Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Salma Rashid Kikwete (6 total)

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima na uhai. Kabla sijaanza naomba niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya. Kwa kweli Serikali ya Awamu ya Tano ikiongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli imefanya mambo mengi na makubwa katika nyanja mbalimbali. Kila eneo kwa kweli imefanya kazi kubwa na ni kazi ambayo kwa kipindi kifupi imeweza kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi za pekee vilevile zimfikie Mheshimiwa Mama Samia Suluhu, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Kassim Majaliwa ambaye yeye ndiye Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni. Shukrani nyingine za pekee ziwafikie Waheshimiwa Mawaziri wote ambao wako kwenye Serikali hii ya Awamu ya Tano, hongereni sana kwa kazi nzuri na kubwa ambazo mnazifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nataka nizungumzie maeneo makubwa mawili; kwanza nizungumzie afya ya mama na mtoto pamoja na eneo la UKIMWI kwa ujumla wake. Kabla sijaenda kwenye maeneo hayo, niseme kwamba Serikali hii ina dhamira ya makusudi kabisa ya kuhakikisha kwamba wananchi wa Tanzania wanaishi kwa kuwa na afya bora na nzuri zaidi na ndiyo maana kwa misingi hiyo hata ukiiangalia bajeti ya mwaka 2016/2017 inatofautiana sana na bajeti ya mwaka 2017/2018. Hii ni kuuthibitishia umma kwamba Rais, Mheshimiwa Magufuli ana dhamira ya dhati kuwaweka Watanzania kwenye afya nzuri na afya bora zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie afya ya mama na mtoto. Takwimu zinaonesha kwamba katika vizazi hai 100,000 wanawake 556 hufariki dunia. Wanawake hawa 556 ambao wanafariki dunia hii takwimu ni kubwa zaidi. Hatutaki mwanamke hata mmoja afariki wakati analeta kiumbe kingine. Kwa kweli kwa misingi hiyo hili jambo ni lazima litazamwe kwa jicho la pekee kabisa ndani ya Wizara hii. Nasema haya kwa sababu kubwa za msingi. Sababu ya kwanza, takwimu hizi kwa mara ya mwisho zilikuwa 446 hivi lakini sasa zimetoka kwenye 446 zimefika kwenye 556, hapa ni lazima tupaangalie kwa namna ya pekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachana na vizazi hai, tunaingia kwenye eneo la watoto, watoto 25 kati ya 1,000 wanapoteza maisha. Watoto hawa wanaopoteza maisha lengo letu ndiyo waje kuwa watu wazima hatimaye washike mamlaka ndani ya Taifa lao. Sasa kama hivi leo tunawapoteza watoto hawa nini matokeo ya baadaye? Hili jambo ni lazima liwe kwa mapana yake kama ambavyo tumeangalia katika maeneo mengine tusiruhusu mtoto afe wakati akija duniani. Naiomba Serikali/Wizara ihakikishe kwamba wanaboresha maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine, akina mama waliambiwa waende na vifungashio hospitalini. Leo hii akina mama wanabeba vifungashio vyao na akina mama hawa ni maskini, tunafanyaje juu ya jambo hili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, narudia tena kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, hatimaye nikushukuru wewe kwa kuniona na kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia kwenye Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nawapongeza sana Mawaziri wa Wizara hii kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya. Sambamba na hilo, naomba niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano ikiongozwa na Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya. Kikubwa zaidi, niipongeze Serikali kwa kipaumbele ambacho imeweka kwenye Wizara hii ya Maji na Umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo, naomba niwape pole Watanzania wote kwa matatizo ambayo yametokea nchini kwetu na siyo matatizo mengine bali ni matatizo haya ya mvua ambayo ipo kila kona na yameweza kuathiri maisha ya wananchi wa Tanzania. Vile vile nirudie kutoa pole kwa watoto wetu ambao wamepoteza maisha wakati wakiwa kwenye harakati zao za masomo wakielekea huko kwa ajili ya kufanya mitihani ya kujipima wao wenyewe. Mwenyezi Mungu awalaze mahali pema peponi.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni uhai, maji ni utu, maji huleta heshima na ustawi kwenye familia; lakini siyo familia pekee, bali na jamii kwa ujumla. Kwa mantiki hiyo, tunaamini kwamba Tanzania ina changamoto kwenye eneo hili la maji. Kila mtu kwa njia moja au nyingine anaguswa na changamoto hii ya maji, iwe ni wa mjini iwe ni wa kijijini anaguswa na changamoto hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa zaidi changamoto hii inamgusa mwanamke, kwa sababu mwanamke ndiye mtafutaji wa maji katika familia. Kama nyumbani hakuna maji, mwanamke hawezi kukaa kitako; lazima atoke sehemu moja hadi nyingine kuhakikisha kwamba amepata maji ili maisha yaendelee.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mantiki hiyo, tunaiomba Wizara ya Maji iongeze hiki kiwango, lakini kama siyo kuongeza, tuangalie vyanzo vingine ambavyo vitatusaidia kuongeza hii bajeti yetu ya maji. Kama Waheshimiwa Wabunge wengine waliotangulia walivyosema, tuchukue ile tozo ya sh.50/= tuongeze kwenye maji hatimaye tuwe na sh.100/=. Tukiweka sh.100/= itatusaidia kuongeza bajeti yetu. Kwa mantiki hiyo basi, ile bajeti ya mwaka 2016 ndiyo irejee na kuwa bajeti ya mwaka huu kwa taratibu zake zinazohusika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naelekea kwenye Jimbo letu la Lindi Mjini. Tatizo la maji kwenye Jimbo la Lindi Mjini ni kubwa, tena sana. Lindi Mjini hakuna maji, Lindi Mjini hali ni tete. Pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuja Lindi na akasema ifikapo tarehe 3 Julai, lazima tuhakikishe kwamba maji yamepatikana. Serikali mtuambie, je, maji yatapatikana au hayatapatikana? Tunasubiri kauli ya Serikali ili mwanamke huyu tumtue mzigo.

Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Naomba mengine niyaandike kwa maandishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. SALMA J. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama ili niweze kutoa mchango wangu kwa Taifa langu. Pili, nimpongeze sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa utendaji wake mahiri wenye nia thabiti ya kuwaletea Watanzania maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nawapongeza Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kusimamia sekta ya afya hapa nchini. Nina faraja kubwa kwamba juhudi wanazofanya katika kusimamia sekta ya afya zinaonesha matunda chanya. Nina imani kubwa na utendaji wao na sina shaka kwamba sekta ya afya chini yao itaendelea kuimarika siku hadi siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuongelea jitihada katika kupambana na vifo vya wanawake na watoto. Tafiti mbalimbali zilizofanywa na taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali zimeonesha kuwa Tanzania imejitahidi kwa kiasi kikubwa katika kupambana na tatizo la vifo vya akinamama na watoto walio chini ya miaka mitano. Jitihada hizi ni matokeo ya hatua za dhati zilizochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha kuwa inaimarisha huduma mbalimbali katika sekta ya afya kama vile upatikanaji wa vifaa tiba, chanjo za watoto na huduma za kinga pamoja na tiba za magonjwa kama vile kuharisha, utapiamlo, surua, malaria na maambukizi katika mfumo wa upumuaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na jitihada zilizofanyika katika kupambana na vifo vya akinamama wajawazito na watoto walio na umri chini ya miaka mitano bado kumekuwa na changamoto mbalimbali. Changamoto hizi zimebabishwa na matatizo kama vile upatikanaji wa huduma bora za dharura za uzazi kwa akinamama hasa maeneo ya vijijini ambapo akinamama wajawazito wengi hufariki kwa kukosa huduma za upasuaji wa dharura wakati wa kujifungua; upatikanaji wa damu salama kwa akinamama ambao hupoteza damu nyingi wakati wa kujifungua; hali duni ya akinamama wajawazito hasa maeneo ya vijijini ambapo huhitajika kwenda na vifaa kama vile gloves, pamba, sabuni
na vifaa vingine vya kujifungulia jambo ambalo huwafanya akinamama wengi kuamua kujifungulia kwa wakunga wa jadi ambao baadhi yao hawakupata mafunzo ya kutoa huduma za uzazi; utoaji wa mimba usio salama na kifafa cha mimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza jitihada katika kukabiliana na vifo vya akinamama na watoto vinavyotokana na changamoto zinazojitokeza katika sekta hii ya afya ya mama na mtoto, ni vyema Serikali ikachukua hatua zifuatazo:-

(i) Kuhamasisha jamii itoe taarifa kuhusu ubora wa huduma za afya kwa mamlaka ya Serikali za Mitaa ikiwa ni pamoja na kueleza hali ya upatikanaji wa wataalam wa afya na hali ya matibabu;

(ii) Kusaidia katika kujenga uwezo wa mfumo wa afya wa wilaya ili kuwezesha katika utoaji na usimamiaji wa huduma bora za afya ya uzazi, ikiwa ni pamoja na uzuiaji wa maambukizo ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto;

(iii) Wizara ihakikishe kunakuwa na dawa za kutosha kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya VVU kwa akinamama wajawazito ili kusaidia katika kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa watoto kwa lengo la kuwezesha watoto wengi zaidi kuzaliwa wakiwa salama;

(iv) Kuhamasisha jamii na familia kuunga mkono wanawake na kuwawezesha kuwa na kauli katika masuala yanayohusu huduma zao za afya; na

(v) Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya habari itetee kwa nguvu ongezeko la uwekezaji katika huduma za afya ya wanawake katika ngazi ya Taifa na ya Serikali za Mitaa kwa kutumia vielelezo vinavyoonesha maafa na athari ya vifo vya wanawake vinavyotokana na uzazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kampeni ya kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI toka kwa akinamama kwenda kwa watoto. Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara imekuwa katika vita dhidi ya maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI hasa upande wa maambukizi ya UKIMWI toka kwa mama kwenda kwa mtoto. Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ambao wanakufa kutokana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama zao ni kubwa. Serikali inapaswa kufanya jitihada kubwa za kuhakikisha inaokoa maisha ya watoto hawa ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa la kesho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha jitihada hizi zinafanikiwa, ni vyema Serikali ikahakikisha kuwa:-

(i) Inatoa programu nyingi za uzuiaji wa maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (na kinga nyingine) zikiwemo programu za kuwasaidia wanawake kuwa na afya kwa muda mrefu kwa msaada wa lishe na matibabu;

(ii) Kutoa mafunzo kwa wanasihi wengi, wafanyakazi wa jamii wa kujitolea na wakunga wa jadi ili kuwafikia wanawake wengi na taarifa za kuaminika na ushauri kuhusu mambo ya kufanya wanapokuwa na maambukizi ya VVU. Wanawake wanaoishi na VVU wanahitaji kujua nini cha kufanya, kwa mfano, kuepuka mimba zisizotakiwa na hatari zinazoweza kutokea kwa watoto wachanga kutokana na lishe duni na maambukizi yanayohusiana na ulishaji mbadala; na

(iii) Kuboresha hali ya huduma za afya ili kuhakikisha kuwa watoto wachanga hawaambukizwi wakati wa kuzaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu. Pia nitoe pongezi kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya katika kuboresha elimu. Pamoja na hayo, niwapongeze Walimu wenzangu wote nchini Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya katika sekta hii ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, niwapongeze Walimu wenzangu, wengi wao wameweza kujiendeleza katika maeneo tofauti kuanzia ngazi za chini, hadi kufikia eneo lingine la Masters na Ph.D, hongereni sana Walimu wenzangu popote pale mlipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia suala la elimu na tunazungumzia uboreshaji wa elimu. Tunasema kwamba tunataka tuboreshe; katika maboresho haya, ninachokizungumzia, Walimu hawa wanapojiendeleza ni vema kabisa baada ya kumaliza masomo yao, wasiombe nafasi za kwenda aidha Sekondari au kwenye Vyuo. Kwa sababu tuko kwenye maboresho, msingi wowote ni muhimu sana katika jambo lolote lile. Kwa hiyo, Walimu hawa ni vema wabaki kwenye zile shule kama ni wa Msingi wamejiendeleza wamepata Diploma au wamepata Degree wabaki pale, lakini kitu kikubwa ni vema kabisa Walimu hawa waboreshewe maslahi yao kulingana na elimu yao waliyokuwanayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuje kwenye eneo la Mafunzo ya Ualimu. Nimeona Walimu wengi wamepata fursa juu ya maeneo hayo, lakini sijaona mafunzo kwa eneo la Elimu ya Awali. Sera inatuambia kwamba kwenye kila Shule ya Msingi kuwe na darasa la elimu ya awali. Sasa kama tunataka tuboreshe, ni lazima tuanzie kuboresha kwenye Elimu ya Awali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la ithibati katika ukurasa wa 19 aya ya 37. Tumeambiwa kwamba kulikuwa na suala zima la ukaguzi, Walimu 7,727 walikaguliwa; Msingi 6,413, Sekondari 1,314. Ni vema kabisa, lakini lengo ilikuwa kukaguliwa Walimu 10,818. Hawa ni baadhi tu ya waliokaguliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukija kwenye eneo hili, ili tuweze kuboresha elimu yetu hapa nchini Tanzania, hili eneo la ukaguzi ni lazima lipewe kipaumbele. Kuwe na pesa ya kutosha na kuwe na vitendea kazi. Ili kuboresha eneo hili, ni lazima Walimu wakaguliwe mara kwa mara. Unaweza ukakuta ndani ya miaka; nazungumza haya kwa sababu nina uzoefu juu ya eneo hili, mimi ni Mwalimu kwa taaluma. Unaweza ukakuta zaidi ya miaka miwili au mitatu Mwalimu hajakaguliwa. Sasa unategemea ubora wa elimu hapa utakujaje kama hakuna mtu wa kumsimamia huyu Mwalimu? Kwa hiyo, hili eneo ni lazima lipewe kipaumbele cha namna ya pekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyazungumza haya, napenda nizungumzie eneo la Shule ya Lindi Sekondari. Nimeona maeneo mengi wameboreshewa, wameambiwa itaboreshwa hili, itatengenezwa Shule hii, itafanya hivi, lakini Sekondari ya Lindi ilipata tatizo la kuungua moto; na moto ulikuwa mkubwa na ulipoteza karibu madarasa yasiyopungua sita pamoja na eneo la Mikutano. Serikali hapa mnatuambiaje juu ya shule hii iliyoko Mkoa wa Lindi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la mimba. Suala la mimba ni tatizo na suala la utoro ni tatizo. Sisi kama wanawake tunawapenda sana na ni lengo letu Waheshimiwa Wabunge wanawake kuwatetea watoto wa kike na mwanamke yeyote yule ambaye anaomba nafasi ya uongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala hili la mimba, hasa mimba za utotoni, sikubaliani na kwamba watoto wakipata mimba warudi tena shuleni. Hili sikubaliani nalo hata kidogo! Sababu za kutokukubaliana nazo ni hizi zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunazungumzia suala la mila, desturi, utamaduni na mazingira…(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na dini. Hakuna dini yoyote inayomruhusu mtoto wa kike kupata mimba kabla ya wakati. Biblia inasema na Quran inasema. Tunapofanya mambo yetu ya msingi tuangalie vilevile mambo yanayohusu imani zetu za dini. Suala la mtoto kurudi shuleni, tutafute njia nyingine mbadala. Sisi kama Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuna Kanuni zetu na ndizo tunazozifuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika kwenye suala la mimba, sheria inayofuata hapa mtoto akipata mimba asirudi shuleni. Kama hapa ingekuwa sisi kama Wabunge hatuna sheria na kanuni, ingekuwa tunafanya mambo kila mtu na jambo lake, lakini sheria zinatubana. Nataka kwa hilo sheria zibane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka sheria ibane. Mtoto akipata ujazito asirudi shuleni, atafutiwe njia nyingine ya kuweza kumsaidia mtoto huyu.

TAARIFA...

MHE. SALMA R. KIKWETE: Nashukuru sana kwa kuniunga mkono. Naomba wanawake wote waniunge mkono na wanaume vilevile waniunge mkono. (Makofi)

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivi? Kama hivyo ambavyo sisi tunawatetea...

MHE. SALMA R. KIKWETE: Tuwatetee katika mazingira…

TAARIFA...

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Taarifa hiyo siikubali, naikataa…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila mpangilio)

MHE. SALMA R. KIKWETE: …pamoja na kwamba kwamba watoto hawa wanapata mimba katika umri mdogo; lakini ni lazima tuwatengenezee mazingira wezeshi. Mazingira wezeshi tukisema warudi shuleni watoto hawa, ina maana wengi watapata mimba.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila mpangilio)

MHE. SALMA R. KIKWETE: Wengi watapata mimba katika umri mdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu. Sambamba na hilo, nitoe pongezi zangu za dhati kabisa kwa Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya. Kazi hizi nzuri zinazofanywa tukiziainisha hapa ni nyingi na kwa wingi wake huo kumekuwa na mafanikio makubwa sana ndani ya kipindi chake cha uongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, niwapongeze Mawaziri wetu wa Wizara ya Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mpango na Naibu wake kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya. Kwa ujumla bajeti hii ya Serikali imegusa kila sehemu yaani bajeti ya wananchi. Wananchi wamepunguziwa kwa kiasi kikubwa sana na bajeti inayoonyesha muelekeo na mwelekeo huu ni ushindi wa mwaka 2020 na hatimaye kuelekea kule mbele ya safari 2025, ongezeni hizo juhudi ili tufike 2025, na hatimaye tuzidi kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kwenye maeneo kama mawili/matatu hivi. Eneo la kwanza, wakati Waziri anasoma bajeti ya Wizara ya Fedha alielezea suala la kinu cha kuchakata gesi pale Lindi ambacho kinu hiki kiko eneo linaitwa Likong’o. Baada ya hapo kwa kweli nilipiga sana makofi na nilipiga hili benchi nafikiri watu wengi walisikia. Msingi wangu mkubwa ni kwamba kinu kile kikipelekwa pale matokeo yake tunazungumzia hii nchi ni nchi ya viwanda, na ikiwa ni nchi ya viwanda na wananchi wa Lindi wale watafaidika na kauli mbiu hii ya Awamu ya Tano kwamba iwe ni nchi ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nini limetokea? Wakati anaisoma hii bajeti ya Serikali ambayo ndio inayotoa mwelekeo nini kinafanyika ndani ya Taifa, hakukuwa na jambo lolote lililojitokeza juu ya kinu kile na wananchi wa Lindi wanasubiri. Hata kama sio leo au kesho, lakini wapewe mwelekeo ni nini kinafanyika. Kikubwa zaidi hii ni gesi na gesi itaongeza uchumi wa Lindi, kiwanda kile kikijengwa Lindi kama Lindi hakuna kiwanda hata kimoja. Wananchi wa Lindi ni maskini lakini sio maskini kwa sababu hakuna rasilimali, ni kwa sababu mimi naamini wakati ulikuwa haujafika na sasa wakati umefika na wananchi wale wa Lindi kufurahia matunda ya nchi yao. Naomba atakapokuja Mheshimiwa Waziri anipe mwelekeo nini hatima ya kinu kile cha kuchakata gesi ndani ya Mkoa wetu wa Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maji. Nilizungumzia suala la maji, sasa ninachosubiri hapa ni matokeo. Je, kati ya tarehe 3 mpaka 10 mwezi wa saba maji haya yatapatikana au hayatapatikana, kwa sababu maji ni kilio kikubwa sana ndani ya Mkoa wa Lindi hasa Wilaya ya Lindi Mjini na maeneo yake ya jirani. Tanzania tumejaliwa tuna mito, mabonde na tuna maziwa, kama tukiwekeza vizuri matatizo haya yatapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niende kwenye eneo la elimu. Mimi kwa taaluma ni mwalimu, sasa hii naiomba niishauri Serikali. Unajua sisi tuna senti, inaanzia senti tano hatukuanzia na senti moja mpaka senti mia moja. Ninachoishauri mimi kama mwalimu nilikuwa napata changamoto na hii changamoto inazidi kuendelea. Wakati zinatengenezwa zile fedha zitengenezwe hizi senti tano, ukiingia leo darasani kumfundisha mwanafunzi senti tano, senti 20 na senti 50 zinafananaje. Ni lazima tumuonyeshe kitu kwa uhalisia, tupeleke vitu wanafunzi wajifunze, hili ni muhimu sana ili wanafunzi waweze kutambua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la elimu kwa kweli tumepiga hatua, tumefanya mambo mengi sana kwenye elimu kwa kipindi kifupi. Tumeboresha shule zote zina madawati, upande wa walimu wa sanaa wote wamejaa, lakini tatizo sasa ni baadhi ya walimu kwenye maeneo ya sayansi. Sasa hapa ni lazima tuwekeze vya kutosha ili watoto wetu wafanye kazi kwa vitendo, halafu hii nitairudia tena na walimu wale ambao wamejifunza na hatimaye wakapata aidha Shahada au Diploma zao wasiendelee kwenda kwenye vyuo kwa sababu lengo ni kuboresha elimu, wabaki kwenye shule zile za msingi, jambo kubwa hapa waboreshewe mahitaji yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tatizo lingine kubwa, kuna suala zima la nyumba za walimu bado hapa tupo nyuma. Kwa kuwa tuna tatizo la nyumba za walimu, vijana wengi hapa wamezaliwa katika mazingira ambayo sisi tunayajua, sasa kijana aliyezaliwa na kukulia Dar es Salaam leo hii umpeleke kule Chikonje ambako mimi ndio nilianzia ile kazi yangu kwa mara ya kwanza, akifika akiangalia, akisikia yale mabundi na wanyama wengine wanalia mwalimu anakusanya na anaondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja, lakini nitakuwa ni mtovu wa fadhila… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu. Hatimaye nikushukuru wewe Mheshimiwa Naibu Spika kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia kwenye Wizara hii ya Afya ambayo ni muhimu sana kwa ustawi na maendeleo ya mwanadamu katika muktadha ufuatao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, usipokuwa na afya njema huwezi kwenda shule; usipokuwa na afya njema maendeleo hayawezi kufanyika; usipokuwa na afya njema kitu kitakachojitokeza hata uchumi wa Taifa letu utapungua kwa ajili ya kukosa nguvu kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya katika Taifa letu. Sambamba na hilo namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Afya pamoja na Naibu wake na watendaji wote wa Wizara hii bila kuwasahau madereva na wahudumu ambao wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru sana Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii kwa kutupatia fedha kiasi cha shilingi 1,200,000,000 katika Jimbo la Lindi Mjini. Shilingi milioni 400 zimetolewa kwa ajili ya Hospitali ya Kituo cha Afya cha Mingoyo, lakini shilingi milioni 700 zimetolewa kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Mnazi Mmoja. Tunaishukuru sana Serikali.
(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, pamoja na mazuri ambayo yameweza kujitokeza, lakini Lindi tuna mambo yafuatayo; hatujajua hatma yetu ya Mkoa wa Lindi kuwa na Hospitali ya Mkoa na Hospitali ya Wilaya. Ukiuliza hivi, unaambiwa Sokoine ni Hospitali ya Mkoa. Wakati mwingine unaambiwa Sokoine ni Hospitali ya Wilaya. Mheshimiwa Waziri, naomba utakapokuja hapa utupe ufafanuzi juu ya jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kama Mkoa wa Lindi na kama ambavyo Hospitali ya Sokoine iko pale, lakini kikubwa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa hana gari la kufanyia huduma. Sizungumzii ambulance, tunazungumzia gari la kufanyia huduma, anatumia gari binafsi kuendeshea shughuli za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 28 tu ndiyo ya wahudumu waliopo ndani ya Mkoa wa Lindi. Tuna upungufu wa asilimia 72. Naomba hili liangaliwe kwa jicho la huruma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya UKIMWI nchini Tanzania kwa mujibu wa Tanzania HIV Impact Survey ya mwaka 2016/2017, maambukizi ya wanawake ni asilimia 6.5 na wanaume ni asilimia 3.5. Hii hufanya maambukizi Kitaifa ni 5%. Sasa ndani ya Mkoa wa Lindi ni asilimia 0.3. Nawapongeza sana watu wa Mkoa wa Lindi kwa kupunguza kiasi kikubwa cha maambukizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maambukizi ya UKIMWI yana vitu mbalimbali ambavyo vinasababisha. Kwa hiyo, tuna wajibu sisi kama Watanzania kuepuka vitu vile ambavyo vinaambukiza ili pesa hizi zitakazopatikana baada ya kutumika kununua madawa na vitu vingine, zitumike katika mazingira ya kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia ARVs ndiyo dawa zinazotumika kufubaisha virusi vya UKIMWI. Sasa hizi dawa ziende kwa wakati kwa kunusuru maisha ya watu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu vifo vya akina mama na watoto; haikubaliki nchi kama Tanzania, mwanamke kufa wakati analeta kiumbe kingine duniani. Tunajua kuna mipango na mikakati mizuri sana iliyowekwa, lakini ni lazima itekelezwe na iwekwe kwa wakati. Kuna magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama figo, pressure na kisukari. Ni lazima yawekewe mikakati madhubuti ili kuhakikisha mazingira haya yanakuwa salama katika nchi yetu. Yote haya yanawezekana tu kama bajeti iliyopangwa na Serikali itapelekwa kwenye maeneo husika kwa wakati na ikiwa timilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja.