Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (2 total)

MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. M. A. KABUDI: Mheshimiwa Spika, nashukiuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Napenda kujua ni lini Serikali itakarabati reli kutoka Kilosa – Mikumi hadi Kidatu, ili ianze kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Palamagamba Kabudi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge amefuatilia jambo hili kwa ukaribu. Tumetenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa reli hii ya Kilosa – Mikumi, na tutaanza rasmi mwezi wa saba mwaka huu kwa ajili ya kuihuisha tena reli hii ianze kufanya kazi kama ilivyokuwa inafanya kazi miaka ya zamani. Ahsante.
MHE. PROF. PALAMAGAMBA J. A. M. KABUDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo yanatia moyo wa kuanza kufufuliwa kwa reli hii muhimu kwa uchumi wa Tanzania. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Moja, ningependa kujua ni lini hasa mchakato wote huu utakamilika (timeframe) ili wananchi wa Kilosa lakini Wananchi wa Mikumi na wananchi wa Kilombero wajue ni lini reli hii itaanza kukarabatiwa?

Swali langu la Pili la nyongeza; kwa kuzingatia kwamba Mji wa Kilosa sasa utaunganisha reli tatu, yaani reli ya sasa ya MGR, reli ya SGR na kwa sababu kutoka Kilosa mpaka Kidatu inaanza reli ya TAZARA Kidatu mpaka Mlimba. Maana yake sasa Mji wa Kilosa utaunganisha reli tatu.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuifanya sasa Kilosa kuwa ndiyo logistic hub kubwa katika nchi yetu inayounganisha reli hizi tatu, ukichukua reli ya TAZARA ina uwezo mpaka wa kufika Zimbabwe, Zambia, Afrika ya Kusini na Namibia ili mizigo katika reli hizi iweze kuhamishwa na makontena kwa urahisi katika Mji wa Kilosa ambao sasa una stesheni kubwa mbili ya MGR na SGR na uwezo wa kuungana na reli ya TAZARA. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Profesa kwa sababu swali lake linagusa sehemu kubwa sana ya maeneo ya Mashariki na Kati mwa Tanzania. Kwa kuwa reli hii ilikuwa ni muhimu sana miaka ya nyuma kwa nchi za SADC kuanzia nchi za South Africa mpaka Uganda, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Jemedari Dkt. Samia Suluhu Hassan inao mkakati madhubuti wa kufanyia kazi jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza ni lini, jibu ni Mwaka huu wa Fedha 2023/2024, tumekwishaanza mchakato wa kimanunuzi na pengine ifikapo mwezi Februari tayari tutakuwa kwenye hatua kubwa zaidi.

Swali la pili anauliza ni upi mkakati wa Serikali wa kuifanya Kilosa kuwa logistic hub, kwa sababu tayari reli ya MGR, SGR na TAZARA zinaungana, kwanza nataka kumhakikishie kupitia SGR na MGR, tutajenga kituo kikubwa cha mizigo katika eneo hilo la Kilosa na tayari tumeshaanza upembuzi yakinifu katika kuhakikisha tunatimiza jambo hilo na hivyo kuifanya Kilosa kuwa ni Logistic hub kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameuliza hapo awali kwenye swali lake la nyongeza.