Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Shabani Omari Shekilindi (15 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha afya na nguvu kuweza kusimama mbele ya Bunge hili Tukufu. Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza basi niwashukuru wapigakura wangu wa Jimbo la Lushoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kushukuru hotuba hii ambayo imejaa maudhui mema, niendelee kumshukuru Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri. Andiko linasema nimrudishie nini Bwana kwa wema wake alionitendea, kwani hotuba ya Waziri Mkuu imekuna wengi na inastahili kupongezwa hata Mwenyezi Mungu naamini ameibariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, waislamu tunasema; maa yashkuru-nnasa laa yashkuru-llah (usiposhukuru watu basi hata Mwenyezi Mungu hutamshukuru). Basi nishukuru hotuba hii na pia niwashukuru Watanzania wote kwa kumchagua Rais wetu John Pombe Magufuli Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja nijikite katika kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Hakuna asiyefahamu kwamba Wilaya ya Lushoto ni Wilaya ya kilimo cha matunda na mboga mboga. Wilaya ile na wakulima wanalima kwa zana ambazo ni dhaifu mno, wanalima kwa mbolea ya samadi yaani kinyesi ng’ombe. Wakulima wanapovuna mazao yao huwa wanapata taabu sana, wanunuzi wakati wa mvua barabara hazipitiki na inapelekea mazao yale yanauzwa bei rahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika suala zima la ukusanyaji wa mazao wananchi wa Lushoto wanapata taabu sana. Mimi kama Mbunge wao ambaye wamenituma niwawakilishe kwao, kwani wakati wa kura za maoni walisema tunakutuma wewe mnyonge mwenzetu, mkulima mwenzetu ukatuwakilishe, basi na mimi ninawaahidi kutowaangusha na ndiyo maana mkulima mimi, mnyonge mimi nimesamama mbele ya Bunge hili Tukufu kwa ajili ya wananchi wa Lushoto hususani wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hotuba ya Waziri Mkuu iangalie wakulima wangu wa Lushoto hususan katika suala zima la pembejeo, suala zima la masoko, suala zima la kujenga maghala na kujenga mabwawa kwa ajili ya kilimo cha kisasa cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la maji. Lushoto imezungukwa na vyanzo vingi vya maji, lakini miundombinu ya maji hakuna katika Jimbo zima la Lushoto. Ukianzia Kata ya Ngwelo, Gare, Mlola, Ubili, Makanya, Kwemashai, Mbwei, Ngulwi, Malibwi, Kilole, Kwekanga na Lushoto Mjini. Nakuomba katika bajeti hii basi uwafikirie watu wa Lushoto hususan katika suala zima la maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la afya, tunashukuru tuna Hospitali ya Wilaya ya Lushoto, lakini hospitali ile ina changamoto. Hospitali ya Lushoto hususani wodi ya akina mama wajawazito, ile wodi ni ndogo inastahili kuongezwa. Sambamba na hilo katika Kata za Ngwero, Gare, Magamba, Ubili, Kilole na Kwemashai tunahitaji kujengewa vituo vya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la miundombinu, Lushoto wenyewe tunaita Lushoto ya wazungu, kwani Wazungu Wajerumani walikuwa wanaishi maeneo yale, miundombinu ya barabara imejengwa tangu kipindi cha mkoloni. Kwa hiyo, niiombe Serikali ituangali katika vipaumbele vya barabara, hususan barabara ya kutoka Lushoto kupitia Soni hadi Mombo. Barabara hii ni nyembamba na mvua zikinyesha huwa kuna mawe yanaporomoka yanazuia barabara. Hata juzi kati tarehe 17 zaidi ya siku tatu magari yalilala pale mpaka hata maiti zinatoka Dar es Salaam, Tanga na sehemu zingine basi zilishindwa kupita pale kwa sababu ya mawe yaliyoshuka pale na makalvati kuziba, maji yanatiririka katikati ya barabara ilichukua takribani ya siku tatu, naomba katika bajeti yako hii basi waifikirie barabara ya Lushoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo kuna barabara ya kutoka Mlalo kupitia Ngwelo, Mlola hadi Makanya kwenda kwa Mheshimiwa January, Mlingano kwa Mheshimiwa Majimarefu, Mashewa, barabara hii tunaomba sasa ipandishwe hadhi iwe ya Wakala wa Barabara TANROAD. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya kutoka Dochi kupitia Ngulwi hadi Mombo, kwa kuwa barabara hii ya Lushoto - Soni - Mombo, mara nyingi mvua zinaponyesha barabara ile mawe yanashuka yanaziba barabara ningeishauri Serikali iwe na barabara mbadala ya kutoka Dochi - Ngulwi hadi Mombo ijengwe kwa kiwango cha lami na iweze kupandishwa daraja ili iweze kuwa barabara mbadala kwa ajili ya matatizo yanapotokea na breakdown zinapotokea katika barabara ya Soni - Mombo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hawa ndugu zangu, vijana wenzangu siyo vijana wa Lushoto tu ni Tanzania nzima, vijana wanaojihusisha na bodaboda. Vijana hawa inapaswa walindwe maana bodaboda ni ajira kama ajira nyingine. Bodaboda hawa naomba kama kuna uwezekano watengewe fungu katika bajeti hii kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao kwani katika vipaumbele vinavyotoa ajira ni watu wa bodaboda. Wamepata ajira kwa kuwa watu hawa wana watoto, wanao wake zao na wanawasomesha watoto na bodaboda ndiyo kipato chao, ndiyo ajira yao, ninaomba askari wasiwanyanyase vijana wanaojishughulisha na bodaboda, siyo kwa Lushoto tu ni Tanzania tuwalinde vijana wetu wa bodaboda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima la umeme. Nimshukuru Waziri Muhongo, alituma timu yake wakazunguka katika Wilaya nzima ya Lushoto siyo Jimbo la Lushoto tu, Wilaya nzima ya Lushoto alituma timu yake ikazunguka na kubaini maeneo ambayo hayana umeme na kuyaandika, kuyahakikisha kwamba ameyachukua then atayafanyia kazi. Kwa hiyo nampongeza sana Profesa Muhongo, Mungu akulinde na akuzidishie umri! (Makofi)
Kuna suala zima la michezo. Lushoto kuna vipaji vingi sana, kuna vijana wengi sana ni wanamichezo wazuri na hata timu za Simba na Yanga zinakuja Lushoto kwa ajili ya kufanya mazoezi. Kwa hiyo, niombe sasa, nimuombe Waziri wangu, mpendwa wangu Mheshimiwa Nape Nnauye katika bajeti hii aifikirie Lushoto kimichezo sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, toka mwaka 2014/2015, 2015/2016 pesa za maendeleo hazijafika katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto. Kwa hiyo, naishauri Serikali yangu ipeleke pesa hizi kwa wakati. Pesa hizi kwa kutofika imedumaza kabisa Sekta ya Kilimo pamoja na wakulima kutopata huduma hii muhimu ukizingatia 70% ya wananchi wa Tanzania ni wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa wataalam; katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kuna wataalam 35 tu ambao wanahudumia vijiji 125. Hii inapelekea kila mtaalam kuhudumia wakulima 3,000 kitu ambacho ni vigumu kumfikia kila mkulima. Kwa hiyo, kuna upungufu wa wataalam 55 – 60. Niombe Serikali ipeleke wataalam hawa ili kuwanusuru wakulima wetu hawa. Kwa kuwa Serikali hii ni sikivu na ina mpango mzuri wa kumuinua mkulima wa Tanzania, ni imani yangu wataalam hao watafika kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ruzuku na pembejeo katika nchi hii bado ni tatizo kwani hazifiki kwa wakati pia mara kwa mara hazimlengi mkulima aliyekusudiwa kwani kuna udanganyifu mkubwa unafanyika. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto pembejeo hizi zinatolewa kwenye mazao ya nafaka tu yaani mahindi na mpunga. Niombe wakulima wa mbogamboga na matunda nao wafikiriwe. Kama inavyojulikana Lushoto ni ya wakulima wa mbogamboga na matunda, Serikali isiposaidia wakulima hawa itakuwa haijasaidia wakulima wa Lushoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, miche bora ya kahawa. Kahawa iliyopo Wilaya ya Lushoto ni ya zamani mpaka imepelekea zao hilo kupotea. Hivyo, niombe Serikali ipeleke miche bora na ya kisasa ili kufufua zao hili ambalo ndiyo tegemeo kubwa la wana Lushoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali yako iwatafutie masoko wakulima wa Lushoto hapa nchini na nje ya nchi. Pia Serikali itoe ushuru kwenye mazao haya ya mbogamboga na matunda kwani unawakatisha tamaa wakulima wetu hao. Pamoja na hayo, nimshukuru Waziri wa Kilimo katika hotuba yake iliyoelezea kutoa ushuru kwenye vizuizi na hatimaye ushuru ukachukuliwe sokoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, zao la nyanya limepungua sana katika Halmashauri ya Lushoto kwa kuwa kumezuka ugonjwa unaitwa Kantangaze. Ugonjwa huu umeathiri zao zima la nyanya na ugonjwa huu dawa yake inauzwa ghali mno. Kipimo cha dawa hii miligramu nne inauzwa sh. 4,500 ambayo ni bomba la nyanya lenye kuingia lita 15 wakati huo shamba la nyanya linaingia bomba 20 hadi 25. Kwa hiyo, mkulima wa kawaida hawezi kumudu gharama hizo. Niombe Serikali iwaangalie wakulima hawa kwa jicho la huruma ili mkulima yule wa hali ya chini aweze kumudu kununua dawa hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, unaposema kilimo ni uti wa mgongo kinaenda sambamba na miundombinu ya barabara hasa za vijijini. Naomba Serikali yangu iangalie hilo nalo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri. Napenda kuchangia katika suala zima la nyumba za Walimu hasa wale wanaoishi vijijini.
Pia ujenzi wa vyumba vya madarasa ya sekondari na msingi hasa ukizingatia katika Wilaya ya Lushoto kuna maeneo mengi vijijini hayana shule kabisa. Watoto wanatoka zaidi ya Kilometa 20 hadi 25. Wakati wa mvua nyingi watoto hawa hawaendi shule mpaka mvua itakapopungua.
Naiomba Serikali yangu Tukufu ijenge shule kwenye maeneo hayo, mfano Lushoto Makanya Kagambe, Mazumbai, Ngindoi, Muheza na Mlola.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wetu wanapata mishahara midogo sana ambayo haikidhi haja zao. Naiomba Serikali yangu Tukufu iangalie jinsi gani ya kuwaongezea mishahara Walimu wetu hawa. Pamoja na stahiki zao, walipwe kwa wakati hasa hizi za uhamisho. Sambamba na hayo, makato ya Walimu yamekuwa mengi. Naiomba Serikali yangu ipunguze makato hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la vitabu mashuleni pamoja na miundombinu kwa ujumla. Pia Walimu hawa wapandishwe madaraja kwa wale wote wanaostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa suala la VETA ni suala ambalo lipo kwenye ilani, kila Wilaya iwe na VETA. Wilaya ya Lushoto ni miongoni mwa Wilaya ambazo hazina Chuo cha VETA. Naiomba Serikali ikafungue chuo cha VETA Lushoto na kwa bahati nzuri kuna majengo ambayo yako tayari, kwani ni kuongea na TAMISEMI wawape majengo waliyoyaacha na kuhamia kwenye jengo lao jipya. Nia na madhumuni ni kusaidia vijana wetu hawa ambao hawakuweza kuendelea na masomo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naishukuru Serikali yangu kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi hao, lakini wanafunzi hawa wanapomaliza vyuo, Serikali haiwapatii ajira vijana wetu hawa. Hapo hapo Serikali inatangaza wote ambao wamesoma Vyuo Vikuu kwa mikopo wanatakiwa warejeshe mikopo hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe binafsi najiuliza, vijana hawa bado hawajapata kazi na huu mkopo wataurudishaje? Naiomba Serikali yangu Tukufu iwapatie Vijana hawa ajira ndiyo waanze kulipa mikopo hiyo. Pia Serikali ijue ya kuwa kuna kundi kubwa sana la vijana ambao wapo mtaani hawana ajira. Kwa hiyo, ni muhimu sana kujenga vyuo vya VETA vijana wetu wakimaliza waweze kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri aniangalie kwa jicho la huruma aniletee Walimu wa sayansi. Mungu akubariki mama yangu Mheshimiwa Profesa Ndalichako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri anitembelee katika Wilaya ya Lushoto.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ili uchumi wetu ufikie uchumi wa kati tunatakiwa tuwekeze katika viwanda vyetu vya ndani pamoja na kuvisimamia. Pia tukumbuke viwanda ndio njia pekee inayoweza kutoa ajira kwa vijana walio wengi nchini. Pia kuna vijana wengi ambao hawana ajira, niishauri Serikali iwawezeshe vijana hawa ili wasiwe wanatangatanga kwenda mjini kutafuta ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kuna vijana wengi waliomaliza vyuo na hawana ajira, papo hapo wanaambiwa walipe mkopo waliokopa, vijana hawa watalipaje mkopo kama Serikali yao haijawawezesha kupata ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna asiyefahamu kuwa Wilaya ya Lushoto ni ya wakulima wa matunda na mboga mboga. Hivyo niishauri Serikali iweke kiwanda cha kusindika matunda, kwani matunda na mboga mboga vinaharabika hali inapelekea wakulima kupata hasara katika mazao yao hayo na pia wakulima wetu tunawakatisha tamaa kwa kupoteza nguvu zao nyingi shambani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wengi wamejitahidi kujiajiri kwa kufanya biashara lakini wanasumbuliwa sana na watu wa TRA hasa wafanyabiashara wa Jimbo la Lushoto. Maafisa wa TRA hawana elimu ya biashara, halii inapelekea Maafisa hawa kuwa ndio wamepata uchochoro wa kuwanyanyasa wafanyabiashara hawa. Imefikia hatua mfanyabiashara akutane na simba lakini sio Afisa wa TRA. Naomba Serikali iliangalie hili ili wafanyabiashara wale waweze kufanya biashara yao kwa amani na kujipatia kipato chao cha kila siku.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Waziri wa Habari Mheshimiwa Nape Nnauye kwa hotuba yake nzuri iliyojaa matumaini ya kuona tasnia ya habari ikisonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vipaji vingi vya vijana hasa Wilayani hadi Vijijini, lakini vipaji hivi vinapotea bure na vijana kushindwa kuviendeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali hasa hii tasnia ya michezo ifike Wilayani mpaka Vijijini kwenda kuwanoa vijana hawa ili Serikali iweze kuwawezesha na vijana hawa waweze kutimiza ndoto zao. Sio kutimiza ndogo zao tu pia nchi yetu itakuwa ina kiwango kikubwa cha michezo, kwani kuna wakina Samatta wengi huko Wilayani na hasa Wilaya ya Lushoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu shule za habari, utamaduni na michezo. Niishauri Serikali ifungue shule kila Wilaya ili kuibua vipaji vya vijana wetu. Vijana hawa Serikali imewaacha kwa muda mrefu sana hivyo basi katika bajeti ya mwaka huu 2016/2017 itenge pesa kwa ajili ya kuibua fani za vijana hawa pia niishauri Serikali ije iwekeze katika Wilaya ya Lushoto, katika shule ya michezo, Lushoto ni mji ambao una mazingira mazuri, mazingira haya mazuri iliwavutia timu ya Simba na Yanga kuja kufanya mazoezi yao Lushoto.
Pia niishauri Serikali iweze kujenga uwanja wa michezo katika Mji wa Lushoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wasanii katika nchi hii hakuna asiyejua ya kuwa Tanga kuna vipaji vingi vya wasanii. Hivyo niiombe Serikali iweze kuwajengea uwezo wasanii hawa ili nao waweze kufahamika Kitaifa hata Kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimuombe Waziri wa Habari na Michezo atenge muda wa kutembelea Lushoto. Mungu ambariki sana Waziri wetu Mheshimiwa Nape Nnauye.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu huyu aliyenijalia afya na nguvu kuweza kusimama katika jengo lako hili Tukufu. Pia niwashukuru wananchi wangu wa Lushoto kwa kuniamini ili nije niwawakilishe katika jengo lako hili tukufu. Niendelee kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na timu yake ya Mawaziri, aendelee kutumbua majipu na sisi Wabunge tutaendelea kuyapaka spirit ili yakauke haraka siku ya siku tuyapeleke mahakamani majibu haya ili wakome kuita nchi hii ni shamba la bibi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuwashukuru Mawaziri wangu wawili Mheshimiwa Angellah Kairuki na Mheshimiwa George Simbachawene. Pia niendelee kuwapongeza ndugu zangu wapinzani maana leo naona wameanza kuchangia hoja, wamebakisha tu kusema naunga mkono hoja, lakini kwa uwezo wa Mungu naamini itafikia hatua hiyo sasa naona roho mtakatifu amewashukia leo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mchangiaji mmoja dada yangu Mheshimiwa Grace Kiwelu alisema kwamba tufute mbio za mwenge. Kufuta mbio za mwenge ni sawasawa na kufuta historia ya nchi, hiyo haitawezekana. Kama isivyowezekana kwa CHADEMA kufuta historia ya Edwin Mtei ndani ya CHADEMA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuchangia hoja sasa. Niishauri Serikali iendelee kuanzisha vijiji, kata, Halmashauri, wilaya hadi mikoa kwani hii inapelekea kupeleka huduma karibu na wananchi. Historia ya Jimbo la Lushoto au Wilaya ya Lushoto kwa kweli ni kubwa sana na Rais wetu Mstaafu wa Awamu ya Nne alivyotembelea Lushoto alituahidi Halmashauri ya Mji wa Lushoto na Mlalo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unapoongea juu juu hivi mtu huwezi ukaamini kwamba Wilaya ya Lushoto ni kubwa sana. Nataka niseme ili ujue uhondo wa ngoma uingie ucheze, namuomba Mheshimiwa Waziri wangu Simbachawene atembelee Lushoto ili tunapoongea maneno haya tuwe tunamaanisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Lushoto inapakana na Kenya. Kuna watu wanatoka kwa miguu kufuata huduma Wilayani Lushoto inashindikana wanatumia siku mbili. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu sasa ituangalie kwa jicho la huruma ili kwenye bajeti hii ya 2016/2017 iweze kutupatia Halmashauri ya Mji na iweze kutupatia Halmashauri ya Mlalo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye afya. Suala la vituo vya afya ni tatizo la nchi nzima na naamini Serikali yangu sikivu imejiandaa vyema kuweza kujenga vituo hivi vya afya. Pamoja na hayo kwenye mpango huo naomba sasa Waziri, Mheshimiwa Simbachawene tuangalie Lushoto kwa sababu Jimbo la Lushoto lina kituo cha afya kimoja na zahanati nane. Kwa hiyo, huduma hii ya watu wa Lushoto kwa kweli imekuwa na hali ngumu kiasi kwamba kwa kweli inatia masikitiko. Kituo hiki kiko sehemu moja inaitwa Mlola, kutoka sehemu moja wanaita Makanya kwenda Mlola kwanza hata miundombinu ya barabara hakuna, wananchi wa kule wanapata taabu sana.
Hawa wananchi ni wapiga kura wetu tunawategemea, hawa hawayumbi wala hawayumbishwi, hawajui CHADEMA wanajua tu CCM. Kwa hiyo, nikuombe Waziri wangu katika bajeti ya mwaka 2016/2017 hebu liangalie hilo tuweze kuongeza vituo vya afya. (Makofi)
MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa....
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naomba unilindie muda wangu kwani mtoa taarifa, taarifa hiyo nadhani hajajielewa aipeleke Simanjiro lakini Lushoto ni kijani tupu. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Ulipata asilimia mia?
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Ndiyo ni asilimia mia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naongelea suala zima la afya. Kwa kuwa Serikali yetu ina mpango mzuri wa kujenga vituo vya afya katika Jimbo la Lushoto, niiombe sasa isimamie hawa watu wa MSD kwani dawa hazifiki kwa wakati. Nimechunguza kweli hawa watu wa MSD ni majipu kwani DMO anapeleka pesa za kununulia dawa labda shilingi milioni tano lakini akifika anapewa dawa za shilingi milioni mbili. Kwa hiyo, hili ni jipu naomba lifuatiliwe. Sisi tunalalamikia madaktari wetu kumbe kuna kidudu mtu hapa katikati anakwamisha huduma nzima ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye suala la kilimo. Uti wa mgongo wa Taifa hili ni kilimo lakini huachi kuongelea pia na miundombinu. Miundombinu ya barabara ndani ya Jimbo la Lushoto hasa za vijijini ni tatizo. Wananchi walio wengi hususan wakulima wanakwamisha na miundombinu ya barabara. Kwa hiyo, niishauri Serikali yangu tukufu kwamba katika bajeti hii ya 2016/2017 ipeleke pesa za ruzuku za kutosha katika Halmashauri ili barabara hizi ziweze kutengenezwa kiwango cha kupitika ndani ya mwaka mzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hayo kuna barabara za vijiji ambazo ni tegemezi hata katika Jiji la Dar es Salaam, barabara hii ni ya Mshizihii - Boheloi, inatoa mazao mengi sana. Barabara nyingine ni ya Kwemakame - Ntambwe - Mazumbai - Baga kwa Mheshimiwa January.
Kwa hiyo, hizi ni barabara ambazo zinatoa matunda na mazao mengi sana. Pia kuna barabara inatoka Malibwi – Kwekanga - Kilole - Ngwelo ni ya muhimu sana kwani inachangia pato kubwa la Taifa hili.
Barabara nyingine ni ile inayoingilia sehemu moja wanaita Kwaikileti – Dindira – Bandi – Kwaboli – Migambo. Barabara hii inatoa matunda mengi mno kiasi kwamba hata tukielezea uchumi wa matunda ya Lushoto basi chanzo chake kinatoka maeneo hayo niliyotaja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuzungumzia suala zima la redio ya Taifa (TBC). Nimuombe Mheshimiwa kaka yangu Mheshimiwa Nape, kule kwetu tunasikiliza redio za Kenya tu. Kwa hiyo, ifikie hatua sasa kwenye bajeti hii ya mwaka 2016/2017 basi watutengee mafungu ili wananchi wale waweze kupata taarifa mbalimbali za Taifa lao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naona muda wangu umeisha, naunga mkono hoja asilimia mia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Waziri kwa hotuba yake nzuri iliyojaa matumaini ya Watanzania kujitoa kwenye vibatari hadi kuwa na umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Lushoto tunakushukuru baadhi ya vijiji vimepata umeme. Pia ametuma timu yake imeenda kupima maeneo yote ambayo yamekosa umeme wa REA II na kuwahakikishia wananchi wangu kuwa Jimbo la Lushoto litapata umeme kwa yale maeneo yote yaliyobaki. Mungu ambariki sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri kwa kuwa wananchi wangu wameshakuwa na matumaini makubwa juu ya suala zima la umeme, niendelee kumwombea kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kutimiza ahadi yake hiyo ili ifikapo 2020 wananchi wangu waendelee kuamini Serikali yao ya Chama cha Mapinduzi. Pia napenda kuorodhesha maeneo ambayo hayajapata umeme pamoja na kwamba maeneo mengine ya kata na vitongoji yameshapata umeme. Kata ambazo hazina umeme pamoja na vijiji vyake ni kama ifuatavyo:-
(i) Makanya yote;
(ii) Ngwelo baadhi ya vijiji;
(iii) Kilole baadhi ya vijiji;
(iv) Kwekanga baadhi ya vijiji;
(v) Gare baadhi ya vijiji;
(vi) Kwemashai baadhi ya vijiji;
(vii) Ubiri baadhi ya vijiji;
(viii) Magamba baadhi ya vijiji;
(ix) Kwai baadhi ya vijiji;
(x) Mgambo baadhi ya vijiji;
(xi) Mbwei baadhi ya vijiji;
(xii) Malimbwi baadhi ya vijiji;
(xiii) Lushoto baadhi ya vijiji;
(xiv) Mlola baadhi ya vijiji; na
(xv) Ngulwi baadhi ya vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa binafsi nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri wa bajeti ya Wizara yake pamoja na hotuba yake nzuri iliyojaa mazuri na mambo ambayo yametoa kiu za wananchi. Pamoja na style yake ya kutoa mabegi yaliyojaa mambo yote yanayohusu Wabunge na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Waziri sina budi kumshukuru kwa kunipatia Baraza la Ardhi katika Wilaya ya Lushoto ambalo lipo kwenye Jimbo langu kwani mchakato huu niliufuatilia wakati tupo kwenye Kamati yako ya Ardhi. Hivyo hujasita kuondoa kiu yangu na ya wananchi wa Lushoto kwa kiujumla na kuahidi kuja kufungua Baraza hilo mwezi wa saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu migogoro ya ardhi, Mheshimiwa Waziri migogoro ya ardhi ipo katika nchi nzima lakini ndani ya Jimbo la Lushoto kuna migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima hasa maeneo ya Bwei, Kilole na Mlola, yote haya yanasababishwa na eneo dogo lililopo katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna mwekezaji wa kiwanda cha mbao kinachoitwa Mombo Saw Mill. Kiwanda hiki kilikufa takribani miaka 20 iliyopita, lakini Mheshimiwa Waziri eneo hili linapakana na shule ya sekondari ya St. Mary’s - Mazinde Juu na shule hii ni ya boarding kwa ajili ya wasichana. Mheshimiwa Waziri eneo hili limekuwa ni kichochoro cha watu kuingia katika eneo la shule ukizingatia eneo hilo linapakana na shule hiyo na upande lilipo ndiyo mabweni ya wanafunzi. Father amemfuata mwenye eneo lakini hakuonesha ushirikiano kwa sababu mwenye eneo hili anashirikiana na watu wabaya ambao hawana nia nzuri ya shule hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninakuomba Mheshimiwa Waziri kwa heshima na taadhima na kwa unyenyekevu mkubwa, suala hili uliingilie kati, eneo hili liweze kurudi ili liungane na eneo la shule. Ninashauri hivyo kwa ajili ya kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza, sambamba na hilo eneo hili halijalipiwa kwa muda mrefu sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo ningeomba Mheshimiwa Waziri Mungu akikujalia kufika Lushoto kufungua Baraza la Ardhi, utembelee eneo hilo la Magamba na shule ya sekondari Mazinde Juu kwa ajili ya kupata maelezo ya kina kwenye uongozi wa shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Lushoto kuna muingiliano mkubwa wa watumishi wa ardhi, hii imepelekea ujenzi holela na urasimu wa kupata hati ni tatizo kubwa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimtakie Mheshimiwa Waziri utumishi uliotukuka huku wananchi wa Lushoto wakiendelea kukuombea kwani wana imani kubwa sana na wewe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata nafasi hii. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia afya na nguvu kuweza kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Naomba nimpongeze Waziri Maghembe na timu yake kwani hotuba yake ina vina, imegusa, lakini nimuombe isiwe ya maandishi tu iwe ya vitendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite moja kwa moja katika kuchangia juu ya upandaji wa miti. Miaka ya nyuma misitu iliungua baadhi ya maeneo katika nchi hii, hususani Lushoto, mpaka sasa hivi maeneo yale bado ni mapori hayajapandwa miti. Niishauri Serikali yangu sikivu iandae mikakati kwa ajili ya kupanda miti katika maeneo yale kuanzia Korogwe, Lushoto mpaka kushuka maeneo ya Same kule ni jangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pamoja na kupanda miti iwasaidie pia wakulima mmoja mmoja wa miti waweze kupanda kwenye mashamba yao, kwani ukitaja Lushoto ndiyo kuna wahifadhi, watunzaji wa mazingira wakubwa sana. Leo hii maeneo yale ambayo ni vichaka yanatia aibu. Naiomba Serikali yangu tukufu ipange fungu kwa ajili ya kupanda miti katika milima ile ya Lushoto, pia iwasaidie wakulima hawa mmoja mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie moja kwa moja kwenye mgao na uvunaji. Tunashukuru tumepakana na misitu ya Shume, Mazumbai, Baga, Gare, lakini misitu ile bado haisaidii wananchi. Katika mgao wanaangalia wale watu ambao wana uwezo na kila mwaka watu wanaopewa mgawo ni wale wale. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu na nimuombe Waziri Maghembe kipindi hiki ahakikishe kwamba mgao ule aufuatilie waliopata ni wangapi na ni wa aina gani? Mimi kama Mbunge wao wamenituma baada ya kulalamika kilio hiki kwa muda mrefu sana. Mgao huu pia au uvunaji huu haujazingatia watu wanaochakata viwandani, kwa mtu mmoja mmoja na kwa vikundi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la uvunaji kwa mtu mmoja mmoja. Misitu ya Serikali hii watu wanapeleka kuchakata kwenye viwanda, viwanda viko mbali sana na miti ile. Kuna sehemu wanaita Makanya, Ngwelo, Gare, Ubiri, Lushoto, Mbwei, Malibwi na Kilole, maeneo haya yako mbali sana na viwanda. Kitu cha ajabu na cha kushangaza watu hawa wameweka sheria moja kwa ajili ya kuvuna kwa vikundi au kwa ajili ya kuvuna na chainsaw, wamekataza kuvuna kwa chainsaw wavune kwa shoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana wakulima wangu wale wa miti sasa waruhusiwe kuvuna kwa chainsaw kwani ukitoa mti kutoka Makanya au mtu wa Makanya akivuna mti hawezi kupeleka moja kwa moja mpaka kiwandani, lakini Mheshimiwa Maghembe watu hawa anawakataza anasema kila mtu avune kwa shoka kitu ambacho ni kigumu, ndiyo maana nikasema ameangalia upande mmoja tu kwa ile misitu ya Serikali lakini hajaangalia kwa mtu mmoja mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba Mheshimiwa Maghembe, atakaposimama ku-wind up basi aangalie vitu hivi. Ahakikishe kwamba watu wangu awaruhusu sasa wavune kwa chainsaw. Kwa sababu mtu yule hawezi kukata mti wake kule mpaka akapeleka kiwandani, itakuwa ni shida. Tunawaomba hata mbao za madawati wanashindwa kuvuna wanasema kwamba tumekatazwa kuvuna kwa chainsaw. Kwa hiyo, hili ningeomba baada ya kusimama Mheshimiwa Maghembe basi alitolee ufafanuzi, ili watu wangu waweze kuvuna kwa chainsaw.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru Mheshimiwa Maghembe alitembelea Jimboni kwangu kule Lushoto, alikuta changamoto, pamoja na kwamba sikuwa na taarifa za ujio wake kama angenipa taarifa, basi ningemwambia hali halisi ilivyo, yeye alienda moja kwa moja mpaka ofisini kwa wataalam wake tu, na alipofika kule alichukua maneno ya wataalam akayaacha ya wananchi. Ninamshauri siku nyingine akienda atafute na Wabunge, hii siyo kwa Waziri Maghembe tu, Waziri yeyote atakayeenda site basi atafute Wabunge kwa sababu Wabunge ndiyo wanajua changamoto zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema Lushoto inapakana na msitu, ninamuomba Mheshimiwa Maghembe kuna akina mama kule wanatafuta kuni msituni wanakamatwa, shoka zao zinachukuliwa zinaenda kuhifadhiwa ofisini, mapanga na kila kitu, watu wale ni walindaji wakubwa wa misitu. Nashukuru Mheshimiwa Maghembe alienda pale akawaambia kina mama wale basi waendelee kutafuta kuni na waende na mapanga na mashoko, lakini wasije wakatafuta mti ambao ni mbichi. Kwa hiyo, nimuombe atakaposimama basi aliongelee hilo suala hapa ili liingie kwenye Hansard na watu wangu waweze kupata nguvu kwa ajili ya kutafuta kuni msituni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Waziri wa Maliasili na Utalii, ashirikiane na Waziri wa Viwanda, kuna Kiwanda cha Ceiling Board pale Mkumbara; kiwanda kile kinakufa, hakina tatizo lolote, kina skyline inatoa magogo kutoka Shume kushuka chini. Lakini kwa sasa hivi kinakufa, na kinakufa bila sababu yoyote, ningemuomba sasa Mheshimiwa Waziri Maghembe na Mheshimiwa Mwijage wafike pale Mkumbara Ceiling Board, waone kiwanda kile jinsi kinavyonyanyasika, na watu wa pale jinsi wanavyonyanyasika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa pale hata kulipa bili ya umeme wameshindwa, sambamba na hayo naamini kabisa Mheshimiwa Mwijage na Mheshimiwa Maghembe watakapofika Mkumbara basi moja kwa moja wataenda mpaka kwenye Kiwanda cha Chai Mponde, naamini Mheshimiwa Mwijage kama kweli ana hofu ya Mungu atatoa sauti yake na kufungua viwanda vile, wananchi wa kule wananyanyasika, hata kulipia karo ya shule wanashindwa, hata mlo ni mmoja kwa sababu ya chai yao kiwanda hakijafunguliwa wanashindwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Mwijage, nitamwekea hata mafuta aende Mkumbara Ceiling Board kwa sababu itakuwa ni ziara yake hiyo basi aende mpaka Mponde pale aone wakulima wa chai wanavyonyanyasika…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri. Mchango wangu upo kwenye suala zima la utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Lushoto kuna vivutio vingi vya kitalii lakini vivutio vile havichangii Pato lolote la Taifa letu kwa sababu utalii ule unafanywa kienyeji. Hivyo basi niombe Serikali ifungue chuo cha kitalii Lushoto ili vijana wetu wapate elimu ya utalii ili wasiendelee kufanya kazi ile kienyeji na kuisababishia Serikali kukosa mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niishauri Serikali, yale maeneo yote yenye vivutio yatengenezwe ili watu wasiingie kiholela, ikiwezekana kuwe na vizuizi. Niombe Serikali yangu Tukufu iwaangalie hawa watu wanaovuna mti mmoja mmoja, waweze kuchana mbao zao kwa kutumia chainsaw kwani wakulima hawa hawana uwezo wa kununua mashine za kuchana mbao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo walikuwa wanatumia misumeno ya mikono ambayo hakuna watu wanaoitumia kwa sasa maana walikuwa wanatumia wazee na wazee wengi wameshakufa na waliobaki wamezeeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii pia imepelekea baadhi ya watu ambao hawana nia nzuri hasa polisi wanawakamata sana watu wanaokata miti kwa chainsaw, na askari hawa wameacha kufanya kazi zao nyingine, kazi yao kusikiliza maeneo yanayolia chainsaw ili wakakamate.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la asilimia 20 kumekuwa na tabia ya Maafisa Misitu kuchukua asilimia hizo hata kama mtu anavuna mti wake kwa matumizi yake binafsi. Niombe Serikali yangu iwape Wabunge zile sheria za misitu ili Wabunge tukawaelimishe wakulima wetu wa miti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi yaliyozungukwa na misitu mameneja hawatoi mgao kwa vijiji vilivyozunguka msitu pamoja na vikundi vya kina mama wajane, vijana pamoja na vikundi vya kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu, hasa katika Wilaya ya Lushoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Mungu amlinde na kumzidishia umri pamoja na kumpa afya nzuri.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, huyu ambaye amenijalia afya na nguvu ya kuweza kusimama katika Bunge lako Tukufu na kuweza kuchangia bajeti ambayo iko mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nikupongeze wewe mwenyewe na tutaendelea kukuombea dua sisi Wabunge wote kwani unatosha. Kwa kuwa sisi wengine ni Masharifu basi naamini hakuna kitu kibaya ambacho kitakupata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niendelee kumpongeza Waziri wa Fedha na timu yake kwani bajeti yake kwa kweli ni nzuri na inatia moyo. Tuna uhakika sasa kwamba tunakwenda kwenye Tanzania mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kuchangia suala la kilimo. Nchi yetu inasema kilimo ni uti wa mgongo, lakini inasikitisha tunaposema kilimo ni uti wa mgongo, kilimo hiki kimetengewa bajeti ya shilingi trilioni 1.56, bajeti ambayo ni ndogo sana, haikidhi haja. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu sasa Tukufu iongeze bajeti hii kwani kama tunategemea uchumi wa viwanda, uchumi wa viwanda hautoki sehemu nyingine zaidi ya kwenye mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu zinanyesha mvua za msimu, niishauri Serikali yangu sasa ijenge mabwawa kila maeneo ili kuweza kukinga mvua zile na wakulima wetu waweze kulima kilimo cha umwagiliaji. Kama alivyosema viwanda vinategemea kilimo kwa maana kwamba malighafi zinatoka kwenye kilimo, kwa mfano kule kwangu kuna maeneo mengi sana lakini ni kame, kwa maana hiyo tukiyajengea sasa mabwawa ina maana tutalima kilimo cha umwagiliaji na tutaongeza mnyonyoro wa thamani kwenye mazao yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna asiyejua kwamba Lushoto ni ya kilimo cha mboga mboga na matunda lakini kilimo kile wanalima kwa mazoea. Niiombe Serikali yangu ipeleke ruzuku za pembejeo kwenye kilimo cha mboga mboga na matunda. Wenzangu wote wanaposema ruzuku basi mimi kwa Wilaya ya Lushoto kwa kweli mboga mboga zile na matunda hayajawahi kupata ruzuku. Niishauri Serikali yangu sasa kama ina nia ya dhati, basi iweze kuwezesha kilimo kile kiweze kupata pembejeo za ruzuku.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niingie kwenye afya. Wakati tuko kwenye mchakato wa kampeni tulikuwa tunanadi Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi kwamba kila kijiji kitajengwa zahanati na kila kata itajegwa kituo cha afya. Leo hii katika bajeti nimeona tu mambo ya dawa na madeni ya MSD na vinginevyo lakini sijaona zahanati hata moja wala kituo cha afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kuangalia wananchi wetu kule vijijini kwa kweli ni masikitiko makubwa sana. Laiti ningekuwa na uwezo ningemchukua Waziri wa Fedha akaenda moja kwa moja kwa wananchi wale awaone kwani kuna wananchi kule hawajui hata hospitali. Wananchi wale kwa kweli wako kwenye mazingira magumu, wanalala chini, leo hii ukimchukua ukisema umpeleke hospitalini, kwa kweli hata mwili wake umekakamaa kama mbao. Hata umchome sindano ina maana haingii, sasa huyo unategemea nini, lakini mtu yule amekosa huduma. Niiombe Serikali yangu iende moja kwa moja kwa wananchi wale ili waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tumeongea suala la walemavu, lakini tumeangalia walemavu wa mjini wale ambao tunawaona lakini wa vijijini wala hawajafikiwa. Niombe sasa katika bajeti ya walemavu basi iende moja kwa moja kwa wale walemavu wa kule vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala zima la shilingi milioni 50. Tulikuwa tunapigia kelele kwamba jamani mkituchagua basi shilingi milioni 50 zitakuja tena kwa wakati kwa kila kijiji, lakini leo hii naona bajeti imetengwa tu kwenye mikoa 10. Niishauri Serikali yangu wasipeleke kwenye mikoa 10, watenge hata vijiji vitano vitano kwenye mikoa yote Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Sisi wengine tumeshajiandaa watu wetu tumeshaanza kuwapa pesa ya kufungulia akaunti mahsusi kwa ajili ya pesa hizi. Mpaka sasa ninavyoongea, nina vikundi zaidi ya 100 ambavyo nishavifungulia akaunti wanasubiri pesa hizi. Kwa hiyo, niiombe sasa Serikali yangu Tukufu iweze kupeleka pesa hizi kwa wakati ili nikirudi Jimboni wananchi wale wasije wakaniuliza maswali magumu ambayo nitashindwa kuyajibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye kodi ya bodaboda. Wakati Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli anapita alisema katika watu ambao nitawaangalia ni watu wa bodaboda, leo hii naona watu wale tunazidi kuwaongezea mzigo kwani walikuwa wanalipa Sh. 45,000/= sasa hivi wanatakiwa walipe Sh. 95,000/=. Hebu jamani hili tuliangalie kwa jicho la upendeleo kwani ndugu zangu itafikia hatua sasa bodaboda hawa hawatatuelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napenda kuongelea ushuru wa mitumba. Mitumba hii imeajiri wananchi wengi sana. Leo hii ukifika pale Dar es Salaam au nimtume Waziri wa Fedha pale Dar es Salaam ataona ma-godown ya mitumba ambayo inasafirishwa mikoa yote Tanzania. Niiombe Serikali yangu iondoe ushuru huu ibaki VAT ileile ya mitumba iliyokuwepo siku zote ikiongezwa ina maana tumewapa mzigo watu ambao hawastahili kubeba mzigo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia moja kwa moja niende kwenye suala la mifuko ya nailoni. Unapopiga marufuku matumizi ya mifuko ya nailoni unakuwa umepiga marufuku utunzaji wa mazingira kwani miche inaoteshwa kwenye mifuko ya nailoni. Kwa hiyo, anaposema mifuko ile ipigwe marufuku isitumike ina maana atakuwa amewaambia wananchi wasipande miti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hii asilimia tano ya vijana na asilimia tano ya akinamama, tunaipeleka wapi kama wananchi wetu hawa hatuwasaidii ipasavyo. Tunawapa wananchi asilimia tano kwa ajili ya kupata mitaji ndiyo anakwenda kununua bodaboda ambayo ina kodi kibao, unategemea mwananchi huyu atafaidikaje? Mwananchi huyu tumembebesha mzigo ambapo ni sawasawa na kumpaka mafuta kwa mgogo wa chupa. Kwa hiyo, hebu ifikie hatua sasa Serikali yetu iliangalie hili kwa jicho la huruma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri. Niiombe Serikali yangu ijipange katika suala zima la wafanyabiashara kwani hawa wanaongeza pato kubwa katika Taifa letu, lakini kunakuwa na ukiritimba wa passport pamoja na Visa. Sambamba na hayo VAT inakuwa ni shida kwa wafanyabiashara hawa, yaani mzigo unachajiwa mara mbili ya bei aliyonunulia mfanyabiashara huyu. Suala la utoaji wa passport unachukua muda mrefu kuipata kwa hiyo niishauri Serikali yangu iliangalie hili pass hizo zitoke kwa muda muafaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la Mabalozi wetu hawa imefikia wakati sasa watafute wawekezaji pamoja na wafadhili kwa ajili ya kujenga nchi yetu sasa kiuchumi zaidi.
Katika Jimbo la Lushoto kuna ma-sister wana miaka zaidi ya 60 na wamesaidia sana jamii inayowazunguka na mpaka sasa wanaendelea kusaidia. Wamejenga shule, wamejenga zahanati na wamejenga hosteli na pia wanajitolea kuwafundisha watoto wa maeneo hayo. Kwa kuwa ma-sister hawa ni wa muda mrefu sana na wanaendelea kulipia kodi kama kawaida, lakini kwa sasa hawa wamezeeka na shirika limefika hatua wanashindwa kuwalipia ma-sister wale. Niiombe Serikali yangu iweze kuwapa uraia kwani wakiondoka na kurudi kwao itakuwa ni hasara kubwa sana kwa wananchi wa eneo lile la Kifungilo sekondari pamoja na Kata ya Gare kwa ujumla itakosa huduma muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba Mheshimiwa Waziri atembelee Jimbo la Lushoto au atume Mjumbe ili akaone hali halisi kwa haya niliyoongea hasa kwa suala zima la misaada tunayopatiwa na ma-sister hawa, kwa maelezo zaidi Mheshimiwa Waziri naomba nimwone ili nimwelezee kwa undani zaidi.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Waziri wa Fedha na timu yake kwa kutuletea mapendekezo mazuri ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/2018. Naomba kuchangia suala zima la kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa letu. Naomba niishauri Serikali yangu Tukufu tufungue viwanda vidogo vidogo ambavyo malighafi zake zinapatikana hapahapa nchini hasa kwa wakulima wetu. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumeongeza mnyororo wa thamani katika mazao yetu pamoja na kuongeza ajira kwa wananchi wetu. Pia pembejeo zifike kwa wakati kwa wakulima wetu na pia wakulima wa mbogamboga na matunda nao wapewe pembejeo za ruzuku kwani wakulima hawa wanachangia sana Halmashauri zetu kwa kulipa ushuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali yangu Tukufu kuwe na mkakati maalum kuhusu suala zima la maji. Suala la maji lingefanywa kama suala la madawati lilivyofanywa tungemaliza tatizo la maji kabisa hapa nchini na kusahau kabisa tatizo hili la maji. Hili ni tatizo kubwa sana hapa nchini na kila Mbunge aliahidi kutatua tatizo hili. Naamini kabisa kama tatizo hili halijatatuliwa, Wabunge wengine tutashindwa hata kurudi majimboni kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto kubwa sana katika suala zima la huduma ya afya upande wa dawa pamoja na kutokuwa na vituo vya afya na zahanati hasa wananchi wanaoishi vijijini wana hali mbaya sana. Sisi kama Wabunge tumehamasisha suala la CHF na wanaelewa na kuchangia, lakini wanapofika hospitali wanakuta hakuna dawa zaidi ya kuambiwa wakanunue dawa katika maduka binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, maliasili na utalii, naomba niishauri Serikali yangu Tukufu kuhusu suala zima la misitu yetu kuchomwa moto kila siku hali ambayo husababisha uoto wa asili kutoweka na maeneo ya misitu kubaki vichaka. Nashauri Serikali inunue ndege kwa ajili ya kuzima moto katika misitu yetu inayopata majanga ya moto hasa ikizingatiwa jiografia ya misitu mingi kuna maporomoko makubwa ambayo watu hawawezi kuzima moto unapotokea. Pia maeneo yote yaliyoungua Serikali ipande miti ili kurudisha mandhari ya msitu husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na unyanyasaji mkubwa sana hasa kwa mama ntilie, bodaboda, akinamama wanaouza mbogamboga na matunda pamoja na watu wenye ulemavu. Halmashauri zetu hasa Wakurugenzi wanawatoza ushuru watu hawa bila huruma pamoja na kuwatolea maneno yasiyofaa, kubwa zaidi kuwaongezea ushuru kila uchao. Niiombe Serikali yangu Tukufu iwaonye Wakurugenzi hawa ili wasiendelee kuwanyanyasa wapiga kura wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, sisi Wabunge tunapowaambia Wakurugenzi hawa wanatudharau na kutuita wanasiasa hatuna lolote. Kwa hiyo, niishauri Serikali yangu sisi Wabunge tunapoleta matatizo ya Wakurugenzi, tunaomba yafanyiwe kazi haraka na ikiwezekana mhusika achukuliwe hatua, zaidi ya hapo, majimbo yetu yatakuwa hatarini kuyakosa. Kibaya zaidi Wakurugenzi wengi ni wanasiasa pamoja na hayo wanarubuniwa na baadhi ya wanasiasa walioshindwa ili amharibie Mbunge ambaye yupo madarakani ashindwe au aonekane hafai.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mazao ya biashara kama pamba, kahawa, korosho, tumbaku pamoja na katani. Mazao haya yamesahaulika wakati ndiyo yanatoa pato kubwa katika Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali yangu Tukufu kuhusu TRA. Mzigo unapoingia kutoka nje huwa unatozwa ushuru/kodi, ukitoka bandarini ukifika sehemu kama Kariakoo, TRA tena wanachukua kodi, ukipakiwa kwenda mikoani TRA wanachukua kodi, mwisho wa siku biashara hii inamfikia mtumiaji kwa bei ya juu. Kwa hiyo, niishauri Serikali ipunguze mzigo huu wa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna suala la motor vehicle licence, huwa inakatwa au inalipiwa kila mwaka lakini kuna watu wana magari ambayo yameharibika kwa muda mrefu mpaka limefikia kuchakaa mtu anaamua kuliuza kama skrepa. Cha ajabu mtu huyu anapofika TRA kwa ajili ya kuripoti ili arudishe kadi ya gari anaambiwa unadaiwa lazima ulipe, hii inasumbua sana watu wengi na ukizingatia walio wengi hawana uwezo tena. Kwa hiyo, niishauri Serikali iliangalie suala hili upya ili wananchi wetu ambao hawana uwezo wasije wakachukua maamuzi ambayo hawajayapanga na kama kuna uwezekano ifutwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nimtakie Waziri afya njema pamoja na timu yake kwa ujumla.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati wote wawili kwa kuwasilisha hoja zao vizuri. Pia ni-declare interest kwamba na mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu tulitembelea mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Mji Mpya Kigamboni, lakini mradi ule haujatengewa hata shilingi tano. Sasa basi niishauri Serikali ili jengo lile lisiendelee kulipa kodi wala wafanyakazi basi nadhani mradi ule urudishwe sasa kwenye Halmashauri ya Kigamboni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tulitembelea mradi wa utafiti wa nyumba bora na vifaa vya ujenzi. Kwa kweli kama tuna nia ya dhati tuwezeshe wakala wale wa nyumba na vifaa vya ujenzi. Tulifika pale wataalam walikuwa hata sita hawafiki, lakini vitu wanavyofanya ni vitu vikubwa sana. Sasa niishauri Serikali yangu kwamba wataalam wale wapewe uwezo ili waongezeke, waende mpaka Wilayani, naamini kabisa kwamba wataalam wale wakiongezeka na wakifika Wilayani vijana wetu watapata ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefika pale wanatengeneza vigae na tofali. Vigae vile wanatengeneza kwa nyuzi za katani, huoni sasa wataalam wale wakiwa wengi wataenda Wilayani mpaka vijijini na kwenda kufundisha vijana wetu wale na hao vijana wakishapata taaluma ile basi waende kwenye Halmashauri wajisajili ili kazi za Halmashauri zikitokea waanze kupewa kazi na kuanzakujenga majengo kama ya zahanati, maabara, shule na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mradi nimeuona ni mradi mzuri sana. Naamini kama kweli Serikali yetu tukufu ina nia ya dhati basi iwekeze kwenye mradi ule. Wakala wale ni wa kweli wanafanya kazi nzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la migogoro ya ardhi. Migogoro ya ardhi ni kitu ambacho kimekithiri hapa nchini kwetu Tanzania. Sina imani kabisa kwamba migogoro hii inaweza kuisha kwa jinsi tunavyoenda sasa. Niishauri tu Serikali yangu kwamba kama tunataka migogoro hii iishe basi tuhakikishe kwamba tunaandaa utaratibu mzima wa maeneo yote ya hapa nchini yanapimwa na watu wanapata hati zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuhakikishe kwamba watu wetu wa Wilayani hususan Maafisa Ardhi wanapewa zana na vifaa vya kutosha kuweza kupima ardhi hii kwa haraka. Mheshimiwa Waziri wa Ardhi na Dada yangu Naibu Waziri wa Ardhi Mheshimiwa Angeline Mabula wanafanya kazi moja nzuri sana kiasi kwamba hata Watanzania walio wengi wanaimani kubwa sana nao. Walitutangazia kwamba wameshafuta mashamba zaidi ya 200 lakini kuna shamba la mwekezaji mmoja kule Mnazi anaitwa Renash Enterprises Plot No. 292, title deed 11,247 ekari 2,442; na title deed 1746 ekari 1,188; title deed 4144 yenye ekari 562.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kushangaza mwekezaji yule analima tu eneo hili tena eneo kidogo sana ambalo ni ekari 562. Eneo lote lililobaki amelitelekeza, ni vichaka, kuna mapori makubwa ambayo kwa kweli hayastahili kuwa pale wakati watu wana shida ya ardhi. Nimuombe Waziri wangu na Naibu Waziri wa Ardhi, title hizi zifutwe na mpaka sasa taratibu zilishafuatiliwa lakini naambiwa kwamba Ofisi ya Ardhi Kanda ya Kaskazini bado hati ile haijafutwa. Sasa nimuombe Waziri wangu atakapoamka ku-wind up basi aniambie kwamba hati ile itapatikana lini ili Halmashauri yangu iendele kupata mapato yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie kwenye kilimo, naishauri tu moja kwa moja Serikali ijenge mabwawa mengi ya kutosha hapa nchini kwa ajili ya wakulima waweze kulima kilimo cha kisasa na cha umwagiliaji. Pamoja na hayo, wapeleke pembejeo kwa wakati pia hakuna asiyefahamu kwamba Lushoto ni ya wakulima wa matunda na mboga mboga, wakulima wale wanachangia sana kwa kutoa ushuru mwingi Halmashauri, lakini Serikali sijawahi kusikia Serikali inatenga ruzuku za pembejeo kuwapa wakulima wale wa matunda na mboga mboga. Ninaishauri Serikali yangu kwamba iwatengee wakulima wale wa mboga mboga na matunda nao waweze kupata ruzuku ya pembejeo.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la maji. Kama inavyofahamika maji ni janga la Kitaifa basi nashauri kwa kuwa EWURA wanatoza pesa kupitia nishati hii ya mafuta, niiombe sasa EWURA itenge asilimia 50 kwa ajili ya kupeleka maji vijijini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu
Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze
kuchangia hoja ambayo ipo mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze
Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ambayo imesheheni
mambo mazuri. Pia nipongeze Kamati zote tatu kwa maana
ya Kamati ya UKIMWI, Kamati ya Katiba na Kamati ya Sheria
na Bajeti kwa kuwasilisha vizuri maoni yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nimshukuru
Mwenyezi Mungu pamoja na ninyi, ambaye ametujalia afya
na nguvu kuweza kuhudhuria na kusema chochote katika
Bunge lako hili Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa
moja katika kuchangia na nianze na afya. Kama
unavyofahamu Chama chetu cha Mapinduzi ambacho
ndiyo chenye Serikali Ilani inasema kila kata itajengwa kituo
cha afya na kila kijiji itajengwa zahanati. Kwa kuzingatia hilo
sasa kwenye Jimbo langu la Lushoto nimebahatika kujenga
zahanati kumi na tatu na vituo vya afya viwili. Zahanati
karibia tatu zimeisha zinahitaji madaktari na nyingine kama
tano zimepigwa bati lakini bado usafi na zilizobaki bado
zinahitaji kumaliziwa. Kwa hiyo, sasa niombe Serikali yako
Tukufu kwamba ipeleke pesa katika halmashauri ili iweze
kumalizia zahanati zile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Lushoto ina
Majimbo matatu na Hospitali ya Wilaya moja. Takribani
Wilaya ya Lushoto ina wakazi zaidi ya laki sita lakini hospitali ile imehemewa yaani inajaza kiasi kwamba kwa kweli sijui
nieleze nini. Niiombe Serikali na niishauri katika bajeti hii
inayokuja basi watenge bajeti ya kutosha ili Hospitali ile ya
Wilaya iweze kupanuliwa hususan chumba cha akina mama
wajawazito na chumba cha mama na mtoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nielekee kwenye kilimo.
Niiombe Serikali yangu tukufu ijielekeze katika sekta ya kilimo
kwani kama tunavyofahamu kilimo ndiyo uti wa mgongo
wa Taifa letu hili na kimebeba takribani asilimia sabini.
Niiombe Serikali yangu itenge mafungu ya kutosha katika
kilimo na pia iwawezeshe wakulima wetu wadogo wadogo
hawa hususan wa vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Lushoto ni ya
milima na mabonde, ni ya wakulima wa bustani mfano
mbogamboga na matunda. Wakulima wale wanachangia
asilimia kubwa katika Halmashauri zetu lakini cha kushangaza
hawapati pembejeo. Niiombe Serikali sasa kwa jicho la
huruma iwaangalie wakulima wale wa mbogamboga
hususan wale waishio Lushoto waweze kupata pambejeo.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hayo
naiomba Serikali iweze kujenga mabwawa katika Wilaya ya
Lushoto kwani mvua nyingi sana zinanyesha kule lakini
zinaharibikia baharini. Kwa hiyo, niiombe Serikali sasa ijenge
mabwawa ili wananchi wetu waweze kulima kilimo cha
umwagiliaji. Pia hii itakuwa ni fursa kwa vijana wetu na ili
wasikimbilie mjini basi tuwajengee miundombinu ili waweze
kujiajiri wenyewe na kulima kilimo cha umwagiliaji. Naamini
hii italeta tija kwa vijana wetu na wala hawatakimbilia mjini.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye miundombinu.
Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Mbarawa kwa kazi
kubwa anayoifanya. Ila nimuombe sasa kuna barabara hiyo
tangu ninasoma darasa la kwanza kila siku naambiwa
itapanda hadhi, lakini haipandi. Barabara hiyo imeanzia
Mlalo - Ngwelo - Mlola - Makanya ikaenda mpaka kwa mzee wangu Mheshimiwa Kitandula. Nimuombe sasa
Mheshimiwa Waziri Mbarawa hebu afumbe macho tu
barabara ile ipandishwe hadhi kwani ni muda mrefu sana
na kila nikisimama kwenye Bunge lako Tukufu naisemea
barabara ile. Kwa heshimiwa kubwa na taadhima niliyokuwa
nayo kwake nimuombe basi barabara safari hii ipandishwe
hadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara zetu za
mchepuko. Kama unavyofahamu Lushoto ni ya milima na
mabonde kwa hiyo Lushoto bila barabara kwa kweli hatuwezi
kusafiri. Lushoto kuna barabara kuu moja tu ikipata
breakdown basi sisi Lushoto tumekwisha hata mahitaji
tunashindwa kupata. Kwa hiyo, niiombe Serikali yako Tukufu
sasa Mheshimiwa Mbarawa kwamba kuna barabara
ambayo inatoka Dochi - Ngulwi mpaka Mombo ni ya
mchepuko na itakuwa mbadala kwa ajili ya breakdown
itakayotokea maeneo ya Soni - Mombo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara aliahidi
Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne kilometa nne mpaka
sasa sijapata maelezo yake. Niiombe sasa Serikali yako Tukufu
hebu tuweze kupatiwa kilometa nne zile angalau tuweze
kutengeneza Mji wetu wa Lushoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sasa Serikali hususan
Waziri wa TAMISEMI kwamba zile barabara ambazo zipo
Halmashauri zirudi kwa Wakala wa Barabara yaani
TANROADS. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna hii Idara ya
Ardhi kule Halmashauri nayo irudi kwa Mkuu wa Wilaya kwa
sababu ndiye anayesuluhisha migogoro ya ardhi zaidi kuliko
Halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu; Wilaya ya Lushoto
kama nilivyosema ina Majimbo matatu lakini haina chuo cha
VETA. Kwa hiyo, nimuombe mama yangu mpendwa Waziri
wa Elimu atujengee hata chuo kimoja cha VETA kwani maeneo yapo tayari, kuna karakana, gereji na majengo
mengine. Kwa hiyo, nimuombe Waziri wangu huyu aweze
kuliona hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefanikiwa kujenga
maboma zaidi ya ishirini, lakini bado hayajaezekwa kwa
maana ya kupigwa bati. Sasa basi niiombe Serikali yako na
Waziri wa TAMISEMI apeleke pesa za kutosha kule kwenye
Halmashauri ili maboma yale ambayo tumeyajenga kwa
nguvu za wananchi tuwape moyo wasije kukata tamaa juu
ya hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la umeme; kwanza
nimpongeze kaka yangu Mheshimiwa Muhongo kwa kazi
kubwa anayoifanya na Naibu wake, ila nimuombe kitu
kimoja maana tunapata maswali magumu sana kule vijijini,
unakaa tu hapa Bungeni unapigiwa simu haya vijiji vingapi
vimepata umeme unawaambia jamani bado hata orodha
hatujaipata. Kwa hiyo, nimuombe Waziri wangu sasa niweze
kupata ile orodha ya vijiji ili niweze kuwajibu watu wangu
wale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ajira kwa vijana; kama
unavyofahamu sasa hivi vijana ni wengi mno hususan vijana
wa bodaboda na wauza mitumba.
Kwa hiyo, niiombe Serikali sasa wajengewe uwezo ili
waweze kujiajiri wenyewe na kama unavyofahamu sasa hivi
vijana wengi wemejiunga na vikundi na wana SACCOS zao.
Pia hizi SACCOS naomba ziundwe kisheria ili zitambulike na
kukopesha hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kuunga
mkono hoja.