MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu yake mazuri Waziri Mkuu naomba nimuulize swali la nyongeza. Haijalishi kwamba ni kiasi gani cha pesa kilichochukuliwa, ufahamu wangu ulikuwa ni hizo lakini nimepata majibu kwamba ni bilioni 6. Sasa hizi shilingi bilioni 6 kwa sababu hii ni haki ya wananchi, je, wanchi hawa wanazipataje?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, stahili ya msingi hapa ni wakulima kupata haki yao ya msingi lakini kwa kuwa tulianzisha huo uchunguzi na tulihusisha vyombo vyetu na vina utaratibu kwa hiyo vitakapokamilisha kabisa uchunguzi hatua kali zitachukuliwa. Inawezekana pia moja kati ya hukumu itakayotolewa ni pamoja na kurejesha fedha kwa wale wote waliothibitika kwamba fedha hizo wamezipoteza na hiyo ndiyo njia sahihi ambayo tunatarajia vyombo vyetu vinaweza vikatoa maamuzi hayo ili wakulima waweze kupata stahiki yao ili waendelee pia kuboresha kilimo kwa msimu ujao. Tutaendelea kufanya hilo kwa mazao yote ambayo fedha hii inapotea, tutawasiliana kuona sheria zinazotumika lakini ni vyema tukaona kabisa kwamba sheria inayowataka wakulima warejeshewe fedha inaweza kuwa nzuri zaidi ili haki yao isiweze kupotea kabisa. Serikali itasimamia jambo hilo pia.