Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita (51 total)

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Februari 2010 Wizara ya Madini wakati ule wakati akijibu swali hili ambalo liliulizwa na Mbunge wa wakati huo Prof. Sarungi majibu ya Serkali yalikuwa haya haya kuhusiana na utafiti wa eneo lile kwa madini ya Helium, miaka 10 baadae 2021/2022 GST kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na kupita na kufanya utafiri lakini bado hawakuwahi kufika eneo lile. Leo ni miaka 12 sasa toka tumepata majibu haya lakini madini haya yameanza kuzungumzwa toka mwaka 1952. Nilitaka nipate comitment ya Sarikali sasa, kwa sababu ni muda mrefu imekuwa ikizungumziwa juu ya kufanya utafiri kwenye ya eneo lile lakini haufanyiki kwa wakati.

Je, kipindi hiki cha mwaka huu wa bajeti kwa mujibu ya Serikali eneo hili litanyiwa utafiti ili kuondokana na haya ambayo yamekuwa yakifanyika huku nyuma na wananchi waweze kunufaika na madini ya eneo lile?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili kwenye tarafa hiyo hiyo tarafa ya Jirango Kijiji cha Upege eneo la form kuna madini pale ya dhahabu na leseni amepewa mtu wa Barec toka mwaka 1997 lakini mpaka sasa zaidi ya miaka 20 na kitu hayajaanza kuchimbwa madini yale. Nataka pia nipate commitment ya Serikali ni lini sasa madini yataanza kuchimbwa kwenye eneo lile Utegi alimaarufu kama farm ili kuongeza mapato lakini kuongeza na kutoa ajira kwa vijana ndani ya Wilaya yetu ya Rorya. Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kwanza kumpongeza ndugu yangu Mheshimiwa Wambura Chege kwa jinsi anavyowapambania wapiga kura wake na hususan hawa wachimbaji wa madini na jinsi anavyopigania maslahi ya rasilimali ya hii ya madini iweze kufanyiwa kazi ili nchi yetu iendelee kuneemeka kwa utajiri tulionao wa madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la kwanza kuhusu ni lini hii gesi asilia ya Helium itaanza kuchimbwa katika eneo la jimbo lake. Napenda kumjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba tafiti za kutafuta haya madini Helium katika nchi yetu zinaendelea katika sehemu mbali mbali kama nilivyotaja katika kujibu swali lake la msingi, na hata kwa kuongezea katika bonge la Mto Rukwa kuna utafiri mkubwa ambao pia unaendelea na ambao viashiria vimeonyesha kwamba Tanzania huenda ikawa nchi ya kwanza Dunia kwa kuwa na akiba kubwa ya madini hayo kuliko nchi zote duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa hali halisi ilivyo kwa sasa hivi tafiti zinaendelea na mara tafiti hizi zitakavyojiridhisha kwamba tumepata akiba ya kutoka katika maeneo mbali mbali juhudi za kuwapata wawekezaji wa kuchimbua madini haya ya gesi asilia ya Helium yataweza kuendelea. Kwa hiyo, nimuhakikishiue Mbunge kwamba utafiti ambao tumepangia bajeti hii inayokuja uendelee kufanywa kwa kina zaidi utatuletea majibu sahihi kwamba ni lini hayo madini yataanza kuchimbwa katika jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili anapenda kufahamu kwamba madini ya dhahabu ambayo nayo yamekuwa yakiendelea kufanyiwa utafiti katika Kijiji cha Utegi katika tarafa ya Gilongo katika Jimbo lake yataanza kuchimbwa lini maana tafiti zimeendelea kwa muda mfefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshsimiwa Mbunge kwamba katika eneo hilo maeneo yaliyogundulika kwamba kuna dhahabu ni maeneo ya shamba maalum la Serikali linaitwa farm kwa jina mashuhuri. Lakini utafiti ambao umekuwa ukiendela kwa miaka mingi sasa bado unaendelea, na mara wale watafiti watakapokuwa wamejiridhisha kwamba kuna madini pale taratibu zitafuatwa kulingana na vifungu vya 95 na 96 ya sheria yetu ya madini sura 123 ili waweze sasa kupata vibali vya kuchimba madini hayo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali kwanza, kwa vile wananchi wachimbaji wa Njombe, kupitia chama chao cha wachimbaji kinaitwa WANANJO, walishafikisha kilio kwa Mheshimiwa Waziri na Waziri akatoa maelekezo kwa Katibu Mkuu kwamba, watafutiwe na watengewe maeneo kama inavyofanyika maeneo mengine katika nchi yetu. Na kwa vile mchakato huo ulishafanyika na RMO alishafikisha hayo mapendekezo ya maeneo wizarani.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali, ni lini sasa wananchi hawa watapewa hayo maeneo ambayo tayari yameshatambuliwa kwamba, ni muhimu kwa uchimbaji wa wachimbaji wadogo wa Njombe?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa, ameongelea kuwasaidia kwa kupitia training mbalimbali pamoja na mikopo. Wananchi, wachimbaji wale, hawana Habari na hiyo training ni kalenda ambayo Wizara wamejipangia. Naomba tupate uhakika na wao wasikie, ni lini mafunzo haya yatafanyika katika Mkoa wa Njombe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Deodatus Mwanyika, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la kwanza ambapo anataka kujua kwamba, wachimbaji wadogo walioahidiwa maeneo ya kuchimba makaa ya mawe, na ninafahamu ni katika eneo la Ludewa, ni lini watapewa hayo maeneo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia kwamba, taasisi yetu husika ambayo ni Tume ya Madini walishakwenda kupima maeneo hayo na mpaka sasa wameshapata kilometa za mraba 10.33 ambazo zinatosha kutoa leseni za wachimbaji wadogo 120. Na wanaendelea kutafuta maeneo ya ziada ili kuwapatia wachimbaji wote wadogo maeneo ya kuchimba kulingana na maombi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili, napenda kumhakikishia Mbunge, Ndugu yangu Mwanyika ambaye nampongeza sana kwa jinsi anavyowapambania wachimbaji wake wadogo kule katika jimbo lake ya kwamba, ratiba ilishapangwa. Taasisi yetu husika imeanza kuzunguka katika Kanda ya Ziwa tunavyoongea wanatoa mafunzo mbalimbali. Na mwaka huu wa fedha kabla haujaisha watakuja pia na Mbeya na GST nao wale wanaofanya mambo ya jiolojia watakuja kutoa semina katika mwaka ujao wa fedha ya jinsi ya kuchukua sampuli na jinsi ya kutambua maeneo yenye madini kwa ajili ya kunufaisha wachimbaji wadogo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Abubakar Assenga, Mbunge wa Kilombero, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kutokana na utafiti uliofanywa na GST na kubaini kwamba, katika maeneo husika madini yapo. Je, Serikali iko tayari sasa kuendelea na utafiti katika maeneo mengine jirani ambapo madini hayakupatikana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kwenda Jimboni Kilombero katika maeneo ambayo madini hayo yanapatikana au kumekuwa na dalili za uwepo wa madini ili kwenda kujenga uelewa zaidi kwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Kassinge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwenda kufanya utafiti katika maeneo mengine, jibu ni ndio. Wizara inaendelea kupitia taasisi yake ya GST kufanya utafiti katika maeneo yote ya nchi yetu kubaini maeneo yenye madini ya aina mbalimbali, ili tuweze kuyafahamu na kuweza kuwagawia wachimbaji wadogo na wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali katika dunia kwa sababu, Rais wetu naye alitusaidia sana kupitia Royal Tour kuyatangaza na wawekezaji wanazidi kumiminika nchini kwa hiyo, zoezi la utafiti linaendelea nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili la mimi kwenda Kilombero na kuendelea kuangalia maeneo yaliyopatikana kwa ajili ya wachimbaji wadogo, ndio, niko niko tayari kutembelea katika maeneo hayo. Nipende tu kumjulisha kwamba, hata sasa katika maeneo ambayo madini yameshabainika tuna zaidi ya leseni 22 za wachimbaji wadogo ambao wanaendelea na tafiti na uchimbaji wa madini ya vito pamoja na madini ya dhahabu.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha eneo la Liganga na Mchuchuma, eneo la Njombe kwa ujumla mpaka maeneo ya Mufindi hayajafanyiwa utafiti kabisa. Pamoja na kueleza kwamba, nchi nzima inafanyiwa utafiti ni lini sasa Serikali itaifanya GST ianze utafiti kwenye maeneo ya Njombe ambayo hayajafanyiwa utafiti?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwanyika, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika Nyanda za Juu Kusini hasa Mikoa ya Ruvuma, Njombe na hususan kule Ludewa, kuna maeneo makubwa sana yenye madini ya chuma na madini ya makaa ya mawe. Wizara inaendelea kuchakata kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Uwekezaji utaratibu mzuri wa kuwapata wawekezaji wakubwa wa kuyachimba madini hayo, lakini pia, tuko katika hatua za mwisho kabisa za kubainisha maeneo ya kuwagawia wachimbaji wadogo ili madini hayo yaweze kuleta tija kwa Taifa letu na raia wake.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Huu ukanda wa Milima ya Udzungwa unaelekea kwa kiwango kikubwa kwenye Wilaya ya Kilolo na huu ukanda unaungana na Kata ya Udekwa na Kata ya Ukwega ambayo pia, inaaminika kuwa na madini. Je, Wizara iko tayari kutuma wataalam kufanya utafiti ili kama madini hayo ya dhahabu yapo, kama ilivyo kule Ulanga, yaweze pia kuchimbwa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nyamoga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama nilivyotangulia kusema, kama Wizara ya Madini, kupitia taasisi zake GST na hata STAMICO, tuko katika mpango mahususi wa kuendelea kufanya utafiti wa kubaini maeneo yote yenye madini nchini na itahusisha pia, eneo lake na sehemu alizozitaja kwa sababu, lengo letu kama Taifa ni kuhakikisha kwamba, rasilimali madini inakwenda kuzalishwa ili iletee Taifa letu tija. Nimhakikishie kwamba na nitumie pia nafasi hii kuiagiza taasisi yetu ya GST katika mpango kazi wao wa mwaka huu waweke katika utaratibu na ratiba safari ya kuelekea kule kufanya utafiti kwenye eneo la Mheshimiwa Mbunge.
MHE. ENG. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Wilaya ya Hanang, Kata ya Basutu, tuna mgodi wa dhahabu, lakini uzalishaji wake uko chini sana. Je, Serikali iko tayari kushirikiana na mwekezaji ili kuongeza uzalishaji wa dhahabu kwenye eneo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara, tunashirikiana na wawekezaji na wachimbaji wadogo. Vilevile sisi kama Wizara lengo letu kubwa ni kusimamia upande wa sera, kanuni na sheria, lakini pia kutoa elimu na kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata fursa za kufikia taasisi za kifedha ili waweze kukopeshwa vifaa ama fedha baada ya kukidhi vigezo ili uzalishaji uweze kuendelea na waweze kupata tija kwa juhudi ya uchimbaji wa madini.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Aidha, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa madini hayo katika Wilaya yetu ya Kakonko ni uthibitisho wa utajiri na hazina kubwa ya madini katika Wilaya yetu.

Je, ni lini sasa Serikali itaanza uchimbaji mkubwa ili wananchi na Serikali iweze kufaidi kwa kiwango kikubwa zaidi? (Makofi)

Swali la pili, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwawezesha wananchi na wachimbaji wadogo wadogo mtaji ili uchimbaji uweze kufanyika kwa tija? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Aloyce John Kamamba Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa lini uchimbaji mkubwa utafanyika katika maeneo yenye madini Wilayani kwake, napenda kumjulisha kwamba Taasisi yetu ya Utafiti wa Kijiolojia na Madini (GST) wanaendelea na utafiti katika maeneo mbalimbali nchini na pale wanapobaini kiwango cha madini yanayopatikana katika eneo husika wanaendelea kutangaza fursa za uwekezaji kwa wawekezaji wakubwa wenye mitaji mikubwa, ambao kimsingi wakija wanaingia katika ubia na wachimbaji wadogo walioko katika maeneo yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili Wizara ya Madini tumeshaingia makubaliano na taasisi za kifedha za ndani ikiwepo Benki ya KCB, NMB, NBC, CRDB ya kuwapa wachimbaji wadogo mitaji waliokidhi vigezo ili waweze kuchimba madini hayo kwa tija. (Makofi)
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kumuuliza Waziri Wilaya ya Mbogwe ina migodi midogo midogo inayomilikiwa na wachimbaji wadogo.

Je, Wizara imejipangaje kuwanufaisha wachimbaji hao wadogo ili kusudi na wao waone matunda kwenye Serikali yao?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika nchi yetu tuna wachimbaji wadogo katika sehemu mbalimbali, wenye leseni na moja ya kazi kubwa ya Wizara kupitia Taasisi zake za STAMICO na GST ni kuwajengea uwezo kwa kuwapa elimu juu ya Sheria ya Madini, Kanuni za Madini na namna ya uchimbaji bora pamoja na kuwatafutia fursa kwa wawekezaji wakubwa wanaokuja kutafuta madini katika maeneo ambayo yameshafanyiwa utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuishii hapo wachimbaji wadogo hawa pia tunaendelea kuwapelekea elimu ya kujiunga na kujisajili, waweze kufanya uchimbaji wenye tija kupitia taarifa za kijiolojia zinazoonesha madini yanayopatikana katika maeneo yao huko.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza nishukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri kwamba Mkoa wetu wa Iringa na sisi tuna madini ya kutosha. Mkoa wetu wa Iringa tunao Mgodi wa Nyakavangala uko katika Jimbo la Isimani. Na kwa kuwa taarifa ya jiorojia na utafiti, inaonesha kwamba eneo hilo limeshaonesha. Je, ni hatua gani sasa inayofuata ili wachimbaji wa eneo hilo waweze kuchimba kwa tija na ili Mkoa wetu wa Iringa uweze kupata mapato kutokana na madini?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nipongeze sana wanawake waliothubutu kuanza uchimbaji wa madini nchini, na sasa wameanzisha chama cha TAWOMA. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhamasisha wanawake wengi zaidi waweze kuchimba madini nchini na ukizingatia sensa inaonesha kwamba wanawake tuko wengi zaidi na Mheshimiwa Waziri alisema tunalipa vizuri?

Nimpongeze Mheshimiwa Rais alifungua uwekezaji mkubwa sana wa mwanamke pale Geita, Sarah Masasi, ili wanawake wengi tuweze kuchimba madini na kuwekeza katika madini nchini. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa swali lake la kwanza kwamba kwa kuwa utafiti wa awali umeshafanywa na taasisi zetu kubaini uwepo wa madini ya dhahabu katika eneo la Nyakavangala, napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba hatua zinazofuata sasa ni kufanya utafiti wa jiofizikia ambao ndio unaohitajika kwa sasa ili usaidie kutambua mikondo inayoweza kuwa na mashapo ya dhahabu, na kwa njia hiyo wale wachimbaji waweze kuchimba kwa tija. Aidha, GST kwa kushirikiana na STAMICO sasa wamepanga kwenda kuendelea na utafiti katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa swali lake la pili, ni kwamba Serikali ya Mama Samia kwa kuzingatia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi unaotutaka tuwape wachimbaji wadogo wakiwepo wanawake maeneo ya kuchimba madini imetuagiza sisi tuendelee kuwa walezi wa sekta ndogo ya wachimbaji wakiwepo wanawake.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika kutekeleza hilo sisi Wizara ya Madini, kwanza tumeteua mabalozi wa madini ambao Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati ni moja wa mabalozi na vinara wa madini hapa nchini, kazi ambayo anaifanya kwa dhati, na mpongeza kwa kuleta swali hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi mamia kwa maelfu ya wanawake wanafaidika kupitia mnyonyoro wa sekta hii ya madini. Zaidi ya leseni 20 zimeshatolewa kwa vikundi mbalimbali vya wachimbaji wa madini. Na wanawake hawa wamekuwa wakichangia pia katika kukusanya maduhuli ya Serikali. Kwa mfano kikundi kimojawapo cha TAWOMA mshikamano kilichopo katika eneo la Nyamisiga, Halmashauri ya Msalala kule Kahama wamechangia ujenzi wa zahanati. Hizo ni juhudi kuonesha kwamba Wizara imezingatia suala hili la uchimbaji wa wanawake wadogo, na ninampongeza sana Mheshimiwa kwa kuleta swali hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuwaomba wanawake popote walipo Tanzania kwenye madini wajiingize katika biashara hii maana ina tija na Serikali inawatambua na itawa-support.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii kuishukuru sana Wizara kwa majibu mazuri.

Mheshimiwa Spika, ndani ya Wilaya yangu kuna vikundi vya vijana ambao wamejiunga pamoja katika shughuli mbalimbali za utafutaji na uchimbaji wa madini. Kuna vikundi kama Chugu, Chiswala na wanaapolo group, changamoto walionayo ni ukosefu wa vitendeakazi sahihi vya uchimbaji. Je, Wizara ina mpango gani wa kuwasaidia vijana hawa vitendea kazi ili nao waweze kupata mapato halali ya kuwezesha kujikimu kimaisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yahya Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Taasisi yake au Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), limeingia makubaliano na Taasisi za Kifedha hapa nchini, ikiwepo benki ya NMB, CRDB, KCB na Benki hizi zimeanza kutoa mikopo ya kuwawezesha wachimbaji wadogo. Hadi sasa zimeshatoa jumla ya Shilingi Bilioni 36 ambazo zimepopeshwa na inaendelea na jitihada ya kuzungumza na taasisi hizi ili waweze pia kutoa msaada wa vifaa.

Mheshimiwa Spika, vilevile Wizara inaendelea kuhakikisha uchimbaji mdogo unaendelea kurasimishwa nchini na katika mwaka wa fedha 2021/2022 tumeweza kutoa leseni za uchimbaji mdogo 6,000. Niendelee kumuomba Mheshimiwa Mbunge, kwamba ahamasishe vikundi katika Jimbo lake, wajipange na waweze kufuatila uwezekano wa kupata mikopo hiyo kupitia mabenki ambayo tumeingia makubaliano nao kupitia STAMICO. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kati ya hawa 21 hawa Nane ndiyo wako kwenye source ya eneo lenyewe la uchimbaji, ndiyo maana hawajakubaliana na masharti ya wale Wawekezaji. Wizara ningewaomba wao wafanye kila linalowezekana ili kuwaweka vizuri, kwa sababu wale mashamba Nane waliobaki ni kwa sababu hawaoni kama wanapata haki zao zinazowastahili.

Swali la pili, ningeomba Mheshimiwa Waziri mara baada ya Bunge hili kuisha tuende nae mpaka kwenye eneo la tukio ili akajiridhishe yeye mwenyewe. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Robert Chacha Maboto, Mbunge wa Bunda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa swali lake la kwanza, kama nilivyokwishasema katika jibu langu la msingi, kwamba Mahakama imetoa fursa waendelee kujadiliana na endepo majadiliano hayo hayatazalisha ridhaa na wao waingie kwenye ubia kama wenzao, taratibu za kisheria, Sheria ya Madini Sura ya 123, Kifungu cha 97 kinachoeleza jinsi ambavyo suala la compensation, reallocation na resettlement, yaani fidia au kuhamishwa na kuwekewa sehemu mbadala au kujengewa makazi mengine utafuatwa kwa ushirikiano na Wizara ya Ardhi na Mthamini Mkuu wa Ardhi wa Serikali. Kwa hiyo, tumejipanga katika kuhakikisha kwamba maridhiano ama yafikiwe au sheria ifuatwe ili madini hayo yenye thamani katika maeneo hayo yaweze kuchimbwa na kunufaisha Taifa.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa swali lake la pili, ni mtu wa field sana niko tayari baada ya Bunge hili tutapanga ratiba pamoja nae, tuone siku muafaka ambayo naweza kufika ili tukashuhudie maeneo hayo na kumaliza mgogoro uliopo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Spika,
nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itawalipa fidia stahiki wananchi wa mitaa ya Mwasonga, Madege na Sharifu wanaoguswa na mradi wa uchimbaji wa madini ya mchanga kupitia Kampuni ya Nyati katika Wilaya ya Kigamboni.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna kampuni ya uchimbaji wa madini ya mchanga mzito unaitwa heavy sands katika Jimbo lake, na kampuni husika inaitwa Nyati na hivi sasa ninavyojibu swali lake majedwali yote ya malipo ya fidia yameshakamilishwa, wapo watakofidiwa wapatao 1,198 na Mdhamini Mkuu wa Serikali ameshamaliza kazi yake na hivyo mpango wa malipo yao unaweza ukafanyika ndani ya miezi miwili ijayo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naulizia kuhusiana na eneo la Bunda. Eneo lile limekua ni muhimu sana kwa maisha na uchumi wa wachimbaji wadogo wadogo katika Wilaya yetu ya Bunda.

Je, kwa nini Serikali isiende pale na kulikata lile eneo ili sehemu nyingine ibakie kwa wachimbaji wadogo wadogo.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la rafiki yangu Mheshimiwa Charles, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Madini, kazi yetu ni kusimamia Sera, Sheria na Kanuni. Wawekezaji wa machimbo ya madini wawe wa ndani au wa nje, kazi yetu ni kuwasimamia na inapotokea kwamba eneo lina maslahi mapana ya Kitaifa na wenye eneo wamegoma kabisa kutoa ushirikiano, tunachofanya ni kufuata sheria zilizowekwa za huo utaratibu unaobainishwa katika Kifungu cha 97 cha Sheria yetu ya Madini Sura ya 123, kwa kuangalia suala la fidia, suala la kuhamisha watu na kuwapangia makazi mengine kwa mujibu wa sheria ambayo inashirikisha Wizara ya Ardhi pia, Sheria ya Vijiji au Sheria nyingine inayohusika na masuala ya ardhi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wanawake ni kundi maalum ambalo linatakiwa kuwezeshwa na kutambuliwa kisheria katika sheria zetu mbalimbali, je, ni nini mkakati wa Wizara kuhakikisha wanawake wanaingia kisheria kwenye hii Sheria ya Madini.

Mheshimiwa Spika, pili, Songwe pia ni moja ya mikoa maarufu sana kwa uzalishaji wa madini; je, ni lini Serikali itakuja kuwapatia wanawake wa Mkoa wa Songwe mafunzo juu ya uchimbaji wa madini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la kwanza, Serikali inawatambua wanawake kipekee kabisa, siyo kama kundi maalum bali kama wadau muhimu katika sekta hii ya uchimbaji madini, na ndiyo maana tumeendelea kuwashirikisha wanawake katika mafunzo mbalimbali. Wizara imeendelea kuwafundisha faida za kushiriki katika uchimbaji wa madini, na imewahamasisha wajiunge kwenye vikundi ambavyo mpaka sasa hivi Tanzania tuna zaidi ya vikundi 20 vya wachimbaji wanawake na hata kule Songwe pia tumeendelea kuhamasisha na wapo wachimbaji wanawake wasiopungua 15.

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili, Wizara ina mkakati maalum wa kutoa mafunzo nchi nzima na baada ya Bunge hili taasisi zetu za GST, Tume ya Madini na STAMICO, wamepanga kwenda kutoa mafunzo katika Mkoa wa Songwe.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Serikali kuhusiana na utayari wao kwenye suala la madini muhimu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tumeona thamani ya fedha kwenye ongezeko la asilimia 9.4 kwenye bajeti ya GST mwaka wa fedha huu unaoendelea ambapo mapato yame-shoot mpaka asilimia 141.
Ni kwa nini sasa Serikali isilete mkakati wa dharura kwa ajili ya ku-fund GST ili iweze kufanya tafiti za kisayansi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili; sasa hivi tunapozungumza GST imefikia wapi na Serikali imefikia wapi kwenye masuala ya critical minerals kwenye utafiti na uchimbaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Nusrat Hanje, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la kwanza; ili kuboresha teknolojia ya kutafuta madini na hasa tafiti ya madini haya ya kisasa, GST kupitia Wizara yetu ya Madini imeanza mkakati rasmi wa kuanzisha mashirikiano na wadau mbalimbali wa ndani na nje na kuandika maandiko mahsusi ambayo yatatusaidia kupata fedha za kuwekeza katika utafiti wa madini ya kimkakati. Tuna Kampuni ya Noble Helium ambayo inashirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na GST, tuna Kampuni ya Rocket Tanzania Limited.

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili kuhusu hatua ambazo tumeshafikia katika kutafiti na kuzalisha madini ya kimkakati; ni kwamba sisi kupitia Tume yetu ya Madini kama Wizara, tayari tunatoa leseni za utafiti wa madini ya kimkakati kwa ajili ya utafutaji wa madini na uchimbaji wa madini. Na Serikali imekuwa na ubia na baadhi ya kampuni hizo na kwa ruhusa yako naomba nitaje chache.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mkoa wa Lindi, tuna kampuni inayoitwa Lindi Jumbo Limited wenye leseni ya uchimbaji wa kati na wanaendelea na utafiti na sasa hivi wamefikia hatua ya kuendeleza ujenzi wa eneo la mradi.

Mheshimiwa Spika, hapo hapo Mkoani Lindi tuna Kampuni inaitwa Ngwena Tanzania Limited, wana leseni za utafiti wa madini ya kinywe na sasa hivi wako katika hatua ya uthamini kwa ajili ya ulipaji wa fidia. Na pia wale wa Jumbo nao wanafanya utafiti wa madini ya kinywe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa hizi chache nipende tu kumhakikishia kwamba sasa hivi Tanzania imeamka na wawekezaji wakubwa wa ndani na nje wanajihusisha na utafutaji wa madini ya kimkakati. Ahsante sana.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza lenye sehemu (a) na (b) kama ifutavyo: -

(a) Je, Mhesnimiwa Naibu Waziri, anaweza kunieleza ni vikundi vingapi na kwa kiasi gani vya wanawake wa Mkoa wa Ruvuma wamekopeshwa fedha hizo?

(b) Serikali ina mpango gani wa kutumia survey data ili kuwa ni dhamana ya kuweza kuwakopesha hao wachimbaji wadogo wadogo kwa sababu wachimbaji wengi hawana dhamana ya kuweka kwenye mikopo yao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili madogo au swali moja lenye kipengele (a) na (b) la Mheshimiwa Jacqueline Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Ruvuma kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa idadi ya waliokopeshwa kutoka Mkoa wake, hatujaweka mchanganuo wa kimkoa lakini kwa ujumla wakiweko wachimbaji wadogo wanawake na wanaume hadi sasa zaidi ya vikundi na wachimbaji wadogo 110 wameshafikiwa na mikopo kutoka mabenki ya ndani ambayo yamekubali kukopesha wachimbaji waliokidhi vigezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa swali lake la pili kuhusu data za jiolojia kutumika kama dhamana ya kupata mikopo ya benki, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi ni kwamba, tutakapokuwa tumepata hivi vifaa vya kuwasaidia wachimbaji wadogo kwenye utafiti, data zile sasa zitatumika kama mojawapo ya vigezo ikiwepo pia wao kuweka kumbukumbu za uchimbaji wao, ndiyo maana hata waliofanikiwa kufanya hivyo hadi sasa, watu 110 walio kwenye mnyororo wa thamani wa madini wameshakopeshwa zaidi ya Bilioni 80 na Benki ya NMB na Benki ya CRDB pia imeshawakopesha kiasi cha Bilioni 65. Kwa hiyo, Bilioni 145 zimeshawasaidia wachimbaji waliojipanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa wito kwa wanavikundi walioko katika Mkoa wake nao wajipange, waweke taarifa zao sahihi na mitambo hii ikija tutafanya utafiti na wataweza kutumia kama moja ya vigezo. Ahsante.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Serikali pamoja na kuwa imeweka utaratibu wa kutoa mikopo kupitia taasisi za kifedha, lakini mikopo hii imekuwa na masharti magumu amabyo wachimbaji wetu wadogo wengi wameshindwa kuweza kuyafikia.

Je, Serikali haioni haja sasa ya kupunguza masharti na ikiwezekana iweze kutoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo ili tuweze kuwasaidia katika uchumi wa madini.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kasaka, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, masharti ya kibenki yanaonekana kuwa ni magumu kwa sababu wachimbaji wadogo hawajapata uelewa mzuri wa namna ya kujipanga kupata mikopo hii. Kazi yetu kama Wizara imekuwa ni kutoa elimu ya vigezo muhimu ambavyo wanatakiwa wazingatie ili waweze kukopeshwa au waweze kukopesheka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo Wizara tutaendelea kujadiliana na mabenki na kuona namna ya kutengeneza masharti rafiki na rahisi kueleweka ili wachimbaji hawa waweze kupata mikopo bila usumbufu. (Makofi)

Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, swali la nyongeza.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na wanawake hawa kupata mikopo kuna shida kubwa sana kwenye biashara ya madini wanawake kupata masoko. Serikali ina mpango gani wa kujipanga kuhakikisha wanawake hawa pamoja na kwamba wanapewa mikopo lakini pia watafutiwe masoko ili bishara zao ziende vizuri?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwakagenda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti suala la masoko sio issue tena nchini kwetu baada ya Wizara kuanzisha masoko ya madini na vituo vya kununua madini nchini. Kwa sasa tuna zaidi ya masoko 47 na vituo 84 na bei elekezi hutolewa na Wizara kila wakati na kwa madini ya dhahabu bei ya dunia hutumika katika kuwapa bei stahiki.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, na ninaomba niishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri ambayo yamesheheni taarifa za kutosha. Naomba niulize maswali madogo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba pamoja na hayo madini ambayo yametajwa kwa idadi kubwa shughuli ya uchumi kwa maana ya uchimbaji haijaanza kufanyika, na hii inawezekana ni kwa sababu hamasa na elimu haijatolewa kwa ajili ya wananchi kuweza kuchimba.

Je, Serikali iko tayari kutoa hamasa na elimu ili wananchi waanze kuchimba madini hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; katika taarifa ambayo imetajwa na Serikali imetajwa kwa ujumla kwa mfano Kata ya Katazi.

Je, Serikali iko tayari kufanya utafiti wa kina kujua exactly deposit hiyo inapatikana wapi? ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa swali lake la kwanza; ni kweli uchimbaji bado haujapata kasi katika wilaya yake, lakini nimhakikishie kwamba, kama ni kutokana na uelewa mdogo Tume ya Madini wamejipanga kuzunguka nchi nzima kuhamasisha wachimbaji wadogo katika maeneo yenye madini ili waweze kujipanga waunde vikundi na tuweze kuwasaidia kwa ukaribu wafaidike na madini waliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa swali lake la pili ni kweli taarifa hizi tulizozitoa hapa ni taarifa za utafiti wa awali unaofanywa na taasisi yetu ya GST, lakini utafiti wa kina ufanywe kwa kutumia vifaa vya kisasa vya uchongaji. Na kutambua umuhimu wa kuwasaidia wachimbaji wadogo Wizara ya Madini imeagiza kupitia Taasisi yake ya STAMICO mitambo mitano ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wafahamu kiwango cha madini kinachopatikana katika maeneo yao ili wanapokwenda kuanza kuzalisha wachimbe madini wakiwa na uhakika kwamba watapata tija kutokana na juhudi zao. Ahsante sana.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, kwanza majibu ya Serikali yamenishangaza kidogo, kwa sababu hapa wanazungumzia TanzaniteOne lakini ukiangalia TanzaniteOne tayari walishauza hisa kwa Sky Associate Group Limited.

Swali langu, kwa sababu hawa Sky Associate inaonekana kwamba walikuwa hawajasajiliwa na BRELA hapa Tanzania, je, mmiliki wa iliyokuwa TanzaniteOne ni TanzaniteOne wenyewe au hao Sky Associate Group Limited? Hilo ni swali langu la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, wafanyakazi wa iliyokuwa TanzaniteOne hawajawahi kufukuzwa au kuondolewa kazini; je, hadi sasa wanazungumzia mahakamani miezi 11 lakini wanadai zaidi ya miezi 60 mpaka sasa.

Je, na hii miezi mingine iliyobaki watalipwa lini na kwa utaratibu gani na nini msimamo wa Serikali kwenye jambo hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mrisho Gambo, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa wamiliki wa mgodi kwamba kulikuwa na ubia ya mwingine zaidi ya TanzaniteOne pamoja na mwenzake aliyemtaja ni kwamba mgodi huu uliingiwa ubia kati ya TanzaniteOne na kampuni yetu ya Madini ya STAMICO. Kwa mujibu wa mikataba iliyokuwepo hakukua na mwingine na ndiye ambaye aliingia huu ubia na ndiye ambaye alikuwa mwendashaji wa mgodi na mwenye dhamana ya kuajiri na kufukuza wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, kwa swali la pili, malipo au madai wanaodai hawa wanaodai haki zao ambayo ipo kwenye kumbukumbu na ndio ambayo malalamiko haya yamefikia Wizarani ni hiyo shilingi bilioni 2.5 na sio bilioni 60 anayotamka na kama kuna madai ya nyongeza. Kwa kuwa suala hili tayari lipo bado kwenye mifumo ya kisheria, vyombo vyetu vya kisheria vitaendelea kulifuatilia na kufanyia kazi kwa mujibu wa taratibu na kanuni za Wizara husika.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa kuwa wafanyakazi hawa waliokuwa TanzaniteOne wamekuwa wanasumbuka muda mrefu sana.

Je, Serikali sasa haioni ni wakati muafaka wa kukaa na mwekezaji mpya waangalie wafanyakazi wenye sifa, waweze kupewa ajira katika hii kampuni mpya ambayo imekuja badala ya TanzaniteOne? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Catherine Magige, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wafanyakazi hawa 540 wanashauri lililoko mahakamani na shauri lao ni la muda mrefu na wanamalalamiko ambayo hayajafanyiwa kazi, siamini kama mwendeshaji mpya wa mgodi huu wa TanzaniteOne atakuwa tayari kuwachukua watu ambao tayari wana mgogoro na eneo lile ambalo wanalifanyia kazi. Kwa hiyo, mimi ningeshauri tu kwamba shauri lao lifuatiliwe hadi mwisho, ila kama kuna wenye sifa na mwenye mgodi mpya anaona kwamba anaweza kaujiri bila kujali mtafaruko au kesi waliyonayo, sisi kama Wizara hatutoingilia hilo.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nilikuwa nataka kufahamu ni lini Serikali itaweza kusimamia malipo ya wahanga wa kesi ya mwaka 1994 katika kata ya Bulyanhlu?Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Iddi, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Madini, siku zote iko tayari kusikiliza kero za wadau wake wa sekta ya madini na kama malalamiko haya yakifikia Wizarani, sisi tutalifanyia kazi bila kusita.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake lakini naomba atoe kauli hapa kwamba Je, baada ya utafiti kukamilika inawahakikishiaje wananchi wa Urambo kwamba wachimbaji wadogo wadogo nao watapa vitalu ili wanufaike na madini yao. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Margaret Sitta kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tumepewa dhamana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kwamba tafiti za madini zinapokuwa zimekamilika na maeneo yenye madini yamepatikana tunahakikisha kwamba yametengwa maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Spika, ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Mama Sitta kwa sababu amekuwa ni mpambaji mkubwa kuhakikisha kwamba wananchi wa Jimbo la Urambo hawaachwi nyuma katika kuwekeza kwenye biashara ya madini.

Mheshimiwa Spika, kwa ajili hiyo basi nitumie fursa hii kutoa wito kwa Mikoa yetu yote ya kimadini na wilaya zake, tafiti za madini zinapokamilika na maeneo yenye madini yanapokuwa yamepatikana kuhakikisha kwamba wanayatenga maeneo mahsusi kwa ajili ya wachimbaji wadogo na wawape kipaumbele wale ambao madini haya yamepatikana kwenye maeneo yao.(Makofi)
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Je, ni lini Mheshimiwa Waziri atakuja katika Mkoa wetu wa Iringa katika machimbo ya Nyakavangara, Kata ya Malengamakali, Jimbo la Ismani ili aje aone changamoto kubwa za wachimbaji wadogo wadogo pamoja na uwezeshaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kumjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Madini kupitia taasisi zetu za Tume ya Madini, GST na STAMICO tumeweka mkakati kabambe wa kuzungukia nchi nzima kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo, kutatua kero zao na kuhakikisha kwamba wanafuata sheria, kanuni na taratibu katika kujipatia maeneo ya kuchimba madini. Hatukuishia hapo tumehakikisha kwamba katika maeneo yote yenye machimbo tunaanzisha masoko ya madini na vituo vya kununulia na kuuzia madini.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Waziri kwa majibu mazuri pamoja na kwamba hayajaleta sana matumaini kwa wananchi. Pamoja na majibu haya nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza nataka nijue tu kwamba pale utafiti utakapokamilika nini nafasi ya wachimbaji wadogo kupewa nafasi kuchimba madini kwenye eneo lile?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nataka nijue maeneo yanayozunguka eneo la Utegi kama Kowak, Mika na maeneo mengine nini nafasi ya kuanza utafiti kwenye maeneo yale ili eneo litakapokamilika utafiti wa awali kwenye eneo la kwanza iendane sambamba na eneo la pili na haya maeneo mengine?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Jimbo la Rorya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala zima la upatikanaji wa maeneo ya machimbo ya madini kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi hutegemea kukamilika kwa utafiti. Utafiti unapokuwa umekamilika na kwa jinsi ambavyo utafiti huo huchukua gharama kubwa na kampuni zinazofanya utafiti huu ni kampuni kubwa zenye uwezo wa uchimbaji mkubwa, sisi kama Wizara tuna mamlaka ya kumegua eneo ambalo wachimbaji wadogo wanaweza wakakatiwa, waweze nao kupata maeneo yao ya kuchimba kama ambavyo sera yetu inasema kwamba lazima tuwape wachimbaji wadogo maeneo ya kuchimba.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, swali lake hilo la kwanza la wachimbaji wadogo kupatiwa maeneo ya kuchimba linachukuliwa kwa uzito mkubwa na tutawahakikishia kwamba watapewa maeneo.

Mheshimiwa Spika, maeneo ambayo anayazungumzia kwamba ni lini utafiti huo utakamilika na kuweza kuanza uchimbaji, ni wazi kwamba utafiti ndio utakaotupa jibu kwamba ni lini uchimbaji utaanza katika maeneo hayo.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kutokana na ripoti ya GST, Wilaya ya Liwale imeonekana kuwa na madini mengi sana ya dhahabu, kito na sapphire. Tayari wawekezaji wako kule na wachimbaji wadogo wameshaanza kazi, lakini Wilaya ya Liwale haina Ofisi ya Madini pale, matokeo yake wale wachimbaji wadogo na wawekezaji wengine wanakwenda Tunduru kuuzia madini. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka ofisi pale Liwale ili kuwarahisishia wachimbaji wadogo kupeleka madini yao Tunduru badala ya kuuzia Liwale?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, sisi Wizara ya Madini tumeendelea kujenga masoko ya madini na kuanzisha vituo vya kuuza na kununua madini katika maeneo yote yenye madini nchini. Kwa hiyo nimhakikishie kwamba ni suala la muda tu katika mzunguko wetu kadiri mapato yanavyoruhusu, tutafika huko Liwale na tutajenga soko na tutahakikisha kwamba wachimbaji wake walioko huko wana masoko ya kuuzia madini yao kwa bei iliyo sahihi na bila kupunjwa na mtu yeyote.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nataka kumuuliza Naibu Waziri kumekuwa na RL nyingi kwa maana ya leseni zilizoshikiliwa na Serikali katika Halmashauri ya Msalala Kata ya Ntobo. Sasa ni lini Serikali itaachia maeneo haya ili wachimbaji wadogo wadogo wa Jimbo la Msalala waweze kutumia haki yao ya msingi kuchimba katika maeneo yale?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kumjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo yote yaliyoshikiliwa na Serikali au maeneo yote ambayo yameshikiliwa na kampuni kubwa za utafiti wa madini ambayo anaomba au anadai ni lini watarudishiwa wananchi. Watarudishiwa wananchi pale ambapo utafiti utakamilika au sisi tumebaini kama Wizara kwamba watumiaji wake hawana mpango wa kuyatumia na hivyo tutaweza kukaa nao na kuyarejesha Serikalini tuweze kuwekea utaratibu wa kupewa wadau au wawekezaji ambao wako tayari kuwekeza.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ili niulize swali moja dogo la nyongeza. Jiwe la rubi lenye uzito wa kilo 2.8 lipo kwenye maonyesho kwa sasa Dubai na jiwe hili linasadikika linatoka Tanzania na kwamba siku chache zijazo kutakuwa na mnada wa kuuza jiwe hili. Je, kama nchi tunanufaika vipi na mnada huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kitandula, Mbunge wa Mkuranga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli mnamo tarehe 13 Aprili, 2022 Wizara ya Madini ilipata taarifa kupitia mitandao ya kijamii kwamba kuna jiwe la madini ya rubi lenye uzito wa kilo 2.8 na ambalo linadaiwa kuwa na thamani ya dola za Marekani milioni 120, sawa na zaidi ya bilioni 240 za Kitanzania ambalo limepewa jina la Bad All Hamal na ambalo linakwenda kuwekwa mnadani ndani ya siku 30 baada ya mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan na jiwe hilo kudaiwa kwamba limetoka Tanzania.

Mheshimiwa Spika, mara baada ya kupata habari hizi Wizara ya Maliasili imechukua hatua za haraka kutafuta kama habari hizi ni za kweli na kama kweli jiwe hili kweli limetoka Tanzania na kwa sababu jiwe hili limeshavuka mipaka liko kwenye nchi nyingine, taarifa hizi sasa tunazozikusanya ili tuweze kutoa taarifa sahihi katika Bunge lako Tukufu zinahusisha Nchi ya Dubai na tayari Ubalozi wetu uliopo Dubai na sisi tunafanya mawasiliano kufuatilia ukweli na uhalisia wa thamani ya jiwe hili. Pia baada ya ufuatiliaji wa awali tumebaini kwamba mmiliki halali au tuseme sasa wa jiwe hilo yuko nchini Marekani katika Jimbo la California na mawasiliano naye pia tumeshafanya tangu jana. Hivyo sasa suala hili linazidi kupanua wigo wake kidiplomasia kwamba linahusisha nchi tatu; Nchi ya Tanzania, Dubai na Marekani.

Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie tu kwamba tutakapokuwa tumepata nyaraka za usafirishaji wa jiwe hili kama kweli limetoka Tanzania tukapata nyaraka zinazoonyesha thamani na asili ya hili jiwe kwamba limetoka wapi. Tutakapokuwa tumepata na nyaraka za mauzo kati ya mmiliki wa sasa na wa hapo awali, sisi tutaleta taarifa katika Bunge lako Tukufu za uwepo wa jiwe hili na kama ni la kwetu, niwahakikishie Watanzania kwamba haki yao haitapotea sheria, kanuni na taratibu zetu zitatumika kuhakikisha kwamba rasilimali hii inakwenda kunufaisha Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, sisi Wizara ya Madini tunaendelea kuwahakikishia Watanzania kwamba tumesimama imara kudhibiti na kusimamia rasilimali madini kwa manufaa ya nchi yetu. (Makofi)
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona. Nina swali linalofanana na hilo. Kule Lupaso kwenye Kijiji cha Matemwe, kunafanyika uchimbaji: Je, Serikali inafahamu kwamba kuna uchimbaji unaendelea pale?

Je, uchimbaji ule unanufaisha vipi Halmashauri na Serikali kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba nikiri kwamba sina hakika na tuko tayari baada ya Bunge hili nikutane na Mheshimiwa Mbunge na watendaji wetu tuweze kujua na kufuatilia kuhusu machimbo hayo. (Makofi)
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Naibu Waziri, kuhusiana na wanawake wanaoshiriki katika madini Mkoa wa Arusha lakini naomba kuuliza maswali mawili.

Swali la kwanza; wanawake wanapojishughulisha na shughuli za madini Mkoani Arusha wanakutana na changamoto nyingi sana; je, ni nini Mkakati wa Serikali wa kutatua changamoto zinazowakabili wanawake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Wilaya ya Ngorongoro yamegundulika madini mengi, lakini inaonekana kwamba wanawake hakuna mazingira yanayowawezesha kushiriki katika shughuli za madini. Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba maeneo ya madini kwenye Wilaya ya Ngorongoro yanapimwa ili wanawake nao waweze kushiriki ipasavyo katika shughuli hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Ole–Shangai, Mbunge wa Ngorongoro, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa changamoto za wanawake Serikali imeendelea kutoa elimu, kuwahamasisha wajiunge na vikundi mbalimbali ambavyo nimevitaja kwenye swali la msingi ili waweze kusaidiwa kupata elimu juu ya sheria, kanuni na taratibu za madini pamoja na kufahamu fursa za biashara na uwekezaji kwenye sekta ikiwa ni pamoja na kuelekeza namna ya kupata mitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili kuhusu Wilaya yake ya Ngorongoro, ni kweli kwanza nimpongeze Mbunge maana yake mwisho wa mwezi uliyopita aliniomba nifanye Wizara kwenye Jimbolake ili kwenda kubaini changamoto zinazowakabili wachimbaji wa madini. Tukagundua kwamba Ngorongoro ina madini mengi sana ya vito, lakini uendelezaji wa sekta uko chini sana hasa kwa upande wa wanawake. Nitumie fursa hii kumhakikishia kwamba baada ya ziara ile tuliagiza Taasisi yetu ya Jiolojia na Utafiti wa Madini pamoja na Tume ya Madini waende kule wakahamasishe ile jamii na wabainishe maeneo yenye madini ili wanawake nao wa Ngorongoro wajiunge waweze kufaidi fursa hii iliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukuishia hapo, Wizara hii imeteua Mabalozi wa Madini, wanawake wanaongozwa na Dkt. Ritta Kabati ambao kazi yao ni kuwahamasisha wanawake wote wanaopenda kujiingiza katika biashara ya madini, wafahamu biashara ya madini na fursa zilizoko za wawekezaji, ahsante sana. (Makofi)
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka kufahamu ni lini Serikali itaipatia Kampuni ya Peak Resources leseni? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba utaratibu wa kupata leseni za madini uko katika mfumo wa kieletroniki na mfumo huo unafikika kwa njia ya kimtandao. Baada ya mtu kuingia kwenye mtandao na akaomba leseni utaratibu mzima wa jinsi ya kujaza fomu, ada zinazohitajika unalipiwa kimtandao na kwa kawaida kama mifumo iko sawa na hakuna break down kwenye system ndani ya wiki, mbili leseni huwa zinatoka, lakini kama kuna changamoto kwenye leseni yoyote, Ofisi yetu ya Madini iko wazi saa zote na tuko tayari kutoa ushirikiano ili leseni anayoisemea iweze kupata.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru na nasikitishwa kwa majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mgodi wa North Mara walifanya tathmini pamoja na kubomoa nyumba na mazao ya wananchi mwaka 2013, ambapo walifanya tathmini kwa phase sita, baadae baada ya miaka kadhaa wakaja wakasema wanahitaji phase nne tu ambazo wamelipa zikabaki phase mbili zenye wananchi 1,586 na wakasema kama walivyosema kwamba wangelipa kifuta jasho ambapo mpaka sasa hivi wananchi hawa hawajaweza kulipwa kifuta jasho takribani miaka kumi, ningependa kujua ni lini Serikali itahakikisha inasimamia sheria zile za madini na za ardhi kuhakikisha kwamba wananchi hawa wanalipwa fidia yao stahiki ya kubomolewa nyumba, mazao na muda uliopotea kutofanya shughuli za maendeleo kwa muda wa miaka kumi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, mwaka 2018 baada ya wananchi hao kuona kwamba inachukua muda hawalipwi hicho kifuta jasho kinachosemwa waliifungua kesi Mahakama Kuu, ambapo Waziri wa Madini Mheshimiwa Biteko alienda kule Nyamongo akawasihi wananchi waondoe hii kesi mahakamani mwaka 2018 lakini mpaka sasa hivi wananchi hao bado hawajaweza kulipwa. Mwaka huu mapema walifuatilia kwa Mthamini Mkuu wa Serikali na akakiri kwamba hajapokea document yoyote ile au taarifa yoyote ile ya kutoka mgodini kuhakikisha kwamba wananchi wanaweza kulipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kujua ni kwa nini pale ambapo mgodi au ardhi ya wananchi inatwaliwa Serikali inashindwa kufuata sheria zilizopo kuhakikisha kwamba wananchi wanalipwa stahiki zao mara moja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya Mheshimiwa Esther Matiko, kama ifuatanyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali lake la kwanza kwamba ni lini hawa wananchi wanaokaa katika Phase Mbili zilizobaki ambazo hazijafidiwa watalipwa. Napende tu kumhakikishia kwamba baada ya kampeni kumwajiri Mkandarasi aliyefanya tathmini kufahamu watu wanostahili kulipwa na kufahamu kiwango ambacho kinastahili kutolewa kama kifutajasho kwa sasa hivi ndani ya miezi miwili ijayo utaratibu wa malipo hayo utaenda kufanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali lake la pili, kwamba ni kwa nini Serikali isisimamie sheria yake na kuhakikisha kwamba wananchi ambao waliondoa kesi Mahakamani mwaka 2018 wanalipwa, napenda tu kumhakikishia kwamba Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan ni Serikali inayopenda kutenda haki, nasi kama Wizara kwa niaba yake tunasimama kidete kuhakikisha kwamba wananchi hawa baada ya hizi tathmini kuwa zimeshafanyika na sasa tumeshafikia mwisho wake na wanakwenda kupata malipo yao, ahsante sana. (Makofi)

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI:
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuweza kuongezea katika majibu mazuri ambayo ameyatoa Naibu Waziri wa Madini. Nilitaka kuzungumzia suala la fidia kwa nini fidia zinachelewa kulipwa na kwa nini pengine hali inatokea namna hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la fidia ucheleweshaji wa fidia wakati mwingine unatokana na udanganyifu unaokuwepo kwenye maeneo husika. Kwa mfano, katika masuala mazima ya kuwa na tuna lugha rahisi inaitwa tegesha, unakuta mazao yanaota kwa haraka kwa siku mbili mazao yapo ambayo yanakuwa ni pandikizi kwa hiyo katika suala zima la kufanya uthamini kadri unavyokwenda unakuta kuna mabadiliko kwenye lile eneo, lakini wanasahau kwamba Serikali huwa inachukua picha za anga kabla ya kufanya zoezi na inaangalia picha za nyuma na kuweza kujua kabla ya uthamini kuanza kulikuwa na nini pale na unapoanza uthamini unakuta kuna mali nyingi zinaongezeka, upandaji wa mazao ambayo mengine yanapandwa usiku na mchana. Kwa hiyo, wakati mwingine niwaombe tu wananchi ya kwamba Serikali ina nia na dhamira njema ya kuweza kulipa fidia, kwa hiyo tuache ule udanganyifu ambao unachelewesha haki za Watanzania katika kulipwa fidia zao.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na uhalisia huohuo kwamba Serikali ilikwishafanya uthamini na ikaelewa kwamba ni watu wangapi wanahaki ya kulipwa maeneo yao katika maeneo yambayo wamechukua Wawekezaji.

Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo hili kutokana na kwamba wao Wawekezaji wameshapata faida ya kutosha na sasa mashimo ndiyo yatakayobaki na wananchi wamesubiri kwa muda mrefu na ni tatizo la muda mrefu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Agnes Marwa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kwamba tathmini zote zimeshafanyika na kiwango cha malipo kinachostahili kulipwa kimeshajulikana, mchakato unaoendelea kwa sasa ni huo wa kuhakikisha kwamba wanaostahili kulipwa, kiwango wananchostahili kulipwa na maelewano ya wao kukubali malipo hayo ndiyo yanayoendelea na Wizara tutaendelea kusimamia hilo liweze kutekelezwa.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza kabisa nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini pamoja na hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali tayari ina taarifa za miamba yenye madini katika Mkoa wa Rukwa na Songwe. Je, ni lini sasa itatoa taarifa na kusambaza kwa wananchi ili wananchi hawa waweze kuomba leseni kwa ajili ya uchimbaji? (Makofi)

Swali la pili, ni nini sasa mpango wa Serikali kwa kuwapa mitaji wachimbaji wadogo wakiwemo wanawake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, taarifa za kijiolojia za maeneo yenye madini nchini hutolewa na GST kupitia chapisho la kitabu cha madini yapatikanayo Tanzania ambacho toleo la mwisho lilitolewa mwaka 2019. Kutokana na tafiti zilizoendelea kuna aina nyingi za madini zimeendelea kugundulika na hivyo toleo la tano limekamilika, tuko kwenye hatua za kuandaa uzinduzi wa kitabu kipya cha madini hayo na siku ya uzinduzi wa hicho kitabu tutawaalika Wabunge wote na wadau mbalimbali wa madini waweze kupata nakala ya vitabu hivyo ili taarifa hizi ziweze kuwafikia walengwa katika maeneo ya Wilaya zote za nchi yetu.

Swali lake la pili kuhusu mpango wa kuwapatia wachimbaji wadogo mitaji ulikwishawekwa kupitia maelewano na mabenki ya ndani, kwamba watoe mikopo kwa wachimbaji wadogo waliokidhi vigezo na tayari mabenki ya ndani yameshatoa zaidi ya shilingi bilioni 145 kwa wachimbaji wadogo wenye leseni, ahsante sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kuwa Wilaya ya Nyang’hwale wachimbaji wadogo wadogo wameendelea kuvumbua maeneo mbalimbali kama vile Isonda, Igalula, Isekeli, Shibalanga, Ifugandi, Rubando, Lihulu, Bululu pamoja na Mahagi.

Je, Wizara ina mpango gani wa kupeleka mitambo ya kufanya utafiti ili uchimbaji ule uwe wa kuendelea?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kupeleka mitambo ya kuwasaidia wachimbaji wadogo, Wizara kupitia taasisi yake ya STAMICO imeagiza mitambo mitano ambayo tayari ilishaagizwa na mingine mitano pia imeshaagizwa kwa ajili ya kuwa na zana mahsusi kwa ajili ya kusaidia uchimbaji wa wachimbaji wadogo waweze kufanyiwa upimaji wa maeneo yao wajue aina ya madini na kiasi kinachopatikana.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Kwanza nimpongese Meneja wa TANESCO wa Wilaya ya Igunga kwa hatua kadhaa ambazo ameendelea kutupa ushirikiano katika kutatua tatizo hili kwa niaba ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; pamoja na changamoto hii ya malipo ilijitokeza, lakini pia kumekuwa na changamoto ya kukatika umeme mara kwa mara pake katika Mji wa Igunga hususan mjini kati pale, maeneo ya Mwamashimba, Igulubi, Nanga, Bukoko, Ikumba na Ikunungu. Je, nini kauli ya Serikali au Serikali ina mpango gani wa kutatua hii changamoto ya dharura ambayo inaathiri shughuli za kiuchumi za wananchi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ukiangalia katika utekelezaji wa mipango hii ya Serikali pale katika jimbo letu. Kulikuwa na mpango pia wa Serikali kuongeza nguvu kwa kujenga kituo cha kuzalisha umeme. Je, Serikali ina mpango gani katika hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI K.n.y. WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mbunge Ngassa kwa sababu ni mfuatiliaji mzuri sana wa miradi ya maendeleo katika jimbo lake. Kuna wakati hata mimi alinichukua kutoka Wizara ya Madini kwenda kumsaidia changamoto za wananchi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala lake la kwanza, napenda kumjulisha kwamba Serikali imeanza kutekeleza Mradi wa Gridi Imara wenye thamani ya shilini bilioni 500 ambao utakwenda kujenga kwanza vituo vya kupooza umeme katika kila wilaya; pili kujenga njia ya kusafirishia umeme; na tatu kufanya marekebisho makubwa kwenye njia ya umeme ili umeme nchini uwe wa uhakika, lakini pia Bwawa la Nyeyere litakapokamilika nadhani hiyo adha ya kukatika kwa umeme itakuwa ni historia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili, kuhusu hawa wananchi ambao anasema waliahidiwa kuunganishiwa umeme, ni kwamba Wizara ya Nishati inaendelea na mchakato na mchakato huo utakapokamilika watafahamishwa, ahsante sana.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, sababu kubwa ya kutokushiriki kikamilifu kwa vijana na wanawake katika shughuli hii ya madini ni mikopo kwa maana ya capital.

Je, Serikali haioni sababu ya kuwapa vijana mitaji ili kusudi washiriki kikamilifu katika sekta hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kumjibu Mheshimiwa Mchungahela mtetezi makini wa watu Jimbo la Lulindi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli changamoto kubwa ya vijana, wanawake na wachimbaji mbalimbali ni ukosefu wa mitaji. Katika kutanzua changamoto hii Wizara ya Madini kupitia Shirika lake la Taifa la Madini (STAMICO) wamewaweka wakfu walezi wakuu wa wachimbaji wadogo na hatua za awali za kuwasaidia zimehusisha kutoa elimu ili wafahamu namna ya kufanya uchimbaji wa tija, Sheria ya Madini, pia kuingia katika makubaliano na taasisi za kifedha hapa nchini zikiwemo Benki za NMB, CRDB na Azania ili waweze kuwakopesha wale ambao wamekidhi vigezo.

Mheshimiwa Spika, ili waweze kusaidiwa, wananchi wa Jimbo lake na Watanzania wote ambao wamepata hamasa ya kujihusisha na biashara ya madini ni vizuri waunde vikundi ili kuwa rahisi kuwafikia na kuwasaidia kupitia vikundi na wajiunge na Chama cha Wachimbaji wadogo wa Madini Tanzania ambao sasa hivi wapo kwenye mchakato wa kuanzisha benki yao ili waweze kupata mitaji na waweze kuchimba kwa wakati kwa tija zaidi na wa ufanisi.
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, Mheshimiwa Kisangi angependa kufahamu ni kwa kiasi gani wananchi kwenye maeneo tajwa wananufaika na uwepo wa madini haya kwa maana ya CSR?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Stella Ikupa kwa swali lake zuri, kwa sababu manufaa ya wanaokaa katika maeneo yanayochimbwa madini, yako ya aina mbalimbali. Kwa upande wa Serikali kodi zinazokusanywa kutokana na hiyo mirabaha pamoja na ada za ukaguzi zinaingia kwenye Mfuko Mkuu wa Taifa na kuingia kwenye bajeti ambayo kila mwaka Mama Samia anapitisha na miradi mbalimbali ya maendeleo kama barabara, zahanati na shule zinapata fedha hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa upande wa wawekezaji wenyewe au wenye leseni huwa wanatoa michango kwenye miradi mbalimbali ya jamii katika maeneo hayo, sambamba na kutoa ajira katika maeneo ya migodi. Hivyo, manufaa yapo mengi katika mtizamo huo. Pia wale wanaojiongeza, wanafanya huduma za kuwahudumia wenye migodi kama akina mamalishe wanavyokwenda kupika pale na kutoa huduma mbalimbali.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tunayo Sheria Tanzania Extractive Industry Transparency Initiative Act ya mwaka 2016, Section Number 16 ambayo inataka mikataba yote ya Sekta ya Uziduaji iwekwe wazi na iwekwe wazi kwenye website pamoja na vyombo vya habari media zote Tanzania. Nataka kujua commitment ya Serikali, kwa sababu EITI wanakuja validation Tanzania mwaka huu.

Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba mnalinda reputation ya nchi kwa kuwa na sheria ambayo haitekelezeki kwa muda mrefu toka 2016? (Makofi)

Swali la pili, nataka commitment ya Serikali ni lini suala hili linakwenda kukamilika kwa sababu limekaa kwa muda mrefu sana? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimjibu Mheshimiwa Jesca Kishoa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa swali lake la kwanza, Wizara yetu ya Madini na wakifanya kazi pamoja na TEITI na mamlaka nyingine ya Serikali ikiongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wako katika mchakato ambao unachambua na kufanya kazi kwa kushirikiana na kampuni zote zilizowekeza katika sekta za rasilimali hizi ili kuona namna bora ya kuweka wazi hiyo mikataba kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya Taasisi ya Kimataifa ya EITI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kwamba ni lini? Kwa ratiba tuliyonayo tunategemea kwamba kufika Mwezi wa Kumi mwaka huu taratibu zote zitakuwa zimekamilika na hivyo mikataba hiyo itakuja kuwekwa wazi kwa mujibu wa matakwa ya Taasisi ya Kimataifa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Kwa kuwa, Serikali imeendelea kukaidi na kukiuka sheria katika uingiaji na usimamizi wa mikataba ya uziduaji ambayo ni madini gesi na mafuta na pamoja na matakwa yale ya TEITI lakini pia kuna matakwa ya Sheria Kifungu 12 cha (The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) No. (5) Act, 2017) ambayo…

MWENYEKITI: Mheshimiwa swali.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ambayo inataka mikataba yote iletwe hapa Bungeni. Kwa nini Serikali inaendelea kukiuka matakwa haya ya kisheria? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali haina mpango wala haifanyi maksudi kwamba lazima sheria iliyowekwa ikiukwe. Sheria zote zinasimamiwa na Serikali na Wabunge wote nasi Watendaji wote wa Serikali tumeapa kusimamia sheria ya nchi na Katiba ya nchi, kwa hivyo kama kuna ambayo haitekelezwi ni suala lingine la kuangalia tu mikakati ya Serikali ya kujisimamia na kuhakikisha kwamba sheria zinatekelezwa kwa mujibu wa jinsi zilivyotungwa lakini hakuna utaratibu wowote wa kwamba Serikali inakusudia na inavunja sheria yeyote.

MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, katika Mgodi wa Kebaga wachimbaji wadogo ambao wanachimba pale wanapata wakati mgumu wa kuuza dhahabu kwa sababu wataalam wanaokwenda kufanya tozo zile za dhahabu wanachelewa kwenda pale, hawana siku maalum ya kwenda kufanya tathmini.

Je, lini Serikali itaweka utaratibu mzuri wa siku zile za kwenda kuhakiki ili kutoa nafasi kwa wachimbaji wale kuuza madini yao? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, upo ushuru unaokusanywa pale na hakuna risiti za EFD ambazo zinatolewa, wanapewa risiti za kawaida; je, huu ni utaratibu ambao unakubalika na sheria?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusu kuchelewa kununuliwa kwa madini ya wachimbaji wadogo, ninapenda kurejea majibu yangu ya msingi kwamba kwa kufahamu umuhimu wa shughuli za uchimbaji wa madini pale, tumeanzisha kituo kidogo cha ununuzi wa madini na mchimbaji yeyote ambaye ameshachimba madini yake akifika pale tathmini hufanyika na biashara hufanyika.

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili kwamba kunakuwa na ucheleweshaji katika kuwahudumia hawa wachimbaji wadogo na wanatoa risiti ambazo ni za karatasi, kama changamoto hiyo ipo, nitamwomba Mheshimiwa Mbunge baada ya kipindi hiki tukutane na tuwasiliane na RMO kule tujue changamoto hiyo hutokana na nini ili tuweze kuishughulikia kikamilifu.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Swali la kwanza, tunaishukuru Serikali ndani ya muda mfupi imeweza kujenga maghala takribani kumi ndani ya Wilaya ya Chunya kwa ajili ya baruti. Lakini maghala haya yapo pale Chunya mjini na maeneo ya uchimbaji wa dhahabu yako kule vijijini.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba vibali hivi vinaweza kuwafikia wale wafanyabiashara wa baruti kwenye maeneo yale ya uchimbaji kule vijijini?

Swali la pili kwa mujibu wa majibu ya Mheshimiwa Waziri, Serikali imeshaingia Mkataba wa Minamata kwa ajili ya kupunguza matumizi ya zebaki na baadaye kuitokomeza kabisa. Lakini kwa kipindi hiki cha mpito matumizi ya kemikali hii ya zebaki bado inaendelea kutumika kwa ajili ya kuchenjua na ukamatishaji dhahabu.

Je, Serikali ina mpango gani kutoa elimu kwa wachimbaji hawa wadogo wa dhahabu ili madhara yasiendelee kutokea zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Kasaka kama ifuatavyo: -

Kwa upande wa swali lake la kwanza napenda kumfahamisha kwamba Serikali imeendelea kuboresha utaratibu wa kuweka urahisi wa upatikanaji na matumizi ya baruti katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kufikia mwaka huu mwezi huu wa sita Waziri wa Madini kwa mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa kifungu cha (8) cha Sheria ya Baruti ya mwaka 1963 Sura ya 45 amepewa mamlaka ya kutoa leseni kwa viwanda vya kutengeneza baruti hapa nchini na tayari kuna viwanda vitatu vimeshapewa hiyo leseni ya kuzalisha baruti jambo ambalo limepelekea kuwepo kwa upatikanaji wa zebaki kwa wingi nchini, lakini sambamba na hilo kifungu Na. 4 cha Sheria ya baruti Sura ya 45 imempa Waziri mamlaka ya kuteua wakaguzi wa baruti na hao sasa wameshateuliwa na wako katika kila Ofisi ya Madini ya Mikoa yetu yote ya madini nchini na wanafanyakazi chini ya Kamishna wa Madini ambaye anawapa kibali cha kutoa leseni za store na masanduku ya kuhifadhia baruti.

Mheshimiwa Spika, kana kwamba hiyo haitoshi, pia anawapa kibali cha kuweza kutoa leseni na mpaka sasa hivi tuna leseni 256 za maghala yaani magazine, leseni 338 za store yaani store yenyewe na leseni 114 za masanduku (storage boxes) ya kuhifadhia baruti na Kamishna kwa kutumia hawa wakaguzi wa baruti amewapa mamlaka ya kushirikiana na ofisi zetu za madini kila mkoa kuhakikisha kwamba baruti zinawafikia wachimbaji wadogo kwa njia iliyo salama na kwa njia rahisi kabisa kupatikana karibu na maeneo ya migodi.

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili ambalo anataka kujua kwamba hii zebaki sasa ambayo ni hatarishi kwa mazingira iko katika mikakati ya kwenda kuondolewa matumizi yake, lakini kwa kipindi hiki cha mpito kabla haijaondolewa matumizi yake Serikali inafanya nini kutoa elimu, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba mpaka sasa hivi Wizara imeshatoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo zaidi ya 600 na namna salama ya kutumia zebaki.

Katika Mkoa wa Shinyanga tumetoa elimu hiyo katika maeneo ya Mwimbe, Mwambomba, Kalole, Zambazare na Mwakitolyo na katika mwaka huu wa fedha ambayo bajeti yake inakwenda kusomwa leo Bungeni, tunategemea kuendelea kutoa elimu hiyo katika mikoa yote ya kimadini nchini ikiwemo Songea, ikiwemo Chunya, ikiwemo Songwe, Singida, Geita na maeneo mbalimbali ili wachimbaji wadogo waweze kutumia zebaki kwa makini mpaka hapo njia za mbadala zitakapopatikana, ahsante sana.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana matumizi ya zebaki kwenye maeneo yetu wachimbaji wadogo wadogo hasa Jimbo la Msalala yamekuwa na athari kwa wachimbaji wenyewe, lakini pia kwenye mazingira yanayozunguka pale. Sasa kabla Serikali haijaenda kuzuia matumizi ya zebaki ni teknolojia ipi ambayo mmeianzisha kama mbadala wa matumizi ya zebaki?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, nimweleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari kuna teknolojia mbadala ambayo inaendelea kutumika katika uchenjuaji wa madini ya dhahabu na teknolojia hiyo inaitwa ni cyanide na matumizi ya cyanide ni aina ya utaalam ambao ile kemikali yenyewe inapokuwa imetumika kuchenjua na kukamatwa kwenye mabwawa ya kuchenjulia madini huyeyuka na kupotea hewani bila kuacha madhara yoyote na hiyo ndiyo teknolojia ya kisasa ambayo tunaendelea kutumia na kuendelea kuitambulisha kwa wachimbaji wadogo.
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, Halmashauri ya Mji wa Bunda, Kata ya Guta, Mtaa wa Kinyambwiga kuna uchimbaji wa madini pale lakini kwa sasa kuna mgogoro kati ya wenye mashamba na wenye leseni. Je, ni nini kauli ya Serikali kwenye mgogoro huu?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini na kwa ridhaa yako namuomba Mheshimiwa Mbunge alete swali hilo kama swali la msingi halafu tutalijibu hapa Bungeni. (Makofi)
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na kwa kuwa madini ya Tanzanite yanaruhusiwa kuuzwa duniani kote ikiwa ni pamoja na India na Marekani.

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa vibali ili madini hayo pia yaweze kuuzwa kwenye mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Mwanza na nchi ya Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini napenda kumjibu Mheshimiwa Gambo kwamba madini ya Tanzanite ni madini ya kipekee kabisa ambayo yanapatikana nchini Tanzania tu na kwa ajili hiyo Serikali iliweka utaratibu wa kusimamia uzalishaji, uchakataji, uongezaji wake thamani palepale Mererani. Lakini katika kipindi tulichoko sasa hivi tuko katika hatua za kufanya tathmini ya utaratibu uliowekwa na Serikali ambapo baada ya kujiridhisha kwamba kuna utaratibu mwingine mzuri wa kuruhusu madini hayo yauzwe kila mahali ndani ya nchi na nje ya nchi, bila kuathiri uhalisia wa hali iliyokuwepo ya mwanzo ya utoroshaji wa kiholela tutakwenda kuweka utaratibu mahususi ili madini hayo yaweze kuanza kuuzwa popote pale maadam pia yatakuwa yameshaongezewa thamani na kupewa vibali vya kutoka ndani ya eneo la Mererani ambalo ni eneo tengefu kwa sasa.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujua ni njia gani nzuri Serikali inatumia kwenye matumizi ya cyanide, kwa sababu madhara ya zebaki ni bora zaidi kuliko madhara ya cyanide ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, nipende tu kumuhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba handlings kwa Kiswahili tunasema jinsi unavyo itumia cyanide kwa usahihi kwa kutengeneza yale malambo na kuweka tiling zile za kuzuia ili isivuje chini ya ardhi, ni njia ya uhakika kabisa kwamba ukishaitumia na ukaiacha ika-evaporate ndani ya anga/hewani haiachi madhara yoyote na ni salama zaidi kuliko zink ambayo upoteaji wake au biodegradability yake ni ngumu zaidi ya kuhifadhi katika maeneo ambayo hakutakaa kuwe na leakage.

Kwa hiyo, utaalam wa cyanide siyo mgumu kama ambavyo yeye anadhani na ni wa uhakika zaidi na ni salama zaidi kuliko zebaki.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, utafiti uliofanyika Aprili, 2018 huko Tennessee Marekani, unaonesha kwamba sehemu zenye machimbo ya makaa ya mawe karibu na mito kuna upungufu wa viumbe wa majini kwa asilimia 53 wakiwemo samaki. Swali la kwanza; je, sisi Serikali yetu imefanya utafiti huo na kuja na majibu haya?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, sasa hivi tunaanza kuchimba makaa ya mawe Kiwira Coal Mine na Mto Kiwira na Mto Songwe vimeathirika kwa namna hiyo. Je, ni hatua gani zinazochukuliwa kwa Serikali ili kusiendelee kupatikana kwa athari hizo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Mlaghalila, Mbunge wa Kyela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa taarifa anayosema kwamba kuna tafiti za kidunia zinazothibitisha kwamba uchimbaji wa makaa ya mawe una uhusiano na kupungua kwa samaki katika maziwa na mito; nikiri kwamba sisi hatuna scenario kama hiyo katika Nchi yetu ya Tanzania kwa sababu hatuna uchimbaji katika maeneo ya karibu na mito ambayo ina samaki au maziwa ambayo kuna upungufu uliobainika kwa tafiti za kisayansi.

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba katika eneo la machimbo ya makaa ya mawe lililoko Kiwira na Kabulo tuna Mradi unaoitwa Kiwira-Kabulo Coal Project ambao uko chini ya taasisi yetu ya STAMICO. Katika eneo Kasumulu, Wilaya ya Kyela ilianzishwa site ndogo ya heka mbili kwa ajili ya kuwa selling point ya yale madini kutokana na shida ya barabara ya kutoka Kabulo kwenda Kiwira kuliko na kituo kikubwa cha makaa ya mawe ya STAMICO. Kwa sasa hivi, barabara hiyo ya kilomita saba ilishakamilika na utaratibu wa kuhamisha kile kituo umeshafanyika na kuna tani 1,200 za makaa ya mawe mpaka kufikia mwezi Agosti, 2022 yatakuwa yameondolewa yote, ila tahadhari zote zilichukuliwa.

Mheshimiwa Spika, kwanza; kulingana na Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, Kifungu 57(1) hairuhusiwi kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka ukingo wa mto. Site iliyotengwa kule katika mradi huu wa makaa ya mawe kule Kasumulu upo mita 120; lakini kana kwamba hii haitoshi makingamaji ya kuchepusha maji yasielekee mtoni yamejengwa na kuna mashimo makubwa kama mvua itanyesha na maji yakatiririka yakaingia mle yakakaukia humo. Pia kana kwamba hiyo haitoshi, kulingana na Kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004, sisi kama Wizara ya Madini tunazingatia sana suala la utunzaji wa mazingira.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria hiyo, Kifungu cha 107(2) cha Sheria ya Madini Na. 123, kinazingatia utunzaji wa mazingira kwamba baada ya ile site kuachiwa tutapenda kuirejesha na kuzungushia fence na kutumika kwa matumizi ya kufundisha wananchi wa eneo la Kyela na Ileje namna ya kutengeneza makaa mbadala ya makaa ya mawe yanaitwa Coal Breakage. Kwa hiyo, hakuna athari ya mazingira na sisi tupo makini. Ahsante sana.
MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Ziko Leseni zimetolewa kwa ajili ya shughuli za utafiti kwenye maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Jimboni Nachingewa lakini wahusika hawajafanya shughuli hiyo iliyokusudiwa kwa muda mrefu sasa.

Je, Serikali haioni sasa iko haja ya kupitia sheria yetu ili kuweza kuondoa utitiri wa hawa watafiti ambao kimsingi hawatimizi majukumu hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana na mimi baada ya kipindi hiki cha Bunge ili kwenda Jimboni Nachingwea kuona halihalisi iliyoko na kuwatia moyo wachimbaji wadogo wadogo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kumjibu Mheshimiwa Chinguile, Mbunge makini wa Nachingwea, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu waliopewa leseni na wamezilaza hawazifanyii kazi; mwezi wa tisa na mwezi wa kumi tulitoa kama ndiyo kipindi cha mwisho, waweze aidha kufanyia leseni zao kazi au zifutwe. Tangu tangazo hilo litoke, zaidi ya leseni 7,000 zimeshahuishwa na kuna wale ambao hawajaweza kuhuisha mpaka tarehe 30 mwezi uliopita, mchakato wa kuzifutia hizo leseni unaendelea. Hatukuishia hapo, zilizokwishaharibiwa kwa kutofanyiwa kazi huko nyuma, maeneo zaidi ya 48 zimegawiwa kwa wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Spika, hivyo hata katika jimbo lake, wale ambao watashindwa kuendeleza leseni kwa mujibu wa tangazo hilo la Serikali kupitia Wizara ya Madini, watarudisha hizo leseni na tutawapa wale ambao wako tayari.

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili, mimi niko tayari baada ya Bunge hili, nitampangia ratiba. Tutafika huko tuwatie moyo wachimbaji wadogo wanaofanya shughuli zao na kuwahamasisha wengine watumie fursa zilizoko katika Wizara ya Madini kupata uwekezaji ambao utawainua katika Maisha yao. ahsante sana. (Makofi)
MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa ilitokea katika historia ya Nchi yetu Tanzania ikatawaliwa na wakoloni na kwa kuwa wakoloni hawa walifanya tafiti mbalimbali za madini hapa nchini, sambamba na kuchimba madini hayo.

Je, ni lini Wizara ya Madini itawaomba wakoloni hawa waje kufunga mashimo waliyoyaacha kwa maana ya kufanya mining closure?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; naomba kujua kama Wizara ya Madini wanazo tafiti zilizoachwa na wakoloni ili waweze kuziweka wazi kwa Watanzania ili waweze kuwekeza kwenye madini. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Ndaisaba George Ruhoro, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la kwanza, kuhusu wakoloni ambao walifanya tafiti, wakachimba madini na wakaacha mashimo na yeye kutaka kujua mpango wa haya mashimo kuja kufungwa, nipende kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba, wakoloni wa Kijerumani ambao walifanya utafiti mkubwa wa madini ya makaa ya mawe na hata dhahabu katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu ikiwepo kule Ngara na maeneo ya Sekenke Singida waliondoka kabla hawajayamaliza madini katika machimbo hayo, hivyo hawakuhangaika kuyafunga na mashimo haya yamekuwa msaada kwetu katika kuendeleza tafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo mengine leseni zimeshatolewa na mashimo haya yamekuwa yakitoa mwongozo wa kubaini madini yaliyopo ili tuendelee kuyavuna na hivyo basi kwa ajili ya jibu la swali lake hilo pia kwa kipengele cha hayo mashimo, wale waliopewa leseni sasa kulingana na Sheria yetu ya Madini, Sura ya 125 ndio wamepewa wajibu wa kuandaa closure plan, mpango wa ufungaji wa mgodi kulingana na Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 ambao unamtaka mwenye mgodi aweke utaratibu wa jinsi atakavyorejesha ile ardhi katika hali yake salama baada ya mradi kumaliza uhai wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa swali lake la pili, hizo takwimu za tafiti zilizofanywa na wakoloni tutazipataje. Kwa bahati nzuri wajerumani walivyofanya tafiti za madini katika nchi hii kuanzia mwaka 1925, waliacha takwimu za kutosha, data zipo katika archives zetu katika taasisi yetu ya GST hapa hapa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuibua hilo swali ili nitumie fursa hii kutoa rai kwa Watanzania wanaopenda kufanya biashara za madini kwamba tunazo data za tangu enzi za ukoloni mwaka 1925, waje wazifuatilie kule, maktaba ipo na wanaweza wakapata taarifa za kijiolojia za kuwaongoza katika kwenda kuendeleza kwenye uchimbaji wa madini husika katika maeneo yaliyofanyiwa utafiti. Ahsante sana.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, ni lini Serikali sasa itawaangalia wachimbaji wadogo wa Mkoa wa Njombe ambao walishaomba leseni za kuchimba makaa ya mawe kule Ludewa na Wizara imeshawaahidi na wakaunda vikundi, lini watawapa leseni?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deodatus Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna wachimbaji wengi nchini ambao wameomba leseni za uchimbaji na bado hawajapata na hasa wa jimbo lake ambapo kuna maeneo ya machimbo ya makaa ya mawe ambayo yapo katika eneo linalomilikiwa na Taasisi nyingine ya umma ya NDC. Kwa sababu ya utaratibu kwamba yale maeneo yana wamiliki wengine sisi tukitoa leseni ni lazima wale waliopewa leseni wakaombe mwenye surface right kuingia katika uchimbaji na mchakato wa kuwasaidia wachimbaji wadogo ili wapate maeneo ya kuchimba ni moja ya dhamana tuliyopewa sisi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nimwahidi tu Mbunge kwamba baada ya Bunge hili mwezi Julai, mimi binafsi nitafika katika maeneo hayo yenye wachimbaji ambao wamepata leseni au wanaomba leseni hawajapata, tujue changamoto zinazowakabili ili tuzitatue na waweze kupata maeneo maana ni dhamira yetu kwamba wachimbaji wadogo wapewe maeneo ya kuchimba ili wapate tija kutokana na rasilimali madini yaliyopo katika nchi yetu. (Makofi)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Natumia fursa hii kwanza kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri wa Madini na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kwa ushirikiano mkubwa ambao tumeufanya hadi kufikia hatua hii.

Mheshimiwa Spika, mwekezaji anatumia upungufu uliomo kwenye Sheria yetu ya Madini na Sheria ya Ardhi kuendelea kuchelewesha au kukwamisha mazungumzo yanayoendelea; na kwa sababu hiyo kuendelea kuwatesa wananchi ambao wamekaa kwenye mgogoro huu kwa zaidi ya miaka 22.

Mheshimiwa Spika, sasa, kwa nini wakati tunaendelea kubishana, Serikali isichukue jukumu la kulipa fidia yenyewe, halafu ikaendelea kujadiliana upungufu wa kisheria unaoendelea kuwepo eneo hilo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; naipongeza sana Serikali kwa tathmini ya awali inayoendelea kule Samina. Eneo linalofanyiwa tathmini linafanana kabisa na maeneo nane yaliyobaki. Kwa nini sheria ile ile ambayo imetumika kufanya tathmini kwa wananchi wa Samina isitumike kwenye maeneo mengine ambayo sasa hivi Serikali inasema bado inafanya mazungumzo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Kanyasu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Serikali kulipa fidia, napenda kumjulisha kwamba, Serikali inapotoa leseni kwa mwekezaji, yule mwenye leseni ndiye anakuwa na Haki Madini pale na ndiye mmiliki wa madini. Hivyo, siyo tena Serikali yenye wajibu wa kulipa fidia ya aina yoyote. Kwa hiyo, kwa maridhiano kati ya mwenye leseni na wananchi na viongozi wa eneo lile, akikubali kuwalipa fidia kama anavyoomba kwamba fidia ilipwe hata kabla hajaweza kuhamishwa, hilo tunawaachia wao kupitia mfumo ulioko wa maridhiano na mahusiano mema na jamii.

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili, kwamba kwa nini Serikali isilipe? Majibu ni kama hayo tu kama nilivyotangulia kusema, kwamba Serikali siyo mmiliki tena wa yale madini. Amepewa Haki ya madini yule aliyepewa leseni na ndiye mwenye dhamana ya kufanya kazi na wananchi ili waweze kulipa.

Mheshimiwa Spika, pia nitumie fursa hii kumjulisha Mheshimiwa Mbunge na nampongeza kwa namna anavyofuatilia swali hili kwamba, tulishaunda Kamati kati ya Wizara, Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya ya Geita ambayo inaendelea na mazungumzo ya kutafuta namna bora ya kuwafidia wale watu ambao ni lazima wahame, kama hao wa Samina ambao karibu hatua za mwisho zinafikiwa na hawa wengine ambao walisema hawatayahitaji maeneno yao lakini itafutwe namna bora ya kuwashika mkono au kwa ajili ya usumbufu ili waweze kuendelea na maisha yao.