Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita (31 total)
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani juu ya uchimbaji wa madini ya Helium katika Kijiji cha Nyamusi hasa ikizingatiwa kuwa Wananchi wamezuiwa kufanya shughuli yoyote katika eneo lenye Madini hayo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza tangu niteuliwa kuwa naibu Waziri wa Madini kuzimama katika Bunge lako tukufu, naomba nitumie nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kusimama kibali cha kusimama mbele ya bunge lako alaasiri hii ya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kipekee kabisa nimshukuru Mheshimiwa Raisi wetu mpendwa mama Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini na kunipa dhamana hii kubwa ya kulitumikia Taifa letu kupitia sekta hii ya Madini na nimuahidi kwamba nitaifanya kazi hii kwa weledi mkubwa na uaminifu wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya salamu hizo naomba sasa kwa niaba ya Waziri wa Madini nipende kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege (Mbunge wa Jimbo la Rorya) kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa taarifa kwa Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuwa kwa sasa hakuna maombi ya leseni za utafutaji au uchimbaji wa madini ya Helium yaliyopokelewa kutoka katika Kijiji cha Nyamusi. Hata hivyo, katika eneo hilo kuna chanzo cha maji moto ambacho kitalaam ni kiashiria cha uwepo wa madini ya Helium kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa awali na watafiti mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania Geological Survey of Tanzania au kwa kifupi (GST) inaendelea kuhakiki vyanzo vyote vyenye viashiria vya uwepo wa madini ya Helium katika maeneo mbalimbali nchini ambapo katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 GST kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilifanya uhakiki kwenye mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Dodoma na Shinyanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nipende kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa katika mwaka wa 2022/2023 GST itafanya tena utafiti zaidi katika eneo hilo. Vilevile nipende kutoa taarifa kwamba Wizara yangu haijazuia wananchi kuendelea na shughuli katika eneo hilo. Hata hivyo, nitoe wito kwa wananchi kuendelea kuliacha wazi eneo hilo ili kuepusha migogoro na usumbufu iwapo madini hayo yatagundulika kuwa yapo ya kutosha kuchimbwa na wawekezaji kupatikana, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza kuwasaidia Wachimbaji wadogo wa madini katika Mji wa Njombe kama inavyofanya kwenye maeneo mengine?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuwasaidia wachimbaji wadogo Wizara kupitia Shirika la Madini la Taifa imeandaa mkakati maalumu kwa ajili ya kuwasaidia na kuwaendeleza wachimbaji wadogo nchini ikihusisha wachimbaji waliopo Mkoani Njombe, pia. Mkakati huo ambao umeanza kutekelezwa mwaka wa fedha 2021/2022 umejikita kwenye maeneo manne muhimu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza ni Mpango wa Mafunzo (Training Calendar) kwa mwaka mzima ambao utafanyika nchi nzima. Mpango huo uliandaliwa kwa kushirikisha wachimbaji wadogo kupitia uwakilishi wa vyama vyao (FEMATA) na ambao kwa sasa upo tayari kwa utekelezaji. Mafunzo haya yatatotelewa kwa kuhusisha Taasisi mbalimbali zinazohusika na utozaji wa kodi na tozo mbalimbali kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Tume ya Madini pamoja na Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa pili ni Mpango wa kuwawezesha wachimbaji wadogo kukopesheka katika taasisi za fedha ambapo tayari Shirika limeishaingia makubaliano na Taasisi za fedha za ikijumuisha CRDB, NMB na KCB ambazo zipo tayari kuwakopesha wachimbaji hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Tatu ni Kuingia makubaliano na GST (Geological Survey of Tanzania) taasisi yetu ya jiolojia, ambayo itawasaidia wachimbaji wadogo kujua taarifa za mashapo katika maeneo yao kabla hawajaanza kuchimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Nne ni Kupata mitambo ya uchorongaji mahususi kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kwa kuanzia Shirika limeagiza mitambo 5 ya uchorongaji mahususi kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE K.n.y. MHE. ABUBAKARI D. ASENGA) aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapima upatikanaji wa madini ya dhahabu katika Jimbo la Kilombero na maeneo jirani ya Mlima Udzungwa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Damian Assenga, Mbunge wa Jimbo la Kilombero, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Taasisi yake ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), imefanya utafiti wa awali na kuchora ramani kwenye maeneo yote yaliyoko katika Jimbo la Kilombero katika mfumo wa Quarter Degree Sheet (QDS). Tafiti hizi za awali zinaonesha kuwa kuna uwepo wa madini ya dhahabu na madini ya vito katika Kata ya Chisano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, GST pia ilifanya utafiti wa awali na kuchora ramani ya eneo la Hifadhi ya Milima ya Udzungwa na maeneo jirani. Hata hivyo, utafiti umeonesha kwamba, hakuna taarifa zozote za uwepo wa madini ya thamani katika milima hiyo. Ahsante.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza: -
Je, Serikali ina taarifa juu ya madini yanayopatikana Kakonko na wananchi wananufaikaje nayo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (Geological Survey of Tanzania - GST), Wilaya ya Kakonko ina madini yafuatayo; dhahabu katika Kata za Nyamtukuza, Gwanumpu, Muhange na Kasuga. Pia ina madini ya vito aina ya Agate katika Kata za Gwanumpu na Kasanda na ina madini ya ujenzi katika Kata zote za Wilaya ya Kakonko.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara imetoa leseni 27 za wachimbaji wadogo wa madini katika maeneo tofauti ya Kakonko kama ifuatavyo:- Dhahabu leseni 21, mawe ya chokaa leseni Mbili, shaba leseni Moja, kokoto leseni Tatu, mchanga leseni Moja, chuma leseni Moja na mawe leseni Moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na uwepo wa leseni za uchimbaji mdogo wa madini ambapo migodi huhitaji watu wengi wa kuzalisha, hivyo kwa njia hiyo wananchi wananufaika na ajira za moja kwa moja katika migodi kwa kutoa huduma mbalimbali kama chakula, malazi, usafirishaji na kadhalika, hivyo kuongeza manufaa ya kiuchumi kwa wananchi wa Wilaya husika na hususani kwa Wilaya ya Kakonko. Ahsante sana.(Makofi)
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza: -
Je, ni maeneo gani yametambuliwa kuwa na madini Mkoani Iringa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati (Mbunge wa Viti Maalum) kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Taasisi yake ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), ilifanya utafiti wa awali na kuanisha madini yanayopatikana katika Mkoa wa Iringa. Miongoni mwa madini yanayopatikana katika Mkoa wa Iringa ni dhahabu katika Kata za Sadani, Ikweha, Malengamakali, Mlolo, Ifunda, Kalenga, Idodi na Pawaga; shaba katika kata za Mahenge, Kiwele, Pawaga, Nyang’oro, Malengamakali na Kihongota; madini viwanda aina ya chokaa katika Kata za Kiwele, Idodi, Inyigo, Ifunda na Kihongota; udongo wa mfinyanzi (ball clay) katika Kata za Ifunda na Rungemba; kaolin katika Kata za Mbalamaziwa, Nyanyembe, Nyololo na Ifunda; kyanite katika Kata ya Mlowa; bauxite katika Kata ya Rungemba; chuma katika Kata ya Mawindi; na vito katika Kata za Isimani, Idodi na Kiwele.
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza: -
Je, Serikali ina taarifa juu ya upatikanaji wa madini Nanyumbu na Je, wananchi wananufaikaje?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahya Ally Mhata, Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu, kwa Niaba ya Waziri wa Madini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Taasisi yake ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), ilifanya utafiti wa awali katika Wilaya ya Nanyumbu iliyopo kwenye Quarter Degree Sheet (QDS) 316 na kubaini uwepo wa madini mbalimbali. Utafiti huo ulionesha kuwepo kwa madini ya dhahabu katika vijiji vya Lukwika, Chungu, Chipuputa na Masuguru. Katika kijiji cha Masuguru utafiti huo ulibaini pia uwepo wa madini ya sapphire, Acquamarine na rhodolite. Aidha, Wilaya ya Nanyumbu imebainika kuwa na madini mengine yakiwemo madini ujenzi.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini katika Wilaya ya Nanyumbu imetoa leseni za uchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu 73, madini ya chuma nane, madini ujenzi mbili, madini ya vito 10 na leseni mbili za utafutaji wa madini ambapo moja ni kwa ajili ya utafutaji madini ya nikeli na nyingine ni kwa ajili ya madini ya dhahabu. Aidha, katika maeneo hayo shughuli za utafiti na uzalishaji zinaendelea. Kufuatia shughuli hizo wananchi wamekuwa wakijipatia kipato, ajira na mzunguko wa biashara kuwepo katika vijiji hivyo.
Mheshimwa Spika, ahsante sana.
MHE. ROBERT C. MABOTO aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kumaliza mgogoro kati ya Wananchi na Wawekezaji wenye leseni ya uchimbaji madini Kata ya Guta – Bunda?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Robert Chacha Maboto, Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mgogoro uliopo unahusisha wamiliki wa mashamba waliojichukulia haki madini (Mineral Rights) bila kufuata sheria kwenye eneo ambalo leseni zilikwishatolewa kwa mwekezaji aitwaye JB & Partners ambaye alipewa leseni ndogo za uchimbaji (PMLs) nane (8). Leseni hizi zimo ndani ya mashamba 21 ya wakazi wa maeneo ya Mtaa wa Stooni, Kata ya Guta Wilaya ya Bunda. Mpango uliopo ili kumaliza mgogoro huo ni kuendelea na majadiliano ili kufikia maridhiano kati ya wamiliki wa mashamba hayo na mwekezaji aliyepewa leseni. Hadi sasa kupitia majadiliano wamiliki wa leseni wamekwishaingia maridhiano na kusaini makubaliano ya uchimbaji kwa ubia na wamiliki wa mashamba 13 kati ya 21 wanaotambulika katika eneo hilo la uchimbaji.
Mheshimiwa Spika, kwa mashamba 13 mgogoro wake ulifika tamati na machimbo kufunguliwa na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mara mnamo tarehe 6 Oktoba, 2022 na shughuli za uchimbaji zinaendelea. Wamiliki wa mashamba nane waliobaki waliogoma kufanya majadiliano na walifungua kesi ya ardhi (Land Case No. 12 of 2021) katika Mahakama ya Musoma ambayo inaendelea kusikilizwa. Hata hivyo, wamiliki wa mashamba hayo nane wamepatiwa nafasi nyingine ya majadiliano na katika maeneo yao uchimbaji umesimamishwa hadi pale watakaporidhiana. Endapo watashindwa kuridhiana ndani ya muda uliowekwa kwa mara nyingine basi taratibu nyingine za kisheria zitafuatwa kwa mujibu wa Kifungu cha 97 cha Sheria ya Madini, Sura 123. Ahsante sana.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wanawake wanakuwa wachimbaji wa madini nchini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia STAMICO ina jukumu la kuwasadia wachimbaji wadogo wa madini wa makundi mbalimbali nchini wakiwemo wanawake. Aidha, STAMICO imeandaa na kutekeleza mikakati mbalimbali kuhakikisha wanawake pia wanakuwa wachimbaji madini nchini.
Mheshimiwa Spika, mikakati hiyo inahusisha, pamoja na mambo mengine, kutoa mafunzo mbalimbali ya nadharia na vitendo kwa wachimbaji wadogo wakiwemo wanawake kupitia vituo vya mfano tulivyonavyo katika maeneo ya Katente (Bukombe), Lwamgasa (Geita) na Itumbi (Mbeya); kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata taarifa sahihi za mashapo kwa kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ambapo kwa sasa STAMICO imeagiza mitambo mitano ya uchorongaji maalumu kwa ajili ya wachimbaji wadogo nchini ili kuwasaidia kufanya utafiti.
Mheshimiwa Spika, mkakati mwingine ni kuwaunganisha wachimbaji na taasisi za Kifedha zikiwemo Benki za CRDB, NMB na KCB kwa lengo la taasisi hizo kuweza kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo nchini wakiwemo wanawake. Ahsante sana.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani kuiwezesha GST kufanya utafiti wa kisayansi na teknolojia kuhusu Critical Minerals ili kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini imeielekeza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuandaa taarifa kuhusiana na madini mkakati (Strategic/Critical Minerals) hasa madini teknolojia ikiwemo madini muhimu kwa ajili ya nishati ya kijani (green energy minerals). GST imeanza kuandaa andiko kuhusiana na madini haya na kuainisha ni madini yapi ndiyo ya kimkakati kwa mtizamo wa dunia na nchi, matumizi ya madini hayo na mahala yanapopatikana.
Aidha, GST imebaini maeneo ya kufanya tafiti za jiofizikia katika maeneo sita (blocks) kwa nishati ya kijani (green energy) na matumizi ya magari ya umeme. Serikali inaendelea kutafuta wadau wa maendeleo ambao watashirikiana katika kufanya tafiti za jiosayansi. Ahsante sana.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuwawezesha wachimbaji wadogo wanawake kwa kuwapa mikopo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha wachimbaji wadogo hususan wanawake wanapata mikopo, Serikali kupitia STAMICO imepanga kununua mitambo mitano (5) midogo ya uchorongaji (utafiti madini) ambapo taratibu za ununuzi wa mitambo hii zinakamilishwa hivi sasa. Mitambo hiyo itawazesha wachimbaji wadogo kujua kiasi cha mashapo yaliyopo katika maeneo yao. Aidha, STAMICO imeingia makubaliano ya ushirikiano (MoU) na baadhi ya mabenki nchini kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo wakiwemo wanawake. Benki hizo ni CRDB, NMB na KCB ambapo katika utekelezaji wa makubaliano hayo, benki hizo zimejengewa uelewa wa sekta ya madini na namna nzuri ya utoaji mikopo kwa sekta hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Madini imekuwa ikiwahamasisha wachimbaji wadogo hususan wanawake kujiunga katika vikundi ili kurahisisha utoaji huduma mbalimbali zinazolenga kuwawezesha kupata fedha, vifaa vya uchimbaji na uchenjuaji wa madini. Ahsante sana.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -
Je, kwa mujibu wa tafiti ni madini aina gani yanapatikana katika Mkoa wa Rukwa na katika maeneo gani?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege Mbunge wa Jimbo la Kalambo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa mikoa iliyobarikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali. Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) mkoa huu una madini yafuatayo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dhahabu katika kata za Kabwe, Namanyere, Msenga na Ninde. Shaba katika Kata za Kirando, Namanyere, Msenga, Kala na Ninde. Risasi katika Kata za Namanyere na Ninde, Makaa ya Mawe katika Kata za Chala, Kipande, Muze na Ntendo. Madini ya viwandani kuna chokaa Kata ya Ntendo, na Kyanite Kata ya Msenga. Chumvi Kata za Kirando, na Kipeta. Ulanga Kata za Mkwamba, Mwazye, Kaoze na Senga. Vito katika Kata za Chala, Kipande, Senga na Malangali. Rare Earth Elements Kata za Mkwamba na Msenga. Chemichemi za majimoto zenye kuambatana na gesi ya helium katika Kata za Kirando na Msenga, na Chuma katika Kata ya Katazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, madini mengine ni madini ujenzi ambayo ni kokoto na mchanga ambayo yanapatikana katika Wilaya zote za Mkoa wa Rukwa ahsante sana.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza: -
Je, nini hatma ya madai ya maslahi ya waliokuwa wafanyakazi wa mgodi wa TanzaniteOne?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa Wizara ya Madini imepokea malalamiko ya kutolipwa mishahara ya waliokuwa wafanyakazi wa Kampuni ya TanzaniteOne Mining Limited (TML) iliyokuwa ikichimba madini katika eneo la Kitalu ‘C’ Mirerani.
Mheshimiwa Spika, Wizara ilifuatilia suala hili na kubaini kuwa wafanyakazi 540 walifungua shauri katika Tume ya Usuluhishi na Upatanishi (CMA) Arusha na shauri hilo Na. CMA/ARS/ARD/112/2018 ni la madai ya malimbikizo ya mishahara ya miezi 11 na stahiki zao zingine.
Mheshimiwa Waziri, shauri hilo lilisikilizwa na hukumu ilitolewa kuwa TML ilipe wafanyakazi hao jumla ya shilingi 2,529,331,585 kama malimbikizo ya mishahara yao ya miezi 11 na stahiki zao zingine.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hukumu kutolewa hadi sasa wafanyakazi hao hawajalipwa stahiki zao. Hata hivyo, kwa kuwa suala hili limesikilizwa na kutolewa maamuzi na Mahakama, na bado lipo kwenye taratibu za kisheria, Wizara ya Madini inasubiri taratibu za mahakama kukamilika ili kujua hatima ya suala hili, ahsante sana.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: -
Je, Serikali ina taarifa gani juu ya Madini yanayopatikana Wilaya ya Urambo na lini itawasaidia Wananchi ili wanufaike na Madini hayo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Jimbo la Urambo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa tafiti zilizowahi kufanywa na GST kuhusu madini yapatikanayo nchini, Wilaya ya Urambo ina madini mbalimbali lakini ni kidogo sana. Madini hayo ni kama vile dhahabu, urani, shaba, malbo, udongo mfinyanzi au clay na miamba migumu ya ujenzi mfano granite. Pamoja na Wilaya hiyo kuwa na kiwango kidogo cha madini kwa tafiti zilizokwishafanyika, zipo leseni Nne (04) za uchimbaji mdogo. Lakini katika leseni hizo, leseni Tatu (03) ni za uchimbaji mdogo wa madini ujenzi na leseni Moja (01) ni ya uchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu.
Mheshimiwa Spika, GST ambayo ni taasisi yetu ya Jiolojia (Geological Survey of Tanzania) inaendelea kuhuisha kitabu chake cha madini yapatikanayo katika Mikoa yote Tanzania Bara na kwa sasa tayari Mkoa wa Tabora na Wilaya zake ikiwemo Wilaya ya Urambo ni moja kati ya mikoa itakayofanyiwa utafiti kwa lengo la kuhuisha kitabu hicho.
Mheshimiwa Spika, mara baada ya utafiti huo kukamilika, ramani ya uwepo wa madini hadi ngazi ya kijiji itaandaliwa na wananchi kupata taarifa hizo kupitia Serikali ya Kijiji na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya. Taarifa hizo zitawasaidia wananchi wote ikiwa ni pamoja na wananchi wa Wilaya ya Urambo kuwekeza katika sekta ya Madini kwa ujumla.
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -
Je, ni lini uchimbaji wa madini ya dhahabu utaanza katika eneo la Utegi, Tarafa ya Girango?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini imeendelea kutoa leseni za utafutaji wa Madini nchini. Katika Eneo la Utegi kuna leseni za utafutaji wa madini za Kampuni ya North Mara Gold Mine Limited na ABG Exploration Limited. Kwa sasa kampuni hizi zinaendelea na utafutaji wa madini katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, uchimbaji wa madini hutegemea kukamilika kwa mafanikio kwa zoezi la utafutaji wa madini ambalo huhusisha shughuli za kijiolojia. Aidha, shughuli hizi huchukua gharama kubwa na muda mrefu. Kwa msingi huo, eneo la Utegi linatarajiwa kuanza uchimbaji baada ya utafiti kukamilika na kuonekana kwa mashapo yenye kutosheleza kuanzisha uchimbaji kwa faida. Aidha, Serikali kupitia Tume ya Madini inafuatilia kwa karibu shughuli za utafutaji wa madini zinazofanyika nchi nzima.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI K.n.y. MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha Wanawake wanashiriki kikamilifu kwenye mnyororo wa madini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Wazari wa Madini, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wamekuwa wakishiriki kwa kiasi kikubwa kwenye sekta ya madini kupitia vyama mbalimbali ikiwemo Shirikisho la wachimbaji wadogo nchini (FEMATA) lenye lengo la kuwaunganisha wachimbaji wadogo wa madini wakiwemo wanawake pia Umoja wa Wanawake Wachimbaji Madini (TAWOMA) ambao unajumuisha wanawake wote wanaojishughulisha na shughuli za uchimbaji na utengenezaji bidhaa mbalimbali zinazotokana na madini. Pia wako Muungano wa Wanawake Wanaouza Bidhaa Mbalimbali Migodini (WIMO) na Chama cha Tanzania Women in Mining and Mineral Industry (TWIMMI) ambacho kimeundwa kwa lengo la kuwaweka pamoja wachimbaji wa madini wanawake na wote walioko kwenye sekta ya madini ili kuweka mazingira bora ya kuwawezesha wanawake na ustawi wa sekta ya madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na uwepo wa vyama hivyo Wizara imekuwa ikisaidia wanawake kwenye sekta ya madini katika mnyororo mzima kwa kuwapa leseni za uchimbaji, uongezaji thamani na uuzaji madini, ahsante sana.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: -
Je, ni lini Wananchi wa Kitongoji cha Nyamichele watalipwa fidia kutokana na madhila waliyoyapata kutoka Mgodi wa Barrick?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Mgodi wa Barrick North Mara kwa sasa hauhitaji eneo la Kitongoji cha Nyamichele kama wananchi walivyokuwa wametarajia hapo kabla.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Mgodi wa North Mara kutohitaji eneo hilo, kuna utaratibu ambao unaandaliwa na mgodi huo wa kutoa kifuta jasho kwa wananchi waliopata madhila kutoka kwa mgodi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka wapimaji wa miamba ya madini katika Mikoa ya Rukwa na Songwe?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imekwishafanya utafiti wa miamba katika Mikoa ya Rukwa na Songwe na kuchora ramani za miamba katika kipimo cha skeli ya 1:100,000 ambazo hutumika kuonesha uhusiano wa miamba na madini. Ramani hizi za miamba zinapatikana GST na ndizo kwa sasa hutumika kuvutia uwekezaji katika sekta ya madini kwa maeneo hayo. Ahsante sana.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itawasaidia wanawake na vijana wa Kata za Mitesa na Nanjota wanaojihusisha na uchimbaji madini Lulindi?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Lulindi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Mtwara umebarikiwa kuwa na madini mbalimbali yakiwemo madini ya ujenzi ambayo huchimbwa zaidi na wananchi hasa wanawake na vijana. Aidha, Tume ya Madini imetoa leseni za uchimbaji madini ya ujenzi na chumvi kwa vikundi 11 vya wanawake na vijana. Vikundi hivyo ni pamoja na Mtazamo Group, Wazawa Group, Mwambani Group, Wasikivu, Songambele Group, Tusaidiane, Nguvu Kazi Youth Group katika Halmashauri ya Mji wa Masasi na Kikundi cha Kiumante kilichopo katika Manispaa ya Mtwara – Mikindani; Vikundi vya Makonde Salt Group, Mapinduzi na Umoja wa Vijana vilivyopo katika Halmashauri ya Mtwara Vijijini.
Mheshimiwa Spika, ili kuweza kuwasaidia wanawake na vijana wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini katika Kata za Mitesa na Nanjota, tunawashauri Wanawake na Vijana wajiunge kwenye vikundi na kusajiliwa katika Halmashauri husika. Kufanya hivyo itakuwa rahisi kuwahudumia na kuwasaidia kupatiwa leseni za uchimbaji na mikopo kutoka Halmashauri husika na hata mabenki.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha kujiunga katika vikundi ili kuweza kupatiwa huduma kwa ufanisi na kwa haraka zaidi.
MHE. STELLA I. ALEX K.n.y. MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: -
Je, Mkoa wa Dar es Salaam umefaidika vipi na uzalishaji wa madini ya ujenzi yaliyozalishwa katika Mkoa huo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba Mkoa wa Dar es Salaam unazalisha na unanufaika na madini ujenzi, hata hivyo wastani wa asilimia 60 ya madini ujenzi yanayotumika kwenye ujenzi wa miradi ya kimkakati katika Mkoa huo yanazalishwa kutokea Mkoa wa Pwani katika Wilaya za Mkuranga, Bagamoyo, Kisarawe na Kibaha.
Mheshimiwa Naibu Spika, madini ujenzi yanayozalishwa katika Mkoa wa Dar es Salaam yanajumuisha mchanga, kifusi na limestone, ambayo yanazalishwa katika Wilaya za Kigamboni, Ilala na Kinondoni. Kwa mwaka wa fedha 2022/2023, makusanyo ya mrabaha na ada ya ukaguzi yatokanayo na madini hayo katika Mkoa wa Dar es Salaam yalifikia kiasi cha shilingi bilioni 1.9.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini itaendelea kuimarisha usimamizi katika uzalishaji wa madini ujenzi katika Mkoa wa Dar es Salaam na nchini kote kwa ujumla ili kuongeza manufaa ya madini hayo kwa mwananchi mmoja mmoja na Taifa.
MHE. JESCA D. KISHOA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaweka wazi mikataba ya sekta ya uziduaji kama The Extractive Industries Transparency Initiative inavyotutaka?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni mwanachama wa Asasi ya Kimataifa ya EITI (Extractive Industries Transparency Initiative). Ambalo jukumu lake kuu ni kuhamasisha Serikali kuweka mifumo ya uwazi katika rasilimali madini, mafuta na gesi asilia ili kuboresha mapato na manufaa yanayotokana na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa rasilimali hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza takwa la uwekaji wazi wa mikataba Taasisi ya TEITI imeandaa Mpango kazi (Roadmap) kwa ajili ya utekelezaji wa kazi ya uwekaji wazi mikataba. Mpango huo umewekwa wazi kwa ajili ya utekelezaji kulingana na matwaka ya Kimataifa ya Taasisi ya EITI. Kwa hivyo, katika mwaka wa fedha 2023/2024 TEITI imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa mikataba inawekwa wazi, ikiwa ni pamoja na kushauriana na mamlaka nyingine za Serikali namna bora ya kutekeleza mikataba na takwa hili. Ahsante.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:-
Je, kuna mkakati gani wa kutatua kero zinazowakabili wachimbaji na wasafirishaji wadogo wa dhahabu Mgodi wa Kebaga?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Michael Mwita Kembaki, Mbunge wa Tarime Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Kebaga kilichopo Wilaya ya Tarime kina madini ya dhahabu ambayo wachimbaji wadogo wanachimba.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha wachimbaji hao wanafanya shughuli zao ipasavyo, Wizara kupitia Tume ya Madini imeanzisha kituo kidogo cha ununuzi wa dhahabu katika eneo la Kebaga ambapo wachimbaji huuza madini yao. Aidha, Tume ya Madini hufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa lengo la kuhakikisha wachimbaji na wachenjuaji wa dhahabu wanafanya kazi hizo kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Madini na kushughulikia kero zozote zinazowasilishwa na wachimbaji wa mgodi huo, ahsante sana.
MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: -
Je, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha utaratibu wa kupata baruti na zebaki unakuwa rahisi na vibali vitolewe kwa ngazi ya kijiji kwa wachimbaji wadogo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Jimbo la Lupa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuimarisha usimamizi, upatikanaji na matumizi ya baruti hapa nchini. Ili kurahisisha upatikanaji wa vibali vya baruti Wizara imesogeza huduma hiyo katika Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa yote ya kimadini nchini ikiwemo Chunya. Aidha, Serikali imesajili na kutoa vibali vipya vya biashara ya baruti kwa kampuni 25 ambazo hutoa huduma hiyo hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini katika kipindi cha mpito kwa matumizi ya zebaki imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ikiwemo kushirikiana na Ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya ufuatiliaji wa taratibu za uingizaji na usambazaji wa kemikali ya zebaki nchini ili kubaini changamoto za upatikanaji wa kemikali hiyo na kuandaa takwimu za kiasi cha matumizi ya zebaki ili kujua kiasi kinachohitajika nchini ili kurahisisha utoaji wa vibali vya uingizaji na kuwatambua na kuwasajili waingizaji na wasambazaji wa kemikali ya zebaki nchini kwa mujibu wa Sheria ya Kemikali nchini ili biashara hiyo ifanyike kwa uwazi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kemikali ya zebaki kutumika katika shughuli za ukamatishaji wa dhahabu, tafiti za kisayansi zimebainisha kuwa kemikali hiyo isipotumika vizuri ni hatari kwa afya ya binadamu na mazingira, jambo lililosababisha Serikali kusaini Mkataba wa Minamata (Minamata Convention) ambao utekelezaji wake unapelekea kupunguza matumizi ya zebaki au kuondoa kabisa pale inapowezekana.
Mheshimiwa Spika, kutokana na madhara ya matumizi ya zebaki, Serikali kupitia mradi wa Environmental Health and Pollution Management Program –imeanza kutafuta njia mbadala ya uchenjuaji kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu ili kuondokana na madhara yanayotokana na matumizi ya kemikali hiyo. Mradi huo unafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) na kutekelezwa chini ya Baraza la Udhibiti na Usimamizi wa Mazingira (The National Environmental Management Council - NEMC), ahsante.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza: -
Je, uchimbaji wa madini kando ya mito na maziwa ni chanzo cha upungufu wa samaki?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Anyigulile Jumbe Mlaghila, Mbunge wa Jimbo la Kyela, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tunafahamu kuwa uchimbaji wa madini umegawanyika katika aina kuu mbili, uchimbaji juu ya ardhi na ule wa chini ya ardhi (surface and underground mining) na unafuata Sheria ya Madini, Sura 123 ambayo hairuhusu uchimbaji wa madini katika vyanzo vya mito na maziwa. Endapo shughuli za uchimbaji zitafanyika kando ya mito au maziwa, zitafanyika umbali wa mita 60 kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya Mwaka 2004.
Mheshimiwa Spika, aidha, kabla ya shughuli za uchimbaji wa madini kufanyika katika eneo husika tathmini ya mazingira hufanyika na kutathmini athari za kimazingira ikiwemo viumbe hai pamoja na vyanzo vya maji. Hivyo, hakuna uhusiano wa moja kwa moja kwa uchimbaji wa madini na upungufu wa samaki katika mito na maziwa. Ahsante sana.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE aliuliza: -
Je, lini Serikali itatoa leseni kwa wachimbaji wadogo wa madini Kata za Nditi na Kiegi – Nachingwea na maeneo mengine ya Mkoa wa Lindi?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amandus Julius Chinguile, Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini hadi Oktoba 2023, imetoa jumla ya leseni 2731 za uchimbaji mdogo wa madini katika Mkoa wa Lindi. Aidha, leseni zaidi ya 200 za Uchimbaji Mdogo wa Madini zimetolewa katika Vijiji vya Kiegei na Nditi Wilayani Nachingwea.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini itaendelea kutoa leseni za madini katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Wilaya ya Nachingwea na maeneo mengine ya Mkoa wa Lindi kadri itakavyokuwa ikipokea maombi ya leseni kutoka kwa wananchi ili kuwezesha ushiriki wao katika uchumi wa madini, ahsante sana.
MHE. NDAISABA G. RUHORO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi wa Jimbo la Ngara wananufaika na uchimbaji wa madini ya Nickel?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, Mbunge wa Jimbo la Ngara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchimbaji wa madini ya Nickel katika eneo la Kabanga unafanywa na Kampuni ya Tembo Nickel Corporation Limited iliyopewa leseni mnamo tarehe 25 Oktoba, 2021. Mradi huo unatarajiwa kuchangia ushuru wa huduma kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kiasi cha dola za Marekani milioni 65, sawa na takribani shilingi bilioni 151 kwa kipindi cha uhai wa mgodi huo. Aidha, mradi huo unatarajia kutoa ajira za moja kwa moja 978 kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Aprili, 2022 mradi ulikuwa umetumia jumla ya dola za Marekani milioni 1.5 katika ununuzi wa bidhaa na huduma ndani ya nchi. Kati ya hizo, Dola 125,673 zilitumika kufanya ununuzi katika Wilaya ya Ngara. Hivyo, nitoe rai kwa wananchi wa Wilaya ya Ngara na Taifa kwa ujumla kuchangamkia fursa zilizopo katika mradi huo. Aidha, kupitia Sheria ya Wajibu wa Makampuni kwa Jamii (Cooperate Social Responsibility - CSR), mradi huo ulichangia takribani Shilingi milioni 39 kwa mwaka 2021 na unatarajiwa kuchangia jumla kiasi cha shilingi milioni 207.8 mwaka huu 2022, ahsante sana.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: -
Je, lini Wananchi wa Nyambalembo, Magema, Katoma, Mizingamo, Katumai na Nyakabale wanaoishi eneo la leseni ya GGM watalipwa fidia?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikishughulikia mgogoro baina ya wananchi na Mgodi wa GGM kwa kufanya majadiliano na mgodi huo ili kutafuta muafaka wa namna bora ya kumaliza migogoro katika kila eneo husika, ikiwa ni pamoja na ulipaji wa fidia stahiki. Majadiliano hayo yanaendelea katika maeneo ambayo bado hayajapatiwa utatuzi wa pamoja kuhusiana na ulipwaji wa fidia. Majadiliano yakikamilika Wizara itatoa taarifa. Kwa maeneo ambayo hayakuwa na ubishani wa upande wowote, zoezi la uthamini wa ardhi na mali za wananchi wanaoishi katika maeneo hayo, linaendelea kwa ajili ya ulipwaji wa fidia.
Mheshimiwa Spika, aidha, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa, taratibu za uthamini wa ardhi na mali za wananchi wanaoishi katika eneo la Samina ambalo nalo liko ndani ya leseni ya GGM zinaendelea, ahsante sana.
MHE. AGNES E. HOKORORO K.n.y. MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: -
Je, nini mpango wa Serikali kuhakikisha uchimbaji wa Mbunyu unatekelezwa katika Kata ya Chiwata - Ndanda? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Madini ilitoa leseni mbili za uchimbaji wa kati zenye namba ML 591/2018 na ML 592/2018 kwa Kampuni ya Volt Graphite Tanzania Public Limited ili kuendesha shughuli za uchimbaji wa madini ya kinywe (graphite) katika Mradi wa Mbunyu katika Jimbo la Ndanda. Hata hivyo, mradi haukuanza shughuli za uchimbaji tangu kutolewa kwa leseni hizo kutokana na kuchelewa kwa makubaliano kati ya Kampuni hiyo ya Volt Graphite na wanunuzi (off-takers). (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari kwa sasa mwekezaji amesaini mkataba na Kampuni ya Property Matrix Limited kwa ajili ya kufanya tathmini ya ulipaji fidia kwa wananchi waliopo katika eneo la mradi. Aidha, Kampuni ya Volt Graphite ipo katika majadiliano ya mwisho na wanunuzi (off-takers) wa graphite ili kuruhusu kuanza kwa ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani madini hayo, ahsante sana.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Je, ni Wanawake wangapi wanaomiliki Migodi ya Madini nchini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa heshima na taadhima, kabla sijajibu hili swali, naomba sekunde 30 tu niweze kutoa pole kwa wananchi wangu wa Jimbo la Longido wanaoishi katika Tarafa ya Enduimet, Kata ya Olmolok ambao Shule yao ya Sekondari ya Enduimet iliungua moto jana na watoto wa kike 345 sasa hawana makazi na hawana chochote. Nawahakikishia kwamba, ninashirikiana na Serikali yetu sikivu kuanzia ngazi ya Wilaya na Mkoa, tutahakikisha huduma hizo muhimu za kupata mablanketi, vitanda na magodoro zinafanyiwa kazi ili waendelee kusoma kwa amani katika shule hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya pole hizo sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, shughuli za madini zimekuwa zikifanyika kupitia watu binafsi na kampuni ambazo ndani yake kuna wanawake na wanaume. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ilibainika kuwa, nchini kuna takribani wanawake milioni tatu wanaoshiriki katika mnyororo wa thamani wa madini.
Mheshimiwa Spika, tafiti ndogo iliyofanywa na TAWOMA kwa kushirikiana na Shirika letu la STAMICO kwa wanawake 992 katika Mikoa ya Shinyanga, Geita, Mara na Simiyu, ilibainika kuwa, wanawake 17 sawa na asilimia 1.7 wanamiliki migodi, wanawake 67 sawa na asilimia 6.8 wanamiliki maeneo ya uchimbaji. Yaani maduara katika leseni za uchimbaji madini na wanawake 855 sawa na asilimia 86.2 wanajishughulisha na kazi zinazohusiana na uchimbaji pamoja na uchenjuaji wa madini huku wanawake 53 sawa na asilimia 5.3 wanatoa huduma maeneo ya uchimbaji.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuwasimamia na kuwapatia leseni wanawake wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini ili kuongeza mchango wao kwenye sekta hii na kuimarisha uchumi wao. Wizara inaamini kuwa mwanamke akiwezeshwa, jamii nzima imewezeshwa. Ahsante sana.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza: -
Je, Vijiji vinavyozunguka Kiwanda cha Gesi ya Kiwanda kilichopo Kata ya Itagata Rungwe vinapata faida gani kutokana na kuwepo kwa kiwanda hicho?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Gesi kilichopo Kata ya Itagata Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya ni kiwanda cha kuzalisha Gesi Ukaa (Carbon Dioxide) na kinamilikiwa na Kampuni ya TOL Gases Limited.
Mheshimiwa Spika, faida za kiwanda hiki kwa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe kwa kipindi cha kuanzia Januari, 2020 hadi Oktoba, 2024 ni pamoja na malipo ya kiasi cha shilingi milioni 213 kama ushuru wa huduma (Service Levy) kwa halmashauri; kuchangia kiasi cha shilingi milioni 159 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Isebe; vyumba viwili vya madarasa, pamoja na Ofisi ya Shule ya Sekondari Itagata; ujenzi wa uzio katika Shule ya Msingi ya Katumba na ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa darasa katika Shule ya Sekondari ya Itagata; pamoja na Ofisi ya Kijiji, na kutoa ajira za kudumu 112 na ajira za muda mfupi takribani 150 kwa wananchi wanaotoka maeneo yaliyo jirani na kiwanda kama sehemu ya uwajibikaji wao kwa jamii, kwa mujibu wa Kanuni za Uwajibikaji wa kampuni za Uchimbaji madini kwa Jamii (corporate social responsibility - CSR).
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa leseni ya madini ya mradi huu ipo katika Halmashauri mbili za Wilaya za Rungwe na Busokelo, kwa mwaka 2024 kampuni ya TOL Gases Limited iliwekeana mkataba na Halmashauri ya Busokelo kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mabweni ya Shule ya Msingi Lupata kwa thamani ya shilingi milioni 39.7 ambapo mradi huo umekamilika.
Mheshimiwa Spika, vilevile kampuni ya TOL Gases inatarajia kukaa na Halmashauri zote mbili mwezi Desemba, 2024 ili kuandaa na kuweka mpango wa utekelezaji wa CSR kwa mwaka 2025.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza:-
Je, upi mpango wa kuondoa tatizo la ucheleweshaji wa Vibali kwa Wachimbaji Wadogo na kutozwa mapato kwenye mchanga Mgodi wa Kebaga?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mgodi wa Kebaga kuna umiliki wa leseni namba PML000851 na 000852 zinazomilikiwa na Bibi Virginia Mkandala na Bwana Samson Gesase. Mgodi huo ulikuwa na changamoto ya kukosa Meneja wa Mgodi hivyo kushindwa kudhibiti uchimbaji na uchenjuaji wa madini katika eneo hilo. Hivyo, Tume ya Madini iliweka utaratibu wa kusimamia mgao wa mawe ambapo vibali vya ugawaji vilikuwa vikitegemea utayari na wito kutoka kwa wamiliki wa leseni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa hapakuwa na utaratibu mzuri wa kusimamia hatua zote za uzalishaji, Tume ya Madini ililazimika kutoza tozo za Serikali kwenye hatua za ugawaji wa mawe. Mgodi huo kwa sasa umeboresha usimamizi kwa kuteua Meneja wa Mgodi ambaye anasimamia shughuli zote za uzalishaji. Hivyo, kuanzia tarehe 1 Aprili, 2024 yaani mwezi uliopita Tume ya Madini imesitisha zoezi la mgao wa mawe na shughuli za uzalishaji katika mgodi huo zinaendelea kufanyika kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura 123.
MHE. HUSSEIN N. AMAR K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: -
Je, ni sababu gani zinazozuia kuanza utekelezaji wa Mradi wa Urani Mkuju - Namtumbo wakati ulishapata leseni ya uchimbaji na ujenzi?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, leseni ya uchimbaji mkubwa wa madini (Special Mining Licence) ilitolewa kwa Kampuni ya Mantra Tanzania Limited mwaka 2013. Hata hivyo, mara baada ya leseni kutolewa, bei ya urani ilishuka kwenye soko la dunia hali iliyosababisha uendelezaji wa mradi huu kuchelewa. Kampuni ilisubiri kuimarika kwa bei ya urani ambapo kwa sasa bei yake imeimarika na kampuni iko tayari kuendeleza mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Mazingira, imeelekeza ifanyike Tathmini ya Kimkakati ya Mazingira (Strategic Environmental Assessment – SEA) ya Ikolojia ya Mikumi – Selous Game Reserve ambapo mradi wa Mto Mkuju unatarajia kufanyika kwa kuzingatia SEA ya ikolojia hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kutokana na Kampuni ya Mantra Tanzania Limited kuwa imekamilisha maandalizi ya kuanza uchimbaji, Serikali imeshampata mkandarasi wa kufanya tathmini hiyo ya mazingira na ameshaenda site tangu tarehe 3 Novemba, 2024 na anatarajiwa kuikamilisha kazi hiyo kwa muda wa miezi sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya SEA itakapokamilika, itawawezesha kuanza mradi huu muhimu kwa uchumi wa Taifa na kwa wananchi, ahsante sana. (Makofi)