Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (45 total)

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyokiri Mheshimiwa Waziri, sheria hii ni ya muda mrefu lakini imekuwa ikikinzana
sana na baadhi ya mila, desturi za makabila na baadhi ya sheria za dini ambazo baadhi ya makabila na sheria za dini zinatambua mtoto wa kike hata akiwa na miaka kumi akishavunja ungo ni mtu mzima. Hivyo, haioni sasa hiyo pia ilikuwa ni kichocheo kikubwa cha watoto wadogo kuolewa kabla ya wakati? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa sheria hii ya ndoa imechelewa na kusababisha ongezeko kubwa
la ndoa nyingi kuvunjika na kusababisha watoto wa mitaani kuongezeka, sasa Serikali haioni kwa kuwa Katiba bado itachukua muda, sheria hiyo iletwe hapa ili tuifanyie marekebisho?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Moja, kuhusu suala la umri wa msichana au mvulana kuoa pamoja na suala la imani, dini na desturi. Kwa wale
ambao wametabahari (wame-specialize) katika eneo hili la Sheria za Ndoa watafahamu kwamba hili ni moja ya maeneo ambayo yanahitaji umakini mkubwa sana ili kufikia muafaka wa nini kifanyike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bara la Afrika Tanzania ndiyo ilikuwa nchi ya kwanza kufanikiwa kutunga Sheria ya
Ndoa. Uganda toka mwaka 1966 chini ya Ripoti ya Kalema mpaka leo wameshindwa kuwa na Sheria ya Ndoa, kwa sababu ya mambo hayo ya mila, desturi na imani. Kenya ambao mwaka 1968 waliunda Tume ya Spry, wameweza kutunga sheria mpya ya ndoa ambayo haifanani na ya kwetu kwa maana ya kwetu ni bora zaidi baada ya Katiba yao mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii ya ndoa ilipotungwa mwaka 1971 ili kuweza kuvuka, yalikuwepo maarugu (rationale). Maarugu hayo yaliyosababisha baadhi ya vipengele ambavyo leo vina upungufu, ndiyo yaliyowezesha sheria hii kupita na moja lilikuwa ni umri wa mtoto kuolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waraka wa Serikali Na.1 wa mwaka 1969, Ibara ya 7 inaeleza kinagaubaga kwamba huo ndiyo ulikuwa umri pia uliopitishwa na Umoja wa Mataifa.
Sasa kwa kuzingatia muktadha wa leo, mazingira ya leo, ni dhahiri kabisa kwamba eneo hilo linahitaji kufanyiwa
marekebisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo tu kwa mtoto wa kike; ukisoma kifungu cha 15(2) kinaruhusu mtoto wa kike lakini
hata mtoto wa kiume kuoa chini ya umri wa miaka 14 na hiyo ilikuwa kukubaliana na mazingira ya wakati ule, kwa
sababu makundi mawili mwaka 1971 yaliikataa Sheria ya Ndoa, ilikuwa ni Baraza la Maaskofi Katoliki na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania na ilikuwa ni vyema baadhi ya maoni hayo kuyachukua ili tuvuke, lakini baadhi ya mambo hayo sasa kwa muktadha wa leo yamebadilika, tutayafanyia kazi na yanahitaji uangalifu mkubwa ili tusikwame kama
walivyokwama Uganda na Kenya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni masuala yanayohitaji afua
mbalimbali (interventions) ili kuweza kuyavusha.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ahsante kwa mwalimu wangu. Napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mwalimu wangu utakuwa unajua kwamba katika siku za karibuni kumekuwa na vitendo vingi vya utesaji na vimekuwa vikitajwa hadharani, lakini Mahakama zitapewa nguvu zaidi kama Tanzania itaridhia mikataba ya Kimataifa. Kuna mkataba mmoja muhimu wa Convention Against Torture mpaka leo Serikali inasuasua kujiunga.
Je, ni lini Serikali itaridhia mkataba huo muhimu ili Mahakama zipate nguvu zaidi kushughulikia masuala haya? Pamoja na kwamba suala hilo limetajwa katika Katiba, lakini mkataba huo ni muhimu.
Swali la pili, hadi sasa mfumo uliopo hauruhusu Ripoti ya Haki za Binadamu kujadiliwa katika Bunge, inawasilishwa lakini haijadiliwi na kwa maana hiyo, Waheshimiwa Wabunge hawana uelewa wa pamoja au uelewa mkubwa wa kujua kiasi gani madhara ya haki za binadamu na namna zinavyokiukwa kwa kulinganisha hata ripoti ya karibuni ya Amnesty International inayoonesha kwamba ukiukwaji wa haki za binadamu Tanzania ni mkubwa sana.
Je, kwa weledi wako, ushawishi wako, karama ulizopewa na Mwenyezi Mungu, ni vipi utaweza kuishawishi Serikali ili ripoti hiyo iweze kujadiliwa ili Waheshimiwa Wabunge wajue yapi yanatokezea katika nchi yao?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kama alivyoeleza, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenyewe inakataza vitendo vyovyote vya kumtesa, kumtweza na kumdhalilisha mtu. Tafsiri ya Ibara hiyo ya Katiba imewekwa wazi na Mahakama na Rufaa katika kesi ya Mbushuu Mnyaroje dhidi ya Serikali ambapo Mahakama ya Rufaa ilieleza wazi kabisa kwamba vitendo vyovyote vinavyomtesa mtu, kumtweza na kumdhalilisha, havikubaliki na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Rufaa ilikwenda mbele zaidi, ilitumia mikataba ya Kimataifa ile ambayo Tanzania imeridhia na ile ambayo haikuridhia kama msaada kwao wa kutafsiri maana ya neno au maneno utesaji, udhalilishaji na utwezaji. Kwa hali hiyo basi, maoni hayo kwamba mkataba huu dhidi ya utesaji ambao tayari misingi yake imo ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ambayo tayari Mahakama ya Rufaa ambayo ndiyo Mahakama ya mwisho ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeyakubali, yatafikiriwa ili kwa wakati muafaka jambo hilo lifanyike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Ripoti ya CHRAGG kuletwa Bungeni, maoni hayo nimeyapokea na labda kwa upya wangu nitauliza ni jinsi gani yanafikishwa, maana hata kikao kimoja cha Baraza la Mawaziri sijakaa ili nijue utaratibu wa kuyafikisha, kujadiliwa ili nikiongozwa njia ya kuku mgeni kamba kuwa imefunguka, basi nitajua jinsi ya kwenda nalo.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Na mimi naomba nimwulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa kuna wananchi ambao wanakamatwa kwa uhalifu mbalimbali, aidha wa kubandikiziwa kesi na kupata kipigo kikali sana na kufanyiwa majeraha kwenye miili yao na kufikishwa kwenye vyombo vya mahabusu bila kupatiwa huduma za afya, hamuoni kama mnakiuka haki za binadamu?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kama jambo hilo limetokea Zanzibar, pia kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, vitendo hivyo ni vitendo vya kukiuka Katiba kama vimetokea. Kwa yule viliyemtokea kama vimemtokea; moja, anayo nafasi ya kuiambia Mahakama ameteswa au amefanywa hivyo na hatua kuchukuliwa. Pia kuchukua hatua hizo kuziarifu mamlaka nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ushahidi upo kama ilivyovyoelezwa, Serikali na vyombo vyake inao utaratibu wa kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo ambavyo Katiba yenyewe imevizuia, sheria imevizuia, lakini hiyo haina maana hakuna binadamu wanaofanya hayo. Tumepewa amri kumi na Mwenyezi Mungu, mara nyingi tunazihalifu, lakini haina maana kwamba hazipo. Kwa hiyo, yakitokea hayo, tuarifiwe.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri aliyoyatoa katika swali hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kabisa kwamba baadhi ya askari polisi wetu wanashindwa kutumia sheria ambayo inawaelekeza namna ya kukamata watuhumiwa na mara nyingi sana polisi wamekuwa wakiwahukumu watuhumiwa kwa kipigo kikali sana kabla hawajawafikisha Mahakamani na wakiwafikisha Mahakamani, Mahakama zinawaona watuhumiwa kwamba hawana hatia. Kama Mahakama ilivyoamua hivi majuzi kwenye kesi ya Bwana Mdude, Nyangari na wenzake huko Mbozi.
Je, Serikali iko tayari kwa Wizara hizi mbili; ya Sheria pamoja na Mambo ya Ndani kupiga marufuku na kuchukua hatua dhahiri na za wazi kwa polisi ambao wanaidhalilisha Serikali kwa kuwaumiza raia kwa kipigo?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Selasini, naye ana heshima ya kuwa mdogo wangu kwa sababu Lamwai ni kaka yetu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna umuhimu wa Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara na Mambo ya Ndani kukaa chini na kuyapitia mambo hayo. Moja ya msisitizo ambao umekuwepo katika Wizara hizi mbili ni kuendelea kuwapa polisi mafunzo ya juu ya haki za binadamu, lakini pia jinsi ya kutumia mamlaka waliyonayo ya kukamata watu na kuzuia uhalifu kwa namna ambayo inaheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaheshimu Sheria ya Kuanzisha Jeshi la Polisi na inaheshimu sheria zilizowekwa. Kwa hiyo, tutakaa na kulijadili.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ambayo kidogo hayajatosheleza, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hamu na haja ya Waheshimiwa Wabunge wengi, toka nimeingia Bungeni hapa mwaka 2010, Wabunge wengi wanahitaji sana mabadiliko ya sheria ndogo ndogo ili mambo yaweze kuendana na wakati. Iko Sheria ya Ndoa ambayo inasema lazima mtoto awe na miaka 14 kuweza kuolewa; lakini mimi nimekuwa mwalimu muda mrefu, najua miaka 14 kwa sheria ya leo ilivyo ya elimu msingi, anakuwa bado ni mtoto yupo form two na tunasema elimu msingi mtoto atoke chekechea mpaka form four na ni elimu ya lazima. Kwa hiyo, unakuta ile sheria imepitwa na wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka juzi nilisema hapa kuhusu Sheria ya TMAA ya Madini kwamba Halmashauri kule zinapata ile ruzuku (service levy) ambayo unakuta hawajui source yake imetoka wapi kwa sababu hawashiriki katika kuangalia pato lao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ipo Sheria ya Elimu Namba 25 ya mwaka 1978, imepitwa na wakati. Sasa yote hayo nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwamba mwaka 1980 Serikali iliunda Tume kwa ajili ya kuangalia Sheria Mbalimbali na mabadiliko ili iweze kuletwa Bungeni, mpaka leo Tume hiyo ni kama vile imeshindwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, Bunge liwe na Tume yake, Serikali iwe na Tume yake ili na sisi tuonekane kweli tunatunga sheria. Maana toka nimekuja mwaka 2010 hapa sijawahi kuona Mbunge kaleta hoja binafsi hapa na ikapita. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge wana hoja binafsi nyingi, lakini wakileta hapa hakuna kinachoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iruhusu Bunge liwe na Tume ili sisi wenyewe tuanze kutunga sheria na Serikali iwe na Tume, tuzilete pamoja tuweze kujadili ili tuweze kufanya marekebisho ya sheria kadri mambo yanavyokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lini Serikali italeta hoja ya kuruhusu Bunge iwe na Tume yake binafsi?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la nyongeza la Sheria kuliruhusu Bunge kuwa na Tume yake, liko nje ya mamlaka na uwezo wangu, kwa sababu ni suala la Bunge lenyewe, lakini nitalitolea indhari, haitakuwa muafaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kazi za Tume hii, Tume hii imefanya kazi nyingi na baadhi yake zimezaa matunda. Kwa mfano, sheria ambazo zimetokana na utafiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria ya Tanzania ni pamoja na Sheria ya Upimaji wa Vinasaba wa Binadamu (The Human DNA Regulation Act No. 8 of 2009); Sheria ya Mtoto (The Law of the Child Act No. 21 of 2009); Sheria ya Makazi na Mahusiano Kazini (The Employment and Labour Relations Act No. 6 of 2004); Sheria ya Watu Wenye Ulemavu (The Disability Act No. 9 of 2010); hizi ni baadhi ya sheria tu ambazo zimetungwa kutokana na kazi ya Tume ya Kurekebisha Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa iko Sheria ya Ndoa ambayo mchakato wake unaendelea kuhusu moja, umri wa mtoto kuoa na kuolewa. Niseme leo, kuna jambo ambalo haliko sahihi; ukiangalia kuhusu umri wa miaka 14, naomba mwende muisome ile sheria, inaruhusu mtoto wa kike kuolewa na miaka 14 na mtoto wa kiume kuoa na miaka 14.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu kile mwaka 1971 kiliwekwa ili kukidhi mahitaji ya jamii mbili, Wamasai na Mabohora. Sasa ikifika wakati hali imebadilika, umuhimu huo haupo, tutalijadili. Kwa hiyo, umri wa miaka 14, someni sheria, siyo kwa msichana tu, ni kwa hata mtoto wa kiume kuruhusiwa kuoa chini ya miaka 14 kama Mahakama imeruhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakubali, mtoto wa kiume kuoa miaka 14 hajafikia umri wa kuoa; na mtoto wa kike kuolewa miaka 14 hajafikia umri wa kuolewa, lakini jambo hili linataka mwafaka wa kijamii kama ambavyo mwaka 1970 ilikuwa ni muhimu kuwaangalia Wamasai na Mabohora ambao ni sehemu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maadam mchakato unaendelea, tunaendelea kuzungumza Inshallah siku itafika, jambo hilo litapita.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ambaye ni mwalimu wangu nampongeza sana kwa majibu mazuri. Kama hawatamharibu, ataenda vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba yeye mwenyewe kama mzazi na kama mwalimu umri wa mtoto wa kiume kuoa miaka 14 hakubaliani nao na umri wa mtoto wa kike kuolewa hakubaliani nao. Sasa Serikali kwa mujibu wa Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, maana yake anataka kuniambia Serikali inataka watoto wadogo waendelee kuolewa. Kwa hiyo, watoto wa kike wasipate haki yao ya kucheza na kupata elimu na kuwa viongozi wa umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hukumu ilikuwa ni miezi sita na imeshapita na rufaa haijakatwa. Sasa naomba niulize swali, kwa nini Mheshimiwa Waziri sasa asilete Muswada Bungeni ili amri hiyo ya Mahakama ya Rufaa itekelezwe ili kuwapa haki watoto wadogo wa kike na kiume wapate haki ya kusoma na kuwa viongozi wa Taifa hili?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale wote ambao wamesoma Legal Anthropology wataelewa kwamba mambo ya mila, desturi, imani ya dini na itikadi hayataki haraka, yanataka muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo yoyote na bahati mbaya, aah, kwenye Kiswahili hakuna bahati mbaya. Kuna umuhimu sasa wa vyuo vyetu kufundisha Legal Anthropology. Huwezi kubadili mila, desturi, imani ya dini na itikadi kwa kutumia sheria peke yake tu, utakuwa unajidanganya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka katika utamaduni ambao umekuwa na mila siyo nzuri ya ukeketaji. Sheria ipo, imezuia, lakini kwa sababu bado ni suala la imani na itikadi kwa watu, leo wamelihamishia kwa watoto wachanga. Sasa nazungumza kama Profesa wa Sheria, ni hatari. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Waitara Chacha, rafiki yangu mkubwa, anajua kabisa kuna mila na desturi za anakotoka leo, mimi siafikiani nazo, lakini zinahitaji elimu, zinahitaji uelewa. Ni vigumu sana mtu anayetoka nje ya eneo hilo kuelewa kwamba mapenzi ni pamoja na kipigo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namsihi Mheshimiwa Waitara, tukae nje, tukutane. Namsihi na nimesema hivi kwa masihara haya kwa sababu ni mtu tumeshibana, hawezi kunichukulia tofauti. Tutalijadili, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutalijadili, ahsante
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kama Serikali inatenga bajeti, je, Mheshimiwa Waziri anajua kwamba Wazee wa Baraza wanakopwa na hawalipwi kwa wakati posho zao na wengine mpaka wanafikia kukutwa na umauti wakiwa wanadai pesa nyingi sana idara ya mahakama, je, hilo analitambua?
Mheshimiwa Spika, lakini la pili, kwa posho ya sh. 5,000
na uzito wa kesi wanazoamua wazee hawa hamuoni kwamba Serikali yenyewe inachochea vitendo viovu vya rushwa na mambo mengine katika mahakama zetu katika kutoa maamuzi? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ni kweli yapo malimbikizo ya posho ya Wazee wa Baraza na mpaka sasa malimbikizo hayo ni sh. 335,479,000; na tunatarajia kwa fedha ambayo imetengwa mwaka huu kuweza kulipa malimbikizo hayo ya fedha hizo wanazodai Wazee Wa Baraza.
Mheshimiwa Spika, pia tunatambua kabisa kwamba kiwango cha sh. 5,000 kwa mazingira ya leo ni kiasi kidogo ndiyo maana Serikali na Mahakama inafanya jitihada ya kuona uwezekano wa kuongeza posho hiyo, sio tu kwa Wazee wa Baraza wa Dar es Salaam bali Wazee wa Baraza wa Mahakama zote nchini.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni kweli kwamba kuna mpango wa kujenga Mahakama pale Mlimba, lakini sijui itachukua muda gani; ingawa hapo anaposema kwamba ni Mahakama, ni kibanda tu cha TAZARA wameazima na mara nyingi Mahakimu huwa hawapo muda mrefu sana. Labda kwa sababu hakuna Mahakama ambayo inatambulika rasmi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mahakama eneo la Utengule, kule alikotoka Chief Kiwanga, kwenyewe hakuna kabisa Hakimu. Kwa hiyo, watu wanapata shida sana katika kupata huduma. Je, pamoja na kuwa na mpango wa Serikali kujenga hiyo Mahakama hapo Mlimba ambapo ni Makao Makuu ya Jimbo, Serikali iko tayari sasa kupeleka Mahakimu kwenye maeneo ambayo kuna Mahakama lakini hakuna Mahakimu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Waziri huyu ameteuliwa hivi karibuni, je, yuko tayari sasa kufanya ziara kwenye Jimbo la Mlimba kuangalia hali halisi na miundombinu ili anapokwenda kwenye bajeti tuone kwamba anaikumbuka Mlimba na kuiwekea mafungu ambayo yanastahili ili wananchi wapate haki zao? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na ombi lake la kuhakikisha kuwa Mahakama za Mwanzo katika Wilaya ya Kilombero, yaani Jimbo la Mlimba na Kilombero zinapata Mahakimu ili kusogeza huduma ya utoaji haki katika eneo hilo; hasa tukizingatia kuwa Wilaya ya Kilombero kama ilivyo Wilaya ya Loliondo, Kiteto, Manyoni ni Wilaya ambazo kijiografia maeneo yake ni makubwa sana na umbali ni mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kabisa Wizara pamoja na Mahakama tutahakikisha Wilaya za aina hiyo, yaani Kilombero, Kiteto Loliondo na Manyoni, zinapata aina ya msisitizo katika kuhakikisha kwamba Mahakama zake za mwanzo zina Mahakimu wengi ili kupunguza umbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kabisa unapotoka Mlimba mpaka kwenda Kilombero kilometa 260 ni mikoa kwa sehemu nyingine. Kwa hiyo, tutalizingatia kabisa katika kuhakikisha kwamba Mahakama hizo kutegemea na Ikama iliyotolewa na Serikali, zinapata Mahakimu wa mwanzo wengi ikiwa ni pamoja na Utengule alipotoka Chifu Kiwanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la ziara ya kwenda Mlimba, naipokea kwa mikono miwili; huu ni wakati wa mavuno; kwa hiyo, nitapata mchele na pepeta; siyo kama takrima, lakini kama ukarimu wa watu wa Mlimba.(Makofi)
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Hali inayojitokeza Mlimba ni sawasawa na inavyojitokeza Jimbo la Mbagala. Niliwahi kuuliza swali la msingi, nikaambiwa kwamba mwaka huu watajenga Mahakama katika Jimbo la Mbagala, lakini tatizo ni viwanja. Tayari tumeshapata viwanja eneo la Kijichi na Chamazi. Je, ni nini tamko la Serikali kuhusu kujenga Mahakama katika Jimbo la Mbagala? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mpango wa kujenga Mahakama ya Mwanzo huko Temeke; na sasa tutahakikisha tunajua Temeke sehemu gani?Hata hivyo, nimelipokea suala la Mbagala, tutalifanyia kazi na kuona hii Mahakama ya Mwanzo ambayo imepangwa kujengwa Temeke mwaka 2017/2018 itakuwa sehemu ipi na kama siyo Mbagala, basi suala la Mbagala tutalichukulia kwa umakini unaostahili.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa Wilaya ya Mlele haina Mahakama kabisa, ni lini watajenga Mahakama ya Wilaya ya Mlele? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mipango iliyopo katika Mahakama, Wilaya ya Mlele imepangwa kujengewa Mahakama ya Wilaya mwaka 2017/2018 na nimalizie hapo hapo na Wilaya za Mpanda na Tanganyika mwaka 2019/2020. (Makofi)
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ina Mahakama moja iliyopo Lupembe na Mahakama hii jengo lake ni chakavu sana na ina nyufa nyingi, lakini pia ipo kwenye hifadhi ya barabara. Tayari wananchi wameshatoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Mahakama hii? Ahsante sana.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, maadam wameshapata ardhi na wameshachukua hatua za mwanzo, namwomba Mheshimiwa Hongoli tuonane ili nijue taratibu nyingine zinazostahili kufuatwa ili tukamilishe jambo hilo na Mahakama iweze kuanza kujengwa mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Hongoli tuonane ili nipate taarifa hizo ili nami nizifikishe kwa Mtendaji wa Mahakama halafu tuone tunafanya vipi kwa sababu tayari maandalizi ya awali ya kiwanja na naamini kina hati; kama ni hivyo, basi hatua zinazofuata zitakuwa ni rahisi zaidi.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na nina swali moja la nyongeza. Najua kwenye Wizara Mheshimiwa Waziri hana muda mrefu sana, lakini Mahakama ya Mkoa wa Manyara iliyojengwa pale Babati Mjini, Mtaa wa Negamsi ni Mahakama ya Mwanzo, ya Wilaya, mpaka ya Mkoa, kuna baadhi ya wananchi hawajalipwa fidia zao, mpaka leo wameachia eneo hilo kwa Mahakama. Ni miaka 14 sasa tangu 2004. Pamoja na ugeni wake katika Wizara, je, yuko tayari kufuatilia kwa karibu ili wananchi wale, ndugu zake, wajomba zake wapate fidia zao?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana kabisa na maoni aliyoyatoa na nitafuatilia kuona fidia ya hao watu ambao walitoa ardhi yao kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama hizo, linafanyiwa kazi haraka. Nitalifuatilia kwa karibu na najua watu wengine wanaweza kuwa wanashangaa ukaribu huo umetoka wapi? Ni kwa sababu katika mishipa yangu pia nina damu ya Kibarbaigi.(Kicheko)
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Serikali imekiri kwamba Chunya ni kati ya Wilaya kongwe nchini Tanzania, kwa kweli mwaka huu Chunya inafikisha miaka 75 ya kuwepo kama Wilaya, kwa hiyo kutokuwa na Mahakama ya Wilaya ni kama hatuitendei haki. Kwa hiyo, haya majibu ya Serikali nayashika mwaka kesho tukijaaliwa mwezi kama huu nitaionyesha Serikali jibu lake hili. Sasa naomba niulize swali moja la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuweka mkakati wa kujenga Mahakama ya Wilaya katika Wilaya ya Chunya, Serikali ina mpango gani wa kuweza kujenga Mahakama zingine kwenye Tarafa, kama Tarafa ya Kipembawe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa sasa wa Wizara, katika ujenzi wa Mahakama 15 za Wilaya na zingine Mahakama za Mwanzo na ukarabati wa baadhi ya majengo, tunakwenda awamu kwa awamu kutokana na upatikanaji wa fedha na bajeti. Hivyo, nimwondoe tu hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba pindi pale bajeti itakaporuhusu tutaangalia pia umuhimu wa kushuka ngazi za Mahakama za Mwanzo ili huduma hii iweze kuwafikia Watanzania wengi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kwa hivi tunatumia teknolojia mpya ya ujenzi wa majengo ya Mahakama kwa gharama nafuu, tunaamini kabisa katika miaka michache ijayo kutokana na upatikanaji wa fedha itakuwa ni rahisi pia kuweza kuzifikia Mahakama za Mwanzo ili wananchi wa Jimbo la Lupa na wenyewe waweze kupata huduma hii kwa ukaribu kabisa.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba kwa ruhusa yako sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika siku za karibuni kupitia Vyombo vya Habari tulimuona Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akitoa maagizo kwa Waziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kikatiba, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, je, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana Mamlaka Kikatiba kutoa maagizo kwa Waziri kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika level ya Jumuiya ya Afrika Mashariki tunashuhudia Mawaziri wakizungumzia masuala mbalimbali ambayo hayahusu Muungano, yakiwemo masuala ya kilimo, masuala ya biashara na shughuli nyingine. Je, Mheshimiwa Waziri anataka kudhihirisha sasa au anataka kutuambia kwamba, Tanzania Bara itaendelea kula kwa niaba ya Zanzibar hadi lini? Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema amesoma katika magazeti na magazeti siyo njia au sababu ya kueleza mambo hayo, ndio. Yeyote anayetumia magazeti hajui mamlaka na nafasi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maagizo ya Serikali yanatolewa kwa nyaraka, kwa barua. Sijawahi kupokea maagizo kwa gazeti au sms, napokea maagizo kwa barua au waraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayo mamlaka yote ya mambo yote yanayohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama nchi huru. Kwa hiyo, katika mambo yote yanayohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mkuu wa nchi ni mmoja tu, ni Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Yeye peke yake ndiye Amiri Jeshi, hakuna mtu mwingine yeyote wa kuyaamuru Majeshi ya Tanzania isipokuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa sababu yeye peke yake ndiye Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu na Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa Zanzibar ni Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwenye heshima na hadhi ya Urais kwa mambo yote yasiyokuwa ya Muungano yanayoihusu Zanzibar, lakini pia ni Mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nafasi yake hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia usawa wa wabia wa Muungano katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atatoka Tanzania Bara, Makamu atatoka Tanzania Zanzibar na ikiwa Rais atatoka Tanzania Zanzibar Makamu atatoka Tanzania Bara. Huo ndio usawa uliowekwa ndani ya Katiba na Ibara iko wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo basi, anayeiwakilisha nchi hii katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mambo yote ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muungano wetu ni wa aina yake ya kipekee na mara nyingi umewafanya watu wasielewe, ndiyo maana katika mambo yote duniani inayoonekana ni Jamhuri ya Muungano, lakini ndani ya Tanzania yenyewe kuna pande mbili, Tanzania Bara ambayo mambo yake yanasimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Tanzania Zanzibar ambayo mambo yake yanasimamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Ndio maana nchi hii ina Katiba mbili, Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Katiba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. (Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Sheria Namba 4 ya mwaka 1992 ya Jamhuri ya Muungano inampa mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuigawa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kimikoa, Kiwilaya na kadhalika kwa kadri anavyoona. Pia Sheria Namba 2 (E) ya mwaka 1997 ya Katiba ya Zanzibar, pia inampa mamlaka Rais wa Zanzibar, kuvigawa visiwa vya Zanzibar Kimikoa, Kiwilaya kwa kadri anavyoona. Je, ni nani aliye na mamlaka zaidi juu ya Zanzibar. Je huu siyo mgongano wa Kikatiba? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yeyote yenye Katiba zaidi ya moja, kama ilivyo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tofauti na India ambayo ni Muungano una Katiba moja. Tanzania ni sawa sawa na Ethiopia yenye Katiba 13.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili ujue ni jinsi gani unatafsiri na kuisoma Katiba ziko njia kuu tatu; unaangalia Originalism, Textualism na Purposive. Kwa maana hiyo haya ni mambo ambayo pia yamerejewa na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania. Kwa anayeangalia utaratibu wa kuziangalia Katiba mbili zinavyotekelezwa na zinapoonekana zina mgongano kazi ya kwanza ya Mahakama ni kufanya harmonization of interpretation. Hiyo nikusaidie nenda ukasome kesi ya Attorney General versus Butambala iliyoamuliwa na Mheshimiwa Jaji Samatta wa Mahakama ya Rufaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, ukitumia purposive approach hakuna mgongano kati ya Ibara hizo mbili. Maana yake Mamlaka ya Juu Residuary Power inabaki na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na mjomba wangu Profesa Kabudi na timu yake kwenye Wizara ya Katiba na Sheria, itakumbukwa mwaka mmoja na zaidi uliopita niliuliza hapa na kuiomba Wizara itusaidie tufungue jengo la Mahakama ambalo tumeshalijenga, tumelikamilisha ni zuri na la kisasa, nikaahidiwa hapa kwamba Serikali itasaidia kukamilisha utaratibu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana, sasa ni mwaka na utaratibu haujakamilika. Sasa kama jambo hili limeshindikana Serikali ituambie ili tubadilishe matumizi tufanye shughuli nyingine kwenye lile jengo la Mahakama ambalo nia yetu ilikuwa ni kusogeza huduma za kimahakama kwa watu wetu.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Nape swali hilo nilichukue nilifanyie kazi, kwa sababu amesema ni mwaka mmoja na nusu na mimi leo ni mwezi wangu wa Kumi wa Uwaziri. Naomba anisaidie tuonane nilifuatilie ili tuone jengo hilo linatumika kwa Mahakama.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Profesa mwenzangu kwa majibu mazuri na yenye msimamo. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Mahakimu wengi wa Mahakama za Mwanzo wanafanya kazi katika mazingira magumu na wanapokwenda kwenye Mahakama za vijijini huwa wanatumia usafiri wa mabasi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia usafiri kwa ajili ya usalama wao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Mahakimu wengi wanakaa katika nyumba za mtaani za kupangisha. Katika nyumba hizo huwa baadhi yao kuna watuhumiwa wanaowajua sehemu walipo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Mahakimu hao wanapata nyumba maalum kwa ajili ya usalama wao? Ahsante sana.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wanafanya kazi katika maeneo magumu hasa maeneo ya vijijini yenye matatizo ya usafiri. Kutegemea hali ya bajeti itakavyokuwa inaboreka Serikali ina mpango wa kuwapa vyombo vya usafiri, hasa Mahakimu ambao wanahudumia maeneo makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu nyumba za Mahakimu Serikali pia inatambua umuhimu wa Mahakimu kuwa na nyumba na kwa kuwa sasa imeanza na mpango wa ujenzi wa Mahakama mara baada ya zoezi la ujenzi wa Mahakama litakapokuwa limefikia mahali pazuri basi Serikali ina mpango pia wa kufikiria kuanza kujenga nyumba za Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo hasa katika maeneo ambayo yana matatizo makubwa. (Makofi)
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa Mahakimu wengi wamekuwa wanaenda shuleni kwa kujiendeleza kwa maana ya shule ya sheria kwa vitendo (Law School of Tanzania), lakini wengi wao wameachwa wakifanya kazi kwenye Mahakama za Mwanzo, Mahakama ambazo haziendani na taaluma zao, huku katika Mahakama zetu za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi kuna upungufu wa Mahakimu. Nataka kujua ni lini Serikali sasa ita-upgrade wanafunzi hawa ambao wamepitia elimu ya sheria kwa vitendo ili waweze kufanya kazi kulingana na taaluma yao. (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inawapongeza sana Mahakimu wote ambao wamechukua hatua ya kujiendeleza kielimu na pia kwenda katika Shule ya Sheria kwa Vitendo au Taasisi ya Sheria kwa Vitendo. Kwa kuzingatia hilo kila mwaka Mahakama imekuwa na mpango wa kupitia wale waliopata sifa ili waweze kupandishwa madaraja kulingana na elimu walioyoipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulivyosema ni sahihi kabisa kwamba lengo la Serikali sasa ni kuhakikisha pia kwamba Mahakimu wote wa Mahakama za mwanzo ambapo ndiko kwenye mashauri mengi wawe ni wale ambao wana Shahada za Chuo Kikuu na kwa maana hiyo baada ya miaka michache ijayo Mahakama zote za Mwanzo zitakuwa na Mahakimu ambao wana Shahada ya Kwanza ya Sheria ukizingatia kuwa huko ndiko kwenye mashauri mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo kuendelea ku-upgrade hao ambao wamejiendeleza na tunawapongeza na tunawatia moyo waendelee kufanya hivyo. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri bado nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, licha ya elimu kutolewa lakini bado kuna matatizo kuhusu haki ya ardhi. Sasa Serikali inaonaje kutoa kipindi maalum, narudia, kipindi maalum kwa muda muafaka kwenye luninga au kwenye redio kusudi elimu hii iwafikie hasa wanawake kwa wakati muafaka na kwa muda muafaka?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa sehemu kubwa ya ardhi inatumiwa sana na wanawake; kama asilimia 70 wanawake wanatumia hii ardhi hasa kwa uzalishaji mali hasa kwa kilimo. Hata hivyo wanawake hawa hawana maamuzi kuhusu ardhi hii. Je, Serikali inatoa kauli gani hasa ya kueneza elimu hii na kutokana na kwamba kwenye makabila mengine bado kuna mfumo dume ambao hauwapi ridhaa wanawake kumiliki ardhi? ahsante.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Dkt. Christine Gabriel Ishengoma kwa sababu alifanya utafiti mmoja ambao ulikuwa ni utafiti mzuri sana kuhusu mfumo wa kumiliki ardhi kwa watu wanaotoka katika makabila ambayo ni matrilineal au matriarchal. Yaani wale ursine local matriarchal wa makabila ya Pwani kama Wazaramo, Wakwere, Wakutu, Waluguru, Wanguu, Wakaguru lakini pia wale matrilineal ambao ni Wamwera, Wayao, Wamakua, Wamakonde na kuonesha ni jinsi gani katika maeneo hayo mfumo ule ambao sasa sijui ni mfumo jike, lakini umiliki wa ardhi unatoa maeneo ambayo yangesaidia watu wa mfumo dume kujifunza; na labda ndiyo maana katika historia ya Bunge letu wanawake wengi mwanzoni walioshinda Ubunge wa Majimbo walitoka maeneo hayo ya Wamwera, Wayao, Wamakua na Wamakonde. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nakubaliana naye kwamba kuna umuhimu wa kuwa na kipindi maalum cha mambo ya ardhi katika luninga na redio kwa wakati muafaka ili wanawake wengi wakisikie. Kwa hiyo, nachukua fursa hii kumuahidi kwamba nitaongea na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ili kuandaa vipindi hivi kwa wakati muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili, niseme tu kwamba tuendelee kuelimishana kuhusu umuhimu wa wanawake kumiliki ardhi hasa katika maeneo ya mfumo dume. Vilevile pia niwaombe Mahakimu na Majaji wengi waelewe umuhimu na utofauti wa umiliki wa ardhi katika maeneo ya Tanzania ya Pwani na Kusini yenye mfumo jike katika kumiliki ardhi kwa sababu hukumu zao zimekuwa hazielewi kwanini katika maeneo hayo wanawake wana sauti ya maamuzi. Na kwa maana hiyo basi tuendelee kuimarisha jambo hili ili mwisho wa siku jinsia zote mbili ziwe na haki sawa katika umiliki wa ardhi. (Makofi)
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri mafupi ya Mheshimiwa Waziri Profesa Kabudi. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri kwa kuwa Mahakama hiyo tumeisubiri kwa muda mrefu na umekiri kwamba mkandarasi amepatikana, je mkandarasi huyo anaitwa nani? Na mkandarasi huyo atajenga kwa gharama gani, kwa maana kama amepatikana atakuwa anajulikana na gharama ya ujenzi inajulikana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali dogo la pili; pale pale Kasulu kilomita kama 10 hivi kuna Mahakama ya mwanzo ya Heru Juu, na bahati nzuri mimi kule Heru Juu ndiko ninakozaliwa, Mahakama ile iliangukiwa na mti mwaka 2010 na bahati nzuri Mtendaji Mkuu wa Mahakama alifika pale akaiona. Je, hiyo Mahakama ya mwanzo ya Helujuu ni lini itakarabatiwa, maana haijengwi, inakarabatiwa, ili wananchi waendelee kupata huduma za Mahakama ya Mwanzo katika Mahakama ile? Ahsante.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandarasi ambaye atajenga Mahakama ya Wilaya ya Kasulu anaitwa Morad Tanzania Ltd. ambaye pia ndiye amejenga Mahakama ya Kibaha. Gharama ya ujenzi wa mahakama hiyo nitamuomba Mheshimwa Mbunge baadaye nimpe ili ajue ni kiasi gani. Hata hivyo haitazidi gharama ambayo imetumika kwa ile Mahakama ya Kibaha na kama umeona kitabu cha bajeti ya mwaka huu kule nyuma Mahakama ile ya Kibaha umeiona na ndivyo itakavyokuwa Mahakama ya Kasulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mahakama ya Mwanzo ya Heru Juu, kijiji ambacho na mimi nimewahi kufika na nimekipenda sana, napenda nikuarifu kwamba Mahakama ya Mwanzo ya Heru Juu itaanza kujengwa katika mwaka wa 2017/2018.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Uchakavu katika Mahakama ya Wilaya ya Kasulu ni sawa na hali ilivyo katika Mahakama ya Wilaya ya Mpanda. Jengo ni la kizamani, dogo na halikidhi mahitaji ya sasa ya Wilaya na Mkoa kwa ujumla. Ni lini Serikali itajenga jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Mpanda?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu la mjumbe, niwe na hakika, Mbunge ni Kapufi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Wilaya ya Mpanda imepangiwa kujengwa katika mwaka wa fedha 2019/2020. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kama ilivyo Mahakama ya Kasulu ni chakavu, lakini Wilaya ya Liwale ni Wilaya ambayo ina umri wa miaka 42 mpaka leo haina jengo la Mahakama. Jengo linalotumiwa ni lile jengo ambalo lilikuwa Mahakama ya Mwanzo ambalo sasa hivi limechakaa limefika mahali ambapo mafaili yanafunikwa na maturubai. Je, Mheshimiwa Waziri upo tayari kuijengea Liwale Mahakama ya Wilaya?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Wilaya ya Liwale itajengwa mwaka 2017/2018.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa Jimbo la Kavuu na Mkoa mzima wa Katavi, kutokana na jiografia yake imekaa kama umbo la pweza. Je, Serikali inafikiria nini katika Jimbo la Kavuu, Halmashauri ya Mpingwe kuanzisha Mahakama yenye hadhi ya Wilaya kutoka kwenye hadhi ya Mahakama ya Mwanzo ili kuwanusuru wananchi kwenda katika makao makuu ya Nyonga ambayo wanapita katikati ya mbuga na kuhatarisha maisha yao?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi yake nimeyasikia tutayafanyia kazi, na baada ya hapa namuomba tuonane katika ukumbi wa Bunge ili tuweze kuongea na nielewe hasa nini kifanyike kwa ajili ya eneo hilo. (Makofi)
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni kweli kwamba kuna mpango wa kujenga Mahakama pale Mlimba, lakini sijui itachukua muda gani; ingawa hapo anaposema kwamba ni Mahakama, ni kibanda tu cha TAZARA wameazima na mara nyingi Mahakimu huwa hawapo muda mrefu sana. Labda kwa sababu hakuna Mahakama ambayo inatambulika rasmi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mahakama eneo la Utengule, kule alikotoka Chief Kiwanga, kwenyewe hakuna kabisa Hakimu. Kwa hiyo, watu wanapata shida sana katika kupata huduma. Je, pamoja na kuwa na mpango wa Serikali kujenga hiyo Mahakama hapo Mlimba ambapo ni Makao Makuu ya Jimbo, Serikali iko tayari sasa kupeleka Mahakimu kwenye maeneo ambayo kuna Mahakama lakini hakuna Mahakimu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Waziri huyu ameteuliwa hivi karibuni, je, yuko tayari sasa kufanya ziara kwenye Jimbo la Mlimba kuangalia hali halisi na miundombinu ili anapokwenda kwenye bajeti tuone kwamba anaikumbuka Mlimba na kuiwekea mafungu ambayo yanastahili ili wananchi wapate haki zao? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na ombi lake la kuhakikisha kuwa Mahakama za Mwanzo katika Wilaya ya Kilombero, yaani Jimbo la Mlimba na Kilombero zinapata Mahakimu ili kusogeza huduma ya utoaji haki katika eneo hilo; hasa tukizingatia kuwa Wilaya ya Kilombero kama ilivyo Wilaya ya Loliondo, Kiteto, Manyoni ni Wilaya ambazo kijiografia maeneo yake ni makubwa sana na umbali ni mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kabisa Wizara pamoja na Mahakama tutahakikisha Wilaya za aina hiyo, yaani Kilombero, Kiteto Loliondo na Manyoni, zinapata aina ya msisitizo katika kuhakikisha kwamba Mahakama zake za mwanzo zina Mahakimu wengi ili kupunguza umbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kabisa unapotoka Mlimba mpaka kwenda Kilombero kilometa 260 ni mikoa kwa sehemu nyingine. Kwa hiyo, tutalizingatia kabisa katika kuhakikisha kwamba Mahakama hizo kutegemea na Ikama iliyotolewa na Serikali, zinapata Mahakimu wa mwanzo wengi ikiwa ni pamoja na Utengule alipotoka Chifu Kiwanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la ziara ya kwenda Mlimba, naipokea kwa mikono miwili; huu ni wakati wa mavuno; kwa hiyo, nitapata mchele na pepeta; siyo kama takrima, lakini kama ukarimu wa watu wa Mlimba. (Makofi)
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Hali inayojitokeza Mlimba ni sawasawa na inavyojitokeza Jimbo la Mbagala. Niliwahi kuuliza swali la msingi, nikaambiwa kwamba mwaka huu watajenga Mahakama katika Jimbo la Mbagala, lakini tatizo ni viwanja. Tayari tumeshapata viwanja eneo la Kijichi na Chamazi. Je, ni nini tamko la Serikali kuhusu kujenga Mahakama katika Jimbo la Mbagala? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mpango wa kujenga Mahakama ya Mwanzo huko Temeke; na sasa tutahakikisha tunajua Temeke sehemu gani? Hata hivyo, nimelipokea suala la Mbagala, tutalifanyia kazi na kuona hii Mahakama ya Mwanzo ambayo imepangwa kujengwa Temeke mwaka 2017/2018 itakuwa sehemu ipi na kama siyo Mbagala, basi suala la Mbagala tutalichukulia kwa umakini unaostahili.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa Wilaya ya Mlele haina Mahakama kabisa, ni lini watajenga Mahakama ya Wilaya ya Mlele? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mipango iliyopo katika Mahakama, Wilaya ya Mlele imepangwa kujengewa Mahakama ya Wilaya mwaka 2017/2018 na nimalizie hapo hapo na Wilaya za Mpanda na Tanganyika mwaka 2019/2020. (Makofi)
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ina Mahakama moja iliyopo Lupembe na Mahakama hii jengo lake ni chakavu sana na ina nyufa nyingi, lakini pia ipo kwenye hifadhi ya barabara. Tayari wananchi wameshatoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Mahakama hii? Ahsante sana.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, maadam wameshapata ardhi na wameshachukua hatua za mwanzo, namwomba Mheshimiwa Hongoli tuonane ili nijue taratibu nyingine zinazostahili kufuatwa ili tukamilishe jambo hilo na Mahakama iweze kuanza kujengwa mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Hongoli tuonane ili nipate taarifa hizo ili nami nizifikishe kwa Mtendaji wa Mahakama halafu tuone tunafanya vipi kwa sababu tayari maandalizi ya awali ya kiwanja na naamini kina hati; kama ni hivyo, basi hatua zinazofuata zitakuwa ni rahisi zaidi.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na nina swali moja la nyongeza. Najua kwenye Wizara Mheshimiwa Waziri hana muda mrefu sana, lakini Mahakama ya Mkoa wa Manyara iliyojengwa pale Babati Mjini, Mtaa wa Negamsi ni Mahakama ya Mwanzo, ya Wilaya, mpaka ya Mkoa, kuna baadhi ya wananchi hawajalipwa fidia zao, mpaka leo wameachia eneo hilo kwa Mahakama. Ni miaka 14 sasa tangu 2004. Pamoja na ugeni wake katika Wizara, je, yuko tayari kufuatilia kwa karibu ili wananchi wale, ndugu zake, wajomba zake wapate fidia zao?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana kabisa na maoni aliyoyatoa na nitafuatilia kuona fidia ya hao watu ambao walitoa ardhi yao kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama hizo, linafanyiwa kazi haraka. Nitalifuatilia kwa karibu na najua watu wengine wanaweza kuwa wanashangaa ukaribu huo umetoka wapi? Ni kwa sababu katika mishipa yangu pia nina damu ya Kibarbaigi. (Kicheko)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri haya ya kaka yangu Profesa Kabudi, nina maswali mawili madogo tu ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, wananchi wengi sana wanakosa haki zao, kwanza kwa kutojua kwamba wanapaswa kudai fedha zao walizolipa kama faini baada ya kushinda kesi na pili kwa sababu nakala za hukumu custodian wake ni Mahakama yenyewe.
Je, Serikali haioni kwamba kwa kutotoa maelezo kwa hawa warufani wakati rufani zao zikiwa zinasomwa kwamba wanatakiwa wafuatilie zile faini walizolipa baada ya kushinda, Serikali haioni kwamba inawadhulumu na au inaendelea kuwaadhibu kutokana na kutowarejeshea fedha zao?
Swali la pili, kwa kuwa Mahakama huwa inatoa muda maalum wa kukata rufaa na mtuhumiwa yule anapokata rufaa Mahakama inakuwa inajua. Je, ni kwa nini Mahakama inapopokea fedha zile isiziingize kwenye akaunti ya akiba kwa ajili ya kusubiri rufani itakapoamuliwa na badala yake inaingiza kwenye akaunti ya mapato na hivyo kusababisha fedha zile zinatumika, zinapohitajika inakuwa shida kupatikana?(Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, moja ni kweli inawezekana wananchi wengi hawafahamu kwamba mara baada ya kuwa wameshinda rufaa zao wana haki ya kurejeshewa faini ambayo walikuwa wamelipa. Kwa hiyo, Wizara pamoja na Mahakama tutafanya jitihada kutoa elimu na maelezo kwa wananchi kwamba mara wanapokuwa wameshinda rufaa zao za mwisho basi waweze kufuatilia malipo ya rufaa zao kwa sababu ni haki yao. (Makofi)
Kuhusu swali la pili, kwa kuwa utaratibu wa Serikali ni kwamba, faini zinachukuliwa kama maduhuli na zinakatiwa risiti ya Hazina, basi jambo hilo tutakaa na Hazina ili tuweze kuona utaratibu unaoweza kutumika ili kuhakikisha kwamba malipo ya faini yanarejeshwa kwa haraka iwezekanavyo ili wananchi ambao wamelipa fedha hizo waweze kuzipata hela zao kwa wakati. (Makofi)
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali kuwa mepesi kabisa, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Machi, 2012 Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Mizengo Pinda aliutangaza Mkoa wa Simiyu kuwa mkoa mpya, lakini mpaka ninavyoongea hivi ni takriban miaka sita mkoa huu hauna Mahakama ya Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo linalotumika kuendeshea Mahakama ya Mkoa na Wilaya ya Bariadi ni jengo ambalo ni la Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi ambaye ndio ameipangisha Mahakama.
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali, kwa kitendo cha kumpangisha Mwenyekiti wa Halmashauri ni jambo ambalo linaleta mkanganyiko na hofu kwa wananchi kwamba kwa kuchelewesha kujenga jengo la Mahakama ya Mkoa ni moja ya maslahi kati ya Mwenyekiti wa Halmashauri na Serikali. (Makofi)
Je, ni lini Serikali italeta mkakati wa haraka ili kuweza kujenga Mahakama hiyo ya Mkoa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Mkoa wa Simiyu tuna changamoto ya Mahakimu. Mkoa wa Simiyu una Hakimu mmoja ambaye anahudumia Wilaya sita, lakini pia Hakimu wa Mahakama ya Wilaya anahudumia Wilaya nne; Wilaya ya Busega, Wilaya ya Itilima, Wilaya ya…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nini mkakati wa Serikali wa kuharakisha kujenga Mahakama hizi katika Mkoa wa Simiyu? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, tayari ujenzi wa Mahakama ya Mkoa katika Mkoa wa Simiyu imeshaanza kujengwa, msingi umeshakamilika na hatua nyingine za ujenzi zinafuata. Kwa sababu tunatumia ujenzi wa aina ya moladi tuna hakika kabisa jengo hilo litakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Mahakama ya Mkoa, pia Mkoa wa Simiyu utajengewa Mahakama Kuu katika mpango huu unaoendelea. Kuhusu idadi ya Mahakimu, ni kweli kumekuwa na upungufu wa Mahakimu siyo tu kwa Mkoa wa Simiyu, bali nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mahakama iko katika utaratibu wa kuajiri Mahakimu zaidi baada ya kuwa imepata ikama kupitia Tume ya Ajira ya Mahakama na hao wakipatikana, miongoni mwa mikoa ambayo itakumbukwa na kupangiwa Mahakimu ni Simiyu.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona niulize swali dogo la nyongeza. Swali lililoulizwa namba 167 linafanana kabisa na Wilaya ya Ngara. Wilaya ya Ngara haina jengo la Mahakama, inatumia jengo la DC.
Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya Ngara? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ngara imepangiwa kujengewa Mahakama ya Wilaya katika mwaka wa 2019/2020 na pia Mahakama ya Mwanzo Lulenge mwaka 2019/2020. (Makofi)
MHE. JOSEPH MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Mahakama ya Mwanzo ya Bukindo, Bukonyo na Ukara zina hali mbaya sana kimiundombinu, achilia mbali upungufu wa watumishi. Nataka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuboresha mazingira haya ili haki ya wananchi wa Visiwa vya Ukerewe iweze kupatikana kwa haraka?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Wilaya ya Ukerewe, imepangiwa kujengewa Mahakama ya Mwanzo katika eneo la Ilangala katika mwaka wa fedha unaoanza sasa wa 2018/2019.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninayo maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa amesema lengo la chuo hiki cha mahakama ni kutoa elimu ambayo inasaidia watumishi walioko makazini waweze kuboresha ufanisi na utendaji wao; je, haoni sasa ni muhimu kwa chuo hiki pia kuanzisha kozi maalum kwa watumishi wengine wa Idara ya Mahakama wakiwemo makarani na wakalimani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Serikali imeanzisha msaada wa huduma ya msaada wa kisheria na kwa kuwa kule Lushoto nako tuna watoa msaada wa kisheria; je, haoni kwamba ni muhimu chuo hiki kikasaidia watoa msaada wa kisheria katika Halmashauri ya Lushoto kuwajengea uwezo ili waende kuwasaidia wananchi huko vijijini? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kuhusu kutoa elimu kwa ngazi ya makarani na watu wa masijala ya mahakama, nakubaliana naye kabisa kwamba wakati umefika na maadam chuo kimeweka kikosi kazi cha kupitia upya mitaala na mafunzo mbalimbali ya kozi mbalimbali katika chuo hicho, nachukua maoni yake na nitawasilisha katika kikosi kazi hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kutoa elimu kwa paralegal kwa ajili ya msaada wa kisheria pia wazo hilo ni zuri na siyo tu kwa Lushoto, nadhani kwa maeneo yote ya Mikoa ya Kaskazini ambayo yako karibu na Chuo cha Lushoto.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Swali la kwanza, majibu ya Serikali yanaonyesha kwamba uchapishaji wa mara kwa mara wa ripoti hizi ni muhimu sana, kwanza kwa best practice, openness na ease of reference.
Ni kitu gani kimefanya ripoti hizi zisichapishwe kwa miaka minne mfululizo? La kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, naiunga mkono sana Serikali kwa juhudi zake za kupunguza mlundikano wa kesi Mahakamani kwa ku-appoint Majaji wengi. Hata hivyo, kuna practice hii ya Majaji kwenda likizo mwezi Desemba na Januari ambayo ni ya historia tu. Je, Serikali haioni kwamba umefika wakati sasa wa kuwapangia Majaji likizo wakati wowote wa mwaka (Januari mpaka Desemba) badala ya kuwaweka wote kazini na kwenda likizo Desemba mpaka Januari?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, moja ya sababu iliyosababisha Law Reports kutotoka kwa wakati, kwanza ilikuwa ni mabadiliko makubwa sana ya Editorial Board. Editorial Board ya Law Reports hizi ni Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na pamekuwa na mabadiliko makubwa pale ambayo yalifanya kazi ya uhariri wa hizo kesi ichukue muda kwa sababu siyo kuzihariri tu ni pamoja na kuzichambua na kuzihariri.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tatizo hilo limeonekana na ndiyo maana tumeamua kuchapa ripoti zote nne kwa wakati mmoja na baada ya hapo Mahakama na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tumekubaliana kwamba sasa tutaanza kutoa annual reports.
Napenda tu kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari katika huu mwaka wa 2018 tumekwishaandaa asilimia 42 ya mashauri yaliyoamuliwa. Kwa hiyo, ni mategemeo yetu mwisho wa mwaka tutatoa ripoti ya mwaka 2018.
Mheshimiwa Spika, kuhusu likizo ya Majaji mwezi Desemba mpaka Januari, nikubaliane na wewe kabisa kwamba ni utamaduni wa nchi za Commonwealth kwamba Desemba na Januari Majaji wote wanakwenda likizo kwa sababu huko kwa wenzetu Uingereza mwezi Desemba na Januari kila kitu kinasimama na miezi hiyo watu hawafungwi ili wamalize Krisimasi ndiyo waende jela. Ni utamaduni tumeurithi, kwa hiyo, nitamshauri Mheshimiwa Jaji Mkuu tuuangalie kwa mukhtadha na mazingira ya Tanzania. (Makofi)
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Na mimi naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, sambamba na Mahakama nyingi kuwa chakavu na wale wazee wa Mahakama maslahi yao ni duni, ni lini Serikali itakarabati Mahakama zote na kuboresha stahiki za wazee wale?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, moja, Mahakama inatekeleza mpango wa miaka kumi wa ukarabati na ujenzi wa Mahakama zote. Baada ya Bunge leo anione ili niweze kumpa mpango wote wa miaka kumi, lakini tuonane hapa hapa Bungeni. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, pili, wazee wa Mahakama, tutaangalia maslahi yao ili yazidi kuboreshwa.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nadhani sasa umefika wakati kwa Serikali kuamua kuangalia haya mambo ya majengo ya Mahakama kwa sababu duniani kote haki ndiyo inajaaliwa, lakini kumekuwa tu na mazoea ya kujibu kwa sababu nimemuona Mheshimiwa Lameck Airo akiwa na hoja hii miaka mitatu iliyopita na ni miaka 11 sasa toka Wilaya hii ianzishwe. Sasa uhakika ni upi? Kila mwaka anauliza wanasema mwaka unaofuata, kila mwaka anauliza anaambiwa mwaka unaofuata. Sasa Waziri atuthibitishie kwamba ni kweli bajeti inayokuja hiyo Mahakama itajengwa kwa Wilaya ya Rorya.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Jimbo la Bunda kuna Mahakama ya Nyamswa, imekuwepo muda mrefu sana hiyo Mahakama ilijengwa na Mtemi Makongoro miaka hiyo mpaka leo, ni lini sasa Serikali itaenda kukarabati ile Mahakama na kuifanya iwe ya kisasa kwa ajili ya kusaidia watu wa Jimbo la Bunda? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimhakikishie Mbunge aliyeuliza swali kwamba Mahakama hiyo itajengwa katika mwaka huo wa 2019/2020 na siyo Mahakama hiyo tu bali Mahakama zote ambazo zimepangwa kujengwa katika mwaka huo kwa Mkoa wa Arusha ikiwa ni Arumeru na Ngorongoro; kwa Mkoa wa Dodoma ikiwa Bahi; kwa Mkoa wa Geita ikiwa Geita; kwa Mkoa wa Kagera ikiwa ni Muleba, Bukoba, Ngara, kwa Mkoa wa katavi ikiwa ni Mpanda na Tanganyika; na kwa Mkoa wa Kigoma ikiwa ni Uvinza na Buhigwe.
Vile vile kwa Mkoa wa Kilimanjaro ikiwa ni Same; kwa Mkoa wa Lindi ikiwa ni Nachingwea; kwa Mkoa wa Manyara, Babati, Hanang’, kwa Mkoa wa Mara ni Rorya na Butiama; kwa Mkoa wa Mbeya itakuwa Rungwe; kwa Mkoa wa Morogoro Gairo, Mvomero, Morogoro, Malinyi; kwa Mkoa wa Mtwara, Newala, Mtwara, Tandahimba; kwa Mkoa wa Mwanza, Kwimba; zote hizo ni Mahakama ambazo zitajengwa kwa mwaka wa fedha 2019/2020 na fedha yake inatokana na mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo vyanzo vya fedha vipo na bado zipo Wilaya nyingine nyingi ambazo Mahakama zitajengwa mwaka huu wa 2019/2020. Kwa hiyo ningependa nimhakikishie hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Mahakama ya Nyamswa, kabla ya Bunge hili kuanza nilifanya ziara ya Mkoa wa Mara na mahali ambapo nilipita pia ni Nyamswa. Hili ni jengo la zamani ambalo linahitaji kukarabatiwa na hilo litatafutiwa fedha katika mpango wa dharura, itakapopatikana ili Mahakama hiyo ya Nyamswa iweze kukarabatiwa. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Wilaya ya Tanganyika ni Wilaya ambayo haina Mahakama ya Wilaya, sambamba na Mahakama za Mwanzo ni zile ambazo zimechakaa na hazina watumishi wa kuzifanyia kazi hizo Mahakama. Je, ni lini Serikali itapeleka watumishi wa Mahakama za Mwanzo sambamba na Mahakama ya Wilaya na ujenzi wa Mahakama ya Wilaya? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Wilaya katika Wilaya ya Tanganyika itajengwa mwaka 2019/2020 na kama nilivyosema fedha imepatikana kwa hiyo tuna uhakika kwamba Mahakama hiyo itajengwa kwa kipindi hicho huko Tanganyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu watumishi wa Mahakama, ningependa kusema kwamba upo upungufu wa watumishi wa Mahakama ya Mwanzo 3,000 kwa sababu sasa hivi wako watumishi 6,000 na wanahitajika watumishi wengine 3,000. Wizara inaendelea kuwasiliana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupata vibali vya ajira. Mara vibali hivyo vitakapopatikana miongoni mwa Mahakama ambazo zitapewa kipaumbele ni Mahakama za Mwanzo naamini pia zitagusa Wilaya ya Tanganyika. (Makofi)
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Profesa mwenzangu. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Tarafa ya Magoma ina Kata Nane na katika Kata hizi ina Mahakama moja tu ya Mwanzo ambayo ni hiyo ya Mashewa na huu mradi umechukua muda mrefu bila kufunguliwa. Nataka Serikali iniambie ni tarehe ngapi Mahakama hii itakuwa imefunguliwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, maneno anayoelezwa hapo Mheshimiwa Waziri, naomba kama kutakuwa na uwezekano aende. Hayo anayoambiwa kwenye karatasi yanalingana na jinsi Mahakama yenyewe inavyotengenezwa kule nilipo? Nitaomba twende wote ili akahakikishe, aone kwamba imechukua muda mrefu, wanafanya kazi bila kudhibiti na tunapata usumbufu sana kwa walalamikaji na washtakiwa kwenda zaidi ya kilometa 35. (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kata ile inahitaji Mahakama zaidi na naamini katika mpango utakaofuata wa maendeleo wa miaka 10 wa Mahakama baada ya huu unaoisha 2020 kukamilika, tutatazama tena maeneo ambayo Kata zao ni kubwa na Mahakama ni chache ili katika mpango huo wa awamu ya pili wa ujenzi wa Mahakama nchini maeneo hayo yaweze kuangaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la pili la kutembelea eneo la Mashewa ili kujionea jinsi Mahakama hiyo inavyojengwa, niko radhi kufika huko na sina wasiwasi Profesa kwa sababu na mimi mjomba wangu ni fundi kama wewe, kwa hiyo nitafika na kuondoka salama. (Kicheko)
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuweza kujenga hiyo Mahakama ya Mwanzo, ni Mahakama nzuri na ya kisasa. Swali la nyongeza, kwa kuwa, Mheshimiwa Waziri amesema Mahakama ya muda itaanza kabla ya mwisho wa mwezi Juni. Je, ni lini maandalizi ya kuhamisha mafaili ya kesi zilizopo Kiomboi kwenda Iguguno yataanza ili wakati wa uzinduzi na mafaili yawepo? Tusije tukapeleka wafanyakazi halafu kukawa hamna mashauri ya kusikiliza?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Kiula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeyapokea mapendekezo yake ya kuhakikisha kuwa kabla ya mwezi Juni, 2019 mafaili yawe yamehama kutoka Mahakama ya Kiomboi kwenda Iguguno. Nami nimhakikishie kuwa, ushauri huo tumeuchukua, tutaufanyia kazi na tutahakikisha kabla ya tarehe hiyo, mafaili hayo yatakuwa yamekwishahamia katika Mahakama ambayo imepangwa.
MHE. ALHAJI ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wilaya ya Misenyi katika Mkoa wa Kagera ni wilaya iliyoanza mwaka 2007 mpaka leo ina miaka 11, lakini haina Mahakama ya Wilaya. Wilaya ile ni ya mpakani, kuna wahamiaji haramu, kuna nyarubanja kahawa, kuna matatizo mengi sana. Sasa nataka kuiuliza Serikali yangu, ni lini wilaya hii itapata haki ya kuwa na Mahakama ya Wilaya ili kuwapunguzia adha wananchi?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Alhaji Bulembo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kabisa kwamba, Wilaya ya Misenyi inayo mashauri mengi hasa yanayohusu masuala ya ardhi na mimi mwenyewe binafsi mwaka jana nilitembelea Wilaya ya Misenyi na nilifika na kuoneshwa eneo ambalo limetengwa ili kujenga Mahakama ya Wilaya ya Misenyi. Kwa hiyo, niahidi kwamba, tulikuwa tumepanga kuanza kujenga Mahakama ya Wilaya ya Misenyi mwaka 2017/2018, tunabadilisha mipango ili tuweze kuiwezesha Mahakama hiyo kuanza kujengwa mapema iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Mbunge avute subira wakati wa bajeti tunaweza kuwa na maelezo mazuri zaidi ni lini ujenzi wa Mahakama ya Misenyi utaanza na kama nilivyosema mimi mwenyewe nimefika na kweli Misenyi kuna mashauri mengi sana ya ardhi.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza. Pia namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri.

Mheshimiwa Naibu Sika, wosia wa mdomo au wa matamshi una changamoto nyingi. Kwa kuwa mazingira ya ndugu au mashuhuda huweza kubadili wosia kwa mtoa wosia, sasa hivi tuko kwenye ulimwengu wa sayansi na teknolojia, je, kwa nini Serikali isifanye utaratibu wa kurekodi wosia wa mdomo na kuhifadhi RITA ili wanawake na watoto wasipoteze haki zao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa mujibu wa gharama za RITA kutunza wosia unatunza kulingana na mali aliyonayo mweka wosia ambayo ni kuanzia Sh.5,000 hadi Sh.50,000. Je, Serikali haioni umefikia wakati wa kufanya marejeo ya gharama hizo? Ahsante sana.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa maswali ya nyongeza kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge Kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumefikia kipindi cha utaalam wa kisayansi, nakubaliana na yeyee kwamba wosia usiwe tu wa mdomo, lakini tutumie njia ya kurekodi wosia huo kutoka kwa wazazi, kutoka kwa jamii. Pia nataka kumhakikishia kwamba Ofisi za RITA ziko katika kila Wilaya kwenye Ofisi ya DAS na tutajitahidi kama Serikali kuweza kuziwezesha kuwa na mashine za kurekodi wosia.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka kumhakikishia kwamba kuna Mashirika mengi Yasiyo ya Kiserikali ambayo yamekuwa yanafanya kazi na jamii mbalimbali, kwanza kutoa elimu juu ya umuhimu wa kuweka wosia na pili jinsi ya kuandika wosia. Kwa hivyo Serikali yetu kwa kutumia sheria iliyopitishwa mwaka 2017 ya Misaada ya Sheria tutafanya pamoja ili kuhakikisha kwamba tunaboresha uandikaji wa wosia kwa wahusika.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, amesema sawa kwamba gharama kuanzia milioni 50, gharama ni Sh.5,000, kuanzia milioni 51 mpaka millioni 200 gharama za uandikishaji ni Sh.20,000. Kuanzia milioni 201 mpaka milioni 500 ni shilingi 30,000 na kuanzia hapo na kwenda juu ni shilingi 50,000. Ukitazama gharama hizi kwa kweli sio kubwa sana na kama tutapata mawazo kama uliyoyatoa hapo na kutoka kwa wananchi na kutoka kwenye ofisi zetu tunaweza tukatazama upya gharama hizi kulingana na mahitaji yatakavyojitokeza ili iwe ni motisha kwa wazazi, kwa ndugu kuweza kujiandikisha na kutumia huduma hii ya Serikali na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Ahsante.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Kila mwananchi wa Tanzania ana haki ya kulindwa na Serikali yake na sasa hivi kumetokea wimbi kubwa sana kwenye Nchi ya Afrika Kusini, wageni wanauawa, wanatekwa, wanachomwa moto na wanateswa sana. Je, Serikali ya Tanzania imechukua hatua gani kuwalinda Watanzania wote ambao wako Nchini Afrika Kusini kwa kipindi hiki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ulivyosema, suala hilo ni la Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Ni suala ambalo limekuja mahali pasipokuwa pake kwa sababu bado ipo siku ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na linaweza kuwa ni swali ambalo linajitegemea. Hata hivyo, msizoze, acha kuzoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwanza ninapenda kusema kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Afrika ya Kusini zina mahusiano mazuri sana ya kindugu na ya muda mrefu. Ndiyo maana nichukue fursa hii pia kumpongeza Cyril Ramaphosa kuchaguliwa kuwa Rais wa Afrika Kusini; na inshallah tukijaliwa tutahudhuria kuapishwa kwake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la usalama wa Watanzania siyo wa Afrika ya Kusini tu, usalama wa raia wa Tanzania popote walipo ni jukumu la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhakikisha Watanzania popote walipo wapo salama. Kwa hiyo, suala hilo linafuatiliwa na Serikali ya Afrika Kusini yenyewe imeziandikia Nchi zote za Afrika; moja, kuomba radhi kwa yale yote yanayotokea nchini mwao ambayo yanaonekana kuwa ni ya ubaguzi na yanayoifanya Afrika ya Kusini ionekane ni nchi ambayo haikumbuki ilivyosaidiwa na Waafrika wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali ya Afrika ya Kusini yenyewe imetuletea andiko kupitia Ofisi ya Ubalozi kuomba radhi kwa yale ambayo yanatokea. Nasi tunachukua hatua moja ya kuhakikisha raia wote waliko Afrika Kusini wako salama; na wale ambao watapata matatizo tumewaambia watoe ripoti kwenye balozi zetu ili hatua za kuwalinda na usalama wao kuwepo zichukuliwe. Kwa hiyo, hilo ndilo jibu.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Mahakama ya Mwanzo iliyopo Kata ya Bukundi katika Tarafa ya Nyalanja jengo lake ni chakavu sana la miaka 60. Je, Serikali haioni haja ya kutuweka kwenye mpango wa kutujengea jengo jipya au kutufanyia ukarabati? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya kwa kufuatilia kwa karibu sana ujenzi wa Mahakama katika Jimbo lake la Meatu ili wananchi wa Meatu wapate haki yao kwa ukaribu na kwa ufanisi zaidi. Nalichukua suala hilo la Mahakama ya Bukundi nalo tutaliingiza katika mpango wa ukarabati au ujenzi mpya wa Mahakama katika mwaka wa 2025/2026.
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Wananchi wa eneo la Nkaiti, Wilayani Babati wamekuwa wakifuata huduma za Mahakama kwa umbali mrefu. Je, ni lini sasa Serikali itakwenda kujenga Mahakama ya Mwanzo katika eneo hili?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba kulichukua swali hilo ili tuweze kulifanyia kazi na wenyewe pia waweze kuingizwa katika ujenzi wa Mahakama katika mwaka ujao wa fedha ili kuwafikishia huduma muhimu za upataji wa haki.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nataka kujua mpango wa Serikali kujenga Mahakama nzuri na ya kisasa katika Wilaya ya Momba ili kuepukana na changamoto za kupangapanga? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stella, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Momba ni moja ya wilaya ambazo zipo katika mpango wa ujenzi wa Mahakama mpya za wilaya na mara ya taratibu zote zitakapokuwa zimekamilika za upatikanaji wa fedha, basi Mahakama hiyo itajengwa katika Wilaya ya Momba.