Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Hussein Nassor Amar (8 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuweza kusimama mahali hapa kwa siku ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ndiyo mara yangu ya kwanza kusimama kwenye Bunge hili la Kumi na Moja, napenda kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Nyang’hwale kwa kunipa kura nyingi sana za kishindo mimi pamoja na Waheshimiwa Madiwani. Kwa kipindi cha pili Halmashauri yetu iko ndani ya mikono ya CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, pia napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa Mpango wake mzuri ambao ameuweka hapa mezani. Pia napenda niseme jambo moja ambalo lilizungumzwa jana, upande wa upinzani walisema Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwenye kampeni zake alipiga push-up.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema kwamba zile zilikuwa ni mbinu, lakini hata ninyi kuna mizunguko mlikuwa mkiifanya, ile zungusha pamoja na helicopter nyingi kwenye Jimbo langu mara nne, lakini hamkufua dafu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kujielekeza kwa kuipongeza hotuba hii nzuri. Na mimi pia naungana na wenzangu kuhusu ujenzi wa reli. Ujenzi wa reli utaongeza mapato makubwa sana katika nchi yetu, lakini pia sisi wananchi tunaoishi pembezoni mwa nchi ni kwamba vifaa mbalimbali vitashuka bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa mfano, cement kwa Kanda ya Ziwa ni shilingi 18,000/=, shilingi 20,000/= mpaka shilingi 22,000/=; wakati Iringa Mheshimiwa aliyekuja kuwekeza nchini kwetu, Mheshimiwa Dangote, amesema kwamba cement itashuka bei mpaka shilingi 8,000/=. Kwa kupitisha kwa njia ya barabara, tutaendelea kuipata ile cement wananchi wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla kwa bei kubwa. Lakini pindi reli ile itaanza kufanya kazi, naamini kabisa kwamba cement na mazao mbalimbali kwa kuja Dar es Salaam na mali mbalimbali kutoka na kwenda Kanda ya Ziwa, zitashuka bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu ni mzuri, lakini kuna jambo moja naomba nishauri, kuna bwana mmoja na jeshi kubwa sana, hakuingizwa kwenye Mpango huu, naye anaitwa mzee watoto wa mitaani. Mpango huu haukuwekwa. Kwa nini? Kwa sababu jeshi hilo kila mwaka linaongezeka. Serikali ina mpango gani kupunguza watoto wa mitaani? Mtaa hauzai! Serikali ina mpango gani kuhusiana na suala hilo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Nyang’hwale, mimi nimekuwa Mbunge wao takriban huu ni mwaka wa sita, nimekuwa nikipigania tatizo kubwa la maji. Mkondo wa Ziwa Victoria unaanzia kwenye Jimbo la Nyang’hwale, lakini cha ajabu wananchi wa Nyanghwale hawana maji.
Mwaka 2013, Waziri Maghembe nilikataa kupitisha bajeti yake; bahati nzuri Serikali kupitia Benki ya Dunia tuliweza kupewa mradi huo wenye thamani ya fedha shilingi bilioni 15.7. Cha ajabu, mpaka leo hii pesa ambayo imetoka ni shilingi bilioni 1.8. Bajeti ya mwaka 2015/2016 tuliongezewa shilingi milioni 752 lakini fedha hiyo haijatoka. Sasa hivi Wakandarasi wamesimama, hawaendelei na kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, kwa mwaka wangu wa sita waje wamejipanga vizuri Wizara ya Maji. Sitakubaliana! Sisi wananchi wa Nyang’hwale tuna mkosi gani? Naiomba Serikali ya Chama cha Mapinduzi, ni Serikali sikivu.
Ndugu zangu, naomba nizungumzie suala la elimu bure. Naishukuru Serikali, imeanza kutekeleza; lakini kuna jambo moja sikuliona ndani ya Mpango kuhusu elimu. Kuna familia nyingine, kaya moja unaikuta inajaza darasa; lakini kuna kaya moja ina watoto wawili. Je, ndani ya Mpango huu, kaya moja ina watoto inajaza darasa moja, kaya mbili zinajaza madarasa mawili.
Ndugu zangu, tujaribuni kuliangalia; ndani ya Mpango tuwekeeni utaratibu mzuri. Yule ambaye ana watoto kuanzia 10, 20, au 30, awekewe naye Mpango mzuri. Nusu ichangie Serikali na nusu achangie. Hili suala ni la msingi sana. Kuna wengine wana wanawake kumi, wengine watano na wengine wamejaliwa kuzaa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alifanya ziara kwenye jimbo langu. Alikuja akaahidi Kituo cha Afya Kalumwa, kukipandisha kuwa Hospitali ya Wilayana tayari imeshapandishwa, lakini ukifika pale, hali ni mbaya! Kuna wodi ya akina baba ina vitanda nane. Wagonjwa wa aina zote wanalazwa mle. Naiomba bajeti hii inayokuja, Wizara ya Afya mje mmejipanga vizuri kwa ajili ya kuboresha hospitali yetu ya Wilaya ya Nyang’hwale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miundombinu, kwa kweli miundombinu ya Wilaya ya Nyang’hwale, kuna barabara moja ambayo imeahidiwa kuanzia mwaka 2010 alipokuja Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, alituahidi kutujengea barabara kutoka Busisi kupita Busorwa, kupita Karumwa, Nyang’hwale kupita Msala kwenda Kahama. Leo miaka mitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alikuja tena mwaka 2011 wakiwa katika msafara huo, Mheshimiwa Waziri Maghembe alikuwa yumo, Mheshimiwa Majaliwa alikuwa yumo, Mheshimiwa Rais wetu huyu wa sasa hivi wa Awamu ya Tano alikuwa Waziri wa Ujenzi na Mheshimiwa Jakaya Kikwete, walisimama na wakalizungumzia suala la barabara tutajengewa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwenye Mpango huu, barabara hii haimo. Naomba sasa hii awamu ya hapa kazi tu, atutekelezee. Anaielewa vizuri hiyo barabara, alituahidi akiwa Waziri na leo ni Rais wa nchi. Ninaomba ahadi ya Rais, iwekeni humo barabara hiyo kwenye Mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo. Wananchi wa Nyang’hwale tuna mabonde mazuri sana, tuna mito mingi, maji yale yanaporomoka yanakwenda Ziwani. Naomba tuweke mpango mzuri wa kuyatega yale maji yaweze kuwasaidia wakulima wetu. Tuweze kupata maji kwa mifugo na matumizi ya binadamu, pia tuweke mpango mzuri wa kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema tunataka tunyanyue viwanda vidogo vidogo, vya kati na vikubwa: Je, material hayo yatapatikana vipi? Sisi wananchi wa Nyang’hwale ni wakulima wa mpunga, tunategemea mvua za masika, lakini kama tutatengenezewa mabwawa mazuri, kwa umwagiliaji tutalima mara mbili au tatu na tutakuwa watu wazuri sana wa kuweza kuongeza kipato chetu kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa afya njema kwa siku ya leo na kuweza kusimama hapa. Pia nimshukuru Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa na Baraza lote la Mawaziri kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya ya kutumbua majipu. Ni kazi nzuri sana inayofanyika pamoja na kwamba wengine wanakasirika lakini ndiyo ilikuwa kiu ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kuunga mkono hotuba hii nzuri ambayo imesheheni mambo mazuri. Napenda niwakumbushe wenzetu Kambi ya Upinzani, kuna mchangiaji mmoja alisema kipindi cha nyuma kwamba ninyi wana CCM mnapenda sana kupongeza, mimi sipongezi, wakati Mwenyezi Mungu anasema usiposhukuru kidogo hata kikubwa hauwezi ukashukuru. Hata kwenye maombi kwanza unamshukuru Mwenyezi Mungu kwa alichokupa na unachohitaji unaendelea kuomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, napenda niikumbushe Serikali yangu Tukufu, tunaambiwa tunalalamika, hatulalamiki tunakumbushana. Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni kwenye Jimbo langu la Nyang’hwale tulimweleza matatizo yetu na akaahidi. Tulikuwa na ahadi ambayo tuliahidiwa na Rais wa Awamu ya Nne kuhusu barabara ya kutoka Kahama – Nyang’hwale - Busolwa - Busisi kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami. Pia alipokuja Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa kampeni nilimkumbushia hilo na akaahidi kwamba barabara hiyo itajengwa. Kwa hiyo, naendelea kukumbusha barababa hiyo ijengwe angalau kwa kilometa chache kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda niishukuru Serikali yangu kwa ahadi yake ya kusambaza umeme vijijini. Jimbo la Nyang’hwale tayari tumeshapata umeme lakini ni kwa kiwango kidogo sana. Vijiji vingi havina umeme na Watanzania wengi waliopo Jimbo la Nyang’hwale wanasuburi kwa hamu umeme kwa ajili ya kufanya kazi zao mbalimbali ambazo zinahitaji umeme. Wanahitaji wafunge mashine ndogondogo kwa ajili ya kukamua alizeti, mpunga na mambo mengine.
Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Nishati muda utapofika utukumbuke sana Jimbo la Nyang’hwale kutukamilishia ahadi ambazo ametuahidi mara nyingi kutupa umeme katka Jimbo la Nyang’hwale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Jimbo langu la Nyang’hwale tuna tatizo kubwa la maji, nimeshaongea tangu nilivyoingia mwaka 2010. Nimezungumzia suala la maji kwa nguvu zote na Serikali ilisikia na ikaitikia wakatuahidi kutujengea mradi wa maji. Tuliahidiwa mradi mzuri na mkubwa wa kutoka Ziwa Victoria na kusambaza maji katika Jimbo la Nyang’hwale. Tumepangiwa shilingi milioni 15.7 ndani ya miaka mitano na huu wa sita tumeshapewa shilingi bilioni 1.9. Naomba sasa ili niweze kurudi tena Bungeni mwaka 2020 mradi huo wa maji ukamilike.
Mheshimiwa Waziri Mkuu kama utapenda tuwe pamoja tena mwaka 2020, naomba mradi huu ukamilike. Waziri wa Maji nipe hayo maji ili mama zangu na dada zangu waweze kunipa kura tena niwe na jambo la kusemea vinginevyo sirudi tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la afya. Kwenye Jimbo langu kuna hospitali ambayo imepandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Wilaya lakini kwa bahati mbaya hospitali ile ina majengo ya kizamani, haina wodi, haina x-ray na vifaa tiba hakuna. Kuna wodi mbili tu, wodi moja ya akina baba wanachanganywa wagonjwa wa maradhi yote mle ndani na wodi ile ina vitanda kama tisa tu. Kwa hiyo, naomba ili sasa iwe Hospitali ya Wilaya tuletewe vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na vifaa tiba na kupanua majengo ikiwemo majengo ya wodi ya kulaza wagonjwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alipokuja Jimboni kwangu aliwaahidi wachimbaji wa madini ya dhahabu kwamba watatengewa eneo, kuna eneo moja linaloitwa Mwasabuka huko Nyijundu, alisema watagawiwa wachimbaji wadogo wawe huru wapewe leseni ili waweze kuchimba na waweze kusaidiwa na Serikali ili waweze kunyanyua kipato chao na kipato cha Serikali.
Naomba kumkumbusha Waziri wa Nishati na Madini kwamba ahadi hiyo aifuatilie ili wananchi hawa, vijana hawa ambao wanapata kipato chao kutokana na uchimbaji wa madini basi wawafikirie na kuweza kuwatekelezea ambayo waliwaahidi wakati wa kampeni wasione kwamba tulikuwa tunawadanyanga kwa ajili ya kutupa kura, waone kabisa tulikuwa tukiwaahidi mambo yaliyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu, naishukuru Serikali imeanza kutekeleza mpango wa elimu bure. Kama walivyosema wachangiaji wengine, tuangalie stahiki za walimu wetu, wazipate kwa muda ili wawe na ari na kasi na nguvu mpya kabisa ya kuweza kusimamia suala la elimu. Kwa sababu stahiki zao zinachelewa, zikichelewa amani ama imani ya kazi inashuka. Kwa hiyo, naiomba Serikali ijaribu kuangalia sana stahiki zao ili waweze kuwa na moyo wa kufanya kazi hiyo bila kutetereka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda kuongelea kuhusu wafugaji. Katika Jimbo la Nyang’hwale wafugaji wetu wamesahaulika. Nimeangalia katika mipango yote iliyopita sijaona wafugaji wa Jimbo la Nyang’hwale wamefikiriwa nini, hakuna soko, malambo wala majosho. Kwa hiyo, naomba wafugaji wa Jimbo la Nyang’hwale nao wafikiriwe kuboreshewa soko la mazao ya mifugo yao. Nimeangalia kwenye kitabu cha mpango, Mkoa wa Simiyu vinajengwa viwanda vitatu vya ngozi lakini Geita hakuna kiwanda hata kimoja cha ngozi, inakuwaje namna hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa Jimbo la Nyang’hwale na wakulima wote wa Tanzania kwa kweli wamekuwa wanakata tamaa kutegemea kilimo kwa sababu soko la mazao siyo la uhakika, pembejeo zinakuja mbovu, za gharama kubwa na zinachelewa kufika. Naiomba Serikali, kwa sababu wimbo mkubwa ni kwamba tuwasaidie wakulima, hebu tujaribu kweli kuwasaidia wakulima kwa kuwasaidia pembejeo na soko lao liwe la uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kusahau napenda nimkumbushe Mheshimiwa Waziri Mkuu, kulikuwa na mchakato wa Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale na bahati nzuri ulishaisha na Serikali ikatamka Makao Makuu ya Nyang’hwale yatakuwa Karumwa. Kwa bahati mbaya mpaka sasa hivi hati ya kujulisha kwamba Makao Makuu ya Nyang’hwale yako wapi haijatoka.
Mheshimiwa Waziri Mkuu utakaposimama hapa, waambie wananchi wa Jimbo la Nyang’hwale, hawa wapinzani hususan CHADEMA niliowashinda vibaya sana wanapiga kelele na kusema kwamba haya Makao Makuu hayapo mnadanganywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Naomba utakaposimama uwajibu hawa Watanzania wa Nyang’hwale pamoja na hao wapinzani, waelewe Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale yako Karumwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia kuhusu ardhi. Tuna ardhi nzuri, tunaomba ipimwe ili wananchi wetu waweze kunufaika na ardhi yao. Kwa bahati mbaya kuna zile hati za kimila, wananchi wetu wamepimiwa tangu mwaka 2011 mpaka leo hawajazipewa, ni zaidi ya hati 800 na kitu. Serikali ina mpango gani sasa kuwapa hizo hati za kimila ili ziweze kuwasaidia hawa wananchi kupata mikopo midogo midogo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala ambalo napenda kulizungumzia ni UKIMWI. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya UKIMWI na dawa za kulevya. Tunajaribu kuangalia matatizo makubwa ya UKIMWI yanaanzia wapi, tumejaribu kuzunguka na kuongea na wadau mbalimbali wakatushauri na kutuambia na sisi wenyewe kwa kuona kwa macho matatizo ya UKIMWI yanaanzia kwenye ulevi. Kuna ulevi wa aina nyingi, kwanza mirungi, viroba, bangi, watakapokunywa na kuvuta wanajisahau wanaingia kwenye ngono zembe. Kwa hiyo, angalieni sana UKIMWI unaanzia wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali iweke utaratibu mzuri kutoa elimu ya UKIMWI kuanzia chekechea, shule za msingi, sekondari mpaka vyuo vikuu waelezwe UKIMWI unaanzia wapi na ni tatizo gani. Serikali ipange utaratibu wa kutoa elimu kwenye shule za msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali na hii bajeti ambayo imesomwa na Waziri Mkuu kuhusu shilingi milioni 50. Nategemea kwangu kupata shilingi bilioni 3.2, naamini kabisa ikitolewa elimu nzuri kwa hawa ambao wanalengwa, watanyanyua vipato vyao lakini kwanza wapewe elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri. Halmashauri yangu ina vipato vingi lakini vidogovidogo lakini mapato yale hayakusanywi. Kwa nini hayakusanywi? Wanatumia stakabadhi za kuandika kwa mkono. Naomba zile mashine zisambazwe katika Halmashauri zote…
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umemaliza, naomba ukae.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja asilimia mia moja kwa mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Kwanza naanza kumshukuru mwenyenzi mungu ambaye amenijalia afya njema kwa siku ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kumwambia Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, kwamba sitaunga mkono hotuba hii mpaka hapa atakaponipa majibu yaliyo sahihi. Kwa nini nasema hivyo, leo mimi ni Mbunge katika Jimbo la Nyang‟hwale nina umri wa miaka sita katika nafasi hii ya Ubunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2010 Mheshimiwa Rais aliyepita wa Awamu ya Nne alikuja kuomba kura kwenye Jimbo hilo la Nyang‟hwale, akatuahidi kutujengea barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kahama kupita Wilaya ya Msalala, Nyang‟olongo, Bukwimba, Nyang‟hwale, Busolwa, Busisi na Sengerema kwa Mheshimiwa Wiliam Ngeleja. Mwaka 2012 Mheshimiwa Rais alikuja kwa mara ya pili akiwa ameongozana na Waziri Mheshimiwa Jumanne Maghembe, Rais wa sasa, Mheshimiwa Majaliwa na Mheshimiwa Stephen Masele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, alikuja akafanya mkutano wa hadhara pale, akatuahidi tena neno lile lile, kwamba nitawajengea barabara ya kiwango cha lami kutoka Kahama - Nyang‟hwale kuunganisha Sengerema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015 mgombea Urais, Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan naye alikuja akasema maneno yale yale. Tulimuomba na akasema barabara hii itajengwa kwa kiwngo cha lami. Mwaka 2015 Rais wa Awamu ya Tano Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli niliomba na kukumbusha na akasema mimi nilikuwa Waziri wa Ujenzi kipindi kile, sasa nikiwa Rais barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi waliamini na wakatoa kura nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais na mimi mwenyewe Mbunge. Leo nina sababu gani ya kuunga mkono hoja hii, viongozi wangu Wakuu wa Kitaifa wametoa ahadi na ahadi hii haimo ndani ya hiki kitabu, naunga mkono nini? Ninaomba Mheshimiwa Waziri, utakapokuja kuhitimisha hapo, bila kutoa majibu sahihi leo sikubali kuunga mkono na nitashika shilingi, itakuwa ni mara yangu ya kwanza leo. Huyo anayesema hawezi sijui yeye ndiye aliyenileta Bungeni? Mimi nasema sitounga mkono hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna lami ambayo tuliahidiwa, ujenzi wa barabara ya lami kutoka Geita kuja Nyang‟hwale yenye urefu wa kilometa 80, tangu mwaka 2013 tumeweza kujengewa kilometa sita. Kwenye kitabu hiki leo nimesoma nimepangiwa kilometa 2.78, kilometa 80 zitajengwa baada ya miaka mingapi? Nina haja gani ya kuunga mkono hoja hii? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ninaomba leo uniambie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niende kwenye upande wa mawasiliano. Jimbo langu lina Kata 15, lakini ni Kata sita tu ndizo zenye mawasiliano. Kata tisa ambazo ni Bukwimba, Kafita, Nyugwa, Kakola, Nyamtukuza, Nyabulanda, Shabaka, Nyijundu, Kaboha hazina mawasiliano ya simu. Lakini cha ajabu kwenye kitabu chenu hiki mmesema hivi; Busolwa kuna Mnara lakini haujawashwa, kuna kama Kata sita ziko hapa pembeni mmeonesha kwamba haujawashwa. Hebu niambiwe sababu gani kwa nini minara hiyo haijawashwa na iko tayari leo zaidi ya miaka miwili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wananchi wa Jimbo la Nyang‟hwale wanamsikiliza leo Mbunge wao, hawamuoni kwenye tv lakini wanamsikiliza kwenye redio kwamba leo Mbunge wetu…
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante, muda wako umekwisha ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kuunga mkono hotuba ya Waziri. Pia naipongeza Serikali kwa mipango yake mizuri ya kusambaza umeme nchi nzima hata huko vijijini ili kuchochea maendeleo kwa wananchi na kuongeza pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Nyang‟hware lina kata 15 na vijiji 62 hadi leo hii ni kata mbili zimefikiwa na umeme, nazo ni Kata ya Khalumwa na Nyang‟hware. Hata hivyo, Kata ya Khalumwa ndipo yalipo Makao Makuu, ni Kijiji kimoja tu ndiyo kina umeme. Pia Kata ya Nyang‟hware ni kijiji kimoja tu ndiyo umeme umefika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Busolwa tayari line imeshafika, lakini umeme haujawaka. Pia Kata ya Nyijunau nyaya za umeme zimepita juu kuelekea Kata ya Nyang‟hware ila Nyijundu haina umeme. Kata ambazo hazina kabisa umeme ni hizi: -
Kata ya Bukwimba na vijiji vyake; Kata ya Nundu na vijiji vyake; Kata ya Izunya na vijiji vyake; Kata ya Kafita na vijiji vyake; Kata ya Kakora na vijiji vyake; Kata ya Nyijundu na vijiji vyake; Kata ya Busolwa na vijiji vyake; Kata ya Kaboha na vijiji vyake; Kata ya Shabaka na vijiji vyake; Kata ya Mwingiro na vijiji vyake; Kata ya Nyaburanda na vijiji vyake; na Kata ya Nyamtukuza na vijiji vyake.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, tukiipitisha bajeti hii umeme upelekwe kwenye kata hizo, nitashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa hotuba yao nzuri sana. Pia naipongeza Serikali kwa kutimiza baadhi ya ahadi zake, hasa kwenye miundombinu ya barabara. Kwa Wilaya ya Nyang’hwale kuna barabara mbili za TANROADs, moja inayotoka Wilaya ya Geita – Nyang’hwale na ya pili inayotoka Busisi – Sengerema – Nyang’hwale – Kahama hizi zina hali nzuri kwa sababu zina matengenezo ya kila mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukumbusha kwamba kuna ahadi ambazo ziliahidiwa katika Kampeni ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne mwaka 2010. Katika ahadi hizo ni pamoja na kuijenga barabara ya kutoka Kahama - Nyang’holongo – Bukwimba – Karumwa – Nyijundu
– Busolwa – Ngoma – Busisi Wilayani Sengerema; kwa kiwango cha Lami. Kifupi kutoka Kahama – Nyang’hwale – Sengerema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano alipokuja kujinadi katika Jimbo la Nyang’hwale aliahidi pia kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; napenda kujua, je ni lini upembuzi yakinifu utaanza na kukamilika? Swali la pili; je ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza na kukamilika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa afya njema na kuweza kusimama Bungeni hapa leo na kuweza kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri Ummy na Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa hotuba yao nzuri ambayo wameiwasilisha leo. Napenda pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kutupatia gari la wagonjwa katika Kituo chetu cha Afya Nyang’hwale. Mwaka 2017 tulipata gari moja na nashukuru mwaka huu tumepata gari lingine, hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nyang’hwale kituo cha Afya na Hospitali ya Wilaya ya Nyang’hwale, ama Wilaya ya Nyang’hwale kwa ujumla tuna upungufu mwingi katika vituo vyetu vya afya na hospitali. Upungufu wenyewe ni kama ufuatao:-

Tuna upungufu wa dawa, Wauguzi, Madaktari na vifaa tiba. Vifaa tiba kama vile X-ray na Ultra Sound. Upungufu huu unasababisha wananchi wetu kupata usumbufu mkubwa kufuata huduma hizi Mkoani Geita. Kwa hiyo tunamwomba Mheshimiwa Waziri ajaribu kuangalia upungufu huu ili kuwapunguzia adha wananchi wetu kufuata matibabu Mkoani Geita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bima ya afya. Watu wengi wamekuwa hawaoni faida ya bima ya afya sababu ni ipi. Sisi Wabunge tunajitahidi sana kuwahimiza wananchi wajiunge na bima ya afya, lakini wanashindwa kujiunga kwenye bima ya afya kwa sababu kwa wananchi ambao wameshajiunga na bima ya afya hawaoni faida yake. Vipi hawaoni faida yake? Ni kwamba wanapokwenda hospitali wanapata huduma, lakini huduma ya dawa wanakuwa hawaipati wanaambiwa waende wakanunue dawa hakuna dawa. Kwa hiyo hii inawafanya wananchi wakate tamaa kubwa ya kujiunga na huduma hii ya bima ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alifika katika jimbo letu na akaahidi Kituo cha Afya cha Kalumwa kiwe hospitali ya wilaya, lakini mpaka leo hii hatuoni mpango wowote wa Wizara kutupa hati ya kuipandisha hadhi kukipandisha hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya ya Nyang’hwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa hospitali hii ipandishwe hadhi ili tuweze kupata dawa kulingana na wilaya; kwa sababu hospitali hiyo inahudumia vijiji zaidi ya 110, lakini pia wilaya za jirani zinakuja kupata huduma katika hospitali hiyo. Kwa hiyo kituo hicho kitakapopandishwa na kuwa hospitali ya wilaya naamini kabisa bajeti yake itakuwa ni kubwa na inaweza ikakidhi angalau kidogo kupunguza makali ya mahitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba wizara ijaribu kuangalia. Tuna wodi moja pale ambayo ilijengwa mwaka 1958. Wodi ile inalaza wagonjwa 10 tu na leo hii hospitali ile inapokea wagonjwa wengi sana. Kwa hiyo tunaomba sasa tuweze kujengewa wodi ambayo ni ya kisasa na inaweza kubeba wagonjwa walio wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara kwa mikakati yake ya kupambana na ugonjwa wa saratani ya shingo ya uzazi. Ukweli ni kwamba naipongeza Serikali kwa kuanza kutoa chanjo kwa ajili ya kukinga tatizo hilo. Pia naomba sasa Wizara ishuke kule chini iende kutoa elimu ili kuondoa ile imani potofu waliyonayo wananchi wetu, kwamba tutakapochomwa sindano hiyo huwezi ukapata tena mimba, wengi wanaelewa hivyo, kwa hiyo naomba elimu hiyo iende ikatolewe kule chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Waswahili wanasema kinga ni bora kuliko kutibu. Kwa nini nasema hivyo; Wizara imeshagundua tatizo la chanzo cha ugonjwa wa saratani ya shingo ya uzazi. Jana nilisikia kwenye majibu ya Mheshimiwa Waziri hapa alisema kwamba chanzo chake ni kwamba inatokana na kuambukizwa na wanaume ambao hawajakata govi zao. Kwa hiyo naiomba sasa Wizara iende ikatoe elimu kwa walio na govi hizo ili waweze angalau zitolewe kuwakinga hawa. Kwa lugha nyingine wanaume ambao hawajafanyiwa tohara. Kwa hiyo naomba itolewe elimu kule ili kuweza kuwakinga hawa akinamama na maambukizi haya ambayo yanatoka kwa akinababa ambao hawajafanya tohara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naanza kumpongeza Waziri kwa hotuba yake nzuri ya matumaini makubwa kwa Watanzania. Pia naipongeza Wizara ya Afya kwa juhudi zake za kuhakikisha kuwa Watanzania wanakuwa na afya bora wakiwemo wananchi wa Nyang’hwale.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kama Mbunge kwa Wizara hii ni kuhakikisha pesa zinakwenda kwa wakati katika hospitali, vituo vya afya na zahanati zetu. Wizara imepanga kutoa chanjo kwa watoto wa kike ya saratani ya shingo ya kizazi. Kikubwa elimu itolewe huko vijijini ili wananchi waondokane na hofu ya chanjo hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu; Kituo cha Afya Kharumwa kina upungufu wa wataalam wa afya, vifaatiba, X-ray na kadhalika, pia dawa hazitoshi, wodi hazitoshi na zilizopo ni ndogo sana zina vitanda vinane kwa wanaume na wodi ya mama na mtoto ina vitanda 20 tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri ya Nyang’hwale vitambulisho vya wazee bado hawajapewa, kwa hiyo hawapati haki yao ya matibabu bure. Je, ni lini watapewa vitambulisho vyao?

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua kali zichukuliwe kwa watu wanaonajisi na kubaka watoto wadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kutoa gari la wagonjwa Kituo cha Afya Kharumwa. Wananchi wanawapongeza sana na wanaomba kwa Mungu muendelee na moyo huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri ni lini Kituo cha Afya Kharumwa kitapandishwa na kuwa Hospitali ya Wilaya? Hadi sasa inaitwa Hospitali ya Nyang’hwale lakini haijapata hati hadi leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga mkono hoja bajeti hii ya Wizara.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kuipongeza hotuba ya Waziri wa Madini. Pia nwapongeza Waziri na Naibu wote wa Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa ushauri wangu kidogo kuhusiana na upotevu mkubwa wa mapato yatokanayo na madini ya dhahabu. Mfano, kuna wachimbaji wadogo Wilayani Nyang’hwale ambao wanachimba na kupata dhahabu bila ya kulipa mapato ya Serikali. Sababu kuu ni kutowapatia leseni ya uchimbaji au kutowatambua lakini yako maeneo mengi yanayochimbwa kama Kijiji cha Chibaranga, Ifugandi, Bululu, Isonda, Nundu, Nyamalapa, Iyenze, Ujulu, Isekelinyugwa, Nyijundu na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu, kwa kuwa Wilaya ya Nyang’hwale haina maeneo yaliyopimwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Maeneo niliyoyataja yapimwe na kutolewa leseni ili Serikali iweze kukusanya mapato kirahisi pia kuwaepusha wachimbaji kusumbuliwa na kuhamahama.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.