Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita (40 total)

MHE. DKT. STEPHEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri Mkuu katika ziara yake Wilayani Ngorongoro mwaka jana aliahidi nyongeza ya kilometa 50 kwenye ujenzi wa barabara unaoendelea. Je, ahadi hii itatekelezwa lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 – 2020 imeainisha ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 65 kutoka Sanya Juu hadi Longido; ni lini ujenzi wa barabara hii utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze sana Wabunge wa Chama cha Mapinduzi waliopo Mkoa wa Arusha, ninatambua juhudi nyingi wanazozifanya ili kuhakikisha miundombinu ya barabara katika mkoa inaimarika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza sana Mheshimiwa Olenasha kwa sababu amefuatilia barabara hii ya Loliondo – Mto wa Mbu, na mimi niseme tu kwamba tutaendelea kuhakikisha kwamba barabara zinajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri Mkuu alitembelea Loliondo na aliahidi ujenzi wa barabara ya nyongeza kwa kilometa 50, kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili tunalishughulikia na tunaangalia kadri itakavyowezekana katika bajeti hii inayokuja nyongeza ya hii barabara tutaendelea kujenga. Kwa sababu barabara hii inayo urefu wa kilometa 218 kwa hiyo karibu asilimia 25 sasa barabara hii inajengwa, sasa tukiendelea kuongeza tutapata asilimia 50 na hatimaye barabara hii itakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, barabara hii ya Sanya Juu hadi Longido imetamkwa katika Ilai ya Uchaguzi, na niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako Tukufu kwamba tunaendelea kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi na tuna kipindi cha miaka mitano nah ii barabara tutaitazama katika bajeti zinzaokuja ili tuhakikishe ahadi za Chama cha Mapinduzi na tuna kipindi cha miaka mitano nah ii barabara tutaitazama katika bajeti zinazokuja ili tuhakikishe ahadi za Chama cha Mapinduzi zinatekelezwa kikamilifu. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Kabla ya yote nipende kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano ya Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutupatia mradi huu mkubwa wa kutuletea maji safi na salama kwa ajili ya binadamu na mifugo toka Mlima Kilimanjaro Mto Simba.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa wananchi wa hizi Kata tatu zilizolengwa na mradi huu wana shauku kubwa ya kupata maji haya ikizingatiwa kwamba Wilaya hii ni kame, Je, mradi huu unategemewa kukamilika lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kufahamu uhaba wa maji katika Wilaya ya Longido Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji alipotembelea Longido mwaka jana aliwaahidi wananchi wa Kijiji cha Wosiwosi wanaoishi pembezoni mwa Ziwa Natron lenye maji yasiyofaa kwa matumizi ya binadamu pamoja na wananchi wa Kata ya Tingatinga katika Kijiji cha Tingatinga kwamba atawapatia mabwawa ya maji; je, ahadi hii ataitimiza lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ya kipekee anavyowatetea wananchi wake wa Longido. Kubwa tu itambulike kutokana na changamoto kubwa sana kwa Mji ule wa Longido katika suala zima la maji, Wizara yetu ikaona haja ya kuwapatia wananchi wale maji safi na salama na ya kuwatosheleza, lakini anataka kujua ni lini mradi ule unakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi ule unakamilika mwishoni mwa mwezi Mei. Mimi kama Naibu Waziri nilipata nafasi ya kufika pale katika kuhakikisha tunausukuma mradi ule ili wananchi waweze kupata maji safi na salama. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, nilipofika katika ule utekelezaji wa mradi nimemkuta Mkandarasi amelala, nilimtikisa kwa mujibu wa mkataba ili mwisho wa siku wananchi wake wapate maji. Nataka nimhakikishie tutashirikiana ili wananchi wake waweze kupata maji safi na salama kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la ahadi ya Mheshimiwa Waziri ya mabwawa, nataka nimhakikishie ahadi ni deni. Sisi kama Wizara ya Maji kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ameahidi tutatekeleza kwa wakati katika kuhakikisha wananchi wake wanapata maji.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona na naomba niulize swali dogo la nyongeza kuhusiana na mada hii iliyoko mezani.Kwa kuwa Wilaya ya Longido haina chuo hata kimoja, chuo chochote cha Serikali; na kwa kuwa Wilaya hii ya Longido ni ya wafugaji kwa karibu asilimia 100 na ni wilaya ya uhifadhi wa wanyamapori kwa sababu tuna maeneo ya WMA na ya uwindaji, je, Serikali haiwezi kuja kutujengea VETA hasa inayolenga tasnia ya ufugaji mifugo na uhifadhi wa wanyama na mazingira na ikiwezekana Chuo cha Walimu wa Sayansi kwa sababu kuna uhaba mkubwa wa Walimu wa sayansi nchini na tuna ardhi ya kutosha na maji ya Kilimanjaro yanakuja?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba mikoa na wilaya zote nchini zinakuwa na vyuo vya VETA. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeanza kwenye baadhi ya maeneo ambako tayari kuna ujenzi unaendelea na kuna mipango ya kuhakikisha kwamba wilaya zote zinakuwa na vyuo vya VETA. Kwa hiyo, hata Longido tutafika na wakati tunafanya hivyo, tutaangalia zile fani ambazo zitawasaidia wananchi wa pale kuweza kujiendeleza.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri aliyonipa Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijauliza, nichukue fursa hii kuishukuru Serikali kwa sababu ya kazi kubwa na nzuri wanayoifanya kuinua hali ya elimu katika Wilaya ya Longido. Historia ya Wilaya ya Longido…
Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa. Swali ni kwamba kwa upande wa ubora wa elimu ukizingatia kwamba ubora wa elimu unategemea uboreshaji wa shule kuanzia ngazi ya chekechea; na kwa kwa sababu vitongoji vya Wilaya ya Longido viko mbali na shule za msingi zenye elimu za chekechea (shule za awali).
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mpango gani katika kuhimiza wananchi wajenge shule na Serikali ipeleke walimu waliosomea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa kuwa tatizo la shule za msingi la miundombinu halina tofauti na Shule zetu za Sekondari katika Wilaya ya Longido; je, Serikali imejipangaje kutusaidia kuziba mapengo yaliyopo katika madarasa yapatayo 58, maabara 27, mabweni 73, nyumba za walimu
252, maktaba nane...
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna uhaba wa walimu wa sayansi wapatao 27? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS - TAWALAZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, katika muda mfupi tangu alipochaguliwa kuwa Mbunge amefanya mengi, ofisini kwangu ameshakuja zaidi ya mara tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zake nazipokea kwa niaba ya Serikali, naomba sana nimhakikishie kwamba wananchi waendelee na juhudi wanazozifanya. Tunatambua juhudi zao. Pale ambapo atakamilisha darasa lolote la awali, tuwasiliane ili tuweze kupeleka walimu wa madarasa ya awali ambao wamesomeshwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili kuhusu kumalizia maboma ambayo wananchi wameanzisha na yamefika kwenye lenta, naomba nimhakikishie kwamba katika fedha za ruzuku ya maendeleo ambazo tutazipeleka kuanzia mwezi wa Saba tumewapa kipaumbele Wakurugenzi wazingatie sana kumalizia maboma ambayo yameanzishwa na wananchi. Ahsante sana. (Makofi)

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona na kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, wananchi wa Longido wamekuwa wakisubiri kwa hamu kukamilishwa kwa mradi mkubwa wa maji safi na salama kutoka Mlimani Kilimanjaro, Mto Simba kuja Longido. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwamba mradi huu kwa kasi inayoendelea sasa hivi unatarajiwa kukamilika lini?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru kwa jinsi anavyofuatilia utekelezaji wa miradi ya maji katika Jimbo lake na Serikali hii ya Awamu ya Tano tayari ina mkataba wa zaidi ya bilioni 16 kwa ajili ya Halmashauri yake ya Longido.
Mheshimiwa Spika, uko mradi mkubwa unaotoa maji Mlima Kilimanjaro kilomita 64. Kulikuwa na matatizo ya kupata bomba la chuma lakini Serikali, Wizara imeingilia kati Mkandarasi ameingia mkataba na kiwanda cha kuzalisha mabomba na mabomba yameanza kuingia tayari kule site.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wake kwamba kuanzia sasa tunaenda haraka ili tuhakikishe wananchi wake wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Longido katika harakati za kujiongezea mapato ya ndani ya kuinua kipato cha wananchi wake walijenga mnada wa mifugo katika Kata ya Kimokouwa inayopakana na Kata ya Namanga iliyoko mpakani mwa Kenya na Tanzania ili pia kuwatengenezea wachuuzi wa mifugo mazingira rafiki ya kuweza kufanya biashara ya mipakani (cross border trade) na kwa kuwa baada ya Halmashauri kumaliza mnada ule wakaanza kuhamasisha wananchi waliokuwa wanapitisha ng’ombe maporini kupeleka kuuza katika minada ya Kenya ambayo ndiyo inayutumika katika maeneo ya Longido, jana Waziri akaenda akatoa maagizo ya kuwapangia bei ya kulitumia soko lile kitendo ambacho kimewakera wananchi…
Naomba Waziri mwenye dhamana aliyekwenda jana kutoa directives za bei ya mifugo atoe kauli itakayowafanya wananchi wa Longido na Halmashauri kuelewa kwamba soko hili ambalo wamejenga kwa nguvu zao wenyewe na wafadhili bila Wizara kuwekeza hata shilingi watatoa justification gani ya kwenda kulitwaa na kulipangia bei ambayo sio rafiki ni kandamizi, hii ni sawa na kuvuna usichopanda?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tasnia hii ya mifugo inaendeshwa kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni zake. Tunafahamu kwamba Longido kumejengwa mnada kupitia miradi ya Serikali kupitia ule Mradi wa MIVAF unaosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnada ule kimkakati uko mpakani na sisi katika tasnia hii ya mifugo kama Taifa kwa mwaka mmoja kwa tathmini tuliyoifanya ng’ombe 1,600,000 wanatoroshwa kwenda nje ya nchi. Pia tunapoteza jumla ya shilingi 263,000,000,000 kama Taifa ikiwa ni mapato yetu yanayotokana na tasnia hii ya mifugo hasa export royalty.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwambie Mheshimiwa Kiruswa kwa sababu nafahamu kwamba ni Mbunge makini na ana timu makini iliyoko kule ya DC na Mtendaji kwa maana ya Mkurugenzi, watupe ushirikiano. Hatufanyi jambo hili kwa ajili ya kuwakomoa, tunafanya jambo hili kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za nchi yetu lakini tunafanya jambo hili kwa ajili ya kuhakikisha Taifa letu linanufaika na rasilimali zake. Ahsante sana.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, pamoja na majibu mazuri ya Waziri hususan anaponieleza mkakati wa Serikali katika kuinua kiwango cha elimu ya awali. Namshukuru sana kwamba ametamka wazi kwamba kuna vitabu vya kiada vinachapishwa na kuna vitabu vya ziada viko katika mchakato wa kutolewa. Sasa swali langu la kwanza ni kwamba, je, vitabu hivi vitasambazwa lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa inaonekana Serikali imejikita kupeleka madarasa ya elimu ya awali katika shule za msingi kwa kuzingatia kwamba jamii nyingi za kifugaji wanaoishi katika Wilaya kwa mfano Wilaya yangu ya Longido, Simanjiro, Kiteto, Ngorongoro na Monduli hata Siha wanaishi mbali na shule kutokana na jiografia. Sasa Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba elimu hii bora katika ngazi ya awali inawafikia watoto hawa wadogo ambao hawawezi kufikia hizo shule zenye madarasa ya awali?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuhusiana na vitabu katika jibu langu la msingi nimesema kwamba tayari vitabu sita vya kiada; na vitabu vya kiada ni vile ambavyo ni lazima kwa mujibu wa muhtasari mwanafunzi awenavyo tayari vimekwishachapwa ambavyo viko katika hatua ya uchapaji ni vitabu vya ziada yaani vya nyongeza zaidi ya vile ambavyo ni vya lazima katika muhtasari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lake la pili kuhusiana na umbali wa shule, kama nilivyosema Serikali imetoa maelekezo kwamba kila shule ya msingi ni laizma iwe na darasa la awali. Kwa hiyo, nitoe wito kwake nafahamu kwenye jamii za wafugaji kunakuwa na changamoto kwamba Halmashauri ishirikiane na Serikali Kuu kuona kwamba kama kuna utaratibu wa tofauti na uliowekwa na Serikali wa kuchukuliwa kwa ajili ya jamii za wafugaji Serikali iko tayari. Lakini Halmashauri ndiyo ina jukumu la kutoa mapendekezo pale ambapo wanaona utaratibu wa kisera ni mgumu kulingana na mazingira yao.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza na kabla sijauliza maswali yangu kwanza nipende kumpongeza Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa kazi nzuri wanazozifanya katika kuinua sekta ya mifugo. Lakini hasa niishukuru Serikali kwa ajili ya soko hilo lililojengwa kule mpakani mwa Kenya na Tanzania katika Kijiji cha Eworendeke, na nitoe rai kwamba waachiwe halmashauri waendeshe kwa sababu ndio waliobuni Wizara itoe tu oversight.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza kwa kuwa jamii hii ya kifugaji ili mifugo iwaletee tija wanahitaji malisho, maji, tiba ya chanjo na kutibu magonjwa sambamba na masoko ya uhakika na ninashukuru kwamba soko la Eworendeke linaweza kuja kuwa soko la uhakika waondokane na adha ya kupeleka mifugo huko nje ya nchi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutusaidia hasa wafugaji wa West Kilimanjaro waweze kupata hayo maeneo ya kulishia hasa ukizingatia kuna mgogoro mkubwa ambao umekuwa ukitokea kila wakati wa kiangazi kwenye yale mashamba pori yaliyotelekezwa na Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili linamhusu Waziri wa Maliasili kwa sababu maswali yangu yalichanganywa, kwa sababu niliuliza swali moja kwa ajili ya Wizara ya Utalii na majibu niliyopata sikuridhika nayo. Eneo lote la Wilaya ya Longido ni Pori Tengefu na dhana ya WMA ilipoanza mchakato ulifuatwa WMA ndiyo ikapatikana. Mchakato ukapitiwa…
Mheshimiwa Mwenyekiti, WMA ya Lake Natron imepitia mchakato wote. Ni kwa nini WMA hii haitangazwi na imebakia kutangazwa tu na kitu kinawezekana?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mbunge huyu mpya kwa kazi kubwa nzuri anayoifanya ya kuwasimamia wafugaji wa eneo hili la Longido.
Mheshimiwa Mwenyekiti, anataka kwanza, Mheshimiwa Mbunge namna ambayo tutakavyoweza kushirikiana nao kama Halmashauri, nataka nimhakikishie ya kwamba sisi kama Wizara tutawapa ushirikiano na hatutafanya kazi ile ya usimamizi wa moja kwa moja isipokuwa tutakuwa pale kwa pamoja kuhakikisha kwamba kodi zote za Serikali ambazo zinasimamiwa na Wizara zitakuwa zinapatikana kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya suala la West Kilimanjaro, naomba nimhakikishie na niwahakikishie wafugaji wote wa eneo lile, ikiwa ni pamoja na Longido, Siha na kwingineko ya kwamba mkakati wetu mahususi wa Wizara ni kuhakikisha kwamba wafugaji ng’ombe hawafi tena. Wakati maeneo ya asili ambayo yanamilikiwa na Wizara yetu kwa maana ya ranchi ziko pale. Tumekubaliana ya kwamba wafugaji watapewa ruksa ya kupewa vitalu katika maeneo yale anaingiza ng’ombe wake, ng’ombe mmoja kwa kiasi cha shilingi 10,000; anamlisha, anamnywesha katika ranchi ile kwa muda wa miezi mitatu ananenepa na kumtoa kumpeleka sokoni.
Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Kiruswa na wafugaji wote nchini ya kwamba tumejipanga vyema na tutawasaidia katika jambo hilo.

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa majibu mazuri aliyoyatoa.
Kuhusu hili suala la WMA kutangazwa katika lile eneo naomba kwanza niweke vizuri tu kwamba WMA ni hatua ya kwanza ya uhifadhi ambayo inashughulikiwa na vijiji vinavyozunguka maeneo ya hifadhi, baada ya hapo inakuja pori tengefu baada ya hapo pori la Akiba, baada ya hapo hifadhi ya Taifa. Sasa tumeshafika tayari kwenye pori tengefu hatuwezi kurudi tena chini kwenye WMA, lile eneo litaendelea bado kuwa ni pori tengefu, lakini baadae tutaangalia kama sifa zinaliruhusu kuwa ni pori la akiba baada ya hapo tutaendelea kupanda zaidi badala ya kurudi nyuma. (Makofi)
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa asilimia 95 ya wakazi wa Longido ni wafugaji na ndicho wanachokitegemea kwa uchumi wao; na kwa kuwa mvua kubwa za mwaka huu zimeharibu miundombinu ya mabwawa likiwemo bwawa la Kimokolwa lililopasuka, Emuriatata na Sinoniki; na kwa kuwa mabwawa mengine matatu yanayotegemewa…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumwuliza Mheshimiwa Waziri ana mpango gani au ametutengea fedha kiasi gani kurekebisha miundombinu hiyo iliyoharibika?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Kiruswa anataka kujua ni kiasi gani tumewatengea? Tunayo hela ambayo tumeitenga kwa ajili ya kuweza kuwasaidia wananchi wa Longido kwenda kurekebisha miundombinu yao ya mifugo ikiwa ni pamoja na mnada wa mifugo wa pale Longido.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la miundombinu iliyopasuka kutokana na mvua nyingi zilizonyesha nchini, naomba mimi na yeye Mheshimiwa Mbunge tuweze kukutana na kuweza kulijadili na kuona ni namna gani tutaweza tukatoka kwenda kuwasaidia wananchi.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza kwa niaba ya wananchi wa Longido ambao pia nina furaha kwamba Madiwani wao karibu wote leo wapo hapa kama wageni wa Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido sawa na Busokelo, kwamba tuna utajiri mkubwa wa madini ya rubi. Kwa kuwa madini ya rubi ukiyakata ili kuyaongezea thamani kulingana na utaratibu uliotolewa na Serikali yanasagika. Kwa kuwa Mawaziri walishatembelea na wakajua changamoto hiyo, wanatuambia ni lini utaratibu huo utakamilika ili wananchi waweze kuyauza mawe haya waendelee kunufaika?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mimi pamoja na Naibu Waziri mwenzangu, Mheshimiwa Nyongo tulikwenda Longido na hasa kwenye eneo la Mundarara anbako kuna machimbo ya rubi. Wananchi wa kule wanajihusisha na shughuli hiyo na changamoto aliyoizungumza Mheshimiwa Mbunge walitueleza kwenye mazungumzo yetu na wao. Jambo ambalo linapaswa lieleweke hapa ni kwamba Sheria yetu mpya ya Madini imezuia kabisa usafirishaji wa madini ghafi kwenda nje ya nchi. Lengo ni kwamba tunataka teknolojia na ajira zibaki ndani ya nchi kuliko kuzisafirisha kwenda nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo madini ambayo yana upekee wa aina yake katika ukataji. Serikali kupitia Wizara ya Madini na Tume ya Madini tunaandaa mwongozo wa namna bora zaidi ya kuwasaidia wananchi ili waweze kupata fursa ya kuuza madini haya.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya niweze kuuliza swali la nyongeza kwa Waziri wa Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wananchi wa Wilaya ya Longido wanaoishi katika vijiji 32 vilivyopo Ukanda wa Magharibi unaokwenda mpaka Ziwa Natron waliungana wakatenga eneo la Hifadhi la Wanyamapori ambalo wameliita Lake Natron Wildlife Management Area, wakapita mchakato mzima na hatua zote za usajili ikabaki kipengele kimoja tu ambacho kipo katika dhamana ya Waziri ya kuwapatia user right yaani haki ya matumizi ya rasilimali ya wanyama pori katika eneo hili. Jumuiya hii imetumia rasilimali nyingi kupitia mchakato ambao wote mnaujua siyo wa bei nafuu na umetumia fedha za wafadhili na za Serikali, ni lini sasa Jumuiya hii itapewa user right wawe kuanza kulisimamia na kutumia rasilimali ya eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali Dkt. Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuna mchakato mrefu sana wa kusajili WMA na kama Mheshimiwa Mbunge ananihakikishia kwamba taratibu zote za awali zimekwishatimia, nitakwenda kufuatilia na kuona kama kipengele kilichobaki kinamhusu Waziri peke yake basi nitamshauri Mheshimiwa Waziri kutoa hiyo user right.
MHE. DKT. STEPHEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Waziri. Pamoja na majibu yake mazuri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza ni kuhusiana na uhalisia na Mto Ngarenanyuki. Mto huu ni moja ya mito michache ambayo imetokea katika maeneo yaliyohifadhiwa, unatokea katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha, chanzo chake ni salama na unapitisha maji mengi ya kutosha na kutiririsha katika nyanda za chini ambapo unapotoka ndani ya hifadhi, kijiji cha kwanza unafikia Kijiji cha Ngarenanyuki yanatiririka mpaka Kijiji cha Ngabobo na zamani za kale yalikuwa yanatiririka mpaka Kijiji cha Jimbo langu la Longido cha Ngereani.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba; kwa kuwa maji haya yalipoingia Kijiji cha Ngarenanyuki wananchi wakagundua kwamba ni maji safi ya kuoteshea nyanya; wamekatakata mto mifereji mashine za kunyonya maji mtoni mpaka mto ukakaushwa na maji hayatiririki tena kwenda kwenye vile vijiji vya kusini zaidi. Serikali ina mpango gani wa kusanifu miundombinu ya umwangiliaji wa kisasa itakayowezesha matumizi bora ya maji haya ili yaendelee kutiririka kufikia jamii zilizo chini zaidi kwenye nyanda za chini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kuwa tunakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi na uwezekano wa maji haya kutosha wakulima wa nyanya waliopo Ngarenanyuki, Ngabobo Mpaka Ngereani kuwafikia wote kwa mtiririko wa asili. Serikali haioni kwamba ni bora sasa wajenge tanki kubwa la kuvuta maji Ngereani ili nao waendeleze kilimo cha umwangiliaji wa nyanya; hasa ukizingatia kwamba ni kilomita 10 mpaka 20 tu katikati Ngereani kutoka mtoni?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stephen Lemomo Kiruswa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, maswali yake yote mawili yamegusa utaalam ambao upo ndani ya Serikali ingawa haupo ndani ya Wizara yangu. Ni jambo la msingi alilolizungumza, kwamba kila Mtanzania anawiwa na dhima ya kulinda rasilimali za maji na hasa hasa kwa sababu haya maji mazuri yametoka katika eneo limeifadhiwa yalikuwa yanatiririka vizuri kwenda kwenye vijiji. Sasa wananchi wameya-tap na kuyachota na kupeleka kwenye miradi ya umwagiliaji bila kuzingatia ushauri mzuri wa kitaalam wa kutumia maji kidogo na kuzalisha zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, basi natoa ushauri kwa Tume ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Bonde washirikiane, kwa sababu hizi ni mamlaka za Serikali, waende katika eneo husika wakawaelimishe wananchi kuhusu kilimo bora cha umwangiliaji bila kuchukua maji mengi kutoka kwenye mto ule ili maji yale yaifadhiwe yaendelee kutumika vile vile kwa shughuli zingine na kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kuhusu ujenzi wa tanki kubwa litatokana na ushauri ambao wataalam wataona kadri inayofaa katika kutumia maji ya Mto Ngarenanyuki. Ahsante sana.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijamuuliza maswali ya nyongeza, nichukue fursa hii kumpongeza Naibu Waziri wa Utawala Bora na Utumishi japokuwa ni muda mfupi tu tangu apewe dhamana ya kusimamia nafasi hiyo utendaji wake unaonekana na kasi yake nafikiri ni sehemu ya kasi anayohitaji Rais wa nchi kuona katika utendaji wa Mawaziri wetu. Hongera sana mama, nakuomba uendelee kukaza buti umsaidie Rais kazi aliyokupa dhamana ya kuifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hilo, swali langu la kwanza, kwa kuwa katika Wilaya ya Longido lenye jumla ya vijiji 49, kuna vijiji 22 ambavyo mpaka sasa hivi havina Watendaji wa Kijiji walioajiriwa, wako wanaokaimu tena wengine wamekaimu kwa miaka mingi. Ni lini sasa Serikali inakwenda kuipatia Halmashauri ya Wilaya ya Longido kibali cha kuajiri Watendaji hao ili kuziba pengo lililopo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, naomba kupata majibu kwamba kwa kuwa katika baadhi ya zahanati tulizonazo katika Wilaya yangu ya Longido na vituo vya afya na kuna vingine viko mbioni kukamilishwa kama kile cha Kimokorwa, Engarenaibo na kadhalika ambavyo vinajengwa kwa nguvu za wananchi na naamini Serikali mwaka huu watatupatia bajeti ya kuvimalizia. Pia Hospitali ya Wilaya ambayo nayo imeanza kujengwa na inakwenda kasi na hata Siha nimeona Hospitali ya Wilaya ambayo imejengwa jumba la ghorofa linakalibia kukamilika.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba watumishi watapatikana ili facility hizi ziweze kutoa huduma shahiki kwa Watanzania? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza yote kwa pamoja ya Mheshimiwa Mbunge Kiruswa wa Longido, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana kwa pongezi, nazipokea, aendelee tu kuniombea kwa Mungu ili nisiwaangushe Watanzania wote na Mheshimiwa Rais mwenyewe. Pia na yeye binafsi nimpongeze kwa kazi nzuri ambayo anaifanya kwenye Jimbo lake la Longido hususani katika kufuatilia huduma zinazotolewa na watumishi wa umma kwa wapiga kura wake wa Jimbo la Longido.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu tu kwa ufupi na kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nafasi zote za kukaimu; kwanza kukaimu ni nafasi ya muda, wala siyo ya kuthibitishwa. Naomba niwaeleze Watanzania wote kwa faida ya wengine, kwa sababu kuna wengine huwa wanafikiri kwamba ukipewa nafasi ya kukaimu, basi ndiyo leeway yako ya kuthibitishwa, hapana. Kukaimu unakaimu kwa muda na mara nyingi watu wengi wamekuwa wakikaimu kwa muda mrefu kwa sababu watu wamekuwa wakikaimishwa kienyeji bila kufuata utaratibu. Utaratibu ni kwamba unapotaka kumkaimisha kiongozi yeyote yule ambaye ameshafikia katika ile level ambayo tunaita superlative substansive post (nafasi ya uongozi) basi unatakiwa kupata kibali kutoka utumishi. Utumishi wakupatie kibali.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mwaka 2018 mwezi Septemba, Serikali yetu imetoa waraka kwamba nafasi zote zile za kukaimu zisizidi miezi sita. Unapotaka yule Afisa aendelee kukaimu, basi unatakiwa utoe sababu nyingine wewe kama Mwajiri kwa nini unataka aendelee kukaimu? Hiyo yote ni katika lengo la kuboresha ili viongozi wetu wasiwe wanakaimu kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, kwenye jibu langu la msingi nimesema katika Jimbo lake la Longido tumetoa vibali na nafasi za ajira 177. Katika hizo 177, 65 zinakwenda katika Sekta ya Afya, 69 zinakwenda katika Sekta ya Elimu na zinazobaki nyingine zote zinakwenda katika kada nyingine mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika zile kada nyingine ambazo ni za kimuundo, zenyewe hazihitaji kukaimishwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge mwaka huu wa Fedha 2018/2019, hizi nafasi 177 tutakuwa tumeshazijaza katika Wilaya ya Longido hususan Jimbo lako.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri, Mwanjelwa kwa majibu mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongeze jibu kwenye swali linalohusiana na Watendaji wa Serikali za Mitaa. Hii hoja ya Mheshimiwa Mbunge wa Longido ni kweli, lakini naomba niseme tu kwamba kupata Watendaji kwenye ngazi za Halmashauri na huu ni mwaka wa bajeti kwenye Bunge hili Tukufu, tunatarajia Wakurugenzi ambao ndio waajiri wa watu hawa, Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Mitaa watakuwa wameingiza kwenye bajeti zao ili tupitishe na waweze kupata ajira. Kwa hiyo, Wakurugenzi wanapaswa kujua upungufu wa maeneo yao ya kiutendaji, kama wakiwasiliana na Ofisi ya TAMISEMI kwamba hawa watu wanafanya kazi kubwa sana waweze kusaidiwa utendaji katika ngazi ya chini. Ahsante.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona na kunipa fursa niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa moja ya changamoto za maendeleo vijijini ni ukosefu wa barabara zinazopitika na kwa kuwa TARURA imeundwa ili ku-address changamoto hiyo. Kwa kuwa katika Wilaya nyingi nchini, TARURA haina mitambo ya kutengeneza au hata kufungua hizo barabara vijijini ikiwemo Wilaya ya Longido. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba Wilaya zote ambazo TARURA haina mitambo ya kufanyia kazi wanapata mitambo hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, niseme kweli tumekuwa na chombo hiki TARURA na imeanza kufanya kazi vizuri na Waheshimiwa Wabunge watakuwa mashahidi. Yako maeneo ambayo yalikuwa na changamoto kipindi cha nyuma sasa yanafayiwa kazi vizuri. TARURA watasimamia shughuli za ujenzi wa barabara za vijijini kama wanavyosimamia TANROADS, kwa maana hiyo wakipata fedha uko utaratibu wa kutangaza, tunapata wazabuni, wakandarasi mbalimbali wanakwenda kufanya matengenezo ya barabara kwa utaratibu ule ule kulingana na Sheria za Manunuzi.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi na TARURA wamefanya kazi nzuri na kwa muda mfupi wameshazitambua barabara zote na kuziingiza kwenye mfumo kwa sababu kulikuwa na changamoto ya barabara zingine ambazo zilikuwa hazitambuliki. Hivi karibuni wamepita karibu maeneo yote nchini kufanya sasa uhakiki kuona kama kuna sehemu barabara ilisahaulika iweze kuingia katika mtandao wa barabara.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba eneo la Longido ni sehemu ambayo pia TARURA wamefanya kazi ya kutambua barabara. Kama nilivyosema ni kazi yetu sisi Bunge tukiwapa fedha za kutosha ninaamini barabara zote zitaboreshwa kulingana na changamoto zilizoko katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Ahsante sana.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Naomba kuuliza kuhusu watumishi waliochishwa kazi kwenye hili zoezi wenye vyeti vya Darasa la Saba wakaenda chuo; kwa mfano kuna waliokwenda Chuo cha Simanjiro cha Mifugo wakapata vyeti, waka- perform vizuri wakaenda kusoma Diploma ya Udaktari wa Mifugo katika chuo cha Serikali kule Tengeru, lakini baada ya zoezi kupita walipogundulika tu kwamba hawana cheti cha form four – lakini hawajadanganya – wakaachishwa kazi.

Je, Serikali inaweza kutoa tamko gani kuhusu hawa ambao wanaona kwamba wameonewa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza lazima tukumbuke kwamba tarehe 20 Mei, 2004, baada ya hapo wale wote ambao walikuwa wametoa taarifa zisizo sahihi tulitoa msamaha hadi tarehe 31 Desemba, 2017 kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi na wale wote waliojiendeleza, kwa mfano katika masuala ya recategorization.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme, Serikali tunasisitiza, tunathamini, tunaheshimu recategorization kwa wale wote wanaojiendeleza kimasomo. Nimesema kwamba hadi hiyo tarehe 31 Desemba, 2017 kama walijiendeleza na vyeti vyao viko sahihi, watuletee Utumishi tutahakiki watarejeshwa kazini. Ahsante.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, naomba sasa niulize maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa moja ya chimbuko la migogoro ya mipaka katika vijiji vyetu ni kutokuwepo kwa alama imara na zinazoonekana kati ya mipaka iliyobainishwa kati ya Kijiji na Kijiji, Kata na Kata, Tarafa na Tarafa mpaka hata Wilaya na Wilaya:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakiki kuweka alama madhubuti na kutengeneza ramani zitakazowezesha jamii zenye migogoro ya mipaka kujitambua na kuheshimu mipaka hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa katika Jimbo langu la Longido tuna migogoro michache sugu ambayo imekuwepo tangu Wilaya ya Longido ianzishwe zaidi ya miaka 20 iliyopita, ambayo ni mpaka wa Kijiji cha Wosiwosi Kata ya Gilailumbwa na Kata ya Matali Kijiji cha Matali ‘B’ na mpaka huo huo ulio Kaskazini mwa ziwa Natron una mgogoro na eneo la Ngorongoro ambapo Kitongoji cha Ilbilin kimevamiwa na wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro na kuanzisha vituo vyao vya kudumu pamoja na eneo la Engaruka na sehemu ya Kitumbeine vijiji vya Sokon na Nadare.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari baada ya Bunge hili kuja katika Jimbo langu atusaidie kutatua migogoro hiyo sugu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.(Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishamkubalia hata kwenye Kamati, huyu ni Mjumbe wa Kamati yangu na ni Mjumbe makini sana na ni mchambuzi mzuri sana wa masuala ya ardhi. Tulishakubaliana kwamba tutatafuta nafasi ikiwezekana kabla ya mwisho wa mwaka huu tufike huko kwenye site ili tuzungumze pamoja na viongozi wenzangu wa Wilaya namna bora ya kukabiliana na hiyo migogoro. Kwa hiyo, Dkt. Kiruswa nitakuja huko kushirikiana ili kuhakikisha hiyo mipaka inatatuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili juu ya alama zinavyoonekana, katika uwekaji wa mipaka ya vijiji na vijiji huwa kunakuwepo na alama. Labda nimjulishe kwamba Seriakli kupitia Wizara ya TAMISEMI ndiyo huwa inatangaza, Mheshimiwa Rais ndiyo huwa anatangaza uanzishwaji wa mamlaka wa WIlaya, Mikoa na Vijiji vinatangazwa kwenye Ofisi ya Rais, kwa hiyo kuna mipaka ambayo huwa inawekwa pamoja na coordinates zinawekwa kwenye GN, zinatangazwa kwenye GN kwamba Wilaya fulani na Wilaya fulani itapakana na alama za msingi huwa zinawekwa kwenye GN na kwenye vijiji tunapopima huwa kunakuwa na alama zinatangazwa na zinawekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kama kuna matatizo ya kutokukubaliana kati ya kijiji na kijiji huko kwenye Wilaya yake nitakwenda lakini alama hizi za vijiji huwa zinawekwa na wanakijiji wanakubaliana ni alama gani na kila tunapopima huwa tunaweka mawe ambayo yanakuwa na alama na namba ambazo zile coordinates ndiyo zinaingizwa kwenye GN inayotangazwa maeneo ya mipaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mawe yale huwa tunaweka, sema labda pengine mawe yale yanafukiwa chini labda yeye angependa yawekwe juu, kwa hiyo kama kuna maeneo ambayo yana mwingiliano mkubwa, tuko tayari kuweka alama zinazoonekana badala ya zile ambazo tunaweka chini. Lakini sehemu kubwa huwa tunaweka alama na zile alama zina namba ambazo huwa zinatangazwa kwenye Gazeti la Serikali. (Makofi)
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona, ili niulize swali la nyongeza kuhusu madini. Sisi katika Wilaya ya Longido tuna madini ya aina ya Ruby, na kuna mgodi wa miaka mingi, unaoitwa Mundarara Ruby Mine na sasa hivi wachimbaji wadogowadogo wameibuka wametokeza baada ya kujua madini haya yana thamani na ninaamini Serikali itakuja kuwajengea uwezo.

Lakini swali langu ni kwamba, huu mgodi ambao ulianzishwa tangu kabla ya uhuru, ni wa nani, na kama ni wa Serikali, Serikali inafaidikaje na huu mgodi na ni asilimia ngapi kama kuna ownership ya joint venture na mwekezaji?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, pale Mundarara, kuna mgodi ambao ni mgodi wa uchimbaji wa Ruby. Mgodi ule kabla, miaka ya 60, ni kwamba mgodi ule ulikuwa ni mali ya Serikali, na sisi tumeweza kufuatilia na tuliunda Tume ili kuona ni namna gani mgodi ule uliweza kuporwa. Nipende tu kusema kwamba tumelifuatilia na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mgodi ule unamilikiwa sehemu na Serikali na kuna kampuni nyingine ambayo ilikuwa inamiliki, lakini mgodi ule mpaka sasa hivi, asilimia 50 tunaumiliki sisi yaani Wizara ya Madini kupitia Shirika la Madini yaani la STAMICO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, mgodi huu ulikuwa na mikiki mingi, ambako Tume tumeituma, tumetuma Tume ya watu maalumu, wafuatilie, watushauri tuone namna gani ya mgodi ule kuurudisha Serikalini au kutafuta namna ya kuweza kuungana na mchimbaji mwingine au mwekezaji mwingine na Serikali iweze kupata mapato yake kupitia shirika la madini la STAMICO.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza kwa Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Spika, natanguliza shukrani zangu za dhati kwa sababu Mheshimiwa Prof. Mbarawa amepambana bega kwa bega nami mpaka yale maji ya Mlima Kilimanjaro yakawafikia wananchi wa Wilaya ya Longido. Sasa hivi ametutengea shilingi bilioni 2.9 kusambaza yale maji na wale wananchi wanaoishi pembezoni mwa bomba watapata maji wao pamoja na mifugo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kilichobaki kuhusiana na mradi huo ni kwamba Mheshimiwa Rais alipokuja Namanga kuzindua mpaka wa pamoja mwezi Februari, 2019 aliwaahidi wananchi kwamba mradi huo kwa sababu unaleta maji mengi mpaka Longido utaongezewa extension ili uwafikie wananchi walioko njiani mpaka Namanga. Je, ahadi hii ya Rais itaanza kutekelezwa lini?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa Rais alitoa ahadi hiyo nasi wakati wote tunatekeleza ahadi za Mheshimiwa Rais pamoja na viongozi wote wa juu. Kazi tunayofanya sasa hivi ni kufanya usanifu kutoa maji kutoka Longido mpaka huko kwenye mpaka wetu wa Namanga. Mara baada ya usanifu huo kumalizika kazi ya ujenzi itaanza mara moja.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kazi hii itaanza mara moja na tumejipanga kuhakikisha kazi hii tutaifanya kwa pesa zetu za ndani na kwa kutumia wataalamu wetu wa ndani. Tunaamini tukifanya hivyo kazi itakamilika haraka iwezekanavyo.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona na kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza kwenye Wizara hii ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, sisi katika Wilaya ya Longido na hata Monduli pia, tumepitiwa na umeme wa msongo mkubwa na napenda kuishukuru Serikali kwa sababu wameshalipa fidia kwa watu wale ambao walistahili kufidiwa, lakini pia naomba kuuliza kwa sababu vijiji vilivyopitiwa katika Wilaya yangu ya Longido ni vitano; Eorendeke, Kimokorwa, Oromomba, Ranchi na Engikaret kuna maeneo mahsusi ambayo jamii iliyatenga kama maeneo ya wazi wakitarajia kwamba fidia yake itakwenda kurudishwa ndani ya kijiji waweze kufanyia miradi ya maendeleo kama kujenga shule, zahanati na kuboresha miundombinu mbalimbali ambayo ni pungufu sana ikiwa ni pamoja na barabara katika vijiji vile.

Mheshimiwa Spika, je, ni lini Wizara itarejesha hizo fedha za maeneo ambayo jamii iliyatenga kama maeneo ya wazi kwa vijiji husika au halmashauri ili tuweze kufanyia hayo maendeleo ambayo tayari wananchi wameshabainisha? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa na nimpongeze kwa kufuatilia masuala ya nishati hususan fidia ya wananchi wake.

Mheshimiwa Spika, ni kweli maeneo aliyoyataja ikiwemo Wilaya ya Longido yamepitiwa na njia ya msongo wa KV 400 kutoka Singida – Namanga na tumeshalipa fidia takribani kama shilingi bilioni 44 na maeneo aliyosema ambayo yalikuwa ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za jamii, thamani yake ya fidia ni kama shilingi bilioni 10, utaratibu unaendelea wa kuweza kuyalipa katika maeneo mbalimbali ili pesa hizo ziweze kuchangia shughuli za maendeleo, nakushukuru.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza.

Pia naomba nitumie nafasi hii kuiomba Wizara ya Mifugo kabla sijauliza maswali yangu waje wakutane na wadau wa mifugo na wafanyabiashara katika Wilaya yangu ya Longido waweze kutathmini matokeo chanya na matokeo hasi ya operesheni hii ambayo imeingizia Serikali fedha nyingi tu ambazo swali langu la kwanza ninaomba kufahamu kwamba kati ya fedha hizi ambazo zimepatikana ni miradi gani ya maendeleo katika sekta ya mifugo ambayo ama imetekelezwa au imepangwa kutekelezwa ili wafugaji hawa waone tija ya fedha hizi zinapoingia Serikalini?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, ninapenda kufahamu pamoja na changamoto ya hawa wanaosimamia operesheni ambao wamedhulumu watu ambao wamekamatiwa mifugo bila kuwa na hatia na wengine wenye hatia waliofilisika, lakini na wao kwa taarifa yangu hawajalipwa stahiki zao. Ni lini Serikali itakwenda kuwalipa stahiki zao kwa kazi kubwa waliyofanya?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa
Spika, Mheshimiwa Mbunge kwanza amehitaji kufahamu ni miradi kiasi gani ambayo imetekelezwa kupitia fedha hizi ambazo tunazikusanya.

Mheshimiwa Spika, sisi Wizara yetu katika Vote ya 99 ambayo tunapangiwa Bunge hili tukufu bajeti yetu ya maendeleo ni shilingi bilioni 5.6 lakini katika hizo bajeti shilingi bilioni 5.6 tunakarabati minada, tunarekebisho majosho, mfano kwenye bajeti kiasi cha majosho 75 kwa Halmashauri nchini zinakarabatiwa, lakini majosho 20 yanajengwa kwa shilingi milioni 500, lakini pia tunajenga kiwanda cha chanjo pale Kibaha TVLA zaidi ya shilingi milioni 600.

Mheshimiwa Spika, fedha tunapopangiwa na Serikali kila Wizara na sisi tunapopokea na kwa mwaka huu wa fedha shilingi bilioni tano zinaendelea kurudi kwa wafugaji wetu kwa kukarabati miundombinu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge amependa kufahamu swali lake la pili kwamba watumishi hao wanaofanya operesheni wanakuwa wanafanya kwa awamu mbalimbali, lakini wanahitaji malipo. Serikali imekuwa ikiwalipa watumishi hao ambao wamekuwa wakifanya operesheni ya kudhibiti utoroshwaji wa mifugo na madeni yao yameshapunguzwa, sasa watumishi hao kote nchini wanadai shilingi milioni 662.9 na hizo fedha zimeshakaguliwa Mheshimiwa Mbunge, hivi karibuni mchambuzi ukishakamilika Wizara ya Fedha watalipa fedha hizo.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza na linakwenda kabisa sambamba na tatizo alilonalo Mheshimiwa Sanga kule Kitulo. Zoezi la uwekaji mipaka ya Hifadhi za Taifa na maeneo ya jamii halikuwa shirikishi kabisa katika Jimbo langu la Longido katika eneo linalotutenga na Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro. Kuna eneo la buffer zone la hekta 5,000 ambazo lilitengwa tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza kwamba liwe ni eneo la buffer zone lakini matumizi yaliyoruhusiwa ni kuchunga tu. Hivi leo baada ya beacon kuwekwa bila kuwashirikisha wananchi wanaanza kupelekeshwa kuchungia katika buffer zone. Naomba kuiuliza Wizara, je, wako tayari kutoa tamko kwamba eneo la buffer zone katika ukanda wa msitu wa Mlima Kilimanjaro na Hifadhi ya Taifa zina access ya wachunga mifugo wa Longido na Siha kuchungia?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, maeneo ya buffer zone yana miongozo yake na Wizara itaangalia kama inaruhusu kutumika kwa shughuli zingine. Hata hivyo, kwa sababu Kamati ya Mawaziri ilishafanya maamuzi ikapitia baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa na migogoro na maamuzi hayo tunatarajia kwamba yataanza kutekelezwa baada ya Bunge lako hili Tukufu, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba awe na subira tumalize Bunge, tuangalie sasa kama yale maeneo anayoyasema yeye yatakuwa ndani ya maamuzi ya Kamati ya Mawaziri ambavyo vijiji 920 tayari vitakuwa vimefaidika na maeneo hayo. Kama kitakuwa hakimo basi Wizara itaendelea kushirikiana naye kuangalia ni kitu gani ambacho tunaweza kufanya ili tusiweze kuathiri maeneo ya machunga (malisho) na kwenye maeneo ya hifadhi.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa elimu ya vyuo vya kati na vya chini ni kiungo muhimu katika ujenzi wa uchumi na kupunguza umaskini nchini. Kwa kuwa watoto wengi wanaosoma katika hivi vyuo vya chini ni wa maskini. Je, Serikali ina mpango gani wa ku-extend ule Mfuko wa Mikopo wa Elimu ya Juu ili hawa watoto wa maskini wanaotaka elimu katika vyuo vya chini waweze kupata mikopo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumekuwa na utaratibu wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu lakini siyo hawa wa level ya elimu ya kati. Tukiangalia gharama za vyuo hivi kwa mwaka, Serikali inachangia au inagharamia kwa kiasi kikubwa sana. Kwa Vyuo vyetu vya FDC ada yake ni Sh.250,000/= kwa wanafunzi wale wanaokaa bweni na Sh.145,000/= kwa wanafunzi wa kutwa lakini kwa vyuo vyetu vya VETA, vina gharama ya Sh.120,000/= kwa wale wanafunzi wa boarding na Sh.60,000/= kwa wale wanafunzi ambao wako day. Hata hivyo, tunarudi pale pale kulingana na wigo na bajeti ilivyo, nadhani Serikali tutaangalia kitu gani cha kufanya lakini mpaka hivi sasa Serikali inatoa ruzuku ya kutosha kabisa kuhakikisha kwamba vyuo hivi vinakwenda na kuwapunguzia mzigo wananchi wa kulipa gharama hizi kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa ajira ya mwisho ya watumishi wa vituo vya afya na zahanati iliyotoka iliwachukua baadhi ya watabibu waliokuwa wanafanya kazi kwa mkataba na wengi walipoomba zile ajira walikuwa na nafasi ya kuomba kwamba wabaki wapi. Katika Wilaya yangu ya Longido kuna mmoja aliyekuwa anahudumia zahanati ya Kijiji cha Nondoto ambayo ndio inahudumia kata nzima hakuna nyingine alipoomba kubaki pale alipangiwa kwenda Mtwara. Je, Serikali ina mpango gani wa kuipatia zahanati hiyo mganga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa Mbunge wa Longido kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika ajira watumishi ambao wanaomba kuajiriwa na Serikali wanakuwa na option ya kuchagua vituo ambavyo wanakwenda kufanya kazi. Na katika mfumo wa ajira za hivi karibuni ambazo zimefanyika mwezi Mei mpaka Juni watumishi wote wamepangiwa kwenye vituo ambavyo waliomba kupitia mfumo wa kieletroniki wa ajira kwenda kufanya kazi katika vituo hivyo. Na watumishi wote wamepelekwa kwenye vituo ambavyo waliomba kwenda kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge inawezekana tulimwitaji sana mganga huyu katika kituo hicho lakini uchaguzi wake aliomba kituo kingine na ndio maana amepelekwa. Lakini jambo la msingi ni kupata mganga katika zahanati ile na mimi nimelichukua hili tutalifanyia kazi ili kuhakikisha tunapata mganga kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma katika zahanati ambayo Mheshimiwa Mbunge ametaja, nakushukuru.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, lakini kabla sijauliza, niseme tu kwamba sijapata majibu kamili ya swali langu kwa sababu nilitaka kujua kwamba elimu ya viziwi itatolewa lini kwa wanafunzi wote wa shule zetu nchini ili kuweza kuondoa hicho kizingiti cha mawasiliano; lakini naona mjibu swali, Serikali inaonekana ina-focus katika kutengeneza mtaala wa kuboresha elimu kwa wale ambao ni viziwi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo naomba niulize maswali haya madogo ya nyongeza; swali la kwanza;

Je, katika nchi yetu tuna shule ngapi zinazotoa elimu kwa viziwi kwenye ngazi ya Msingi, Sekondari na Vyuo?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili ningependa kujua kwamba kwa kuwa katika nchi yetu lugha rasmi zilizo, zinazotumika kwa mawasiliano ni Kiswahili lugha yetu ya taifa nani ya kimataifa pia na kingereza; nikitaka kupata kitabu au Mtanzania akitaka kupata kitabu cha sign language kwa kiingereza na sign language ya Kiswahili atavipata wapi? Ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Kiruswa katika nchi nyingine wanafundisha hivyo compulsory kwa wanafunzi wote kusoma lugha ya alama?

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, kwanza ni-declare interest kwa sababu mimi nimekuwa nikisaidia watoto viziwi kusoma. Nina wachache wanasoma Kenya, nina watatu wanafikia kidato cha nne mwaka huu, na kitabu wanachotumia kinaitwa Kenya Sign Language. Lakini pia nilipokuwa nasoma Marekani nimeona American Sign Language; lakini hapa kwetu nafahamu shule moja ya msingi ambayo inasomesha viziwi iko Moshi -Kilimanjaro - Himo na wale wanasoma kwa Kiswahili. Sasa kunakuwa na crush, kwamba wale watoto walioko Kenya wakija wakikutana na hawa viziwi walioko Tanzania wengine wanaongea sign language ya Kiswahili lakini wenzao wanaongea sign language ya kiingereza. Sasa nilikuwa nataka kujua jinsi ambavyo tungeweza kuwa na hivyo vitabu vya sign language…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana, haya ahsante.

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: …katika lugha hizo ili tuweze kutoa hiyo…

SPIKA: Haya, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri eneo hili nyinyi ndio wataalam, majibu tafadhali Mheshimiwa Juma Kipanga. (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Kiruswa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ameuliza suala la shule maalum mahsusi kwaajili ya wanafunzi wetu hawa wenye ulemavu wa usikivu. Tuna shule za msingi 14 ambazo ni mahsusi kabisa kwa ajili ya wanafunzi wetu hawa ambao wana matatizo ya usikivu. Pia shule za sekondari zipo 25, lakini vile vile tunachuo cha ualimu maalum kabisa ambacho kiko Patandi.

Mheshimiwa Spika, katika majibu yangu ya swali la msingi nilizungumza kwamba hivi sasa tunaboresha au tuko kwenye mikakati ya kuhakikisha kwamba tunakwenda kutoa elimu hiyo kama alivyoshauri Mheshimiwa Mbunge, kuanzia ngazi ya elimu msingi mpaka chuo. Lakini katika muktadha wa vitabu nimezungumza katika majibu ya msingi kwamba tumetunga kamusi ambayo inatumia hiyo lugha ya alama.

Mheshimiwa Spika, lakini wanafunzi hawa jukumu letu kubwa sana ni kuhakikisha kwamba tunapata walimu wa kufundisha lugha hizi za alama. Kwa upande wa vitabu, vitabu vinavyotumika ni vitabu vya kawaida kabisa kwa sababu wao wanaweza kuona suala lililokuwepo ni namna gani ni kuweza kufundishwa au kufundishika. Kwa hiyo jukumu letu tunaoenda nalo hivi sasa ni kuhakikisha kwamba tunatengeneza walimu wa kutosha wa kuweza kutumia lugha ya alama; na katika chuo chetu kikuu cha Dar es Salaam sasa tunatoa stashahada ya mwaka mmoja katika kipengele hiki cha lugha ya alama ili kuhakikisha kwamba tunapata walimu wa kutosha wakuweza kufanya service delivery na kutoa elimu hii kwa wanafunzi wetu hawa. Ahsante.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Nitumie fursa hii kumwomba Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba maji ya Ngaresero hayataweza kufika katika Wilaya ya Longido, kwa hiyo, nafikiri kuna haja ya kurekebisha hapo. Hata hivyo, nashukuru kwa jitihada ambazo Serikali inaenda kufanya katika kutupatia maji kwa gharama yoyote, iwe ni mabwawa au chemichemi ama chanzo chochote cha maji salama katika eneo la Wilaya ya Longido.

Mheshimiwa Spika, naomba tu kutumia fursa hii kuikumbusha Serikali kwamba, kuna ahadi ambayo imerudiwa tena na tena ya kutoa tawi la maji ya Mto Simba ambayo yamekwenda mpaka Mjini Longido na sasa hivi yanaelekea Namanga. Naiomba sana Serikali Kijiji cha Eilarai eneo la Motong’ wapate maji maana ni Kijiji cha kwanza kilichopitiwa na bomba hilo kubwa na wananchi wale wameendelea kunikumbusha kwamba ahadi imetolewa na Mawaziri watatu hadi sasa; Mheshimiwa Waziri Mbarawa, Mheshimiwa Waziri Kamwelwe na huyu aliyeko sasa hivi wakati ule akiwa Naibu Waziri. Kwa hiyo, ni lini Serikali itakwenda kuwapelekea watu wa Imotong’ maji safi na salama ya Mto Simba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kuhusu maji ya Mto Simba, ni mpango mkakati wa Wizara kwenda kutumia mito, maziwa na vyanzo vyote vya maji kuhakikisha maeneo yote tunayafikia. Kwa upande wa Longido, Mheshimiwa Mbunge tuna mpango wa kuendelea kuona chanzo hiki cha maji cha Mto Simba kinakwenda kutumika katika mwaka wa ujao wa fedha.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, ndiyo, ndiyo kabisa!

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na nitumie fursa hii kuiasa Wizara ya Maliasili na Utalii kwamba wanapofanya kila jitihada kuzuia mifugo isiingie ndani ya hifadhi hawafanyi juhudi kuzuia wanyama wasiingie ndani ya maeneo ya jamii.

Mheshimiwa Spika, kwa taarifa hiyo watambue pia kwamba mifugo na wanyamapori wote ni wanyama kuna maeneo ambayo wanaingiliana vizuri kiasi kwamba hata ningependekeza kwamba maeneo ambayo hamna wanyamapori kama misitu asili mifugo waruhusiwe kulisha kwasababu wanatengeneza mazingira ya ekolojia ya majani katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, swali langu ni kwamba kwa vile kuna hako kafuta jasho au kifuta machozi hawa wanyama wanapoingilia katika maeneo ya jamii.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba hicho kifuta machozi au kifuta jasho kinawahishwa kwasababu kuna tabia ya kuiweka mpaka hata mtu anakuja kupewa ameshasahau na maumivu aliyoyapata?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ni kweli wananchi wanapokutana na adha hii ya tembo kuingia kwenye mashamba yao Wizara ya Maliasili na Utalii ina utamaduni wa kulipa kifuta jasho, na kifuta jasho kinategemea ni aina gani ya uharibifu uliofanyika.

Mheshimiwa Spika, kuna waliopata adha ya kupoteza maisha, lakini kuna wale ambao wamepoteza mazao huwa tunafanya tathmini pale tu ambapo tembo wanakuwa wameingia kwenye maeneo hayo na baada ya kufanya tathmini basi Serikali huwa inachukua jukumu la kulipa kifuta jasho.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu wa fedha tumetenga bilioni mbili kwa ajili ya kulipa kifuta jasho. Nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kifuta jasho cha aina yoyote ambacho kinatokana na uvamizi wa tembo Serikali itakilipa ahsante.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulizwe swali la nyongeza kwenye Wizara hii ya Maji.

Kwa kuwa Wilaya ya Longido ni moja ya wilaya kame sana nchini na kwa kuwa tuna baadhi ya milima ambayo inavyanzo vya chemchem kwenye misitu ya Serikali kama mlima Gilay, Mlima Kitumbeine, Mlima Longido na chemchem iliyopo matali A na chemchem zinazotoka upande wa West Kilimanjaro Kata za Ormololi na Kamwanga na kuna mabonde ambayo yangeweza kuchimba mabwawa pamoja na visima kirefu... (Makofi)

NAIBU SPIKA: Swali Mheshimiwa.

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, Je, Serikali ina mpango kusaidia kumaliza kero ya maji kwa wananchi wa Jimbo la Longido.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali ni kuona kwamba maeneo yote ambayo yana matatizo ya maji tunakwenda kuyashughulikia. Mheshimiwa Dkt. Steven tumekuwa tukiwasiliana kwa karibu na nampongeza sana kwa ufuatiliaji wake wa karibu wa suala hili. Nachoweza kumhakikishia kama tulivyozungumza, Kijiji cha Opkeli, Kata ya Mundarata; Kijiji cha Ogira, Kitongoji cha Ingokin, maeneo haya yote tunakwenda kuyashughulikia. Lengo ni kuona maeneo yale yote maji yanakwenda kutoka bombani iwe kwa chanzo cha maji cha kisima ama chanzo kingine cha maji.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Nami naomba kuuliza swali dogo la nyongeza kuhusiana na ahadi ya Serikali ya kupeleka matawi ya maji katika vijiji vilivyopo pembezoni mwa bomba kubwa la maji safi na salama yaliyotoka katika mto simba Mlimani Kilimanjaro kwenda Longido na vijiji hivyo ni Eliarai hasa Kitongoji cha Himotong, Tingatinga, Ngareiyani na Sinya?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge. Kiukweli historia kubwa ambayo umeiacha Longido ni juu ya ule mradi wa shilingi bilioni 16 ambao tumeutekeleza katika Jimbo lako.

Kwa hiyo, eneo lile ambalo limepitwa na bomba kuu vijiji upande wa kulia wa bomba kuu na kushoto, zaidi ya kilometa 12 navyo tutavipatia huduma za maji safi na salama. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Kabla sijauliza maswali yangu, naomba tu niweke wazi kwamba sijaridhishwa na majibu ya Serikali kwa swali langu kwa sababu nilitegemea kwamba nitapewa mchanganuo wa hii bilioni 11.33 kwa kuonesha katika kila kijiji ni watu wangapi wamefidiwa kiasi gani na kiasi gani kimekwenda kwenye maendeleo ya vijiji husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini haiishii hapo Kijiji hiki cha Engikaret mahesabu yake hayapo katika jibu moja kwa moja. Ukiangalia hiyo bilioni 11.33 kwa mchanganuo uliotolewa inaonesha ni shilingi bilioni 1.669 tu ndiyo imefika na hiyo bilioni 9.660 sijaelewa kwamba mahesabu yake yamekwenda wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo swali langu la kwanza la nyongeza ni kuhusu kijiji cha Engikaret. Kwa kuwa, kulikuwa na wananchi 46 ambao walileta malalamiko yao kwamba wako kwenye njia ya umeme na wakaenda wakafanyiwa tathmini na kuna wengine 66 waliletwa hivi karibuni.

Je, watu hawa ambao kwa ujumla wao sasa ni zaidi ya watu 112 watalipwa lini hiyo fidia?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuna umeme ambao ulielekezwa Tarafa ya Ketundeine, umeme wa REA ukifanywa na kampuni yetu ya TANESCO. Kasi ya umeme huo ni ndogo sana na tulitegemea mwezi Julai mwaka jana ungewashwa katika vijiji 10 vya awali kwenye Tarafa hiyo yenye vijiji 19. Je, umeme huu wa Ketundeine utakamilishwa lini? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Steven, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji mkubwa ambao ameendelea kuufanya katika eneo lake. Niseme tu kwamba huo mchanganuo aliousema wa item moja moja kwa ajili ya wananchi baada ya hapa nitauagiza utengenezwe na nitaweza kumpatia kwa ajili ya kuona nani amelipwa nini ili aweze kuwasemea wananchi wake vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika eneo la malipo nieleze tu kwamba tulipata changamoto kidogo. Katika kijiji cha Engikaret tulivyofanya tathmini mara ya kwanza ilionekana kwamba ni eneo la kijiji lakini wakati pesa imekwenda kulipwa wakaja wananchi wengine takriban 40 na zaidi wakasema wana haki katika eneo hilo na sisi tukawafanyia tathmini kutoka kwenye ile ya kijiji ili wao walipwe. Kabla ya pesa ile haijalipwa wakajitokeza wananchi wengine zaidi ya 50 wakiwa na malalamiko hayo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hali hiyo, yakawepo makubaliano kati ya TANESCO na Ofisi ya Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya kwamba kwa kuwa lile eneo lote lilifanyiwa tathmini likiaminika ni la Serikali basi Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Halmashauri zitathmini ni nani anastahili kulipwa nini katika eneo hilo na pesa ile ambayo tayari ipo katika akaunti ya Halmashauri iweze kutumika kwa ajili ya malipo hayo. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, pesa tayari imeshalipwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri na yeye anaendelea na utaratibu wa kuhakiki ni nani anastahili kulipwa kama mmojawapo wa wale ambao wako katika eneo hilo.

Katika swali la nyongeza la pili, ni kweli kwamba mradi huo wa vijiji 19 umechelewa. Tulikubaliana na mkandarasi ukamilike kabla ya mwezi Juni mwaka huu na siku siyo nyingi Mheshimiwa Waziri wa Nishati atakuja kuzindua mradi huo kabla ya Mwaka huu wa Fedha kuisha.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo mawili ya nyongeza, lakini pia nitumie fursa hii kuishauri Serikali kwamba, kwa kuwa barabara zetu za vijijini haziachi kuharibiwa na mvua kila wakati, nashauri kila Wilaya ambayo haina mtambo wa kutengeneza barabara, wapewe mtambo ili kuweza kunusuru barabara hizi badala ya kungojea makandarasi wapatikane ndipo barabara zifanyiwe repair? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza. Kuna mkandarasi anaitwa Balcon Construction Tanzania Ltd. ambaye amepewa contract ya shilingi 115,357,520/= kutengeneza barabara ya kwenda Kitongoji cha Esokonem mlimani Gelai kwenye Kata ya Gelailumbwa, ambaye ametelekeza barabara, baada ya kuiharibu barabara hiyo ambayo imetengenezwa kwa nguvu ya wananchi na kutifua mawe makubwa kiasi kwamba haipitiki tena. Tangu mwezi wa Kumi na Moja mwaka 2020 barabara hiyo imesimama, haipitiki. Naomba Serikali iseme neno kuhusu hilo: Je. Serikali itamchukulia hatua gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kuna barabara za mitaa ya Mji Mdogo wa Longido na ambazo zilikuwa ni sehemu ya ahadi ya Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, kutoka pale kwa DC kwenda Makao Makuu ya wakazi wa Halmashauri ya Longido, ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami na tangu mwezi wa Kumi na Moja mwaka 2020 kazi imesimama kwa sababu mkandarasi hajalipwa certificate ambayo amewasilisha; je, Serikali itatimiza lini takwa lake la kumlipa mkandarasi huyo ili kazi imalizike? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amejaribu kuitaka Serikali tueleze ni hatua gani tutachukua kwa Mkandarasi ambaye ameitelekeza barabara aliyoitaja iliyopo jimboni kwake. Kwa kuwa taarifa hizi ndio nazipata hapa, naomba niiagize TARURA Makao Makuu kwa kushirikiana na Mkoa wa Arusha waweze kutuletea taarifa haraka iwezekanavyo ili sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI tujue ni hatua gani tutachukua. Endapo itabainika kwamba Mkandarasi huyo ametelekeza barabara basi tutamnyang’anya hiyo contract na tutatangaza upya ili tupate mkandarasi mwingine atakayemalizia hiyo barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ahadi ambayo ilitolewa na Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ya barabara kutoka DC kwenda Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Longido eneo hilo ambalo ametaja Mheshimiwa Mbunge, kazi hiyo imesimama na amesema sababu ya kusimama ni yule Mkandarasi kutokulipwa fedha. Naomba hili nilifuatilie ili tuone ni hatua gani ambazo ofisi zetu zimekuwa zinachukua kwa sababu mpaka Mkandarasi labda hajalipwa maana yake kutakuwa labda wana-process zile certificates ambazo amekuwa amezileta katika Ofisi ya Rais TAMISEMI. Kwa hiyo naomba nilifuatilie ili tuweze kui-fast truck na kuirahisisha ili waweze kulipwa na hiyo barabara iweze kukamilika. Ahsante sana.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa katika baadhi ya shule zetu za sekondari zilizoanzishwa kabla ya Serikali kuweka mkazo kwamba, lazima shule kabla haijasajiliwa iwe na maabara, kuna shule chache zimebaki zikiwa hazina maabara kabisa kama Shule ya Flamingo iliyoko katika Wilaya ya Longido, Tarafa ya Ketumbeine, Kata ya Meirugoi. Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga fedha za kutosha, ili kila shule ya kata iwe na maabara ukizingatia kwamba, sayansi ni muhimu? Pia wananchi wanajitahidi kuchanga, lakini bajeti ya TAMISEMI imetoa 25,000/= tu kama umaliziaji wa maabara ambazo zimeshafikia hatua ya juu; hii ambayo haina kabisa Serikali ina mpango gani kutusaidia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anataka kufahamu upi niseme ni mkakati wa Serikali wa kuhakikisha katika zile shule zote, yaani ikiwemo Shule yake ya Flamingo iliyopo katika jimbo lake, ambazo hazina maabara tunazikamilisha. Moja ya mpango wetu na ndio maana katika bajeti mtaona kabisa tumetenga fedha, moja kwa ajili ya kuhakikisha tunamalizia maabara zote ambazo wananchi walikuwa wamezianzisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tumezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha katika yale maeneo ambayo kuna shule za sekondari za kata ambazo hazina maabara zinaanzisha ujenzi, ili sisi tuweze kuongezea fedha. Kwa hiyo, moja ya huo mkakati ni pamoja na kumalizia katika sekondari ya Mheshimiwa Mbunge. Kwa hiyo, nimhakikishie kabisa kwamba, hata hiyo Sekondari ya Flamingo itakuwa na maabara, tutapeleka vifaa na watoto watasoma sayansi kwa vitendo. Ahsante.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuna uhaba mkubwa wa walimu nchini na Serikali imekuwa inawaajiri kwa awamu kidogo kidogo na bado pengo ni kubwa, imebidi shule nyingi zitumie walimu wa kujitolea na ajira zinapotangazwa unakuta mwalimu aliyejitolea amepangiwa kwenda shule mbali na ile aliyojitolea.

Je, Serikali haioni sasa ni muhimu wale walimu wote waliojitolea na walimu wale wakuu wamewapendekeza kwamba ikitokea ajira waajiriwe palepale walipojitolea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kiruswa, Mbunge wa Longido kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tungetamani walimu wote ambao wanajitolea katika maeneo yao husika wapangiwe maeneo hayo lakini bahati mbaya inatokana na ule uhaba ambao unatokana. Kwa mfano kama sasa hivi tuliomba taarifa za walimu wote wanaojitolea mashuleni tukaletewa nafasi walimu wanaojitolea 70,000 na nafasi ambazo zimetangazwa na Serikali ni 6,000 kwa hiyo nafikiri unaweza kuona ni changamoto kiasi gani tunapitia katika kukabiliana na janga hili.

Mheshimiwa Spika, Serikali bado ina nia njema kuhakikisha kwamba itaendelea kuajiri walimu kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha na bajeti ambayo tutakuwa tunajipangia na kila mwaka tutakuwa tunaendelea kufanya hivyo walau kuhakikisha kwamba tuna accommodate hili ambalo Mheshimiwa Mbunge amelieleza. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Kiruswa kwa swali lake la nyongeza kwa nini tusiajiri walimu ambao wanajitolea. Ni kweli kigezo kikubwa ambacho tutakitumia katika kuangalia wenye vigezo ni wale ambao wanajitolea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka kukiri sasa hivi yapo malalamiko hata hao wanaojitolea kuna wengine wameleta barua za fake za kusema kwamba wanajitolea wakati hawajitolei. Kwa hiyo, jana tumepokea pia maelekezo yako suala hili ni tete, nafasi ni 6,949 mpaka juzi walioomba wameshafika 89,958. Kwa hiyo, suala hili naomba utuamini Serikali tutatenda haki; hata hao wanaojitolea tutawachambua kama ni kweli wanajitolea.

Mheshimiwa Spika, pia kuna walimu wamemaliza 2012, 2013, 2014, 2015 hawajaajiriwa kwa hiyo upo pia mtazamo ndani ya Wizara labda tuangalie hawa ambao wamemaliza siku nyingi wanajitolea na hawajapata ajira kwa sababu muda wao wa kuajiriwa pia unapungua kwa sababu lazima waajiriwe kabla ya miaka 45. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana uiamini Serikali suala hili ni tete, walioomba wenye vigezo ni wengi, nafasi ni chache lakini tutatenda haki kama ulivyoelekeza bila kubagua dini, kabila, jinsia wala upendeleo wa nafasi yoyote. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa Serikali ilianza ujenzi wa barabara ya lami inayotoka Sanya Juu kwenda Kamwanga ambapo ingeungana na nyingine inayotoka Rombo kuja mpaka Kamwanga na barabara hii imesimama ujenzi wake pale Kijiji cha Elerai wakati zimebaki zimebaki kilometa 42.8 tu kukamilika.

Naomba kufahamu Serikali itaendeleza lini ujenzi wa barabara hii ambayo sasa ni mwaka wa pili tangu isimame?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Kiruswa, Mbunge wa Longido kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ni kati ya barabara ambazo zimeainishwa kwenye bajeti yetu na kama tulivyoahidi kwenye bajeti zetu tuna uhakika bajeti itakavyoanza kutekelezwa basi itaendelea kutekelezwa kama tulivyoahidi kwenye bajeti yetu ambayo imepitishwa, ahsante.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwanza nitangulize shukrani za pekee kwa sababu Serikali yetu imeendelea kutambua umuhimu wa kujenga shule za bweni katika wilaya za wafugaji ambapo kwa wastani mtoto hutembea hadi kilometa 13 kwa siku kufika shuleni.

swali langu la kwanza; kwa kuwa kuna shule kadhaa za bweni kongwe ikiwepo Shule ya Bweni ya Longido ambayo ilikuwepo kabla ya uhuru na ya Keitumbeine, Serikali ina mpango gani wa kuzikarabati shule hizi za msingi ambazo baadhi ya miundombinu yake ni chakavu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa idadi ya watu inaendelea kuongezeka na hizi shule za bweni tulizonazo za msingi zinazidi kuwa ndogo, Serikali ina mpango gani wa kuongeza miundombinu ya madarasa na nyumba za walimu na mabwalo ili watoto waendelee kusoma katika mazingira mazuri na rafiki? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika,
ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kiruswa, Mbunge wa Longido kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la msingi amejaribu kuainisha kwamba mpango upi wa Serikali wa kuhakikisha tunakarabati shule kongwe za msingi nchini. Wakati tunapitisha bajeti yetu moja ya jambo ambalo tulizungumza hapa Bungeni ni kwamba tumeshazitambua shule 726 kongwe zilizojengwa kabla ya uhuru na zile ambazo zilijengwa mara baada ya uhuru ambazo zimechakaa.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali sasa hivi ni kutafuta fedha kuhakikisha kabisa kwamba tunazikarabati shule zote kongwe na ahadi ya Serikali ipo palepale kwamba tutazikarabati ikiwemo Shule ya Msingi ya Longido ambayo Mheshimiwa Mbunge ameieleza.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, mpango mkakati wa Serikali ni upi kutokana na ongezeko la idadi ya watu na linapelekea wanafunzi vilevile kuongezeka hususan katika kujenga mabweni, mabwalo na madarasa ya kisasa. Kama nilivyoeleza awali kwamba na Wabunge wote ni mashahidi katika hili, kwamba sasa hivi Serikali tumekuwa tukijenga au tukikarabati mabweni, madarasa pamoja na miundombinu mingine ambayo inaboresha elimu hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kabisa kwamba bado tuna mipango mingi. Miongoni mwa mipango tuliyonayo sasa hivi, tuna mpango mpya wa shule bora, lakini vilevile tuna mpango wa BEST, SEQUIP na EQUIP. Mipango ipo mingi sana, yote lengo lake ni kuhakikisha kwamba tunaongeza miundombinu mashuleni na kuboresha miundombinu ya elimu nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Wabunge wote waondoe wasiwasi, Serikali ya Awamu ya Sita tutahakikisha tunawafikia wote katika Majimbo yao. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona na naomba nitumie fursa hii pia kukupongeza kwa Kiti hicho ulichokikalia, kwa kweli umekitendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu dogo la nyongeza linahusu ahadi ya muda mrefu sana ya barabara ya lami ambayo iliahidiwa itoke Longido mpaka Siha kuunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Kilimanjaro kutokea Longido ambayo iko kwenye Ilani ya mwaka 2015 mpaka sasa sijajua hatua ya Serikali katika kutekeleza ahadi hiyo imefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyosema kwenye majibu mengine barabara aliyoitaja iko kwenye Ilani na imeahidiwa na viongozi wa Kitaifa. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Kiruswa kwamba ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami utategemea na upatikanaji wa fedha na kadri Serikali tunavyoendelea kupata fedha nataka kukuhakikishia kwamba ni azma ya Serikali kuijenga hiyo barabara ikiwa ni pamoja na kutimizia ahadi za viongozi kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, tuvute tu subira, cha msingi tuendelee kufanya makusanyo ya fedha. Basi tutakapopata, hizo barabara zitajengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Lakini kabla ya maswali yangu niweke hii kumbukumbu kwa usahihi kabisa, kwamba kwanza nashukuru Serikali kwa kutupatia jamii ya Longido maji safi na salama kutoka Mto Simba ambayo mpaka sasa yamekuwa toshelevu katika Mji wa Longido ambako ni Makao Makuu ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru pia kwa sababu kazi inaendelea kuelekea Kimokouwa, Eworendeke na Namanga, na ni mradi ambao bado haujakamilika. Nashukuru pia kwa kuwa imefika Engikaret, lakini bado hayajafikiwa Kiserian na baadhi ya maeneo yaliyokusudiwa kama kitongoji cha Wasinyai na Yambaluwa Yambalua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza la nyongeza. Kwa kuwa mradi huu bado una hayo mapungufu ya kufikisha maji katika maeneo hayo;

Je, ni lini Serikali itakwenda kukamilisha huo mradi wa kufikia maji maeneo yote yaliyolengwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa wananchi waliopitiwa na bomba hilo kutoka kule chanzo chake, waliopo kitongoji cha Emotong, ni kitongoji kikubwa sana ile scheme nyingine inayokwenda mpaka Larang’wa na Kamwanga haipitiki huko kabisa;

Je, ni lini watu wa Emotong, Tingatinga, a Engerian ambao nao waliahidiwa kwamba watapata matawi ya haya maji na bado hawajayapata watapata hayo maji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nami nipende kupokea shukrani zake kwa sababu amekiri kazi kubwa ambayo Wizara tumeendelea kufanya katika jimbo lake; na huo tu ni mwanzo wa mageuzi makubwa ambayo wizara inaendelea kuyafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika kwa miradi hii tunatarajia kadri pesa tunavyoendelea kupata, na mwaka ujao wa fedha tutaendelea kuhakikisha hii miradi inakamilika. Hii ni kwa sababu lengo la Wizara ni kuona kwamba miradi inakamilika na wananchi wanapata maji safi na salama ya kutosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitongoji cha Tingatinga na maeneo hayo mengine vilevile wao pia wapo kwenye Mpango Mkakati wa Wizara kuona nao wao pia wanakwenda kunufaka na maji safi na salama. Hivyo nikutoe hofu Mheshimiwa Mbunge kama ulivyoona kazi imeweza kufanyika kwenye maeneo mengine na maeneo haya pia kazi itakuja kufanyika na maji bombani yatapatikana.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza kwenye suala hili la msingi lililolenga Wizara ya Fedha.

Katika mpaka wa Namanga kuna tatizo kubwa sawa la Tunduma la msongamano wa magari ambayo wakati mwingine huchukua hata zaidi ya siku tatu yakingojea kuwa cleared yaweze kuendelea na safari na adha kubwa inayotokea ni kwamba hakuna miundombinu ya vyoo, mahali pa kuoga wale wanaokaa kwenye malori na wanachafua sana mazingira.

Mheshimiwa Spika, je, Serikali inampango gani wa kuhakikisha kwamba wakati mipango ya kutengeneza maeneo sahihi ya kuengesha haya malori na sisi Longido tuna sehemu TANROADS wametenga zaidi ya hekari 200 na ujenzi unaendelea, wana mpango gani wa kuhakikisha kwamba wananchi wa mipakani hawapati magonjwa ya mlipuko kwa sababu ya msongamano wa magari na hakuna miundombinu ya kijamii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, Mbunge wa Longido kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la nyongeza la Mheshimiwa Mwenisongole, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa wa Jimbo la Longido kwamba Serikali inazifahamu hizo changamoto na tupo kusaidiana na wenzetu, sisi ndiyo tunaojenga vile vituo tunayatambua hayo na tutahakikisha katika mpango wa karibu tunakwenda kuondoa hizo changamoto ikiwa ni pamoja na kujenga hiyo miundombinu ya haraka ili wananchi wasiweze kupata adha ikiwa ni pamoja na kuangalia utaratibu wa kupunguza ile misongamano kwa kujenga barabara na maegesho makubwa ili magari yatakayokuwepo kwenye foleni ni yale tu ambayo yanatakiwa kwenda kwenye Vituo vya Forodha, ahsante.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA Mheshimiwa Naibu Spika, nakuskuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswli madogo mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa barabara hii itakapokamilika itakuwa imekamilisha mzunguko wa Mlima Kilimanjaro kwa barabara ya lami, na hivyo itaongeza na kuchochea kasi ya ukuaji wa utalii wa Mlima Kilimanjaro na hifadhi ya Mlima Kilimanjaro vilevile. Kuna barabara nyengine ambayo ilipendekezwa kwenye ilani tangu mwaka 2015, inayotoka Longido kuja kuungana na hii ya lami katika eneo la Sanya Juu, na barabara hii pia itapita ndani ya Hifadhi ya Jamii ya Indumet.

Je, Serikali imeweka mpango gani wa kuhakikisha kwamba barabara hii ya kuunganisha hiyo Wilaya ya Longido na Mkoa wa Kilimanjaro na maeneo ya hifadhi na uzalishaji wa zao ya West Kilimanjaro inakwenda kujengwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna barabara pia muhimu ya TANROADS inayotoka Longido mpaka Oldonyolengai mlima mwingine wa kitalii na maarufu duniani, pale ambapo itaungana na ile inayotoka Loliondo kuja mpaka Mto wa Mbu.

Je, Serikali itaanza lini kama ilivyo ahidiwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020/2025 kufanya usanifu wa barabara ya lami kwa ajili ya barabara hiyo muhimu kwa biashara ya utalii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ninaomba kujibu swali moja la nyongeza ya Mheshimiwa Kiruswa, muhimu sana kama ifutavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge kwamba wote kwamba ahadi zote ambazo zipo kwenye Ilani ya Uchaguzi za Chama cha Mapinduzi na zile ambazo zinazotolewa na viongozi wakuu wa Serikali zitatekelezwa kama zilivyopangwa, hiyo ni kwa awamu kutokana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa naibu Spika, barabara mbili ambazo umezitaja zote ni muhimu sana, na unapojenga barabara hizi, hii Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi unajua ni Wizara wezeshi, ukijenga barabara pale Mlima Kilimanjaro, utaongeza idadi ya watalii na mapato yataongezeka na utekelezaji wa Ilani utatekelezwa vizuri zaidi.

Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge nikwambie kwamba barabara ya Longido-Sanya Juu itaanza kujengwa kadri tukipata fedha pia Longido Oldonyolengai ambayo umeitaja nayo ni muhimu sana na tutaifanyia kazi, lakini nikupongeze kwa kazi unayoifanya ya kuwasemea wananchi wako wa Jimbo lako, ahsante sana.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali ilishaahidi kujenga shule bora ya mfano ya wasichana katika kila mkoa nchini; na kwa kuwa shule hiyo ya mfano katika Mkoa wa Arusha tulikubaliana kwamba itajengwa katika Jimbo la Longido; na kwa kuwa tulishatenga eneo la kujengwa shule hiyo katika Kata ya Angekahang, ni lini ujenzi wa shule hiyo ya mfano kwa ajili ya wasichana wetu itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mpaka sasa hivi tumeshaainisha maeneo yote 26 ambayo shule hizi zitajengwa baada ya kupata mapendekezo kutoka katika kila mkoa. Kwa hiyo, kinachosubiriwa sasa hivi tu ni fedha itoke na baada ya hapo tutapeleka fedha kwa awamu ya kwanza katika mikoa 10 ambayo tumeainisha mwaka huu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge atupe muda eneo lake halitabadilishwa na kazi hiyo itafanyika kama ambavyo imekusudiwa. Ahsante sana.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo ya nyongeza, lakini kabla sijauliza maswali yangu madogo kuna kumbukumbu naomba kuiweka kwa usahihi kuhusiana na suala zima la ushuru na tozo za minada ya mifugo katika Wilaya ya Longido tulipata heshima kubwa ya kutembelewa na Rais kama wiki mbili zilizopita tarehe 18 na kuna Waandishi wa Habari ama wamempa Rais habari ambayo siyo sahihi, baada ya kufungua kiwanda kikubwa cha nyama ambacho kimezinduliwa kilijengwa na wawekezqji kwa zaidi ya shilingi bilioni 17 akapata taarifa kwamba inazalisha chini ya kiwango kwa sababu Halmashauri ya Wilaya ya Longido inatoza kodi na ushuru mkubwa unaosababisha wafugaji kupeleka mifugo Kenya.

Mheshimiwa Spika, kumbe Halmashauri ya Wilaya ya Longido haijawahi kuchukua hata shilingi katika kile kiwanda tangu kianze na kodi zinazokusanywa zinaenda Wizarani na taarifa hiyo ilitoka katika taarifa ya Ikulu wananchi wa Longido walikereka sana na hiyo kauli, nikaomba sasa basi nitoe hapa wasikie kwamba nimewasema na ndipo sasa niulize maswali yangu mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kwa kuwa viwanda hivi vilivyojengwa nchini hivi karibuni vya kisasa ikiweko hicho cha Eliya Food Products kilichoko Longido zinapata malighafi pungufu kulingana na uwezo wake.

Je, Serikali imeweka mpango na mkakati gani wa kuhakikisha kwamba malighafi ya kulisha hivyo viwanda inapatikana?

Swali la pili; kwa kuwa Wilaya ya Longido ni Wilaya ya wafugaji kwa asilimia 95 na afya ya mifugo inategemea kwa asilimia kubwa upatikanaji wa maji hasa maji ya mabwawa - malambo yale.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuyafufua mabwawa na malambo yaliyofukiwa na udongo kwa miaka mingi katika Wilaya ya Longido na hasa Kiseriani ambapo maji kidogo yaliyobaki mwaka huu yanakwamisha wanyamapori? Juzi nimeweka post ya Pofu aliyekuwa anatolewa na Wamasai amekwama katikati ya lile bwawa pamoja na binadamu, sisi tunatumia maji ya mifugo na binadamu pia.

SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Kiruswa..

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Wizara ya Maji inawahusu mtatusaidiaje kufufua mabwawa yaliyofukiwa katika Wilaya ya Longido?

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Stephen Kiruswa Lemomo Mbunge wa Longido kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza linahusu mkakati wa Serikali wa kuhakikisha viwanda hivi vinapata rasilimali, tumejipanga juu ya kuhakikisha tunaweka utaratibu wa unenepeshaji kupitia vikundi na kwa watu binafsi. Mkakati wetu ni kuwa na wanenepeshaji wasiopungua 500 nchi nzima ambao miongoni mwao watakwenda kuingia mikataba na viwanda, kwa mfano kiwanda cha Eliya Foods kimeshaanza utaratibu huo wa kuwa na suppliers ambao wanawapa mikataba kwa ajili ya kupeleka ng’ombe pale kiwandani na hii itatusaidia sana hata katika lile jambo la mwanzo alilolizungumza la tozo kwa kuwa utaratibu tuliouweka wale wote watakaokuwa na mikataba na viwanda vinavyofanya uchakataji kwa ajili ya export tutawaondoshea baadhi ya tozo hizo ili kurahisisha vile viwanda viweze kupata malighafi kwa urahisi na kwa bei nzuri.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni hili la maji katika bajeti ya mwaka 2021/2022 tunayo malambo ambayo tunayatengeneza kwenye maeneo mengine ya nchi hii, lakini nafahamu Longido uko mradi mkubwa wa maji ambao unakwenda kuwahudumia wananchi wa Longido. Tumekaa na wenzetu wa Wizara ya Maji na nimpongeze sana yeye Dkt. Kiruswa na timu nzima ya pale Longido Mkoani Arusha kwa kuwashawishi wenzetu wa Wizara ya Maji waweze kutoa matoleo ambayo yatatengeneza mabirika yahudumie mifugo na wakati huo huo yaweze kuhudumia wanadamu na sisi ndani ya Serikali tunaendelea na ushauriano ili kusudi jambo hili liweze kufanikiwa.

Mheshimiwa Spika, hivyo mradi ule mkubwa wa maji uliokwenda kuzinduliwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha kwamba uweze kuhudumia maji haya yaweze kuhudumia binadamu na mifugo pia. Ahsante sana.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa nilitaka niongezee jibu sehemu ndogo ili Mheshimiwa Mbunge ambaye anawasemea sana wananchi wa Longido aweze kulibeba hilo jibu. Wizara ya Fedha pia kushirikiana na Wizara ya Mifugo tunaangalia upya sehemu ya tozo ile ambayo tuliiweka ambayo inahusu pia sekta ya mifugo pamoja na maeneo mengine ambayo yamesababisha upande wa huku Serikali Kuu iweze kuongeza hiyo sehemu ambayo ameisemea, kwa hiyo naamini kwenye kikao hiki hiki kinavyoendelea tukiwa tumeshakamilisha Mheshimiwa Mbunge atarudi Longido akiwa na jibu lililosahihi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu sehemu ya kufufua bwawa tayari tumeshakamilisha makubaliano na Waziri wa Maji ambaye anafanyakazi nzuri sana, tumeshatoa fedha za kununua mitambo ya kuchimba mabwawa ambako kila ukanda wa nchi hii utakuwa na mtambo wake wa kuchimba mabwawa. Kwa hiyo kwa wafugaji hata kama wataamua kuchimba bwawa kila baada ya mazizi mawili Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wetu amesema wachimbe tu na wata-manage wenyewe kutoa maeneo ya kuchimba hayo mabwawa. (Makofi)