Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (26 total)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nichukue fursa hii kuzishukuru sana Kamati zote kwa taarifa nzuri walizoziwasilisha. Jukumu letu sisi ni kupokea mapendekezo yote yaliyotolewa na kamati hizo pamoja na Wabunge waliochangia.

Nichukue fursa hii kuishukuru sana Kamati ya Katiba na Sheria kwa mchango mkubwa iliyoutoa hasa wakati tulipokuwa tunakabiliwa na kupitisha sheria zile muhimu kwa ajili wa ulinzi wa rasilimali na mali zetu za asili yaani sheria ya The Natural Wealth and Resources Permanent and Sovereignity Act 2017Act No. 5 of 2017, The Natural Wealth and Resouces Contracts (Review and Re-Negotiation of Unconscionable Terms) Act No. 6 of 2017 na The Written Laws Miscellaneous Amendments Act No. 7 of 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wa Kamati ulikuwa mkubwa sana na ndiyo maana kama wote tunakumbuka schedule of amendment iliyoletwa na Kamati ilisaidia sana kuboresha sheria hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo nishukuru sana mchango uliotolewa kuhusu utungaji wa kanuni. Ni kweli kabisa sheria zikitungwa zinahitaji kanuni ili ziweze kutekelezwa na moja ya sheria ambayo ilihitaji kanuni hizo ni mabadiliko ya Sheria ya Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuhimiza ukamilishaji wa Kanuni za Madini na kazi hiyo ilikamilika na nimshukuru sana Waziri wa Madini ingawa alikuwa katika likizo ya uzazi yaani maternity leave aliweza kupata nafasi ya kurudi na kuweza kuzitia saini kanuni zote tarehe 9 Januari, 2018.

Pia nimshukuru sana Katibu Mkuu Kiongozi ambaye na yeye kwa mujibu mamlaka aliyopewa chini ya Sheria ya Executive Urgency aliweza kutia sahihi amri mbili za kufuta baadhi ya mamlaka ambazo zimeondolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikubaliane na Mheshimiwa Daniel Mtuka, Mbunge wa Manyoni Mashariki kwamba kuna umuhimu wa kuimarisha ubora wa utungaji wa sheria ndogo na utungaji wa kanuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamini kabisa mabadiliko yaliyoanza kufanyika katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yataongeza ufanisi katika utungaji wa sheria na kanuni ndogo ndogo. Ni eneo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi zaidi na nina imani chini ya Mwanasheria Mkuu mpya wa Serikali Dkt. Adelardius Lubango Kilangi tutaongeza ufanisi wa kupitia sheria na kuzifanya ziwe bora zaidi na baada ya muda mfupi mabadiliko zaidi katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yatafanyika ili kuhimiza na kuimarisha ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia nafasi hii kusema kwamba inapokuja kwenye maswali ambayo yameulizwa na Ndugu Ayoub Jaku namwomba tu kwamba maswali yake yote hayo aliyoyauliza yaje Bungeni kwa kanuni za kawaida za Bunge, kwa sababu hapa tunajielekeza katika taarifa iliyotolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia nafasi hii kuishukuru Kamati kwa maelezo iliyotoa kuhusu kazi kubwa inayofanywa na mahakama. Ni kweli kabisa mahakama zinakabiliwa na upungufu wa Mahakimu na Majaji lakini Serikali iko katika hatua ya kukamilisha upekuzi wa wale wote wamependekezwa kuwa Majaji au Mahakimu ili kuhakikisha kwamba tuna Majaji au Mahakimu ambao hawana tuhuma za ufisadi, hawana tuhuma za rushwa, lakini pia ni waadilifu na wanaoweza kutekeleza majukumu yanayotakiwa kwa ufanisi na weledi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa nieleze kuhusu suala la makosa mbalimbali na faini kuwa chini. Hiyo ni moja ya changamoto na ambazo zinafanyiwa kazi na Tume ya Kurekebisha Sheria, ni kuona ni mfumo gani utumike utakaotusaidia kuhakikisha kwamba faini haziwi chini baada ya muda mfupi kutokana na thamani ya fedha ya Tanzania kushuka. Kwa hiyo, maeneo yote hayo yanafanyiwa kazi ili uhakikisha kwamba faini zitaendana na hali ya mabadiliko ya kiuchumi nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la utawala wa sheria na utalawa bora. Ningependa kuwahakikishia Watanzania wote kwamba taasisi zote na mihimili yote inayohusika na utawala bora inafanya kazi inavyotakiwa. Moja ni Mahakama za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwepo Mahakama ya Rufani ina uhuru kamili, inafanya maamuzi na maamuzi yake yanaheshimiwa na nchi. Kwa hiyo Watanzania wowote au wananchi wowote ambao wanaona haki zao zimeminywa wanao uhuru kamili chini ya Katiba kwenda mahakamani na mashauri yao kuamuliwa na daima Serikali imekuwa inaheshimi maamuzi ya mahakama kwa jinsi yanavyokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imekuwa inafanya kazi nzuri ya kuelekeza maeneo gani ya utawala bora na haki za binadamu yafanyiwe maboresho ili kuboresha zaidi. Kwa hiyo, naishukuru sana Kamati ya Katiba na Sheria kwa maoni na miongozo mbalimbali waliotoa kusaidia kuboresha hali hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, duniani kote daima utawala bora, utawala wa sheria na demokrasia ni mambo yanayohitaji daima kufanyiwa kazi ili kuyaboresha. Leo nimesafiri na Balozi wa nchi moja ya Ulaya na nilimkumbusha kwamba mpaka leo tunavyozunguza nchi ya Switzerland katika baadhi ya maeneo ya nchi ya Switzerland wanawake hawaruhusiwi kupiga kura na hii ni nchi ya Switzerland, lakini mpaka leo wanawake hawaruhusiwi kupiga kura, wanaopiga kura ni wanaume tu. Nchi za Ulaya mpaka leo kwa daraja lile lile na cheo kile kile mwanamke analipwa chini kuliko mwanaume.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Wabunge, Wabunge Wanawake wanalipwa chini kuliko Wabunge Wanaume sihalalishi, lakini nataka nieleze kwamba kila nchi ina changamoto. Wabunge Wanawake hawa wangekuwa kwenye baadhi ya nchi za Ulaya wangepokea mshahara mdogo kuliko Wabunge Wanaume.

Kwa hiyo, changamoto hizi za kuboresha demokrasia daima zipo na Taifa lolote haliwezi kusema limekamilika ni lazima liendelee kuboreshwa. Kwa maana hiyo tunapokea michango yote iliyotolewa yenye lengo la kuboresha demokrasia yetu na haki za binadamu ili tuweze kuwa na hali bora zaidi bila kubeza hatua kubwa ambayo Tanzania imepiga katika demokrasia, Tanzania imepiga katika haki za binadamu, Tanzania imepiga katika usawa wa wanaume na wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo naomba pia kuunga mkono hoja iliyotolewa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Katiba na Sheria
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kwa unyenyekevu mkubwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu-Wataala kwa kuniwezesha leo asubuhi kuwasilisha Mpango wa Makadirio ya Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kwa namna ya pekee namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha Waheshimiwa Wabunge kushiriki na kuchangia hotuba ya Wizara yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee nachukue fursa hii kukushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi ya kuwasilisha hotuba yangu na kwa umahiri wako katika uendeshaji wa Vikao vya Bunge na kwa kusimamia mjadala huu vizuri. Nimshukuru Mheshimiwa Dkt. Adeladus Lubango Kilangi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ushirikiano ambao ananipa katika kutekeleza majukumu yangu na kipekee kwa kuungana na mimi katika kujibu baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa mjadala wa hotuba yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine naishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa maoni na ushauri ambao wanaipatia Wizara na Taasisi zake katika kutekeleza majukumu yetu vizuri. Napenda nikuhakikishie wewe binafsi, Kamati yako na Waheshimiwa Wabunge wote kuwa tumepokea kwa unyenyekevu na shukrani maoni, hoja na ushauri mliotupa wakati wa mjadala wa bajeti yetu. Kwa niaba ya Wizara tunaahidi kuyafanyia kazi masuala yote yaliyojitokeza katika mjadala huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mjadala wa hotuba aliyoitoa Mheshimiwa Waziri Mkuu na katika mjadala wa hotuba ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Waheshimiwa Wabunge walitoa hoja mbalimbali ambazo kwa namna moja au nyingine ziligusa Wizara yangu na Sekta ya Sheria kwa ujumla. Tumezipokea hoja zote zilizotolewa na tunaahidi kuzifanyia kazi na kuleta mrejesho wake Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kuongea na wale waliochangia kwa maandishi na kuichambua bajeti yetu kwa kina. Michango yenu ni nyenzo muhimu ya kuboresha utendaji kazi wa Wizara na taasisi zake ili sekta ya sheria ikidhi matarajio ya Watanzania na iwe na mchango chanya katika maendeleo yao ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla wa Wabunge 40 wamechangia hotuba yetu, ambapo Wabunge 34 wamechangia kwa maandishi na Waheshimiwa Wabunge sita wamechangia kwa kuzungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa uniruhusu nianze kujibu hoja mbalimbali zilizotolewa na nitoe indhari tu kwamba hoja zote nyingine ambazo sitazijibu zitajibiwa kwa maandishi. Nianze na hoja zilizotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni kuhusu uhaba wa watumishi wa Mahakama wenye sifa zinazotakiwa katika kada mbalimbali. Napenda kusema kwamba upo uhaba wa watumishi katika kada mbalimbali kama Mahakimu, Wasaidizi wa Kumbukumbu na Makatibu Mahsusi. Hata hivyo, kwa mwaka wa 2017/2018 vibali vilipatikana na ajira kutolewa. Mfano, Majaji 12 na Mahakimu 194 wameajiriwa; Wasaidizi wa Kumbukumbu 90 na Makatibu Mahsusi 30 wameajiriwa pia. Aidha, watumishi 298 wa idara nyingine waliajiriwa. Kwa mwaka ujao wa fedha 2018/2019 ajira 513 za kada mbalimbali zinategemewa kutolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ya Kamati ni kwamba Watendaji wanawanyanyasa Majaji na Mahakimu na kujiingiza kwenye maamuzi ya kesi, lakini pia sheria ya uendeshaji wa Mahakama iboreshwe kudhibiti nidhamu na ikiwezekana kuwarejesha kwenye nafasi zao za awali. Wizara, Tume ya Utumishi wa Mahakama na Mahakama tumefanya mikutano ya pamoja na Kamati ya Katiba na Sheria mara kadhaa ikiwemo kupitia bajeti ya Wizara na taasisi zilizo chini yake. Kwa bahati mbaya hatukupata fursa ya kupewa hoja hii na kujadiliana na Kamati wala Mwenyekiti wala Kamati katika suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, suala hili lina historia ndefu kwa sisi tuliokuwepo na kushiriki kwenye maboresho ya Mahakama. Mapendekezo ya maboresho ya uendeshaji wa Mahakama na hatimaye kutungwa Sheria Na. 4 ya mwaka 2001 na muundo wake kupitishwa na Mheshimiwa Rais mwaka 2014 yana historia ndefu ya mapendekezo ya Tume za Mheshimiwa Msekwa, Mheshimiwa Jaji Bomani na Mheshimiwa Jaji Mroso.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa, takwimu na hata viashiria mbalimbali vinaonesha kuwa Mahakama kwenye nyanja karibu zote inapiga hatua kubwa ya maendeleo ya uendeshaji pamoja na kazi yake ya msingi ya utoaji haki. Tume ya Utumishi wa Mahakama chini ya Mheshimiwa Jaji Mkuu na hata Wizara ama mimi Waziri hatujapokea malalamiko yoyote juu ya kunyanyaswa ama kunyanyasana kuingilia shughuli za kazi nje ya majukumu yao ya kiutendaji kwa watendaji husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo kuna tatizo la mtu mmoja mmoja kama binadamu, ni vyema litolewe taarifa husika na suala husika kwenye mamlaka husika za kikatiba na kisheria, yaani Tume ya Utumishi wa Mahakama na ama niletewe mimi kama Waziri ili yashughulikiwe kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo. Serikali kwa maana ya Wizara, tutaendelea kushirikiana na Tume ya Mahakama kwenye kusimamia na kuendeleza maboresho ya Mahakama kwa manufaa ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ilikuwa ni kuwahamisha watumishi bila kulipwa stahili zao kwa kuzingatia umuhimu wa kujaza nafasi mbalimbali hasa za madaraka (duty post) watumishi wamekuwa wakihamishwa na kulipwa sehemu ya stahili zao kabla ya kuhama na sehemu inayobaki inamaliziwa baadae.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ushauri wa Mahakama kurudia kuezeka paa la Mahakama Kuu ya Kanda ya Shinyanga, ningependa kusema kwamba mradi wa Mahakama Kuu ya Shinyanga ulikamilika mwaka 2016, mara baada ya kukamilika kulikuwa na tatizo la kuvuja kwa maeneo machache ya paa hilo. Kwa kuwa mradi ulikuwa bado kwenye kipindi cha matazamio (defect liability period) mkandarasi alirekebisha na sasa tatizo hilo halipo tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu zabuni za ujenzi wa miradi ya maendeleo kwa Mahakama kwamba zitolewe kwa uwazi, kipaumbele kitolewe kwa makampuni ya ndani ya Wakandarasi yanayokidhi vigezo na uwezo wa kukamilisha mradi kwa wakati na kwa mujibu wa mikataba husika; napenda kusema kwamba Mahakama imekuwa ikitekeleza miradi yake kwa uwazi wakati wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto kubwa ya ukosefu, uhaba na miundombinu ya Mahakama na kwa kuzingatia uchache wa rasilimali fedha, ukilinganisha na mahitaji halisi ya Mahakama na gharama kubwa za ujenzi, Mahakama ilifanya utafiti wa kubaini teknolojia ya ujenzi yenye gharama nafuu iitwayo moladi ambayo inapunguza gharama kwa takribani asilimia 40 mpaka 45.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchambuzi wa zabuni za miradi ya Mahakama za Wilaya na za Mwanzo iliyotangazwa mwaka 2016/2017 ilionesha kuwa waombaji wa zabuni waliokuwa na gharama za chini kabisa zilikuwa ni shilingi bilioni 1.2 kwa Mahakama za Wilaya na shilingi milioni 898 kwa Mahakama za Mwanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na gharama kubwa, Mahakama ilisitisha zabuni hizo na kutumia teknolojia mbadala ya moladi ambayo ni ya Watanzania japo ni teknolojia yenye asili ya Afrika ya Kusini na teknolojia hii imehuishwa na Chuo Kikuu cha Ardhi. Kanuni na taratibu zote za ununuzi wa umma zilizingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe nimefungua Mahakama Kigamboni ya utaratibu wa moladi, ni mahakama nzuri kwa gharama ambayo mtu hawezi kuamini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upungufu wa udahili katika Taasisi ya Mafunzo kwa Vitendo (Law School of Tanzania), ningependa nieleze kwamba hakuna upungufu wa wahitimu wa sheria katika vyuo vikuu nchini. Sasa hivi tuna vitivo vya sheria 17 nchini. Kwa hiyo, hakuna upungufu wa wahitimu wa sheria. Suala la kwenda Law School, zipo sababu nyingi kwa nini baadhi ya wanafunzi hawaendi Law School.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, wapo ambao wamesoma sheria lakini lengo lao siyo kuwa Wanasheria. Wamemaliza degree ya sheria na hawakutaka kuendelea na sheria, wamekwenda kufanya kazi nyingine. Na mimi namfahamu mwanafunzi mmoja ambaye amemaliza sheria, amemaliza na Law School, amekuwa Advocate, ameacha na sasa anajifunza u-pilot wa ndege. Aliniambia kazi ya sheria ilikuwa ya baba, Uwakili ulikuwa wa baba, nimemaliza ya baba, sasa nafanya mimi ninayotaka. Sasa hivi ninavyosema, anajifunza Urubani chini ya shirika fulani la ndege silitaji. Kwa hiyo, wapo ambao wakimaliza degree ya sheria hawana interest ya sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wapo wanaoangalia perspective ya soko. Ukiangalia katika private sector ya practice ya sheria, napenda niseme kwamba miongoni mwa maeneo ambayo watu hawatengi fedha kwa ajili ya huduma, ni sheria. Hakuna hata mtu mmoja humu ndani ya Bunge hili ambaye ana Family Lawyer ambaye amempangia bajeti kwa mwaka atam-retain amlipe kiasi fulani. Kwa hiyo, vijana wetu hawa nao ni mahiri na wajanja, wakiona kwamba huku hakuna maendeleo mazuri, basi wanakwenda kwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ni kweli huko nyuma wanafunzi walikuwa napewa mikopo moja kwa moja, lakini sasa mikopo inatolewa kwa wale ambao wanastahili kwa kutumia means test na katika maeneo ya kipaumbele. Sheria siyo mojawapo ya eneo la kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuanzisha matawi mbadala ya taasisi ya sheria, napenda kusema kwamba jambo hilo tumekuwa tunalifikiria na kulitafakari kwa makini, lakini jitihada yetu kubwa kwanza ni kuimarisha ubora wa taasisi hii pale ilipo na baada ya kuimarisha ubora ndipo tutaweza kufikiria mambo ya kupanua kwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufahamu kwamba sasa tuna vitivo 17 vya sheria. Mahali pekee ambapo wanasheria wote hawa wanakutana na kupikwa ni kwenye Law School of Tanzania. Kwa hiyo, kabla ya kuanza kufikiria kuanzisha matawi, ni lazima tufanye utafiti wa kutosha ili tuhakikishe wanasheria wote wana utamaduni, mila na desturi zinazofanana kwa sababu sasa wanatoka kwenye vyuo vingi tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imetushauri pia kuhusu Ofisi ya Taifa ya Mashitaka kwamba pawe na ushirikiano kati ya Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, Mahakama, Polisi na vyombo vingine vya upelelezi ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya ofisi pamoja na kuongeza wigo wa utoaji haki bila kuingilia uhuru wa vyombo vingine. Ushauri huu umepokelewa na utafanyiwa kazi. Ofisi ya Huduma ya Mashitaka itaendelea kuimarisha na kuboresha mahusiano na ushirikiano na taasisi na wadau wa haki jinai na ndiyo maana katika mabadiiko ya sheria ambayo tunategemea kuyaleta Bungeni, ni pamoja na kuanzisha Criminal Justice Forum ambayo itahusisha taasisi mbalimbali lakini pia kuwe na Government Legal Team ambayo itahusisha mambo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine wa Kamati ni kwamba Ofisi hii ya Taifa ya Mashitaka ihakikishe inafungua ofisi zake katika Mikoa na Wilaya zilizoainishwa katika taarifa ya bajeti kwa lengo la kuongeza wigo wa utoaji haki. Napenda kusema kwamba ushauri umepokelewa na utafanyiwa kazi. Ofisi imeainisha maeneo itakayofungua ofisi kuwa ni Mkoa wa Songwe, Wilaya ya Kinondoni, Wilaya ya Ilala na Wilaya ya Kigamboni na kwa kadri inavyowezekana, basi tutafungua katika Wilaya na Mikoa mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Kamati ilizungumzia suala la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, kwamba kuwepo kwa malalamiko mengi kuhusu uvunjwaji wa haki za binadamu, ukiukwaji wa misingi ya utawala bora nchini pamoja na tuhuma za kushikiliwa watu Magerezani, Polisi na sehemu nyinginezo nchini pasipo kuwepo utoaji haki au majibu yanayoridhisha. Kamati ilishauri Tume ifanye ukaguzi katika sehemu zote nchini zenye malalamiko hayo na kutoa taarifa kwa mujibu wa sheria ili kutatua changamoto hizo endapo zitabainika. Ushauri umepokelewa na utazingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora itatembelea sehemu zilizolalamikiwa zikiwemo Magereza na Vituo vya Polisi na taarifa itawasilishwa kwenye mamlaka husika kwa hatua stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Kamati imetoa maoni kuhusu Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania. Kamati imeshauri Tume ya Kurekebisha Sheria kufanya mapitio ya sheria mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha kunakuwepo na mfumo wa sheria nchini unaozungumza lugha moja (uniformity of law) na hivyo kuondokana na mgogoro wa kisheria usio na lazima (unnecessary conflict of law) unaoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji. Napenda niseme kwamba ushauri unapokelewa na utazingatiwa. Aidha, Tume katika kufanya mapitio ya mifumo ya sheria mbalimbali itahakikisha kutokuwepo kwa migongano baina ya sheria wakati wa kutoa mapendekezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Kamati ya Bajeti nayo ilikuwa na maoni yafuatayo; moja, bajeti iliyotolewa ya mwaka 2018/2019 haikidhi mahitaji ya msingi ya Mfuko wa Mahakama na kwamba Serikali ihakikishe inaongeza bajeti ya mfuko. Maoni ya Kamati yatazingatiwa, bajeti ya mfuko kwa fedha za matumizi ya kawaida na maendeleo kutoka Serika itaongezwa kadri mapato ya Serikali yanavyoongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Kamati ilitoa maoni kuwa kutokukamilika kwa utaratibu wa kuwezesha mifumo ya ukusanyaji maduhuli kielektroniki (E-pos machine), tunasema Serikali kupitia Mahakama tayari imeanza kutumia mfumo wa kielekroniki (Pos machine) ambapo Mahakama zote za Mkoa wa Dar es Salaam zinatumia mfumo huo. Utaratibu utafanyika pia mikoani kwa kuongeza mashine hizo kama Kamati ilivyoshauri. Aidha, mawasiliano yanaendelea kufanyika kati ya Wizara na Wizara ya Fedha ili vifaa hivyo viweze kupatikana kwa bei nafuu na kwa wakati ili kuongeza mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale waliochangia kwa mdomo, nianze na Mheshimiwa Kombo. Niseme kwamba suala la Joint Finance Commission na suala la Joint Account lilitolewa maelezo mazuri sana jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano) na majibu ya Serikali ni hayo hayo kwamba jambo hilo ni kama lilivyokuwa limeelezwa kwenye Wizara hiyo. Tume ipo na mchakato wa kuanzisha akaunti hiyo unaendelea kwa taratibu za kiserikali na hapo utakapokamilika, basi mambo hayo yatatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kutekeleza matakwa ya Katiba, lakini ni jambo ambalo utekelezaji wake unahitaji maandalizi ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mwingiliano kati ya Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoshughulikia mambo yasikuwa ya Muungano ya Tanzania Bara na Mahakama Kuu ya Zanzibar, napenda kukubaliana nawe kwamba Mahakama zote hizo zina mamlaka sawa (concurrent jurisdiction) lakini pamoja na kuwa na concurrent jurisdiction, yapo mashauri ambayo yanaweza kuwa yamefanyika Tanzania Bara yakalazimika kujadiliwa na Mahakama Kuu ya Zanzibar ikiwa yatakuwa na uhusiano na Mahakama Kuu ya Zanzibar na vivyo hivyo yapo ambayo yatafanyika Zanzibar, lakini yakasikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania kutegemea ni wapi palipokuwa chanzo cha mgogoro au kesi hiyo, mtandao unaohusika na nyezo zilizotumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pamoja na hizo mahakama kuwa na concurrent jurisdiction, lakini upo wakati ambapo moja inaweza ikasikiliza mashauri yaliyotoka upande mwingine kwa kutegemea muktadha na aina ya tatizo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la OIC, tarehe 4 Aprili, 2018 Wizara ya Mambo ya Ndani ilijibu na kutoa maelezo mazuri kuhusu suala la OIC na nadhani majibu hayo yanakidhi suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mashehe wale wa Uamsho na wale wa Zanzibar, suala hili lipo Mahakamani na Wizara iahidi tu kwamba itazidi kuhamasisha uchunguzi ukamilike ili kesi hiyo iendelee. Kesi za namna hii ni very complex na wakati mwingine ushahidi wake kuukusanya unahitaji muda na umahiri na wakati mwingine unahitaji ushirikiano na taasisi na vyombo vilivyo nje ya nchi ambako pia tunalazimika kuomba ushahidi kwa njia mbalimbali. Ni imani yangu kwamba jambo hili litapata muafaka na litapata suluhisho wakati uchunguzi utakapokuwa umekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mheshimiwa Kiteto kuhusu Mabaraza ya Ardhi; Tume ya Marekebisho ya Sheria ilifanya utafiti kuhusu Mabaraza ya Ardhi. Taarifa hiyo ilifikishwa kwa Waziri na nimetoa maelekezo, kuna maeneo ambayo nimeomba yafanyiwe utafiti zaidi. Kwa hiyo, mara baada ya maeneo hayo ya nyongeza ambayo nimewarudishia Tume ya Kurekebisha Sheria yatakapokamilika, basi Serikali itashauriwa ifanye nini kuhusu Mabaraza haya ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, Serikali ilitoa ahadi hiyo Septemba ya mwaka 2016, lakini baada ya kutafakari kwa makini suala la mabadiliko ya Sheria ya Ndoa linahitaji umakini mkubwa sana. Wewe unafahamu vyema ni sisi Tanzania peke yetu tuliofanikiwa mwaka 1971 kutunga Sheria ya Ndoa. Uganda ambao walikuwa wa kwanza kuanza mchakato huu mwaka 1966 chini ya Ripoti ya Kalema mpaka leo wameshindwa kuwa na sheria moja ya ndoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kenya ambao walianza juhudi za kuwa na sheria moja ndoa ya mwaka 1968 hawakufanikiwa mpaka baada ya mauaji yaliyotokea. Wametunga sheria, sheria imepita na baadhi ya mambo ambayo sheria imeyakataza, sasa watu wameanza kuyadai na moja ya mambo ambayo sheria ya Kenya ya sasa ya ndoa inayakataza na sasa yameanza kudaiwa, tena wanaodai ni wanawake, ni kufuta talaka. Hii ni kwa sababu Sheria ya Ndoa ya Kenya imefuta talaka, lakini wote tumeona sasa jitihada kubwa tena ya hadharani na inaongozwa na wanawake kudai sheria ya kuwaruhusu talaka irejeshwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema nini? Mashauri ya ndoa, mirathi, mashauri yanayogusa mila na destruri, yanayogusa dini na itikadi, ni vyema kuyaendea kwa uangalifu mkubwa. Najua kabisa na niseme tu kwa unyenyekevu, somo hili la ndoa nimelifundisha kwa miaka 19, siyo eneo jepesi. Kuhusu kwa mfano, umri wa mtoto kuolewa mpaka ninavyozungumza sasa umri wa mtoto wa kike kuolewa Uingereza ni miaka 16. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, zipo sababu kubwa na mukhtadha wake tuambiane, mwaka 1971 wakati sheria hii ya ndoa inapitishwa, elimu ya mwisho ya mtoto ilikuwa darasa la saba. Asipoendelea kwenda form one, ina maana amekaa nyumbani na turudi twende kwenye jamii na kila mmoja nyumbani kwake. Hivyo, mtoto wa kike aliyevunja ungo, kipi chema, aolewe azae katika ndoa au azuiwe kuolewa mpaka afike miaka 15 wakati huko kwingine hakujafungwa na anaweza akapata ujauzito? Atakapoupata ujauzito huo akazaa huyo mtoto, kama ni mkatoliki hatabatizwa mpaka aende akafanye maungamo na maungamo hayo ya kikatoliki ni ya yeye mama, sio baba aliyemzalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ukiifumua leo, kuipitisha ndugu zangu ni ngumu. Yapo mambo matatu ndani ya hii Sheria ya Ndoa ambayo kwa Kanisa Katoliki hayakubaliki. Moja, hawakubali kubadili ndoa ingawa Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inaruhusu kubadili ndoa ya mke mmoja kuwa ndoa ya wake wengi. Baraza la Maaskofu Katoliki lilipinga, lakini Mwalimu ambaye alikuwa ni mkatoliki aliwaambia, situngi sheria ya wakatoliki, natunga sheria ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Sheria ya Ndoa ya sasa inaruhusu kubatilishwa na ndoa na Mahakama za kawaida. Kanisa Katoliki halikubali. Mimi sio Mkatoliki, lakini kwa Kanisa Katoliki ndoa inabatilishwa tu na Askofu baada ya kushauriwa na Judicial Vicar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakapofungua hii, we are opening a pandora box. Ukiangalia tuna tafsiri tofauti ya ndoa. Zipo ndoa ambazo kwao ni sakramenti; wapo ambao ndoa kwao ni covenant. Kwa hiyo, unapokuwa na mchanganyiko huo mkubwa kiasi hicho ni vyema ukafanya mambo kwa tahadhari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo ndani ya sheria hii bado yana vikwazo kwa Waislam, ni compromise. Sheria yoyote iliyofikiwa kwa compromise, be careful when you want to change it. Sheria hii ni very progressive katika maeneo mengine. Ndiyo sheria ya kwanza duniani kuwaruhusu wanawake kuwa na nguvu hasa wanawake wasomi na watalaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chini ya Sheria ya Ndoa ya Uingereza, cohabitation maana yake mke na mume waishi ndani ya nyumba moja muda wote. Ndiyo maana wanawake wa Kiingereza hawakuweza kupanda vyeo kwenda kufanya kazi nje ya maeneo ambayo waume zao wanafanya kazi. Mwaka 1971 Sheria ya Ndoa, cohabitation maana yake siyo kuishi ndani ya nyumba moja, mnaweza kuishi sehemu mbali lakini kwa makubaliano, kwa simu na kwa barua. Tafsiri hiyo ni cohabitation. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya hii Sheria ya Ndoa ya kwetu, malipo ni jukumu la mwanaume kuitunza familia (the necessity of life). Kwa hiyo, yapo maeneo mengi ambayo sisi tumepiga hatua ambayo nchi nyingine bado hawajapiga hatua. Hiyo haina maana tusiangalie yaliyopungua. Niliwaeleza hapa na ninarudia, mpaka leo Ulaya Wabunge wanawake wanapata mshahara mdogo kuliko Wabunge wanaume kwa sababu ni wanawake. Kwa hiyo, sihalalishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema, kila nchi ina sababu ya kutokufanya mambo fulani na yanahitaji muda; na moja ni Sheria ya Ndoa. Tukiindea kwa haraka tutavuruga zaidi kuliko kujenga. Kwa hiyo, tujenge muafaka wa taratibu, kwa sababu Sheria ya Ndoa ni jamii sio mtu. Ndiyo maana Sheria ya Ndoa ya sasa kuhusu ugoni (adultery) niwaambie, ndani ya sheria ya sasa ya ndoa adultery inaweza kuwa evidence; the marriage has broken down irreparably and therefore the Court can grant divorce. Humo humo adultery kwa kutambua yako makabila hapa ambayo adultery siyo sababu ya kuvunja ndoa, sheria hii ya ndoa inatoa kibali cha compensation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nayafahamu makabila mawili ambayo bila kumfumania mke wako ugoni, unaona hujaoa. Kwa hiyo, mambo haya yanahitaji umakini. Kwa hiyo, mtanifuata baadae nitawaambia. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuliendee kwa utaratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Serikali imekata rufaa kuhusu Sheria ya Umri wa Mtoto Kuolewa, lakini tunapokata rufaa, hatukati rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa on matters of facts. Tunakata rufaa on points of law. Ule uamuzi bahati mbaya sana tunaangalia matokeo, hatuangalii hoja za uamuzi ule. Ukizifuata hoja za uamuzi ule, hakuna sababu ya kuwa na Viti Maalum.

Ndiyo. Ukifuata hoja ya uamuzi ule, hakuna sababu ya kuwa na Viti Maalum, kwa sababu huo pia ni upendeleo ambao hauruhusiwi na Katiba kwa Ibara ya 13. Maana yake nini? Ndiyo maana Katiba inaruhusu positive discrimination, affirmative action. Ni affirmative action inayoruhusu Viti Maalum. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa historia ya Tanzania, bila affirmative action, idadi ya Wabunge wanawake humu wengi watatoka Mtwara na Lindi, kwa sababu ni matrilineal na ndiyo wamekuwa wanaleta Wabunge wengi wa kuchaguliwa. Suala la Tarime, ni ajali kwa mila na desturi. Ninapenda niliweke vizuri, kwa mila na desturi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lengo kubwa la sheria hiyo…

KUHUSU UTARATIBU . . .

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: MheshimiwaMwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ndiyo maana nasema kwamba lengo la Serikali kwenda Mahakama ya Rufaa ni kubakiza principle ya positive discrimination, principle ya affirmative action ili kwa kuangalia hali halisi ya Tanzania wanawake waendelee kupata nafasi katika vyombo vya maamuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na lengo lake sio suala la umri wa mtoto kuoa au kuolewa, someni arguments za yule Jaji ninayemheshimu sana kwa sababu tumesoma darasa moja, hoja ni ile ya argument. Ni sawasawa na hesabu, unaweza ukasema jibu ni nne, lakini mwalimu hasahihishi jibu, mwalimu mzuri wa hesabu anaangalia method uliyotumia, sasa kama method mbaya itavuruga. Ndilo ninalotaka kuwaambia, itavuruga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo vikuu ina maana wasichana watapungua idadi yao, si ni usawa tu, kila usawa una mipaka yake kwa hali halisi ya nchi yenyewe. Ndiyo maana mwanamke ni mwanamke na mwanaume ni mwanaume ingawa wote ni binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro ameleta suala la bajeti ya Law School of Tanzania, suala hilo litaangaliwa. Kuhusu Mjumbe kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwa ndio Mjumbe wa Governing Council, nakubali viko vyuo vingine 17 ambavyo pia naviheshimu sana.

Kwa hiyo, jambo hilo ni jambo la kujadiliwa, lakini wakati Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinawekwa pale, ni kwa sababu ndicho ambacho kwa lugha ya Kilatini, primus inter pares. Huo ukweli pia hautafutika, kwamba Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika vitivo vyote vya sheria, siyo Tanzania tu, Afrika ya Mashariki ni primus inter pares.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana na wewe unafahamu, umekwenda mara nyingi Kenya. Nikifika Kenya huwa lazima niwatambie, tumewapa Kenya Majaji Wakuu watatu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; Jaji Chesoni, Jaji Gicheru na Jaji Mutunga. Tumewapa Uganda Jaji Mkuu Benjamin Odok; sasa hivi Jaji Mkuu wa Gambia Jalo ametoka Dar es Salaam. Kwa hiyo, kitabaki kuwa primus inter pares, kwa lugha ya kawaida first among equals (wa kwanza kwa walio sawa). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuvumilie tu, lakini hawazuiwi kubadili kama wakiona hawataki huyu wa kwanza kwa walio sawa aendelee kuwawakilisha. Ni hiari ya vituvo vya sheria. Na mimi kwa sababu pia nina conflict of interest, nitaacha jambo hilo liamuliwe na watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uandikishaji wa watoto, Mkoa wa Ruvuma nao utafikiwa. Tulianza na pilot, sasa tutasambaza mikoa yote. Hii ilikuwa ni pilot scheme kuona ni jinsi gani itafanya kazi, lakini sasa itagusa watoto wa nchi yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara, wazo hilo limechukuliwa linafanyiwa kazi na Tume ya Kurekebisha Sheria imeshakamilisha utafiti kuhusu Sheria mpya ya Usuluhishi, yaani Sheria mpya ya Arbitration na itakapoletwa tutashukuru sana kupata mchango wako ni jinsi gani ndani ya sheria hiyo tuwe na vifungu vya kuanzisha hii International Commercial Arbitration.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni mengi ya ndugu yangu, Mheshimiwa Lema, nimeyapokea. Amesema nisiwe muoga, inategemea nisiwe mwoga wa nini? Ninachoogopa ni kutenda dhambi na kuikosa pepo. Uoga huo wa kuogopa dhambi na kuikosa pepo, nitakuwa nao, lakini pia siwezi kuwa jasiri katika mambo ambayo hayahitaji ujasiri. Kwa hiyo, nimeyazingatia yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu matumizi ya Sheria ya Money Laundering, tutayafanyia kazi maoni haya yote aliyoyatoa. Kama kweli wako watu ambao wako ndani kwa money laundering ya dola 1,800 au kiasi fulani, basi ni suala la kupitia na kuona je, sheria ifanyiwe marekebisho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mheshimiwa Lema amesema tumeongea, niseme katika kesi hiyo ya Mwale, wale wawili wengine ni ndugu zangu, lakini sasa mimi ni Waziri wa Katiba na Sheria, lazima niheshimu utaratibu. Sikupenda kulisema, lakini ni vyema niseme kwamba kati ya wale wawili walioshtakiwa na Mwale, wawili ni ndugu zangu. Sasa tuache sheria iende na ningependa jambo hilo lishughulikiwe kwa mkondo wa sheria ili baadaye haki itendeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Ndassa, masuala yako yamechukuliwa yote na yatazingatiwa kuhusu Mahakama hizo kumi na Mahakimu wanne tu, lakini pia ukarabati wa majengo ya Mahakama hizo katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Sabreena nakushukuru sana kwa uliyoyasema. Jambo lolote linaloondoa uhai wa binadamu linahitaji liangaliwe kwa umakini. Nchi yetu ilipita katika kipindi kigumu. Mauaji yale ya Rufiji na Kibiti hayakuwa ya kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme wakati mwingine Watanzania ni vyema tukakumbushana, nchi moja ya Ulaya ilipokabiliwa na aina hiyo ya matukio ilitoa amri kwa askari wake to shoot on sight, sitaitaja humu ndani ya Bunge kwa sababu siyo vizuri kuitaja nchi nyingine, lakini Balozi wa nchi hiyo alipokuja kuniona kwa mambo hayo nilimkumbusha, kwa sababu kipindi hicho nilikuwa naishi huko. Ilitoa amri ya ku-shoot on sight na Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe anajua. Sisi hatujafikia mahali, pamoja na matukio hayo ya idadi kubwa ya askari polisi kuuawa kutoa amri ya ku-shoot on sight. Kwa hiyo, nilimkumbusha Balozi yule kwamba hata ninyi mlipopita katika kipindi kigumu, mlifikia hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tujitahidi kuyakabili mambo hayo, tuombe Mwenyezi Mungu atusaidie kuepuka hayo. Kwa sababu mwanadamu akiondolewa hekima, busara na kiasi, anakuwa hayawani. Usimwite mwanao hayawani, kwa sababu hayawani ni lahaja ya kimvita kwa maana ya mnyama. Mwanadamu akishakosa hiyo, anakuwa hayawani. Kwa hiyo, tumwombe Mwenyezi Mungu atuepushe kuingia katika uhayawani ili tusiuane hovyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mabaraza ya Ardhi, nichukue tahadhari hiyo niliyosema, tumeshaiagiza Tume ya Kurekebisha Sheria ili ituletee mapendekezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea maoni mengi ya maandiko ambayo mengi tumeshayajibu na tutawapa Waheshimiwa Wabunge wahusika ili wapate majibu tuliyowapa na mengine yanafanana na haya ambayo yameletwa na Kamati, kwa hiyo, ili tuweze kuwatendea haki wale wote waliotuletea maoni yao kwa maandishi, wote tumehakikisha kuwa wanajibiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yamehusu Law School of Tanzania ambayo tayari nimeshayaeleza, mengine yamehusu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu kuboresha utendaji wao ambayo tayari Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameyajibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mengine yamehusu Tume ya Haki za Binadamu ambapo pia tumeeleza kwamba Tume ya Haki za Binadamu itatembelea sehemu zinazolalamikiwa yakiwemo Magereza na Vituo vya Polisi na taarifa itawasilishwa kwa wahusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo ambao wameomba Mahakama za maeneo yao, nao pia tutahakikisha tunatekeleza kwa sababu tulitoa ahadi. Kwa mfano, Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi ambaye alikuwa ameomba ile Mahakama ya Mtae ambayo imejengwa mwaka 1926 ifanyiwe ukarabati. Tutahakikisha katika mwaka huu wa fedha Mahakama hiyo ya Mtae huko Mlalo ambayo ina umri wa miaka mingi inafanyiwa marekebisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Zainab Mndolwa Amir wa Viti Maalum CUF, naye amezungumzia kuhusu ukarabati wa majengo ya Mahakama, tutaendelea kuyafanyia kazi. Swali hilo hilo pia limeulizwa na Mheshimiwa Lucy Fidelis Owenya kuhusu ukarabati wa Mahakama, tutayafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najaribu kuangalia maswali ya upande wa pili ili nihakikishe nimeyagusia pia. Mheshimiwa James Millya wa Simanjiro, Mbunge wa CHADEMA kuhusu Tume ya Utumishi wa Mahakama Tanzania kumshauri Mheshimiwa Rais kufanya teuzi kutoka ndani ya mfumo wa Mahakama kwamba kitendo cha kuteua Majaji kutoka nje ya mfumo wa Mahakama kutawakatisha tamaa watumishi walio ndani ya Mahakama kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu kumjibu Mheshimiwa Millya kwamba sifa za mtu anayefaa kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu zimeainishwa kwenye Ibara ya 109(7)(a) mpaka (c), hizo ndiyo sifa. Na mimi niseme toka Majaji waanze kuteuliwa kutoka katika sehemu mbalimbali, imeleta tija kubwa katika Mahakama. Kwa hiyo, hii mixing ya watu kutoka ndani na nje ya Mahakama kwenye private practice na kwenye taasisi nyingine ambayo haivunji Katiba ya nchi, maadamu inazingatia sifa na inazingatia recommendations za Judicial Service Commission, utaratibu huo ni vizuri ukaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lucia Michael Mlowe, Mbunge wa Viti Maalum CHADEMA aliuliza kesi kuchukua muda mrefu Mahakamani. Napenda tu kumjibu kwamba hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa ili kukamilisha kesi na kuhakikisha hazichukui muda mrefu. Hii ni pamoja na kesi katika kila ngazi ya Mahakama kuwekewa muda maalum wa kukaa Mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kila Hakimu na kila Jaji amepangiwa idadi maalum ya mashauri anayopaswa kumaliza kila mwaka na tatu, kila ngazi ya Mahakama iliyo na mashauri yasiyozidi umri uliowekwa katika ngazi inayoendeshwa, zoezi maalum la kuziondoa na kumaliza mlundikano, lakini pia kuendesha vikao vya case flow management na Bench-Bar Meetings zimesaidia sana kumaliza huo mlundikano wa kesi na kuupunguza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kesi ya Mwale ambalo liliulizwa na Mheshimiwa Lathifah Hassan Chande, Mbunge wa Viti Maalum CHADEMA; Mheshimiwa Lucy Fidelis Owenya, Mbunge wa Viti Maalum CHADEMA; Mheshimiwa Risala Saidi Kabongo, Mbunge wa Viti Maalum CHADEMA; na Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu CCM; majibu yameshatolewa. Kwa taarifa yenu, tarehe 20 Aprili, keshokutwa, Mahakama ya Rufaa itatoa uamuzi kuhusu appeal ya akina Mwale na hao jamaa wawili kuhusu suala zima la nolle prosequi. Kwa hiyo, tusubiri Mahakama ya Rufaa kesho kutwa itoe uamuzi kuhusu suala hilo ili tujue kesi hiyo inaendelea vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Serikali kuweka ukomo wa upelelezi wa kesi, swali ambalo liliulizwa na Mheshimiwa Lucy Fidelis Owenya, Mbunge wa Viti Maalum CHADEMA, napenda kusema kwamba kesi zinatofautiana. Kuna kesi zinazohusisha maslahi ya umma na nyingine huhitaji ushahidi kutoka nje ya nchi na hivyo kuchukua muda mrefu. Hivyo, siyo rahisi kuweka ukomo wa upelelezi wa kesi kwa sababu inaweza kuwa na athari kwa mhanga mwenyewe na mhalifu. Ni muhimu kuwa na mizania kwa pande zote. Kwa hiyo, siyo rahisi kusema upelelezi ukome lini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuchanganya watuhumiwa wa makosa madogo, swali lililoulizwa na Mheshimiwa Lucia Michael Mlowe, Viti Maalum, CHADEMA, niseme kwa kweli uhalifu wote ni sawa na Penal Code yetu ilikuwa amended kuondoa tofauti kati ya felony na misdemeanor.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani palikuwa na tofauti ya felony na misdemeanor, lakini Penal Code Bunge hili hili liliondoa tofauti ya felony na misdemeanor. Kwa maana hiyo Tanzania leo hakuna kosa dogo wala kubwa, makosa yote yako sawa. Tukitaka turudi kwenye utaratibu wa felony na misdemeanor basi tubadili sheria hapa Bungeni ili tuwe na makosa ya misdemeanor ambayo ni makosa madogo na felony ambayo ni makosa makubwa. Bila kufanya hivyo, sasa Tanzania makosa yote yako sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mrundikano wa mahabusu Magerezani, hilo nalo limetolewa maelezo na litatolewa maelezo zaidi wakati wa Hotuba ya Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lililoulizwa na Mheshimiwa Ritta Kabati kuhusu vitendo vya ukatili kwa wanawake, Tume inajitahidi kuchukua hatua za kushughulikia suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lililoulizwa na Mheshimiwa Risala Saidi Kabongo, Mbunge wa Viti Maalum CHADEMA, kuhusu Tume ina jukumu la kuchunguza uvunjwaji wa haki za binadamu na msingi wa utawala bora, mfano wananchi kukutwa kwenye viroba kando ya fukwe za bahari na kutekwa.

Napenda kusema kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 33 cha Sheria ya Tume, Sura ya 391, taarifa zake za mwaka zinawasilishwa kwa Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya haki za binadamu na utawala bora Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Tume imekamilisha taarifa zake hadi mwaka 2015/2016 na zitawasilishwa Bungeni mwaka ujao wa fedha. Aidha, taarifa za mwaka 2016/2017 ziko tayari na zinasubiri Taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema michango ya maandishi ni mingi na wote tumeijibu na tutahakikisha Wabunge wote wanapewa majibu yao kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
WAZIRI WA SHERIA NA KATIBA: Mheshimiwa Spika, na mimi nataka niungane na wale wote ambao wamewapongeza Waziri na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii kwa kuwasilisha bajeti yao. Pia niendeleze machache ya yale aliyoyasema Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, panapokuwa na sheria msingi na sheria ya zamani panakuwa na kipindi cha mpito na ni imani yangu kwamba haya yaliyotokea ni ya kipindi cha mpito. Katika kipindi cha mpito zipo changamoto za utekelezaji wa sheria na panapokuwa na changamoto kazi kubwa ya mamlaka za Serikali ni kuona ni jinsi gani kipindi hicho cha mpito kinatekelezwa na kama kuna changamoto zozote zinatatuliwa kiutawala. Kwa hiyo, nisingeenda kusema kwamba Waziri amevunja sheria, ninachoweza kusema ni kwamba kipindi cha mpito kina changamoto kati ya sheria iliyokuwepo na sheria msingi iliyokuja ili kusaidia kupata utaratibu ambao mwisho wa siku una tija kubwa.

Mheshimiwa Spika, maadam Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema na kwa mujibu wa Sheria ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kifungu cha 21 ushauri wake is binding. Kwa hiyo, nikiwa Waziri ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali is binding mpaka a-overcatch na maadam haja-overcatch basi huo ndio msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije kwenye suala hili ambalo linatugusa sisi wote nalo ni suala la mifugo inayokamatwa katika maeneo ya hifadhi. Hili kama nilivyosema ni suala nyeti, ni suala zito, ni suala ambalo huwezi kulipuuza ni lazima nikitumia lugha yako ufungue masikio mawili. Nini maana ya kufungua masikio mawili, uko upande wa sheria na uko upande wa utekelezaji wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa upande wa sheria na wewe unaifahamu hii sheria vizuri kabisa, hii sheria ni miongoni mwa sheria iliyochukua zaidi ya miaka nane kutungwa. Ilikuwa na majadiliano mengi na miongoni mwa maeneo ambayo yalizungumzwa yalikuwa eneo hili hili tunalolizungumza leo la mifugo kuingia katika maeneo ya hifadhi na kulishwa na hatua gani zichukuliwe na limeendelea kuwa hivyo. Ni kweli kabisa kifungu cha 18 cha sheria kinazuia mifugo kwenda kulishwa ndani ya maeneo ya hifadhi na kinaeleza kabisa mifugo ikikamatwa ndani ya hifadhi suala zima la kutaifishwa.

Mheshimiwa Spika, Sheria hiyo hiyo kama unakumbuka ilijadiliwa sana kwamba ziko nyakati na yako majira ambayo kweli kabisa kunakuwa na ukame uliopitiliza, malisho hayapatikani na inawezekana kabisa bila kuchukua hatua mifugo mingi ikafa. Ndio maana kwa busara ya Bunge wakati ule kwenye kifungu cha 21 kilisema; “Any person shall not serve with the written permission of the director previously solved and obtained graze any livestock in any game controlled area.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mara nyingi jambo hili limekuwa pia halijaangaliwa kwa hiyo yako mazingira kwa sababu amesema kuna maeneo watu wanaruhusiwa kuingia, kuna maeneo watu wanazuiwa. Si ajabu huko walikoruhusiwa kuingia haikuwa suala la rushwa au arbitrariness lilikuwa uwezekano mkubwa sisemi ni hivyo kwamba walipata ruhusa katika kufanya jambo hilo na ikitokea hivyo watu hao basi wametekeleza matakwa ya sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mifugo inayokamatwa kwenye kifungu cha 111 cha Sheria kinaruhusu utaifishaji wa mifugo na nisikisome kimeeleza kwa kirefu sana. Kifungu hicho hicho cha 111(4) kinaeleza wazi mifugo hii ikikamatwa inachukuliwa kuwa ni mali ya Serikali na baada ya hapo ukienda kifungu cha 114(2) kinahusu suala zima la uuzaji wa hiyo mifugo na kinasema wazi; “The value of a livestock shall be calculated on the basis of the normal price of the livestock on a sale in open market between a buyer and a seller in dependent of each other.”

Mheshimiwa Spika, lazima tukiri, eneo hili ni miongoni mwa maeneo ambayo yametatiza sana na yamewakera watu wengi kwamba mifugo imekamatwa, lakini kwenye mnada kumekuwa na mazingira yanayoonesha ama bei ilipangwa au imeuzwa kwa bei ya chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa kulizingatia hilo nipende kulieleza Bunge hili kwamba Serikali jambo hili imelisikia na imelizingatia. Kesi nyingi hizi ziko tayari kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ambaye kwa mujibu wa Katiba ana mamlaka ya mwisho kuhusu uendeshaji wa kesi hizi, lakini alipokea malalamiko na bango kitita ninalo la kesi moja moja. Baada ya kuzichambua kesi zote amechukua hatua zifuatazo:-

Mheshimiwa Spika, hatua ya kwanza kama nilivyoeleza kwenye bajeti ya uvuvi, ameachia jumla ya ng’ombe 553 wanaomilikiwa na wafugaji wanne na mifugo hiyo imekwisharejeshwa, na hizo kesi nne baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuzipitia ameamua kutokukata rufaa. Hakuona kama kuna sababu ya kukata rufaa na mara moja mifugo hiyo imeachiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna jumla ya kesi tano zina rufaa katika Mahakama ya Rufani ambapo Mkurugenzi wa Mashtaka amekata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu na nimemuomba Mkurugenzi wa Mashtaka nielewe ni kwa nini katika hizi kesi tano amekata rufaa/amekwenda Mahakama ya Rufani. Tatizo hapa siyo suala la ng’ombe, ni suala la tafsiri ya sheria iliyotolewa na Mahakama Kuu ambayo Mkurugenzi wa Mashtaka anaamini ikibaki ilivyo inaweza kuwa na madhara makubwa baadae kwa uhifadhi.

Mheshimiwa Spika, pia ziko kesi nne ambazo washtakiwa wenyewe wamekata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa Mahakama ya Wilaya kuwatia hatiani na kutaifisha mifugo. Katika eneo hili Mkurugenzi wa Mashtaka ameahidi kukutana na watu hao na kuhakikisha kwamba rufaa zao zinasikilizwa mapema ili kuhakikisha kwamba wakishinda na kama yeye hatakuwa na sababu ya kukata rufaa mifugo hiyo pia iachiwe. Kesi hizo moja itatajwa kesho tarehe 23/5 na nyingine tarehe 30 Mei.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naamini kabisa tarehe 23/5 na 30/5 kesi hizi nne za rufaa zitakuwa zimepatiwa ufumbuzi ambao ama unaweza ukaelekea mifugo hiyo kuachiwa kama wale wenye kesi wataelewana kwamba rufaa hiyo isiendelee na Mkurugenzi wa Mashtaka akiona hana sababu ya yeye pia kukata rufaa. Kwa hiyo, ningesihi tu tusubiri hiyo kesho na tarehe 30 Mei tuone hizo rufaa nyingine nne zimekwendaje.

Mheshimiwa Spika, pia zipo jumla ya kesi 23 kati ya 27 ambazo watuhumiwa walilipa faini bila kupelekwa mahakamani na wakarejeshewa mifugo yao. Pamoja na kulipa faini ambayo ni kati ya shilingi 10,000 mpaka 300,000 lakini hata katika kesi hizo kumekuwa na malalamiko. Malalamiko hayo hatukuyapuuza na moja ya kesi iliyolalamikiwa ambayo ilielezwa kwamba mke wa mfugaji huyo alipigwa risasi na askari pori kisa alikuwa anafuatilia maeneo ya malisho na kwamba hakuna hatua iliyochukuliwa.

Mheshimiwa Spika, baada ya uchunguzi uliofanyika na kupata majibu jana, taarifa hizi si za kweli kwani mama huyu alipigwa risasi na mtu ambaye sitaki kumtaja jina ambaye si askari na amefunguliwa kesi ya mauaji namba 27 ya mwaka 2017. Natoa huu mfano tu kuonesha kwamba ni lazima tufanye uhakiki wa kina ili tusimuonee mtu, lakini pia tusilee uzembe ambao unaweza kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hatua nyingine ambayo kwa kuzingatia unyeti wa jambo hili ambalo tumeona kama Serikali tulichukue ni kuhakikisha kwamba tunakutanisha wadau wote, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Mashtaka ya Taifa na Ofisi ya Rais TAMISEMI ili kuandaa mwongozo maalum ambao utakaotumika katika masuala yote yanayohusu mifugo inayoingia ndani ya hifadhi. Ni jinsi gani ukamataji ufanywe, ni jinsi gani mifugo hao watunzwe na jinsi gani ya kuharakisha kesi na baada ya kesi nini kitokee.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu tumebaini kwamba mara nyingi mambo haya yanapofanywa kwa mtindo wa operation yanapokosa mwongozo wakati mwingine hutokea hitilafu, na hitilafu hizo ili tuzitatue basi vyombo vyote hivi vitakutana kwa pamoja na baada ya hapo tutakuwa na standard operating procedure na standard operating manual ambayo itaongoza shughuli zote zinazohusu mifugo kuingia ndani ya hifadhi na kulisha.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la ushahidi, kwa sababu moja ya sababu ambazo zimekuwa zinapelekea mifugo hii kukamatwa na kubakizwa ni ili zitumike kama ushahidi mahakamani. Naomba niliahidi Bunge lako kwamba nitatafuta mimi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuonana na Jaji Mkuu ili tuone utaratibu mwingine unaoweza kutumika katika ukusanyaji wa ushahidi na utunzaji wa ushahidi ili baadaye uweze kutumika Mahakamani bila kuvunja sheria za nchi ili tusilazimike labda wakati wote kuwa na mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mkurugenzi wa Mashtaka anasema alipeleka shauri hili Mahakama ya Rufaa kuiomba Mahakama ya Rufaa iruhusu mifugo ikikamatwa na kama kesi itachukua muda mrefu iuzwe, ile fedha itunzwe ili wafugaji wakishinda warudishiwe fedha lakini wale wafugaji waliohusika walipinga utaratibu huo kwamba wangependa wabaki na wale ng’ombe wao wenyewe na sio fedha, lakini hilo nalo pia tutalijadili na mamlaka husika.

Mheshimiwa Spika, ni kweli mifugo inapobaki kwa muda mrefu ili itumike kama ushahidi, mingi inakufa na hata kesi inaposikilizwa, mifugo hiyo inakuwa imekufa na ikishinda, Serikali yenyewe inakuwa haina mifugo na wale wafugaji wanakuwa hawana mifugo. Lakini kwa sababu ni suala la Mahakama, mniruhusu tu ili mimi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali tukae tumwombe Jaji Mkuu aone ni utaratibu gani mpya unaoweza kutumika katika kutunza ushahidi bila kuwashikilia ng’ombe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ni jambo ambalo lipo mikononi mwa Jaji Mkuu, siwezi kulisemea. Ninachoweza kusema ni kwamba tutakwenda kushauriana naye halafu yeye atoe maamuzi ili ikiwezekana pasiwe na ulazima wa ng’ombe kukaa hata miaka miwili wakati wanasubiri kesi ili njia nyingine itumike. Pia huwa kuna mtindo wa kuhakikisha iwapo mfugaji atashindwa ni jinsi gani Serikali ina-recover na iwapo mfugaji atashinda ni namna gani anarudishiwa fedha.

Mheshimiwa Spika, nimechukua muda mrefu kidogo kulieleza hili kwa sababu ni suala ambalo linagusa maisha ya watu, livelihood yao na ustawi wao na Serikali haiwezi kulifumbia macho, lakini kwa mujibu wa sheria ilivyo, hivi ndivyo inavyotakiwa kuwa lakini tutachukua hatua zinazostahili ili kuzikamilisha. Mara kila kesi tukayoshindwa Serikali na ambapo hatutakata rufaa, mifugo hiyo itaachiwa mara moja na pale tutakapolazimika kukata rufaa, basi tutajiridhisha kwamba zipo sababu compelling za sisi kukata rufaa ili kuhakikisha tunafanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa wafugaji, ningerudia tena kuwasihi wafugaji wasiingize mifugo katika maeneo ya hifadhi na wanapolazimika kufanya hivyo kwa sababu ya ukame uliopitiliza, basi watumie utaratibu wa sheria wa kuomba kibali na wakipata kibali hicho na masharti maalum wanaweza kulisha mifugo yao mpaka hali hiyo ya ukame inapoweza kuwa imebadilika.

Mheshimiwa Spika, mimi mwenyewe natoka kwenye kundi la wafugaji na labda ndiyo maana naweza kuonekana naongea hivi, lakini Watanzania waelewe kwamba sifanyi hivyo kwa sababu pia natoka kwenye jamii inayofuga, lakini tunajua kwamba mifugo ni muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi kama wewe ni wahifadhi, maana yake pia tunajali hifadhi zilizopo kwa sababu na zenyewe ni sehemu ya maendeleo yetu. Kwa hiyo, ni lazima tuwe na uwiano kati ya uhifadhi ambao ni muhimu sana lakini pia kuendeleza sekta ya ufugaji. Nawasihi sana wafugaji kwa kiasi kikubwa kabisa wa-comply na sheria. Na sisi upande wa Serikali tutajitahidi kabisa kuhakikisha kwamba sheria iliyopo haitumiki kwa namna ambayo inaleta madhara yasiyostahili na pale kwenye vitendo vya rushwa au uzembe, tutachukua hatua haraka na tuwaombe watu watoe taarifa ili PCCB na mamlaka nyingine zichukue hatua inayostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami napenda niungane na Wabunge wenzangu kumpongeza sana Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Engineer Masauni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni ngumu na nzito kama ilivyo Wizara ya Ulinzi. Unapozungumzia Polisi na unapozungumzia Jeshi unazungumzia coercive instruments of the State. Hiyo fact, ni lazima tuifahamu, we are dealing with coercive instruments of the State and which are indispensable.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana ukiisoma Biblia hasa Agano la Kale na hasa Zaburi, Wanajeshi na Walinzi wamependelewa sana na Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kuwauliza wataalamu wa maandiko, kwa nini inazungumziwa Mungu wa Majeshi, Majeshi, Majeshi? Wakasema hata huko kulikuwa na vurugu na ndiyo maana ulinzi uliwekwa ndani na nje na ibilisi alipoasi akatupwa huku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, daima watu ambao kazi yao ni ulinzi wa milki iwe ni ulinzi wa ndani wa milki au ulinzi wa nje wa milki, lazima watumie nguvu wakati mwingine inapolazimika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ni lazima wafanye hayo ndani ya mujibu wa sheria. Pia ni lazima wote tufahamu these are coercive instruments of the State. Wengi hapa mmesoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vyuo vingine, mmesoma Development Studies (DS 100), hayo ndiyo mliyofundishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa vyombo ambavyo ni coercive instruments of the State ni lazima uviendee kwa namna inayostahili. Ukienda kinyume, vitachukua hatua kwa sababu ya kulinda Katiba. Zaidi hivyo ndiyo vyombo pekee vinavyoapa hata kufa ili kulinda nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumeapa kuiheshimu Katiba, lakini wao pamoja na kuapa kuiheshimu Katiba, wamekwenda mbali zaidi, ndiyo peke yao wanaoapa katika viapo vyao, kuna kufa kwa niaba ya nchi. Ila hiyo haina maana wafanye mambo kiholela, lakini daima tujue, nasi tumepata bahati, tumepita katika kipindi kigumu mwaka jana. Watanzania tunasahau haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingine za Ulaya nami nimekuwa na bahati, nimekaa miaka michache Ulaya, miaka 10 michache sana, lakini katika vipindi vigumu. Walifika zile nchi zilitangaza hata state of emergency. Mamlaka hayo Rais anayo ya kutangaza hali ya hatari chini ya Ibara ya 32 kwa eneo lenye matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kuchukua hatua ya kudhibiti hali ya Kibiti na Rufiji, hatukufika mahali Rais wa Jamhuri ya Muungano kutangaza hali ya hatari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Italia, Ujerumani na Uingereza, walipopitia katika hali hii na sitaki kuitaja nchi, Askari wao walipewa haki ya ku-shoot on site, sisi hatukufika hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri tuvipongeze vyombo hivi kwa ku-contain hali ngumu lakini bila kulifikisha Taifa ama Rais kutumia mamlaka yake ya Ibara ya 32 ya kutangaza hali ya hatari kwa eneo la Rufiji, Ikwiriri au kufika kutoa amri ambayo ingekuwa na madhara. Tuwapongeze, tuwape nguvu. Kwa kufanya hivyo, wamekufa. Polisi wamekufa; cold blood on behalf of the United Republic of Tanzania. Mimi na ninyi hatukuapa kufa.

Wao wameapa kufa. Watu walioapa kufa kwa niaba yenu muwastahi, lakini zaidi muwaombee Mwenyezi Mungu kwa sababu ndio peke yao wamechukua dhamana hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio watu wa kuwabagaza, kuwazoza, kuwakejeli, kuwadharau na kuwadhihaki. Mtakatifu Agustino wa Hippo aliwaonya watu wa Carthage walipoanza kuwa na majivuno, akasema siku wanaosafisha mitaro watakapoacha kusafisha mitaro ndipo watu mtakapojua umuhimu wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimesimama ili kutoa maelezo ya mambo mawili ambayo yameelekezwa kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo nadhani yanaangukia katika Sekta ya Sheria. Haya ni yale yanayohusu kesi ya Mashehe wa Uamusho wa Zanzibar na suala la Akwilini. Mambo haya yote mawili hayaihusu Wizara ya Mambo ya Ndani. Mambo yote haya mawili yanamhusu Mkurugenzi wa Mashtaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda Watanzania wote tuelewe, Mkurugenzi wa Mashtaka ameanzishwa kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 59B ambayo inaeleza wazi kabisa kwamba:

“kutakuwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ambaye atateuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa zilizoainishwa katika Ibara ndogo ya (2) na Ibara ya 59 na amekuwa na sifa hizo mfululizo kwa muda usiopungua miaka 10. Mkurugenzi wa Mashtaka atakuwa na uwezo wa kufungua, kuendesha na kusimamia mashtaka yote nchini.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwasomee Ibara ya (4):-

“Katika kutekeleza mamlaka yake Mkurugenzi wa Mashtaka atakuwa huru, hataingiliwa na mtu yeyote au mamlaka yoyote na atazingatia mambo yafuatayo:-

(a) Nia ya kutenda haki;
(b) Kuzuia matumizi mabaya ya taratibu za utoaji haki;
na
(c) maslahi ya Umma.”

Ibara hiyo hiyo unaikuta katika Katiba ya Zanzibar, Ibara ya 56A ambayo inaeleza wazi kabisa, hakuna anayeruhusiwa kumwingilia DPP hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana hata Zanzibar Ibara ya 56A inatamka wazi na niende kifungu cha nane (8) na chenyewe kiko very clear, “Hakuna mtu anayeruhusiwa kumwingilia Mkurugenzi wa Mashtaka.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Bunge hili hili lilipitisha Sheria Na. 27 ya mwaka 2008, The National Prosecution Services Act.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Ibara ya 19 ya kifungu hicho iko wazi kabisa. Mkurugenzi wa Mashtaka ana- enjoy security of tenure kama anavyo-enjoy Jaji wa High Court na ndiyo maana Rais hawezi kumwondoa DPP akishamteua. Ili amwondoe DPP na akidhani amefanya makosa au amekwenda kinyume, ni lazima amuundie Tribunal; na tribunal hiyo ni lazima iwe na Majaji watatu na mmoja awe wa Court of Appeal.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, aliondolewa na kupandishwa cheo kile kile cha Security of Tenure, huwezi kumshusha chini. Sifa yake ni kama ya High Court Judge, ndiyo maana huwezi kumtoa DPP kumpeleka chini. Ndiyo, hawezi na pale hakuondolewa, amepandishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkurugenzi wa Mashtaka ana uhuru kamili wa kufungua mashtaka na kuyafuta, ndiyo maana katika haya mambo mawili ambayo nataka kuyazungumza na kwa sababu Mkurugenzi wa Mashtaka hawezi kuingia Bungeni nimemwomba leo anipe maelezo ili nilieleze Bunge hatua anazozichukua kuhusu suala la Mashehe wa Uamsho na suala la Akwilini, yeye hawezi kuja hapa. Alikuwa Singida nimemwomba aje leo Dodoma ili atoe maelezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mashehe wa Uamsho wa Zanzibar ni suala nyeti sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea. Kwa hiyo, jambo hili nataka niwaambie Watanzania kwamba Serikali inatambua uwepo wa kesi hii na kuwa imechukua muda mrefu Mahakamani. Kwa hiyo, ni nia ya dhati ya Serikali kuona kuwa kesi hii inafikia mwisho. Hata hivyo ucheleweshwaji wake unasababishwa na mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme ni bahati mbaya sana watu tunaowajadili sasa wana heshima na hadhi ya Mashehe, lakini hawakuingizwa kwa sababu ya heshima ya hadhi ya Ushehe, ni kwa sababu kuna tuhuma za ugaidi. Tuhuma hizi ni lazima zipelelezwe. Kesho na keshokutwa akitokea mwanasiasa au nani ameshutumiwa, lazima yafanyiwe uchunguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa sababu adhabu yake ni kubwa na ndiyo maana Mashtaka ya Mauaji na mashtaka ya aina hii upelelezi wake unachukua muda mrefu ili mjiridhishe kabisa, mnapowapeleka Mahakamani kweli uko ushahidi unaotosha. Kwa sababu baada ya hapo wakitiwa hatiani adhabu yake ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kesi hii upelelezi pia umefanyika nje ya nchi ambapo tumeomba baadhi ya taarifa na vielelezo ili viletwe visaidie katika kesi hiyo. Ndiyo maana Mwendesha Mashtaka kupitia ofisi yangu ambayo ndiyo ina mamlaka ya kusaini hizo documents za kuomba nchi nyingine zitusaidie kuleta ushahidi, kazi hiyo imekuwa inafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inachukua hatua za kuharakisha upelelezi huo ili ukamilike mapema iwezekanavyo. Ndiyo maana nimesema hivi leo DPP alikuwa Singida nimemwita ili nipate maelezo haya ya kuliarifu Bunge lako. Naamini mambo haya yakikamilika, basi hatua za kisheria zitachukuliwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kutoa hotuba yangu leo asubuhi na kuwawezesha Waheshimiwa Wabunge kuchangia hotuba ya Wizara yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee, nachukua fursa hii kukushukuru wewe binafsi, kwanza kwa mchango wako mkubwa kwangu katika taaluma ya sheria. Mimi na Dkt. Harrison George Mwakyembe baada ya kuhitimu Shahada ya Sheria wakati wa mafunzo ya sheria, tukiwa State Attorney grade III Mheshimiwa Chenge ulikuwa Mkurugenzi wa Mambo ya Kimataifa na ulitusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pia, kwa miaka mitano niliyoazimwa katika Ofisi ya Makamu wa Rais kushughulikia mambo ya mazingira, ambapo tulifika tukatunga Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, wewe ulikuwa msaada kwangu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka, naomba niliseme ndani ya Bunge hili, kazi ya Muswada ule haikuwa rahisi, ilinizulia watu wengi na maadui wengi, wengine walioona husuda ya fedha niliyolipwa; na wengine ambao hawakuelewa kwa nini sheria ile itungwe. Kwenye kikao kimoja unakumbuka nilitolewa kwa hali iliyokuwa haikunifurahisha. Hata hivyo, wewe uliniambia jambo moja na leo nataka niliseme; “In public service, learn to swallow your pride. In public service learn to suppress your eagle.” Kweli mambo hayo sasa naona umuhimu wake ndani ya jengo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa George Masaju, Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ushirikiano alionipa katika kutekeleza majukumu yangu na kwa kuungana na mimi katika kujibu baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine, naishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge la Katiba, Sheria na Utawala pamoja na Kamati ya Bajeti kwa maoni na ushauri wao ambao wameipatia Wizara na Taasisi zake katika kutekeleza majukumu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizihakikishie Kamati na Waheshimiwa Wabunge wote kuwa tumepokea maoni, hoja na ushauri mliotupa katika mjadala wa Bajeti yetu na tunaahidi kufanyia kazi masuala yote yaliyojitokeza katika mjadala huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Kambi ya Upinzani, nashukuru pia kwa maoni yenu yaliyotolewa na kukubaliwa na Bunge hili kutoka kwa Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa mambo ya Katiba na Sheria; ni mdogo wangu, kaka yake Mheshimiwa Tundu Lissu, Ndugu Alute Mughwai na mimi tumesoma pamoja Milambo. Kwa sababu hayupo, sipendi kuleta mambo ya mila hapa ndani, lakini wale wote tunaotoka Singida mnajua mila yetu na heshima kwa watu, eeh, kwa neno lililokataliwa jana, waliotangulia kwa ngariba kabla ya wewe. (Makofi/Kicheko)
Mhesimiwa Mwenyekiti, niseme hili, nimeshangaa sana kuwa watu katika jengo hili kubagazana. Waheshimiwa Wabunge kama ni kawaida, ni kawaida mbaya. Hatuwezi kubagazana. Jengo hili siyo la kubagazana; na tunabagazana kwa sababu kwa bahati mbaya tumepoteza pia uelewa mzuri wa lugha ya Kiswahili. Tunazungumza Kiswahili kikavu kama alivyosema Mheshimiwa, Riziki Shahari Mngwali, tumepoteza uelewa wa Kiswahili wa kutumia lugha ya kumfanya mtu mpuuzi ajue ni mpuuzi bila kumwambia mpuuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukimsikia muingereza anakwambia your stupid, siyo muingereza. Muingereza mstaarabu ndani ya Bunge, atakwambia I am sorry, your level of appreciation of issues is diminishing, which means you are stupid! Yes. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ugeni una faida wa kusema mambo ambayo hayakufurahishi. Nimefundisha wanasheria, na mimi nimefundishwa. Mwanasheria yeyote worth being called a lawyer, he must have sense of respect and more so, as officer of the court to the judiciary. Ndiyo maana naanza kuelewa kwa nini nchi nyingine Bajeti ya Mahakama hailetwi Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa vitu ambavyo vinanisumbua na nilisema siku ya hotuba ya Mheshimiwa Mbowe na ninamheshimu sana kwa maturity yake, niliomba tusii-drag judiciary in our mucky politics. It is abominable! It is flabbergasting! Tusii-drag Mahakama katika mazungumzo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitaanza na suala la uteuzi wa Majaji, ikiwa ni pamoja na Jaji Mkuu na naomba mnisikilize; na kama hamniheshimu kwa umri wangu, I am above 60, mniheshimu kwa utu wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua nafasi ya Rais inagombewa, anachaguliwa…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafasi ambayo ndiye mkuu wa nchi, naomba mnisikilize.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafasi ya Rais tunayempigia kura, Rais wa Tanzania, Rais wa South Africa hapigiwi kura, anachaguliwa na Wabunge kama alivyo Waziri Mkuu. Ndiyo maana South Africa chama ni juu. Rais Zuma, chama kinaweza kikamwondoa leo, ndiyo kama kilivyomwondoa Mbeki. Hapigiwi kura. Lakini Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, anapigiwa kura. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Spika wa Bunge, anapigiwa kura. Mtu pekee wa mhimili ambaye hapigiwi kura, anateuliwa, ni Jaji Mkuu. Mnajua kwa nini?
Ni msingi wa kuhakikisha mtu huyu anayeteuliwa kushika nafasi hiyo, aachwe bila laumu ya mpumbavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme hivi, katika uteuzi wa Jaji, nafasi ya Jaji katika hili, kwanza siyo kweli kwamba hapajawahi kuwa na Kaimu Jaji Mkuu kwa kipindi. Mara baada ya Jaji wa mwisho wa Tanzania, muingereza Windham kumaliza muda wake, Tanzania 1965, Mwalimu hakuona sababu ya kuwa tena na Jaji Mzungu. Ndipo jitihada zilianza za kutafuta Jaji mwafrika na huyo Jaji alipatikana kutoka nchi ya Trinidad and Tobago Telford Philip Georgies. Ilichukua muda kwa sababu Majaji walikuwa wanasita kuja kwa sababu ya elimu ya watoto wao. Ni mwafrika, tena alikuwa mweusi kuliko wewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa vitu nawasifu waafrika, wamekaa kule miaka 500, wengine ni weusi kuliko sisi; na ni Waafrika kuliko sisi kwa sababu wameishi ugenini. Ndipo nafasi ile ilikaa kwa kipindi kirefu ikisubiri Jaji Telford Philip Georgies afike nchini aapishwe. These are facts. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, alichaguliwa mwingine akaimu kwa sababu daima nafasi ya Jaji Mkuu haiwezi kuwa wazi hata kwa dakika moja. Ndiyo maana hata Jaji Mkuu akisafiri, akiteuliwa mwingine kukaimu, anaapishwa. Hakuna Kaimu Jaji Mkuu ambaye haapishwi, hata kama atakuwa Kaimu Jaji Mkuu kwa siku mbili, ataapishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiangalia Katiba, iko wazi kabisa, inamruhusu Rais kuteua Kaimu Jaji Mkuu na haiweki mipaka. Haiweki, haiweki.Ukienda kwenye Katiba mpaka mwaka 2000 wakati Mwenyekiti akiwa Attorney General kabla ya hii 2005 kufanya marekebisho kupunguza maneno, niwasomee tafsiri ya Jaji Mkuu ilikuwa inasemaje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jaji Mkuu maana yake ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Rufani aliyetajwa katika Ibara 115(1) ambayo sasa ni 118 ya Ibara hii, ambaye ameteuliwa kwa mujibu wa masharti ya Ibara ndogo ya pili ya Ibara hiyo ya 118 au iwapo Jaji Mkuu hayupo au anashindwa kutekeleza kazi zake kwa sababu yoyote, Kaimu Jaji Mkuu aliyeteuliwa kwa mujibu wa masharti ya Ibara 118(4) ya Katiba hii na Kaimu Jaji Mkuu naye hayupo au anashindwa kutekeleza kazi yake, Jaji Mkuu, Jaji wa Mahakama ya Rufani aliyeko kazini kwa wakati huo na ambaye yuko kwenye daraja la juu zaidi la madaraka kupitia Majaji wote wa Mahakama waliopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiisoma ya sasa inaeleza wazi kabisa Jaji Mkuu ni nani, maana yake ni Jaji Mkuu anayetajwa kuteuliwa na ambaye majukumu yake yameelekezwa katika Ibara ya 118 ya Katiba. Ukiisoma hiyo ni pamoja na Kaimu Jaji Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake nini? Watu wengine wote wanaoteuliwa kukaimu, hawaapishwi. Ni Jaji Mkuu tu. Kaimu Jaji Mkuu anaapishwa, peke yake.Maana yake, kitendo cha kumwapisha kinampa mamlaka na ulinzi kamili wa cheo hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uteuzi wa Jaji Mkuu, mimi nalisihi Bunge liheshimu Mamlaka ya Uteuzi. Rais anayo mamlaka kamili ya uteuzi na Rais anavyo vigezo vingi vya uteuzi na Rais msidhani ni mtu anayetembea, ni taasisi. Hivyo, kwa sababu ni taasisi, haina macho mawili tu, ina zaidi ya macho mawili, tuiache ifanye kazi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwasihi sana Waheshimiwa Wabunge, tuache Kaimu Jaji Mkuu afanye kazi yake. Tusimfikishe mahali tukamtweza. Kwa sisi wanasheria, tuheshimu sana mhimili huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo napenda nilizungumzie ni kuhusu Rais. Ndiyo maana dada yangu Mheshimiwa Riziki Shahari Mngwali ametoa, ni kweli alichokisema. Kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba tulikuwa na Kamati tatu; Kamati ya Maadili na Haki za Binadamu chini ya Mzee Ussi, Mwenyekiti; Kamati ya Muungano, chini ya Mzee Butiku, Mwenyekiti na Kamati ya Mihimili, mimi nikiwa Mwenyekiti. Watu walionisaidia sana, nikiri ni Kibibi Mwinyi Hassan kutoka Unguja, Zanzibar na Mheshimiwa Riziki Shahari Mngwali kutoka Tanzania Bara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kuzunguka kule tulikuta nafasi ya Rais watu hawaielewi. Nimekuja na maoni hapa na mengine nimeyaacha. Watu hawaelewi nafasi ya Rais, yaani kama kuna nafasi ilikuwa inazungumzwa mpaka tunashtuka, ni nafasi ya Rais, mpaka tukajiuliza hawa Watanzania kwa nini nafasi hii hawaielewi? Tukabaini, tunachanganya mambo mengi katika nafasi ya Rais. Ndiyo maana tukasema, ni vyema tukapambanua tuelewe nafasi ya Rais na Rais ni nani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais anazo nafasi tatu; moja, ni Mkuu wa Nchi (Head of State); pili, ni Kiongozi wa Serikali na tatu ni Amiri Jeshi Mkuu. Sasa yako madaraka ya nafasi ya Rais kama Mkuu wa Nchi na kama Amiri Jeshi Mkuu yanayompa hadhi tofauti ambayo haistahili kubezwa na ndiyo maana Bunge kwa Kanuni limezuia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, Rais ni taswira ya nchi. Kwa nafasi yake ya Mkuu wa Nchi Rais ni taswira ya nchi. Malkia wa Uingereza kwa nafasi yake ya ukuu wa nchi, ni taswira ya nchi (Head of State). Kwa maana hiyo, yeye ndiyo alama ya umoja, yeye ndio alama ya uhuru wa nchi na mamlaka yake. Kumuonesha kwamba yeye ni alama ya uhuru wa nchi, ndiyo maana Rais peke yake anafuatana na mtu ambaye tumezoea kumwita mpambe, ambaye amevaa mavazi ya kijeshi. Maana yake ni kwamba anawaonyesha kwamba huyu ndiye alama ya Serikali yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo Rais ana dhamana ya kukuza na kuhifadhi umoja wa kitaifa, ana dhamana hiyo. Sasa ukiangalia madaraka ya Mkuu wa Nchi, yale huwezi kuyapunguza; lakini ukiangalia mamlaka yake ya Amiri Jeshi Mkuu, huwezi kuyapunguza na ukiangalia mamlaka yake kama Mkuu wa Serikali, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania majukumu ya Rais kama Mkuu wa Serikali, akiwa Mkuu wa Serikali, hayo unaweza kuyapunguza. Unaweza kuyasimamia, unaweza kuyadhibiti. (Makofi)
Mdogo wangu Tundu Lissu asubuhi ameeleza zile makala ya mimi na Mlimuka na ya Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe tuliyoandika wakati wa mfumo wa chama kimoja, tena tukielekea mabadiliko makubwa ya Katiba ya mwaka 1985. Niseme hivi, mwaka 1985 hii Katiba, Mzee Chenge yuko hapa, kwa maudhui hii siyo Katiba ya mwaka 1977, ni Katiba ya mwaka 1985. Iliandikwa yote upya. Kwa nini ilitwa Katiba ya mwaka 1977, ni kwa sababu The Constituent Assembly haikuwa convened. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa sababu Constituent Assembly haikuwa convened na kwa nini Mwalimu haku-convene Constituent Assembly?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu wapo watu wanaoamini the Constituent Assembly is only convened once. Only convened once. Ndiyo maana nilipokuwa amidi, Kiswahili cha dini ni amidi. Nilipokuwa amidi wa Shule Kuu ya Sheria, nimeanzisha course mpya ya Legal History na nimeifundisha mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nilianza course ya Legal History? Ni kwa sababu niligundua vijana wetu wengi wanaidhani Tanzania ni hii ilivyo leo. Hii ilivyo leo haikuwa hivi. Kabla ya mabadiliko yale, Bunge hili Wabunge wengi humu ndani walikuwa ni wa kuteuliwa na siyo wa kuchaguliwa, ndiyo! Tena nina fahari sana ya kuwa Mbunge wa Kuteuliwa, ndiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitawaambia kuwa sisi wasomi hakuna Doctorate unayoiheshimu kama Honorary (Honoris Causa), ndiyo. Unapokuwa Doctor Honoris Causa, tena ukiwa multi…
Kwa hiyo, wakati huo Waziri Mkuu yuko hapa hakuwa Mbunge wa kuchaguliwa, walikuwa ni Wabunge wa kuteuliwa. Ndiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo, Bunge lilikuwa ni Kamati ya Halmashauri Kuu ya Chama. Sasa mtu asiyejua historia atabeza mafanikio yaliyofikiwa.
Ndiyo maana Wangazija wana msemo, ukitaka kujua mafanikio ya mtu usiangalie kimo alichofika, angalia shimo alikotokea. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme mara baada ya kile kitabu kutoka, ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Harrison George Mwakyembe yupo, wako Mabalozi waliodhani Mwalimu angetutia kizuizini, yuko hapa. Leo ninyi mnaongea Sheria ya Kizuizini hayupo! Tuliongea wakati yupo. Don’t dare me, don’t dare me. We spoke when the law was law and when the President was President. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndiyo maana Katiba hii kwa mapendekezo ya wakati huo Mwalimu anaondoka ilikubaliwa kabisa, lazima madaraka ya Rais yapunguzwe. Someni mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya mwaka 1983/1984 na yalipunguzwaje? Moja ya kuyapunguza ilikuwa ni kuanzisha cheo cha Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Uwaziri Mkuu wetu huu, siyo kama wa Uingereza, huu ni kama wa Ufaransa. Kwa sababu ni kama wa Ufaransa ambapo Mzee Joseph Sinde Warioba alitumwa kwenda kujifunza, Mzee Msekwa alitumwa India na Canada, Waziri Mkuu wetu huyu mkisoma Katiba anatokana na chama chenye Wabunge wengi na anapigiwa kura ndani ya Bunge. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, aina hii ya Katiba yetu ambayo una Mkuu wa Nchi ambaye amechauguliwa na wananchi moja kwa moja, siyo kama wa Afrika Kusini na una Waziri Mkuu anayetokana na chama chenye Wabunge wengi au anayeungwa mkono na wengi, kinaweza kukupa aina ya government inayoitwa kwa Kifaransa kohavision.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna hiyo, madaraka ya Rais yakawa yamepunguzwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kubwa lililofanyika mwaka huo, ilikuwa ni kuweka ukomo wa Rais. Mwalimu alitawala kama Rais miaka 23, anaondoka madarakani sisi ilikuwa ndiyo nchi ya kwanza Barani Afrika kuweka ukomo wa Rais kuwa ni vipindi viwili vya miaka mitano mitano. Eeh, kule Cameroon, Rais Ahidjo; Wafaransa walipomchoka Rais Ahidjo, wakamwambia anaumwa; alipoondoka akagundua haumwi, hawezi kurudi. Rais Sédar Senghor wa Senegal alikuwa ndiye Rais wa pili kung’atuka na yeye kuweka term limit. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu muhimu ndani ya Katiba hii, lilikuwa ni kuweka sura ya haki za binadamu. Hazikuwepo wakati huo, hazikuwepo. Ndizo hizo leo, Ibara ya 12 mpaka ya 29, hazikuwemo. Hayo ndiyo maendeleo na mapito ambayo nchi hii imeyapitia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya mwaka 2005 kuhusu haki za binadamu, yaliyondoa clawback clauses zote. Tena yalikwenda mbali, hayakuondoa tu clawback clauses, yaliondoa hata enabling clauses.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachotaka kusema katika mambo ya Katiba, eeh, lecture room, kwa sababu Waswahili wana msemo, mwana wa muhunzi asiposana hufukuta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu zangu, tumefika hapa tulipofika kwa sababu nchi hii imejaliwa kuchukua maamuzi kwa wakati, lakini maamuzi hayo ni lazima yajenge umoja wa Taifa, maamuzi hayo ni lazima yajenge mshikamano, ni lazima yajenge utu, ni lazima yalenge ustawi wa watu. Ndiyo maana katika Katiba hii kama kuna Ibara naisoma kila siku, ni Ibara ya nane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, at the bottom line wananchi ndio source ya mamlaka yote, sio sisi. Kwa hali hiyo, nashauri sana tutunze heshima ya Rais akiwa Mkuu wa Nchi, tutunze heshima ya Rais akiwa Amiri Jeshi, lakini inapokuja kwenye nafasi ya ukuu wa Serikali, isimamiwe na ishauriwe. Hapa ndani ni kupitia kwa Waziri Mkuu na Baraza la Mawaziri lililomo humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja mbalimbali zimetolewa, jumla ya Waheshimiwa Wabunge 24 wamechangia hotuba yetu ambapo Wabunge 17 wamechangia kwa maandishi na Wabunge saba wamechangia kwa kuzungumza. Miongoni mwa mambo ambayo yamezungumzwa, yako ambayo yamegusa vyombo na mambo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na hoja zilizotolewa kuhusu Mahakama; hoja kubwa iliyotolewa na Mahakama ni kuhusu ujenzi wa majengo ya Mahakama. Ujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu, za Wilaya na za Mwanzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kueleza kwa ujumla kwamba moja ya changamoto kubwa zinazoikabili Mahakama ya Tanzania ni uhaba na uchakavu wa miundombinu. Mathalani katika ngazo ya Mahakama za Wilaya, tuna majengo katika Wilaya 30 na Wilaya nyingine huduma zinatolewa katika majengo ya kuazima kutoka taasisi nyingine za Serikali. Aidha, tuna Wilaya 23 zinapata huduma za Mahakama katika Wilaya za jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa upande wa Mahakama za Mwanzo kuna Mahakama 960 tu kati ya Mahakama 3,963 zilizopo nchini. Sasa katika kukabiliana na changamoto hii, Wizara kwa kushirikiana na Mahakama imeanza kutekeleza mpango wa ujenzi katika ngazi zote za Mahakama. Kwa hiyo, kupitia mpango huo, katika kipindi cha miaka mitano tumepanga kuhakikisha kwamba mikoa yote itakuwa na majengo ya Mahakama, ndani ya miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika hiyo miaka mitano, imepangwa kujenga Mahakama za Wilaya 109 na Mahakama za Mwanzo 150 katika maeneo mbalimbali nchini. Kwa hiyo, kwa msingi huo ni matarajio yetu kuwa hadi mwaka 2021 Wilaya zote nchini ziwe na majengo ya Mahakama, huo ndiyo mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika mpango huo yapo maeneo ambayo tunaomba msaada, moja likiwa Jimbo la Mheshimiwa John Mnyika, tusaidiwe kupata viwanja, mahali ambapo tunaweza tukajenga Mahakama na pia Wilaya nyingine. Nimetaja yako Mheshimiwa Mnyika kwa sababu nimeona umeleta mchango wako kwa maandishi na nimeu-note. Sasa tukishapata viwanja hivyo, itatusaidia sisi kuweza kujenga Mahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limeelezwa na michango ya Waheshimiwa Wabunge wengi ni kuhusu Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo kukaa muda mrefu katika kituo kimoja. Sasa hili limechangiwa na gharama za uhamisho na vituo vya kuhamishwa kwa watumishi wote wa Mahakama ambao ni pamoja na Mahakimu wa Mwanzo. Gharama ya zoezi hili inakwenda takriban shilingi bilioni 2.3.
Kwa hiyo, Wizara yangu kwa kuthamini kwamba ni vyema Mahakimu au Mahakama za Mwanzo wakawa wanapata uhamisho, kwa sababu kukaa mahali pamoja muda mrefu na wewe unakuwa sehemu ya ile jamii.
Kwa hiyo, tunashirikiana Wizara na Mahakama kuhakikisha kwamba tunaongea na Hazina ili kulifanyia suala la upatikanaji wa fedha za uhamisho wa watumishi wakiwemo Mahakimu waliokaa kituo kimoja kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo limezungumzwa kuhusu Mahakama ni juhudi za kuondoa mlundikano wa mashauri katika ngazi zote za Mahakama. Sasa Mahakama ya Tanzania pia imeweka muda maalum wa mashauri kuwa mahakamani. Kwa Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya, shauri linatakiwa kukaa mahakamani kwa muda wa miezi 12. Mahakama za Mwanzo, shauri linatakiwa kukaa muda wa miezi sita tu. Kwa Mahakama za Mwanzo hazina mashauri yanayozidi miezi sita. Sasa kama ambavyo tumeeleza katika hotuba yetu na maelezo ya Mahakama, Mahakama ya Tanzania imejiwekea mpango wa kuondoa mlundano wa mashauri katika ngazi zote za Mahakama, iwe ni Mahakama ya Hakimu Mkazi au ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya zina mashauri 2,912 yanayoangukia kwenye mlundikano. Mashauri hayo yako katika Programu Maalum ya Uondoaji wa Mlundikano wa Mashauri inayoendelea nchi nzima. Nachukua fursa hii tena kuipongeza Mahakama kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kuhakikisha kwamba kesi zote za uchaguzi wa Wabunge na Madiwani zinamalizika ndani ya muda uliopangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni la kihistoria na ni vyema tukaipongeza Mahakama, kwa sababu ni mara ya kwanza kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi zimemalizika katika kipindi kifupi. Huko nyuma tunafahamu, mpaka kipindi cha Bunge kilikwisha kesi bado zinaendelea Mahakamani. Kwa hiyo, ni imani yangu kwangu kwamba rasilimali fedha ikiongezeka, uhamisho wa Mahakimu utafanyika, ajira zaidi zitapatikana na majengo ya Mahakama zaidi yatajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia ingawa Mwanasheria Mkuu wa Serikali amelizungumzia na mimi pia napenda nilizungumzie. Suala lolote linamlohusu Mtanzania yeyote au mtu yeyote kufunguliwa mashtaka na kupelekwa Mahakamani au
kuwekwa mahabusu au rumande, siyo suala ambalo mtu yeyote angelifurahia. Tungependa uhalifu usiwepo, tungependa wahalifu wasiwepo, lakini hulka ya binadamu, tunatenda makosa. Makosa yakitendeka kwa mujibu wa sheria, lazima mtu aitwe, ahojiwe, kesi ifunguliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimeanza na hilo, niliseme wazi. Serikali haifurahii kuona watu wako ndani. Ingetokea muujiza leo pakawa hakuna uhalifu na Magereza yakafungwa, lingekuwa ni jambo la furaha kubwa sana, lakini huo ni utashi na mapenzi ambayo ni vigumu kuyatekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama alivyosema Mwanasheria Mkuu wa Serikali, moja ya mambo ambayo yamezungumzwa sana humu ndani, ni suala la kesi inayohusu Mashehe wa Zanzibar ambao wameshitakiwa chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi (Prevention of Terrorism Act) ambayo inatumika Tanzania Bara na Zanzibar. Sasa maadam suala hili liko mahakamani, kama alivyosema Mwanasheria Mkuu wa Serikali, sisi kazi yetu kubwa tuharakishe uchunguzi na kesi ikamilike mahakamani. Sasa uchunguzi unategemea mambo mengi ambayo pia siyo vyema kuanza kuyazungumza ndani ya Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufanya hivyo tutakuwa badala ya kuisaidia kesi hii, labda tukaivuruga zaidi. Kwa hiyo, naomba tuendelee kuviachia vyombo vinavyofanya shughuli hiyo pamoja na Mahakama na wachunguzi lakini kwa kadri inavyowezekana kesi hii kama kesi nyingine zozote zile imalizwe mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumziwa na Waheshimiwa Wabunge ni suala zima la Katiba mpya. Napenda nirudie maelezo yale yaliyotolewa. Katika jambo hili niseme kama nilivyoeleza katika maelezo yangu kwenye Kamati nilipoulizwa, Serikali inatambua umuhimu wa Katiba mpya, lakini Katiba siyo kitabu hiki tu. Ziko nchi hazina katiba iliyoandikwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waingereza hawana Katiba iliyoandikwa. Ukiwauliza Waingereza leo Katiba yao ni nini? Ni mila na desturi. Israel haina Katiba iliyoandikwa; na kwa kuwakumbusha, Zanzibar toka mwaka 1964 baada ya Mapinduzi mpaka mwaka 1979 haikuwa na Katiba iliyoandikwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, mimi na Mheshimiwa Dkt. Harrison George Mwakyembe tutamkumbuka Mwalimu wetu wa Katiba, Profesa Srivatava aliyetuambia Katiba siyo hicho kitabu, ni ujumla wa maisha yenu yote, matamanio yenu, matarajio yenu na shida zenu. Hii ambapo Waingereza wenyewe hawakuwa na Katiba ya kuandika na mpaka leo hawataki, walituandikia sisi na sijui niliseme maana yake nimekuwa Waziri, wakiamini kwamba ninyi hamna uwezo wa kuwa na mila na desturi zinazostahili kuwa Katiba. Kwa hiyo, wawaandikie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Katiba yetu ya uhuru ya mwaka 1961, actually it was a schedule to an Act of Parliament which was passed by the House of Commons. The Tanganyika Order in council and accented by the Queen, not in Buckingham Palace, in St. George Chapel, Windsor . (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, maana yake kama alivyosema dada, Mheshimiwa Riziki Shahari Mngwali, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa siyo Rasimu tu; tuliangalia Rasimu tu na nimekutaja kwa kazi kubwa uliyofanya. Tulitoa Juzuu hii, maoni ya wananchi kuhusu sera, sheria na utekelezaji, iwe sehemu ya hiyo Katiba inayoishi. Ndani ya mambo hayo, niwasomee moja tu ambalo wananchi walituambia, ni safari za viongozi, ukurasa wa 38 kwamba safari za viongozi ziwe na kikomo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huyu anasafiri sana? Wakasema, malengo ya safari za nje za viongozi yawe wazi kwa wananchi. Niwaambie jambo moja walilolisema, na mimi ningetamani
liwe, matumizi ya neno mheshimiwa, mapendekezo ya wananchi. Mapendekezo ya wananchi kuhusu matumizi ya neno mheshimiwa yalikuwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, neno mheshimiwa lisitumike kwa Wabunge na viongozi wengine wa umma, badala yake neno ndugu litumike ili kuondoa matabaka na kuwakweza viongozi juu ya wananchi ambao kimsingi ndio waliowaweka madarakani. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sehemu kubwa kama alivyosema Mheshimiwa Shahari Mngwali…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKTI: Mheshimiwa Waziri, malizia tu.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Mheshimiwa Shahari Mngwali, kitu kikubwa kilichozungumzwa na wananchi humu, ni maadili ya viongozi. Moja, wananchi walipendekeza viongozi wote wakiapishwa, waape maadili ya viongozi. Tunaapa au hatuapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi, mimi, mimi…
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kitabu hiki nitakikisha tunakipa uzito unaostahili kwa sababu ndiyo maoni ya wananchi ya Katiba inayoishi. Kwa hiyo, tayari matashi ya wananchi yameanza kutekelezwa. Ndiyo maana kwa sasa kama nilivyosema kwenye Kamati, kazi tunayoifanya ni kazi ya kuzichambua sheria, ndiyo maana haina kasma. Si ni kazi za siku zote, ndiyo maana haikutengewa fedha, kwa sababu ni kazi tunayoifanya ndani ya Serikali. Ni kazi ya kila siku, tunaangalia sheria zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, nawaambia mambo makubwa kama haya hayataki shinikizo. Mambo makubwa kama haya yanataka umuombe Mwenyezi Mungu akufanye uwe mwerevu kama nyoka na mpole kama hua ili ufikie unapotaka Taifa likiwa moja. (Makofi)
(Hapa kengele ya pili ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi na Wabunge wametoa maoni mengi na ninataka niwahakikishie kwamba maoni yote tumeyapokea na kwa utaratibu uliopangwa na Bunge, tutahakikisha kila aliyetoa hoja yake, jibu lake linapatikana kwa utaratibu uliopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nami nianze kwanza kwa kuwapongeza sana Waziri na Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, nimesimama kwa kuelewa kwamba sekta ya mifugo na uvuvi zinagusa sana mambo ya sheria. Katika utekelezaji wa sheria, tufahamu kwamba sheria inaweza kuwa nzuri lakini utekelezaji wake ukawa na kasoro hapa na pale. Kasoro zinazojitokeza katika utekelezaji wa sheria zisitufanye tuone kwamba ile sheria haifai kabisa.

Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa na wewe unafahamu kabisa kwa sababu unatoka kwenye eneo hilo ni kuweka uwiano kati ya uhifadhi na matumizi ya rasilimali ili wananchi wetu waweze kuneemeka. Kwa hiyo, pamoja na mambo yote tunayoyazungumza, napenda Waheshimiwa Wabunge tuzingatie kabisa kwamba sheria hizi zote zimetungwa kwa nia njema ili kwa upande mmoja tuhifadhi wanyamapori, misitu na samaki kwa faida yetu sisi na vizazi vijavyo. Hata hivyo, najua kwamba katika utekelezaji kumekuwa na matatizo ya hapa na pale.

Mheshimiwa Spika, nimesimama kueleza jambo fupi tu kuhusu baadhi ya mifugo iliyokamatwa na kutaifishwa katika mbuga zetu za hifadhi. Nalisema hilo kwa sababu linaangukia pia katika Ofisi ya Mashtaka na chini ya Mkurugenzi wa Mashtaka.

Mheshimiwa Spika, nipende kueleza Bunge lako kuwa baada ya kupata malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi kupitia kwa Waziri wa Mifugo, jana Mkurugenzi wa Mashtaka amepitia mashtaka mbalimbali ambayo yamefikishwa mbele yake ili kuona ni yapi anaweza kuyachukulia hatua. Kwa kupitia mamlaka yake aliyonayo kwa sheria na katiba, ameamua kuachia ng’ombe 553 za wafugaji katika eneo la Swagaswaga ambao baadaye wataelezwa utaratibu. Kwa hiyo, Mkurugenzi wa Mashtaka ameamua kwamba katika kesi hizo nne katika eneo la Swagaswaga ambalo linahusu ng’ombe 553 hatakata rufaa na amri imetolewa ng’ombe hao waachiwe kuanzia leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zipo jumla ya kesi tano zina rufaa katika Mahakama ya Rufaa ambapo Mkurugenzi wa Mashtaka amekata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu. Kesi hizi kwa sababu ziko Mahakamani tunaomba ziendelee lakini ambacho tutajitahidi kuiomba Mahakama ziharakishwe kusikilizwa.

Mheshimiwa Spika, pia ziko kesi nyingine ambazo wenyewe wafugaji wamekata rufaa. Tungewaomba wafugaji wenyewe waliokata rufaa katika kesi hizo ni vyema wakashauriwa kufuta rufaa zao ili pia kuharakishwa kuachiwa kwa mifugo yao, kwa sababu kama kesi ziko kwenye Mahakama ya Rufaa zitaendelea kusikilizwa.

Mheshimiwa Spika, kuna jumla ya kesi 23 kati ya 27 ambapo watuhumiwa walilipa faini bila kupelekwa Mahakamani na wakarejeshewa mifugo yao. Pamoja na kulipa faini ambayo ni kati ya shilingi 10,000 na shilingi 300,000 lakini bado kuna malalamiko kuwa wamelipishwa faini kubwa kinyume cha sheria. Tungependa wale wote ambao wana malalamiko ya kweli wayawasilishe ili pia yaweze kufanyiwa kazi ili pale panapolazimika haki itendeke.

Mheshimiwa Spika, la jumla na mengine tutayazungumzia siku ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka baada ya kuwa ametengeneza maelekezo mahsusi kwa Wapelelezi na Waendesha Mashtaka kwa ajili ya kesi zinazohusu wanyamapori na kuzinduliwa na Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sasa anajipanga kutengeneza mwongozo mwingine kwa ajili ya Maafisa wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili ziweze kuweka utaratibu wa kushughulikia kesi zinazohusu mifugo, uvuvi na atashirikiana na Mahakama ili kuona jinsi gani kesi zinazohusu mifugo zitaendeshwa mapema.

Mheshimiwa Spika, katika Bunge hili tutaleta Muswada wa kuanzisha Mahakama Zinazotembea (Mobile Court). Ni imani yetu kwamba Mahakama hizo zikiundwa kwa kushirikiana na Wizara zinazohusika operation hizi zitakapofanywa basi hiyo mahakama inayotembea itakuwa hapo ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kuunga mkono hoja. Pili, nianze kwa kukushukuru sana wewe na pia nimshukuru sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Shukrani zangu zina msingi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipata heshima ya kukusimamia Masters yako na uliandikia kuhusu The Rights to Clean and Health Environment na case study yako ilikuwa ni Geita Gold Mine. Ingawa nilikusimamia lakini nilijifunza na sikujua hayo ni maandalizi ya baadaye ndani ya utumishi wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nimshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye na yeye nilimsimamia PhD yake katika somo hili hili alilolizungumza leo na yeye kwake nimejifunza sana. Sikujua kwamba nilikuwa naandaliwa kuja kufanya kazi ambayo itahusiana na hawa wanafunzi wangu wawili ambao pia ni walimu wangu wakati huo, yaani Naibu Spika na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ni heshima kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, nimshukuru sana na mimi Mwalimu wangu aliyenisimamia PhD yangu Ujerumani, chuo ambacho sasa kinafikisha miaka 70 na yeye amestaafu. Kwa sababu miaka ile ya mwisho wa 80 na mwanzo wa 90 wakati tunayazungumzia haya aliyoyaeleza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa nchi za Ulaya yalikuwa ni mapinduzi makubwa. Sikujua kwamba baadaye nitapata fursa ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kunipa fursa ya kuitumikia nchi hii na kunipa jukumu la kuisaidia nchi hii kutunga sheria hizi za madini na mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, falsafa na muktadha wa usimamizi wa madini katika nchi zetu umebadilika. Napozungumza falsafa narudi kwenye Kitabu cha Ibrahim Hussein cha Mashetani, yule shetani mmoja aliyekuwa daima anasema weltanschauung, weltanschauung. Weltanschauung maana yake ni muono mpya wa mambo ambayo yalikuwa dhahiri lakini watu walikuwa hawaoni yakiwa dhahiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unyonyaji wa madini yetu na mataifa ya nje lilikuwa ni jambo dhahiri lakini hatukuliona kuwa ni dhahiri na likapambwa, likarembeshwa likafanya kuonekana ni jambo la kawaida na tukashindwa kutofautisha kati ya uwekezaji (investment) na unyonyaji (exploitation). Kwa hiyo, kwa muda wote huu sheria zetu za madini zilijikita katika unyonyaji (exploitation) na hatukuwa tumeweka mazingira mazuri ya uwekezaji (investment) kwa faida ya nchi zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hatua tulizozichukua ni hatua za kimapinduzi na ni lazima zipingwe kwa nguvu zote na wale wote waliokuwa wanafaidika na hali hiyo. Kwa hiyo, ni jukumu letu kusimama kidete pamoja na Rais wetu kuhakikisha kwamba hii weltanschauung (msimamo) mpya tunausimamia kwa nguvu zetu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana mingoni mwa mambo makubwa ambayo yamefanywa na sheria hii ni kuondoa kabisa Mining Development Agreements, zilizoingiwa ndizo za mwisho. Kuanzia sheria hii ilipopitishwa, hakuna tena MDA ni Special Mining License, Mining License na Primary Mining License. Kwa sababu ya matatizo ya utendaji ndani ya Wizara na Kamisheni sasa Special Mining License na Mining License zitatolewa kwa kibali cha Baraza la Mawaziri. SML ni Baraza la Mawaziri ili Serikali nzima ishiriki katika kuhakikisha kwamba leseni za madini za wachimbaji wakubwa zinatolewa kwa manufaa na maslahi ya nchi yetu, hakuna tena MDA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunahangaika na MDA zilizokuwa zimeingiwa lakini hakutakuwa na mpya ili tuondokane na kuwa na matabaka mawili ya wachimbaji wanaochimba kwa leseni na wanaochimba kwa mikataba maalum, wote sasa watachimba kwa masharti ya leseni na asiyetaka hivyo asije. Madini haya babu wa babu zetu, babu zetu, baba zetu na sisi tumeyakuta hayajaoza, asiyetaka kuja kuchimba madini haya kwa masharti haya ayaache na sisi tutakufa, tutazikwa watakuja watoto, wajukuu na vitukuu wetu watavikuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema madini ni utajiri unaokwisha na ni muhali kuyatumia kwa matumizi ya kawaida. Ni lazima yatumike katika uwekezaji wa kukuza ustawi wa watu na maendeleo ya nchi katika miundombinu na viwanda na uwekezaji wa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yoyote inayochimba madini for recurrent expenditure imefilisika. Madini ni lazima yaende katika strategic investment; standard gauge railway, Stiegler’s Gorge, viwanda na miundombinu. Maana yake tuvune madini kwa kiasi, tusiyavune madini kwa pupa kama vile mwisho wa dunia ni sisi, tutakufa tutaiacha nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuvune madini kwa kiasi ili vizazi vijavyo navyo viyakute madini na yale tutakayokuwa tumeyachimba wakute faida yake katika sekta nyingine za uchumi; miundombinu, vyuo vikuu, viwanda. Hivyo ndivyo ilivyofanya nchi ya Nigeria na ndiyo hilo Naibu Spika ulilizungumzia katika Taslifu yako ya Masters, intergeneration equity. Sisi kwa lugha ya zamani ni mawakili wa mali za Mungu siyo kwa matumizi yetu sisi tu lakini kwa vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naonya hii shauku/hamu/pupa ya kutaka tuyachimbe madini yote; tuyabakize mengine kwa viazi vijavyo. Bara la Afrika tumekuwa tunasukumwa na nchi za nje kutaka tuchimbe madini yetu kwa namna hiyo. Ndiyo maana baada ya hatua hii iliyochukuliwa, nashukuru sana nchi nyingine za Afrika zimefuata na nchi ya mwisho ambayo nilitegemea ingefuata mfano wa Tanzania ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Zambia wamefanya hivyo na nchi nyingine ili tuyatunze haya madini ya Afrika kwa vizazi vijavyo kama ambavyo Norway wao mafuta wanayoyachimba wanaweka akiba kwa ajili ya vizazi vijavyo na kuna fedha ambayo imewekwa itatumika miaka 50 baada ya tone la mwisho la mafuta na gesi ya mwisho kwisha. Kwa hiyo, unaona wenzetu wanavyofikiria na sisi pia ndiyo malengo ya sheria hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mabadiliko haya ya kisheria, Mheshimiwa Rais ametusaidia sana, moja ni la makinikia. Makinikia yalisemwa si mali ni mchanga hauna maana lakini sote tumeona mara baaada ya makinikia kuzuiwa kwenda nje ndiyo tumejua kwamba makinikia ni mali, ni rasilimali. Ndiyo maana ndani ya mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017 imetamka wazi kuwa sasa makinikia nayo ni mali inayouzwa kama mali inayojitegemea, si kama sehemu ya yale madini yaliyokuwa yamepimwa. Kwa hiyo, limetusaidia na ndiyo maana tangu sheria hii imetungwa hakuna makinikia ambayo yameshatoka nje ya nchi ili uwekwe utaratibu wa kuyaongezea thamani makinikia kama bidhaa inayojitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo hatukulijua ndani ya makinikia kuna aina ya madini ingawa kiasi chake ni kidogo lakini yana thamani kubwa sana yanaitwa rare-earth, ya thamani kubwa sana. Kwa hiyo, utaratibu mpya umekwishafanyika na kanuni zimekwishatungwa na Mheshimiwa Waziri zitakazosimamia suala hilo la makinikia na itakuwa ni marufuku kuyasafirisha makinikia nje ya nchi kinyume na masharti yaliyowekwa na Sheria ya Madini na Kanuni zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mambo ambayo pia yamezungumzwa na kuulizwa sana hapa ni kuhusu kishika uchumba cha majadiliano kati ya Barrick na Tanzania. Kwanza nichukue fursa hii tena kumshukuru Mwenyezi Mungu na pili nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani kubwa sana aliyotupa sisi kusimamia majadiliano hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sakata hilo lilipoanza tulitishwa, tuliambiwa tutafilisiwa, hatutafika popote na hiyo ndiyo ilikuwa sababu kwa kiasi kikubwa ya kuwaficha wajumbe wengine kwa sababu bahati mbaya nchi yetu tumeacha kujadili masuala, tunajadili watu. Watu wangejua mmoja wa wajumbe hao ni Chacha, basi huyo Chacha angechambuliwa mpaka angechacha kama chakula kilichokaa siku nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mazungumzo yale yaliyokamilika tarehe 19 Oktoba, 2017 yalikuwa ya mafanikio. Mafanikio mimi kama mmoja wa watu walioshiriki, siyo kile kilichopatikana lakini kile ambacho kimetuwezesha sasa kuangalia Tanzania ya kesho katika matumizi yake ya madini. Hii ni kwa sababu tumerithi mikataba ambayo iliyokuwa ina matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yale makubaliano yalikuwa makubaliano ya msingi na baada ya hapo tumeingia katika majadiliano ya kina ambayo napenda kusema kwamba yanaendelea vizuri kati ya timu ya Serikali na Barrick na majadiliano hayo yanakaribia kufikia hatma yake. Kwa mujibu wa ratiba ambayo tulikuwa tumepeana, mwisho wa mwezi Juni au katikati ya Julai tutakuwa tumefikia katika hatua za mwisho na ukamilishaji wake ni pamoja na utaratibu wa ulipwaji wa malipo hayo ya Dola milioni 300. Kwa hiyo, tunaendelea na Inshallah, ndiyo maana ya neno Inshallah, maana Inshallah ni mapenzi ya Mungu (Allah) siyo hiyari yako, Inshallah, Inshallah mazungumzo hayo yatazaa matunda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba shughuli hiyo haikuishia tu na Barrick, tunafanya mazungumzo na kampuni nyingine. Tumekwishamaliza mazungumzo na Kampuni ya Tanzanite One Mining Limited, mazungumzo ambayo yalifanikiwa na kusainiwa makubaliano tarehe 15 Aprili, 2018. Wao wamekiri makosa waliyoyafanya, watalipa kodi na tozo zote na pamoja na hiyo watatoa fidia kwa Serikali; na tayari installment ya kwanza ya fidia hiyo imeshalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunaishi dunia ambayo tumejifunza, utakapotaja mambo kama hayo wale wasiotutakia mema ambao wanafungua kesi kesho na keshokutwa, watajua mna kiasi gani maana yake nyumba yenye fedha/mali ndiyo wezi huinyemelea. Ndani ya Serikali na kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali atajua fedha hizo zilipoingia na zilipo kwa sababu haziingii kama maduhuli ya Wizara ya Madini, zinaingia kama fidia kwa Taifa na zina utaratibu wake na zinasimamiwa na Katibu Mkuu Kiongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nchi tumejifunza hata hiyo fidia hatutaitamka katika kadamnasi lakini ndani ya Serikali na wale wanaoruhusiwa kujua watajua ni kiasi gani Tanzanite One Mining Limited wamelipa. Maana yake tumejifunza sasa hivi kesi zimeongezeka kwa sababu wanajua tuna hela, kwa hiyo ni upuuzi pia kusema kila kitu. Unapowaambia watu una pesa unaita watu kuja kukuibia lakini fedha ipo, utaratibu upo, Paymaster General na Auditor General yupo na nashukuru sana Tanzanite One Mining Limited kwa kutekeleza ya kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeanza pia mazungumzo na Ashanti Gold na tutaendelea nayo tena Julai, tumekwishakutana nao mara moja. Tutafanya majadiliano na kampuni nyingine za tanzanite, kampuni kama 10 zinazovuna tanzanite. Tutafanya mazungumzo na kampuni zote, Kampuni ya Williamson Diamond Limited ambayo karibu tutaanza nao mazungumzo lakini pia Al - Hillary.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni mlolongo wa mazungumzo na kila yatakapokwenda Taifa litakuwa linaarifiwa, lakini kwa muktadha na hali ya leo kiasi cha fedha kitaingizwa Hazina na hatutapenda kukitangaza sana na watu watafahamu kwa njia nyingine ili tuepukane na hali ambayo tumejifunza kwamba baada ya watu kujua tuna fedha, tunajenga standard gauge railway, tumenunua ndege saba sasa yanakuja madeni mengine ya miaka ya 70. Mtu alikuwa na deni toka mwaka 1978 leo ndiyo analikumbuka, nje huko na ukilisoma unajiuliza tangu mwaka 1978 huyu mtu hizi fedha mbona alikuwa hadai, ni kwa sababu sasa wamejua kuna kitu. Kwa hiyo, nawaomba Watanzania watuelewe, waielewe Serikali yao na waivumilie inapopambana na hali hii ya unyonyaji mkubwa na hatua ambazo imezichukua ili kuyarekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nimpongeze sana Waziri wa Madini na Naibu Mawaziri wa Madini. Naomba tena kurudia kuunga mkono hoja, niliogopa nisije nikapigiwa kengele kabla sijaunga mkono hoja mwanzoni, ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishukuru sana Kamati ya Katiba na Sheria na Kamati ya Sheria Ndogo kwa taarifa nzuri ambazo wameziwasilisha mbele ya Bunge hili. Mengi ambayo wameyaainisha katika ripoti zao kama mapendekezo tutayafanyia kazi ili kuboresha huduma zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Watanzania tuna bahati kubwa sana ya kuzaliwa katika nchi hii ya Tanzania na katika mfumo ambao unatoa haki na uhuru kwa watu kuliko nchi nyingi nyingine. Watanzania tuna uhuru, tuna haki ambazo zinalindwa na Katiba lakini viko pia viko vyombo vingi ambavyo vimeundwa kuhakikisha kuwa haki hizo ambazo ziko ndani ya Katiba zinaheshimiwa au zinafuatwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni miongoni mwa nchi chache sana katika Bara la Afrika ambazo hazifiki nne, ambazo zimewaruhusu raia wake kuweza kuishtaki Serikali katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu. Hivi tunapozungumza sasa katika Mahakama hiyo yako mashauri 113 ambayo yamepelekwa na Watanzania dhidi ya Serikali. Nchi moja ya jirani baada ya kufanyiwa hivyo imejiondoa katika Mahakama hiyo. Tunavyozungumza leo asilimia 75 ya mashauri yote katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu yanatoka Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Watanzania sasa wana haki na wameitumia haki hiyo kwenda kufungua mashtaka dhidi ya Serikali kwa madai mbalimbali katika Mahakama ya Afrika ya Mashariki. Tunapozungumza sasa mashauri 13 ya Watanzania wanaodai kuwa haki zao za binadamu zimevunjwa yako katika Mahakama ya Afrika ya Mashariki. Nchi nyingine zimehakikisha raia wao mashtaka hayo hayaendi na sina haja ya kuzitaja kwa sababu zinafahamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tunavyozungumza sana yako zaidi ya mashauri ya Kikatiba 40 katika Mahakama Kuu ya Tanzania; mashauri matano ya Kikatiba katika Mahakama ya Rufaa, hayo yote yanaonyesha kwamba tunao mfumo na taasisi zinazowawezesha Watanzania kusimamia haki zao. Ndiyo maana hivi karibuni Mahakamu Kuu, katika kesi ya Emmanuel Simphorian Masawe imetoa mwongozo wa jinsi ambavyo Mkurugenzi wa Mashtaka atatumia mamlaka aliyonayo kuhusu suala zima la kutoa certificate ya kuzua bail inapohitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi tunajadili suala la haki za binadamu hapa nchini bila kuangalia maamuzi ya Mahakama. Labda hilo nisiwalaumu Watanzania, nijilaumu mimi pamoja na Maprofesa na wasomi wengine ambao tumeshindwa kuandika commentary ya maamuzi ya Mahakama ya Rufaa ambayo yametoa tafsiri ya vifungu mbalimbali vya Katiba ndiyo maana kila mtu amekuwa anasoma Katiba ilivyo bila kwenda kwenye maamuzi mbalimbali ya Mahakama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuipongeza sana Mahakama, inafanya kazi kubwa. Kwa kweli Mahakama ya Tanzania iko mbali sana. Wote ambao walisikiliza hotuba ya Jaji Mkuu siku ya Jumatano, hotuba ya kurasa 40 na niko tayari, hotuba hiyo kuichapa na
kuwagawia Wabunge wote waone mambo aliyoyasema kwa ufasaha na umakini Profesa Ibrahim Hamis Juma. Jaji Mkuu wa mfano, Jaji Mkuu mweledi, Jaji Mkuu mcha Mungu alieleza wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Law Day, bahati mbaya sana Watanzania mambo madogo tunayafanya kuwa makubwa. Mimi naona aibu kubwa sana kuona Wanasheria nchi hii wanajadili suala la Mkuu wa Mkoa kupita kwenye red carpet wanasahau ile ilikuwa ni siku ya kuzindua Mwaka wa Mahakama na anayezindua Mwaka wa Mahakama ni Head of State na anayemwakilisha Head of State ngazi ya Mkoa na Wilaya ni RC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda muone Mwaka wa Mahakama unavyozinduliwa Uingereza, unazinduliwa na Askofu Mkuu wa Canterbury, kwa nini? Ni kwa sababu kwa Waingereza Askofu Mkuu wa Canterbury kwa protocol ni namba mbili na hakuna anayeuliza kwa sababu ni taratibu yao. Head of State (Malkia) hawezi kuhudhuria ile sherehe, anayehudhuria ni number two, ni Archibishop of Canterbury. Kwa hiyo, hii ni Head of State na wala tusiikuze kwa sababu ni kuzindua Mwaka wa Mahakama. Nawaomba Wanasheria Tanzania wazingatie mambo muhimu yaliyozungumzwa na Jaji Mkuu, tuache nani kapita kwenye red carpet, yellow carpet au green carpet, hayo siyo mambo ya msingi kwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuipongeza sana Mahakama. Mahakama imefanya kazi kubwa sana katika kupunguza mlundikano wa mashauri. Kwa Mahakama ya Mwanzo imejipa muda kwamba ndani ya miezi sita mashauri yawe yamekwisha na mpaka sasa mashauri ambayo yamevuka miezi sita ni 16 tu. Mahakama ya Wilaya imejipa mwaka mmoja kuwa imemaliza mashauri na mpaka sasa kesi ambazo zimezidi mwaka mmoja ni 837. Katika Mahakama Kuu ni miaka miwili na kesi ambazo zimevuka miaka miwili ni 1,860. Katika Mahakama ya Rufani ni miaka miwili na kwa kesi ambazo zimevuka miaka miwili ni 729.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa kuiongezea Mahakama idadi ya wafanyakazi mwaka jana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia mamlaka aliyonayo ndani ya Katiba akishauriwa na Judicial Service Commission aliteua Majaji wawili (2) wa Mahakama ya Rufaa na Majaji kumi (10) wa Mahakama Kuu. Mwaka huu kwa kutumia mamlaka yake hayo hayo, akishauriwa na Judicial Service Commission amechagua Majaji sita (6) wa Mahakama wa Rufaa na katika Majaji hao wanne (4) ni wanawake na wawili (2) ni wanaume, namba kubwa sana. Kwa hiyo, pia akina mama ndani ya nchi hii mjipongeze na kujisifia kwamba mwaka huu mmeweza kutoa Majaji wa Rufaa wanne (4). Hayo ndiyo mambo ya kujadili badala ya kujadili mambo madogomadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Rais ameteua Majaji wa Mahakama Kuu kumi na tano (15). Kwa mara ya kwanza katika Majaji hawa kumi na tano (15), Mheshimiwa Rais ameweza kuteua Mahakimu wa Kawaida (Resident Magistrate) mmoja (1) kutoka Bukoba, kijana mdogo na mwingine kutoka Shinyanga aliyekuwa Hakimu wa Shinyanga ili kuonyesha kwamba Ujaji unaendana pia na weledi lakini pia ujasiri na kusimamia sheria na haki. Kwa hiyo, niipongeze sana Mahakama kwa kufanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la Mahakama zinazotembea (Mobile Court) tulisema hata wakati ule tulipondoa hiyo hoja katika Bunge, tuliondoa hoja hiyo kwa sababu Jaji Mkuu ana mamlaka ya kuzianzisha Mahakama hizo bila kuleta sheria Bungeni. Ametumia mamlaka aliyonayo, Mahakama hizo amezianzisha na zitaendelea kufanya kazi. Tayari magari mawili yamefika na yataanza kufanya kazi katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mkoa wa Dar es Salaam Mahakama hizo zinazotembea itakuwa Bunju Wilaya ya Ilala, Chanika Wilaya ya Temeke, Buza na Kibamba Wilaya ya Ubungo. Kwa Mkoa wa Mwanza ambao pia una mashauri mengi, gari linakwenda Mwanza na litatoa huduma hizo kwenye Wilaya ya Ilemela huko Buhongwa na Igoma na Wilaya ya Nyamagana kule Buswelu. Baadaye magari yatakapoongezeka huduma zitasambaa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mlivyomsikia wenyewe Mheshimiwa Rais ametoa maagizo linunuliwe gari La Mobile Court na gari hilo liwe na Mahakimu wanawake kwa ajili ya kushughulikia kesi za mirathi za wanawake. Tutatekeleza maagizo hayo ili tuhakikishe tuna Mahakama inayotembea kwa ajili ya kushughulikia kesi za mirathi ya wajane ambazo Mheshimiwa Rais amesema kesi zao zinachukua muda na wanaonewa. Kwa hiyo, Mahakama hizo zinazotembea zitaendelea kufanya kazi na hakuna mahali tulipovunja sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa watu wayajue magari haya. Ndani ya magari hayo kuna huduma nyingi, kuna televisheni kwa ajili ya kurekodi ushahidi, kuna computer, printer na lifti ya kuwainua watu wenye ulemavu, kuingia na kushuka. Kwa hiyo, hiyo bei ya gari siyo gari tu ni pamoja na facilities nyingine ambazo ziko ndani ya gari hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuipongeza sana Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali. Ni Ofisi ambayo imeanza hivi karibuni lakini imefanya kazi kubwa sana. Imesimamia kesi nyingi za mashauri ya usuluhishi na mpaka sasa inasimamia mashauri 42 ya usuluhishi kwa weledi mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuboresha jambo hilo pia tutaanzisha kitu ambacho kinaitwa Haki Mtandao. Hivi karibuni Mahakama imeshaweka mtandao siyo lazima wafungwa au mahabusu watoke gerezani kwenda Mahakamani. Mambo ya kuahirisha kesi yatafanywa hukohuko mfungwa akiwa gerezani na Hakimu akiwa Mahakamani, kwa kutumia video link kesi hiyo itamalizwa na itaondoa tatizo la kubeba mahabusu kwa magari. Ni kweli kabisa mahabusu wako wengi na Serikali inachukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa tunapunguza idadi ya mahabusu hasa wale wa kesi ndogo ndogo kwa kuwapeleka katika community service.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo limezungumzwa hapa na napenda nilizungumzie pia, nalo ni suala la haki ya tendo la ndoa kwa wafungwa. Napenda kusema kwamba tendo la ndoa si haki ya msingi ni jambo la hiari, ndiyo maana wako Waseja na Watawa wa hiari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tusilifanye suala la tendo la ndoa kuwa suala la msingi. Ni moja ya haki ambayo mfungwa anaweza kunyimwa kwa sababu siyo haki ya msingi. Hanyimwi chakula, mavazi na maji kwa sababu ni haki ya msingi lakini tendo la ndoa ni la hiari. Wako ambao ni rijali lakini kwa hiari wameamua wasilifanye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, si vyema tukaanza kujiingiza katika mambo hayo ambayo kwa kawaida si utamaduni wa Waafrika kuanza kuzungumzia mambo ya tendo la ndoa. Ndiyo maana sisi ni mambo binafsi mno. Sasa tusianze kuiga mila nyingine, hata huko kwenyewe tendo la ndoa, kwa sisi tunaofahamu huko halifanywi gerezani, wale wafungwa huwa wanaruhusiwa kwenda kutembelea familia zao. Wenzetu kule ukihukumiwa mwisho wa mwaka huendi gerezani, unaripoti gerezani tarehe 2 Januari, ni utaratibu wao. Kwa hiyo, wale wenye umuhimu wa kufanya hivyo wanaruhusiwa kwenda huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda kabisa Bunge hili lisichukue muda mrefu katika jambo hili. Suala hili liliwahi kuwa ni moja ya maeneo yaliyofanyiwa utafiti na Tume ya Kurekebisha Sheria na likaonekana kwa nchi yetu halifai. Nchi moja ya jirani walitaka kufanya hivyo walishindwa kwa sababu ni suala la faragha, sasa kila mtu anajua mnaingia, hata uwezo unapotea. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo tumelipokea tutalifanyia kazi ni kuwachanganya wafungwa wenye umri tofauti, vijana na watu wazima. Hili ni suala la msingi sana na tutalifanyia kazi. Tutazimbelea Mahakama na kwa kweli tutahakikisha kwamba wafungwa hawa wanatenganishwa, hili ni moja ya jambo ambalo tunalipokea. Tayari Tume ya Kurekebisha Sheria imetoa ripoti inayoitwa Review of Police and Prisons Legislation, tutaona nini kifanyike ili kuhakikisha kwamba jambo hili linazingatiwa ili tutenganishe wafungwa kwa rika na umri wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la matumizi ya Kiswahili katika utungaji wa sheria, ni kweli kabisa wakati umefika wa kuanza kuzitunga sheria zetu kwa Kiswahili. Hata hivyo, napenda nitoe indhari siyo tahadhari maana ipo tofauti kati ya tahadhari na indhari. Ni kwamba hata tutakapoanza kuandika sheria nyingi kwa Kiswahili na sasa tayari tunaandika Miswada mingi kwa Kiswahili lakini someni Miswada ya Kiswahili si Kiswahili cha mtaani, ni Kiswahili chenye istilahi mbalimbali za kisheria ambazo ina maana baada ya muda itabidi tena watu wajifunze na wazielewe istilahi hizo na nyingine zinaweza kuwa zinakera masikioni kwa sababu hazijazoeleka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukiangalia Sheria ya Kiswahili ya Usimamizi wa Mazingira neno monitoring ni kupelemba lakini upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania neno kupelemba lina maana tofauti kabisa na ukienda huko usilitumie maana yake ni kumtongoza mwanamke. Kwa hiyo, hata huko pia tutakapoanza kutumia Kiswahili tujue kutakuwa na istilahi ambazo pia itabidi watu wazifahamu lakini ni kweli kabisa ni muhimu kuanza kutunga sheria zetu nyingi kwa Kiswahili badala ya Kiingereza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchelewashaji wa kesi, hili tumeshaliwekea mkakati wa kuhakikisha kwamba tunapunguza ucheleweshaji wa kesi. Ucheleweshaji huo wa kesi unachangiwa na uchunguzi na sasa tunafanya jitihada kubwa kuhakikisha kuwa uchunguzi wa masuala mbalimbali ya kesi unamalizika kwa muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo changamoto, zipo kesi nyingine zimechukua muda mrefu kwa sababu uchunguzi unahusisha kupata ushahidi kutoka nje ya nchi. Nashukuru kwa kuanza kutumia huu mtindo wa e-Justice hivi karibuni kuna kesi ambayo imesikilizwa ambapo shahidi alikuwa Ufaransa na kesi imefanyika Tanzania na shahidi aliweza kutoa ushahidi kutoka Ufaransa bila yeye kulazimika kuja. Kwa hiyo, ni moja ya maeneo ambayo tutayafanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuongezewa idadi ya Majaji na Mahakimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu zangu napenda kusema kwamba tunaishukuru sana Kamati kwa mambo mengi ambayo imeyaorodhesha. Kwa Watanzania kwa ujumla, napenda sana tujue hatuna nchi nyingine nje ya Tanzania na labda tunaichezea kwa sababu hatujaenda kuona nchi nyingine ambazo zimechezea amani yake zimeishia wapi. Siyo lugha nzuri na wala haipendezi kutaka kuleta mabadiliko kwa kuanza na vitisho, nchi hii itaendelea kuwepo na itaendelea kuwa na amani kama sisi wenyewe tutaamua kuwa na amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni lazima Watanzania tuwe na staha, tumefika mahali sasa tumeanza kukosa staha. Baadhi ya lugha tunazozisikia ndani na nje ya nchi haziendani kabisa na Utanzania wetu, utanzania ni pamoja na kustahi/kuyaheshimu mamlaka. Mkuu wa nchi ni taswira ya nchi hii, mkuu wa nchi anawakilisha nchi hii, kwa hiyo, siyo vyema tunapoanza kumbeza, kumzalilisha na kumdharau na tukadhani kwamba hiyo ndiyo demokrasia. Ni lazima tutofautishe kati ya demokrasia na laxity, there is a big difference between democracy and laxity. Tulizoea laxity na wakati wa laxity umekwisha. Kwa hiyo, demokrasia ni pamoja na kujua na mipaka yako na heshima hasa kuheshimu mamlaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa uvumilivu mkubwa sana alionao. Amevumilia upumbavu, upuuzi na ujinga mwingi lakini tusiendelee kufanya hivyo kwa sababu sisi wengine
ambao tumepewa kazi ya kuhakikisha heshima hiyo inalindwa tutatekeleza wajibu wetu na tutatekeleza bila tashwishwi hata kama baadaye watu watasema tumebadilika kwa sababu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Dakika moja Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja za Kamati zote mbili. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, mobile court, kutokana na msongamano ulivyo na tulishawahi kushauri kwa nini Mahakama nazo haziendi jela au mahabusu na kupunguza msongamano?

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo hilo limechukuliwa na moja ya hatua ambazo tumekubaliana, tunaanza katika awamu hii ni kuanza kutemebelea Magereza. Mkurugenzi wa Mashtaka pamoja na Mahakimu wakitembelea Magereza wana haki ya kutoa maamuzi ya kuwaachia baadhi ya wafungwa pale ambapo Mkurugenzi wa Mashtaka ameridhika kwamba watu hao kwa kweli kesi zao ni ndogo na tayari amekwishafanya hivyo. Katika hotuba ya bajeti tutaeleza idadi ya mahabusu walioachiwa baada ya ziara za DPP kuanza katika Magereza mbalimbali.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
WAZIRI WA MAMBO NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kuunga hoja mkono iliyoletwa mbele yetu na Dkt. Augustine Maiga, Waziri wa Katiba na Sheria ambaye amewasilisha hii hoja kwa umahiri mkubwa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchangia katika maeneo machache ya hoja iliyoletwa kwetu na Balozi Dkt. Maiga. Kwanza kuhusu mashauri ya nje; kama alivyoekeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali toka kuundwa kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali mafanikio yetu yamekuwa makubwa. Ndani wiki mbili zilizopita na waliosoma gazeti la Citizen juzi tumeweza kushinda kesi ya Valambhia ambao walikuwa wanaidai mabilioni ya fedha Benki ya Tanzania. Sasa kama alivyoeleza Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kesi ya Sterling Construction, kwanza kampuni hii sio ya Kanada kama ilivyoandikwa kwenye hotuba ya Kambi ya Upinzani. Kampuni hii ni ya Uingereza na kabla ya hapo ilikuwa kampuni ya Italy ambapo deni lake lilinunuliwa na kampuni ya Uingereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwa tumefanya maelewano yote, wao wenyewe kampuni ya Sterling Construction Company waliomba the Supreme Court of Quebec kiwango cha fedha walicholipwa na ile hukumu iwe siri. Kwa hiyo, maagizo ya kwamba hukumu na kiasi cha fedha kilicholipwa iwe siri, hayakuwa maombi ya Tanzania, yalikuwa maombi ya kampuni ya Sterling Construction ya Uingereza na ilikubaliwa na the Supreme Court of Cubec na sisi kuyaweka hadharani itakuwa ni contempt of court, lakini pia itakuwa ni kuvunja uungwana wa maelewano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme pia walitueleza wazi kwamba mnafanya makosa makubwa sana mara nyingine mnapoyaweka mambo haya wazi kwa sababu mna kesi na watu wengine na si ajabu wakijua kiwango ambacho ninyi mmetupa na wao wanaweza wakakidai au kikaleta maswali mengi. Kwa hiyo suala hilo ni wazi ni maombi ya Sterling na uzuri hukumu wa Jaji wa Canada ambaye kwanza alianza kwa kutupa pole ya askari wetu kule Congo kuuawa alieleza wazi. Kwa hiyo sio Serikali ya Tanzania ni Sterling Quebec lakini kiwango kilicholipwa siku wakikubali taarifa hiyo iwe wazi, ni kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uteuzi wa Majaji, ningependa suala hili nieleze kabisa, Majaji wote walioteuwa, wameteuliwa na Mheshimiwa Rais kwa ushauri wa Judicial Service Commision. Nami nichukuke nafasi hii kukupongeza sana wewe ulipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwaka 2000 na mwaka 2005 ulileta mabadiliko ndani ya Bunge hili ambayo moja yalipanua na kuongeza divest ya wajumbe wa Judicial Service Commision.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakumbuka kabla ya wewe kuleta hayo mabadiliko ya Katiba, Judicial Service Commision ilikuwa na watu wachache na wote walikuwa kwenye mhimili wa Mahakama lakini ni wewe mwaka 2000 mara ya kwanza na 2005 mara pili uliyefanya mabadiliko makubwa kuishauri Serikali kufanya hivyo, ikiwa ni pamoja na kuboresha haki za binadamu, wewe ukiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ulileta mabadiliko hapa Bungeni ambayo yaliondoa clawback clauses zote. Sisi ndio Katiba pekee katika Bara la Afrika inapokuja kwenye haki za binadamu haina clawback clauses, someni ya Kenya, Uganda, Zambia, Zimbambwe na nchi nyingi, lakini kazi hiyo aliifanya Mheshimiwa Andrew John Chenge mwaka 2005 akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Ndio maana daima nabeba Katiba hii mwisho hapa A. J. Chenge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndio aliingiza haya mabadiliko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo watu wa umri mdogo humu wanapapukia mambo wasiyoyajua, wangejua tulipotoka wangejua tulipofika. Kwa hiyo ni jukumu letu hawa walio wadogo tuwakumbushe tulikotoka na ndio maana Katiba hii Mheshimiwa Chenge wewe ni miongoni mwa watu walioisaidia Judicial Service Commision. Kwa sababu hiyo basi, uteuzi wa Majaji umebadilika; leo hii Majaji hawatoki katika mhimili wa mahakama tu, wanatoka kwenye vyuo vikuu, wanatoka kwenye Mawakili binafsi na huo upanuzi wa aina ya Majaji wanaoingia, imeongeza ubora wa hukumu lakini pia imeongeza ubora wa utendaji katika Mahakama zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kwa kutumia mamlaka ndani ya ibara 109(7) na (8) hatoi fadhila, anateua watu wenye sifa na sababu za kuwa Majaji baada ya kuwa amependekezewa na Tume ya Mahakama. Kwa hiyo, nataka nisisitize, Rais hatoi zawadi katika kuteua Majaji. Nami narudia tena kwa ndugu zangu, hakuna kazi ambayo naiogopa na tuwaombee sana Majaji na mkitaka kujua ugumu wa kazi ya kuwa Jaji, kaisomeni Zaburi ya 15 na baada ya hapo muisome Zaburi 51 na Zaburi ya 32. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakishazisoma Zaburi hizo tatu za toba katika kipindi hiki cha kwaresma watawaombe sana Majaji. Si kazi ya kukurupukia ni kazi ya kumwombea mtu huyo aliyopewa kwa sababu amechukua kazi ambayo ni ya Mwenyezi Mungu mwenyewe, yeye pekee ndiye Hakimu wa kweli wengine wote wanajitahidi kufanya hivyo.

Kwa hiyo si kazi kuendelea kuwabeza na ndio maana naunga mkono nchi nyingine ambazo mambo ya mahakama hayajadiliwa kabisa katika Bunge. Sisi tumeruhusu kuyajadili mambo hayo, lakini tuyajadili kwa hekima, kwa kiasi, kwa saburi, lakini kwa unyenyekevu mkubwa maana hatupo katika viatu vya watu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala la Sheria ya Ndoa, sio kweli kwamba Sheria ya Ndoa ya Tanzania ya mwaka 1971 ni sheria kandamizi, ni sheria ya kimapinduzi. Narudia tena Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ni sheria ya kimapinduzi na nchi nyingine mpaka leo zimeshindwa kutunga sheria ya aina hii. Kwa hiyo tusichukulie suala moja tu la umri wa mtu kuoa au kuolewa likawa ndio kigezo cha kusema sheria hii ni kandamizi. Hata hilo suala la mtu kuoa au kuolewa, mtu akikisoma kwa makini kifungu hicho hakizungumzii msichana tu bali pia kinamzungumzia mvulana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ndani sheria zetu wapo wavulana wanaoweza kuona chini umri ya mdogo, soma kile kifungu vizuri, kinasema either paties or one of them. Sheria hii ni sheria ya kimapinduzi kwa sababu ndio sheria kwanza mwaka 1971 iliyowakomboa wanawake wa Kitanzania hasa wenye ajira sasa kuweza kwenda kufanya kazi eneo lolote na Tanzania na kupanda vyeo. Kwa sababu kabla ya hapo sheria tulioachiwa na Waingereza ilikuwa mwanamke lazima akae mahali alipo mumewe na hilo liliwanyima wanawake fursa kama akina Dkt. Christine Ishengoma asingeweza kuwa Mkuu wa Mkoa Iringa akamwacha Profesa Morogoro, ilikuwa lazima akae Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisimtolee mfano yeye tu, nitolee mfano sasa mwingine, kwa sababu sheria kabla ya mwaka 1971 Cohabitation maana yake ilikuwa lazima siku zote mlale katika chumba kimoja, lakini leo chini ya sheria hii kwa hiyo habitation pamoja na whatsApp pamoja na simu. Hilo limewakomboa wanawake wa Tanzania kuweza kwenda kufanya kazi maeneo mbalimbali ya nchi. Ni makosa kuita sheria ya namna hiyo ni sheria kandamizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, katika umliki wa mali hii ndio sheria ya kwanza katika Bara la Afrika iliyotambua kwamba mwanamke aliyeolewa anaweza akamiliki mali kwa jina lake, someni sheria za nchi zingine, hata Uingereza, hata Ujerumani imewachukua miaka mingi mwanamke ndani ya ndoa kuruhusiwa kumiliki mali kwa jina lake. Alimiliki mali kwa jina la mumewe au kwa jina la baba yake. Sisi tuliosoma nje tulishangaa kwamba mwanafunzi wa kike Ujerumani hawezi kupanga chumba mpaka baba yake atie saini ya ile form, hapa wanasaini tu. Hapo tulishangaa kwa kujua wanawake wa Ulaya, wenye sifa sawa na kazi sawa wanalipwa mshahara kidogo kuliko wanaume eti tu ndani ya mwezi kuna siku ambazo hazieleweki kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja kama hiyo huwezi kuileta hapa, kwamba kuna siku ambazo mwanamke haeleweki na hiyo alipwe mshahara mdogo. Mpaka leo ipo katika nchi Ulaya. Kwa hiyo kuna mambo sheria hii imefanya makubwa ambayo ni vizuri tuyaelewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu umri wa mtoto kuolewam, hili suala ni suala very sensitive, tukitaka tuliibue tutagombana humu. Uingereza yenyewe mpaka leo umri wa mtoto wa kike kuolewa ni miaka 16, lakini leo wasichana wengi Uingereza hawaolewi kwa sababu ya fursa mbalimbali za elimu na mwamko lakini n I mpaka leo. Ukienda kwenye Sheria ya Kanisa Katoliki kwenye Canon Law, Canon namba 1083 inasema wazi kabisa umri wa msichana kuolewa ni miaka 14, kwa mvulana kuoa ni miaka 16 na hii sio mimi, ni Canon Law ya Kanisa Katoliki ambayo ndani ya vitabu ipo wazi. Kwa hiyo kwa kanisa katoliki binti anaweza kuolewa na miaka 14 mvulana 16, ingawa mamlaka za kidunia zilipo zimeruhusiwa kubadili, lakini mpaka leo Canon Law haijabadishwa kifungu cha 1068 na kifungu 1071 ambacho kilitolewa na baba Mtakatifu Paul wa Sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sitaki kwenda kwenye mifano ambayo daima tunapenda kuitoa kwenye dini ya Kiislam, lakini hata huko kwa madhebebu ya Shafii ni miaka 15; kwa madhehebu ya Hanbali miaka 15 kwa madhebebu Maliki ni miaka 17; kwa madhehebu ya Hanafi ni miaka 12 kwa mvulana, miaka tisa kwa msichana na kwa madhehebu ya Ja’fari, hawa Shia ni miaka 15 na tisa. Tusiende kwenye majadala huo, tuache sheria ilivyo na busara itawale, kwenda kwenye haya tutaingia kwenye mambo ambayo si vizuri kuyaingia kwa sasa. Hata hivyo, nirudie kueleza, Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 tofauti na ilivyoelezwa ni sheria ya kimapinduzi, iliyokuja kwa wakati muafaka na unaostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningependa pia nieleze kuhusu haki za binadamu kwa kifupi. Tumetoka kwenye Baraza la Umoja wa Kimataifa la Haki za Binadamu, Geneva mwezi Februari, tumetoa maelezo kule na baada ya maelezo ya Tanzania, Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa kwa kinywa chake ametupongeza kwa utekelezaji mkubwa wa haki za binadamu katika eneo la elimu, eneo la afya, eneo la maji. (Makofi)

WABUNGE FULANI: Aaaaaaa.

MWENYEKITI: Nakuongezea muda kidogo Profesa. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja na tuliungwa mkono na nchi zote za Afrika, sisi ndio tunaongoza kwa idadi kubwa ya magazeti ambayo yanatoka kila siku ya aina zote na tunamshukuru Mungu kwamba sio sisi tuliyoyabeba magazeti haya kuyapeleka Geneva, tulikuta Umoja wa Kimataifa wanayo magazeti hayo. Walishangaa kabisa uhuru mkubwa tulionao wa haki za magazeti ya risasi yaani wanaojimwaga, yapo, kwa sababu ni diversity, ya muziki yapo na magazeti ambayo ni very critical, yapo. Hata hivyo, pia sisi ndio nchi ya kwanza ambayo magazeti mengi ni magazeti binafsi, magazeti ya Serikali ni mawili tu Dalynews na Habari leolakini magazeti mengine yapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vituo vya redio sisi ndio tuna vituo vingi kuliko vyote, vituo vya redio vingi na kwenye vituo vya redio huingilii. Vingi vinaeleza mambo ya nchini. Kwa hiyo Umoja wa Matifa umetuondoa katika tuhuma hizo ambao watu walizipigia kelele, tumechukuliwa ni nchi ya mfano kwa sababu katika Universal Decralation of Human Rights, haijapanga haki, civil and political rights, economic and social rights zipo sawa na sisi tunaongoza katika economic and social rights. Sio tu Afrika lakini pia katika Bara la Afrika na Asia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo ya kufanyiwa kazi na haya maeneo ya kufanyiwa kazi yanafanyiwa kazi na mahakama. Mwaka huu na mwaka uliopita Mahakama za Tanzania zimetoa land mark decision moja on private investment, judgment ya Court of Appeal kuhusu kesi ya Tigo ambayo watu wengi hawajaisoma ambapo Mahakama ya Rufaa tena, hukumu ya Jaji Mkuu Juma ime-reaffirm the right to private property na kesi hii haikuwa dhidi ya Serikali, ilikuwa kesi ya mfanyabiashara mmoja tapeli aliyetaka kuidhulumu Tigo shares zake, mwaka jana Mahakama ya Rufaa imetoa hukumu muhimu sana inayoeleza uwazi kabisa mipaka ya DPP katika kutekeleza majukumu yake na kumpa mwongozo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu Mahakama Kuu imetoa mwongozo katika utoaji wa bail. Sasa mara nyingi watu tunataka majibu ya mkato, badala ya kutaka process ya mahakama iende na baada ya hapo mahakama itoe mwongozo. Baada ya kumweleza Kamishna wa Umoja wa Mataifa kuhusu mambo hayo na kumkabidhi zile judgment, alisema zile judgments zinafaa zitangazwe dunia zima jinsi ambavyo Mahakama za Tanzania zipo mbali katika kufafanua na kusimamia haki za binadamu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

WAZIRI WA MAMBO NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Kuridhia Itifaki ya Kinga na Maslahi ya Kidiplomasia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (The East Africa Community Protocol on Information and Communication Technology)
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nitajitahidi, naomba kuchukua fursa hii kwanza kukushukuru mwenyewe kwa kuongoza kikao hiki, lakini pia kuwashukuru Wabunge waliochangia na Wabunge wote lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Mbena kwa maoni ya Kamati na Mheshimiwa Salome Makamba kwa maoni ya Kambi ya Upinzani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru Mheshimiwa Ruth Mollel, Mheshimiwa Daniel Nsanzugwanko, Mheshimiwa Cosato Chumi na Mheshimiwa Almas Maige.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuanza na jambo ambalo wewe, unalifahamu vizuri zaidi kwa sababu wakati huo ulikuwa Mwanasheria wa Serikali. Jumuiya ya Afrika Mashariki ya zamani ilivunjika mwaka 1977 na ni vyema tukasema ukweli mpaka Jumuiya ya Afrika Mashariki inavunjika nchi ya Uganda iliendelea kutoa michango yake yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nchi ya Uganda, chini ya Iddi Amin iliendelea kutoa michango yake yote mpaka Jumuiya inavunjika, ni ukweli wa Kihistoria kwamba nchi ambayo haikutoa michango yake kabla ya hapo inafahamika, lakini baada ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuvunjika katika namna ile iliyovunjika na Tanzania kulazimika kufunga mpaka na Kenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jitihada zilifanyika chini ya aliye chaguliwa kuwa msuluhishi na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa aliyeitwa Victor um Rishi ambaye nina hakika unamfahamu na mlikutana na mimi nilipata bahati ya kufundishwa na Victor um Rishi mwaka 1984 nilipokwenda kusomea kozi ya mambo ya Diplomasia Mjini Cairo nchini Misri na nchi hizi zikakubaliana katika kitu kilichoitwa The East African Community Mediation Agreement ya mwaka 1984.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika makubaliano hayo, waliangalia net assets na net liabilities na baada ya hapo, mali lazima ziendelee kuwa mali za jumuiya, mali za pamoja ingawa jumuiya imevunjika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakumbuka, Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki iliendelea kuwa ni mali ya pamoja, pamoja na jumuiya kuvunjika na ilikuwa Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili, Soroti Flying School ya kufundisha marubani ilibaki Uganda na ikawa mali yetu wote. Tatu, Interuniversity Council for East Africa, nayo ilibaki Uganda. Kwa hiyo, baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, mali zilizobaki kuwa zetu wote, baada ya usuluhishi wa Dkt. Victor Umbricht, zote zilikuwa Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye East African Development Bank, ilikubaliwa kwamba daima Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji atatoka Tanzania. Akawa Idd Simba, akawa George Mbowe. Nilitaka niweke rekodi hii vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ambayo katika net assets haikufaidika ni Uganda na ndiyo maana ndani ya mkataba ule, ilikubaliwa tuwe na compensation to Uganda for short fall of net assets, interest payments; na Kenya na Tanzania tulipewa viwango vya kuifidia Uganda na kama tutashindwa kuifidia Uganda, tutalipa riba ya asilimia saba. Wewe ulihusika, katika hilo. Nilitaka lieleweke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mkataba huo kusainiwa mwaka 1984 na unafahamu haikuwa rahisi, nchi iliyotoa ushirikiano mkubwa ilikuwa ni Uganda. Ndipo kila nchi mwanachama, kama tunavyofanya leo, ilipeleka katika mabunge yake sheria ya kuridhia The East African Mediation Agreement. Kenya walifanya hivyo mwaka 1985 chini ya The East African Mediation Agreement Act Cap 4 of The Laws of Kenya. Tanzania ilifanya hivyo hivyo, chini ya The African Community Mediation Agreement Act, ya mwaka 1987 ambayo ni sura ya 232 ya sheria za Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nimeanza na hiyo? Hakuna ombwe panapotokea mgogoro hata kama mkataba huo na sheria hiyo haijatamka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana wewe pia ulihusika ukiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mkataba wa sasa, The Treaty of the Establishment of the East African Community ya sasa, is a framework agreement. Kila jambo tutakalotaka kulitekeleza, lazima tujadiliane itifaki, kwa sababu tulianza kwa kutokuaminiana baada ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 1977 kuvunjika. Ndiyo maana itifaki hii inazungumza maslahi na kinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kujua nini kitatokea Jumuiya ya Afrika Mashariki ikivunjika, rudi kwenye treaty, soma Ibara ya 145, 146, 147 na 149. Kwa pamoja zinaeleza nini kitatokea, siyo tu Jumuiya ya Afrika Mashariki ikivunjika, lakini nchi ikijitoa. Chini ya Ibara ya 145 ya mkataba wa sasa, nchi ina haki ya kujitoa na chini ya Ibara ya 146, nchi inaweza ikasimamishwa uanachama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyote hivyo vikitokea, tukienda kwenye Ibara ya 149, ndiyo tunajua nini hatima ya mali zilizomo? Kwa nchi iliyojitoa yenyewe kwa hiari yake, kwa nchi iliyosimamishwa uanachama, vyote vipo na hilo ndilo lililomfanya Dkt. Victor Umbricht kuandika kitabu kuhusu Multilateral Mediation, Practical Experience and Lessons, cha mwaka 1989; Mediation Cases, The East African Community and Short Commence on Mediation Efforts Between Bangladesh, Pakistan, India, Vietnam, USA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, likitokea hilo ambalo hatutarajii litokee tena, kwa sababu sasa mwaka huu tunasherekea miaka 20. Ile ilikufa ndani ya miaka 10; likitokea, utaratibu wa Kimataifa upo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, wewe ulikuwa ni mmojawapo na sisi wengine tulikuwa tunasaidia, tulihakikisha mkataba huu wa sasa, unatungwa kwa namna ambayo tutajenga imani kila siku zinapoendelea. Kwa hiyo, niwahakikishie, huu mkataba ni kwenye haki, maslahi na kinga, lakini tuusome pamoja na treaty nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, ndani ya kipindi hiki cha miaka 20, tumejenga jumuiya imara na ili jumuiya hii iendelee kuwa imara ni lazima ibebwe na misingi miwili; pragmatism and flexibility.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Sudani ya Kusini; nchi zote zinazojiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya nchi tatu zilizoianzisha, ni lazima ziingie kwenye kitu kinaitwa, Accession Treaty. Kuna Accession Treaty kati ya Jamhuri ya Rwanda na Jumuiya ya Afrika Mashariki; na Accession Treaty kati ya Jamhuri ya Burundi na Kumuiya ya Afrika Mashariki; na hivyo hivyo Accession Treaty kati ya Jamhuri ya Sudani Kusini na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Accession Treaty, ili nchi hiyo iweze kufungwa na mikataba yote inayoikuta wakati inajiunga na jumuiya hiyo. Kwa hiyo, hapa ni kukwepa lile suala la retrospective application, kwamba kwa kuingia mkataba siku ile, moja ya vifungu ni kwamba, ninafungwa na yale yote niliyoyakuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Sudani imefungwa na mambo yote iliyoyakuta, lakini ndani ya mkataba huo na sisi na Sudani ya Kusini, kipo kipindi cha mpito, Sudani ya Kusini imepewa kipindi cha mpito lakini inafungwa na yale yote iliyoyakuta kwa sababu imeasaini The Accession Treaty kama Burundi na Rwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jumuiya hii pia tuna ile tunasema dhana ya undugu (solidarity principal) na nchi ya Sudani Kusini, inahitaji kipindi cha mpito kwa sababu nyote mnafahamu hali ambayo Sudani ya Kusini imepitia. Sudani ya Kusini imekuwa katika migogoro iliyonayo toka mwaka 1956 mpaka leo. Kwa hiyo, haya mnayoyaona kwamba Sudani inakwenda taratibu, haifanyi makusudi, lakini ni kwa sababu imeomba iwe na kipindi cha mpito, kuiwezesha kuunda taasisi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika mfumo wake wa kodi na mamlaka ya kodi, Sudani ya Kusini inasaidiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wanafunzi wake wanasoma katika Chuo cha Kodi na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuwasaidia kuwa na mfumo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize la wafanyakazi wa Afrika Mashariki. Kwanza tufahamu katika ule mkataba wa Umbricht, Sura ya 10, ilieleza kuhusu National Provident Fund ya watumishi wote wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na fedha yao yote ambayo ilikuwa imetunzwa Uingereza kwenye Crown Agency, na fedha hizo zilitumwa kwenye kila nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Tanzania tulikuwa na wafanyakazi 31,831 na hawa waliingia katika makubaliano na Serikali walipwe shilingi bilioni 111 kwenye deed of settlement na wafanyakazi hao walilipwa wote na walipewa miezi sita kwa yule ambaye hakuridhika, apeleke malalamiko, hakuna aliyepeleka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya miezi sita, wakajitokeza wafanyakazi 5,598, wakidai shilingi trilioni 2.15, wakaenda Mahakama Kuu, wakashindwa; wakaenda Mahakama ya Rufaa, wakashindwa; wakaenda kwenye East African Court of Justice, wameshindwa. Kwa hiyo, Serikali ilishatekeleza jukumu lake la kuwalipa fedha kwa mujibu wa Deed of Settlement na maadamu wameshindwa kwenye Mahakama zote, Serikali haiwezi kutoa hisani zaidi ya hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali haidaiwi hata senti tano. Orodha ya wafanyakazi wote ipo kutoka Crown Angency, walio hai na walikufa. Wamechukua haki yao Mahakamani, wameshindwa. Kwa hiyo, tuweke rekodi sawa, hakuna mfanyakazi wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeidai Serikali fedha yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nahitimisha kwamba, naomba kutoa hoja.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima, naomba nichukue fursa hii kukushukuru tena wewe binafsi kwa kunipa nafasi ya kuwasilisha mpango na makadirio ya bajeti ya Wizara muda wa asubuhi na sasa kuniruhusu kufanya majumuisho ya mjadala.

Nakushukuru kwa kuongoza mjadala wa bajeti yetu kwa umahiri na kwa msingi huo, maoni na michango iliyotolewa yameiwezesha Wizara kupata maoni na ushauri utakaotusaidia kwenye kutekeleza majukumu yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ulivyoendesha kikao leo mimi nimefurahi sana, kwamba leo Mabalozi ambao kwao Bunge lao huwa ni zogo na fujo, wameona jinsi ambavyo Bunge hili ni la kistaarabu pamoja na kelele chache. Sisi ambao tumepata bahati nadra sana kuishi huko, tumeona Mabunge yao, viroja vyao, vituko vyao, wale waliodhani leo watafanya viroja ili Wazungu watuone hatufai, sasa tumewadhihirishia hao Wazungu kwamba sisi tuko mbali sana. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niwaambie na natamani wawepo; Ujerumani Spika mwanamke alikuwa haruhusiwi na walipoamua kuwa na Spika mwanamke, anaitwa Clara Zetkin, ilibidi wamtungie sheria kumtangaza kuwa mwanaume ili aweze kuwa Spika. (Makofi)

WABUNGE FULANI: Ahaa.

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu anavaa suruali ilibidi wapitishe sheria ya kumruhusu kuvaa suruali. Sasa sisi tumeishi huko tumeyaona hayo tunayafahamu hayo sisi hapa hakuna suala la mwanamke kuwa Spika kule bado ni issue tena kubwa sana. Kwa hiyo, nimefurahi sana leo tumeonyesha umahiri wetu na uungwana wetu kwa kiasi kikubwa na kwa namna hiyo nakupongeza sana ulivyoendesha kikao cha leo, ulivyosimamia kanuni na ulivyozitafsiri. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya kipekee naishukuru kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nje ya Ulinzi na Usalama chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Mussa Azan Zungu, na wajumbe wote wa Kamati kwa ushirikiano mkubwa waliotupatia wakati wa maandalizi ya bajeti na kwa hotuba nzuri waliyoitoa. Tunashukuru kwa maelekezo, maoni na ushauri ambao kamati hii imekuwa ikiupata na nataka niahidi yale yote ambayo leo wametushauri Wizara itayazingatia na itayatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimshukuru sana Mheshimiwa Salome Wickliffe Makamba nina mwendi labda nitoe siri leo. Salome Wickliffe Makamba marehemu baba yake Wickliffe Makamba na mama yangu Patricia Mwendi ni mabinamu na ndiyo maana mtoto wake anajina la babu yangu Mwendi, kwa hiyo mfahamu nafurahi sana mimi niko huku yeye yuko huko tumetoa hotuba leo na leo Gairo, Mamboya, Berega, Magubike wamefurahi sana kwa hiyo tumepokea maoni na ushauri ulioutoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee namshukuru sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Augustine Phillip Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria ambaye hapo awali alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Mahiga aliweka msingi mzuri katika Wizara hii ambayo inaniwezesha kutekeleza majukumu yangu kwa ufanisi namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Mahiga kwa ushirikiano mkubwa alionipa mara mbili Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alinituma niende pamoja na Mheshimiwa Dkt. Mahiga nje na nilijifunza mengi sana kwake katika mikutano hiyo nje na leo hii namshukuru hakuwa mchoyo wakati huo kuniandaa leo kuchukua na kuvaa viatu vyake ingawa dhahiri ni vikubwa lakini namshukuru sana pia anavyoendesha Wizara ya Katiba na Sheria nilikotoka. Mwalimu na mwanafunzi wanapopokezana vijiti ni jambo la fahari na ni nchi chache kitu kama hicho kinatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho lakini siyo kwa umuhimu naomba kumshukuru Dkt Damas Ndumbaro Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwa kazi kubwa anayoifanya katika Wizara hii kwa kipindi cha miezi takriban miwili na toka niingie kwenye Wizara hii amekuwa na mchango mkubwa katika utendaji kazi wangu na ufanisi wa Wizara. Yeye amesafiri mara nyingi nje ya Nchi kuliko mimi na huko ametuwakilisha vizuri sana nichukue fursa hii kumpongeza sana alivyotuwakilisha vizuri Argentina, alivyotuwakilisha vizuri Brussels, Pretoria, Kigali, Uganda amefanya kazi nzuri na mimi najivunia sana kazi yake. (Makofi)

Mheshiiwa Naibu Spika, pia nimshukuru Katibu Mkuu Dkt. Faraji Mnyepe, Naibu Katibu Mkuu Mheshimiwa Balozi Muombwa Mwinyi, Mabalozi wote wote Wakurugenzi Wakuu wa vitengo na watumishi kwa kujituma ni imani yangu kuwa ushirikiano huu na kujituma kwenu kutaimarika wakati mnatekeleza bajeti ya mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mjadala wa bajeti yetu jumla ya Waheshimiwa Wabunge 13 wamechangia kwa maandishi na jumla ya Wabunge wanne wamechangia kwa kuongea kwa namna ya pekee nawashukuru Wabunge waliochangia kwa kuongea na maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao mizuri waliyoitoa wakati wa majadiliano hapa Bungeni, tumepokea maoni mazuri ambayo yamelenga kuboresha utendaji wa kazi wa Wizara na Sera ya Kidiplomasia ya kiuchumi ni dhahiri Waheshimiwa Wabunge wote wanatamani kuona mchango wa Wizara hii katika maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuwahakikishia kuwa chini ya uongozi wangu na viongozi wengine wa Wizara tutahakikisha kuwa mfumo wa utendaji kazi wa Wizara unabadilika na Wizara inatoa mchango stahiki na kwa ujumla maoni na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wakichangia bajeti hii ni ushahidi kwamba Bunge hili linatambua umuhimu wa mapendekezo ya kujenga hoja. Kwa hiyo, ningependa niangalie nifafanue baadhi ya hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, ningependa nieleze msingi wa sera yetu ya mambo ya Nje umewekwa bayana na Baba wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika waraka aliotoa kwa watumishi wote wa Wizara ya Mambo ya Nje unaitwa argue don’t shout na inasema an official guide on foreign policy by the President na katika Waraka huu wa argue but don’t shout mwalimu ameweka wazi baadhi ya mambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, aliloliweka wazi ni kututaka tujue dunia inabadilika lakini pamoja na dunia kubadilika mambo ya msingi tuyashikilie lakini tujue kuna wakati itabidi tubadilishe mbinu na mikakati ya kufikia lengo tunalolitaka. Mwalimu hakutuambia tushikilie misingi tu na kuacha kuangalia hali halisi ya dunia alitutaka tuangalie hali halisi ya dunia bila kupoteza misingi. Na wengi siku hizi wanamzungumza Mwalimu bila kuwa na uhakika wa yale wanasema.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu hakuwa ni mtu ambaye alikuwa anakubali nchi hii iburuzwe. Kuna nyakati Mwalimu alichukua maamuzi katika sera ya Mambo ya Nchi za Nje ambao wengi hawakuyatazamia mwaka 1964 Tanganyika na Zanzibar zilipoungana. Tanganyika palikuwa na Ubalozi wa Ujerumani Magharibi, Zanzibar palikuwa na Ubalozi wa Ujerumani Mashariki, mara baada ya Muungano huo Ujerumani Magharibi ilitaka kumlazimisha Mwalimu kuiondoa Ujerumani Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu aliwaomba muda ili jambo hilo lishughulikiwe kwa utaratibu Wajerumani kwa sababu ndio waliokuwa wanaipa Tanzania misaada mingi kuliko nchi yoyote walidhani wanaweza kumburuza akubali maoni yao. Wale wote wenye umri mkubwa kuliko mimi wanajua, Mwalimu alichukua hatua ambayo hawakuitarajia. Moja aliwafukuza wataalam wote wa Kijerumani isipokuwa Wamissionari, pili aliwarudishia Wajerumani fedha yao doch mark milioni 40 na Jengo la Nkurumah Hall Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambalo sasa halijamaliziwa Mwalimu alisema limaliziwe.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Kuhusu Utaratibu.

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Lakini pia Mwalimu alichukua hatua nyingine kubwa mwaka 1965 Wazungu wabaguzi...

NAIBU SPIKA: Naomba ukae Mheshimiwa ukiniona nakuongelesha hivyo ni kwa sababu sitaki kukukumbusha kanuni zinasemaje huyu aliyesimama hapa ni Waziri mtoa hoja. Kanuni yako inasemaje? Naomba ukae Mheshimiwa Mwakajoka. Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Na wakati huo wale Wazungu wachache wa Arodesia walipojitangazia uhuru Umoja wa Nchi za Afrika ulitoa maazimio kwamba Uingereza iwaondoa Wazungu walowezi wachache Rodessia katika utawala na wasipofanya hivyo nchi za Afrika zivunje uhusiano wa Kibalozi na Uingereza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni nchi mbili tu zilifanya hivyo ni Ghana na Tanzania, na matokeo ya Ghana kuvunja uhusiano wa kibalozi na Uingereza marehemu Kwame Nkurumah alipinduliwa na wanajeshi wakiongozwa na Achiempong aliesoma San Hast nchi ya pili kufanya hivyo ilikuwa na Tanzania ilivunja uhusiano wa Kibalozi na Uingereza kuanzia mwaka 1965 mpaka mwaka 1972 Kerbado Mwalimu aliwarudishia Waingereza msaada waliokuwa wameuleta wa paundi milioni tano, huyo ndiyo Julius Kambarage Nyerere. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hoja za leo ninazozisikia watu watatamani tupate misaada hiyo na tuvunje misingi. Watu watatamani tupige magoti ili tupate misaada. Nasema hivi chini ya utawala huu wa Chama cha Mapinduzi nchi hii haitapiga magoti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kamwe nchi hii haitapiga magoti wamethubutu wameshindwa hii ndiyo nchi pekee katika Bara la Afrika haijashindwa vita hatukushindwa Uganda, hatukushindwa Sychelles, hatukushindwa Comoro hii ndiyo nchi pekee imewapeleka wapigania uhuru kwao tumewapeleka Zimbabwe, tumewapeleka Msumbiji, tumewapeleka Namibia hii ndiyo nchi iliyopokea watu wenye shida wengi kuliko wote na kwa kufanya hivyo Mwalimu alilipa gharama kubwa ambayo Dkt. Magufuli atailipa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu kwa kusaidia nchi hizo aliitwa M-communist na mimi nilishangaa kwa mara ya kwanza tunamkatoliti m-communist na hila hizo hizo husuda hiyo hiyo wivu huo huo upo sasa kwa sababu nchi hii chini ya Dkt. Magufuli tumeamua kujitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na mara nchi ya Afrika inapoamua kujitegemea maadui wanatumia vibaraka ndani ya nchi, mabaraka ndani ya nchi…

WABUNGE FULANI: Wako humu, wako humu ndaniii!

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, huo ni usaliti kwa nchi yetu tusikubali kuwa mabarakara wa mabeberu tusikubali kutumiwa hii nchi ni yetu. Niwakumbushe mara baada ya hali ngumu ya uchumi mwaka 1985 Benki ya Dunia na Benki ya IMF walipozilazimisha nchi zote kutuacha na nchi za mwisho kutuacha ilikuwa ni nchi za Nordic. Bado nchi hii ilisimama haikupiga magoti haiwezi kupiga leo magoti wakati tuna foreign reserve ya miezi mitano hatukupiga magoti wakati hatuna foreign reserve wakati mzee Mwinyi anaingia hatuwezi kupiga magoti leo tuna foreign reserve ya miezi mitano aslan kamwe halitatokea hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na ndiyo maana Mwalimu kwenye hii argue don’t shout anatutahadharisha anasema wale wa nje ni opponents hawa wa ndani wanaokuchimba ndiyo enemies kwa hiyo, we are facing enemies internally but we are facing opponent outside our enemies are eternal outside are opponents. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijibu hoija mbalimbali. Ya kwanza ni hoja kuhusu Tanzania kuwa na kigugumizi kuridhia mkataba wa makubaliano ya eneo huru la biashara Barani Afrika – AFTA. Serikali ieleze Bunge ni lini itatuletea mkataba huo Bungeni ili uridhiwe. Ningependa kusema hivi, mkataba huu tumekwisha usaini Tanzania imeusaini mkataba huu na saa hizi tuko katika mchakato wa kuupitia ili tuone faida zake na…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbilinyi, Mheshimiwa Prof. Kabudi naomba unyamaze kidogo Mheshimiwa Mbilinyi na Mheshimiwa Salome na Mheshimiwa Mwakajoka tafadhalini sana. Mheshimiwa Mwakajoka tafadhali, Mheshimiwa Mbilinyi tafadhali na Mheshimiwa Makamba nimewataja hii ni mara ya mwisho hii ni mara ya mwisho Chief Whip wa opposition nimewataja Wabunge wako watatu mara ya mwisho. Mheshimiwa Prof. Kabudi.

Naomba ukae Mheshimiwa Selasini kwa sababu unaufahamu utaratibu nimekuambia nimewataja Wabunge wako kwa sababu we ndiyo kiongozi wako na uwambie watulie wamekaa hapo karibu na wewe. Mheshimiwa Kabudi naomba uendelee.

MHE JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa mimi ni Chief Whip.

NAIBU SPIKA: Chief Whip hausimami akiwa amesimama Waziri Chief Whip huwezi kusimama akiwa amesimama Waziri hata yeye angekuwa amesimama wakati Waziri amesimama hawezi kusimama naomba ukae, naomba ukae Mheshimiwa Selasini. Naomba uendelee Prof. Kabudi

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala kwamba hakuna takwimu za Kitaifa zinazoonyesha idadi kamili ya Watanzania wanaoishi Nje ya Nchi, na kile wanachokifanya huko. Na kwamba Serikali inapaswa kuhakikisha inaanzisha kanzi data ningependa kueleza kwamba hivi sasa Wizara inaendelea na maandalizi ya Sera ya Taifa ya Diaspora na yapo katika hatua nzuri. Mara baada ya kukamilisha sera hiyo tutaingia katika hatua ya kuwaandikisha Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Watanzania kuandikishwa ni la hiari kwa hiyo tunawaomba watanzania wote wanaoishi Nje ya Nchi wasikose kwenda kujiandikisha kwenye balozi zetu ili tuweze kuwatambua na kuwafahamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la uraia wa Tanzania ningependa kueleza kwamba suala la uraia linasimamiwa na Sheria ya Uraia Namba 6 ya mwaka 1995 ambayo imebainisha kuwa uraia wa Tanzania upo katika makundi matatu uraia wa kuzaliwa, uraia wa kurithi na uraia wa tajinisi (kuandikishwa) kwa mujibu wa sheria hiyo, aina ya uraia wa kuandikishwa uraia wa pacha haupo katika sheria za Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kubadili msimamo kwamba Tanzania imebadili msimamo wake kuhusu ushirikiano na nchi za Morocco na Israel na je mabadiliko hayo ya msimamo wa nchi yanalindwa na yaliridhiwa na Bunge? Na nini msimamo wetu kama Taifa juu ya tabia za kidikteta, ukiukwaji wa haki za kibinadamu, unyanyasaji na uonevu zinazoanza kuibuka na kujionyesha wazi miongoni mwa baadhi ya viongozi wa Mataifa mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ningependa nieleze kwamba Tanzania haikuvunja uhusiano na Israel mwaka 1973 kwa sababu ya suala la Palestina. Tanzania ilivunja uhusiano wa kibalozi na Israel mwaka 1973 kwa sababu baada ya Israel kuzishambulia nchi za Kiarabu na kuteka maeneo ya Sinai kwa upande wa Misri na kuteka maeneo ya Golan kwa upande wa Syria hiyo ndiyo ilikuwa sababu iliyoifanya Tanzania wakati huo kuvunja ushirikiano wa Kibalozi na Israel.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo nchi mbalimbali ikiwemo nchi ya Misri yenyewe na nchi nyingi za Kiarabu zimeanzisha uhusiano wa kibalozi na Israel. Hatuoni sababu sisi kutokuanzisha uhusiano wa ubalozi na Israel. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kuanzisha uhusiano wa kibalozi na Israel na kufungua ubalozi hakujatuondoa katika msimamo wetu wa kuunga mkono harakati za Wananchi wa Palestina. Na msimamo wetu uko wazi wala hauna kigugumizi, wala hauna tashwishwi tunasema tuwe na Israel iliyo salama na tuwe na Palestina iliyohuru katika hilo hatubadiliki na ndiyo maana mpaka leo tunavyozungumza miongoni mwa nchi ambazo zimeitambua Palestina na zina ubalozi wake hapa nchini ni Tanzania Palestina wana ubalozi wao Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo uhusiano wetu wa kibalozi na Israel hata kidogo hautatuondoa sisi kusimama kwa upande wa Palestina. Na ndiyo maana kama kuna nchi ambayo tumepiga kura kuunga mkono maazimio yake katika Umoja wa Mataifa, ni Palestina. Nina orodha ya maazimio 23 ambayo Tanzania imepiga kura in favour of Palestine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ningependa kuwahakikishia kwamba hatujatetereka lakini ni ukweli leo hii huwezi kuacha kuwa na mahusiano na Israel wakati nchi zote za Kiarabu zinamahusiano na Israel na yako mambo ambayo tunayahitaji kutoka Israel katika upande wa uchumi, upande wa kilimo, upande wa IT. Lakini hilo halitatuondoa katika kusema kwamba Palestina iwepo na iwe huru lakini pia Israel iwepo na iwe salama na maazimio hayo yapo mtu ambaye anapenda kuyapata atayapata jinsi ambavyo Tanzania imepiga kura kuunga mkono Palestina katika mambo yake mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Morocco na Saharawe na mgogoro wa Morocco Saharawi kwenye eneo la Sahara Magharibi. Tanzania inaunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika katika usuluhisho wa mgogoro huo, Tanzania inaendelea kuzisihi pande zote kukaa kwenye meza ya mazungumzo ili kupata suluhu ya kudumu ya mgogoro huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ndiyo maana kutokuegemea upande wowote tumekuwa tunahudhuria mikutano yote inayohusu Saharawi, tunahudhuria mikutano yote inayohusu Morocco. Na niseme hivi hata nchi hizo zenyewe ambazo zinawahisani watu wa Saharawi zinauhusiano wa kibalozi na Morocco mfano wa nchi hiyo ni Algeria na nchi ya Morocco kufungua ubalozi wake hapa nchini haukuifanya sisi tuiambie Saharawi ifunge ubalozi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo leo Tanzania Saharawi ina ubalozi wake Morocco inaubalozi wake na sisi tunashirikiana na wote bila kuwabagua na tunawahimiza wamalize matatizo yao kwa kufuata maazimio ya Umoja wa Mataifa. Na tunaishukuru Algeria ambayo pamoja na mvutano wote haijavunja uhusiano wa kibalozi na Morocco hata wakati nchi nyingine zilipovunja uhusiano wa kibalozi na Morocco. Kwa hiyo hatuoni sababu ya kufanya hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwa hoja alizozitoa Mheshimiwa Suzan Anselem Jerome Lyimo Mbunge wa Viti Maalum CHADEMA ambaye ameishauri Serikali kufanyia kazi changamoto za kupandishwa vyeo watumishi wa Wizara ambao wamekaa kwenye cheo kimoja kwa muda mrefu. Na kutaka kujua Serikali inampango gani wa kupeleka mbadala wa watumishi waliorudi Makao Makuu kwenye Balozi zetu na kuishauri Wizara kutoa mafunzo ya Kideplomasia kwa mabalozi wetu wanaoenda kuhudumu kwenye Balozi zetu nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako tukufu kwamba tayari katika mwaka huu wa fedha tunaoumaliza jumla ya wafanyakazi 87 wamepandishwa vyeo, 66 wamepandishwa vyeo na 21 Wizara imependekeza wapandishwe vyeo vya huo msereleko. Tunayo barua kuotoka Ofisi ya Rais, Manajimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora yenye Kumb. Na. BC.46194/03D/44 ya tarehe 16 Aprili 2019 na barua yenye Kumb. Na. BC.46/97/03D/45 ya tarehe 30 Aprili, 2019. Barua hizi zimetoa kibali cha kuwapandisha vyeo jumla ya watumishi 66 na kuwabadilisha kazi recategorization jumla ya watumishi watatu. Jitihada hiyo itaendelea kama ambavyo tumekuwa tunafanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala kutoa mafunzo ya kidiplomasia kwa Mabalozi wetu wanaoenda kuhudumu kwenye Balozi zetu. Ningependa kulihakikishia Bunge lako tukufu kwamba hicho ndicho kinachofanyika, hakuna Balozi anayepelekwa nje bila kufanyiwa mafunzo katika Chuo cha Diplomasia. Sio Mabalozi tu hata Watanzania ambao wanaochaguliwa kwenda kufanya kazi kwenye Mashirika ya Kimataifa ambao Serikali imeawaidhinisha waende, nao pia wanafanyiwa mafunzo haya na ninakubaliana na yeye kabisa kwamba kuna umuhimu wa sisi wote kujifunza etiquette za Kibalozi na Kidiplomasia ikiwa ni pamoja na Wabunge ili tuweze kuelewa hizi etiquette za kidiplomasia zinatakiwa ziwe namna gani.

Mheshimiwa etiquette Spika, kuhusu Mheshimiwa Riziki Said Lulida wa Lindi ambaye ameulizia suala la mjusi toka Tendaguru, Lindi au kwa jina la kiingereza Dinosaur. Ningependa nieleze kwamba ni kweli ukienda kwenye Jumba la Makumbusho ya Elimu ya Viumbe yaani Museum for Natural History ya ...yako masalia ya Dinosaur wa sita kutoka Tanzania ambayo wakati huo ilikuwa chini ya utawala wa Wajerumani na kwa kweli masalia hayo yalitolewa Tendaguru na ukifika pale wameeandika yametolewa Tendaguru, Lindi.

Mheshimiwa Naibu Spika, masalia hayo ni mchanganyiko wa mifupa halisi mjusi mkubwa Dinosaur na cas, cas ni maeneo ambayo mifupa haikupatikana walitengeneza ili kukamilisha umbo la wanyama hawa. Masalia yalichukuliwa kutoka kilima cha Tendaguru kuanzia mwaka 1909 mpaka mwaka 1913 wakati wa ukoloni wa Mjerumani.

Mheshimiwa Naibu Spika, takribani tani 250 za masalia pamoja na mimea silichukuliwa na kupeleka Ujerumani. Majina ya kitaalamu ya Dinosaur hao ni Brachiosaurus, Branchai, Kentrosaurus, Diastosaurus, Digasaurus, Erliphosaurus, Bambegi na Arosaurus na huyu Brachiosaurus Branchai ni mrefu na anachukua urefu wa ghorofa tatu. Na mimi kwa miaka tisana na siku nne nilizoishi pale Berlin hakuna Watanzania waliokuja kunitembelea sikuwapeleka kwenda kuyaona hayo masalia ya Dinosaur ni makubwa na bado ipo mifupa mingine ambao ipo kwenye sera ipo kwenye maghala ambayo bado hayajaunganishwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo upo umuhimu wa Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ujerumani kuzungumza kuhusu suala hilo. Kabla ya Ujerumani Mgharibi na Ujerumani Mashariki kuungana, Ujerumani Mashariki ambapo ndipo yalipokuwa hayo masalia kwenye Chuo Kikuu cha Berlin walikuwa wameanza utaratibu wa kujenga Makumbusho ya Elimu ya Viumbe hai Arusha ili waweze kuleta leprechaun mfano wa hao Dinosaur. Kuna umuhimu tena wa kufufua mazungumzo na Serikali ya Ujerumani ili tuchukue hiyo hatua ya kwanza kabla ya kuingia kwenye hiyo hatua ya pili ya kuomba masalia haya yarudi. Kwa sababu yanahitaji utaalamu wa hali ya juu kuyatunza na tunadhani hali ya hewa ya Arusha inafaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ombi lake kwamba watu wa Tendaguru waweze kufaidika na mijusi hawa ambao wapo Berlin, wazo hili tumelichukuka na sisi tutazungumza na Serikali ya Ujerumani kuona ni kwa kiasi gani Wajerumani na hasa wanaohusika na mambo ya utafiti wataikumbuka Tendaguru ambapo hao mijusi walichukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Timotheo Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini kwa maelezo aliyoyatoa kuhusu hali ya haki za binadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Machi tulipata nafasi ya kwenda kwenye Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Kimataifa na tulipofika palikuwa tayari taarifa zimepelekwa nyingi sana kwamba Tanzania hali ya haki za binadamu haiko sawasawa. Tulitoa maelezo na maelezo yale yaliwaridhisha na kwa maana hiyo Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa aliiondoa Tanzania katika ripoti yake ya nchi zinazovunja haki za binadamu, aliiondoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliwaeleza bayana wenzetu kwamba moja hakuna haki ambazo hazina mipaka, haki zote zina mipaka. Mipaka hiyo imewekwa ndani ya Katiba wazi kabisa, hakuna uhuru wa yoyote kuingilia uhuru wa mtu mwingine. Kwa hiyo, mpaka wa kwanza wa haki za binadamu ni pale haki ya mtu mwingine inapoanza. Kwa hiyo, hakuna haki ambayo haina mpaka na Katiba yetu imeweka wazi kabisa katika Ibara ya 30 ni mipaka gani imewekwa kuhusu haki za bindamu nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kama iliyoelezwa sisi mahakama zetu na tatizo kubwa tulionalo sisi na hapo wa kulaumia ni mimi na Dkt. Mwakyembe. Kosa kubwa tulilolifanya mimi na Dkt. Mwakyembe ni kutokuandika commentary ya Katiba yetu. Kwa hiyo, watu wengi wanaposoma haki za binadamu wanasizoma silivyo ndani ya Katiba bila kuwa na commentary ya kuwaonesha ibara hii ya Katiba tayari Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa imetoa tafsiri hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishe sisi ndio nchi inayoongoza katika hukumu zetu za haki za bindamu kuwa cited na Mahakama za nchi nyingine za Commonwealth. Kesi ya kwanza iliyoamuliwa na Mahakama Kuu iliyotupa umaarufu mkubwa kabisa na kunukuliwa na mahakama zaidi ya 56 ni kesi ya Horaria vs Pastory. Horaria binti wa Kihaya ambaye alizuiwa kurithi mali kwa sababu ni mwanamke.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mahakama Kuu ya Tanzania kuhumu ya Jaji Mwalusanya ilisema haki hiyo, sheria hiyo ya mila inavunja Katiba na baada ya hapo hiyo ndio imekuwa reference ya nchi nyingi kuhusu haki za wanawake zinapovunjwa na sheria za kimila. Kwa hiyo sisi Tanzania tumepiga hatua kwamba hata sheria za kimila zimewekewa mpaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hivi majuzi zimetoka kesi mbili maamuzi ya Mahakama ya Rufaa kwenye kesi ya Mheshimiwa Freeman Mbowe na Mheshimiwa Esther Matiko, kabla ya hizo kesi kuamuliwa nilifuatwa na watu wa nje wengi sana wakati huo nikiwa Waziri wa Katiba na Sheria wakinisihi niiambie mahakama hizo kesi zifutwe, jibu langu lilikuwa we are not a banana republic allow the court to do their job. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma leo hukumu hizo mbili zimeweka misingi mizuri sana tisa ya jinsi gani mahakama zishughulikie suala bail (suala la dhamana). Ningeshawishika ili kuwafurahisha na labda wanisifie na wanipambe hao watu wa nje ningeimbia mahakama bwana hii kesi iacheni, tungekuwa tumekosa judgement nzuri kabisa ya Jaji Rumanyika ambaye ameweka sasa misingi mizuri tisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nina imani hukumu hiyo sasa itakuwa ni precedent ingawa sio binding katika nchi nyingine za Commonwealth. Kwa hiyo mahakama zetu zinafanya kazi kubwa sana na ndani ya ile hukumu kuna mstari watu wengi hawausemi. Sasa hivi hawa Wabunge wawili hawawezi kusafiri nje ya nchi bila permission of the court kwa sababu wali-jump bail, lakini kikubwa kwenye judgement hiyo ni ile misingi tisa ambao sasa mahakimu wote ni lazima waizingatie wanapotaka kumnyima mtu dhamana na ni misingi imewekwa vizuri na itawasaidia sana walio chini yake na sana itakuwa binding to all subordinate courts.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi baada ya hukumu hiyo Mheshimiwa Naibu Spika niliwaita baadhi ya hao waliokuja kunisii nifanya hivyo, nikawambia hii misingi tungeipata wapi? Kwa sababu kuna tabia ya hawa wenzetu wa nchi za Magharibi na nchi za Magharibi hazina moral authority za kutufundisha haki za binadamu. Naawaambia na uzuri nimekaa nao miaka tisa, nimesoma nao wajinga pia kule wengi na nimefaulu nikawashinda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi nchi hizi za Afrika we have never enslaved anybody, we have never colonized anybody, we have never plundered property of anyone, wao wametu- enslave, wametu- colonize na wame-plunder our resources, hawawezi kuwa na moral authority. Nchi za Magharibi sisi hatujawahi kusababisha vita yoyote, wao wamesababisha vita kuu mbili, na vita zote kuu mbili zimekuwa na madhara kwa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Vita ya Kwanza ya Dunia ilipokwisha makoloni yote ya Wajerumani yaliwekwa chini ya league of nations yaligawanywa, Tanganyika huku, Rwanda na Urundi kule. Na nchi hii kwa miaka mitatu ilikuwa na haina jina, haina mwenyewe, Cameroon ikagawanywa, Togo ikagawanya, waliacha ... West Africa ambayo leo ni Nambia. Na matokeo yake we became the cinderella of West Africa, the British did nothing, the British did nothing for this country. The biggest university we have tumeijenga wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waingereza hawajatuachia University they did nothing. Hata reli ile ile aliyoacha Mjerumani na sasa tunajenga nyingine. Vita Kuu ya Pili ya Dunia wamechinjana Warusi peke yao walikufa milioni 20. Sisi hatukumkamata shoga kumtia kwenye gas chamber kama walivyofanya Wajerumani, sisi hatukumkamata chotara tukamtia kwenye gas chamber, sisi hatukumkamata Myahudi na kumtia kwenye gas chamber, sisi hatukukamata mashoga na kuwatia kwenye gas chamber. Wao wamefanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, so they have no moral authority of telling us anything, tutaendelea kuheshimu haki za binadamu kwa sababu ni muhimu kuziheshimu, tutaendelea kuheshimu Katiba yetu kwa sababu ni muhimu kuiheshimu. Lakini sio kwa sababu kuna mtu anayetuambia tuiheshimu na tuchukue jitihada zote kulinda haki za binadamu kwa sababu binadamu wote ni sawa, huo ndio msingi wa Katiba ya TANU, huyo ndio msingi wa Katiba ya CCM na huo ndio msingi wa Katiba yetu. Binadamu wote ni sawa na wanastahili heshima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wao hawakutuheshimu na wao hawakutuchukulia kuwa sawa. Nchi hii imewahi kuingizwa katika ushauri wa ajabu kina Mzee Mkuchika wapo hapa mwaka 1958 tulilazimshwa kufanya uchaguzi na ninasema hivi kwa sababu wanafunzi wapo waelewe. Tukaambiwa ili mjiandae kupata uhuru lazima tuwafundishe kupiga kura, tukaambiwa kila jimbo la uchaguzi tuchangue Wabunge watatu Mzungu, Mhindi na Mwafrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanachama wengi wa TANU walikataa ikiwa ni pamoja na Katibu Mkuu wa TANU wa wakati huo Zuberi Mtemvu ambaye alijitoa akaunda chama chake cha African National Congress. Tulivuka huo mtihani, tumevuka mitihani mingi na huu mtihani tutauvuka tena kwa ushindi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1985 benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa lilitupigisha magoti kwa sababu tulikuwa hatuna uwezo wa kiuchumi. Sasa tunajenga Stiegler’s Gorge itatupa umeme tunajenga Standard Gauge Railway tutasafirisha mizigo. Baada ya hapo huduma zetu za kijamii katika elimu, afya na maji haitategemea tena fedha kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tuwe ndio kizazi cha mwisho cha kutegemea misaada, wajukuu zetu na vitukuu vyetu wasiishi fedheha hii tena. Fedheha hii iishe na sisi, tunavuna haya kwa sababu bado hatujafikia mahali pa kujitegemea na mimi nashukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchukua hii miradi ya kimkakati ambayo baadaye italifanya Taifa hili lijitegemee liwe lenye nguvu, na mimi nimefarijika sana na ningependa kuwaambia Watanzania wote Mheshimiwa Rais leo amemaliza ziara ya Zimbabwe, tumekuwa Afrika ya Kusini siku nne, tumekuwa Namibia siku mbili. Zimbabwe ilikuwa tukae siku mbili lakini wakamuomba aongeze siku ya tatu. Ndugu zangu wanamuona ni Mwafrika mahiri, shupavu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawaambia Watanzania wote wenye umri wangu tumshukuru Magufuli kwa kufanya mambo haya makubwa ambayo Baba wa Taifa aliyajenga, Mzee Mwinyi akaichukua nchi hii kipindi kigumu, tumepigishwa magoti tumekataa na waliofuata wamejenga msingi. Mkapa, Kikwete na sasa Magufuli na Magufuli ndio atakuwa Rais wa mwisho kwa maoni yangu aliyemuona Nyerere akiwa mtu mzima. Na ni vizuri Mungu atambariki kwa kukamilisha miradi yote ya Mwalimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie tulipifika Pretoria moja ya sababu kubwa ya kushangiliwa kwanza kuwaona Rais aliyestaafu na Rais aliyemwachia wapo pamoja na wameshuka pamoja is very rare, lilikuwa ni jambo la fahari. Nchi nyingine Rais Mstaafu na Rais aliye madarakani hata kusalimia hawasalimiani. Jambo kubwa, kwa hiyo Mheshimiwa nilikuwa kwenye uwanja nimeona aliyeshangiliwa zaidi kuliko wote ni Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumekwenda Nambia, tumekwenda Zimbabwe na kote watu wametupokea vizuri, na safari imekuwa ya mafanikio makubwa na manufaa makubwa kwa nchi yetu. Leo hawatanikasirisha leo sikasiriki ng’oo, ndio leo sikasiriki ng’oo, mtazoza mpaka mtachoka. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maswali tuliyoyapata kwa maandishi na ambayo tumeyajibu na mengi yanafafan na yale ambayo yamekwishatolewa, kuna swali kutoka Mheshimiwa Lucia Michael Mlowe, Mheshimiwa Ritta Kabati, Mheshimiwa Rhoda Edward Kunchela, Mheshimiwa Christopher Chiza, Mheshimiwa Janet Mbene, Mheshimiwa Mwanne Mchemba, Mheshimiwa Sonia Juma Magogo, Mheshimiwa Hamoud Abuu Jumaa, Mheshimiwa Zuberi Kuchauka, Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mheshimiwa Zainab Mndolwa Amir na Mheshimiwa Janeth Moris Masaburi.

Mheshimiwa Naibu Spika, michango yote hii tumeipokea na tumeipa majibu na tutasambaza majibu yote ya maswali hayo ya maandishi tuliyoletewa.

Mheshmiwa Naibu Spika, ningependa tena nichukue fursa hii kukushukuru sana Naibu Spika, kuwashukuru Wabunge wote kwa michango mikubwa waliyoitoa kwa Wizira yetu na imani yangu Inshallah katika mwaka huu wa fedha ambao tutauanza baada ya Bunge la hili la Bajeti kukamilika tutaendelea kutekeleza vipaumbele vyote vilivyopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, hatutakaa kimya nchi yetu inapobezwa, hatukaa kimya nchi yetu inapotukanwa, hatutakaa kimya nchi yetu inapochokozwa. Tutajibu tutafafanua tutaeleza tulifanikiwa Geneva tutafanikwa New York na tutafanikiwa mahali popote, huu sio wakati wa kukaa kimya, huu sio wakati wa kupuuza, kila linalotolewa lijibiwe tena lijibiwe kwa stahili kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumaliza, mimi sipendi sana kujieleza mimi ni nani, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri amesema na Mheshimiwa Naibu Waziri na Mheshimiwa Ummy Mwalimu ni wanafunzi wangu wa jurisprudence mara baada ya kuwa nimerejea toka masomoni nje, nimewafundisha jurisprudence, lakini mara nyingi katika nchi hii sio mara ya kwanza kuombwa na nchi yangu kufanya kazi ngumu. Mheshimiwa January Makamba yupo hapa, Sheria ya Mazingira hiyo anayoitumia aliyeisimamia, aliyeitunga na kuhakikisha inakuja Bungeni wakati Mheshimiwa Chenge kaka yangu akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi na ninaomba niwasomee Hansard na nimsome wakati huo Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mheshimiwa Arcado Ntagazwa anasema nini kuhusu Palamagamba Kabudi ndani ya Bunge hili mwaka 2004. (Makofi)

Anasema; “Nimalize sehemu hii ndogo kwa kumshukuru na kumpongeza, ataniwia radhi kama nitatamka jina lake yabidi nifanye hivyo, Dkt. Palamagamba Kabudi, Mhadhiri wa Sheria katika Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Dkt. Palamagamba Kabudi ndio Mshauri Mwelekezi (Consultant) kwa lugha ya kiingereza wa Mradi wa Kubainisha Mfumo wa Kitaasisi na Kisheria katika jitihada za Taifa letu kuhifadhi na kusimamia mazingira, kujihakikishia maendeleo endelevu. Tunawashukuru Benki ya Dunia, waliohisani mradi huo na kupitia kwa Dkt. Palamagamba Kabudi Tanzania tuna mahali pa kujidai, kwani kwa yakini kuwa nchi yetu tunao wataalam wazalendo wanaokidhi sifa zitakiwazo Kimataifa. Maana Dkt. Palamagamba Kabudi sio peke yake, wako zaidi kama huyu.” Hiyo ilikuwa tarehe 10 Novemba, 2004. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Sheria ya Kupambana na Rushwa inatungwa mwaka 2004, wakati upinzani chini ya Dkt. Wilbrod Slaa na Hamad Rashid na CCM wameshindwa kuelewana, mimi ndio niliyeitwa ku-facilitate maelewano hayo. Sasa naomba nimnukuu Dkt. Wilbrod Slaa, Kiongozi wa Upinzani wakati huo Bungeni, ambaye aliongea baada ya Halima Mdee kumaliza kuongea; anasema hivi: “Kwa bahati mbaya, Waziri ame-quote mifano ya mtu mmoja mmoja walioleta hisia zao, lakini taarifa ya mwisho iliyokuwa summed up na Profesa Kabudi ambaye alikuwa rapporteur wetu ambaye mimi ndiye nikaja kuwakilisha, haikusema hivyo.” Mwaka 2007 brokered, compromise between the opposition and CCM, tena na Dkt. Slaa na Hamad Rashid. (Makofi)

Kwa hiyo, mtu yeyote ambaye ana wasiwasi au anaishi kwa hofu ya Kabudi, aendelee kuishi na hofu hiyo. Yeyote anayeishi na hofu ya Kabudi aendelee kuishi na hofu hiyo. Kabudi hatatetereka, Kabudi hataacha kufanya kazi. Kwa hiyo hatatetereka, ishini na hofu ya Kabudi, Kabudi anaishi kwa neema ya Mungu. (Makofi/Kicheko/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, msisahau ndani ya Bunge hili, mimi kwenye timu hii nimeingia wakati wa dirisha dogo. Nimesajiliwa kwenye dirisha dogo, hilo mlifahamu. Kwa hiyo, endeleeni kuishi na hofu ya Kabudi, endeleeni kuishi na husuda ya Kabudi, endeleeni kuishi na wivu wa Kabudi, lakini yeye atafanya kazi bila uoga wala bila kutetereka, kwa sababu nchi yangu ni muhimu kuliko mimi mwenyewe. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mama yako!

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii ni kubwa kuliko sisi wote, kwa hiyo, nitaitumikia nchi hii bila uoga, bila wasiwasi, bila chuki kwa sababu ni wajibu niliyoitiwa na mwezi huu ni Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, nawaomba wote muisome Surat Yussuf mtaelewa. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Ipo.

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Wakristo mkasome kitabu cha Mwanzo Sura ya 42 mpaka 48 kisa cha Yusufu na nduguze, mtajua. Huyu ndio Yusufu, msimpeleke utumwani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kueleza hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kukushukuru tena kwa kunipa nafasi ya kuhitimisha hotuba ya Makidirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022. Jumla ya Waheshimiwa Wabunge 12 wamechangia hotuba hii, kati ya hao Waheshimiwa Wabunge 10 wamechangia kwa kuzungumza ndani ya Bunge na Waheshimiwa Wabunge wawili wamechangia kwa njia ya maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri. Tumepokea maoni na ushauri wao ambao unalenga kuboresha utendaji wetu na utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa ujumla. Maoni na ushauri wao uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge ni wenye tija na tunaahidi kufanyia kazi. Aidha, tunaishukuru sana Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria na Kamati ya Bunge ya Bajeti kwa maoni yao mazuri ambayo tutayazingatia na kuyatekeleza katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu baadhi ya hoja zilizotolewa na Wabunge wakati wa michango yao na nyingine tutaziwasilisha kwa maandishi kwa ufafanuzi zaidi. Mheshimiwa Joseph Anania Thadayo kuhusu suala lake la Mabaraza ya Ardhi, lile la upande wa Mahakama, uliliweka vizuri nami nisingependa tena kulizungumzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Mabaraza ya Ardhi na changamoto, napenda kufafanua kwamba Mabaraza ya Ardhi yameanzishwa rasmi na sheria inayotawala mabaraza hayo. Mwaka 2000 Serikali ilifanya tathmini kupitia Tume ya Kurekebisha Sheria kuhusu utendaji wa Mabaraza ya Ardhi hayo na kubaini kuwepo kwa changamoto zifuatazo: changamoto za kimfumo, changamoto za kimaadili na changamoto ya uhaba wa rasilimali mali na changamoto ya kiutendaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, uamuzi wa Serikali ni kuwa mabaraza hayo yabaki chini ya Wizara ya Ardhi na TAMISEMI na yaboreshwe. Kwa hiyo, Wizara ya Katiba na Sheria inaendelea kushirikiana na Wizara husika ili kuboresha mifumo ya utendaji wa Mabaraza hayo ya Ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji masuala yote aliyoyaainisha yanayohusu vifungu vya Katiba vya 133 na Ibara ya 135 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mambo hayo tumeyapokea, ni mambo yanayohusu Muungano na yatawasilishwa Serikalini ili yajadiliwe na Ofisi ya Makamu wa Rais, lakini pia Tume ya Pamoja ya Ushirikiano.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, napenda nitoe indhari kwake kwamba Katiba haijitekelezi yenyewe, inatekelezwa na sheria, ndiyo maana yako mambo ndani ya Katiba ambayo huchukua muda kutekelezwa kwa sababu lazima sheria zijielekeze katika utekelezaji mzuri wa aina hiyo. Mambo ambayo ndani ya Katiba yamechukua muda kutekelezwa siyo kwa sababu Serikali haitaki yatekelezwe, lakini ni mambo ambayo yanahitaji mashauriano, majadiliano, maelewano ili hatomaye yatakapotekelezwa yatekelezwe kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, maoni yaliyotolewa na Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespha Kabati, kwanza ni kuhusu kucheleweshwa kwa mashauri bila sababu za msingi na ametoa mifano ya mashauri ya mauaji na ubakaji hasa huko Iringa. Hata hivyo, ningependa kusema kwamba, zipo sababu nyingi za mashauri hayo kuchelewa na sababu hizo ni mtambuka zinazohusu Mahakama, wadaawa, mawakili, mashahidi na wadau wote wa utoaji haki kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikija katika mashauri ya ubakaji na hasa yanapohusu wanafamilia, moja ya changamoto kubwa zinazopatikana ni ndugu kutokutaka kupelekana Mahakamani ili kulindana na Mahakama haiwezi kutoa maamuzi kuhusu masuala hayo bila mashahidi kwenda Mahakamani na kutoa ushahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naafikiana na Mheshimiwa Ritta Kabati kwamba, kesi za mauaji ni nyingi kiasi katika Mkoa wa Iringa na sababu zake inafaa zibainishwe na wataalamu wa sosholojia na anthropolojia, kwa nini Iringa kesi za mauaji ni nyingi ili twende kwenye kiini cha matatizo ya watu wa Iringa kwa mujibu wa maelezo yake kwamba mauaji ni mengi, hatimaye pia tupunguze idadi ya kesi zinazokwenda Mahakamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, katika kesi za mauaji nazo zinahitaji uchunguzi wa kutosha kabla ya kutoa maamuzi yanayohusika. Kwa hiyo, nalo ni eneo ambalo litafanyiwa utafiti zaidi ili kujua ni kwa kiasi gani tutapunguza idadi ya mashauri ya mauaji katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa maoni ya Mheshimiwa Agnesta Lambert Kaiza, moja ningependa kumweleza kwamba sababu za mahabusu kulundikana mahabusu, siyo moja tu, ziko sababu nyingi sana ambazo ameshazieleza Naibu Waziri. Kuhusu masharti ya dhamana katika mashauri ya jinai yameainishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 148 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Aidha, kifungu hicho kinaeleza wazi kuwa pale ambapo masharti ya dhamana yanataka kuweka Mahakamani mali isiyohamishika, siyo lazima kuweka hati ya umiliki wa mali hiyo, bali ushahidi wowote unaothibitisha umiliki wa mali hiyo. Kwa hiyo, wananchi hawahitaji kupeleka hati hiyo, isipokuwa ushahidi wowote unaothibitisha umiliki wa mali hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mahakama pia imetoa mwongozo wa utoaji dhamana unaoelekeza mambo muhimu ya kuzingatia katika kutoa dhamana. Hata hivyo, kama mdaawa yeyote hakuridhika na tafsiri ya Mahakama ya kifungu hicho katika mchakato wa kutoa dhamana, ana haki ya kukata rufaa katika Mahakama ya juu. Wote tunafahamu kwamba Mahakama ya Rufaa ya Tanzania katika uamuzi wake uliotolewa tarehe 5 Agosti, 2020 katika Shauri la Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Dickson Paul Sanga kupitia shauri la rufaa namba 175 la 2020 ilitoa uamuzi wa kueleza kuwa Kifungu cha 148 (5) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashitaka ya Jinai ni kifungu halali kwa kujibu wa Katiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mahakama ilieleza kuwa kifungu tajwa kinalenga kushughulikia zuwio la dhamana kwa washitakiwa wote waliofunguliwa mashitaka Mahakamani ambapo endapo wataruhusiwa kupata dhamana kunaweza kusababisha kuvurugika kwa amani, utulivu na usalama wa nchi, raia na watuhumiwa wenyewe. Ni rai yangu kwa niaba ya Serikali kwamba, watu wajiepushe na makosa haya na waendelee kuwa raia wema. Siyo nia ya Serikali wala Mahakama kuwanyima watu uhuru wao, lakini Serikali na Mahakama huchukua hatua hizo pale inapobidi na kwa maslahi mapana ya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maoni yaliyotolewa na Mheshimiwa Mwasi Damas Kamani; moja, Tume ya Kurekebisha Sheria imekuwa inafanya mapitio ya mifumo ya sheria mbalimbali ili sheria hizo ziakisi mabadiliko yanayotokea na anayeweza kupeleka maombi hayo ni pamoja na Serikali yenyewe pamoja na Mahakama na hata raia anaweza akaiomba Wizara ya Katiba na Sheria kama mlivyofanya sasa, kupeleka maoni hayo kwa Tume ya Kurekebisha Sheria ili iyafanyie utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusisitiza kwamba Sheria ya Tume ya Marekebisho ya Sheria haiielekezi tume hiyo kuleta ripoti yake Bungeni. Kwa hiyo, tume haileti ripoti zake Bungeni badala yake, inapeleka ripoti zake kwa Waziri wa Katiba na Sheria ambapo huziwakilisha Serikalini ili zifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo mambo mengi aliyoyaeleza yanahusu sekta ya uchukuzi, sekta ya bima, lakini kwa sababu ameyaelekeza kwa upande wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Waziri wa Katiba na Sheria atayaangalia hayo; na kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, tutahakikisha kwamba mambo hayo nayo tunayatazama na kuona namna gani yafanyiwe kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, maoni ya Mheshimiwa Salome Wyclife Makamba; moja ni kuhusu kupitia sheria za kusimamia mambo ya umri wa ndoa. Kwenye jambo hili ningependa nieleze kwa makini sana kwamba, maelezo yaliyotolewa huko nyuma kuhusu Sheria ya Ndoa ni vizuri tukazingatia kwamba Sheria ya Ndoa isihukumiwe kwa kifungu kimoja tu. Ule msemo wa samaki mmoja akioza, wote wameoza, siyo sahihi kwa Sheria ya Ndoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, narudia kusema niliyowahi kuyasema, Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ndio sheria ya kimapinduzi ya ndoa katika bara la Afrika, is the most progressive law of Marriage in Africa kwa hiyo tusiihukumu kwa kifungu kimoja tu. Kifungu hicho kwa maoni yangu wakati ule na bado nayasimamia shauri hilo hilo lingeweza kupelekwa Mahakama ya Rufaa sio kupitia kifungu cha 13 cha ubaguzi bali kupitia kifungu cha haki ya kuishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja hapa kama ni afya ni the right to life, lakini kwa kutumia sheria ya kifungu cha ubaguzi, tunaingia katika mtego kusahau kwamba kwa hali halisi ya Tanzania lazima tuwe na ubaguzi chanya kwa faida ya wanawake, lazima tuendelee kuwa na ubaguzi chanya kwa faida ya wanawake, ndio hiyo inaitwa affirmative action ambayo pia ni ubaguzi lakini ni ubaguzi wa aina gani? Ni ubaguzi chanya na hadhari yetu ilikuwa tukiendelea kutumia mwanya wa ubaguzi kwa kifungu hiki tunaweza kuwa tunavunja msingi muhimu ambao umefanya wanawake wa Tanzania wapate ubaguzi chanya ili waendelee, wawakilishe Bungeni na ili wawe katika sehemu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama ni kuhatarisha Maisha, ningekuwa mimi napeleka shauri hilo Mahakamani, ningepeleka chini ya the right to life na sio the right against discrimination. Hata hivyo, uamuzi wa shauri la Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Rebecca Jumi, Rufaa Na. 204 ya mwaka 2017 – 2019, Wizara ilianzisha mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Ndoa na Sheria ya Usimamizi wa Mirathi ili kuainisha umri wa kuolewa au kuoa kwa mwanamke na mwanaume mtawalia na hatimaye Februari, 2021, Serikali iliwasilisha Bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ndoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara iliwasilisha mapendekezo ya kubainisha wasimamizi na warithi wa mali moja wa mwenza anapofariki. Kwa kuwa marekebisho ya Sheria ya Ndoa yanaihusisha jamii kwa ujumla wake, Serikali ilishauriwa kuwashirikisha wananchi ili kupata maoni kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo. Kwa hiyo tarehe 17 Machi, 2021, Wizara ilianza tena kufanya mikutano baina yake na viongozi wa dini na baadaye makundi mengine ili kupokea maoni husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara imeandaa mpango kazi wa kuyafikia makundi yote katika jamii ili kupata maoni yatakayowezesha kupatikana kwa sheria iliyoridhiwa na wote. Hadi sasa Wizara imeweza kukusanya maoni kutoka Mkoa wa Arusha, Mwanza na Dar es Salaam kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kimila na kidini. Wizara itakapokamilisha zoezi la kukusanya na kupokea maoni katika eneo la mirathi na ndoa itayawasilisha mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Ndoa na Mirathi ili kuendana na hali ya maendeleo tuliyonayo bila kuathiri mila, desturi, tamaduni na dini zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, maoni yaliyotolewa na Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi tumeyapokea na ushauri wa Mbunge umezingatiwa isipokuwa ule wa kwenda kulala gerezani huo ni mgumu kidogo, lakini mengine yote tumeyapokea, tutaona jinsi ya kuyakamilisha. Yale matatizo ya wale waliodhaniwa wamevamia hifadhi na matrekta yafuate utaratibu wa kawaida ili kuona ukweli uko wapi, lakini kama kweli waliingia katika hifadhi na hayo matrekta na ni hifadhi ambayo ipo katika bonde la Mto Kilombero ambalo ndilo linalolisha kiasi kikubwa cha maji Mto Rufiji, yaweza ikawa ni uhujumu uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Mheshimiwa Mohamed Salum Mohammed Shaafi, Mbunge wa Chonga, kwanza sijawahi kusikia Mahakama Kuu ya Tanzania imeinyang’anya Mahakama Kuu ya Zanzibar shauri lolote, kwa sababu Mahakama haifungui kesi inapelekewa kesi. Kwa sababu Mheshimiwa Salum Mohammed Shaafi ni Mswahili anayekifahamu kiswahili vizuri nataka kuamini hakukosea aliyoyasema na kama ni sahihi aliyoyasema hata mara moja hakuna mahakama yeyote inayoinyang’anya mahakama nyingine kesi kwa sababu mahakama sio ambulance, haifuati mgonjwa, mahakama inapelekewa kesi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna kesi inayohusu raia wa Tanzania wenye asili ya Zanzibar katika Mahakama Kuu ya Tanzania basi yupo aliyeipeleka, lakini haiyumkini kabisa Mahakama Kuu ya Tanzania, ikainyang’anya Mahakama Kuu ya Zanzibar kesi. Hakuna mahakama inayojipelekea kesi, lakini kama ni shauri linalosemwa, ningependa niseme hivi, shauri ambalo lipo mahakamani na linaendelea ni shauri la Mashekhe wa Uamsho.

Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo tarehe 15 Septemba, 2020, shauri la jinai namba 21 la 2014 lililokuwepo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mkoa wa Dar es Salaam lilifunguliwa rasmi katika Mahakama Kuu ya Kanda ya Dar es Salaam mara baada ya upelelezi kukamilika. Mnamo tarehe 17 Septemba, 2020, mchakato wa kuhamisha kesi husika Mahakama Kuu yaani zinaitwa committal proceedings ulikamilika, kesi hiyo ilikuwa ianze kusikilizwa tarehe tarehe 25 Machi, 2021, lakini kutokana na msiba uliotupata ilisogezwa mbele hadi mwanzoni mwa mwezi Aprili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Mahakama Kuu imeanza kusikiliza kesi hiyo namba 121 ya 2021 kuanzia tarehe 12 Aprili, 2021 na mahakama yenyewe ina uwezo wa kusema ina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo au haiwezi, sio mimi wala mtoa hoja. Kwa hiyo tuiachie Mahakama Kuu ya Tanzania ambayo sasa imeanza kusikiliza shauri hilo, yenyewe itajua mwenendo unavyokwenda na yeyote ambaye hataridhika na maamuzi ya Mahakama Kuu bado anayo nafasi ya kukata rufaa Mahakama ya Rufani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo madam suala sasa lipo mahakamani, mikono yetu na midomo yetu sasa imefungwa suala hilo ni sub judice tuiachie Mahakama Kuu sasa iisikilize shauri hilo na ile video inayotembea sana ilikuwa ni video ya maneno hayo niliyoyasema mwaka 2018 kabla ushahidi haujakamilika. Sasa ushahidi umekamilika committal proceeding zimekamilika, kesi ipo Mahakama Kuu, tuiachie Mahakama Kuu itoe uamuzi wake na baada ya kutoa uamuzi wake asiyeridhika ipo Mahakama ya Rufani na mahakama hii ni Mahakama ya Muungano ndio maana yapo mashauri kutoka Mahakama Kuu Zanzibar yanakwenda Mahakama ya Rufani na yapo mashauri kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania yanakwenda Mahakama ya Rufani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Zanzibar mashauri ambayo hayaji huko ni mashauri yaliyoanzia kwenye Mahakama za Kadhi au mashauri yanayohusu tafsiri ya Katiba ya Zanzibar, mengine yote yanakwenda mpaka Mahakama ya rufani na ndio pekee mahakama ya Muungano na inasikiliza rufani kutoka pande zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie tena, Mahakama Kuu ya Tanzania haijainyang’anya Mahakama Kuu ya Zanzibar kesi yoyote, ila kesi zimepelekwa na hizi mahakama mbili zina kitu kinaitwa concurrent jurisdiction, sasa haiwezekani mmoja amnyang’anye mwingine, sasa tumtafute mwingine lakini kama yalikuwa ni makosa ya tafsiri, maana yake kesi imefunguliwa huku basi hilo ni jambo linguine, Mahakama yenyewe itaamua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona nilieleze hilo ili tuondoe munkari katika jambo ambalo linahitaji umakini mkubwa kabisa ili lisilete dhahama katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu makosa yasiyokuwa na dhamana; kama nilivyosema uhuru wa mtu yeyote ndani ya Katiba yetu umewekewa mipaka. Tunazungumzia uhuru bila kwenda kwenye Ibara ya 30 ya Katiba yetu. Ibara ya 30 imeweka mipaka kwa uhuru wowote ule na mpaka wa kwanza mkubwa ni mwanzo wa uhuru wa mwenzako, ndio mwisho wa uhuru wako kwa hiyo hakuna uhuru usiokuwa na mipaka. Uhuru wowote una mipaka na hayo yameelezwa kwenye Ibara ya (30) ya Katiba yetu na pia kwenye maamuzi ya Mahakama ya Rufani ya kesi ya kukuchia ambayo Mahakama ya Rufani iliweka vigezo vya kuwekwa kwa mipaka hiyo ambavyo vipo wazi kabisa. kwa hiyo hata kwenye suala la dhamana mipaka ipo ili kuyalinda na kuyaainisha hayo ambayo yapo ndani ya sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, maoni yaliyotolewa na Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka ni ya msingi sana kuhusu suala la Liwale. Tupende kueleza tu kwamba palitokea changamoto katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa Mahakama katika Mkoa wa Mtwara na Lindi. Mkoa wa Lindi haukuwa na Mahakama hata moja ya wilaya, tumeshajenga mahakama tatu Mchauka na Liwale ipo katika hatua hiyo. Kwa hiyo Liwale haijasahaulika ila ni kwa sababu ya changamoto kubwa ya mahitaji ya mahakama katika wilaya hiyo na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika muda mfupi tutaona ni jinsi gani pia Liwale tuiweke katika msimamo huo unaostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niliweka kiporo kidogo suala lililoletwa na Mheshimiwa Restituta Taska Mbogo. Ni kweli kabisa kabla ya uhuru sheria za kimila zilikuwa hazitambuliwi kabisa, wakoloni waliziona sheria za kimila ni sheria za kishenzi na ndoa za kimila ni ndoa za kishenzi, lakini pia Waafrika walikuwa hawapelekwi mahakamani walikuwa wanahukumiwa na Machifu au Watemi na rufaa zao zilikuwa zinakwenda kwa Mkuu wa Wilaya. Zikitoka kwa Mkuu wa Wilaya, kwa Mkuu wa Jimbo, zikitoka kwa Mkuu wa Jimbo zinakwenda kwa Gavana. Mahakama ilikuwa ni kwa ajili ya Wazungu na Wahindi tu, ndio maana tunapata Uhuru mwaka 1961 waliopigania uhuru wa nchi hii na mmoja Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye yeye mwenyewe katika essay yake ya Socialism and Rural Development anaeleza ubovu wa baadhi ya mila zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu Nyerere bado aliona ni muhimu kwanza kuzitambua sheria za kimila kuwa ni sheria za watu wastaarabu na sio sheria za watu washenzi, ndio maana mwaka 1963 tunafanya codification ya Customary Law lakini codification hiyo ya Customary Law ya mwaka 1963 ilifanya pia mabadiliko ndani ya hizo sheria za kimila na ilitungwa chini ya Sheria za Serikali za Mitaa, kwa mfano kuhusu suala la wanawake kurithiwa wanapokuwa wamefiwa na wanaume zao, sheria ile iliongeza kipengele iwe kwa hiyari yake kama hataki asirithiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hiyo ilikuwa imepiga hatua kubwa kuliko sheria ya maandishi kwa sababu ndio sheria ambayo ilisema kitanda hakizai haramu, maana yake nini, haikutaka ubaguzi wa watoto ndani ya ndoa. Kwa hiyo sio kila sheria ya mila ichukuliwe jinsi ilivyo, ilifanyiwa marekebisho ili iendane na hali inayotakiwa. Sasa sheria hii imetungwa chini ya Sheria za Serikali za Mitaa, ndio maana ni muhimu tena Mabaraza ya Madiwani wa Halmashauri za Mitaa wazipitie tena sheria za mila na kuziuhisha kwa mazingira yaliyopo, lakini kuzituhumu na kusema sheria zinazotungwa na Bunge tu ndio sheria nzuri, tunarudi kuwatukana wahenga wetu kama walivyotukanwa na wakoloni kwamba sheria zao ni za kishenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siamini sheria za mila ni za kishenzi, yapo maeneo ni muhimu yarekebishwe, lakini kuzitupa moja kwa moja tukumbuke msemo wa Kiswahili Mkataa asili ni mtumwa. Hii isieleweke natetea sheria za kimila hivi hivi, lakini leo tuna mwanya mwingine, Katiba yetu ina sura nzima za haki za binadamu, bado mtu anaweza kwenda mahakamani kusema sheria hii ya kimila kwenye eneo hili inakwenda kinyume na haki za binadamu na mahakama ikafanya marekebisho ya sheria hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mambo yaliyorekebishwa na mahakama ni kuhusu kwa makabila yale ya ubabani, maana yake hapa Tanzania kuna makundi mawili ya makabila, makabila ya ubabani na makabila ya umamani, hakuna mjomba ni umamani. Kuanza kusema hawa ni wa upande wa wajomba ni kuwadhalilisha akinamama, ni makabila ya ubabani (Patrilineal) na makabila ya umamani (matrilineal).

Mheshimiwa Naibu Spika, huku kwenye makabila ya ubabani ukiisoma kesi ya Benardo Ephrahim dhidi ya Horaria Pastory na Gervas Kaizelege, Mahakama ilisema wazi kabisa sheria ya kumzuia mwanamke kurithi ardhi ni kinyume cha Katiba, ndio sheria ya Tanzania sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sio hivyo tu, ukisoma shauri lililofanywa na Jaji Kisanga kwenye kesi ya Haji Athuman Issa dhidi ya Routama Mituta imesema hivyo hivyo kwamba, sheria yeyote inayomnyima binti kurithi mali ikiwa ni ardhi ni kinyume cha Katiba. Kwa hiyo tuzisome sheria hizo na maamuzi ya mahakama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naona hatari, Watanzania tumeanza kusahau kwamba sisi mfumo wetu wa sheria ni wa common law na kwenye common law huisomi sheria tu, unaisoma sheria pamoja na maamuzi ya mahakama ili kupata jurisprudence ya eneo hilo. Ningeelewa msimamo huu kama ingekuwa tupo continental Europe na nina bahati ya kusoma katika mifumo yote miwili; nimesoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, common law nimesoma Freie Universität Berlin ambayo ni civil law. Kwenye civil law hoja hiyo ina msingi, lakini sisi ni lazima daima turejee katika mashauri ya mahakama ili kujua sasa tafsiri ya sheria ni nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo sisi ni watu wa common law, tuache na sisi wanataaluma sasa tuanze kutoa commentary ili watu wanaposoma kifungu cha Katiba ajue na maamuzi ya Mahakama ambayo yametoa tafsiri hiyo. Hata kabla ya hapo kuna Jaji mmoja Mkuu wa Tanzania tunamsahau mara nyingi sana na ndio alikuwa Jaji Mkuu wa kwanza Mtanzania Jaji Augustino Said; katika shauri la Ndewauyosia Daughter of Mbehanso dhidi ya Emmanuel Son of Malasi ya mwaka 1968 alisema Sheria ya Wachaga ya kuwazuia wasichana kurithi kihamba ni kinyume. Kwa hiyo ukiyachukua maamuzi yote haya, tayari yamekwishakupa mwelekeo wa nini msimamo wa sheria za Tanzania kuhusu hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni rai yangu, kuna mradi ambao ulianza katika Tume ya Kurekebisha Sheria kwa sababu mwaka 1963 codification ya Customary Law ilifanywa tu kwa makabila ya ubabani, makabila ya umamani hawakuwafanyia codification ya matrilineal na hayo yameleta matatizo makubwa na hasa katika mahakama zetu. Baadhi ya Mahakimu wanaofanya hivyo ni mahakimu ya jinsia ya kike kwa sababu hawajui mfumo wa sheria wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa mmojawapo ni wa Morogoro ambapo baadhi ya watoa haki hawaelewi kwamba kule wasimamizi wa ardhi ya ukoo ni wanawake; ni mama na dada. Kwa hiyo mama na dada wanapokwenda kusema kaka hakuwa na haki ya kufanya hivi kimila hawaelewi na mara nyingi hawaelewi kwa nini wasimamizi wa mirathi ni madada na sio makaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo asilimia 20 ni muhimu Serikali sasa itafanya juhudi ili sheria za kimila za watu wa umamani ambazo mimi naamini zitawasaidia wale wa sheria za mila za ubabani na wao kubadilika wakati ndio huu. Tukizipitia zile sheria hatuna haja ya kwenda kwa wataalam wa gender wa Marekani, wataalamu wa gender wa Ulaya, twende kwa wataalam wa gender wa Kimwera, Kimakua, Kiyao, Kimakonde, Kikwere, Kizaramo, Kikaguru, Kikutu, Kinguu na Kiluguru, tutapata majibu ya jinsi gani ya kumfanya mwanamke achukue nafasi yake ambayo anaichukua katika jamii hizo za sheria za umamani. Tofauti na sisi wengi ambao tunaishi katika sheria za ubabani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona nilieleze hili kwa muda kidogo ili niliweke wazi kwamba tunao utajiri ambao utatusaidia ndani ya Tanzania kubadilisha sheria zetu kwa sababu shida kubwa ya gender studies tumeanza kusoma European gender studies.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikwenda katika mkutano mmoja, wao matatizo yao makubwa sasa ni kwa nini bei ya sidiria ni kubwa kuliko bei ya shati. Sasa leo mjadala wa bei ya sidiria kuwa na bei kubwa kuliko shati Tanzania haina maana, sisi maana ni wanawake waweze kumiliki mali, wanawake waweze kufanya hivyo, lakini kwa wao mambo ya kumiliki mali na kufungua akaunti yalikwisha, sasa wanahangaikia bei ya sidiria na bei ya shati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni jambo ambalo linahitaji umakini na niliona niliweke mwisho ili nilitolee ufafanuzi na tulifanyie kazi. Mengine yale yote tutayajibu kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuhitimisha naomba tena Bunge lako likubali na kuidhinisha kiasi cha shilingi 78,464,886,000 kwa ajili ya Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Taasisi zake na shilingi 153,228,859,000 kwa ajili ya Mfuko wa Mahakama kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa shukrani nyingi sana kwa kupewa nafasi hii ya kuchangia katika Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Nichukue nafasi hii kumpongeza sana Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda, Katibu Mkuu na watumishi wote wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa hotuba nzuri ya bajeti ya suala ambalo ni muhimu sana ambalo ni elimu na maarifa, sayansi na teknolojia kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuliendeleza gurudumu hili la mapitio ya uboreshaji wa Sera ya Elimu na Mitaala katika nchi yetu. Serikali ya Awamu ya Sita imefanya jambo kubwa sana kukamilisha sera hii na sasa kuileta kwa wananchi ili wananchi waweze kuijadili na kutoa maoni yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Elimu ni muhimu sana. Serikali ya Awamu ya Sita na zilizopita zimewekeza sana katika miundombinu (hardware). Yawe ni majengo, ziwe ni maabara na sasa inajikita katika eneo muhimu sana la kuwekeza katika software na software ya elimu ni sera na mitaala. Hili ni zoezi muhimu na ni vyema niiombe Wizara makongamano na mijadala hii ambayo tumeiona iendelee katika maeneo mbalimbali ya Tanzania ili wananchi watoe maoni yao katika jambo hili muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja ambalo napongeza sana katika mwelekeo mpya wa sera ni sasa kuitoa elimu ya lazima kutoka darasa la saba na sasa kwenda kidato cha nne. Takribani sasa miaka 58 toka elimu ya lazima ilipotolewa darasa la nne kwenda darasa la saba na maamuzi yale ya kijasiri yaliyofanywa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1968 kutoa elimu ya lazima toka darasa la nne kwenda darasa la saba. Katika kipindi cha mpito kuanzisha shule ambazo ziliitwa extended primary school, yaani zile shule za darasa la nne zikaongezewa darasa la tano, la sita na la saba na wale wanafunzi walipofika darasa la saba wakafanya mtihani mmoja na wanafunzi wa darasa la nane middle school na ndiyo ikawa mwisho wa middle school. Kwa hiyo mambo haya yanayofanyika ni mambo makubwa takribani miaka 58 baada ya kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naunga mkono suala la kuwa na elimu ya msingi ya miaka sita ikifuatiwa na elimu ya sekondari ya miaka minne. Jambo hili pia siyo jipya sana, wale waliosoma miaka ya 1920, 1930 na 1940 palikuwa na aina mbili ya shule wakati ule, mmoja wa hao waliosoma ni Baba yangu. Palikuwa na District Schools na kwenye District Schools wanafunzi walisoma darasa la kwanza mpaka darasa la sita na baada ya hapo wakaenda kwenye central schools. Kwenye central schools walisoma miaka miwili, darasa la saba na la nane na baadaye wengine walikwenda kwenye taaluma kama vile Ualimu kwa miaka mitatu na wengine waliendelea darasa la tisa na darasa la kumi ili kupata sifa ya kwenda kusoma diploma ya elimu Makerere. Tutakapopata muda wa kuchangia haya tutayachangia zaidi ili kuzidi kuboresha hili jambo zuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo naomba nichangie katika maeneo mawili au matatu kama muda utaruhusu. Eneo la kwanza ni FDC, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi na eneo la pili elimu ya watu wazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa katikati palitokea upotoshaji kwamba Vyuo vya Wananchi - FDC ni vyuo vya CCM, siyo kweli. Vyuo vya Wananchi -FDC vilivyoanzishwa mwaka 1975 vilikuwa ni wazo la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere baada ya kutembelea nchi za Nordic na hasa Sweden alipokuta kule wana aina hii ya vyuo na vyuo hivyo ndiyo vikaanzishwa mwaka 1975 na kwa miaka mingi sana vilikuwa vina hisaniwa na Shirika la Fedha la SIDA la Sweden na lilipojitoa watu waliona labda vyuo hivi vitakufa lakini nashukuru vinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Wizara ya Elimu sasa iwekeze kwa kiasi kikubwa sana katika hivi Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi na ikiwezekana Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi viwe katika kila Kata ya nchi yetu. Kwanini nasema hivyo? Bado tuna kundi kubwa la wanafunzi waliomaliza darasa la saba hawakufaulu kwenda sekondari. Bado tuna kundi tena la wanafunzi waliomaliza Kidato cha Nne lakini hawakufanikiwa kupata taaluma. Pia tuna kundi la wanafunzi ambao wamesomea fani mbalimbali hata Vyuo Vikuu lakini hawana cha kufanya katika maeneo wanayoishi kutokana na kukosa stadi mbalimbali katika kilimo, ufugaji, ujasiriamali na ili waweze kujitegemea ninaona vyuo vya kufanya kazi hiyo ni Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mabadiliko haya ya Sera na Mitaala, kijana atakayemaliza Kidato cha Nne na sasa anaamua haendelei anakwenda kijijini au anakwenda kujiajiri bado atahitaji kuwa na mafunzo ya orientation. Mafunzo ya kumuandaa kwenda kwenye jamii, mafunzo ya kumuandaa kwenda kufanya anachokitaka kukifanya na chuo cha kufanya kazi hiyo mimi naona ni Chuo cha Maendeleo ya Wananchi - FDC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wale ambao tayari watakuwa wamejiajiri wana fani mbalimbali, wana taaluma mbalimbali, wana kazi mbalimbali, kila mara watahitaji kupata mafunzo ya maeneo mapya yanayojitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliusikiliza kwa makini sana mchango wa Mheshimiwa Jumanne Kishimba katika kongamano lile la sera mpya ya elimu na mitaala mipya ya elimu. Alipoeleza kwamba leo kuna uhitaji mkubwa sana wa mafundi wa simu, leo kuna uhitaji mkubwa sana wa mafundi wa pikipiki. Sasa ili kufanya mambo haya hatuwezi kuitegemea VETA ifanye hivyo. Mimi naona vyuo vya kufanya kazi hiyo vitakuwa ni Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi kwa sababu vyenyewe vinaweza kuwa na mafunzo ya muda mfupi lakini pia kuwa na mafunzo ya outreach program kuwafikia vijana na kuwafikia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuweke umuhimu sana katika vyuo hivi na sasa tuwekeze zaidi, na mimi niishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa shilingi 645,764,808 kukarabati Chuo cha Kilosa cha Maendeleo ya Wananchi pale Ilonga. Chuo kile sasa kina mandhari nzuri, kina kazi nzuri lakini kinapungukiwa na vifaa, kinapungukiwa pia na wakufunzi. Kwenye suala la wakufunzi ningependa katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi tuwe na aina mbili ya wakufunzi. Tuwe na wakufunzi wa kudumu ambao ni permanent lakini pia tuwe na wakufunzi wa kujitoela katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili nalitilia umuhimu sana kwa sababu nchi hii inahitaji aina hii ya vyuo ili kuwawezesha vijana wetu na wananchi wote kila wakati kunoa maendeleo yao na kuendelea kuwa muhimu katika jamii zao. Kwa hiyo, tuviongezee fedha vyuo hivi. Tuviongezee rasilimali vyuo hivi, tuviongezee wataalam vyuo hivi, lakini ningependa pia nimuombe Waziri wa Elimu, suala hili la FDC sasa pia liingie ndani ya sera ya elimu ambayo tunaifanyia mapitio na maboresho sasa ili iwe ni sehemu ya mfumo wa elimu katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo ningependa kulichangia ni elimu ya watu wazima. Mara baada ya kupata uhuru, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitangaza maadui watatu ambao ni ujinga, umaskini na maradhi. Kwenye ujinga tulikuja na suala la elimu ya watu wazima na tumefanya vizuri sana, mkazo wa elimu ya watu wazima wakati ule ilikuwa ni katika eneo la kusoma, kuandika na kuhesabu. Katika kusoma, kuandika na kuhesabu tumefanya jitihada kubwa sana lakini wakati umefika sasa na hili pia ningependa liingie katika sera ya elimu, tuje na mtazamo mpya kuhusu elimu ya watu wazima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya watu wazima siyo tu kwa wale ambao hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu. Elimu ya watu wazima inahitajika na watu wote hata wenye Phd kama mimi. Hata mimi pia nahitaji elimu ya watu wazima, maana yake tuwe na mtazamo mpya sasa wa elimu ya watu wazima ambayo itawagusa watu wote wa rika zote, wa elimu zote, wa mahitaji yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili kutokana na uzoefu. Katika miaka ya 1990 na miaka ya mwanzo ya 2000 ilionekana kuna umuhimu sasa wa kutunga Sheria za Mazingira na kuwafanya Majaji na Mahakimu wetu wazimudu sheria mpya za mazingira na wawe na elimu ya mazingira, mimi ni mmoja wa watu ambao Umoja wa Mataifa ulinichukua niwe mmoja wa wataalam waelekezi wa kuandaa mitaala ya kuwasaidia Majaji na Mahakimu kujua elimu ya watu wazima. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufanya jambo hilo niliona umuhimu wa kujifunza elimu ya watu wazima kwa ngazi zote. Kwa hiyo, nisisitize sana umuhimu wa elimu ya watu wazima katika nyanja zote na sera iliangalie hilo katika upana wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na mengine ya kuchangia katika suala la sayansi na teknolojia, tuwekeze katika maeneo mapya lakini hilo nitatoa mchango wangu kwa maandishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikujua kwamba muda ni mfupi lakini nashukuru sana. Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, Elimu ya Watu Wazima iingie katika sera ya sasa ya elimu ili tuweze kusonga mbele kama Taifa jipya linalojitambu na kujifahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Rahim kwa ruzuku ya uhai na afya. Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Nichukue fursa hii kuwapongeza kwa dhati kabisa Mheshimiwa Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi; Mheshimiwa Mhandisi Godfrey Kasekenya, Naibu Waziri Ujenzi; Mheshimiwa Atupele Mwakibete Naibu Waziri Uchukuzi; Balozi Mhandisi Aisha Amour, Katibu Mkuu Sekta ya Uchukuzi; Bwana Gabriel Migire, Katibu Mkuu Sekta ya Uchukuzi; Bwana Ludovick Nduhiye, Naibu Katibu Mkuu Ujenzi na Dkt. Ally Possi, Naibu Katibu Mkuu Uchukuzi. Nawapongeza kwa kazi nzuri wanayofanya katika Sekta hii muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu na kwa ustawi wa Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba yangu na ya wananchi wote wa Jimbo la Kilosa, namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa fedha nyingi za kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika Jimbo la Kilosa. Tunamshukuru sana kwa mabilioni ya fedha ambayo ameyaleta Kilosa kujenga barabara na madaraja kupitia TARURA na TANROADS. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa TARURA tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutupa shilingi bilioni nane na milioni 300 kwa ajili ya kujenga Daraja la Berega ambalo litaunganisha Wilaya ya Kilosa na Wilaya ya Kilindi ya Mkoa wa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kupitia TARURA kutupa shilingi milioni 500 kujenga Daraja la Masombawe kule Mamboya, lakini shilingi milioni 800 kujenga Barabara ya Mvumi – Ngege ambaye baadaye itatuunganisha na Wilaya ya Gairo, lakini Barabara ya Parakuyo shilingi bilioni 150 na pia kutoa shilingi milioni 800 kwa ajili ya ukarabati wa barabara na mifereji katika Mji wa Kilosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa TANROADS, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutupa shilingi 4,714,000,000 kwa ajili ya kumalizia Madaraja ya Kobe, Kwa Ilonga na Mazinyungu na madaraja haya yatakapokamilika sasa Barabara ya Dumila – Ludewa – Kilosa itakuwa imekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefarijika sana kuona katika ukurasa wa 287 wa bajeti ya sasa kwamba Wizara imetenga fedha kwa ajili ya feasibility study na detailed design ya Daraja la Mto Mkondoa. Daraja hili ambalo liliondolewa na mafuriko ni daraja muhimu sana na hasa ukizingatia kwamba kwamba sasa tutaanza kujenga Barabara ya Kilosa – Ulaya – Mikumi na daraja hili ni muhimu na kwa muda wote huu tulikuwa tunatumia daraja la reli kuvuka Mto Mkondoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi yangu kwa Serikali kwamba feasibility study hii na detailed design isihushishe Daraja tu la Mto Mkondoa, lakini lihusishe Kingo yote ya Mto wa Mkondoa kuanzia Mkadage kwenye Daraja la SGR mpaka Magomeni ili kuimarisha kingo za Mto Mkondoa unaohamahama lakini pia kuzuia mafuriko kwa ajili ya Mji wa Kilosa. Ifahamike Wajerumani walipojenga reli ya kati walijenga mabwawa matano ya punguza ikiwa ni pia pamoja na Bwawa la Kidete. Naomba pia bwawa hili Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Wizara ya Kilimo washirikiane ili Bwawa hili likikamilika litakuwa kinga nzuri kabisa ya mafuriko kwa Mji wa Kilosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kuomba ujenzi wa Reli ya Kilosa – Kidatu kama ilivyoainishwa katika bajeti ufanyike. Reli hii ni muhimu sana kuunganisha Kilosa, Mikumi na Kidatu. Itaunganisha reli ya kati na reli ya SGR kutoka Kilosa kwenda mpaka Mlimba ambako itaunganisha na reli ya TAZARA. Maombi yangu huko mbele ya safari ikiwezekana reli yote hiyo ya Kilosa – Mikumi mpaka Mlimba ama iwe ya cape gauge au iwe ya SGR ili kurahisisha usafiri wa mizigo kati ya Reli ya TAZARA na Reli ya NGR na Reli ya SGR. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii sasa kuzungumzia maombi mengine ambayo nayaomba na hii ni ya ujenzi wa lami wa Barabara ya Chanzuru kupitia Kimamba kupitia Parakuyo kupitia Mkata station kwenda Melela. Barabara hii itakamilisha mzunguko wa Barabara ya Melela kuja Kilosa, Kilosa kwenda Mikumi na hivyo kuongeza ufanisi wa usafiri katika eneo hilo na kuufanya Mji wa Kilosa sasa kuwa ni Mji wa Kimkakati katika usafarishaji na uchukuzi nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kikao cha G7 kilichofanyika Hiroshima Japan, Serikali ya Marekani imetangaza kupitia Parternship for Global Infrastructure and Investment, kwamba itatoa fedha sasa kufufua Reli ya Benguela the Lobito Corridor maana yake kutoka Ndola kwenda Lubumbashi kwenda mpaka Lobito. Huu ndio wakati sasa na wao wamesema wanaweza pia kuiunganisha Tanzania. Sasa tunapata fursa ambayo ni vizuri tukaitumia vizuri ya kuunganisha Bahari ya Hindi na Bahari ya Atlantic na ukiiangalia Afrika ni nchi mbili ambazo zinaunganisha bahari hizi mbili yaani DRC na Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa reli hii itakapoanza maana yake tunaweza tukaitumia fursa hiyo vizuri kutoa mizigo Dar es Salaam mpaka Lobito ikaenda Marekani na Nchi za Carribean na kutoa mizigo kutoka Nchi za Carribean zikaingia Lobito zikaja Dar es Salaam kwenda Nchi za Asia na Nchi za Mashariki ya Mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake nini? Ni lazima sasa tuimarishe Reli ya TAZARA ili iwe na ufanisi mkubwa sana bila kufanya hivyo ina maana mizigo mingi ya DRC na mizigo mingi ya Zambia sasa itakwenda Bandari ya Lobito badala ya kuja katika Bandari zetu za Tanzania. Kwa hiyo, tuna umuhimu wa kuongeza ufanisi wa bandari zetu, tuna umuhimu wa kuongeza ufanisi wa Reli ya TAZARA ili badala ya kupoteza mizigo, sasa tuweze kuunganisha Bahari ya Antlantic na Bahari ya Hindi kupitia bandari zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bandari hizi tusiimarishe Dar es Salaam tu. Tuimarishe Tanga, Mtwara na tuanze kujipanga kujenga bandari nyingine zaidi na katika bandari hizi ambazo tuzifikirie kuzijenga iko bandari moja tusiiache kuifikiria ni Bandari ya Kilwa. Tumeamua sasa Kilwa iwe Bandari ya Uvuvi, lakini tuangalie uwezekano wa baadaye Kilwa kuwa bandari ya mizigo mingi. Bandari ya Kilwa ina historia ndefu toka wakati wa Ibni Batuta na ndio bandari pekee katika upande huu wa magharibi wa Bahari ya Hindi yenye kina kirefu cha asili na ina milango miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo miaka ijayo Insha Allah Bandari ya Kilwa ndio inaweza kuwa Bandari ya trust shipment ya meli kubwa kuingia kushusha mizigo na baadaye kwenda bandari ndogo. Sisi tuna bahati kubwa sana, tuna uwezo pia wa kuifanya Pangani kuwa bandari. Kwa hiyo, katika master plan ya bandari pamoja na hizo zilizotajwa ya Tanga, Bagamoyo, Dar es Salaam na Mtwara lakini tuanze kufikiria pia kuimarisha Bandari ya Kilwa ili isiwe ya uvuvi tu. Bandari ya Kilwa ndio bandari ambayo miaka ijayo itakuwa bandari kubwa kuliko zote katika Afrika ya Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuifanyie bandari hiyo sasa maandalizi makubwa ili Kilwa ichukue nafasi yake na tuanze kufikiria kutoa Reli ya SGR kutoka Kilwa kuja kuunga ama Pugu au maeneo ya Pwani, ili baadaye mizigo ikitoka Kilwa iweze kwenda moja kwa moja katika Reli ya SGR na kwenda moja kwa moja mpaka sehemu nyingine. Kwa hiyo, tunaweza kuona utajiri mkubwa ambao Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala ameijalia Tanzania katika haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia, ni sasa Tanzania lazima tuanze kujiweka sawa kuanza kutumia magari na mabasi ya umeme. Dunia inahama kutoka kwenye magari ya mafuta, dunia inahama kutoka kwenye magari ya gesi, dunia sasa inakwenda kwenye magari ya umeme. Tuanze kufikiria mwendokasi Dar es Salaam badala ya kutumia gesi na petrol itumie umeme. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Profesa.

MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyezi Mungu ametujalia vyote, naona muda wangu umekwisha, naunga mkono hoja asilimia 100 kwa Wizara hii, lakini Mheshimiwa Mbarawa asiisahau Kilosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu rahimu kwa ruzuku ya uhai na afya, pia nikushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa dhati kabisa kumpongeza Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa Waziri, CPA Mary Masanja Naibu Waziri, Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbas na Naibu Katibu Mkuu Anderson Mutatembwa na Watumishi wote katika Wizara hii kwa kazi nzuri mnayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuanza na suala ambalo linatupa usumbufu mkubwa sana katika Jimbo la Kilosa nalo ni tembo kuharibu mazao na miji ya watu na kwa muda mrefu wananchi wetu hawajapewa kifuta machozi kwa uharibifu huo wa tembo na maeneo ambayo yameathirika sana ambayo ningeomba Wizara itusaidie kuwalipa kifuta machozi kwa haraka ni Kata ya Kimamba A katika maeneo ya Soko Msuya, Mkwajuni na Sikutari, Kimamba B, maeneo ya Uhindini, Kigamboni, Pusa na Mji Mwema, Kata ya Ludewa eneo la Peapea na Kata ya Madoto eneo la Mbwade na Kata ya Parakwio eneo la Mkata Stesheni na Mkata. Tutashukuru sana kupata kifuta jasho kwa wananchi lakini pia tupewe kituo cha kupambana na tembo hao kwa sababu tembo kutoka Hifadhi ya Mikumi wanakuja sana katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kuchangia ni kuhusu Dodoma. Dodoma sasa ni Makao Makuu ya Nchi yetu, Dodoma sasa ni Jiji na ningependa kabisa kutoa ushauri kwa Wizara ya Maliasili na Utalii. Makao Makuu ya Nchi yanastahili kuwa na hifadhi kubwa. Kwa hiyo ninashauri Dodoma ipewe hifadhi, ianzishwe hifadhi kubwa inayoendana na heshima ya Mkoa huu lakini heshima ya Jiji hili. Pamoja na hayo tufikirie kuanzisha eneo kubwa la msitu (park) ambayo Miji mingine mikubwa wanayo, Berlin wana park kubwa sana ya Tiergarten. Sasa imefika mahali Dodoma pia tuwe na park kubwa sana ili Mji huu na eneo hili lilingane na hali na hadhi ya Mji. Tunaomba hifadhi kubwa ianzishwe katika Mji wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuchangia eneo jingine na hili ni kuhusu utalii.

MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa taarifa.

MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nilikuwa nampa taarifa Mheshimiwa Mbunge anayechangia kwamba Kondoa tayari tuna hifadhi mbili. Tuna Hifadhi ya Mkungunero ambayo ina wanyama wote na tunayo Hifadhi ya Swagaswaga nayo pia ina wanyama wote na pia pale Kondoa tuna eneo ambalo tumelitenga ni kubwa kwa ajili ya hichi anachokiongelea Mheshimiwa Mbunge Wizara inaweza ikachukua ikatengeneza hiyo park kubwa na Dodoma ikawa ina eneo kubwa ambalo litakuwa ni kivutio kwa Waheshimiwa Wabunge na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Profesa Palamagamba unaipokea hiyo taarifa?

MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo lakini naiboresha huko ni Mkoa wa Dodoma lakini Dodoma ni kubwa ni pamoja na Jiji la Dodoma. Kwa hiyo, naipokea hiyo taarifa lakini naongezea Jiji la Dodoma na lilikuwa maarufu sana kwa tembo na ndiyo maana inaitwa Dodoma, Idodomia maana yake hapa tembo walikuwa wanazama na njia yao ndiyo leo University hii ya UDOM ndiyo maana mara nyingi hurudi kuja kusalimia maeneo waliyoishi miaka na miaka ya nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ambalo ningependa kulichangia ni kwenye utalii na hapa nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa Royal Tour na tunasubiri kwa hamu sana hii film nyingine ya The Hidden Tanzania na ninaamini katika film ya The Hidden Tanzania hifadhi ya Kitulo itakuwemo. Ni hifadhi ya aina yake kabisa duniani na inastahili kutangazwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo jingine katika utalii ni upekee wa Tanzania katika utalii duniani na eneo la upekee wa Tanzania katika utalii duniani ni eneo la utalii wa vivutio vitokanavyo na hali ya jiolojia ya nchi (geo - tourism). Huu ni wakati sasa wa kusukuma geo – tourism, geo – conservation na kuanzisha geo – park nyingi iwezekanavyo. Hapa nataka nitoe maeneo 11 ambayo tukiyafanyia kazi hiyo, mengine tayari yametambuliwa na kuhifadhiwa, mengine bado. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni Kilimanjaro. Sasa tuutangaze Mlima Kilimanjaro kuwa ndiyo mlima mrefu kuliko yote duniani wa aina ya volcano. Ndiyo mlima mrefu kuliko yote duniani wa aina ya volcano na Mlima Kilimanjaro hauna vilele viwili, una vilele vitatu kijiolojia navyo ni Shira ambayo ni extinct, Mawenzi ambayo ni extinct na Kibo ambayo ni dormant. Taarifa hizo zimo kwenye kitabu kinaitwa, “Kilimanjaro Mountain Memory and Modernity” kimechapwa na Mkuki na Nyota mwaka 2006, kina kurasa 321. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili muhimu sana ni Mautia Hill – Kongwa. Hiki ni kilima pekee duniani chenye madini ya aina ya Yoderite na jambo la kusikitisha, nakuomba Mheshimiwa Waziri chukua hatua za haraka hata ikiwezekana leo kwenda kukinusuru kilima hiki. Saa hizi ukipita pale karibu na Kongwa Ranch utaona wanachimba limestone. Kilima hiki kikipotea tumepoteza kilima pekee duniani chenye madini ya aina ya Yoderite. Kitangazwe kuwa ni kimehifadhiwa kiwe geo–park na wewe Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya Madini tukinusuru kilima hiki. Wanakuja watalii na wanasayansi toka Marekani, Ujerumani, Austria kwenda pale Mautia Hill – Kongwa na sasa ukona pana mchirizi kuna mtu anachimba limestone. Tukinusuru kilima hiki ambacho ni utajiri duniani wa pekee. Hakuna mahali pengine duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ni Ngorongoro. Tulitangaze sasa Bonde la Ngorongoro kuwa ndiyo bonde kubwa duniani la aina ya volcano (the largest caldera in the world, the largest caldera in the world). Sehemu ya nne ni Empakai. Hili ni moja ya bonde la volcano lenye kina kirefu duniani (one of the deepest calderas in the world). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya tano ni Yalumba kule Ludi -Kibakwe na Ikora kule Katavi. Hapo una miamba ya zamani kuliko yote duniani ya mfumo wa aina ya eclogites hupati sehemu nyingine duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la sita ni Oldonyo Lengai. Huu ni mlima pekee duniani wenye volcano ya aina ya cobaltite na saba ni Kimondo cha Mbozi (iron meteorites) na nane ni Mwadui. Mwadui ni moja ya Kimberlite kubwa duniani inayozalisha almasi kwa faida. Tisa ni Igwiti – Tabora, hiki ndiyo kilima chenye volcano ya aina ya kimberlite kule Igwiti – Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumi ni Tendaguru. Tendaguru ambayo najua iko kwenye Jimbo la Mchinga la Mama Salma Rashid Kikwete. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tendaguru ndiyo kwenye masalia ya viumbe wakubwa duniani hawa dinosaurs, ambao walichimbuliwa na sasa wako katika Jumba la Makumbusho Berlin. Kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi tumezungumzia kujenga kituo kule. Kituo hicho kijengwe kiboreshwe na wenzetu Wajerumani sasa nyaraka na taarifa zote zipo na wametoa kitabu katika mambo yote ya Tendaguru kinaitwa, “Dinozauria Fragmente Zur Geschichte dea Tendaguru Efbideschion Undiire Objecte Nohis Hundadet Enzeks Bisdoiz Zauthousand Axzen” yaani kwa Kiswahili ni “Vipande vya Dinosauria, historia na masalia ya msafara wa kipaleontolojia kwenda Tendaguru Tanzania mwaka 1906 – 2018” na Mheshimiwa Waziri miaka yote tisa niliyokaa Berlin kila walipokuja wageni niliwapeleka kwenye museum Naturkunde ambayo iko kwenye Chuo Kikuu cha Humboldt Universitat zu Berlin ambako kwa bahati Mke wangu Dkt. Amina alifanya PhD yake pale, na ninazo picha ambazo nitazileta za watu wote walioshiriki kuchimba ile masalia. Tutengeneze Tendaguru iwe ni moja ya vivutio vikubwa vya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, 11 ni Olduvai Gorge. Hii ndiyo bonde la kwanza duniani kukaliwa ni viumbe vya kwanza vyenye umbile la binadamu. Ndiyo chimbuko la kwanza la binadamu, ndiyo the first home of Zinjathropus Australopithecus Boisei. Hapa tufikirie upya zile nyayo. Wataalamu wa sayansi watusaidie ziendelee kufukiwa au sasa zifukuliwe ili watu wazione na katika kundi hili sehemu ya 12 ni Mapango ya Amboni. Haya ni mapango yanayotokana na limestone na yalitokea miaka milioni 150 iliyopita na katika kipindi cha Jurassic na kwa miaka milioni 20 yalifunikwa na maji. Najua yako mapango 10 ni moja tu ambalo linatumika. Tuone hayo tisa kama tunaweza tukaongeza mengine ili eneo nalo hilo liwe hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba sana Mheshimiwa Mchengerwa na Wizara tuyahifadhi maeneo haya, tuyatambue maeneo haya, tuyatangaze maeneo haya na tuwe ndiyo watu wa kuonyesha dunia tunavyo vitu vya pekee ambavyo sehemu nyingine duniani havipo isipokuwa Tanzania tu na hii ni hali ya jiolojia ya nchi yetu ambayo Mwenyezi Mungu ametusaidia kuiumba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo ningependa kushukuru ni kwenye upande wa malikale na kumbukumbu za Taifa. Nashukuru sana Mheshimiwa Waziri katika hotuba yako ukurasa wa 93 umetangaza kwamba Pango la Magubike katika Jimbo la Kilosa ni moja ya maeneo sita ya malikale ambayo mmebaini yanakidhi vigezo vya kuwa Urithi wa Taifa. Nawakaribisha sana mje tufanye, tutunze hilo pango la Magubike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nakushukuru sana kuwa njia ya kati ya biashara ya utumwa na vipusa kutoka Ujiji hadi Bagamoyo pia vijiji viwili vya Jimbo la Kilosa vimo, Mamboya alikozaliwa Babu yangu na Rubeho. Nawakaribisha sana kufika katika maeneo hayo ili tuhifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Kilimatinde ambako anatoka Baba yangu na hapa Kilimatinde Mheshimiwa Naibu Waziri ameshafika. Ile nyumba waliyokaa Askari wa Kijerumani iliyokuwa officers mess leo ndiyo nyumba ya Kasisi pale inaanza kubomoka. Lile boma la mawe linaanza kubomoka. Yale makaburi matatu ya Maafisa wa Kijerumani waliofia Kilimatinde yameanza kuharibiwa. Yale makaburi saba ya Wajerumani Askari yameanza kuharibiwa. Naomba na kile kisima ambacho watumwa walikunywa maji kabla ya kushuka kwenye bonde la ufa pale Kilimatinde na ninaamini ndiyo iliyozaa Kilimatinde ya Pemba na ndiyo iliyozaa Kilimatinde ya Oman na ndiyo iliyozaa Kilimatinde Liverpool, ningeomba maeneo hayo pia yahifadhiwe ili yawe urithi wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Kilosa naomba Stesheni ya zamani ya Kondoa, jengo ambalo halitumiki kati ya Kimamba na Kilosa lije litengenezwe ili ibaki kuwa ni kumbukumbu ya aina ya stesheni ambazo Wajerumani walizijenga lakini ile stesheni ina umuhimu mkubwa sana. Hiyo ndiyo ilikuwa njia ya watumwa na inaelekea watumwa hao kutoka Kondoa walipitia njia ya kutoka Kondoa kuja Mamboya wakashuka kuja mpaka pale, na tufahamu kwamba sehemu kubwa ya reli ya kati kutoka Morogoro mpaka Dodoma zamani ndiyo ilikuwa njia ya utumwa na njia ya biashara ya vipusa. Kwa hiyo nitashukuru sana lile jengo mkishirikiana na Shirika la Reli Tanzania kulitengeneza kulihifadhi kati ya Kimamba na Kilosa limepandwa miti linahitaji utaalamu ili nalo liwe sehemu ya vivutio vya utalii katika Kilosa ambayo sasa tuna tunnel zile tano za SGR lakini pia tunaomba kufungua sasa geti jipya kutoka Mji wa Kilosa kuingia katika Mbuga ya Mikumi ili watalii wakifika Kilosa na SGR waweze kwenda Mikumi na ninaamini kabisa katika hilo mtatusaidia kufungua haraka sana geti la Kilosa Mjini ili watalii hawa waweze kuingilia Mikumi lakini pia waweze kuingilia Kilosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa hayo yote nakushukuru sana kwa kuchangia na ninaunga mkono hoja asilimia 100 na ninaomba fidia ya kifuta jasho kwa ajili ya tembo kule Kilosa. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Rahim, kwa ruzuku ya uhai na afya ambayo imeniwezesha kuja kutoa mchango wangu. Aidha, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kutoa mchango na mimi nianze kwanza kwa kumshukuru kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake madhubuti lakini kwa kasi kubwa ya maendeleo ambayo tunayaona katika nchi yetu, ikiwa ni pamoja na kuendeleza miradi ya kielelezo na miradi mikubwa lakini pia ustawi wa wananchi unazidi kukua katika nyanja zote chini ya uongozi wake mahiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumpongeza kwa dhati kabisa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Fedha, pamoja na Naibu Waziri, Mheshimiwa Hamad Hassan Chande, Katibu Mkuu Dkt. Dr. Natu El-Maamry Mwamba na Naibu Makatibu Wakuu kwa bajeti hii mwanana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba katika bajeti hii Jimbo la Kilosa katika miradi mikubwa tumewekwa, ikiwa ni pamoja na kujenga barabara ya kutoka Kilosa kwenda Mikumi pia kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa daraja kubwa la Mto Mkondoa. Ni imani yangu kwamba fedha hii itapatikana katika mwaka huu wa fedha na ni miradi hiyo kuanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia kuhusu umuhimu wa sekta ya nyuki na hasa katika mazao yake ikwemo asali katika kukuza uchumi wa nchi yetu na kuipatia nchi yetu fedha za kigeni. Tanzania ni nchi ya pili kwa kuzalisha asali nyingi katika Bara la Afrika, nchi ya kwanza ni Ethiopia, Tanzania ni ya pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ndiye supplier mkubwa wa asali na mazao ya asali kama vile Nta kwenye soko la Umoja wa Ulaya kutoka Afrika (European union). Inakadiriwa kuwa Tanzania inauza nje wastani wa tani 770 za asali na tani 283 za Nta kwa mwaka. Aidha, inakadiriwa kuwa sekta ya ufugaji nyuki na mauzo yake yanaleta wastani wa dola za Kimarekani 5,182,126 kwa mwaka katika miaka minane iliyopita kila mwaka hizo fedha ziliingia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii inaajiri na kuhusisha takribani watu milioni mbili waishio vijijini katika maeneo mbalimbali hususani Tabora, Singida, Katavi, Morogoro kule Kilosa. Mfano kule Singida kuna Kijiji cha Nyuki na Jiji la Nyuki. Pia Kilosa Kata za Maguha na meneo Unone katika Kata ya Ludewa wote wanafanya shughuli hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii ina uwezo mkubwa wa kukua na kuongeza mapato ya nchi kwa kuuza asali na nta na mazao mengine nje ya nchi. Tunaweza tukauza vumbi yaani pollen, tunaweza tunaweza tukauza royal jelly yaani maziwa ya nyuki. Hata hivyo, sekta hii inakabiliwa na changamoto nyingi hasa inapokuja katika kuuza asali na nta nje ya nchi. Kikwazo kikubwa au changamoto kubwa ni urasimu mkubwa na fomu nyingi na nyaraka nyingi ambazo wale wanaouza asali nje ya nchi wanatakiwa kuzijaza na kila unapojaza iwe ni nyaraka au ni fomu lazima wanatozwa, wanalipa tozo. Kwa hiyo, eneo hili pia lina tozo nyingi takribani 30 katika hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba wanaweza kuuza asali nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Tanzania wanajaza fomu 31 ukilinganisha na nyaraka sita Rwanda, matokeo yake asali yetu nyingi msimu huu wa kurina asali ukifika maeneo kama Itigi, utakuta malori mengi yanakusanya asali inakwenda Kenya na ikifika Kenya itauzwa nje kwa jina la Kenya, moja ya sababu kubwa ni urasimu huu na tozo nyingi ambazo zimewekwa katika sekta hii hasa kwa wale ambao wanataka kuuza asali yao nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mtu anayetaka kusafirisha asali nje anatakiwa aende kwenye taasisi nyingi na akienda kwenye taasisi hizo mifumo yao haisomani. Kwa hiyo, anajikuta taarifa ambazo ametoa kwenye Taasisi moja inabidi taarifa hizohizo azirudie kwenye Taasisi nyingine. Anatakiwa aende kwa Wakala wa Misitu (TFS), anatakiwa aende TCCIA apate Certificate of Origin, anatakiwa aende Veterinary ili ahakikishiwe kwamba nyuki waliotoa hiyo asali walikuwa ni salama, anatakiwa aende Tanzania Atomic Energy Commission, anatakiwa aende TASAC anatakiwa aende TRA, anatakiwa aende TBS, anatakiwa aende TPA na hao wote mifumo yao haisomani na matokeo yake tunapoteza ufanisi wa kupeleka asali nyingi nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyohuyo anayepeleka asali nje anajikuta anatakiwa kupata aina hiyohiyo ya cheti au ruhusu au payment kutoka sehemu mbili tofauti lakini juu ya jambo hilohilo. Kwa mfano, anatakiwa aende veterinary ili apewe sanitary certificate ya kutoa ushahidi kwamba nyuki aliyetoa asali hiyo alikuwa salama, halafu anatakiwa aende Wakala wa Misitu ili apate sanitary certificate ya kuonesha kwamba asali hiyo ni salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapendekeza fomu hizi zipitiwe upya tukilinganisha na za wenzetu nchi ya Rwanda, Kenya na Uganda ili tuwe na ufanisi na tija zaidi katika kupeleka mazao haya ya asali. Mimi nina uhakikia kabisa tukiboresha mifumo yetu, tukitoa hamasa kwa watu mbalimbali na sekta binafsi kununua, kuchakata na kuuza asali nje, tunao uwezo kwa mwaka kuingiza dola milioni 20 kutokana na asali na mazao ya asali kama nta na royal jelly. Wote tunafahamu kabisa royal jelly ina bei kubwa sana na faida kubwa tuliyonayo sisi maeneo yetu ambayo tunafuga nyuki maeneo haya mengi hayana mazao yanayotumia viuatilifu au mbolea, maana yake asali hii ni organic na ina uwezo wa kuwa na bei kubwa katika masoko ya Ulaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mapendekezo yangu Mheshimiwa Waziri tupitie tena zile fomu kutoka 30 tuzipunguze ikiwezekana zifike tisa kama ilivyo kwa Rwanda. Pia tupunguze tozo katika sekta hii, nashauri pia tutoe fedha ya kutosha ya kuwahamasisha wafugaji wa nyuki katika maeneo mbalimbali, Tabora, Singida yote Itigi na Manyoni lakini Kilosa na maeneo mengine yoyote yale ili wananchi wetu waweze kuwa na mizinga ya kisasa ya kufuga nyuki lakini yenye ubora na tukusanye asali hiyo na tuichakate na kuuza nchi za nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili naomba kupongeza Serikali kwa hatua ya kuondoa ushuru wa bidhaa unaotozwa kwa magari yanayotumia nishati ya umeme ambayo yamo katika hotuba ya bajeti ukurasa wa 107 na 108. Kwa mujibu wa ripoti ya Africa E-Mobility Alliance inaonyesha kuwa Tanzania kuna electric vehicles, yaani kwa maana ya magari, pikipiki, bajaji skuta 5000 na sisi ndiyo tunaoongoza katika eneo hili la Afrika Mashariki kwa kuwa na hizi electric vehicles nyingi, pia tunazo kampuni karibuni kumi ambazo zinaagiza aina hii ya magari. Kwa hiyo, kuondoa ushuru wa bidhaa katika eneo hili utaongeza kuingizwa nchini kwa magari mengi, pikipiki nyingi na skuta nyingi ambazo zinatumia umeme badala ya mafuta na hivyo kutunza mazingira lakini pia kupunguza matumizi ya fedha za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili Tanzania tumefika mbali na mambo haya wakati mwingine hatuyasemi, sisi ndiyo nchi pekee katika Afrika Mashariki ambayo tunayo kampuni ambayo sasa inabadili magari haya ya mafuta kuwa magari yanayotumia umeme. Kampuni hiyo ni Kampuni ya Hanspaul ipo pale Arusha na wao wanashirikiana na kampuni ya Ufaransa na Kampuni ya Gardy Electronics, hawa sasa wanabadili magari yanayotumia mafuta kwenda kuwa katika mfumo wa umeme na wamejenga vituo vya kuongeza umeme vinavyotumia solar katika sehemu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo langu ni kuwa jitihada hii ipewe musukumo ili tuweze kuanza kutengeneza magari ya umeme sisi wenyewe ndani ya nchi yetu. Tumejaliwa kuwa na madini yote ya kimkakati ambayo yanahitajika katika magari ya umeme Nickel, Cobalt, Lithium pamoja na Graphite, kwa hiyo, hatua hii ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza pia Chuo cha Ufundi cha Arusha kipewe fedha zaidi, kwa sababu ndiyo chuo ambacho kimeanza kufundisha mafundi wa kuhudumia magari haya ya umeme, kuyatenegeneza magari haya ya umeme na wakitoka katika kuhudumia magari haya ya umeme na kuyatengeneza magari haya ya umeme waende sasa kwenye kuunda magari ya umeme, pikipiki za umeme, skuta za umeme na vitu vinavyotumia umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya kwa sababu mara nyingi Watanzania tunafanya vitu vikubwa sana lakini ni wazito wa kuvitangaza, ni wazito wa kuvieleza. Kwa hiyo, niwapongeze sana Hanspaul Group, na wengine, pia Chuo cha Ufundi Arusha kuingia katika sekta hii ya magari ya umeme. Dunia ya sasa inahama kutoka kwenye magari ya mafuta kwenda kwenye magari ya umeme na magari yanayotumia Gesi asilia. Tanzania tuwe ndiyo nchi inayofanya mambo yote hayo kwa kasi kubwa sana. Nchi za jirani zinakuja kubadili magari yao ya mafuta kuwa magari ya umeme kwa ajili ya utalii na duniani zinatangazwa kwamba magari yale yametengenezwa katika nchi zao kumbe magari hayo yote yamekuja Arusha yamebadilishwa na kuwa magari ya umeme lakini dunia inafahamu kwamba magari hayo yametoka kwenye nchi hizo. Kwa hiyo, ninapendekeza tuseme kwa sauti kubwa kwamba shughuli hii inafanywa Tanzania pia tuwape hawa wanaofanya kazi hii motisha mbalimbali ikiwa ni pamoja na hii hatua ya kufuta au kuondoa huu ushuru wa bidhaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo ningependa kulizungumzia ambalo pia tuwekeze katika hilo, tuwekeze katika haki miliki ya umahususi wa kijiografia yaani geographical indications. Maeneo hayo tuyatumie kuuza bidhaa ambazo zinatoka katika maeneo hayo. Moja ya mazao ambayo tunaweza tukayatangaza kwa bidii kubwa sana ni Kakao. Kakao ya Kyela ina ubora mkubwa sana duniani na inatumika kuchanganya na kakao hafifu kutoka nchi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuja na kakao hii, kakao hii inauzwa Ufaransa, ili kuonesha kwamba Kakao hii ya Tanzania ina thamani kubwa ndiyo maana wanaonyesha kwamba asilimia 75 ya kakao katika chocolate hii imetoka Tanzania, imetoka Tanzania kwa sababu ina ubora mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiishie tu katika hayo pia tuanze kutangaza kutumia umahususi wa kijiografia wa mazao mengine ya kilimo ili yapate bei ya juu. Kwa mfano, Kahawa ya Mbinga ndiyo kahawa inayolimwa bila kutumia mbolea ni organic. Kahawa ya Manyovu na hivi vyote vitatusaidia siyo tu kupata fedha ya kigeni lakini kuitangaza nchi yetu kwamba ina bidhaa za ubora wa hali juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchele wa Kyela, mchele wa Kilombero na sasa kuhusu Mvinyo wa Dodoma. Mvinyo wa Dodoma una ubora mkubwa sana duniani, ndiyo maana mvinyo wa Dodoma unachukuliwa na nchi nyingine kwenda kuongeza ubora wa mivinyo yao ambayo ni hafifu. Kwa hiyo, ni wakati sasa wa nchi yetu kuwekeza pia katika maeneo hayo ambayo yanaonekana siyo muhimu lakini duniani ni muhimu sana, hatimiliki ya mazao yote yenye umahsusi wa kijiografia yaani geographical indicators. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja katika bajeti hii mwanana na bora sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Rahim kwa kuturuzuku uhai na kutujalia afya ya kukutana leo hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua nafasi hii kukushukuru kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Nshirikiano wa Afrika Mashariki. Nichukue hatua hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa Diplomat Number One kwa kuimarisha sauti ya Tanzania katika medani ya uhusiano wa Kikanda na Kimataifa pia kwa msukumo mkubwa aliouweka katika diplomasia ya uchumi na matunda ya juhudi hizo yako dhahiri kwetu sote. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza diplomat number two Mheshimiwa Dkt. Stergomena Lawrence Tax, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwa umahiri alioudhihirisha katika kuendeleza na kuimarisha diplomasia ya Tanzania, leo kwa hotuba yake ya kwanza katika Bunge hili aliyoitoa kwa ustadi na umahiri mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja naye nawapongeza Naibu Waziri Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Katibu Mkuu Balozi Dkt. Samwel William Shelukindo, Naibu Katibu Mkuu Balozi Tatma Mohammed Rajab na watumishi wote wa Wizara kwa kazi nzuri mnayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo mawili ambayo na mimi ningependa niongeze sauti yangu na Wizara imeyafanya vizuri sana. Moja ni eneo la diaspora na la pili ni eneo kuhusu diplomasia ya utamaduni (cultural diplomacy) ikiwa ni sehemu na nguzo muhimu ya diplomasia ya uchumi (economic diplomacy). Hapa nikiazima maneno ya Prof. Ali Mazrui, diplomasia ya utamaduni itatupa soft power ambayo yeye aliita Parks Tanzaniana akituweka katika kundi moja na Parks Americana na Parks Britannica.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki kwa kuanzisha hii digital hub ya kuwaandikisha diaspora. Hatua hiyo ni hatua muhimu sana ya kuwasajili diaspora wote wa Tanzania walioko nje ili tuweze kujua wako wapi, wanafanya nini na kujua mchango wanaoweza kuutoa katika maendeleo ya uchumi na kijamii ya nchi yetu, hiyo itaiwezesha Serikali kuwa na mkakati wa kushirikisha diaspora ya Tanzania katika maendelo ya uchumi na jamii ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalisema hili mimi mwenyewe nikiwa na uzoefu kwa kuwa nimeishi Ujerumani kwa miaka tisa, siku sita na siku tatu. Kwa hiyo hii hatua ni muhimu na ninaipongeza sana na niwashukuru washiriki wote ambao wamewezesha Wizara kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naipongeza Wizara kwa kuwa katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuwapatia hadhi maalumu watu wenye asili na nasaba ya Tanzania ambao wameacha kuwa raia wa Tanzania baada ya kuchukua uraia wa nchi nyingine. Hiyo itakuwa ni hatua muhimu ya kuondoa usumbufu na changamoto za watu hawa wanazozipata hasa wanaporejea nyumbani kuja kuona ndugu zao au kufanya shughuli nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la hadhi maalumu ndilo lenye muafaka hapa Tanzania, nami nasema ni bora kama wanavyosema waswahili ni bora kenda mkononi kuliko kumi porini. Sasa tuna kenda mkononi ambayo ni hadhi maalumu. Mimi ningeomba Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje pia Wizara ya Mambo ya Ndani ikamilishe jambo hili ili hawa wenzetu waweze kupata hadhi maalumu waondokane na usumbufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni bora kuliko lile ambalo tunaendelea kulisema na tunajua bado halina muafaka, suala la uraia pacha bado halina muafaka hapa nchini lakini halina muafaka duniani, kwa hiyo tushikilie hili ambalo tuna muafaka nalo tulisukume kwa haraka ili liende. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti nilioufanya huko duniani ni asilimia 49 tu ya nchi duniani zinaruhusu uraia pacha na asilimia 51 duniani hazirihuisu uraia pacha. Utaona asilimia 51 bado haziruhusu uraia pacha, maana yake jambo hili hata katika ngazi ya dunia bado halijapata muafaka. Hii ni pamoja na nchi ambazo tuna uhusiano nao wa karibu ambapo wako Watanzania wenye asili ya nasaba ya Tanzania bara, asili ya nasaba ya Tanzania Zanzibar ambao wako Oman. Oman hairuhusu uraia pacha, Saudi Arabia hairuhusu uraia pacha, lakini pia ziko nchi ambazo zina diaspora wengi sana duniani ambazo pia haziruhusu uraia pacha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri ni India, ina diaspora wengi sana nje lakini katika Katiba yake imekataza kabisa uraia pacha lakini imekuja na hadhi maalumu kuwatambua watu wanaowaita Persons of India Origin au Overseas Indians ambao wanapewa kitambulisho na wanakuwa na haki zote. Nchi nyingine ya kiafrika ambayo ina diaspora wengi sana duniani Ethiopia, ina diaspora karibuni milioni tatu Marekani na Ulaya na yenyewe pia haikubali uraia pacha, lakini inatoa kitambulisho maalumu kwa waethiopia waliokuwa nje, ambao wakirudi nchini kwao Ethiopia wanakuwa na haki zote ambazo wanazihitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika nchi za Umoja wa Ulaya. (Europian Union). Nchi 15 zinakubali uraia pacha, nchi 12 hazikubali uraia pacha na ambazo hazikubali uraia pacha ni pamoja na Ujerumani, Uholanzi, Austria na Denmark. Kwa upande wa Ujerumani, wao hata mtoto aliyezaliwa Ujerumani na watu ambao siyo raia wa Ujerumani hapewi hadhi yoyote, ndiyo maana baadhi ya sisi ambao watoto wetu wamezaliwa Ujerumani tuliporudi hapa walivyofikisha miaka 18 tulipoambiwa twende Ubalozini kuomba wakane uraia wa Ujerumani, Wajerumani walishangaa kwa sababu toka walipozaliwa wao hawakuwa raia wa nchi hiyo, kwa sababu kwa Wajerumani uraia ni damu. Aina yao ya uraia ni Jus Sanguinis ni uraia wa damu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hapa Tanzania suala la uraia pacha lina hisia kali, it is an emotive issue. Katika utafiti nilioufanya nimeona kwamba Bunge Oktoba Mwaka 1960 wakati tuna Serikali ya Madaraka, uliletwa Muswada Bungeni kuhusu uraia wa Tanganyika na aliyekuwa Waziri Kiongozi wa wakati huo au Chief Minister Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hiyo iliwekwa kwenye Hansard katika suala la uraia, lilileta msuguano mkubwa na hasa baada ya kuwa mwaka 1958 Waingereza walipotupa masharti ya uchaguzi wa kura tatu. Kila Jimbo liwe lina Mbunge Mzungu, Muafrika na Muasia na kundi kubwa la vijana wa TANU, kujitoa TANU na kuunda Chama Cha African National Congress of Tanganyika wakisema Tanganyika ni kwa Waafrika tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu aliyasema haya Tarehe 28 Oktoba Mwaka 1961 katika Hansard na naomba nimnukuu na ndiyo msingi wa kwa nini uraia pacha Tanzania haukukubalika wakati huo. “Now Sir, what we are trying to do, we are establishing a citizenship of Tanganyika, what is going to be the best of this citizenship of Tanganyika. We, the Government kwa sababu alikuwa Chief Minister, elected by the people of Tanganyika say loyalty to the country is going to be the basis of determining the citizenship of Tanganyika. In order to be certain as far as human responsible to be certain, the citizens of Tanganyika are going to be loyal to Tanganyika and Tanganyika only. We have said although other countries do accept it, we are not going to accept dual citizenship in Tanganyika” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ni maneno ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa Waziri Kiongozi katika Bunge la Tanganyika, Bunge la Madaraka tukijiandaa kupata uhuru wa nchi yetu.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Prof. Palamagamba Kabudi.

MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mwenyezi Mungu Rahim kwa ruzuku ya uhai na afya. Nichukue pia fursa hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Nishati. Nami niungane na wale wote wanaokutakia kila lakheri katika azma yako ya kugombea nafasi ya Rais wa IPU. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninajua una hakika miongoni mwa watu ambao wanafuraha kubwa ya wewe kupanda katika nafasi hiyo ni mimi. Fahari ya Mwalimu yoyote yule ni kumuona mwanafunzi wake aliyemsomesha, aliyemlea anapanda na kupanda na kupanda zaidi. Kwa hiyo mimi ambaye nilipata bahati ya kuwa Mwalimu wako katika ngazi mbalimbali nakuombea kila la kheri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele na kuiwezesha sekta hii ya nishati kwa hali ya juu. Ila nimpongeze Mheshimiwa January Makamba, Waziri wa Nishati pamoja na Stephen Byabato, Naibu Waziri, Katibu Mkuu Eng. Mramba, Naibu Katibu Mkuu, Mbutuka kwa kazi nzuri mnayoifanya.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utakuwa katika maeneo matatu nikipata fursa. Kwanza ni Wilaya ya Kilosa, pili Mradi wa Julius Nyerere na tatu Umeme wa Joto Ardhi. Mradi wa REA ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake, na ndio mradi ambao unabadili hali ya maisha ya watu wetu vijijini. Na mimi nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais na Wizara ya Nishati kwa kutoa fedha zote kwenye Jimbo la Kilosa lenye kata 25 na vijiji 37 ambavyo havina umeme. Nishukuru sana kwa hilo.

Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa tumepata mkandarasi ambaye utendaji wake wa kazi hauridhishi kabisa. Lakini katika hilo nikushukuru sana wewe mwenyewe Mheshimiwa Waziri, niwashukuru sana Mtendaji Mkuu wa REA Eng. Hassan Said, Meneja wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Fadhili Chilombe, Mameneja wa Kilosa, Meneja wa Mvomero na wale waratibu vijana wawili ambao sasa wamechukua hatua za kuhakikisha kwamba jambo hili sasa linashughulikiwa.

Mheshimiwa Spika, Mkandarasi amepewa deadline ya tarehe 30 Juni awe amepeleka umeme katika vijiji 20 asipofanya hivyo achukuliwe hatua. Mheshimiwa Waziri naomba msukumo wako mkandarasi huyu atekeleze mkataba. Amepewa fedha zote na kwa hiyo hana sababu ya kuendelea kusuasua; na kama hatafanya hivyo ifikapo tarehe 30 Juni basi hatua zichukuliwe. Hatuwezi kuendelea kuwa na mkandarasi ambaye ana fedha na hafanyi kazi.

Mheshimiwa Spika, baada ya hilo ya REA na ugoigoi wa mkandarasi nimeletewa simu leo kutoka Kijiji cha Matongolo – Dumila kwamba inaelekea transformer imezidiwa. Mimi naamini kabisa Meneja wa Mvomero ambaye ndiye anayesimamia huko atalichukulia hatua ili liweze kurekebishwa.

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo nije kwenye Bwawa la Mradi wa Mwalimu Julius Nyerere. Huu ni mradi ambao Watanzania wote hatuna budi kuwa na fahari nao na kuuenzi sana. Ni mradi ambao aliuasisi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Na mnapokuwa na mradi huo ambao umeanzishwa na muasisi wa Taifa lenu na akashindwa kuutekeleza ninyi ambao mnapata heshima ya kuukamilisha mnapata baraka nyingi sana za Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo mimi ninahakika kabisa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wewe Waziri, watendaji wa TANESCO na wote waliohusika katika mradi huu Mwenyezi Mungu atawapa baraka kwa sababu mmetekeleza mradi ambao ulikuwa ndani ya moyo wa muasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kutekeleza mradi huu nchi yetu, TANESCO, wahandisi na wataalamu ewote wa Tanzania tumepata uzoefu na utaalamu wa kujenga kwa ufanisi zaidi miradi ijayo ya umeme wa maji kama vile Rumakali na Ruhuchi. Tajiriba hii tuliyoipata, tajiriba kwa kiingereza ni experience, tajiriba hii tuliyoipata kama nchi itatusaidia sana huko tuendako kuwa na muala katika kutekeleza miradi hii ya maendeleo na muhala maana yake ni coherence.

Mheshimiwa Spika, mradi huu una upekee wa aina yake na ni lazima tuuenzi kwa kadri tunavyoweza. Ukubwa wa bwawa hili kwa kweli ni ziwa, kwa sababu ni bwawa ambalo lina ukubwa wa kilomita za mraba 1,194.4 ni kubwa zaidi ya Ziwa Eyasi lenye kilomita za mraba 1,050 ni kubwa zaidi ya Ziwa Natroni lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,040 na ni kubwa zaidi Ziwa Manyara lenye kilomita za mraba 470. Kwa hiyo bwawa hili kwa kweli linatupa heshima ya Ziwa na Bwawa hili ni muhimu sana kama ambavyo alilifikiria Baba wa Taifa. Moja ni kuzalisha umeme lakini moja ilikuwa ni kudhibiti mafuriko ya Mto Rufiji. Na mimi naamini kabisa sasa tatizo la mafuriko ya Mto Rufiji yamekwisha, lakini pia bwawa hili litatusaidia katika kilimo, katika Utalii.

Mheshimiwa Spika, katika utalii nimeambiwa kwamba bwabwa hili baada ya kuwa limejaa katika ujazo wake litakuwa na visiwa visivyopungua sita litakuwa ni bwawa la aina yake Duniani lenye utalii pia wa visiwa ndani ya bwawa hilo. Nishukuru sana kwa juhudi kubwa zinazochukuliwa mpaka sasa katika mikoa yote kumi na wilaya 26 zenye mito inayopeleka maji katika bwawa hili. Ni vizuri kabisa tujue hilo hiyo mikoa 10 na wilaya 29 zenye mito inayopeleka maji katika bwawa hili zinawajibu mkubwa sana wa kutunza mito hiyo, vyanzo hivyo vya maji ili kuhakikisha maji yanaendelea kutiririka. Watu waendelee kuelimishwa katika maeneo hayo na wajue maji yanatoka sehemu nyingi. Maji yanayokwenda kwenye hili bwawa yanatoka Chunya, Sikonge, y Manyoni, Tunduru, Kilombero, Chamwino, Chemba, Songwe, Mbeya na Makete; na zaidi kabisa ni kutunza Wetland ya Kilombero bila Wetland ya Kilombero kutunzwa bwawa hili itapata shida.

Mheshimiwa Spika, mimi niombe kwa dhati kabisa Mheshimiwa Waziri January Makamba kwa kushirikiana na wenzako katika Ofisi ya Rais, Makamu wa Rais Mazingira, Wizara ya Maji, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya TAMISEMI kuhamasisha watu wote katika mikoa hii kumi na Wilaya hizi 24 kujua wajibu mkubwa walio nao wa kutunza mito na vyanzo vya maji ili bwawa hili liendelee kwa manufaa yetu. Na tutakapoata hizi megawatt 2115 tutakuwa tumepata umeme mwingi wa kutuwezesha kuleta maendeleo makubwa.

Mheshimiwa Spika, bila umeme huwezi kuwa na viwanda, miundombinu na huwezi kufanya chochote. Ndiyo maana Mwasisi wa Soviet Union Vladimir Lenin alipochukua uongozi alipochukua uongozi wa Soviet Union kazi yake ya kwanza ilikuwa ni kupeleka umeme. Kazi ya kwanza aliyoifanya Kwame Nkrumah Ghana baada ya Ghana kupata uhuru ilikuwa ni kujenga Bwawa la Umeme la Akasombo ili aweze kuleta maendelo kwa Ghana. Kwa hiyo suala la bwawa hili ni suala muhimu sana. Kwa hiyo ningeomba Wizara zote na wadau wote na sisi Wabunge tuone fahari na bwawa hili lakini sasa tuongeze juhudi katika kutunza mazingira ili mradi yaweze kwenda katika bwawa.

Mheshimiwa Spika, hatua tuliyofika kwa Mheshimiwa January Makamba sasa ni sawasawa na pilot ambaye ametangaza ndege kutua. Tunaitakia ndege hiyo itue salama na kama kutakuwa na landing turbulences basi pilot ashike usukani ndege itue salama.

Mheshimiwa Spika, jambo jingine ambalo ningependa kulichangia ni hili la umeme wa joto ardhi. Katika maonesho haya nimepata elimu kubwa sana kuhusu joto ardhi. Na mimi naomba Wizara, Mheshimiwa January Makamba, jambo hili ambalo mmelianza sasa na mtakalolianzia kule Ngozi na yale maeneo mengine manne mliongeze juhudi kubwa sana. Kama tu pale Ngozi kwa awamu ya kwanza tutapata megawatt 70. Megawatt 70 si umeme mchache tunaamini katika maeneo mengine 52 tutafanikiwa kupata umeme mwingi zaidi.

Mheshimiwa Spika, Kenya sasa wanazalisha megawatt 1000 kutokana na joto ardhi, sisi kwa vyanzo vyote tulivyonavyo tutapata umeme mwingi sana naomba kuunga mkono hoja na kwa asilimia zote.

Mheshimiwa Spika, kila lakheri katika mbio zako za unakoelekea. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kukushukuru sana kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia katika bajeti hii ya Serikali ya mwaka 2022/2023. Nachukua fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu Rahim kwa kunijalia uhai, na kwa kunipa afya ya kuniwezesha kusimama hapa leo ili nami nitoe mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake madhubuti, kwa uongozi wake bora na kwa mwaka huu kutuletea mapendekezo ya bajeti yanayoakisi maslahi na matlaba yaani expirations za Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha, nichukue fursa hii kumpongeza sana Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu, Naibu Waziri Mheshimiwa Hamad Hassan Chande, Katibu Mkuu wa Wizara na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bwana Emmanuel Mpawe Tutuba na Manaibu Katibu Wakuu na wote katika Wizara ya Fedha kwa kutuletea bajeti nzuri yenye ubunifu na inayozingatia mahitaji na matarajio ya wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba yangu binafsi na ya wananchi wa Jimbo la Kilosa ambalo nimepata heshima ya kuwawakilisha, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi ambazo ametupatia wana Jimbo la Kilosa katika mwaka huu wa fedha 2021/2022 katika sekta ya afya, elimu, maji, barabara, madaraja, mawasiliano vijijini, kilimo cha umwagiliaji na kadha wa kadha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa elimu, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutupatia jumla ya Shilingi 2,347,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Berega ambayo tumepata Shilingi bilioni moja. Shule ya Sekondari ya Berega itakuwa ni ya aina yake. Kwa upande wa O‘Level ni shule ya Kata kwa upande wa A’Level wao ni shule ya Kitaifa kwa ajili ya wavulana Bweni, Sayansi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutupa Shilingi milioni 470 kujenga Shule ya Kata ya Maguha. Wote mnaosafiri kwenda Dar es Salaam, mara baada ya kupita Mtumbatu ambako mnanunua nyanya, vitunguu, maharage na vinginevyo, mtaiona Shule ya Berega na mtaiona Shule ya Maguha. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa jumla ya Shilingi bilioni 2.405 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya na zahanati. Namshukuru kwa namna ya kipekee kwa kutoa jumla ya Shilingi milioni 900 kujenga kituo cha afya katika milima ya Uponera. Wale wanaoifahamu milima ya Uponera haifikiki kwa urahisi. Kutoka Gairo mpaka Uponera ni muda wa saa nne. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. Maisha ya akina mama wengi waliofariki wakati wa kujifungua wakishuka kwenda Mamboya mwendo wa saa nne au kwenda Gairo mwendo wa saa tano, sasa yanakwisha kwa Shilingi milioni 900 ambazo Mheshimiwa Rais ametoa kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Uponera katika Kata ya Mamboya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nashukuru kwa kituo cha afya cha Kata ya Chanzulu Ilonga; Shilingi milioni 515 na Kituo cha Afya cha Ntembo Kata ya Mabula Shilingi milioni 450; pia kwa Shilingi milioni 200 kwa ajili ya kujenga ICU katika hospitali ya Wilaya ya Kilosa, bila kusahau zahanati mbili za pembezoni mwa Jimbo letu ambalo ni kubwa sana, yaani Zahanati ya Unone Kata ya Rudewa Shilingi milioni 80 na Zahanati ya Lumbiji kwa Shilingi milioni 80.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa madaraja, namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa upendeleo wa aina yake. Kwanza kwa kutupa fedha ya kujenga daraja la Berega katika Mto Mkundi ambalo linagharimu Shilingi 7,900,000,000/=. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni kuenzi jitihada alizozifanya Rais wa Awamu ya Pili, Benjamin William Mkapa aliyejenga daraja, kwa bahati mbaya likasombwa na maji; pia Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete aliyejenga daraja ambalo bado lipo lakini limevunjika. Kwa hiyo, Shilingi bilioni 7,900,000,000/= zitajenga daraja hilo, nasi kwetu tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kwa ajili ya Shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujenga daraja la Masombawe Kata ya Berega; na Shilingi milioni 160 kwa ajili ya kujenga daraja la watembea kwa miguu, bodaboda na baiskeli kwa Kijiji cha Ruwemba ambacho kukifikia unatumia mwendo wa saa nne kupita wilaya tatu ili kufika Kijiji cha Ruhemba katika Kata ya Kidete. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tunamshukuru kwa fedha aliyotupa kwa ajili ya miradi ya maji hasa katika Mji Mdogo wa Dumila. Kwanza alitupa Shilingi 1,200,000,000/= na sasa ametupa Shilingi bilioni 530 ili kuhakikisha Mji wa Dumila unapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda nimshukuru pia Mheshimiwa Rais kwa Shilingi milioni 700 kwa ajili ya kujenga tanki la maji na mfumo wa maji katika Kata ya Rudewa katika Jimbo la Kilosa. Hii ni baadhi tu ya miradi ambayo imepatiwa fedha na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika mwaka huu wa fedha na katika mwanzo wa uongozi wake. Sisi wana Kilosa tunamshukuru sana na kwa lugha ya Kikaguru nimwambie Kwimage Lugano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nategemea kabisa katika bajeti hii tunayoijadili sasa barabara ya Rudewa kwenda Kilosa itakamilika kwa ujenzi wa madaraja manne yaliyosalia; daraja la Mto Kobe, daraja la Mto Kilonga na daraja la Mazinyungu na hatimaye daraja kubwa la kuvuka Mto Mkondoa kwenda Mikumi na baadaye kwenda Iringa, Mbeya, Tunduma na Zambia. (MakofI)

Mheshimiwa Spika, vile vile tunashukuru sana kwa fedha ambayo tunajua imepangwa kwa ajili ya kuanza kujenga barabara ya Kilosa kwenda Mikumi. Barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu na itasaidia sana katika utalii, na pia katika mazao ya miwa na mazao mengine yanayolimwa katika Jimbo la Kilosa na Mikumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa bajeti tunayoijadili, napenda sana kumshukuru Waziri wa Fedha, kwa kupendekeza kusamehe kodi ya ongezeko la mtaji, (Capital Gain Tax), kwenye uhamishaji wa haki na taarifa za madini kwenda kwenye kampuni za ubia zinazoundwa baina ya Serikali na wawekezaji na uhamishaji wa hisa, (Free Carried Interest) kutoka kampuni ya ubia kwenda kwa Serikali. jambo hili litarahisisha utekelezwaji wa mikataba hiyo, pia litarahisisha mazungumzo kwa sababu lina faida kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami nichukue nafasi hii kumshukuru tena Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa heshima kubwa sana aliyonipa na kwa kuniamini kwa kiasi kikubwa sana kunikabidhi majukumu ya kuwa Mwenyekiti wa Timu Maalum ya Rais ya Majadiliano ya Serikali, yaani kwa kiingereza (Special Presidential Government Negotiation Team). Ni heshima kubwa sana ambayo sitaisahau katika maisha yangu yote nitakayokuwa duniani. Sijawahi kupata heshima kama hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatua hizi ambazo Waziri wa Fedha amezichukua kwenye suala hili la capital gain tax litatusaidia sana. Tuna aina mbili ya free carried interest na ningeomba nitumie nafasi hii kuzifafanua. Iko aina ya free carried interest, yaani hisa ambazo Serikali inapewa bila kulipiwa za aina mbili, iko ambayo ni diluted free carried interest shares na iko ambayo ni non dilutable free interest carried shares; nini tofauti yake?

Mheshimiwa Spika, ile ya kwanza ambayo siyo dilutable, kila mwekezaji anapoongeza hisa wewe usipoongeza mtaji thamani ya hisa zako inashuka na mwisho inaweza kufifia kabisa. Tanzania tumechukua aina ya pili ya non dilutable free carried interest maana yeke nini? Yeye kila anpoongeza mtaji wewe unabaki na asilimia 16 ileile katika ule mtaji ulioongezeka. Maana yake thamani ya hisa zako haishuki. Nchi nyingi za kiafrika na ninaomba nisizitaje kwa heshima ya nchi hizo, zilichukua aina ya kwanza ya dilutable ndiyo maana nyingine zilianza na asilimia 50 leo zina asilimia Mbili. Nyingine zilianza na asilimia 20 leo zina asilimia Tano, lakini sisi kwa aina hii ya hisa tutaendelea kuwa na asilimia hiyohiyo katika maisha yote ya mgodi au mradi huo bila hisa hizo kupungua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo tumelifanya katika Mabadiliko ya Sheria ya 2017 ya kuunda kampuni za ubia za madini kati ya Mwekezaji na Serikali. mara nyingi tunasahau jambo hili muhimu sana, iko tofauti kati ya rasilimali na mali. Madini ni rasilimali, lakini ili yawe mali ni lazima yatolewe leseni kama ambavyo ardhi ni rasilimali, lakini ili ardhi hiyo iwe mali ni lazima upewe Tittle Deed, yaani Hati ya Umiliki. Huko nyuma sisi tulibaki na rasilimali, lakini license au leseni zilipewa kampuni za nje. Kwa hali ya sasa katika majadiliano yote yanayoendelea leseni sasa zinamilikiwa na kampuni ya umoja ya ubia. Maana yake sasa unamiliki leseni ambayo ni mali na madini ambayo ni rasilimali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hilo ningependa nifafanue, ile free carried interest sio kwai le kampuni hodhi ni kwa mgodi husika na mradi husika. Kwa hiyo, kwa mfano katika kampuni ya Twiga Minerals Serikali ina asilimia 16 katika Mgodi wa Bulyankulu, ring fenced, asilimia 16 katika Mgodi wa North Mara, ring fenced, na asilimia 16 katika Mgodi wa Buzwagi ambao unakaribia kufungwa, ring fenced na asilimia 16 katika Kampuni ya pamoja. Maana ya ku-ring fence ni kwamba, faida au hasara ya mgodi mmoja haiwezi kuathiri faida au hasara ya mgodi mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumefanya pia hivyo katika Kampuni ya Tembo Nickel, itayaoanza kuchimba madini ya nickel ambayo ni madini ya kimkakati kule Kabanga. Serikali ina asilimia 16 kwenye Mgodi wa Kabanga, lakini pia ina asilimia 16 katika smelter itayaojengwa Kahama, pia ina asilimia 16 katika kampuni hodhi. Hivyohivyo ndivyo tumefanya kwa kampuni nyingine za Nyati Sand Minerals, lakini pia Kampuni ya Faru itakayochimba madini ya graphite huko. Kwa hiyo, maamuzi hayo yaliyochukuliwa na Waziri wa Fedha yanatusaidia kutoka katika kawaida tuliyoizoea ambayo imekuwa haitupi faida zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naona kengele ya pili imegonga. Na nisikuweke mahali pagumu kuamua nikae au nisikae. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na nitachangia katika maandishi tofauti ya aina tatu za mikataba ya concession ya PSA na mikataba ambayo sasa tunaingia. Hiyo, nitachangia kwa maandishi au nikipata nafasi nyingine wakati wa bajeti hii kabla ya kupiga kura, kama inaruhusiwa, nitaomba tena nipate nafasi nilieleze hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa heshima hii na ninamshukuru sana Waziri wa Fedha kwa ubunifu na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa heshima aliyonipa, lakini kwa upendo kwa wana-Kilosa. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Rahim wa ruzuku ya uhai, lakini na afya ambayo imetuwezesha kukutana leo kujadili bajeti hii ya Wizara ya Uchukuzi. Nami nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa ambao umefanyika katika mashirika mbalimbali yaliyo chini ya Wizara hii, lakini leo nitajikita zaidi katika suala la reli. Nimpongeze sana Mheshimiwa Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu Profesa Godius Kiharara na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Ally Possi na wafanyakazi wote kwa bajeti nzuri ambayo wametuletea.

Mheshimiwa Spika, uwekezaji katika reli ni uwekezaji muhimu sana na uwekezaji ambao utadumu kwa muda mrefu, tukitilia maanani kwamba reli hii tunayoitumia sasa ilijengwa na Wajerumani takribani miaka zaidi ya 120 iliyopita na mpaka leo inafanya kazi. Kwa hiyo tunawekeza kwa kizazi cha leo, lakini tunawekeza kwa miaka 100 mingine ijayo ambayo naamini wengi wetu katika chumba hiki tutakuwa ni sehemu ya makerubi na maserafi tukimwimbia Mungu bila mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nipongeze sana uwekezaji katika SGR ambao utatuunganisha na Burundi, DRC, Rwanda na Uganda, lakini pia kufufua reli hii ya MGR ambayo ni muhimu na sasa kuanza kukarabati reli ya TAZARA. Kwenye reli ya TAZARA ni muhimu sana tuikarabati ili tuweze kuiunganisha na reli ya Benguela inayotoka Zambia Kapiri Mposhi kwenda Lobito.

Mheshimiwa Spika, huu ni wakati wa kuanza kujiandaa kuunganisha Bahari ya Atlantic na Bahari ya Hindi kupitia Bandari ya Dar es Salaam na Bandari ya Lobito. Ningependa tuwe na mkakati wa kuifanya Bandari ya Lobito isiwe bandari shindani bali iwe bandari ya kusaidiana na Dar es Salaam ya kutoa mizigo Latin America na Caribbean kuja Afrika kwenda Asia na kwenda China, kwa sababu yapo madini kule Latin America, yapo madini kama vile brockite yanakwenda China leo. Kwa hiyo kuwe na mkakati wa kuigeuza Lobito kuwa bandari rafiki na si bandari shindani. Tuanze kuwekeza katika TAZARA na tayari wenzetu wanafufua reli ya Benguela inayokwenda Lobito.

Mheshimiwa Spika, reli ni kitu muhimu sana na niipongeze sana Serikali kwa kuwekeza katika kufufua reli ya MGR, yaani hii reli ambayo tunaitumia sasa iliyojengwa na Wajerumani. Ningemwomba Mheshimiwa Waziri aje na maelezo ya kutosha kwamba kuna mikakati gani iliyopo ya kufufua yale mabwawa matano ambayo Wajerumani waliyajenga kati ya Kilosa na Gulwe ili kuilinda reli ya kati; Bwawa la Kidete, Bwawa la Kimagai, Bwawa la Msagali, Bwawa la Kibibo na Bwawa la Ikowa. Najua Bwawa la Msagali limeanza kujengwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, lakini tumeambiwa Bwawa la Kidete na mabwawa mengine Wizara ya Uchukuzi, kwa maana ya Shirika la Reli, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Maji watashirikiana.

Mheshimiwa Spika, naomba tuanze haraka na Bwawa la Kidete kwa sababu Bwawa la Kidete si tu kwamba linatunza reli lakini ndilo linalozuia mafuriko katika Mji wa Kilosa; na liendane na ujenzi wa kingo za Mto Mkondoa eneo la Magomeni na eneo la Kisaki katika Mji wa Kilosa. Hii itatusaidia pia katika kilimo na uvuvi. Pale Kidete lile bwawa zamani lilikuwa lina samaki wengi sana ambao walilisha Miji ya Kilosa, Kimamba na Morogoro. Wakati huo tukiwa wadogo palikuwa na treni ambayo sijui kwa nini ilipewa jina hilo, ilikuwa inatoka Dodoma mpaka Morogoro iliitwa Malaya. Kazi yake moja ilikuwa ni kubeba mizigo hiyo ya samaki kutoka Kidete.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni la reli kati ya Kilosa na Kidatu. Fedha zimetengwa kwa ajili ya kukarabati na kufufua reli ya Kilosa na Kidatu. Hapa nina maombi mawili. Ombi la kwanza tufikirie hiki kipande cha Kilosa – Kidatu na chenyewe kiwe cha cape gauge ili treni ikitoka Kilosa isilazimike kubadili mzigo Kidatu na badala yake iende moja kwa moja mpaka Mlimba na Mlimba iweze kwenda mpaka Kapili Mposhi na Kapiri Mposhi mpaka Durban na Durban mpaka Walvis Bay. Kwa hiyo ningependekeza tuone uwezekano wa kipande hicho kijengwe kwa cape gauge badala ya meter gauge. Tujenge pia barabara ya lami kati ya Stesheni ya sasa ya Kilosa ya SGR pale Kondoa na Stesheni ya Kilosa ya MGR ili iwe rahisi kwa mizigo na watu kutoka kwenye stesheni ya SGR Kondoa na kuja kwenye stesheni ya MGR pale eneo la Uhindini.

Mheshimiwa Spika, kingine ambacho ningependa tufikirie sasa ni kwamba, reli itakayojengwa kwenda Mchuchuma isiishie Mchuchuma, iongezwe kutoka Mchuchuma kwenda Kidatu kwenda Kilosa; ndivyo hivyo Wajerumani walivyokuwa wamepanga kuijenga reli hiyo walipotaka kuliendeleza eneo la Ruhuhu Valley kuwa ni eneo la ujenzi wa viwanda. Wajerumani walikuwa wameamua eneo la Ruhuhu kuja Kidatu kuja Kilosa lifanane na Ruhr Valley ya kule Ujerumani ambayo ina Miji ya Dortmund, Essen, Dusseldorf, Bornholm na Kolon; wajenge viwanda. Kwa hiyo reli iongezwe iende mpaka Kidatu na Kilosa ili mzigo mkubwa huo wa madini ya chuma, makaa ya mawe, vanadium, titanium, aluminium na rare earth iweke kutoka huko na kwenda Kahama kwenye refinery ya Tembo ili tuweze kuyeyusha na kupata metal. Kwa hiyo ningeomba hilo nalo lifikiriwe.

Mheshimiwa Spika, kuhusu hilo hilo suala la hapo, Wajerumani walikuwa wamepanga bandari yao kubwa iwe Bandari ya Kilwa. Tuanze kufikiria kuifanya Bandari ya Kilwa kuwa trans-shipment port kama iliyo Salalah kule Oman. Tuanze kufikiria kujenga reli kutoka Kilwa iungane na Kidatu, iungane na Kilosa kutoka Kilwa iende Mbamba Bay; na wenyewe Wajerumani Mbamba Bay waliita Sphinx Hafen ili bandari hizo zifane.

Mheshimiwa Spika, katika suala hilo hilo la reli, ningependekeza pia tujenge reli kutoka Dumila – Dakawa kuja kuunganisha na stesheni ya Mkata ili kuunganisha viwanda vya sukari vya Kilombero, Kilosa na Mtibwa. Tuigeuze reli hii; kama ilivyosemwa; iweze kubeba mizigo ya ndani.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu muda hautoshi, naiomba Wizara, Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu Profesa Kahyarara waje Kilosa tuone jinsi ya kufanya Kilosa kuwa ni mojawapo ya maeneo ya kuzalisha vitunguu na kuzalisha mbogamboga wanazoziona barabarani Dumila ili sasa treni iweze kuchukua mizigo hiyo ya nyanya, vitunguu na mbogamboga kwa ajili ya matumizi ya ndani, lakini pia kwa ajili ya matumizi ya nje.

Mheshimiwa Spika, nije kwenye suala la Air Tanzania na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Sote tunafahamu Shirika la Ndege la Afrika Mashariki lilivunjika tarehe 5 Februari, 1977 katika hali iliyokuwa ngumu sana na tukafanikiwa pilot mmoja kurusha ndege moja tu ambayo ndiyo ilikuja na baada ya hapo tukawa hatuna ndege. Hata hivyo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere tarehe 31 Machi, 1977 akisaidiwa na Waziri wake aliyemwamini sana Mheshimiwa Amir Habib Jamal walianzisha Shirika la Air Tanzania Corporation., likawa na ndege mbili za boeing 737 Kilimanjaro na Serengeti, likawa na ndege nne za Fokker Friendship na ndege mbili za twin water.

Mheshimiwa Spika, shirika letu la ndege limepita katika vipindi mbalimbali, lakini sasa limefufuka tena na limeanza kukua. Tayari muamana, kwa maana ya reliability ya huduma za reli zimeongezeka, na hii imeweza kujenga itibari (trust) ya Shirika la Ndege.

Mheshimiwa Spika, mwaka huu ni mwaka wa 60 tangu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iundwe, mwaka huu ni mwaka wa 25 tangu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipofariki dunia ingawa amegoma kufa. Napendekeza kwa Serikali kwamba ndege yetu kubwa ya Dreamliner ambayo haijaja tuipe jina la Julius Nyerere kazi iendelee kwa kuuenzi Muungano wa miaka 60, lakini pia kumpa heshima Baba wa Taifa ambaye miaka 25 iliyopita Mwenyezi Mungu alimchukua, lakini yu hai.

Mheshimiwa Spika, kwa kufanya hivyo hatutakuwa wa kwanza. Shirika la Ndege la Afrika ya Kusini ndege yao kubwa kuliko zote ya Air Bus A340–600 mwaka 2003 Mandela alipofikisha miaka 85 waliipa jina la Nelson Mandela. Kwa hiyo ndege hii ipewe jina la Julius Nyerere kazi iendelee miaka 60 ya Muungano ili kumuenzi Baba wa Taifa. Kwa namna hiyo tutakuwa tumeungana na wenzetu ambao pia wamempa Baba wa Taifa heshima kubwa, mojawapo ikiwa ni Nchi ya Guinea.

Mheshimiwa Spika, Nchi ya Guinea imekipa chuo kikuu katika mji wa Kankan Guinea jina la Julius Nyerere University; na sisi tuna vyuo viwili vya Julius Nyerere, tuna chuo cha Julius Nyerere Guinea lakini sasa tuwe na ndege ambayo itaruka katika anga ikibeba jina la mtu huyu ambaye miaka 60 aliunda Taifa ambalo leo ni Taifa na si mkusanyiko wa makabila na leo ni nchi yenye heshima, nchi inayojivunia na imeweza kumtoa Mheshimiwa Rais wa kwanza Mwanamke katika nchi hii. Katika utawala huu na uongozi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ndege hiyo tuipe jina la Julius Nyerere Kazi iendelee.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja, lakini niombe kiwanja cha ndege katika mji wa Kilosa. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Rahimu kwa nafasi hii ya kuweza kuchangia na ninakushukuru wewe mwenyewe kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Spika, ninaipongeza sana Wizara ya Maliasili na Utalii na hasa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na watumishi wote, kwa hotuba nzuri ya bajeti waliyoitoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara hii nii Wizara muhimu sana kwa sababu ndiyo inayosimamia rasilimali za nchi yetu ambazo zina thamani kubwa isiyomithilika na ndiyo sura ya nchi yetu, ndiyo hifadhi ya nchi yetu, ndiyo hazina ya nchi yetu. Kwa hiyo, ni Wizara muhimu sana na mimi ninaanza kabisa kwa kuunga mkono hoja na kuomba Wizara hii iongezewe fedha ili iweze kuyafanya mambo hayo kwa ukamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuchangia mambo matatu; la kwanza ni kuhusu mazungumzo kuhusu madhila yanayotokana na ukoloni wa Wajerumani na kurejeshwa kwa malikale na mali za kitamaduni ambazo ziko Ujerumani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa ninaomba kuanza na tanbihi au indhari (caution). Mazungumzo ambayo yameanza ningetoa indhari kwamba inaonekana sasa wenzetu wa Ujerumani badala ya kujua kwamba sisi ni Taifa, wameanza wao moja kwa moja kwenda kwenye jamii hizo, moja kwa moja kwenda kwenye makabila hayo na kusahau kwamba sisi leo siyo mkusanyiko wa makabila ambayo...

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, subiri kidogo.

Maafisa ambao hamjatangazwa bado, subiri mtangazwe halafu mtatoka. Watoke wale ambao wameshatangazwa, wale ambao bado kutanganzwa mtulie kidogo hapo mtatoka mkishatangazwa. (Makofi)

Mheshimiwa Profesa Kabudi.

MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Spika, hilo ni muhimu sana kwa sababu kuna kila dalili sasa kuonekana kwamba ni maeneo fulani tu ndiyo yaliyopata madhila ya ukoloni wa Kijerumani, wakati ni nchi nzima na maeneo yote yalipata madhila ya kikoloni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sina muda wa kusema kwa sababu leo nimekuja na kitabu ambacho ningependa watu wakisome waone kwamba Tanzania nzima ya leo iliathirika na ukoloni wa Kijerumani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba jambo hili liratibiwe, lisimamiwe na liongozwe na Serikali yenyewe, kwa sababu yako mambo ya msingi Serikali ya Ujerumani lazima ikiri na iwajibike kwa mambo mabaya yaliyofanyika na isitake tena kuturudisha kwenye mikataba kama ya Mangungo ya kwenda kwenye familia moja moja na jamii moja moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili ambalo ningependa kulizungumzia ni utajiri na utalii wa lugha, niliizungumzia kwenye bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na ninaomba tena kulileta hapa.

Mheshimiwa Spika, tuna utajiri mkubwa wa lugha ambao tunaweza pia kuutumia kama utalii, Tanzania ndiyo nchi pekee katika Bara la Afrika na duniani kote ambayo makundi yote makuu ya lugha yapo hapa. Ninaomba makundi haya makuu ya lugha yaifanye Tanzania kupeleka maombi UNESCO ili Tanzania iorodheshwe katika urithi wa Kimataifa yenye makundi hayo ya lugha, yaani Wabantu, Wakushi, Wakhoisani na Waniloti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa Wakhoisani ndiyo hawa Wasandawe na Wahadzabe, lakini pia wale wanaozungumza Lugha ya Afro-Asiatic yaani Wairaqw na Wambulu. Hili ni jambo muhimu sana, ni kitu cha pekee na adhimu na tutumie nafasi hii, siyo tu kuzitangaza lugha hizi, makundi haya makuu manne ya lugha pamoja na Afro-Asiatic kuwa urithi wa Kimataifa, lakini tuwekeze katika kutunza lugha hizi za asili kwa sababu zinabeba maarifa, zinabeba hazina kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninawashukuru sana wale wote ambao wamefanya utafiti kuhusu lugha hizi na tukifanya hivyo haturejeshi ukabila, bali tunatunza utajiri wetu mkubwa na anuai kubwa tuliyonayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulichangia ni kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa maeneo ya malikale na uendelezaji wa utalii wa kihstoria.

Mheshimiwa Spika, kwanza ninachukua nafasi hii kuipongeza sana Wizara kwa kupanua wigo wa utalii kutoka kwenye utalii wa wanyama tu, sasa kwenda kwenye utalii wa maeneo mbalimbali. Iwe ni utamaduni, iwe ni mila, iwe ni desturi, iwe ni vyakula. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa nianze kwa ule utalii wa hifadhi; Hifadhi ya Kitulo tuipe kipaumbele ya juu sana kuitangaza kama Kitulo na ninaiomba Wizara tusipeleke wanyama katika hifadhi hiyo. Watu hawaji kuona tu pundamilia na swala, watu wanakuja kuona maua ya asili. Ile ndiyo hifadhi ya aina ya peke yake duniani. Sasa kwa sababu hifadhi ile imeanza kukabiliwa na matatizo ya ukame, tutafute njia ya kuwa na sprinklers za kumwagilia maji ili mwaka mzima yawepo na yale maua yaliyokauka yavunwe, yahifadhiwe na yauzwe nje kama maua pekee yanayotoka kwenye Bustani ya Mungu iliyoko Kitulo na tuepuke sana kudhani utalii ni wanyama tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa ninachukua nafasi hii kukupongeza sana kwa jambo ambalo umelifanya ambalo limeongeza Utalii wa Ndani, haya matamasha ya ngoma za kienyeji. Sasa, sijui Tamasha hilo ni Tulia Traditional Dances au kama ni Dr. Tulia Traditional Dances na katika tamasha hili, marathoni imenishinda lakini tamasha hili kwa sababu ambazo wewe unazifahamu siwezi kulikosa, lakini hii iwe kwa nchi nzima. Tuwe na matamasha ya aina hiyo ya utamaduni wetu na iwe ni sehemu ya kuendeleza utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, Makumbusho ya Taifa na Idara ya Mali ya Kale iongezewe fedha ya kutosha ili kufanya utafiti na kuhakikisha maeneo haya yanahifadhiwa ili yawe sehemu ya urithi wa Taifa, sehemu ya urithi wa Kimataifa, lakini pia sehemu ya utalii.

Mheshimiwa Spika, ninachukua nafasi hii kuipongeza sana Wizara kwa kutoa fedha katika bajeti ya maendeleo ya kuanza kujenga Nyumba ya Makumbusho ya Marais na hii ingefuatiwa na Jumba la Makumbusho mengine hapa Dodoma, lakini kila mkoa sasa ufikirie kuwa na nyumba ya makumbusho ambayo itatunza maeneo na utamaduni na mila na desturi za aina ile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona katika nchi za wenzetu, ukifika tu unakwenda kwenye makumbusho. Mji wa Addis Ababa peke yake Ethiopia, sitaki kuzungumzia Ulaya, Mji wa Addis Ababa una zaidi ya makumbusho 12 na ukifika pale utaona utamaduni wote wa Addis Ababa na sehemu ya mwisho ambayo watakupeleka kwenda kuiona ni Kanisa Kuu Utatu Mtakatifu, Addis Ababa ambako wamezikwa wafalme wote ikiwa ni pamoja na Haile Selassie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi pia maeneo hayo tungeyatambua, tungeyabainisha ili tuyahifadhi, ikiwa ni pamoja na Ikulu ya Chamwino, ikiwa ni pamoja na majengo mbalimbali hapa Dodoma, Boma la Dodoma lakini pia ikiwa ni pamoja na Jamatin hii ya Dodoma na Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu la Waanglikana la Diocese of Central Tanganyika ambalo ni miongoni mwa majengo ya kale na limejengwa kwa mfano wa Hekalu la Jerusalem, lakini kikubwa lilijengwa wakati wa njaa kubwa ili watu hawa wamkumbuke Mungu yupo na wasife na njaa, waliweza kuvuka awamu hiyo na wakajenga kanisa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maeneo yote hayo yahifadhiwe, lakini pia iwe ni pamoja na reli yote ya kati na stesheni zote ambazo zilijengwa na Wajerumani. Inaanza kuleta hofu tunapoanza kubadilisha mwonekano wa majengo haya ya reli ya zamani. Tuyatunze, tuitunze Meli ya MV Liemba na iwe ni sehemu ya rasilimali za watu kija kuziona. Ninachukua hatua hii kuipongeza sana Serikali kwa kuyatangaza Mapango ya Kipatimu kuwa ni mapango yaliyohifadhiwa na yaliyotumika wakati wa Vita ya Majimaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo hilo ninalisema kwamba wengi tunadhani kwamba Vita ya Majimaji ilikuwa sehemu moja tu ya Tanzania lakini Vita ya Majimaji iliyoanzia kwa Wamatumbi ilisambaa kwenda Kilosa kwa Wavidunda, ilishuka kwenda kwa Wangoni, Songea. Kwa hiyo, ninaipongeza sana hatua hii ambayo imechukuliwa na ninaomba Wizara sasa pia iweke juhudi hiyo katika Mapango ya Magubike kule Kilosa, Mamboya kule Kilosa ili nayo yawe katika hifadhi hii ikiwa ni pamoja na Kituo cha Stesheni cha Kondoa ambacho leo hakitumiki na ndiyo ilikuwa mahali waliposhushwa watuma lakini baadaye Wajerumani walijenga stesheni ya reli pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo ningepanda kulizungumza ...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzjai)

SPIKA: Dakika moja malizia Mheshimiwa, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Spika, ni kuhusu kuhifadhi Misitu ya Itigi (Itigi Thickets). Hii ni misitu ambayo iko Tanzania na Zambia tu, tumeanza sasa kulima korosho, alizeti, lakini tuchukue hatua ya kuitunza Itigi thickets na kuhakiksha tunaziorodhesha katika urithi wa Kimataifa ili zitunzwe, lakini pia zitusaidie kupata asali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa kwa jimbo langu tunaomba fedha ya malipo ya athari za tembo au ndovu, lakini pia, ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kilosa, ili kuhakikisha watalii wanaokwenda Mikumi wanaingia pale. Nilipoomba uwanja wa ndege watu wengine hawakuelewa kwamba, hiyo mbuga ipo huko.

Mheshimiwa Spika, nilianza kwa kuunga mkono hoja, ninaomba kuunga mkono hoja na mengine nitatafuta njia ya kuyachangia. Ndiyo maana nakushukuru sana na nilikuja na vitabu vyote, ili kuonesha mambo haya yote, ikiwa ni pamoja na hawa dinosaur na vitabu vipo hapa kuhusu mafuvu yote ya vichwa, vitabu vipo hapa, lakini muda hautoshi. Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na kunivumilia. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia katika hotuba ya bajeti ya Wizara hii muhimu kwa maendeleo ya wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Rahim, kwa ruzuku ya uhai na afya, lakini pia namshukuru sana kwa kutuwezesha mwaka huu ambao ni muhimu sana kwa Taifa letu, yaani miaka 60 ya Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutimiza miaka 60. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaijadili hotuba hii ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika bashasha hiyo ya miaka 60 ya muungano wetu ambao umebaki siku nane tuusherehekee. Katika miaka hii 60, kazi kubwa imefanyika katika miaka hii mitatu ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutekeleza na kutimiza ndoto za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye katika hotuba yake ya Ujamaa na Maendeleo Vijijini ya Mwaka 1968 alisema “kitovu cha maendeleo cha Watanzania ni kwenda vijijini.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu alisema wakati mataifa mengine yanafanya juhudi ya kwenda katika anga za juu na kupeleka binadamu na vifaa huko katika mwezi na sayari nyingine, sisi twende vijijini ili tupeleke maendeleo katika sekta zote. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kwamba katika miaka hii mitatu ya mwisho kufikia miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ambayo imeleta mabadiliko makubwa katika vijiji vyetu vyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ya sasa huko vijijini ni tofauti na ilivyokuwa huko nyuma. Nami ninaamini kabisa, Baba wa Taifa huko aliko anaona fahari ya mtu ambaye amekuja kutumiza ndoto zake na azma yake ya kuyabadili maisha ya Watanzania. Daima katika hali kama hiyo watatokea mabarakala, watatokea watu ambao lengo lao ni kufifisha juhudi hizo ili kuwaondoa katika mstari ambao mnakwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wote tusimame katika mstari ule ule alioujenga Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na ukaendelezwa na Mheshimiwa Marehemu Ali Hassan Mwinyi, Mheshimiwa Benjamin Mkapa, Mheshimiwa Jakaya Kikwete, Mheshimiwa John Pombe Magufuli na sasa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Huu siyo wakati wa kucheza ndwele huu ni wakati wa kushikamana na kusonga mbele, ili kuleta maendeleo kwa wananchi wetu na hasa tukizingatia kwamba, sasa dunia inabadilika na sisi lazima twende na kasi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameboresha maisha ya Watanzania katika nyaja zote; elimu, afya, maji, nishati, barabara, miundombinu na kilimo. Kwa sababu hiyo, tuna sababu zote za kujivunia na kusimama naye katika uongozi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa. Sikupenda kutumia jina hili, lakini nalitumia kwa sababu nimesikia mtaani wanamwita “mtu kazi” sasa sijui “mtu kazi” maana yake ni nini? Sijui ni Mandonga, lakini nalitumia kwa sababu ndivyo watu wanavyomwita “Mtu Kazi” kwa kazi kubwa anayoifanya katika Wizara hii akisaidiwa na Waheshimiwa Manaibu Waziri wake wote wawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nachukua nafasi hii pia, kuungana na wengine wote kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Dugange na Mheshimiwa Zainab Katimba, kwa kazi nzuri ambayo mnaifanya katika Wizara hii, ikiwa ni pamoja na Katibu Mkuu Ndg. Adolf Ndunguru na Manaibu Katibu Wakuu wote wanne, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na wengine wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nachukua nafasi hii kutoa pole sana kwa wote waliopatwa na adha na kadhia ya mafuriko. Sisi Mkoa wa Morogoro na Jimbo la Kilosa tulikumbwa na mafuriko toka tarehe 05 Desemba, mwaka 2023. Nachukua nafasi hii kumshukuru sana Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Adam Kigoma Malima na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Ndugu Shaka Hamdu Shaka, kwa kutusaidia sana wakati wa mafuriko yale ya mwezi Desemba, Januari na yanayoendelea mpaka sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bila umahiri wao, bila wao kusimama kidete, hali ile ilikuwa mbaya. Hapo hapo pia, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa misaada mingi tuliyoipata wakati huo wa mafuriko. Tulidhani Morogoro imeepuka mafuriko, lakini mafuriko yamerudi tena, kwa hiyo, tunawapa pole wenzetu wote wa Rufiji, Kilombero, Mlimba, Ifakara na maeneo mengine Inshallah, Mwenyezi Mungu atatuepusha katika kadhia hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hilo, nachukue nafasi hii kuishukuru sana Ofisi ya Raisi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, na hasa Mtendaji Mkuu wa TARURA Engineer Victor Seff, mara baada ya sisi kupata mafuriko na miundombinu kuharibika, alitembelea aneo la Kilosa na kukagua miundombinu. Tunashukuru sana kwa fedha ambayo tumepata kiasi cha shilingi 859,710,178 ambazo zimesaidia kufungua baadhi ya barabara pamoja na kujenga mitaro katika mji wa Kilosa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru sana fedha hizo zimetusaidia kujenga mitaro katika Mji wa Kilosa katika Kata ya Mbumi ambayo miaka yote ilikuwa inapata mafuriko, lakini safari hii haikupata kabisa hata tone la mafuriko. Pia tunashukuru kwa fedha hiyo ambayo imekwenda kutengeneza Barabara ya Magole Estate kwenda Mabwegere katika Kata ya Kiteko.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba, tunajua nchi nzima imepatwa na matatizo haya, lakini tungeomba tupate msaada zaidi wa kufungua tena Barabara ile ya Magole Estate kwenda Mabwerebwere, Barabara ya Rudewa – Unone – Kisare, Barabara ya Mbigiri – Mabano, Barabara ya Parakuyo – Twatwatwa – Manyara na Barabara ya Lumuma – Msowero kwenda Mnozi, ili nazo ziweze kufunguka na mazao mengi ya wakulima katika maeneo hayo yaweze kwenda katika masoko yanayohitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, shughuli zimesimama, lakini siyo kwa makusudi isipokuwa ni kwa sababu ya tatizo hili lililotupata. Kwa hiyo, tunaipongeza sana TARURA, nami naungana na wale wote wanaoona kwamba huu ni wakati sasa wa Serikali kutoa fedha kwanza kwa TARURA ili kurekebisha hii miundombinu iliyopata matatizo. Tulichukue kuwa ni jambo la dharura na kweli liwe dharura. Maana ya dharura ni kutenga fedha ya kutosha katika eneo hilo hata kama itakuwa na maana ya kupunguza katika maeneo mengine ili tuweze kuvifungua vijiji, tuweze kuunganisha vijiji na miji, vijiji na wazalishaji na vijiji na watumiaji wa mazao hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inapotokea dharura, basi ni muhimu pia kuichukulia kama dharura. Kwa hiyo, ni imani yangu kabisa TARURA watapewa fedha ya kutosha. Nachukua nafasi hii kuungana na wote wanaosema kwamba, kama kuna taasisi katika nchi hii zinazofanya vizuri kwa fedha ambayo wanapewa, ambayo wakati mwingine haikidhi mahitaji yao, basi TARURA ni moja ya taasisi hizo. Hiyo ndiyo busara ya maamuzi ya Serikali ya CCM ya kuzungumzia mambo ya maendeleo vijijini, ndiyo maana leo tuna TARURA, leo tuna REA, leo tuna RUWASA kwa sababu tunaamini kabisa nguzo kubwa ya nchi hii ni maendeleo vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi ambazo ametupatia katika sekta ya elimu katika Jimbo la Kilosa, na kubwa namshukuru kwa kutuwezesha kukarabati shule yenye umri wa miaka 107 ya Kilosa Town ambayo baada ya kupata shilingi milioni 150 sasa imepata madarasa mapya tisa na tumeweza kukarabati yale madarasa kongwe ili yabaki kama historia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusisitiza katika shule hizi zote kongwe, yale madarasa ya zamani tusiyabomoe, tuyakarabati tuyatunze yawe ni sehemu ya historia na kumbukumbu ya nchi yetu. Tumekumbwa na matatizo ya kubomoa majengo mengi ya kale tukiyaona siyo mali, kumbe ni mali kubwa sana na ndiyo inayoonesha historia ya nchi ilikotoka na ilikofika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyotusaidia kuikarabati shule hii yenye umri wa miaka 107 ambayo sasa inaendelea kutoa elimu. Katika eneo hili tumshukuru sana kwamba katika Jimbo la Kilosa kata zote 25 zina shule za kata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulibaki na kata tatu; Kata ya Berega, Kata ya Maguha na Kata ya Madoto. Sasa zote zina shule za kata na tumeanza kujenga shule nyingine za kata katika maeneo ambayo yamezidiwa na wingi wa wananfunzi. Kwa mfano, Kata ya Dumila tumeanza kuongeza shule nyingine ya sekondari kwa mapato ya ndani na nguvu za wananchi katika eneo la Mkundi. Pia katika Kata ya Mtumbatu tumeweza kufanya hivyo katika eneo la Kitange ili kupunguza umbali wa wanafunzi kutoka Kitange kwenda kusoma katika Shule ya Sekondari ya Mtumbatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la elimu ni muhimu sana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Profesa, ni kengele ya pili hiyo.

MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Naibu Spika, basi …

NAIBU SPIKA: Ahsante kwa mchango mzuri.

MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja katika eneo hili, lakini tuongeze fedha zaidi kwa TARURA na tuongeze fedha zaidi kwa upande wa miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko na mvua. Nashukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu Rahim kwa ruzuku ya uhai na afya ambayo imetuwezesha kukutana tena leo asubuhi hii. Pia nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuiendeleza nchi yetu, ambayo bajeti hii itakuwa na msukumo mkubwa zaidi katika kuleta maendeleo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu wote wa Wizara ya Fedha, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Katibu Mkuu na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Bwana Lawrence Mafuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nijikite katika mambo ambayo, zaidi yatagusa upande wa mipango. Nakubaliana na wale wote waliozungumza kwamba mipango ndio moyo na nguzo ya Taifa letu. Nakubaliana kabisa na nukuu ya Mheshimiwa Waziri Professor Kitila Mkumbo kutoka kwa Mheshimiwa Hayati Benjamin Mkapa kuhusu umuhimu wa mipango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hata Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, miongongi mwa mambo ambayo aliyasema mara kwa mara, alisema; “kupanga ni kuchagua.” Kwa hiyo, tunachokipanga tuchague kile ambacho kitasukuma maendeleo ya nchi yetu na watu wake ikiwa ni pamoja na maslahi yao pia matilaba (aspirations) zao. Hawa Watanzania wana-aspire nini na wana matilaba gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika upande huo ningependa nizungumzie suala moja muhimu ambalo Taifa hili hatuna budi kuliwekea umuhimu mkubwa na kuwekeza fedha nyingi tunavyoweza, kwa sababu sasa tunawekeza fedha kidogo katika eneo hilo, nalo ni eneo la Research and Development (Utafiti na Maendeleo). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali huko nyuma kuona umuhimu wa utafiti na maendeleo, ilianzisha Shirika la TIRDO ili liwe ndio Shirika la kuchochea research and development (utafiti na maendeleo) kwa upande wa viwanda. Ikaanzisha kiwanda cha CAMARTEC kule Arusha iwe ndio chombo cha utafiti na utengenezaji wa bidhaa kwa ajili ya kuboresha kilimo chetu. Pia ilianzisha taasisi mbalimbali za utafiti; TAWIRI kwa ajili ya wanyamapori, TAFIRI kwa ajili ya uvuvi, TAFORI kwa ajili ya misitu, NIMR kwa ajili ya madawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili la utafiti ni lazima sasa tuliwekee kipaumbele. Tusipofanya hivyo tutakuwa hatucheleweshi maendeleo ya sasa tu, lakini tutakuwa tunadumaza na kufubaza maendeleo ya miaka ijayo. Taifa hili halina budi sasa kuanza kuwekeza kwa maendeleo makubwa ya miaka 50 au 60 ijayo na kufanya hivyo, moja, ni kuimarisha vituo hivi vya utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuiboresha TIRDO ifanye research katika industrial research organization na haya yote tulijifunza kutoka India. National Planning Commission tulijifunza kutoka India, TIRDO tulijifunza kutoka India, NEMC tulijifunza kutoka India na COSTECH tulijifunza kutoka India. Tufanye tathmini, tujue hayo mafunzo tuliyoyatoa huko huku kumekuwa na upungufu gani ili tuyaimarishe na tujiimarishe katika research. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuimarishe research katika vyuo vyetu. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilikuwa na taasisi nzuri sana ambayo nashangaa na mimi ni mmoja wao, kwa nini baadaye tuliibadili? Ilikuwa inaitwa Institute of Production Innovation (Taasisi ya Ubunifu katika Uzalishaji) baadaye tukaibadili na Profesa Schoeman kutoka Ujerumani akahamia Namibia. Leo Namibia ndio wenye Institute of Production Innovation bora zaidi katika Bara la Afrika, wakati wazo lilitoka kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sasa vyuo vikuu vyetu viimarishwe katika eneo hili la RnD, ili viweze kushiriki katika kufanya utafiti utakaotufaa katika miaka ijayo. Pia sasa tuwekeze katika maeneo mengine ya utafiti na eneo moja ambalo napendekeza tuweke katika utafiti ni Space Science na Space Economy (Uchumi wa Anga na Sayansi ya Anga). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili sizungumzii jambo la kubuni. Tayari pale Chuo cha St. Joseph University of Tanzania wanayo St. Joseph University of Tanzania Satellite Development Team, ambayo inaongozwa na Dkt. Amani Bura, kijana Mtanzania ambaye amesoma India na China na sasa wametengeneza satellite ambayo ina uwezo wa kukusanya data na taarifa kuhusu mazao na mabadiliko ya tabianchi. Sasa hivi wanahangaika kupata shirika litakaloweza kurusha hiyo satellite yao kwenda angani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamekuwa wakizungumza na Shirika la India na Urusi. Nadhani jambo hili sasa Serikali ingelichukua liwe lake, ili kuhakikisha satellite hiyo inarushwa ambayo imetengenezwa na Watanzania chini ya Mtanzania Dkt. Amani Bura, kijana ambaye ni mbunifu na amekwenda katika jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niishukuru COSTECH ambayo ilitoa shilingi milioni 40 kwa mradi huo. Sasa miradi ya aina hiyo iwe mingi na huu wa St. Joseph University of Tanzania wa satellite uimarishwe na hawa vijana wapewe moyo na ikiwezekana watambuliwe kwamba, wamefanya jambo ambalo watu tulidhani ni suala la ndoto. Wakati Profesa Henry Mgombelo na Dkt. Mnenei wakizungumzia mambo haya miaka ya 1980, tulidhani ni ndoto lakini leo Dkt. Amani Bura na wenzake wameliwezesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile twende mbali zaidi tuongee na China, India na Urusi waje wajenge launching pad hapa ya kurusha rockets za kupeleka satellite angani. Sisi Tanzania tuna maeneo ambayo wanaweza kujenga launching pad ya rocket za kupeleka satellite. Inaweza kuwa Mafia, Kilwa na mahali popote pale. Jambo hili tulifanye haraka. Sisi shida yetu wakati mwingine tunakwenda goigoi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuongee na India, China na Urusi, ili Tanzania katika Bara la Afrika sisi ndio tuwe na mitambo ya kurusha rockets za kupeleka satellite angani na ukichukua sisi tupo karibu na Ukanda wa Ikweta na tuna anga ambalo ni angavu kwa muda mrefu na hali ya hewa ambayo haina matatizo ya mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo jambo lingine ambalo ningependa kulichangia. Ukurasa wa 45 wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi inazungumzia kuanzisha kilimo cha mimea dawa kitakachotoa malighafi kwa ajili ya kiwanda cha kuzalisha dawa zitokanazo na mimeadawa. Ukurasa wa 139 unazungumzia kuanzisha kituo kikubwa cha utafiti na uchunguzi wa mimeadawa na kuanzisha kiwanda cha kimkakati cha kuzalisha dawa zitokanazo na mimea yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wiki mbili nilikuwa nimealikwa nchini China na Chama cha Kikomunisti cha China kwa ziara ya wiki mbili ya wataalamu kutoka katika think tanks, wataalamu 27 kutoka nchi 23; katika hizo tatu ni za Afrika. Wachina walinipa heshima mimi kuwa ndio kiongozi wa wabobezi hao wote kutoka duniani katika ziara hiyo. Tumetembelea maeneo mbalimbali tumeona wanavyopanga China miaka 50 ijayo ambavyo maisha ya watu yatakuwa bora. Moja ya mambo ambayo wamewekeza ni utengenezaji wa dawa kutokana na mimeadawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maadam Ilani ya Chama Cha Mapinduzi imeeleza hilo, mimi ningeihimiza Serikali sasa; nililisema hili katika Bunge hili na narudia tena twende India na sasa twende China kile kiwanda kina zaidi ya umri wa miaka 300 kikitengeneza dawa mbalimbali za mimeadawa. Hili limo kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, tusisite kwenda kule. Wenzetu China wamekwishafika katika eneo la Mwezi ambalo dunia hatuioni toka Mungu aumbe, lakini bado hawajadharau mimeadawa yao, bado hawajadharau maarifa yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningependekeza kabisa Serikali, Wizara ya Fedha na Wizara ya Mipango tulichukue hili jambo kwa uzito mkubwa (ukurasa wa 45 na 139 wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi) ili tuweze kulitekeleza na kuliendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi sasa hapa nchini. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Profesa jielekeze kuhitimisha, dakika 10 zimekwisha. Ninakuongezea dakika tano.

MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninahitimisha kwa kusema kwamba, Serikali ichague mikoa ambayo itakuwa engine ya kusukuma uchumi wa nchi hii. Hivyo ndivyo wamefanya Wachina kwa Jimbo la Jiangsu na Fujian. Sisi hapa Tanzania Mkoa ambao unaweza kuwa ndio Mkoa wa kusukuma uchumi wa nchi hii ni Mkoa wa Morogoro. Jambo hilo walilitambua Wajerumani, Waingereza na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tuwekeze katika Mkoa wa Morogoro katika nishati ya maji mabwawa yote matatu, Kihansi, Kidatu na Mwalimu Nyerere yapo Morogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Morogoro ina kila aina ya ambayo inaweza kusukuma uchumi wa nchi hii. Pia katika Mkoa wa Morogoro wilaya ya kuwekeza zaidi ni Wilaya ya Kilosa, kwa sababu ndio Wilaya unganishi ya reli tatu; Reli ya SGR, TAZARA na Kati. Pia, ukichukua ile triangle ya Kimamba – Kilosa – Ilonga ndipo kwenye utafiti mkubwa wa kilimo. Tukiwekeza katika Wilaya ya Kilosa kujenga reli mpya kutoka Dumila kwenda Mkata Station na kuigeuza Mkata Station kuwa ndio kituo kikubwa cha machinjio ya ng’ombe ili nyama hiyo iingie katika Reli ya SGR kuja Dodoma kwenye Kiwanja cha Msalato kwenda Dar es Salaam kiwanja cha ndege, kwenda nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwekeza na kuchagua mikoa michache miwili au mitatu na kuifanya kuwa ndio engine locomotives za kusukuma uchumi wa nchi yetu hii, ninaamini tutapiga hatua kubwa. Mimi nina imani kubwa kabisa na Wizara ya Mipango na Tume ya Mipango na nipo tayari kukaa nao tuangalie jinsi ya kuja na mpangomkakati wa kimaendeleo wa Wilaya ya Kilosa, Jimbo la Kilosa na Mkoa wa Morogoro, ili Mkoa wa Morogoro iwe ndio Jiangsu na Fujian ya Tanzania, ili iweze kupiga hatua kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo naunga mkono hoja bajeti hii ipite, ili kazi ya maendeleo chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan iendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 2) wa Mwaka 2018
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima naomba nichukue fursa hii kukushukuru wewe binafsi na Bunge lako tukufu kwa kunipa nafasi ya kufanya majumuisho ya mjadala kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali yaani The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No. 2), Bill, 2018. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuongoza mjadala wa muswada huu kwa umahiri na kwa msingi huo maoni na michango iliyotolewa yameiwezesha Serikali kuboresha maudhui ya Muswada huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee napenda kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria chini ya Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa (Mbunge) kwa ushirikiano mkubwa waliotupatia wakati wa kuujadili muswada huu. Maoni na ushauri waliotupatia Kamati baada ya kusikiliza maoni ya wadau yalitusaidia kuboresha maudhui ya muswada huu kama inavyoonekana katika jedwali la marekebisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Bunge lako litaona Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Kamati ambayo ilifanya kazi ya kuchambua muswada huu kwa niaba ya Bunge hili imekubaliana na mapendekezo ya Serikali katika sehemu zote za muswada na imetoa maoni ya kuhusu namna bora ya kutekeleza masharti yanayopendekezwa katika muswada huu. Naishukuru sana Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru pia Mheshimiwa Ally Saleh (Mbunge) ambaye aitoa maoni kwa niaba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani kwenye Wizara ya Katiba na Sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu kwa ushirikiano waliotuonesha mimi pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa maandalizi na majadiliano ya muswada
huu katika hatua zote. Pia nawashukuru watendaji wa Wizara walioshiriki kwenye hatua za maandalizi na majadiliano ya muswada huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mjadala wa muswada huu jumla ya Wabunge watano wamechangia muswada huu. Kwa namna ya pekee niwashukuru Wabunge waliochangia kwa kuongea na wale waliochangia kwa njia ya maandishi ingawa sijayapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao mizuri waliyoitoa wakati wa majadiliano kwenye Kamati na hapa Bungeni. Tumepokea maoni mazuri ambayo yamelenga kuboresha muswada huu kwa ujumla maoni na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wakichangia muswada hii ni shahidi kwamba Bunge hili linatambua umuhimu wa mapendekezo ya kurekebisha sheria hizi na leo nawashukuru sana kwa kuuchangia muswada huu kwa ustaarabu bila kubagazana sana wala kuzodoana. (Makofi)

Katika michango yao Wabunge wametoa hoja mbalimbali ambazo ningependa kuzitolea ufafanuzi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ningependa kueleza kwamba Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali yaani Solicitor General sio ofisi mpya kwa maana ya kuwepo, ofisi hii ilikuwepo mpaka mwaka 1965 ambapo Bunge hili kwa Sheria ya The Solicitor General, Transfer of Duties and Powers Act of 1965, Act No.11 of 1966 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alihamisha, hakufuta, alihamisha shughuli na mamlaka ya Solicitor General kwenda kwa Attorney General na sheria hiyo ingawa ilichapwa mwaka 1966 lakini kwa mujibu wa kifungu cha kwanza ili apply retrospectively ilitoka Oktoba, 1965.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kulifahamisha Bunge lako tukufu kwamba Solicitor General wa mwisho kwa title hiyo alikuwa ni Mheshimiwa Mark Bomani na mwaka huo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alimteua Mheshimiwa Mark Bomani kuwa ndiyo Mwanasheria Mkuu wa kwanza wa Serikali Mtanzania na kwa maana hiyo aliona huyo huyo aliyekuwa Solicitor General mamlaka yake yawe transferred kwake anapokuwa Attorney General. Lakini kumsaidia kufanya kazi vizuri, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wakati huo alimpa Attorney General ma- assistant General watatu ambao pia ningependa Bunge lako Tukufu na wananchi wa Tanzania wafahamu. Alimteua Bob Makani kuwa Assistant Attorney General, pamoja na Arnold Kileo pamoja na Joseph Sinde Warioba kwa hiyo mamlaka ya Solicitor General yalikuwa transferred na sasa imependeza wakati huu na imempendeza Rais madaraka hayo yaliyokuwa yamehamishiwa kwa Attorney General sasa yarudi kwa Solicitor General mwenyewe. Kwa rejea, nendeni tena msome Act No. 11 of 1966 ndiyo mtajua kwamba ofisi hii sio mpya, ilikuwepo ila mamlaka yalihamishwa na sababu ya wakati huo kumpa Bomani mamlaka hayo yote ilikuwa ni idadi ndogo ya wanasheria wa Tanganyika waliokuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusisahau kwamba miaka hiyo hapakuwa na wanasheria wengi wa Tanganyika. Wanasheria wa kwanza wa Tanganyika waliorudi Tanganyika baada ya kusoma sheria Uingereza wa kwanza alikuwa Mkondya mwaka 1962, wa pili alikuwa Juma Mawalla mwaka 1962, wa tatu alikuwa Mark Bomani mwaka 1963 na ndiyo maana Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika wakati huo ilichukua hatua ya kuwachukua wanafunzi wake wafuatao ambao walikuwa wamemaliza degree zao Makerere ili waende kusoma sheria kuongeza idadi ya wanasheria. Sasa idadi ya wanasheria imeongezeka, mashauri yameongezeka, kwa hiyo, imeonekana ni vyema tena kuirejesha ofisi ya Solicitor General. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uteuzi wa Administrator General, imeelezwa vizuri maoni ambayo yalitolewa na Mheshimiwa Salome Wycliffe Makamba ambaye kwa mila na desturi ninatakiwa kumheshimu. Mama yangu na baba zake ni mabinamu kabisa wa damu, kwa hiyo, nitakuwa na staha kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nieleze tu kama yale aliyoyaeleza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwamba uteuzi na kama alivyoeleza Mbunge kwamba uteuzi wa Administrator General na majukumu anayoyafanya haikuwa sahihi kuwekwa chini ya Waziri. Ana sifa ya kuwa Jaji wa Mahakama Kuu kama alivyo Director of Public Prosecution.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niwakumbushe wanasheria wote, mamlaka yoyote inapokwenda nje ya mamlaka iliyopewa Mahakama zina uwezo wa kufanya marekebisho kwa rejea. Tusome kesi ya Patman Garments Industries Limited versus Tanzania Manufactures Limited ambayo ni 1981, Tanzania Law Reports kesi Namba 303, uamuzi wa Mwakasendo, Justice of Appeal. Tusome uamuzi wa Kisanga Justice of Appeal kwenye kesi ya Kukutia Ole – Pumbuni versus Attorney General, 1993 Tanzania Law Reports, Case Number 159, lakini pia tusome kesi ya Mohamed Nyaikoze versus Sophia Mussa ya mwaka 1971 ambayo iko kwenye 1971 High Court Digest Number 413, utaona iko very clear mamlaka yoyote hayatakiwi kutumikiwa arbitralily au unpropotional, lakini pia msome kesi ya Christopher Mbote Nyirabu versus Methusela Paulo Nyagaswa iliyoamuliwa pia na Court of Appeal.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkizisoma zote hizo na hasa wanasheria, mnapokuja kuchangia hapa msiache kusoma hizo kesi. Wasiokuwa wanasheria nawasamehe, lakini ambao ni wanasheria kama akina Mheshimiwa Mtolea turejee kwenye hiyo ili tuwasaidie wasiokuwa wanasheria kuelewa vizuri tafsiri ya sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa suala la Tanganyika Law Society pia limeelezwa vizuri na baadhi ya wasemaji. Ningependa nieleze tu sheria hiyo sio ad hominem, hatuleti hapa sheria ambayo ni ad hominem na wala haimlengi mtu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ningependa niwakumbushe Watanzania, Sheria ya Tanganyika Law Society ilitungwa wakati wa ukoloni na baadae kufanyiwa marekebisho. Tanganyika Law Socoety is a statutory body, is not association or society made under The Societies’ Act na inagusa taaluma ambayo ni vizuri ikasimamiwa kwa umakini kuliko taaluma nyingine yoyote ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lawyers are maidens of justice, are the dispenses of justice na ndio maana standards zinazowatawala wanasheria daima lazima ziwe juu kuliko watu wengine wote. Kwa hiyo, niwashukuru wale ambao wameeleza suala hilo kwa umakini na ni kweli kabisa Serikali inatambua upungufu uliopo katika Sheria ya Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, hivyo Serikali inaona kuna haja na umuhimu wa kufanya mashauriano ya kina na chama hicho kutokana na kuacha misingi ya kuanzishwa kwake na kujihusisha na mambo yasiyohusika na kuanzishwa kwake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nahitimisha. Moja ambalo ningependa pia kulizungumzia ni Mamlaka ya DPP ambalo nalo pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali amelieleza vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo niwashukuru tena Wabunge wote waliochangia muswada huu kwa umahiri wao, kwa umakini wao, lakini pia kwa kuchangia kwa namna ambao inastahili muswada wa namna hii kuchangiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2018
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kukushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami nichangie hoja hii. Nianze moja kwa moja kwa kuunga mkono hoja iliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia sehemu mbili tu; Sehemu ya Tano ya Muswada ambayo Serikali imeiondoa na suala la ndugu yangu Mheshimiwa Mtolea kuhusu extended jurisdiction. Nasikitika kwamba wengi waliolizungumzia suala hili sasa hivi hawamo ndani ya Bunge na lengo langu lilikuwa nitoe ufanuzi na wenyewe wakiwepo ili wasikie maelezo haya.

Mheshimiwa Spika, Mahakama ni mhimili kama ambavyo Bunge ni mhimili, kama ambavyo Executive ni mhimili. Ndiyo maana nchi nyingine za Ulaya kwa kujua Mahakama ni mhimili bajeti yake na mambo yake huwa hayapelekwi Bungeni.

Mheshimiwa Spika, Mahakama ni mhimili, Bunge ni mhimili na Executive ni mhimili. Hawa wanasheria wameondoka, nilitaka niwakumbushe lecture ya first year, Constitutions and Legal System. The Judiciary enjoys sovereignty and the Parliament enjoys sovereignty. Katika dhana nzima ya separation of powers, the Parliament can only check the Executive and not the Judiciary. Ndiyo maana nimesikitika sana, wanasheria ndani ya Bunge kuanza kuzungumzia mhimili wa Mahakama kwa lugha ya kejeli, dharau na kuibagaza Mahakama. Mkitaka kujua ugumu wa kuwa Jaji, someni Zaburi ya 15.

Ndiyo maana kama kuna kazi nilimwomba Mungu aniepushe nayo ni kuwa mhukumu. Ndiyo maana nchi za wenzetu, bajeti ya Mahakama, masuala ya Mahakama hayaletwi ndani ya Bunge, kama ambavyo Mahakama haiwezi kujadili maamuzi ya Bunge. The decision of the Speaker or Chair in the Parliament cannot be impeached or questioned in a Court of law and equally the Parliament cannot question the Chief Justice, cannot question the Judiciary. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa bahati mbaya hii lugha imeanzishwa na wanasheria na bahati mbaya hawapo. Nilitaka wawemo humu na namshukuru sana Mheshimiwa Simbachawene, kila siku hunikumbusha nisiwakumbushe marks zao darasani. Namheshimu mdogo wangu Simbachawene, sitawakumbusha marks zao darasani, ni lazima tujue. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, maadam huu ni mhimili, mhimili wa Mahakama hauwezi kuja hapa kuleta jambo, unaituma Executive, kama ambayo mambo ya Bunge Spika haji kuyaleta hapa, anaituma Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwa hiyo, Muswada huu basically ulikuwa ni Muswada wa Judiciary na mwenye mamlaka ya mwisho ubaki au utoke ni Chief Justice ambaye yeye peke yake ndiye anayemwapisha Head of State na yeye peke yake Rais akiwa impeached ndiye anayetia saini ya kumwondoa baada ya impeachment, siyo mtu wa kuja kubagazwa ndani ya ukumbi huu.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana siku Chief Justice alipoamua kuja hapa ilibidi Spika aende akae naye kwenye gallery. Spika huwa anakaa kwenye gallery? Hamkujiuliza? Why did the Speaker escort the Chief Justice here na kukaa naye kwenye gallery? Ni kwa sababu ni mhimili mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, suala hili lililetwa na mhimili. Mhimili wa Mahakama baada ya mashauriano ya muda mrefu na kuona jambo hili halieleweki, Jaji Mkuu kwa mamlaka yake aliniarifu kwamba ameshafanya majadiliano na mashauriano huko kunakohusika na kwa mamlaka yake anauondoa Muswada huu na sasa atatumia mamlaka yake aliyonayo kikatiba na kisheria kuzitangaza hizi mahakama chini ya Judicature and Application of Laws Act, section 4 na chini ya section 10 ya The Magistrate’s Court Act. Akifanya hivyo hapitii uchochoro, anatimiza mamlaka aliyonayo na mamlaka hayo anayo Chief Justice, Spika na Rais. Rais ana uwezo wa kutunga sheria peke yake, decrees, proclamation na instruments. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana mwaka 1964 Mwalimu kwa kutumia mamlaka yake ya kutunga sheria peke yake alitoa decree mbili baada ya Muungano: Moja, kutangaza Katiba ya muda ya Muungano na pili kutangaza Serikali ya Muungano, by decree. Mamlaka hayo Rais anayo au by instrument, mamlaka hayo Rais anayo au by proclamation, mamlaka hayo Rais anayo. Waraka wa Spika, circular yake inayohusu taratibu za kuendesha Bunge ni sheria. Hivyo hivyo kwa Jaji Mkuu, Waraka wake, circular yake ya kuendesha Mahakama ni sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine nataka kusema kwamba dhana hii ya Mahakama siyo mpya. The Chief Justice, our current Justice is a person inbuilt with humility. Hakustahili kuleta jambo hili hapa kwa sababu tayari lilikwishaagizwa na Waraka wa Mahakama Na.2 wa tarehe 14 Machi, 1977 na Jaji Mkuu Francis Nyalali na naomba niwasome, kupeleka Mahakama ya Wilaya na ya Hakimu Mkazi Vijijini. Nitasoma paragraph tatu tu. Ya kwanza inasema: -

“Ingawa kwa mujibu wa Fungu la 9 la Sheria ya Mahakimu (Magistrates Court Act, 1963), Mahakama ya Wilaya inayo mamlaka kimahakama katika wilaya nzima ilipo na kadhalika Mahakama ya Hakimu Mkazi inayo mamlaka ya aina hiyo katika mkoa mzima ilipo. Vikao vya Mahakama hizo kwa desturi na mazoea hufanyika mahali pamoja tu yaani kwenye Makao Makuu ya Wilaya na Mkoa, palipo na makao ya kudumu ya Mahakama hizo. Matokeo yake ni kwamba kesi zote katika kesi hizo husikilizwa siku zote kwenye makao hayo ya kudumu yaliyomo mijini na wanavijiji kuzifuata haki zao huko mijini.”

Mheshimiwa Spika, naruka nakwenda paragraph ya nne, inasema:-

“Kuna jambo lingine muhimu sana. Huu mtindo wa watu vijijini kuzifuata Mahakama hizi mijini hugharimu fedha nyingi sana katika kuwafikisha na kuwalipa posho. Kwa mujibu wa sheria, mashahidi wanaotoka karibu na kikao cha Mahakama haiwagharimu kitu. Hivyo basi, ili kupunguza gharama kubwa za utekelezaji wa haki ya kuongeza hadhi ya Mahakama na sheria kwa watu, iko haja ya kubadilisha mtindo wa watu kuzifuata Mahakama na kuweka mtindo wa Mahakama kufuata watu.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nisome ya mwisho kwa umuhimu wa maelezo ya leo, inasema:-

“Kwa utekelezaji mwema wa agizo hili kila Msajili wa Wilaya wa Mahakama Kuu pamoja na Naibu Msajili Mkuu Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, atayarishe ratiba au mpango utakaowezesha motokaa za Idara ya Mahakama zilizopo Wilayani na Mikoani zitumike kuzipeleka Mahakama kwa watu katika kila wilaya isipokuwa zile motokaa tu zilizotengenezwa kwa watumishi wengine maalum. Nakala ya ratiba hizo zitawasilishwa kwa Msajili wa Mahakama Kuu”. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili siyo jambo jipya, Waraka huu hapa. Kwa mantiki hii, kwa kweli the Chief Justice was doing a courtesy to the Parliament, he was not obliged, or compelled. When a person comes with gesture of humility, don’t abuse his sense of humility. I am indeed flabbergasted, perturbed with this kind of behavior. We can’t continue in this way. If we condone this type of behavior, we are not only demeaning the Parliament, we are demeaning the entire legal fraternity. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa fedha zilizotumika kununua haya magari na yamenunuliwa na yanakuja, yatazinduliwa na yatatumika, zilipitishwa na Bunge hili hili. Someni development budget.

Kumbukeni Vote 40, nendeni mkaangalie, fedha hiyo ni pamoja na fedha iliyojenga Law School of Tanzania, ndiyo fedha ambayo kila siku natangaza Mahakama za kujenga hapa, Mahakama za Mwanzo zinazojengwa kwa mtindo wa Moladi, za Wilaya, Mahakama Kuu, pamoja na Mobile Courts. Fedha yote ni package hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa anayesema fedha hiyo haikupita katika Bunge, akasome Vote 40 na siyo hela ya Serikali. Unajua humu ndani tuko Mawaziri ambao unatakiwa ukiwa Waziri wa Wizara hizo uwe na hekima kubwa: Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Mambo ya Ndani na wa Ulinzi na Kujenga Taifa. Mimi nikishaomba hela hapa, ni hela ya Mahakama wala siingilii. Nikishamwombea fedha Attorney General, simwingilii matumizi ya fedha yake, kwa sababu tayari Katiba inamlinda equally Jeshi la Wananchi, equally Polisi. Kwa hiyo, fedha hiyo ni fedha ambayo tumeipa Mahakama. Tukishaipa Mahakama hatuiingilii matumizi yake, wala mimi sihusiki na tenda za huko. Ni mhimili kama ambavyo Bunge likishapewa fedha kupitia kwa Waziri Mkuu, Waziri Mkuu haliingilii Bunge wala matumizi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nisisitize tena kwa Wabunge, Sehemu hii ya Tano ilikuwa ni sehemu ya mhimili wa Mahakama, mhimili wa Mahakama umeiondoa. Sitaki kudanganya Mahakama hizi Jaji Mkuu ana mamlaka ya kuzianzisha na kabla ya kwenda Australia kwenye Mkutano wa Majaji Wakuu wa Commonwealth ameniambia anazianzisha kwa mamlaka yake, zitaanza kufanya kazi kwa mamlaka yake na zitakwenda sehemu mbalimbali kwa mamlaka yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakuna anayelazimishwa kwenda kwenye hizo Mahakama. Wanasheria mko huku, ni choice of forum. Mheshimiwa Mtolea, is choice of forum. Ukiamua kwenda kwenye hizo Mahakama ujue mipaka yake ni nini. Hutaki, unataka wakili, nenda Mahakama za kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama kwa ndugu zangu wa Zanzibar, ukiona haki yako ya binadamu Zanzibar imevunjwa ukifungua shauri la kudai haki yako ya binadamu chini ya Katiba ya Zanzibar mwisho ni Mahakama Kuu ya Zanzibar. Ndivyo Katiba ya Zanzibar inavyosema. Ukitaka liende kwenye Makahama ya Rufaa, fungua chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Kwa hiyo, it is a choise of forum, hakuna anayelazimishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hatuwezi kuendelea kujadili jambo ambalo, nami nilishangaa limekujaje kwenye hotuba, kwa sababu tayari Serikali imeliondoa. Sasa kwa sababu mkamia maji, watu walikuwa wamekamia maji, waliyakamia, sasa hawakunywa. Kwa sababu hawakunywa maji waliyoyakamia, ndiyo zogo hili. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, tujikumbushe wanasheria, mwenda tezi na omo marejeo ni ngamani. Siku itakapofika ya Farao asiyemjua Yusufu, tukatoka humu, tutarudi Mahakamani, tutarudije huko? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Shule ya Sheria Tanzania wa Mwaka 2024
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kukushukuru tena kwa kunipa nafasi ya kufanya majumuisho ya mjadala kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Shule ya Sheria Tanzania wa mwaka 2024 (The Law School of Tanzania Amendment Bill, 2024).

Mheshimiwa Spika, jumla ya Waheshimiwa Wabunge watatu wamechangia Muswada huu; Mheshimiwa Olelekaita, Mbunge wa Kiteto, Mheshimiwa Seif Said Khamis Gulamali wa Manonga na Mheshimiwa Godwin Kunambi, Mbunge wa Mlimba.

Mheshimiwa Spika, maoni yaliyotolewa na wachangiaji wa Muswada huu ni muhimu sana katika kuendelea kuimarisha Shule ya Sheria Tanzania na Kamati imefanya kazi kubwa katika kuuboresha Muswada huu. Kuhusu kutamkwa kwa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, Jedwali la Marekebisho ya Serikali limefanya hivyo na ningependa kufafanua kwamba, toka mwanzo halikuwa lengo la Serikali kumwondoa. Tulisema anaweza kuwa Mjumbe yeyote wa Governing Board ya Tanganyika Law Society, tukiamini kwamba ukienda by construction Rais yumo kwenye statutory interpretation. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unapotunga sheria wakati mwingine clarity ni muhimu. Kwa hiyo, ninataka niweke wazi kabisa, Rais wa Tanganyika Law Society hakuwa ameondolewa. By construction alikuwemo lakini tumeona tuliweke wazi na ndiyo maana Schedule of Amendment sasa tumemtaja. Kwa kufanya hivyo sasa tumeongeza; badala ya kuwa Mtiva au Amidi wa Kitivo cha Sheria au Shule ya Sheria, sasa wamekuwa wawili. Mmoja atatoka kwenye Kitivo au Shule ya Chuo cha Umma na mwingine ama kwenye Kitivo au Shule ya Chuo Kikuu Binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo naomba niliweke hivi, Dean au Amidi au Mtiva wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliwekwa siyo tu kwa sababu nyingine. Sibadili msimamo lakini napenda tuelewe; katika mila, desturi na kunga za vyuo vikuu duniani, vyuo vikongwe vinapewa hiyo heshima siyo kwa sababu vingine siyo vyuo. Vyote ni vyuo lakini viko vyuo ambavyo kwa mila, desturi na kunga, kwa Kilatini vinaitwa Primus Inter Pares (First Among Equals). (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda mijadala mingine inapokihusisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitivo au sasa Shule Kuu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kifahamike kuwa chenyewe ni Primus Inter Pares (First Among Equals). Kwa kufanya hivyo hakidhalilishi kabisa vyuo vingine. Ili kuondoa tashwishwi na ili kuondoa hofu tumeona tuweke hivi lakini nimelisema hili ili tujue mila na desturi. Kwa mujibu wa Bunge hili msimamo wa Serikali ni huo, sasa tutakuwa na wawili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maoni mengine tumeyachukua yale ya jumla na naamini yatatusaidia kwa kadri tunavyoweza. Ni kweli kabisa Shule ya Sheria Tanzania tayari inatoa mafunzo kwa Paralegals kwa mujibu wa Sheria ya Msaada wa Kisheria Sura ya 21 ya Sheria za Tanzania. Tayari Shule ya Sheria inatoa mafunzo kwa Mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwenye mambo ya usuluhishi (Arbitration) na tayari pia inatoa mafunzo kwa niaba ya Tanganyika Law Society kwenye mambo ya CLE.

Mheshimiwa Spika, wazo alilolitoa Mheshimiwa Kunambi la kuongeza wigo au la kuongeza uga wa ambao watahusika na chuo hicho, kuhusisha hao wengine ambao uliwataja nalo litafikiriwa kwa sababu chuo hiki lengo lake ni hilo.

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao mizuri. Tumepokea maoni mazuri ambayo yanalenga kuboresha, siyo tu Muswada huu hata masharti mengine ya Sheria Mama. Kwa ujumla maoni na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge ni ushahidi kwamba, suala la marekebisho ya sheria kwa lengo la kuboresha utekelezaji madhubuti wa sheria zilizopo linamhusu kila mmoja wetu katika Bunge hili na ni jambo endelevu. Ndiyo maana kila mwaka Serikali inakuja na Muswada wa aina hii ili kuboresha masharti ya sheria zetu na kuzifanya ziendane na wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)