Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Kiza Hussein Mayeye (4 total)

MHE. KIZA H. MAYEYE aliuliza:-
Mkoa wa Kigoma umebarikiwa kuwa na Ziwa Tanganyika, Mto Malagarasi na vyanzo vingine vya maji lakini Mkoa huu unakabiliwa na changamoto kubwa ya maji.
Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Kigoma hususan katika Jimbo la Kigoma Kaskazini katika kuhakikisha wanapata maji ya kudumu ya kwenye mabomba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiza Hussein Mayeye, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji inaendelea kutekeleza miradi wa maji vijijini katika Halmashauri ya Wilaya Kigoma iliyopo Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma. Hadi kufikia mwezi Septemba, 2017 jumla ya miradi mitatu ya maji ya Nyarubanda, Kagongo na Nkungwe imekamilika na wananchi wanapata huduma ya maji. Mradi mmoja wa Kalinzi upo katika hatua za mwisho na utekelezaji wake umefika asilimia 90. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri hiyo imetengewa shilingi milioni 649.8 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi ya maji vijijini.
Vilevile Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Ubeligiji imeanza utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji vya Halmashauri za Mkoa wa Kigoma utakaogharimu shilingi bilioni 20.6 na itatekelezwa katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2017 hadi 2021. Mradi huo utanufaisha wakazi 207,785 katika vijiji 26 vya kipaumbele katika Halmashauri za Mkoa huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mijini, Serikali inatekeleza mradi wa maji Mjini Kigoma kwa gharama ya Euro milioni 16.32. Mradi huo unahusisha ujenzi wa chanzo cha maji ukingoni mwa Ziwa Tanganyika eneo la Amani Beach chenye uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 42 kwa siku, ikilinganishwa na lita milioni 12 zinazozalishwa sasa. Kazi nyingine zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa matanki matano yenye ujazo wa lita milioni mbili kila moja na tanki moja lenye ujazo wa lita 500,000; ulazaji wa bomba kuu lenye urefu wa kilometa 22 na mabomba ya kusambaza maji urefu wa kilometa 132, ujenzi wa vioski 70 vya kuchotea maji katika maeneo mbalimbali.
Aidha, katika kuboresha huduma ya usafi wa mazingira, mabwawa ya kutibu majitaka yenye uwezo wa kutibu mita za ujazo 150 kwa siku yatajengwa pamoja na ununuzi wa gari la kunyonya na kusafirisha majitaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwezi Oktoba 2017, kwa ujumla utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia
76 na unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba 2017. Kukamilika kwa mradi huo kutaongeza upatikanaji wa majisafi na salama kutoka asilimia 69 za sasa hadi kufikia asilimia 100.
MHE. KIZA H. MAYEYE aliuliza:-
Kukosekana kwa Madaktari Bingwa na wataalam wengine katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma kunafanya wagonjwa wengi kupewa rufaa ambazo zingeweza kushughulikiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa:-
Je, ni lini Serikali itapeleka Madaktari Bingwa na wataalam wengine wa kutosha katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiza Hussein Mayeye, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa wa Kigoma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma inahitaji Madaktari Bingwa wa fani mbalimbali ili iweze kutoa huduma za kibingwa. Aidha, Wizara inatambua kuwa, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma kwa sasa ina Daktari Bingwa mmoja tu katika fani ya watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia uamuzi wa Serikali wa kuzihamisha Hospitali za Rufaa za Mikoa kuwa chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Serikali inaendelea na zoezi la kufanya tathmini ya kina kujua hali halisi ya Madaktari Bingwa na fani zao katika hospitali zote za mikoa, kanda, hospitali maalum na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilisha tathmini hii, Wizara itawapanga upya Madaktari Bingwa kwa uwiano kulingana na mahitaji ya hospitali za mikoa, kanda maalum pamoja na Taifa. Lengo ni kuwa hospitali ya mkoa iwe na Madaktari Bingwa ikiwemo pamoja na Hospitali za Rufaa ya Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2017/2018, Serikali imegharamia mafunzo ya Madaktari Bingwa 125 ambao wameingia mkataba wa kutumikia katika maeneo watakayopangiwa baada ya kuhitimu masomo kwa lugha ya kitaalam bonding. Mkoa wa Kigoma utakuwa ni moja ya mikoa itakayonufaika.
MHE. KIZA H. MAYEYE aliuliza:-
Wastani wa juu wa kuzaa kwa mwanamke wa Kigoma ni mara saba juu ya wastani wa kitaifa, lakini wanawake hawa wana hatari ya kupoteza maisha wakiwa wanajifungua kutokana na miundombinu mibovu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha uzazi salama na kutokomeza kabisa vifo vya mama na mtoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO atajibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Kiza Hussein Mayeye, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kigoma kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wastani wa wanawake kuzaa katika Mkoa wa Kigoma ni 6.7 wakati wastani wa kitaifa ni watoto 5.2 kwa kila mwanamke. Hivi sasa Serikali inatekeleza mpango mkakati wa miaka mitano wa kuanzia mwaka 2016 – 2020 kwa jina la kitaalam linajulikana kama (National Road Map Strategic Plan…
Hivi sasa Serikali inatekeleza mpango mkakati wa miaka mitano wa mwaka 2016 – 2020 (National Road Map Strategic Plan to Improve Reproductive Maternal, New Born, Child and Adolescent Health in Tanzania) unaolenga kuboresha afya ya uzazi, mama, mtoto na vijana.
Katika kutekeleza mkakati huu, Wizara imezingatia maeneo makuu matatu…
:…Wizara imezingatia maeneo makuu matatu ambayo ni huduma ya uzazi wa mpango, huduma wakati wa ujauzito na huduma wakati wa kujifungua. Wizara katika kuhakikisha inatokomeza vifo vya mama na watoto katika Mkoa wa Kigoma imeweza kutekeleza afua mbalimbali kama vile:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI inatekeleza mpango wa kukarabati na kupanua vituo vya afya 208 nchini ili viweze kutoa huduma za uzazi wa dharura, ambapo katika Mkoa wa Kigoma vituo vitatu vilipata fedha za ukarabati wa shilingi milioni 400, ambavyo ni Uvinza, Mwamgongo na Janda…
… na vituo vya afya sita vilipata kila kimoja shilingi milioni 500 ambavyo ni Mabamba, Nyakitonto, Kiganamo, Nyamidaho, Lusesa na Gwanumpu.
Aidha, Kituo cha afya cha Kagezi na Kimwanya vinajengewa vyumba vya upasuaji na jengo la kuhudumia mama na mtoto kupitia wadau wa Global Affairs Canada chini ya Shirika la World Vision.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili, kuimarisha huduma ya uzazi wa mpango kwa kutoa mafunzo kwa watoa huduma ya afya, na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa uzazi wa mpango. Kwa Mkoa wa Kigoma katika kipindi cha miaka miwili watumishi 150 wamepatiwa mafunzo ya namna ya kutoa huduma za dharura kwa mama mjamzito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kupandisha hadhi vituo vya afya ili viweze kutoa huduma ya upasuaji na damu salama, ambapo kati ya vituo 16 vilivyopo 11 vimepandishwa hadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, kuboresha huduma ya rufaa kwa kununua magari na boti za kubebea wagonjwa katika vituo vilivyopo katika ukanda wa Ziwa Tanganyika.
MHE. KIZA H. MAYEYE aliuliza:-

Serikali imekuwa ikiwapandisha madaraja walimu lakini haitoi malipo stahiki kwa madaraja hayo mapya kwa kipindi kirefu tangu walipopandishwa madaraja yao:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba walimu wanapata stahiki zao mara wanapopandishwa madaraja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiza Hussein Mayeye, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilisitisha kupandisha walimu na watumishi wengine madaraja katika mwaka wa fedha 2015/2016 na 2016/2017 kutokana na uhakiki wa watumishi uliohusisha uhalali wa vyeti, elimu na ngazi za mishahara. Lengo la uhakiki ilikuwa ni kuhakikisha kuwa Serikali inabaki na watumishi wenye sifa na wanaostahili kulipwa mishahara. Kutokana na sababu hiyo, ni kweli wapo watumishi ambao walipandishwa madaraja ambao hawajalipwa mishahara mipya, wapo waliopata mishahara mipya na baadaye kuondolewa na wapo ambao hawakupandishwa kabisa pamoja na kwamba walikuwa na sifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kurekebisha changamoto hizo, Serikali ilitoa maelekezo kuanzia Novemba, 2017 kwa waajiri wote wakiwemo Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhuisha barua za kupandisha madaraja watumishi hao ili waweze kulipwa stahiki zao. Aidha, kwa wale ambao walikuwa na barua lakini taarifa zao zilikuwa hazijaingizwa kwenye mfumo, waajiri walielekezwa kuhuisha barua zao kuanzia tarehe 1 Aprili, 2018 ili waanze kulipwa stahiki zao. Serikali itaendelea kuweka kipaumbele na kutenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha watumishi wenye sifa na kupanda madaraja wanalipwa stahiki zao.