Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Hawa Subira Mwaifunga (4 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama na kuchangia katika Wizara hii ya Viwanda na Biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu, mimi ni mmoja kati ya Wajumbe wa Kamati hii. Nitakayoyazungumza ndiyo ambayo tumekutana nayo na ndiyo yaliyopo. Mheshimiwa Waziri hotuba yake ni nzuri sana ukiisoma, lakini uhalisia uliomo humu haumo, kwa sababu ukienda kule uraiani, kule kwenye viwanda kuangalia uhalisia, haupo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeingia ubia na viwanda tofauti tofauti, lakini Serikali haiangalii hivi viwanda vinafanyaje majukumu yake na mwisho wa siku tunajikuta kila siku tunapoteza mapato, kila siku tutapoteza wawekezaji kwa kudhani kwamba tunaweza kufanya miujiza hii nchi iendelee kuwa ya viwanda, hakuna! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya nchi hii inatakiwa kwanza ilinde viwanda tulivyonavyo. Kabla hatujasema tunakwenda kutengeneza viwanda vingine ama kuanzisha viwanda vingine, vilindwe hivi vichache vilivyopo ambavyo vinazalisha kwa chini ya asilimia 50. Viwanda vinazalisha chini ya asilimia 50, leo tunafikiria tutengeneze viwanda vingine eti Tanzania iende kuwa nchi ya viwanda, wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vipo, lakini wafanyabiashara wenye viwanda wana matatizo mengi kweli kweli! Naishauri Serikali, Mheshimiwa Waziri, narudia tena, waendelee kukaa na wafanyabiashara wenye viwanda, wasikilizeni hoja zao, matatizo yao ili hawa basi, waliopo hapa leo waweze kuwa mabalozi wa wawekezaji wengine ambao tunawategemea waje hapa. Hatuwezi kutegemea kuleta wawekezaji wengine, wakati hawa waliopo wana matatizo lukuki ambayo yanawakabili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima kwanza tutoe haya tuliyonayo hapa, tuyarekebishe, hawa wafanyabiashara leo watakuwa mabalozi wa kwenda kututangaza vizuri nchi ya Tanzania ili iweze kuwa nchi ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa, tumekwenda kama Kamati kwenye Kiwanda cha TANALEC, tumekuta transformer zaidi ya 2000 zinatengenezwa zinakwenda Kenya. Tanzania tunaagiza transformer kutoka India, transformer 200, Mkoa wa Katavi zimelipuka baada ya kuwashwa tu! Halafu TANESCO wanawaomba TANALEC wawatengenezee zile transformer ambapo TANALEC wamegoma! Nasi tukawaambia, haiwezekani, wapeleke huko huko walikonunua transfomer hizo zitengenezwe ndiyo wazirudishe hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hili suala wanasema sijui Sheria ya Manunuzi; sidhani kama Sheria ni Msahafu! Sheria zinabadilika! Hebu Waheshimiwa Wabunge tusaidiane basi kuangalia hizi sheria wapi ni mbaya, wapi zinatatiza ili wafanyabiashara waweze kufanya biashara zao wakiwa huru, wasifungwe na hizi sheria ambazo zinawatatiza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kiwanda cha Nondo Tanzania, wanazalisha nondo nyingi kweli kweli, lakini hawana masoko! Miradi ya Serikali inakuja mikubwa mikubwa, nondo zinaagizwa kutoka nje! Tunafanya nini? Tunasema nchi ya viwanda, viwanda gani kama hivi vilivyopo havifanyiwi kazi! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kila siku kwenye viwanda watu wanaondoa wafanyakazi kwa sababu hakuna biashara! Hawa vijana waende wapi? Matokeo yake ndiyo tunakabwa kila kukicha kwa sababu vijana hawana ajira na ajira nyingi tunategemea zitoke kwenye viwanda, leo viwanda vinafungwa, hawa vijana waende wapi? Akinamama waende wapi? Hizi panya-road zitakwisha lini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, kama kweli Serikali ina dhamira ya dhati ya kutaka nchi hii iwe ni nchi ya viwanda, iende kwenye huo mfumo ambao mnasema ni wa kati, yaani watu wetu wawe na maisha ya kawaida, basi ni lazima tuboreshe viwanda nyetu vya ndani ili viwanda hivi vikifanya vizuri wawekezaji watakuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nikiiangalia bajeti hii ya Serikali, TIC (Tanzania Investment Center) hawana bajeti zaidi ya mshahara. Wanafanyaje majukumu yao? Wataletaje hao wawekezaji? TBS, mamlaka nzito, kubwa inafanya kazi kubwa; ukiangalia, hawana fedha zaidi ya mshahara. Tunafanyaje mambo haya ndugu zangu? Tutafika kweli?
Mheshimiwa Naibu Spika, bado tunazungumza suala la EPZ; kwanza hii EPZ nafikiri sisi Wabunge hapa ambao tunaelewa ndiyo tunafahamu EPZ ni nini. Huko kwetu watu hawaelewi chochote. Unapowaambia habari ya EPZ, hawakuelewi! Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu ya uraia, angalau hata tunapokwenda kuomba maeneo, Watanzania wawe wanajua kitu gani ambacho kinaombewa haya maeneo ili wasiwe wagumu kutoa maeneo yao yaweze kuwekezwa hivi viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia, nenda EPZ leo, hakuna chochote kinachonunuliwa kutoka Tanzania, hakuna! Nimeuliza na nikamwuliza hata Mtendaji Mkuu pale, kwa nini hakuna chochote kinachonunuliwa hapa? Tukaambiwa tunazalisha chini ya kiwango.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, hadi vifungo ambavyo wanatengenezea mashati, suruali, wanasema tunaagiza nje! Nikauliza, tunanufaika na nini hapa kama Watanzania?
Mheshimiwa Naibu Spika, wako vijana na wanawake wamewekwa pale, ukiuliza mshahara wao, utalia! Je, hawa watu baada ya kuondoka, wanatuachia nini? Kuna teknolojia yoyote Watanzania ambayo tutabaki nayo ili kesho na kesho kutwa watoto wetu waweze kuikuta hiyo teknolojia, waweze kufaidika nayo? Hakuna! Wamejaa wenyewe pale, wako wenyewe tu. Mheshimiwa Waziri unajua, tunaomba sana Serikali ihakikishe inawasaidia Watanzania kuelewa na kufahamu kabla hatujafanya maamuzi. Maamuzi tunayafanya juu, lakini huko chini Watanzania hawana taarifa nayo! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo kuna deni kubwa! Deni la shilingi bilioni 60 limezaa shilingi bilioni 190! Mheshimiwa Waziri ukija hapa kumaliza, tuambie hizi shilingi bilioni 190.9 imekuwaje mpaka zimefikia hapa kwa mwaka mmoja, eti ni fidia! Watazitoa wapi ikiwa bajeti yenyewe ni shilingi bilioni 81? Ndugu zangu tunadanganyana hapa! Hatuna kiwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimkumbushe tu Mheshimiwa Waziri, watu wa Tabora tunahitaji viwanda, tuwekee hata hicho kimoja tu kwanza, halafu mambo mengine yatafuata wakati ukiwa unaendelea na mikakati yako mingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niiombe Serikali sasa, iangalie kwa umakini bajeti ya Wizara hii. Hii Wizara ni mtambuka; ni Wizara ambayo inaingiza vitu vingi sana ambavyo vipo. Hebu basi Serikali ibadilike na ione uwezekano wa kuiangalia bajeti ya Wizara hii ili kweli tuweze kufika kwenye nchi ya viwanda kama tunavyofikiria. Kama tutaendelea kusuasua, mipango ikawa mingi, mikakati mingi, fedha hakuna, haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba basi sasa ifike mahali tuamue, kama tunataka kutengeneza viwanda, tuamue tunaanza na nini? Haya mambo leo kuna hiki, kuna hiki, kuna hiki kwa bajeti ya shilingi bilioni 41 ambayo ni ya maendeleo, tunawadanganya Watanzania, hatutafika. Tunasema leo, tunaishauri Serikali leo, lakini mwisho wa siku haya maneno yataendelea kuwepo kwa sababu hakuna kinachokwenda kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, yangu yalikuwa hayo. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Awali ya yote ningependa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na kuweza kusimama katika Bunge hili Tukufu ili niweze kuchangia hotuba ya Wizara ya Viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze na Mkoa wa Tabora. Siku zote mcheza kwao hutunzwa. Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Tabora siku zote wamekuwa wakipiga kelele kuhusiana na suala zima la viwanda, Mheshimiwa Waziri Mwijage anafahamu, watendaji wake wote wanafahamu na wakati wote wamekuwa wakitupa ahadi za kwamba watatuletea wawekezaji katika mkoa wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Tabora kuna Kiwanda cha Nyuzi, kiwanda hiki alipewa mwekezaji mwenye asili ya Asia. Baada ya mwekezaji huyu kupewa kiwanda kile kitu kikubwa ambacho ameweza kukifanya katika kiwanda cha nyuzi ni kuondoa mitambo yote iliyokuwepo pale kwenye kiwanda kile kuisafirisha na kuipeleka kwao na kutuachia hall pale katika kiwanda kile.

Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumza hili kwa sababu nina ushahidi nalo. Ukienda katika kiwanda kile huwezi kumkuta mfanyakazi hata mmoja zaidi ya Wahindi wawili ambao wanazunguka katika kiwanda kile.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda kile hakinufaishi vijana wa Tabora, hakinufaishi wazawa wa Tabora na wala hakinufaishi wanawake wa Mkoa wa Tabora.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa mwekezaji huyu aliamua kwenda mbali zaidi hadi kuamua kuuza majengo yaliyokuwa yanamilikiwa na kiwanda kile. Leo majengo yale yanatumiwa na Ofisi ya Uhamiaji pale juu, ukienda pale kwenye barabara ya Kilimatinde kuelekea kule njia ya kwenda Jimbo la Igalula utaona yale majengo. Juu wameweka ofisi ya uhamiaji chini yapo magofu tu ambayo haieleweki yanafanya kazi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Mheshimiwa Waziri atuambie ni lini basi watamwondoa mwekezaji huyu, watuletee mwekezaji mwenye nia thabiti ya kuwekeza katika Kiwanda cha Nyuzi? Malighafi za uwekezaji katika kiwanda kile zipo kwa sababu Tabora tunalima pamba, lakini pia majirani zetu wa Kahama, Shinyanga na maeneo mengine yanayolima pamba tunayopakana nayo yanaweza kufikisha malighafi zile kwa urahisi na kile kiwanda kikaendelea kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri kutuletea mwekezaji imeshindikana, kiwanda tunacho, mwekezaji waliomuweka hafai, tunaomba sana waende wakapitie kiwanda kile wakiangalie, tukifufue kiwanda cha nyuzi na sisi wananchi wa Mkoa wa Tabora tuweze kunufaika na rasilimali hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Tabora kuna jengo la SIDO. Kwa masikitiko makubwa sana jengo hili haijawahi kuwanufaisha hata siku moja wakazi wa Mkoa wa Tabora. Matokeo yake leo hapa ninavyozungumza, SIDO Mkoa wa Tabora wamekodisha kwa Mratibu wa Mafunzo wa VETA bwana Kaali ambaye ameweka ofisini yake pale na kutengeneza furniture na kuziuza. Hivi ndiyo yaliyokuwa malengo ya SIDO hayo ama ilikuwa ni nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaomba Mheshimiwa Waziri aje anipe majibu ya kunitosheleza ili niweze kujua kwa nini SIDO imepewa mwekezaji eti yeye ndiye anatengeneza makochi yake pale na furniture zake halafu Watanzania wa Mkoa wa Tabora, hawanufaiki na hiyo SIDO. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuzungumzia ya nyumbani kwetu, sasa naomba nizungumze mambo mengine kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara wenye viwanda, wamekuwa na malalamiko mengi siku zote na kwa bahati nzuri mimi mwenyewe ni mmoja kati ya wajumbe wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira na siku zote malalamiko haya yalipotufikia tumekuwa tukiyafikisha sehemu husika, lakini bado kumekuwa na maendeleo ya kulalamika kwa wafanyabiashara hawa kwamba mambo wanayoyahitaji kwa kweli hayatekelezwi sawasawa na Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema tunakwenda kwenye nchi ya viwanda tunakwendaje kwenye nchi ya viwanda waliopo sasa yale wanayolalamikia hayafanyiwi kazi ipasavyo? Tutegemee kulete wawekezaji wengine ili waweze kufanya kitu gani kipya ambacho kitawavutia wale watu?

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali iweze kuangalia hawa wafanyabiashara wetu wenye viwanda nchini. Sasa hivi wafanyabishara wenye viwanda nchini ndio wamekuwa kama vile wanatakiwa wafanye kila jambo. Kosa dogo mfanyabiashara anakwenda kutozwa faini badala mfanyabiashara huyu kupewa maelekezo nini afanye lakini imekuwa wakifika NEMC ni milioni 50, akifika Waziri ni milioni 30, sasa hawa watu watafanya kazi hii kwenye mazingira yapi? Tunawakatisha tamaa, hawa wafanyabiashara wanahitaji kuwekeza, lakini wanashindwa kutokana na mlolongo wa mambo ambayo yanawakera.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfanyabiashara yoyote au mwekezaji anapotoka nje lazima apate mwenyeji kutoka ndani ajue mwenzetu amefikia wapi, anafanya nini kuendeleza kiwanda chake, sasa mwisho wa siku itafika mahali ataanza kuambiwa mabaya kwanza halafu ndipo aambiwe yale yaliyo mema. Zaidi ya amani na utulivu ambayo ataambiwa ndilo litakuwa jambo la kwanza mengine ataambiwa hapo ukifanya hivi tayari, ukifanya hivi tayari, mambo yanakuwa si mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda kilichopo hapa Dodoma (Dodoma Wine) huyu mwekezaji anafanya kazi nzuri kweli kweli, mwekezaji huyu ana wateja wengi kweli kweli, lakini anashindwa kuzalisha kwa ufanisi kwa sababu kila kukicha akifungua ofisi yake watu wa Halmashauri hawa hapa, akifungua ofisi NEMC hawa hapa, akifungua ofisi watu wa mazingira hawa hapa. Wote hawa kila mmoja anakwenda kwa wakati wake na anahitaji fedha kutoka kwa huyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo tukumbuke huyu ameajiri, huyu anatakiwa kulipa kodi ya Serikali, huyu anatakiwa kufanya mambo kibao katika nchi hii, anafanyaje biashara zake? Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, hawa wawekezaji wetu wachache tulionao ambao ni waaminifu, waweze kuangaliwa mazingira yao ya kufanyia biashara zao ili waweze kufanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda cha General Tyre kimekuwa ni hadithi za Alfu Lela Ulea. Niseme tu Mheshimiwa Waziri tulikwenda tumetembelea na waliahidi kwamba kiwanda hiki kingefanyiwa upembuzi yakinifu. Mwaka wa jana bajeti yake ilikuwa Sh.150,000,000 kwa ajili ya upembuzi yakinifu, leo imeandikwa Sh.70,000,000, sijui ni kwa ajili ya nini, kwa sababu ni pesa ndogo sana ambayo haiwezi kwenda kufanya huo upembuzi yakinifu ambao wanasema.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo majibu mengine ambayo tumepata ni sasa hivi wanatafuta mwekezaji, kwa hiyo mwekezaji mwenyewe ndio atakayekwenda kufanya huo upembuzi yakinifu. Tunasema ni hadithi za Alfu Lela Ulela kwa sababu haya mambo yameanza kusemwa tangu tukiwa wadogo tunasikia General Tyre mpaka leo bado tunaisikia General Tyre.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wenye viwanda wana malalamiko makubwa sana kuhusiana na umeme usio wa uhakika, umeme unakatikatika wakati wowote. Sasa wale wanapokuwa wameshawasha mashine zao, umeme ukikatika kwa ghafla, ukija kurudi unawasababishia hasara kubwa sana katika mitambo yao kwa sababu umeme unavyorudi haujulikani umerudi kwa nguvu ya aina gani. Kwa hiyo nimwombe Sana Mheshimiwa Waziri kwa kushirikiana na Mheshimiwa wa Nishati waangalie kwa kiasi kikubwa ili kuona ni jinsi gani wanavyoweza kuwasaidia wafanyabiashara kwenye suala zima la umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na ziara katika Mkoa wa Tanga. Tanga ni moja kati ya mikoa inayoongoza kwa kuwa na viwanda vingi vingi sana, lakini pale Tanga umeme wa uhakika haupo. Hizo megawatt walizopewa na TANESCO haziwatoshi kuweza kuendesha shughuli za viwanda. Kwa hiyo, naomba sana wauangalie mkoa ule ili uweze kufufua vile viwanda na tayari watu wameanza kuamka kuvifufua; waweze kuleta ajira kwa Watanzania hasa vijana na wanawake ambao hawana ajira za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara wenye viwanda hasa hao wanaofanya biashara ya cement wamekuwa na malalamiko juu ya upendeleo, kwamba kuna baadhi ya wafanyabiashara wanapendelewa kwenye masuala mengine na wao hawapewi upendeleo huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanga Cement wanatengeneza clinker ambayo inatengeneza cement…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi, nimshukuru Waziri Kivuli wa Kambi rasmi ya Upinzani kwa hotuba yake nzuri. Ahsante,
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia, lakini niseme mimi pia ni Mjumbe katika Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira. Tumetoa ushauri kwenye taarifa yetu, lakini ni vema basi kuna mambo mengine ambayo tunaweza tukayazungumza angalau Wabunge wenzetu waweze kutuunga mkono katika Kamati yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningependa kuanza na suala zima la mazingira. Kwa masikitiko makubwa niseme kwamba Ofisi hii ya Makamu wa Rais siku zote imekuwa ikipewa bajeti kidogo sana pamoja na kwamba Wizara ya Mazingira ni Wizara mtambuka, lakini bado Serikali imeendelea kuipa pesa kidogo Ofisi ya Makamu wa Rais ka upande wa Mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na udogo wa fedha hiyo, pamoja na udogo wa bajeti hiyo, bado fedha hii kupatikana kwake haipatikani kabisa. Tangu tulivyokutana mara ya mwisho na Ofisi ya Makamu wa Rais, mwezi Januari, kwa masikitiko makubwa mpaka leo tunavyozungumza hapa hawajawekewa hata shilingi moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama tunategemea mazingira ya nchi yetu ndiyo kila kitu katika ustawi wa nchi yetu, lakini bado katika Ofisi ya Mazingira bado fedha haiendi, watumishi pale wanashindwa kutekeleza majukumu yao kutokana na uwezo mdogo wa fedha walio nao. Wameishia watu wa NEMC, sasa hivi wanachokifanya fedha ambayo wanaitumia ni fedha ya kutoza faini kwa watu. Yaani sasa hivi imefika mahali wanapata fedha kwa ajili ya makosa ya watu, sasa sijui ni Serikali ya aina gani ambayo inaendeshwa kwa fedha ambazo ni makosa ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi hali ya mazingira nchini kwetu ni mbaya sana kuliko ambavyo tunaweza kuifikiria. Tumetembea kwenye maeneo mbalimbali, lakini baadhi ya miradi ambayo ilikuwa imepangiwa kwenye bajeti hii hatukuweza kufanikiwa kuiona kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Tumetembelea eneo moja tu ambalo tulikuwa kama vile tumeenda beach, tulipelekwa eneo la ufukwe la Ocean Road; ndilo eneo ambalo pekee tulipelekwa kama Kamati kwenda kuona sehemu ambayo wanategemea kujenga ukuta kwa ajili kuzuwia mmomonyoko ambao unakuja unasogea mpaka kufikia Ikulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini maeneo mengine yote ambayo yalikuwa yamewekwa kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka huu ya mazingira hakuna eneo lingine ambalo tumeweza kwenda zaidi ya maeneo ambayo Bunge lilitusaidia tumeweza kufika, kama Mwadui pamoja na Geita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipotembelea Mgodi wa Mwadui tulijionea hali halisi ya mazingira katika mgodi ule na kiukweli wanajitahidi kwa kiasi kikubwa kuhakikisha kwamba maeneo ya mazingira katika mgodi ule yanalindwa pamoja na maeneo ya pembezoni ambayo wananchi wanaishi. Eneo la Mgodi wa Mwadui pamoja na wananchi wake wameweza kupewa elimu ya upandaji wa miti na jinsi ya kuvuna miti ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwadui walichowafundisha watu wanaoishi maeneo ya Kishapu ni kuhakikisha kwamba hawakati miti kama vile inavyofanyika maeneo mengine. Eneo lile wamefundishwa kukata miti kwa kukata matawi na kuacha shina liendelee ili ule mti uweze kuendelea kuwa mkubwa badala ya kukata mti mzima na kuacha kisiki na kutegemea kwamba watu waendelee kupanda miti mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetembelea Mgodi wa Geita. Mgodi wa Geita kiukweli kwa kuhusiana na suala zima la maji machafu wamejitahidi kwa namna moja ama nyingine kuweza kuweka bwawa ambalo linahifadhi yale maji machafu. Lakini kwenye maeneo ya mazingira, hasa kwenye maeneo ya miti kwa kweli hawafanyi vizuri kwa sababu hali ni mbaya, wananchi wanakata miti sana, wananchi wanatengeneza mikaa kwa wingi kweli kweli! Kwa hiyo, tuliwashauri angalao kwenye maeneo ambayo yanawazunguka basi waweze kusaidia wale wananchi wa pale waweze kuwa wanapanda miti na kusaidia mazingira yaweze kuwa mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikwenda kwenye Mradi wa Ziwa Victoria. Huku ni masikitiko makubwa sana, kwasababu imefika mahali hali ya mazingira katika Mradi wa Ziwa Victoria kwa kweli si nzuri na hairidhishi. Tungemuomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kwenye majumuisho yake hebu ajaribu kutuambia katika huu Mradi wa Ziwa Victoria nini hasa kinachoendelea? Kwa sababu inavyoonekana kama Tanzania tunajitahidi kwa namna moja ama nyingine kuweza kuzuia hali ya mazingira ya Ziwa Victoria kuwa sawa, lakini ukiangalia nchi jirani ambazo zinatuzunguka na tulizoingianazo mkataba bado zenyewe hazitekelezi mkataba ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tufike mahali sasa na Watanzania tuangalie na nchi jirani za wenzetu ili yale ambayo tunakubaliana kwenye mikataba yetu yaweze kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia kuhusu suala zima la viwanda, sasa hivi viwanda vingi vya samaki Mwanza vinafungwa na vinafungwa kwa sababu ya ukosefu wa samaki katika Ziwa Victoria. Hali ni mbaya, kiwanda ambacho kilikuwa kinaweza kufanya kazi saa 24 leo wanaweza wakafanya kazi kwa shift mbili peke yake, ikizidi sana ni shift moja. Leo viwanda vya samaki vya Mwanza baadhi vimefungwa na baadhi vinaendelea kufanya kazi kwa kusuasua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ningependa kumshukuru Waziri wa Nishati na Madini kwa kukubali mapendekezo yetu na maoni yetu ya kumuomba waanze kununua transfoma zinazotengenezwa nchini kwetu. Kiwanda cha Tanelec kinatengeneza transfoma nzuri na Mheshimiwa Waziri pamoja na Kamati tumesikia wamesema kwamba, kuanzia sasa wataanza kununua transfoma kutoka nchini kwetu. Hilo ni suala zuri naomba nikupongeze Mheshimiwa Waziri na tufanye hivyo ili kuweza kuinua uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyotangulia kusema Mjumbe mwenzangu, Wizara ya Fedha imetengewa bajeti lakini mpaka leo tunavyozungumza tunakwenda karibu robo iliyobaki kumaliza bajeti, lakini fedha iliyokwenda ni only 7 point something billion. Jamani katika bilioni 42, bilioni saba kwenye Wizara ya Viwanda ni kitu gani ndugu zangu! Nafikiri hapa tunafanya masihara, tunaweza tukawa tunalaumu, lakini mwishowa siku Serikali; Mheshimiwa Mpango na Hazina yako hebu jaribuni kuangalia basi. Zile Wizara ambazo angalao mnasema kwamba zina kipaumbele hebu zisaidieni kuziwekea fedha ili waweze kutekeleza majukumu yao badala ya kukaa mnatusaundisha (mnatushawishi) kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila wanapokuja watu wa Wizara ya Fedha ni habari ya kusaundishwa (kutushawishi) tu, lakini utekelezaji haupo. Ilifika mahali tuliwarudisha, tuliwafukuza na tukawaambia hatutakaa tusikilize taarifa yenu kwa sababu haina jipya. Kila wanapokuja wanakuja na yaleyale kumbe tatizo ni ukosefu wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wizara hii kuna kitu kinaitwa Fair Competition, hawa watu wanafanya kazi kubwa sana, yaani hawa watu ndio ambao wanazuia bidhaa fake kuingia nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Fair Competition wanafanya kazi ngumu lakini hawana watu ambao wanafanya kazi hizo. Leo Fair Competition kati ya wafanyakazi 125 wanaohitajika wana wafanyakazi 53 tu nchi nzima. Hebu fikiria mtegemee hawa watu waweze kufanya kazi nzuri, kazi hiyo wanaifanya kutokea wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Angellah Kairuki alituelea hapa kwamba, Ofisi yake ya Utumishi imeanza kuruhusu ajira; Mheshimiwa Angellah Kairuki, sijui ajira hizo zinakwenda upande gani? Kwa sababu kama kwenye Wizara mbalimbali hakuna watumishi ambao wanaajiriwa! Mheshimwia Waziri, hebu utatueleza ukweli, hawa watumishi mnawaajiri kwenye idara zipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kusikitisha ni kwamba hawa watu wa FCC pia waafanya kazi nyingine ambazo ni za hatari sana, wanaingia bandarini wanakutana na watu, lakini…
(Hapa, kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Na mimi ningependa kuchangia katika Wizara hii na ninaomba nitoe masikitiko yangu makubwa sana kwa Wizara ya Maliasili kutokana na mambo yanayoendelea katika Mkoa wa Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliongea na Mheshimiwa Waziri Maghembe kuhusu matatizo ambayo yamewapata wananchi wa Sikonge kutokana na Maafisa wa Idara ya Misitu na Wanyamapori walioko katika Wilaya ile. Watu hawa wanachukua ng’ombe wao, wanasukumiziwa hifadhini, wanasema kwamba, ng’ombe hawa wamefika hifadhini, wanachukua ng’ombe wanatozwa faini ya shilingi milioni mbili mpaka milioni tano kwa ng’ombe mmoja, kuna mwanakijiji mmoja ambaye ametozwa faini ya shilingi milioni 22 kwa ng’ombe wake 22 kuingia katika hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa nilimueleza Mheshimiwa Waziri nikiwa hapo na hao wananchi na aliniambia niandike, nilimuandikia, mpaka sasa ninavyozungumza Mheshimiwa Waziri hakuna suala lolote ulilolifanya. Askari hao wamefikia hatua mbaya ya kuwafanyia vibaya wananchi hawa, wanawavua nguo, wanawatandika bakora na wanawalazimisha kufanya mapenzi na miti. Mheshimiwa Waziri nilikueleza na messsage niliyokuandikia ninayo. Haya mambo hatuelewi hii nchi ni Tanzania ama hii ni nchi gani? Hawa wafugaji ni Watanzania ama hawa wafugaji ni wafugaji wanatoka nchi gani? Tunaomba sana Waziri anapokuja ku-wind up atuambie hawa wafugaji wanatakiwa waende wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kwamba nina dakika tano, naomba nimuambie Mheshimiwa Waziri, suala linaloendelea sasa hivi Kaliua, kesho kutwa wanaelekea Ulyankulu. Jambo la ajabu ni kwamba wananchi hawa walipewa hati na GN Serikali ikatangaza, matokeo yake wananchi hawa wamenyang’anywa hati zao na wanaambiwa waondoke katika maeneo ya hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa vijiji saba hawa hawaelewi kwamba watakwenda wapi, wameshakaa pale zaidi ya miaka 30 wanaambiwa waondoke, hawaelewi wataondoka waende wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niweze kumsaidia Mheshimiwa Waziri, vijiji saba hivyo ni Kijiji cha Seleli, Mwendakulima, Sasu, Kashishi, Nyasa, Iyombo na Ilega. Hawa wananchi mpaka sasa hawaelewi hatima yao, pamoja na Mkurugenzi kuwahakikishia usalama wao kwamba mpaka ripoti ya Waziri Mkuu itakapotoka ndiyo watajua kitu cha kuambiwa, lakini cha ajabu Wizara ya Maliasili inachukua hatua kabla hata hiyo ripoti ya Waziri Mkuu haijasema nini kinachofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini ripoti ya Waziri Mkuu ndiyo ingekuja kutueleza kwamba, nini kifanyike, hawa watu waende wapi na ndipo wale watu wangeanza kuondolewa. Lakini leo watu wanaondolewa, wameishi zaidi ya miaka 30, wanaambiwa ni eneo la hifadhi, hawaambiwi hawa watu wanakwenda wapi? Hatuelewi huko watu wanaenda wapi, tunawatia watu hasira zisizo hata na sababu, ajabu ni kwamba Mkuu wa Wilaya ya Kaliua anasema maagizo haya amepewa na Mheshimiwa Rais, huyu Mheshimiwa Rais anayejinasibu kwa kutetea wanyonge yuko wapi aende akawatetee wanyonge wale?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mama mjamzito amejifungua ana mtoto wa siku tatu analala nje na mtoto wake, lakini cha ajabu wanatoka wanakwenda kuchoma mpaka vyakula ambavyo wale watu wamejiwekea, wanavunja nyumba wanakata mabati, wanakata miti, sasa mnawatoa watu, kama mnataka waende wakajenge kwingine haya mabati mnayakata kwa nini? Vyakula vyao mnachoma kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aje atuambie kama ni maelekezo yeye ametoa na Wizara yake ama Mheshimiwa Rais ametoa haya maelekezo. Chonde chonde, wananchi wa Wilaya ya Kaliua wanateseka na njaa, wanalala nje bila msaada wowote na bado wanapigwa, wanawake wanabakwa na watoto hawaelewi watakwenda wapi. Haya ni mambo ya… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante