Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. William Vangimembe Lukuvi (14 total)

MHE. ABDALLAH H. MTOLEA aliuliza:-
Bunge liliridhia nyumba za NHC zilizowekwa katika kundi A ziuwe, kundi B zikarabatiwe, kundi C zijengwe upya:-
Je, kwa nini hadi leo baadhi ya nyumba zilizoagizwa kuuzwa hazijauzwa kwa wapangaji wake?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba swali hili limekuwa likiulizwa sana kwenye Bunge hili, lakini nataka nimjulishe mdogo wangu, Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea kwamba hakujawahi kutolewa uamuzi rasmi wa Serikali wala Bodi ya Shirika au halijawahi kuwepo azimio rasmi la Bunge hili kufikishwa Serikalini kutaka Serikali kufikiria kuuza nyumba hizo ulizozitaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti uliofanywa mwaka 2010 ulionesha kuwa nyumba zinazomilikiwa na National Housing zina tija kubwa kwa Shirika na Taifa, hivyo nyumba hizo zilizotajwa hazitauzwa kwa kuwa ziko kwenye maeneo yenye thamani kubwa na ni mtaji wa kuliwezesha shirika kujenga nyumba nyingi zaidi zitakazowanufaisha wananchi wote na si wapangaji wachache. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la sasa la shirika ni kuendelea kuzifanyia matengenezo nyumba zake na kuvunja nyumba kama hizo ambazo mamlaka za manispaa na halmashauri mbalimbali zimezi-condemn nyumba hizo na zile zilizochakaa vilevile ili kujenga nyumba mpya za kisasa zitakazotoa fursa zaidi kwa Watanzania wengi kuuziwa wakiwemo wapangaji hao.
MHE. PASCAL Y. HAONGA aliuliza:-
Katika Kijiji cha Isenzanya Wilayani Mbozi, shamba lenye ukubwa wa hekari 1,000 linalohodhiwa na Mzungu aitwaye Joseph Meya halijaendelezwa kwa miaka mingi sasa huku wananchi wa kijiji hicho wakiwa hawana maeneo ya kilimo:-
Je, Serikali haioni ni wakati muafaka wa kulirejesha shamba hilo kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA (K.n.y. WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pascal Yohana Haonga, Mbunge wa Jimbo la Mbozi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bwana Joseph Meier na Bi. Enala Mgala kwa pamoja wanamiliki shamba lenye ukubwa wa hekta 330.16 ambayo ni sawa na ekari 825.4 kwa Hati Na. 257 MBY LR lililopo katika Kijiji cha Isenzanya, Wilaya ya Mbozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wamiliki hawa wameendeleza kipande kidogo cha shamba hili kwa kupanda kahawa na mazao ya msimu kama mahindi na maharage. Hata hivyo, kutokana na mahitaji ya ardhi kuongezeka, wananchi wa Kijiji cha Isenzanya kwa nyakati tofauti kupitia kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi wamekuwa wakiiomba Serikali kuwapatia ardhi hiyo ili waitumie kwa kilimo. Katika kutekeleza azma hiyo, November 2015 Mkurugenzi wa Halmashauri alifanya mkutano uliojumuisha wamiliki na wanakijiji wa Kijiji cha Isenzanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mkutano ukaguzi wa shamba kufanyika mpaka sasa mazungumzo na wamiliki wa shamba yanaendelea. Aidha, Sheria ya Ardhi, Namba 4 ya Mwaka 1999 imeeleza wazi namna ya utoaji wa maeneo pale ambapo mmiliki anakiuka masharti yake. Halmashauri kupitia Afisa Ardhi Mteule inayo mamlaka ya kusimamia utekelezaji wa sheria husika. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira wakati Serikali ikiendelea na utaratibu wake.
MHE. QAMBALO W. QULWI aliuliza:-
Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kuwa ardhi yote ya Tanzania inapangwa, inapimwa na kumilikishwa kisheria kama namna mojawapo ya kuondoa migogoro hususan ya wakulima na wafugaji nchini?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Qambalo Willy Qulwi, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kupanga na kupima ardhi yote nchini kama namna mojawapo ya kupunguza migogoro baina ya watumiaji wa ardhi, hususan wakulima na wafugaji na watumiaji wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Na. 6 ya Mwaka 2007, uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ni jukumu la mamlaka ya upangaji ambazo ni halmashauri za wilaya na vijiji. Aidha, kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Mipangomiji Na. 8 ya Mwaka 2007 kinaelekeza kuwa jukumu la upangaji na uendelezaji miji lipo chini ya mamlaka za upangaji ambazo ni Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji, Wilaya na Mamlaka za Miji Midogo. Wizara yangu imekuwa ikizihamasisha na kuzijengea uwezo mamlaka za upangaji katika kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi na kuandaa mipango kabambe ambayo ndiyo dira ya kuongoza uendelezaji wa ardhi katika maeneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa ardhi yote ya Tanzania inapangwa, inapimwa na kumilikishwa kisheria. Mikakati hiyo ni pamoja na kuandaa Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha kila Kipande cha Ardhi Nchini ambayo itahusisha halmashauri zote nchini; kusajili makampuni binafsi ya kupanga na kupima ardhi yenye weledi wa kufanya kazi hizo kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo na kununua vifaa vya kisasa vya upimaji vitakavyosambazwa kwenye kanda nane za usimamizi wa ardhi kwa lengo la kuharakisha upimaji wa ardhi katika wilaya mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa suala la upimaji wa ardhi ni endelevu, natoa rai kwa halmashauri zote nchini kutenga fedha za kutosha katika bajeti zao kila mwaka kwa ajili ya kurahisisha na kuharakisha zoezi la kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi na mipango kabambe na hivyo kuwezesha kukamilika kwa azma ya kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini kwa wakati.
MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza:-
Shirika la Nyumba lilianzishwa kwa ajili ya kusaidia watumishi wa umma pamoja na wananchi wenye maisha ya chini na Mkoa wa Simiyu ni mpya ambapo tayari kuna watumishi wengi ambao hawana nyumba za kuishi ikiwemo Wilaya za Itilima na Busega:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga nyumba katika Mkoa mpya wa Simiyu pamoja na wilaya zake kwa kutumia Shirika la Nyumba?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Itilima, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Nyumba la Taifa lilipokea maombi ya ujenzi wa nyumba kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Itilima mwaka 2014. Baada ya kupokea maombi hayo shirika liliendelea na hatua nyingine za maandalizi ikiwa ni pamoja na kuandaa mpango wa kina wa matumizi ya ardhi, kuandaa michoro ya nyumba na kukadiria gharama za nyumba husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika liliingia makubaliano na Halmashauri ya Wilaya ya Itilima ya kujenga jumla ya nyumba 14 tarehe 2 Julai, 2005. Kati ya nyumba hizo 13 za Wakuu wa Idara na moja ni ya Mkurugenzi wa halmashauri. Utekelezaji mradi huu ulipangwa kuanza mara moja baada ya halmashauri kulipa kiasi cha shilingi bilioni 400 ikiwa ni awamu ya kwanza ya malipo ya nyumba husika. Hata hivyo, Halmashauri ya Itilima haijafanya malipo hayo hadi sasa na hivyo kuchelewesha kuanza kwa mrai huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzipongeza Halmashauri za Momba, Busekelo, Mlele, Mvomero, Monduli, Uyui, Kongwa na Geita na nyingine kwa ushirikiano ambao umewezesha watumishi wao kujengewa nyumba na Shirika la Nyumba la Taifa. Natoa wito kwa halmashauri zote uhitaji wa nyumba kuwasilisha maombi ya kujengewa nyumba na Shirika la Nyumba ili maombi hayo yaweze kufanyiwa kazi na kuwapatia makadirio ya gharama za ujenzi ili kazi hiyo iweze kufanywa na Shirika la Nyumba.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Mwaka 2016 Serikali kupitia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi aliahidi kuipatia Wilaya ya Mbulu Baraza la Ardhi la Wilaya:-
• Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa na hatimaye Wilaya ya Mbulu kuwa na Baraza la Ardhi la Wilaya?
• Je, ni kwa nini Serikali isipime ardhi ya wananchi wa Wilaya ya Mbulu na kuwapatia hati ili kuondoa migogoro ya ardhi?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, mwishoni mwa Julai, 2018 Wizara kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetangaza nafasi za ajira kwa ajili ya kupata Wenyeviti 20 wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya. Wenyeviti hawa ni kwa ajili ya Mabaraza 17 ambayo hayana Wenyeviti. Vilevile Wenyeviti wawili ni kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye Mabaraza katika Mikoa ambayo imeelemewa na mashauri mengi na ina Mwenyekiti mmoja kama Dar es Salaam na Mwenyekiti mmoja ni kwa ajili ya Baraza la Mbulu ambalo litafunguliwa na kuanza kufanya kazi punde taratibu za kupata watumishi wengine zitakapokamilika. Kwa ushauri wa Mkoa na Wilaya Baraza hili litakuwa Makao Makuu ya Wilaya ya Mbulu.
(b) Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila kipande cha ardhi nchini kinapimwa. Azma hii inatekelezwa kwa kupeleka huduma zote za sekta ya ardhi ikiwemo huduma za upimaji katika Ofisi za Ardhi za Kanda na Wapima wa Wilaya. Aidha, Wizara imekalimisha taratibu za kupeleka vifaa vya kisasa ambavyo vitasaidia zoezi hili la upimaji na TEHAMA katika ngazi za Kanda vyenye thamani ya shilingi bilioni 4.3 ambavyo zimekabidhiwa kwa viongozi wa Kanda wiki hii ambavyo vitasaidia sana katika kurahakisha zoezi hili la upimaji katika Wilaya zetu katika Kanda husika.
Mheshimiwa Spika, napenda kukumbusha kuwa jukumu la upimaji ni la Mamlaka ya Upangaji, hivyo, Halmashauri zote zinatakiwa kushirikiana na Wizara kupitia Afisa Ardhi, Ofisi za Ardhi za Kanda, kuhakikisha kuwa azma ya kupima kila kipande cha ardhi nchini inafikiwa.
MHE. DEVOTHA M. MINJA aliuliza:-
Serikali iliahidi kutaifisha mashamba makubwa ya uwekezaji yasiyoendelezwa:-
Je, mpaka sasa mashamba mangapi yametaifishwa?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Morogoro, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua dhidi ya wamiliki wote wa ardhi nchini ambao wameendelea kukiuka masharti ya umiliki yaliyomo katika Hati Miliki walizopewa. Kwa upande wa mashamba, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015, Disemba mpaka sasa imebatilisha miliki za mashamba 32 yenye ukubwa wa jumla ya ekari 67,393.6, Mashamba haya yapo katika Halmashauri za Kinondoni, Temeke, Kilosa, Mvomero, Morogoro, Iringa, Kibaha, Busega, Muheza, Lushoto, Bukoba na Arumeru.
Mheshimiwa Spika, mbali na mashamba hayo Wizara yangu imeendelea kupokea mapendekezo ya kubatilisha miliki za mashamba yasiyoendelezwa kutoka kwenye Halmashauri mbalimbali nchini, zikiwemo Halmashauri za Wilaya ya Tarime, Serengeti na Mkinga ambapo taratibu za ubatilishaji wa mashamba hayo zinaendelea kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa Halmashauri zote nchini ambazo zimebaini kuwepo kwa mashamba yasiyoendelezwa au mashambapori katika maeneo yao kuendelea kuwahimiza Maafisa Ardhi wa Wilaya zao kutuma ilani za ubatilisho au ilani za utelekezaji ardhi kwa wamiliki wa mashamba hayo kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi, Sura 113 na kuwasilisha mapendekezo ya kubatilisha miliki za mashamba hayo katika Wizara yangu ili taratibu za kuyabatilisha zikamilishwe kwa mujibu wa sheria.
MHE. JOSEPH L. HAULE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itafuta umiliki wa mashamba pori ya muda mrefu ya Mauzi Estate, Miyombo Estate, Sumagro Estate Kisanga Estate (Lyori Estate) yaliyopo kwenye kata za Tindiga, Masanze, Kilangali na Kisanga na kuyagawa kwa wananchi wanyonge ili waweze kupata maeneo hayo wanayoyahitaji sana ili kufanya shughuli zao mbalimbali za kujiletea maendeleo?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Leonard Haule, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuchukua hatua dhidi ya wamiliki wote wa ardhi nchini ambao wameendelea kukiuka masharti ya kumiliki ardhi ikiwemo kutoendeleza ardhi kwa mujibu wa sheria na taratibu; kuendeleza ardhi kinyume na masharti ya umiliki; na kutolipa kodi ya pango la ardhi.

Kwa upande wa mashamba, katika kipindi cha kuanzia Disemba, 2015 mpaka sasa, jumla ya milki za mashamba 45 zimebatilishwa katika maeneo mbalimbali nchini. Kwa Mkoa wa Morogoro, jumla ya mashamba 15 yamebatilishwa ambapo mashamba 10 kati ya hayo yapo katika Wilaya ya Kilosa anapotoka Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu iliunda timu ya kupitia mashamba yote yaliyobatilishwa katika Mkoa wa Morogoro pamoja na kukagua mashamba yenye sifa za kubatilishwa. Mashamba ya Mauzi Estates, Sumagro Estates, Kisanga Estates na Miyombo ni miongoni mwa mashamba ambayo timu yangu iliweza kuyakagua na hatua za ubatilisho wa milki zinaendelea. Jumla ya mashamba yaliyokaguliwa na kupendekezwa kubatilishwa ndani ya Mkoa wa Morogoro ni 23 na yote yapo katika Wilaya ya Kilosa. Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imeelekezwa kufanya taratibu za ubatilisho kwa mashamba hayo haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ambazo zimebaini kuwepo kwa mashamba yasiyoendelezwa katika maeneo yao, kuwasilisha Wizarani mapendekezo ya kubatilisha milki za mashamba husika ili taratibu za kuyabatilisha zikamilishwe kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi (Sura113).
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa Hatimiliki kwa Vijiji vilivyopimwa na kusajiliwa ambavyo bado havijapewa Hati?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya mwaka 2001, vijiji vilikuwa vinapimwa na kupatiwa Hatimiliki ambayo ilikuwa inatolewa kwa Halmashauri za Vijiji kwa kuzingatia Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1923. Baada ya Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na.5 ya Mwaka 1999 kutungwa na kuanza kutumika mwezi Mei, 2001, ilielekeza kuwa vijiji vilivyotangazwa na kusajiliwa vitapimwa na kupatiwa cheti cha ardhi ya kijiji badala ya Hatimiliki iliyokuwa inatolewa hapo awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cheti hicho hutolewa kwa mujibu wa Kifungu cha 7(7) cha Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya Mwaka 1999 ili kuipatia Halmashauri ya Kijiji majukumu ya kusimamia ardhi pamoja na kuwapatia haki ya ukaaji na utumiaji wa ardhi ya kijiji wanakijiji wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Cheti cha Ardhi ya Kijiji kinathibitisha mamlaka ya Halmashauri ya Kijiji kusimamia ardhi ya kijiji tofauti na Hatimiliki ambayo ilimaanisha Halmashauri ya Kijiji kumiliki ardhi ya kijiji na hivyo kuwanyima fursa wanakijiji kumiliki ardhi kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, cheti hiki hutolewa na Kamishina wa Ardhi kwa kijiji husika kikiwa kinaonyesha mipaka ya ardhi iliyowekwa na kukubaliwa na pande zote zinazopakana na kijiji husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi Julai, 2019 Wizara imewezesha uandaaji na utoaji wa vyeti vya ardhi ya vijiji 11,165 kati ya vijiji 12,545 vilivyosajiliwa. Serikali inaendelea na utaratibu wa utatuzi wa migogoro ya mipaka ya vijiji kwa maeneo ambayo bado hayajapatiwa vyeti ambayo haizidi asilimia 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa rai kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa zinashirikiana na wadau wengine katika kusimamia utatuzi wa migogoro ya mipaka baina ya vijiji kwa njia ya maridhiano ili taratibu za upimaji na utoaji wa vyeti wa vijiji ufanyike.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO aliuliza:-

Suala la kupima na kupanga Miji ni jukumu la Serikali:-

(a) Je, Kwanini Serikali isije na mkakati endelevu wa kupanga Miji yote ambayo imetangazwa kwenye gazeti la Serikali?

(b) Je, kwanini Serikali inatoa hoja nyepesi kwamba kazi ya kupima na kupanga Miji ni kazi ya halmashauri wakati inajua kwamba halmashauri nyingi nchini hazina nguvu ya kifedha kufanya kazi hiyo?

(c) Mji wa Kasulu ni mkongwe; je, ni lini Serikali itasaidiana na Halmashauri ya Mji wa Kasulu kupanga Mji huo?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, heshima yako.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Nicodemus Nsanzugwanko, Mbunge wa Kasulu Mjini lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza utekelezaji wa mkakati wa kupanga Miji yote ambayo imetengazwa kwenye gazeti la Serikali kwa kuandaa mipango kabambe ya Majiji, Manispaa na Miji. Aidha, Serikali imeainisha upya maeneo yote ambayo yameiva kuendelezwa kimji kwa ajili ya kuyatangaza katika gazeti la Serikali kuwa maeneo ya mipango yaani planning areas na hivi sasa maeneo ambayo tumeshayatangaza kwamba yameiva kimji mtayaona kila Mbunge ataona kwenye bajeti yangu vijiji na maeneo ambayo yametangazwa kuiva kimji yanayofika 455.

(b) Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu namba 7(1) na (5) cha Sheria ya Mipango Miji namba nanne ya Mwaka 2007, jukumu la kupanga na kupima Miji ni la mamlaka za upangaji ambazo ni Halmashauri za Majiji, Manispaa na Miji na mamlaka ya Miji midogo. Hata hivyo Serikali imeendelea kuzisaidia halmashauri kupanga na kupima Miji yao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo. Kwa mfano, katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 Serikali kupitia Wizara imetoa jumla ya shilingi bilioni 6.4 kwa halmashauri 29 kwa ajili ya upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi. Aidha, inawezesha uandaaji wa mipango kabambe Miji 18 hivi sasa kupitia program ya kuzijengea uwezo mamlaka za Miji ambayo iko chini ya Ofis ya Rais, TAMISEMI.

(c) Mheshimiwa Spika, mwaka 2008 Serikali iliandaa mpango wa muda wa kati wa matumizi ya ardhi wa Mji wa Kasulu wa miaka 10 (2008 - 2018) ambao ulikuwa unatumika kuongoza na kusimamia uendelezaji wa mji huo wa Kasulu ambako ndiko Mheshimiwa Nsanzugwanko ni Mbunge wake. Mpango huo uliisha muda wake mwaka 2018 hivyo ni jukumu la Halmashauri ya Mji wa Kasulu kuanza mchakato wa kuandaa mpango mwingine kabambe wa kuongoza na kusimamia uendelezaji wa Mji wa Kasulu.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI (K.n.y. MHE. RUTH H. MOLLEL) aliuliza:-

Migogoro ya wakulima na wafugaji imekuwa tatizo sugu katika maeneo mengi nchini pamoja na kazi kubwa ambayo imefanywa na Serikali:-

(a) Je, Serikali imetenga kiasi gani cha bajeti kwa ajili ya kupanga matumizi ya ardhi nchi nzima?

(b) Kijiji cha Matenzi Kata ya Beta Wilayani Mkuranga kina wafugaji takribani 10,000: Je, Serikali ina mkakati gani wa kupima eneo hilo kabla migogoro haijaanza?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ruth Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kwa mujibu wa Sheria ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi Na. 6 ya mwaka 2007, ni jukumu la mamlaka ya upangaji ambazo ni Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi kwa ngazi ya Taifa na Halmashauri za Wilaya na Vijiji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitenga fedha za kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kila mwaka. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 hadi 2019/2020 Serikali imetenga shilingi bilioni saba za matumizi ya kawaida na maendeleo kwa ajili ya kupanga matumizi ya ardhi na kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2018/2019 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi, iliendelea kuwezesha upangaji wa matumizi ya ardhi katika vijiji vyote vinavyozungukwa na hifadhi za misitu na hifadhi za Taifa. Kazi hii itaendelea katika mwaka wa fedha 2019/ 2020 ikijumuisha upangaji wa matumizi ya ardhi katika vijiji vyote vinavyopitiwa na Mradi wa Bomba la Mafuta pamoja na wilaya zote mpakani mwa nchi jirani. Aidha, wadau mbalimbali wa maendeleo wamekuwa wakiwezesha mamlaka za upangaji kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Uandaaji wa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi Na. 6 ya mwaka 2007, kifungu cha 33(1) kinatoa mamlaka kwa Halmashauri za vijiji kujiandalia mipango ya matumizi ya ardhi. Vilevile, vifungu vya 9(1) na 21(2)(b) vya Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya mwaka 1999 na miongozo ya kuandaa mipango ya vijiji wa mwaka 2013 vinatoa mamlaka kwa Halamshauri za Wilaya kujengea vijiji vyake uwezo na kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi pamoja na kuratibu kazi hizo.

Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi imeshajengea uwezo na kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga. Hivyo, ni jukumu la Halmashauri hiyo kuendeleza kazi ya kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji vyake kwa kutoa kipaumbele kwenye vijiji vyenye migogoro ya matumizi ya ardhi na tishio kwa hifadhi ya ardhi na mazingira, hususan hicho Kijiji ambacho Mheshimiwa amekitaja cha Beta ambacho anasema kina mifugo zaidi ya 10,000.
MHE. ZAINAB M. AMIR aliuliza:-

Wananchi wengi wamejenga makazi yao bila kuzingatia mipangomiji na matokeo yake kuvunjwa nyumba zao bila kupata fidia pindi Serikali inapoanza ujenzi unaozingatia mipangomiji:-.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia wananchi elimu stahiki ili waepukane na adha hiyo?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Mndolwa Amiri, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya kuwaelimisha wananchi kuhusu ujenzi unaozingatia mipangomiji ili kuepuka madhara mbalimbali ikiwemo kubomolewa nyumba zao bila kulipwa fidia. Mikakati hiyo ni pamoja na kutoa elimu kwa njia ya vyombo vya habari kama vile redio, luninga, magazeti, vipeperushi, machapisho mbalimbali, mitandao ya kijamii pamoja na tovuti ya Wizara.

Mheshimiwa Spika, sambamba na utoaji wa elimu kupitia vyombo vya habari, viongozi wa Wizara wamekuwa wakitumia mikutano ya hadhara katika ziara zao nchini kutoa elimu kuhusu umuhimu wa wananchi kujenga kwa kufuata utaratibu hususan katika maeneo ambayo yametangazwa kuwa ni maeneo ya kimipangomiji. Aidha, kupitia kaulimbiu ya ‘funguka kwa Waziri wa Ardhi’ Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na mambo mengine amekuwa akipokea changamoto mbalimbali kuhusu ujenzi holela mijini na kutoa elimu stahiki kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kujenga kwa kufuata utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Spika, kwa maeneo ambayo yameendelezwa bila kupangwa, Serikali imetoa fursa kwa wananchi kurasimishiwa makazi yao na kupatiwa hatimiliki. Urasimishaji makazi pamoja na mambo mengine unasaidia kuwapatia wananchi fursa ya kutumia ardhi yao kama mtaji, kutoa miundombinu ya msingi, kupunguza migogoro, kuvutia uwekezaji na kuweka huduma za kijamii. Katika maeneo mengine ambayo urasimishaji haufanyiki, utambuzi wa milki na uhakiki hufanyika na wananchi wa maeneo hayo kupewa leseni za makazi ambazo zinasaidia kuimarisha usalama wa milki na kutumika kama dhamana za mikopo kutoka katika taasisi za kifedha.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kusisitiza kuwa wananchi wazingatie sheria na taratibu za uendelezaji miji ili kujiepusha na ujenzi holela. Aidha, wananchi waepuke kujenga mijini bila kuwa na vibali vya ujenzi ili kuepuka maafa na madhara kwa mali zao.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafanya tathmini ya mashamba pori yasiyoendelezwa Mkoani Morogoro?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwezi Julai 2020 hadi Julai 2021, jumla ya mashamba 160 yamekaguliwa katika Mkoa wa Morogoro. Kati ya mashamba hayo, mashamba 123 yapo Kilosa, Kilombero (3), Mvomero (13) na Morogoro (21). Aidha, mwezi Aprili, 2021 Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan, amebatilisha umiliki wa mashamba 11 yenye ekari 24,159 kutokana na wamiliki wake kukiuka masharti ya umiliki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inafanya utaratibu wa kuyapanga na kuyapima kwa ajili ya matumizi ya wananchi, uwekezaji na ardhi ya akiba na hivi sasa wataalam wanaofanya kazi hiyo wako kwenye maeneo hayo. Kwa sasa Serikali inaendelea na ukaguzi wa mashamba mengine katika Wilaya za Morogoro, mashamba 44 na Mvomero, mashamba 86. Baada ya ukaguzi huo hatua za kisheria zitafuata kwa wamiliki watakaokiuka masharti ya umiliki.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa ukaguzi na uhakiki wa mashamba katika Mkoa wa Morogoro ni zoezi endelevu likiwa na maslahi mapana ya Taifa ya kuhakikisha kuwa tunaondoa migogoro inayojitokeza kwa kuwepo mashamba yasiyoendelezwa ipasavyo.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza agizo la Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutaka mwananchi aliyevamia ardhi ya Kijiji cha Nyarututu/Kabanga kurejesha ardhi hiyo kwa Serikali ya Kijiji ili itumike kwa faida ya wananchi?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Ardhi ya Kijiji cha Nyarututu yenye ukubwa wa ekari 130 ilipangwa na Serikali ya kijiji cha Nyarututu kwa matumizi ya Umma. Hata hivyo, kumekuwa na mgogoro unaoendelea ambapo Bwana Zacharia Kabutelana amefungua kesi dhidi ya viongozi wa kijiji akidai kwamba aliwahi kupewa eneo hilo na Serikali ya Kijiji.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Bwana Zacharia amefungua maombi Baraza la Ardhi na Nyumba katika Shauri Na. 18/2019 ambapo lipo kwenye hatua za kusikilizwa. Kutokana na eneo hilo kuwa na maslahi ya Umma, Mkurugenzi amepeleka maombi Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ili naye awe sehemu ya kesi hiyo na kuwakilishwa na Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya. Afisa Ardhi wa Halmashauri hiyo ameagizwa kufuatilia kwa karibu shauri hili ili kuhakikisha maslahi ya Serikali yanalindwa.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali italifuta shamba la Mwakinyumbi Estate lililotelekezwa kwa muda mrefu na kuwapa wananchi wa Hale na maeneo jirani ili waweze kufanya shughuli za kiuchumi?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Shamba la Mwakinyumbi Estate lilimilikishwa kwa barua ya toleo yenye Kumb Na. TRKF/76/ 65/AOM kwa muda wa miaka 99 toka tarehe 1 Aprili, 1989 kwa matumizi ya kilimo. Mmiliki alipewa masharti ya umiliki kwa mujibu wa Sheria za Ardhi. Miongoni mwa masharti hayo ni uendelezaji wa shamba na ulipaji wa kodi ya pango la ardhi kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, ukaguzi uliofanyika wa ndani umebaini kuwa shamba hilo limetelekezwa na hakuna uendelezaji wowote uliofanyika na kwa sasa shamba hilo linadaiwa kiasi cha shilingi milioni 174.73 ikiwa ni kodi pamoja na malimbikizo kwa muda wa miaka 17 kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka huu 2021. Kutokana na hali hiyo, Serikali ilianza kuchukua hatua za kisheria za kubatilisha miliki ya shamba husika kwa kutuma ilani ya kusudio la ubatilisho wa milki kwa siku tisini (90). Mmiliki hakuwasilisha utetezi wowote juu ya ilani ya ubatilisho aliyotumiwa kufuatia uvunjaji wa masharti kama ilivyoainishwa katika barua yake ya toleo. Hivyo, Serikali kwa sasa inaendelea na hatua za ubatilisho hatua zilizobaki mimi naandika barua kwa Mheshimiwa Rais kumshauri shamba hilo afute.

Mheshimiwa Spika, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, ufutaji wa mashamba yaliyotelekezwa nchini ni zoezi endelevu kwa mujibu wa sheria ikiwa na lengo la kulinda maslahi mapana ya Taifa, wananchi na wawekezaji. Hatua hii inapunguza migogoro ya matumizi ya ardhi ambayo imekuwa ikijitokeza katika maeneo mbalimbali nchini.