Contributions by Hon. Dr. Advocate Damas Daniel Ndumbaro (25 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa na inastahili pongezi kwa kufanya mambo yafuatayo katika Jimbo la Songea Mjini. Ujenzi wa barabara kilomita kumi kwa kiwango cha lami, kuboresha elimu na kuboresha huduma za afya. Pamoja na hayo Jimbo la Songea Mjini linakabiliwa na changamoto zifuatazo:-
(i) Ukosefu wa vituo vya afya katika Kata za Ruvuma, Lilambo na Ndilimalitembo;
(ii) Ukosefu wa ambulance na X-ray katika Kituo cha Afya cha Mjimwema ambacho kinahudumia zaidi ya wagonjwa 100,000 kwa mwaka;
(iii) Ujenzi wa Mtwara Corridor by-pass katika eneo la Jimbo la Songea Mjini;
(iv) Upatikanaji usioridhisha wa pembejeo za kilimo kama vile mbolea na bei elekezi ambayo inabadilika kila kukicha;
(v) Soko lisilo na uhakika la mazao kama vile mahindi na mbaazi;
(vi) Ukosefu wa barabara ya uhakika (lami) inayounganisha Mji wa Songea na Jimbo la Lichinga – Msumbiji;
(vii) Ukosefu wa barabara ya lami inayounganisha Mkoa wa Ruvuma na Morogoro;
(viii) Ukosefu wa viwanda vya kusindika bidhaa za kilimo; na
(ix) Malipo ya fidia kwa wananchi waliohamishwa Songea Airport; wananchi wa eneo la EPZA Mwenge mshindo na wananchi wa eneo la Bonde la Mto Luhira.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuchangia kwenye bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria. Awali ya yote namshukuru Mheshimiwa Waziri na Watendaji kwa taarifa nzuri ya bajeti ambayo wametuletea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nitoe shukrani kwa Mheshimiwa Waziri na watendaji wote wa Shule Kuu ya Sheria kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuchuja wanasheria na kada hii ya sheria ili tuwe na wanasheria wazuri. Pamoja na mambo hayo yote, kuna changamoto nyingi ambazo zinaikabili Shule Kuu ya Sheria.
Kwanza, bajeti finyu. Kwenye bajeti ya matumizi mengineyo, tukumbuke kwamba Shule Kuu ya Sheria inahudumia takribani vyuo vikuu 17 ambavyo vinatoa wahitimu wa shahada ya kwanza ya sheria, lakini bajeti yake ni ndogo katika matumizi mengineyo na haifiki hata asilimia
22. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna tatizo la kisheria. Ukisoma kifungu cha 15 (1)(d) ya Sheria ya Shule Kuu ya Sheria Na. 18 ya 2007, imeanzisha Governing Council ambapo Wajumbe wake, mmoja kati ya Wajumbe ni Mkuu wa Kitivo cha Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama nilivyosema, kuna vyuo vikuu 17 vinavyotoa shahada ya kwanza ya sheria, ni kwa nini sheria hii imetoa upendeleo kwa chuo kikuu kimoja kupeleka Mkuu wake wa Kitivo katika Governing Council wakati tuna vyuo vikuu 17. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati sheria hii inataungwa mwaka 2007, hivi vyuo vingi vilikuwepo. Kwa hiyo, ni mapendekezo yangu Mheshimiwa Waziri akiona inafaa, itendwe haki jinsi ya kupata mwakilishi wa Vitivo vya Sheria vya Vyuo Vikuu vyote Tanzania badala ya kupendelea chuo kikuu kimojan kwa sababu upendeleo huo ni ubaguzi ambao unapingwa kikatiba kwa mujibu wa Ibara ya 13(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya pili kwa Wizara hii ni suala la usajili wa vyeti vya kuzaliwa. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ametueleza kwamba ni asilimia 28 tu ya watoto wote wanaozaliwa wanaandikishwa na kupata vyeti. Hivyo tuna upungufu wa asilimia 72. Upungufu huu ni mkubwa sana, tuna kila sababu ya kuwa- address upungufu huu kuhakikisha kwamba kila mtoto anayezaliwa anapata cheti cha usajili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zilizopo katika kiambatisho ‘D’ ukurasa wa 94 kinatupa mshtuko ambao inabidi Wizara na Serikali iangalie vizuri zaidi. Katika mikoa 26 takwimu zimeonesha kwamba ni mikoa 12 tu ndipo takwimu zake zimeonesha pale. Kuna mikoa 14 haijaonesha ule usajili wa under five years jinsi ulivyofanyika. Katika hiyo mikoa 14, upo Mkoa wa Ruvuma na Jimbo la Songea. Kwa hiyo, hii inaonesha kwamba watoto hawa wa under five years wanakosa haki zao za msingi katika kusajiliwa mara baada ya kuzaliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosa haki huko ni kukiuka Ibara ya 7 ya Tamko la Haki za Watoto Duniani la mwaka 1989, ni kukiuka Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini pia ni kukiuka kifungu cha 6(3) cha Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, Sura ya 13. Ni ushauri wangu kwa Serikali na kwa Wizara kwamba ni muhimu sana kuhakikisha kwamba suala la usajili wa under five years linafanyika nchi nzima ili kuhakikisha kwamba siyo tu tunapata takwimu, lakini pia tunatekeleza haki za watoto hao kama zilivyoelezwa katika nyaraka hizo za kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nieleze kuhusiana na ukosefu wa Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara. Katika hotuba nzima aliyoelezea Mheshimiwa Waziri Profesa Kabudi, sijaona mahali ambapo ameelezea kuwepo au kuanzishwa kwa Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa Migogoro (International Commercial Arbitration).
Mheshimiwa Mwenyekiti, tufahamu kwamba mikataba mingi ambayo tunaingia kama nchi, tunalazika kuweka arbitration clause ya kupeleka migogoro yetu ya kibiashara katika nchi mbalimbali duniani, nchi ambazo hatujui mambo yao ya kisheria yakoje, systems zao ni ngumu, matokeo yake tunakuja kupata maamuzi ambayo yanakuja kutuathiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na hilo, ni ushauri wangu kwamba ni vizuri tuwe na Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa Migogoro hapa nchini ambacho kitasaidia sana kutatua migogoro mingi ya kibaishara na sisi tulazimishe. Nchi jirani kama Rwanda wameanzisha Kigali International Arbitration Center ambayo inakuja kwa juu sana. Tusipokuwa makini itachukua districts zote katika Afrika Mashariki na Kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi tunapaswa kujipanga kuhakikisha kwamba tunaanzisha kituo hicho ambacho kina faida. Sheria nyingi ambazo tumezitunga za kulinda rasilimali za nchi hii ambazo ni nzuri sana, tunahitaji kuzilinda zaidi kuwa na mifumo ya utatuzi wa migogoro ambayo tunaiamini na inaeleweka. Hivyo, kuanzishwa kwa kituo kama hicho, hakuepukiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kama hicho kikianzishwa ni muhimu sana kwa kusaidia wataalam wa ndani kujenga uwezo wao katika utatuzi wa migogoro ya kibiashara ya Kimataifa. Kituo kama hicho kikiwepo hapa ndani kitatuokolea fedha nyingi sana ambazo tunatumia kwenda kutatua migogoro katika nchi mbalimbali. (Makofi)
Hivyo basi, ni ushauri wangu Mheshimiwa Waziri na Wizara nzima waone umuhimu wa kuanzisha kituo kama hicho. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima na afya njema kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuchangia hoja iliyo mbele yetu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua nafasi ya kipekee, kama wenzangu walionitangulia, kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake madhubuti na makini unaoendelea kugusa, siyo tu wananchi wa Tanzania, bali wa kuigwa katika nchi za Bara la Afrika na dunia kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa uongozi wake ndani ya Bunge hili. Aidha, napenda kuwapongeza sana Mheshimiwa Spika na Naibu Spika kwa namna ambavyo mnaliongoza Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kumpongeza kwa kipekee, Mheshimiwa Prof. Palamagamba Aidan Mwaluko Kabudi, Mbunge, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwa uongozi makini na kuhakikisha tunapata ufanisi mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara anayoiongoza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Andrew Chenge, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu na Mheshimiwa Najma Martaza Giga kwa namna wanavyoonesha uwezo mkubwa wa kuongoza Bunge katika kipindi hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Kamati ya NUU kwa ushauri na maoni yao katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Pia nawashukuru sana Wabunge wenzangu wote kwa ushirikiano wao wanaoendelea kunipa. Nawaombea kila la heri katika utekelezaji wa majukumu yao hapa Bungeni na kwenye majimbo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya kipekee, napenda kuwashukuru wananchi wenzangu wa Jimbo la Songea Mjini kwa imani kubwa wanayonipa na wanayoendelea kuionesha. Nitaendelea kuwa nao karibu na kushirikiana nao katika kuleta maendeleo makubwa na naahidi kuwa sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishukuru sana familia yangu, ikiongozwa na mke wangu mpendwa, Flora Ndumbaro, kwa uvumilivu kwangu na kwa namna wanavyonisaidia na kuniunga mkono katika majukumu yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, shukrani za dhati ziende kwa Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Mabalozi, Wakurugenzi, Watumishi na wasaidizi wangu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa ushauri na msaada wao katika utekelezaji wa majukumu yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, nianze sasa kujibu hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Kwanza, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Ni dhahiri kwamba michango yao itatusaidia sana katika kufanikisha shughuli za Wizara na kuimarisha ufanisi wa utendaji wa Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya kwanza ambayo napenda kuiongelea ni suala la kuondoka kwa Balozi wa Jumuiya ya Ulaya hapa nchini. Mtoa hoja alisema Serikali ieleze ni kwa nini iliweka shinikizo la kumwondoa Balozi huyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara na kama Serikali tulipokea tamko kutoka ka wenzetu wa Jumuiya ya Ulaya mnamo tarehe 5 Novemba, 2018 likisema kwamba limemuita Balozi huyo nyumbani kwa majadiliano. Suala la kuja Balozi yeyote hapa nchini, kuishi kwake na kuondoka kwake kunaratibiwa na Mkataba wa Vienna unaohusu mahusiano ya kidiplomasia wa mwaka 1961. Katika mkataba huu, nchi ambayo imemleta Balozi huyo ina mamlaka ya kumwondoa pasipo kutoa sababu kwa nchi nyingine yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tulipata taarifa ya kuondoka kwa Balozi huyu hatukupewa sababu yoyote ile. Hivyo, kututaka leo tutoe sababu wakati sisi siyo tuliomwondoa na sisi hatukuambiwa ni kwa nini ameondoka, siyo sahihi. Waliomwondoa ndiyo wako kwenye nafasi ya kutoa sababu ni kwa nini walimuondoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna hoja ya Brexit. Mtoa hoja amesema Serikali itoe msimamo wake kuhusiana na hoja ya Brexit. Brexit ni hatua ya Uingereza kujitoa katika Jumuiya ya Ulaya. Sisi tuna mahusiano mazuri na Jumuiya ya Ulaya na Uingereza lakini pamoja na mahusiano hayo mazuri hatuingilii mambo yao ya ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu za Uingereza kujitoa zinamhusu yeye, kwa sababu sera yetu sisi hatuingilii mambo ya ndani, tunasubiri maamuzi ya mwisho ya Brexit. Endapo watajitoa ndipo tutaanza mchakato wa kuanzisha mahusiano binafsi na Uingereza au wataalam wanasema bilateral relations. Kwa hivi sasa kwa kuwa mahusiano yetu na Jumuiya ya Ulaya ni mazuri tusingependa kuingia katika suala hili la Ulaya na Brexit. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia suala la EPA liliongelewa na kusema kwamba nchi nyingine zimeshasaini EPA ispokuwa sisi. Naomba nitoe taarifa kwamba zaidi ya asilimia 50 ya nchi za Afrika hazijasaini EPA. Katika Afrika Mashariki, kati ya nchi sita ni nchi mbili tu zimesaini EPA, nchi nne, ambazo ni nyingi, hazijasaini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hawajasaini siyo kwamba hawaipendi, nchi nyingi ikiwemo Tanzania tume-raise concern. Sisi Tanzania tumehoji vifungu nane vya mkataba wa EPA. Katika vifungu nane hivyo tume-raise issues 12 ambazo tunasema zikiwa-addressed tutasaini mkataba wa EPA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja kati ya issues, niwasaidie tu, ni kwamba mkataba huo unakwenda kupoka mamlaka ya Bunge hili hasa kwenye kutunga sheria zinazohusiana na fedha au kodi. Sasa hatuwezi kusaini mkatana ambao unapoka mamlaka ya Bunge pasipo Bunge lenyewe kuridhia. Kwa hiyo, suala hilo siyo la kwetu sisi tu, ni la Bunge hili na ni la Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, imeongelewa pia hoja kuhusiana na haki za binadamu. Naomba niseme, haki za binadamu ni suala mtambuka na zinaangaliwa sana kwa mujibu wa Kikanda. Sisi Afrika tuna Mkataba wa Afrika wa Watu na Haki za Binadamu, wenzetu wa Ulaya wana Mkataba wa Haki za Binadamu, neno watu halipo, hiyo ni tofauti kubwa sana ya mtazamo wa haki za binadamu kati ya Afrika na Ulaya. Ndiyo maana sisi kwa muktadha wetu tumeanzisha Mahakama yetu iliyoko pale Arusha ili masuala ya haki za binadamu kwa muktadha wa Kiafrika tuyashughulikie kwenye Mahakama zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokuja sasa kuanza kucheza ngoma ambazo siyo za kwetu tunakuwa tunapotoka. Kwenye hili, naomba nirejee ushauri mzuri aliyoutoa Mheshimiwa Mnzava kwamba katika kutatua changamoto za haki za binadamu Tanzania tuna mihimili ya kutosha; tuna Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mahakama Kuu ambayo ina mamlaka kwenye haki za binadamu, Mahakama ya Afrika Mashariki ambayo pia inashughulikia haki za binadamu na Mahakama ya Afrika inayoshughulikia haki za binadamu ambayo iko Arusha. Kwa kuonesha umuhimu Mahakama hizi mbili, ya Afrika Mashariki na ile ya Afrika, ziko Tanzania, ziko Arusha, tumeziweka hapa kwa sababu tunapenda na tunalinda haki za binadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tu niseme katika haki za binadamu tuko vizuri pengine kuliko nchi ambazo watu wengi wanaziongelea. Niwape mfano tu, kuna nchi ambazo tunazisema sana humu ndani, hazijasaini Mkataba wa Haki za Mtoto Duniani lakini mnadhani kwamba hizo ndiyo zinatimiza haki za binadamu. Nchi hizo hazijasaini Mkataba wa Rome Statutes ambao unashughulikia masuala ya ICC.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwenye kipengele cha haki za binadamu tuko vizuri. Tufuate vyombo hivi ambavyo vipo, tuache kupeleka masuala ya haki za binadamu sehemu ambako hakuhusiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua fursa hii, kwa namna ya kipekee, kumpongeza sana Waziri, Mheshimiwa Prof. Palamagamba Kabudi. Najua wengi wangetamani Mheshimiwa Prof. Kabudi aweze kujibu mambo ambayo siyo mazuri. Mheshimiwa Prof. Kabudi anafanya kazi vizuri, tuna wazalendo wachache sana nchi hii kama yeye. (Makofi/Vigelegele)
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, watu huwa tunasubiri mpaka mtu afe ndipo tumsifie.
Naomba mimi nimsifie Mheshimiwa Profesa Kabudi wakati bado anaishi na angalau na yeye mwenyewe apate pongezi hizi. (Makofi)
MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu.
NAIBU SPIKA: Kanuni inayovunjwa Mheshimiwa Mbilinyi?
MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu, nikishaeleza ndiyo nitasema, naomba nafasi kwanza.
NAIBU SPIKA: Unasimama kwa mujibu wa Kanuni gani? Usiwe mbishi bila sababu na wewe ni Mbunge wa siku nyingi, kanuni inayovunjwa ni ipi. (Makofi)
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, endelea.
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbilinyi, naomba ukae, Mheshimiwa Naibu Waziri endelea.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, wazalendo kama Mheshimiwa Prof. Kabudi ni wachache. Hii ni tunu ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia, tunapaswa kuienzi na kuilinda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Prof. Kabudi ameifanyia mema nchi hii, mambo ya kihistoria, ametuletea sheria mbalimbali nzuri na anaongoza Wizara hii kwa ufanisi wa hali ya juu. Naomba Waheshimiwa Wabunge wote tuchukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Prof. Kabudi, tumtakie maisha marefu ili aendelee kutumikia Tanzania kizazi na kizazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
WABUNGE FULANI: Unga mkono hoja.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa sisi wote uhai na afya na kutuwezesha kuendelea kuwatumikia Watanzania kupitia Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru wewe binafsi kwa kuendesha mjadala huu vizuri kabisa. Pia nimshukuru Mwenyekiti wa Kamati, Makamu Mwenyekiti wa Kamati pamoja na Kamati nzima ya Maliasili na Utalii kwa hotuba yao na ushauri wao. Katika hotuba yao wametoa mapendekezo 14 ambayo Wizara imeyapokea kwa mikono miwili na tunaahidi kwamba mapendekezo hayo tutakwenda kuyatekeleza kwa kushirikiana nao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii pia kuwashukuru Wabunge 78 ambao wamechangia hoja ya Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini pia Wabunge 16 ambao wamechangia kwa maandishi. Hoja zao, michango yao na maelekezo yao tumeyapokea na kuahidi kwamba ushauri wote walioutoa tutautumia ili kuboresha utendaji wa Wizara hii na hatimaye kuleta tija kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niruhusu niongelee mambo machache sana ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyaelezea.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ni migogoro iliyopo kati ya wahifadhi na wananchi. Imetamkwa hapa kwamba wananchi kadhaa wamefariki, lakini niseme pia na wahifadhi 12 wamefariki. Roho hizi za Watanzania ni nyingi sana, sina mamlaka hayo lakini ningekuwa nayo ningekuomba Bunge lako Tukufu lisimame angalau kwa sekunde 15 kuwakumbuka Watanzania hawa ambao wamefariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais mama Samia haipendi kuona mwananchi wake yeyote anakufa kwa sababu yoyote ile. Sisi kama Wizara ya Maliasili na Utalii hatufurahishwi na jambo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, mmesema hapa kwamba wananchi wengi wamefariki kutokana na migogoro kati ya wahifadhi na wananchi, lakini nami nimesema hapa askari 12 wameuawa pia katika migogoro hiyo. Tufike sehemu tuseme sasa inatosha. Tutafute ufumbuzi wa suala hili na ufumbuzi ni wa kwetu wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, sisi kama Wabunge tuelimishe wananchi wetu kwamba maeneo ya uhifadhi tusiingie kufanya shughuli nyingine, lakini hata tutapokamatwa na hao askari tusilete resistance ambayo inasababisha mapigano na baadaye kupoteza maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara tumeanza kuchukua hatua; hivi ninavyoongea askari wetu 61 tumewafukuza kazi. Hivi ninavyoongea askari 40 wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi. Moja kati ya kazi za kwanza ambazo mimi na Naibu Waziri tulifanya ni kwenda Ifakara kufukuza kazi askari watatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wetu ni rahisi sana; tukipata malalamiko yenye ushahidi usiokuwa na shaka, sisi tunaitisha parade na tunamfukuza huyo askari kwa aibu na fedheha. Kwa sababu hatupendi askari ambaye amepata mafunzo anakiuka miiko ya kazi yake. Tunachohitaji ni ushirikiano toka kwa wananchi, ushirikiano toka kwa Waheshimiwa Wabunge na sisi kama Wizara tunahakikisha tukipata ushirikiano huo suala hili limekwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuwashauri wananchi wetu, chanzo cha migogoro hii mpaka kuuana wakati mwingine ni rushwa; askari wetu wanaomba rushwa ili waingie kulima, askari wetu wanaomba rushwa ili waruhusu wafugaji waingie. Sasa ile pesa ya rushwa ikiisha anataka aongezewe rushwa, ndipo mgogoro unapoanza. Wananchi tukatae kutoa rushwa kutoka mwanzo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namba yangu mimi na namba ya Mheshimiwa Naibu Waziri na namba ya Katibu Mkuu ziko wazi kwa mtu yeyote kupokea malalamiko yoyote yenye Ushahidi ili tuweze kuchukua hatua. Ninaamini suala hili sasa linakwenda kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhakikisha kwamba nidhamu ya askari wetu hawa inakaa vizuri, kwa sababu hivi sasa bado zile Kanuni za Jeshi Usu hazijasainiwa. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba nitasaini kanuni hizo Jumatatu ili kuanzia tarehe Mosi, Julai, askari atakayekiuka miiko yake ya kazi haendi kwenye mahakama za kawaida, anakwenda kwenye mahakama za Kijeshi na anafukuzwa kazi mara moja. Kwa hiyo hii tunaamini italeta sana ufumbuzi kwenye hoja hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, limeongelewa suala la vitalu hapa na ushauri mwingi umetolewa. Naomba niseme tumepokea ushauri huo wote. Hata hivyo, niongeze kitu kidogo tu, kwamba Wizara hii imekuwa na desturi ya kubadilisha Mawaziri kila baada ya miezi 18 na chanzo kikubwa cha Mawaziri kubadilishwa ni mfumo wa zamani wa ugawaji wa vitalu ambao ulikuwa umegubikwa na wingu kubwa la sintofahamu, rushwa na upendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo mpya uliowekwa wa kielektroniki umekuja kutibu matatizo hayo. Jambo lolote jipya haliwezi kuwa perfect a hundred percent, litakuwa na dosari hapa na pale. Tusichukue dosari hizo kubomoa mfumo huu mpya ambao una uwazi, una ushirikishwaji, unaleta wadau wapya kwenye sekta hii na unaondoa rushwa. Turekebishe matatizo hayo taratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu ambao umeshaanza kutumika katika minada minne tumeweza kuuza vitalu 12, lakini vitalu hivyo 12 ambavyo vimeuzwa vimetuletea fedha ambayo inatusaidia sasa kwenda kujenga madarasa. Inatusaidia sasa kwenda kujenga hospitali, inatusaidia sasa kwenda kujenga barabara na la muhimu zaidi tunasaidia kwenye ujirani mwema kati ya uhifadhi na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Festo hapa amesema kule Kitulo anataka ujirani mwema; fedha inatoka hapa. Nimhakikishie Mheshimiwa Festo kwamba hilo jambo litakaa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli pia performance ya vitalu imeshuka. Ilianza kushuka kabla mfumo huu haujaingia. Kilichosababisha kushuka kwanza ilikuwa ni katika nchi za wenzetu ambako watalii wengi ndio wanatoka, hasa Marekani, walianza kuweka zuio ili hizi trophies zisiende. Walivyozuia kutokana na harakati za wapigania haki za Wanyama, tukajikuta kwamba soko la trophies kule Marekani likashuka, likishuka na uwindaji wao unashuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Marekani walifungua, lakini baada ya Marekani kufungua hivi juzi European Union nao wametoa azimio la kuzuia trophies zisiingie huko. Sasa siyo jambo letu sisi peke yetu, tumeungana na nchi nyingine zote za SADC tunafanya mchakato ili kuondoa zuio hilo. Haya pamoja na ugonjwa wa Covid-19 ndiyo yamechagia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa utalii wa uwindaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona Serikali yetu imeanza kuchukua hatua stahiki kabisa na hatua madhubuti kupambana na ugonjwa huu wa Covid-19. Tunaamini tutakavyoweza kuweka sawa suala la Covid-19 na kuondoa hili zuio la kutoka European Union na kuboresha mfumo huu wa uwindaji wa vitalu wa kielektroniki tutaweza kupandisha tena performance ya uwindaji wa kitalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda huu mfupi mimi na Mheshimiwa Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara tumeshakutana na wawindaji na vyama vyao mara tatu. Tuliitisha mkutano Morogoro, siku nzima tumeshinda nao, asubuhi mpaka jioni. Tumeongea nao tumepata maoni na maoni yao ni muhimu sana katika kuboresha utendaji wa Wizara. Tunaomba tuwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba hili nalo tunakwenda kuliweka sawa kabisa, na tutaboresha kuondoa sintofahamu yoyote ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja mahususi kabisa kutoka kwa Mheshimiwa Olelekaita, Mbunge, wakili msomi. Hoja yake iko kwenye mawanda mawili; moja, alisema kwamba sheria hiyo haipo; pili, akasema sheria hiyo ni ya uonevu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikubaliane naye labda kwenye hiyo hoja ya pili, lakini ya kwanza sheria ipo. Sheria ya Wanyamapori, Kifungu cha 116 kinasema; Sheria ya TANAPA Kifungu cha 28 na Sheria ya TFS Kifungu cha 95, ila tunahitaji kuwa na mjadala wa eneo hilo ili tuweze kuliboresha zaidi, ili kuondoa kelele na malalamiko kutoka kwa Watanzania hao wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, na kazi hiyo ni kazi ya Bunge hili Tukufu, ndiyo kazi yake kushughulikia sheria kama hizi, kuzirekebisha, kuzitunga na ndiyo maana sisi tuko humu ndani kwa ajili ya kazi hiyo. Kwa hiyo Mheshimiwa Olelekaita, wakili msomi, ambaye mimi huwa nawasiliana naye sana, karibu sana tuje tuongee hili. Naamini pia tutaliweka sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la wanyama wakali na waharibifu sambamba na kifuta jasho. Juzi hapa tulifanya semina kwa Waheshimiwa Wabunge ambao wanatoka kwenye maeneo hayo kwa lengo la kuwapa uelewa nini chanzo cha tatizo hili.
Niseme, nashukuru sana mjadala wa leo unaonesha kwamba Waheshimiwa Wabunge wengi wametambua chanzo ni nini. Baada ya kutambua chanzo ni nini sasa, tujielekeze tutawezaje kuondoa changamoto hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, njia ya kuondoa changamoto hii ni moja tu; turudi kwenye mpango bora wa matumizi ya ardhi. Vijiji, halmashauri na Wizara; haya maeneo tuyaainishe. Wakati mwingine wananchi wanaingia kwa sababu hawajui; ameshajenga, ameshalima ndiyo anajua kwamba hii ni shoroba.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni wakati kuanzia kwenye vijiji, kuanzia kwenye halmashauri na nasema halmashauri kwa sababu sisi wote humu ni Madiwani. Kwa hiyo kwenye halmashauri zetu tukatoe kipaumbele kwenye kitengo cha maliasili katika halmashauri. Kwa sababu kila halmashauri ina kitengo cha maliasili, lakini hatukipi umuhimu unaostahiki. Imesemwa hapa wana mabunduki ya zamani, hawana risasi, hawana usafiri, lakini wako chini ya halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama Wabunge, ambao pia kama Waheshimiwa Madiwani, tulichukue jambo hili kwa umakini mkubwa sana. tutakavyorudi kwenye Mabaraza yetu ya Madiwani tujiulize ni kwa kiasi gani tunaweza kuimarisha kitengo cha maliasili ili kupunguza kadhia hizi ambazo zinajitokeza. Tukishazipunguza sasa ndipo tutaweka mchakato zaidi wa kuweza kuangalia kwamba zile chache zinazoweza kuwezekana tuweze kufanya vipi katika jambo zima la kifuta jasho na kifuta machozi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Lukuvi kwa ufafanuzi mzuri ambao ameutoa. Yeye ni Mbunge mzoefu na ni Senior Minister. Jambo hili la migogoro ya mipaka alilifanyia kazi vizuri sana, yeye ndio aliongoza Kamati ile ya Mawaziri nane; amefanya kazi nzuri iliyotukuka, kilichobaki ni utekelezaji wake tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nisingependa kurudia aliyoyasema, lakini niongeze jambo moja. Katika zile hekta ambazo zimefutwa, kuna hekta mahususi 29,000 kwa ajili ya wafugaji. Tutakwenda kuzigawa hekta hizo ili wafugaji waweze kupunguza kadhia yao. Najua haitaondoa kabisa tatizo lao, lakini tutaweza kupunguza. Ili tatizo liondoke kabisa tunapanga uelimishaji zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, na Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Ndaki, ameshaiomba Wizara ya Maliasili na Utalii tufanye mkutano wa Kitaifa wa pamoja wa Maliasili pamoja na Mifugo. Mkutano huo unakuja kuanzia sasa mpaka Oktoba tutakuwa tumeshaufanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, imeongelewa hapa kuwa watu wameshinda kesi lakini mifugo yao haijulikani ilipo, hawajakabidhiwa. Nchi hii inaongozwa na utawala wa sheria na sheria inatafsiriwa mahakamani. Mtu akienda mahakamani ameshinda kesi lazima apate kile alichokishinda mahakamani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaahidi Waheshimiwa Wabunge na niliahidi Bunge lako Tukufu kwamba, tutafuatilia kesi zote hizi ili haki za wale walioshinda kesi mahakamani zisipotee. Tumelichukua jambo hilo kwa umakini wa hali ya juu na niwaahidi tutakwenda kutekeleza. Kama ambavyo tumekuwa tukipokea maombi ya Wabunge na kutekeleza kwa haraka na hili tutalitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata kesho nimealikwa kutembelea kwenye majimbo la Wabunge wawili na nakwenda baada ya bajeti hii. Hiyo yote ni kuonesha kwamba pamoja na kwamba Wizara hii ni muhimu sana katika uchumi, lakini pia ina umuhimu katika mustakabali na maslahi ya wananchi wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, limeongelewa suala la WMAs na wewe unalifahamu vizuri sana kwa sababu ulikuwa consultant wakati hili jambo linaanzishwa. Kwenye hilo kwa sababu ulikuwa ndio mwanzilishi wa hili, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wakupigie makofi kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna WMAs 38 lakini ambazo zinafanya kazi ni 22 tu, hizi 16 zimekufa. Labda niseme WMAs ni nini; WMA ni kifupi cha Wildlife Management Area, kwamba Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi iliona ni bora na ni vyema kukabidhi madaraka ya kusimamia wanyamapori kwenye maeneo ya vijiji kwa wananchi kupitia Serikali za vijiji. Vijiji kwa mkusanyiko kadhaa vinatengeneza kitu kinaitwa authorized association. Wakitimiza masharti yyale wanapata usajili, wakipata usajili wanafanya uhifadhi na uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo ambazo zinafanya vizuri sana kama ile ya Ikona. Imeonesha wanataka kufikia mapato ya shilingi bilioni 2.6 kwa mwaka. Sasa angalia, hiyo ni WMA moja inapata fedha hiyo, lakini wengine wameingia kwenye migogoro ya uongozi, wameshindwa kuhifadhi na ukishindwa kuhifadhi wanyama wanatoweka na wawekezaji wanakimbia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hizi 16 ambazo wameshindwa kufanya majukumu yao, wanyama wametoweka na hali imekuwa ni ngumu, ndizo ambazo tumesema Wizara tunaziangalia kwa jicho la kipekee.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepanga pia ku-build capacity na kuendelea kuwa karibu na hizi WMAs kwenye utendaji. Kuwashauri zaidi kwa sababu kuna wengine wameingia kwenye mikataba ya kiunyonyaji ambayo haiwasaidii. Tunarudisha kwenye mfumo sasa tuweke mikataba mizuri ili hizi zote 22 ziweze kufanya vizuri na hatimaye zile 16 tuzirudishe kwenye mstari stahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja mahususi pia zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge. Moja, tumepokea maombi mengi sana ya kuhusu vibali vya kuvuna kwa wananchi ambao walilima katika maeneo ya hifadhi kimakosa, walikuwa wamezuiwa. Kama nilivyosema wakati wa kulima kuna kuwa na makubaliano na wakati wa kuvuna wanataka kuwe na makubaliano mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kupitia Bunge lako hili Tukufu naomba Wizara itoe maelekezo, hayo makubaliano ya rushwa hatuyataki. Naagiza leo wananchi wote ambao walilima katika maeneo ya uhifadhi, waruhusiwe kuvuna kwa kibali maalum. Maelekezo haya ni kwa nchi nzima, kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge hakuna haja ya kuja kuomba tena jambo hili tumelitolea maelekezo mahsusi kwa nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kibali mahsusi kwa mamlaka ile husika kwa sababu unapoingia kwenda kuvuna unaingia eneo la hifadhi kwa hiyo unapewa kibali. Baada ya kibali hicho tunawaomba Waheshimiwa Wabunge watusaidie, wasirudi tena kulima kwenye maeneo hayo, ili mwakani tusilijadili hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Asenga aliongelea kwamba pale Mang’ula kuna kona moja kali sana ambayo inasabababisha ajali, Watanzania wanafariki na ikiinyooshwa ile kona inakula eneo la hifadhi la mita 50. Kubadilisha mpaka wa hifadhi ni Mamlaka ya Mheshimiwa Rais, lakini naomba nijivishe kilemba cha ukoka, niagize pale mkandarasi anyooshe zile mita hamsini, nitaenda kumwomba msamaha Mheshimiwa Rais kwamba nimeingilia mamlaka yake na abariki maamuzi hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mkandarasi yule anyooshe pale ili tupunguze ajali kwa Watanzania ambao wanafariki. Bahati nzuri kona ile naifahamu kwa kuwa nimesoma Ifakara, lakini nimeoa kule, naenda kusalimia wakwe kila siku na naona madhara ya kona ile. Kwa hiyo hili nalo naomba, watendaji wa Wizara wamenisikia utekelezaji wake huo uanze leo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imegawa namba 14 hotlines kwa ajili ya kupokea malalamiko ya wananchi kutokana na wanyama wakali, hiyo yote ni kusaidia kupunguza kero hii. Namba hizo ni za bure, ukipiga wala huchajiwi, tunaomba kupitia Bunge lako Tukufu, tuwaambie watanzania wote, ambao wana matatizo ya kukabiliana na wanyama wakali, watumie namba hizo kutoa taarifa ili askari wetu nao waweze kufika kwenye eneo husika kwa haraka kabisa, tutaendelea kuzisema namba hizo kwa wananchi mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, imeongelewa hapo hoja mahsusi ya miundombinu ya Burigi - Chato, mimi nimetembelea, nimefika nimejionea tunahitaji kuboresha miundombinu ya Burigi - Chato na bajeti hii ndiyo imebeba fedha za kuboresha miundombinu ya Burigi - Chato kwa hiyo Mheshimiwa Dkt. Oscar ukiipitisha bajeti hii tume-solve tatizo la Burigi - Chato, tushikamane twende kumaliza tatizo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ufafanuzi ambao nimeutoa kwa hoja zote ambazo zimewakilishwa na Wabunge hapa, pia hoja ambazo Wabunge wamezitoa kimaandishi na sisi tutazijibu pia kimaandishi na kuzileta kwako.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana wewe, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao na maelekezo yao, niwaombe sana sasa tupitishe bajeti hii ili twende kwenye utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kutoa pongezi za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Tano na Wizara ya Afya kwa kazi nzuri ya kuboresha huduma za afya. Pamoja na changamoto hizo, napenda kutoa maoni yangu kuhusu changamoto zifuatazo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Kituo cha Afya Mjimwema - Songea Mjini; kituo hiki cha afya kinafanya kazi kama Hospitali ya Wilaya, hivyo basi kufanya kazi kubwa kuliko uwezo wake. Kituo hiki cha afya kinakabiliwa na changamoto zifuatazo; ukosefu wa wodi ya wanawake na wanaume, ukosefu wa x-ray, MRI na vifaa tiba vingine, ukosefu wa gari la wagonjwa (ambulance) na uchakavu wa majengo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Songea una jumla ya wakazi 230,000 lakini hakuna Hospitali ya Wilaya. Tunahitaji Hospitali ya Wilaya ili kuhudumia wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vituo vya afya; Wilaya ya Songea Mjini yenye jumla ya wakazi 230,000 na kata 21 haina Hospitali ya Wilaya. Tunahitaji vituo vya afya angalau vitatu katika Kata za Ruvuma, Ndilima Litembo na Mletele.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi hii ili nami nichangie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kutoa pongezi za dhati kabisa kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kutekeleza ipasavyo Ilani ya Chama cha Mapinduzi, hasa katika sekta hii ambayo tunaiongea hivi leo. Ni wazi kwamba Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Ilani ya CHADEMA zote zinaongelea kufufua Shirika la Ndege la Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza hilo, Serikali ya Chama cha Mapinduzi kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imenunua ndege sita. Siyo hilo tu, katika bajeti ambayo Mheshimiwa Waziri ameisoma hapa, kuna viwanja 16 vya ndege ambavyo vitatengenezwa. Viwanja hivi vitasaidia hizi huduma za ndege. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, sisi wengine Majimbo yetu yako mbali sana, umbali wa kutoka hapa Dodoma kwenda Songea ni mkubwa, hizi ndege zitatusaidia sana kufanya mawasiliano. Kama kuna mtu anaona ndege hizi hazimsaidii, basi tuweke bayana kwamba viwanja vya ndege katika Jimbo lake visitengenezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sisi watu wa mikoa ya kusini tuna kila sababu ya kuipongeza Wizara; Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri, kwa kukamilisha Barabara muhimu sana inayojulikana kwa jina la Mtwara Corridor.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa ukitoka Mtwara unapita Masasi, Tunduru, Namtumbo, Songea, mpaka Mbinga, barabara hiyo imekamilika kwa kiwango cha lami. Kipande kilichosalia cha Mbinga – Mbamba Bay tayari mkandarasi ameshasaini na tunaamini barabara hiyo itakamilika haraka ili kufungua fursa zilizopo katika Kanda ya Kusini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hiyo barabara ya Mtwara Corridor kuna kipande kidogo kimoja kimebaki cha kilometa 11, nayo ni bypass ya Songea Mjini kutoka Kata ya Seed Farm kupitia Kata ya Msamala na hatimaye Kata ya Luwiko. Ili kuhakikisha kwamba Mtwara Corridor inakamilika kwa ukamilifu kabisa, lazima kipande hicho kikamilike. Mheshimiwa Waziri, nimesoma hotuba yako kwa makini sana, sijaona hizo kilometa 11. Hivyo, ni rai yangu kwamba kilometa hizo 11 ziweze kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa usafiri katika Ukanda wa Kusini kuna mpango wa kujenga reli kutoka Bandari ya Mtwara mpaka Mbamba Bay ili kuweza kuhudumia Liganga na Mchuchuma, Miji ya Songea, Miji ya Masasi na miji mingine. Fedha iliyotengwa katika kitabu hiki kwa mradi huu bado ni ndogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wote wa Ukanda wa Kusini wakiongozwa na wananchi wa Jimbo la Songea Mjini wana hamu ya kuiona reli hii ikijengwa, ikifanya kazi, ikitoa huduma na ikiunganisha Tanzania na nchi mbili; ya Msumbiji pamoja na ya Malawi. Kwa hiyo, tunatarajia hili nalo Mheshimiwa Waziri atalichukua alifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Songea, wananchi ambao wameachia maeneo yao wanadai fidia katika upanuzi huo. Naomba kumkumbusha Waziri, Mheshimiwa Profesa Mbarawa na Naibu Mawaziri, kwamba naomba hilo nalo litiliwe maanani ili tuondoe kero hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, niipongeze tena Serikali ya Chama cha Mapinduzi, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa Wizara ya Uchukuzi kwa mafanikio makubwa katika sekta za ujenzi wa barabara ya Mtwara Corridor kutoka Mtwara – Mbinga; ufufuaji wa Shirika la Ndege la Tanzania; ufufuaji wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL); ujenzi wa reli ya Kati kwa kiwango cha SGR; na utendaji mzuri wa bandari zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi hiyo nzuri, naomba kuchukua fursa hii kueleza changamoto zinazolikabili Jimbo la Songea Mjini ambazo zinafanya utekelezaji wa Ilani ya CCM kuwa ngumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya mchepuko wa Mtwara Corridor -Songea Mjini (kilometa 11); ili Mtwara Corridor ikamilike ni lazima kipande cha mchepuko cha kilometa 11 kilichopo Songea Mjini katika Kata za Seedfarm, Msamala na Ruhumiko. Kutokukamilika kwa kipande hiki ambacho ni sehemu ya mradi namba 4197 ni kikwazo kikubwa sana katika mradi mzima wa Mtwara Corridor.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Songea Mjini hakuna hata barabara moja iliyotengewa fedha katika bajeti ya mwaka 2018/2019. Naomba sana barabara hii ya kilometa 11 ya mchepuko ya Mtwara Corridor - Songea Mjini ipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Songea Mjini hakuna barabara hata moja katika bajeti nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana sana Mheshimiwa waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano barabara ya Mtwara Corridor - Songea bypass kilometa 11 iingizwe.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Nachukua nafasi hii kutoa pongezi za dhati kabisa kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu Utamaduni na Michezo kwa taarifa nzuri ambayo amewasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu. Pia nampongeza Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wote kwa namna ambavyo wanaiongoza Wizara katika kufikia malengo yake na kuwatumikia Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla nasema kwamba Wizara tumepokea maelekezo na michango ya Waheshimiwa Wabunge ambayo tunaahidi tutakwenda kuifanyia kazi katika kuboresha sekta za utamaduni, sanaa na michezo ili ziweze kufanya vizuri zaidi kuliko ambavyo iko sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niruhusu kutoa ufafanuzi kwenye baadhi ya maeneo pamoja na michango yangu. Eneo la kwanza ni kuhusu ukarabati wa uwanja wa Benjemin William Mkapa. Uwanja huu ndiyo uwanja pekee ambao unatambulika na Shirikisho la Soka Barani Afrika kwa sasa katika nchi zote za CECAFA. Ndiyo maana tumepata nchi nyingi na vilabu vingi nje ya Tanzania kuomba kuja kutumia uwanja huu, vikiwemo vilabu vyetu pendwa vya Simba na Yanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanatumia uwanja wakati ukarabati unaendelea hivyo mkandarasi analazimika kusimama kipindi fulani ili kuruhusu mechi ziweze kucheza. Kama pale ambapo tumekuwa na African Football League, tumekuwa na mechi za Simba na Yanga za kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumekuwa na nchi ya Burundi na Gambia wakitumia uwanja huo, hiyo inasababisha ucheleweshaji kidogo. Pia, wakati muda wa mkandarasi umekwenda kwa asilimia 40, kazi aliyofanya imekwenda kwa asilimia 24, hii inatokana na sababu hizo ambazo nimezisema. Pia, fedha ya awamu ya pili ambayo Wizara ya Fedha imeitoa kwa wakati ndiyo imefika kwa mkandarasi. Akiitumia fedha hii yote atafika sambamba na muda na fedha ambayo imetolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya mkutano na mkandarasi pamoja na consultant ambaye ni TBA na Kamati ilivyotembelea niliwaambia Waheshimiwa Wabunge kwamba TBA anafanya kazi nzuri sana kusimamia mradi ule. Ahadi ya mkandarasi ambayo na mimi naomba kuitoa katika Bunge lako hili tukufu ni kwamba atamaliza ukarabati kwa wakati. Sisi kama Wizara, kama Serikali, tunatarajia Tarehe 24 Agosti, 2024 mkandarasi atukabidhi uwanja uliokarabatiwa. Endapo atachelewa tutam-charge liquidated damages ili aweze kuwajibika kwa uzembe wowote ambaoo atakuwa ameufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili ni AFCON 2027 ambapo sisi Tanzania, Kenya na Uganda tutakuwa wenyeji. Sisi nchi hizi tatu tumeipa jina AFCON hii inaitwa Pamoja AFCON. Kwa sababu ni kwa mara ya kwanza katika historia ya Bara la Afrika, nchi zaidi ya moja zinaandaa mashindano kama haya, kwa hiyo tunaita Pamoja AFCON.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya Pamoja AFCON mwaka huu Septemba nchi hizi tatu zitakuwa wenyeji wa pamoja wa mashindano ya CHAN. CHAN ni AFCON ya wachezaji wa ndani, inatumika kama rehearsal kabla ya kwenda kwenye AFCON kubwa. Kwa hiyo, tayari tunaendelea na maandalizi hayo, sisi Tanzania tutakuwa na vituo viwili, Dar es Salaam na Zanzibar, Kenya vituo viwili na Uganda pia watakuwa na vituo viwili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naongelea AFCON ya 2027. Kwa upande wa Tanzania tutakuwa na viwanja vitatu. Kiwanja cha kwanza ni cha Benjamin William Mkapa ambacho kama ambavyo nimesema kitakuwa tayari Agosti mwaka huu. Kiwanja cha pili ni kiwanja cha Amani pale Jijini Unguja Zanzibar na tunaona kabisa Disemba mwaka jana uwanja ule ulizinduliwa rasmi kwa maana uko tayari. Uwanja wa tatu ni uwanja wa Arusha ambao tayari tunategemea ndani ya mwezi huu wa pili mkandarasi atakabidhiwa site.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeyasema haya ili kuwatoa hofu Waheshimiwa Wabunge na kuwatoa hofu Watanzania wote kwamba maandalizi ya AFCON 2027 yanakwenda vizuri. Tayari viwanja viwili vipo na cha tatu kwa maelekezo na ahadi ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan tutaumaliza kwa wakati na sisi tutakuwa wenyeji hatuwezi kukubali kupoteza heshima hii ambayo Bara la Afrika limetupatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo nachukua nafasi hii kuwatoa hofu Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kwamba maandalizi ya AFCON yanakwenda vizuri tutakwenda kwa wakati. Kwenye hili nampongeza sana Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Fedha, yuko kwenye hatua za mwisho kuhakikisha kwamba program ya EPC+F inakamilika na ndani ya mwezi huu wa Februari uwanja wa kisasa kabisa utajengwa katika Jiji la Arusha. Uwanja huu tayari sisi tumeshaupa jina, unaitwa Uwanja wa Samia Suluhu Hassan. Utakuwa uwanja mzuri zaidi katika ukanda wetu huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeongelewa Uwanja wa Dodoma; Uwanja wa Dodoma siyo sehemu ya maandalizi ya AFCON. Uwanja wa Dodoma ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi hususan katika Ibara ya 243 capitals (A). Chama cha Mapinduzi kiliahidi kitajenga uwanja wa kisasa jijini Dodoma sasa huu ndiyo utekelezaji wa hayo. Tunasema kwamba uwanja huu utakwenda sambamba na ule wa Dodoma ili tuweze kukaa vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwa mwenyeji si tu kuwa na uwanja bali ni pamoja na kuwa na timu nzuri. Tunajipanga, kama mmeona timu yetu ambayo imekwenda AFCON sasa hivi ilikuwa na wachezaji takriban saba ambao wana umri wa miaka chini ya 22. Wengi hawakucheza walikuwa wamekaa benchi lakini pale benchi ni darasa la wao kujifunza. Mwaka huu wamekaa benchi AFCON, AFCON ya mwakani 2025 tunataka tupambane ili wacheze angalau nusu. Ikifika 2027 hawa under 23 ndiyo watakuwa wachezaji ambao watatuvusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nasisitiza, ukiangalia tulikuwa na wachezaji 27 waliokwenda AFCON, 13 wanatoka kwenye vilabu vya ndani, 14 wanatoka kwenye vilabu vya nje. Napenda kuongelea hivi vilabu vya ndani, ni vilabu vitano ambavyo vyote ama vinashiriki au vimeshiriki mashindano ya Afrika. Hivyo, ushiriki wa vilabu vyetu katika mashindano ya Afrika unawakomaza wachezaji wetu kuweza kufanya vizuri zaidi kwenye Timu ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri hapa, timu yetu ya Taifa imesifiwa sana kwamba ilikuwa na ukuta mzuri ndiyo maana tumeweza kutoa suluhu zile mechi mbili. Ukuta ule mzuri tunaongelea wachezaji wawili pale katikati kwenye central defense, Mwamnyeto na Baka. Hao ni wachezaji ambao wanachezea Dar es Salaam Young Africans. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Yanga walifika fainali mwaka jana, na safari hii wanacheza Champions League. Uzoefu ambao kina Baka na Mwamnyeto wameupata wakiwa Yanga ndio unatusaidia sasa. Hivyo, tunaendelea kuimarisha ushiriki wa vilabu vyetu katika mashindano ya Afrika ili tukichanganya na wachezaji wale wa nje tuweze kupata timu nzuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imesemwa hapa kwamba Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa unatumika sana, hata sisi tumeliona. Tunakarabati Uwanja wa Uhuru, tayari tumeshampata mkandarasi na tayari tunafanya vizuri katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ya Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha kwamba sekta hizi tatu, Utamaduni, Sanaa na Michezo zinaendelea kufanya vizuri na sisi wasaidizi wake tutaendelea kumsaidia hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema moja la mwisho…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa muda umekwenda.
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuagiza sisi wasaidizi wake kwamba tuchukulie hizi sekta tatu za utamaduni, sanaa na michezo kama ajira na uchumi. Sisi tumepokea falsafa hiyo, tunaifanyia kazi; na ndiyo maana sekta hizi zinaongoza kwa ukuaji kwa asilimia 19. Tunachotaka kukifanya sasa asilimia hizo asilimia 19 tuweze kuzitafsiri katika uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana naunga mkono Taarifa ya Kamati. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nichangie kwenye suala hili la kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Songea wamenituma nifikishe ujumbe kwa Wizara ya Kilimo na kwa Serikali. Wananchi wa Songea wanasema kwao zao la mahindi ni chakula, kwao zao la mahindi ni biashara, kwao zao la mahindi ni siasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Songea wanasema hawana viwanda wanategemea mahindi. Wananchi wa Songea wanasema mahindi ndiyo uhai wao lakini sasa hivi wana kilio kikubwa sana. Katika msimu uliopita mbolea haikupatikana kwa wakati. Katika msimu uliopita bei ya mbolea ilikuwa inabadilika kama homa za vipindi. Katika msimu uliopita upatikanaji wenyewe wa mbolea ulikuwa ni shida na ukiwanyima mbolea maana yake umewaua kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Songea wanajitahidi sana kuzalisha mahindi. Takwimu za mwaka 2015/2016 wananchi wa Songea na Mkoa wote wa Ruvuma walizalisha mahindi tani milioni 1.9. Mahitaji na matumizi kwa mkoa mzima ni tani 400,000, hivyo kulikuwa na ziada ya tani milioni 1.5. Uwezo wa NFRA kununua ilikuwa ni tani 10,000 tu ambayo ni sawasawa na asilimia 0.7 ya ziada yote. Hii inamaanisha kwamba kulikuwa na asilimia 99.3 ya uzalishaji ambao haukuweza kununuliwa, ni ziada hii. Sasa NFRA hawawezi kununua, soko la nje mipaka imefungwa, huku ni kuwaumiza na kuwaua wakulima wa mahindi wa Songea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu tunategemea tuzalishe mahindi kwa wingi zaidi kuliko mwaka jana na yale ya mwaka jana bado hatujauza. Tunaiomba Wizara, kuna option mbili tu hapa; tuongeze fedha NFRA za kununua mahindi na kama hilo haliwezekani tufungue mipaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kule Songea tuna bahati tuna mipaka miwili, Malawi na Msumbiji, turuhusuni tuuze mahindi. Hakuna sababu ya kumtaka mkulima ambaye amelima kwa juhudi zake, amevuna kwa juhudi zake na hii ni ziada, Serikali inathibitisha kwamba ni ziada, auze kwa kibali, kwa nini? Tunaomba suala la mahindi Songea lipewe kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kutokana na ugumu wa suala la mahindi, wananchi wa Songea pamoja na wananchi wa Jimbo la Peramiho wameanza kulima strawberry na wanategemea ndege ambayo Mheshimiwa Rais aliipeleka Songea (Bombardier), ibebe zile strawberry kwenda Dar es Salaam kwenye soko lakini sasa hivi ile ndege haipo, haiendi tena Songea mnazidi kutuua. Tunaomba mturudishie ile ndege iendelee kubeba zile strawberry. Mheshimiwa Jenista wananchi wetu wanataka ile ndege itubebee strawberry zetu na kuzipeleka kwenye soko Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu alipotembelea Songea aliagiza Kiwanda cha Tumbaku kifufuliwe. Katika speech ya Mheshimiwa Waziri ameahidi kiwanda kitafufuliwa lakini hajasema ni lini kitafufuliwa. Naomba Mheshimiwa Waziri aje na kauli thabiti ni lini Kiwanda cha Tumbaku Songea kitaanza kufanya kazi angalau atufute machungu sisi wananchi wa Songea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kunipa tani nyingi sana katika ujenzi wa vihenge. Songea ametoa tani 81,000 lakini capacity hiyo haina maana kama ununuzi wake ni mdogo. Kwa nchi nzima ununuzi ni tani 30,000 maana ile shilingi bilioni 15 inaweza kununua tani 30,000 tu, sasa hizi tani 81,000 alizonipa zitakuwa hazina faida kama NFRA hawawezi kununua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niongelee suala la mbolea hasa hii mbolea ya Minjingu. Kinachofanya mahindi yaweze kuzaa vizuri ni nitrogen katika mbolea ile. Minjingu ni mbolea ambayo ina nitrogen kidogo zaidi kuliko mbolea nyingine, percent ya nitrogen ni 9, sasa mkiandelea kutulazimisha kutumia mbolea ya Minjingu wakati kuna tatizo hili la kitaalam hamtatusaidia. Ni wazo zuri la kufufua viwanda vya ndani lakini nalo liangaliwe. Tunachotaka sisi mbolea ambayo inatumika iweze kutumika vizuri, iweze kusaidia uzalishaji siyo tu kukuza mahindi. Kwa hiyo, hili suala la kulazimisha kutumia Minjingu nalo tuliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ameongelea mambo mtambuka katika bajeti yake na mimi naomba niongee mambo mtambuka katika hoja yangu. Moja, nimelisema hatuna viwanda sisi, kiwanda chetu ni mahindi lakini pili kama tukiruhusiwa kuuza soko letu ni Msumbiji, barabara ya kwenda Msumbiji ni ya vumbi, inapitika kwa shida. Kwa hiyo, huku NFRA hawanunui mahindi, soko la nje limefungwa, hata likifunguliwa barabara ni mbovu. Kwa hiyo, tunaomba hilo nalo liangaliwe ili na sisi tuweze kuuza mazao yetu nchi nyingine za jirani ikiwemo Msumbiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ametembelea Songea na anajua kwamba Songea mbolea ndiyo kila kitu. Nitaomba atakapokuja kuhitimisha aje na kauli thabiti kuwahakikishia wananchi wa Songea kwamba msimu huu unaokuja watapata mbolea kwa wakati, kwa bei nafuu na kwa bei ambayo itakuwa ni moja kwa msimu mzima. Mpango ambao umewekwa wa kununua mbolea kwa pamoja ni mzuri sana, lakini ni sawa na mtu kununua gari zuri, kuwa na hilo gari zuri ni kitu kimoja lakini kuliendesha ni kitu kingine. Tunataka usimamizi na utekelezaji wa mpango huu wa kununua mbolea kwa pamoja (bulk procurement) ufanyike kwa ufanisi wa hali ya juu ili kuondoa hii kero ambayo imewakuta wananchi wa Songea katika msimu huu.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kupata nafasi nichangie Wizara ya Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote ningependa kuchukua fursa hii kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri ambayo inafanya kupitia Wizara ya Fedha, lakini kwa namna ya kipekee nimshukuru Mheshimiwa Waziri Dkt. Philip Mpango pamoja na Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji kwa kazi nzuri ambayo wanawafanyia Watanzania. Pia nitoe shukrani kwa viongozi wengine wa Wizara, Katibu Mkuu, Dotto James, Naibu Makatibu Wakuu, Dkt. Kazungu, Bi. Amina Shabani na Bi. Susan Mkapa kwa kazi nzuri wanayotufanyia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha ni Wizara muhimu sana. Ni Wizara muhimu kwaasbabu kila mtu anaangalia fedha, kila mtu anataka fedha kwa hiyo, ni vigumu sana kwa watu wengi kuona mazuri yanayofanyika. Lakini mazuri yapo na mazuri haya utayaona kama utaamua kuangalia takwimu za utendaji wa Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka uliopita Wizara hii ilipanga kukusanya kama Wizara shilingi bilioni 522 lakini ikakusanya shilingi bilioni 655, utendaji wa asilimia 126, takwimu zinaongea na kama kila Wizara ingeweza kufanya performance ya asilimia 126 tungekuwa pazuri zaidi. Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri kazi yenu tunaiona, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara hii ina jukumu moja kubwa muhimu la kuhakikisha kwamba uchumi wa nchi unakua, uchumi unaongezeka na hilo likifanikiwa ndipo faida ya kukua kwa uchumi itakwenda kwa kila mtu. Kwenye hilo Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri mmefanya kazi nzuri, uchumi wetu unakuwa kwa asilimia 7.1 mwaka uliopita kutoka asilimia 7.0 mwaka uliotangulia. Kwa hiyo, kama nilivyosema takwimu zinaongea, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia mmefanyakazi nzuri katika kudhibiti mfumuko wa bei. Tutaongea mengi, tutawapiga mawe, tutawatukana, lakini takwimu hiyo inawabeba kwamba mmefanya kazi nzuri. Mfumuko wa bei umeshuka kutoka 5.3 mwaka 2017 kufikia 3.8 mwezi Aprili, 2018. Hii ni kazi nzuri mnayoifanya ninyi mkiongozwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu niongee suala la umaskini. Wizara hii inahusishwa sana na suala la umasikini wa wananchi. Watu wengi wamesema sana kuhusiana na suala la umasikini lakini umaskini ni suala la kitaalam.
Mheshimiwa Spika wenzetu wachumi mimi siyo mchumi, lakini wenzetu wachumi wameweka vigezo na viashiria vya kupima umaskini siyo suala tu kwamba mimi sina hela mfukoni hapa nikajiita maskini siyo sahihi, kuna viashiria vya kitaalam. (Makofi)
(i) Kuna kiashiria cha umri wa kuishi; wastani wa umri wa kuishi kwa Mtanzania umeongezeka, hicho ni kipimo cha umaskini. Unavyoongeza wastani wa kuishi wa Mtanzania maana yake maisha yake yameboreka, maana yake umaskini umepungua. (Makofi)
(ii) Kingine ni vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano, kwenye kigezo hicho pia Wizara hii imefanya vizuri katika kuondoa umaskini, lakini muhimu zaidi ni upatikanaji wa huduma za kijamii. Hiki ni kipimo kikubwa sana cha umasikini katika nchi husika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaongelea huduma ya afya, huduma ya elimu, huduma ya miundombinu mbalimbali. Na tunajua huduma ya afya imeboreka sana na inaedelea kuboreka, tunajua elimu sasa ni elimu bure. Sisi tunafurahia elimu bure lakini ni Wizara yako ambayo inatoa fedha kwa ajili ya elimu bure hii. Hiki ni kipimo ambacho lazima tukiangalie kwenye kupima umaskini. Tunaongelea miundombinu Waheshimiwa Wabunge hapa ni mashahidi kila mtu anapata barabara ya lami katika Jimbo lake, kuna ujenzi wa reli ya standard gauge unajengwa. Hivi ndivyo vipimo vya umasikini ambavyo inabidi tuvitumie na kwenye hilo Wizara hii imefanyakazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niruhusu niongelee kuhusu suala muhimu sana, suala hili ni la ulipaji kodi, sisi Watanzania tunakuwa na tabia ya kuchangua mifano kutoka kwenye nchi zilizoendelea ambayo inatunufaisha katika hoja ambayo tunaitaka kwa wakati ule. Moja ya kitu ambacho tunapenda kuiga sana sisi Watanzania ni demokrasia ya nchi za Magharibi. lakini niwaombe Waheshimiwa Wabunge na wannachi wa Tanzania, tuige kitu kimoja, ulipaji kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tofauti kubwa ya nchi zilizoendelea na nchi maskini na nchi maskini ni katika ulipaji kodi. Endapo tunaiga hilo na tukakubali kwamba sasa ni wakati wa kulipa kodi kwa hiari ndipo tutaweza kujenga uchumi wa nchi yetu. Chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali yoyote duniani ni ulipaji kodi na usipolipa kodi sheria za kodi ni kali sana. Tunaongelea hapa rufaa zilizopo kwenye Baraza la Kodi, lakini kwa wenzetu kesi kama za kodi hata hazichukui muda zinakwisha haraka, aliyekwepa kodi atafilisiwa na anachukuliwa hatua kali za kisheria. Kwa hiyo, niwaombe Watanzania tuige ulipaji wa kodi wa nchi zilizoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kuna suala la elimu ya kodi. Watu hawawezi tu kuibuka kulipa kodi pasipokupewa elimu ya kodi. Katika mitaala yetu ya elimu kuanzia shule za msingi, sekondari mpaka chuo kikuu tuhakikishe somo la kodi liwe somo la lazima. Usitake mtu mzima umwambie leo alipe kodi wakati kuanzia shule ya msingi hujamfundisha kodi ni nini kwahiyo ni vizuri elimu ya kodi iweze kuchukua nafasi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, binafsi kupitia Tamasha la Maji Maji Selebuka ambalo naliandaa mimi, tunafanya mdahalo wa shule za sekondari kuhusiana na elimu ya kodi kila mwaka kwa kushirikiana na TRA. Niwapongeze watu wa TRA kwa kushirikiana na mimi katika kutoa elimu ya kodi kwa wanafunzi wa shule za sekondari wa Mkoa mzima wa Ruvuma. Ni vizuri juhudi hizi sasa zikasambazwa na kuenezwa nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niongelee suala la michezo ya kubahatisha (gaming activities). Wengi wameliongelea hili na madhara yake kwa vijana lakini naomba niliongelee kama chanzo cha mapato ambacho kinaweza kikatusaidia sana kuendeleza michezo. Huku nyuma, fedha zilizokuwa zinatokana na gaming activities ilikuwa ni chanzo cha mapato kwa ajili ya timu zetu za Taifa.
Mheshimiwa Spika, ninaomba Mheshimiwa Waziri…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tulikuwa tunajadili taarifa hizi mbili za Kamati za Bunge. Nikianza na taarifa ya Kamati ya Bajeti, katika ukurasa wa 10, kipengele 2.2.3 kimeongelea diplomasia ya uchumi. Nichukue fursa hii kuishukuru Kamati kwa kuipongeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kazi nzuri inayofanya kwenye diplomasia ya uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, badala ya kujadili ripoti hii na mambo ambayo yameandikwa katika ukurasa wa 10 na 11 yanayohusu Wizara ya Mambo ya Nje, baadhi ya wachangiaji wamejikita kujadili mambo ya ushoga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Waheshimiwa Wabunge tunatumwa na wananchi kuja kuipa Serikali maagizo. Kwa ruhusa yako, naomba uniruhusu niwaulize Waheshimiwa Wabunge kama kuna Mbunge yeyote ametumwa na wananchi wake kuja kutetea ushoga humu Bungeni. Kama yupo anyooshe mkono juu au ajifanye kama anajikuna. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama huyo Mbunge hayupo ambaye ametumwa na wananchi wake, basi anyamaze milele kuanzia sasa. Ili nchi hii iweze kuendelea tunahitaji kujituma na kuchapa kazi sisi wenyewe. Tunahitaji kulipa kodi kwa mujibu wa sheria za nchi. Hakuna mwekezaji wa nje atakayekuja kuikomboa nchi hii. Wawekezaji watakuja kuchuma na ili wachume vizuri wanatuvuruga kwa kutupa masharti hayo mbalimbali kama vile ya kutaka tukubali mambo ya ushoga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea sovereignty of the country. Watu wengi wanadhani sovereignty ni kitu chepesi sana. Suala la
sovereignty lilianza kukubalika mwaka 1648 kupitia Westphalia Treaty. Baada ya vita ya miaka 30 umwagaji mkubwa wa damu na majadiliano ya miaka minne ukapatikana mkataba wa Westphalia ambao ndiyo umeleta suala zima la sovereignty. Leo tunalichukulia suala hili kiwepesi wepesi sana. Tunataka uhuru wetu huu wa kujiamulia mambo tuukabidhi kwa watu wengine, hilo halitawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesemwa sana kwamba hatuna uhuru wa vyombo vya habari. Mimi naomba kusema kwamba Tanzania tuna redio 158, TV 34, magazeti 216 na tuna mitandao ya kijamii 224. Hii yote imeonyesha kitakwimu tuna uhuru wa vyombo vya habari. Pia tuko huko kuongea, kuikosoa Serikali na kutoa maoni pasipo bugudha yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono taarifa hizi za Kamati zote mbili. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge na Mkutano wa Nne wa Bunge pamoja na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati Mheshimiwa Rweikiza; Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Ridhiwani na Wajumbe wote wa Kamati ya Sheria Ndogo kwa michango yao kwa mawazo yao, kwa maelekezo yao ambayo wameitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niongelee eneo moja linalohusu zuio au katazo kwa askari wetu wa Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu wasiweze kufanya shughuli nyingine. Hili ni moja kati ya Jeshi Jipya ambalo limeanzishwa mahususi kabisa ili kulinda rasilimali ambazo tunazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni nchi ambayo inasifika sana kwa kuwa na rasilimali za maliasili bora kabisa duniani. Rasilimali hizo zinapaswa kuendelea kulindwa na ndiyo maana Serikali iliona umuhimu wa kuanzishwa kwa Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichokifanya kwenye Kanuni hiyo ni kujaribu kuimarisha utendaji na nidhamu ya Jeshi, kwa kuondoa uwezekano wa kuwepo kwa mgongano wa kimasilahi. Kwa sababu, askari hawa ambao wanafanya kazi katika maeneo ya maliasili na utalii, wasije wakashawishika na wao kujiingiza katika shughuli zinazofanana na maliasili na utalii. Tukiruhusu hilo, baada ya kulinda rasilimali hizo watakuwa wao wanazitumia kupitia shughuli zao za ziada wanazozifanya. Kwa hiyo, hatuwazuii kufanya shughuli nyingine kama za kilimo au biashara nyingine yoyote ili mradi isiingiliane na masuala ya uhifadhi na utalii na isiwe na mgongano wa kimasilahi na mwajiri wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunashukuru kwa Kamati kuibuka na hoja hiyo. Tumejadili na Kamati na tumewaeleza kwamba nia ya Serikali siyo kujaribu kuwakomoa askari hao; siyo kujaribu kuwatoa kabisa na kuwaongezea umasikini, la hasha, ni kuleta nidhamu na kuondoa uwezekano wa kuwepo mgongano wa kimasilahi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tufahamu kwamba askari hawa wanapewa silaha, wanakabidhiwa kulinda hayo maeneo. Sasa ukiwaruhusu wafanye shughuli za kibiashara, kwenye maeneo ambayo wamekabidhiwa kulinda, kwanza wata-take advantage dhidi ya private sector nyingine, kitu ambacho tutakuwa tunakwenda kuua private sector yetu; na pili, kutakuwa na uhujumu wa rasilimali hizo kwa sababu anayelinda unamruhusu pia aweze kuzivuna au kuzitumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja na kuwasilisha. Ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, awali ya yote nitoe shukrani za dhati kwa Kamati kwa taarifa yao nzuri ambayo wamewasilisha leo katika Bunge hili tukufu na ambayo kwa uwazi kabisa imesifia utendaji mzuri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sifa hizo ambazo tumezipokea kwa mikono miwili toka kwenye Kamati zinatokana na kazi nzuri ambayo Wizara inaifanya katika kudumisha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi mbalimbali duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipimo cha mahusiano ya kidiplomasia kipo cha aina tofauti. Kila mtu anaweza akajaribu kutaka kupima kwa vile anavyopenda yeye lakini kuna vipimo rasmi ambavyo wataalam wanavitumia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, moja, tunaangalia tuna balozi ngapi katika nchi mbalimbali na balozi ngapi zina uwakilishi hapa nchini. Kwa kipimo hicho tumefanya vizuri sana na tunakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia tunaangalia tunashirikiana kiasi gani na nchi mbalimbali. Hivi juzi Waziri wa Ulinzi amepokea msaada wa magari ya jeshi kutoka Marekani. Hicho ndicho kipimo cha uhusiano wetu wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Marekani, uhusiano mzuri kiasi kwamba tunaweza kushirikiana hata katika masuala ya ulinzi na usalama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia mahusiano yetu na Jumuiya ya Ulaya ni mazuri sana. Jumuiya ya Ulaya imeleta Balozi wake, ameshawasili na anafanya kazi vizuri na sisi tumepeleka Balozi Brussels na kwa maana hiyo tayari Jumuiya ya Ulaya imeshaweza kuleta fedha, Euro milioni 62, kuthibitisha mahusiano hayo mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukitaka kuelewa misingi ya diplomasia duniani, watu wengi sana wamechangia na niwaombe wote waliochangia kwanza wakasome Montevideo Convention ya mwaka 1933, lakini pili, wakasome Westphalia Treaty ya mwaka 1648, hizi nyaraka mbili ndiyo miongozo thabiti ya kidiplomasia duniani. Tusije tukachangia tukadandia gari wakati hatujui gari linaelekea mwelekeo upi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niruhusu nitoe ufafanuzi kwa faida ya Waheshimiwa Wabunge na kwa faida ya Watanzania wote ambao wanatuangalia. Mheshimiwa Salome Makamba wakati anachangia amesema kwamba Wizara ilitoa majibu mabaya dhidi ya Serikali ya Marekani. Naomba niliambie Bunge lako tukufu kwamba Wizara haijatoa kauli yoyote kuijibu Serikali ya Marekani na kwa misingi hiyo, nimuombe Mheshimiwa Salome Makamba alithibitishie Bunge hili ni taarifa ipi ambayo Wizara imetoa dhidi ya Serikali ya Marekani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia limeongelewa suala la wanafunzi na Watanzania waliopo China na tishio la ugonjwa unaosababishwa na virus anaitwa corona. Kwa sababu suala hili ni muhimu, nalo naomba nilitolee ufafanuzi; mpaka tunavyoongea hivi sasa, katika Jimbo la Huan na Mji wa Hubei kuna wanafunzi wa Kitanzania 437 na kuna familia moja ya Kitanzania yenye watu wanne, hivyo kufanya Watanzania waliopo katika jimbo hilo kuwa 441.
Mheshimiwa Spika, kwa taarifa ambazo tunazipata mara tatu kwa siku, kama vile dozi ya panadol, hakuna Mtanzania ambaye ameathirika na ugonjwa huo. Hivyo niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla kwamba Watanzania waliopo China katika Jimbo la Huan wako salama salimini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia tumeruhusu Watanzania wengine kutoka kwenye majimbo mengine waweze kurejea pale wanapopenda wao kurejea kwa sababu tunaheshimu uhuru wao wa kuweza kutembea na kuja huku kusalimia ndugu kwa sababu hawatoki katika jimbo hatarishi. (Makofi)
SPIKA: Ahsante Mheshimiwa.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii nami niweze kuchangia hoja iliyoko Mezani. Katika mijadala ambayo imeendelea kwa siku kadhaa humu ndani, tumekuwa tukijadili sana kuhusiana na makosa dhidi ya maadili. Michango mingi imekuwa ikionyesha kwamba kana kwamba hatuna sheria hiyo.
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kulijulisha rasmi Bunge lako Tukufu pamoja na Watanzania wote kwamba sheria hizi tunazo toka mwaka 1934. Tulizifanyia mabadiliko mwaka 1959, lakini tukafanya mabadiliko makubwa zaidi mwaka 1998 kupitia Sheria za Makosa ya Kujamiiana. Kwa hiyo, sheria hizi zipo na ni kali. Sasa changamoto imekuwa ni kwenye utekelezaji wake.
Mheshimiwa Spika, naomba nitoe taarifa pia kuwa tarehe 5 Aprili, 2023 Tume ya Kurekebisha Sheria kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini na wadau wengine mbalimbali ilifanya kongamano la tathmini ya utekelezaji wa sheria hizi za makosa dhidi ya maadili. Mchakato huo bado unaendelea. Sisi Serikali bado tunaendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kujua ni kwa nini utekelezaji wa sheria umekuwa na changamoto.
Mheshimiwa Spika, kama ulivyoelekeza leo, tutakuja na matokeo ya tathmini hiyo na ikibidi kufanya marekebisho ya sheria hiyo, tutafanya marekebisho. La msingi ni kwamba sheria zipo, hatuhitaji kutunga sheria nyingine, sana sana ikibidi tuweze kufanya marekebisho ya sheria hizo.
Mheshimiwa Spika, kwa maana ya muda, ninaomba niishie hapo, lakini muhimu zaidi naunga mkono hoja iliyowekwa Mezani na Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi hii, ya kuweza kuongea na Waheshimiwa Wabunge waliopo humu ndani na kupitia Bunge lako Tukufu kwa Watanzania wote. Nina mambo manne ambayo ningependa kuyasema. Jambo la kwanza nichukue nafasi hii kuishukuru sana, Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Kwa taarifa nzuri ambayo wamewasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu. Wameainisha maeneo ambayo tumefanya vizuri na pale kwenye changamoto wametueleza ili sisi tuweze kutekeleza vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikuahidi, Wizara tumepokea ushauri huo na tutaenda kuutekeleza; na utekelezaji huo unaanza leo. Kwa hiyo, kuanzia kesho mkiona utekelezaji unaendelea, msishangae, Serikali hii ni Sikivu. Tunasikia maoni ya Waheshimiwa Wabunge na tunayafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, watu wameongea sana na wanaendelea kuongea. Jambo moja lililoongelewa ni kwamba Wizara ya Maliasili na Utalii inataka kuwapokonya ardhi Wamasai. Naomba nitoe angalau ufafanuzi kidogo. Tanzania hakuna mwenye ardhi, hakuna kabila lenye ardhi Tanzania, ardhi yote ni mali ya Mheshimiwa Rais. Kwa mujibu wa sheria tulizozitunga humu ndani, anaweza akaitwaa muda wowote. Haki ya wewe ambaye ardhi hiyo inatwaliwa ni fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wameongea Waheshimiwa Wabunge hapa kuhusiana na mambo ya fidia. Hii dhana ambayo inakwenda na mpaka vyombo vya nje vinaandika: “Government of Tanzania is Grabbing Maasai Land,” ni upotoshaji! Hakuna sheria hiyo. Tukienda huko tutarudi wakati wa ukoloni, tutasema Ngoni Land, Sukuma Land, Nyakyusa Land; tulishatoka huko toka mwaka 1963. Kwa hiyo, turudi kwenye msimamo, tuelewe mwenye ardhi ni nani; na mamlaka yake ni yapi kwa mujibu wa sheria ambazo tumezitunga? Tukitaka kumnyang’anya Mheshimiwa Rais mamlaka hayo, tuje tutunge sheria, tuseme kuanzia sasa ardhi imilikiwe na makabila kama zamani. (Makofi/Kicheko)
SPIKA: Mheshimiwa Waziri hapo kwenye ardhi kumilikiwa na Rais, nadhani upaweke vizuri kisheria. Ardhi inamilikiwa na Umma, Rais anaishika kwa niaba ya Umma. Sasa isije ikaleta picha ambayo pengine inaweza kusababisha mkanganyiko. Ardhi ni ya Umma wote wa Watanzania lakini Rais anaishikilia hiyo ardhi kwa niaba yetu sisi sote. (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa mwongozo wako. Nilichokuwa ninasisitiza hapa ni kwamba, kwa sababu ardhi ni ya Umma, hakuna kabila moja linalomiliki ardhi. Ni Umma wa Watanzania wote; ndiyo maana ukienda Zanzibar utawakuta Wangoni wanakaa kule; ukija Songea utawakuta Wamasai wapo kule, kwa sababu ardhi ni ya Umma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja ya tatu ambayo ningependa kuiongea ni suala la haki za binadamu, limeongelewa sana hapa. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tazania inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ni Serikali inayojali haki za binadamu. Hatutafanya chochote kinyume cha haki za binadamu. Kwa kuwa tunaheshimu haki za binadamu, pia hatutaingilia uhuru wa vyombo vya habari kwa sababu ni haki za binadamu, lakini kama umekwazwa na vyombo vya Habari, mamlaka za kisheria zipo. Unaweza ukaenda Mahakamani au TCRA kwenda kuvishtaki. Ila Serikali ikikifungia chombo cha Habari, ni ukiukwaji wa haki za binadamu, hatutafanya hilo.
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ambalo ningependa kulisema, watu wameongelea hapa Sheria ya Ngorongoro ya Mwaka 1975. Toka imetungwa ni miaka mingi sana. Mliyoyaongea Waheshimiwa Wabunge yameonesha mapengo yaliyopo kwenye sheria ile. Msingi wa sheria ile ni nguzo tatu; nguzo ya uhifadhi, nguzo ya utalii na nguzo ya maendeleo ya jamii. Inaonekana nguzo hizi sasa zimeshindikana kushikiliwa kwa Pamoja. Kwa hiyo, sasa kwa mapendekezo ya Kamati na maoni yenu, sisi kama Wizara mapema iwezekenavyo tutaleta mabadiliko ya sheria hii na endapo Bunge hili Tukufu litaridhia, basi yataweza kupita na kuamua kwa mujibu inavyofaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nisistize kwamba Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo Mheshimiwa Rais amenipa mimi na Mwenzangu Mheshimiwa Mary upendeleo wa kuisimamia, tutahakikisha haki ya kila Mtanzania wakiwemo Wamasai walipo Ngorongoro inalindwa. Hakuna litakalofanyika kinyume cha sheria wala kuvunja haki zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge kabla hajawa Mbunge alishakuja ofisini akiwa Mwenyekiti na alikuja kuongelea haki za watu wa Ngorongoro. Hakuwa Mbunge lakini nilimpokea, tukakaa na tukaongea na nikamweleza msimamo kwamba tunapenda haya mambo yaende kwa kuelewana, kwa kukaa Mezani pasipo kumkandamiza mtu. Hiyo ndiyo approach ya Serikali, tufike sehemu tutatue tatizo pasipo kukwaruzana; wale wapate haki yao na Serikali ipate ambacho ni haki ili Ngorongoro isife. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii na ninawapongeza sana Kamati kwa taarifa hiyo nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kuongeza Mamlaka ya Mahakama ya Afrika Mashariki
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kutumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waheshimiwa Mawaziri wote ambao walijadili Itifaki hii na kupendekeza iletwe Bungeni kwa ajili ya kupitiwa na kujadiliwa na kufanyiwa maamuzi, kwa sababu maamuzi yao ndiyo yamefanya tuwe na mjadala huu leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru sana Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa kupokea Itifaki hii, kuijadili na hatimae kutoa maelekezo kwa Serikali kama ambavyo imefanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge Saba ambao wamechangia michango yao mbalimbali, niruhusu niwataje kwa sababu ni wachache sana. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Abdullah Ali Mwinyi - Mwanasheria msomi, kwa kutoa darasa la mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki leo. Naamini wale wagombea wetu wangekuwepo hapa leo, wangejua nini wanatakiwa kwenda kufanya wakienda kule Arusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Mollel, ametupa darasa la historia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki toka mwaka 1917 mpaka hii tuliyokuwa nayo leo. Pia ameelezea kwa ufasaha sana ni kwa nini tumechelewa kufika hapa ili kuwatoa hofu Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote. Ninamshukuru Mheshimiwa Zainab Katimba, kama ambavyo amesema Mheshimiwa Jerry Silaa, wamejipanga pale leo kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri. Ninamshukuru sana Kaka yangu, Wakili Msomi, Mheshimiwa Tadayo Joseph, nae ametoa mchango mzuri sana na amesisitiza kwamba hii sasa inakwenda kuleta ushindani wa haki ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mawanda ya kufanya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana pia Mbunge jemedari, Mheshimiwa Aida Joseph Khenani. Mimi namuita Mbunge jemedari kwa sababu aling’oa mbuyu na ndiyo maana yuko hapa na tumeona mchango wake. Nimwambie tu Mheshimiwa Aida kwamba asiwe na wasiwasi, Mahakama hii haiendi kupora au kupoka mamlaka ya Mahakama yoyote, ila inakwenda ku-supplement pale ambapo tumekuwa na pengo na kumekuwa na tafsiri tofauti katika Itifaki hii, hatimaye kwenda kuongeza confidence kwa wafanyabiashara wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Jerry William Silaa, kwa jina maarufu Meya Mstaafu, nae ametoa mchango wake mzuri sana katika kuhakikisha kwamba Itifaki hii inafika vizuri. Ninamshukuru mchangiaji wa mwisho, Mheshimiwa Olelekaita, ni rafiki yangu sana, Mwanasheria Msomi, na yeye amechambua vizuri sana ikiwemo kuidadavua Ibara ya 5 ya Mkataba wa Kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo imesemwa, Jumuiya ya Afrika Mashariki inabebwa na nguzo muhimu Nne. Nguzo ya Kwanza ni Umoja wa Forodha, ili kuhakikisha kwamba masuala ya forodha yote katika Jumuiya yanakwenda sawa. Nguzo ya Pili ni Soko la Pamoja. Nguzo ya Tatu ni Umoja wa Sarafu, Nguzo ya Nne ni Shirikisho la Kisiasa ambalo bado halijakamilika katika uanzishwaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa madhumuni na majukumu ya nguzo hizi ambayo kimsingi ni kuongeza mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, suala la migogoro ni la kawaida. Suala la umuhimu na matakwa ya kutafsiri Itifaki mbalimbali ni la kawaida. Kwa hivi sasa Itifaki hizo zimekuwa zikitafsiriwa na nchi zenyewe, hivyo kuleta mgongano wa hapa na pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, michango ya Waheshimiwa Wabunge imesema bayana kabisa, sasa tunakwenda kutoa tofauti hiyo. Hivi sasa kuna uwezekano kwamba kifungu kimoja cha itifaki kikatafsiriwa tofauti Tanzania, kikatafsiriwa tofauti Kenya, kikatafsiriwa tofauti Uganda, kikatafsiriwa tofauti Rwanda, Burundi na South Sudan kutegemeana na Majaji waliokaa kwenye nchi hiyo wameangalia vipi, ili kuondoa mgongano huo ndiyo maana Mahakama hii ilipendekezwa iongezewe mamlaka yake. Kwa hiyo, hiki tunachokwenda kukifanya ni kuongeza mtangamano, tunaimarisha Jumuiya na kuondoa migogoro ambayo ilisababisha jumuiya hii kuvunjika mwaka 1977.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muhimu zaidi tunakwenda kuleta confidence kwa wafanyabiashara wetu. Tunakwenda kuongeza confidence kwa wawekezaji katika Ukanda huu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwamba wakiwekeza fedha zao, wakifanya biashara, kuna chombo madhubuti cha pamoja chenye uhakika cha utatuzi wa migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mahakama hii iko Tanzania ni fursa kwetu sisi ambao ni wenyeji, tunaenda kuongeza ajira zaidi na kuifanya Tanzania iweze kung’ara zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Itifaki hii ni muhimu, na kwa kuwa imejadiliwa sana na Waheshimiwa Wabunge na kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa sana, niruhusu sasa niliombe Bunge lako Tukufu baada ya maelezo hayo yote niliyoyatoa, baada ya kupokea taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, na baada ya michango thabiti ya Waheshimiwa Wabunge, kwa mujibu wa Ibara ya 63(3)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ambavyo imefanyiwa mabadiliko, naomba sasa Bunge lako Tukufu katika Mkutano wake huu wa Nane, likubali kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kuongeza Mamlaka ya Mahakama ya Afrika Mashariki (The Protocol to Operationalize the Extended Jurisdiction of The East African Court of Justice).
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia maoni na mawazo kuhusiana na taarifa ya Kamati mbili; Kamati ya Katiba na Sheria na Sheria Ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuzishukuru Kamati hizi mbili kwa namna ambavyo inatusaidia Serikali hususani sisi Wizara ya Katiba na Sheria. Kamati hizi zinafanya kazi nzuri ya kutoa ushauri na maelekezo ambayo wakati wote tumeyapokea na kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba nichukue nafasi hii kusema kwamba naunga mkono taarifa za Kamati zote mbili. Tumepokea ushauri wa Kamati zote mbili na niahidi kwamba Serikali hii ni Serikali Sikivu, tutakwenda kuzifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu niseme mambo machache; la kwanza ni haki za binadamu ambazo zimeelezwa kwenye Katiba hasa Ibara ya 12 hadi 28.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulifanya mabadiliko ya Katiba mwaka 1984, tukaingiza haki hizi, lakini tunapozisoma hizi haki ni vizuri tusome sambamba na Ibra ya 29 pamoja na Ibara ya 30 ya Katiba ambayo sio tu inaelezea haki hizi unaweza ukazifurahia kwa kiasi gani, lakini inaelezea umuhimu na wajibu wa kulinda haki za watu wengine wakati unafurahia haki hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imeelezwa hapa kwa mfano haki ya faragha ambayo imeelezwa kwenye Ibara ya 16 na hii imekuwa ikitamkwa sana. Ni kweli sheria imetoa haki ya faragha, lakini unapofanya faragha lazima uzingatie sheria za nchi, usije ukatumia faragha mle ndani kufanya uhalifu. Ukifanya uhalifu ile faragha yako itachukuliwa na tutaanza kufuatilia ule uhalifu ambao unaufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia limeongelewa suala la Shule ya Sheria (Law School) yameongelewa mengi, lakini Mheshimiwa Swalle ameongea suala moja muhimu sana kuhusiana na ajira za wanasheria kutakiwa kwamba kila mwanasheria lazima awe amepitia Law School.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tumelipokea na tunakwenda kufanya tathmini na tutarudi kwenye Bunge hili kuwaambia tathmini yetu ni nini ili kwa kazi ambazo hazihitaji Law School na mtu ana degree ya sheria tumruhusu akafanye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani kwenye tume ya usuluhisho wa migogoro ya kazi, ajira inataka watu ambao wamesomea fani za sosholojia waweze kuajiriwa, watu waliosomea fani za sheria waweze kuajiriwa, lakini huyu wa sheria lazima aende Law School. Sasa unaona hapa mzani haujakaa sawia, tumelipokea na tunaenda kulifanyia kazi Serikali hii ni Sikivu, tutarudi katika Bunge hili tukufu kuomba ridhaa yenu ili tuweze kuondoa tatizo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limeongelewa hapa ni matumizi ya lugha ya Kiswahili katika kutafsiri sheria zetu. Hivi sasa tuna sheria 446 kati ya hizo, sheria 216 zimekwishatafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili. Kazi hiyo ni endelevu na Serikali inaendelea kupambana ili kuhakikisha kwamba sheria zote hizi zinatafsiriwa katika lugha ya Kiswahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho, ningependa kuongelea kuhusiana na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka ya Taifa (National Prosecution Services Office).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya mabadiliko makubwa kwenye sheria hii na hivi sasa baada ya kumpata Mwendesha Mashtaka Mkuu, Bwana Sylivester Mwakitalu, amefanya mabadiliko makubwa, amefanya ugatuzi, anafanya usimamizi na sasa hivi uendeshaji wa mashtaka umebadilika sana, hasa chini ya Awamu ya Sita kwa sababu ya mabadiliko hayo. Hii tume ambayo Mheshimiwa Rais ameiunda, inakwenda kuangalia mfumo mzima wa sheria za jinai ambao ulikuwepo toka wakati wa ukoloni na tunaamini sasa itasaidia kwenye maboresho haya ambayo Ofisi ya NPS imekuwa ikiyafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kwa mara nyingine kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi ambavyo anatuongoza hususan katika Wizara hii ya Katiba na Sheria. Namshukuru Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa kazi nzuri ambayo wanawafanyia Watanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee nikushukuru tena wewe kwa namna ambavyo unaliendesha Bunge la Kumi na Mbili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, tumepokea maoni ya kamati mbili; Kamati ya Katiba na Sheria pia Kamati ya Bajeti ikieleza mambo mengi mbalimbali ambayo Wizara tunapaswa kuyatilia maanani ili kuhakikisha kwamba haki siyo tu inatendeka lakini pia inaonekana ikitendeka.
Mheshimiwa Spika, kwa moyo wa dhati kabisa nazishukuru Kamati zote mbili na hasa Wenyeviti wake; Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama na Mheshimiwa Sillo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, kwa maoni yao. Nawaahidi kwamba tumeyapokea na tutakwenda kuyatekeleza.
Mheshimiwa Spika, nawashukuru pia wanakamati wote wa Kamati zote hizo mbili na Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa michango yao kwa Wizara ya Katiba na Sheria siku hii ya leo.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya hoja chache zilizotolewa. Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imejipanga kumfanya kila Mtanzania aweze kuzielewa sheria, aweze kuzitekeleza na kuzitii ili lile suala la kutokujua sheria isiwe utetezi, liweze kuondoka kabisa. Kwa kufanya hivyo, tumejikita katika kutafsiri sheria kutoka kwenye lugha za Kiingereza kwenda kwenye lugha ya Kiswahili. Mpaka hivi sasa katika sheria 466 tulizonazo katika nchi hii, sheria 212 zimeshatafsiriwa. Kila sheria mpya ambayo inatungwa, itakuja kwa lugha ya Kiswahili ili mwananchi aliyeko Kijijini, aliyeko kule Songea na Mbeya, aweze kuzifahamu sheria hizi, kuzitii na kuzitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maboresho ya Mahakama yameongelewa vizuri sana Mheshimiwa Naibu Waziri, niongeze jambo la muhimu. Pamoja na miundombinu ambayo imewekwa na inaendelea kuwekwa, Mahakama imeleta mfumo wa kuwasiliana na mwananchi wa kawaida, kupitia namba ya simu ambayo ni huduma ya bure, kila mwananchi anaweza akapiga na kutuma meseji bure. Tumeitaja namba hiyo ni 0752 500 400; na mpango huo umepewa jina unaitwa “Sema na Mahakama,” kwa saa 24 ndani ya siku saba katika wiki.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa mtu yoyote anaweza akatumia mfumo huo kutoa kero zake, kutoa hoja zake, hata pale ambapo anahisi kwamba kuna kesi imeendeshwa kinyume cha maadili, kuna viashilia vya rushwa, basi atumie mfumo huo. Tahadhari tu ni kwamba mfumo huo siyo rufani; mfumo huo ni kuelezea kero za kiutawala zilizopo, na wala hutaweza kutangua maamuzi yaliyotolewa kihalali kabisa.
Mheshimiwa Spika, pia kumetolewa hoja na Waheshimiwa Wabunge kuelezea mfumo wa jinai na kwa jinsi gani umekuwa ukichelewesha mashauri za kesi za jinai. Niwaeleze Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote, sasa hivi tuna mkakati wa kuuchukua mfumo mzima wa jinai na kuuingiza maabara ili kuweza kujua changamoto hasa ni nini? Baada ya hapo, tuufanyie mabadiliko makubwa sana mfumo wote wa jinai. Tukifanya hivyo tutaondoa kero za kucheleweshwa kesi.
Mheshimiwa Spika, katika hilo, tunaangalia maeneo matatu; eneo la kwanza, tunaangalia Ofisi ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali, wengi hupenda kumwita DPP. Ili tuweze kufanya kazi vizuri, mmesema hapa Waheshimiwa wabunge, lazima tuitendee haki ofisi hiyo. Lazima tuipe vitendea kazi na mambo mengine ili kesi ziweze kwenda vizuri.
Mheshimiwa Spika, pia tunaangalia Mahakama na Mfumo wa Jinai, wapi kuna vikwazo? Tunaenda kuangalia pia Magereza na mfumo wa jinai tunaamini tukifanya hivi ndani ya mwaka huu wa fedha na kuendelea tutakuwa tumetatua matazo makubwa yanayoikabili mfumo wa jinai.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Neema Lugangira amesimama na kutoa hoja ambazo zinagusa sheria mbili; moja ni sheria ya vyama vya siasa; na ya pili ni sheria ya uchaguzi. Mahususi ameongelea kwa jinsi gani sheria hizi hazimtendei haki mwanamke katika uwanja huu wa siasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Neema tumepokea maoni yako kwa uzito mkubwa kabisa. Naomba nichukue fursa hii kuiagiza Tume ya Kurekebisha Sheria kuanzia kesho waanze kuzifanyia kazi sheria hizi mbili; na wawashirikishe wadau wote wakiwemo Waheshimiwa Wabunge wanawake, Waheshimiwa wanasiasa wanawake na wadau wengine ili kujua wapi panawakwaza na tuweze kubadilisha sheria hizi.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo Chama cha Mapinduzi kinasema, sheria hizi zinapaswa kuwatumikia watu, na sio watu kuzitumikia sheria hizi. Ni muda sasa wa kuzirekebisha ili kuweza kutenda haki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Agnesta ameongelea sana kuhusiana na Tume ya Haki za Binadamu.
Tunapokea maoni yake na tuko tayari kuboresha tume hizo. Niseme tu kitu kimoja, katika bajeti ya mwaka huu, Tume za Haki za Binadamu - Fungu la 55, fedha ambayo inapendekezwa endapo Bunge hili Tukufu litapitisha ni shilingi bilioni 6.5. Hiyo ndiyo fedha ambayo tunapendekeza. Kwa hiyo, Mheshimiwa Agnesta, hebu tupitishie hii ili Tume iweze kupata fedha hiyo. Katika fedha hiyo, fedha za nje ni shilingi milioni 155 tu. Kwa hiyo, tunataka kwenda kubadilisha utendaji wa Tume ili Fungu hili la 55 likaibadilishe Tume, Tume itende haki, pia Tume iwafikie wananchi na kutatua kero zote zinazowagusa.
Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine tena nakushukuru wewe na Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Katiba na Sheria
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Daktari Jaji Feleshi kwa maelezo aliyoyatoa pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri Pauline Philipo Gekul kwa maelezo ambayo ametoa katika kujibu hoja mbalimbali za waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee kidogo hoja aliyoizungumzia Mheshimiwa Agnesta kuhusiana na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Kwa mujibu wa Mkataba wa Paris umeweka viwango kwamba Tume za Haki za Binadamu zianzishwe ama kwa Sheria ama kwa Katiba, sisi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuona umuhimu wa Tume hii tumeanzisha kwa nyaraka zote mbili Sheria pamoja na Katiba. Tumeiweka kwenye Katiba ili isiweze kuguswa na kuchezewa na mtu yeyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha kuweka Tume hii katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni dhamira wazi kabisa kwamba Serikali imeipa Tume hii heshima kubwa sana na kwamba haiwezi kuchezewa au kufutwa na mtu yeyote kirahisi. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Agnesta akubaliane nami kwamba Tume hii ni Tume ambayo sisi kama Serikali tunaiheshimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikiongeza Bajeti ya Tume kila mwaka. Mwaka 2021/2022, Bajeti ilikuwa ni bilioni 5.5, lakini leo nasimama hapa mapendekezo ya Bajeti endapo Bunge hili litaridhia na endapo Mheshimiwa Agnesta ataunga mkono ni Shilingi Bilioni 8.1 ongezeko takribani ya Shilingi Bilioni 2.6. Hiyo inaonyesha kwamba Serikali inaongeza kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya Mheshimiwa Agnesta ni Fedha ya Maendeleo. Fedha ya Maendeleo inatumika kujenga Miradi ya Miundombinu na Tume hii kwa sasa hivi haihitaji Miradi ya Miundombinu. Fedha za Operations ya Tume inatokana na OC na katika mwaka huu wa fedha mpaka kufika Machi, Tume imeishapata bilioni 2.2 na imetumia fedha hizo kufanya kazi za kutosha sana. Kwa hiyo kuna utofauti hapa Mheshimiwa Agnesta kati ya fedha za maendeleo na fedha za operations, fedha za operations ziko kwenye OC na tayari Tume hii imeishapokea asilimia 69.79, takribani asilimia 70 na hatujamaliza mwaka. Hii asilimia 30 iliyobaki itakamilika mpaka kufika Juni. Kwa hiyo Tume imepata fedha hizi za operations, maendeleo ni miradi ambayo Tume hii haina miradi kwa sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye hoja alizozitoa Mheshimiwa Luhaga Mpina. Hoja ya kwanza ameshajibu AG, nisingependa kurejea lakini niseme tu pale ambapo mtu ameshinda kesi, amemshinda mtu yeyote yule achilia mbali Serikali, kuna utaratibu wa kisheria wa kukazia hukumu. Sasa hawa watu wana haki ya kufuata utaratibu huo wa kukazia hukumu, iwe dhidi ya Serikali iwe dhidi ya mtu mwingine yeyote sheria zetu zimeweka utaratibu mzuri. Tukiaanza kulitumia Bunge kukazia hukumu za Mahakama, tutakuwa tunaingilia Mhimili wa Mahakama, kwa hiyo tusimame kwenye misingi ambayo tumejiwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Mpina, ameongelea suala la Tume ya Haki Jinai. Tume ya Haki Jinai hii ni maono na maelekezo na matakwa ya Mheshimiwa Rais, ili kuboresha mfumo wa haki jinai ambao tuliurithi toka wakati wa ukoloni. Kwenye hili tunapaswa kumpongeza sana sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuja na wazo hili na sisi tunaamini matokeo ya Tume ya Haki Jinai yatasaidia kuboresha mifumo ambayo tunayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mpina, ameongelea suala la Azimio la Kufuta Hasara ya Fedha kama ambavyo liko kwenye taarifa zangu. Alichokisema yeye ni ni kwamba hili jambo lililetwa lakini halijajadiliwa. Sasa hili ni jambo la Ushahidi, niombe kiti chako kitoe mwongozo kwa sababu tunahitaji sasa kwenda kwenye Hansard na kupitia kumbukumbu zote, tujue kama anachokisema ni kweli au siyo kweli na hatuwezi kukimaliza hapa bila kuomba Mwongozo wa Kiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Mpina ameongea suala la Ofisi ya Mwendesha Mashtaka kushindwa kukusanya shilingi bilioni 170. Najaribu kutafuta nitumie maneno gani kwa sababu tayari kiti kilishatoa mwongozo kwamba mambo yote yaliyokuwemo kwenye Taarifa ya CAG tutayajadili kwa mujibu wa utaratibu na Kanuni za Bunge tulizojiwekea. Sasa akinitaka mimi na Serikali tujibu leo, wakati utaratibu huo haujafika, tunakiuka hata miongozo ya Bunge ambayo tumejiwekea sisi wenyewe. Kwa hiyo tumwambie Mheshimiwa Mpina, tukifika wakati wa kujadili Taarifa za CAG jambo hili tutaliongea na Serikali itatoa maelezo yake wakati huo ukifika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mpina, vile vile ameongelea suala la upekuzi wa Mikataba na akasema kwamba kuna Mikataba kwa mujibu wake yeye anaona haijafanyiwa kazi na AG. Jambo hilo liko kwenye aya ya 53 ya Taarifa ya Bajeti ambayo tumeileta leo. Kwenye hili tunapaswa kumpongeza sana Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa sababu katika mwaka huu wa fedha amepekua mikataba mingi zaidi kwa asilimia 11 kuliko ilivyokuwa mwaka jana. Kwa hiyo amefanya ufanisi zaidi, mtu ambaye amefanya ufanisi tunapaswa kumpigia makofi mengi na kumpongeza na kwa taarifa tu ni kwamba mikataba yote iliyosainiwa ndani ya kipindi husika imepekuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa aya hii ya 53, hakuna Mkataba ambao haujapekuliwa. Ameongelea Mikataba ambayo imethaminishwa ambayo kwa mujibu wa taarifa hii ukurasa wa 28 ni mikataba 567. Mikataba yote iliyopekuliwa ni 1,304. Sasa siyo kila mkataba una thamani ya fedha, kuna mikataba mingine ni memorandum of understanding au ni makubaliano ambayo hayataji fedha mle ndani ambayo ina thamani ya fedha milioni 567. Kwa hiyo niseme kwamba hoja hizo ambazo amezisema Mheshimiwa Mpina ni hoja ambazo sisi tumezifanyia kazi isipokuwa hili moja tu ambalo tutaomba Kiti kitupe mwongozo kwa kadri kitakavyoona inafaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami nichukue nafasi hii kukupongeza sana kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa IPU. Jana nilipokutana nawe nilikuomba nikupe mkono na ulipokubali nilisema kwamba nina bahati ya kupewa mkono na Rais wa IPU. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo ana-support sekta ya michezo. Tumeshuhudia mafanikio makubwa katika Sekta hii, tume-qualify kwa mara nyingine kwenda AFCON mwakani na tumekuwa wenyeji wa AFCON 2027 na kabla ya hapo tutakuwa wenyeji wa CHAN, 2025. Haya yote ni kazi nzuri. Sisi wasaidizi wake tunahakikisha kwamba tunapambana kuiweka Sekta ya Michezo katika muktadha unaostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika sekta ya michezo, tuna Chuo kimoja cha Michezo kinaitwa Chuo cha Maendeleo ya Michezo cha Malya. Chuo hiki, kwa asilimia 56.8 kipo katika Mkoa wa Mwanza na asilimia 43.2 kipo katika Mkoa wa Simiyu. Katika miaka minne iliyopita Serikali na Wizara hii na hasa watangulizi wangu wamefanya kazi nzuri ya kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya chuo hiki. Takribani shilingi bilioni nne zimewekezwa pale katika kuboresha miundombinu ya ujenzi wa hosteli, kutatua changamoto ya maji, kujenga viwanja na ukarabati wa viwanja vya ndani, kujenga jengo la utawala pamoja madarasa. Kazi yangu ni kuendeleza kazi hiyo nzuri ambayo watangulizi wangu wameifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuendelea kuwa na center of sports excellence katika kila Mkoa wa Tanzania. Pale Malya tayari ni center of excellence na inatumika kama Center of Excellence for East Africa, hatuna mpango wa kuhamisha Chuo cha Malya.
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, hatuna mpango wa kusema tunaondoa project yoyote Malya, tutaendelea na project katika mikoa yote. Tunawaomba wenye Mikoa hiyo watupe maeneo kama ambavyo Ilemela wamatupa eneo…
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kasalali Mageni.
TAARIFA
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba Chuo cha Malya, hakina Center of Sports Excellence kwa sababu Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo ilisaini mkataba wa ujenzi wa kituo hicho. Kwa hiyo, hakipo na kama kingekuwepo Serikali isingesaini mkataba.
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 22 Agosti, 2021, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akipokea timu ya under 21 ya Taifa, naomba kwa ruhusa yako nimnukuu alisema maneno yafuatayo: “tuna mpango wa kujenga akademia ya michezo kwenye Chuo cha Michezo cha Malya, Mwanza. Pia kujenga viwanja vitatu vya kisasa vya mazoezi kwenye Mikoa ya Geita, Dar es Salaam na Dodoma, na kuja kujenga Sports Arena mbili Dar es Salaam na Dodoma.”
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Waziri kwamba anachokizungumza kwamba ameshakifanya, hakijafanyika. Kilichofanyika ni mpango mzuri wa Mheshimiwa Rais wa kujenga hiki kitu, na kazi nzuri ya utekelezaji iliyofanywa na Waziri, Mheshimiwa Mchengerwa na Msaidizi wake Dkt. Abbas, ambayo yeye yuko busy kuiharibu. (Kicheko)
SPIKA: Mheshimiwa Waziri, Dkt. Damas Ndumbaro, unaipokea taarifa hiyo?
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, siipokei hiyo taarifa. Mheshimiwa Kasalali, anapaswa kuelewa nini maana ya Center of Excellence? Center of Excellence ni kituo cha umahiri ambacho kinatoa huduma stahiki kwa Tanzania kwenye michezo. Kwa Afrika Mashariki our Center of Excellence ni Malya. Atofautishe na academia. Nukuu aliyoisema ya Mheshimiwa Rais inasema, ‘akademia,’ itajengwa akademia pale Malya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa akademia ni kuendele kuimarisha Center of Excellence. Kwa hiyo, asichanganye nukuu ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa akademia…
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, kuhusu Utaratibu.
SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro, inaonekana kuna kanuni inavunjwa. Mheshimiwa Kasalali Mageni.
KUHUSU UTARATIBU
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, Kuhusu Utaratibu, Mheshimiwa Waziri, ameamua kulidanganya Bunge hadharani kwa sababu, kwa mujibu wa barua ambayo Wizara yake iliiandikia Halmashauri ya Ilemela, nanukuu: “Yahusu Maombi ya Kiwanja Na. 677A, Losi Busweru cha Ujenzi wa Kituo cha Ufundishaji Michezo kwa Ubora.”
Mheshimiwa Spika, kwa barua ambayo consultant aliwaandikia Wizara kwamba, naomba niisome kidogo kwa ruhusa yako.
SPIKA: Sawa. Sasa ngoja kidogo…
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, kwa barua hii ambayo wao walimwandikia contractor wakiomba kuhamisha Center for Excellence, kutoka Malya ambayo mkataba umesainiwa na Serikali imesaini Mkataba wa Ujenzi wa Center for Excellence Malya, na wao wanaomba kuhamisha Center of Excellence ya Malya kupeleka Ilemela, halafu Waziri anasimama na kulidanganya Bunge kwamba ilishajengwa, sasa atuambie hapa, kwamba huu mkataba ambao tunao hapa ni wa Serikali au ni wa nani? Ulikuwa ni wa kujenga nini pale Malya? (Makofi)
SPIKA: Sawa. Waheshimiwa Wabunge, hoja hii alipokuwa amechangia Mheshimiwa Kasalali Mageni, aliihusisha na Taarifa ya CAG kwa maana ya kwamba utaratibu usipofuatwa ndiyo inapelekea zile hoja za CAG. Sasa, naona mjadala wetu unakoelekea tutatoka nje kabisa ya Taarifa ya CAG. Sasa nataka kufanya maamuzi juu ya jambo hili ili tumalize Taarifa za CAG, halafu kuna mambo kama mawili matatu hivi ambayo yatatuhitaji kuyafanyia kazi.
Kwa hiyo, kwa sababu lililetwa hapa Bungeni na linataka kutupeleka nje ya taarifa ambayo tunayo, kwa sababu, Mheshimiwa Kasalali, aliitumia hiyo kama mfano, siyo kwamba ipo kwenye Taarifa ya CAG kwamba, pengine kuna jambo liko namna Fulani; sasa, tukubaliane hivi, Mheshimiwa Waziri kuhusu hoja hii utapewa nafasi baadaye. Mheshimiwa Kasalali Mageni, kuhusu hoja hii utapewa nafasi baadaye. Tutoe nafasi kwa Mheshimiwa Waziri kutoa ufafanuzi juu ya hoja zingine.
Hoja ya kuhamisha hiyo sijui ni uwanja wa mpira ama ni Center of Excellence ama ni akademia, kutoka Kwimba kuelekea Ilemela tutaijadili baadaye kidogo. Tumalizie kwanza hoja ya CAG.
Waheshimiwa Wabunge, nadhani tumeelewana vizuri. Tumeelewana vizuri?
WABUNGE FULANI: Ndiyo. (Makofi).
SPIKA: Sawa. Mheshimiwa Waziri, kwa sababu utapata nafasi baadaye kidogo ya kutoa ufafanuzi kuhusu jambo hili, maana Mbunge baada ya kukupa hii taarifa nimeona linatoka kabisa nje ya Taarifa ya CAG. Kwa hiyo, kama unayo mengine ya kufafanua ni sawa, kama huna, basi tuliache hili, nitakupa nafasi baadaye ili tuwe na jambo hilo Mezani. Ni sawa Mheshimiwa Waziri?
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ni sawa.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 2) wa Mwaka 2018
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuchangia muswada huu muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nitoe shukrani zangu za dhati kwa WaziriPro Kabudi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kazi kubwa ambayo wameifanya katika muswada huu. Muswada huu umebeba sheria 13 ukijumuisha vifungu 108; kuufikisha hapa ulipofika si kazi ndogo, kwa hiyo, tunatoa pongezi za dhati kwenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi nichangie masuala machache, suala la kwanza ni Sheria ni ya Mamlaka ya Majukumu ya Kabidhi Wasii. Sheria hii inapendekeza Kabidhi Wasii na Msaidizi wake waweze kuteuliwa na Rais. Lakini haijaishia hapo tu, nimesema ni mtu au watu ambao lazima wawe na sifa ya kuteuliwa kuwa Majaji. Kwa hiyo sio kama Rais atateua kila mtu hapana huyo mtu awe na sifa ya kuweza kuwa Jaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uteuzi huu wa Rais unazingatia Katiba, ukisoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa kwenye ibara ya 36 (1), (2) na (3) zinampa Mamlaka Rais kuteua viongozi wa taasisi mbalimbali. Kwa hiyo leo tukisema tutunge sheria ya kupingana na Katiba sisi ndio tutakuwa tunafanya kosa. Kwa hiyo iko sahihi kabisa hasa ukizingatia kwamba mtu huyu anapewa mamlaka ya kusimamia sheria tisa, sio sheria moja sheria nyingine tisa, kwa hiyo ni nafasi muhimu sana nafasi ambayo uteuzi wake mamlaka yanapaswa kuwa ni Rais.
Mheshimwa Mwenyekiti, naomba niongelee mabadiliko katika Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kuna mabadiliko mengi yanapendekezwa hapa ukiachilia mbali yale ya tafsiri ambayo yanatokana na kubadilika kwa muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Naomba niongelee suala la uchukuaji wa ushahidi wa kieletroniki, wengi wameongea na kuna mjadala mkubwa pia kuhusiana na suala hili. Kifungu kinachoongezwa hapa, ni kifungu cha 57(5) kinaleta suala jipya. Lakini tujiulize suala lipya hili linakuja
kutibu kitu gani? Lazima tuzingatie ukweli kwamba moja kumekuwa na maendeleo makubwa sana katika teknolojia hii ya electronic, lakini pili watuhumiwa nao wanahitaji haki yao ya kuhakikisha kwamba walichokisema wakati wa upelelezi ndio hicho hicho kinawasilishwa mahakamani hivi leo. Kwa hiyo Sheria ya Ushahidi Sura Namba 6 ilifanya marekebisho kupitia kifungu cha 40A, kifungu cha 76 na kifungu cha 78(a) kuruhusu kupokelewa ushahidi wa kielektroniki Mahakamani. Sasa Sheria ya Ushahidi imeruhusu kupokelewa, lakini kulikuwa hakuna sheria ambayo inasema ushahidi huo utapatikana vipi, utakusanywa vipi, utarekodiwa vipi? Sasa mabadiliko haya ya kifingu cha 57(5) yanakuja kutibu hilo sio tu tuongelee upokelewaji wake Mahakamani, lakini tuhakikishe huu ushahidi tunaupataje ili tusije tukaleta matatizo katika upatikanaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Bunge lako tukufu lirejee kwenye Written Laws Miscellaneous of Amendment Act No. 2 of 2017 ambayo ndio ilijadili na kupitisha upokeaji ushahidi wa ushahidi wa kielektroniki Mahakamani. Sasa wakati ule linajadiliwa hili ziliongelewa sheria mbalimbali kama Cyber Crime Act, Sheria ya Ushahidi, Sheria ya Mawasiliano na Electronic Transaction Act ambazo kwa ujumla zilikuwa zinachagiza upokelewaji wa ushahidi huo Mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kifungu cha 57(5) kilichopendekezwa kuna mambo ambayo ni vizuri sana tuyazingatie, moja; sehemu (b) inasema Mtu atakayefanyiwa hayo mahojiano ya kielektroniki lazima atataarifiwa kwamba sasa tunatumia teknolojia hii ili asichukuliwe kwa ghafla na ili kumpa haki yake. Lakini sehemu (c) inasema kwamba kile kilichorekodiwa nakala pale pale atapewa yule aliyofanyiwa hiyo recording.
Kwa hiyo hii inahakikisha na kuondoa kabisa uwezekano wa kwenda kuibadilisha ile nakala iliyobaki mikononi mwa polisi kwa sababu huyo mtuhumiwa aliyerekodiwa atakuwa nayo. Lakini pia baada ya mahojiano hayo kutakuwa na certificate/kutakuwa na hati na ambayo itakuwa imesainiwa pia na yule mtu aliyekuwa amefanyiwa hiyo recording. Kwa hiyo kifungu hiki hakiepukiki, tunakwenda sambasamba na teknolojia na hakiondoi haki ya ku-record kwa maandishi niliyokuwa nayo zamani ila kinakuja kuongeza vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu kingine ni cha 188 ambacho kinaelezea kwa upana wake jinsi ya kuwalinda mashahidi, hivi sasa kwenye kesi mbalimbali mashahidi wanashindwa kutoa ushahidi kutokana na kutishiwa na kifungu hiki niipongeze sana Serikali kwa sababu kimeazimwa kutoka kwenye Rome Statute sheria ambayo imeanzisha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya ICC imeazimwa kule, kwa hiyo ina kiwango cha kimataifa na sisi tunakileta kiwango cha kimataifa katika sheria zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niruhusu niongelee kuhusiana na masuala ya mali ya uhalifu, hapa hatuongelei mali kwa ujumla wake, tunaongelea mali iliyopatikana kwa njia ya uhalifu. Wanasheria wanafalsafa moja wanasema mtu asinufaike kutokana na uhalifu wake, no one should benefit from his own wrong. Kama umechuma mahali kutokana na uhalifu acha sheria ichukue mkondo wake, lakini naomba nitoe ufafanuzi kwamba suala la kukamata mali duniani kote lazima linafanyika exparte, kwa nini? Mali inaweza ikawa ni fedha iliyoko benki. Unapotaka kwenda Mahakamani msikilize pande zote mbili siku ya pili ile fedha imehama benki utaikamata wapi? Mali inaweza ikawa ni nyumba, gari, unapoweza kufanya application ukaisikiliza mtu anahamisha hiyo mali, kwa hiyo kukamata dunia yote inafanyika exparte. Isipokuwa ku-dispose, kuuza hiyo inakuwa interpret na sheria hii haijasema kwamba itauza exparte hapana, imesema itakamata exparte.
Mheshimiwa Mwenyekti, naomba kuwakilisha naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2018
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Muswada huu wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.3 wa mwaka 2018. Muswada huu unafanya marekebisho kwenye sheria tano mbalimbali ambazo zinajumuisha jumla ya vifungu 27. Ningeomba nichangie kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, suala la kwanza, niwapongeze sana Serikali kwa kuja na mapendekezo mazuri sana. Ukisoma Muswada huu katika sehemu yake ya pili, ya tatu na ya nne ambayo inarekebisha Sheria ya Mahakama ya Rufaa, Sheria ya Mwenendo wa Kesi za Madai pamoja na Sheria ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi, kwa ujumla wake vimeleta kitu kipya katika mfumo wa Sheria, lakini kitu kipya ambacho ni kizuri i.
Mheshimiwa Spika, moja kati ya changamoto kubwa katika uendeshaji wa kesi mbalimbali imekuwa ni mbinu za kisheria ambazo zinatumika Mahakamani na baadaye zinapelekea kunyima haki. Sasa katika sehemu hizi tatu yamekuja mapendekezo kwamba mbinu hizi za kisheria (legal technicalities) ziwekwe pembeni sasa ili kuhakikisha kuwa haki inapatikana, tena kwa haraka, kwa uwiano sawia na kwa gharama nafuu. Ni wazi kabisa kwa mtu yeyote ambaye amewahi kujeruhiwa na mbinu za kisheria huko Mahakamani atapokea mapendekezo haya ya Serikali kwa mikono yote miwili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Nne pia inaongelea kuwapa Mamlaka Mahakimu wa Mahakama za Hakimu Mkazi ili waweze kusikiliza rufaa zinazotoka kwenye Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya kama vile Majaji wa Mahakama Kuu. Tunaongelea hapa Kifungu cha 41A ambacho kinatoa Mamlaka sasa kwa Mheshimiwa Jaji Mkuu kuwateua Mahakimu wa Mahakama za Hakimu Mkazi kuweza kusikiliza rufaa kama Mahakama Kuu yaani kitaalam inaitwa extended jurisdiction.
Mheshimiwa Spika, hii ni muhimu sana, inakwenda kutibu ugonjwa mkubwa sana wa ucheleweshaji wa rufaa za ardhi ambao umekuwa ukilalamikiwa na kila mtu. Katika mashauri mbalimbali yanayohusiana na ardhi rufaa zake zimekuwa zikichelewa kutokana na uhaba wa Majaji wa Mahakama Kuu sasa zile rufaa zinazohusiana na ardhi
zitakwenda sasa kwa Mahakimu ili ziweze kushughulikiwa kwa haraka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo napenda kuliongelea katika Muswada huu ni kwamba sasa Sheria imeweka tahafifu zaidi kwa rufaa katika masuala ya ardhi. Endapo kesi itaanzia Mahakama Kuu kwa hivi sasa, mtu akitaka kukata rufaa kwenda Mahakama ya rufaa hahitaji tena kuomba kibali cha Mahakama Kuu. Hapa tunarudi kule kule, tunaondoa zile legal techinicalities ambazo zimekuwa zikiwasumbua watu kwa muda mrefu. Kuomba kibali kutokwenda Mahakama ya Rufaa ni kazi ngumu sana, inachukua muda mwingi sana, inachukua fedha nyingi sana hivyo kupoteza haki. Tunaipongeza Serikali kwa kuamua kufanya mabadiliko haya kwenye Kifungu cha 47(1) ili kupunguza urasimu huo ambao utasaidia kuokoa muda, fedha na hatimaye kuleta haki kwa warufani mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, pia ningeomba kuongelea Sheria ya Baraza la Michezo Tanzania, Sura ya 49. Kuna mambo mengi yemeingizwa lakini ningeomba niliongelee kwa ufupi suala moja; kutambua kwamba sasa hivi michezo yetu siyo michezo ya ridhaa pake yake. Tumeshafikia kwenye michezo ya kulipwa katika ngumi, soka na michezo mingine, lakini sasa tulikuwa tumefungwa na sheria. Sasa hivi mabadiliko haya yanakwenda kutambua na inapokuwa ni michezo ya kulipwa maana yake vijana wetu tunawapa ajira zaidi, tunatoa fursa, kwa hiyo, haya ni mabadiliko mazuri sana ambayo Serikali imekuja nayo.
Mheshimiwa Spika, katika Sheria hiyo, tunaiomba Serikali ifikirie katika siku zijazo, tena ikiwezekana za hivi karibuni, kuleta mabadiliko ambayo yataingiza utatuzi wa migogoro katika sekta ya michezo, kwa sababu sekta ya michezo sasa hivi ina migogoro mingi na utatuzi wake umekuwa ukibakia katika sekta husika kwa kutegemea Katiba zao.
Mheshimiwa Spika, hizo Katiba zinaleta matatizo zaidi kuliko kutatua matatizo. Ni wakati sasa Serikali ifikirie kuanzisha chombo cha usuluhishi wa migogoro ya michezo cha Kitaifa ambapo migogoro yote ya michezo ikishashindikana katika vyama vyake husika ama endapo mgogoro huo unamhusu mwanachama na chama chenyewe, basi uletwe kwenye hicho chombo cha kitaifa cha kusuluhisha migogoro.Mabadiliko haya yanakwenda mbali zaidi, yanaongelea Sheria ya Takwimu. Ningependa kuongelea tafsiri ambayo imeongezwa ya maneno “official statistics na statistical information” ambayo hayakuwepo hapo awali, lakini kwa sasa hivi maneno haya yameongezwa na kuongeza maneno hayo yameleta tafsiri nzuri zaidi ambayo haikuwepo hapo awali.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla Serikali imekuja na mapendekezo mazuri sana hata sisi tuliokuwa kwenye Kamati tuliyaunga mkono karibu yote na tulifikia kwenye hatua nzuri sana, hivyo naomba kuunga mkono hoja. Ahsante.
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata nafasi ya kuchangia katika Muswada huu muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nitoe pongezi kwa Wizara, Mheshimiwa Prof. Ndalichako, Naibu Mheshimiwa Olenasha pamoja na Katibu Mkuu na Watendaji wote kwa kutuletea Muswada huu muhimu sana katika maslahi na maendeleo ya tasnia ya ualimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiofichika kwamba kwa muda mrefu tasnia hii ya ualimu ambayo sisi wengine ndiyo imetulea imekuwa ikidharaulika, haitambuliki na haiheshimiki. Ukilinganisha na fani nyingine kama madaktari, wahandisi na wanasheria kumekuwa na tofauti kubwa. Madaktari, wahandisi na wanasheria wamekuwa na sheria zao za kutambua na kulinda taaluma yao na kwa kupitia sheria hizo tumeona fani hizi zimeweza kukua, kuendelea, kuheshimika na hatimaye kupata maslahi mazuri. Hivyo Muswada huu unakuja kutibu tatizo ambalo limewakuta walimu kwa muda mrefu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiusoma vizuri Muswada utagundua unaongelea mambo makubwa matatu. Moja, ni usajili na utambuzi kwa walimu, kwanza kuwatambua na hatimaye kuwasajili ambalo ni jambo jema kabisa. Kwa sababu hata kama unataka kumuongezea mtu maslahi na unataka kumuelimisha zaidi kwanza lazima umtambue na umsajili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni maadili. Wote tumekuwa tukisema na tukilalamika kwamba maadili ya walimu yameshuka. Sasa Muswada huu unakuja kushughulikia suala hilo la maadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Muswada huu pia unaongelea maslahi. Tunaposema maslahi wengi tunakimbilia kwenye fedha lakini hata kumuendeleza mwalimu kitaaluma ni maslahi kwa sababu akiendelezwa kitaaluma ndipo ataweza kupata kipato zaidi. Ukimsajili na kumtambua ndipo atapata maslahi zaidi, zitatokea fursa walimu wa aina fulani wanahitajika ndani na nje ya nchi, kwa sababu umewasajili na umewatambua basi pia suala la maslahi linakuja vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye suala la maslahi ni vizuri pia kusisitiza kwamba tunapofanya usajili lazima Mheshimiwa Waziri na timu yake kuangalia ni kwa jinsi gani kutakuwa na kipengele cha kuweza kuongelea maslahi bayana katika sheria hii. Tunajua ni professional instrument lakini lazima kuliongelea hilo kwa sababu maslahi kwa walimu imekuwa ni kilio cha muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maslahi liliwahi kuongelewa na moja kati ya viongozi ambao wanaheshimika sana duniani, Chancellor wa Ujerumani Angela Merkel alivyoulizwa kwamba kwa nini anawalipa walimu kule Ujerumani mshahara mkubwa zaidi kuliko fani nyingine. Akasema kwamba ninyi madaktari, wanasheria na wahandisi mnataka mlipwe zaidi ya walimu waliowafundisha. Kwa hiyo, hapo nasisitiza suala zima la maslahi, tuhakikishe kwamba katika kuuboresha Muswada huu suala la maslahi liwekwe bayana. Umeongelea vizuri maslahi ya kuendelezwa kitaaluma lakini tuweke pia na maslahi mengine kwa walimu hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Muswada huu vizuri na kama umesikiliza mawasilisho yaliyofanywa na Mheshimiwa Waziri leo pamoja na Kamati ni wazi kabisa kuna baadhi ya walimu toka wameajiriwa na wamefanya kazi kwa zaidi ya miaka 20 hawajawahi kupata mafunzo yoyote ya ziada kwa sababu hawajatambuliwa. Sasa hii ni fursa kwa walimu hao na wengine wa namna hiyo kuweza kupata mafunzo kama hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha mwalimu kuwa na leseni na ni utaratibu ambao upo kwenye nchi nyingi tu duniani ikiwemo nchi ambayo tunapenda sana sisi kuinukuu mambo yake, Marekani nao wana utaratibu wa kutoa leseni kwa walimu, ni kitendo ambacho kinaongeza hadhi ya mwalimu. Mtu kuitwa licensed teacher inamuongezea hadhi na heshima, anaweza akatumia leseni ile mpaka kwenda kwenye nchi nyingine za Afrika Mashariki na dunia na ikamsaidia katika kufanya mambo yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hizi leseni kwa walimu zitaondoa walimu makanjanja. Tunalalamika kwamba elimu imeshuka lakini wanaofundisha hawa siyo walimu kweli ni walimu ambao wamejipachika joho la ualimu wakati siyo walimu, tunawaita walimu makanjanja, leseni zitawakimbiza. Sasa ndiyo muda huu wa kutibu matatizo ya kushuka kwa elimu yanayotokana na walimu makanjanja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leseni hizi zitawafanya walimu hawa nao binafsi waweze kukua kitaaluma lakini ziwafanye waweze kupata soko la nje na ndani. Nitoe mfano hivi sasa lugha ya Kiswahili inakua duniani na walimu wa Kiswahili wanahitajika duniani. Je, Tanzania tuna walimu wangapi wa Kiswahili, hiyo takwimu hatuna lakini kupitia leseni hizi tutajua tuna walimu wangapi na kuwatafutia soko walimu hawa katika nchi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kwa makini kifungu cha 21 cha sheria hii ambacho kimewekwa vigezo vinavyomfanya mwalimu aweze kusajiliwa au asisajiliwe. Ukisoma kwa makini vigezo hivyo vimeweka uwazi wa hali ya juu, havijatoa tu mamlaka ya jumla, ipo bayana mno ni kwa kiasi gani mtu anaweza akasajiliwa na asisajiliwe, kiasi kwamba hata ukikataliwa kusajiliwa unajua ni kwa nini umekataliwa kwa sababu kifungu cha 21 cha Muswda huu kimejieleza vizuri sana. Ndito unaona hapa sasa nia nzuri ya Serikali katika kuhakikisha kwamba kila mwalimu mwenye sifa hawezi kukosa kusajiliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nidhamu, maadili na miiko ya ualimu ndiyo msingi wa mafanikio na kukua kwa taaluma ya ualimu. Muswada huu unasisitiza hivyo vitu kwamba lazima kuwe na nidhamu, maadili na miiko. Hivi sasa ukimkamata mwalimu unaanza kutafuta tumshughulikie vipi wakati chombo kama hiki hakipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Niipongeze Serikali kwa kuleta Muswada huu na naomba niseme kwamba ninaunga mkono Muswada huu ili tuendane sambamba na nchi nyingine za Afrika Mashariki na dunia nzima katika kukuza elimu kwa kupitia kuwasajili walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante
Muswada wa Sheria ya Tume ya Mipango wa Mwaka 2023.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nami nitumie hadhara hii na fursa hii kukupongeza sana wewe na kukutakia kila la kheri katika mchakato wa kuiwakilisha nchi katika Bunge la Dunia. Sisi tuna imani na wewe, tuna imani na uwezo wako, tunajua utailetea sifa kubwa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii pia kwa dhati kabisa kuishukuru Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama pamoja na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Florent Kyombo pamoja na Wajumbe wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Muswada ambao nimewasilisha leo unahusu Urekebu wa Sheria. Kwa mujibu wa Sheria ya Urekebu wa Sheria, Sura ya Nne, Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Mwandishi Mkuu wa Sheria za Serikali (CPD) ndiyo wenye mamlaka ya kufanya urekebu huo wa sheria. Nichukue fursa hii kumshukuru sana na kumpongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na CPD kwa kazi nzuri ambayo wameifanya ya kuleta Muswada huu. Umechelewa lakini umekuja na Kamati na Bunge lako limeunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge 15 ambao wamechangia Muswada huu na kwa ufupi wote wameunga mkono, nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Kamati ilitoa maelekezo mawili; la kwanza ni kwamba Miswada hii sasa iwe inakuja kwa lugha mbili, lugha yetu pendwa ya Taifa ya Kiswahili, lakini pia na lugha ya Kiingereza. Serikali hii ni Sikivu, tumelipokea hilo na tayari tumeshaweka schedule of amendment ili ikipita leo hoja hizo nazo ziwe sehemu ya sheria hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kuna hoja kutoka kwa Mheshimiwa Salome Wycliffe Makamba, pacha wangu. Amehoji Sheria ya Ushuru wa Forodha yaani Amendment of the Excise, Management and Tariff Act, Sura 147 hususan kifungu cha 100. Mheshimiwa Salome hajapinga mabadiliko, ameyaunga mkono, kwenye hilo naomba kumshukuru sana. Hoja yake ni kwamba fedha zile zimekwenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nijibu hoja hiyo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mwaka 1995 Serikali ya Chama cha Mapinduzi ilifanya mabadiliko makubwa katika Mfumo wa Ukusanyaji Kodi Tanzania. Ikaunda chombo kipya kinaitwa Mamlaka ya Kodi Tanzania. Mamlaka ya Kodi Tanzania iliunganisha Idara ya Sales Tax, Idara ya Income Tax na idara ya Excise Duty. Idara hizi zilikuwa zinafanya kazi independently na kila moja ilikuwa na mfumo wake. Baada ya kuunganisha sasa zote zikaja chini ya Mamlaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa katika kuunganisha huku kuna vitu vilikuwa havijapitiwa na ndiyo maana ya urekebu wa sheria. Tunaposema urekebu wa sheria au revision siyo amendment wala siyo kutunga sheria mpya, ni kurekebisha makosa madogo madogo ya kiuandishi ambayo yametokana na mabadiliko ya sheria. Katika hili niseme mamlaka makubwa anayo CPD pamoja na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, pale mabadiliko yanapokuwa na uzito mkubwa na yakapelekea hata kubadilisha maana, ndipo tunakuja kuomba ridhaa ya Bunge. Kwa hiyo Mheshimiwa Salome kwanza aishukuru Serikali kwa kuleta haya. Serikali hii ingekuwa siyo makini, siyo transparent basi jambo hili lisingefika hapa, angemaliza Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kwa sababu ya uwazi wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi tumelileta kuiambia Bunge kwamba wakati tunabadilisha sheria mwaka 1995 tulisahau jambo hili, sasa tuliweke sawa, lakini muhimu zaidi ni kwamba ameunga mkono hoja hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa fedha zilikwenda wapi? Ukurasa wa nne wa taarifa niliyoisema, lakini kwenye paragraph au ibara ya 8 ya Muswada uliowekwa mezani imesemwa wazi kwamba fedha hii yote kuanzia mwaka 1995 ilikuwa inaingia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na ukitaka kuiona utakwenda kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali utaisoma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati wa mchango ulijaribu kufungamanisha fedha hii na pre-bargain hivi ni vitu viwili tofauti, hii ni kodi ya kawaida siyo suala la pre-bargain. Mheshimiwa Salome unajua wewe ni Mwanasheria Msomi unaelewa kabisa, lakini ulitaka tu kutuma ujumbe kwa wananchi na mimi najibu ili kutuma ujumbe kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la good faith au nia njema amelisema vizuri Mheshimiwa Mheshimiwa Simbachawane…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa dakika moja.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Ahsante. Mheshimiwa Spika, hili suala la kulinda watu au kuwapa kinga halianzi tu na Maafisa Usalama wa Taifa hata Waheshimiwa Wabunge humu ndani tuna kinga. Ukisoma Ibara ya 100(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1977, Wabunge tuna kinga kwa mambo ambayo tumeyafanya humu ndani, tukitoka nje ya Bunge hili hatuna kinga lakini humu ndani tuna kinga, tumepewa kinga ile ili tusikwaze katika kutekeleza majukumu yetu, lakini kama tunafanya kwa nia njema.
Mheshimiwa Spika, hata humu ndani ukifanya pasipokuwa na nia njema ndipo utaona Kiti kinasimama na kinasema huyu aende kwenye Kamati ya Maadili, ujue nia yako haikuwa njema. Kwa hiyo, hata hiko kipimo cha nia njema humu ndani napo kipo hatujakianzisha sasa, na wapo watu wengi ambao wana kinga na hiki kipimo cha nia njema kinatumika kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi hii, ninalishukuru Bunge lako tukufu kwa kuunga mkono jambo hili, naomba sasa niseme ninaomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Yatokanayo na Urekebu wa Sheria wa Mwaka 2023 .
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nami nitumie hadhara hii na fursa hii kukupongeza sana wewe na kukutakia kila la kheri katika mchakato wa kuiwakilisha nchi katika Bunge la Dunia. Sisi tuna imani na wewe, tuna imani na uwezo wako, tunajua utailetea sifa kubwa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii pia kwa dhati kabisa kuishukuru Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama pamoja na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Florent Kyombo pamoja na Wajumbe wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Muswada ambao nimewasilisha leo unahusu Urekebu wa Sheria. Kwa mujibu wa Sheria ya Urekebu wa Sheria, Sura ya Nne, Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Mwandishi Mkuu wa Sheria za Serikali (CPD) ndiyo wenye mamlaka ya kufanya urekebu huo wa sheria. Nichukue fursa hii kumshukuru sana na kumpongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na CPD kwa kazi nzuri ambayo wameifanya ya kuleta Muswada huu. Umechelewa lakini umekuja na Kamati na Bunge lako limeunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge 15 ambao wamechangia Muswada huu na kwa ufupi wote wameunga mkono, nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Kamati ilitoa maelekezo mawili; la kwanza ni kwamba Miswada hii sasa iwe inakuja kwa lugha mbili, lugha yetu pendwa ya Taifa ya Kiswahili, lakini pia na lugha ya Kiingereza. Serikali hii ni Sikivu, tumelipokea hilo na tayari tumeshaweka schedule of amendment ili ikipita leo hoja hizo nazo ziwe sehemu ya sheria hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kuna hoja kutoka kwa Mheshimiwa Salome Wycliffe Makamba, pacha wangu. Amehoji Sheria ya Ushuru wa Forodha yaani Amendment of the Excise, Management and Tariff Act, Sura 147 hususan kifungu cha 100. Mheshimiwa Salome hajapinga mabadiliko, ameyaunga mkono, kwenye hilo naomba kumshukuru sana. Hoja yake ni kwamba fedha zile zimekwenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nijibu hoja hiyo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mwaka 1995 Serikali ya Chama cha Mapinduzi ilifanya mabadiliko makubwa katika Mfumo wa Ukusanyaji Kodi Tanzania. Ikaunda chombo kipya kinaitwa Mamlaka ya Kodi Tanzania. Mamlaka ya Kodi Tanzania iliunganisha Idara ya Sales Tax, Idara ya Income Tax na idara ya Excise Duty. Idara hizi zilikuwa zinafanya kazi independently na kila moja ilikuwa na mfumo wake. Baada ya kuunganisha sasa zote zikaja chini ya Mamlaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa katika kuunganisha huku kuna vitu vilikuwa havijapitiwa na ndiyo maana ya urekebu wa sheria. Tunaposema urekebu wa sheria au revision siyo amendment wala siyo kutunga sheria mpya, ni kurekebisha makosa madogo madogo ya kiuandishi ambayo yametokana na mabadiliko ya sheria. Katika hili niseme mamlaka makubwa anayo CPD pamoja na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, pale mabadiliko yanapokuwa na uzito mkubwa na yakapelekea hata kubadilisha maana, ndipo tunakuja kuomba ridhaa ya Bunge. Kwa hiyo Mheshimiwa Salome kwanza aishukuru Serikali kwa kuleta haya. Serikali hii ingekuwa siyo makini, siyo transparent basi jambo hili lisingefika hapa, angemaliza Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kwa sababu ya uwazi wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi tumelileta kuiambia Bunge kwamba wakati tunabadilisha sheria mwaka 1995 tulisahau jambo hili, sasa tuliweke sawa, lakini muhimu zaidi ni kwamba ameunga mkono hoja hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa fedha zilikwenda wapi? Ukurasa wa nne wa taarifa niliyoisema, lakini kwenye paragraph au ibara ya 8 ya Muswada uliowekwa mezani imesemwa wazi kwamba fedha hii yote kuanzia mwaka 1995 ilikuwa inaingia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na ukitaka kuiona utakwenda kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali utaisoma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati wa mchango ulijaribu kufungamanisha fedha hii na pre-bargain hivi ni vitu viwili tofauti, hii ni kodi ya kawaida siyo suala la pre-bargain. Mheshimiwa Salome unajua wewe ni Mwanasheria Msomi unaelewa kabisa, lakini ulitaka tu kutuma ujumbe kwa wananchi na mimi najibu ili kutuma ujumbe kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la good faith au nia njema amelisema vizuri Mheshimiwa Mheshimiwa Simbachawane…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa dakika moja.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Ahsante. Mheshimiwa Spika, hili suala la kulinda watu au kuwapa kinga halianzi tu na Maafisa Usalama wa Taifa hata Waheshimiwa Wabunge humu ndani tuna kinga. Ukisoma Ibara ya 100(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1977, Wabunge tuna kinga kwa mambo ambayo tumeyafanya humu ndani, tukitoka nje ya Bunge hili hatuna kinga lakini humu ndani tuna kinga, tumepewa kinga ile ili tusikwaze katika kutekeleza majukumu yetu, lakini kama tunafanya kwa nia njema.
Mheshimiwa Spika, hata humu ndani ukifanya pasipokuwa na nia njema ndipo utaona Kiti kinasimama na kinasema huyu aende kwenye Kamati ya Maadili, ujue nia yako haikuwa njema. Kwa hiyo, hata hiko kipimo cha nia njema humu ndani napo kipo hatujakianzisha sasa, na wapo watu wengi ambao wana kinga na hiki kipimo cha nia njema kinatumika kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi hii, ninalishukuru Bunge lako tukufu kwa kuunga mkono jambo hili, naomba sasa niseme ninaomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, naafiki.