Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Shabani Omari Shekilindi (36 total)

MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Barabara ya kutoka Mlalo kupitia Ngwelo – Mlalo – Makanya – Mlingano – Mashewa ni ya muda mrefu sana na ipo chini ya halmashauri licha ya kwamba barabara hiyo ni kichocheo cha uchumi kwa Majimbo manne:-
Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kupandisha hadhi barabara hiyo na kuwa chini ya TANROADS?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, maombi ya kupandishwa hadhi barabara ya Mlalo – Ngwelo – Makanya – Mlingano hadi Mashewa kuwa barabara ya mkoa yanaendelea kufanyiwa kazi na Wizara yetu sambamba na maombi kutoka mikoa mingine. Aidha, kutokana na umuhimu wa barabara hiyo, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) itaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hiyo kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Wilaya ya Lushoto ni miongoni mwa Wilaya kubwa na Kongwe nchini ambapo ina takribani watu laki tatu lakini haina Mahakama ya Ardhi hivyo Wananchi hufuata huduma hiyo hadi Wilaya ya Korogwe licha ya kwamba majengo tunayo:-
Je, ni lini Serikali itaanzisha Mahakama hiyo katika Wilaya ya Lushoto ili kuwapunguzia adha wananchi wake wanaofuata huduma hiyo Wilayani Korogwe?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Shekilindi naomba Waheshimiwa Wabunge wafahamu kuwa, lengo la Serikali la kuunda Mabaraza ya Ardhi katika kila Wilaya ni kusogeza huduma za utatuzi wa migogoro ya ardhi karibu na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua hilo, katika mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali kupitia Wizara yangu kupitia Gazeti la Serikali Namba 545 ilitangaza kuanzisha jumla ya Mabaraza 47 ambayo yataundwa nchini likiwemo Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Lushoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu na unyeti wa utatuzi wa migogoro ya ardhi katika Wilaya Kongwe ya Lushoto tarehe 6 Julai, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alizindua rasmi Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Lushoto. Kuanzia tarehe hiyo, Baraza limeshaanza kutoa huduma kwa wananchi wote wa Wilaya ya Lushoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kwa kutupatia jengo kwa ajili ya uanzishwaji wa Baraza hilo. Vilevile nitoe wito kwa Wakurugenzi wote nchini kuharakisha kutoa majengo kwa ajili ya ofisi za Mabaraza ili huduma hii muhimu iweze isogezwe karibu na wananchi na kuweza kupunguza kama siyo kumaliza kabisa kero mbalimbali za migogoro ya ardhi nchini.
MHE. MBONI M. MHITA (K. n. y. MHE. SHABAN O. SHEKILINDI) aliuliza:-
Jimbo la Lushoto linakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji hususan katika maeneo ya Umiri, Makanya, Kwemashai, Gare, Mlola, Mbwei, Malibwi na Kilole:-
Je, ni lini Serikali itawapatia wananchi hao maji safi na salama ili waondokane na adha hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omar Shekilindi, Mbunge wa Jimbo la Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutatua tatizo la maji Halmashauri ya Lushoto, inatekeleza mradi wa maji wa Mlola ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 50, mradi wa maji wa Malibwi umefikia asilimia 85 wakati miradi ya maji katika maeneo ya Kwemashai na Ngulu umefikia asilimia 15.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji Ubiri ulijengwa mwaka 1972 na unahudumia watu 2,013. Hata hivyo, huduma ya maji inayotolewa haitoshelezi mahitaji, hivyo Halmashauri ina mpango wa kutoa maji kutoka Kijiji cha Ngulu pindi mradi wa Ngulu utakapokuwa umekamilika bila kuathiri malengo yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha miradi katika Vijiji vya Makanya, Kilole na Mbwei imewekwa katika mpango wa utekelezaji wa program ya maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya Pili. Mradi wa Gare ambao unahitaji kufanyiwa upanuzi na kuongeza idadi ya vituo vya kuchotea maji utaingizwa katika mipango ya Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa kuwaondolea adha ya upatikanaji wa maji katika Mwaka wa Fedha 2016/2017, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 3.4 ili kukamilisha miradi inayoendelea kutekelezwa.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Wilaya ya Lushoto ina hospitali moja ya Wilaya ndani ya Halmashauri mbili na Majimbo matatu, hospitali hii inategemewa na watu zaidi ya 500,000.
Je, ni lini Serikali itaifanyia upanuzi hospitali hiyo hasa wodi ya akina mama wajawazito?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omar Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto imepanga kufanya upanuzi wa miundombinu ya Hospitali ya Wilaya katika mwaka wa fedha 2016/2017 ambapo zimetengwa shilingi milioni 50 kwa awamu ya kwanza. Fedha hizo zitatumika kujenga jengo ambalo litakuwa kwa huduma za mama na mtoto, zikiwemo wodi za wajawazito. Hadi kukamilika jengo hilo linatarajiwa kugharimu shilingi milioni 350.
Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali ni kuimarisha vituo vya afya vilivyopo ili viweze kuwa na uwezo wa kufanya upasuaji mdogo wa dharura hasa kwa mama wajawazito ili kupunguza msongamano katika Hospitali ya Wilaya.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Serikali iliahidi kujenga vyuo vya VETA kwa kila Wilaya ili kuwasaidia vijana kujifunza stadi za kazi mbalimbali:-
Je ni lini Chuo cha VETA kitajengwa katika Wilaya ya Lushoto?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shaaban Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaanza ujenzi katika Wilaya ya Lushoto mara baada ya kukamilisha miradi ya Vyuo vya VETA iliyoanzwa. Vyuo hivyo ni pamoja na Ludewa, Namtumbo, Kilindi, Chunya, Ukerewe, hiyo ni kutokana na tatizo la upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inashauri kwamba wakati juhudi mbalimbali zinaendelea za kutafuta fedha na ufadhili wa kujenga vyuo, wananchi wa Lushoto waendelee kutumia Chuo cha VETA kilichopo katika Mkoa wa Tanga na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) vilivyopo Muheza na Handeni na vyuo vingine vilivyosajiliwa na Mamlaka ya VETA nchini.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU) kilichopo Lushoto kwa mafanikio makubwa kimeweza kutumia teknolojia rahisi inayoitwa Grapho Game, kwa kiswahili ni Grafo Gemu kupunguza idadi kubwa ya wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika darasa la kwanza na la pili katika shule kadhaa zilizopo Wilaya ya Lushoto na Bagamoyo na pia SEKOMU kwa kutumia teknolojia hiyo imewezesha watu wazima kujua kusoma na kuandika katika kijiji cha Kwemishai – Kibohelo – Lushoto.
(a) Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka sasa kuwatumia wataalam walioko SEKOMU akiwemo mtalaam aliyeshiriki kutayarisha maudhui katika teknolojia ambayo imeweka msisitizo katika mbinu za kufundishia kusoma ya kifoniki ambayo hujikita katika utambuzi wa sauti za herufi zinazounda maneno?
(b) Je, Serikali haioni ni jambo muhimu kabisa kwa kupitia mpango huu muhimu na maalum kama walivyofanya nchi ya Zambia na Finland kuidhinisha matumizi ya teknolojia hiyo iwe kama teknolojia suluhisho (IT Solution) kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa madarasa ya mwanzo ya elimu ya msingi wenye changamoto ya kujua kusoma na kuandika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Seriakli inatambua umuhim,u wa kuimarisha stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa wanafunzi wanaosoma madarasa ya chini hususan elimu ya awali, darasa la kwanza hadi darasa la nne na watu wazima wasiojua kusoma na kuandika kwa kuwa stadi hizo zinawawezesha kupata umahiri katika stadi za KKK.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itawasiliana na mtaalam wa Grafo Gemu (kiswahili) ili kufahamu jinsi teknolojia hiyo inavyofanya kazi. Wizara itakapojiridhisha na ufanisi wa matumizi ya teknolojia hiyo, itafuata taratibu stahiki na kuidhinisha matumizi ya teknolojia hiyo shuleni.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Jimbo la Lushoto linakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji hususan katika maeneo ya Ubiri, Makanya, Kwemashai, Gare, Mlola, Mbwei, Malibwi na Kilole:-
Je, ni lini Serikali itawapatia wananchi hao majisafi na salama ili waondokane na adha hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omar Shekilindi, maarufu kama Bosnia, Mbunge wa Jimbo la Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Vijij vya Ubiri, Makanya, Kwemashai, Gare, Mlola, Mbwei, Malibwi na Kilole. Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi katika vijiji hivyo ambapo kwa mradi wa Mlola ujenzi wake umefika 85%; miradi ya maji katika maeneo ya Kwemashai na Ngulu imefikia 75%; wakati mradi wa maji Malibwi umekamilika na wananchi wanapata huduma ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji wa Ubiri ulijengwa Mwaka 1972 ili kuwahudumia wakazi 2,013. Hata hivyo kutokana na ongezeko la wakazi huduma ya maji inayotolewa kwa sasa haitoshelezi mahitaji. Hivyo Halmashauri ina mpango wa kutoa maji kutoka Kijiji cha Ngulu pindi mradi wa kijiji hicho utakapokuwa umekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Gare ambao ulijengwa na Wamisionari Mwaka 1978 haukidhi mahitaji ya sasa, hivyo Halmashauri imeuweka kwenye mpango wa kuufanyia upanuzi na usanifu wa kina ili kuuongezea uwezo na idadi ya vituo vya kuchotea maji. Aidha, miradi katika Vijiji vya Makanya, Kilole na Mbwei imewekwa katika mpango wa utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji awamu ya pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa lengo la kuwaondolea adha ya upatikanaji wa maji wananchi wa Halmashauri ya Lushoto, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.66 kwa ajili ya Halmashauri hiyo kukamilisha miradi inayoendelea kutekelezwa pamoja na kuanzisha miradi mipya.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Wilaya ya Lushoto haina Chuo cha Ufundi (VETA) na kuna vijana wengi waliohitimu elimu ya msingi na sekondari:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga Chuo cha Ufundi (VETA) ili vijana hao waweze kupata elimu ya ufundi ya kuwasaidia katika kujiajiri?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kwa ajili ya kuandaa rasilimali watu watakaotumika katika viwanda ili kufikia lengo la Serikali kuwa na uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025. Vyuo hivi vitasaidia kuwaandaa vijana kwa kuwapatia ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa ikizingatiwa kuwa kundi kubwa la vijana wetu halipati fursa ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na mpango wake wa ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vya Mikoa na Wilaya ikiwemo Lushoto kutegemeana na upatikanaji wa fedha. Lengo ni kila Mkoa na Wilaya kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi.
Mheshimiwa Spika, aidha, pamoja na ujenzi wa vyuo hivyo, Wizara itaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Kukuza Stadi za Kazi (Education and Skills for Productive Jobs – ESPJ) ambapo katika mradi huu Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vitakarabatiwa ili kuongeza fursa za mafunzo ya ufundi stadi sambamba na elimu ya wananchi. Hivyo, katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea na jitihada hizi, nashauri wananchi wa mikoa na wilaya zote ambazo hazijawa na vyuo vya VETA kutumia vyuo vya ufundi vilivyopo nchini hususan kwenye mikoa na wilaya jirani ili vijana wetu wapate ujuzi na stadi hizi muhimu kwa maendeleo yao na nchi kwa ujumla.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Kata za Gare, Kwai, Kwemashai, Makanya, Kilole, Ngwelo na Ubiri hazikufikiwa na REA III mpaka sasa:- Je, ni lini sasa Serikali itafikisha umeme kwenye kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Alhaji Shaabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza Miradi ya Kupeleka Miradi ya Umeme Vijijini kupitia Wakala wa Nishati (REA). Mradi wa REA III mzunguko wa kwanza ulianza Julai, 2017. Vijiji vitakavyopelekewa umeme kwenye Jimbo la Lushoto ni pamoja na Magamba, Kwegole, Kwehungulu, Kwebarabara, Maboi, Milemeleni, Kungului, Shume A, Makunguru, Shume B, Ngazi, Mhezi, Kwezindo, Kweboi, Nkelei, Viti, Langoni B, Vuli A na Kwemakulo, Mradi huu unatarajiwa kukamilika Juni, 2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya mradi huu zinahusisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 5.67, njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 46, ufungaji wa transfoma 23 za 50 kVA pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 520. Gharama za mradi ni shilingi bilioni 1.9.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vijiji vya Kata ya Gare, Kwai, Kwemashai, Makanya, Kilole, Ngwelo na Ubiri vitapatiwa umeme katika mzunguko wa pili wa mradi wa REA III utakaoanza Julai, 2019 na kukamilika Juni, 2021. Ahsante.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Wilaya ya Lushoto ina hospitali moja ya Wilaya ambayo inabeba mzigo mkubwa sana wa watu. Aidha, wodi ya wajawazito ni chumba kidogo sana na hakuna kabisa wodi ya mama na mtoto. Je, ni lini Serikali itajenga vyumba hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Hospitali ya Wilaya ya Lushoto bado ina changamoto ya msongamano katika wodi za akina mama wajawazito kwa sababu haina eneo la kutosha kukidhi wingi wa akina mama wajawazito wanaohudumiwa. Wodi ya akina mama wajawazito iliyopo imetokana na uamuzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kubadilisha matumizi ya baadhi ya majengo ili yatumike kama wodi ambapo jumla ya shilingi milioni 30 zilitumika katika mwaka wa fedha 2016/2017 kutengeneza wodi tatu ndogo ndogo yaani wodi ya akina mama wajawazito kabla ya kujifungua, wodi ya akina mama wajawazito baada ya kujifungua yenye uwezo wa kuhudumia akina mama sita kwa wakati mmoja, chumba cha upasuaji chenye vitanda vitatu vya upasuaji na wodi ya akina mama na watoto wachanga baada ya kujifungua kwa kawaida au upasuaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kukabiliana na changamoto hiyo, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepeleka shilingi milioni 400 katika Kituo cha Afya cha Mlalo; shilingi milioni 500 katika Kituo cha Afya cha Mnazi na shilingi milioni mia tano katika Kituo cha Afya cha Kangagae.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa matumizi ya fedha hizo ni kujenga vyumba vya upasuaji, wodi za mama na mtoto kabla na baada ya kujifungua na maabara kwa lengo la kuboresha huduma kwa mama wajawazito ikiwemo huduma za dharura za upasuaji kwenye maeneo hayo, hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano kwenye Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa wodi ya kisasa ya wajawazito (maternity complex) ni miongoni mwa vipaumbele vya juu vya Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ndiyo maana katika mwaka wa fedha 2018/2019 imetenga shilingi milioni 25 kuanzisha ujenzi unaotarajiwa kukamilika mwaka 2019/2020.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Wilaya ya Lushoto imezungukwa na misitu lakini misitu mingi imeungua kwa moto:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kurudisha uoto ule wa asili uliopotea kutokana na misitu kuungua?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, misitu iliyoungua moto katika kipindi cha kuanzia Agosti, 2016 hadi Februari, 2017 ni mitano ambayo ina jumla ya hekta 357.05 kati ya misitu 11 ambayo ina jumla ya hekta 22,855. Misitu hiyo ni Msitu wa Hifadhi Asilia Magamba wenye jumla ya hekta 9,381, zilizoungua ni hekta 338; Msitu wa Mkussu wenye hekta 3,674, zilizoungua ni hekta 3.8; Msitu wa Shagayu wenye hekta 7,830, zilizoungua ni hekta 2.75; Msitu wa Baga I wenye hekta 3,572, zilizoungua ni hekta 12; na Msitu wa Ndelemai wenye hekta 1,421, zilizoungua ni hekta 10.5.
Mheshimiwa Naibu Spika, misitu ya asili iliyoungua au kuharibiwa inaweza kurejeshwa kwa namna mbili. Mosi, kupanda miti maeneo yaliyoungua; na pili, kuliacha eneo liote miti lenyewe kwa kutofanya shughuli zozote za kibinadamu. Njia ya kwanza hutumika zaidi kwenye misitu ya kupandwa. Kutokana na asili ya eneo la Lushoto, njia nzuri zaidi ya kurudishia miti eneo lililoungua ni kuacha kufanya shughuli zozote za kibinadamu ili uoto wa asili urejee wenyewe. Aidha, kupanda miti isiyo ya asili ndani ya misitu ya hifadhi unaharibu uasilia wa msitu na huenda ukaleta matokeo hasi katika uoto wa asili uliopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia Wakala wa huduma za Misitu Tanzania unaendelea kutoa Elimu kwa jamii ili wananchi wanaoishi jirani na misitu ya hifadhi wawe makini wanapotumia moto wakati wa kusafisha mashamba yao, kwani chanzo kikuu cha moto wote uliounguza misitu katika kipindi hiki umetokana na wananchi kutayarisha mashamba yao bila kuchukua hatua za tahadhari.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Kuendesha bodaboda ni ajira kama zilivyo ajira nyingine nchini:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea uwezo vijana hao ili kuifanya kazi hiyo iwe rasmi na yenye kutambulika kama kazi nyingine zozote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika kutambua bodaboda kama mojawapo ya usafiri wa kubeba abiria nchini kisheria, mwaka 2017 ilifanya marekebisho ya Kanuni za Usafirishaji za Mwaka 2010 ambapo waendesha bodaboda walirasimishwa kwa kupatiwa leseni za usafirishaji. Leseni hizo zinatolewa na Mamlaka za Miji, Wilaya na Majiji kwa niaba ya SUMATRA ili kuhalalisha shughuli za uendeshaji bodaboda.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuwajengea uwezo waendesha bodaboda, Serikali inatekeleza mipango ifuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kutoa mafunzo ya udereva kupitia Jeshi la Polisi kwa waendesha bodaboda na hatimaye kupatiwa leseni za udereva. Aidha, kama ilivyo katika vyombo vingine vinavyotoa huduma za usafirishaji, usalama wa waendesha bodaboda na abiria umeendelea kusimamiwa na kulindwa wanapotekeleza majukumu yao barabarani.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhamasisha uundwaji wa vikundi vya waendesha bodaboda ili hatimaye viweze kuwezeshwa kwa mitaji na mafunzo kupitia Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na wadau wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu ni kuwapatia maeneo ya kuegesha bodaboda na kuyatambua pamoja na kuwapatia vitambulisho na nne ni kuwapatia waendesha bodaboda mafunzo ya ujasiriamali na hatimaye kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu na kuwaunganisha na taasisi nyingine za fedha zinazotoa mikopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, ni kuwapatia elimu juu ya faida ya kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja na kuwaunganisha na mifuko husika.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Serikali imekuwa na utaratibu wa kukarabati shule zake za msingi na sekondari nchini:-

Je, ni lini Serikali itazifanyia ukarabati Shule za Msingi Kwemashai, Bandi, Milungui, Kilole na Shule za Sekondari za Ntambwe, Ngulwi - Mazashai na Mdando?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2018/2019, Serikali kupitia Program ya Lipa Kulingana na Matokeo (EPforR) imepeleka jumla ya shilingi milioni 467 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili, matundu sita ya vyoo na madarasa mawili katika Shule ya Msingi Shukilai (Shule ya Elimu Maalum) na ujenzi wa mabweni mawili Shule ya Sekondari Magamba, ujenzi wa bweni moja na madarasa mawili Shule ya Sekondari Umba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mwaka wa Fedha 2018/2019, Serikali imetoa shilingi bilioni 29.9 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma 2,392 ya madarasa nchi nzima ambapo kati ya fedha hizo Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto imepewa kiasi cha Sh.512,500,000 kwa ajili ya kukamilisha maboma 46 ya madarasa shule za sekondari. Serikali itaendelea kukarabati na kujenga miundombinu ya elimu kwa awamu kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Hospitali ya Wilaya ya Lushoto ni ya muda mrefu na hata ujenzi wa majengo yake ni wa kizamani ambao hauendani na utoaji huduma na Serikali ina utaratibu wa kukarabati na kuongeza majengo katika Hospitali za Wilaya:-

Je, ni lini Hospitali ya Wilaya ya Lushoto itakarabatiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Lushoto ni miongoni mwa Hospitali Kongwe za Wilaya nchini na imekuwepo tangu mwaka 1967. Tangu kuanzishwa kwake, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleleo imefanya ukarabati na upanuzi wa majengo kama ifuatavyo:-

(i) Mwaka wa fedha 2006/2007, ujenzi wa jengo la mapokezi, jengo la wagonjwa wa nje, jengo la famasi, jengo la maabara na jengo la upasuaji kupitia mradi wa KfW;

(ii) Kwa mwaka wa fedha 2008/2009, ujenzi wa jengo la kuhifadhia maiti kwa maana ya mortuary na uwekaji wa vigae (tiles) katika wodi zote;

(iii) Kwa mwaka wa fedha 2011/2012, ujenzi wa jengo kwa ajili ya ndugu wa wagonjwa kusubiria yaani waiting bay;

(iv) Kwa mwaka wa fedha 2014/2015, ukarabati mkubwa wa jengo la upasuaji;

(v) Kwa mwaka wa fedha 2016/2017, ukarabati wa jengo la mapokezi, jengo la wagonjwa wa nje, jengo la famasi, jengo la maabara, jengo la wodi ya watoto na ujenzi wa jengo la dawa za ziada la Halmashauri kwa maana ya buffer store;

(vi) Kwa mwaka wa fedha 2018/2019, ujenzi wa kichomea taka (Incinerator) na shimo la kutupia kondo la nyuma la uzazi kwa maana ya placenta pit;

(vii) Kwa mwaka wa fedha 2018/2019, ukarabati wa jengo la CTC linalovuja unaendelea kupitia ufadhili wa AMREF.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kukarabati miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya nchini kwa kadri upatikanaji wa fedha utakavyokuwa unaruhusu.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Wananchi wa Wilaya ya Lushoto wamejitahidi kujenga maboma mengi ya maabara lakini mpaka sasa Serikali haijawaunga mkono:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuunga mkono juhudi hizo za wananchi kwa kumalizia maboma haya?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFlSI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikisha nguvu za wananchi imekamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara 13 katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kati ya maabara 159 zinazohitajika.

Aidha, maabara 138 zinaendelea kujengwa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri na nguvu za wananchi. Katika mwaka wa fedha 2019/20, Halmashauri inaendelea na hatua za mwisho za ukamilishaji wa maabara katika Shule za sekondari za Mlongwema, Kwemalamba, Lukozi, Ngwelo na Shume zilizopatiwa shilingi milioni 5 kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R).
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Barabara ya Mlalo kupitia Ngwelo – Mlalo –Makanya- Mlingano mpaka Mashewa ni ya muda mrefu sana ipo chini ya halmashauri licha ya kwamba barabara hiyo ni kichocheo muhimu cha uchumi katika majimbo manne ya Lushoto, Mlalo, Bumbuli na Korogwe Vijiji.

Je, ni lini Serikali itaipandisha hadhi barabara hiyo na kuwa chini ya TANROADS kutokana na umuhimu wake kiuchumi kwa wananchi wa majimbo hayo?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali ninaomba kwenye jibu langu nifanye marekebisho kidogo Mheshimiwa Mbunge kuna kosa la kiuchapaji ni Mbunge wa Lushoto siyo Mbunge wa Bumbuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara iliyotajwa na Mheshimiwa Mbunge kwa sasa ni barabara ya wilaya inayohudumiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Serikali kuanzisha Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), imesitisha utaratibu wa kupandisha hadi barabara za Wilaya kuwa barabara za Mikoa (kwa kigezo cha kutohudumiwa ipasavyo) kwa vile TARURA imeanzishwa mahsusi kwa jukumu la kuendeleza barabara za wilaya nchini kikiwemo barabara ya Mlalo kupitia Ngwelo – Mlalo- Makanya – Mlingano mpaka Mashewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale inapobidi barabara kupandishwa hadhi, upandishaji wake utafanyika kwa kuzingatia vigeo vya kitaalam kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 13 ya Mwaka 2007 na kanuni zake za Mwaka 2009. Hivyo, Mheshimiwa Mbunge anashauriwa kufuata taratibu zilizoweka katika Sheria tajwa ili barabara hiyo ipandishwe hadhi.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka maji katika Kata za Kwai, Kilole, Kwekanga na Makanya katika Jimbo la Lushoto?
WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Jimbo la Lushoto kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutatua tatizo la maji katika Wilaya ya Lushoto, Serikali tayari imekamilisha miradi ya Maji katika vijiji vya Mlalo/Mwangoi, Mlalo/Lwandai, Malibwi na Ngulu. Wananchi katika vijiji hivyo tayari wanapata huduma ya majisafi na salama na miradi mingine ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa, Kata ya Kwai kuna mradi wa maji unaotoa huduma katika Kijiji cha Kwai. Aidha, Kata ya Kwai na Makanya zipo kwenye mpango wa muda wa kati wa utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji utakaotoa huduma ya maji katika vijiji 16 ambapo usanifu wake ulikamilika na kupata kibali cha utekelezaji. Mradi huo, umepangwa kutekelezwa katika mwaka ujao wa fedha wa 2020/2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Kata ya Kilole, Kwekanga na Makanya Wizara imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 57 kwa ajili ya kufufua visima vifupi vilivyopo ambavyo havifanyi kazi. Kazi hii itafanyika kupitia mpango wa malipo kwa matokeo (Payment by Results). Tayari vifaa vya ujenzi wa miradi hiyo vimenunuliwa na utekelezaji wa mradi unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Aprili 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa kuwaondolea adha ya upatikanaji wa maji wananchi, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.18 kwa Halmashauri ya Lushoto ili kukamilisha miradi inayoendelea kutekelezwa katika vijiji vya Shume, Manolo, Madala, Gologolo, Ngwelo ambayo itahudumia jumla ya watu 48,781.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI Aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuvipatia umeme vijiji 32 vya Jimbo la Lushoto ambavyo havina umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto na tabibu wetu humu ndani, kwa wale ambao tunaamini kikombe, kama ifuatavyo:- (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini kwa awamu kadri ya upatikanaji wa fedha. Malengo ya Serikali ni kufikisha umeme katika vijiji vyote vya Tanzania Bara ifikapo Desemba, 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iko katika hatua za mwisho kukamilisha maandalizi ya ujenzi wa mradi wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa pili (REA III round two). Kwa Wilaya ya Lushoto Mradi wa REA III mzunguko wa pili unapeleka umeme katika maeneo ya vijiji vyote 32 vya Jimbo la Lushoto ambavyo havikupata umeme kupitia miradi ya kusambaza umeme ya awamu ya pili na awamu ya kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi za mradi ya kusambaza umeme kwa Wilaya ya Lushoto zinajumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33; urefu wa kilomita 131.8; njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 0.4 umbali wa kilomita 381.9; ufungaji wa transfoma 99 za 50kVA; pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 1,984. Mradi unakadiriwa kugharimu shilingi bilioni 16.8. Utekelezaji wa mradi utaanza Februari, 2021 na kukamilika ifikapo Desemba, 2022.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga minara ya simu kwenye maeneo ambayo hayana mawasiliano ya simu katika Jimbo la Lushoto?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imetekeleza miradi ya ujenzi wa minara ya mawasiliano ya simu katika maeneo mbalimbali Wilaya ya Lushoto. Mpaka sasa kuna miradi 16 ya ujenzi wa minara katika Wilaya ya Lushoto katika kata 15 ambapo tayari miradi 8 imekamilika na miradi mingine 8 iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Miradi hiyo iko katika Kata za Baga, Kwai, Kwekanga, Malibwi, Malindi, Manolo, Mayo, Mbaramo, Mgwashi, Mlola, Mponde, Rangwi, Shume, Ubiri na Vuga. Miradi ya ujenzi wa minara katika Kata za Kwekanga, Kwai, Malindi, Manolo, Mbaramo, Mayo, Mponde na Mlola imekamilika na tayari inatoa huduma za mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa minara ya mawasiliano unaendelea katika Kata za Shume, Ubiri, Rangwi, Mgwashi, Vuga, Baga, Kwai na Malibwi. Ujenzi wa minara hii utakamilika mwezi Disemba 2021. Aidha, Kata zilizobaki Mfuko utazifanyia tathmini na zitaingizwa katika zabuni zijazo.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Jimbo la Lushoto lina Kituo kimoja cha Afya na sasa wananchi wameanza kujenga Vituo vya Afya viwili vya Gare na Ngwelo.

Je, Serikali ipo tayari sasa kutoa fedha kwa ajili ya kumalizia vituo hivyo na ni lini itafanya hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa za Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Jimbo la Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha huduma za afya katika Wilaya ya Lushoto kuanzia mwaka wa fedha 2017/ 2018 - 2019/2020, Serikali imetoa shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wodi ya wazazi katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto pamoja na ukarabati na upanuzi wa Vituo vya Afya vya Mlola, Kangagai na Mnazi ili kuviwezesha kutoa huduma za dharura za upasuaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Machi 2021, Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maboma matatu ya zahanati. Serikali inatambua na kuthamini juhudi za wananchi wa Jimbo la Lushoto katika ujenzi wa Vituo vya Afya. Serikali itaendelea kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya nchini, vikiwemo vituo vya afya vilivyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi Jimboni Lushoto kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza: -

Je ni lini Serikali itapeleka Watumishi wa kada ya Ualimu na Afya katika Wilaya ya Lushoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua mahitaji ya walimu na watumishi wa kada ya afya nchini kote ikiwemo Wilaya ya Lushoto. Wilaya ya Lushoto ina upungufu wa walimu kwa asilimia 44.4 na watumishi wa kada ya afya kwa asilimia 66.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali iliajiri watumishi 9,675 katika kada za afya na uwalimu ambapo Wilaya ya Lushoto ilipelekewa walimu 86 na watumishi wa kada ya afya 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la ajira ni endelevu na Halmashauri ya Lushoto itapewa kipaumbele. Ahsante.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Uwanja wa Michezo katika Mji wa Lushoto?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Taifa ya mwaka 1995 ibara ya 7(i) – (vii), jukumu la ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya michezo ni jukumu la Serikali Kuu, Mamlaka ya Serikali za Mitaa pamoja na Wadau wa Sekta ya Michezo zikiwemo Taasisi, Mashirika na Watu Binafsi. Hivyo, napenda kuzikumbusha na kuzielekeza halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Lushoto kuzingatia matakwa ya Sera ya Michezo kwa kutenga fedha kutoka katika mapato ya ndani kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu ya michezo kwenye maeneo yao. Ahsante.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha huduma za afya kwa Wazee badala ya kutumia Dirisha la Wazee ambalo linawatesa?
WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimuwa Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuimarisha huduma za afya kwaa wazee. Kwa miaka mingi wazee wamekuwa wakipatiwa huduma mahsusi kwa kupitia madirisha maalum ya huduma za afya kwa wazee yaliyotengwa katika vituo vya kutolea huduma za afya. Katika kuimarisha huduma za afya kwa wazee, Wizara katika Mwaka huu wa fedha 2022/2023 imepitishiwa muundo mpya ambao umewezesha Wizara kuanzisha seksheni ndani ya Kurugenzi ya Tiba inayoshughulika na Huduma za Afya ya Wazee, Huduma za Utengamao na Huduma za Tiba Shufaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, chini ya Seksheni hii mpya, Utaratibu wa huduma mbalimbali za afya ya wazee utafanyika na maboresho ya huduma za afya kwa wazee yatapokelewa na kuchakatwa na kupatiwa majawabu kwa wakati. Rasimu ya mwongozo wa utekelezaji wa mkakati wa huduma za afya kwa wazee ipo katika ngazi ya maboresho hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uzee na kuzeeka havikwepeki, Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuwaenzi wazee wetu.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati Mahakama ya Wilaya ya Lushoto?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshmimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Tanzania inaendelea kutekeleza kwa awamu Ujenzi na ukarabati wa majengo yake sehemu mbalimbali hapa nchini. Katika mpango huu, yapo majengo ambayo yanahitaji kujengwa upya kutokana na hali yake na ufinyu wa jengo ikilinganishwa na mahitaji ya sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kulingana na hali ya jengo la Mahakama ya Wilaya ya Lushoto, imeamuliwa kuwa jengo hili lijengwe upya badala ya kukarabatiwa lile jengo lililopo kwani ni la zamani sana, finyu na baadhi ya miundombinu yake hairuhusu ukarabati mkubwa. Hivyo, kulingana na Mpango, jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Lushoto litajengwa kwenye kipindi cha fedha 2024/2025. Aidha, kwa sasa jengo lililopo litaendelea kufanyiwa matengenezo madogo madogo hadi litakapopatikana jengo jipya.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza: -

Je, ni lini maeneo mengi ya Mji wa Lushoto yatapimwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, halmashauri ni mamlaka ya upangaji kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya mwaka 2007, hivyo majukumu ya kisheria ya kutenga bajeti, kwa ajili ya kupanga na kupima yapo ndani yao. Hata hivyo, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetoa mkopo wenye thamani ya shilingi bilioni 55.6 kwa halmashauri 55, Vyuo vya Ardhi vya Tabora na Morogoro na Chuo Kikuu Ardhi Dar es Salaam, kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ni miongoni mwa halmashauri zilizokopeshwa fedha hizo ambapo jumla ya shilingi milioni 208 zimetolewa kwa ajili ya kupima viwanja takriban 2,600 katika maeneo ya Lushoto Mjini, Mnazi, Mlola, Mlalo na Lukozi. Pamoja na jitihada hizi za Serikali, natoa rai kwa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto na Halmashuri zote nchini kuhakikisha kuwa zinatenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapa pembejeo wakulima wa mbogamboga nchini?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika msimu wa 2022/2023, Serikali imeendelea kutekeleza mpango wa utoaji wa ruzuku za viuatilifu, mbegu na mbolea kwa mazao yote yanayozalishwa nchini. Kwa kipekee utekelezaji wa mpango wa ruzuku ya mbolea ni kwa mazao yote ya nafaka, mbogamboga, mikunde na mazao mengine yote yaliyozalishwa na wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha wakulima ndio wananufaika na pembejeo za ruzuku, wanapaswa kujisajili kwa kuainisha mashamba na mazao anayozalisha na hivyo kuweza kununua pembejeo za ruzuku kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na Serikali. Lengo la Serikali kutoa ruzuku za pembejeo kwa mazao yote, ni kupunguza gharama kwa wakulima, kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza upatikanaji wa malighafi za viwanda.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua zao la kahawa Wilayani Lushoto?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya waziri wa kilimo ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Shaban Omari Shekilindi Mbunge wa Lushoto kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanzisha kitalu cha miche ya kahawa katika eneo la Jegestal ili kuwezesha upatikanaji wa miche kwa wakulima wa kahawa Wilayani Lushoto. Hadi kufikia tarehe 15 Mei, 2023 jumla ya miche 227,905 imezalishwa na imeanza kusambazwa kwa wakulima mwezi Mei, 2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania imekiwezesha Chama Kikuu cha Ushirika cha Usambara kuingia mkataba na Kampuni ya Mambo Coffee Company Ltd na kupata cheti cha kilimo hai (Organic Certification) kitakachowezesha chama hicho kuuza kahawa yake kwenye soko maalum. Hatua hizo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kufufua na kuendeleza kilimo cha zao la kahawa katika Wilaya ya Lushoto.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: aliuliza: -

Je, lini Serikali itapeleka maji safi na salama katika Kata ya Kwekanga?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Jimbo la Lushoto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua adha ya maji wanayoipata wakazi wa Kata ya Kwekanga yenye Vijiji vitano vya Kwekanga, Mziragembei, Bombo-Kamghoboro, Mategho na Mshangai. Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali katika Mwaka wa fedha 2023/2024, itafanya utafiti wa maji chini ya ardhi (Hydrogeological survey) pamoja na kuchimba visima virefu katika Kata za Kwekanga, Kwai, Kilole, Malindi, Makanya na Lushoto Mjini. Kazi hiyo inatarajiwa kufanyika na kukamilika mwezi Disemba, 2023. Uendelezaji wa visima hivyo utafanyika mara baada ya uchimbaji kukamilika na maji kupatikana.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Vituo vya Afya katika Kata ya Kwai na Makanya Lushoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Jimbo la Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 Serikali ilitenga shilingi bilioni 117 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya 234 kwenye Kata za kimkakati ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ambayo iliyotengewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Lunguza HC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuboresha miundombinu ngazi ya Afya ya Msingi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya afya kwenye Kata za kimkakati kote nchini zikiwemo Kata za Kwai na Makanya.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka Gari la Wagonjwa katika Kituo cha Afya cha Mlola Wilayani Lushoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Jimbo la Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mahitaji ya kuwa na magari ya wagonjwa kwenye Vituo vya Afya na Hospitali ili kurahisisha huduma za rufaa kwa wagonjwa. Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali imetenga shilingi bilioni 35.1 kwa ajili ya ununuzi wa magari 316 ya kubebea wagonjwa.

Mheshimiwa Spika, magari haya yameanza kupokelewa kwa awamu na yatagawiwa katika Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ambayo itapata magari mawili kwa ajili ya huduma za rufaa za wagonjwa.
MHE. SHABAN O. SHEKILINDI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Lushoto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Lushoto ni kituo cha daraja A kilianza kujengwa mwaka 2014 kwa gharama ya shilingi 417,000,000 na hatua iliyofikiwa ni umaliziaji. Ujenzi wa kituo hicho unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Juni 2022. Nashukuru.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza: -

Je, lini Serikali itakarabati shule chakavu za msingi katika Jimbo la Lushoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Jimbo la Lushoto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kufanya ukarabati wa shule chakavu nchini ikiwemo zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ambapo katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, Serikali imetoa shilingi milioni 796.5 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Shule ya Msingi Mshangai na Kwemshai katika Jimbo la Lushoto.

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2023/2024, Serikali imetoa shilingi milioni 180 kwa ajili ya ukarabati wa Shule Kongwe nne za Nyankei, Mhelo, Hemtoye na Mbaramo. Ahsante.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Je, lini Serikali itakarabati shule chakavu za msingi katika Jimbo la Lushoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Jimbo la Lushoto kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kufanya ukarabati wa shule chakavu nchini ikiwemo zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ambapo katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, Serikali imetoa shilingi milioni 796.5 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Shule ya Msingi Mshangai na Kwemshai katika Jimbo la Lushoto.

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2023/2024, Serikali imetoa shilingi milioni 180 kwa ajili ya ukarabati wa Shule Kongwe nne za Nyankei, Mhelo, Hemtoye na Mbaramo. Ahsante.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Je, TARURA ina mpango gani wa kujenga barabara kwenye kona kali na milimani kwa kutumia zege katika Jimbo la Lushoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto ya uwepo wa kona na miinuko mikali katika baadhi ya barabara za Jimbo la Lushoto. Kwa kutambua umuhimu wa barabara hizo, Serikali imekuwa ikitenga fedha na kujenga vipande vya matabaka ya zege katika maeneo yenye milima mikali na kona ili kuondoa changamoto ya upitaji kwa vyombo vya usafiri kwa kuzingatia vipaumbele na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2023/2024, TARURA inajenga tabaka la zege lenye urefu wa meta 900 katika Barabara ya Halmashauri ya zamani – Kwembago - Irente kwa gharama ya shilingi milioni 512.74. Aidha, katika mwaka 2024/2025, shilingi milioni 181.75 zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa maeneo yenye kona kali na miinuko katika Barabara ya Dochi - Gare kwa kujenga kwa tabaka la zege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha katika bajeti zijazo ili kuondoa changamoto hizi kwenye maeneo yenye milima na kona kali kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Je, ni lini wazee wanaostaafu watapata mafao yao kwa wakati?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mafao ya pensheni kwa wastaafu yanalipwa kwa mujibu wa Sheria zinazosimamia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambapo zinaelekeza mifuko kulipa mafao ndani ya siku 60 tangu mwanachama anapostaafu. Kwa sasa, mifuko imeboresha mifumo yao na wastaafu wote wanalipwa mafao yao kwa wakati ndani ya siku 60.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-

Je, lini Serikali itafanya upanuzi wa Barabara ya Mombo hadi Lushoto kwa kuwa ni nyembamba kiasi cha magari makubwa kushindwa kupita?
WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ukarabati kwa kiwango cha lami na upanuzi wa Barabara ya Mombo hadi Lushoto yenye urefu wa kilometa 31.36. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa barabara hiyo. Ahsante sana.