Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Janeth Maurice Massaburi (2 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JANETH M. MASSABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira mwingi wa rehema ambaye yeye ndiye amenipa kibali kuwa katika Bunge hili leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipekee naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu mpendwa wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuwa Mbunge katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Spika pamoja na ninyi Wenyeviti wote. Kwa kipekee vilevile niwashukuru Wabunge wote kwa mapokezi mazuri na upendo waliouonesha kwangu. Naomba Mwenyezi Mungu azidi kuwabariki Wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuzidi kuwatetea wananchi wengi wa Tanzania walio wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikishukuru chama changu, Chama cha Mapinduzi, chama chenye kuleta matumaini kwa Watanzania hasa wanyonge kwa kunilea vyema na kunishauri, na hapa nilipo ni Chama changu cha Mapinduzi ndiye mlezi thabiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuishukuru familia yangu, wazazi wangu, watoto wangu, shemeji zangu, majirani ndugu na marafiki kwa kunilea na kunipa moyo na hasa wakati mgumu nilipoondokewa na rafiki yangu mpenzi wangu Didas Massaburi. Mwenyezi Mungu azidi kumpokea katika makao yake ya milele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu mimi nimeona kuna mambo mazuri mengi, lakini si maana kwamba yote ni mazuri tu na ndiyo maana kuna miaka mitano ya kujisahisha na ndiyo maana kuna bajeti za kila mwaka, penye mapungufu unajaza, unatoa wazo la kuleta manufaa.

Katika mpango wa miaka mitano (2016/2017 - 2020/ 2021) wametenga kanda tano maalum za kiuchumi. Kuna eneo maalum la uwekezaji la Bagamoyo hilo liko Mkoa wa Pwani, lengo kuu ni kujenga bandari ya kisasa ambayo itaruhusu meli kubwa na eneo hili litakuwa lango kuu la biashara za kikanda na kimataifa, lakini kutakuwa pia na viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kituo cha viwanda cha Kurasini Dar es Salaam. Mradi huu pia utaimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na mataifa mengine kupitia uwekezaji katika miundombinu ya kubiashara na ujenzi wa viwanda; huo kumbuka ni Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu kuna maeneo maalumu ya uwekezaji ya Mkoa wa Kigoma. Lengo kuu la mradi ni kuwa na eneo maalumu wa uwekezaji llitakalokuwa na bandari huru (free port). Kutakuwa na mitaa ya viwanda, kongani za kitalii na kituo cha biashara. Hili limetengwa kutumia vizuri fursa za kijiografia ambayo itaweza kuhudumia nchi za Kongo, Burundi, Rwanda na Zambia. Kumbuka ni Mkoa gani huo? Ni Kigoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo la uwekezaji Mkoa wa Mtwara eneo hili pia kutakuwa na uwekezaji jumla ya hekta 110 ambazo zimetengwa maalum kwa lengo la kujenga bandari huru ambapo kuna kampuni ambazo zinaendelea kufanya utafiti katika eneo lile na vilevile watajenga viwanda, Mkoa wa Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tano ni Mkoa wa Ruvuma, kuna uwekezaji wa jumla ya hekta 2030 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vikubwa (heavy industries) vitakavyotumia malighafi ya gesi na chuma. Viwanda vya kuongeza thamani na mazao ya kilimo kama korosho na viwanda vya vito vinatoka Mtwara hii ni Mikoa mitano Pwani, Dar es Salaam, Kigoma Mtwara na Ruvuma hii Mikoa yote inatoka Kanda ya Ziwa? Mikoa inatoka Chato? Tusipotoshe wananchi wetu, Watanzania wana akili sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna vipaumbele kwa mwaka wa fedha 2018/2019. Miradi mikubwa ambayo naona inasemwana sana, mradi wa Stiegler’s Gorge naona umekuwa ni mjadala mkubwa. Hata hivyo hiki ni chanzo cha nishati ya umeme. Tumesema Tanzania ya viwanda bila umeme hatuwezi kuwa na viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile kuna reli. Nakumbuka mimi katika Bunge la mwaka 2005 mpaka 2010 kulikuwa na mjadala wa Bunge kuhusu reli, barabara zinaharibika magari makubwa yanatumia barabara kila mwaka kuna fedha za kutengeneza barabara. Sasa sisi tunashauri Serikali inatekeleza, imekuwa kazi! Shirika la ndege… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JANETH M. MASSABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tena nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pamoja na pongezi naomba nichangie Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/2019 kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miundombinu ya barabara, naomba niipongeze Serikali kwa hatua mbalimbali za kuboresha barabara zetu hapa nchini. Hata hivyo kuna dosari kadhaa ambazo zinatakiwa kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano barabara za Mkoa wa Dar es Salaam, barabara ya Tabata Dampo kuelekea Tabata Segerea - Kinyerezi - Malamba Mawili - Msigani mpaka Mbezi, barabara hii imekuwa kero kubwa na adha ya foleni hasa nyakati za kuanzia saa 12.00 asubuhi mpaka saa 4; na saa 10.00 jioni hadi saa 3.00 usiku, na ikizingatiwa barabara ndiyo lango la kubebea mitambo mikubwa ya Mradi wa Gesi Kinyerezi. Kwa sababu hizo na nyingine tunaiomba Serikali ipanue barabara hiyo kutokana na idadi kubwa ya watu na watumiaji wengine kama mradi wa Kinyerezi (Mradi wa Gesi).

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Segerea Sheli kuelekea Seminari hadi Majumba Sita, tumeiomba Serikali iweke barabara hii kwenye mpango wa dharura wa muda mfupi na pia iwekwe kwenye mpango wa kujenga barabara hiyo na Daraja la Seminari ili wananchi waweze kutumia barabara hiyo kwa manufaa. Barabara hii Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli, wakati wa Kampeni ya Uchaguzi Mkuu 2015 akiwa Vingunguti aliahidi kuwa barabara ya Segerea Shelil (Oil Com)kupitia Segerea Seminari hadi Majumba Sita ijengwe kwa kiwango cha lami na daraja lake. Kwa muda huu yafanyike matengenezo ya dharura hasa pale eneo la Sheli (Oil Com) ambapo njia inapitika kwa shida sana. Wakazi wa eneo hilo wamekata tamaa. Kwa kuanzia angalau kifusi cha mawe ili kunyanyua barabara maana pamechimbika sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara kuu na barbara za mitaa; barabara nyingi hazifanyiwi matengenezo kwa wakati, hali hii inasababisha Serikali yetu ya CCM ilaumiwe. Naomba Serikali iweke kitengo madhubuti kitakachofanana na kuendana na kasi ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli Rais wetu ili kitengo hiki cha ukaguzi wa barabara kuu na barabara za mitaani kiweze kutambua tatizo mapema kuliko tatizo litolewe na vyombo vya habari. Hali hiyo huwa inaleta fedheha kubwa, ikizingatiwa kuna viongozi na watendaji katika ngazi za kata na kadhalika walitakiwa kujua tatizo kabla. Kitengo cha ukaguzi kiongezewe vitendea kazi kama magari na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji Dar es Salaam. ninaipongeza Serikali kwa kuboresha upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa asilimia 70; wananchi wa Dar es Salaam wamefurahi sana kwa kupata maji. Hata hivyo tunaiomba Serikali iharakishe upatikanaji wa maji katika maeneo ambayo hutegemea chanzo kingine cha maji, kwa mfano wananchi wa Kipera – Pugu, Majohe, Chanika, Msongola, Kitunda, Chamazi na maeneo ya Mwinuko ambao hawapati maji ya uhakika. Tunaomba kasi iongezwe zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu ya ufundi na ujuzi, Serikali iangalie kwa upana zaidi kwa kuanzisha vyuo vingi vya ufundi ili viweze kutengeneza rasilimali watu wenye ujuzi wa fani mbalimbali kama mafundi wa mitambo midogo midogo, mafundi wa kutengeneza vifaa vya umeme, vifaa vya ujenzi; vifaa ambavyo soko lake litatokana na matumizi yetu ya kila siku sisi Watanzania. Kwa mfano kutengeneza vifaa vya ngozi (viatu, mikanda, mabegi, vifaa vya umeme aina zote za majumbani, vifaa vya ujenzi pamoja na vifaa (vipuri) vya mitambo midogomidogo pamoja na ujuzi wa aina nyingine ambazo zinaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kiteknolojia na kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili la mafunzo ya ufundi na ujuzi itasaidia kuruhusu vijana wengi wanaomaliza darasa la saba, kidato cha nne na kidato cha sita, kupata mafunzo na baada ya hapo kupelekwa kwenye viwanda husika. Serikali si vibaya ikafuata mfumo uliotumika katika nchi ya Singapore ya kufanya mapinduzi ya kuwafundisha vijana wao wengi mafunzo ya ufundi na ujuzi kwa kuanzisha vyuo vingi vya ufundi na ujuzi mbalimbali na walitilie nguvu katika masuala ya vifaa vya umeme.

Mheshimwia Mwenyekiti, naunga mkono hoja pamoja na maoni yangu, nawasilisha.