Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Abdallah Majurah Bulembo (12 total)

MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Najielekeza hapo kwenye wavuvi. Kwa kuwa wavuvi katika Ziwa Victoria nyavu wanazotumia wanazinunua madukani na Serikali ipo na bandari ipo; Serikali ituambie ni lini itayafunga yale maduka yanayouza nyavu zisizotakiwa kuvuliwa na lini itaweza kuleta sheria hapa Bungeni kuzuia viwanda vinavyozalisha nyavu zinazosababishia wavuvi hasara? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyekiti wa Jumuiya anapomuuliza mdhamini wake inakuwa shida kidogo. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kupambana na uvuvi haramu kwa ujumla, Serikali sasa hivi inachokifanya, inashambulia maeneo yote, yaani hatuendi kwa wavuvi peke yao, tunamchukulia hatua yeyote aliyeko katika ule mnyororo wa thamani wa uvuvi kwa maana kwamba mzalishaji wa zana haramu, msambazaji, mtunzaji, mhifadhi na yeyote. Kwa hiyo, anayeuza akipatikana anachukuliwa hatua kama mhalifu mwingine yeyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, tumekwenda hatua zaidi hata ya kudhibiti uingizwaji wa nyavu nchini, acha wenye viwanda ambao tunawakagua mara kwa mara na kwa kweli mwenye kiwanda hapa nchini akipatikana anazalisha nyavu zisizoruhusiwa tunachukua leseni yake na kufunga kiwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunakagua hata uingizaji, kwa sababu wako watu wanaagiza nyavu kutoka nchi za nje kwa kisingizio kwamba zinapita Tanzania zinakwenda nchi nyingine, lakini baada ya kuwa wamesha-clear pale bandarini, wanafanya maarifa hizi nyavu zikifika mpakani Tunduma au pengine, zinarudi nchini. Kwa hiyo, hata hawa sasa hivi tunashughulika nao, tunahakikisha wanatoka nje ya mipaka yetu na hizo nyavu zao. Tukimkamata tunamchukulia hatua kama sheria inavyotaka.(Makofi)
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kuwa kituo cha Mbezi Luis kimeshapata mwekezaji LAPF, Serikali inatuambiaje kuhusu kituo cha Boko na cha Temeke, wamewatafuta akina nani watakaosaidia kujenga vituo hivi kwa haraka ili kuondoa msongamano Dar es Salaam? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bulembo, Mbunge Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishukuru sana
swali la Mheshimiwa Mbunge na ndiyo maana nimesema Mbunge Maalum kwa sababu ana hadhi maalum katika nchi hii kutokana na nafasi zake alizokuwa nazo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa hivi Serikali tumepata wadau wetu wa LAPF tumeanza na kituo kile lakini hata hivyo tunaenda kutafuta wadau wengine kwa ajili ya kujenga kituo kile katika eneo la Boko na kituo cha Kanda ya Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, niwaelekeze wenzetu wa Jiji la Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam na wadau wengine hasa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, ikiwezekana wakae na Halmashauri ya Mkuranga, kwa sababu eneo la kimkakati tayari lipo ambalo halina haja ya kulipa fidia kuona ni jinsi gani tuta-fast track hiki kituo ambacho tunaweza tukakijenga eneo la Mkuranga kwa watu wa Kusini ili wakapata unafuu zaidi.
Kwa hiyo, tunachukua mambo yote haya kwa kushirikisha wadau mbalimbali lengo ikiwa ni kujenga vituo ambavyo vitasaidia suala la usafiri katika nchi yetu.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa kama alivyosema muuliza swali wa kwanza TBC wameweza kupata shilingi bilioni tatu, naomba kumuuliza Mheshimiwa mjibu swali.
Ni lini Serikali itaweza kununua vifaa vidogo TVU au AVIWEST vifaa vile tukio linapotokea wanaweka pale pale tunakwenda kwenye breaking news, lakini TBC leo kwenye breaking news wanakodi vifaa, kifaa kimoja kinanunuliwa kama shilingi milioni 50 au shilingi milioni 60, hii ni aibu katika Serikali yetu.
Serikali waniambie ni lini wataweza kununua vifaa hivyo na kuvisambaza Tanzania kwa sababu masafa marefu hayasikiki. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana, kama nimempata vizuri Mheshimiwa Mbunge hii TVU ni kwa upande wa televisheni na ambapo tayari TBC imeshanunua vifaa hivi, ahsante.(Makofi)
MHE. ABDALLA M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kabla sijauliza swali, naomba unipe nafasi kidogo niseme maneno mawili kidogo.
Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Silinde kama ameona mali za Chama cha Mapinduzi zinaweza kuja kuombwa Bungeni, nafikiri ni dalili nzuri kwamba naye anaelekea kuja CCM, karibu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu linasema hivi, maombi haya yanayoletwa kwa ajili ya Shule ya Jumuiya ya Wazazi, Wizara naomba iniambie; je, kwa nini msishirikiane na Mbunge mkaimarisha shule nzuri ya Julius Nyerere ambayo inaonekana imeharibika, haifai, haina huduma nzuri, mpaka mwende kutafuta mali za CCM? (Kicheko/Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nadhani Mheshimiwa Alhaji Bulembo alikuwa anatoa ushauri na mimi napenda kumpongeza sana kwa juhudi kubwa anayofanya katika shughuli zake.
Mheshimiwa Spika, nadhani ushauri huu kama Serikali tumeupokea, kwa sababu Mheshimiwa Alhaji Bulembo wewe ni mlezi wa watoto na ndiyo maana umeamua kujenga shule hizi na kuzisimamia. Kwa hiyo, tutakachokifanya ni kuboresha maeneo mbalimbali ili watoto wetu waweze kusoma kwa kadiri iwezekanavyo.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Waziri kwa sababu nchi hii ina tatizo kubwa sana la sukari na katika Mkoa wa Kagera umesema tuanzishe viwanda vya maziwa, ukitoka pale Bulembo kwenda Busheregenyi, kwenda Msira kwenda Rugongo, kwenda sehemu za huko kama unaenda Kasharu; maeneo yale ni maeneo ya tingatinga kuweza kulima mashamba ya miwa na watu wajasiliamali wadogo wakaanzisha viwanda vidogo vidogo.
Ni lini unaenda Misenyi kukaa na wananchi? Ofisi yako ikawaambie kwa sababu uwezekano wa kupatikana miwa upo ili waweze kuanzisha viwanda vidogo vidogo?(Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, namsukuru Mheshimiwa Bulembo. Hilo la kwenda Busheregenyi kwa bibi zangu halina mjadala, lakini napenda nikueleze kwamba ninaye mwekezaji sasa katika maeneo hayo ambaye anataka kuingia ubia na Jeshi la Magereza sehemu Kitengule, kushirikiana na Jeshi la Magereza kutumia uoto ule kuweza kulima miwa ya kuzalisha sukari. Kwa hiyo, tutalijadili mimi na pacha wangu, yule mwekezaji yupo serious anataka kuwekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatafuta wawekezaji lakini Waheshimiwa Wabunge muelewe, mwekezaji humleti leo akaanza leo. Mkijua huo mchakato wa kuweza kuchukua ardhi mpaka kuzalisha, ndiyo maana nikaanzisha ule utafiti wa wepesi wa kufanya biashara. Ndiyo mambo ambayo tunayarekebisha na tutayarekebisha kusudi angalau wawekezaji wachukue muda kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala na Mheshimiwa Bulembo ni kwamba Busheregenyi mnaweza kupata huduma Kagera Sugar na mkapata huduma Magereza watakapokuwa wameanzisha kiwanda wale wawekezaji.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa watu wanaokwenda kwenye Magereza ni wahalifu na huwa wamehukumiwa, naomba Wizara ya Mambo ya Ndani iniambie na itoe kauli hapa, ni lini Gereza la Muleba litaenda kuzungushiwa fensi, maana yake leo Gereza la Muleba lina uzio kwa maana wafungwa wakiamua kuondoka leo, kesho wanaondoka, mtawakamata wale viongozi bure, sasa nataka commitment ya Serikali ni lini itafanya emergence ya kwenda Muleba kuweka uzio wa Magereza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, ni kweli Gereza la Muleba linahitaji kuwekewa uzio, tunatambua na tumejipanga kwamba wakati wowote ambapo tutakamilisha kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa uzio huo tutafanya hiyo kazi. Jambo hilo tunalitambua na lipo katika vipaumbele vyetu.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na swali la msingi kwa kuwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi imesema watoto wote wasome bure, katika jimbo la Kaliua shule ya msingi Ushokola walimu wanafundishia nje na walimu hawatoshi. Ni lini Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi itaona hili tatizo la Kaliua kuongezea walimu wa shule za msingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Bulembo, Senior MP, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la bwana Bulembo bahati nzuri siku nne zilizopita nilikuwa na viongozi kutoka katika Wilaya ya Kaliua, walifika ofisini kwangu pale lakini ili kujadili ajenda za kimaendeleo. Ninasema Senior MP kwa sababu mwanzo alikuwepo na hivi sasa mnajua kazi zake kubwa anazozifanya katika nchi hii na juzi alikuwepo kule Mkoa wa Tabora nadhani ndio maana ameweza kufanya verfication ya tatizo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kikubwa zaidi nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge; nilikubaliana na viongozi waliotoka Kaliua kwamba nitafika Kaliua. Naomba nikuhakikishie kwamba nitatembelea shule ile ili kubaini mahitaji halisi. Hata hivyo Serikali tutaweka mpango, namna ya kufanya ili tuweze kujenga miundombinu na kuwapatia walimu ili vile vile wananchi wa eneo lile wapate fursa ya kusema tulitembelewa na mjumbe wa Kamati Kuu ambaye anasimamia suala zima la utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Vicheko/Makofi)
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa kama alivyosema muuliza swali wa kwanza TBC wameweza kupata shilingi bilioni tatu, naomba kumuuliza Mheshimiwa mjibu swali.
Ni lini Serikali itaweza kununua vifaa vidogo TVU au AVIWEST vifaa vile tukio linapotokea wanaweka pale pale tunakwenda kwenye breaking news, lakini TBC leo kwenye breaking news wanakodi vifaa, kifaa kimoja kinanunuliwa kama shilingi milioni 50 au shilingi milioni 60, hii ni aibu katika Serikali yetu.
Serikali waniambie ni lini wataweza kununua vifaa hivyo na kuvisambaza Tanzania kwa sababu masafa marefu hayasikiki. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana, kama nimempata vizuri Mheshimiwa Mbunge hii TVU ni kwa upande wa televisheni na ambapo tayari TBC imeshanunua vifaa hivi, ahsante.(Makofi)
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kama alivyojibu mjibu swali, kwa kuwa hawa Wazee wa Mahakama wanalipwa nafikiri Sh.5,000/= au Sh.7000/=. Je, huo mchakato wanaoufanya wanajiandaa kuongeza kiwango cha hawa Wazee kwa sababu ni kazi ya hiyari? Isije kuwa wanashindwa kwenda Mahakamani ndiyo maana haki inachelewa kupatikana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema hapa Mheshimiwa Bulembo kwamba tunachokifanya ni kufanya tathmini ya kina jinsi gani tutafanya kuhakikisha wananchi wanapata haki. Siwezi kusema kwamba kiwango hiki kitaongezeka kwa sababu kuna mambo mengi ndani yake yanaendelea hapa, isipokuwa kwamba tuamini Serikali inafanya kazi na mwisho wa siku ni kwamba miongoni mwa kuondoa kero nyingi za wananchi ni kushughulikia Mabaraza ya Kata, ili kulinda haki za watu kwa kuyashughulikia na kuyaunda vizuri Mabaraza ya Kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali inafanya kazi hii hatima yake itakapofika, basi tutapata mwelekeo maalum wa Serikali wa jinsi gani jambo hili tunaenda kuli- handle vizuri kwa maslahi mapana ya wananchi.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Dar es Salaam pale kwenye kulaza bomba la kutoka Bagamoyo kuja Chuo Kikuu kuna watu walivunjiwa na watu wengine wakakataa wakapelekwa mahakamani, walipopelekwa mahakani wameshindwa mpaka leo wanasema wanalindwa na wakubwa hawataki kuvunja nataka Wizara iniambie wanavunjiwa lini ili Dar es Salaam tupatae maji Chuo Kikuu? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanayo taarifa kwa sababu wameshapewa notice kwamba wanavunjiwa, kwa hiyo ni wakati wowote hatua za kuvunja zile nyumba zitafanyika.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kutokana na swali la msingi, naomba kuuliza Wizara ya Kilimo hapo. Kwa kuwa wakulima wa kahawa ni sawasawa na wakulima wa pamba. Wakulima wa pamba wamewaruhusu waliofanya biashara ya mkataba waweze kuendelea na shughuli hiyo, lakini wakulima wa kahawa katika nchi wa mkataba hawazidi watano mpaka sita. Kwa nini Wizara inakuwa double standard, msimu umeanza sasa hivi wiki ya pili watu hawa hawataki kuwapa kibali cha kuweza kukusanya kahawa kwa sababu ni biashara yao. Naomba tujue hawa haki yao wanaipata wapi?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, utaratibu tuliouweka sasa hivi lengo lake la kwanza ni kuhakikisha kwamba wakulima wanapata malipo stahiki kwa jasho lao. Mfumo tuliokuwa nao sasa hivi kwa kiwango kikubwa ulikuwa hautoi malipo stahiki kwa jasho la wakulima na moja ya njia zilizotumika kuwanyima haki wakulima ilikuwa ni mfumo wa kununua kahawa kwa kulipa advance kutoka kwa wafanyabiashara na hasa katika Mkoa ambako Mheshimiwa Bulembo anatoka maarufu kwa jina la Butura. Ili kukabiliana na Butura, lazima kuweka mfumo unaofafana maeneo yote.
Mheshimiwa Spika, jana nilisema hapa ndani wakati nachangia hoja ya Bajeti Kuu ya Serikali kwamba pale ambapo mikataba hiyo iliingiwa officially kwamba kuna mkataba na mamlaka za Serikali zinatambua mikataba hiyo kama ilivyo kwenye pamba, pamba mtu haingii mkataba mtu na mtu mmoja, mikataba hiyo inaingiwa kupitia mamlaka za Serikali, kama wako wakulima wa kahawa ambao wameingia mikataba kwa njia hiyo, nilielekeza kwamba wapeleke habari hiyo haraka Bodi ya Kahawa ili waweze kupata utaratibu wa kuuza kahawa kwa mtu waliyeingia naye mkataba.
Mheshimiwa Spika, ile mikataba ya kuingia kienyeji ndiyo utaratibu uliokuwa unasababisha watu kupoteza haki yao na jasho lao kwa kuuza kwa watu ambao wanawapa malipo kidogo kwa kahawa ya bei kubwa.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kama alivyosema Ranchi ya Missenyi ni ya mfano na huo mfano ni kutokuwa na mifugo.
Swali langu la msingi sababu inayosababisha Ranchi ya Missenyi isiwe na mifugo ni kwa sababu zile blocks mmewapa watu ambao siyo wafugaji wa mbali, wao kazi yao ni kukodisha. Je, kwa utaratibu mpya mlionao mtawajali wakazi wa eneo la Misenyi, kwamba ndio wapewe maeneo hayo ya ranchi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli kwamba palikuwa na kasoro kadha wa kadha ambazo zilisababishwa na kuwapatia watu ambao si wafugaji na matokeo yake wakawa wanakwenda kuwakodisha watu wengine. Hivi sasa baada ya kuingia sisi tumekubaliana kufanya mabadiliko na ndiyo maana tumezirudisha ranchi zile Wizarani kwa ajili ya kuanza kugawa upya na tumeanza kazi hiyo ya kupokea maombi, kuyapitia na kujiridhisha kwamba huyu kweli ni mfugaji na tuweze kumpatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa faida tu ni kwamba pamoja na kufanya hivyo, tumekubaliana kwamba hatupo tayari kuona ng’ombe yoyote aliyepo katika maeneo yanayozunguka ranchi zetu anakufa kwa sababu ya kukosa malisho na maji, hivyo tumekubaliana ya kwamba wafugaji wanaozunguka pamoja na wafugaji wa Jimbo la Mheshimiwa Dkt. Diodorus Kamala waweze kulipia kwa muda wa miezi mitatu. Ng’ombe mmoja analipia shilingi 10,000 anaingia katika ranchi, anapewa eneo, ananenepeshwa na akimaliza anatoka badala ya ile kuendelea kuwapga faini kwa sababu ya kuingia katika eneo la ranchi. Hivyo, tumekubaliana kurasimisha hatua hizi.