Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Godfrey William Mgimwa (6 total)

MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la umeme hasa kwenye uunganishaji limekuwa ni tatizo kubwa hasa kwenye maeneo ya mita. Wananchi wengi na wateja wengi wamekuwa wakilalamika kwamba mita ambazo wanafungiwa zinaharibika baada ya muda mfupi. Ningependa kujua kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba je, analifahamu hili na kama analifahamu, hatua gani zitachukuliwa, ili kuhakikisha kwamba, utaratibu huu mbovu unasitishwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Jimbo la Kalenga limekuwa lina changamoto kubwa katika masuala haya ya umeme na nina vijiji kadhaa ambavyo mpaka dakika hii viko gizani na vinahitaji umeme. Kijiji cha Lupalama katika Kata ya Nzii, Kijiji cha Kipera, Kijiji cha Itagutwa, Kijiji cha Magunga na Lyamgungwe; ningependa kusikia commitment ya Mheshimiwa Waziri, je, ana utaratibu gani na mpango gani kuhakikisha kwamba, vijiji hivi vinapata umeme? Na kama je, yuko tayari kuungana na mimi kwenda moja kwa moja Kalenga ili kuweza kuwapa hamasa wananchi wangu? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, wakati REA wanapofunga umeme ni mara nyingi sana imekuwa ikitokea kwamba zile mita inaonekana kama hazina nguvu, tatizo siyo kwamba mita ni mbovu, tatizo tu ni kwamba umeme unaokuja ni wa low voltage.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge ni vizuri tukawaeleza baada ya REA kuunganisha umeme sasa, umeme tunaotumia ni wa low voltage ambao ni kilovolt 30 na mwingine 11 zaidi ni 132. Kuanzia Julai mwaka huu kuna mradi sasa wa kuongeza nguvu za umeme ambao ni kilovolt 400 utapita kwenye maeneo ambayo tuliyataja. Kilovolt 400 zitakapoingia na kuanza matatizo ya kukatika kwa umeme kwenye tatizo la mita yatakoma mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na vijiji alivyotaja Mheshimiwa Mgimwa, vijiji vitano vya Lupalama, Lupelo, Magunga na vingine ni kweli kabisa havijapata umeme na tulishavitembelea, kwa sasa tumezungumza na Mheshimiwa Mgimwa, kati ya vijiji vitakavyoanza kupatiwa umeme kwenye Jimbo lake tutaanza na hivi vijiji vitano ambavyo Mheshimiwa Mgimwa amevitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ameomba sana tupate fursa ya kutembelea kule mimi pamoja na Mheshimiwa Waziri tumekuwa tukitembelea sana maeneo ya Morogoro, hata hivyo, bado tumhakikishie baada ya Bunge lako Tukufu kuisha mimi na Mheshimiwa Mbunge bado tutakwenda kutembelea zaidi, hata akisema mara tano bado tutakwenda kuhakikisha wananchi wanapata umeme.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuweka minara kwanza niipongeze sana Serikali kwamba imeendelea kupeleka minara katika Jimbo la Kalenga kwa kasi zaidi. Tatizo ninalolipata ni kwamba baada ya kusimikwa ile minara upatikanaji sasa au uanzaji wa kuanza kupata mawasiliano unatumia muda mrefu sana. Ningependa kujua Serikali ina mkakati gani ili mara baada ya kuwekwa ile minara mawasiliano yaanze kupatikana kwa muda unaostahili. (Makofi)
Swali langu la pili, narudi tu kwenye majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba amesema vijiji vilivyotamkwa hapa mwishoni vya Kaning‟ombe na Ikuvilo vitapita katika utaratibu wa kupitia UCSAF lakini katika tovuti ambayo nimekuwa nikiipitia ya UCSAF nitoe tu statistics kidogo inaonyesha kwamba kwa mwaka 2015 zilitangazwa zabuni175, Kata zilizopata wazabuni 116 hii kwa ni Tanzania nzima, idadi ya vijiji 156, miradi kuanza ilikuwa ni Mei, 2015. Lakini katika orodha hii yote hakuna vijiji ambavyo tayari vilishaanza kupatiwa mawasiliano ni zero, kupitia mradi ya UCSAF.
Ningependa kujua Serikali ina mikakati gani kuhakikisha kwamba inaipa pesa UCSAF ili kwamba miradi ambayo imeorodheshwa iweze kukamilika kwa wakati? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mgimwa naomba nikiri kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwahangaikia watu wake, anafanya hivyo katika maeneo mengi ambayo Wizara yetu inaisimamia ikiwa ni pamoja na barabara, mawasiliano hayo ambayo leo ameyauliza na masuala mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie kwamba yale tunayomweleza anapofuatilia ofisini tunamthibitishia kwamba tutayatekeleza. Nimhakikishie kwamba Awamu hii ya Tano ya Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli inatenda inachoahidi. Mkakati wa kuhakikisha minara ambayo inajengwa inaanza kufanya kazi tutaifuatilia, kwa hili aliloliuliza nadhani ameuliza tu kuongezea utamu, tumemwambia kwamba mnara huo utaanza kufanya kazi mwishoni mwa mwezi Juni kama tulivyoongea, ni kweli na tutafuatilia. (Makofi)
Kuhusu mirafi ya UCSAF, naomba nimhakikishie kama nilivyosema hii Serikali inatenda inachoahidi, katika mwaka huu wa fedha hizo zilizotengwa miradi iliyotangazwa tutahakikisha inakamilika. Lakini usisahau kwamba miradi mingine tuliyoongelea hapa haitekelezwi na UCSAF peke yake mingine inatekelezwa na TTCL na Viettel ambayo katika tangazo hili miradi hiyo hutaiona.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Tatizo ambalo lipo katika Jimbo la Mheshimiwa Mendrad Lutengano, ni sawasawa na tatizo ambalo liko katika Jimbo langu la Kalenga. Ningeomba kujua Miradi ya Maji ya Weru, Itengulinyi, Supilo, itakamilika lini kwa sababu wakandarasi wamekuwa wakipiga makelele na kudai pesa zao za malipo?
Ningependa kujua kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, ni lini sasa Wakandarasi hawa watalipwa, ili kwamba, miradi iweze kuendelea na wananchi wangu waweze kupata maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna miradi ya maji mingi sana ilisimama. Wakandarasi wali-demobilize mitambo kutoka maeneo ya miradi na sababu kubwa ilifanya kwamba, flow ya fedha, wakandarasi walifanya kazi walikuwa hawajalipwa, certificates zilienda Wizarani, lakini watu walikuwa hawajalipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu letu kubwa tulilofanya ni kuhakikisha pesa zinakusanywa kama nilivyosema awali. Hivi sasa nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge wakandarasi wote karibuni sasa hivi kila Halmashauri pesa sasa zimeshapelekwa, ilimradi wakandarasi waweze kurudi site.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilikuwa na Naibu Waziri wa Maji hapa tukifanya mjadala katika hayo, imeonekana sasa hivi hali imeenda vizuri zaidi. Kama tutafanya analysis kama huko Makete kama watu hawajaanza kurudi site, lakini ni kwamba kweli wakandarasi walitoa mitambo mwanzo, lakini fedha sasa hivi baada ya makusanyo mazuri tumeshapeleka site huko ilimradi wakandarasi walipwe, kazi iweze kuendelea. Tutaangalia kama huku katika Jimbo lako kama kuna matatizo kidogo bado yapo, tutaangalia jinsi gani tutafanya kuyatatua kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hili niweze kuzungumzia hata pale kwa ndugu yangu wa Mufindi pale, ndugu yangu Mheshimiwa Chumi, kulikuwa na suala la pampu pale, tumefanya harakati, hivi sasa ile pampu inafungwa baada ya kupata uhakiki wa kutosha. Lengo letu ni kwamba, miradi yote ikamilike na wananchi waweze kupata maji.

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri – TAMISEMI, kuhusu Jimbo la Kalenga tayari nimeshaongea na Mheshimiwa Mbunge na tumeangalia vitabu, tumeshapeleka shilingi milioni 365. Nikawa nimemuomba Mheshimiwa amfahamishe Mkurugenzi kwamba, kama kuna certificate zozote walizonazo mezani watuletee, ili tuweze kukamilisha malipo Wakandarasi waendelee na kazi.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa, tatizo ambalo linaonekana la kuwanyanyasa wananchi ambalo linafanywa na Polisi linafanana sana na malalamiko mbalimbali ambayo yanatoka katika Idara ya Uhamiaji kwamba Idara ya Uhamiaji nao wanafanya unyanyasaji mkubwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ningeomba kujua kwa sababu katika Idara hii kuna watumishi ambao hawajalipwa mishahara yao kwa kipindi kirefu sana. Serikali inasema nini au ina tamko gani kuhusu watumishi hawa wa ajira mpya ambao hawajalipwa mishahara yao ili Serikali iweze kutoa majibu yanayoeleweka, kwamba watalipwa lini mishahara yao watumishi hao wa ajira mpya?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza suala la watu kunyanyaswa lina pande mbili. Sisi tumesema yale ambayo tunajiridhisha nayo tunachukua hatua, lakini suala la kutimiza wajibu ni suala la Watanzania wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Askari wapya ambao hawakuwa wamelipwa mishahara yao, nimhakikishie Mbunge kwamba tatizo hilo kweli lilikuwa kubwa na niwaombe radhi wale askari wetu ambao wamefanya kazi kwa muda bila kupata haki yao, kwa sababu mshahara na posho siyo hisani ni haki yao. Serikali imeshafanya kazi kubwa. Mwanzoni kulikuwa na idadi kubwa waliokuwa wanadai zaidi ya 297, lakini Askari 181 tayari walishapewa mishahara yao na watapewa na yale ambayo yalikuwa malimbikizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na tatizo ndani ya Wizara na nilishatoa maelekezo. Kuna watu bado wanafanya kazi kwa mazoea wakidhani labda Askari anatakiwa aishi kimsoto msoto hivi. Hakukuwa na sababu ya kutokupeleka majina yale Utumishi na kuyaingiza kwenye mfumo ili waweze kulipwa. Kuna watu kwa sababu zao wenyewe na nilielekeza wachukuliwe hatua, wamekaa na majina hayo kwa muda mrefu bila kupeleka Utumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naelekeza kwa wale wachache ambao walikuwa bado wanafanyiwa uhakiki waharakishe haraka, wale wanaostahili waweze kulipwa na walipwe na malimbikizo yao ili waweze kufanya kazi bila manung’uniko.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya kupeleka mawasiliano katika Jimbo langu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, swali hili nimeuliza mwaka 2014 nikajibiwa kwamba 2015 nitapata majibu ya uhakika, sikupata majibu. 2015 nikapata nafasi ya kuuliza nikaambiwa 2016, leo hii ni 2017 naambiwa ni 2018. Naomba niweze kupata majibu ya uhakika leo kwamba ni lini sasa vijiji hivi vilivyoorodheshwa vitapata minara ya simu na wananchi wangu waweze kupata mawasiliano hayo ya simu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; katika minara ya simu ambayo inajengwa katika maeneo mbalimbali katika Jimbo langu la Kalenga service levy hailipwi moja kwa moja kwenye Halmashauri, inaenda kulipwa kwenye makampuni yenyewe ambayo mengi yapo Dar es Salaam. Wananchi katika Jimbo langu wanakosa mapato ya ndani kutokana na minara hiyo ya simu. Ningependa kujua kutoka Wizarani, je, ni namna gani sasa wanaweza kuwapelekea fedha hizi wananchi ambao nao wanatakiwa kwa namna moja au nyingine waweze kupata faida kutokana na minara hii ya simu, kwa sababu inayotumika pale ni ardhi?
Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba fedha ambazo yanapata makampuni haya au faida ambazo zinapata kampuni hizi zinakwenda pia kuwasaidia wananchi katika maeneo husika? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, tunapojibu maswali hapa huwa tuna dhamira ya dhati ya kutekeleza kile tunachokijibu na kwa kawaida Wizara huwa tunajiandaa kujipanga kutekeleza kile ambacho tunakijibu hapa. Inapofika wakati wa bajeti inaweza ikatokea kama ilivyotokea kwa eneo hili kwamba Mfuko wetu wa Mawasiliano kwa Wote huwa unakosa fedha, unapokosa fedha tunatarajia tuifanye hiyo kazi mwaka unaofuata, hiyo inabakia dhamira yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba dhamira yetu ni kuhakikisha vijiji hivi kama tulivyosema katika jibu la msingi, tunavitekeleza katika mwaka huu wa 2017/ 2018 na fedha tunatarajia kuziomba na tunaamini mtazipitisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ile minara ya simu pale inapojengwa kwa kawaida yale makampuni yanaingia mikataba na ama vijiji au mwenye ardhi husika, kwa kawaida Wizara hatuingilii sana katika mikataba hii ya kulipa gharama za ardhi inayotumika na wawekezaji katika minara ya simu. Hata hivyo, nalichukua wazo lake au pendekezo lake ili tuangalie namna gani Wizara inaweza kusaidia katika kuhakikisha minara hii ambayo imewekwa katika Jimbo hili la Kalenga inatumika na inawanufaisha wananchi kupitia mikataba yao ambayo wameweka.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nitakuwa na swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Halmashauri nyingi zimekuwa hazitengi fedha hizi kwa ajili ya vijana na akina mama; lakini vile vile tuna tatizo sasa hivi ambalo tungekuwa makini zaidi kuliangalia suala la ndugu zetu walemavu, kwamba kuweze kuwa na uwezekano sasa wa kuzitenga fedha kutoka katika hizi asilimia 10 kwa ajili ya walemavu, vijana na akina mama.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa sababu majibu ya msingi yameshatolewa ningependa kufahamu kwa hizi Halmashauri ambazo kwa ujumla zimeshindwa kutenga fedha hizi kwa ajili ya vijana kama mimi akina mama; na kama tulivyoongea kuhusu walemavu ningependa kufahamu sasa.
Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba inazibana halmashauri hizi ili ziweze kupata mapato ya ndani kwa uhakika na kuhakikisha kwamba inatenga fedha hizi kwa ajili ya makundi haya? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali la nyongeza ambalo linawagusa akina mama na vijana nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kupitia Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI ameshatoa waraka tangu mwaka jana mwezi wa saba kuelekeza Halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba wanatenga asilimia 10 kwa ajili ya mikopo ya vijana na wanawake na hilo ndiyo maana nimesema hapa kupitia Bunge lako Tukufu kwamba ni lazima watenge na wasipotenga sasa Serikali itaanza kuchukua hatua za kiutumishi dhidi ya Wakurugenzi ambao hawatengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kwa sababu kinachotakiwa kufanyika ni kutenga kile ambacho kimekusanywa, kama kimekusanywa bilioni 10 basi asilimia 10 ya bilioni 10 lazima itengwe kwa ajili ya wanawake na vijana. (Makofi)