Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Anne Kilango Malecela (7 total)

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika,
nashukuru. Pamoja na majibu ya Serikali, lakini naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, kwa mfano tu Wilaya ya Same mwaka 2016, wasichana wadogo waliopata mimba na kufukuzwa shule ni 64 ambao hawa ni wa O-Level ikiwa ina maana mimba hizi ni za utotoni. Mwaka huu 2017 mwezi wa Kwanza, wa Pili na wa Tatu, miezi mitatu tu wamefukuzwa wanafunzi wa shule kwa mimba za utotoni 42 na kati ya hao akiwepo mtoto wa darasa la sita ikiwa ina maana ni kati ya miaka 12 mpaka 14.
Mheshimiwa Spika, hivi Serikali haioni kwamba kuna umuhimu mkubwa sana wa kuwa na mitaala ambayo itawafundisha watoto hawa kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari, ambayo itawafanya waelewe athari za kupata mimba utotoni ambazo ni muhimu sana? Mitaala hii itaweza kuwasaidia watoto hawa kujitambua na kufahamu umuhimu wa kutokukubali kupata mimba utotoni.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali
inafanya jitihada kubwa sana kupambana na madawa ya kulevya sasa hivi na naiunga mkono, nai-support na tunashukuru sana. Jitihada hii ni kwa sababu Serikali imeona athari hasa inayowapata vijana wa kiume na wa kike kwa
kutumia madawa ya kulevya, lakini watoto wa kike
wanapata athari mara mbili, kwanza athari ya madawa ya kulevya na mimba za utotoni.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuleta mkakati
mkubwa kama ule wa madawa ya kulevya ili tupunguze athari za mimba za utotoni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali linalohusiana na masuala ya mitaala kama ifuatavyo:-
Kimsingi katika elimu ya Msingi na elimu ya Sekondari wanafunzi wanapewa maarifa kuhusiana na masuala ya Kibaiolojia na sayansi yanayohusisha hata masuala ya maumbile ya miili yao, kwa hiyo kimsingi suala hilo linafanyika labda tunaloweza kuahidi hapa ni kutoa msisitizo wa kuona kwamba wanafunzi hao wanapewa dozi zaidi hasa kwa kuwachukua hawa watoto wa kike na kuwapa elimu ya ziada kwa ajili ya kuwanusuru katika mazingira hayo.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza tunao mpango wa kudhibiti ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambao ni jumuishi kwa sekta takribani tisa za Serikali yetu na mpango huu umezinduliwa mwaka jana mwezi Desemba na Mawaziri tisa wa Serikali hii ya Awamu ya Tano na Mawaziri wameonesha comittment kubwa sana ya kuweka utaratibu
wa kumlinda mtoto wa kike dhidi ya ndoa za utotoni lakini pia mimba za utotoni na vitendo vyote vinavyohusu ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike.
Mheshimiwa Spika, tunachokihitaji kwa sasa ni
kupewa fedha kwa ajili ya kutekeleza mpango huo na kwenye mpango huu tunalenga kupunguza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa kiwango cha asilimia isiyopungua 50 kufikia mwaka 2022. Kwa hivyo, mpango huu kama tutapangiwa fedha, tunapanga kuanza kuutekeleza mwezi Julai mwaka 2017. Kwa hivyo, mpango tunao pia tuna mikakati mbalimbali inayoendelea kama ya elimu ya malezi chanya (Positive Parenting Education) kwa watoto ambao umefanyika kwenye Wilaya 72 za Nchi yetu
na tunawalenga zaidi viongozi wa kimila, wazazi pamoja na watu mashuhuri wenye kufanya maamuzi kwenye jamii.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, napata taabu kidogo maana yake na mimi ni mwalimu, iwapo Serikali tutaacha kwenda kwenye specialization na tukafanya watoto wote wakasoma sayansi. Mimi nina wasiwasi kwamba tutapata wanasayansi wabovu zaidi.
Je, Serikali haioni kwamba specialization ni important kuliko ambavyo sasa tunakwenda kumfanya kila mtoto asome sayansi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, specialization inaanza na msingi na niseme tu kwamba tunawahitaji wataalam wa aina tofauti tofauti. Kuna hao specialization ambao wanakuwa wamekuwa vertical yaani anajikita katika eneo moja pia tunawahitaji wale ambao wanakua kimapana (wide knowledgeable people) ambao wanaweza wakaoanisha upande huu na upande huu. Kwa hiyo, katika ku-specialize kupo lakini lazima kuwe na msingi ni wa eneo gani ambalo huyu mtu atafanya specialization. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi. Hivi Serikali ina mpango gani mahsusi wa kuwaangalia na wanawake wa vijijini, kwa sababu mipango mingine yote imefeli kwa wanawake wa vijijini kupata mikopo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa yeye pia ni Kada wa Chama cha Mapinduzi, naomba nimkumbushe kwamba kwenye Ilani ya Uchaguzi pamewekwa maelekezo kwamba kila Halmashauri nchini itenge asilimia tano ya bajeti yake kutoka kwenye Own Source kwa ajili ya kuwakopesha akinamama, huu Mfuko unajulikana kama Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo wanawake wote, wakiwemo wanawake wa vijijini, hata wale anaowapenda sana wa kule Same, nao wanaweza wakatumia fursa hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi yetu ssi Waheshimiwa Wabunge ni kuingia kwenye vikao vya Halmashauri wakati tunapanga bajeti na kushiriki kuhakikisha asilimia tano ya akinamama inatengwa, asilimia tano ya vijana inatengwa. Pia tusiishie hapo, pesa zinapopatikana tuziweke pembeni pesa za Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Wabunge ni Wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ambayo huwa inahusika kugawa hizi pesa kwenye vikundi mbalimbali. Kwa hiyo baada ya kuwahamasisha wananchi wetu waombe mikopo hii ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, pia tushiriki kwenye vikao vile vya Halmashauri ambavyo vinagawa pesa hizi kwenye vikundi mbalimbali vya akina mama ili ziwafikie kwa uhakika wananchi hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kupitia Benki ya Wanawake tunatengeneza mifumo sasa ambayo itawafikia Watanzania popote pale walipo, hata wa kijijini, sasa hivi matumizi ya simu ni kwa zaidi ya watu milioni 36 hapa nchini, kwa hiyo njia hii itawafikia watu wengi zaidi hapa nchini kwetu. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu wananchi wa Madaba wameonesha kuhamasika sana kulima tangawizi, hata mimi ninalima tangawizi Madaba. Je, Serikali haioni kwamba kiwanda cha Mamba Miamba ambacho kitakuwa tayari by March next year, kitahitaji tangawizi nyingi sana siyo kutoka Same tu pamoja na Madaba.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapatia wananchi wa Madaba ardhi ya uhakika ili walime tangawizi kwa wingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuchukue kilio cha mama vilevile kama kilio cha Mheshimiwa Joseph Mhagama. Serikali inaona umuhimu huo na tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha mambo pale yanakaa sawasawa wananchi walime tangawizi waje, kulisha katika kiwanda cha Mama Anne Kilango Malecela. (Makofi
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshmiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa masoko ya nje yanatawaliwa sana na ubora wa mazao na kwa kuwa wanunuzi wa tangawizi kule nje wanapenda sana organic ginger. Sasa Serikali ina mpango gani wa kupeleka elimu kwenye zile sehemu ambazo zinalima sana tangawizi kama vile Mkoa wa Kilimanjaro, Mkoa wa Kigoma, Mkoa wa Mbeya na Mkoa wa Ruvuma?
Mheshimiwa Spika swali la pili, kwa kuwa Kiwanda cha Tangawizi cha Mamba Miamba kilichopo Wilayani Same kinategemea kuanza kusindika tangawizi ya kupeleka nje ya nchi katikati ya mwaka 2018.
Je, Serikali itatumia njia gani kuwafanya wananchi ambao wamekata tamaa kulima tangawizi kutokana na bei kushuka sana ili waendelee kulima tangawizi kwa sababu kiwanda hiki cha Mamba Miamba kitahitaji malighafi kwa wingi? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Spika, kwa idhini yako napenda nichukue fursa hii kumtambua Mama Malecela kama Malkia wa Tangawizi. Suala la tangawizi amelifanyia kazi sana. Nichukue fursa hii kushukuru Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambayo ameshughulikia pacha wangu, zimetengwa pesa nzuri zaidi ya shilingi bilioni
• kusudi hicho kiwanda kiwe na hadhi ya Kimataifa, kizingatie ubora kama nilivyoeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu maswali mawili uliyoniuliza, moja la ubora, Wizara yangu inayosimamia SIDO kwa kutambua suala la viwango, maeneo yote ninaojenga sasa katika mikoa yote mipya tunajenga ofisi za SIDO, sheli, maabara, mahali pa kuchakatia chakula kwa viwango vitakuwa ni kipaumbele; Katavi, Rukwa, Geita, Simiyu ndiyo nakwenda kuanza nalo na pesa tayari ninazo kama nilivyoeleza juzi. Kwa hiyo, nitawafundisha wananchi hasa akina mama kuzalisha vyakula kwa viwango vya kuuza Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa suala la pili kwamba tutafanyaje, ndiyo tangawizi ilikuwa inauzwa Sh.3,500 najua leo bei imeshuka, sawa sababu mojawapo ni muanguko wa bei za bidhaa, commodity price duniani zote zime-dive. Tutafanya nini?
Kazi ninayofanya sasa ni kutafuta masoko makubwa, masoko mengi ya Kimataifa ile demand pool iwawezeshe wananchi wetu waweze kuuza zaidi lakini zaidi kupitia ESDP II tutaongeza tija (productivity) katika uzalishaji kusudi watu walime sehemu kubwa kwa gharama ndogo ile productivity iweze kupeleka hiyo tangawizi. Kwa sababu kiwanda chako hakina mfano, tangawizi yote itakwenda Mamba, ichakatwe, tupeleke Bandari ya Tanga iende duniani kuuzwa.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Tanzania, wanajenga sana zahanati, madarasana mifereji.
Je, Serikali haiwezi kuwa na mpango Maalum kwamba wananchi wakijenga kiasi fulani Serikali nayo inakuwa na kiasi fulani inachukua kumalizia kwa sababu watanzania wanajenga mno? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ni kama amerudia yale ambayo nilikuwa nawaasa Waheshimiwa Wabunge, kwamba hakika kwa kushirikishana wananchi pamoja na Serikali kwa pamoja tunafika na ndiyo maana nikatoa mfano nilivyokuwa nimeenda Moshi Vijijini, Kituo cha Afya ya Kiaseni nimekuta wananchi wamejitoa na Serikali nayo ikapeleka nguvu, hakika tukishirikishana tutaweza kutoka. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi. Kwa kuwa mwaka 2015 nilipokuwa Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki nilitoa ufadhili wa gari la golisi kwenye Kituo cha Kata ya Maore kwa ajili ya Jimbo la Same Mashariki; nina uhakika Serikali inalifahamu hilo. Kwa kuwa, lile gari sasa halina matairi, linahitaji kufanyiwa maintainance kubwa. Je, Serikali mnatoa ahadi gani leo hapa ili wananchi wa Same Mashariki wasikie?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mhesimiwa Mbunge Anne Kilango Malecela kwa kusaidia kazi za Ofisi ya Polisi katika Jimbo la Same Mashariki kuweza kufanya kazi na wanakukumbuka sana. Nimefika mwenyewe Same nimeona wakikukumbuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Serikali inatambua jitihada alizofanya Mheshimiwa Mbunge na tutaongea na Kamanda wa Polisi wa Mkoa ili tuweze kuona namna ambavyo tunaweza tukaunga mkono jitihada hizo ambazo Mheshimiwa Mbunge ulizifanya. Hata hivyo niendelee kukuomba uendelee kuwakumbuka wananchi wa Same kwani wanakukumbuka sana ili vitu kama vile matairi wasiendelee kuvikosa, waendelee kupata kama ulivyokuwa unafanya.