea, unakuta mtoto amefaulu anakaa
Kata ya Ilala, lakini yule mtoto anapelekwa kwenda kusoma Msongola. Msongola ni mbali; na hakuna mzazi ambaye anaweza kumlipia mtoto wake nauli kila siku ya kutoka Ilala kwenda Msongola. Kwanza mazingira yenyewe ni magumu na ukiangalia kwa watoto wetu wa kike wanakutana na changamoto nyingi sana wanapokuwa wanakwenda huko mashuleni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu kutoka Kata ya Ilala kwenda Msongola kwanza ukifika Msongola kwenyewe hakuna tena basi ambalo linaenda huko kwenye hiyo shule.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mtoto inabidi atumie pikipiki. Pikipiki kutoka kituo ambacho anatoka kwenda kwenye shule ni shilingi 10,000. Ina maana ni shilingi 20,000 kwa siku. Hakuna mzazi ambaye anaweza kutoa shilingi 20,000 aweze kumlipia mtoto wake kila siku.
Mheshimiwa Spika, lingine ni kuhusu watoto wetu wa Dar es Salaam wanafeli kwa sababu hiyo na tuligundua taarifa ilipokuja kwamba Mkoa wa Dar es Salaam umekuwa wa mwisho na Wilaya ya Ilala ndiyo imekuwa ya mwisho kieliemu. Watoto wengine wameamua kupanga vyumba
huko karibu na shule. Unakuta mtoto wa kike amepanga chumba, lakini kile chumba ana-share na mvulana. Kwa hiyo, unaweza ukajua kabisa kwamba hapa hakuna kitu chochote ambacho kinaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba kupitia Wizara hii ambayo najua inashughulikia mambo ya elimu, watoto waweze kupangiwa sehemu waliyofaulu. Mtoto kama anakaa Ilala, amefaulu Ilala, apelikwe shule ya Kata ya Ilala. Kama anakaa Kipawa, basi apelekwe shule hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana kwa sababu siyo kwamba nafasi hazipo; nafasi zipo lakini sijui wanatumia utaratibu gani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine nilikuwa nataka kuongelea…
SPIKA: Mheshimiwa Bonnah, Maafisa Elimu wako ndio wanahusika na hilo, nakushauri tu. Endelea tu Mheshimiwa Bonnah.
MHE. BONNAH M. KALUWA: Sawa.
Mheshimiwa Spika, lingine nililotaka kuongelea ni kuhusu fao la kujitoa. Linasema kwamba mtu anatakiwa afikishe miaka 55 ndiyo aweze kupewa yale mafao yake. Sasa hivi kuna watu wanaajiriwa kwa mkataba, anapewa kazi ya mkataba wa mwaka mmoja au miwili. Ina maana
amepata mkataba wa kazi wa miaka miwili, halafu amalize hapo asubiri mpaka miaka 55! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, licha ya hayo, kutokana na maisha magumu ya sasa hivi yanayoendelea, kwanza mtu unakuwa hauko sure kama utaishi kwa muda wa miaka 55. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aangalie tena upya kuhusu hili fao la kujitoa ili watu waweze kupewa mafao yao wanapomaliza kazi na kazi zenyewe kama nilivyosema ni kazi za mkataba. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kitu kingine nilichokuwa nataka kuongelea ni Mfuko wa Barabara. Pamoja na kwamba kuna miradi mingi inaendelea katika Mkoa wa Dar es Salaam lakini pia pamoja na Jimbo la Segerea, lakini tunajua kuna barabara zetu nyingi ambazo ndiyo barabara za mitaa
ambapo Waziri wa TAMISEMI ndio anahusika nazo. Katika Kata ya Kiwalani pamoja na Kata ya Minazi Mirefu kuna mradi mmoja wa DMDP. Huo mradi umekuwa ukipangiwa kila mwaka, sasa hivi mfululizo ni miaka mitano kwamba barabara za mitaani zitatengenezwa, lakini mpaka sasa hivi hatujajua. Tukiuliza Manispaa, bado wanasema kwamba wanasubiri TAMISEMI ili waweze kuwaletea taarifa rasmi ni lini wataanza kutengeneza hizo barabara.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri atakapomaliza, atueleze ili hawa wakazi ambao wanasubiri barabara zao kutengenezwa na kuna wengine tayari wanasubiri kulipwa kwa sababu kuna nyumba ambazo inabidi zibomolewe, wapate muda specific
ni lini barabara zinaanza kutengenezwa ili wajue na sisi tujue kwamba ni muda gani barabara hizo zitaanza kutengenezwa na mimi Mbunge maswali yapungue.
Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia katika hii Wizara ya Miundombinu. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri pamoja na Wizara yote katika miradi ambayo inaendelea katika Mkoa wa Dar es Salaam. Pia napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuifanya katika sekta ya miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nianze mchango wangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kitabu cha Wizara ya Miundombinu lakini kuna barabara ambazo naona zinaweza zikatusaidia katika Mkoa wetu wa Dar es Salaam, mwaka 2014 hizi barabara ziliainishwa kwamba zitaanza kujengwa mwaka 2015, lakini kwa sasa hivi nimeangalia nimeona tu kwamba wamesema ndiyo wanataka kufanya tathmini, ina maana hawajaweka hata hiyo bajeti ya tathmini au kujua ni lini zitaanza kujengwa. Barabara ambayo inatoka Kimara inapitia Jimbo la Kibamba na pia inakuja mpaka Banana lakini pia inakwenda mpaka Kitunda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri aangalie hizi barabara, kwa sababu hizi barabara za Dar es Salaam, inaweza ikaonekana Dar es Salaam kwamba kuna barabara nyingi zinatengenezwa lakini Dar es Salaam kuna foleni kubwa, hii barabara kama ikitengenezwa inaweza ikatusaidia wakazi wa Dar es Salaam ili foleni iweze kupungua. Kwa sababu, watu ambao wanatoka Mbezi wanatumia hii barabara kupitia Jimbo la Segerea na baadaye wanapitia Ilala kwa ajili ya kukwepa foleni na kuongeza hata watu wafike makazini mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho nilikuwa nakiangalia nilijua Mheshimiwa Waziri atakiweka ni fidia ya wakazi wa Kipunguni Kata ya Kipawa. Mwaka 2016 kwenda 2017 nilisimama nikaongea kuhusu hii fidia ya wakazi wa Kata ya Kipawa, ambao wamehamishwa kwa ajili ya kupisha upanuzi wa Airport, lakini naona hapa Mheshimiwa Waziri hajaweka bajeti wala hajawazungumzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wakazi tangu mwaka 1995 wako pale wanasubiri kuhamishwa na wanasubiri malipo yao. Mpaka sasa hivi hawajalipwa na hakuna kitu chochote ambacho kinaendelea na hakuna kitu chochote wanachokijua kwamba Serikali itawalipa lini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiingia katika Kata ya Kipawa, Mtaa wa Kipunguni sehemu ya hawa wakazi wanapokaa imeshakuwa kama vile watu wamehama kwa sababu watu hawawezi kufanya maendeleo yoyote wameambiwa wanasubiri malipo yao. Kuanzia mwaka 1995 mpaka leo hakuna kitu chochote walicholipwa na kuna watu wengine ambao walikuwa wanasubiri hizi pesa wameshakufa na wengine ni wastaafu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namwomba Mheshimiwa Waziri kwa sababu nilishakwenda na Naibu Waziri tukafanya mkutano na hawa wananchi, akasema kwamba wampe miezi mitatu, lakini sasa hivi ni zaidi ya miezi nane, hakuna jibu lolote ambalo Mheshimiwa Naibu Waziri wala Mheshimiwa Waziri amelitoa. Naomba Mheshimiwa Waziri aweze kuniambia ni lini hawa wakazi wa Kipawa wataweza kulipwa pesa zao. Kwa sababu kwanza sheria inazungumza watu wasiondoke walipwe fidia ndiyo waweze kuondoka, lakini wale watu wameondoka na mpaka sasa hivi hawajui kinachoendelea. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja kumalizia kwenye bajeti yake aniambie ni lini atawalipa wakazi wa Kipawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nataka kuzungumzia bomoa bomoa ambayo imepita Majimbo ya Ukonga, Segerea na Ilala. Nina masikitiko makubwa sana kwa Mheshimiwa Waziri, hawa wakazi ambao wamekaa walikuwa wamejenga pembeni ya reli, tunayo Serikali kuanzia Serikali ya Mtaa, Serikali ya Kata lakini wamewachia hawa watu wamejenga na baadaye mmekuja kuwabomolea, hata mlivyowabomolea hamjafuata utaratibu Mheshimiwa Waziri. Mtu amekaa kwenye nyumba yake miaka 50 unamwamsha saa 10 ya usiku akupishe unabomoa, jamani hiyo siyo haki! Kwanza tunawaonea sana wananchi, saa kumi ya usiku kuwatoa watu kwenye nyumba zao, wengine wana wagonjwa, wengine wanaumwa na wengine ni wazee mnaenda kuwabomolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishafanya kikao na wakazi ambao waliambiwa wajiandae watabomolewa kwa sababu ya kupisha reli ya kisasa ambayo inajengwa. Nami nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri, hakuna mtu yeyote awe anatoka Jimbo la Segerea au Ilala ambaye anakataa maendeleo, lakini watu wanakataa ile process waliyotumia, jinsi walivyokwenda. Walisema kwamba tunawapa miezi mitatu ili waweze kujiandaa waondoke, lakini kabla ya hata siku kumi tangu wametoa barua wameenda saa kumi ya usiku kuwavunjia nyumba zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo reli wenyewe wameweka jiwe kwamba mwisho wetu mtu asijenge hapa, lakini wamebomoa wameenda wamelipita mpaka lile jiwe walilojiwekea wenyewe. Tunajua Sheria ya Manispaa inasema kwamba wakazi wa Mjini wanatakiwa kukaa mita 15 na wa Kijijini ni mita 30, watu wa reli wameenda wamebomoa mita
30. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwombe Mheshimiwa Waziri atuambie kwamba ni sheria gani imetumika kuwavunjia wakazi wa Mnyamani Buguruni, Ukonga pamoja na Ilala kwako Mheshimiwa Zungu. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu hawa wakazi mpaka sasa hivi hawana sehemu ya kukaa, wako nje na hawajui kama mtawalipa au hamtawalipa. Kwa sababu sasa hivi kumezuka tabia, kila mtu ambaye anaenda kufanya kitu ambacho siyo kizuri anasema maagizo yametoka juu, ni uwongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie jamani hawa ni watu wetu, tumesema kwamba tunawasaidia watu wanyonge. Sasa tunawasaidiaje watu wanyonge kwa kuwavunjia nyumba zao. Mheshimiwa Waziri naomba akija kujibu haya mambo anieleze wakazi hawa aliowavunjia kupisha hii reli ya kati ametumia sheria gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho nataka kuongelea ni miradi ya DMDP ambayo ilitakiwa barabara zijengwe Kiwalani pamoja na Minazi Mirefu. Leo ni mwaka wa nne, kila mwaka tukikaa hapa tunapanga kwamba tutaanza kujenga mwaka kesho na mpaka sasa hivi nimeangalia kitabu hakuna bajeti ya miradi ya DMDP kuhusu hizo barabara za Kiwalani pia barabara za Minazi Mirefu. Watu hawa wamekuwa wakikaa kwenye barabara ambazo siyo nzuri kwa muda mrefu. Sasa hivi ni miaka karibu 15 wanaahidiwa kwamba huu mradi utaanza, ulikuwa uanze mwaka jana mwezi wa Nane lakini mpaka sasa hivi haujaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishie hapo, Mheshimiwa Waziri naomba majibu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipanafasi hii. Kwanza naomba nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa ambayo inafanya hususani kweye mambo ya usambazaji wa dawa, lakini pia nichukue nafasi hii kumpongeza sana Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy kwa kazi kubwa ambayo anaifanya, sisi wote Watanzania tunaiona, tunakupongeza sana na kama mwanamke tunajivunia wewe kuwa hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Naibu Waziri wa Afya kwa kazi kubwa wanayoifanya ambapo wanazunguka na kuangalia ni sehemu gani kuna changamoto, lakini pia na kuendelea kutatua hizo changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo, naomba sasa niongee changamoto ambazo zinalikabili Jimbo langu. Jimbo langu mwaka 2016/2017 lilikuwa lina watu 773,000; Jimbo langu lina kata 13 lakini mpaka sasa hivi Jimbo langu halina kituo cha afya. Najua haya mambo yako TAMISEMI Mheshimiwa Ummy, lakini naliongelea kwako kwa sababu wewe ndiye unayeangalia sera, na sera yetu ya afya inasema kila kata iwe na kituo cha afya na kila kijiji kiwe na zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi watu wa mijini hatuna kijiji, tuna mitaa. Kwa hiyo, nilikuwa nakuomba sana Mheshimiwa Ummy, Jimbo la Segerea, nilisimama mwaka 2016 na 2017 nikiongelea usimamizi wa sera, tunahitaji tupate kituo cha afya. Kutoka kata ya Kisukulu mpaka Amana ni kilomita tisa, kwa hiyo, wananchi wanapata shida sana. Unaweza ukaangalia kwamba labda kwa sababu sisi tunakaa mjini ndiyo maana; labda kwa sababu kuna hospitali nyingi ambapo wananchi wanaweza kutibiwa, lakini ujue kwamba tuna changamoto moja kwamba mtu anapotoka sehemu ya mbali kwenda Amana kwanza kuna foleni ya magari, lakini pia kuna changamoto nyingine ni za mrundikano wa watu kwa sababu watu wote wanakwenda Amana, ni kwa sababu hatuna kituo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na Mheshimiwa Waziri mimi katika Jimbo langu, mfano, kama ukiongelea kata ya Vingunguti ina watu 200,000 na mpaka sasa hivi haina kituo cha afya wala zahanati yake pia haina miundombinu mizuri. (Makofi)

Kwa hiyo, nilikuwa nakuomba Mheshimiwa Ummy, Mheshimiwa Waziri na Wizara yote ya Afya muangalie vizuri Jimbo la Segerea, msimamie hizo sera ili tuweze kupata kituo cha afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nimeshafanya na Naibu Waziri tumekwenda kata ya Segerea, tukaenda kata ya Mnyamani. Halmashaauri ya Manispaa ya Ilala imeshatoa fidia kwa nyumba ambazo zilikuwa zinaizunguka Hospitali ya Plan International kwa ajili ya kupanua kile kituo ili kiweze kuwa kituo cha afya. Tumeshafanya hivyo, Mkurugenzi tayari ameshatoa hela sasa tunawasubiri ninyi Wizara ili muweze kutuboreshea sasa na kukipandisha hadhi kiwe kituo ili wananchi wanaokaa Jimbo la Segerea wasiweze kwenda Amana au wasiwe kwenda sehemu zingine waweze kuishia pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nilitaka kuongelea suala la delivery kits ambalo wajumbe wengine waliweza kuliongelea. Mambo ya uzazi ni mambo ya baraka lakini pia ni mambo ya maumbile na pia ni mambo ya majaliwa. Kwa hiyo, nilitaka niongee na Mheshimiwa Waziri, na kwa sababu Mheshimiwa Waziri ni mwanamke najua atalifanyia kazi. Kuna watu wengine ambao wako vijijini akina mama wenzetu hawawezi kununua kwa shilingi 22,000 au shilingi 25,000. Sasa nilitaka niiombe Serikali waangalie wanaweza kuwasaidiaje akina mama wenzetu ambao wako kijijini ambao hawawezi kutoa hizo fedha ili waweze kupata hiyo delivery kits.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunakuomba sana Mheshimiwa Waziri uweze kunaangalia. Tunajua kwamba lazima na sisi wananchi lazima tuweze kuchangia kiogo katika Serikali lakini pia lazima tuangalie na wananchi wenzetu ambao wanakaa nje ya mijini kwa sababu sisi wa Mijini pengine tunaweza tukawa tuna hizo pesa za kutoa ili tuweze kuangalia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza napenda nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali kwa miradi mikubwa ambayo inaendelea ikiwemo kwenye Mkoa wangu wa Dar es Salaam na mikoa mingine. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wote ambao wanatoka katika Wizara yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, nataka niongelee kuhusiana na TARURA. Asilimia 80 ya barabara ziko TARURA, lakini Mfuko wa Barabara unaipa TARURA asilimia 30. Tumekuwa na barabara mbovu ambazo haziwezi kutengenezwa, zinaishia tu kwenye kuandikwa na kuwekewa bajeti, matokeo yake hazitengenezwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri na Wizara nzima waangalie ni jinsi gani watakavyoisaidia TARURA kwa sababu, wanavyoipa asilimia 30 hakuna kitu chochote ambacho kinaendelea. Kwa mfano, barabara zangu, barabara ya Airport, Mheshimiwa Waziri anajua kabisa ndege nyingi zinaletwa, tunaenda tunazindua na kila kitu lakini barabara ni mbovu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiwa unatoka Airport unaingia pale opposite na Airport barabara ambayo inakwenda Karakata Kipawa ni mbovu sana na kule watu wamejenga hoteli na vitu vingine ambavyo vingeweza kuongeza uchumi kwa wananchi wetu, lakini watu hawawezi kwenda kulala kule kwa sababu barabara zetu ni mbovu. Kwa hiyo, naomba sehemu ambazo wanaona kwamba zinaleta maendeleo at least zile sehemu ambazo wanaona ziko karibu na Airport basi mngeweza kuzifanyia mpango au strategy maalum kwa ajili ya kuzipendezesha ili watu wanaokuja hapa nchini kwetu wakitoka tu Airport sio wanakutana na barabara mbovu, wakutane na barabara nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka kuongelea wananchi wangu wa Kata ya Kipawa, Mtaa wa Kipunguni na Magharibi. Nimeshafanya mikutano tofauti na Waheshimiwa Mawaziri wawili au watatu juu ya madai yao ya mwaka 1992, mimi bado niko shule, lakini mpaka sasa hivi hao wananchi hawajalipwa. Mheshimiwa Waziri kila siku namwambia kwamba wale wananchi wanaendelea kuwa maskini kwa sababu tangu wamefanyiwa tathmini mwaka 1992 mpaka leo hawajalipwa, wanakuja wanawalipa watatu, wanaondoka, wanakuja wanawalipa wanne wanaondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, wakati anakuja ku-wind up naomba aseme kwamba hao watu atawalipa au waendelee na shughuli zao zingine, kwa sababu kuwaweka wanavyowaweka, hawawaambii kama wanawalipa, hawawaambii kwamba waondoke, wapo tu kwenye njia panda hawajui kinachoendelea. Naomba sasa awaambie waendelee na shughuli zao kwa sababu mpaka sasa hivi kuna wengine wamekufa na wengine bado wanaendelea na wao wamesema kwamba watu wasijenge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la tatu nataka niongelee kuhusiana na wananchi wangu aliowabomolea wale waliokuwa kandokando ya reli. Sheria inasema kwamba mjini ni mita 15, kijijini ni mita 30, lakini cha ajabu wananchi wa Kata za Kipawa, Buguruni na Ilala kwa Mheshimiwa Zungu wote wamekwenda kuwabomolea mita 60. Tunajua kwamba wanafanya maendeleo, wanataka treni ipite lakini sasa hawa wananchi wamebaki maskini. Hilo naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho anielezee hawa wananchi wangu watalipwa au hawalipwi ili sasa tujue kama tunaenda sehemu nyingine ili tuweze kupata msaada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine niongelee kuhusiana na madaraja. Kuna madaraja ambayo yako mpaka kwa mpaka. Naongelea daraja la seminari yaani daraja linalounganisha Segerea pamoja na Kipawa. Hili daraja tangu mwaka 2012 baada ya mafuriko yale Mbunge akiwa Makongoro Mahanga mpaka leo halijawahi kutengenezwa. Kila siku namwambia Mheshimiwa Waziri hili daraja inaonekana utengenezaji wake kiwango chake cha pesa ni kikubwa, naomba walichukue TARURA kwa sababu Manispaa ya Ilala haiwezi kulitengeneza, haina uwezo. Sasa Mheshimiwa Waziri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mawazo yangu katika Mpango wa Bajeti wa 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nishukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa miradi mikubwa ambayo inaendelea nchi nzima lakini specifically katika Mkoa wangu wa Dar es Salaam. Kuna mambo mengi ambayo yamefanyika katika Mkoa wa Dar es Salaam, tuna barabara za juu lakini pia hata hii treni ambayo inajengwa sasa hivi ya kisasa imepita kwenye Mkoa wetu wa Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuishukuru Wizara ya Afya kwa kuleta pesa katika Jimbo langu la Segerea kwa ajili ya vituo vya afya. Vilevile nimshukuru Waziri wa Miundombinu kuhakikisha kwamba Jimbo la Segerea linakuwa na miundombinu mingi, japokuwa tuna changamoto chache lakini naamini kabisa mtazimaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, sasa naomba nitoe mchango wangu katika mpango wa 2019/ 2020 . Nashauri mpango utakaokuja 2019/2020 kuwepo na mpango wa kibajeti wa kuhakikisha kwamba tunamaliza mafuriko katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya na Morogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Dar es Salaam japokuwa sasa hivi siyo mji mkuu wa Serikali lakini bado ni mji maarufu na mji ambao unaiongezea kipato kikubwa Tanzania. Mafuriko yanapotokea kwanza yanaathiri uchumi, uchumi wa mtu mmoja mmoja lakini pia hata uchumi wa Serikali. Kama juzi hapa kulikuwa na mafuriko tuliona hata mabasi yetu mengi yalishindwa kutembea lakini pia wafanyabiashara walifunga maduka yao lakini siyo tu kwa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Mikoa ya Dodoma, Morogoro pamoja naMbeya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri katika mpango unaokuja basi aweze kuweka mpango wa kibajeti wa kuweza kumaliza kabisa mafuriko haya ili wananchi waweze kukaa au wafanyabiashara waweze kufanya biashara zao vizuri na Taifa liweze kupata kipato. Kwa sababu tunapokuwa tunayashughulikia haya mambo wakati yanapotokea tunashindwa kuyamaliza. Kwa hiyo, nashauri sana kuwepo na mpango kwa ajili ya kumaliza mafuriko katika mikoa ambayo nimeitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine nashauri kuwepo na mpango wa kurasimisha makazi holela ambayo yapo kwenye mikoa tofauti tofauti kama Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa mingine. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mpango aje na mpango wa kuweza kushirikisha wadau na sekta binafsi ambao wanaweza wakaongea na hawa watu ambao wako kwenye makazi holela waweze kushirikianao nao, aidha, kuwajengea nyumba kwa kuingia nao ubia labda anaweza kupewa apartment moja halafu nyingine wakachukua hao watu wanaojenga kwa ajili ya kusaidia kuondoa hayo makazi holela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakapoweza kuingia ubia na hawa wananchi ambao wanakaa kwenye makazi holela basi hata uchumi unaweza kukua kwa sababu kwanza tunawaongezea thamani ya maeneo yao lakini pia lile eneo ambalo tunaliita makazi holela linakuwa limetoka. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Dkt. Mpango aweze kuja na mpango ambao utaweza kuwasaidia wananchi ambao wanakaa kwenye makazi holela washirikiane nao kwa ajili ya kuwajengea nyumba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nilichokuwa nataka kuongelea ni kwa ajili ya kutengeneza miundombinu.

Mheshimiwa Waziri aje na miundombinu rafiki kwa wajasiliamali wetu ambao wako Dar es Salaam kama mama ntilie, bodaboda, waweze kuwatengenezea miundombinu rafiki. Hawa watu hii ndiyo ajira yao, mfano bodaboda wapo Tanzania nzima na ajira nyingi ya vijana sasa hivi imekuwa ni bodaboda. Sasa hivi kinachoendelea ni kwamba wanapata ajali nyingi lakini pia wamekuwa na matatizo ya hapa na pale mara wanakamatwa na mambo kama hayo. Kama Mheshimiwa Waziri akija na mpango wa kuwatengenezea miundombinu mizuri ambapo wenyewe watakuwa wanapita lakini pia kuwatambua kwamba Dar es Salaam nina bodaboda kadhaa, hiyo pia itaisaidia Serikali kuweza kupata kipato wanapolipa kodi kujulikana kwamba hawa bodaboda wapo wapi sambamba na mama ntilie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine nataka niongelee kuhusiana na suala vijana wetu wanaomaliza vyuo. Vijana wetu ambao wanaomaliza vyuo wamejengwa katika mazingira kwamba unapomaliza chuo moja kwa moja unaenda kuajiriwa. Tofauti na watu ambao wamesoma ualimu, udaktari na vitu ambavyo unaweza ukaenda ukaajiriwa, mfano, kama mtu amesoma udaktari, anaweza akaajiriwa kwenye hospitali binafsi, mtu ambaye amesomea ualimu anaweza akaajiriwa shule binafsi lakini wale waliosoma sayansi, Serikali ije na mpango wa kuwajenga ili wakimaliza chuo wajue kwamba wanakuja kujiajiri na siyo kwamba wanakuja kuajiriwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inasema sasa hivi tunajiandaa kwa ajili ya kwenda kwenye uchumi wa kati, vijana wetu wengi hawawezi kushindana na vijana ambao wanatoka East Africa kwenye kufanya kazi. Mfano kama sasa hivi tunasema Serikali ya Awamu ya Tano ni ya viwanda lakini hatujawaandaa wale vijana kwamba wakimaliza tu chuo waje kufanya kazi kwenye viwanda, wanaishia tu kupata kazi ambazo ni za vibarua na kazi nyingine ambazo haziwezi kuwasaidia kiuchumi ili kupata wanachokipata. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja aje na mpango wa kuangalia vijana wetu ambao wanamaliza vyuo waweze kujiajiri wenyewe na isiwe wanamaliza chuo kwa ajili ya kuajiriwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimwa Mwenyekiti Ahsante, kwanza naomba nichukue nafasi hii kuipongeza Wizara ya TAMISEMI, lakini pia kuwapongeza Mawaziri wote pamoja na Serikali nzima kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya kuhakikisha kwamba wanalitoa Taifa letu kwenye uchumi wa chini na kulipeleka kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa speed ambayo inaonekana, sina mashaka kabisa, 2025 kama tutakuwepo, basi tutakuwa wote tunaona tumefika kwenye uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sana naomba nichangie mchango wangu kwenye upande wa TARURA. TARURA kama walivyosema wenzangu, inapewa asilimia 30, lakini TARURA ina kilometa 130,000 na TANROAD wana kilometa 30,000. Sasa TARURA wana kuwa hawawezi kufanya kazi zao vizuri kwa sababu bajeti ni ndogo sana.

Mheshimiaw Mwenyekiti, kwa sababu sheria hizi zilivyokuwa zinatungwa zamani, ilikuwa bado hawajaunganisha zile barabara mkoa kwa mkoa, lakini kwa sasa hivi watu wa TANROAD wameshaunganisha barabara zao mkoa kwa mkoa na nyingine wameshaunganisha wilaya kwa wilaya. Kwa hiyo, naomba niishauri Serikali iweze kubadilisha sheria ili watu wa TARURA waweze kuongezewa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa kuna tatizo kubwa sana hasa sisi Wabunge tunapoenda kufanya mikutano yetu. Tunaenda kufanya mikutano yetu tunaahidi wananchi kwamba hapa sehemu hii itajengwa barabara na ndivyo tunavyokuwa tumeaambiwa na watu halmashauri pia na watu wa TARURA wanakuwa wamepanga bajeti yao, lakini ukiangalia sana unakuta kwamba TARURA wana matatizo ya bajeti. Dar es Salaam kuna matatizo makubwa ya barabara, ukiangalia barabara za Jimbo la Segerea tuna barabara moja ambayo iko Kata ya Kimanga, sasa hivi hiyo barabara inajengwa kwa miaka mine, lakini tatizo kubwa ni bajeti, TARURA haina pesa ya kumalizia ile barabara iweze kumalizika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna barabara nyingi mfano kama Jimbo la Ukonga barabara ziko kwenye hali mbaya, barabara ya Pugu, barabara ya Majohe, Barabara ya Kitunda – Banana, barabara zote hizo zinasubiri TARURA, lakini TARURA hawana bajeti walipanga mwaka jana hizo barabara zitajengwa, lakini haziwezi kujengwa kwa sababu bajeti hakuna. Sasa nataka nishauri Serikali kwamba hii sheria ibadilishwe, TARURA waongezewe fedha ili waweze kupanga kuendana na mipango yao wanayoipanga, lakini kama tutaendelea hapa kwamba TARURA watakuwa wanapewa asilimia 30, haiwezekani, itakuwa mipango yetu ya kusema kwamba tunajenga barabara Fulani, barabara hazitajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ni mbaya sana ukiangalia Kata ya Kipawa pale tuna terminal one, two na three tunategemea kufungua airport ya kisasa terminal three, lakini opposite na hiyo airport barabara ni mbovu sana, sasa tunasema kwamba tunakaribisha wawekezaji, wanapokuja hapa inatakiwa pia miundombinu iwe mizuri. Sasa mwekezaji anatoka tu airport anakutana na barabara mbovu, kwa kweli hiyo inamkatisha tamaa. Niwaombe sana tuangalie hili suala la kuongeza fedha kwenye Mfuko wa TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ninachotaka kuongelea ni kuhusiana na ushirikiano wa hizi taasisi mfano TARURA, DAWASA, Wizara ya Maji pamoja na TANESCO, unakuta barabara imetengenezwa, TARURA wametengeneza barabara baada ya miezi miwili DAWASA wanakuja wanachimba wanapitisha miundombinu yao, mashimo yale yanakaa miezi hata sita hayajawahi kuzibwa. Sasa huu pia ni upotevu wa mapato ya Serikali kwa sababu baada ya kuchimba wanakuja wanaziba ni kutengeneza vitu mara mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kama inawezekana, kama kuna mradi ambao unafanyika sehemu Fulani, taasisi hizi za Serikali ziweze kuwasiliana ili wakae waone kwamba hapa tunapitisha mradi fulani, waweze kuweka miundombinu yao kwa pamoja, sio barabara imejengwa TANESCO wamekuja, DAWASA wamekuja TANESCO wanakuja ooh hapa tunapitisha nguzo, kwa hiyo inabidi tubomoe barabara. Naomba sana hilo jambo lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuongelea ni kuhusiana na suala la elimu. Tumekuwa tuna tatizo kubwa sana, watoto wetu wanapoanza shule darasa la kwanza. Sasa kama sasa hivi mwaka jana wamemaliza wanafunzi 22,285, mwaka huu wameingia wanafunzi 44,656, tunajua hawa wanafunzi wameingia na sasa hivi Serikali imeleta utaratibu kwamba wanafunzi wote wanakuwa kwenye system. Sasa Serikali inashindwajwe kujua kwamba mwaka 2020 mwezi wa Kwanza wataingia watoto fulani ili sasa tusije tukaanza yale mambo ya zima moto. Kwa hili kwa kweli nichukue nafasi hii kuwapongeza sana viongozi wa Dar es Salaam, Mkuu wangu wa Wilaya Sophia Mgema, Mkurugenzi wangu pia na Mkuu wa Mkoa wamekuwa wakifanya kazi kubwa kuhakikisha madarasa ya zimamoto yanajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu tusiwe tunafanya kazi kwa zimamoto tuna hesabu sasa hivi za watoto ambao wameanza shule ya awali, lakini pia tuna hesabu ya watoto ambao wanaanza darasa la kwanza, tunajua kwamba baada ya muda gani watoto watamaliza shule. Sasa kuepukana na haya matatizo ya kufanya kazi kwa zimamoto tuiombe sana TAMISEMI iweze kuandaa miundombinu na tukisema miundombinu hatusemi tu miundombinu ya madarasa tunahitaji tupate miundombinu ya vyoo, kama sasa hivi kuna watoto wengi wanakuwa kwenye shule moja tunahitaji tupate miundombinu ya vyoo lakini tupate miundombinu mingine ambayo itawawezesha wale watoto waweze kusoma vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongelee kuhusiana na zahanati au vituo vya afya. Kwanza nichukue nafasi kumshukuru sana Mheshimiwa Jafo kwa kuleta milioni 500 kwenye kituo chetu cha Plan International lakini nataka tu nikwambie Mheshimiwa Jimbo la Segerea lina wakazi milioni moja elfu kumi na sita, tuna kituo kimoja tu cha afya. Sasa kwa kuwa na kituo kimoja tu cha afya kwa jimbo zima kama lile na lenye wakazi kama wale bado tuna changamoto kubwa. Tunaomba tupate kituo kingine na tuna maeneo makubwa mfano kama zahanati ya Seregea ina eneo kubwa sana la kujenga kituo cha afya. Pia ukienda Kinyerezi pia kuna zahanati pia ina eneo kubwa la kujenga kituo cha afya na Tabata. Tungeomba tupate hivi vituo vya vinne ambavyo vinaweza vikatusaidia katika Jimbo la Segerea kwa sababu mambo mengine yote yanaweza yakaishia kwetu kwenye Jimbo la Segerea kabla hatujaenda Amana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kwanza niipongeze Serikali kwa kazi ambayo inaendelea kufanya hususan kwenye mambo ya masuala ya miundombinu, lakini nataka nichangie kwenye Sekta ya Miundombinu. Katika Jimbo la Segerea kuna wananchi ambao wanadai fidia tangu mwaka 1997, wananchi ambao walipisha Airport Terminal Three, hao wananchi mpaka sasa hivi hawajalipwa, kwa hiyo naiomba Serikali kwa sababu tuko sasa kwenye Bunge la mwisho ili iweze kuangalia ni jinsi gani inaweza ikatoa tamko au ikawalipa hawa wananchi kwa sababu imekuwa ni muda mrefu sana na kila siku tukisimama hapa tunaongelea kuhusu hao wananchi. Pia nimekuwa nikifuatilia bajeti zinavyotoka nione hata kama kuna bajeti wamepangiwa kwa ajili ya malipo yao sijawahi kuona bajeti yoyote katika hii miaka miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka niiulize Serikali, je, ni lini sasa itawalipa hawa wananchi kwa sababu nimekuwa hapa huu unaenda mwaka wa tano lakini nimekuwa nikichangia kila mwaka kuhusiana na hawa wananchi, lakini hawajaweza kulipwa. Naomba sana Kamati ya Miundombinu pamoja na Mawaziri wote ambao mmoja mmoja wameshawahi kufika kwenye Jimbo langu na wakafanya mikutano na wakawaahidi hawa wananchi kwamba watarudi kwa ajili ya malipo yao. Sasa umefika wakati wa kuwalipa hawa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho nataka kuchangia ni kuhusiana na miundombinu ya barabara. Tunajua watu woe kwamba Mkoa wa Dar es Salaam kwa sasa kutokana na mvua ambayo inaendelea miundombinu ya barabara imeharibika sana na Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na kwamba sio Makao Makuu ya Nchi lakini pia ni mji maarufu na ndio mji ambao unaingiza kipato kikubwa katika Nchi ya Tanzania. Sasa hivi kwa Mkoa wa Dar es Salaam miundombinu yake ni mibovu sana. Nataka niishauri Serikali tukisema tu kwamba tuangalie bajeti ambayo tuliipitisha 2019/2020 ambayo ndio ikatengeneze ile miundombinu, bajeti haitoshi kwa sababu tumeshaongea sana na watu wa TARURA wanataka kufanya kazi lakini hawana bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nina ushauri kwa Serikali, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha jana alituambia kwamba, wanapanga asilimia moja ya bajeti kwa ajili ya majanga na kwa tafsiri yangu kwamba majanga sio tu lazima watu wafe, majanga ni kama haya yaliyotokea sasa hivi miundombinu ya barabara mibovu lakini pamoja na watu wamepata maafa mengi sana kuhusiana na mvua. Sasa asilimia moja ukisema nusu ya hiyo asilimia moja ni bilioni 30. Sasa kama tukipewa bilioni 15 sisemei kwa Jimbo la Segerea peke yake, lakini nasemea kwa Mkoa wa Dar es Salaam ili waweze kurekebisha hiyo miundombinu ambayo imeharibika, kwa sababu kwa kawaida, kama nilivyosema tukisema bajeti ambayo iliyopangwa 2019/2020 TARURA hawana pesa hizo. Sisi kama Wabunge au mimi kama Mbunge nimekuwa niliongea sana na watu wa TARURA kuhusiana na miundombinu ambayo imeharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano kwenye Jimbo langu kuna barabara kama sita hivi hazipitiki kabisa ukianza na ile barabara ya Vingunguti ambayo inatokea Vingunguti Mataa mpaka Barakuda, hiyo barabara haipitiki kabisa na watu hawataki kupitisha magari yao kwa sababu ina mashimo makubwa na watu wanaenda kujaa kwenye hii barabara ya Tabata. Sasa barabara hii ya Tabata utakuta foleni kuanzia saa moja mpaka saa nne na ndio maana inasababisha hata uchumi kushuka kwa sababu watu wanakaa muda mrefu barabarani badala ya kuwa makazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Serikali itawaaachia tu TARURA kwamba ndio wenyewe wawe waendelee na hii kwa ajili ya kurekebisha hizi barabara naomba sana Serikali iwaongezee TARURA pesa na kila siku nimekuwa nikisimama hapa naomba TARURA waongeze bajeti kwa sababu hali ya mijini kutokana na miundombinu na barabara zetu ni chakavu na hazijafanyiwa matengenezo kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kutokana na hiyo bajeti hiyo aliyosema kwamba kuna asilimia moja ambayo anaiweka, aweze kuwapa watu wa TARURA ili waweze kufanya marekebisho yaliyotokea Dar es Salaam nzima au Tanzania kote mvua inakonyesha. Kwa hiyo, naomba sana kwenye masuala ya miundombinu kwa sababu mjini sasa hivi pamekuwa hapafanyiki kitu chochote sababu ya foleni. Kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Mwenyekiti…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutumia nafasi hii kwanza kukushuru wewe mwenyewe kwa kunipa nafasi hii, lakini nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi kubwa ambayo wameifanya katika nchi yetu ya Tanzania katika hiki kipindi cha miaka minne ambacho tunaendelea sasa kumaliza na kuwa kipindi cha miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda tu kupongeza kwamba tulikuwa tuna mambo mengi ambayo tuliomba au tuliyaweka kwenye Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi 2015- 2020 na mambo hayo tukiangalia mpaka sasa asilimia 90 au asilimia 88 yote yameshatekelezwa. Kwa uchache tu ninapenda kutaja barabara ambazo zimejengwa, barabara ambazo ni kubwa kwa Mkoa wa Dar es Salaam; tuna flyover ambayo iko pale TAZARA imejengwa kipindi cha Awamu ya Tano, lakini pia tuna barabara ya Ubungo ambayo ni interchange imejengwa kipindi cha Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tuna barabara sita ambazo zinatoka Dar es Salaam mpaka Pwani ambazo zimejengwa kipindi cha Awamu ya Tano. Lakini pia tuna barabara nyingine ambayo inajengwa Nakanazi pamoja na Kasulu ambazo zinajengwa kwa bilioni 260; zimejengwa Awamu ya Tano. Tuna Daraja la Busisi ambalo linajengwa kwa miezi 48, Mheshimiwa Rais ameshalizindua kwa hiyo tuna vitu vingi ambavyo tunaweza kujivunia katika Serikali ya Awamu ya Tano au Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ambayo imeweza kuvitekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutumia nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Mhehimiwa Jafo, pamoja na Manaibu wake wote kwa kazi kubwa ambayo wameifanya katika Nchi ya Tanzania, hususani kwenye Jimbo langu la Segerea ambapo kwa sasa tuna barabara nyingi za lami ambazo zimejengwa katika kata mbili zilikuwa chini ya Mradi wa DMDP lakini najua ziko chini ya TAMISEMI, barabara za kilometa 16 na masoko sita lakini pia na bustani mbalimbali ambazo wameweza kubadilisha mazingira ya hizi kata mbili. Kwa hiyo, natumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa kuleta maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nampongeza kwa kusimamia na kuangalia suala zima la elimu bure ambapo mpaka sasa hivi tumekuwa na ongezeko kubwa la watoto shuleni, ni kwa sababu wamekuja kwa sababu ya elimu bure. Kwa hiyo, nipende kutumia nafasi hii kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Waziri Jafo kwa mambo makubwa ambayo anayafanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ninataka kuliongelea ni kuhusiana na barabara zetu za ndani. Pamoja na pongezi hizo lakini bado tunamuomba Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Jafo, aweze kufanya kazi kubwa kwa kuangalia barabara za Mkoa wa Dar es Salaam lakini pia na mikoa mingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano kama barabara za Mkoa wa Dar es Salaam katika Jimbo la Segerea, Jimbo la Ukonga na Jimbo la Ilala, barabara sasa hivi zina hali mbaya sana, na zina hali mbaya sana kwa sababu ya mvua. Mvua imekuwa kubwa na mvua imeharibu miundombinu na imeharibu miundombinu ni kwa sababu kuna mifereji na barabara nyingi ambazo hazijaweza kutengenezwa kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninataka nimuombe Mheshimiwa Jafo; TARURA haiwezi kubadilisha mazingira yaliyopo sasa hivi kwa bajeti ambayo tumekuwa tukipanga. Kwa kweli barabara ni mbovu sana na ninajua TARURA wanataka kufanya kazi lakini bajeti yao ni ndogo.

Katika Jimbo la Segerea tuna mafuriko makubwa, mafuriko yamechukua sehemu kubwa. Kama unavyojua Mheshimiwa Jafo kwenye jimbo letu ndiyo umepita Mto Msimbazi, kwa hiyo, katika ule mto umepita sasa hivi unaingia, sio kwamba wananchi wameufuata Mto Msimbazi, sasa hivi maji ndiyo yanawafuata watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ya Vingunguti kuna makaburi ambayo sasa hivi yanaondoka na maji. Unakuta makaburi mengi sana, makaburi kama 200 ya Kata ya Vingunguti yameondoka na maji na hayo makaburi zamani yalipokuwa yamepangiwa hayakupangiwa kwenye mto lakini kutokana na uchakavu wa miundombinu, kutokana na uchakavu wa mifereji hayo maji yameacha njia yake na yameshaenda sasa kwenye nyumba za watu na hatimaye kusababisha hayo makaburi kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tuna mradi mkakati ambao mmeujenga Kata ya Vingunguti, machinjio ya kisasa. Mheshimiwa Jafo machinjio ya kisasa tunakupongeza sana, ni machinjio mazuri ambayo yatawasaidia wafanyabiashara wadogowadogo hata kufanya shughuli zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri barabara ya kukufikisha kwenye hayo machinjio ni barabara mbovu sana, imeharibika kutokana na miundombinu ya mvua na kutokukarabatiwa kwa muda mrefu. Kwa hiyo ninakuomba sana katika bajeti yako hii ya 2020/2021, naomba utuangalie katika hizo barabara ambazo tumezitaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ninachotaka kuongelea ni kuhusiana na Ugonjwa wa Corona. Nitumie nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy, pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wanaifanya. Nimpongeze Mkuu wangu wa Mkoa, Paul Makonda, pamoja na Mkuu wangu wa Wilaya, Dkt. Sophia Mjema, ambao wamekuwa wakifanya kazi kubwa kwa ajili ya uhamasishaji wa watu jinsi gani ya kujikinga na huu ugonjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze Wizara kwa kazi kubwa ambayo imefanya kwa ajili ya kutoa utaratibu kwanza wa utoaji taarifa kwamba ni Waziri na Mheshimiwa Waziri Mkuu ndio watakaohusika kutoa taarifa nani ana Corona na wagonjwa wangapi wapo. Hiyo inatusaidia sisi kutokupata taarifa ambazo sio makini au sio sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kutoa ushauri kutokana na huo Ugonjwa wa Corona. Kuna wananchi wetu wengi ambao walikuwa wanafanya biashara mfano kama hizi biashara za mamantilie au biashara za kupika, biashara nyingi tu ambazo zimeathiriwa na Ugonjwa wa Corona. Sasa wananchi wengi wamechukua mikopo benki kwa sasa hivi kwa kuwa biashara hakuna na hawa wananchi wako nyumbani.

Ninaomba kupitia Wizara ya Fedha kuongea na Benki Kuu ili waangalie hizi benki ndogondogo kama wanaweza kuwasaidia hawa wananchi ambao walikuwa wanalipa labda kwa mwaka mmoja, waweze kuongezewa mwaka mmoja mbele. Kwa sababu sasa hivi kama watawaacha waendelee hivi ina maana wananchi wengi wanaweza wakauziwa vitu vyao. Kwa hiyo, ninaomba sana Wizara ya Fedha ifanye kitu kama hicho ili kuweza kuona kwamba hawa wananchi wetu tunawakinga na janga hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watendaji wetu, kwa sababu kila kata kuna bwana afya, sasa hawa mabwana afya kwa wakati huu tunamuona tu Mheshimiwa Makonda anatoa taarifa au anahamasisha pamoja na yeye kuhamasisha lakini bado tuna watendaji wa afya ambao tayari wana utaalam wa afya ambao wanaweza kwenda mitaani waweze kuwaelekeza watu jinsi ya kujikinga na Ugonjwa wa Corona. Kwa hiyo, ninaomba hawa watendaji wa afya kwa kipindi hiki waweze kutembea na kuweza kuwaambia watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine…

(Hapa kengele Ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda umekwisha Mheshimiwa Bonnah, ahsante sana.

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kwanza kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Segerea kwa kunirudisha kwa awamu ya pili lakini shukrani za pekee ziwaendee wajumbe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika Mpango wa Miaka Mitano ambao Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameweza kuuwasilisha hapa. Napenda niweke mawazo yangu katika huu Mpango; napendekeza kwamba kuwepo na mpango kwa Mkoa wa Dar es Salaam kwenye suala la miundombinu. Nasema hivyo kwa sababu ukiangalia kwa sasa hivi Mkoa wa Dar es Salaam unachangia mapato makubwa katika Taifa na ni mkoa wa kibiashara lakini pia ndiyo Mkoa ambao una Manispaa sita katika mikoa yote ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu ni kwamba katika Mkoa wa Dar es Salaam miundombinu iliyopo sasa hivi mvua ikinyesha kwa nusu saa Dar es Salaam nzima inasimama. Katika kusimama huko mapato mengi yanapotea kwa sababu watu wanapokuwa hawafanyi kazi wanasubiri mvua iishe au kuna mafuriko ambayo yametokea, hakuna mama ntilie ambaye anapata wateja, hakuna bodaboda ambaye anatembea lakini pia kunakuwa kuna mambo mengi ambayo yanasimama kutokana na miundombinu ya Mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mapendekezo ni kwamba katika huu Mpango wa Miaka Mitano Serikali ije na mpango wa kuhakikisha kwamba Mkoa wa Dar es Salaam unatengenezewa miundombinu ambayo itakuwa ya permanent. Kwa sababu kwa sasa hivi kila mvua inaponyesha Mkoa wa Dar es Salaam lazima tuchukue siku tatu au nne tunahangaika na mafuriko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika bajeti yetu hii ya mwaka. Mfano bajeti ya TARURA, kwa Manispaa ya Ilala wanapata bilioni tano, bilioni tano inatengeneza barabara moja na ukiangalia Wilaya ya Ilala kilometa 1,200 bado hazijawekewa lami. Kwa hiyo, tukifuata hii bajeti ambayo ni ya mwaka kwa mwaka katika Mkoa wa Dar es Salaam, hatuwezi kufikia malengo ambayo tunataka kuyafikia. TARURA wakipewa shilingi bilioni tano, wanatengeneza barabara moja. Mfano sasa hivi kuna barabara moja ambayo inatengenezwa; barabara ya Vingunguti – Barakuda ambayo ina kilometa 7.6. inatengenezwa kwa shilingi bilioni 7.8. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama TARURA wanapata shilingi bilioni tano kwa mwaka kwa majimbo matatu, nikimaanisha Jimbo la Ilala, Segerea pamoja na Ukonga, ina maana haya majimbo mengine yote mawili yatakuwa yamekaa hayafanyi kitu chochote na wala hawana fedha za ukarabati. Ukiangalia Mkoa wa Dar es Salaam, Kata ambazo ziko pembezoni mwa mji, water table yake iko juu sana. Kwa hiyo, barabara yoyote ambayo inatakiwa kutengenezwa na iweze kudumu, basi hiyo barabara inatakiwa iwe imepangiwa fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iangalie ni jinsi gani italeta mpango ambao unaweza ukaenda kufanya kazi katika Mkoa wa Dar es Salaam. Kwa sababu ukizungumzia Dar es Salaam, siyo sawa na Bukoba, siyo sawa na Kigoma na wala Shinyanga.

Kwa hiyo, sisi watu wa Dar es Salaam na wananchi wetu ambao wako Mkoa wa Dar es Salaam, wanachangia mapato makubwa katika Taifa. Kwa hiyo, tunaiomba sana Serikali, ili tumalizane na hili jambo la mafuriko, maana kila mwaka tunapata mafuriko zaidi ya mara mbili au mara tatu. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Kweli kabisa.

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ili tumalizane na hili jambo la mafuriko, tunaomba Serikali ije na mpango ambao utaweza kumaliza mafuriko ya Dar es Salaam kwa mara moja. Hili jambo linaweza likatusaidia, wananchi wetu waweze kuendelea kufanya kazi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nililokuwa nataka kuongelea ni kuhusiana na Miradi ya DMDP ambayo inaboresha makazi. Hii miradi phase ya kwanza imemalizika, sasa tunaenda phase ya pili, lakini mpaka sasa hivi hii miradi imesimama. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali iweze kufanya mpango hii miradi iweze kuendelea kwa sababu ndiyo inayoleta matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi. Kwa hiyo, naomba sana katika huu Mpango, Serikali ije na mpango maalum katika Mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nami pia napenda niungane na Watanzania wenzangu kutoa pole kwa kumpoteza kiongozi wetu Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Pia nichukue nafasi hii kusema pamoja na kwamba tuko kwenye majonzi makubwa lakini tutaendelea kumuenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ambayo ameifanya na ametuachia. Pia najua kazi sasa inaendelezwa na Mheshimiwa Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa hiyo, nichukue nafasi hii pia kumpongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee masuala matatu. Kwanza, nitaanza na vitambulisho vya wazee wetu ambavyo tumewapa kwamba wanapofika hospitalini waweze kuhudumiwa kwa sababu wenyewe ni wazee na wana miaka 60. Hivi vitambulisho kwa sasa havifanyi kazi, wazee wengi wamekuwa wakienda katika hospitali mbalimbali, siyo tu kwenye Mkoa wangu au Jimbo langu, sehemu mbalimbali wanaambiwa kwamba dawa hakuna.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka niiombe Serikali kwa sababu hii imekuwa ni changamoto sisi Wabunge tunapoenda kufanya mikutano sehemu mbalimbali tunakutana na changamoto hizi, wazee wanalalamika kwamba wana vitambulisho lakini hawahudumiwi. Kwa hiyo, naomba niiombe Serikali kwamba kama inaweza kusitisha hivi vitambulisho au inaweza kuwapa hivi vitambulisho na ikawapa waweze kupewa dawa basi ifanye hivyo kwa sababu hivi vitambulisho vimekuwa tu kama picha yaani hawawezi kuvitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo linafanana na hilo ni kuhusiana na akina mama wajawazito wanapokuwa wanaenda hospitalini kwa ajili ya kupimwa au kufanyiwa huduma mbalimbali hawapati zile huduma, wengi wao wanaambiwa watoe pesa. Kwa hiyo, naiomba Serikali iweze kuliangalia suala hili ni kwa nini jambo hili linatokea.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka niongelee, ni kuhusiana na issue ya fidia mbalimbali kwenye Majimbo yetu ambapo wananchi wametoa maeneo yao kwa sababu ya kuiachia Serikali ili iweze kupitisha miradi. Katika miaka yangu mitano kuanzia 2015 mpaka 2020, nimekuwa ninaongelea jambo moja la fidia ya wakazi wa Kipunguni, Kata ya Kipawa ambao wameiachia Serikali Uwanja wa Airport. Leo ni miaka 24 wakazi hao hawajalipwa pesa zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017 wakati Mheshimiwa Naibu Waziri akiwa Mheshimiwa Kwandikwa aliongea hapo kwamba kuna bajeti imepangwa kwa ajili ya kuwapa wale wananchi fidia yao lakini haijawahi kutoka mpaka leo. Hawa wananchi wametoa maeneo yao kwa miaka 24 na mpaka sasa hivi maeneo yao mengine yapo tu hawawezi kuyaendeleza, hawawezi kufanya kitu chochote cha wenyewe kujipatia kipato, nyumba zao tayari Airport wameshakuja kuweka mawe yakisemekana kwamba hilo ni eneo la Airport, hawa wakazi kwa kipindi cha miaka 24 wako tu wamekaa hawaelewi kinachoendelea.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naiomba Serikali itoe tamko kama hawa wakatizi waendelee na shughuli zao katika hizo nyumba au katika hilo eneo, hiyo fidia haitalipwa ili wajue waendelee na mambo yao. Kwa sababu katika kipindi cha miaka 24, ukipita hilo eneo kwanza huduma za kijamii zenyewe, hazipo. Barabara ni mbovu, halafu wengine hawawezi kuziendeleza nyumba zao.

Mheshimiwa Spika, kama unavyojua, mtu akiwa na eneo lake; shamba lake au nyumba, kama hana pesa, anaweza akachukua leseni yake ya makazi au hati akaenda kukopa, lakini wale hawawezi. Wakienda benki yoyote wanaambiwa kwamba hilo eneo ni la Airport, lakini pia Serikali kwa muda wa kipindi cha miaka mitano ambayo mimi nimo humu Bungeni na kila mwaka nilikuwa nauliza maswali na katika kuchangia naulizia, hawajawahi kusema watawalipa au hawawalipi; watalichukua hilo eneo au hawalichukui. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nilikuwa naomba jibu la Serikali ili wajue kwamba wenyewe wapo pale au wanaondoka? Watalipwa au hawalipwi; ili masuala mengine yaendelee? Kwa sababu sisi Wabunge tunapokwenda huko, tunapata malalamiko mengi sana kutoka kwa hawa wananchi; na kweli kulalamika ni haki yao kwa sababu kama fidia ilifanyika 1997, mpaka leo ina maana hata hiyo kama watalipwa, watatumia sheria gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kuhusiana na mradi wa umeme ambao unapita Kinyerezi unakwenda Chalinze. Hawa watu wa Kata ya Kinyelezi Kifuru pia wamechukuliwa eneo lao sasa ni miaka minne, mpaka leo hawajalipwa. Siku zote wamekukwa wakija hapa kumwona Waziri, wamekuja kumwona Katibu, lakini pesa hazilipwi na mpaka sasa hivi tayari nimeona TANESCO wameshaanza kuweka nguzo zao.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Serikali iwalipe wananchi kwa sababu wanapotoa maeneo yao, nasi tunasema Serikali inawasaidia wananchi kiuchumi, maeneo yao hayo ndiyo yanawategemea. Kwa hiyo, Serikali iweze kuwalipa hao watu wa Kipunguni kama inawalipa. Kama haiwalipi, iseme. Serikali iwalipe watu wa Kinyerezi kwa sababu Kinyerezi nimeona tayari wameshaanza mradi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nililotaka kuongelea ni kuhusiana na issue nzima ya Mkoa wa Dar es Salaam kuhusiana na miundombinu. Sisi watu wa Dar es Salaam hatuwezi kusimama hapa tukaomba mbolea, sijui vitu gani; sisi hatulimi kitu chochote. Sisi uchumi wetu sana sana ni kuhusiana na miundombinu. Yaani wananchi wetu wakiweza kupita vizuri kwenye maeneo yao ili kwenda kwenye kazi zao na biashara zao, kwanza inawaongezea Serikali mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukubaliane, Dar es Salaam haiwezi ikalingana na mkoa wowote hata kama siyo Makao Makuu. Kwanza ndiyo inachangia pato kubwa katika nchi yet una ndiyo ina wakazi wengi. Kwa sasa hivi Dar es Salaam ina wakazi karibu milioni sita. Sasa tuna mradi unaitwa DMDP; huu mradi Hayati Mheshimiwa John Pombe Magufuli aliahidi kwamba utaanza kutekelezwa mwezi wa Tatu, lakini mpaka sasa hivi hakuna chochote kinachoendelea, tunavyofuatilia, mradi wa DMDP II bado haujatekelezwa na wala hakuna matayarisho yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nilitaka niseme, sisi wakazi wa Dar es Salaam tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, ametuwekea miradi mikubwa sana ya miundombinu, lakini bado kutokana na wingi wetu na kutokana na umuhimu wa Jiji la Dar es Salaam, bado tunahitaji huo mradi wa DMDP. Tunaiomba sana Serikali iweze kuamua, kama umekwama mahali iweze kuukwamua ili huu mradi uweze kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi Dar es Salaam mvua inanyesha. Kwa Wabunge wote wa Dar es Salaam; wa Majimbo pamoja na wa Viti Maalum hakuna mtu anaweza kurudi Dar es Salaam sasa hivi kutokana na mambo yanayoendelea. Barabara ni mbovu, zimejaa maji, mafuriko yanaendelea na wananchi wanadhani kwamba labda sisi tumekaa huku hatufuatilii kitu chochote wala hatusemei. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaomba na kwa sababu tuliahidi, tuliahidi katika kampeni na lilikuwa ndiyo jambo kubwa, wananchi waliomba kwa kusema kwamba, sisi tunaomba miundombinu. Tukaahidi kwamba tutakapopata tu nafasi, miundombinu itaanza kutekelezwa; na tulikuwa na mradi wa DMDP ambao ulianza, lakini sasa hivi haupo tena.

Mheshimiwa Spika, naomba sana, haya ambayo nimeyasema kuhusiana na fidia pamoja na mradi, naomba sana sana uweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nami nashukuru kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Ummy kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa TAMISEMI na wasaidizi wake wote. Nimekuwa hapa katika miaka yangu mitano, namjua uwezo wake na ninajua yupo sehemu sahihi. Kwa hiyo, nampongeza sana.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nichangie katika suala la TARURA. Katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 – 2025, ukurasa wa 71 - 82, Serikali imesema itajikita kuongeza fedha TARURA ili iweze kupambana na matatizo yake au kutatua matatizo yake kuhusiana na barabara.

Mheshimiwa Spika, kama walivyosema Wabunge wenzangu TARURA ni taasisi ambayo kwanza inafanya Wabunge wengi tuweze kuonekana kwamba hatufanyi kazi especially sisi Wabunge wa Mjini ambao tunatakiwa kuonekana kwamba barabara za mitaa zinatengenezwa, lakini pia barabara zingine. Kutokana na huu ufinyu wa bajeti wa TARURA na kwa sababu tumekuwa tukienda nao kila mahali, tunaahidi haya mambo na hayatokei.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hii imetufanya sisi Wabunge hasa wa mjini kuonekana kwamba hatufanyi kazi kabisa na tunakuja tu huku Bungeni kwa ajili ya kuuza sura. Sasa naomba Mheshimiwa Rais, Mama yetu Mama Samia wakati anawaapisha Makatibu, alitoa kauli alisema kwamba, Manispaa ambazo zinakusanya pesa nyingi ziweze kutenga asilimia fulani kwa ajili ya kutengeneza barabara zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Dar es Salaam, Manispaa zote zinakusanya pesa nyingi. Ukianzia na Manispaa ya Ilala, lakini cha kushangaza pamoja na kwamba Manispaa ya Ilala ndiyo tunaongoza kwa mapato, lakini bado wananchi wetu wanaotuchangia wanatembea kwenye barabara mbovu sana. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri Ummy, kwa sababu Mheshimiwa Rais wakati anatoa hii kauli nafikiri Wakurugenzi na Wataalam wetu walikuwa wameshakaa vikao vyao na wameshapanga bajeti. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Ummy aweze kulitolea kauli hili jambo la Mheshimiwa Rais kwamba Wakurugenzi watatenga vipi fedha kuhusiana na barabara zetu za mitaa.

Mheshimiwa Spika, ufinyu wa bajeti umefanya Mkoa wa Dar es Salaam kuonekana barabara zake ni mbovu sana. Mfano Jimbo langu la Segerea, katika miaka mitano TARURA wameshindwa kujenga barabara ya Airport – Karakata ambayo ina urefu wa kilometa moja na nusu. Tumekuwa tunaahidi kila mwaka lakini barabara haijengwi na lile eneo la Airport ni eneo ambalo wageni wote wanaokuja, yaani ni kama mlango wa Tanzania. Wageni wanapofika tu pale ina maana wanakutana na barabara mbovu. Kwa hiyo kama Mheshimiwa Ummy atatoa kauli hii kwa Wakurugenzi wetu ili waweze kuangalia ni sehemu gani ambayo ni vipaumbele ambavyo sisi tumeviweka kwa ajili ya kuboresha mazingira basi itakuwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, TARURA hao hao kuna barabara sasa hivi inajengwa; Barabara ya Vingunguti – Barakuda wameijenga kuanzia mwanzo mpaka katikati, wameishiwa na pesa, kwa hiyo barabara hii imefungwa. Hii inawasababishia wananchi matatizo makubwa, ina maana daladala haziwezi kupita pale, hakuna usafiri wowote ambao unaweza kupita pale na imekuwa pia ni changamoto kwetu sisi Wabunge, ina maana ukiamka tu asubuhi unakutana na hayo matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia TARURA hii hii pamoja na ukusanyaji mkubwa wa mapato wa Wilaya ya Ilala, kuna barabara ambazo za Kimanga, barabara ambayo ni kilometa mbili imejengwa kwa miaka mitano. Vile vile TARURA wameshindwa kumalizia Barabara ya Liwiti - Chang’ombe, mpaka sasa hivi haijawahi kumaliziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Ummy na najua kabisa ana uwezo huo, aweze kuitolea kauli hasa Mkurugenzi wetu wa Manispaa ya Ilala. Kwanza napenda nichukue nafasi hii kumpongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kwa kazi kubwa anayoifanya. Kwa kweli Mkurugenzi wetu ni mchapakazi, lakini pia anafanya kazi nyingi kwa ajili ya kutusaidia na tunaelewana vizuri. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Ummy atoe kauli ili sisi sasa tuweze kutengenezewa hizo barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kuliongelea ni jambo la kuhusiana na DMDP. Najua pia hii DMDP ipo TAMISEMI. Mheshimiwa Mama yetu Mama Samia alikuja katika Wilaya ya Ilala, ndiye aliyezindua kampeni na matatizo aliyoyakuta pale yalikuwa ni matatizo ya barabara. Pia kuna ahadi ambazo tumezitoa pale kuhusiana na Mradi wa DMDP naongea hivyo kwa sababu huu mradi wa DMDP kuna hati hati kwamba umefutwa. Kwa hiyo tuna ahadi pale ambayo tuliahidi na Mheshimiwa Mama Samia. Jimbo la Segerea kuna matatizo makubwa, kwanza tuna bonde la Mto Msimbazi ambalo tuliahidi kwamba ikifika mwezi Januari tutaanza kuweka kingo.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi ni mwezi Aprili kingo hazijaanzwa kuwekwa na wananchi wanaendelea kupata mafuriko na wananchi wanaendelea kuhama. Kila mwaka wanahama zaidi ya wananchi elfu arobaini katika Jimbo la Segerea, kwa sababu ya hilo bonde la Mto Msimbazi. Kwa hiyo tunaomba Serikali iweze kuamua hili jambo na kuweka hizo kingo ili wananchi waweze kama tulivyoahidi kwamba tutalitengeneza hili Bonde la Msimbazi ili wananchi waendelee kukaa lakini pia na maji yaendelee kupita. Kwa hiyo tunaomba hicho kitu kisitolewe.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni barabara zetu za DMDP ambazo tumeziahidi tukiwa na Mheshimiwa Mama Samia kwamba barabara hizi kuna wananchi kule wanasubiri na wanajua kwamba tumeahidi kuna barabara ambazo zitajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika Wilaya ya Ilala hasa huku kwetu Mheshimiwa Zungu anapenda kusema maji matitu Segerea, water table yetu ipo juu sana, kwa hiyo mvua ikinyesha kidogo hata hizi barabara ambazo tunaziwekea changarawe zinakuwa haziwezi kufanya kazi. Kwa hiyo nilikuwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Bonnah, tayari muda wako.

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia Mpango wa Maendeleo wa 2022/2023. Kabla ya hapo, naomba kuchukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya na niwaombe tu Watanzania wenzangu tuendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kawaida Rais anaanza kujiandaa kugombea miaka kumi au miaka mitano, lakini Mheshimiwa wetu, Mheshimiwa Rais hajajiandaa na amekabidhiwa nchi na nchi inakwenda vizuri. Kwa hiyo, ni jambo zuri sana la kumtia moyo pamoja na kumpongeza, hakujiandaa, lakini ameweza kufanya mambo yote ambayo yanaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nichukue nafasi hii kuipongeza Wizara ya Ujenzi kwa kitendo ambacho kinaendelea kwenye jimbo langu, ambapo wanafanya tathmini, lakini naomba, ikumbukwe kwamba, hii tathmini inayofanyika hili zoezi limechukua muda mrefu sana tangu mwaka 1997. Kwa hiyo, naomba Wizara watakapomaliza kufanya tathmini, hawa watu walipwe. Naiomba Serikali kabisa iwalipe hawa watu isije ikawafanyia tathmini halafu ikawaacha tu hivyohivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kuchangia Mpango wa Maendeleo; ukurasa wa 78, Biashara na Uwekezaji. Tukiongelea Mkoa wa Dar-es-Salaam sehemu yoyote ambako tunahitaji Serikali uchumi ukue ni lazima kuwe na usalama. Mkoa wetu wa Dar-es-Salaam kwa muda mrefu umekuwa na matukio mbalimbali, hasa matukio ya panya road na kuna sehemu mikoa mingine inawezekana ikawa na mambo hayo, lakini sisi tuna hao panya road.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali katika mpango huu wa 2022/2023, kuwe na mpango maalum ambao utakuja kuwafanya wananchi ambao wanakaa Mkoa wa Dar-es-Salaam au na majiji mengine, mfano kama Mbeya, Arusha, Mwanza, waangalie watafanya mpango gani ili kuona kwamba, hawa vijana kwa sababu, vijana wengi ambao wanashiriki kwenye haya mambo ya panya road au na wizi mwingine mbalimbali ni vijana wengi ambao hawana kazi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri aje na mpango ambao unaweza kuwasaidia vijana wetu waweze kupata kazi waachane na haya mambo ya panya road. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na Mkoa wa Dar-es-Salaam pia, hapo hapo. Mkoa wetu wa Dar-es-Salaam mwaka 2018 kwa sababu, sehemu yoyote ambayo tunahitaji uchumi ukue ni lazima tuwe na usalama. Mwaka 2018 kulikuwa kuna mchakato unaendelea kwamba, wanataka waanze sasa kuweka kamera za barabarani na wenzetu wa Zanzibar tayari wameshaweka. Hili jambo limeshapita siku nyingi, lakini leo ni 2022 hizi kamera hakuna, wala hakuna kitu chochote ambacho kinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wetu wa Dar Es Salaam kama kungekuwa na usalama wa kutosha ina maana wafanyabiashara wengi wangekuwa wanaweza kufanya biashara zao masaa 24 lakini sasa hivi ukiangalia Mkoa wa Dar es Salaam, mtu ambaye anafanya biashara yake ya M-Pesa biashara tu ya kawaida ni lazima Saa 12 awe amefunga kwa sababu usalama ni mdogo. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iingize kwenye mpango huu wa maendeleo ni jinsi gani itakuja na mpango wa usalama katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia Mkoa wa Dar es Salaam ni Mkoa ambao ni lazima utofautishwe na Mikoa mingine, kwa sababu huwezi kusema inafanana na Mkoa wa Iringa au Mkoa wa Dodoma. Dar es Salaam ndiyo unaoongezea Serikali mapato. Kipato cha Taifa kwa asilimia Themanini kinatoka Dar Es Salaam. Kwa hiyo ni lazima tunaposema Dar es Salaam ni Mkoa ambao kwanza una watu wengi na ndiyo Mkoa ambao umeongoza katika sensa kwa watu wengi. Ni Mkoa ambao una watu waliotoka sehemu mbalimbali, ukiachilia hilo ndiyo Mkoa ambao una airport kubwa ya Kimataifa, Bandari na Reli. Kwa hiyo, tunaomba katika mchakato huu wa maendeleo Mkoa wa Dar es Salaam utengenezewe page yake tofauti kutokana na unyeti wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Dar es salaam ni Mkoa ambao una mambo mengi na una biashara kubwa na wafanyabiashara wengi. Sisi hatulimi, watu wetu wanategemea kufanyabiashara ndogo ndogo, biashara kubwa pamoja na wafanyakazi. Kwa hiyo, tunapouangalia Mkoa wa Dar es Salaam tuungalie kwa mambo tofauti tusije tukauweka uwe sawa na Mkoa kama wa Mkoa wa Singida au Mkoa wa Dodoma, ni Mkoa tofauti na naomba uwe na mambo yake tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 104, umeongelea ardhi na makazi. Mkoa wa Dar Es Salaam mvua zikinyesha…

MHE. SALIM MUSSA OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. SALIM MUSSA OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kumpa taarifa Mheshimiwa mzungumzaji kwenye suala la usalama na comfortability ya Wawekezaji ndani ya Jiji la Dar es Salaam. Pia suala la fire ni tatizo kubwa sana. Dar es Salaam wanayo magari matatu tu ambayo yana umri sawa na umri wangu zaidi ya miaka 30 hadi leo. Ipo haja Serikali kuweza kuweka mkakati madhubuti wa kuweza kuongeza magari ya fire.

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante taarifa naipokea. Nilikuwa naongelea kuhusu suala la ardhi na makazi ukurasa 103 hadi 104. Mkoa wa Dar es Salaam tukienda kwenye masuala ya miundombinu labda na Mkoa wa Mbeya na Arusha. Dar es Salaam kutokana na geografia ya Mkoa wenyewe ulivyo na wingi wa watu, ukienda kwenye masuala ya makazi naomba Mheshimiwa Waziri aangalie ni jinsi gani watakuja na mkakati katika suala la miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe mwenyewe ni mkazi wa Dar es Salaam unajua kwamba hakuna Mwekezaji atakuja wakati wa masika Dar es Salaam, pale Mnazi mmoja pamejaa maji ndiyo anatoka airport mvua ambayo imenyesha saa moja, aje aseme kwamba hii ni sehemu nzuri ambayo mtu anaweza kuwekeza haiwezekani! Kwa hiyo, ni sehemu ambayo mvua ikinyesha ni taabu na isiponyesha ni taabu. Kwa hiyo, ninaomba Mheshimiwa Waziri aangalie ni jinsi gani kutakuwa na mkakati wa kuiwezesha Dar Es Salaam iweze kupendeza, hata mvua ikinyesha isionekane imenyesha na hata isiponyesha ionekane haijanyesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili linahusiana na suala la DMDP, mwaka jana hapa tulikaa tukaongea suala la DMDP ni jinsi gani Serikali inaenda kujenga Bonde la Mto Msimbazi, tukaambiwa kwamba huu mradi unaanza mwezi Machi, lakini mpaka leo huu mradi haujaanza na wala huo mpango sijajua umefikia wapi, tumeongea hapa mara nyingi tu kuhusiana na masuala ya DMDP. Kwa hiyo, mimi nataka nimwombe Mheshimiwa Waziri kwamba hili suala la DMDP na miundombinu ya Dar es Salaam asilifananishe na Mikoa mingine, kwa sababu hata hizi fedha zitakazokopwa kwa Dar es Salaam kurudishwa haitachukua muda kama Mikoa mingi ukizingatia Dar es Salaam wafanyabiashara ni wengi, pia watumiaji barabara ni wengi na magari mengi ambayo yanapita, kwa hiyo ni rahisi sana kurudisha hizi pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri amalize huo mchakato ambayo walikuwa nayo kwa ajili ya hiyo miradi ya DMDP ili Bonde la Mto Msimbazi liweze kujengwa, pia barabara za DMDP ambazo tulikuwa tumezipanga tangu mwaka jana kwamba sasa zinaenda kujengwa barabara za DMDP ziweze kujengwa, maana tangu tumeongea mpaka sasa hivi hakuna kitu chochote ambacho kinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kwa ajili ya kuiletea nchi yetu maendeleo. Pia nichukue nafasi hii kuwapongeza Wizara ya TAMISEMI kwa kazi kubwa wanayoifanya katika majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo ningependa kuongelea suala la TARURA. Kwanza nawapongeza sana TARURA kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya, hususan kwenye Jimbo la Segerea. Pamoja na pongezi hizo kwa kazi kubwa wanayoifanya TARURA Jimbo la Segerea au Wilaya ya Ilala, kuna mambo mengi au kuna barabara nyingi ambazo ningependa kwa mwaka huu TARURA waziangalie. Kuna barabara nyingi sana ambazo TARURA wamezijenga na wamebakisha vipande vidogo vidogo sana. Ukichukulia kama barabara ya Kata ya Liwiti, barabara ya Chang’ombe, wamejenga kilomita moja lakini imebaki kipande kidogo sana. Kwa hiyo, naomba kwa mwaka huu wa bajeti TARURA waweze kumaliza hicho kipande. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna kipande kingine ambacho kinapita Kisukulu, kuelekea Bonyokwa, naomba na hicho kipande kiweze kumaliziwa kwa sababu ni vipande vidogo vidogo sana. Haiwezekani kipande kama cha kilomita moja kikakaa kwa muda wa miaka mitatu yaani kuna na barabara kilomita mbili wameitengeneza ya lami, lakini kuna na barabara ndogo sana ambayo wameiacha, kwa hiyo ile barabara ya kilomita mbili ambayo wametengeneza na kuaca kipande kidogo hicho kinaondoa kabisa maana ya ile barabara waliyotengeneza. Kwa hiyo, nawaomba TARURA, hivi vipande vidogo vidogo katika Jimbo la Segerea, waweze kuvimaliza kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine nilitaka kuongelea kuhusiana na Miradi ya DMDP. Tumezungumza hapa mwaka 2021 nikiongelea Bonde la Mto Msimbazi kwamba litaanza kujengwa mwezi wa Tatu mwaka huu, lakini mpaka sasa hivi halijaanza kujengwa. Bonde la Mto Msimbazi lilikuja na barabara zake ambazo tulikuwa tumeahidiwa na wataalamu wetu kwamba litajengwa pamoja na barabara ambazo zimefuatana, nikiongelea barabara ya Segerea - Seminari ipo kwenye mradi wa Bonde la Msimbazi na pia ukichukua barabara ya Kisukulu – Maji Chumvi – Migombani, ipo kwenye Bonde la Mto Msimbazi. Mpaka sasa hivi tunavyoongea, bado hili Bonde la Mto Msimbazi halijaanza kujengwa wala hizi barabara hazijaanza kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na nimemwulizia sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa sababu ndiyo walikuwa wanapitisha huu mradi wa DMDP, mpaka sasa hivi hatujajua. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu, kwa sababu sisi tayari tulishawaahidi wananchi kwamba itakapofika mwezi wa Tatu litaanza kujengwa.

Mheshimiwa Spika, kama unavyojua, Mkoa wa Dar es Salaam mvua kidogo ikinyesha au isiponyesha Dar es Salaam, ikanyesha sehemu nyingine, yale maji yanapita kwenye Bonde la Mto Msimbazi na kwa sababu ya miundombinu chakavu iliyopo katika Jiji la Dar es Salaam, yale maji yanawafuata wananchi. Zamani tulikuwa tunasema kwamba Bonde la Mto Msimbazi watu wamejenga karibu na bonde, lakini hapana, ni kwa sababu lile bonde sasa hivi limekuwa chakavu sana, kwa hiyo, maji yanaenda kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tulikuwa tunaomba sana majibu, tutakapomaliza huu Mkutano wetu wa Bajeti, tunarudi kwa wananchi na watatuuliza, mlituahidi kwamba Bonde la Mto Msimbazi litaanza kujengwa, lakini halijaanza kujengwa mpaka sasa hivi pamoja na hizo barabara nilizozitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna barabara moja ya Banana - Kitunda – Kivule ambayo inapitisha zaidi ya magari 3,500 kwa siku. Nimeona hii barabara ni ambayo ni ya lami, sasa hivi imetengewa shilingi milioni 560 kwa ajili ya kuiwekea changarawe. Sasa utaona kwamba barabara iliyokuwa ya lami inarudishwa kwenye changarawe; na hii barabara mwaka 2021 ilitengewa shilingi milioni 400, ikatengenezwa kwa changarawe; na mwaka huu imetengewa shilingi milioni 560 inatengenezwa kwa changarawe.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri aweze kuangalia barabara zetu ambapo kuna maeneo ambayo wananchi wengi wanaishi. Mfano kama hii barabara ninayoisema, ina kilometa 12.5 na wananchi ambao wanaishi kule ni zaidi ya 300,000. Kwa hiyo, sasa ukisema kwamba unaitengea barabara shilingi milioni 560 ili iwekewe changarawe, bado hujatatua tatizo, kwa sababu baada ya hapo, mvua itakaponyesha, ina maana matatizo yataendelea. Kwa hiyo, tulikuwa tunamwomba Mheshimiwa Waziri, kwa sababu barabara hii ipo katika mradi wa DMDP, tunaomba huo mradi uweze kusainiwa mapema ili hizi barabara ziweze kujengwa. Barabara zetu… (Makofi)

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Bonnah Kamoli, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mtemvu.

T A A R I F A

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa mzungumzaji juu ya DMDP. Ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam siyo tu eneo hilo analolizungumza la nyimbo la Segerea, lakini hata kwenye Jimbo la Kibamba ahadi ilitokea kilometa 107 mwaka 2020 mbele ya Rais aliyepo sasa akiwa Makamu wa Rais kwamba zitajengwa na DMDP III lakini mpaka sasa bado kuna mtu kakalia kwa miezi minne kusaini mkataba huo. Ni kweli nakuunga mkono ili tupate majibu Mheshimiwa Waziri akija kutoa hoja.

SPIKA: Mheshimiwa Bonnah Kamoli, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hiyo. Nami nataka niongezee tu kwamba, sisi wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam tukija hapa tunaomba barabara na maji. Tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri aangalie ni jinsi gani atatuboreshea barabara zetu ambazo tunaona zinawasaidia wananchi kwa ajili ya kufanya shughuli zao za maendeleo za kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, barabara hizi tulizosema kwamba zimeingia kwenye mradi wa DMDP, ni barabara kubwa. Mfano, hiyo barabara moja ambayo inatoka Kimanga ya kilometa 3.5, obvious huwezi kuiweka kwenye TARURA, itachukua muda mrefu. Tuna barabara nyinginye ya Bonyokwa - Kimara ambayo ina kilometa 4.6, na yenyewe pia imewekwa kwenye mradi DMDP. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba hizi barabara ambapo hatuombi zote zitengenezwe lakini hizi ambazo zitawasaidia wananchi waweze kufanya shughuli zao kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine nilichokuwa nataka kuongelea, kwanza niishukuru wizara kwa kutujengea vituo vya afya Kinyerezi, Segerea pamoja na Kiwalani. Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri Jimbo la Segerea ndiyo lenye wananchi wengi Tanzania nzima. Kwa hiyo, kuwa na Kata ambayo haina hata zahanati inakuwa ni changamoto sana. Kwa sababu unakuta Kata moja; mfano, Kata ya Buguruni ina wananchi karibu 300,000, lakini hawana zahanati. Kwa hiyo, tunaomba wapate zahanati. Pia Kimanga pamoja na Kisukulu, hizi Kata zote hazina zahanati. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aje na haya majibu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia. Naomba nianze kuchangia kwenye Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba mwaka jana Serikali iliongeza bajeti ya TARURA, lakini bado kuna matatizo makubwa ya barabara. Katika Mkoa wa Dar es Salaam, kama kila siku tunavyoongea Wabunge wa Dar es Salaam, wakazi wa Dar es Salaam wanatumia sana barabara kwa sababu Mkoa wa Dar es Salaam ni mkoa wa kibiashara na watu wengi wanapofanya biashara wanatumia barabara. Kwa hiyo kwa mpango ambao unaenda nao TARURA, TARURA ni kila mara bajeti yao haitoshi na kwa sasa hivi kwa huu mpango wa kugawana fedha kwamba mfano, Mkoa wa Dar es Salaam ugawane na mkoa mwingine tuseme kama vile labda Mkoa wa Kigoma au mikoa mingine ambayo haina watu wengi.

Mheshimiwa Spika, sisi watu wa Dar es Salaam bado tunahitaji sana barabara kwa sababu wananchi wetu kazi zao nyingi zinatumia barabara na zinatokana na barabara.

Mheshimiwa Spika, ninaongea kuhusiana na barabara za Mkoa wa Dar es Salaam specially Jimbo la Segerea, bado tunahitaji barabara. Nasi watu wa Dar es Salaam hatuhitaji tena barabara za changarawe. Kwa hiyo, katika Mkoa wa Dar es Salaam, barabara hizi za TARURA tunaomba tuongezewe bajeti ili wafanyabiashara wetu waweze kufanya kazi vizuri na mapato yaweze kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ninalopenda kuongelea ni kuhusiana na mradi wa DMDP. Mradi wa DMDP Phase II mpaka sasa hivi ninavyoongea haujamalizika. Bado kuna sehemu nyingi sana zina matatizo. Mfano, Stendi ya Kinyerezi. Stendi hii imejengwa, ni nzuri, lakini haina sehemu ya kupumzikia, haina sehemu ya kusimama, yaani bado haijamalizika, na hii iko kwenye phase II. Mpaka sasa hivi mradi wa DMDP Phase II haujamalizika na hii inaifanya mpaka hii DMDP Phase III ambayo ametoka kuiongelea hapa Mbunge aliyemaliza kwamba itaanza, tuliambiwa kwamba wanaanza mwaka 2022 mwezi wa Tatu, lakini mpaka leo hizi barabara hazijaanza; ilikuwa pamoja na Bonde la Msimbazi, halijaanza.

Mheshimiwa Spika, kama alivyoongea hapa mwenzangu kwamba tunavyoenda kuwatangazia wananchi kwamba kuna miradi ambayo inategemea kuanza kwenye makazi yao halafu mradi hauanzi mpaka mwaka mmoja unapita, ni shida sana kwetu Wabunge kwenda kujielezea kwa nini huu mradi umesimama mpaka sasa hivi. Mpaka sasa hivi hatujui huu mradi utaanza lini? Tulikuwa tunaomba Mheshimiwa Waziri akija kujibu, basi atuambie huu mradi wa DMDP utaanza lini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine ninachotaka kuongelea; hili ninalotaka kulisema, siyo kwamba siungi mkono wafanyabiashara kuondolewa barabarani. Ninachokipinga mimi, tumesema sawa wafanyabiashara wanaondolewa barabarani, mfano Kariakoo na sehemu nyingine ambazo kuna watu wengi. Siku hizi kumekuwa na tabia, mtu anatoka jijini ndani kabisa huko mjini, anakuja sehemu kama Bonyokwa, anamkuta mama wa watu anajiuzia nyanya; anavunja lile banda la kuuzia nyanya, anachukua na zile nyanya. Anasema ni kwa sababu yule mama amekaa barabarani. Hiki siyo kitu kizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaunga mkono kwa maeneo ya nje, hao waliokaa barabarani kuondolewa ni sawa, kwa sababu ni pamoja na usalama wao; lakini hawa ambao wapo kwenye mitaa; mtu anakuja kumvunjia au kumwondolea mtu biashara yake sehemu ambayo hata Manispaa haijajenga barabara, hakuna kitu chochote ambacho kinahusiana na Serikali imefanya hilo jambo, ametengeneza kibanda chake yuko sehemu ya vumbi, mtu anatoka huko anakuja anamwondolea chakula chake, na biashara zake na ukiangalia ile sehemu hakuna hata gari moja linalopita. Sasa unapomwondoa pale, atapitiwa na gari gani? Kwa sababu barabara mbovu au hakuna barabara inayopita hapo, unakuja unamwondolea, huo ni unyanganyi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba kabisa TAMISEMI iangalie ni jinsi gani hawa watu wake inawaelekeza. Kwa sababu hawa watu ambao wanaitwa Mgambo wanakuwa hawana busara, kwa sababu kwa akili za kawaida umemkuta mtu, unamnyang’anya vitu vyake, halafu unavichukua unaenda navyo Manispaa, siyo vizuri. Hili jambo liishe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wafanyabiashara wote wa Kinyerezi ambao wako mtaani, mtu kaweka banda nje ya nyumba yake, wamebomolewa na hakuna kitu chochote ambacho kinafanyika. Hilo naomba watakapokuja waweze kutusaidia kwamba hawa Mgambo wavunje huko Kariakoo au sehemu nyingine ambazo kuna watu wengi, lakini huku wamama wanapojifanyia biashara, maisha yenyewe sasa hivi ni magumu, wamama wanajihangaikia, wanawafuata kule kule kwenye mitaa ya ndani kwenda kuwavunjia, siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kuongelea ni kuhusiana na tathmini ambayo inaendelea kwenye Jimbo langu la Segerea. Namwomba Mheshimiwa Waziri, hawa watu wamekaa tangu mwaka 1997, naishukuru Serikali sasa hivi inawafanyia tathmini na imepeleka daftari la uhakiki. Naomba watakapomaliza uhakiki hizi fedha ziwepo. Isije tena ikakaa miezi mingine sita.

Mheshimiwa Spika, ikikaa miezi sita, zoezi limefutika tunaanza upya. Kwa sababu sheria inasema kila baada ya miezi sita. Tangu tumeanza kufanya tathmini, sasa tuko mwezi wa Tano, bado tuna mwezi mmoja. Kwa hiyo, naiomba kabisa Wizara ya Fedha, tutakapomaliza, tuna siku 19 waende wakawalipe hawa wananchi ili waweze kuondoka. Tusije tena tukakaa miezi sita halafu ikaonekana kwamba hela hazijawa tayari. Kwa hiyo, wananchi wangu nitakuwa nao, nitawaambia tunaanza tathmini upya.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Nimesikia hiyo. (Kicheko)

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, jambo lingine ninalotaka kuongelea ni kuhusiana na walimu.

MBUNGE FULANI: Ehe!

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Tunaishukuru sana Serikali, imeweza kuleta pesa nyingi sana ajili ya kujenga madarasa na kutengeneza miundombinu ya elimu. Tulikuwa tunaomba Serikali iajiri walimu ili hiyo kasi ya kuwa na madarasa mazuri iendane na uwepo wa walimu wa kufundisha. Kama wenzangu walivyosema kwamba darasa moja anafundisha mwalimu mmoja, tutakuwa hatupati matokeo mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia madarasa yaendane na miundombinu ya walimu kwa sababu mwalimu anapokuwa anafundisha yuko kwenye darasa zuri, lakini hana ofisi nzuri ya kukaa. Naomba hizi pesa zinazoletwa ni nyingi sana, tunashukuru, lakini zinaletwa tu kwa ajili ya madarasa, hakuna ofisi za walimu. Tunaomba walimu pia wajengewe ofisi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante nashukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia mchango wangu katika Wizara ya TAMISEMI. Kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya pamoja na kutembelea katika majimbo yetu kuja kufanya ziara kwa ajili ya kuangalia changamoto ambazo ziko katika majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka Mkoa wa Dar es Salaam na ninatoka Wilaya ya Ilala ambapo majimbo yetu majimbo mawili, Jimbo la Segerea pamoja na Jimbo la Ukonga yako pembezoni mwa mji. Katika majimbo yetu haya mawili kuanzia juzi na jana hali sio nzuri na kwa sababu Mheshimiwa Waziri anaijua vizuri Dar es Salaam na yeye mwenyewe ametokea Dar es Salaam kwa kweli anakielewa ninachokiongea. Nimekuwa nikichangia hapa kwa muda wa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2020, 2021, 2022 na leo 2023 kuulizia mradi wa DMDP ambao ulikuwa utekelezwe 2021 na haya matatizo yote yanayoendelea Mkoa wa Dar es Salaam na mpaka sasa hivi unamwona Mbunge mwenzangu Jerry Slaa hayupo hapa, si kwa sababu hayuko anatembea, yuko katika Jimbo lake kuna mafuriko makubwa sana, na pia Mheshimiwa Zungu naye hayupo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam hata mvua ikinyesha Kisarawe maji wa Kisarawe yote yabakuja katika Wilaya ya Ilala especially kwenye Majimbo ya Segerea, Ukonga pamoja na Jimbo la Ilala. Na ni kwa nini haya maji yanakuja pale? ni kwa sababu kuna miundombinu mibovu; ukianzia mifereji mpaka barabara zetu ni mbovu. Kwa hiyo tulikuwa tunautegemea sana sana Mradi wa DMDP ambao tumeambiwa kila mwaka unatekelezwa, kila mwaka unatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshaongea hapa, tumeshampeleka Mheshimiwa Waziri tumemwonesha sehemu tunazotoka, hali ni mbaya sana. Kwa mfano katika Jimbo la Segerea Kata ya Buguruni, Kata ya Bunyokwa, Kata ya Vingunguti; na kwa Kata ya Vingunguti juzi wananchi pamoja na Mnyamani wananchi wameshindwa kutoka ndani, imebidi tuombe usaidizi kutoka kwa kampuni ya SGR ambao wanatengeneza barabara ili waweze kutusaidia kutoa yale maji. Hali ni mbaya; na yote hiyo sio kwa sababu yoyote ni sababu ya mifereji mibovu na michakavu ambapo kila wakati mmesema kwamba mnakuja kuturekebishia hii mifereji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana wewe ulikuja katika Jimbo letu la Segerea pia ukaenda mpaka Jimbo la Ukonga kuangalia hali ilivyo. Wananchi wetu wa Mkoa wa Dar es Salaam hakuna biashara yoyote wanayoifanya kama mvua ikinyesha. Mvua ikinyesha siku mbili, mfano kama jana na juzi, pamoja na leo nimesikia mvua inanyesha, hakuna watu wanaoenda kufanya kazi, hakuna mama ntilie anayepika chakula, hakuna bodaboda wanaofanya biashara na hawa wote wanaingiza kipato pia wanaiingizia kipato Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Mkoa wa Dar es Salaam ni mji maarufu pamoja na kwamba si makao makuu. Watu wote wanaoishi Dar es Salaam wanategemea kufanya biashara lakini pia kuna wawekezaji wanatoka sehemu mbalimbali. Kwa jana na leo mwekezaji yeyote akija pale hawezi kufanya biashara yoyote wala hawezi kutamani kuwekeza, maana yake mazingira ya miundombinu hayamvutii. Maji ni machafu, mirundikano, mifereji michafu, barabara mbovu, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba sana sana, sisi tunaomba sana sana na kwa niaba ya Wabunge wenzangu hawa ambao hawapo tunaomba Mradi wa DMDP uanze, ambao ndio mmekuwa mnatuahidi kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama huu mradi ungekuwa umeanza na Mto wetu wa Msimbazi umetengenezwa basi haya mafuriko yangekuwa hayapo. Kwa hiyo tunaomba, umetuahidi kwamba huu mradi utaanza mwezi wa sita tunaomba uanze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka niongelee ni jambo la fidia. Katika Jimbo la Segerea kuna wananchi ambao walipisha airport, ninamshukukuru Mheshimiwa Waziri pamoja na Mkurugenzi wa TAA wamelisimamia hili jambo limefikia sasa sehemu nzuri, nilichokuwa ninaomba hawa wananchi wameishafanyiwa tathmini pia pamoja na biashara zao ambazo zilikuwa zinaendelea katika hilo eneo, kama walikuwa wana wapangaji, kama walikuwa wana nini, hao watu wote wameishaondoka, tunaomba sasa Mheshimiwa Waziri hawa watu walipwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeongea hapa na Mheshimiwa Waziri kasema kwamba wameishamaliza wanachukua sasa daftari kulipeleka Wizara ya Fedha, sasa tunaomba litakapofika huko Wizara ya Fedha lisije tena likakaa, likakaa tena miezi Sita, kwa sababu sheria inasema baada ya miezi sita tunaanza upya na mtakuwa Serikali mmepata hasara kwa sababu kwenda kufanya tathimini mnawalipa watu wa ardhi, nasi ikifika baada ya miezi sita tunafuta, tunaanza upya kwa sababu vitu vinapanda na sheria inasema kila baada ya miezi sita.

Kwa hiyo, niwaombe kwamba hawa wananchi sasa wamevumilia vya kutosha, tathmini tayari mmeishafanya na imeishamalizika tunaomba ikichelewa sana mwezi ujao wawe wameishapata hela zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuongelea ni kuhusiana na Walimu especially ambao wanatoka Jimbo la Segerea. Kuna walimu wengi sana Mheshimiwa Waziri ambao wanapata likizo lakini hawalipwi malipo yao. Mfano, katika Jimbo langu la Segerea kuna karibu Walimu 150 wanadai pesa zao za likizo tangu 2015 mpaka sasa hivi hawajazipata. Sasa walimu wetu wanafanya kazi kubwa sana tunawavunja moyo, tunaomba hawa watu wapewe pesa zao za likizo ili waweze kufanya kazi zao vizuri. Kwa sababu kumuacha Mwalimu anaendelea kufanya kazi hii halafu akipata likizo hapewi pesa siyo jambo zuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri, nawapongeza sana watu wa TARURA kwa kazi kubwa wanayoifanya, lakini sasa TARURA bajeti yao imekuwa ni ndogo sana. Kwa mfano, katika Wilaya yetu ya Ilala tunaomba kabisa kwamba TARURA waongezewe bajeti, bajeti ni ndogo sana na ndiyo maana barabara zao nyingi hawawezi kutekeleza. Kwa hiyo tunaomba katika mambo ambayo yatafurahisha Mheshimiwa Waziri ni kuiongezea bajeti TARURA, tumeishasema hatuitaji barabara za changalawe tena Mjini, tunahitaji tupate barabara za lami, kwa hiyo mtakapo waongezea itakuwa ni vizuri hata kwetu sisi ili tuweze kuangalia sehemu ambazo, kama ulivyopita Mheshimiwa Waziri, kwenye Jimbo langu jiografia ya Jimbo langu ina Kata…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa muda wako umeisha.

BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante ninaomba nimalizie suala moja. Mheshimiwa Waziri jambo lingine tunaomba mthibitishe Mkurugenzi wetu ili aweze kufanya kazi akiwa comfortable. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kutoa mchango wangu katika Wizara ya Miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ya kuleta maendeleo katika nchi yetu, pia nimpongeze Waziri pamoja na Katibu Mkuu, Naibu Mawaziri wote wawili kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sasa Mheshimiwa Waziri kwamba kuna mchakato ambao unaendelea kwenye Jimbo langu ni wa kulipa fidia ya wakazi wa Kata ya Kipawa, ambao sasa hivi imefikia sehemu nzuri nafikiri kwamba wameshaenda watu wa Wizara ya Miundombinu kufanya uhakiki na ninajua watakapomalizika hawa basi itaenda Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri kwamba hili jambo sasa lifikie mwisho na ninawashukuru sana katika miaka yote karibu miaka 30, ambayo mmeweza sasa hivi kufanya tathmini lakini pia na kuhakikishia kwamba hawa watu mnawalipa kwa mwaka huu na tunamshukuru pia Mheshimiwa Rais. Wakazi wa Kata ya Kipawa Jimbo la Segerea wamenituma nije nitoe shukrani zao, kwanza kwa kuwafanyia tathmini mpya lakini kwa kuwaonesha kwamba watalipwa mwaka huu, nimshukuru sana Mkurugenzi wa Airport. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo naomba pia nishukuru kwa mara ya kwanza barabara yetu ya Kinyerezi – Bonyokwa – Kimara sasa ipo kwenye bajeti. Barabara hii kwa muda mrefu sana tumeiongelea ambayo ni kilometa sita point ngapi hizo. Tumeiongelea kwa muda mrefu sana kwamba tunaomba hii barabara ijengwe, hii barabara ni muhimu sana, kwa sababu hii barabara imepita kwenye Majimbo matatu na hii barabara ikijengwa Mheshimiwa Waziri itatusaidia sana wakazi wa Segerea lakini pia Jimbo la Ubungo lakini pia Jimbo la Kibamba, kwa hiyo tunaomba kama mlivyoiweka kwenye bajeti tunaomba basi wananchi wetu waweze kuiona imeanza kujengwa ili na sisi sasa tujue kwamba tatizo la miundombinu katika haya Majimbo yetu matatu yanakwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri nililokuwa nataka kuongelea ni kuhusiana na madereva taxi wa airport terminal two. Terminal two pale kumekuwa na malalamiko mengi sana Mheshimiwa Waziri, madereva taxi wa terminal two. Jambo la kwanza wanacholalamikia ni kuhusiana na kwamba hawaruhusiwi kutoka terminal two kwenda terminal three. Kwa hiyo, tunaomba muwaruhusu waende terminal three kwa sababu baadhi ya hawa madereva taxi wa Jimbo la Segerea Mheshimiwa Waziri wengi wao wamechukua mikopo baada ya kuona terminal three inajengwa. Kwa hiyo, sasa hivi tunavyoendelea kuwazuia inawapa shida sana, tunaomba muwaruhusu na wenyewe waende terminal three waweze kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika terminal two pia Mheshimiwa Waziri tozo zimekuwa nyingi kwa hawa madereva taxi. Tozo zimekuwa nyingi wanakuwa wanalipa michango midogo midogo mingi, naomba kama itawezekana Mheshimiwa Waziri hawa watu waweze kupunguziwa hizi tozo, tozo ni nyingi sana na wanavyoendelea kuwekewa tozo nyingi, ndiyo wanafanya abiria waweze kuchukua taxi kwa bei ya ghali na wengine sasa kuchukua hizi ambazo zinaitwa Uber. Kwa hiyo, tunaomba sana muangalie hizo tozo pia kuangalia ni jinsi gani wanaweza wakaungana na wenzao terminal three. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri nililokuwa nataka kuongelea ni kuhusiana na barabara ya Banana – Kitunda. Mheshimiwa Waziri hii barabara ni barabara ambayo inapitisha magari 5,000 au 8,000 kwa siku. Hii ni barabara kubwa sana ni barabara ya TANROADS sasa hivi ina hali mbaya sana kwa sababu ni barabara ya lami, lami imekwisha mpaka jana Mwenyekiti wa eneo hilo anaomba grader apitishe juu ya lami kutokana na yale mashimo. Kwa hiyo, tunaomba sana hii barabara iangaliwe kwa sababu ndiyo barabara ambayo inaenda mpaka Jimbo la Ukonga tukizingatia kabisa Jimbo la Ukonga ndilo lenye wananchi wengi wanaokaa kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana hii barabara iangaliwe kwa sababu ndiyo barabara ambayo inaenda mpaka Jimbo la Ukonga, tukizingatia kabisa Jimbo la Ukonga ndilo lenye wananchi wengi wanaokaa kule. Kwa hiyo, ukifika pale, sehemu ambayo unaitwa Matembele Mheshimiwa Waziri sehemu ambayo unaweza kwenda kwa dakika mbili, inabidi uende kwa dakika 20 kunatokana na yale mashimo lakini pia kutokana na wingi wa magari. Kwa hiyo tunaomba sana mtuangalizie hii barabara kama mnaweza kuifanyia maintenance ili iweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri ni barabara ambayo ni ya Tabata - Kinyerezi. Hii barabara pia inapitisha magari mengi na ni barabara ya TANROADS, imezidiwa. Nimeona mmeweka ‘X’ kwenye baadhi ya nyumba, lakini sasa hatujajua wale wananchi wanauliza, kwamba pamoja na kuwekewa ‘X’ huu mradi utaanza lini? Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba mnapofikia kuwawekea wananchi ‘X’ tuwe tayari tumeshajua wanaondoka lini na wanalipwa lini? Kwa sababu mnapowawekea ‘X’ wanaanza sasa yale maswali, kwamba tumeshawekewa ‘X’, miradi yao mingi haiwezi kuendelea, wanaanza kujiandaa kwa kuondoka, lakini pia hamjui mkishaweka ‘X’ mnakuwa mmeshaondoka. Kwa hiyo, tunaomba sana sana, hii ‘X’ ikiwekwa tuwe tumeshakaa na wananchi tunawaambia mradi unaanza lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la mwisho ninalotaka kuliongelea ni kuhusiana na SGR. Namshukuru sana na ninawapongeza sana SGR kwa kazi kubwa wanayooifanya. SGR imepita kwenye jimbo langu, kwenye kata tatu; Kipawa, Vingunguti, Mnyamani, na Buguruni. Hizi sehemu zote Mheshimiwa Waziri zimezibwa. Hatukatai maendeleo, tunakubali kwamba maendeleo yawepo na yakija maendeleo ni lazima tupate usumbufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi kubwa ambayo wanaifanya SGR, nawapongeza sana na nampongeza Mkurugenzi, lakini tunaomba katika hizi kata tatu tupatiwe sehemu moja ya kupitia. Kwa sababu sasa hivi mtu kama anatoka Mbezi inabidi azunguke aende mpaka Ukonga ndiyo aende Airport. Kwa hiyo, tungepatiwa sehemu moja ya kupita kwa sababu hii miradi, wataalam walisema itaisha baada ya miezi sita, lakini tulienda pale tukazunguka, miezi sita mpaka sasa hivi imeisha na mpaka sasa hivi watu bado wanaendelea kupata usumbufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, wanafunzi wameshajitengenezea sehemu nyingine za hatari za kupita. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba Mkurugenzi pamoja na Ma-engineer wa SGR waangalie katika hizi kata tatu, ni sehemu gani wanaweza wakaitengeneza kwa haraka ili sisi tuweze kupita hiyo sehemu? Kwa sababu sehemu zote zimezibwa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu katika hii Wizara ya Ardhi. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, kwanza kwa kuondoa riba na kwa kuwaongezea wananchi muda wa kuweza kulipa. Pia nampongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Makatibu pamoja na Watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache tu ambayo nataka nichangie yanayohusu jimboni kwangu. Kwanza kuna jambo moja ambalo linaendelea jimboni kwangu kuhusiana na urasimishaji. Mheshimiwa Waziri jambo la urasimishaji tunalipenda kwa sababu linawasaidia wananchi ili waweze kupata hati. Sasa jambo hili limekuwa kero. Tumefanya mikutano na hizi kampuni ambazo zinakuja kwa wananchi katika kata nyingi sana, ukianzia Kata ya Minazi Mirefu, Kata ya Tabata, Kinyerezi, Kiwalani, mpaka leo hawa wananchi hawajapata hati zao. Hizo kampuni ambazo zinakuja kwa ajili ya urasimishaji zinachukua muda mrefu sana, halafu tunapokuwa tunaenda kufanya mikutano yetu, kwa mfano, kama Diwani au Mbunge anafanya mkutano, basi kero kubwa za wananchi kwa Jimbo la Segerea ni kuhusiana na kampuni za urasimishaji. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba sana Mheshimiwa Waziri hili jambo ulifuatilie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo linaendelea katika Jimbo la Segerea ni kuhusiana na uwanja. Mheshimiwa Waziri unajua na ninafikiri nilikwambia, tuna uwanja wetu ambao ulikuwa unaitwa kwa jina la maarufu Uwanja wa Sigara. Huu ni uwanja ambao uko Kata ya Liwiti. Huu uwanja umekuwa unatumiwa na wanafunzi na watu mbalimbali katika mambo mbalimbali ya michezo kufanya mazoezi na watu wengine ambao wana shughuli mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2020 kuna mtu alijitokeza akasema kwamba hili eneo ni lake, lakini kipindi kile tuliweza kuzuia na akaondoka, lakini sasa Mheshimiwa Waziri kwa kipindi hiki mwezi wa Nne ambapo tuko hapa Bungeni, nasikia tayari huyo mtu ameishajitokeza katika Uwanja wa Sigara, na hivi ninavyokwambia, ameshapeleka grader limesafisha kabisa ule uwanja. Kwa hiyo, sehemu ambazo zilikuwa zinatumika kwa ajili ya mambo ya michezo na mazoezi mbalimbali, huu uwanja sasa hivi haupo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kata ya Liwiti pamoja na Jimbo la Segerea walitaka wajue, hili eneo lilikuwa ni eneo la wazi, inakuaje mtu anajitokeza na anasema ni eneo lake na anapeleka grader linaanza kufanya kazi na vyombo na Serikali ipo tu inaangalia. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri utusaidie tuweze kupata majibu ili pia tuweze kuwaambia wananchi, ni jambo gani linaendelea katika Uwanja wa Sigara? Kwa sababu ni wengi ambao tunalalamika na huu uwanja una kazi nyingi za kiserikali zinafanyika hapo. Kwa sasa hivi hatuwezi kufanya kitu chochote kwa sababu tayari ameshaenda pale, amepeleka grader, ameshaanza kuziba, hakuna kitu chochote ambacho kinaendelea. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri ufuatilie jambo hilo, utakapokuja kufanya wind-up uweze kutuelezea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwenye Kata hiyo hiyo ya Liwiti, kuna wananchi karibu 1,800 Mtaa wa Amani Ladwa. Hawa wananchi 1,800 Mheshimiwa Waziri wote wana leseni za makazi, lakini wote wamewekewa huduma za jamii kwa maana ya maji, umeme na vitu vingine ambavyo vinahusisha huduma ya jamii. Jambo la kushangaza na la kusikitisha, ametokea mwananchi anasema kwamba lile eneo lote ni la kwake. Kwa hiyo, anahitaji wananchi wahame au wasipohama waweze kumlipa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawa wamekaa kwenye hiyo sehemu kwa miaka 40, kuna watu wapo wanasomesha watoto, kuna watu wanasomesha wajukuu, imekuwaje siku zote hizo huyo mtu asijitokeze, mpaka leo baada ya miaka 40 ndiyo aje kusema hilo ni eneo lake? Tulikuwa tunaomba Waziri uingilie huu mgogoro ili watu waweze kujua ni jambo gani linaendelea katika huu mtaa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kusema kwamba hivi anavunja sheria, kwa sababu hatujajua. Kwa sababu huwezi kujua, watu wamekaa miaka 40 na wanalipa leseni, wana huduma zote za kijamii. Kama watu wangejua kwamba hili eneo siyo lao au Serikali ingekuwa inajua kwamba hili siyo eneo la hawa watu, ina maana hata hizo huduma za kijamii wasingewekewa, na ni watu 1,800 Mheshimiwa Waziri na huyu ni mtu mmoja. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iweze kuingilia kati, tuangalie ni jinsi gani mnaweza mkawakomboa hawa wananchi. Kwa sababu hakuna mtu ambaye anaweza kuwahamisha wananchi 1,800 yeye akiwa peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kwenye Jimbo la Segerea nina kata kama nne ambazo ndiyo zenye makazi holela. Amezungumzia hapo mjumbe aliyemaliza. Tuna Kata ya Vingunguti, tuna Kata ya Buguruni, na Kata ya Mnyamani. Kwa hiyo, tulikuwa tunasubiri huo mradi ambao mna-plan kwenye miji ili nasi tuweze kufaidika. Kama unavyojua, Vingunguti, Buguruni pamoja na Mnyamani ni karibu sana na mjini. Kwa hiyo, tunaomba katika huo mradi ambao mtauanza wa ku-plan miji, basi na hizi kata zetu tatu mweze kuziingiza ili wananchi hawa nao waweze kufaidika, kwa sababu wanakaa mjini, pamoja na kwamba sasa hivi hawana uwezo wa kujenga nyumba zao, lakini najua Serikali mnaweza mkatengeneza mradi pale, wananchi wakafaidika na Serikali ikafaidika zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, kwa hiyo, naomba masuala yangu matatu yaweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi hii na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu kabisa, Wizara ya Uchukuzi na Miundombinu na mambo yote ambayo yanahusu maendeleo na maisha ya binadamu.

Mheshimiwa Spika, napenda nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan, lakini pia niwapongeze Mawaziri wote kwa kufanya kazi nzuri pamoja na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, watendaji wa Serikali nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kuchangia mchango wangu katika Wizara hii nilipenda niongelee jambo moja kuhusiana na fedha ambazo zilipelekwa kwenye bajeti ya TARURA ya mwaka 2021/2022. Kama unavyojua kwamba hizi fedha tuliziomba mwaka 2021 na Mheshimiwa Rais akatusikiliza Wabunge akaongeza bajeti ili tuweze kutengeneza barabara zetu, kwa sababu Mheshimiwa Rais alivyokuwa anafanya ziara aligundua kwamba sehemu nyingi/mikoa mingi/majimbo mengi barabara ni mbovu ndio maana akaongeza ile bajeti kwa watu wa TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mimi nilipata taarifa kutoka kwa watendaji wangu wa TARURA kwamba fedha ambazo tulikuwa tunazitegemea kwenye Jimbo letu shilingi milioni 800 sasa zinaelekezwa kwenye Postikodi. Namshukuru Mheshimiwa Nape Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia alilisemea juzi kwamba hizo fedha zirudishwe kwenye miradi ya TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nilikuwa ninaomba Mheshimiwa Waziri husika wa TAMISEMI alisemee hili jambo kwa sababu kuna majimbo mengine hizi fedha zimeshachukuliwa na kuna majimbo mengine tayari zimeshawekewa mipango ya kwenda kwenye hizo Positikodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba sana sana hili jambo lisifanyike, wananchi wetu tumewaahidi, tumeshafanya mipango mingi na tumeshakaa mikutano mingi na wananchi kwa ajili ya hizi fedha. Mfano kwenye Jimbo langu nimeshakaa kwa ajili ya hizi fedha ambazo ninazisubiri shilingi milioni 800 na Kata ya Segerea Machimbo zinakwenda kufanya kazi hii. Kwa hiyo, zikitolewa itaonekana kama mimi Mbunge nimezungumza mambo ya uongo. (Makofi)

Lakini jambo lingine ambalo nilikuwa nataka kushauri mambo ambayo tumeyapanga hapa na tukayapangia bajeti, wataalam wanapata wapi nguvu ya kutoa bajeti ambayo sisi tumepanga na tumepitisha Bungeni na kuelekeza kwenye miradi mingine? Hii inakuwa sio sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu sisi tunaongea na wananchi direct ndio wametupa vipaumbele vyake na tukishaongea hapa tukipitisha tunategemea wenyewe wananchi wafanye kazi kwa ushirikiano na sisi. Sasa wenyewe wanapokaa huko na kupanga mipango yao bila kutuhusisha sisi inakuwa sio sawa. Naomba hilo lifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili sasa naanza mchango wangu kwenye Wizara hii. Katika Jimbo langu la Segerea, eneo la Airport kuna wakazi wangu 1,800 tangu mwaka 1997 hawa watu wamehamishwa, wameambiwa kwamba wanatakiwa wahame hilo eneo. Wengine wamefanyiwa tathmini, wengine hawajafanyiwa tathmini mpaka hii leo, nimekuwa nikiongea hapa kwa kipindi chote nikisimama hapa kuwaongelea hawa wakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo hilo sasa Kipawa, Mtaa wa Kipunguni hakuna maendeleo yoyote. Kwanza tunavyopanga mipango yetu ya kupeleka barabara au kupeleka maji lile eneo wanaliruka wanasema hili eneo hawa wananchi wake watahama, kwa hiyo, hakuna haja ya kupeleka hii mipango ya maendeleo.

Kwa hiyo, kwa kipindi hicho chote nilichokielezea hakuna mwananchi pale anayefanya maendeleo yoyote na kama unavyojua mtu anaweza akawa ana leseni yake ya makazi, anataka aende kuchukua mkopo hawa wananchi hawawezi kwenda kuchukua mkopo kwa sababu airport wamekwenda kuweka jiwe lao la msingi pale kuonesha kwamba hicho ni kiwanja chao na wakati hawajawalipa hawa wananchi. Kwa masikitiko kabisa hili jambo nimeliongea na mwaka jana nimeliongea, lakini Serikali halilifanyii kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi hiyo sehemu imekuwa watu wanaishi hawaelewi na kibaya zaidi wamekwenda wamewalipa watu nusu, wameacha nusu. Kwa hiyo, wale nusu waliobaki pale wanaendelea kupata shida hawawezi kufuga kuku, hawawezi kupata mkopo wowote, hawawezi kufanya kitu chochote kwa sababu hilo eneo linajulikana ni eneo la airport na wameshaweka hilo jiwe lao. Kwa hiyo wanawafanya hawa wananchi waendelee kuwa masikini sio sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nilitaka kuongelea ni kuhusiana na watendaji wetu wa TANROADS, nawapongeza wanafanya kazi nzuri, lakini kuna mahali inabidi warekebishe, yaani TANROADS wanapokuwa wanataka kuweka viraka wanatoboa barabara kuanzia mwanzo mpaka mwisho halafu wanaondoka wanakwenda wanakaa miezi mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukizingatia barabara zetu ni mbovu, halafu sisi watu wa Segerea tunatumia barabara moja, barabara ya Tabata ambayo inatoka inakwenda mpaka sehemu zingine. Sasa unapokwenda unaitoboa ile barabara halafu unaondoka, unawatafutia watu matatizo kwa sababu watembea kwa miguu wanapitia hiyo barabara, magari wanapitia hiyo barabara, lakini bodaboda pia wanapita hiyo barabara.

Kwa hiyo, tunaomba watendaji wa TANROADS waongeze speed, wanapokuwa wanaparua hizi barabara au wanazichimba wazifunike haraka.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nilitaka niongelee hao hao TANROADS, kuna barabara nyingi ambazo wenyewe ndio wanaziangalia, kwa mfano barabara ya Tabata nilikuwa ninashauri ile barabara ijengwe upya kwa sababu hii kila siku kuifanyia marekebisho ni kupoteza gharama kubwa, ile barabara imeshakuwa mbovu tunaomba ijengwe upya. (Makofi)

Lakini pia barabara yetu ya Kinyerezi – Bonyokwa – Kimara; hii barabara tangu TANROADS wameanza kuifanyia upembuzi yakinifu sasa hivi ni miaka mitatu na tulikuwa tunategemea kwamba hii barabara itaanza kujengwa sasa hivi, lakini mpaka sasa hivi na mimi nilishawahi kukuambia Waziri kwamba hii barabara ni muhimu sana. Kwa sababu ndio inayotoa watu mjini wanapitia Bonyokwa wanakwenda Kimara, kwa hiyo mkitujengea hii barabara mtakuwa mmetusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama unavyojua Mheshimiwa Waziri na Wabunge wenyewe Dar es Salaam ndio inayoingizia mapato hili Taifa asilimia 70 kwa hiyo, Dar es Salaam ikiwa ina barabara nzuri ina maana hayo mapato yataongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kitu kingine sisi watu Dar es Salaam hatuna kitu kingine tunachoomba zaidi ya barabara na maji. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Maji, tulikuwa tunalalamika maji Mkoa wa Dar es Salaam, lakini amefanya, nampongeza sana yeye pamoja na Naibu wake pamoja na Mkurugenzi, lakini kwenye masuala ya barabara yaani bado sana Mheshimiwa Waziri. Tunaomba mtuangalizie hizo barabara zetu ambazo tunazisema kila siku.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu katika hii Wizara. Nitaendelea Mheshimiwa Lucy alipoishia. Naomba niongelee suala la asilimia 10 ambalo na wenzangu wameongelea sana. Namwomba Waziri asiitoe hii asilimia 10 kwa sababu, kwa sababu inawasaidia sana akina mama, mfano Mkoa wetu wa Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Dar es Salaam asilimia 90 ya watu wanaoishi Mkoa wa Dar es Salaam ni wafanyabiashara. Kama unavyojua, asilimia nne inaenda kwa akina mama, asilimia nne inaenda kwa vijana na asilimia mbili kwa walemavu. Asilimia nne inayoenda kwa vijana ni hawa vijana ambao wamemaliza vyuo na hawana kazi. Sasa tutakapowaondolea hii asilimia nne itakuwa kwamba tumewaumiza sana. Kuna vijana wengi ambao wanafaidika kutokana na hii asilimia nne ambayo wanaipata kutoka kwenye Manispaa zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, akina mama wengi sana ambao wanaendesha familia zao ni kutokana na hii asilimia 10 ambayo inapatikana kwenye Manispaa zetu. Nami nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala pamoja na Afisa Maendeleo Francisca Makoye, wanafanya kazi kubwa kuangalia Wilaya ya Ilala akina mama wanapata fedha hii asilimia 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia tu katika Jimbo langu la Segerea, katika mwaka ambao umepita tu, watu ambao wamekopeshwa kutokana na hii asilimia 10 wamekopeshwa Shilingi bilioni 4.6 kwa mwaka mmoja. Kwa hiyo, tunaomba hii fedha isitolewe, inasaidia kuendesha maisha ya watu na pia inawatengenezea vijana ajira. Tuna vijana wengi ambao wamemaliza vyuo vikuu hawana ajira, na tumekuwa tukiwaomba kwamba mtu anayetafuta kazi, wakati anaendelea kutafuta kazi basi wajiunge vikundi waende kutafuta mikopo Manispaa. Mkisema kwamba muitoe hii asilimia 10 ikabaki hiyo ambayo mnaipeleka kwenye miundombinu, mtakuwa mmewaumiza sana vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuliongea ni suala la miundombinu hususan mradi wa DMDP. Tumeshakuja kwako Waziri Dkt. Mwigulu tukiongelea mradi wa DMDP. Mkoa wa Dar es Salaam tunataka huko mbele uwe ni Mji wa biashara. Haiwezekani tukawa na mkoa ambao ni wa kibiashara lakini miundombinu yake mibovu. Kila nikisimama hapa huwa naongelea suala la DMDP na miundombinu. Miundombinu ya Mkoa wa Dar es Salaam, ikinyesha mvua dakika 10, Dar es Salaam nzima inasimama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia, asilimia 70 ya mapato ya Tanzania yanapatikana Dar es Salaam. Sasa ni kwa nini Wizara ya Miundombinu pamoja na Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu huu mradi wa DMDP bado haujaanza? Ndiyo mradi ambao tunautegemea sana na ndiyo unaoweza kutuokoa. Haiwezekani Mji wa biashara ukaonekana una miundombinu mibovu. Hata sasa hivi ukishuka pale Segerea Kata ya Kipawa, kitu cha kwanza kuona ni barabara mbovu. Tunahitaji tupate wawekezaji kutoka nje. Tutapataje wawekezaji na barabara hizo mbovu? Tumekaa sana na Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu tukiomba huu mradi uanze, tukaambiwa kwamba huu mradi utaanza mwezi wa Tatu, leo tuko mwezi wa Sita. Ameongea pale mwana-Dar es Salaam mwenzangu, mpaka sasa hivi hatujui huu mradi unaanza lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni mradi wa Mto Msimbazi. Mradi huu ilikuwa uanze mwezi wa Tatu mwaka huu 2022, wakasema tayari wameshapeleka Wakandarasi wako wanafanya designing na mambo mengine ya kitaalam, lakini mpaka sasa hivi hatujapata taarifa ni lini huu mradi wa Mto Msimbazi unaanza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua, Mkoa wa Dar es Salaam mvua inanyesha saa yoyote, na kutokana na miundombinu mibovu maji yanaenda kwenye nyumba za watu. Kwa hiyo, nilitaka nijue, ni lini mradi wa Mto Msimbazi utaanza? Kwa sababu kuna nyumba nyingi sana zimeondoka kutokana na huu Mto Msimbazi. Kama ninavyochangia siku zote, ni kwamba, Mto Msimbazi au maji yanayoingia kwenye nyumba za wananchi siyo kwa sababu wananchi wameufuata Mto Msimbazi, ni kutokana na miundombinu mibovu, na ule Mto kutokana na kutokufanyiwa matengenezo au marekebisho; ule mto umepanuka na mvua kidogo tu ikinyesha unaingia kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tulikuwa tunaomba, mliahidi mwaka 2021 kwamba mtaanza kujenga mwezi wa Tatu, umeshafika, na hakuna kinachoendelea. Mpaka sasa hivi sijajua ni kitu gani kinaendelea kutokana na huu Mto Msimbazi pamoja na mradi wa DMDP. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya masuala ya miundombinu ya Mkoa wa Dar es Salaam ni muhimu sana, kwa sababu sisi tunavyotoka hapa, tunaenda kuwaahidi wananchi kwamba kuna hiki kitatengenezwa na hiki kitatengenezwa, lakini tukirudi hapa, kinaendelea kitu kinaitwa mchakato; tukitoka mchakato, tunaingia process. Hivi vitu haviishi! Watu wanasema kwamba Dar es Salaam inajengwa sana barabara, nataka niwakumbushe, Dar es Salaam ndiyo inayokusanya mapato asilimia 70 ya hili Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutakapopata barabara nzuri, na wafanyabiashara wetu watakapofanya kazi vizuri, ndiyo na fedha zitakapopatikana ili kwenda kujenga sehemu nyingine. Kwa hiyo, tunaomba Dar es Salaam Mheshimiwa Waziri aiangalie kwa macho mawili, kwa sababu, ndiyo Mji wa wafanyabiashara. Kama nilivyosema, asilimia 90 ya wakazi wa Dar es Salaam ni wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nililokuwa nataka kuongelea ni kuhusiana na fidia ya wananchi. Leo siongelei tu fidia ya Kata ya Kipawa, kuna fidia mbalimbali. Unapoenda kuchukua sehemu ya mtu ambaye alikuwa amejenga nyumba yake, ardhi yake, unaichukua, unakaa nayo kwa kipindi cha miaka 10 bila kumlipa yule mtu, unamletea umasikini. Tuna sehemu nyingi ambazo Serikali imechukua na imewaahidi wananchi itawalipa, mmeweka miundombinu yenu, wananchi wanashindwa kufanya kazi, inabaki wananchi wanaendelea kudai. Yaani wananchi wanatoka Dar es Salaam, wanakuja Dodoma. Sasa hii Serikali ni kuwatia umasikini wananchi. Tunaomba Mheshimiwa Waziri hii tabia muache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnataka kuchukua eneo la mtu, basi mpeni fedha ili yeye aondoke na ninyi mchukue ile sehemu. Kama mlivyofanya kwenye Kata ya Kipawa Airport, mpaka sasa hivi, tangu mwaka 1997 hamjawalipa wale wananchi. Halafu pia mkaenda mkaweka na jiwe lenu la msingi, yaani kuonesha kwamba ninyi mmeshaichukua ile ardhi kabla hamjawalipa wale wananchi. Wale watu wameendelea kuteseka. (Makofi)

Mheshi,iwa Mwenyekiti, sasa juzi nimeuliza swali, Mheshimiwa Waziri akasema kwamba wale wananchi wanafanyiwa tathmini upya. Nami nimefurahi kwa sababu wanafanyiwa tathmini upya, na wakasema kwamba wameshapeleka barua Jiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, last week nimekwenda Dar es Salaam, hakuna barua yoyote ambayo imekwenda Jiji. Kwa hiyo, ninachokiomba Mheshimiwa Waziri utakaposimama, nilikuwa naomba Waziri husika aweze kuniambia hiyo barua ya wananchi wa Kata ya Kipawa Mtaa wa Kipunguni imepelekwa wapi, ili hao wananchi waweze kujua wanaanza lini kulipwa? (Makofi)

(Hapa kengele iliia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni jambo la muhimu sana. Jambo lingine la kuongelea ni kuhusiana na wafanyabiashara wa Mkoa wa Dar es Salaam.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kamoli, kengele ya pili ilikuwa imeshalia.

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)