Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Rukia Ahmed Kassim (1 total)

Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli Tanzania wa Mwaka 2017
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nikaweza kuchangia katika Muswada huu uliopo mbele yetu. Kabla ya hapo kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kunijaalia nikiwa na uhai na uzima nikaweza kusimama katika Bunge hili Tukufu na nikaweza kuchangia kama hivi nitakavyoweza kusema katika Muswada huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza naishukuru Serikali kwa kuiondoa ile ibara ya 2(2) katika Muswada huu ambao kidogo ungeleta sintofahamu kati yetu sisi Wazanzibari na wenzetu wa huku Mainland kwa kuona kuwa suala hili sio la Muungano.

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo nataka niende kwenye Muswada. Muswada huu NASAC unatokana na neno NASACO. Kwa mujibu wa uelewa na kumbukumbu za huko nyuma tunasikia maana yake mimi nilikuwa ni mdogo, NASACO ilikuwa inafanya kazi vizuri sana. Kwa hiyo, Serikali ilipoleta Muswada huu ikaita jina la NASAC ni kuwa tunategemea nayo itafanya vizuri kama vile ilivyofanya NASACO. NASACO ilifanya vizuri lakini baadaye labda Serikali ituambie kulitokea nini mpaka NASACO mwisho ilishindwa na ikafa kabisa.

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo, NASAC sasa tunaambiwa kama itakuwa yeye ni mdhibiti (regulator) na wakati huo huo atakuwa ni operator. Kwa hiyo, naishauri Serikali vitu hivi vitofautishwe kabisa; kuwe kuna mdhibiti ambaye atadhibiti na pia kuwe na operator ambaye atafanya kazi kama mawakala wengine wa kibiashara, aingie katika mashindano ya kibiashara pamoja na makampuni mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ikiwa Serikali itafanya hivyo, itatofautisha mambo mawili haya, basi nadhani sheria hii itakwenda vizuri na NASAC kama ambavyo tunategemea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye bandari zetu kuna upotevu mkubwa wa fedha na pia kuna wizi mkubwa ambao unafanyika. Wizi huu unatokana na kweli lazima tusifiche ni TRA. Sasa pale palikuwa pana SUMATRA na TPA; nadhani SUMATRA haina kosa na wala haijafanya vibaya, TPA haina tatizo lolote, lakini wizi na upotevu mkubwa ni kwa wenzetu TRA ambao ndio wanaosababisha wizi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa watuambie Serikali je, NASAC itaziba vipi mwanya huu wa upotevu wa pesa ambao unasababishwa na baadhi ya wafanyakazi wa TRA ambao sio waaminifu. Wakishatuambia hilo ndio tutajenga imani kubwa kama kweli NASAC itafanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi na-declare interest kama ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu; wakati tulipokuwa tukiwasikiliza wadau, aliyekuwa Mkurugenzi wa SUMATRA alituambia kama yeye aliwahi kusafirisha kontena sita
akiambiwa ni majani ya chai na kumbe ni bangi. Kwa sababu sheria ilikuwa inawabana SUMATRA hawezi kujua kilichomo ndani ya lile kontena wala TPA hawajui, anayejua ni TRA peke yake. Kwa hiyo, TRA ndio ali-take advantage kusafirisha kitu kile huku akijua kuwa ni bangi lakini ikawa SUMATRA yeye hajui. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa watuambie je, NASAC itaziba vipi mwanya huu wa upotevu wa fedha hizi, kwa sababu sisi tunajua bandarini kuna wizi mkubwa na fedha nyingi sana za Serikali zinapotea bandarini. Ndio maana Serikali inaumia na hili na imetuletea chombo hiki kuja kudhibiti wizi huu. Sasa lakini watufafanulie je, watafanyaje wakati TRA pale ipo na wao ndio source ya matatizo yote tuliyonayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, TRA imesababisha wafanyabiashara wadogo wafe kabisa kibiashara, anapokuja tajiri na mali nyingi pale wanaficha, wanadanganya, hawasemi kilichomo katika yale makontena na badala yake wanawatoza ushuru mdogo tu na wafanyabiashara wakubwa wale wanapitisha mali huku ukiwa ni wizi Serikali inapoteza mapato. Mfanyabiashara mdogo pengine wame-share na mwenzie wameleta kontena moja tu la biashara, watawapiga bakora ya ushuru kiasi cha kuwaambia kuwa nyie nendeni mkafie kwenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawawezi tena kufanya kazi mara ya pili kwa sababu ya ushuru wanaotozwa pale. Sasa NASAC ituambie itawasaidiaje wafanyabiashara wadogo waweze kufanya kazi na wale wakubwa watoe ushuru ambao unastahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, mimi sitaki niende mbele sana katika hili isipokuwa nai-support Serikali kwa kuleta Muswada huu na naipongeza iweze kudhibiti mapato ya Serikali kikamilifu.