Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (4 total)

MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI aliuliza: -

Je, lini Serikali itakarabati na kufufua reli kutoka Kilosa hadi Kidatu?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi, Mbunge wa Kilosa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa vipindi tofauti imeendelea kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji katika maeneo mbalimbali nchini. Kuhusu ufufuaji wa reli kutoka Kilosa hadi Kidatu, Serikali kupitia TRC katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 imetenga jumla ya shilingi bilioni 3.4 kwa ajili ya kuanza kazi za awali za marekebisho na ufufuaji wa njia katika kipande hiki chenye urefu wa kilomita 108 ambayo imefungwa kwa muda mrefu zaidi. Reli hii inaunganisha Reli ya Kati na TAZARA eneo la Kidatu. Aidha, kwa sasa TRC imekamilisha tathmini ya kihandisi ikiwemo makadirio ya gharama ya mradi (Engineering estimates) na inaendelea na ukamilishaji wa nyaraka za zabuni kwa ajili ya kumwajiri Mkandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kumuomba Mheshimwa Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi - Mbunge, pamoja na wananchi wa Kilosa kuwa na subira wakati Serikali inaendelea na juhudi ya urejeshwaji wa njia hii ambayo ni muhimu kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo na abiria. Lengo la Serikali ni kuendelea kufanya maboresho katika maeneo yenye mahitaji ili wananchi waweze kuendelea kupata huduma za usafiri na usafirishaji.
MHE. DENNIS L. LONDO K.n.y. MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI aliuliza: -

Je, lini Serikali itaandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi wa Jimbo la Kilosa kutokana na uwepo wa migogoro ya muda mrefu ya Wakulima na Wafugaji?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Wilaya ya Kilosa umeandaliwa mwaka 2008 na utamaliza muda wake mwaka 2028. Mpango huu ndio mwongozo wa uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji vya wilaya.

Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Desemba, 2023 jumla ya vijiji 58 vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi katika Wilaya ya Kilosa kati ya vijiji 138 vilivyopo sawa na asilimia 42, ambapo kati ya vijiji hivyo, vijiji 23 vipo katika Jimbo la Kilosa na vijiji 35 vipo katika Jimbo la Mikumi. Wizara kupitia Tume itaendelea kuziwezesha mamlaka za upangaji katika uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji mbalimbali nchini vikiwemo vijiji 10 vya Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa katika mwaka wa fedha 2024/2025. Natoa rai kwa halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatenga fedha katika bajeti zake kila mwaka kwa ajili ya uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi. Ahsante.
MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Substation ya umeme katika eneo la Dumila – Kilosa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TANESCO itatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Morogoro hadi Dumila yenye urefu wa kilometa 66 na ujenzi wa kituo cha kupoza Umeme katika eneo la Magole – Dumila kupitia mpango wa Gridi Imara awamu ya pili unaotarajia kuanza mara tu baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza mwaka 2026.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zilizofanyika katika hatua za awali za mradi huu ni kufanya upembuzi yakinifu na taratibu za kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huu zinaendelea. Kukamilika kwa mradi huu kutawezesha eneo la Dumila na maeneo jirani kuwa na umeme wa uhakika na gharama za mradi ni takribani dola za Marekani milioni 39, ahsante
MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Chanzuru hadi Melela – Kilosa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Barabara ya Chanzuru - Melela – Kilosa yenye urefu wa kilometa 64.5 imekamilika. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami, ahsante.