Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Shamsia Aziz Mtamba (2 total)

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, pamoja na kupita bomba la gesi katika maeneo mengi ya Mtwara na Lindi, bado vijiji na mitaa mingi haina mtandao wa umeme. Je, ni lini REA III itamaliza tatizo hili kwa mikoa ya kusini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, mkandarasi aliyepewa kusambaza mtandao wa umeme Mtwara yupo slow sana. Je, Serikali inachukua uamuzi gani kwa mkandarasi huyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameuliza; ni lini REA III itamaliza tatizo la kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mtwara. Nataka nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kuwa Mkandarasi wa Mkoa wa Mtwara ni JV Radi Service Limited na ameshalipwa asilimia kumi na yupo Mkoani Mtwara akiendelea na kazi ya upimaji wa njia ya umeme, na kwa kuwa Wizara tumetoa maelekezo kwamba vifaa vyote vya mradi huu REA III vipatikane ndani ya nchi, wakandarasi wanachoendelea nacho sasa ni namna ya kutafuta vifaa vyote na kuagiza ndani ya nchi, na nimhakikishie kazi hii itafanyika kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anaulizia hatua gani zitachukuliwa dhidi ya mkandarasi huyu. Naomba nimwambie ratiba ya REA iko awamu mbili, awamu ya kwanza ni 2017 hii Julai mpaka 2019, kwa hiyo mkandarasi huyu yupo ndani ya muda. Na kwa kuwa amelipwa asilimia 10 na ameanza kazi, nimthibitishie tu zoezi la upelekaji umeme katika Mtwara kwa mkandarasi huyu JV Radi Service itakamilika kwa wakati.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipatia nafasi, ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Tatizo lililopo Lupembe linafanana kabisa na tatizo lililopo Mtwara Mjini, viwanda vingi vimekufa ikiwemo Kiwanda cha Kubangulia Korosho cha Oram ambacho kilikuwa kinatoa ajira kwa wananchi wengi wa Mkoa wa Mtwara. Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua viwanda hivyo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge, kupitia Sera yetu ya Uendelezaji wa Viwanda endelevu, sisi wenyewe kama nchi tuliona kwamba, masuala yote yanayohusiana na uzalishaji yaondoke sasa kwenye mikono ya Serikali iende katika mikono ya sekta binafsi. Jambo ambalo tunafanya sisi ni kuhakikisha kuwa tunaweka mazingira wezeshi kwa kuhakikisha kuwa ile miundombinu inayohitajika pamoja na uunganishaji wa taarifa na vikwazo vyote ambavyo vinawakabili hao wawekezaji viweze kutatuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa korosho, kwanza tunashukuru kwamba kwa sasa hali ya korosho/bei ya korosho imekuwa ni nzuri, lakini sisi kama Taifa tusingependa tu kuuza korosho zikiwa ghafi. Kwa misingi hiyo, tunaendelea kufanya jitihada ya kuhakikisha kuwa viwanda mbalimbali vya korosho vinaimarishwa ili kuhakikisha kuwa tunapata tija katika zao hili.