Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Rehema Juma Migilla (2 total)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naishukuru Kamati yangu ya Guantanamo ambayo imeshiriki kwa namna moja katika kuleta taarifa hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mwanakamati nitajikita zaidi katika suala la elimu. Ni wazi kuwa Serikali yetu ipo katika hatua za kuelekea katika Tanzania ya viwanda, lakini hatuwezi kufikia Tanzania ya viwanda bila kuwa na wataalam ambao wataenda kuvihudumia hivi viwanda. Wataalam hao ni wanafunzi na hawa wanafunzi hawawezi kupata yale yanayohitajiwa kama hawatakuwa na walimu wazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi walimu wamekuwa na changamoto nyingi sana zinazosababisha mpaka morale ya kufanya kazi ipotee. Sababu mojawapo kwanza ni kudhalilishwa kwa walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi walimu wanadhalilishwa sana kana kwamba hawana taaluma, leo hii na siku za nyuma baadhi ya ma-DC, ma-RC hata Wakurugenzi wamekuwa ni watu wa kuwadhalilisha walimu, wanawatandika fimbo, kuna walimu wameshadekishwa vyumba vya madarasa, kwa kweli hali hii inasababisha mpaka morale ya kazi ipungue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine la kushusha vyeo walimu. Hili suala limekuwa sasa hivi ni too much. Mwalimu mwenye professional yake, leo kwa sababu ambazo ziko nje ya uwezo wake, anashushwa cheo na Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya, eti tu kwa sababu shule imefelisha, je, anayefanya mtihani ni Mwalimu au mwanafunzi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba majibu ya Serikali, kazi au majukumu ya kushusha vyeo au kutoa nidhamu na maadili kwa walimu yako chini ya Tume ya Utumishi wa Walimu, sasa nataka nijue, hili jukumu la kushusha vyeo walimu linachukuliwa na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, je, mmeinyang’anya madaraka Tume ya Utumishi wa Walimu na kuwapa hawa viongozi wa Serikali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine linalochangia hadi kuzorota kwa elimu yetu ni kuchanganywa kwa kauli mbalimbali zinazotolewa na viongozi wetu wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa juzi kulikuwa kuna kauli mbalimbali zinazotolewa na viongozi wa Serikali, mfano Mheshimiwa Rais alisema kwamba walimu wasihamishwe kutoka kituo kimoja kwenda kituo kingine mpaka pale atakapopewa mafao yake ya uhamisho. Ghafla kuna kauli imetolewa tena na Wizara ikisema kwamba kuna Walimu wanahamishwa kutoka sekondari kwenda primary.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma, hata kama ukimhamisha kutoka kituo ‘A’ kwenda ‘B’….

T A A R I F A . . .

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu ni Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ila hiyo ni a.k.a. (alias known as). (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine linalochanganya pia ni huku huku kuendelea kupotoshwa au kauli tatanishi. Leo hii Serikali ilisema kwamba hakuna kurudisha watoto shule za msingi mpaka sekondari, lakini leo hii hii Serikali inasema hakuna kukaririsha. Hivi tuelewe lipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tukirudi tena kwenye suala lingine la hizi hizi kauli, Waraka wa Elimu Namba Tatu wa mwaka 2006 umetamka wazi majukumu ya kila mdau wa elimu kuanzia wazazi, Wakuu wa Mikoa hadi na walimu, lakini leo hii Mheshimiwa Rais anasema mzazi asihusishwe kwa mchango wa aina yoyote. Sasa je, hii michango ambayo inapaswa itolewe na wazazi au Serikali inaposema elimu bure, hii ni elimu bure au elimu bila ada? Tunaomba majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia point nyingine kwamba sababu nyingine zinazochangia kuwepo kwa udororaji wa elimu ni kutolipwa kwa madai ya walimu kutokana na vigezo mbalimbali mara uhakiki wa watumishi hewa, mara uhakiki wa wenye vyeti fake, sasa tunataka tujue huu uhakiki wa wenye vyeti fake na watumishi hewa utaisha lini ili hawa walimu waweze kulipwa madeni yao mbalimbali kama madeni ya uhamisho, madeni ya kupanda madaraja nauli na vitu mbalimbali? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niendelee kuhusu uendeshaji wa shule za private. Shule hizi hazipo kwa kuwa tu eti zimejiamulia zenyewe. Shule hizi za private zimeanzishwa kwa kufuata kanuni na taratibu mbalimbali mojawapo ikiwa ni kupata usajili toka Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Serikali imeanza kuziingilia hizi shule. Shule hizi zimewekeza, zinalipa ada na mzazi mwenyewe ameguswa, hakuangalia gharama, hakuangalia masharti mbalimbali akaamua kupeleka mtoto kwa matakwa yake yeye mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii shule za private wanaambiwa wasikaririshe watoto. Wakati mwanzo walipewa masharti na wakakubali na Serikali ikawapa usajili, lakini leo hii haieleweki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nijue, hii Serikali ina mpango wa kuturudisha kule kwenye idadi ya kuongeza division four na tukose division one au two...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi jioni hii nichangie kuhusu Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Utumishi na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze Mawaziri wote Wizara hizi mbili, Mheshimiwa Jafo na timu yake Mheshimiwa Kakunda na Mheshimiwa Kandege, lakini vile vile Mheshimiwa Mkuchika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Naanza kuchangia kama ifuatavyo na nianze na suala la elimu. Ni ukweli usiopingika kuwa elimu yetu kwa sasa imedolora na inashuka kiwango siku hadi siku. Hii inatokana na ukweli kwamba nchi yetu imeifanya elimu kama huduma na kuwaandaa watu kuwa ni wa kufaulu mitihani tu na si kwenye uwekezaji. Kama nchi haina kipaumbele kwenye elimu na inaifanya elimu kama huduma obviously hatuwezi kufika mbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali yetu, kama kweli tunataka elimu yetu ikue naomba sana ijikite kwanza kuifanya elimu ni uwekezaji na badala ya huduma. Vilevile ili elimu hii iweze kuwa na tija kwa hawa vijana ni lazima basi hii mitaala ya elimu ifanyiwe reformation, kwa sababu sasa hivi ukiangalia inawaandaa tu wanafunzi kufaulu mitihani, lakini hakuna ujuzi wowote inayowapatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kijana anamaliza darasa la saba, anamaliza form four, anamaliza form six mpaka Chuo Kikuu hana ujuzi wa aina yoyote, matokeo yake kila siku wanatembea na bahasha mitaani mpaka zinapauka. Naiomba Serikali yetu kama kweli tunataka tujikite katika elimu basi haya ninayoyasema, mitaala ifanyiwe reformation na ijikite zaidi katika kuwapa wananfunzi skills ili wahitimu hawa wanapomaliza, kama ni kidato cha nne basi ajue anatoka na ujuzi gani badala ya kuwa anazurura mitaani. Leo hii vijana hata wa chuo kikuu badala ya kuwa ni job creators wamekuwa ni job seekers, naomba hili suala tuliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya ualimu na walimu. Kazi hii ya ualimu inaonekana kama ni kazi ya watu waliofeli, mimi ni mwalimu by profession, inaniuma sana jamii inaiona hii kazi ya ualimu kama ni kazi ya waliofeli. Hii inajidhihirisha unapoangalia kwenye matokeo hata ya form four, division one, division two wanaenda high school, halafu divison three hadi four ndio wanaopelekwa ualimu. Kama tanataka kweli tuwekeze kwa nini hii division one na division two ndio wasipelekwe ualimu? Mpaka jamii inamuona mwalimu ni mtu mjinga mpaka inafikia anaulizwa yaani umekosa hata nafasi ya kwenda kwenye ualimu! Jamani ualimu ni kazi kama zilivyo kazi zingine wote tuliomo humu tumepita kwa mwalimu kwa nini huyu mwalimu leo hathaminiki? Naomba Serikali impe hadhi mwalimu kama inavyompa mtu mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwalimu wa Tanzania ana changamoto nyingi sana ambazo zinamkumba. Leo hii walimu wamekosa morali wa kufanya kazi na takwimu zinaonesha wanafanya kazi chini ya kiwango, yote hii inasababishwa na Serikali kwa kutowajali walimu. Walimu wana stahiki nyingi sana ambazo wanazidai lakini Serikali haitekelezi. Wana madeni ya arrears, wana madeni ya nauli, ya nini Serikali haitekelezi. Nataka nijue leo hii Serikali inatumia vigezo gani pindi inapowalipa hawa wafanyakazi au walimu stahiki zao mbalimbali. Kwa mfano katika Jimbo la Tabora mjini kuna hizi shilingi bilioni mia mbili zilizotolewa na Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kuwalipa walimu, lakini ni walimu 18 tu ndio wamelipwa wakati kuna idadi kubwa ya walimu hawajalipwa. Sasa nataka TAMISEMI mtuambie ni vigezo gani ambavyo mnavitumia kuwalipa hawa walimu stahiki ili hali wana madeni mengi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa kuanzisha elimu bure, elimu bure inaende sambasamba na kutoa posho kwa walimu wakuu wakuu wa shule na waratibu wa elimu kata. Hata hivyo ndugu walimu wana mishahara midogo sana. Tunaomba basi katika hii posho mnayowapa walimu sijui wakuu wa shule ma-headmaster na waratibu wa elimu kata basi na walimu na wenyewe wapewe hata kidogo, kwa sababu hawa wakuu wa shule mnaowapa pesa hawafanyi kazi peke yao wanafanya kazi na walimu wengine, nao tunaomba muwape hata kidogo kama motisha ya kuweza kufanya kazi vizuri na kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nizungumzie mchakato wa kuhamisha walimu wa sekondari wa arts na kuwapeleka primary. Mheshimiwa Haonga amesema ni ukweli usiopingika ni wazo zuri, lakini approach inayotumika sio nzuri. Walimu hawa walivyokuwa wanasoma kwenye vyuo vyao walisomea masomo mawili, leo hii unawaambia wakafundishe kule watafundisha kitu gani? Mbaya zaidi hakuna hata induction course ambayo mmewaandalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali basi angalau iwape induction course hawa walimu ili waweze kwenda kufundisha kwenye mazingira yale. Tukumbuke kwamba walimu hawa wamekuwa trained kufundisha wanafunzi wenye kimo kikubwa, leo wakafundishe watoto wadogo wataweza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado njia za ufundishaji watoto wa sekondari ni tofauti na watoto wa primary. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali yetu kama kweli tunadhamiria kuinua kiwango hiki cha elimu, japokuwa ni approach, nzuri basi hawa walimu wapatiwe induction course angalau ya mwezi hata mmoja kwenye methodologies. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nizungumzie hii Tume Utumishi wa Walimu. Tume hii inafanya kazi kubwa sana na naiomba Serikali iiongezee pesa ili iweze kufanya kazi yake kwa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye kazi nyingine ambayo inafanywa na Wizara ya TAMISEMI. Kazi moja wapo ni kuhakikisha inatatua migogoro inayotokana na ardhi. Mkoa wa Tabora hususani Manispaa ya Tabora walikumbwa na bomoa bomoa, watu hawa walijenga katika maeneo ambayo walipewa kisheria na bado Serikali yetu ikaweka hadi miundombinu kule na bado walikuwa wanachukua hadi kodi lakini leo hii hawa watu wanaambiwa wahame lile eneo ilhali walipimiwa na Serikali na wako pale kisheria lakini hatuoni dalili zozote za kupewa fidia au kutafutiwa eneo jingine. Naiomba sana Serikali iwanusuru watu hawa, tunaomba basi watu hawa wapatiwe eneo jingine au wapewe fidia waweze kuanza maisha mengine mapya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni katika uwezeshaji wa vikundi vya wanawake na vijana, ile asilimia 10 ya mapato ya ndani. Hizi asilimia zipo kisheria lakini halmashauri zimekuwa hazitengi pesa kwa ajili ya kuwapatia vijana, hali inayopelekea vijana sasa hivi wafanye kazi ambazo ni tofauti na ndoto zao. Tunajua kabisa kila mmoja ana kazi ya ndoto yake, lakini vijana wengi sasa hivi wanafanya kazi ya kuendesha boda boda, wanawake wengi wamekuwa bar maid ni kazi ambazo ziko nje ya ndoto zao. Kama Serikali itahimiza halmashauri kutenga asilimia 10 vijana hawa watanufaika na wataacha kuhangaika huko mitaani. Tunaiomba Serikali hizi halmashauri zisizipe mzigo mkubwa yaani mapato yarudi kule kwenye Serikali za mitaa badala ya kwenda Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ni kuhusu utumishi. Tulipiga kelele sana kuhusu watumishi wa darasa la saba. Ni kweli kabisa watumishi hawa waliajiriwa na Serikali na Serikali hii ndio tena ikawatoa kazini, lakini Serikali hii tena imewarudisha kazini, ni jambo zuri na wazo zuri, lakini suala langu ni hili, je, Wizara ina mpango gani au itawalipa kwa fungu lipi watu ambao hawajafanya kazi kwa muda mrefu sana? Pia kuna watu ambao tayari walishaajiriwa ku-cover hizi nafasi za watu walioko darasa la saba, je, hawa watu ambao sasa wameshaajiriwa kuziba zile nafasi za watu wa darasa la saba watatolewa kazini au vipi? Naomba majibu.