Contributions by Hon. Shamsi Vuai Nahodha (22 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumnukuu Mwanafasihi wa Kiingereza…
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Shakespeare aliwahi kusema maneno yafuatayo: “There is a time to hate and time to love”. Nimewasikiliza wenzangu kutoka Zanzibar kwa makini sana. Naheshimu sana mawazo yao kwa sababu kila mmoja anayo haki kwa mujibu wa Katiba kutoa mawazo yake, nayaheshimu sana. Nimekuwa nikijiuliza sisi Watanzania tunaotoka Zanzibar hatudhani kwamba, wakati umefika kufungua ukurasa mpya! Hatudhani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka mingi kila baada ya kumalizika uchaguzi tangu mwaka 1995 tunaingia kwenye mifarakano ya kisiasa, watu wengi sana pamoja na mimi, tulifikiri matatizo ya Zanzibar ni ya kisiasa na kwa msingi huo yanaweza kumalizwa kisiasa! Ndiyo maana watu wanaoipenda Zanzibar na marafiki wa Zanzibar walipendekeza kwamba, vyama viwili vikuu, Chama cha Mapinduzi na CUF, wafikirie tena juu ya mfumo wao wa uchaguzi. Walisema huenda tofauti hizi zinazoonekana na mfumo wa mshindi wa uchaguzi kuchukua kila kitu pengine ndiyo sababu ya mfarakano! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana mwaka 2010 ushauri huo ulikubaliwa, vyama vyetu vilishirikiana kufanya marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar na tukaunda Serikali ya pamoja, Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Kwa bahati mbaya tulifikiria sasa ulifika wakati matatizo haya na mifarakano hii itakuwa imekwisha kwa sababu vyama vikuu viwili vyenye nguvu zinazokaribiana vitafungua ukurasa mpya kwa sababu wanafanya kazi katika Serikali ya pamoja. Kwa bahati mbaya sana jambo hilo halikusaidia sana, tumerudi kulekule tulikotoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nina mapendekezo na namwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu anisikilize vizuri, nina ushauri. Kwa kuwa, suluhu ya Zanzibar haikupatikana au haijapatikana katika misingi ya kisiasa, basi Viongozi, tukiwemo Viongozi wa Zanzibar na Viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, tufikirie mambo mengine, ni yepi hayo! Tumejaribu kwenye siasa hatujafanikiwa vizuri! Naamini uchache wa rasilimali na hali ya uchumi ya Zanzibar inachangia sana kwa kiasi kikubwa hali hii ya mitafaruku isiyokwisha Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitasema jambo moja mtashangaa! Bajeti ya Zanzibar ya mwaka uliopita 2015, ilikuwa takribani bilioni 840 hivi, hata hizo zilizopangwa zilipangwa tu kwenye bajeti. Inawezekana utekelezaji wake umetekelezwa kati ya asilimia 60 mpaka asilimia 70. Sasa mnapokuwa na uchache wa rasilimali na mnapokuwa na siasa za mvutano kama tulizonazo Zanzibar, wanasiasa mara nyingi, wanadhani madaraka ya kisiasa ndiyo yanaweza kuamua kila kitu! Kwa maana hiyo, tunadhani sasa mipango yetu ya kupunguza umaskini yote itamalizwa ukiingia Serikalini, kwa maana hiyo, uchaguzi wetu unakuwa mgumu sana kwa sababu, kila mmoja anakimbilia Serikalini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndipo dhima ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano inapotakiwa ianzie. Uchumi mkubwa ni lazima uchukue dhima usaidie uchumi ulio dhaifu. Nimekuwa Waziri Kiongozi kwa takribani miaka 10 na nimebahatika kufanya kazi kwenye Serikali ya Muungano miaka mitatu, tumezungumza kwa muda mrefu suala la kugawana mapato kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Ndugu zangu wale tunaoipenda Tanzania na tunaoipenda Zanzibar tufikie mwisho, tulimalize suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, amani ya Tanzania inategemea sana mustakabali wa uchumi wa Zanzibar. Tunaweza kusema hapa, umuhimu wa historia, tuwafundishe vijana umuhimu wa historia, lakini vijana wa leo kwa bahati mbaya sana wanaishi na kuona kile kinachofanyika leo! Naomba sana tujitahidi na Bunge hili lazima litoe uongozi kwenye jambo hili, kadri tunavyoendelea kuchelewa kulifanyia kazi jambo hili, tunaongeza watu wasioutakia mema Muungano bila sababu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuwa kwenye Bunge la Katiba tulizungumza jambo hili na tukapendekeza lifanyiwe kazi. Kwa bahati mbaya sana utaratibu na mchakato wa Katiba iliyopendekezwa hatujui lini Katiba ile itapitishwa! Ushauri wangu…
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa SADC na kuendesha vyema Mkutano wa 39 wa Jumuiya hiyo
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono Azimio la Bunge la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwenyekiti wa SADC. Nina sababu tatu za kuunga mkono Azimio lililoko mbele yetu. Kwanza Azimio hili linatukumbusha historia ya ukombozi Kusini mwa Bara la Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mtakumbuka mwaka 1960 mpaka 1980 Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere aliwaongoza viongozi wenzake kuunda Umoja wa Nchi zilizo mstari wa mbele kwa ukombozi Kusini mwa Afrika na hatimaye kuundwa kwa Jumuiya ya SADC. Viongozi hao ni Agostinho Neto wa Angola, Marehemu Khama wa Botswana, Keneth Kaunda wa Zambia, Samora Machel wa Msumbiji na Mzee Robert Mugabe wa Zimbabwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Baba wa Taifa aliitumia ardhi ya Tanzania rasilimali alizotujalia Mwenyezi Mungu katika kuendeleza mapambano ya kudai uhuru Kusini mwa Afrika. Pamoja na umasikini wa Tanzania Baba wa Taifa alijitahidi na kutoa mchango mkumbwa sana, lakini kwa bahati mbaya wako baadhi ya watu wanadhani kwamba mchango alioutoa Baba wa Taifa katika kupigania uhuru haulingani na hadhi anayopewa Baba wa Taifa katika baadhi ya nchi Wanachama. Ni matarajio yangu kwamba kufanyika kwa mkutano huu katika ardhi aliyozaliwa Baba wa Taifa kutatukumbusha historia iliyo tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili azimio hili linatukumbusha kwamba ajenda ya ukombozi Kusini mwa Afrika na Afrika kwa ujumla bado haijakamilika. Waafrika tusipokuwa makini, siku moja tusishangae, ukoloni mamboleo unaweza kurudi katika Bara la Afrika. Ni wajibu wetu tufanye kila linalowezekana tushirikiane kulinda uhuru huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatu, Azimio hili linasisitiza juu ya umuhimu wa nchi za SADC kuendeleza awamu ya pili ya agenda ya mapinduzi na Uhuru wa Kiuchumi katika Jumuiya hii ya Afrika ya Mashariki. Kwa kuwa harakati za kupigania uhuru katika awamu ya kwanza ziliratibiwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni matarajio kwamba awamu ya pili ya mapambano ya Uhuru wa Kiuchumi yataratibiwa tena hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi kama Wabunge na kama wawakilishi wa Watanzania, ni matarajio yetu kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hataongoza mapambano haya ya ukombozi wa kiuchumi. Nalisema hili kwa sababu ipo dhana na hata Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wakati wa Mkutano alisema wazi kwamba yapo baadhi ya Mataifa wanachama wa SADC yanafanya biashara kubwa zaidi na nchi zilizoko nje ya Jumuiya kuliko zinazofanya ndani ya Jumuiya. Nafikiri jambo hili halikubaliki hata kidogo. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono Azimio la Bunge. (Makofi)
Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuwa mchangiaji wa mwanzo katika Wizara hii, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Mheshimiwa Spika, majeshi ya ulinzi yana mchango mkubwa sana siyo katika kudumisha amani tu na usalama lakini katika kukuza uchumi, maendeleo na ustawi wa nchi. Nchi ambazo zimefanikiwa sana katika kuleta maendeleo ya watu wao wameyatumia vizuri sana majeshi yao ya ulinzi, mfano mzuri nchi kama Marekani, China na India walifanya uamuzi mahsusi wa kujinyima na kuwekeza kwenye masuala ya uzalishaji hasa mashirika ya uzalishaji yanayoongozwa na Jeshi. Matokeo yake basi masuala ya utafiti wa mambo muhimu sana wa mataifa hayo yanayohusiana na uchumi, tiba na elimu yamefanywa na wanajeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, najua Tanzania na hasa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa bajeti wanayopewa ni ndogo sana, lakini kutokana na dhamira aliyoionesha Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tunakumbuka hivi karibuni alisema anatamani sana Jeshi la Ulinzi lifanye kazi zinazohusiana na masuala ya uzalishaji kwa kadri inavyowezekana. Kwa maana hiyo basi, tunaiomba Serikali ili tuweze kutimiza dhamira hiyo ya Mheshimiwa Rais tujinyime, lakini tufanye kila lililo katika uwezo wetu kuwekeza katika jambo hilo.
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Ulinzi wa Tanzania lina uwezo mkubwa sana wa kufanya shughuli ambazo hivi sasa katika nchi yetu zinafanywa na makampuni ya watu binafsi na wakati mwingine makampuni yanayotoka nje ya nchi. Sisi tunajua Jeshi letu la Ulinzi lina uwezo mkubwa sana wa kutengeneza madaraja, kuweka njia kubwa za umeme.
Mheshimiwa Spika, huwa ninasikitika sana ninapoona ziko shughuli ambazo Jeshi la Wananchi wa Tanzania wanaweza kuzifanya vizuri tena kwa weledi mkubwa lakini wanapewa watu binafsi. Wakati mwingine tunafanya jambo la hatari sana kiulinzi na usalama, nitatoa mfano.
Mheshimiwa Spika, niliwahi kutembelea nchi moja lakini sitaitaja Ulaya tukawa tunaangalia na wale wenyeji nikawauliza mbona barabara zenu ziko hivi pana sana, akaniambia hamjui sisi likitokea la kutokea nchi ikiingia kwa mfano kwenye vita barabara hizi zinafungwa na zinageuka kuwa njia za kupitia ndege za kijeshi.
Mheshimiwa Spika, sasa sisemi tunaweza tukafikia huko, lakini inasikitisha utakuta kampuni ya ujenzi kutoka nje inakuja katika nchi yetu inajenga barabara na madaraja Jeshi la Wananchi wa Tanzania halishirikishwi, halijui! Hatari yake kiulinzi na usalama ikitokea hali ya hatari kuna baadhi ya madaraja hata vifaru haviwezi kupita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati mwingine njia hizi za umeme tunawapa kazi makampuni kutoka nje yanaweka njia kubwa za umeme jambo ambalo ni hatari sana, Jeshi la Ulinzi na wataalam wake hawashirikishwi, mimi nasema hili ni jambo la hatari sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ambalo Jeshi wanaweza kutoa mchango mkubwa iwapo watapewa fedha za kutosha. Wanajeshi wetu wapo na tunao wataalam kidogo katika masuala ya teknolojia ya habari na napenda kusema katika dunia ya leo, nafasi ya Jeshi kutumia silaha kubwa kama vifaru kwenda kwenye vita naiona katika karne hii na karne inayokuja inaweza ikapungua sana, lakini karne itakayokuja kuna uwezekano mkubwa sana wa mataifa mbalimbali watatumia cyber katika kuzishambulia nchi wanazotaka kuzishambulia na kwa maana hiyo Jeshi letu lijiandae kwenye eneo hilo. Ndiyo maana nasema Serikali ifanye kila linalowezekana iisaidie Wizara ya Ulinzi kuhakikisha kwamba wataalam wetu wa jeshi wanafunzwa ipasavyo katika masuala ya teknolojia ya habari na cyber kwa ujumla wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, najua tutasema hatuna fedha labda nitoe ushauri kidogo wa namna ya kupata fedha. Najua bajeti hii haitoshi, lakini zipo Wizara ambazo zinaweza kufanya maamuzi ya makusudi kabisa kuunga mkono shughuli ambazo zinafanywa na Jeshi kwa sababu shughuli zao pia zinasaidiwa na Jeshi. Kwa mfano, Wizara ya Biashara na Viwanda washirikiane na Jeshi, Wizara ya Elimu, Sayansi, Ufundi na Teknolojia ishirikiane na Jeshi, isishirikiane tu kwa maneno, hata inapowezekana watoe fedha kulisaidia Jeshi. Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ishirikiane na Wizara ya Ulinzi na kila inapowezekana wanaweza kutoa fedha katika kuunga mkono miradi ambayo inatekelezwa na Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ninalotaka kuchangia ni kwamba kwa muda mrefu vijana wetu wamekuwa wakipewa mafunzo katika Jeshi la Kujenga Taifa, lakini vijana hawa baada ya muda wao wa kujitolea unapomalizika wanarudi kwenye mitaa. Hili ni jambo la hatari. Vijana hawa tayari tumeshawapa mafunzo ya kijeshi na kwa bahati mbaya sana hatuna utaratibu wa kufanya tathmini wanaporudi uraiani vijana hawa wanafanya nini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nadhani sasa wakati umefika kwa Wizara ya Ulinzi kwanza ifanye utafiti na tathmini vijana hawa wanaporudi uraiani wanafanya nini. Lakini la pili Wizara iweke taarifa maalum ya vijana waliopitia Jeshi la Kujenga Taifa ili zikitokea nafasi katika Halmashauri zetu za kazi za ufundi, kazi za vibarua wanaangalia vijana wetu ambao wamepitia kwenye Jeshi la Kujenga Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho, najua tuna ukosefu wa fedha lakini nadhani wakati umefika wa kuviimarisha vyuo vya ufundi vilivyopo katika Jeshi la Kujenga Taifa ili viweze kutoa mafunzo mazuri kwa vijana wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nakushukuru sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa heshima hii ya kutoa mchango wangu. Katika mchango wangu nitazungumzia hoja nne kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa. Mwaka 1966 Waziri Mkuu wa Zamani wa Singapore Lee Kuan Yew alitembelea Ghana na alipokutana na mwenyeji wake alitambulishwa kwa msomi wa Shahada ya Uzamivu katika somo la fasihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili lilimsikitisha sana, lakini hakusema neno mbele ya mwenyeji wake. Aliporudi Singapore alifanya Mkutano na Waandishi wa Habari akasema maneno haya, kama angepata nafasi za kuzishauri nchi za kiafrika, basi angeshauri nchi za kiafrika ziwekeze kikamilifu katika Sekta ya Kilimo, kwa sababu kilimo ndiyo sekta yenye uwezo wa kuondoa umasikini katika Bara la Afrika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno hayo hayo Mwalimu Nyerere Baba wa Taifa aliyarudia tena mwaka 1985 wakati akihutubia Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi, alisema maneno hayo hayo kama Tanzania inataka kujenga Taifa linalojitegemea, basi tuwekeze katika Sekta ya Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya kwanza kilimo kitaendelea kuwa na mchango mkubwa sana katika maendeleo ya Taifa hili kwa miaka mingi ijayo na Sekta hii ina ajiri zaidi ya 70% ya Watanzania. Kwa hiyo, kama tunataka tupunguze umaskini miongoni mwa Watanzania, basi tuwekeze katika Sekta ya Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nieleze tu namna Wizara ya Kilimo inavyotekeleza Miradi yake ya Kilimo ya Maendeleo. Wizara hii inatekeleza Miradi miwili ya kilimo, Mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora na Ujenzi wa Mabwawa 18 ya Kilimo cha Umwagiliaji Maji. Nimezitafuta takwimu ili nione kwa jinsi gani Mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora unavyoweza kutusaidia katika kukuza kilimo, kwa bahati mbaya mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti taarifa hizo sikuzipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Ujenzi wa Mabwawa 18 mpaka sasa katika kipindi cha miaka mitatu Wizara imetekeleza mabwawa matatu yamekamilika na mengine 15 yako katika hatua mbalimbali za ujenzi. Kwa kutumia busara ya kawaida, Wizara ilitakiwa ijenge mabwawa manne kila mwaka badala ya kujenga mabwawa yote kwa wakati mmoja kama wanavyofanya. Kama wangefanya hivyo, leo ninavyozungumza wangekuwa wamejenga mabwawa 12 na mabwawa sita yaliyobaki yangemalizwa mwaka kesho, kwa bahati mbaya hawakufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya pili licha ya Wizara hii kupatiwa wastani wa shilingi trilioni moja kila mwaka kwa ajili ya Maendeleo ya Kilimo, tija katika Uzalishaji wa mazao ya kilimo bado uko chini sana, nitatoa takwimu kuonyesha wenzetu nchi jirani wanavyofanya vizuri kwenye Sekta hii kuliko sisi. Nchi moja ya jirani ina eneo la kumwagilia maji lenye hekta 650,000 wanauza mazao ya kilimo nje ya nchi yenye thamani ya dola bilioni 3.2.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Tanzania tuna eneo la kumwagilia maji lenye ukubwa wa hekta 827,000, tunauza nje mazao yenye thamani ya dola bilioni 2.3, utaona kwa jinsi gani tulivyokua tuko nyuma. Nilitegemea fedha hizi za bajeti zingetumika katika kuwapa wakulima mbegu zilizobora, huduma bora za ugani, utafiti wenye matokeo sahihi kwa wakulima lakini nalo hili naona halikufanyika kwa usahihi. (MakofI)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya tatu ni kwamba, njia muafaka ya kuongeza tija katika uzalishaji iwe katika Sekta ya Kilimo au Sekta ya Viwanda ni kuwekeza kwenye elimu bora inayosisitiza juu ya ufundi, ujuzi na ugunduzi. Kwa bahati mbaya elimu yetu bado haikidhi kiwango hicho cha ubora na mara nyingi tunafundisha masomo ya jumla jumla badala ya masomo yanayosisitiza ujuzi, weledi na umahiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatumia wastani wa shilingi bilioni 500 kila mwaka kwa ajili ya Mikopo ya Elimu ya Juu, lakini kama nilivyosema, fedha hizo mchango wake ni mdogo sana katika kukuza uchumi na sababu yake ni hiyo niliyoeleza hapo juu. Tatizo letu ni nini? Tatizo letu tunafundisha masomo ya jumla jumla ambayo hayana uhusiano wa moja kwa moja katika kupunguza umasikini. Ningetarajia tungefundisha masomo kama usimamizi wa mipango, usimamizi wa maendeleo, usimamizi wa rasilimali watu, usimamizi wa viwanda, usimamizi wa sekta ya afya, na mambo ambayo yana uhusiano moja kwa moja na kupunguza umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningetarajia tungefundisha masomo ya ukalimani, ufundishaji wa Kiswahili kama lugha ya kigeni ili tusafirishe watalamu nchi za ughaibuni. Kwa upande wa teknolojia ningetarajia tungewafundisha vijana masuala ya sayansi ya data (data analytic) akili bandia (artificial intelligence), cyber na blockchain. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya nne ni kwamba, baadhi ya matumizi ya Serikali kwa maoni yangu, badala ya kusaidia kuongeza tija, yanaibebesha Serikali mzigo mkubwa sana. Nitatoa mfano. Mfano wa kwanza, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Maliasili, na Wizara ya Maji wananunua mitambo inayofanana na wote wanafanya kazi ya kuchimba mabwawa pamoja na kutengeneza barabara. Baada ya muda mfupi tu vifaa vinaanza kutelekezwa porini kwa sababu gharama za mafuta zimeongezeka sana na gharama za matengenezo zimekua kubwa sana. Badala vifaa hivyo kuwekwa katika sehemu moja na kila anayehitaji akakodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya tano, Chuo Kikuu cha Dodoma kina shule nzima ya teknolojia ya habari. Wakati huo huo Wizara ya Habari na Teknolojia ya Habari inajenga Chuo cha Umahiri wa TEHAMA. Kwangu mimi haya ni matumizi mabaya sana ya fedha. Tatizo letu kama Taifa siyo majengo, tatizo letu ni walimu walio bora, vifaa vilivyo bora, na mazingira bora. Sasa fedha ambazo zinatumika kujenga Chuo kipya zingepelekwa Dodoma ili kutengeneza Chuo cha Umahiri katika hii Jumuiya ya Afrika Mashariki ili vijana wetu wapate mafunzo mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya sita, mfumo wetu wa Vyuo Vikuu ni utaratibu wa kwamba Chuo Kikuu kimoja kinafundisha kila somo na kwa maana hiyo hatusisitizi umahiri na weledi. Kwa maoni yangu, haya ni matumizi mabaya sana ya rasilimali katika Taifa. Ingekuwa vizuri kama Taifa tugawe Vyuo Vikuu kulingana na uchaguzi wa weledi na ubobezi wa masomo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano nashauri Chuo Kikuu cha Dodoma kingefundisha masuala ya sayansi, teknolojia na uvumbuzi; Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kikafundisha masomo ya sayansi ya jamii, Muhimbili kikaendelea kama kilivyo na SUA kikaendelea kama kilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ni kwamba, Wizara ya Elimu ina dhamira ya kufundisha masomo ya ufundi na amali katika shule zote za sekondari sambamba na kuwa na Vyuo vya Technical Tanzania nzima, nia ni nzuri, dhamira ni nzuri lakini uwezo haupo wa kutekeleza jambo hilo kubwa. Kwa maoni yangu, badala ya shule zote za sekondari kufundisha masomo haya, ningependekeza tukawekeza kwenye Ujenzi wa Vyuo vya Kisasa vya Ufundi katika kila Kanda. Kwa mfano, Kanda ya Kusini, Kaskazini, Mashariki, Magharibi, Kanda ya Kati, Kusini Juu pamoja na Kanda ya Ziwa na Vyuo hivi vipewe walimu walio mahairi katika ufundishaji na vifaa vya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo langu lingine, masomo yatakayofundishwa katika Vyuo hivyo, yawe ni masomo yanayoendana na shughuli kuu za uchumi wa Tanzania kama kilimo, ufugaji, madini, gesi asilia, ujenzi wa miundombinu na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni kwamba, nchi yetu kama nilivyosema awali ni nchi ya kilimo. Sasa nchi ambayo inategemea sana Sekta ya Kilimo kuleta maendeleo, ingefanya uamuzi wa kimapinduzi wa kuzalisha mbolea yake ya ndani badala ya kuagiza nje. Bahati nzuri tunayo gesi asilia, tunayo samadi, tungechanganya pamoja samadi na gesi asilia tungeweza kutengeneza mbolea badala ya kutumia zaidi ya shilingi bilioni 300 kuagiza mbolea kutoka nje. Jambo hili halifurahishi hata kidogo na wala siyo heshima kwa Taifa huru kama Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mambo ya Nje ina mchango mkubwa sana katika kukuza uchumi, ustawi na maendeleo ya Taifa letu. Wizara hii ina wajibu mkubwa sana wa kutafuta wawekezaji walio makini, kutafuta wataalam na kujenga mahusiano kati ya nchi yetu na Mataifa ya nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalizungumza jambo hili kwa sababu kama kuna tishio kubwa la usalama wa Taifa letu na usalama wa Mataifa basi umaskini duniani ndiyo tatizo kubwa sana. Kwa hiyo, tunaitarajia Wizara ya Mambo ya Nje itekeleze wajibu huo kwa weledi ili nchi yetu iweze kupata matarajio hayo tunayoyatarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mambo ya Nje imejitahidi kuwaunganisha na kuwashajihisha Watanzania wanaoishi nchi za nje kuwekeza ndani ya nchi yetu, kuleta utaalam na kutoa ushauri katika mambo ya kitaalam.
Kwa bahati mbaya kidogo, mchango wa Watanzania hao walioutoa si mkubwa wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri hapa na ametueleza mchango ambao Watanzania walio nje waliutoa kwa nchi yetu ni takribani shilingi za Tanzania bilioni 36. Fedha hizi kwa maoni yangu ni kidogo sana ukilinganisha na wenzetu. Labda nitoe mfano wa wenzetu wa Kenya, mchango wa Wakenya wanaoishi nje ya nchi yao ni takribani dola bilioni moja. Kwa mnasaba huo basi nasema tunayo kazi ya ziada ya kuifanya ili kuwashajiisha Watanzania hawa waweze kutoa mchango mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa katika Bunge hili katika Bunge lililopita, moja ya malalamiko makubwa sana ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyaeleza ni mikataba yetu mingi ambayo tunaingia si mizuri. Kwa utafiti usio wa kina sana inaelekea utaalamu wetu katika kuingia makubaliano ya mikataba si wa kiwango cha juu sana. Kwa hiyo, naishauri Wizara ya Mambo ya Nje ifanye kila linalowezekana kukisaidia Chuo chetu cha Diplomasia ili kiweze kutoa mafunzo mazuri ya international negotiation. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikifuatilia mara nyingi utendaji wa Mashirika ya Kimataifa, najua Waheshimiwa Mabalozi wamefanya kazi nzuri sana nje ya nchi huko, lakini kama tutafanya ulinganisho wa mchango ambao Watanzania tumeutoa katika Mashirika ya Kimataifa, ukilinganisha na nchi kama Ghana, Senegal na Kenya, wataalam wanaofanya kazi katika mashirika hayo Watanzania ni wachache sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya, ukiwa huna wana diplomasia wa kutosha kwenye mashirika hayo, itakuwa vigumu sana kuweza kuwavutia watu wengine ndani ya nchi hata nafasi hizo zikitoka Watanzania wanakuwa hawapati taarifa za kutosha. Kwa hiyo, naishauri Wizara ifanye kila linalowezekana, kwanza tuwape Watanzania mafunzo ya kutosha lakini tuhakikishe kwamba Watanzania wengi zaidi wanafanya kazi katika Mashirika ya Kimataifa ili wawe chachu na wafungue milango kwa Watanzania wengine ambao wangependa kupata fursa hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, kwa bahati nzuri mimi ni miongoni mwa wanafunzi ambao walipitia Chuo cha Kidiplomasia na Mheshimiwa Shahari ni miongoni mwa Walimu ambao walitufundisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana inaonekana kama Chuo cha Diplomasia pamoja na mchango wake katika kuandaa Mabalozi na Maafisa wa Ushirikiano wa Kimataifa, Serikali haikiendelezi kiasi cha kutosha. Serikali na Wizara ya Mambo ya Nje imekuwa ikishauriwa kwa miaka mingi kukiimarisha Chuo cha Diplomasia kwa kukipatia vifaa na wataalam lakini pia kukipatia eneo ambapo chuo hiki kinaweza kikatanuliwa ili kiweze kutoa fursa nyingi zaidi. Kwa bahati mbaya takriban miaka kumi na tano eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya chuo hicho bado halijaendelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara ya Mambo ya Nje ikiunganishe Chuo cha Kidiplomasia na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili kunyanyua hadhi yake. Kama ilivyo Taasisi ya Diplomasia na Ushirikiano wa Kimataifa Nairobi ilivyounganishwa na Chuo Kikuu cha Nairobi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, naomba kuunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza mchango wangu kwa kunukuu maneno ya Biblia takatifu; “watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Taifa tunapoangalia matatizo yanayotukabili ama yasababishwa na kiwango cha chini, ama yanasababishwa na ukoesefu wa maarifa, hasa ya sayansi na teknolojia. Tangu tupate uhuru mpaka sasa tunapoangalia mipango yetu ya maendeleo bado dhamira ya mipango yetu haijabadilika sana, lengo letu ni kupambana na umasikini na kukuza uchumi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo baadhi ya watu wanajiuliza mbona tumechukua muda mrefu sana kukabiliana na matatizo ya umaskini? jibu nitalitoa baada ya kunukuu maneno ya Abraham Lincoln, mmoja wa Marais wa Marekani, alisema maneno ha yana ninaomba tuyatafakari. Alisema, nikipewa kazi ya kukata mti na nimepewa saa sita, saa nne za kwanza nitazitumia kwa kunoa shoka na saa mbili za mwisho ndiyo nitaanza kati ya kukata mti; sasa tatizo letu la msingi lipo hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Taifa tunaujua ukweli huu, lakini bado tunashindwa kuutekeleza kwa vitendo. Kwa maoni yangu, ninapoangalia mpango sioni waziwazi kama elimu ndicho kipaumbele chetu namba moja. Watu wenye maarifa ya kutosha na sahihi wana uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo makubwa katika Taifa lao. Wanaweza kulibadilisha jangwa kuwa ardhi ya kilimo, nitatoa mfano. Hakuna jambo linalonisikitisha sana kama kiongozi na kama Mtanzania ninapoona nchi ya Misri ambayo asilimia 60 ya nchi yake ni jangwa, wamejifunza sayansi na uhandisi wa kutumia maji ya kilimo cha umwagiliaji maji zaidi ya miaka 1,000. Watanzania tuna mito, tuna maziwa, tunashindwa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Marehemu Baba wa Taifa alitambua sana umuhimu wa elimu hasa ya ufundi, ndiyo maana alitujengea vyuo vingi sana vya kati vya elimu ya ufundi, lakini kwa bahati mbaya sana viongozi tuliokuja baadaye tulivibadilisha vyuo hivi na kuwa vyuo vikuu. Kama kuna kosa la kiufundi tumelifanya basi ni jambo hili. Ushauri wangu ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, naiomba Wizara ya elimu kama kweli tuna lengo la kupambana na umasikini tuwekeze fedha za kutosha, angalau asilimia 20 ya bajeti kwa ajili ya ufundishaji vijana wetu, hasa masomo ya sayansi na teknolojia, ili kukuza uwezo wa vijana wetu wa kufikiri, wa kubuni, wa kutatua matatizo na kutafuta mbinu na vifaa vya kutatua matatizo yetu. Na kama tunatoa elimu ambayo haina uwezo wa kuwasaidia vijana kufikiri, basi tunapaswa kufikiri upya. Na kama tunadhani elimu ni ghali basi naomba tuujaribu ujinga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwanza napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimefarijika sana kutokana na mambo mawili. Kwanza, mwaka 2008 nilipokuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali katika Baraza la Wawakilishi, Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, lilipitisha Azimio la mapendekezo ya kuondolewa suala la mafuta na gesi katika orodha ya Muungano. Azimio hili, liliungwa mkono na Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi. Wawakilishi, kutoka Chama cha Mapinduzi waliunga mkono na wawakilishi kutoka Chama cha CUF waliunga mkono Azimio hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa Oktoba, 2015, suala la mafuta na gesi lilikuwa ni ajenda muhimu sana katika uchaguzi huo. Chama cha CUF kililitumia suala hilo katika kuombea kura na Chama cha Mapinduzi kikafanya hivyo kule Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka mingi Wazanzibari tumekuwa tukiiomba Serikali ya Muungano itafute njia ya uchumi itakayoisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupata fedha za kutosha kwa ajili ya kushughulikia masuala ya kupunguza umaskini na kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar. Kutokana na umuhimu wa sekta hii, kwa uchumi na maendeleo ya Zanzibar, Serikali ya Muungano sasa imeridhia suala la mafuta na gesi kuondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Muungano imefanya busara ya hali ya juu sana, naipongeza sana. Jambo hili lina maslahi makubwa sana kwa Zanzibar na kwa Muungano, lakini inanisikitisha sana wapo miongoni mwetu ambao tumekuwa tukipigania jambo hili litolewe kwenye orodha ya Muungano ili Zanzibar iweze kutafuta mafuta na gesi kwa maslahi ya Zanzibar, sasa hivi tunaanza kuwa na kiguu cha nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaanza nasikia baadhi yetu wanasema oooh, suala hili limefanywa kinyume na misingi ya Katiba na hao tunaosema haya ni kule upande wa Zanzibar ambao tungepaswa jambo hili tuliunge mkono. Naiomba sana Serikali ya Muungano wa Tanzania tusivunjwe moyo na jambo hili, tuendelee mbele jambo hili lina maslahi makubwa sana kwa uchumi wa Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nilipokuwa nikichangia bajeti ya Wizara hii hii mwaka jana, nilisema kuna haja ya uchumi mkubwa kusaidia uchumi mdogo. Mwaka huu, napenda niseme nimefarijika sana kwa kumsikia Waziri Mheshimiwa Makamba akitupa taarifa hapa kwamba kuna mradi maalum unaosimamia uvuvi wa ukanda wa Pwani ya Magharibi ya bahari ya Hindi. Mradi huu bila shaka una umuhimu mkubwa sana kwa uchumi wa Zanzibar. Kama tunavyojua Zanzibar inategemea sana uvuvi na kwa maana hiyo ikiwa asilimia 50 ya wananchi wa Zanzibar wanategemea uvuvi, bila shaka mradi huu utatoa mchango mkubwa sana. Tumeambiwa hapa kiasi cha milioni mia nne sabini na sita, zimepelekwa Zanzibar ili kusaidia wavuvi wadogowadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, namwomba Mheshimiwa Waziri kwa kupitia mradi huu, mradi wa usimamizi wa Ukanda wa Kusini Magharibi mwa Bara Hindi, ni vizuri ukaanzisha mradi maalum au mfuko maalum wa kusaidia wavuvi wadogowadogo. Nalisema hili kwa sababu fedha ambazo hivi sasa zinatolewa si haba, lakini si nyingi sana, kwa maana hiyo naomba Wizara hii, ama mradi huu unaweza kuwekwa chini ya mradi wa Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu, ama unaweza kuwekwa chini ya usimamizi wa mradi huu nilioueleza. Mheshimiwa Waziri uamuzi ni wenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ninayoieleza hapa ni kwamba, kuna haja ya kupata fedha za kutosha kwa ajili ya kuwasaidia wavuvi wadogowadogo pia kwa ajili ya kuimarisha mazingira ya baharini. Kama unavyojua, kipindi kilichopita kiasi cha miaka miwili, mitatu hivi iliyopita, tulikuwa na mradi wa kuwasaidia wavuvi wadogowadogo pamoja na …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. SHAMSHI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutamka rasmi kwamba naunga mkono hoja.
The Finance Bill, 2022
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Spika, nchi yetu imebarikiwa na Mwenyezi Mungu kuwa na vivutio vingi sana vya utalii lakini kwa bahati mbaya idadi ya watalii wanaotembelea nchi yetu na kiwango cha mapato tunachokikusanya katika sekta hiyo hakilingani hata kidogo na uzuri wa nchi yetu. Zipo nchi tunazopatakana nazo zinavivutio vichache sana vya utalii lakini idadi ya watalii wanaotembelea nchi hizo na kiwango cha mapato wanachokikusanya ni kikubwa kuliko sisi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano wa karibu tu. Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inapata watalii 500,000 kwa mwaka, wakati sisi Tanzania Bara tunapata idadi ya watalii 800,000. Zanzibar inavivutio viwili tu vya utalii; magofu ya kihistoria na fukwe, lakini kwa maoni yangu hata Tanzania Bara vivutio hivyo vipo, magofu ya kihistoria yapo, fukwe mwanana zipo; Lindi, Mtwara na Mkoa wa Pwani; mbuga za wanyama. Sasa nahisi kuna tatizo mahali fulani. Ama takwimu za idadi ya watalii wanaotembelea nchi yetu hazikusanywi kwa usahihi, ama huduma zetu za utalii hazijafikia kiwango cha kuridhisha, ama huduma zetu za utalii ni ghali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napendekeza mambo yafuatayo ili kukabiliana na hali hiyo. La kwanza, Serikali iwaagize mabalozi wetu watupatie taarifa za hatua za kukuza utalii zinazofanywa katika nchi wanazofanyia kazi ili tujifunze yale mazuri wenzetu wanayofanya. Ushauri wa pili, Serikali iweke mifumo imara ya TEHAMA itakayoweza kukusanya taarifa sahihi za watalii na mapato ya Sekta ya Utalii na mifumo hiyo iunganishwe moja kwa moja na Wizara ya Fedha ili Wizara ya Fedha waweze kuiangalia. La tatu, Serikali iimarishe Chuo chetu cha Utalii ili kiweze kutoa huduma bora na zinazofikia kiwango cha Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna nchi moja jirani yetu wana chuo maarufu sana kinachoitwa Utalii College. Chuo hiki kimekuwa kikitoa wanafunzi wenye uweledi wa hali ya juu sana katika huduma ya utalii. Kwa maoni yangu, nadhani siyo vibaya tukajifunza mambo mema kutoka kwa majirani zetu. Tukitembelee chuo hicho ili tuone mambo waliyofanya vizuri na sisi tuyafuate ili tuweze kuimarisha chuo hiki.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza, napenda kusema naunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimefanya utafiti wa muda mrefu hivi na nikafanya utafiti wa viongozi wa tatu wa Asia na nikabaini viongozi hawa kuna mambo manne makubwa wameyafanya katika nchi zao halafu baadaye nitalinganisha na kile ambacho kwa mawazo yangu nakiona kinafanyika katika nchi yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Viongozi wenyewe ni marehemu Lee Kuan Yew wa Singapore; wa pili ni Mahathir Mohamed wa Malaysia sasa hivi ana awamu pili lakini nitazungumzia awamu ya kwanza; na kiongozi wa tatu anaitwa Deng Xiaoping aliyekuwa Rais wa Taifa la China kuanzia mwaka wa 1978.
Mheshimiwa Spika, yapo mambo manne wameyafanya, la kwanza, hawa viongozi wote niliowataja watatu ni viongozi ambao wana maono na mipango ya muda mrefu. Pili, sifa yao kubwa ni viongozi wa matendo, wanachokisema ndicho wanachokitenda. Tatu, wanapoteua viongozi na watendaji wanateua wenye uweledi, maarifa, ujuzi, na uzoefu. Jambo la nne ambalo walilifanya viongozi hao ni kuwekeza kwenye sayansi na teknolojia.
Mheshimiwa Spika, nikija hapa kwenye nchi yetu kwa nachokiona kwa mawazo yangu kile anachokifanya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinafanana sana kwa asilimia mia moja na hiki ambacho kinafanywa na viongozi hawa watatu niliowataja. Kwa maana hiyo basi Taifa letu la Tanzania katika kipindi cha miaka mitano na miaka kumi inayokuja Tanzania itakuwa miongoni mwa mataifa yenye ustawi mkubwa sana wa maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, moja ya hotuba za Rais Magufuli aliwahi kutuambia kwamba anasikitishwa sana kuona Tanzania bado inaendelea kuwa Taifa ambalo linatembeza bakuli na Taifa ambalo yeye anaamini lina uwezo sana wa kuwa Taifa linalotoa misaada. Mimi bila shaka nakubaliana naye kwamba Tanzania ina uwezo mkubwa sana tukifanya kazi kwa bidii na chini ya uongozi wake bila shaka katika kipindi kijacho si kirefu sana Tanzania itaweza kufikia katika ndoto hiyo. Hata kama hatukufikia Taifa ambalo linaweza likatoa misaada lakini bila shaka ni Taifa ambalo tutaweza kujitosheleza kwa asilimia mia moja kwa bajeti yetu, ninaamini hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nirudi kwenye yale mambo manne niliyoyaeleza pale mwanzo. La kwanza, Rais wetu Magufuli ni mtu ambaye ana maono, ana mipango ya muda mrefu ya kuliendeleza Taifa hili. Kama kuna jambo ambalo linawafanya Waafrika wadharauliwe duniani, Wazungu wanasema Waafrika kwa kawaida yao wakipanga mipango yao wanapanga mipango ya muda mfupi, pengine miaka miwili na wamekwenda mbali sana miaka mitano lakini tunachokiona Tanzania sasa hivi, tuna mradi huu wa reli ya kisasa ni mradi ambao ukikamilika utadumu kwa takribani miaka mia moja mpaka mia moja na hamsini kama tutaitunza vizuri. Bila shaka inatuonyesha dhahiri kwamba huyu ni kiongozi ambaye ana maono ya muda mrefu. Mradi mwingine ni mradi wa umeme wa Bonde la Mto Rufiji. Mradi huu utakapomalizika bila shaka tukiutunza vizuri utadumu kati ya miaka hamsini mpaka sabini. Kwa hiyo, tunaona bila shaka ni kiongozi wa namna gani, ni kiongozi ambaye ana maono na mipango ya muda mrefu. (Makofi)
Kwa hiyo, tunaona bila shaka ni kiongozi wa namna gani. Ni kiongozi ambaye ana maono na mipango ya muda mrefu. La pili, nimewahi kusikia mahali watu wakilala wanasema ah, Rais Magufuli bwana, anateua Maprofesa, Madaktari; sasa najiuliza, tulitegemea amteue nani? Kiongozi aliye makini, ana ajenda na anajua kwamba kipindi chake cha Urais ni miaka 10, bila shaka unapaswa kuteua watu unaoamini wana uwezo, weledi na maarifa ili wakusaidie kuikamilisha hiyo kazi katika kipindi kifupi. Maana yake miaka 10 katika uhai wa binadamu ni muda mchache sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sina maana kwamba watu wasio na Shahada za Udaktari wa Maprofesa hawana uwezo, la hasha! Sina maana hiyo. Wapo baadhi ya watu elimu yao ni ndogo sana Mwenyezi Mungu kawajaalia kuwa na uwezo huo na maarifa, bila shaka wakipewa nafasi hizo sina matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la tatu ambalo nataka kulisema ni la Sayansi na Teknolojia. Bila shaka Rais Magufuli amejitahidi sana katika Sekta ya Afya. Tumewekeza sana katika sekta hii ya tiba. Ni mategemeo yangu kwamba katika Sekta ya Kilimo, kile ambacho tunakiona kinafanyika katika Sekta ya Afya, ningetamani sana nikione kinafanyika katika Sekta ya Kilimo kwa sababu mapinduzi ya kweli ya Taifa la Tanzania linategemea sana katika Sekta hii ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, najua Serikali inao Mpango wake wa Maendeleo wa Awamu ya Pili lakini nadhani fedha zilizotengwa siyo haba, lakini kama tunataka kupiga hatua kubwa sana ya maendeleo na hasa kutimiza ndoto yetu ya Tanzania ya Viwanda; na ikiwa kilimo ni sehemu kubwa sana ya maendeleo ya viwanda, naiomba sana Serikali yangu Tukufu ifanye kila linalowezekana tuwekeze sana katika Sekta hii ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka 1966 aliyekuwa Waziri Mkuu wa Malaysia aliwahi kusema maneno haya; aliwahi kutembelea Nigeria na Ghana mwaka huo, akasema kwa kile alichokiona Afrika, angepata nafasi ya kuwa mshauri, wa Marais wa Afrika, angewashauri wawekeze kwenye Sekta ya Kilimo. Kwa sababu kilimo ni viwanda na viwanda ni kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukiwekeza kwenye kilimo, tutapata asilimia 100 ya mahitaji yote tunayohitaji ya kwenye viwanda, tutajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 100. Wanasema katika kipindi cha miaka 10 na 20 inayokuja, dunia itakuwa na upungufu mkubwa sana wa chakula. Bila shaka tukiwekeza kwenye kilimo, Tanzania itakuwa ni Taifa la kupigiwa mfano sana. Naishauri sana Serikali yangu Tukufu na Waziri wa Fedha ananisikia, tujinyime tufanye kila linalowezekana hatutakosa kitu tukiwekeza kwenye kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nirudie tu, nasema kwa kile ninachokiona kinafanywa na Rais Dkt. Magufuli, Tanzania inaweza kuwa moja ya Mataifa ya kupigiwa mfano, siyo katika Bara la Afrika, lakini katika Dunia kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme mambo manne la kwanza, nimewasikia baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanasema bajeti ya mwaka huu imeweka mkazo mkubwa zaidi kwenye maendeleo ya vitu badala ya maendeleo ya watu. Mimi naomba nitofautiane na hoja hii na nitatoa sababu zifuatazo; kwanza historia inatuonesha kwamba nchi zote zilizofanikiwa kiuchumi zimewekeza kwenye miundombinu ya msingi hasa umeme na reli. Uingereza wamefanya hivyo, Marekani wamefanya hivyo na sasa Bara la Asia linafanya hivyo. Kwa hiyo Tanzania haijafanya kitu tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge waliokuwepo Bunge lililopita watakumbuka tulilalamika sana hapa kwamba Tanzania inashindwa kuitumia Bandari ya Dar es Salaam na kuifungamanisha na reli na ikaweza kuitumia soko kubwa la nchi zinazotuzunguka na tukafika mbali tukasema yuko kiongozi mmoja simtaji wa nchi moja ya Afrika Mashariki alinukuliwa akisema akipewa Bandari ya Dar es Salaam ataiendesha Bara zima la Afrika. Sasa maneno huumba, tulisema tunamhitaji kiongozi mwenye ujasiri, atakayefanya maamuzi magumu. Tumepata kiongozi tuliyemuomba, anafanya tuliyoyataka, halafu sasa tunafikiri tofauti. Inanikumbusha ule usemi wa watu wa Rufiji; zilongwa mbali zitengwa mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunatarajia na tunategemea Serikali iitumie Bandari ya Dar es Salaam kusafirisha mizigo mizito kuipeleka nchi zinazotuzunguka. Sasa tumeshafanya uamuzi huo kujenga reli tunawezaje kusafirisha mizigo mizito bila kutumia reli. Dunia nzima wataalam wanasema wazi kwamba usafiri ulio rahisi zaidi duniani kusafirisha mizigo mizito hakuna usafiri wowote kuliko reli. Sasa wanaodhani uamuzi wa kuwekeza kwenye reli na uamuzi wa kuwekeza kwenye umeme wa kutosha kutoka Bonde Rufiji si uamuzi wa busara mimi nawaomba tu wafikirie zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili mapinduzi ya kilimo duniani na Mapinduzi ya viwanda Ulaya, Marekani na katika siku za karibuni Asia yamewezekana kwa sababu ya uwekezaji mkubwa sana katika sekta ya umeme na reli. Iko hoja na hapa imesemwa kwamba wako ambao wanaona kwamba kwa nini hatuwekezi kwanza kwenye elimu, afya na maji. Mimi ninachosema kupanga ni kuchagua na hii hoja tunayoileta hapa ni sawa na wale wanaouliza ni lipi linaanza mwanzo kati ya kuku na yai, unaweza kusema ameanza kuku au ameanza yai, sasa ni lazima upate mwanzo sasa elimu ni muhimu, afya ni muhimu lakini nasema lazima tuwe na jambo la kuanza na kwa bahati mbaya hatuna uchumi uliokuwa mkubwa wa kutosheleza kufanya kila jambo kwa wakati mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa lazima tuamue sasa Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kuanza na umeme, reli na kilimo nitaeleza baadae. Nadhani hapa hoja ya msingi ingekuwa kwa nini Serikali haiwekezi kiasi cha kutosha katika sekta ambayo ina uwezo wa kuwatoa watu wengi kwa wakati mmoja katika umaskini, na sekta hiyo basi ingekuwa ni kilimo. Wataalam wanasema wataalam wa uchumi sekta ambayo ina uwezo wa kuwatoa watu zaidi ya asilimia 50 katika umaskini ni sekta ya kilimo, kwa munasaba huo naishauri Serikali ifanye kila linalowezekana iwekeze kwenye sekta ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mtakumbuka nchi yetu hivi karibuni tumesaini mkataba wa eneo huru la uchumi katika Bara la Afrika, sasa kama kuna sekta ambayo inaweza kutusaidia sisi kama Taifa kunufaika na mkataba huu sioni kama kuna sekta zaidi kuliko sekta ya kilimo. Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba ifikapo mwaka 2021 Bara la Afrika litakuwa na watu wapatao bilioni 1.3 kwa maana hiyo kutakuwa na mahitaji makubwa sana ya kilimo. Kwa hiyo, Serikali yetu ikiwekeza kwenye kilimo tutaweza kunufaika tutatengeneza kwanza tutajitosheleza kwa chakula, pili tutapata malighafi kwa ajili ya viwanda na hatimaye nchi yetu itapata fedha nyingi zaidi na kuwekeza kwenye huduma mbalimbali za kijamii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho naomba nitoe ushauri kwa Serikali; hivi karibuni Israel imetoa nia ya kuisaidia nchi yetu kuipatia nafasi za masomo katika sekta ya kilimo zipatazo 100; lakini kwa bahati mbaya sana mpaka sasa tunapopzungumza bado nchi yetu haijatumia fursa hiyo vizuri.
Naiomba Serikali yetu tukufu ifanye kila linalowezekana tuwapeleke vijana wetu wakajifunze mbinu bora za kilimo na hasa kilimo cha umwagiliaji. Nchi ya Israel ni moja ya nchi ambazo zinafanya vizuri sana katika sekta ya kilimo. Lakini ushauri wa pili vijana hawa 100 tutakaowapeleka kila mwaka katika nchi ya Israel watakaporudi tuwape ardhi ipatayo hekari kama 10 hivi au 20 na tuwapatie mikopo ili waoneshe kwa vitendo kile walichojifunza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu Misri wanafanya hivyo, vijana wao ambao wanamaliza chuo kikuu hasa vyuo vikuu vya kilimo na mifugo wanapomaliza masomo wanapatiwa ardhi, wanapatiwa fedha katika kipindi cha miaka miwili au mitatu, wazalishe, wakishazalisha wanategemewa katika kipindi cha miaka miwili au mitatu warudishe mkopo na tukilifanya hicho jambo hilo katika kipindi cha miaka mitano mpaka 10 bila shaka sekta ya kilimo itapiga hatua kubwa sana za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Spika, naomba niseme mambo matatu.
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anaendelea kuiongoza nchi yetu kwa hekima na busara ya hali ya juu sana, hivi karibuni Rais Samia aliamua fedha za mkopo wa UVIKO-19 zijadiliwe na kupangiwa matumizi yake katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, jambo hili limetupa sisi kama Wabunge heshima na hadhi tunayostahili, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, vilevile Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha dhamira ya dhati ya kutekeleza kwa kitendo miradi ambayo iliasisiwa na mtangulizi wake marehemu Mheshimiwa John Pombe Magufuli. Mradi wa bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere, Mradi wa Reli ya Kisasa, na ujenzi wa daraja la Busisi unaendelea kupatiwa fedha na inatekelezwa vizuri sana.
Mheshimiwa Spika, hali kadhalika Mheshimiwa Rais anaendelea kuzungumza na Viongozi wa Vyama vya Siasa ili kuzungumzia mustakabali wa Taifa letu na kuzungumzia maendeleo ya demokrasia, jambo hili ni muhimu sana katika kuleta umoja, maelewano na amani katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapana shaka tunahitaji sana maridhiano na kama Biblia Takatifu inavyosema ni ‘heri wapatanishi maana hao wataitwa wana wa Mungu’. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili mwaka 1962 aliyekuwa Waziri Mkuu wa Singapore Lee Kuan Yew aliwahi kutembelea nchi ya Nigeria na Ghana na katika kitabu chake cha kutoka nchi maskini kwenda nchi tajiri alisema, aliona mambo ya kushangaza Nigeria na Ghana na aliporudi nyumbani kwao Singapore alifanya mkutano na Waandishi wa Habari na akasema maneno haya, ningepewa nafasi ya kuzishauri nchi za Bara la Afrika nini kifanye ili watokomeze umaskini basi ningewashauri mambo mawili: -
Kwanza, waimarishe kilimo kwa sababu wanazo fursa kubwa sana za kilimo, wanayo mito, wanayo maziwa, wanayo ardhi, wanayo hali ya hewa nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, ningewashauri waimarishe utalii kwa sababu wanavyo vivutio vingi vya utalii. Ninachokiona sasa kinafanywa na Rais Samia Suluhu Hassan hapana shaka inadhihirisha anatekeleza mawazo na fikra hiyo iliyoelezwa na Ndugu Lee Kuan Yew. Hivi karibuni Serikali yetu Tukufu imeonesha dhamira ya dhati ya kutaka kuwekeza kwenye Kilimo na hasa kilimo cha umwagiliaji. Jambo hili ni jambo ambalo linanipa faraja sana kwa sababu nimekuwepo kwenye Bunge hili kwa takribani vipindi vitatu, zimekuwepo kelele za Waheshimiwa Wabunge kuitaka Serikali yetu Tukufu iwekeze kiasi cha kutosha katika kilimo cha umwagiliaji, kile kilio ambacho hakijasikilizwa ipasavyo na kusema kweli jambo hili limekuja katika wakati muafaka sana.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa nchi yetu ina eneo lipatalo takribani hekta Milioni 22 linalofaa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji maji, lakini kwa bahati mbaya sana mpaka sasa tumewekeza chini ya eneo la ekari 600,000 nadhani hazifiki 600,000. Kwa hiyo, ninaipongeza sana Serikali kwa mawazo hayo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na wazo hilo la kuwekeza sana kwenye kilimo cha Umwagiliaji, ipo haya ya kuwekeza kwenye vyuo vya utafiti wa kilimo ili tuwapatie vijana wetu maarifa na ujuzi, katika masuala ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameonesha dhamira na nia ya kutekeleza wazo la Lee Kuan Yew ni hili hivi karibuni alishiriki katika kipindi kiitwacho Royal Tour, kipindi chenye lengo la kuitangaza nchi yetu nje ya nchi, kwa ajili ya kuvutia watalii, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa hatua hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, mwaka 1978 aliyekuwa kiongozi wa China Ndugu Deng Xiaoping alizungumza na Rais Jimmy Carter wa Marekani na kumuomba aipatie nchi yake nafasi 5,000 za masomo kwa ajili ya vijana wake. Jimmy Carter alilikubali wazo hilo, akamwambia nimekubali wazo hilo lakini badala ya kukupatia nafasi 5,000 nitakupatia nafasi 100,000 na kuanzia hapo nchi ya China imeendelea kupeleka vijana wao nchini Marekani ili kuwapatia vijana wao ujuzi na maarifa.
Mheshimiwa Spika, China hii inayoonekana hivi leo ni matokeo ya uamuzi huo, ninaiomba Serikali yetu Tukufu tufanye kila linalowezekana tuwekeze katika sekta ya elimu hasa kama tunataka kuharakisha maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, Mwanafalsafa mmoja wa zamani wa China aliwahi kusema, ukitaka maendeleo ya muda mfupi panda maua, na ukitaka maendeleo ya miaka 10 panda miti, lakini ukitaka maendeleo ya karne moja somesha watu wako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali yetu Tukufu ifanye kila linalowezekana aghalau igharamie kuwapeleka vijana masomoni wapatao 1,000 vijana ambao walifanya vizuri sana katika masomo yao, napendekeza sisi hatuna uwezo wa kupeleka vijana wetu wengi Marekani lakini badala yake angalau tunaweza kuwapeleka vijana wetu Korea, China, India, mahali ambapo gharama za masomo zipo chini kidogo ukilinganisha na Marekani na nchi nyingine za Ulaya.
Mheshimiwa Spika, nalisema hili kwa sababu moja ya matatizo makubwa sana yanayolikabili BARA la Afrika ni ukosefu wa ujuzi na maarifa na kama Biblia Takatifu inavyosema watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa. Nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kutoa mchango wangu kuhusu taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1972, aliyekuwa Mfalme wa Dubai wakati huo, Sheikh Rashid Bin Maktoum, alikuwa na ndoto ya kujenga bandari kubwa sana katika ukanda ule wa Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati kwa ujumla lakini kwa bahati mbaya washauri wake kutoka Uingereza walimwambia hapana mradi huu hautakuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa bahati mbaya washauri wake kutoka Uingereza walimwambia hapana mradi huu hautakuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi. Sheikh Maktoum alikataa alisema hapana sikubaliani na ushauri huu. Hata kama mradi huu hautakuwa maslahi ya kiuchumi nitautekeleza kwa sababu ninaamini wajukuu na watoto wangu hawataweza kuutekeleza mradi huu miaka mingi ijayo kwa sababu gharama zake zitakuwa zimepanda sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajifunza nini? Tunachojifunza ni kwamba, tukitaka kupiga hatua ya maendeleo ya haraka kama Taifa tunapaswa kuwa na viongozi, na ninaposema viongozi sina maana ya viongozi wa kitaifa nina maana ya Waheshimiwa Mawaziri, Wabunge, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa; tunahitaji kuwa na viongozi wa aina gani? tunahitaji mambo mawili. Kwanza tunahitaji viongozi wenye maono makubwa, wanaozingatia maslahi ya kizazi kinachokuja kuliko kizazi cha sasa. Pili tunahitaji viongozi wenye ujasiri wa kufanya maamuzi magumu kwa sababu kutakuwa na watu maamuzi hayo wanayatilia shaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nayasema haya; kwa zaidi ya miaka 15 tumekuwa tukizungumza utekelezaji wa mipango ya utekelezaji wa miradi mikuu miwili, mradi wa makaa ya mawe na chuma kule Liganga na Mchuchuma pamoja na mradi wa kusindika gesi asilia kule Lindi. Kwa bahati mbaya katika kipindi cha miaka 15 mpaka leo miradi hii haijatekelezwa
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maoni yangu, nadhani kama miradi hii ingetekelezwa miaka 15 iliyopita, Taifa letu lingepata maslahi makubwa sana ya kiuchumi, na nitayataja. Kwanza gharama za miradi hii zingekuwa chini sana kuliko ilivyo leo, pili tungetekeleza mradi wa gesi asilia miaka 15 iliyopita leo tungenufaika na soko kuu sana linalotokana na uhaba wa gesi asilia duniani unaotokana na vita vya Ukraine na Urusi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika tungetekeleza mradi wa gesi asilia miaka 15 iliyopita leo tungepata gesi nyingi sana inayotumika katika kuendesha mitambo na magari na hatimaye kupunguza uagiziaji wa mafuta kutoka nje. Lakini kwa upande wa chuma leo tungekuwa na chuma cha kutosha kwa ajili ya kutekeleza mradi wa reli ya kati. Hivi sasa Taifa letu linatumia kiasi kikubwa sana za fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza chuma kinachohitajika katika ujenzi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, tungetekeleza miradi miaka 15 iliyopita ingetusaidia sana kwa sababu naamini miaka mitano mpaka 10 inayokuja mahitaji ya gesi asilia duniani yatakuwa yamepungua sana, kwa maana hiyo gesi asilia haitakuwa na faida kubwa kwa Taifa letu. Kwa nini nasema hivyo? Hivi sasa mjasiriamali mkuu sana duniani anayeitwa Elon Musk ameshaanza uzalishaji wa magari yanayotumia umeme. Jambo hilo likifanyika kwa kiwango kikubwa gesi haitakuwa na matumizi makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mataifa mbalimbali tayari yameshaanza utafiti hivi sasa wa namna ya kutumia gesi ya hydrogen kama chanzo kikuu cha nishati. Jambo hilo likifanyika gesi asilia ya Tanzania haitakuwa na maslahi makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa ushauri wa mwanadamu anayeaminika kuwa mtu mwenye busara kubwa sana kupata kutokea hapa duniani Mfalme Suleiman. Mfalme Suleiman aliwahi kusema maneno haya, na sisi kama viongozi tunapaswa kuyazingatia; akasema hakuna wakati mzuri wa kutekeleza mambo makubwa na muhimu kwa wanadamu kuliko sasa hivi. Tusisubiri muda unaokuja kwa sababu huo muda utakaokuja hatuna uhakika kwamba kila kitu kitakuwa sawa. Lakini, mwisho hatujui Mwenyezi Mungu amepanga lini na nini, kesho na kesho kutwa, kwa hiyo tunapaswa kutekeleza leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali tunapaswa kufanya kila linalowezekana sisi kama Taifa tuitekeleze miradi hii sasa kwa sababu hatujui kitakachotokea baada ya miaka mitano au kumi ijayo, linalowezekana leo lisingoje kesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wanasayansi wa zamani, Hippocrates na Thomas Edison waliwahi kusema madaktari wa karne ya 21 watatumia lishe bora katika tiba badala ya kutumia madawa ya kemikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunatambua umuhimu wa lishe bora katika afya ya jamii. Niwakumbushe tu mwaka 2020 wakati wa ugonjwa wa Corona ulivyopamba moto katika nchi yetu, Watanzania mbalimbali wakiwemo baadhi ya Waheshimiwa wenzetu Wabunge walitengeneza dawa asili kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa Corona na kusema kweli dawa hizo zilitusaidia kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja linanisikitisha sana ninapoona Serikali yetu inatumia kiasi kikubwa sana cha fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza bidhaa hasa za chakula ambazo tunaweza tukazizalisha hapa nchini kwa ubora wa hali ya juu sana. Tunaagiza maziwa ya unga wakati Tanzania tuna ng’ombe wapatao milioni 23; tunaagiza juisi za matunda wakati Tanzania ina matunda ya kila aina yanaoyoharibika kwa kukosa soko; tunaagiza mayai na kuku, wakati Tanzania tuna kuku wa kila aina; tunaagiza dawa ambazo tungeweza kuzitengeneza hapa hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti na ndugu zangu, jambo linalonisikitisha zaidi, watoto wa Watanzania ambao ni warithi wetu, tunawalisha vyakula ambavyo vina kiwango kikubwa sana cha sukari na protini yenye kiwango duni sana. Matokeo yake ni nini? Tunadumaza akili na miili ya watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawezaje kama Taifa kuingia katika karne ya 21 tukiwa na watoto ambao uwezo wao wa kufikiri ni umedumaa sana? Sasa niliwahi kusoma mahali, nikawa natafuta siri ya Waisraeli kuwa na watoto wenye kipawa cha hali ya juu sana na nikabaini kumbe hakuna siri, jambo lililo wazi ni lishe bora ndugu zangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mawazo yangu nafikiri sasa wakati umefika sisi kama Taifa tufanye uamuzi wa kimapinduzi, tuiangalie mitaala yetu ya shule za udakitari na sayansi ile ya tiba, badala ya kusisitiza kwenye matumizi ya madawa yasiyokuwa na ulazima, tusisitize kwenye sayansi ya lishe na tiba ya asili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nayasema haya? Inasikitisha sana unapokwenda hospitali kwa ugonjwa tu wa kawaida, mfano una upungufu wa madini fulani fulani, au upungufu wa vitamini, basi madaktari wanakukusanyia multivitamin chungu nzima. Unaweza kwenda hospitali tu una kikohozi au una mafua, badala ya kupewa orodha ya vyakula ambavyo vinaweza kukusaidia na kurudisha haraka afya yako, basi madaktari wanakukusanyia madawa chungu zima. Ndiyo maana napendekeza tuiangalie mitaala yetu, badala ya kung’ang’ania tu kufundisha masomo kama pharmacology ambayo yanasisitiza na kuendeleza soko la madawa ya kemikali kutoka nje, sasa tuweke mkazo kwenye sayansia ya lishe na tiba ya asili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati Marehemu Baba wa Taifa aliwahi kufanya mipango kwamba sayansi ya lishe na tiba asili ziingizwe katika mifumo rasmi ya Serikali; matabibu wa hospitali, shule za utabibu kama nilivyosema, ziwe zinasisitiza juu ya masuala haya. Kwa bahati mbaya sana jambo hilo jema hatukulifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu ana msemo wake maarufu sana na naomba niurudie hapa, anasema hivi: “Waafrika ni watu wa ajabu sana. Wanapoona Wazungu wanafanya jambo hata kama ni la kijinga, watalifurahia, lakini Mwafrika anapofanya jambo hata liwe la maana la kiasi gani, wanalipuuza.” Sasa ndugu zangu mimi nasema masuala ya umuhimu wa lishe na sayansi ya lishe na tiba asili siyo jambo jipya, lakini kwa sababu tu pengine amelisema Thomas Edison na Hippocrates, tunaweza kuliona ni jambo la ajabu. Jambo hili babu zetu, wazee wetu walilitambua zaidi ya miaka 1,000. Sasa nasema wakati umefika jambo hili tulifanyie kazi na tulipe uzito unaostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Spika, katika mchango wangu nitazungumzia mambo matatu. Jambo la kwanza falsafa ya uongozi ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wake Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameonyesha kuwa ni kiongozi msikivu, mpole, mtulivu na anayetumia hekima kubwa sana katika kufanya maamuzi yenye maslahi makubwa kwa Taifa letu. Nitatoa mfano wa mambo manne; moja, Mheshimiwa Suluhu Hassan amefufua na kuimarisha mahusiano ya Tanzania na nchi za nje na kukuza hadhi na heshima ya Taifa letu katika medani ya kimataifa. Pili, Serikali anayoiongoza ina mpango wa kuanzisha Chuo kipya cha Teknolojia, Habari na Mawasiliano hapa Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivi sasa dunia imo katika awamu ya nne ya mapinduzi ya teknolojia, mapinduzi ambayo yanashuhudia matumizi makubwa ya sayansi ya kompyuta na hasahasa matumizi ya kompyuta zinazofikiri kama binadamu, roboti, mitambo inayojiendesha yenyewe bila kumtegemea binadamu. Bila shaka maendeleo haya yanahitaji vijana wenye ujuzi, maarifa, utaalam katika masuala ya sayansi ya habari na teknolojia ya habari na mawasiliano kwa ujumla na bila shaka wazo la Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuanzisha Chuo cha Teknolojia ya Habari limekuja katika wakati muafaka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amefufua Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Kisasa ya Bagamoyo na nne, Rais Samia amefufua Mradi wa Kusindika Gesi Asilia huko Mtwara.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nchi yetu inawekeza fedha nyingi kila mwaka kwa ajili ya ujenzi wa barabara lakini kwa bahati mbaya sana barabara hizi zinaharibika katika kipindi kifupi sana. Kwa hiyo, nchi yetu inalazimika kutenga fedha nyingine kwa ajili ya kuzifanyia marekebisho na matengenezo barabara hizo. Kwa kawaida barabara inahitaji kufanyiwa matengenezo makubwa katika kipindi cha miaka kumi mpaka ishirini, lakini kwa upande wetu hali ni tofauti sana katika kipindi kisichozidi miaka mitatu barabara zetu nyingi zinaharibika na hatimaye tunalazimika kutenga fedha nyingi kwa ajili ya kuzifanyia matengenezo. Nchi yetu ni maskini na haiwezi kumudu gharama za namna hii. Ili kuepuka matengenezo ya mara kwa mara ya barabara, hivyo, napendekeza mambo mawili yafuatayo: -
(i) Serikali iteue wahandisi waadilifu na wenye weledi wanaoweza kuwasimamia wakandarasi wa barabara ili barabara zijengwe kwa kiwango na ubora unaotakiwa. (Makofi)
(ii) Naunga mkono hoja ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti; Serikali iimarishe Kitengo cha Ukaguzi wa Barabara ili kubaini uharibifu mapema na hatimaye kufanya matengenezo yanayohitajika kwa wakati. Jambo hili litatusaidia sana katika kudhibiti matumizi makubwa ya fedha katika matengenezo ya barabara zetu kama Waingereza wasemavyo a stitch in time saves nine, kwa Kiswahili usipoziba ufa utajenga ukuta. (Makofi)
(iii) Mwaka 1987 marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alipokuwa akihutubia Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa alisema maneno yafuatayo: -
“Iwapo nchi yetu inataka kupiga hatua kubwa za maendeleo na za haraka, hatuna budi tuzitumie rasilimali zetu kikamilifu.”
Mheshimiwa Spika, kwa mawazo yangu bado hatujauzingatia ushauri huu wa Mwalimu ipasavyo hasa katika sekta ya gesi asilia. Mwenyezi Mungu ametubariki na kutujalia gesi ipatayo trilioni 57 za ujazo, lakini kwa bahati mbaya sana tumeweza kutumia kiasi hiki cha gesi kwa kiasi kidogo sana. Iwapo tunataka kukabiliana kikamilifu na kupanda kwa bei za mafuta zinazotokea kila wakati tunapaswa kuimarisha uchumi wa gesi. Kwa hiyo, napendekeza Serikali ifanye mambo yafuatayo: -
(i) Serikali iongeze matumizi ya bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Kwa bahati mbaya hivi sasa Serikali imetumia bomba hili kwa asilimia 10 tu. Habari hizi si njema hata kidogo, tunapaswa kuongeza matumizi ya bomba hili. (Makofi)
(ii) Serikali ihakikishe mipango na matumizi ya nishati ya gesi katika matumizi hasa katika kuendesha magari ya Serikali na mizigo ili kupunguza gharama ya usafiri na usafirishaji.
(iii) Serikali iharakishe mipango ya kutekeleza mradi wa kusindika gesi asilia kule Lindi.
Mheshimiwa Spika, hapana shaka tukichukua hatua hizi nilizozieleza tutaweza kupunguza uagizaji wa mafuta kutoka nje kwa kiasi kikubwa na naamini hali hii itatusaidia sana kupunguza makali ya maisha kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru. Naomba nitoe mchango wangu kwa kunukuu maneno ya hekima kutoka katika Quran Takatifu na Biblia. Katika Quran tunaambiwa Mwenyezi Mungu anasema, “Tutawanyanyua wale waliomwamini Mwenyezi Mungu na wale wenye elimu.” Kwenye Biblia tunaelezwa, “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mataifa yaliyo makini na yanayotamani maendeleo ya haraka yamefanya uamuzi wa kimapinduzi kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha katika sekta ya elimu hasa elimu ya sayansi na teknolojia. Hili halishangazi, ndiyo maana nchi kama India, China, Singapore, Vietnam na Korea Kusini zimepata maendeleo ya kupigia mfano katika miaka ya karibuni kwa sababu wamewekeza sana katika sekta ya elimu hasa teknolojia na sayansi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo letu kubwa ninaloliona kama Taifa, ninapoangalia mipango yetu ya maendeleo, tumeweka kiasi kikubwa sana cha fedha katika kutekeleza miundombinu. Naomba samahani sana, nadhani kwenye sekta ya elimu hasa sayansi na teknolojia hatujawekeza kiasi cha kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine linalotukwamisha kama Taifa hatuna mpango madhubuti wa usimamizi wa wafanyakazi na rasilimali watu kwa ujumla (human resource planning and management). Nitalifafanua jambo hili. Kila mwaka tunatenga zaidi ya shilingi bilioni 400 na mwaka huu 2023/2024 tumetenga shilingi bilioni 731 kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu. Tunatayarisha madaktari, wahandisi, walimu, lakini kwa bahati mbaya tukishawatayarisha hatuwaajiri tunawaacha wanazagaa kwenye mitaa. Haya ni matumizi mabaya sana ya rasilimali ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hapa kuna tatizo, ama mafunzo yanayotolewa ya shahada hayana ubora unaotakiwa wa kuwawezesha vijana wetu kujiajiri ama vijana wanalazimishwa kuchukua course ambazo hawana passion nazo, hawazipendi, ama wazazi wao wanawalazimisha, kama mzazi ni daktari anatamani na mwanaye awe daktari; kama mzazi ni mhasibu anatamani mwanaye awe daktari. Pia kuna tatizo kwenye vyuo vyenyewe. Kuna uchache wa course za uchaguzi. Kwa maana hiyo wanafunzi wanalazimika kuchukua na masomo ambayo pengine hawayapendi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ushauri wangu, nafikiri wakati umefika Serikali ingefanya maamuzi mahususi, tukafanya ukaguzi wa idadi ya wafanyakazi tunaoweza kuwaajiri, human resource audit ili tukawasomesha watu tunaoweza kuwaajiri na fedha zinazobaki tukazielekeza kwenye mafunzo ya ufundi stadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa mafunzo ya ufundi stadi, nilikuwa na mawazo kidogo. Kuna tatizo hapa, mafunzo yanatolewa, lakini tatizo letu kama Taifa, vijana wote wa nchi nzima kuna mtaala mmoja tu wa elimu ya ufundi stadi. Hii nadhani siyo sawa, kwa sababu mahitaji ya binadamu ni tofauti, mazingira ya mwanadamu ni tofauti, kazi kuu inayofanyika kwenye jamii ni tofauti kati jamii moja na nyingine; hata rasilimali ni tofauti. Kwa maana hiyo, hatulazimiki kwamba lazima tuwe na mtaala mmoja. Kila wilaya iwe na mtaala unaolingana na mazingira yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, jamii ya wafugaji kwa nini hatuwafundishi ufugaji wa kisasa, ujasiriamali na namna bora ya kuzalisha mazao bora ya ufugali kama vile uzalishaji wa maziwa, utengenezaji wa jibini, utengenezaji wa samli, mtindi, nyama choma na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa watu wanafundishwa mambo ya jumla jumla tu. Jamii ya wavuvi tungefanya hivyo hivyo na jamii ya wafugaji nyuki tungefanya hivyo hivyo. Nadhani tukifanya hivyo bila shaka tija itaonekana sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, nadhani mbali nakuwa na vyuo hivi vya VETA kila Wilaya, Serikali inapaswa kuwa na vyuo vichache sana vunavyofundisha masomo maalumu. Kwa mfano, teknolojia ya habari, mitambo inayotumia akili za bandia, uhandisi, nishati ya jua, teknolojia ya kilimo cha umwagiliaji maji na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo langu la mwisho, Mipango yetu ya Maendeleo haitafanikiwa kama tunavyotarajia kama hatujawekeza kiasi cha kutosha katika sekta ya elimu. Kwa maoni yangu, nadhani sekta ya elimu inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Kwa sababu karne zilizopita utajiri na ustawi wa mataifa ulipimwa kwa kutumia nguvu ya misuli, utajiri wa mafuta, madini na gesi. Katika karne ya 21 ustawi wa mataifa utapimwa kwa kutumia nguvu ya akili, maarifa na sayansi. Naomba nirudie katika karne ya 21 mapambano makubwa na hasa vita kati ya Taifa moja na lingine hayatapiganwa sana kwa kutumia mizinga na silaha tunazoziona, bali mapambano makubwa yatakuwa katika kutumia cyber, yani kutumia teknolojia ya Habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, sisi kama Taifa watu wetu tuwaelekeze huko tu. Nadhani wakati umefika sasa Vyuo vyetu Vikuu na hasa vinavyofundisha mambo ya teknolojia na sayansi kwa ujumla, vinapaswa kuanzisha course maalum za teknolojia ya kidigitali, artificial intelligence na data science kama tunataka kuingia kwenye karne ya 21 kwa mbwembwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. Naomba kuunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi hii adhimu. Nimesikiliza kwa makini sana taarifa mbili, Taarifa ya Kamati ya Bajeti na Taarifa ya Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma. Katika taarifa hizo mbili, nimebaini mambo mawili makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, matumizi ya fedha za umma hayakidhi mahitaji; na pili, utekelezaji wa mipango ya Serikali haufikii malengo tuliyoyapanga. Hiki tunachokiona kwa maoni yangu, siyo kiini cha tatizo la msingi, bali ni matokeo. Kwangu mimi tatizo la msingi ni kutokuwepo kwa mpango madhubuti wa usimamizi na matumizi sahihi ya rasilimali watu katika Taifa letu na nimewahi kulisema jambo hili huko nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kila mwaka anakagua fedha na matumizi yake, lakini wakati Ofisi hiyo ikifanya hivyo, Menejimenti ya Utumishi wa Umma haifanyi ukaguzi wa wafanyakazi na watumishi wa Serikali ambao ndio wenye jukumu la kusimamia matumizi ya fedha za Serikali. Kwa maoni yangu nadhani jambo hili siyo sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utekelezaji wa mipango ya Serikali, hatufikii malengo tuliyoyapanga kwa sababu ama kuna ujuzi na maarifa madogo kwa wafanyakazi, ama fikra na mtazamo wa wafanyakazi haupo sahihi. Hili nitalieleza hapo baadaye, ninakusidia nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri mambo manne baada ya kusema hayo, la kwanza, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ianzishe utaratibu na program maalum ya kuwakagua wafanyakazi ili kubaini uwezo wao, weledi wao utendaji wao, uaminfu wao. Tukifanya hivyo pale ambapo tutabaini kwamba wafanyakazi hawana ujuzi na weledi unaotakiwa tuandae mafunzo ya mara kwa mara ili waongeze ujuzi na maarifa yao na pale ambapo tutabaini kuwa kuna wafanyakazi wanafanya kazi kwa weledi na ni mahiri basi wapandishwe vyeo ili kuwaongezea motisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wataalam wa management wanasema kazi ambayo haitathminiwi, kazi ambayo haipimwi haiwezi kuwa na ufanisi hata kidogo. Kwa maana hiyo basi najua Menejimenti ya Utumishi wa Umma huko nyuma kila wakati wanakuja na nadharia mpya za upimaji wa utendaji wa watumishi wa Serikali. Sasa napendekeza jambo hili ni la maana sana ni lazima tupime utendaji na uwajibikaji wa wafanyakazi wa Serikali ili watakaofanya vizuri wapewe motisha na watakaofanya vibaya tuwapatie mafunzo kama nilivyosema hapo awali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo langu la pili; uteuzi wa watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya Serikali ufanywe kwa ushindani na kwa kuzingatia sifa, elimu, weledei, uzoefu, tabia, ujuzi, mtazamo na fikra. Kwa nini ninalisema jambo hili? Nalisema jambo hili kwa sababu wakati mwingine unaweza kuwa na mtu ana elimu kubwa sana lakini hafanyi kazi kwa ufanisi na hatujiulizi kwa nini hafanyi kazi kwa ufanisi, kwa mawazo yangu kuna tatizo kubwa sana la mind set (fikra na mtazamo). (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtendaji ambaye hana mtazamo sahihi, hana fikra sahihi atakuwa na tabia ya kuchelewesha mambo, nenda kesho rudi kesho kutwa, hana malengo, hana uhitaji wa kujifunza mambo mapya. Wenzetu walioendelea sana na wanaopiga hatua; Wachina, Wajapan, Wahindi wanawapeleka vijana wao nje siyo tu kujifunza teknolojia mpya bali kujifunza utamaduni, mtazamo na fikra, sasa hili ndilo ambalo linafanywa na sisi tulifanye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata dini zetu tunakumbuka kisa cha Yusufu, alipelekwa utumwani, baada ya kufika utumwani alifanya kazi hatimaye akawa Waziri Mkuu. Sina maana kwamba tunapotaka vijana wetu wawe mahiri tuwapeleke utumwani, la hasha! Ninachomaanisha hivi kama mazingira yetu ya kufanyia kazi siyo muafaka tuyabadilishe na tuwapeleke watu wakajifunze mambo mapya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Mtume Muhamad (S.A.W) alipoona mazingira ya kwao Maka hayako muafaka alihama na akahamia Madina na aliifanya kazi yake vizuri sana. Kwa hiyo, kuna umuhimu wa kujifunza katika mazingira mapya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, ninashauri kila Wizara iwe na timu za wataalam wa kuwafundisha wafanyakazi weledi na mafunzo katika kazi. Sisi Waafrika tuna tabia; kazi ya kujielimisha na kazi ya kuongeza maarifa tunaimaliza baada ya kumaliza vyuo vikuu. Sasa mimi mategemeo yangu kwamba sehemu za kazi zinaweza kutoa mchango mkubwa sana katika kuwapatia maarifa na ujuzi wafanyakazi wetu. Naomba tulisimamie jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho; napendekeza Serikali iweke mkazo mkubwa sana katika kuwapeleka vijana wetu hasa vijana wanaosomea uhasibu, ukaguzi na uendeshaji wa mashirika nje ya nchi ili wakajifunze kwa vitendo. Yapo mashirika makubwa sana ya uhasibu duniani na nitayataja hapa; Price Waterhouse Coopers, Deloitte na NS & Young. Sasa ninachomaanisha hapa vijana wetu haitoshi tu kumaliza masomo yao vyuo vikuu bali tuwapeleke katika mashirika hayo makubwa ili kwanza wajifunze namna ya kuendesha mashirika hayo lakini pili wajifunze utamaduni, fikra na mtazamo mpya wa kimaendeleo ili watakaporudi hapa waendeshe mashirika yetu kwa ufanisi unaotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ninapenda kukushukuru na nitoe mchango wangu kwenye maeneo matatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, jeshi letu kwa muda mrefu limekuwa likitoa msaada mkubwa sana wa ulinzi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndani ya Bara la Afrika na nje ya Bara la Afrika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika zama za sasa mbinu na medani za kivita zimebadilika sana na kwa maana hiyo basi, tunao wajibu kama Taifa tuliandae vizuri jeshi letu ili likabiliane na changamoto za karne ya 21. Katika karne hii vita vingi vya kimkakati havitapiganwa kwa kutumia mizinga mikubwa bali kama mwenzangu alivyosema hapa vitapigwana kwa kutumia roboti, mifumo ya cyber na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo basi, ninalotaka kulisema hapa ni kwamba tunao wajibu kama Taifa tuangalie changamoto hizo ili tuweze kuwasaidia wanajeshi wetu. Nitataja maeneo matano ambayo Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania lina changamoto:-
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, mtakubaliana nami katika karne hii maadui wa nchi wanaweza kutumia mifumo ya cyber kuharibu benki, mashirika ya umeme, hospitali, vituo vya hifadhia data na kadhalika, kwa kutumia mifumo ya kisasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya pili, maadui wanaweza kuharibu hewa, maji na kwa kitaalamu tunaita biologically and chemically warfare.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya tatu, kadiri nchi yetu inavyoendelea ndivyo mahitaji ya wahandisi mahiri wanavyohitajika hasa katika miundombinu ya bandari, reli za kisasa, viwanja vya ndege na anga.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya nne, ninayotaka kuielezea hapa ni siasa za dunia katika karne hii zitahamia katika Bahari ya Hindi kwa sababu katika Bahari ya Hindi, kuna rasilimali kubwa sana kama mafuta, gesi asilia, madini, samaki na usafiri wa mizigo. Kwa maana hiyo basi mataifa yenye nguvu yatamimika sana katika eneo hilo. Ninapendekeza hapa Majeshi ya Maji katika nchi wanachama wa maeneo hayo wafanye mafunzo ya mara kwa mara ili waweze kukabiliana na changamoto ya Bahari ya Hindi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya tano, Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania limekuwa likishiriki katika misheni mbalimbali za Kimataifa na kusema kweli jeshi letu limefanya kazi nzuri sana, kwa maana hiyo basi pamoja na umasikini wetu kuna haja sisi kama Taifa tuwaandalie vijana wetu malipo mazuri ya fidia kwa wanajeshi ambao kwa bahati mbaya watapata ulemavu wa kudumu na wale watakaopata vifo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, ninaiomba Wizara ya Ulinzi ishirikiane na Chuo Kikuu cha Taifa Muhimbili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma ili kuandaa vijana wenye taaluma katika kozi nitakazozieleza; kozi za Cyber Security, Space Technology, Military Medicine, Maritime Security pamoja na Mechatronic Engineering ili tupate vijana wenye weledi katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mtakubalina nami kwamba nchi yetu sasa inatekeleza miradi mikuu ya kimkakati Bwawa la Mwalimu Nyerere na reli ya Taifa. Miradi hii inahitaji ulinzi wa hali ya juu sana pamoja na mahitaji ya matengenezo ya kiufundi hasa miradi hii itapokamilika. Kwa maana hiyo basi kuna haja ya kuandaa vijana wetu wa jeshi wenye taaluma kwenye maeneo hayo ili miradi hii ikikamilika na yatakapotokea mahitaji ya matengenezo. Tusikimbilie nje kutafuta wahandisi wa nje, bali jeshi letu litoe msaada wa kiufundi na kitaalamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Spika, mwaka 1987 Marehemu Baba wa Taifa alipokuwa akihutubia Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama chake Cha Mapinduzi alisema; “Tatizo kubwa la Afrika si ukosefu wa rasilimali bali tatizo kubwa la nchi za Kiafrika ni matumizi sahihi ya rasilimali walizopewa na Mwenyezi Mungu.” Maneno haya ya Mwalimu yananifanya nitafakari sana juu ya namna tunavyosimamia uchumi wa gesi katika Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, nimeanza kusikia mipango ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya gesi asilia tangu nilipoingia kwenye Bunge hili Tukufu mwaka 2010. Ni kama miaka 14 hivi na kwa bahati mbaya hatujaweza kutekeleza kikamilifu mipango hiyo ya kutekeleza uchumi wa gesi kama tulivyodhamiria. Nitaeleza jinsi tunavyopoteza fursa mbalimbali za kiuchumi kadiri tunavyoendelea kuchukua muda mrefu kutekeleza mipango hiyo ya uchumi wa gesi na nitatoa mifano kwenye maeneo manne.
Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza, nchi yetu inatumia takribani 50% ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza mafuta kutoka nchi za nje. Kama tungefanya maamuzi kwa wakati mwafaka tukatekeleza miradi ya kuanzisha nishati ya gesi kwa ajili ya matumizi ya magari na mitambo bila shaka tungepunguza sana matumizi ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza mafuta kutoka nje. Jambo hili lingekuwa na maslahi mapana sana kwa ajili ya uchumi wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, eneo la pili, hivi sasa vitendo vya ukataji miti vinaendelea kwa kasi sana katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, hata katika ripoti ya Waziri Mkuu amelisema jambo hili. Naamini kama tungetekeleza miradi hii na mipango ya uchumi wa gesi kwa wakati bila shaka tungeweza kusambaza gesi katika majumba mbalimbali ya wananchi. Sasa badala ya wananchi kuendelea kukata miti wangetumia gesi kupikia na hatimaye tungeweza kuokoa miti na kuimarisha mazingira ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la tatu, hivi sasa tunatumia 40% ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza mbolea kutoka nje na kwa bahati nzuri Mwenyezi Mungu ametubariki hazina kubwa ya gesi asilia hapa nchini. Tungeitumia gesi asilia kikamilifu tungeweza kuanzisha viwanda vya kutengeneza mbolea na tungeweza kuleta mapinduzi makubwa sana ya kilimo hapa nchini. Kwa isivyo bahati hatujalifanya jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la nne na la mwisho, hivi sasa tuna upungufu mkubwa sana wa fedha za kigeni, ningetarajia huu ungekuwa ni wakati mwafaka wa kutekeleza mradi wa muda mrefu wa kusindika gesi asilia ili tuweze kuuza nje kimiminika cha gesi ili tupate fedha za kigeni. Kwa isivyo bahati mradi huu haujatekelezwa.
Mheshimiwa Spika, kwa maoni yangu mradi huu umechukua muda mrefu sana na moja ya sifa kuu ya viongozi ni kufanya maamuzi kwa wakati mwafaka na kutumia fursa zilizopo. Natambua kuna haja ya kufanya majadiliano kwa umakini, lakini nina wasiwasi, kadri tunavyoendelea kuchukua muda mrefu ndivyo tunavyoendelea kupoteza fursa za kiuchumi duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba tuzingatie mambo matatu, laiti tungeutekeleza mradi wa kusindika gesi kwa 100%, miaka mitatu iliyopita tungeweza kuitumia fursa ya vita inayoendelea kati ya Ukraine na Russia kwa ajili ya kuuza kimiminika cha gesi Nchi za Ulaya na kupata pesa za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la pili la tafakari, kadiri tunavyoendelea kutafakari namna tutakavyoitumia nishati ya gesi katika kuendesha mitambo na magari, wenzetu kwa mfano Elon Musk ameshaanza kuzalisha magari yanayotumia betri za umeme.
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu la kutafakari ni kwamba, hivi sasa kuna utafiti mkubwa sana unaoendelea katika Nchi za Ulaya wa kutumia hewa ya nitrogen kama chanzo kikuu cha nishati na bila shaka jambo hili likifanikiwa basi hapana shaka matumizi ya gesi asilia duniani yatapungua sana. Kwa maana hiyo Tanzania kama Taifa tutakuwa tumepoteza fursa kubwa sana ya kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno hayo, naomba nimalize mchango wangu kwa kunukuu maneno aliyoyasema Hayati Baba wa Taifa; “Inawezekana, timiza wajibu wako.”
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu Zilizokaguliwa za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2023; na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, kabla sijaanza mchango wangu naomba kusema mambo machache. Nakupongeza kwa dhati kwa namna unavyotekeleza wajibu wako katika Umoja wa Mabunge Duniani; moja ya sifa ya kiongozi mahiri ni kusema ukweli wa mambo magumu kwa ujasiri, nakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mtaalam wa uchumi wa Marekani Profesa Rostain, aliwahi kusema linalotofautisha nchi zilizoendelea na zinazoendelea ni jambo moja tu, udhibiti na matumizi sahihi ya fedha za umma katika kuleta maendeleo ya wananchi. Nimeona nianze na jambo hili kutokana na umuhimu wa hoja iliyopo mbele yetu katika maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, unaposikiliza kwa makini taarifa za wenyeviti kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, utabaini kwamba kuna matumizi yasiyo sahihi katika fedha za umma. Kwa bahati mbaya matatizo tunayoyajadili leo yamekuwa yakijirudia kila mwaka. Kwa maoni yangu makosa haya hayatokani na ukosefu wa uweledi na ujuzi wa masuala ya kihasibu bali linatokana na udhaifu wa usimamizi na kutokufuatwa kwa maadili ya kazi.
Mheshimiwa Spika, mtaalam mmoja wa uongozi bwana Maxwell, aliwahi kusema maneno yafuatayo: “Everything rises and falls on leadership” kila kitu kinategemea uongozi, kwa hiyo mafanikio na udhaifu wa taasisi unatokana na uongozi. Ili kuondoa kasoro hizo nilizozibainisha hapo juu naomba nipendekeze mambo sita yafanyiwe kazi na Serikali.
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, Serikali inapofanya uteuzi wake wa Wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi za Mashirika yote na Taasisi zote za Umma izingatie taaluma, ujuzi, uweledi, uzoefu na tabia.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, watendaji Wakuu wa Mashirika yote ya Umma wateuliwe kwa kuzingatia tabia zao, umahiri wao, uzoefu wao, elimu zao na mitazamo yao.
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, Serikali iwapeleke Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Umma na Taasisi katika mafunzo ya kikazi nje ya nchi hasa katika mashirika makubwa sana ya kihasibu kwa mfano Deloitte, KPMG, PricewaterhouseCoopers na Ernst & Young ili wajifunze namna ya kuongoza mashirika na utamaduni wa kuendesha makampuni na mashirika ya umma ili yajiendeshe kibiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la nne, hivi sasa tunayo Taasisi ya Uongozi Serikalini, ambayo ipo chini ya Wizara ya Mipango na Uwekezaji. Kwa bahati mbaya taasisi hii haina majengo ya kudumu, haina wahadhiri wa kudumu, haina wataalam wa kudumu.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kwa Serikali taasisi hii ihamishiwe Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili ipate kuwa na sehemu ya kufanyia kazi, wahadhiri wenye uwezo ili watoe mafunzo katika masuala mbalimbali, kwa mfano maendeleo ya uongozi na nitaeleza faida chache sana za taaluma ya maendeleo ya uongozi.
Mheshimiwa Spika, kwanza kuelewa kufanya mipango, kuteua wafanyakazi na wataalam wenye uwezo, kutekeleza na kusimamia miradi ya maendeleo ya Taifa. Mtakumbuka chuo cha zamani cha Mzumbe kilikuwa kinafanya kazi nzuri sana katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, jambo la tano, naiomba Serikali iimarishe mifumo yake hasa katika kutathmini utendaji wa mashirika, najua kazi hii imeshaanza kufanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, naomba kazi hii iendelee.
Mheshimiwa Spika, pendekezo langu la mwisho, Serikali iongeze kasi ya utekelezaji wa kuimarisha, wa kutekeleza agizo la kuimarisha matumizi ya mifumo ya kisasa katika shughuli za Serikali.
Mheshimiwa Spika, Kamati yangu ya bajeti imependekeza sio mara moja sio mara mbili, kwanza mifumo ya TRA, TPA pamoja na halmashauri za wilaya ziunganishwe pamoja na ziowane ili kudhibiti udanganyifu Serikalini na la pili, tumependekeza siyo mara moja, siyo mara mbili, Serikali ianzishe utaratibu wa matumizi ya mifumo ya kidijitali ili malipo ya Serikali yafanyike bila ya kutumia fedha tasilimu.
Mheshimiwa Spika, bila shaka utakubaliana na mimi kama mambo haya sita niliyoyataja yatasimamiwa, yatatekelezwa ipasavyo bila shaka tutapiga hatua kuliko hapa tulipo sasa.
Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ninapenda kukushukuru na nitoe mchango wangu kwenye maeneo matatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, jeshi letu kwa muda mrefu limekuwa likitoa msaada mkubwa sana wa ulinzi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndani ya Bara la Afrika na nje ya Bara la Afrika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika zama za sasa mbinu na medani za kivita zimebadilika sana na kwa maana hiyo basi, tunao wajibu kama Taifa tuliandae vizuri jeshi letu ili likabiliane na changamoto za karne ya 21. Katika karne hii vita vingi vya kimkakati havitapiganwa kwa kutumia mizinga mikubwa bali kama mwenzangu alivyosema hapa vitapigwana kwa kutumia roboti, mifumo ya cyber na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo basi, ninalotaka kulisema hapa ni kwamba tunao wajibu kama Taifa tuangalie changamoto hizo ili tuweze kuwasaidia wanajeshi wetu. Nitataja maeneo matano ambayo Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania lina changamoto:-
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, mtakubaliana nami katika karne hii maadui wa nchi wanaweza kutumia mifumo ya cyber kuharibu benki, mashirika ya umeme, hospitali, vituo vya hifadhia data na kadhalika, kwa kutumia mifumo ya kisasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya pili, maadui wanaweza kuharibu hewa, maji na kwa kitaalamu tunaita biologically and chemically warfare.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya tatu, kadiri nchi yetu inavyoendelea ndivyo mahitaji ya wahandisi mahiri wanavyohitajika hasa katika miundombinu ya bandari, reli za kisasa, viwanja vya ndege na anga.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya nne, ninayotaka kuielezea hapa ni siasa za dunia katika karne hii zitahamia katika Bahari ya Hindi kwa sababu katika Bahari ya Hindi, kuna rasilimali kubwa sana kama mafuta, gesi asilia, madini, samaki na usafiri wa mizigo. Kwa maana hiyo basi mataifa yenye nguvu yatamimika sana katika eneo hilo. Ninapendekeza hapa Majeshi ya Maji katika nchi wanachama wa maeneo hayo wafanye mafunzo ya mara kwa mara ili waweze kukabiliana na changamoto ya Bahari ya Hindi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya tano, Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania limekuwa likishiriki katika misheni mbalimbali za Kimataifa na kusema kweli jeshi letu limefanya kazi nzuri sana, kwa maana hiyo basi pamoja na umasikini wetu kuna haja sisi kama Taifa tuwaandalie vijana wetu malipo mazuri ya fidia kwa wanajeshi ambao kwa bahati mbaya watapata ulemavu wa kudumu na wale watakaopata vifo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, ninaiomba Wizara ya Ulinzi ishirikiane na Chuo Kikuu cha Taifa Muhimbili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma ili kuandaa vijana wenye taaluma katika kozi nitakazozieleza; kozi za Cyber Security, Space Technology, Military Medicine, Maritime Security pamoja na Mechatronic Engineering ili tupate vijana wenye weledi katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mtakubalina nami kwamba nchi yetu sasa inatekeleza miradi mikuu ya kimkakati Bwawa la Mwalimu Nyerere na reli ya Taifa. Miradi hii inahitaji ulinzi wa hali ya juu sana pamoja na mahitaji ya matengenezo ya kiufundi hasa miradi hii itapokamilika. Kwa maana hiyo basi kuna haja ya kuandaa vijana wetu wa jeshi wenye taaluma kwenye maeneo hayo ili miradi hii ikikamilika na yatakapotokea mahitaji ya matengenezo. Tusikimbilie nje kutafuta wahandisi wa nje, bali jeshi letu litoe msaada wa kiufundi na kitaalamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze mchango wangu kwa maneno ya Marehemu Mzee wetu Mwinyi: “Maisha ya binadamu ni hadithi tu hapa ulimwenguni, ewe ndugu yangu kuwa hadithi nzuri kwa watu watakaosimuliwa habari zako.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona nianze kwa maneno haya ili kumkumbusha Mheshimiwa Waziri juu ya umuhimu wa Kiongozi kuacha alama nzuri katika uongozi wake. Kwa muda mrefu Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukiishauri Serikali kuipima ardhi yote ya Tanzania na kuweka mipango bora ya ardhi. Hakuna asiyejua nchi yetu inakabiliwa na migogoro mingi hasa kati ya wakulima na wafugaji kwa upande mmoja na wananchi na hifadhi za Taifa kwa upande mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wenye mapenzi mema na Taifa hili tulitegemea kwamba tungetafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili ili wananchi wetu wasiumizane na ufumbuzi wa kudumu upo katika kuipima ardhi yote ya Tanzania badala ya kupima kijiji kimoja kimoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2023 Wizara ilipata dola za Kimarekani 150,000,000 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 405. Narudia, shilingi bilioni 405. Niliwahi kuzungumza na mtaalam mmoja wa upimaji akaniambia tunahitaji fedha kama shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuipima ardhi yote ya Tanzania. Sasa tunaweza kupima juu ya utekelezaji wa jambo hili, ni jambo ambalo linawezekana sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa badala ya Wizara kuzitumia fedha hizi, shilingi bilioni 405 kwa ajili ya kuipima ardhi, Wizara inashauriwa na watendaji wake itumie zaidi ya 70% ya fedha za mkopo kwa ajili ya kujenga kumbi za mikutano, kulipa posho za wafanyakazi, kugharamia semina na kununua kompyuta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maoni yangu, jambo hili siyo la busara hata kidogo. Hatuwezi kutumia fedha za mkopo kwa ajili ya shughuli za utawala. Kama Mheshimiwa Waziri ameshauriwa hivyo, nakumbuka maneno ya Mwalimu wangu akisema hivi; “Huu utakuwa ni mfano mzuri kwa ushauri mbaya aliopewa Mheshimiwa Waziri” Nasema, huu utakuwa ni mfano mzuri wa ushauri mbaya aliopewa Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo, naomba autafakari vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri mambo mawili. Jambo la kwanza, naiomba Wizara ipime ardhi yote ya Tanzania na kuainisha maeneo ya mashamba, viwanda, maeneo ya wafugaji na kuweka miji ya kisasa katika kila Mkoa. Tusipolifanya jambo hili sasa, hatutaweza kulifanya miaka 50 inayokuja, kwa sababu ardhi itakuwa imeharibiwa sana kutokana na ujenzi mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naishauri Wizara, tutoe hati tuwamilikishe wananchi wanaostahili ili tukusanye mapato ya kutosha kwa ajili ya kugharamia maendeleo ya Taifa letu na kujenga Taifa linalijitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba Mheshimiwa Waziri na watendaji wako mlisikilize vizuri. Naomba nirudie maneno ya Mzee Mwinyi: “Maisha ya binadamu ni hadithi tu hapa ulimwenguni, ewe ndugu yangu, kuwa hadithi nzuri kwa watu watakaosimuliwa hadithi yako.” Mheshimiwa Waziri nafikiri umenielewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Ununuzi wa Umma wa Mwaka 2023.
MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kutumia nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kutoa mchango wangu. Mimi ni Mjumbe wa Kamati yako ya Bajeti, tumeupitia Muswada ulio mbele yetu kadri ya uwezo wetu, hata hivyo nina maoni katika maeneo machache.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu inatumia zaidi ya asilimia sabini ya fedha za bajeti katika masuala ya manunuzi na ugavi, kusema kweli hiki ni kiwango kikubwa sana cha fedha, kwa mantiki hiyo basi Waheshimiwa Wabunge tunao wajibu wa kutunga sheria iliyo madhubuti ili tuweze kuthibiti vitendo mbalimbali vya rushwa na ukosefu wa maadili.
Mheshimiwa Spika, suala la kuwa na sheria nzuri ni jambo moja na suala la kuwa na sheria inayotekelezeka ni jambo jingine. Ili tuweze kuisimamia sheria hii ipasavyo ninapendekeza Serikali ifanye mambo manne. Jambo la kwanza, Serikali inapaswa kuteua watendaji walio makini na wenye weledi, wenye ujuzi wa kusimamia na kuongoza sekta wanazozisimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile tunahitaji kuwa na watendaji na viongozi wenye hekima, wenye, busara na wenye ujasiri wa kufanya maamuzi magumu. Kwa nini ninayasema haya, nasema haya kwa sababu upo utamaduni ambao tumeuzoea ambao siyo mzuri sisi Watanzania, anapotokea mtendaji au kiongozi akapitisha mradi kwa haraka anatuhumiwa rushwa, anaposhindwa kutekeleza kwa wakati pia tunamtuhumu rushwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa usipokuwa makini unashindwa kujua ufanye kipi kati ya haya mawili. Ucheleweshe ili usituhumiwe rushwa au utekeleze kwa haraka utuhumiwe rushwa. Sasa kwa maoni yangu tunahitaji watu walio makini na ujasiri ili wafanye maamuzi yenye maslahi mkubwa na Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nimezungumzia suala la kuwa na watendaji wenye weledi , napendekeza tuwapeleke watendaji , viongozi wanoongoza mashirika hasa ya kibiashara, tuwapeleke nchi za nje wakajifunze uongozi, wakajifunze utamaduni wa kusimamia na kuendesha mashirika haya kibiashara. Nalisema hili kwa sababu mwaka 1978, aliyekuwa Rais wa China wakati ule marehemu Deng Xiaoping aliwapeleka vijana wa Kichina Marekani wapatao laki moja.
Mheshimiwa Spika, matokeo yake leo tunayaona, China leo wana makampuni yenye uwezo mkubwa sana, wana mashirika ya Serikali yenye uwezo mkubwa sana na wakati hizi kampuni hizi za ujenzi tunazoziona zinakuja katika nchi yetu, kutekeleza tender mbalimbali haya ni makampuni ya Serikali, ninatamani na nchi yangu ifikie huko.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ninaishauri Serikali ianzishe Mfuko Maalumu wa Wawekezaji na Wazalishaji wa Ndani. Hivi sasa tuna mifuko midogo midogo ipatayo 30 Serikalini, ambayo ukiuliza utaambiwa yote inatoa misaada na fedha kwa ajili ya uwekezaji na wajasiriamali wadogo wadogo. Kwa maoni yangu nafikiri hali ya kusimamia miradi mingi kiasi hiki, usimamizi wake unakuwa mgumu sana. Kwa hiyo, napendekeza Serikali iunganishe Mifuko hii yote midogo midogo ili tuwe na mfuko moja imara wenye uwezo wa kutoa misaada na fedha kwa wawekezaji wa Tanzania na vijana ambao wana mawazo mazuri ya kibiashara ili watekeleze miradi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la nne, nashauri wawekezaji wa ndani waunganne ili tuwe na kampuni moja yenye nguvu. Kwa nini ninasema hili? Ukiangalia makapuni yanayokuja kuwekeza katika nchi yetu, wanao uwezo mkubwa sana wa mtaji, wana uwezo mkubwa sana wa teknolojia, kwa kusema kweli kama wawekezaji wa ndani kama hawakuungana pamoja hawawezi kushindana na makampuni yenye uwezo mkubwa kiasi hiki. Wakati mwingine makumpuni haya yanapata msaada mkubwa sana kutoka Serikali zao. Kwa hiyo, njia pekee ni kuungana tu, kama Waswahili wasemavyo umoja ni nguvu utengano ni udhaifu.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, tusipofanya hivyo tutaendelea tu kulalamika kwamba Watanzania wawekezaji wa ndani hawapewi msaada unaostahiki na baada ya mwaka moja nina hakika, tutarudi hapa kusema Sheria hii mpya ya Manunuzi ina kasoro ina udhaifu, kumbe tatizo si sheria, tatizo ni weledi, tatizo ni maadili, tatizo ni utashi wa kusimamia yale tunayoyapanga, ndiyo maana nasema sheria nzuri tunaipitisha lakini tuende zaidi kuliko sheria ilivyo, vinginevyo tutaendelea tu kulalamika kwamba sheria haitekelezwi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)