Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Alfredina Apolinary Kahigi (7 total)

MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniamsha mara ya pili. Swali langu la nyongeza, je, Serikali ina mkakati gani katika kuhakikisha kwamba huduma hii haijurudii baada ya kupata usafiri endelevu, ili kadhia hii isiweze kujirudia tena? Ahsante (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwenye majibu yangu ya msingi, Serikali inafanya miradi mitatu ya kuhakikisha kwamba meli tatu katika Ziwa Victoria zinafanya kazi kwa pamoja. Kwa hiyo, tuna uhakika kabisa kwamba hata itakapotokea meli moja imepata hitilafu kutakuwa na meli mbili ambazo zinaendelea kufanya kazi kwa pamoja. Ahsante.
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kwa kuwa luninga zinapoteza watoto wetu katika kupotosha watoto wetu katika maadili, je, Serikali ina mkakati gani wa kutusaidia katika suala hili?
Swali la pili, kuna changamoto katika wasanii wa muziki hasa katika nyimbo zao zina matusi, je, Serikali itatusaidiaje kwa sababu wanawake wanavaaa mavazi ambayo hayana staha Serikali itatusaidiaje kusudi waweze kuacha mambo hayo?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi kuweza kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri sana, tumefaidika sana kama Wizara tunapopata maswali kama haya ningeweza pia kuweza kumshauri Mheshimiwa Waziri kama kuna uwezekano Mheshimiwa Nuru Awadhi aweze kuwa Balozi wa Maadili katika Bunge hili.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ameelezea kwamba luninga zinasaidia sana katika kupotosha mmomonyoko wa maadili katika Taifa letu na mimi niseme kwa namna moja ama nyingine nakubaliana na mawazo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyasema, lakini hilo huwa linatokea tu pale ambapo kunakuwa hakuna chombo maalum cha kuweza kusimamia maudhui mbalimbali ambayo yanarusha na vyombo vyetu vya luninga. Kwa kutambua hilo na ndiyo maana Serikali imeunda vyombo viwili ambavyo ni TCRA pamoja na Bodi ya Filamu ambavyo vyote hivi vina lengo kubwa la kuhakikisha kwamba vinasimamia maudhui yanayorushwa katika vyombo vyetu vya habari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme kwamba pamoja na changamoto hizo, Wizara tumeendelea kuhamasisha jamii kwa ujumla kuhakikisha kwamba suala la maadili ni suala ambalo lazima jamiii kwa ujumla wetu kuendelea kulifanyia kazi siyo suala tu la Serikali kama ambavyo nimejibu kwenye jibu la msingi kwamba ni suala ambalo la Serikali, lakini vilevile pamoja na jamii nzima kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, habari njema ni kwamba Wizara kwa sasa hivi imeandaa kanuni mbili ambazo tunaamini kabisa kwamba kanuni hizo ambazo ni kanuni zinazosimamia maudhui katika redio, maudhui katika mitandao ya kijamii na tunaamini kabisa kwamba kwa kupitia kanuni hizi itakuwa ni muarobaini wa kuhakikisha kwamba mmomonyoko wa maadili katika Taifa letu unadhibitiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nipende kuchukua nafasi kuweza kuomba vyombo vyote vya habari viweze kuzingatia kanuni hizo ili kuhakikisha kwamba tunatunza maadili ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili ametaka pia kuweza kujua kwamba kumekuwa na tatizo la nyimbo ambazo haziendani na maadili ya Taifa letu hususani wanawake ambao wanavaa mavazi ambayo siyo ya staha.
Mheshimiwa Spika, mimi niseme kwamba sisi kama Serikali tunatambua kwamba tuna changamoto hiyo na kitu ambacho tumekifanya kwa sababu tuna vyombo vyetu viwili ambavyo ni vyombo vinasimamia maudhui kwa wasanii kwa maana ya BASATA pamoja na Bodi ya Filamu. Hivi vyombo viwili vimekuwa vikisisitiza mara kwa mara kuhakikisha kwamba wasanii kabla hawajatoa nyimbo zao wanapeleka nyimbo zao BASATA, wanapeleka video zao Bodi ya Filamu ili ziweze kuhaririwa na ziweze kupewa madaraja.

Mheshimiwa Spika, jambo la kusikitisha ni kwamba...
Mimi nikushukuru lakini niseme kwamba tumekuwa tuna changamoto kubwa sana k wasanii wetu hawapeleki nyimbo zao kwenda kuhaliliwa BASATA naomba kuchukue nafasi hii kuweza kuwaambia kwamba wasanii wote wahakikishe kwamba wanapeleka nyimbo zao BASATA ili ziweze kuhaririwa kabla hawajaanza kuchukuliwa hatua. Ahsante. (Makofi)
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wilaya ya Bukoba Vijijini tuna tatizo la ma-engineer wa ujenzi na tulitengewa fedha za force account shilingi milioni 900 kwa ajili ya kutujengea Kituo cha Afya katika kata mbili, kata za Kishanje na Rubafu, lakini hatuna ma-engineer wa ujenzi. Tunajenga chumba cha mama na mtoto, mortuary na chumba cha Mganga katika kata hizo mbili.
Je, ni lini Serikali itatusaidia ma-engineer wa ujenzi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nikupongeze kwa Tulia Marathon mmefanya vizuri sana. Hongera sana. (Makofi)
Pia nampongeza sana Mheshimiwa Mama Kahigi kwa sababu amekuwa mfuatiliaji mzuri sana tokea alipokuwa Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesikia kilio hiki kwa sababu tunajua kwa Mkoa wa Kagera tulikuwa hatuna hospitali zile za Wilaya na ninyi mmeleta concern hizo kubwa na ndiyo maana mwaka huu wa fedha tunaenda kujenga hospitali tatu mpya kule Karagwe, Kyerwa pamoja na Bukoba Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunapeleka infrastructure nyingi sana katika eneo hilo na suala zima la kupata wataalam tutaweka kipaumbele chetu, lengo kubwa ni kwamba vile vituo vya afya na hospitali ambazo tunaenda kuzijenga tuwe na wataalam wa kutosha kwa ajili ya kuweza kusimamia. Kwa hiyo, tunalichukua kwa ajili ya kwenda kulifanyia kazi. (Makofi)
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, ni lini Serikali itawajengea nyumba walimu wale ambao hawana nyumba kabisa katika shule zao? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa mambo mazuri yanaigwa, je, Wakuu wa Mikoa hawaoni kama ni vizuri kumuiga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Makonda nao waweze kutafuta wafadhili wa kuweza kuwajengea walimu nyumba za kuishi na ofisi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la upungufu wa nyumba za walimu, naomba nimsihi Mheshimiwa Mbunge kwamba katika hizo pesa ambazo zimeletwa za EP4R ni wajibu wa halmashauri husika kuangalia kama hitaji kubwa ni nyumba za walimu, hakuna dhambi pesa hizo zikatumika pia katika kuhakikisha nyumba zinajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, naamini ni wazo jema, naomba niwasihi Wakuu wa Mikoa mingine waige mfano mzuri kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge yeye mwenyewe ameliona na anapongeza juhudi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nyingine. Nina maswali mawili ya nyongeza, naomba kuyauliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, katika Wilaya yetu ya Bukoba Vijijini kuna baadhi ya kata nitazisema japokuwa ni nyingi. Katika Kata ya Rubafu -Kijiji cha Bwendangabo, Kata ya Buma - Kijiji cha Bushasha, Kata ya Bwendangabo - Kijiji cha Kashozi, Kata ya Nyakato - Kijiji cha Ibosa; hizo ni baadhi ya Kata ambazo nimezitaja, lakini ni kata nyingi sana katika Wilaya yetu ya Buboka Vijijini au niseme Mkoa mzima wa Kagera tuna shida ya umeme.
Je, Serikali inaona umuhimu wa kuwapa kipaumbele cha kuweza kuwawekea umeme haraka iwezekanavyo? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wananchi wa kata hizo hizo nilizozitaja wamenunua solar. Solar hizo tayari zimeshaharibika. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakiki hizo solar kabla hazijaingia sokoni? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza, amezitaja kata mbalimbali katika Wilaya yake ya Bukoba Vijijini na amewakilisha Mkoa mzima na ameeleza ni namna gani Serikali itaweka kipaumbele. Nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika Mkoa huo wa Kagera kwa awamu hii ya tatu inayoendelea jumla ya vijiji 141 vitapatiwa umeme. Katika Wilaya yake ya Bukoba Vijijini, Kijiji cha Burugo kimeshasambaziwa nguzo na kazi zinaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Kata zile alizozitaja na vijiji alivyovitaja, kwa awamu hii ya kwanza vijiji kwa Bukoba vijijini ni 22, lakini kwa awamu ambayo itaendelea mzunguko wa pili unaoanza Julai vijiji vyote vilivyosalia vitapatiwa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ameuliza masuala ya sola ambazo zimewekwa katika maeneo hayo ya Bukoba Vijijini na maeneo mengine ya Mkoa wake kwamba nyingi zimeharibika. Serikali ina utaratibu ndani ya Serikali na kwa Taasisi mbalimbali. Kwa mfano, kuna masuala ya TBS yanavyoangalia viwango na taasisi nyingine za kiserikali za kuangalia bidhaa zinazoingia ndani ya nchi zisiwe bidhaa ambazo kwa kweli ni fake.
Mheshimwia Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali yetu itaendelea kuziimarisha zile taasisi zinazohusika na kuzuia bidhaa feki ndani ya nchi ili kujiridhisha na vifaa hususani vya masuala ya nishati viingie vifaa bora na wananchi wapate huduma bora. (Makofi)
Mheshimwia Naibu Spika, nakushuruku Mheshimiwa. (Makofi)
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali iko pamoja na Halmashauri ya Wilaya kudhibiti wanyama hawa waharibifu, je, Serikali haioni umuhimu wa kuhakikisha kuwa inawapatia vifaa vya kutosha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tunaelewa kuwa wanyama hawa ni waharibifu, je, hakuna njia nyingine ya kuwadhibiti wanyama hawa badala ya kuwauwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Alfredina Apolinary Kahigi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza kwa jinsi ambavyo amekuwa akishirikiana na Serikali katika kufuatilia masuala haya. Niseme tu kama nilivyokuwa nimesema kwenye swali la msingi, tumechukua hatua kadhaa katika kuhakikisha tunawadhibiti wanyamapori wakali na waharibifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ambayo ipo, ni kweli kabisa vifaa vya kudhibiti bado havitoshi hata hivyo tunaendelea kujipanga vizuri kuhakikisha kwamba tunapata vifaa vya kisasa vitakavyosaidia kuwadhibiti wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo yote ikiwa ni pamoja na kutumia zile ndege zisizowakuwa na rubani lakini pia kufanya shughuli nyingine ambazo zitawafukuza wale wanyamapori kusudi wasilete uharibifu ule ambao umekuwa ukijitokeza katika maeneo mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, ni kweli kabisa hatupendekezi na hatushauri watu kuwaua wanyamapori, kwa sababu wanyamapori wanayo haki ya kuishi katika nchi hii kama Mungu alivyofanya uumbaji yeye mwenyewe kwamba lazima viwepo hapa duniani. Kwa hiyo, hizi ni maliasili ambazo lazima zilindwe. Hata hivyo, pale inapoonekana kwamba wamekuwa wengi tunafanya uvunaji endelevu ndipo hapo tunaweza kuwaua. Ngedere wakizidi ndiyo tunawaua otherwise tunakuwa na idadi ambayo lazima iendelee kuwepo na hatushauri viongozi wetu au wafanyakazi wetu kuwaua wanyama hao.
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika nchi yetu kuna madini ya aina mbalimbali kama vile ruby, sapphire blue, ulanga na tin katika Mkoa wa Kagera, Wilaya ya Karagwe. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutangaza madini haya katika soko la dunia kama inavyotangaza tanzanite, dhahabu na almasi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kahigi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, madini yote ambayo tunayachimba hapa nchini ni wajibu wetu kama Serikali kuyatangaza kwamba yapo ndani ya nchi na kuwavutia wawekezaji waje kuwekeza katika madini hayo. Madini ya tin na madini mengine aliyoyataja tunaendelea na mkakati huo wa kuyatangaza duniani kote na ndiyo maana ataona hata leo akienda hapo nje atakuta tuna maonyesho mbalimbali. Baada ya bajeti hii tutakuwa na vipindi mbalimbali vya redio, televisheni, magazeti na machapisho mbalimbali kwa ajili ya kutangaza utajiri tulionao ndani ya nchi yetu yakiwemo madini ya tin na haya mengine ya vito aliyoyataja. (Makofi)