Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Janeth Maurice Massaburi (2 total)

MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naitwa Nuru Awadh Bafadhili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniruhusu kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa kuna baadhi ya walimu mfano katika Halmashauri ya Jiji la Arusha katika Shule ya Msingi Olkerian, Kata ya Olkerian mpaka leo wanasumbuliwa kulipwa fedha zao za likizo na wakati huo huo tayari walishatumia fedha zao. Wanapouliza wanaambiwa andikeni barua ili muweze kulipwa pesa zenu. Je, Waziru anatuambiaje kuhusu suala hilo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nimpongeze kwa kurudi tena Bungeni, alikuwa ni Mbunge kipindi cha mwaka 2005-2010, hongera sana na karibu tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua yako madeni mbalimbali ya watumishi wanaodai fedha zao za likizo. Nipende tu kusisitiza kwa waajiri kila mwaka pindi wanapoandaa mapendekezo ya bajeti za mwaka wahakikishe wanatenga fedha kwa ajili ya nauli za likizo katika bajeti ya matumizi ya kawaida au bajeti za OC. Vilevile nipende kusema kwamba kwa yeyote ambaye hakulipwa fedha hizo hilo ni deni na kama Serikali tunalitambua na tunalichukua na tutaendelea kufuatilia kuhakikisha kwamba watumishi hawa wanapatiwa malipo yao. Niombe tu anisaidie huko baadaye taarifa kamili ili tuweze kushirikiana katika ufuatiliaji, lakini ni haki ya msingi ya mtumishi na ni lazima walipwe.
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kuna baadhi ya makabila wanatumia njia za kienyeji badala ya kwenda kufanyia tohara vijana wao katika hospitali njia ambazo zinasababisha wakati wa kuwafanyia tohara wakati mwingine kutokwa na damu nyingi na kupoteza maisha. Je, Serikali inatuambia nini kuhusu kuwapa elimu ili waweze kupeleka vijana wao katika hospitali zetu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ni rai yetu kwenye Makabila ambayo yana utamaduni wa kufanya tohara za kiasili maarufu kama kavukavu kama ulivyosema kuwaomba watumie huduma hiyo ya kutoa tohara kwa kwenda kwenye hospitali na kufanyiwa huduma ya tohara ya kitabibu yaani medical circumcision ili kuepukana siyo kutokwa damu nyingi, lakini pia kuepukana na uwezekano wa kuambukizwa magonjwa mbalimbali kwa sababu kule wanakofanya tohara ya kiasili kuna uwezekano mkubwa wakachangia vifaa vya kufanyia tohara yenyewe na hivyo kuhamisha vimelea vya magonjwa, kwa mfano homa ya ini ama virusi vya UKIMWI kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine kwahiyo, nitumie jukwaa lako hili kutoa rai kwa Mangariba wote kwenye makabila ambao wanatoa tohara ya kiasili kuanza kutumia tohara ya kitabibu kwenye hospitali zetu.