Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Advocate Damas Daniel Ndumbaro (1 total)

MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini pamoja na hayo, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Sera ya Tanzania kuhusu Ukombozi wa nchi za Bara la Afrika na nje ya Afrika iliipatia heshima kubwa nchi yetu ya Tanzania. Nataka kujua Sera hii ya Ukombozi mpaka sasa inaendelea hasa kwa zile nchi ambazo bado hazijapata uhuru kama vile Sahara na Palestina?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, hivi karibu tulisikia kuzorota kwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Jumuiya ya Nchi za Ulaya na Tanzania mpaka ikapelekea mwakilishi wao kurudi nyumbani. Nini mustakabali wa kisera kwa pande hizi mbili ambazo zina mzozo huo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Othman Omar Haji, Mbunge wa Gando kwa maswali yake mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ni wazi kwamba Tanzania imejijengea heshima kubwa sana katika Sera yake ya Ukombozi wa nchi mbalimbali Barani Afrika. Heshima hiyo bado ipo kwa Tanzania kwa sababu bado Sera ya Tanzania ya kupinga unyanyasaji, ukoloni na kutweza utu wa nchi yoyote ile inaendelea. Hivyo, msimamo wa Tanzania katika suala la Sahara pamoja na Palestina bado upo kama ambavyo ulikuwepo mara tu baada ya uhuru.

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba Tanzania ni nchi ya kwanza duniani kuwa na Ubalozi Palestina. Bado tuna heshima hiyo na bado tuna mahusiano hayo mazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kuhusu mahusiano kati ya Tanzania na Jumuiya ya Ulaya. Mahusiano ya kidemokrasia na diplomasia kati ya Tanzania na nchi zote duniani yanaratibiwa na Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 na 1963.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa mkataba huo kila nchi inawajibu wa kuheshimu vipengele vya mkataba huo na endapo pande mmoja haitaheshimu vipengele vya mkataba huo, nchi nyingine ambayo imekosewa inawezaikachukua hatua stahiki. Na pale nchi inapochukua hatua stahiki haimaanishi kuwa mahusiano ya kidiplomasia yamevunjika hapana ni sehemu ya utekelezaji wa mkataba wa Vienna.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwakilisha.