Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Hussein Nassor Amar (22 total)

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Tatizo la maji la Halmashauri ya Makambako linafanana kabisa na tatizo lililoko Halmashauri ya Nyang‟hwale. Kumekuwa na miradi mingi ya usambazaji wa maji kutoka Ziwa Victoria, leo takribani miaka minne, miradi hiyo haisongi mbele kwa sababu ya ukosekanaji wa pesa. Je, Waziri anatuambia nini wananchi wa Nyang‟hwale, kuhusu miradi hiyo kwamba itaendelea kwa kasi ili tuweze kupunguza tatizo la maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, ndiye ambaye amekuwa ananipa nyaraka nyingi kutoka kwenye Halmashauri yake na ndiye ambaye alinikabidhi hata ile barua ambayo nilikuja kugundua kwamba mwaka 2013, Wizara ilitoa waraka kuhusu utekelezaji wa bajeti katika Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili tatizo la Nyang‟hwale linafanana na maeneo mengine pia, inawezekana kuna matatizo pia katika Halmashauri ya Mheshimiwa Mbunge, lakini kwa utaratibu tuliouweka sasa kama miradi ipo na uzalishaji upo, wakileta certificate tunalipa pesa; lakini tumegundua kuna maeneo ambayo uzalishaji umekwama kwa matatizo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Wizara ya Maji, tukishirikiana na Mheshimiwa Mbunge tutapeana taarifa, ili tuweze kuona ni nini kimekwamisha na kwa bahati nzuri tuko humu humu ndani kwenye Bunge. Nakumbuka Mheshimiwa Mbunge Lusinde kwake kulikuwa na shida, lakini tumeitatua na sasa hivi mradi unaendelea vizuri. Kwa hiyo, tupeane tu taarifa kuna tatizo gani ili tuweze kuiangalia Halmashauri. Pengine ndani ya Halmashauri kuna uzembe, tutauondoa ili kuhakikisha hii miradi inatekelezeka na hasa kwa kuzingatia kwamba sasa fedha inatolewa. Kwa hiyo, hakuna sababu kabisa kwa nini mradi usitekelezwe.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Mheshimiwa Rais alipokuja mwaka 2015 kwenye mikutano yake ya kampeni katika Jimbo la Nyang‟hwale, aliweza kuwaahidi wachimbaji wadogo wa Jimbo hilo kwamba eneo la Kasubuya litapimwa na kugawiwa wachimbaji wadogo wadogo. Je, Serikali inasemaje kwa hili kwa wachimbaji wadogo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kati ya maeneo 12 tuliyotenga kwenye Mkoa wa Geita pamoja na maeneo mengine ya Kahama ni pamoja na eneo la Kasubuya. Eneo la Kasubuya tumetenga hekta 4,098.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Hussein, wananchi wa Nyang‟hwale tayari wana eneo. Isipokuwa nawaomba sana, hata wakishindwa kupata maeneo pale Kasubuya, tunatenga maeneo mengine. Kule Chato kuna hekta 1,282. Kwa hiyo, wananchi wako bado wanaweza kwenda kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maeneo yale, maeneo ya kwa Mheshimiwa wa Mbunge wa Bukombe tuna hekta 682, wanaweza wakaenda kuchimba Bukombe. Kwa hiyo, tunaendelea kutenga maeneo ili wananchi wa Kasubuya na maeneo mengine wapate maeneo ya kutosha.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri kuhusu mpango wa umeme vijijini. Mimi nina kata 15 lakini nina kata tatu ambazo zimepata umeme na ni vijiji vitatu vimepata umeme, je, Kata zifuatazo zitapata umeme katika mpango huu? Kata ya Bukwimba, Nyugwa, Busolwa, Shabaka, Nyijundu, Nyabulanda, Kafita, Kakola, Mwingilo, Kaboha, Nyabulanda na Izunya, je, serikali katika mpango wake wa mwaka huu tutapata umeme katika Jimbo la Nyang’hwale Kata zote hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika Jimbo la Nyang’hwale ni kata tatu tu ambazo zimepata umeme kwa mpango wa REA Awamu ya Pili, lakini REA Awamu ya Tatu pamoja na tathmini inayofanyika sasa katika REA Awamu ya Pili, vijiji vyote na kata zote zilizobaki za Nyang’hwale pamoja na vijiji alivyovitamka vimeingizwa kwenye mpango wa REA unaoendelea utakaonza mwezi Julai mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kadhalika kama nilivyosema bado TANESCO wanaendelea na kazi za kuunganisha umeme katika maeneo yote na maeneo ya Nyang’hwale ambayo hayatapitiwa yataingizwa kwenye mpango wa TANESCO ili vijiji vyote na kata zote za Nyang’hwale zipate umeme mwaka 2017/2018.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Hussein Nassor Amar, Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Naibu Waziri wa TAMISEMI kwa majibu yake mazuri ya kwamba tumetengewa shilingi milioni 850 katika Halmashauri ya Nyang’hwale. Namuomba Mheshimiwa Waziri kwamba kwa kuwa kuna pesa ambayo imetengwa, shilingi milioni 80 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wenye eneo lile. Naomba amuagize Mkurugenzi zoezi hilo la kuwalipa wananchi lifanyike haraka ili ujenzi huo uanze kujengwa mara moja. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, anayezungumza hapa ni Mbunge wa Jimbo hilo, maana yake yeye anayajua ya huko yalivyo na hizo pesa wameshatenga tayari. Hizo pesa kama zipo sasa, nadhani tusifanye ajizi. Namuomba Mkurugenzi haraka sana, kama vigezo vyote vimetimia, hakuna sababu kuwacheleweshea ulipaji wa fidia. Tunachotaka ni kwamba fidia ilipwe, ujenzi uendelee.
Mheshimiwa Naibu spika, kwa hiyo, moja kwa moja Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tunamwelekeza Mkurugenzi wa Nyang’hwale ahakikishe kwamba kama kuna hiyo fedha imetengwa na ipo, watu walipwe fedha zao ili mradi hii kazi hii isiendelee kuchelewa tena kwa sababu ina maslahi mapana kwa wananchi wa Nyang’hwale.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ya matumaini kwa wananchi wa jimbo la Nyang‟hwale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika kijiji cha Busorwa pameshasimikwa nguzo, nyaya zimetandazwa na transfomer zimeshafungwa takribani zaidi ya miezi minane, kwa nini umeme kijiji cha Busorwa haujawashwa?
Na kwa kuwa kuna baadhi ya vijiji kama vile Izunya, Nyashilanga, Nyamikonze, Nyijundu nguzo na nyaya za umeme zimeshatandazwa lakini transfomer hazijafungwa. Ni lini trasfomer hizo zitafungwa ili umeme huo uweze kuwashwa na kuweza kuchochea maendeleo katika vijiji hivyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, Mheshimiwa Naibu Waziri nakuomba baada ya Bunge hili tuongozane pamoja mimi na wewe ukaone mradi huu unavyosuasua ili uweze kuleta changamoto ili mradi huu uweze kwenda haraka ili wananchi wa jimbo la Nyang‟hwale waweze kupata maendeleo kupitia umeme, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika Jimbo la Nyang‟hwale ni vijiji vitatu tu ambavyo vimeshaunganishiwa umeme, na nitoe masahihisho kidogo, Mheshimiwa na wala siyo vijiji 61, vijiji 62 mbavyo bado kwenye jimbo lako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kijiji cha Busorwa ambacho tayari kina transformer na tayari kina nyaya zimeshafungwa kulikuwa na shida ndogo tu ya vikombe ambavyo vilikuwa havijakamilika, na hivi leo vimekamilika kesho saa tisa mchana Mheshimiwa Hussein wanakuwashia umeme pale Busorwa na mtapata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ni lini vijiji alivyovitaja vitapata umeme. Ametaja vijiji vitatu lakini kuna vijiji 66 ambavyo vimepatiwa kwa nusu lakini vijiji 40 vikiwemo vijiji vya Busorwa kama ulivyotaja, Kakora, Kanegere, Nyamitongo, Nyabushishi, Nyaruzugwa, Nyaruyeye na Izuguna bado havijapatiwa umeme, kwa hiyo vyote tunavipelekea umeme kama ambavyo nimetaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuongeozana naye, kwa idhini yako kama ningepeta nafasi ningependa kwenda kushuhudia vijiji vitano ambavyo amevitaja vya Nyashilanga, Nyamikonze na Izunya ambavyo vitawashwa umeme Ijumaa ijayo. Lakini kwa ridhaa yako niombe kuongozana nawe Mheshimiwa Mbunge mara baada ya Bunge hili ili tukawashe umeme kwenye vijiji vyako kama ambavyo nimekusudia, ahsante sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Tatizo la maji katika Jimbo la Nyangh‟wale ni kubwa sana. Kuna mradi ambao unaendelea pale wa kutoa maji Ziwa Victoria kuyapeleka Wilayani Nyangh‟wale. Mradi huo umekuwa ukisuasua kwa muda mrefu na nimejaribu kuongea na wakandarasi wanadai kwamba wamesimama kuendeleza mradi ule kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Kuna mabomba mengi ambayo yameshasambazwa na yapo nje yanapigwa jua kwa zaidi ya miaka mitatu. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwapatia fedha hawa wakandarasi ili waweze kukamilisha mradi huo wa maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kwamba Bunge lilipitisha Mfuko wa Maji na Mfuko huu tunashukuru kwamba kila mwezi fedha inatoka na ninyi wenyewe ni mashahidi huko mlikotoka kutokana na Mfuko huu tayari yale madeni yanalipwa na tunaendelea kulipa. Kama madeni hayajalipwa basi ujue kuna matatizo madogo madogo ya kiutendaji. Kwa hiyo, Mheshimiwa Hussein mimi nalibeba niangalie kwa nini huko hakujalipwa ili tuhakikishe kwamba mradi huo wakandarasi wanalipwa ili waweze kuukamilisha.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali. Mheshimiwa Waziri wa Maji nimewahi kuonana naye mara nyingi sana kuhusu mradi wa maji kutoka Nyamtukuza kwenda mpaka Bukwimba. Mradi ule umepangiwa 15,000,000,000 mpaka sasa hivi Serikali imeshatoa bilioni 3.5 lakini cha ajabu hata kijiji kimoja hakijawahi kupata maji. Je Serikali ina mpango gani ili kuweza kukamilisha mradi huo wa maji ili wananchi wa Nyangh’wale waweze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Hussein tumeweka utaratibu kuhakikisha kwamba miradi yote ambayo ilianza tunaikamilisha kwanza kabla ya kuingia kwenye miradi mipya. Sasa hivi tunaendelea kuzunguka kubaini mahali popote pale ambapo pamehujumiwa Mheshimiwa Mbunge taratibu za kisheria zitafuatwa.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Halmashauri ya Nyang’wale imeanzishwa zaidi ya miaka minne na pakatokea kosa la kiuandishi katika GN yake, badala ya kuandikwa Nyang’hwale Makao yake Makuu Karumwa, ikaandikwa Makao Makuu Nyang’hwale na taarifa hii tumeshaileta na tayari leo zaidi ya miaka miwili GN ya Nyang’hwale mpaka sasa hivi hatujaipokea. Je, Mheshimiwa Waziri anatuambia nini sisi Wana-Nyang’hwale, kuna tatizo gani ambalo limekwamisha kuitoa GN hiyo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli yapo makosa mengi, siyo kwako tu, lakini utaratibu na masahihisho yote yanafanywa na Katibu wa Bunge. Ikishatolewa ile GN, kama kuna marekebisho, inarudishwa na Katibu wa Bunge anaombwa kurekebisha. Bahati nzuri ya kwako iko tayari imerekebishwa na jana ilikuwa ofisini kwangu. Karibu uje uichukue. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Rais wa Awamu ya Nne alifanya ziara yake katika Wilaya ya Nyang’hwale na kuahidi ujenzi wa barabara kutoka Kahama –Nyang’holongo – Bikwimba – Karumwa – Nyijundu – Busolwa – Ngoma - Busisi (Sengerema) kwa kiwango cha lami. Pia 2010 Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano na yeye alifanya ziara katika Wilaya hiyo ya Nyang’hwale na kuahidi ahadi hiyo hiyo ya ujenzi wa barabara hiyo hiyo. Je, kauli ya Serikali ni lini upembuzi yakinifu utaanza kwa ujenzi wa barabara hiyo ya lami kutoka Kahama - Karumwa - Busisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia sana kuhusu ujenzi wa barabara hii na kwa sababu hiyo anafahamu mimi niliamua kupita barabara hii wakati nikitoka Mwanza na Geita na kweli nimeona umuhimu wa barabara hii walau sasa wataalam watakachokuwa wanaeleza nitakuwa nafahamu wanachosema ni nini. Nikuhakikishie, mara fedha zitakapopatikana kwa shughuli hii kazi hii itafanyika.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa swali langu lilikuwa la Wilaya ya Nyang’hwale na nimejibiwa kimkoa, Nyang’hwale imeshajipanga tayari na imetenga maeneo ya kuweza kujenga Chuo cha Ufundi. Je, Serikali imeshaweka ndani ya mpango 2018/2019 mpango huu wa kujenga VETA katika Wilaya ya Nyang’hwale?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali huwa mipango yake inaenda taratibu na Nyang’hwale ina vijana wengi ambao hawana ujuzi. Je, Serikali iko tayari kuchukua angalau vijana 50 na kuwapeleka katika maeneo mengine mbalimbali nchini kwenda kujifunza ujuzi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, kuhusu kama katika bajeti ya mwaka 2017/2018 tumetenga fedha kwa ajili ya kujenga Chuo cha VETA Nyang’hwale; nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba tunajitahidi kutenga fedha kadri tunapopata kwa ajili ya kujenga Vyuo mbalimbali vya VETA. Kwa sasa hakuna fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya Nyang’hwale; lakini nimwahidi tu kwamba kwa sababu mpango wetu ni kuhakikisha Wilaya zote zinakuwa na Vyo vya VETA tutaendelea kupangilia na kutafuta fedha na kujenga kadri inavyowezekana.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kama tuko tayari kupeleka vijana 50 kwenye Vyuo vingine nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, kama wao watajipanga kama Wilaya sisi tuko tayari kushirikiana nao kuhakikisha kwamba vijana hao wanapata nafasi katika Vyuo vingine.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja. Ningependa kujua Wilaya ya Nyangh’wale Makao yake Makuu ni Karumwa, lakini nikiuliza kila mara hapa kuhusu GN ya Makao Makuu ya Wilaya Nyangh’wale ambayo ni Karumwa, leo hili swali ni mara ya tano, kila nikiuliza naambiwa GN iko tayari lakini cha ajabu mpaka leo hatujakabidhiwa katika Halmashauri yetu ya Nyangh’wale. Je, GN hiyo tutakabidhiwa lini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba uniruhusu nitoke na Mheshimiwa Amar mara baada ya kipindi hiki twende kwenye Idara yetu ya Sheria ili tuweze kumpatia majibu sahihi.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa uzinduzi wa REA Awamu ya Tatu kimkoa wa Geita ulifanyika kwenye Wilaya ya Nyangh’wale, Kijiji cha Nijundu, mwenzi wa sita mwaka jana, lakini cha ajabu mpaka leo hii hata kijiji kimoja kati ya vijiji 35 vya Wilaya ya Nyangh’wale havijapelekewa nguzo.
Je, ni lini sasa Serikali itaanza kupeleka nguzo hizo katika hivyo vijiji ambavyo tumepewa vijiji 35?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Amar kwa swali lake zuri, katika Mkoa wa Geita mkandarasi wake ni JV White Service Limited ambaye ameshaanza kazi, na kwa kuwa ameeleza kwamba mpaka sasa katika Wilaya yake, nataka niseme wakandarasi hawa walipoteuliwa unakuta Mkoa mmoja una mkandarasi mmoja, na Mkoa huo unaweza ukawa na Wilaya mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maelekezo ya hivi karibuni katika Mkoa wa Geita mkandarasi alikuwa ameshaagiza nguzo takribani 3,000 na tulimpa maelekezo aende kila Wilaya. Kwa hiyo, kama mkandarasi mpaka sasa hivi hajafika katika Wilaya ya Nyang’wale naomba nimuelekeze na nimpe agizo kwamba kama vile tulivyotoa maelekezo tulivyokutana kikao cha tarehe 13 Januari, wakandarasi wote wafanye miradi Wilaya zote, wasijielekeze katika Wilaya moja.
Kwa hiyo, ninamuagiza mkandarasi JV White wa Mkoa wa Geita aelekee kwenye Wilaya zote na afanye kazi ya kuunganisha kupeleka hii miundombinu ya umeme kama ambavyo tulikubaliana katika Kikao cha tarehe 13 Januari, 2018.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa mimi Mbunge wa Jimbo la Nyang’wale niliweza kujitolea na kujenga zahanati na kuikamilisha katika Kijiji cha Mwamakiliga na kwa kuwa niliweza kujitolea na kujenga wodi mbili na chumba cha kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya ambayo ni Hospitali ya Wilaya ya Nyang’wale, nimeweza kuyafikisha majengo hayo kiwango cha asilimia 75 na nimekwama. Je, Serikali inasaidia vipi sasa kuweza kuifungua ile zahanati ya Mwamakiliga ili iweze kufanya kazi na kukamilisha majengo hayo yaliyo katika Kituo cha Afya Kalumwa ili yaweze kufanya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Hussein Nassoro Amar kwa kujitoa kiasi hicho kwa ajili ya wananchi wa Nyangh’wale. Nimwombee dua Mungu apokee swaumu yake katika Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa sadaka hiyo kubwa aliyoitoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimhakikishie kwamba sisi tutakuwa pamoja naye, bahati mbaya sikufika pale Kalumwa wala Mwamakiliga nilipokuja kwenye ziara ya Mkoa wa Geita, lakini baada ya Bunge hili nina ziara tena ya kuzunguka mikoani na nitapita Mkoa wa Geita na mahsusi nitafika kwako na kwa Mheshimiwa Musukuma nina ahadi yangu naikumbuka. Nitakapofika pale, nitaongea na wataalam wale tujue ni nini cha kufanya kwa kushirikiana na wenzetu wa TAMISEMI ili kuweza kuunga mkono jitihada nzuri alizozionyesha. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo ya nyongeza, lakini naomba nitumie nafasi hii kuwapa pole wananchi wangu wa Jimbo la Nyang’hwale kwa mauaji ya kikatili ambayo yamefanyika wiki iliyopita, akina mama wanne wamenyongwa kwa kutumia kanga zao na wawili wakiwa wajawazito na mauaji hayo yanaendelea kwa Wilaya za jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali dogo la nyongeza ni kama ifuatavyo; je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha kuisaidia Halmashauri ya Nyang’hwale ili kukamilisha ujenzi wa zahanati iliyopo Iyenze na Mwamakiliga? Serikali ina mpango gani kuisaidia Halmashauri?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, naishukuru AMREF kwa kukamilisha majengo matatu yaliyopo pale Kituo cha Afya Kharumwa. Serikali ina mpango gani baada ya kukamilishwa majengo hayo kuendeleza kwa kutusaidia kuongeza vifaatiba pamoja na wauguzi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kwa dhati kabisa nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada zake za kuhakikisha wananchi wanapata huduma iliyo bora ya afya. Yeye hakika ni mfano bora wa kuigwa kwa Waheshimiwa Wabunge wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza, anauliza Serikali kusaidia Halmashauri kumalizia zahanati, ni nia ya dhati kabisa ya Serikali kuhakikisha kwamba tunasaidia, lakini kinachogomba ni uwezo. Kwa hiyo, kadri bajeti itakavyokuwa imeboreka, hakika hatuwezi tukawaacha wananchi ambao Mheshimiwa Mbunge ameonesha jitihada tukaacha kumalizia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili baada ya kazi nzuri iliyofanywa na AMREF, suala la zima la kupeleka vifaa pamoja na wataalam, ili kazi iliyotarajiwa iweze kuwa nzuri, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba vituo vya afya na zahanati zetu zote zinafanya kazi. Muda siyo mrefu, wakati tunahitimisha, Mheshimiwa Waziri wa Utawala atakuja kusema neno kuhusiana na suala zima la kuajiri watumishi wa Serikali. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mwaka wangu wa nane nikiuliza swali la ahadi ya viongozi wetu ambao wamefika katika Jimbo la Nyang’hwale.
Mwaka 2010, Rais wa Awamu ya Nne alikuja akaahidi katika kampeni zake barabara ya lami kutoka Kahama – Nyang’olongo – Busolwa – Karumwa hadi Busisi, Sengerema kujengwa kwa kiwango cha lami. Mwaka 2015 pia Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli alikuja akaahidi vilevile.
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hii ya ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kahama – Nyang’hwale mpaka Busisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kuratibu ahadi za viongozi wakuu, kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema. Tayari tunaendelea kufanya uchambuzi ili kuendelea sasa kujenga katika kiwango cha lami. Hata hivyo, kwa barabara hii Mheshimiwa Mbunge anayoitaja kuja Kahama ni barabara ambayo kwenye mpango mkakati tumeiweka. Tuwasiliane tu uone namna tulivyojipanga kwa sababu tunaendelea kupata fedha kidogo kidogo ili uweze kuona na wakati mwingine uweze kuwapa taarifa wananchi wa Nyang’hwale kwamba ni lini sasa ujenzi utakuwa umeanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini zile hatua za awali tumeshaanza, tunatambua umuhimu wa barabara hii kuiunganisha kutoka Sengerema kuja Kahama. Pia wananchi wajue kwamba eneo la jirani kabisa kutoka Kahama Mjini kwenda Geita, Bunge limepitisha fedha za kutosha, tutaanza ujenzi wa barabara hii ya lami. Kwa maana hiyo tunatambua umuhimu wa kutekeleza ahadi za viongozi pamoja na Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge niwahakikishie tu kwamba tunaendelea kuhakikisha kwamba ujenzi wa barabara unafanyika.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Napenda kuipongeza Serikali kwa kutenga shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nyang’hwale. Napenda niiulize Serikali, huduma ya X-ray kwa Wilaya ya Nyang’hwale ni shida sana. Kuna ajali mbalimbali ambazo zinatokea na kuifuata huduma ya X-ray karibu kilomita 110. Je Serikali ina mpango gani wa kuleta mashine ya X-ray katika Hospitali ya Wilaya ya Nyang’hwale? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ambayo Waheshimiwa Wabunge wamefanya vizuri kwenye suala zima la afya kwa maana ya ujenzi wa vituo vya afya na zahanati ni pamoja na kwa Mheshimiwa Amar. Naomba nimpongeze kwa dhati kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba X-ray zinakuwepo ndani ya vituo vyote vya afya na ndiyo maana katika maboresho ambayo yamefanyika hivi karibuni ni pamoja na kuongeza jengo la X-ray. Sasa kama X-ray zinakuwepo kwenye vituo vya afya sembuse hospitali ya wilaya! Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tukitoka hapa tuwasiliane tujue nini hasa ambacho kimetokea mpaka hospitali yake ya Wilaya ikose X-ray. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete alikuja jimboni na akaahidi ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kahama – Nyang’olongo – Bukwimba - Kalumwa - Busolwa hadi Busisi Sengerema na Rais wa Awamu ya Tano pia aliahidi hivyo hivyo. Je, Serikali ni lini itatenga fedha ya upembuzi yakinifu ili kuanza kuijenga barabara hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua hii barabara Mheshimiwa Mbunge tumezungumza mara nyingi, ni barabara ambayo inaenda kuunganisha pia katika Jimbo la Msalala kuja Kahama Mjini. Kwa hiyo, kama tulivyozungumza tutaangalia sasa namna nzuri tuweze kuiingiza kwenye usanifu, kwa sababu zile barabara ambazo zinakwenda kuunganishwa na barabara hii Mheshimiwa Mbunge, unajua ile barabara inayokwenda Geita ni muhimu sana kwamba tutaweza kuwa na kipande cha kwenda Sengerema. Ni kipande kifupi Mheshimiwa Mbunge kinahitaji commitment ya fedha siyo nyingi sana. Kwa hiyo, azidi kuvuta subira tutaendelea kutazama kwenye bajeti zinazokuja.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Nataka nipate majibu kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kahama – Nyangolongo - Bukwimba, Kalumwa - Busolwa – Busisi, ni lini ujenzi huo utaanza kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hussein, Mbunge wa Nyang’wale, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ziko barabara nyingi nchini ambazo ziliahidiwa na Mheshimiwa Rais na viongozi wengine wakuu. Ni kweli pia katika eneo hili la Nyang’wale kuna ahadi hii ya barabara kutoka Kahama kwenda hadi Busisi. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge labda baadaye tuonane ili angalau tuzungumze kwa upana ili apate details.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa wachimbaji wa Msalala kero zao zinafanana kabisa na kero ya Wilaya ya Nyang’hwale; nataka kujua ni lini Serikali itatoa leseni kwa wachimbaji wadogo wa maeneo ya Bululu, Ifugandi, Kasubuya, Isonda, Nyamalapa, Lyulu, Lubando na Iyenze ili hao wachimbaji waweze kupata hizo leseni na kuchimba ili waweze kuwa na uhakika wa uchimbaji wao na waweze kupata mikopo kutoka benki waweze kuchimba kisasa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amar kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumetenga maeneo mengi na tumetenga maeneo makubwa, zaidi ya maeneo matano katika maeneo hayo.

Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyozungumza katika majibu ya swali la msingi, nimewaomba wananchi wa maeneo hayo wachangamkie hii fursa, waje waombe tuwagawie maeneo haya. Mpaka sasa hivi tuna maombi mengi ambayo tayari yamekwishatolewa na sisi sasa hivi tuko katika mchakato wa kuwagawia wachimbaji wadogo na ni maeneo ambayo ni mazuri, yana reserve ya kutosha na wataweza kuchimba kwa faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mikopo bado tunaendelea kuweka mchakato mzuri wa kuweza kufanya resource estimation katika maeneo mbalimbali ya uchimbaji ili tupate uhakika wa reserve na benki ziweze kuwaamini hawa kutokana na data ambazo tunaweza kuzitoa katika geological reports zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kutoa fursa au kuwaeleza wananchi wa maeneo haya kwamba, wachangamkie fursa tuweze kuwagawia maeneo ya uchimbaji.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda nimuulize Waziri, kwa kuwa kuna mradi mkubwa wa maji kutoka Nyamtukuza katika Wilaya ya Nyang’hwale, kupita Kakora, Kitongo, Ikangala, Kharumwa, Izunya hadi Bukwimba ambao umekuwa ukisuasua kwa muda mrefu, lakini Serikali ikiwa ikitoa pesa. Je, ni lini sasa mradi huu utakamilika na namwomba Mheshimiwa Waziri baada ya Bunge hili aende akauone mradi huo kwa nini unaendelea kusuasua?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge. Kubwa pamoja na mradi huo, lakini tumeshalipa zaidi ya bilioni moja na milioni mia saba certificate yake kwa Mkandarasi anayedai, ili mradi usikwame.

Kuhusu kusuasua kwa mradi, sisi kama Wizara ya Maji, Wahandisi ama Wakandarasi wababaishaji tutawaweka pembeni, nataka nimhakikishie kabla ya Bunge tutakwenda Nyang’hwale katika kuhakikisha tunaenda kuukagua mradi ule na ikibidi kama Mkandarasi hana uwezo wa kutekeleza mradi huo tutamwondoa mara moja. Ahsante sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kuna tatizo kubwa upande wa watumishi wa Madini na TMA. Kumekuwa na ucheleweshwaji sana wa ushushaji wa mashine upande wa elution na kusababisha hasara kwa wenye elution na pia kwa wachimbaji:-

Je, Serikali imejipanga vipi kuongeza watumishi upande wa TMA na Madini ili ushushaji wa mashine zile za elution iwe wa kila siku ili kupunguza zile hasara wanazozipata watu wenye elution?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna tatizo kidogo kwa wafanyakazi ambao wapo katika Tume ya Madini. Kwa sababu baada ya mabadiliko ya Sheria TMA ilikufa, imeanzishwa Tume ya Madini. Kwa hiyo, sasa hivi wafanyakazi wote, walioko Mikoani wako chini ya Tume ya Madini. Tuna tatizo kidogo kwa wafanyakazi, lakini sasa hivi tuna kwenda kuongeza wafanyakazi wengi zaidi ili waweze kutoa huduma kwenye zile elution.

Mheshimiwa Spika, bado naendelea kusisitiza, watu wote wenye elution tumeona kuna matatizo makubwa sana yanayofanyika, watu wengine wanaenda kule wanafanya mambo ambayo hayaeleweki. Tunaendelea kudhibiti na tunaendelea kutoa tamko kwamba wanapo-load carbon kushusha dhahabu wasijaribu kushusha bila uwepo wa wafanyakazi wa Tume ya Madini. Tunakwenda kuongeza, lakini sasa hivi tunajitahidi kuhakikisha kwamba kila siku waendelee kutoa huduma hiyo.

Mheshimiwa Spika, namhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi, tunaendelea kurekebisha.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri kwamba wake wa Wabunge ama waume wa Wabunge wana haki mbalimbali za kupata huduma kama vile kupita njia za VIP lakini cha ajabu ni kwamba wake zetu wanapata shida sana upande wa VIP. Je, wana haki ama hawana haki ya kupata huduma upande wa VIP, kama vile kwenye feri na viwanja vya ndege?

MWENYEKITI: Kwenye viwanja vya ndege?

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano viwanja vya ndege pamoja na feri.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la ndugu yangu wa Nyang’wale, Mbunge mahiri sana, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli ulio wazi kwamba wake au waume au wenza wa Wabunge wanayo haki yote ya kutumia VIP na sijawahi kuona hilo tatizo ninapotembelea viwanja mbalimbali vya ndege. Kwa hiyo, Mheshimiwa kama lilikutokea tunaomba radhi lakini siyo kitu cha kawaida, wenza wa Wabunge huwa wanapata huduma zote stahiki za VIP.