Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Deogratias Francis Ngalawa (7 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kukupongeza kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Bunge lako Tukufu. Naitwa Deo Ngalawa, Mbunge wa Ludewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipende kukishukuru Chama cha Mapinduzi kwa namna kilivyoiandaa Ilani yake. Ilani yake ni Ilani nzuri ambayo imetengeneza mpango mzuri wa mwelekeo wa Taifa ambako linatakiwa kwenda. Katika chaguzi zetu tuliinadi Ilani na wananchi wakatuchagua. Kwa hiyo, napenda kukipongeza chama. Hawa wanaotoka sasa ni kwa sababu hoja zao nyingi zinapwaya, hawana kitu cha kukizungumzia zaidi ya kutengeneza vijembe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi napenda kujikita katika hotuba ya Mheshimiwa Rais moja kwa moja. Mheshimiwa Rais katika hotuba yake katika ukurasa wa 12 ameizungumzia reli toka Mtwara – Songea – Mbamba Bay mpaka Liganga. Mimi napenda kumshukuru kwa hilo na tulipokuwa tunaizungumzia hiyo reli ya kutoka Mtwara mpaka Liganga ni kwa maana tunazungumzia suala la makaa ya mawe - Mchuchuma na chuma – Liganga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la makaa ya mawe - Mchuchuma na chuma – Liganga limekuwa ni suala la muda mrefu. Nadhani sasa ni kipindi cha miaka 50 limekuwa likizungumziwa na halina utekelezaji wowote. Nimshukuru Waziri Profesa Muhongo, tarehe 4 na 5 alifika kwenye makaa ya mawe Mchuchuma na vilevile alifika pale chuma – Liganga; alijionea type ya wawekezaji ambao tunao na namna gani wanaweza wakaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nisikitike, wana wa Ludewa wana masikitiko makubwa. Wameachia ardhi yao miaka ipatayo 10, ardhi ile haitumiki, hawaitumii kwa maana yao na hakuna utaratibu wowote wa matumaini wa kulipwa fidia katika maeneo ambayo wao wameyaachia.
Sasa nipende kuliambia Bunge lako, wananchi wanataka fidia ya maeneo waliyoyaacha na kibaya zaidi hata ule mpango wa kimkakati wa huyu mwekezaji bado hauonekani!
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na Waziri Muhongo tarehe 5 Mchuchuma, pale Nkoma Ng‟ombe na vilevile tulikuwa Liganga pale Mndindi; Serikali imekuwa ikiwakilishwa na NDC na wawekezaji ni Wachina, lakini katika majadiliano na maongezi yao wana contradiction kubwa. Ile miradi ni mikubwa, kuna mamilioni ya tani za makaa ya mawe, leo nchi inazungumza kwamba haina umeme! Lakini tunaamini mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma ukianza umeme katika Taifa hili inaweza ikawa ni historia.
Mheshimiwa Naibu Spika, umeme utakaozalishwa Liganga una uwezo wa ku-supply ndani ya nchi hii katika miaka isiyopungua 150, lakini leo Taifa bado halijachukua hatua madhubuti. Ni miaka mingi, sisi wengine toka tunasoma, kabla hatujazaliwa tunaambiwa kuna makaa ya mawe – Mchuchuma, tunaambiwa kuna chuma – Liganga! Mwekezaji aliyepo ameonesha incompetence kubwa mbele ya Waziri Profesa Muhongo! Hakuna maandalizi ya kutosha ya hiyo miradi kuanza!
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi nipende tu kushukuru na kumshukuru Mheshimiwa Profesa Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini, aliwaeleza wananchi wetu ukweli kwamba Taifa tunapoamua kuingia mikataba hii iwe ni ya wazi na kusiwepo na uficho wowote.
Mimi ninaamini Waziri usingekuja Ludewa, usingekuja pale Nkoma Ng‟ombe – Mchuchuma, usingekuja Liganga bado wananchi wetu wangekuwa wanaendelea tu kudanganywa danganywa na tusingejua fate yoyote ambayo inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nipende kuchukua fursa hii kwamba, tupate wawekezaji ambao ni serious. Tupate wawekezaji ambao wana uhakika, ili mwisho wa siku watu wetu tuwajengee matumaini, ili nchi iweze kwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukizungumza sana Bungeni kwa nini nchi haiendi, wakati tuna madini ya kutosha, tuna mazao ya kutosha, lakini hatuchukui hatua. Huyu mwekezaji amekuwa akikumbatiwa! Haoneshi dalili yoyote ya namna gani tunaweza kwenda! Fidia hataki kulipa, anaulizwa kama hizo hela anazo anasema hela hana anasubiri kukopa nje ya nchi! What type of mwekezaji is? Sasa investor wa namna hii kweli tunakaa na kumkumbatia namna hii? Mimi nadhani siyo sawa! (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Ludewa wanaisubiria Liganga ianze mara moja kwa sababu, imeshakuwa ni hadithi za muda mrefu. Liganga aanze, Mchuchuma aanze, tuachane na hii biashara kwamba hatuna umeme, hatuna umeme, hatuna umeme! Hii inatakiwa kubaki kuwa ni historia. Lakini mimi ninamuamini Waziri Muhongo atalishughulikia hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna barabara ya Itoni – Njombe kuelekea Manda; barabara hii Mheshimiwa Rais ameahidi kwamba iwekwe lami, lakini nashukuru TANROADS juzi imetangaza kipande cha kilometa 50 kutoka Lusitu kuelekea Mawengi kwamba kitawekwa lami. Kwa hiyo, tunaomba hili lizingatiwe na lifanyiwe kazi haraka vya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna barabara kutoka Mkiu kwenda Madaba na yenyewe Mheshimiwa Rais ameizungumzia kwa kiwango cha lami. Tunaomba lami hiyo iwekwe na wananchi wana matumaini, wana mazao yao mashambani, ila usafiri umekuwa ni shida, pindi hizi lami zikiwa tayari naamini kabisa mazao yatafika kwenye maeneo ya masoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna suala la miundombinu ya mawasiliano ya simu. Leo hii Tarafa nzima ya Mwambao, Ukisi kule Ziwa Nyasa tunapakana na Malawi, vijiji 15 havina mawasiliano ya simu kabisa! Sasa sijajua Serikali inajipangaje na inawaonaje hawa watu? Hawa watu wako mpakani! Huku tunapakana na Kyela na Dkt. Mwakyembe! Huku tunapakana na Nyasa na Engineer Manyanya! Hapa katikati pamekuwa hamna mawasiliano ya aina yoyote! Wananchi wale wameniambia wataanza wao kutafuta hayo mawasiliano. Hatuna mawasiliano ya barabara, hatuna mawasiliano ya simu! Kwenye upande wa barabara wanasema wao wataanza na jembe la mkono. Na ninaiomba Serikali sasa ituunge mkono, ili tuweze kuviunganisha hivi vijiji na waonekane na wao wapo ni sehemu ya nchi hii ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukiahidiwa muda mrefu juu ya daraja la Mto Ruhuhu unaounganisha Wilaya ya Ludewa na Wilaya ya Nyasa. Wananchi wanapata shida na kivuko kile na kivuko kimekuwa hakifanyi kazi. Dada yangu Injinia Manyanya unalifahamu hilo. Tunaomba Serikali ilichukue hilo na ilifanyie kazi, ili mwisho wa siku tuweze kwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mambo mengi sisi wana wa Ludewa. Mheshimiwa Rais alipokuja Ludewa alitoa ahadi ya kipande kidogo cha lami cha kilometa 25 kutoka Ludewa mpaka Lupingu. Kwa hiyo, tungeomba ahadi hizo zitekelezwe.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, muda wako umeisha!
MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwanza kwa kupata nafasi ya kuweza angalau kujadili hotuba ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Kwanza kabisa napenda kutoa kilio changu cha wana wa Ludewa, kwa sababu Ludewa sasa inaonekana ni eneo ambalo limesahaulika kwenye mambo mengi. Hivi ninavyoongea sasa, Jimbo la Ludewa lina uhaba wa Walimu 496, tuna shule 108; katika shule hizo 108 ni shule saba tu ndizo ambazo zina Walimu wanaoweza kukidhi. Shule nyingine zote 101 zina Walimu wanne kushuka chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shule ambayo ina Walimu wawili na shule zilizo nyingi zina Walimu watatu. Kwa hiyo, cha kwanza napenda tu kutoa masikito yangu kwamba tuna uhaba wa Walimu 496 na bahati mbaya kabisa katika kipindi hiki mmetupatia Walimu 30. Hata hivyo kuna Walimu 25 ambao wanastaafu Septemba na kupelekea uhaba wa Walimu 521.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuwasiliana na TAMISEMI, sasa napenda kutoa kilio hiki kwako Mheshimiwa Waziri kwa sababu wewe ndiye msimamizi wa elimu Tanzania. Kwa hiyo, naomba tu mwisho wa siku nikuletee majina kwa watu ambao wanataka kwenda kufundisha Ludewa na ikiwezekana basi mfanye utaratibu mtuletee Walimu. Kwa kweli hali ni ngumu na ndiyo maana nimeamua nije nizungumze katika Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, hata vyuo vyetu vikuu havipeleki wanafunzi kwenda kufanya field kule, kwa sababu ya miundombinu mibovu ya barabara na miundombini mibovu ya mashule yetu, kiasi ambacho kimepelekea hata wanafunzi wenyewe wanaotoka kule kuomba msaada huo. Kwa hiyo, naomba nikuwasilishie hilo na hasa Chuo Kikuu cha Dodoma, kwamba hawawezi kupeleka Ludewa, lakini maeneo mengine yote ya Tanzania wanafunzi wanaweza kwenda kufanya field. Hii inapelekea shule zetu za Ludewa kuwa na pass ya chini kabisa na vijana wetu wengi kufeli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda ku-declare interest, mimi ni mmiliki wa shule. Nianze na ada elekezi. Nadhani shule hizi za binafsi ndiyo zinazoleta fundisho kwa Serikali yetu kwamba ni namna gani shule zinapaswa ziwe na ninadhani zimeshaweka standard ya kuweza ku-move. Kwa hiyo, sababu ya kuweka ada elekezi, siyo za msingi na wala hazifai. Ninajiuliza swali, tusingekuwa na shule za private, watoto tulikuwa tunapeleka Kenya na Uganda. Je, kule Uganda tungeweza kupeleka hizo ada elekezi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suppose huku tungekuwa hatuna na kipindi kile kabla ya St. Marys kuanza, watoto tulikuwa tunapeleka Kenya. Kwa hiyo, kosa letu ni kuboresha elimu, kutengeza miundombinu mizuri, mpaka inapelekea kuwa tunaongoza kwa hamsini bora. Hilo ndiyo kosa ambalo Serikali imeliona. Nadhani Serikali ingeshukuru, kwa sababu ninaamini kabisa wanafunzi wengi ambao wanang‟ara ndani ya mipaka ya Tanzania na nje ya mipaka ya Tanzania, ni wale ambao wanatoka private school, wanatuwakilisha. Kwa hiyo, tungewatengenezea miundombinu mizuri, ikiwezekana hata kuchukua mishahara mlipe nyie Serikali, kwa sababu watoto wanaofundishwa ni watoto wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sababu zile za msingi kupelekea kuweka hizo ada elekezi hamna. Kwa sababu usi-justify makosa unayoyafanya, usi-justify kutokuweka jitihada zozote ili uweze ku-capitalize kwenye shule za binafsi. Play your part, fanya shughuli zako, ninaamini ukitengeneza miundombinu mizuri, ukiwa na Walimu wa kutosha, hakuna mtu atakayeenda kwenye shule zenye gharama kubwa. Kwa hiyo, isifike kipindi Serikali inashindwa kufanya wajibu wake, kwa madai tu iende ika-suppress kwenye hizi shule za binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za binafsi ziachwe ziendelee, kwa sababu yale mazingira yaliyowekwa vizuri, wamiliki wa shule wengi wamekopa mikopo, wana madeni yenye riba kubwa. Kwa hiyo, maana yake utakaposema unatoa ada elekezi, tutashindwa kulipa yale madeni na mwisho wa siku sasa wakati huku tayari shule za private zimeshakaa vizuri, tunabomoa wakati huku kwetu kwenye government schools hatujaparekebisha bado.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni juu ya ujenzi wa Shule ya VETA Shaurimoyo, katika Jimbo la Ludewa. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri hajaiweka kabisa. Shule hii ya VETA kimsingi ilikuwa inaanzishwa pale kwa ajili ya kupokea miradi mikubwa miwili ya makaa ya mawe Mchuchuma na Chuma cha Liganga, kuwaandaa vijana kwenye shughuli za kiufundi ili kuweza kushiriki katika hiyo miradi inayokuja. Nakumbuka mwaka 2012; kama siyo 2012, ni mwaka 2013, Serikali iliji-commit kwamba itajenga chuo hiki. Naamini sababu zile zile za kukitaka kukijenga hazijatoweka, sababu hizo zipo. Mlipeleka wataalam, ardhi imepimwa, hati mmepata, michoro mnayo, BOQs zote mnazo na mlisema mlishatenga hela kwa ajili ya kujenga hicho Chuo cha VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza tena swali hili, Chuo hicho kwanini kimeachwa? Matokeo yake, vile ambavyo wala havikuwepo katika kipindi hicho cha miaka miwili, mitatu iliyopita, leo ndiyo vimewekwa. Sasa watu wa Ludewa wanajiuliza maswali ya msingi, pana tatizo gani? Kwanini kisijengwe na kwanini hakuweka kwenye program yake? Kwenye hili Mheshimiwa Waziri hatutakubali kwa sababu kinachoonekana ni kuibagua Ludewa na Ludewa haitaweza kubaguliwa kwa sababu na yenyewe ipo katika nchi ya Tanzania.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja lakini tunaomba Chuo Ludewa.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kupata nafasi ya kuzungumza na kuchangia hoja ya Wizara ya Viwanda. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa kwa kishindo na Mawaziri wote kwa namna nzuri wanavyofanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu inajikita zaidi kwenye maeneo ya biashara. Hoja ya nchi kutaka kwenda kwenye viwanda ni nzuri, lakini kitu ambacho nakuwa na wasiwasi nacho ni namna ya utekelezaji wa hoja zetu. Ninavyojua, suala la viwanda ni mtambuka, sasa sijajua kwamba Serikali imejiandaaje katika kuhakikisha kwamba inawaandaa Watanzania katika mapokeo hayo. Ki-mind set Watanzania bado hawajawa tayari kwenye hilo, hivyo wanahitaji training ya namna gani ya kuweza kuipokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunapozungumza, tuna wafanyabiashara wengi sana ambao wako informal na kundi hili la wafanyabiashara ni kubwa. Asilimia 70 ya wafanyabiashara wote wa Tanzania wako kwenye kundi ambalo ni la informal. Kwa hiyo, bado Serikali haijafanya mchakato mzuri wa kuhakikisha kwamba tunawaandaa wafanyabiashara wetu ili mwisho wa siku waweze ku-formalise biashara zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa nini hizi biashara ziko informal? Ziko informal kwa sababu sheria haziko friendly. Tuna kundi kubwa la wafanyabiashara ambao wanashindwa ku-formalize biashara zao kwa sababu ya usajili; namna ya kuzisajili zile biashara inakuwa ni ngumu; na namna ya kupata leseni inakuwa ni ngumu. Leo hii tunaambiwa TIN number ni bure lakini ukijaribu kuangalia na kwenda, kupata hizo TIN number kwa ajili ya kufanyia hizo biashara, zile TIN number zina usumbufu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii unaambiwa, unapotaka kuanza kufanya biashara zako ni lazima kwanza utoe kiwango fulani cha hela hata kabla hiyo biashara hujaifanya. Sasa lile linawasumbua sana wafanyabiashara wetu mpaka inafikia kipindi kwamba anaamua acha afanye biashara kiholela, Serikali inakosa kodi na watu wanaweza wakafanya biashara nje ya mfumo sahihi. Nadhani umefika wakati sasa tuendeshe training na ikiwezekana hawa watu wetu tuwatengenezee namna ya kujua fursa za biashara zilizopo na ikiwezekana tupate elimu nzuri ya namna hawa watu wetu watafanya biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la elimu ya ujasiriamali na fursa za biashara bado tuko nyuma. Kuna fursa nyingi ambazo vijana wetu na watu wetu wanazo na wanatakiwa kuzifanya, lakini hawajawa exposed. Nadhani ifike wakati sasa Serikali ifanye hatua za makusudi kuendesha training kwenye vijiji, kwenye mitaa, ili mwisho wa siku watu wajue ni vitu gani wanaweza kufanya. Kwa sababu fursa zipo zinawazunguka, lakini watu hawajui wafanye nini na mbinu gani watumie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tuna Maafisa Biashara kwenye Manispaa zetu, kuna Maafisa Biashara kwenye Halmashauri zetu, lakini tukijaribu kuwauliza Mpango Kazi wao ni upi? Walio wengi wala hawajui. Waulize Maafisa Biashara kwenye Halmashauri zetu, kuna wafanyabiashara wangapi ndani ya Halmashauri? Hawezi kukupa takwimu. Kwa hiyo, hili nalo ni tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ifike mahali Serikali lazima itambue ina wafanyabiashara wangapi? Hata tunapozungumza kwamba kuna mfumo ule PPP maana yake nini? Kwa sababu kuna watu wengine hawajui. Kwa hiyo, kwa kufanya hivyo, maana yake kwanza tutawatambua wafanyabiashara na mwisho wa siku ni kwamba hata unapoamua kupanga kodi, unapanga kodi kwa watu ambao unawafahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la viwanda. Kwenye hotuba yako Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 52, umezungumzia mradi wa kasi mpya wa kuzalisha chuma ghafi. Mara nyingi huwa napata shida, pale unapozunguza kwamba utatekelezwa halafu usiseme utatekelezwa lini.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ndiyo tupo kwenye bajeti ya kwanza ya utekelezaji wa miaka mitano kwa Serikali ya Awamu ya Tano. Naamini unapozungumza mradi, lazima uwe na mahali pa kuanzia na mahali ambapo panatakiwa kuishia. Kwa sababu ukiileta statement too general unakuwa hujatupa tool ya sisi kuku-assess wewe, kwa sababu hata mwakani tukija, utasema hivi hivi, kwamba mradi huu utatekelezwa na Kampuni ya Maganga Matitu Resources Development. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani ifike mahali sasa unapozungumza mradi, hata kama utataka kuutekeleza mwaka 2018, mentioned, kwamba mradi huu utatekelezwa muda fulani na unatarajia labda kwisha muda fulani, hivyo tutakwenda vizuri. Kitu chochote unachokiita ni project lazima kiwe na mwanzo na lazima kiwe na mwisho. That is a project. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini statement zisiwe too general. Leo hii unasema unatekeleza mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma kuendeleza utekelezaji wa mradi unganishi wa makaa ya mawe Mchuchuma na chuma cha Liganga, kwenye ukurasa wako wa 161. Chuma cha Liganga tumeshaanza kukisikia toka 1906, kwa hiyo, ni kabla hatujazaliwa na inawezekana hata kabla babu zetu wengine hawajazaliwa. Kwa hiyo, ifike kipindi sasa Serikali iseme, wakati tunauliza swali hili kwenye Wizara ya Madini walituambia kwamba fidia itaanza kulipwa mwezi Juni, mwaka 2016 na mradi utaanza mwezi Machi, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa natarajia kwenye ripoti ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda ange-mention hii kitu, kwamba mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma na chuma cha Liganga utaanza Machi, 2017 kama swali lilivyokuwa limejibiwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini ili tuwe tunakwenda kwa takwimu. Kwa sababu usipotoa takwimu na muda (time frame) maana yake hatutaweza kuku-assess na kuku- pin.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hii Serikali tumeshazungumza kwamba ni Serikali ya viwanda na tunatarajia kwamba tutaenda kwa kasi kubwa. Natamani kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, aseme kinaga ubaga, kwamba tutaanza muda fulani ili tutakapokuja hapa mwakani tuwe na maswali ya kumuuliza. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, hivi viwanda vya kimkakati kwa sababu ameshasema ni National Flagship Project, haitakiwi kuwa na majibu general. Leo hii watu hawajaandaliwa kwa maana hii miradi itahitaji support. Licha ya ukubwa wa hivi viwanda vinavyokuja kule, nilikuwa natarajia kwamba Mheshimiwa Waziri angesema, kwa sababu makaa ya mawe Mchuchuma na Chuma cha Liganga inaanza, kutakuwa na vitu vya ku-support patakuwa na SIDO; hawa watu tuwaandalie uwezo wa kiufundi ili mwisho wa siku waweze kuji-engage kwenye zile bidhaa au kazi zitakazofanyika na hiyo miradi mikubwa inayokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunavyozungumza hakuna barabara ya lami inayoelekea huko. Wimbo huu umekuwa ukiimbwa muda mrefu na hata marehemu Mheshimiwa Deo Filikunjombe alikuwa akiizungumzia kwa kasi sana hii kitu. Mungu amlaze mahali pema peponi. Haijafanyiwa kitu chochote! Kwa hiyo, tuombe kwamba hivi vitu vingine lazima viwe na support ya sekta nyingine ili kuhakikisha kwamba hili gurudumu linakwenda. (Makofi)
MHE. DEOGRATIAS F NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii ya kuweza kuongea tena katika Bunge lako la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hoja zangu zinajikita katika maeneo machache sana kama mawili hivi au matatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza kabisa ni juu ya flagship project, makaa ya mawe Mchuchuma na Chuma Liganga. Kwa hiyo, tunapozungumza ni flagship project maana yake ni project ambazo zinatiliwa mkazo kwa kiasi kikubwa ili kuweza kuifanya nchi isonge mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, najikita kwanza kwenye fidia. Mradi hauwezi ukaanza kabla fidia haijalipwa na katika valuation ya ulipaji wa fidia, tunaona ripoti inasema wananchi wale wa Ludewa kwa maana ya Chuma na Liganga wanatakiwa walipwe shilingi bilioni 14. Hapo hapo nikijaribu kuangalia bajeti iliyokuwa imepangwa na Wizara hasa Wizara ya Viwanda inaonyesha ni shilingi bilioni 10.
Sasa nakuja kujiuliza swali la msingi, hii shilingi bilioni nne iko wapi? Kwa sababu katika majibu ya awali ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, pindi nilipokuwa nimeuliza swali tarehe 19 Aprili, tuliambiwa kwamba fidia inalipwa mwezi Juni, mwaka 2016. Kwa sasa tumebakiwa na muda mchache sana kuifikia Juni. Tumebakiwa na kama siku kumi au kumi na moja Juni hiyo ifike.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa sababu tulishawaaminisha Wanaludewa kwamba tunalipa hiyo fidia na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri akasema miradi hiyo itaanza mwezi Machi, 2017, nikiwa namaanisha kwamba fidia hizo zitakuwa tayari zimeshalipwa, lakini bado napata utata mmoja, kwenye strategic plan. Kwa sababu naamini nilivyokuwa nimejibiwa kwamba hizi fidia zitalipwa mwezi Juni na mradi ule unaanza 2017 mwezi Machi, naamini kwamba ningeona kwenye ripoti. Ripoti ingesema kwamba mradi huu unaanza Machi, 2017 ili kutengeneza assurance. Tusipozungumza hivyo, bado mwakani tutakuja na hadithi hizi. Hatutaweza kum-pin Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu ni moja tu, tunapozungumzia project, project ina time frame. Kwa hiyo, mwisho wa siku ni lazima utueleze mkakati wako na namna utakavyoanza na maadam umeshatu-assure kwamba mwezi Juni, 2016 unalipa fidia, watu wa Liganga na Mchuchuma na Mradi unaanza mwezi Machi, 2017, kwa hiyo, ipo kwenye plan yako. Hiyo plan inapaswa na sisi tuifahamu. Bila hivyo, nasi inatupa matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili la Mchuchuma, kwa mujibu wa wataalam na Wizara unatarajia kutupa umeme wa megawatt 600, kwa maana ya hii Mchuchuma coal. Kwa hiyo, naamini kuna haja sasa ya kutengeneza nguvu ya kutosha, huu umeme tuufanyie kazi ili uweze kuongeza kwenye pato la nchi, ili twende kwenye uchumi wa viwanda ambao tunautaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachojua, kwenye flagship project kama hii, kuna maeneo mtambuka; kuna suala la VETA. Suala hili la VETA lilizungumzwa sana na hata kipindi hicho Hayati mtangulizi wangu, Marehemu Mheshimiwa Deo Filikunjombe, Mungu amweke mahali pema peponi, alilizungumza kwa kasi, aliliuliza ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano na majibu nakumbuka yalitolewa na Mheshimiwa Mhagama kwamba feasibility study ilishafanyika, michoro ilishakuwa tayari, hati ipo na inatakiwa kuanza kujengwa. Kwa maana ya kuwaandaa vijana kushiriki kwenye mazoezi maalum kwa maana ya kazi na mambo mengineyo ambayo yatakuwepo katika hiyo miradi ya Mchuchuma na Chuma cha Liganga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikijaribu kuangalia documents zetu ambazo sisi Wabunge tumepewa, hiki Chuo sasa hakipo kabisa. Kwa hiyo, inamaanisha kwamba hatuna maandalizi ya kutosha kwa sababu ile VETA ilivyokuwa imewekwa pale, ilikuwa ni kuwaandaa watu katika kazi za ufundi ili ku-support operations ambazo zinakwenda kufanyika ndani ya miradi hii mikubwa inayokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hii shughuli ni mtambuka na inashirikisha vitu vingi, naiomba Wizara ya Madini, Viwanda na hata na Wizara ya Elimu ambayo inashughulika na mambo ya ufundi, tukae pamoja kuhakikisha kwamba miradi hii wakati inaanza, basi tuanze vile vile maandalizi ya ujenzi wa VETA. Kwa sababu ni kitu cha muhimu na bahati nzuri Bunge lako Tukufu lilishaelezwa kwamba kile chuo kitajengwa. Kama hakitajengwa, lazima tupewe sababu za msingi, zimeyeyukia wapi? Kwa nini hakijengwi? Kwa sababu tulishawaaminisha watu VETA ilishaenda mpaka Shaurimoyo kwa ajili ya kutayarisha eneo; eneo walipata limepimwa hati ipo, michoro ipo na BOQ zote zipo, kwa nini hiki chuo kisijengwe? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hilo, kwa kweli tunapaswa tulifuatilie na madamu kwa sababu Serikali ilishasema na sababu za kujengwa zilikuwepo, naamini zile sababu hazijakwisha, bado zipo, kwa hiyo, kijengwe ili tuweze kutoa mafunzo kwa wanafunzi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna suala la Maganga Matitu Resources. Suala hili la Maganga Matitu Resources, hawa wako kwenye partnership na NCD.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa katika mipango ya uanzaji wa miradi ya Mchuchuma wa makaa ya mawe na Liganga chuma. Wizara ya Nishati na Madini tarehe 19/4/2016 ilijibu kuwa fidia ya kulipa wananchi itafanywa mwezi Juni, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe fidia hii ilipaswa kulipwa mwezi Februari 2016. Wizara ya Viwanda na Biashara imetenga sh. 5,000,000,000 Liganga na kwa Mchuchuma sh. 5,000,000,000 kiasi kilichopangwa ni sh. 10,000,000,000 ambacho ni kidogo ukilinganisha na fidia ya sh. 14,000,000,000. Naomba maelezo pesa nyingine ambazo ni pungufu zitapatikanaje ili ziweze kulipwa katika kipindi kifupi kilichobaki cha Juni, 2016.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa nijaribu kujadili mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa. Moja kwa moja nijikite juu ya suala la Liganga na Mchuchuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Liganga na Mchuchuma ni suala ambalo hata tafiti zake zimefanyika toka mwaka 1929. Serikali imekuwa ikilizungumzia suala hili kwa miaka chungu nzima, lakini tulijaribu kupata faraja hasa sisi watu wa Ludewa pale tulipoambiwa kwamba miradi hii inaanza. Ikumbukwe katika Bunge lako Tukufu niliuliza swali tarehe 19/4 juu ya fidia kwa wale ambao wamepisha hii miradi kufanyika. Tulijibiwa kwamba Juni ndugu zetu wale wa Ludewa wangeweza kulipwa fidia yao na vilevile Bunge liliambiwa mradi ule ungeweza kuanza Machi, 2017. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Ludewa waliaminishwa na sasa wanapiga kelele sana juu ya hili. Nipende tu kutoa taarifa katika Bunge lako kwamba hawa watu wanajiandaa kuja Dodoma kujua hatma yao. Vinginevyo waruhusiwe yale maeneo waliyopisha kwa sababu ni maeneo ya kilimo na ndiyo wanayoyategemea waendelee na kilimo chao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mpango Mheshimiwa Waziri anazungumzia sana hili suala la Liganga na Mchuchuma, lakini jinsi ninavyoiona ni kwamba, hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa. Mpango unazungumza hapa kwamba mradi wa umeme wa megawatt 600 unaendelea, sasa najiuliza unaendelea wapi? Mimi sijaona kitu chochote kinachoendelea pale Mchuchuma. Hakuna kitu kama hicho! Labda Mheshimiwa Waziri aje atueleze na alithibitishie Taifa kwamba nini kinachoendelea kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeelezwa juu ya Power Purchase Agreement ndiyo inayosumbua, lakini mpaka sasa hatujui fate yake na mradi utaanza lini? Je, coordination ipoje kati ya Wizara na Wizara na kati ya Waziri na Waziri? Huyu anasema fidia italipwa Juni, sasa hivi tokea Juni ni miezi minne imeshapita hakuna fidia na wala hakuna tamko la Serikali linalosema kitu chochote juu ya fidia hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnapotuaminisha kwenye Bunge sisi tunaenda kuwaambia wananchi Serikali imesema moja, mbili, tatu, nne; sasa leo hii nikienda kule mimi ndiyo ninayeonekana mwongo! Sasa suala la mimi kuonekana mwongo haiwezekani, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja aje na tamko ili tulichukue na kulipeleka kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nijikite kwenye miundombinu. Leo hii tunasubiri suala la standard gauge kwa reli ya kati, tunaowategemea kuja kufanya hii kazi ni Wachina. Leo hii kitu kidogo kabisa cha Liganga na Mchuchuma tunakaa tukiyumbishana kwa suala la Power Purchase Agreement. Ninachofahamu mkataba huu siyo wa jana wala sio wa juzi, lazima kuwepo na continuity, walipoishia wenzetu sisi tuendelee. Kama pana tatizo basi tujue kwamba hili ni tatizo la msingi na tupeane maelekezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tukiwafuatilia Mawaziri wetu hawana majibu na tunarushiana mpira. Ukienda kwa Waziri wa Madini anazungumza hivi, ukienda kwa Waziri wa Viwanda anazungumza hivi, ukienda kwa Waziri wa Fedha anazungumza hivi, inafika wakati tunakata tamaa juu ya suala hili. Waziri alikuja Mchuchuma Januari na alikuwa anazungumzia hili, sasa haya mazungumzo yanachukua muda gani, lazima tuwe na time frame! Ifike mahali tuseme itakapofika tarehe hii basi hii kazi iwe imekwisha, hapo tutakuwa tunaeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni juu ya miundombinu. Kule kwetu Ludewa tumepakana na nchi ya Malawi, kuna eneo la kilometa zinazokadiriwa kuwa 200, eneo hilo halina miundombinu ya barabara hata moja na hilo ni eneo la mpakani. Nakumbuka juzi juzi hapa wenzetu walikuwa wana-demand lile ziwa na pakawa na kitu kama mgogoro. Sasa najiuliza, eneo la mpakani lenye urefu wa kilometa 200 halina miundombinu ya barabara, halina mawasiliano ya simu, hakuna umeme, je, likitokea la kutokea defense yetu ipoje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kulieleza Bunge lako, wananchi kule wameamua kuchukua hatua kulima barabara kwa mikono. Tumeshalima kilometa 40 kwa jembe la mikono na sururu. Sasa kutokana na umuhimu wa eneo hilo kiulinzi na kiusalama na kiutalii Mheshimiwa Waziri aliweke kwenye mpango. Ziwa letu lina matatizo makubwa. Hivi ninavyozungumza wiki iliyopita watu watatu wamefariki kwa sababu ya usafiri na huwa linachafuka halitoi taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda kuchukua fursa hii kuomba Serikali iwasaidie wale watu ambao wameamua bila kulipwa kulima barabara kwa kutumia mikono yao. Eneo la Ziwa Nyasa, eneo kubwa ni eneo la Ludewa kuliko Kyela, Mbinga na Nyasa. Kwa hiyo ni lazima hawa watu tuwape kipaumbele. Tuna vijiji vinavyokadiriwa 20 hakuna mawasiliano ya simu kabisa yaani ukishazama huko umeshazama, taarifa zako huwezi kuzipata. Kwa hiyo, ifike kipindi watu hawa tuwaonee huruma na Serikali itu-support kwenye hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la elimu, mpaka sasa Ludewa ina deficit ya Walimu 521 lakini tunapangiwa Walimu 40. Tumejaribu kulipeleka kwenye Idara na Wizara husika watusaidie. Sasa Mheshimiwa Mpango aliweke kwenye mpango wake kwamba Ludewa tuna uhaba wa Walimu na hata ukiangalia performance imeshuka sana kwa sababu hiyo. Kuna shule kama nane (8) hivi zina Walimu wawili au watatu, maximum ni Walimu wanne na tuna shule za misingi 108. Kwa hiyo, hivi vitu ni lazima tuviweke kwenye mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la afya, kweli Ilani ya Chama cha Mapinduzi inazungumzia vituo vya afya kila kata na pia inazungumzia zahanati kila kijiji. Labda tuzungumze sasa hapa wajibu wetu sisi kama Wabunge ni nini? Wabunge ni wahamasishaji wa maendeleo na vilevile tuna wajibu wa kukusanya nguvu na ku-mobilize watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mimi naomba moja
kwa moja nijikite kwenye Wizara ya Miundombinu. Ikumbukwe kuwa Wilaya yetu ya Ludewa,
eneo kubwa liko mpakani mwa Malawi. Tanzania imepakana na Malawi, lakini eneo kubwa la
mpaka ni eneo la Wilaya ya Ludewa, ukilinganisha na Wilaya za Kyela na Nyasa. Lakini mpaka
sasa ninavyozungumza, eneo lile halina mawasiliano ya barabara, katika eneo la tarafa ile ya
mwambao ambayo ina kata tano na vijiji 15 vilivyoongozana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kuna kipindi palitokea mgogoro, sasa mimi nikawa
najiuliza maswali, hivi mgogoro ule ungeendelea wakati hatuna barabara ya uhakika hali
ingekuwaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, nipende tu kukwambia na niiambie na Wizara wananchi wale
kwa sababu ya kuchoshwa kwa kutokuwa na barabara wameamua kuanza kulima wenyewe
kwa kutumia jembe la mkono. Wanalima kwa sururu, wanalima kwa jembe, wanalima kwa
chepe na mitarimbo. Ile ni dhamira ya dhati kabisa kuionesha Serikali kwamba wale watu wana
uhitaji wa hicho kitu. Vile vijiji vyote tumepangana, tunalima kwa jembe la mkono. Sasa niiombe
Serikali iwa-support wale watu na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri niliwaonesha
hata clips za watu wakiwa wanalima kwa jembe la mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, usafiri mkubwa tunaoutegemea ni usafiri wa maboti, kwa
sababu meli inaweza ikapita mara moja kwa mwezi na isitoshe lile Ziwa huwa linachafuka sana,
kwa hiyo, inafikia kipindi usafiri unakosekana kabisa. Kwa hiyo, niiombe Serikali kwamba sasa
ichukue hatua kwa sababu wenzetu wa Nyasa wanayo barabara inayopita kando kando ya
Ziwa; wenzetu wa Kyela, wanayo barabara inayopita kando kando ya Ziwa. Kwa hiyo,
tuwaombe sasa na sisi upande wa Ludewa tuwe na barabara ambayo inaunganisha, kwanza
itakuza utalii, halafu pili italeta maendeleo kwa sababu kuna mazao kule ya uvuvi ambayo
yanapatikana kwa wingi.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia eneo lile halina mawasiliano ya simu kabisa. Mimi
ninaamini katika nchi nane tulizopakana nazo, eneo ambalo halina mtandao wa mawasiliano
ya simu inawezekana ikawa ni mwambao wa Ziwa Nyasa. Tuna kata tano, tuna vijiji 15 halafu
viko mpakani. Sasa cha kushangaza tumekuwa tukifatilia hii kitu sijajua tatizo liko wapi lakini
ningependa tu niseme watu wa Ludewa nao wangependa kuwa na maendeleo, wangependa
kuwa na mawasiliano ya simu maeneo yale.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu bandari. Pamoja na kuwa wakati mwingine
meli ile inatembea mara moja kwa mwezi, lakini bado bandari zake ziko kwenye umbali mrefu
sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante