Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Alfredina Apolinary Kahigi (3 total)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuongea machache. Mimi nitazungumzia kuhusu mambo ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyekiti wangu Profesa Ibrahim Lipumba, mchumi duniani pamoja na baraza lake, naahidi sitamuangusha Mheshimiwa Lipumba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu, katika Kamati yetu ambayo tumekaa kuna Wilaya 64 ambazo zinakosa Hospitali za Wilaya, mojawapo ni Wilaya yangu ya Bukoba Vijijini hatuna Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Bukoba hawana hospitali ya wilaya, wanatembea mwendo mrefu au wanalipa gharama za kwenda kutafuta matibabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo gharama ambazo wanalipa wanakuwa hawakuzipanga kusudi waweze kwenda kutibiwa huko. Kama wangekuwa na hospitali katika wilaya yao wasingepata usumbufu huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iwaangalie kwa jicho la huruma iwajengee Hospitali ya Wilaya. (Makofi)Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Wilaya ya miaka mingi sana. Wilaya ya Bukoba ni Wilaya ya miaka mingi sana, Wilaya zote ambazo ziko katika mkoa wetu zimetokana na Wilaya hiyo, lakini yenyewe haina hospitali. Watu wengine kwa kukosa hela za kwenda kwenye hospitali za private wanakunywa dawa za mitishamba ambazo hazina vipimo vyovyote, wengine wanakufa, naomba Serikali iliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini namshukuru Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo, lazima nimseme jina, pamoja na Naibu wake na wataalam wao, ni watu wenye moyo mkunjufu. Hili suala tumeliongelea na wameliona na wameahidi kutusaidia katika bajeti hii ambayo tutakaa waweze kutuweka katika list hiyo, nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka huko, kwa kuwa, dakika ni kidogo niizungumzie Ofisi ya Utumishi. Ninamuunga mkono Rais wangu Mheshimiwa Dkt. Magufuli, kazi aliyofanya siidharau ya kutumbua, kazi ya kutumbua na iwe endelevu, ni kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo ninawasikitikia madereva ambao walitumbuliwa. Madereva mimi najua ujuzi wao, leseni zao, kama wanajua kusoma na kuandika, hivyo ndivyo vinavyowafanya wawe na kazi lakini maskini ya Mungu wametumbuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara hiyo iwaangalie sana watakaokuwa wanaajriwa wawaangalie wasiwe wanawafukuza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia suala la maji lililopo katika Jimbo langu. Katika Kata ya Kanyangereko, Vijiji vya Butahyaibega, Bulinda wakati wa kiangazi wanapata shida sana mito inakauka. Hivyo akinamama wanapata shida sana na kauli ya Serikali ni kumtua mama ndoo kichwani. Sambamba na Kata ya Bujugo, Rubafu na Maruku, shida ni hiyohiyo ya maji safi na salama. Naomba suala hili la maji litafutiwe ufumbuzi maana ni kila mwaka shida hii inajitokeza, sijui Serikali itawasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kuhusu Wizara ya Mifugo na Uvuvi; je, ni lini Serikali itawapiga marufuku wafugaji kulisha mifugo yao barabarani kwa sababu inaweza kusababisha ajali kwa madereva na sehemu zingine imekwisha tokea. Hivyo, naomba lishughulikiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kuuliza, je, ni lini Serikali itakarabati barabara zilizo chini ya kiwango.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi nami ili kuweza kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyotuletea mbele yetu. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake ambayo imejaa mambo mazuri mengi, inasomeka na inaeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja nichangie hoja chache ambazo nimezipangilia. Nianze na upande wa kilimo. Mimi natokea Mkoa wa Kagera. Hatujamaliza mwaka mzima Mheshimiwa Rais amepunguza tozo ambazo zilikuwa zinabambikizwa wakulima wa kahawa lakini nami lazima niungane na Wabunge ambao jana walizungumzia zao la kahawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la kahawa, sijui hao ambao wameleta kilio tena kwa mara nyingine wamepewa mamlaka na nani kushusha bei ya kahawa na kuirudisha kilo moja Sh.1,000. Wakulima wa kahawa sisi tunakaa pembezoni mwa nchi ya Uganda na kahawa nyingi huwa zinaenda sehemu ya Uganda, nina wasiwasi hata kama wakiweka ulinzi wa namna gani kahawa zitavushwa zitaenda Uganda na pato la Taifa litapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hapa Mheshimiwa Waziri Mkuu yupo, Waziri wa Kilimo yupo, naomba hili suala walishughulikie haraka sana iwezekanavyo kabla kahawa hazijavushwa kwenda Uganda. Binadamu ana akili kali sana huwezi kumzuia, hata ukiwa na bunduki atafanya njia zozote zile atavusha hizo kahawa. Toka juzi wamenipigia simu wanaomba hili suala tuliongelee kwenye Bunge. Sasa maadam tuko kwenye Bunge, kilio cha wananchi nimekifikisha, hivyo naomba hatua za haraka zichukuliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi upande wa barabara, kuna Wilaya tatu ambazo zina barabara ambayo haina lami lakini barabara ni nzuri. Nashukuru Serikali ya Mheshimiwa John Joseph Magufuli imeshughulikia barabara na nchi yetu ni kubwa. Nishauri kutoka Muleba Kusini kwenda Bukoba Vijijini kwenda Wilaya ya Karagwe tuna barabara ya udongo. Niishauri Serikali kwa kipindi hiki ambacho tunaingia kwenye bajeti, barabara hiyo waitengeneze kwa kiwango cha lami maana ni kilometa 74. Naomba hilo walizingatie kwani barabara hiyo inasaidia Wilaya tatu, kuingiliana ni kitu cha maana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya Omurushaka - Murongo katika Wilaya ya Kyerwa, ina kilomita 120 inaungaisha nchi mbili, Tanzania na Uganda.Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu, naomba na barabara hiyo waishughulikie. Ukienda upande wa Uganda unakuta wana barabara ya lami, ukija huku ni barabara ya udongo. Mvua zikinyesha magari yanapita kwa shida sana, hivyo, kama wakitengenezewa wakawekewa lami itakuwa ni nzuri zaidi na itadumu kwa muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoke kwenye suala hilo nije kwenye afya. Kikao kile tulichomaliza niliomba Wilaya ya Bukoba Vijijini na sisi tujengewe Hospitali ya Wilaya kwani hatuna Hospitali ya Wilaya. Wilaya zote zina Hospitali za Wilaya, lakini ni Bukoba Vijijini peke yake ndiyo haina Hospitali ya Wilaya. Nina matumaini makubwa na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na Naibu wake waliniahidi kwamba watatujengea na sisi hospitali. Nimesikia wanasema Wilaya 27 watajengewa hospitali, sina uhakika kama na Wilaya yetu wameiweka, kama wameiweka nitashukuru sana na sisi kupatiwa nafasi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina akili timamu, naongea kitu ambacho nakijua na wamekuwa na mazoea nikisimama kuongea wanaanza kubeza, lakini siyo wote ni wale ambao akili zao sijui zikoje. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba katika bajeti hii kweli waikumbuke Wilaya yangu, watujengee Hospitali ya Wilaya tuachane na kwenda kwenye hospitali za private na sisi tuwe na hospitali yetu ya kujitegemea moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka upande wa afya nakuja kwenye siasa. Sina vya sijui ni ukurasa gani na nini mimi natwanga tu. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika siasa tuna Msajili wa Vyama vya Siasa, nipende kumtia moyo na kumshukuru sana. Ni Jaji mwenye akili nzuri sana, ni mtiifu na nimshukuru Mheshimiwa Rais aliyemteua kumpa nafasi hiyo. Ujumbe nataka ufike kwa Mheshimiwa Rais; huyu baba hapaswi kumtoa katika nafasi hiyo, ni mvumilivu, ni mstahimilivu ametukanwa sana, lakini mimi nimemsikiliza sana ni baba mwenye moyo safi sana, baba anayependa kulea vyama vyetu, Mheshimiwa Rais aendelee kumweka katika nafasi hiyo mpaka tujue ustaarabu ni nini, anatukanwa bure baba wa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili na Mheshimiwa Mutungi alipo ajue kwamba Mama Kahigi nipo pamoja naye, Mheshimiwa Rais namshukuru sana kwa kutupa Msajili mwenye busara kama huyu, anatukanwa bure, Mungu atawaona. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, niende kwenye miundombinu. Kwenye miundombinu naishukuru Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Mkoa wangu wa Kagera tuna uwanja wa lami ni mzuri mno, lakini hatuna taa za kwenye uwanja ndege haiwezi kuteremka usiku. Ni kitu kimoja tu hicho ambacho wanaweza wakatusaidia, wakatuwekea taa za ndege kuweza kushuka usiku vinginevyo uwanja ni mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.