Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Hussein Nassor Amar (7 total)

MHE. HUSSEIN N. AMAR aliuliza:-
Serikali imekuwa na ahadi nyingi, nzuri za kutekeleza katika kusambaza umeme kwenye maeneo mengi ya nchi yetu.
(a) Katika Wilaya ya Nyang‟hwale ni vijiji vitatu tu vya Nyang‟hwale, Nyarubele, Busegwa na Makao Makuu ya Wilaya ambavyo vina umeme; je, katika bajeti ijayo ni vijiji vingapi vya Jimbo la Nyang‟hwale vitapatiwa umeme?
(b) Je, kwa nini nguzo haziletwi Kharumwa wakati wateja wengi tayari wamefanya wiring kwenye nyumba zao?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Nassor Amar, Mbunge wa Nyang‟hwale lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya vijiji 61 katika jimbo la Nyang‟hwale vitapatiwa umeme katika utakekezaji wa mradi kabambe wa REA Awamu ya Tatu. Kazi ya kupeleka umeme kwenye vijiji hivyo itajumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovolt 33 yenye urefu wa kilometa 50, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovolt 0.4 yenye urefu wa kilometa 372 na ufungaji wa transformer 24 pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 3,578. Kazi hizi zitaanza mwezi Disemba mwaka huu na kukamilika mwaka wa fedha 2019/2020. Gharama ya mradi huu ni shilingi bilioni 6.23.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Kharumwa ambacho ni makao makuu ya Wilaya ya Nyang‟hwale tayari kimepatiwa umeme na kazi ya kupeleka nguzo inaendelea. Hata hivyo TANESCO inakamilisha kazi za kuunganishia umeme wateja wapya wa Kharumwa kadri maombi yatavyofikiwa. Mpaka mwisho wa mwezi wa Disemba mwaka huu vijiji vya Kharumwa vitakuwa vimepata umeme.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU (K.n.y. MHE. HUSSEIN N. AMAR) aliuliza:-
Ili viwanda viweze kufanya kazi kwa ufanisi vinahitaji malighafi ya kutosha.
(a) Je, Serikali iko tayari kutoa bei ya pamba mapema kabla ya msimu wa kilimo kuanza ili wakulima wawe na uhakika wa bei elekezi?
(b) Zao la pamba limekuwa na tatizo kubwa la mbegu zisizo bora na viuatilifu hafifu, je, Serikali imejipanga vipi kwa kuzingatia agizo la Mheshimiwa Rais la tarehe 31 Julai, 2016 alipokuwa akiongea na wananchi wa Geita kwamba hatavumilia kuona wananchi wakiletewa mbegu mbovu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Nassor Amar, Mbunge wa Nyang’hwale, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, bei ya kuuzia pamba ya wakulima hutegemea moja kwa moja bei katika Soko la Dunia ambalo kwa bahati mbaya bei hupanda na kushuka kila wakati. Serikali haipangi bei ya pamba kwa mkulima bali huangalia hali ya bei katika Soko la Dunia katika kupanga bei elekezi ya mkulima. Bei elekezi inapangwa kwa ushirikiano kati ya Serikali, wanunuzi wa pamba na wawakilishi wa wakulima. Aidha, pamoja na mpango wa Serikali wa kujenga viwanda vya pamba kuongeza thamani, Serikali inahamasisha wakulima kufuata kanuni bora za kilimo cha pamba ili kuongeza tija, ubora na baadaye kuwaongezea kipato. Kwa hali hiyo, bei ya pamba hufahamika baada ya kuanza kwa msimu mpya katika Soko la Dunia na kwa hiyo, Serikali haina uwezo wa kupanga bei ya pamba bila kuangalia hali ya Soko la Dunia.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa mbegu bora za pamba na viuatilifu kwa kutumia Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Nchini (TOSCI) na kwa upande wa viuatilifu, Taasisi ya Utafiti na Udhibiti wa Ubora wa Dawa (TPRI) ili kuhakikisha kuwa wakulima wanapata mbegu na viuatilifu vyenye ubora mtawalia.
Aidha, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inafanya rejea ya mfumo bora wa kuzalisha mbegu za pamba kwa maana ya kuuboresha zaidi, hatua hii itasaidia kuongeza upatikanaji wa mbegu bora za pamba kwa wingi na kwa bei nafuu. Aidha, Serikali ina mpango wa kuutumia Wakala wa Mbegu na Mazao kwa ajili ya kufungua mashamba makubwa ya kuzalisha mbegu ya pamba.
MHE. HUSSEIN N. AMAR aliuliza:-
Je, katika bajeti ya Serikali 2016/2017 Serikali ilitarajia kuanzisha Vyuo vingine vya ufundi ikiwemo Nyang’hwale?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Nassoro Amar, Mbunge wa Nyang’hwale kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa kujenga Vyuo vya VETA katika Wilaya mbalimbali kulingana na upatikanaji wa fedha. Wilaya zinazopewa kipaumbele ni zile ambazo hazina Chuo chochote cha mafunzo ya ufundi stadi. Lengo ni kuwapatia vijana ujuzi mbalimbali ambao utawawezesha kuwa na sifa za aidha kuajiriwa au kujiajiri.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Sayansi na Teknolojia inatarajia kuanza ujenzi wa Vyuo vinne vya Ufundi Stadi ngazi ya Mkoa katika Mikoa ya Njombe, Rukwa, Geita na Simiyu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na Wilaya ya Nyang’hwale zipo pia Wilaya nyingine ambazo zina mahitaji ya kuwa na Vyuo vya VETA, Wizara inatambua hilo na itaendelea kutafuta fedha ili kukabiliana na mahitaji hayo. Tunatarajia kuwa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) cha Mkoa wa Geita kitakapokamilika kujengwa kitakuwa na uwezo wa kutoa mafunzo na huduma kwa vijana kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Geita ikiwemo na Wilaya ya Nyang’hwale.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE (K.n.y. MHE. HUSSEIN N. AMAR) aliuliza:-
Serikali imekuwa ikitumia pesa nyingi sana kuanzisha miradi mikubwa na midogo ya maji.
(a) Je, Serikali inaweza kueleza ni miradi gani mikubwa na midogo iliyokamilika na isiyokamilika katika Jimbo la Nyang’hwele?
(b) Je, kama kuna miradi ambayo haijakamilika mpaka hapo ilipofikia imetumia fedha kiasi gani?
(c) Je, ni lini sasa miradi hiyo itakamilika katika Jimbo la Ngang’hwale?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali ya Mheshimiwa Hussein Nassor Amar, Mbunge wa Nyang’hwale, kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Nyang’hwele inatekeleza mradi mkubwa mmoja wa Nyamtukuza kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Mradi huu utahudumia jumla ya vijiji tisa vya Nyamtukuza, Nyarubele, Kakora, Kitongo, Ikangala, Kharumwe, Izunywa, Kayenze na Bukwimba ambavyo vinaendelea na ujenzi. Miradi ya maji iliyokamilika katika Halmashauri ya Nyang’hwale ni Kanyenze, kakora, Ikangala, Nyamtukuza na Kharumwa.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji wa Nyamtukuza unaotuma chanzo cha Ziwa Victoria unatekelezwa kwa jumla ya fedha shilingi bilioni 15 na mpaka sasa Serikali imepeleka fedha shilingi bilioni 3.78 za kutekeleza miradi ya maji na usafi wa mazingira katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale.
Mheshimiwa Spika, lengo kuu la Serikali ni kutuma fedha kwa Halmashauri zote zinazoendelea na ujenzi wa miradi ili kuhakikisha miradi yote iliyoanza inakamilika kabla ya kuanza kwa miradi mipya.
MHE. HUSSEIN N. AMAR aliuliza:-
Kwa juhudi zake Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale ameanzisha ujenzi wa baadhi ya majengo ya zahanati kubwa na za kisasa katika Vijiji vya Nyamikonze na Inyenze.
(a) Je, Serikali ipo tayari kusaidia kukamilisha ujenzi huo?
(b) Je, Serikali ipo tayari kuifungua zahanati iliyojengwa na Mbunge katika Kijiji cha Mwamakilinga ambayo imekamilika tangu Novemba, 2014?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Nassor Amar, Mbunge wa Nyang’hwale, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri ya Nyang’hwale kupitia mapato ya ndani ilitenga shilingi milioni 45 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati ya Kijiji cha Nyamikonze, lakini ukamilishaji haukufanyika kutokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Nyang’hwale kuwa kidogo. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Nyang’hwale kupitia mapato ya ndani imetenga shilingi milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Nyamikonze. Mpaka sasa zahanati haijaanza kufanya kazi na wananchi wa kijiji hicho wanapata huduma za afya katika zahanati ya Mwingiro iliyo karibu na kijiji hicho.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Nyang’hwale katika mwaka wa fedha 2017/2018 imetenga shilingi milioni 90 kutokana na mapato ya ndani kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati katika Kijiji cha Inyenze iliyofikia hatua ya kuezekwa. Fedha hizo bado hazijapatikana kutokana na makusanyo kuwa kidogo. Mara fedha hizo zitakapopatikana utekelezaji utafanyika kama mpango unavyoelekeza. Zahanati ya Mwamakilinga iliyojengwa na Mbunge wa Jimbo hilo, ilifunguliwa na Mheshimiwa Engineer Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Geita tarehe 29 Januari, 2018 na mpaka sasa inafanya kazi.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale alianzisha ujenzi wa majengo matatu katika Kituo cha Afya Kharumwa ambayo yote yalikuwa hatua ya lenta. Majengo hayo ni wodi ya watoto, wadi ya wazazi ambayo ndani ina chumba cha upasuaji wa dharura kwa wajawazito na jengo la kuhifadhia maiti (mortuary). Shirika la AMREF linaendelea na ukamilishaji wa jengo la wodi ya wazazi ambayo ndani ina chumba cha upasuaji wa dharura kwa wajawazito. Ujenzi huo unategemea kukamilika ifikapo tarehe 15, Mei, 2018 kwa gharama ya shilingi milioni 164.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua jitihada kubwa zilizofanywa na Mbunge wa Nyang’hwale, mwishoni mwa mwezi Desemba, 2017 Serikali ilitoa shilingi milioni 400 kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ya Kituo cha Afya Kharumwa. Halmashauri imetenga shilingi milioni 70 kwa ajili ya ukamilishaji wa wodi ya watoto na shilingi milioni 50 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya Kharumwa. Ujenzi huo unaaendelea na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Mei, 2018. Kiasi cha shilingi milioni 280 kilichobaki kitatumika katika ujenzi wa chumba cha upasuaji (theatre), maabara ya kisasa, nyumba ya mtumishi na wodi ya upasuaji (surgical ward) kwa wanawake na wanaume.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE (K.n.y. MHE. HUSSEIN N. AMAR) aliuliza:-
(a) Je, ni lini walimu wataboreshewa maslahi yao pamoja na nyumba za kuishi?
(b) Kwa juhudi za Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale ameweza kujenga madarasa mawili katika Kata ya Izunya kwa lengo la kuanzishwa shule ya sekondari tangu mwaka 2014. Je, ni kwa nini shule hiyo haijafunguliwa hadi sasa ili kuwapa moyo wafadhili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Amar, Mbunge wa Nyang’hwale, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kwa dhati kuhakikisha walimu wa nchi hii wanaboreshewa maslahi yao ikiwemo ujenzi wa nyumba za walimu. Katika kuboresha maslahi ya walimu, Serikali kwa Sheria Na. 25 ya mwaka 2015 ilianzisha Tume ya Utumishi ya Walimu ili iweze kusimamia na kushughulikia masuala yote yahusuyo maslahi ya walimu badala ya maslahi hayo kusimamiwa na chombo zaidi ya kimoja kama ilivyokuwa awali.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwezi Juni, 2015 hadi Desemba 2017, Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni
33.135 kwa ajili ya kulipa madeni ya walimu ambapo walimu 86,234 wamelipwa nchi nzima. Aidha, katika kuhakikisha maslahi ya walimu yanayoboreshwa na kero zao zinaondolewa, jumla ya walimu 52 wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale walilipwa jumla ya shilingi 99,685,990 za madai mbalimbali na wengine 202 walipandishwa vyeo (madaraja) katika mwaka wa fedha 2014/2015 na 2015/2016.
b) Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale, wananchi na uongozi wa Halmashauri ya Nyang’hwale kwa juhudi zao za kutaka kuiwezesha jamii kielimu wakiwemo wa Kata ya Izunya. Ili shule ya sekondari iweze kupewa kibali cha kufunguliwa wakati wa kuanzishwa inapaswa kwa kuanzia iwe na madarasa, kuwe na jengo la utawala, nyumba za walimu, vyoo vya walimu na wanafunzi, maktaba, viwanja vya michezo, samani pamoja na maabara kwa kuzingatia mwongozo uliowekwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa shule tarajiwa ya Izunya ina vyumba vya madarasa manne, vyoo matundu sita ya wasichana na wavulana matundu matano, jengo la utawala lenye vyoo vya walimu liko hatua za mwisho za umaliziaji na maabara zipo kwenye hatua ya jamvi. Hata hivyo, kwa kutambua jitihada za wadau mbalimbali wa elimu akiwepo Mheshimiwa Mbunge, Halmashauri imeazimia kutumia shilingi milioni 50 kutoka fedha za EP4R zilizopelekwa mwezi Februari, 2018 kwa ajili ya kukamilisha maabara zote. Ni matarajio yangu kwamba mara baada ya ujenzi wa maabara kukamilika taratibu za usajili wa shule hiyo zitakamilika. Aidha, naomba niitumie nafasi hii kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge, wadau wetu wa maendeleo na wananchi kwa ujumla kuunganisha nguvu zetu pamoja ili kukamilisha miundombinu inayohitajika katika shule kuweza kufunguliwa ikiwemo ya Kata ya Izunya.
MHE. ALHAJ A. BULEMBO (K.n.y MHE. HUSSEIN N. AMAR) aliuliza:-
Taasisi za umma na taasisi binafsi zimeitikia wito wa Mheshimiwa Rais wa kutengeneza madawati kwa ajili ya shule zetu nchini:-
Je, Serikali na mamlaka husika zimejipanga vipi katika kuhakikisha utunzaji bora wa madawati hayo?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Nassor Amar, Mbunge wa Nyang’wale, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inazipongeza na kuzishukuru taasisi zote za umma na za binafsi zilizoitikia wito wa Serikali wa kutengeneza madawati ya kutosha kwa ajili ya shule zetu nchini. Katika kuhakikisha kuwa madawati yaliyotengenezwa kwa ajili ya shule za msingi na sekondari yanatunzwa vizuri na yanadumu kwa muda mrefu, Serikali kupitia Mwongozo wa Matumizi ya Fedha za Ruzuku ya Uendeshaji (Capitation Grants) wa tarehe 28 Desemba, 2015 imeelekeza kuwa asilimia 30 ya fedha hizo itumike kwa ajili ya ukarabati wa samani ikiwemo madawati kwa upande wa shule za msingi na asilimia 10 kwa upande wa shule za sekondari.
Mheshimiwa Spika, aidha, Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na shule zote wameelekezwa kutotumia madawati hayo kwa shughuli nyingine, kwa mfano, mikutano ya kijiji, vyama vya siasa na matumizi mengine yasiyokusudiwa ili kupunguza kasi ya uharibifu. Ukaguzi wa mara kwa mara umeagizwa kufanyika kwa kushtukiza ili kuhakikisha madawati yaliyopo yanatunzwa vyema.