Primary Questions from Hon. Janeth Maurice Massaburi (10 total)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI (K.n.y. MHE. JANETH M. MASSABURI) aliuliza:-
Je, Serikali haioni kuwa kusuasua kwa Chuo cha Uvuvi Mbegani - Bagamoyo na vyuo vingine kutokana na kukosa bajeti ya kutosha ya kuviendesha vyuo hivyo kumechangia kupoteza ajira kwa vijana ambao kama wangepata mafunzo ya ufugaji samaki wangeinuka kimapato?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Maurice Massaburi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Janeth Maurice Massaburi kwa kuwa ni kiongozi wa mfano kwa ufuatiliaji na kitendo chake cha kuwalipia watoto wake wawili kupata mafunzo ya ufugaji wa samaki katika Chuo cha Mbegani kwa muda wa wiki moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha mafunzo ya uvuvi kwa kuanzisha Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) mwaka 2012 ambapo udahili umeongezeka kutoka wanafunzi 714 mwaka 2011/2012 hadi kufikia wanafunzi 1,196 katika mwaka wa 2016/2017. Pia, FETA imekuwa ikipokea fedha kutoka Serikalini ambapo katika mwaka wa fedha 2017/2018 ilipatiwa jumla ya shilingi milioni 246 kwa matumizi ya kawaida, katika mwaka huu wa fedha wametengewa shilingi milioni 580 kiasi ambacho ni zaidi ya mara mbili ya kile walichokipata katika mwaka uliopita.
Mheshimiwa Spika, kazi kubwa ya maendeleo iliyofanyika katika kipindi hiki cha miaka sita ya uhai wa FETA ni pamoja na kukarabati miundombinu ya vituo vya Mikindani - Mtwara, Kibirizi - Kigoma, Mwanza South pale Mwanza na Gabimori – Rorya. Vituo vya Mwanza South na Kibirizi tayari vimeanza kutumika kutoa mafunzo ya ufugaji wa samaki wakati vile vya Mikindani na Gabimori viko tayari kuanza kazi ya utoaji wa mafunzo na Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma tayari imekwishafanya kazi ya zoezi la usaili ili kupata wakufunzi 18 watakaopelekwa katika vituo hivyo ili kuviwezesha kuanza kazi katika mwaka huu wa fedha wa 2018/2019.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya mazungumzo na Jumuiya ya Ulaya (EU) ambayo imekubali kusaidia Wakala wetu hii FETA katika kujenga uwezo wa kitaasisi ili kupanua mafunzo ya kiufundi yanayolenga kuongeza idadi ya vijana watakaojiajiri ama kuajiriwa katika sekta ya ufugaji samaki. Utekelezaji wa mradi huu unaanza katika mwaka huu wa fedha 2018/2019 kwa kuandaa mitaala, miundombinu ya kufundishia na kujifunzia pamoja na kuwajengea uwezo wakufunzi wetu.
MHE. JANETH M. MASABURI aliuliza:-
Kumekuwa na upungufu wa rasilimali watu katika taasisi za umma na baadhi ya watumishi kushindwa kufanya maamuzi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga fedha kwa ajili ya mafunzo ndani na nje ya nchi kwa watumishi wa umma ili kuwajengea uwezo na kuleta tija kwa Taifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Maurice Masaburi, Mbunge wa Kuteuliwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuwapatia mafunzo watumishi wa umma ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi. Kwa kutambua hilo, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora huandaa sera, kanuni na miongozo inayohusiana na mafunzo katika utumishi wa umma na kufuatilia utekelezaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Menejimenti ya Ajira ya mwaka 1999 na marekebisho yake ya mwaka 2008 kifungu 4.8; Sera ya Mafunzo katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2013 kifungu 4.2; na Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 kifungu G 1 (vifungu vidogo 7, 9, 10 na 11) zinasisitiza kuhusu umuhimu wa kila mwajiri katika utumishi wa umma kuandaa na kutekeleza Mpango wa Mafunzo kwa mujibu wa tathimini ya mahitaji ya mafunzo kwa maana ya (Training Needs Assessment).
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 kupitia Wizara, Idara zinazojitegemea pamoja na Wakala, Serikali ilitenga jumla ya Sh.54,470,327,822 kwa ajili ya kugharamia mafunzo ya ndani na nje kwa watumishi wa umma. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019, jumla ya Sh.39,839,347,632 zimetengwa kwa ajili hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo hususani Australia, India, Japan, China, Indonesia na Jamhuri ya Korea ambapo katika mwaka ule wa 2016/2017 kupitia wadau hao jumla ya watumishi wa umma 654 walipatiwa mafunzo ya muda mfupi na mrefu katika nchi hizo. Aidha, katika mwaka ule wa 2017/2018, fursa za mafunzo zilizotolewa na washirika hao ziliongezeka hadi kufikia 827. Fursa hizo zimewezesha watumishi wa umma kupata uelewa, ujuzi na maarifa mapya ya kumudu majukumu yao katika kutekeleza malengo ya Taifa. Ahsante.
MHE. JANETH M. MASABURI aliuliza:-
Nchi za China na Singapore zinefanikiwa kwa kiwango kikubwa kwa kuwekeza kwenye ujenzi wa Vyuo vya Ufundi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga bajeti ya kutosha ili kuwekeza kwenye Vyuo vya Ufundi ambavyo vitasaidia vijana wengi kupata ujuzi na kujiajiri?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Maurice Masaburi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa nchi kuwekeza katika elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ili kufikia azma ya uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025. Serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi vya mikoa mitano katika Mikoa ya Geita, Rukwa, Njombe, Simiyu na Kagera, pamoja na vyuo vya ufundi stadi vya wilaya 13. Aidha, kupitia mradi wa Education Skills for Productive Jobs (ESPJ) vyuo vyote 54 vya Maendeleo ya Wananchi vinakarabatiwa ambapo awamu ya kwanza vyuo 20 vitakarabatiwa na ukarabati upo katika hatua za umaliziaji. Vilevile kupitia mradi huu Chuo cha Ufundi wa Kati (Technical College) kitajengwa katika Mkoa wa Dodoma kuanzia Mwaka wa Fedha 2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kupitia mradi wa East African Skills for Transformation and Regional Intergration Project Serikali inatarajia kuzijengea uwezo taasisi za Chuo Cha Ufundi Arusha, Taasisi ya Teknolojia Dar-es-Salaam (DIT) tawi la Dar-es-Salaam na Mwanza, pamoja na Chuo Cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT), ili kuwa vivutio vya umahiri katika sekta za nishati, teknolojia ya habari na mawasiliano, usafirishaji na uchakataji wa mazao ya ngozi. Serikali itaendelea kuwekeza katika elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kadri uchumi utakavyoruhusu, ili kuongeza fursa na ubora wa elimu na mafunzo hayo nchini kwa lengo la kuleta tija zaidi na manufaa kwa Taifa.
MHE. JANETH M. MASABURI Aliuliza:-
Nchi yetu imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi zikiwemo bahari, maziwa, mito na mabwawa mengi ya asili pamoja na rasilimali watu kubwa ambao hawana ajira.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha vijana na akina mama kwenye kila Halmashauri nchini kutenga maeneo maalum ya kujenga mabwawa ya kufugia samaki ili makundi hayo yapate kujiajiri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Maurice Masaburi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kupitia Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili Halmashauri zote nchini zimeelekezwa kutenga maeneo ya ardhi kwa ajili ya kuchimba mabwawa ya kufugia samaki, kuendeleza ufugaji wa samaki kwenye vizimba na kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali kwa ajili ya uzalishaji bora na endelevu wa samaki.
Mheshimiwa Spika, jitihada zetu nyingine za Serikali za kuwasaidia wavuvi nchini wakiwemo vijana na akinamama ni kuondoa kodi katika zana za malighafi yaani uvuvi kwa engine za kuvulia, nyavu, kufuta Kodi ya Ongezeko la Thamani yaani VAT kwenye engine za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu na vifungashio ili kupunguza gharama za zana na vyombo vya uvuvi na kutoa ruzuku kwenye zana za uvuvi ambapo mvuvi anatakiwa kuchangia asilimia 60 na Serikali ni asilimia 40.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri zote nchini zimekuwa zikipewa mafunzo ya uvuvi endelevu kwa wavuvi wakiwemo vijana na akinamama kupitia semina, warsha, vipeperushi, makala, redio na luninga kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na wadau mbalimbali. Pia Maafisa Uvuvi katika Halmashauri zote nchini wamepatiwa mwongozo wa ugani katika sekta ya uvuvi kwa lengo la kutoa elimu kwa wavuvi na ukuzaji wa viumbe kwenye maji na kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambapo jumla ya nakala 1,000 zilisambazwa.
MHE. JANETH M. MASSABURI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatunga Sheria kali za kudhibiti madereva wasiofuata sheria za usalama barabarani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Maurice Massaburi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Usalama Barabarani, sura 168 ya mwaka 1973 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002 na kanuni zake, inayotumika Tanzania Bara, na Sheria ya Usafiri Barabarani, Sura ya 7 ya mwaka 2003 na kanuni zake, inayotumika Zanzibar, zinatoa adhabu kwa wale wanaokiuka Sheria ya Usalama Barabarani. Serikali inaendelea kuboresha Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Usalama barabarani ambao tayari ulishasomwa kwa mara ya kwanza hapa Bungeni ili kuzingatia mabadiliko yaliyotokea na mahitaji ya sasa.
Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. JANETH M. MASSABURI aliuiliza: -
Je, Serikali haioni haja ya kupeleka Maofisa Usalama Barabarani Falme za Kiarabu na Vietnam ili kujifunza jinsi ya kudhibiti ajali?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Maurice Massaburi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inao utaratibu wa kutoa mafunzo mbalimbali kwa maofisa wa polisi wa usalama barabarani ndani ya nchi na pia kuwapeleka nje ya nchi kujifunza namna bora ya kusimamia na kudhibiti ajali za barabarani.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2023 Serikali imeshawapeleka maofisa wa usalama barabarani 30 kwenye nchi 15 ambazo ni Marekani, Ujerumani, Japan, China, India, Vietnam, Australia, Switzerland, Falme za Kiarabu, Israel, Tunisia, Misri, Ghana, Rwanda na Afrika Kusini ili kujifunza masuala ya usalama barabarani. Mashirika ya kimataifa na wadau kama JICA, UKAID, WFP, WHO, LATRA, TIRA, TRA, NIT na Baraza la Taifa la Usalama Barabarani wanaendelea kufadhili na kutoa mafunzo juu ya udhibiti na usimamizi wa taratibu za usalama barabarani ili kupunguza ajali nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa nafasi za mafunzo ndani na nje ya nchi kwa maofisa wa usalama barabarani ili kupata ujuzi juu ya usimamizi na udhibiti wa ajali kama alivyoshauri Mheshimiwa Mbunge, nashukuru.
MHE. JANETH M. MASSABURI aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga barabara za mitaa za Mkoa wa Dar es Salaam kwa mfumo wa EPC+F kwa vile Mradi wa DMDP haukidhi haja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Maurice Massaburi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na ukamilishaji wa maandalizi ya Mradi wa DMDP Awamu ya Pili. Tayari wataalam washauri watatu wanaendelea na kazi ya usanifu ambapo mkataba wa kazi hiyo utafanyika kwa muda wa miezi sita kuanzia Tarehe 30 Mei, 2023. Mara tu usanifu utakapokamilika, taratibu za ununuzi wa kuwapata wakandarasi zitaanza kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, EPC+F ni mfumo wa ujenzi wa kimkataba ambapo mkandarasi anafanya usanifu, ununuzi, ujenzi na kugharamia kazi za ujenzi (engineering design, procurement, construction and financing). Serikali kupitia TARURA bado haijaanza kutekeleza mfumo huu. Serikali inapokea ushauri na itapitia na kuufanyia kazi.
MHE. JANETH M. MASABURI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuubadilisha Mkoa wa Dar es Salaam kwa kujenga barabara za mitaa, mifereji na miundombinu mingine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Maurice Masaburi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2021/2022 – 2022/2023 Serikali ilitenga shillingi bilioni 100.06 kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara ambapo kilomita 47.77 za lami, kilomita 1,896.966 za matengenezo ya barabara, madaraja na makalvati 70 pamoja na taa za barabara 862. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2023/2024, jumla ya shilingi bilioni 48.68 zimetengwa kwa ajili ya kazi ya barabara katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango uliopo sasa ni wa kuanza utekelezaji wa Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II), pamoja na maboresho ya Mto Msimbazi na Daraja la Jangwani. Miradi hii itahusisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya barabara, mifereji ya maji ya mvua pamoja na madaraja.
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. JANETH M. MASSABURI aliuliza: -
Je, magari mangapi ya Zimamoto yanahitajika kukidhi mahitaji halisi nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Maurice Massaburi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linahitaji jumla ya magari 237 ya kuzima moto, magari 168 ya uokoaji, magari 28 ya HAZMAT, Crane 38, ambulance 168 na magari 28 ya ngazi ya kuzima moto katika majengo marefu (Turn table ladder). Serikali imeendelea kuliimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kutenga fedha za maendeleo katika bajeti kila mwaka kwa ajili ya ununuzi wa magari ya kuzima moto pamoja na vifaa vingine vya uokoaji ambapo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Jeshi limetengewa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ununuzi wa magari matano ya kuzima moto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kupata mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za Kimarekani milioni 100 utakaowezesha kupata vitendea kazi mbalimbali ikiwemo magari zaidi ya 100 ya kuzima moto na uokoaji kwa nchi nzima, ahsante.
MHE. DOROTHY G. KILAVE K.n.y. MHE. JANETH M. MASSABURI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kujenga barabara kwa kiwango cha lami pembezoni mwa reli ya SGR wakati ujenzi unaendelea?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Reli Na. 10 ya mwaka 2017, hifadhi ya reli ni meta 30 kutoka katikati ya reli kila upande. Katika eneo hili hairuhusiwi kujenga barabara kwa matumizi ya kawaida. Hivyo, haitawezekana kujenga barabara ya lami pembezoni mwa reli ya SGR, ahsante. (Makofi)