Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Timotheo Paul Mnzava (34 total)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nitumie nafasi hii kwanza kabisa kumshukuru Mungu ambaye anatupa uzima, pia nitumie nafasi hii kuzishukuru na kuzipongeza Kamati zote mbili ile ya Kilimo pamoja na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Spika, ningeomba kuchangia kwenye maeneo machache. Ningeomba nichangie kidogo kwenye utalii na baadaye nitaenda kuchangia kidogo kwenye eneo la ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la utalii, tulipokuwa kwenye Kamati tumepata taarifa na tumetembelea Mradi huu wa REGROW. Ni mradi mzuri ambao utasaidia nchi yetu kuinua utalii kwenye maeneo ya Kusini mwa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, naomba kushauri tu, ilizungumzwa asubuhi hapa, tunapotaka kuinua watalii kwenye maeneo ya Kusini lazima twende sambamba na kuangalia namna ya kuboresha na kusimamia uhai wa hizi hifadhi zetu. Imezungumzwa kuhusu Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kuhusu ile barabara, barabara ile ina madhara mengi. Kwa haraka haraka kuna changamoto kama nne zinazosababishwa na barabara hii. Changamoto ya kwanza inarahisisha sana shughuli za ujangili na inasababisha uwepo wa takataka ambazo nyingine ni hatari kwa maisha ya wanyama wenyewe. Taarifa tuliyopewa ni kwamba kuna wastani wa kilo 318 za takataka kwa siku ambazo zinazalishwa kutokana na kuwepo na barabara katikati ya hifadhi.

Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ni kugongwa kwa wanyama. Mwaka 2015/2016 wanyama 361 wamegongwa, mwaka 2016/2017 wanyama 218 na mwaka jana Julai mpaka Desemba 2018 ni wanyama 130. Ukichukua mwaka wa fedha wa 2013/2014 mpaka 2017/2018 ni wafanyama 1,062 wamepoteza maisha kwa sababu ya barabara ile. Idadi hii ni kubwa, ni lazima tufanye maamuzi mazito na magumu.

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba barabara hii ni ya kimataifa na inawezekana kuna mikataba ya kimataifa ambayo inatuongoza kutumia barabara ile. Lazima ifike mahali Serikali au nchi tuamue na tukapokuja kuamua mambo mazito kwa ajili ya maslahi na ustawi wa nchi yetu haswa maslahi ya hifadhi zetu hatuna haja ya kuangalia sana makele yanayotoka huko nje na maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, tumeona hili kwenye Stiegler’s, watu wamepiga kelele nyingi sana lakini tumesema kama Taifa tunahitaji kuwa na uchumi wa viwanda na ili tuwe na uchumi wa viwanda tunahitaji kuwa na umeme wa uhakika. Tumeamua hakuna namna nyingine lazima nchi kutekeleze mradi huu kwa ajili ya kupata umeme wa kutosha kwa maendeleo ya nchi yetu. Kama Mheshimiwa Rais alivyoamua chini ya Serikali yake kuendesha mradi ule, naishauri Serikali iangalie kwa jicho la haraka na la dharura juu ya barabara hii ili tuendelee kulinda maisha na uhai wa Hifadhi ya taifa ya Miukumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze kidogo kwenye sekta ya ardhi. Nitumie nafasi kwa dhati kabisa kumpongeza sana Mheshimiwa wa Ardhi na Naibu wake, wanafanya kazi kubwa tunawaona wanavyoangaika kwenye maeneo mbalimbali ya nchi kutatua migogoro ya ardhi. Nachoomba kuwashauri kama Wizara waendelee kutengeneza utaratibu maalumu na mahsusi wa namna gani ya kuondokana na changamoto za ardhi ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kwenye jambo hili la ardhi nilisikia asubuhi watu wanazungumza hapa na ziko dhana na hisia kwamba kuna watu wanaonewa kwenye mchakato wa kufuta mashamba. Kwanza niseme, nilimshangaa sana kumsikiliza ndugu yangu mmoja akisema kwamba tulikubaliana kwenye Kamati lakini anashangaa huko haikusomwa. Mimi ni Mjumbe wa Kamati na kama ndugu yangu yule angekuwa ni Mtumishi wa Mungu kama nilivyo mimi nisingesema hapa tungeenda kuzungumza kiroho lakini kwa sababu si Mtumishi wa Mungu lazima nitumie nafasi hii kusema, hatukukubaliana jambo la namna hiyo kwenye Kamati yetu ya Ardhi, Maliasili ya Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Rais hafuti tu mashamba kwa kukurupuka, mashamba yanafutwa kwa mujibu wa sheria zilizotungwa na Bunge hili. Bahati nzuri ni Mwanasheria na nimepata nafasi ya kufanya kazi kwenye Wilaya zenye migogoro mikubwa sana ya ardhi na nimewahi kuwa Wakili wa watu waliokuwa na kesi dhidi ya Serikali kwa ajili ya kufutiwa mashamba, nafahamu changamoto ilipo. Kama kuna watu wanaobebembelezwa ni watu wenye mashamba, anapewa onyo, anapewa notice ya siku ya 90 ili ku-remedy breach za conditions za hiyo right of occupancy aliyoipewa, hawafanyi. Technique ambayo inatumika mara nyingi unakuta mtu anakuja dakika za mwisho, siku 90 zimekwisha anaanza kwenda kugusagusa sehemu ndogo anaondoka halafu anasema nimeendeleza, si sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii niseme kwamba nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi aliyoifanya ya kufuta hati za shamba ya baadhi ya wawekezaji kwenye nchi yetu. Ukienda Korogwe leo wananchi wamemwelewa sana Mheshimiwa Rais na wamemshukuru. Bunge hili waliokuwepo muda mrefu ni mashahidi, mtangulizi wangu Profesa Maji Marefu alikuwa kila akisimama analia na mashamba yasiyoendelezwa Korogwe. Leo Mheshimiwa Rais amefuta mashamba watu wanapiga kelele kwa maslahi ya nani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi watu wa Korogwe tunamshukuru Mheshimiwa Rais na tumuombe Waziri wa Ardhi bado kuna mashamba mengine ya akina Chavda yamekaa ni mapori, mpelekeeni Mheshimiwa Rais atafutie wananchi wapate maeneo. Ukienda kule Magoma na Kwa Shemshi kuna ardhi kubwa mashamba yamekaa, hayaendelezwi yamekuwa mapori na wengine wanakodisha, mpelekeni Mheshimiwa Rais atufutie ili wananchi wapate maeneo ya kilimo na makazi. Mimi nawapenda sana wawekezaji lakini lazima tuwe na wawekezaji ambao wanatutendea haki na wanatendea haki masharti ya umiliki waliyopewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia vizuri watu wanalaumu lakini kama kuna mtu anamwelewa Rais ni mimi, ni Rais anayependa haki na ni asiyemuonea mtu. Mimi ninao ushahidi wa baadhi ya mashamba, kwa sababu michakato inaanzia kwenye Halmashauri, yako baadhi ya mashamba ambayo wenzetu kwenye Halmashauri waliwahi kutengeneza na kupeleka kwa Rais yakafutwe. Hata hivyo, yalipofika Wizarani na Mheshimiwa Rais wakaona utaratibu umekiukwa yalirudishwa na Mhesimiwa Rais, tunataka haki ya namna gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nenda Wilaya ya Arumeru, Mheshimiwa Lukuvi anafahamu liko shamba la Karamu Coffee Estate, Halmashauri, Mkoa kote tulipeleka lakini lilipofika juu Rais akasema utaratibu unaonekana hauko sawasawa rudisheni mkarekebishe. Achana na hilo, nenda Kilombero, yuko mtu mmoja alikuwa na nafasi kubwa sana kwenye nchi hii sitamtaja, sasa hivi ni marehemu, Halmshauri walipitisha wakataka yale yafutiwe hati wakapeleka kwa Mheshimiwa Rais akasema hapa kuna uonevu rudisheni, tunataka Rais wa namna gani, tunataka Rais afanye nini tena? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona hapa watu wanasema ooh watu wanaonewa, wanasumbuliwa, wameendeleza, nataka niwaambie ndugu zangu kama kuna Rais tunamshukuru watu wa Korogwe ni Mheshimiwa Rais Magufuli. Sisi watu wa Korogwe hatusimuliwi, tumeona wenyewe, mwacheni Mheshimiwa Rais afanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wote tunawataka wawekezaji lakini waacheni wawekezaji hao wafuate taratibu, sheria na kanuni za nchi yetu na yule ambaye atakiuka achukulie hatua kama ambavyo hatua zimeendelea kuchukulia. Mheshimiwa Lukuvi nakukumbusha tu tunakuomba Korogwe mashamba ya Chavda, Kwa Shemshi na Magoma mwende mkampelekee Mheshimiwa Rais, tufute tuwapelekee Watanzania wakatumie ardhi ile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakuna mtu anayepewa haki bila kuwa na wajibu. Sheria ya Ardhi inayowapa watu haki ya kumiliki ardhi inawapa na masharti na mtu asipokiuka masharti nimesema anastahili zake, stahili ni pamoja na hizo. Kwenye suala la mashamba, mimi kama Mjumbe wa Kamati, kama Mwakilishi wa watu wa Jimbo la Korogwe Vijijini tuko na Mheshimiwa Rais na tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa jambo kubwa alilolifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeuona ule Mradi wa Kurasimisha na Kumilikisha Ardhi uliokuwa unatekelezwa kwenye maeneo ya kule Malinyi, Kilombero na Ulanga, ni mradi mkubwa. Nimefarijika mradi ule, niliambiwa hata Mheshimiwa Waziri kuwa unasimamiwa na vijana, wamefanya kazi kubwa. Hatusemi kwamba wazee hawafanyi kazi kubwa lakini wale vijana kwenye mradi ule wameutendelea haki wanastahili kupewa pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Wizara, tuwe na utaratibu wa kuendeleza mradi huu kwenye maeneo mengine. Safari hii tumepata hela za wafadhili hatujui mbele ya safari tutakuwa na hela za wafadhili au tutazikosa. Kwa vyovyote itakavyokuwa mradi ule ni wa muhimu kutusaidia kupunguza migogoro ya ardhi ndani ya nchi.

Mheshimiwa Spika, mwisho naomba nizungumze kidogo kuhusu Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Hifadhi hii ni kubwa, ndiyo hifadhi ya kwanza kwa ukubwa kwenye nchi yetu na Afrika Mashariki. Ni miongoni mwa hifadhi chache ambazo hazijaathiriwa na shughuli za kibinadamu. Kamati imesema kwenye taarifa yake kwamba changamoto kubwa ni kuelekea kukakuka kwa Mto Ruaha Mkuu ambao ndiyo roho ya hifadhi ile. Niiombe Serikali kwenye jambo hili la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ili tunusuru hifadhi ile tunahitaji kunusuru Mto Ruaha Mkuu.

Mheshimiwa Spika, tukisema kunusuru Mto Ruaha Mkuu watu wanafikiria kwenda kuwafukuza watu wanaolima kule kwenye Bonde la Usangu na maeneo mengine. Kama alivyosema mzee wangu, Mheshimiwa Jitu, tunazo teknolojia za kisasa zitumike. Pia changamoto kubwa ukienda kule Mabarali si tu kwamba wanalima mpunga kwa kutumia yale maji, hapana, lakini watu wanashilikia maji kwa kuzua magugu na vitu vingine hata baada ya muda wa kilimo cha mpunga. Wizara ya Maliasili ishirikiane na watu wa Ardhi na watu wa Kilimo tuwe na teknolojia nzuri ili yale maji yakimaliza kufanya shughuli za kilimo basi yaachiwe yaendelee kutiririka kwenye mto ili usiendelee kukauka. Tukifanya hivyo tutakuwa tumeisaidia sana Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja za Kamati zote mbili na mapendekezo yake, ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, nitumie nafasi hii kukupongeza wewe na viongozi wengine wote wa Bunge kwa namna mnavyotuongoza. Pia nitumie nafasi hii kuzipongeza sana Kamati zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma taarifa hizi za Kamati kwenye uchambuzi wao, ukasoma maoni na mapendekezo ya Kamati zote, unaona kabisa kwamba Wajumbe wa Kamati hizi wamelitendea haki Bunge lako Tukufu. Nimezisoma, kazi yao ni nzuri na ni wajibu wangu kuwapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajadili taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, lakini pia na ile ya Sheria Ndogo. Tunapokuja kwenye uwanja kama huu wa Sheria, kwa sisi tunaoipenda nchi yetu pia lazima tutumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ya kusaidia utekelezaji na usimamizi mzuri wa sheria ndani ya nchi yetu. Speed, kasi na moyo wa Mheshimiwa Rais kuendelea kuteua Majaji kwa wingi kama anavyofanya sasa hivi ni ishara kwamba Mheshimiwa Rais anataka kuusaidia Mhimili wa Mahakama ufanye kazi zake vizuri na utoe haki kwa wakati jambo ambalo ni wajibu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona ni vyema nichangie mambo machache. Kwa muda mrefu tumekuwa tukisikia na ndiyo msingi wa kuwa na Katiba na kuwa na Sheria, kwamba nchi yetu ni lazima iongozwe na iendeshwe kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu. Hata mchangiaji aliyetoka, kaka yangu Mheshimiwa Lema amesisitiza jambo hilo na ni jambo zuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na kelele nyingi kwenye uhuru wa watu kutoa maoni, uhuru wa watu kushirikiana; na mambo mengine ya namna hiyo. Wote wanaozungumza, wanasema uhuru huu upo kwa mujibu wa Katiba, kwa hiyo, wanataka uhuru huu uheshimiwe. Hilo ni jambo zuri, nami naliunga mkono kabisa; na ndiyo mtazamo wangu, ndiyo msimamo wangu na ndiyo mawazo yangu kwamba kama Taifa, lazima tuheshimu uhuru na haki zilizotolewa kwenye Katiba yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tukumbushane kwamba hata huu uhuru tunaotaka tuuheshimu, tunaotaka ufuatiliwe, tunaotaka utekelezwe; haki za binadamu tunazotaka watu wapate; hakuna haki bila wajibu. Katiba hii hii ambayo inapigiwa kelele kwamba imetoa haki za binadamu, imetoa uhuru kwa watu kufanya mambo, imetoa na namna ya kutekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiisoma vizuri Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na kwamba ziko haki, uko wajibu, lakini ukienda kwenye Ibara ya 30 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa masharti, haiachi tu uhuru ukaenda unavyotaka, kila mtu afanye anavyotaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba inatuambia kabisa, lazima kila mmoja kwenye kutekeleza na kutumia uhuru wake, ahakikishe haingilii uhuru wa mtu mwingine, ahakikishe hautumii katika namna ambayo inakwaza na kuumiza watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wale ambao tunapigania haki, tuko sahihi kabisa, lakini lazima tukumbushane kwamba uhuru huu una mipaka. Ibara ya 30(2) inaipa Bunge mamlaka ya kutunga Sheria kutekeleza huo uhuru na hizo haki ambazo tunazo kwa mujibu wa Katiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona kwa kuwa tunajadili taarifa za Kamati hizi ni vyema tukakumbushana jambo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye taarifa ya Kamati ya Sheria Ndogo, kwenye ukurasa wa 36 kama sikosei, Kamati ya Sheria Ndogo imetoa maoni na mapendekezo mazuri sana kuhusu Sheria Ndogo ambazo zinatungwa kwenye nchi yetu; ukurasa wa 36 ile (a), (b), (c), (d) na (e).

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Kamati kwa sababu ushauri walioutoa ni ushauri wa msingi, nami ninauunga mkono na ninaomba ukafanyiwe kazi. Nasema naipongeza Kamati hii kwa sababu gani? Ushauri walioutoa wenzetu kwenye Kamati, umetuonesha pia tofauti ya ile dhana waliyokuwa nayo watu wengine kwenye mawazo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mawazo, dhana na maneno; wako watu ambao wanapinga, wanasema siyo sahihi kuendelea kuiachia Serikali, Taasisi mbalimbali za Serikali kutunga Kanuni. Wako wengine wanasema Kanuni mbalimbali zitungwe ziwekwe ndani ya sheria au zije zijadiliwe Bungeni. Ni dhana zinazungumzwa, lakini ukisoma ushauri huu wa Kamati, unaelewa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba yetu imelipa Bunge mamlaka ya kutunga sheria, ukisoma Ibara ya 64. Ukienda Ibara ya 97(5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatoa mwanya, baada ya kutunga Sheria inaruhusu kutungwa kwa kutungwa kwa Kanuni na sheria nyingine ndogo ndogo zikiwemo Kanuni, zikiwemo Orders na vitu vingine vya namna hiyo. Kwa hiyo, kwanza, Kanuni kutungwa kwenye Wizara, kutungwa kwenye Taasisi mbalimbali za Umma, kutungwa kwenye vyombo mbalimbali, haikiuki Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hilo ni jambo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, hatuwezi kuacha Bunge likawa linatunga sheria zote, kanuni zote na orders zote. Tutakuwa nchi ya namna gani? Kazi zitafanyika namna gani? Bunge hili tunakutana kwa mwaka mara ngapi? Tunafanya kazi mara ngapi kwenye Bunge hili? Huwezi ukaacha kila sheria ikatungwa na Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili mambo yaende vizuri, tutatunga Sheria ya Bunge, lakini sheria hiyo lazima itoe mwanya kwa Taasisi nyingine au Wizara au Idara kutunga kanuni ili mambo yaweze kwenda vizuri. Hata inapotokea kuna jambo la kurekebisha, pia ni rahisi kurekebisha kanuni kuliko utaratibu wa kurekebisha sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya siyo maneno yangu tu peke yangu. Mwanasheria mmoja mbobezi anaitwa John Alder, ameandika Kitabu kinaitwa “Constitutional and Administrative Law”, edition ile ya saba. Kwenye kitabu chake ukurasa wa 147 anajaribu kueleza huo mkanganyiko na hayo mawazo ya watu, lakini mwisho ana-conclude akasema “however, it is difficult to imagine a complex and highly regulated society that could function effectively if all laws had to be made by the Parliament itself.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema niliseme hili, kwa sababu maoni ya Kamati yamejielekeza vizuri, lakini najua yako mawazo ya watu ya namna hiyo. Mimi nadhani utaratibu uliopo ni mzuri, tuache utaratibu huu uendelee. Sheria zitungwe na kama inavyotukumbusha ile Sheria yetu ya Interpretation of Laws, ukisoma kuanzia section ya 36 inatoa utaratibu, hizi kanuni zitungweje? Ziweje? Zifuatane na kitu gani? Zizingatie vitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaratibu uliopo uendele, lakini ushauri wa Kamati uzingatiwe ili kuweza kuboresha utaratibu huu wa kutengeneza Kanuni na Sheria nyingine ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lilitoka kuzungumzwa hapa muda siyo mrefu sana. Tunapokumbushana kuendesha nchi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu, lazima tukumbushane kama nilivyosema, haki na wajibu wa kila mmoja wetu. Sheria zetu na taratibu zetu haziruhusu mambo yaliyoko Mahakamani kujadiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona imekuwa ni utaratibu wa kawaida na kwa masikitiko makubwa, nimewahi kuona hata kwenye Bunge lako hili, mtu ana kesi Mahakamani, amepewa dhamana, amekiuka masharti ya dhamana, akafutiwa dhamana, ana kesi Mahakamani, ana- challenge uamuzi wa Mahakama kumfutia dhamana, mtu anakuja na jambo hili kulileta Bungeni. Tunakuja kufanya nini kwenye Bunge hili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu uko wazi. Mtu anasema kuna kesi ya Mashehe; ndiyo ipo kesi ya Mashehe lakini iko Mahakamani. Unataka tuilete Bungeni humu kufanya nini? Ni lazima sisi kama Wabunge tuwe watu wa kwanza kuheshimu sheria.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge tuwe watu wa kwanza kuheshimu misingi na taratibu na Katiba ya…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mnzava, ahsante.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja za Kamati. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Awali ya yote, nitumie nafasi hii kwanza kabisa kumshukuru Mungu mwingi wa rehema aliyenijalia uzima na kuweza kuwepo humu ndani leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya kutuletea maendeleo watu wa nchi ya Tanzania. Pia nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na Waziri wa Utumishi wanafanya kazi kubwa na wasaidizi wao wote kwenye Wizara, tunaona kazi wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa niruhusu nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa jambo moja kubwa ambalo amelifanya kwenye nchi yetu. Baada ya kuingia kwa Serikali ya Awamu ya Tano Mheshimiwa Rais amekuja na namna tofauti ya kuwapata Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya, Halmashauri za Miji, Majiji na vile vile Makatibu Tawala wa Wilaya na watumishi wengine wa maeneo mengine, tofauti na utaratibu uliokuwa umezoeleka mwanzoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili limetusaidia kuondoa utendaji wa mazoea kwenye Halmashauri zetu. Kama kuna mtu ambaye analipiga vita, atakuwa na matatizo, lakini tunaojua tunaona kwamba jambo hili limetusaidia sana kupunguza urasimu na mazoea kwenye Halmashauri ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwenye eneo la afya. Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, tunaishukuru sana Serikali sisi watu wa Korogwe. Mlichukua Hospitali ya Wilaya ya Korogwe ikaenda Halmashauri ya Mji lakini mmetupa shilingi bilioni 1.5 kutengeneza Hospitali ya Wilaya na inajengwa pale Makuyuni na ujenzi umeanza. Tunaishukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tukumbuke jambo moja, unapotoa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya au shilingi milioni 400 au 500 kwa ajili ya kituo cha afya halafu gharama za kuingiza umeme kwenye hospitali shilingi milioni 200, gharama za kuingiza maji shilingi milioni 150 na hakuna fedha nyingine nje ya hiyo inayotoka, hiyo shilingi bilioni 1.5; inatupunguzia majengo ambayo tungeweza kujenga kwenye hospitali hizi za wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba TAMISEMI itusaidie kukaa na Wizara nyingine kama ya Nishati na Wizara ya Maji. Sisi Korogwe alipokuja Mheshimiwa Waziri wa Maji nilimwomba kutusaidia kusogeza huduma ya maji kwenye hospitali ya wilaya tunayoijenga sasa hivi na alikubali. Bado tunapata shida kwenye upande wa umeme na zaidi ya shilingi milioni 190. Naomba sana Mheshimiwa Waziri aangalie namna ya kuwasiliana na Wizara nyingine kuweza kutusaidia kwenye jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye kitabu humu ndani Mheshimiwa Waziri ametengea Korogwe shilingi milioni 200 kwa ajili ya kituo cha afya Kerenge, tunakushukuru sana. Wewe ulikuja Korogwe unajua shida iliyokuwa Korogwe kulingana na eneo la kujenga hospitali ile ya wilaya, pamoja na shilingi milioni 200 kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kerenge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyo vituo vya afya vingine vitatu Korogwe. Mwaka wa fedha uliopita hatujapata fedha yoyote kwa ajili ya kituo cha afya. Kuna Vituo vya Afya vya Bungwe na Kituo cha Afya Magoma, vina hali mbaya. Ni vya muda mrefu. Mwaka 2018 aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya TAMISEMI anayeshughulika na afya, mama yangu Zainab, alikuja Korogwe na aliwaahidi watu wa Korogwe kwamba watapata shilingi milioni 500 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa Kituo cha Afya cha Bungu. Kwenye kitabu hiki sijaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana kaka yangu, Ubunge wenyewe ndiyo kwanza nimekuja juzi, namwomba, Kituo cha Afya cha Bungu chonde chonde tusaidie tupate hela tukatanue kile Kituo cha Afya. (Makofi/ Kicheko/Kigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kidogo upande wa TARURA. Kwanza tuwapongeze TARURA, wanafanya kazi nzuri. Pamoja na changamoto za kibajeti, lakini wanajitahidi wanafanya kazi nzuri. Sisi Korogwe tuna Jimbo kubwa, jiografia yetu ni kubwa na siyo nzuri. Hela tunayotengewa ukilinganisha na maeneo mengine havilingani. Tunaomba mtupe kipaumbele watu wa Korogwe. Mwaka wa fedha uliopita tumetengeneza barabara 11 tu tena ni kwa vipande, lakini ziko barabara muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale tunapojenga hospitali ya wilaya alipokuja Mheshimiwa Waziri, ukiangalia kwa upande wa juu kuna mlima, ndiyo inapatikana Tarafa ya Bungu. Ili ile hospitali ya wilaya iweze kuwa na faida kwa watu wa Tarafa ya Bungu ya mlimani, iko barabara inaitwa Makuyuni - Zege - Mpakani, Kwemchai – Makuyuni lazima itengenezwe. Bajeti ya kuitengeneza ni zaidi ya shilingi milioni
140. Kabla ya bajeti hii, nimekwenda TARURA zaidi ya mara tatu, nimekwenda ofisini kwa Mheshimiwa Waziri zaidi ya mara nne nikiwaomba ili hospitali ile ya wilaya iweze kutusaidia watu wa Korogwe. Tusaidieni barabara hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya kwenda Kizara; huko mahali mvua ikinyesha kuna eneo la Kizara na Foroforo ni kisiwani kwa sababu barabara ni mbovu. TARURA ukizungumza nao kwamba matengenezo yanahitajika; wanasema yanahitaji hela nyingi na hela tunayopewa ni ndogo, tunawaomba muwaongezee TARURA hela iweze kutusaidia kufanya hii kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumekuwa na shida kwenye upande wa madaraja. Ukiangalia hela wanayopewa watu wa TARURA kutengeneza barabara inakuwa ngumu sana kwa wao kutengeneza madaraja. Ninalo daraja kule Korogwe linaitwa Daraja la Mswaha, ni zaidi ya shilingi milioni 180 kutengeneza lile daraja, lakini utakuta TARURA wanapewa shilingi milioni 400 kwa mwaka mzima wa fedha. Hawawezi kutengeneza daraja kama hilo. Wananchi wanapata shida, wanapata taabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo daraja kule kwa Lukongwe, liko daraja linalotuunganisha watu wa Korogwe na wenzetu wa Bumbuli kule Mbagai, yamesimama kwa muda mrefu, wananchi wanashindwa kuvuka, wanapata shida ya kupita kwa sababu ya hela ndogo ambayo wanapata watu wa TARURA. Mheshimiwa Waziri, nakuomba sana hebu tuangalieni, ili ile hospitali iweze kuwa na faida, tusaidie kwenye hizo barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba Serikali imeweka msimamo. Yapo maelekezo kwamba hakuna kutoa maeneo mapya ya utawala; lakini kuna Halmashauri ya Mji wa Mombo imepewa Mamlaka ya Mji Mdogo tangu 2004. Miji mingine yote iliyopewa Mamlaka ya Miji Mdogo pamoja na Mji wa Mombo ilishakuwa Halmashauri za Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo tu kwa ajili ya kupewa muda mrefu, jioghrafia ya Korogwe Vijijini ni ngumu. Mheshimiwa Waziri ndiyo maana hata kwenye eneo la kujenga hospitali tulipata shida kwa sababu ya aina ya jiografia ya Wilaya ya Korogwe. Pamoja na hayo maelekezo ya Serikali, naomba sana muangalie uhalisia wa jiografia za Wilaya zilivyo, ukubwa wa wilaya zilivyo kuweza kutafuta maeneo mapya ya utawala kwenye maeneo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa jambo hapa kuhusu Ofisi za Wakuu wa Wilaya kuingilia Ofisi za Halmashauri. Zimepigwa kelele nyingi sana. Natambua kwamba Ofisi za Wakuu wa Wilaya zimeanzishwa kwa mujibu wa sheria. Sheria ya Tawala za Mikoa, ukisoma kifungu cha 13 (1) na (2). Ukisoma kile kifungu cha 14, kinasema Mkuu wa Wilaya ndio principle representative wa Serikali na wanasema all executive functions zitafanywa na Mkuu wa Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tujue tunasema Rais wetu ana sehemu tatu; kwanza, ni mkuu wa nchi; pili, ni mkuu wa Serikali; tatu, ni Amirijeshi. Mkuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa ndio Wawakilishi wa Mheshimiwa Rais. Wanaonjaonja na haka kaharufu. Huwezi ukawa Mkuu wa Wilaya ukaona kwenye Halmashauri ndani ya Wilaya yako, Halmashauri inafanya vitu vya ovyo halafu ukaviacha. Ni lazima ufuatilie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni mashahidi. Ziko Halmashauri ambazo Wakuu wa Mikoa walizuia ziara za Madiwani za zaidi ya mamilioni ya shilingi na wakasaidia kuokoa hela za wananchi. Tunachokitaka hapa ni tuweke tu utaratibu mzuri wa namna gani hawa Wakuu wa Wilaya watashiriki kuzisimamia vizuri hizi Halmashauri zilizokuwa chini yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kwamba TAMISEMI mlitoa Waraka Na. 2 wa 2010, unaonyesha ushirika wa Ofisi za Wakuu wa Wilaya kwenye Halmashauri. Kuna mahali kuna upungufu kwenye ule waraka. Unasema Katibu Tawala wa Wilaya ambaye ndiye technical person kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya; naomba ni-declare interest, kabla sijawa Mbunge nilikuwa Katibu Tawala wa Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waraka unasema, ataingia kwenye vikao vya SMT, unasema ataingia kwenye Baraza la Madiwani, lakini kikao cha kila mwezi cha kufanya maamuzi ni Kamati ya Fedha. Katibu Tawala wa Wilaya haingii, anapata wapi taarifa za kumpelekea Mkuu wa Wilaya ili kujua wapi pana shida aweze kuingia hapo? Naomba sehemu hii ifanyiwe marekebisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Makatibu Tawala wa Wilaya na Makatibu Tarafa wamesahaulika. Yako maeneo Katibu Tawala wa Wilaya anakuwa MC wa kusherehesha kwenye shughuli wanapokuja wageni. Hii kitu siyo sawasawa. Naomba wapewe heshima yao, naomba wakumbukwe na wasaidiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiiti, ukienda kwenye Halmashauri za Upinzani kwa mfano, ziko Halmashauri ambazo Mabaraza ya Madiwani yanataka kufanya maamuzi kinyume hata na maelekezo ya Serikali, kinyume hata na sera za nchi. Huwezi ukaacha Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa kuingilia kwenye Halmashauri za namna hiyo. Ni lazima uingie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze kidogo kwenye eneo la utawala bora. Kwanza nilimsikia ndugu yangu, baba yangu Mheshimiwa Ally Saleh asubuhi alisema, ni kweli tuna uhuru, kila mtu ana uhuru na uhuru upo kwenye Katiba…

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba hii inayotoa huo uhuru, kwa mujibu wa haki za binadamu…

MWENYEKITI: Taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde muda wangu

T A A R I F A

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba siyo wajibu wa Wakuu wa Mikoa wala Wakuu wa Wilaya kuingilia Halmashauri. Ofisi za Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kazi yao ni kuIshauri Halmashauri. Kwa hiyo, wao hawana hiyo mamlaka wanayotaka kupewa na Bunge lako Tukufu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mnzava.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei hiyo taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mnzava kwanza pokea hiyo taarifa ya mwanzo.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza siipokei hiyo taarifa kwa sababu sheria iko wazi kwamba Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa ndio wenye jukumu la kusimamia; na hiyo iko kwa mujibu wa sheria siyo kwa matakwa ya mtu. Huwezi kusimamia, halafu mtu unayemsimamia afanye mambo ya ovyo halafu usiingilie, haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kwenye utawala bora. Ibara ya 30(2) inaweka utaratibu wa hizo haki tunazozisema. Unaposema huna haki ya kusema, una haki ya kukusanyika; ibara hii imetoa mwanya kwa nchi kutengeneza Sheria ya Kusimamia Utaratibu huo. Huwezi ukakusanyika kama hali ya usalama inahatarishwa, huwezi ukakusanyika kama kuna jambo haliendi vizuri. Hiyo ni katiba na hakuna katiba inayovunjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona hoja ya mama yangu, namheshimu sana mama yangu Mheshimiwa Ruth Mollel, kuna hoja mbili kwenye ukurasa wake wa 17 na 18 kwenye hotuba yake, anasema TAKUKURU iache kupeleka watu Mahakamani…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: …mpaka itakapoweza kupata ushahidi wa kutosha.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Pia anasema kwamba kushindwa kwa kesi nyingi za TAKUKURU mahakamani ni ishara…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa mwenyekiti, umenipa ruhusa au!

MWENYEKITI: Taarifa kuhusu nini? Kwa sababu anazungumza kitu ambacho kiko kwenye kitabu.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, si kawaida kupiga taarifa!

MWENYEKITI: Ananukuu kitabu kilichoelezea. Hebu endelea Mheshimiwa Timotheo.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa mwenyekiti, taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, anasema kwenye kitabu chake kwamba kushindwa kwa kesi nyingi za TAKUKURU Mahakamani ni ishara kwamba kesi hizo siyo za haki.

Mheshimiwa Mweyekiti, sisi tutakuwa nchi ya ajabu kweli. Hivi ni lazima kila anayeenda Mahakamani ashinde? Hilo ni swali l a kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine hebu tuulizane, hivi ni nchi gani ambayo eti mpaka ushahidi wote ukipatikana ndiyo unaenda kumpeleka mtu Mahakamani. Hili ni jambo endelevu, wakati mwingine unaweza ukamkamata mtu, ukampeleka mahakamani…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Ukaendelea kuafuta ushahidi…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mnzava, malizia.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza TAKUKURU, nataka waendelee kufanya kazi vizuri…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: …waimarishe Kitengo cha Uchunguzi, waimarishe Kitengo cha Prosecution ili wafanye kazi nzuri kwa ajili ya kutetea nchi yetu na kupingana na mafisadi wanaoifisadi nchi yetu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara ya Elimu kwa kazi kubwa wanayoifanya. Elimu; iko haja ya kuangalia au kupitia upya mitaala yetu na Sera ya Elimu ili kuwaandaa wanafunzi kwa level mbalimbali kujiajiri na sio tu kutegemea kuajiriwa, elimu ya stadi za maisha iwekewe mkazo zaidi. Katika maeneo mengi mwananchi wamejitahidi kujenga mabomba kwa ajili ya madarasa na maabara, Serikali iangalie namna ya kuwasaidia wananchi hawa kumalizia majengo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukarabati wa shule kongwe. Serikali imefanya ukarabati wa shule kongwe za sekondari, zipo shule za msingi kongwe na zenye hali mbaya zinahitaji ukarabati mfano kwenye Jimbo la Korogwe vijijini ipo Shule ya Msingi ya Madela Ratuba, shule hii ilijengwa mwaka 1952 na haijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu. Niombee Wizara isaidie ukarabati wa shule hii pia ipo Shule ya Msingi Ng’anzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya ufundi; naiomba Serikai imaarishe elimu ya ufundi. Kwenye Jimbo la Korogwe Vijijini tuna Chuo cha Ufundi Mnyuzi, chuo hiki kikipanuliwa, kikapewa vitendea kazi na kuongeza aina ya course zinazotolewa kitasaidia sana wanafunzi wanaoshindwa kuendelea na masomo kwa mfumo wa elimu ya shule. Chuo hiki kinaweza kusaidia wanafunzi wengi sana wa Wilaya za Korogwe, Lushoto, Muheza na hata Handeni. Naomba sana Wizara itusaidie kuboresha, kupanua na kuimarisha chuo hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Mikopo; bado kuna manung’uniko ya baadhi ya Watanzania maskini kukosa mikopo kwa ajili ya kugharamia elimu ya juu. Ni vyema Bodi ya Mikopo ikaangalia hili lakini pia tayari kufanya marekebisho hata katikati ya masomo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema aliyetujalia uzima, aliyenipa uwezo kuwepo Bungeni leo na kuweza kuchangia bajeti ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji na Naibu wake, wanafanya kazi nzuri Mheshimiwa Waziri ni msikivu sana tunampongeza sana anafanya kazi kubwa na kazi nzuri. Pia tumpongeze Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, kwenye Wizara hii siyo kwa Waziri na Katibu peke yake hata wataalam wao wale watu wa Idara ya Maji Vijijini Mkurugenzi na Msaidizi wake wanafanya kazi nzuri, wanatoa ushirikiano wa kutosha huwa nawasumbua wakati mwingine mpaka usiku nikiwa na changamoto za maji kule kwetu Korogwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niishukuru sana Serikali, kwa muda mrefu watu wa Korogwe tumekuwa tukiangaika na vibali vya mradi wa Vuga, Mlembule, na mradi wa Lusanga, lakini mwezi wa pili hatimaye tumepata vibali vile na miradi ile tayari taratibu zimeanza manunuzi kwa ajili ya wakandarasi kuendelea na kazi zile, tumesubiri kwa muda mrefu kwa hiyo tunaishukuru sana na kuipongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri nikushuku sana kwa ile kazi ya ujenzi wa tenki pale Mombo tulikuwa na changamoto ya mtambo kwa ajili ya kutibu maji, tumeshamaliza michoro, imeshaletwa Wizarani tunaomba mtusaidie ile kazi ifanyike kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana dada yangu Mheshimiwa Mboni, alizungumza kwa uchungu sana kuhusu kero ya maji kule Handeni; na ni kweli Handeni kuna shida kubwa sana ya maji, na miongoni mwa njia za kutatua kero ya maji Handeni ni mradi ule wa HTM, na Wizara ilishafanya mpaka usanifu wa kupanua na kuboresha ule mradi. Sasa ukienda kule Korogwe kuna Kata inaitwa Kata ya Mswaha, ina vijiji vitano, kijiji kimoja kinaitwa Kijiji cha Tabora, ndipo kwenye chanzo cha maji cha mradi huu wa HTM na kuna vijiji vingine vinne Kijiji cha Mswaha Darajani, Mswaha Majengo, Kijiji cha Mafuleta, na Kijiji cha Maulwi Rutuba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji hivi vilifanyia usanifu pia kwamba vitafaidika na mradi huu wa uboeshaji na upanuzi wa mradi huu wa HTM ni muda mrefu wananchi wale wanasubiri Mheshimiwa Waziri tunakuomba sana kazi hii ifanyike na itakapofanyika msiwasahau watu wa Korogwe kwenye Vijiji hivyo maana Kata hiyo ndiyo kilipo chanzo cha maji cha HTM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kule Korogwe kuna eneo linaitwa Bungu, tuliwahi kuwa na mradi wa maji tulipata ufadhili wa watu World Division, tukawa na mradi wa shilingi milioni 969, na ule mradi ulikamika na ulinufaisha vijiji tano, lakini maji yale ni mengi yana uwezo wa kunufaisha vijiji vingine vitatu, Kijiji cha Mlungui, Kijiji cha Kwemshai na Kijiji cha Ngulu. Tunaiomba sana Wizara tuko kwenye maandalizi ya mwisho ya kuleta maombi kwenu ili mtusaidie tuweze kupata fedha za kusambaza na kupeleka maji kwenye maeneo hayo ambayo nimeyataja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi wa maji wa Mwanga, Same, korogwe, mradi huu umesemwa muda mrefu ni mradi muhimu sana unanufaisha Wilaya za Same, Wilaya ya Mwanga na Wilaya ya Korogwe, nimeona kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri kwenye mwaka wa fedha unaokuja tunasema tumetenga bilioni 29 sijaona kama ndiyo tunakwenda kukamilisha ule mradi au bado tutaendelea kusubiri kwa miaka mingine na awamu nyingine zijazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa shida ambayo tunaipata watu wa Korogwe ambao na sisi tumesubiri kwa muda mrefu mradi huu sisi ndiyo tuko mwishoni, tuna Vijiji vitano kwenye Kata ya Mkomazi, Kijiji cha Manga Mikocheni, Kijiji cha Manga Mtindilo, Kijiji cha Mkomazi Kijiji cha Bwiko na Kijiji cha Nanyogie. Vinanufaka na mradi huu na sisi ndiyo tuko mwishoni na tunaambiwa kuna bilioni 29, je mradi huu unakwenda kukamilika? Maana sisi watu wa Korogwe ambao ndiyo tuko mwishoni tunanufaika na mradi huu ukiwa umekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri ukumbuke kwamba tumeusubiri kwa muda mrefu, na changamoto ya maji kwenye vijiji hivyo ni kubwa sana tunakuomba sana utakapokuja kufanya majumuisho utuambie maana mwanzoni pia kwenye vikao vya maandilizi na utekelezaji wa mradi huu watu wa Korogwe tulikuwa tunahusishwa, lakini baadaye kumekuwa na kama sintofahamu hivi hatujui hata kinachoendelea ni nini. Utakapokuja utuambie ni kweli bado watu wa Korogwe ni wanufaika kwenye mradi huu? Na kama ndivyo matumaini yetu yale lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepeleka Wizarani taarifa ya usanifu wa mradi wa maji wa Kijiji cha Mgwashi na kwa Kibomi tangu mwezi wa tatu, hatujapata taarifa yoyote kwamba tutapa lini kibali. Nilikuwa namuomba sana Mheshimiwa Waziri najua watu ni wasikivu kule Wizarani tusaidie tuweze kupata kibali ili mradi huu angalau ukaanze tutekelezwa kwenye maeneo ya Mgwashi na Kwakibomi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hizi fedha za PBR, sisi ni miongoni ambao tulikuwa tunatumaini kwamba tutanufaika na fedha hizi, lakini kwa mwaka huu wa fedha tulikokuwa nao mpaka sasa hatujapata hizi fedha, na sisi tulikuwa tumelenga kwenda kutatua changamoto za maji kwenye baadhi ya maeneo ndani ya Jimbo letu kwa kwenda kufanya ukarabati mdogo wa vyanzo vya maji. Tulikuwa tunategemea kupata fedha hizi kwa ajili ya ukarabati vyanzo vya maji kule Magoma, tulikuwa tunategemea kupata kwa ajili ya kukarabati chanzo cha maji kule Mazinde, tulikuwa tunategemea kwenda kukarabati chanzo cha maji Kerenge na baadhi ya Vijiji vya Kata ya Mashewa. Lakini mpaka leo hatujapata hizi fedha nimejaribu kuuliza Wizarani sijapata majibu ambayo yamekaa vizuri, naomba sana Mheshimiwa Waziri utusaidie tupate hizi fedha twende tukatekeleze hayo mambo kwenye hayo maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ulikuja Korogwe tulikuomba fedha kwa ajili ya kupeleka maji kwenye eneo tunalojenga Hospitali ya Wilaya na tunashukuru kwamba ulikubali na tuliandika ikaja Wizarani baadaye mkaturudishia tulete mchanganuo tukaandaa, tukaleta mchanganuo Wizarani na ukatuhaidi kutupa shilingi milioni 95.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa bahati mbaya sana maji tuliyokuwa tunataka kuyatumia pale chanzo chake ilikuwa ni maji ya kisima, lakini tumegundua chanzo kikubwa na kizuri cha maji ambacho kitakuwa na maji ya mtiririko kwa ajili ya hospitali, pia kwa ajili ya maeneo na Makuyuni na maeneo ya kwa Sunga Mpirani. Kama utaridhia Mheshimiwa Waziri pamoja na kwamba ulikubali, na ukahaidi kutoa milioni 95 nakuomba sana kwa unyenyekevu najua wewe ni msikivu, wewe ni muungwana sana hebu ukubali tukuletee haya marekebisho ili badala ya kutumia chanzo kile cha kisima tutumie chanzo hiki kingine cha maji ya mtiririko na vijiji vingine vya karibu na maeneo yanayojengwa hospitali na vyenyewe viweze kunufaika na maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu Bunge limeanza la bajeti tangu bajeti ya kwanza nilikuwa nataka kuchangia naenda uhamishoni, lakini leo sijaenda uhamishoni nachangia nikiwa kwenye kiti hiki, kwa sababu maji ni jambo muhimu ndiyo maana hata humu unaona kumetulia. Ukisoma vizuri hata kitabu hivi vitabu vya hotuba vya rangi hii nadhani mnanielewa nikisema vya rangi hii kwa mara ya kwanza nimeona hotuba ambayo imegusa vitu tofauti na nyingine utakuta Wizara tatu, Wizara nne hotuba ni hiyo hiyo, lakini leo nimeona hotuba nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba tumesema hapa na nimesema Mheshimiwa Waziri kila mahali nasema tunaomba tunaomba niliposoma hutuba yako kwenye kitabu hichi ukurasa wa 106 changamoto ya kwanza unaionesha ni ukosefu wa fedha. Kwa hiyo, pamoja na maombi yote haya ambayo tunayaweka kama hatuna fedha bado changamoto ni kubwa ni miradi hii itakuwa na shida kwenye kutekeleza, yamekuwepo mawazo humu kwamba iongezwe shilingi 50 na wengine wamesema kwenye mafuta, pia iko hofu kwamba inaweza ikasababisha mfumuko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nishauri tunahitaji kweli ongezeko la fedha kwa ajili ya miradi ya maji kwenye nchi yetu. Ukiangalia lengo tulilokuwanalo la kufika upatikanaji wa maji mwaka 2020 na asilimia tuliyokuwa nayo sasa bila kuwa na mkakati madhubuti wa kupata fedha kwa ajili ya miradi ya maji tutapata shida kwenda kufikia lengo letu. Niombe tu kuishauri Serikali wametusikia Waheshimiwa Wabunge hebu ufanyieni kazi huu ushauri wa Wabunge uliotolewa, ungeniambia kwenye mafuta kunakuwa na mfumuko wa bei nikasema bado yako maeneo mengine, kuna maeneo kwenye mawasiliano kuna watumiaji wengi, tunaweza kuangalia namna ya kuongeza huko ili tupate fedha ajili ya kuweza kusaidia kugharamia miradi ya maji, baada ya kusema hayo nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na timu yake yote, hotuba yangu kwa ujumla imelenga kwenye maombi, naomba sana maombi yangu myapokee, naomba myafanye kazi naomba muwasaidie watu wa Korogwe ili tuondokane na changamoto hii ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja, kwa asilimia 100. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Wizara ya Afya kwa juhudi inazofanya za kuboresha Sekta ya Afya nchini. Katika Jimbo la Korogwe lenye tarafa tatu na kila tarafa ikiwa na kituo cha afya, tuna gari moja tu la kubebea wagonjwa. Gari ambalo na lenyewe limechakaa sana maana ni la muda mrefu, naiomba sana Wizara kwa unyenyekevu mkubwa watusaidie tupate gari la wagonjwa maana vituo vya afya viko mbali na hospitali.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulipokea fedha za ujenzi wa Kituo cha Afya kipya katika Kata za Mkumbara, kituo kimekamilika. Tunaiomba Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI kutupatia vifaa ili kituo hiki kianze kufanya kazi ya kutoa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa watumishi katika Wilaya ya Korogwe kwa zaidi ya 46%; tunaiomba Wizara kusaidia upatikanaji wa watumishi hawa ili kuboresha huduma za afya wilayani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha na kuratibu vizuri huduma za wazee, ni vyema Serikali ikaandaa Sheria ya Wazee kama ilivyo kwa watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, viko vituo vya afya vya muda mrefu kama Kituo cha Afya cha Magoma na Bungu ambavyo vinahitaji ukarabati na upanuzi. Pamoja na uhitaji wa ukarabati na upanuzi, pia vifaa kama vitanda vimechakaa sana vinahitaji kubadilishwa kama siyo kuongezwa. Naiomba Wizara ianzishe utaratibu wa kuongeza vifaa kwenye vituo vya afya kwa awamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ustawi wa Jamii; viko vituo vya kulelea watoto/makao ya watoto ambavyo havina hadhi ya kuwa makao ya watoto na vingine vinatuhumiwa kwa kashfa mbalimbali kama unyanyasaji na ukatili wa kijinsia na Maafisa Ustawi walioko wilayani baadhi yao siyo waaminifu, ni vyema Wizara iimarishe utaratibu wa ukaguzi wa makao ya watoto.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, aliyetujaalia uzima. Pia nitumie nafasi hii kwa dhati kabisa kuipongeza Serikali, kumpongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni mara yangu ya kwanza kuchangia bajeti ya Serikali. Tangu nimekuwa Mbunge hii ni mara yangu ya kwanza kuchangia bajeti. Nafarijika sana kuona kwamba nakwenda kuchangia bajeti ambayo ukiisoma unaiona bajeti inayogusa maisha ya watu wa Tanzania. Yanaweza yakasemwa maneno mengi, kunaweza kuwa na hadithi nyingi, lakini ukweli ni kwamba bajeti iliyowasilishwa inakwenda kugusa maisha ya wananchi wetu kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali. Hii miradi mikubwa tunayofanya, inawezekana matokeo yake yasionekane kwa haraka leo, lakini ni miradi ambayo inakwenda kutuvusha kama Taifa kutoka hapa tulipo tuweze kwenda kwenye hatua nyingine. Unapoona mtu analalamika anasema hali ya uchumi ya watu wetu siyo nzuri, mtu analalamika anasema tume-import sana kuliko ku-export, lakini wakati huo huo miundombinu ya kusaidia tuwe na viwanda vya kutosha kwenye nchi yetu watu wanaipiga vita. Ni vitu vya ajabu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapotaka kuwa na umeme wa uhakika ni kwa ajili ya kusaidia viwanda, unapotaka kuwa na miundombinu ya barabara ya uhakika, kuwa na bandari ya uhakika ni kwa ajili ya kusaidia viwanda, ukipata viwanda vingi ukazalisha vizuri, tutafika huko tunakotaka kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nimeona tangu mjadala huu umeanza tumekuwa tukipigana kelele, mtu anasema, Serikali hii hakuna kitu ilichokifanya. Pia tumefika mahali tunahukumiana kwa kutumia Ilani za Vyama tulizotumia kwenye uchaguzi wetu wa mwaka 2015. Sisi wote tunajua, Vyama vinapokwenda kwenye uchaguzi, Ilani tunazozinadi tunazinadi kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania kwa miaka mitano, ndiyo muda tuliojiwekea kwa uongozi kama Taifa kwa mujibu wa Katiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, muda wa kutekeleza Ilani ni miaka mitano. Miaka mitano haijaisha, pressure hizi zinatoka wapi?mtu anaongea kana kwamba leo ndiyo tunamaliza, Serikali inakwisha, muda wa uongozi umekwisha, tunakwenda kwenye uchaguzi. Hii siyo sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wamezungumza kuhusu shilingi milioni 50, mtu anapiga kelele anasema mliwaahidi Watanzania shilingi milioni 50, ziko wapi? Kwanza nikubaliane kabisa na dada yangu Mheshimiwa Gekul. Tunapoahidi vitu, Serikali iliyopo madarakani iliahidi vitu vingi, kila kitu kinafanyika kulingana na nafasi na wakati ambao tunao. Hizo shilingi milioni 50 za kwenye vijiji, yako mambo yamefanyika makubwa kwenye maeneo ya watu wetu na yanayogusa maisha ya Watanzania, tofauti hata na hiyo shilingi milioni 50 ingekwenda moja kwa moja kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Serikali, tumefanya vizuri kwenye maboma ya shule za sekondari na za msingi, tupeleke na huo moyo kwenye zahanati kwenye vijiji ambavyo watu wetu wapo. Wananchi wetu wanajitoa sana kwenye ujenzi wa zahanati, tumefanya vizuri kwenye maboma shule za sekondari na za msingi, hebu twende tukasaidie na kwenye zahanati. Huyo anayesema kwamba bajeti haigusi maisha ya watu, akaangalie maji, zahanati na barabara, atasema kama bajeti inagusa maisha ya watu au haigusi maisha ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri mambo machache kwa ajili ya kusaidia kuongeza mapato kwenye nchi yetu. Mheshimiwa Waziri wa Fedha unafahamu, inawezekana kabisa wakati mwingine kuongeza kodi kukakupunguzia idadi ya watu wanaoweza kuwa walipa kodi. Inawezekana kabisa kuongeza kodi kukakupunguzia idadi ya watumiaji wa huduma ambayo ingesaidia kupata kodi. Sasa naomba sana Mheshimiwa Waziri hili jambo tuliangalie vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, mimi nilikuwa naangalia tu barabarani mle, miaka michache iliyopita watu waliokuwa wanatumia magari ambayo yamesajiliwa kwa majina yao, ninavyoona kama idadi ile inapungua. Ukiangalia vizuri, inawezekana imesababishwa na kuongezeka kwa kodi ile, lakini kodi ile ingekuwa angalau kwenye kiwango kizuri, ni rahisi kupata watu wengi zaidi na kupata kodi nyingi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili lipo pia kwenye Sports betting. Tunachukua kodi kule, wale waendeshaji wanalipa asilimia 25 ya mapato ghafi wanayopata, lakini na yule mtu ambaye anashinda kwenye ile zawadi anayopata analipa asilimia 20. Wako watu ambao kwa kuona kwamba wanalipa kodi, wengine wameamua kuacha hizo, wameamua kufanya za online, inasababisha kwenda kukosa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshauri Mheshimiwa Waziri, tuangalie namna ya kupunguza kodi hasa kwa wale ambao wanashinda ili ku-encourage watu wengi zaidi waweze kushiriki ili kutengeneza kodi zaidi kwa wale wanaoendesha lakini pia wanalipa kodi kwenye huduma nyingine kama wakifanya matangazo wanatoa ajira kwa watu wetu na vitu vingine vya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye upande wa utalii. Juzi hapa tumefanya mnada wa vitalu. Katika vitalu 26 naambiwa tumefanikiwa kuuza vitatu saba. Hii imechangiwa sana na ongezeko la gharama za kununua vile vitalu. Naiomba Serikali, vitalu hivi vikikaa kwa muda mrefu bila kuwa na watu waliovichukua tunapata hasara sisi kama Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati yako ya Bunge, Ardhi Maliasili na Utalii. Tuliishauri sana Serikali, tunaweza tukaweka makadirio yetu lakini tusiyatangaze, lakini pia tusiwe rigid kwenye hayo makadirio ambayo tumeyaweka, lakini pia tusiongeze sana ili kuweza kusaidia watu wengi waweze kujitokeza na kuja kuomba kununua vitalu ili tufanye biashara na Serikali iweze kupata fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwenye upande wa utalii ni kwenye hoteli. Miaka ya nyuma Serikali yetu iliamua kubinafsisha baadhi ya hoteli. Ziko baadhi ya hoteli nyingine ambazo ziko chini ya Serikali pia ziliuzwa. Watu waliobinafsishiwa hoteli hizi, ukienda vizuri, hoteli nyingi zilizobinafsishwa hazifanyi kazi vizuri na kwa kutokufanya kazi vizuri hazitengenezi vizuri ajira, hazitengenezi vizuri mapato kwa maana ya kulipa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahangaika sana kukuza utalii na utalii ni eneo ambalo tunaweza kutusaidia kama Taifa kupata fedha nyingi, lakini tunakuza utalii, lakini ili tuwaalike watalii wengi zaidi waweze kuja kwenye nchi yetu, wakati huo huo miundombinu tuliyokuwa nayo haiendani na hii kasi ya uingizaji wa watalii kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye nchi yetu ukilinganisha vitanda ambavyo tunavyo vinavyoweza kulipiwa kodi, ukilinganisha na nchi jirani za wenzetu, sisi bado tuko nyuma sana. Tungeweza kutatua tatizo hili kwa kwenda kuziboresha hoteli ambazo ziko ndani ya nchi yetu. Cha kusikitisha zaidi, ziko hoteli ambazo tulizibinafsisha, watu wakachukua zile hoteli, wakachukua mikopo, wakafungua biashara nyingine za namna ile kama hoteli na wakafanya kazi na wanafanya kazi vizuri. Zao zinakwenda vizuri, walizobinafsishiwa na Serikali haziendi vizuri. Naishauri sana Serikali, tuna jambo la kuangalia hapa. Tuangalie namna ya kuboresha hizi huduma za hoteli ili tuweze kuwasaidia watu wetu, tuweze kusaidia nchi yetu kuweza kupata mapato zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakubaliana kwamba kilimo ni miongoni mwa maeneo muhimu katika kutafuta malighali kwa ajili ya viwanda vyetu. Naiomba sana Serikali, tuendelee kuweka mkazo kwenye kilimo, hasa kilimo cha umwagiliaji ili kuhakikisha kwamba watu wetu wanazalisha zaidi na wapate soko la kuweza kulisha viwanda vyetu na waweze kupata fedha, lakini pia viwanda viweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kule Korogwe tunalo bonde ambalo likitengenezwa mradi wa umwagiliaji, tunaweza kulima hekta 5,000. Kwa karne tuliyonayo hekta 5,000 ni eneo kubwa sana. Ukiwa na wananchi 5,000 wamejiingiza kwenye kilimo cha uhakika wanaweza kulima kwa zaidi ya mara mbili kwa mwaka mmoja. Ni kuwa na misimu ya kilimo zaidi ya miwili kwa mwaka mmoja. Ni jambo kubwa sana. Tunatengeneza uchumi mzuri kwa ajili ya maisha ya watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema nichangie hayo machache kuishauri Serikali namna ya kuongeza mpato, kubwa nasema bajeti hii ni nzuri, bajeti hii inafaa, bajeti hii inagusa maisha ya wananchi wetu moja kwa moja, watu wamepiga kelele tulikuwa tunaomba sana tozo zipunguzwe tusiwe na mtiririko wa kodi na ndiyo spirit ya Mheshimiwa Rais, bajeti hii iliyowasilishwa inajibu hoja hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono bajeti hii. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aliyetujaalia uzima. Kipekee nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa uteuzi wa kuwa Waziri kwenye Wizara hii. Odo Ummy tuna imani kubwa sana nawe, tunaamini kwamba utaifanya kazi yako vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza Waheshimiwa Manaibu Waziri kwa kuendelea kuaminiwa, lakini pia najua mna timu nzuri sana TAMISEMI. Mmepata Katibu Mkuu mzuri, Profesa Shemdoe, mtu mahiri, mtu makini san ana pia anaye Naibu Katibu Mkuu kama ndugu yangu Ndugu Gerald Mweri, tuna uhakika na kazi wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie muda huu kushauri mambo machache kwenye eneo la TAMISEMI. Jambo la kwanza ni upande wa TARURA. Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza kuhusu TARURA, nami naendelea kusema na tutaendelea kusema kwa sababu ni kitu muhimu sana kwenye maendeleo ya Halmashauri zetu hasa kwa sisi ambao tunatoka maeneo ya vijijini. TARURA inafanya kazi nzuri, lakini lazima tukubaliane kwamba ziko changamoto zinahitaji kufanyiwa kazi ili kazi hii nzuri inayofanywa na TARURA iweze kuwa na matokeo mazuri kwa watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa ya kwanza ni fedha. Tuseme tutakavyosema lakini pesa wanayopewa TARURA ni ndogo, wanahitaji kuongezewa fedha ili waifanye kazi yao vizuri. Jambo hili siyo kwa TAMISEMI tu, ni jambo la Serikali. Tunahitaji Serikali itusikie kwamba tunahitaji kuona TARURA ikiongezewa fedha iweze kufanya kazi zake vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na hoja ya baadhi ya watu wakihoji kwa nini TARURA au barabara zimetolewa Halmashauri na TARURA imesimama yenyewe inajitegemea? Kwa upande wangu, kuirudisha TARURA Halmashauri ni kurudi hatua moja nyuma na wala siwezi kushauri jambo hilo. Ninachokiomba hapa kifanyike kuwe na mahusiano mazuri kati ya Halmashauri ya TARURA.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge na Madiwani ndio waliokwenda kuomba kura, ndio tunaojua mahitaji ya wananchi, ndio tunaojua vipaumbele vya watu wetu. Lazima TARURA watushirikishe Halmashauri zetu kwenye kuteua barabara za kufanyia matengenezo. Isiwe hisani kwamba akijisikia aseme, asipojisikia asiseme. Watushirikishe tushauriane ili twende tukaangalie maeneo kulingana na mahitaji na vipaumbele vya watu wetu kwenye Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yako ukurasa wa 118 nimeona unazungumzia mradi wa barabara kwenye maeneo ya uzalishaji hasa kwa maeneo ya kilimo. Umeongelea eneo la kule nyanda za juu kusini peke yake. Yako maeneo mengi ya uzalishaji ambayo yana shida kubwa ya barabara. Katika Mkoa wa Tanga, milima ya Usambara ni maeneo muhimu sana hasa kwa kilimo cha chai. Barabara ni mbovu sana, tunahitaji miradi ya namna hii ifike kwenye maeneo yale pia tuwasaidie wananchi. Tunapoteza chai nyingi sana ya wananchi wetu kwa sababu ya ubovu wa barabara, inachelewa kufika kiwandani, watu wetu wanapata hasara. Tunaomba sana mtusaidie kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Asenga ameshauri hapa kuhusu vifaa, hata kama siyo kwenye level ya Halmashauri, basi hata kwenye level ya mkoa angalau TARURA kwenye ngazi ya mkoa kuwe na vifaa. Haiwezekani tukipata dharura tuanze kuhangaika kukopa kwa Wakandarasi na mkiwakosa wananchi wapate hasara. Angalau kila mkoa basi kuwe na vifaa, ikitokea dharura wafanye kazi kwa kutumia wataalam tuliokuwanao kwenye TARURA kwa vifaa walivyokuwa navyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2020 Serikali ilitoa maelekezo ya kuhamisha Halmashauri zote ambazo walikuwa wanafanyia kazi kwenye maeneo ambayo ni nje ya maeneo yao ya utawala kwenda kwenye maeneo yao ya utawala. Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ni moja ya Halmashauri ambazo tulihamisha Makao Makuu ya Halmashauri yetu, lakini tuna changamoto kubwa sana ya usafiri kutoka kwenye Tarafa kwenda kwenye Makao Makuu ya Halmashauri mpya tuliyopeleka sasa. Naomba mtusaidie TARURA wawe na programu maalum ya barabara za kuunganisha angalau Tarafa na Makao Makuu hizi mpya za Halmashauri ili wananchi wetu waweze kufika vizuri na kwa urahisi kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie kwenye upande wa afya. Tunaishukuru Serikali, imefanya kazi nzuri na kazi kubwa sana kwenye Sekta ya Afya. Korogwe tumepata Hospitali ya Wilaya, tumepata Kituo cha Afya cha Mkumbara na sasa tunajenga Kituo cha Afya cha Kerenge, lakini kuna vituo vya afya vikongwe vya muda mrefu. Ninacho Kituo cha Afya kule Korogwe cha Bungu kimejengwa mwaka 1977 mpaka leo hakijawahi kufanyiwa ukarabati, hakina huduma ya upasuaji, kutoka huko kwenda Hospitali ya Wilaya ni zaidi ya kilometa 55. Naomba pamoja na kazi nzuri mnayoifanya tuangalie maeneo haya, tusogeze huduma, tuboreshe vituo hivi vikongwe viweze kufanya kazi yake vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ziko ahadi za viongozi. Waziri Mkuu alipita Korogwe akaahidi kusaidia ukarabati wa Kituo cha Afya cha Bungu. Aliahidi Kituo kipya cha Afya kule Mashewa, tunaomba ahadi za viongozi zikatekelezwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2020 kwenye bajeti ya TAMISEMI nilisema na mwaka huu narudia tena, hamtutendei haki kwa namna mnavyogawa hizi rasilimali tulizokuwa nazo. Huyu ndugu yangu wa Korogwe Mjini hapa ana vijiji na vitongoji jumla 34, mimi nina vijiji 118; ana shule za Msingi 34, mimi nina shule 138; unaposema kila wilaya au kila jimbo lipewe maboma tisa, hamtutendei haki. Sisi wengine tunaumia, tuna maeneo makubwa. Hata kama ni kigezo cha watu, pia tuna watu wengi. Tumefuatilia kwenye hizo Halmashauri nyingine, hawana watu wengi namna hiyo. Tunaomba mtuangalie sisi ambao tuna maeneo makubwa, tunaumia Zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna uhaba mkubwa sana wa watumishi hasa kwa upande wa Halmashauri za vijijini. Halmashauri za vijijini zimekuwa ni maeneo ya watu kwenda kuanza kazi na kuondoka kwenda kwenye maeneo mengine mazuri wanayoyataka wao. Sekta ya Afya na Sekta ya Elimu tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi. Naomba mtusaidie kupunguza tatizo la upungufu wa watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nawaomba TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, hebu tuweke utaratibu mzuri wa mtu kuhama kutoka kwenye Halmashauri moja kwenda kwenye Halmashauri nyingine. Hii tabia kila mtu akitaka kuhama anaandika moja kwa moja, inakuja kutoka Wizarani amehamishwa, mnatuumiza. Tuna shule zina walimu watatu, kuna zahanati ina mtumishi mmoja au wawili, tunawaomba mtusaidie kupunguza changamoto hii ya watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshauri Mheshimiwa Waziri kwenye eneo la kusimamia mamlaka ya Serikali za Mitaa. Tuna ripoti ya CAG imetoka juzi; moja ya maeneo ambayo hatukufanya vizuri ni kwenye Halmashauri. Namwomba sana dada yangu, hatafanya kazi yake vizuri TAMISEMI kwa kukimbizana kwenye ziara katika kila Halmashauri. Kwa siku uende Halmashauri tatu au nne, hakuna kitakachofanyika kule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba, imarisheni sekretarieti za mikoa ili ziwasaidie kuzisimamia Halmashauri. Katibu Tawala wa Mkoa ajue ana jukumu la kuisimamia Halmashauri na Mkurugenzi ajue kwamba yeye immediate boss wake ni Katibu Tawala wa Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa ajue kwamba Halmashauri ikiharibu, naye hatabaki salama. Tuna sekta zote, tuna idara zote pale kwenye Sekretarieti ya Mkoa, zinafanya nini? Kwa nini mpaka tusubiri Waziri au Katibu Mkuu aje? Tuimarishe Sekretarieti za Mikoa zikusaidie wewe na Katibu Mkuu kuzisimamia Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuimarisha Sekretarieti za Mikoa, tunacho kitengo cha ukaguzi wa ndani kwenye Halmashauri zetu. Mimi naomba TAMISEMI mtafakari upya namna ya kufanya kazi na kusimamia hiki kitengo vizuri.

Mambo yote anayoyasema CAG kwenye Taarifa zake siyo mapya. Wakaguzi wa ndani wameshayaibua kwenye Halmashauri zetu, lakini mwisho wa taarifa ya Mkaguzi wa Ndani ni nini? Hatua za taarifa za Mkaguzi wa Ndani zinachukuliwa na nani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, iko haja ya kukiimarisha hiki kitengo sambamba na kuwajengea uwezo Madiwani wetu kwenye Kamati za Fedha na kwenye Mabaraza ya Madiwani kuzifanyia kazi vizuri taarifa za Wakaguzi wa Ndani ili mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine niwaombe, tunazo sheria; hebu TAMISEMI fanyeni kazi ya kupitia sheria. Ziko baadhi ya sheria zinatusababishia kupoteza mapato kwenye Halmashauri zetu. Leo tunapozungumza sisi watu wa Korogwe na watu wa kule Nyanda za Juu Kusini, kuna mgogoro mkubwa sana kwenye kupata ushuru wa mazao kwenye zao la chai, lakini shida ni sheria tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna haja ya kuziangalia sheria, lakini pamoja na sheria hiyo, iko changamoto nyingine kwamba kampuni inafanya kazi kwenye Halmashauri lakini Makao yake Makuu yako kwenye Halmashauri nyingine. Kwa hiyo, kwenye kupata Service Levy tunakuwa na mgogoro mkubwa sana. Tunaomba TAMISEMI mtusaidie kutoa mwongozo wa namna ya kwenda na vitu kama hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tuna imani na Mheshimiwa Waziri kwamba wataifanya kazi hii vizuri. Tuna imani nanyi kuwa mambo yanakwenda kukaa sawa sawa. Tunachowaomba, tusaidieni kuzisimamia Halmashauri zetu vizuri. Tusaidieni kuwaimarisha TARURA, tusaidieni kuimarisha Idara ya Afya kwenye Halmashauri ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetujalia uzima, lakini kipekee nitumie nafasi hii kumpongeza sana Waziri wa Fedha kwa hotuba yake nzuri lakini kwa ujumla nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hotuba hii inatoa mwelekeo mzuri sana wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi na inaonyesha namna gani kama alivyosema Kaka yangu Mheshimiwa Nape Serikali yetu inakwenda kuangaika na shida na matatizo ya watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii kuweka kipaumbele kwenye miundombinu ya barabara, kwenye masuala ya maji, kweye kukamilisha umeme vijijini lakini pia kwenye masuala ya afya na elimu hayo ndiyo mambo ambayo wanahangaika nayo Watanzania. Kama fedha zitakazokusanywa zikitumika vizuri kwenye mambo haya hata huu wasiwasi uliopo kwenye baadhi ya kodi na tozo tulizoongeza utaondoka na niwaombe tu watanzania hatuna namna nyingine ya kuijenga nchi yetu zaidi ya kutafuta na kutengeneza kodi na kukusanya kodi, lazima tulipe kodi tuweze kutengeneza na kuijenga nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kipekee nipongeze kuongeza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 mpaka 35 kwenye magunia ya kitani yale ya duty lakini pia kuongeza ushuru wa forodha asilimia 10 kwa nyuzi za plastiki itatusaidia sana wakulima wa mkonge tunakwenda kuongeza soko na kulinda Mkonge wa Tanzania wa nchi hii. Ni jambo ambalo tunalipigia kelele muda mrefu tunashukuru Serikali, imelisikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende tu moja kwa moja kwenye jambo moja ambalo jana Kaka yangu Mheshimiwa Kitandula alisema wameniachia kulizungumza mimi mdogo wao watu wa Tanga na watu wa Morogoro tunataka tuishauri Serikali haswa kwenye kuongeza mapato na hapa nazungumzia sana mapato kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa. Niombe sana Waziri wa Fedha niombe sana watu wa TAMISEMI, watu wa Wizara ya Kilimo na watu wa Kamati ya Bajeti kama wako hapa watusikilize vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yako kwenye ukurasa wa 53 moja ya maeneo yanayokwenda kufanya marekebisho tunakwenda kuirekebisha sheria ya fedha ya Serikali za Mitaa sura ya 290 na kwenye hotuba yako umesema, tunakwenda kufanya marekebisho, moja ili kubainisha mazingira ambayo kampuni iliyolipa tozo ya huduma haitawajibika kulipa tozo ya uzalishaji na ukasema marekebisho hayo yanalenga kutatua mgongano uliojitokeza kwenye kutafsiri kifungu husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimeingia humu 2018 miaka mitano iliyopita tumekuwa na changamoto sana kwenye jambo hili, lakini Waziri wa Fedha nikuhakikishie hatukuwa na mgongano wowote wa tafsiri kwenye sheria hii, Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Kifungu cha Kumi na Sita inasema corporate entity inayolipa service levy haitalipa produce cess iukienda kwenye sheria yenyewe ya fedha inasema kwa mazao ya biashara mnunuzi anapaswa kulipa asilimia tatu ya farm gate price kama ushuru wa mazao kwa maana ya produce cess hakukuwa na mgongano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa tafsiri ya kisheria mgongano uliokuwepo ulikuwa ni mgongano wa kimaslahi nani afanye nini nani alipe nini tukasumbuana miaka mitano hapa na watu wa Wizara ya Kilimo ni mashahidi tumefanya vikao vingi leo limekuja kujitokeza, niliposoma kwenye hotuba yako na kukusikiliza nimerudi kwenda kuangalia Finance Bill ambayo inakuja, yanakuja marekebisho ya kurekebisha kifungu hichi kwenye Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda kuongeza specifically tunasema corporate entity ambayo inazalisha mazao ya kilimo haitalipa ushuru wa mazao kwa mazao yanayozalisha labda kwa mazao ambayo yanatoka kwa mtu mwingine. Tumesema tunataka kuongeza mapato na mwaka wa fedha tulionao Halmashauri zimekusanya kwa asilimia 88 na tumeongeza makadirio na moja ya vyanzo muhimu vinavyotegemewa ni huu ushuru wa mazao sasa haya mabadiliko yaliyofanyika tafsiri yake ni nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni kwamba yale makampuni wazalishaji wakubwa wa mazao tukichukuwa mfano wa zao la mkonge hawatalipa ushuru wa mazao kwa maana produce cess labda kama wamechukua mazao hayo kutoka kwa mkulima mwingine ambaye hapo sasa tunamzungumzia mkulima mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya jambo hili ni kubwa inakwenda kutupunguzia fedha na mapato kwenye Halmashauri zetu na sisi ambao tunalima tunapata shida kidogo ukienda leo Handeni DC...

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Chumi.

T A A R I F A

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mzungumzaji, kwamba jambo hilo halitaenda kuathiri tu Korogwe hata Halmashauri ya Mji wa Mafinga, hata Halmashauri ya Wilaya Mufindi hata Halmashauri ya Njombe ambayo tunategemea misitu kwa sababu kwa mfano sisi asilimia 50 ya mapato yetu yanatokana na hiyo ambayo inataka ije ifutwe. (Makofi)

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa naomba tu muda wangu ulindwe vizuri. Nina takwimu hapa za Halmashauri nyingi lakini nichukue Halmashauri moja tu ya Korogwe, huko nyuma baada ya kutokea hii mivutano tukaenda mpaka kwenye Kamati ya Bajeti na Mheshimiwa Simbachawene akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, wakasema mgongano wa kisheria hapa nendeni mkatekeleze sheria, sisi wa Mkoa wa Tanga tukaenda kutengeneza By Laws kwamba huyu mkulima mkubwa kabla hajatoa mzigo wake usiondoke mpaka awe amepata ushuru wetu wa mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ni kwamba Sheria ya Fedha inataka mnunuzi ndiyo alipe, wakulima wakubwa wa mkonge wakimaliza kulima wanachukua wanapeleka nje, Halmashauri hatumjui mnunuzi ni nani hatujui ananunua shilingi ngapi tukawa na changamoto, tukaweka sheria kwa mabadiliko haya mnayoyaleta hata ile By Laws haitaweza kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, chukua mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe asilimia 70 ya eneo letu ni mashamba makubwa ya mkonge kwa hiyo mkonge ndio madini yetu, mkonge ndiyo kila kitu na ukitaka kuona hilo mwaka wa fedha tulionao kwenye bilioni moja na milioni tisa na kidogo mapato yanayotokana na ushuru wa mazao kwenye mkonge peke yake ni milioni 425 sawa na asilimia 39 ya mapato yetu. Leo ukiondo produce cess tunapata wapi mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo tu kupunguza mapato lakini pia mnatuletea mkanganyiko, huyu mkulima mkubwa ambaye anaambiwa asilipe produce cess kwa tabia ilivyo pia wananunua kwa wakulima wadogo, tunatofautishaje kati ya mkulima mkubwa na mkulima mdogo mazao yapi yametoka wapi hatuwezi kutofautisha, lakini shida ya pili kama mkulima mkubwa halipi produce cess maana yake mazao ambayo yana uhakika wa kulipiwa ushuru wa mazao ni mazao anayolima mkulima mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake nini ukiwa na mnunuzi independent aliyekuja kutoka nje kwenda kununua mazao kwa wakulima wadogo ni lazima atafuata hiyo tozo tunayotaka tuichukue Halmashauri, kwa hiyo atapunguza bei kwa mkulima wetu ili aweze kupata nguvu ya kulipa ushuru na kununua yale mazao. Wakati huyu mwingine anachukuwa mazao yake anapeleka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilitokea mwaka 2019 mwishoni alikuja mnunuzi kampuni ya Kichina kununua mkonge akakuta kuna ushuru wa mazao kwa wakulima wadogo ukinunua, akatakiwa kulipa, akaona kuliko kulipa ule ushuru ni bora aache, ilitumika busara ya Mkuu wa Mkoa kuwaomba halmashauri wasamehe ili ule ushuru wa mazao hili mnunuzi huyo anunue wakulima wasiumie. Maana yake ni kwamba mazao ya wakulima wadogo yanakwenda kushindanishwa na wakulima wakubwa, akikosekana mnunuzi independent kwa sababu ya hii kodi, wakati hawa makampuni makubwa hawalipi, wakulima wetu watakuwa hawana option zaidi ya kuwauzia hawa wakulima wakubwa ambao wana makampuni na mashamba kule kwenye maeneo yetu, wakienda kuwauzia bei ya mkonge itaporomoka, bei ya mkonge wataipanga wanavyojisikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha na ….

T A A R I F A

MWENYEKITI: Nimemwona Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge, Mtendaji wetu wa CCM Mstaafu anayejenga hoja kwa umakini mkubwa sana, amewakilisha Halmashauri nyingi tu, nilitaka nikiombe Kiti chako, Mheshimiwa Mbunge pamoja na mwingine aliyetoa hoja, tukiahirisha Bunge hapa tukakae na timu yangu ya wataalam wanaoandaa Finance Bill tulipitie hili jambo ili tulirekebishe ili tunavyo print document ya mwisho iwe imekaa sawa kwa maslahi mapana ya nchi yetu. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mnzava unaipokea taarifa?

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili na nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa uungwana huu mkubwa uliounyesha. Kwenye hili Mheshimiwa Waziri wa Fedha nataka niendelee kusema mengine lakini kwa uungwana uliouonyesha kwenye hili naishia hapa tutaonana tuliweke vizuri Mheshimiwa Waziri wa Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie na moja tu maana Mheshimiwa Waziri wa Fedha nimefurahi sina haja ya kuendelea sana nimalizie na moja dogo. Tusaidieni tumeanzisha tozo kwenye zile skimu za umwagiliaji kwa maeneo ambayo yanakuwa yanasimamiwa na Vyama vya Ushirika na skimu za umwagiliaji kwa ujumla, hii iwe chachu ya kutufanya tuongeze fedha zaidi kuwa na miradi mingi, watu wa Korogwe kwa mfano, wanaangaika kwa zaidi ya 20 na Bwawa la Mkomazi bilioni sita inahitajika. Ukienda kilimo wanasema tumepeleka Hazina, ukienda Hazina na tungeweza kupata mapato mengi kwenye maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu kwenye bajeti ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Awali kabisa, namshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, ambaye ametujalia uzima, ametuwezesha kuwa pamoja humu kuifanya kazi hii nzuri ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiye msimamizi wa Wizara hii, maana ni Wizara iliyo chini ya Ofisi yake kwa kazi nzuri ambayo anaifanya kwa nchi yetu na kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee nampongeza sana Ndugu yangu Mheshimiwa Innocent Bashungwa kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa TAMISEMI, na Manaibu wao kwa kuendelea kuaminiwa. Naamini kazi hii ataifanya vizuri, ana timu nzuri TAMISEMI. Nampongeza pia Katibu Mkuu, Profesa Shemdoe na timu yake ya Manaibu Katibu Wakuu, wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo nitumie nafasi hii kutoa mchango wangu kwenye maeneo machache. Eneo la kwanza ni miundombinu ya barabara vijijini. Hapa naizungumzia TARURA. Kipekee kabisa, naipongeza sana Serikali kwa kazi nzuri tuliyoifanya ya kuongeza fedha kwa ajili ya kushughulikia barabara za vijijini. Nikitoa mfano, kule Korogwe tulikuwa na bajeti ya shilingi 670,000,000 kwa miaka kama mitatu mfululizo, lakini kwa mwaka wa fedha tuliokuwa nao, tumepokea zaidi ya shilingi 1,400,000,000/= kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara za vijijini, pia tumepokea shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa daraja kubwa kule Mswaha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee, kwenye fedha hizi namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kukubali kutoa zile shilingi 500,000,000 za Jimbo kupitia kwa Wabunge kwenda kufanya matengenezo ya barabara. Kwa kweli TARURA wamejitahidi kufanya kazi nzuri. Pamoja na kujitahidi kufanya kazi nzuri, yapo maeneo manne naomba nishauri. Eneo la kwanza, pamoja na kuwa fedha zimeongezwa, lakini ukweli ni kwamba bado mahitaji ya fedha kwa ajili ya barabara za vijijini ni makubwa. Naiomba Serikali iendelee kuangalia namna ya kuongeza bajeti kwa ajili ya TARURA ili waendelee kupata fedha nyingi zaidi kufanya miradi mingi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili tuwaombe TARURA, Serikali imekubali kuongeza fedha, na kama Wabunge tunaendelea kuomba fedha iongezwe zaidi; tujitahidi kubuni na kuweka mfumo mzuri wa usimamizi wa matumizi ya hizi fedha ili kazi inayofanywa kwa fedha hizi iwe na thamani halisi ya fedha ambayo imetolewa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la tatu ni la teknolojia. Wakati fulani tumemsikia Mheshimiwa Rais akishauri kwamba kuna teknolojia nzuri iliwahi kuja hapa lakini haikuwahi kufanya kazi, ikaenda maeneo mengine. Ni kweli tunatoa fedha nyingi tunatengeneza barabara na kukarabati, lakini ukweli ni kwamba barabara zetu za vijijini, wanamaliza kutengeneza, ikinyesha mvua ya siku moja, barabara hazipitiki tena. Ni lazima kama nchi tufikirie teknolojia nyingine sahihi zaidi itakayosaidia matengenezo yanayofanywa kwenye barabara zetu yaweze kukaa muda mrefu na wananchi wetu wanufaike na matunda ya kazi hii nzuri iliyofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la nne na la mwisho la kushauri kwenye TARURA, tumeona iko miradi mingi ya barabara inafanyika kwa maeneo ya mijini hasa kwenye maeneo ya Makao Makuu ya Halmashauri ambazo ni za Miji na Manispaa. Maeneo yetu sisi tunaotoka maeneo ya vijijini, tunayo miji ambayo pia ni centre kubwa na nzuri za kibiashara, tuwaombe TAMISEMI kuwaomba TARURA, fikirieni namna ya kuwa na maandiko ya kutafuta fedha kwa ajili ya maeneo haya. Siyo maeneo haya tu peke yake, nimeona kwenye bajeti mnaendelea kuzungumzia kuhusu miradi maalum ya maeneo yale ya uzalishaji, na sehemu kubwa nimeona mnazungumzia eneo moja tu la kule nyanda za juu Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Tanga, Wilaya ya Handeni, Korogwe na Muheza ndiyo zinaongoza kwa kilimo cha Mkonge. Leo tunavyozungumza, moja ya changamoto kubwa wanayopata wanachi wetu na wakulima wadogo wadogo wa Mkonge, ni miundombinu ya kutoa mkonge kutoka mashambani kupeleka kwenye viwanda vya kuchakata. Pia eneo la Lushoto na eneo la milimani la Korogwe kuna kilimo kikubwa sana cha chai, lakini kwa muda mrefu tumesahaulika. Tunaomba TARURA ije na miradi ya namna hii pia kwenye maeneo ya mkonge na maeneo ya chai ili tusaidie kuongeza thamani ya mazao ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni Afya. Tunaishukuru Serikali imefanya kazi nzuri kwenye eneo la ujenzi wa vituo vya afya na pia kwenye kukamilisha maboma ya Zahanati. Nimemsikia ndugu yangu, Mheshimiwa Mabula hapa amesema tuendelee kupunguza bajeti ya ujenzi. Mimi nasema mwendelee kupunguza bajeti ya Ujenzi lakini kwa wale wa mjini kama Nyamagama.

Mheshimiwa Spika, kwa sisi wa vijijini kama Korogwe, miundombinu ni muhimu na vifaa tiba ni muhimu na vyote hivyo ni lazima viende kwa pamoja. Leo ninapozungumza Korogwe vijijini, nina maboma zaidi ya 24 ambayo…

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mnzava kuna taarifa kutoka kwa Mbunge wa Nyamagana, Mwanza Mheshimiwa Stanslaus Mabula.

T A A R I F A

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji ya kwamba hoja ya kupunguza ujenzi haimaanini kuacha ujenzi. Kwa hiyo, kama Korogwe wana uhitaji zaidi wa ujenzi, watajengewa, lakini hoja yangu ya msingi ni kwamba ujenzi uambatane na vifaa zaidi. Sasa sijui kama yeye anaiona hiyo haifai au inafaa, ataichukua. Nakushukuru sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Timotheo Mnzava, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, naipokea na ninajua imemsaidia na yeye kufafanua jambo hili kwa wapiga kura wake kule, sasa wamemwelewa. Mwanzoni hawakuwa wamemwelewa, ndiyo maana nimesema, ujenzi huu uendane na vifaa tiba. Vifaa tiba ni muhimu na ujenzi ni muhimu. Nimesema, kwa mfano Korogwe Vijijini, nina maboma sasa hivi zaidi ya 24 ya Zahanati ambayo yanahitaji kukamilishwa ili wananchi wetu waweze kupata huduma. Ukiwaambia wananchi unaacha, unaweka nguvu kwenye vifaa tiba, tunawavunja moyo. Mambo haya yaende kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais, pamoja na Sera na Ilani kusema tuwe na Kituo cha Afya kwenye kila Kata, tuwe na Zahanati kwenye kila Kijiji, utekelezaji wake ulionekana ni mgumu. Alipoingia Mheshimiwa Rais, Mama Samia, amesema angalau tujihakikishie kila Tarafa kuwa na Kituo cha Afya. Nasi tunashukuru, Tarafa yetu ya Korogwe ambayo ilikuwa haina kituo cha Afya hata kimoja, imepata Kituo cha Afya cha Mnyuzi, shilingi milioni 500, tunaishukuru Serikali. Naiomba sana TAMISEMI, tusimchonganishe Mheshimiwa Rais na wananchi wake. Nikitoa mfano wa Korogwe, nina Tarafa nne; Tarafa moja ya Bungwi ina Kata tisa; ina Kituo cha Afya kimoja; hawajapata kituo afya kingine kwa sababu tayari wana kituo cha Afya.

Mheshimiwa Spika, lakini kituo hicho walichokuwanacho, hata operation hakifanyi. Huduma za upasuaji hakuna, ni cha muda mrefu, ni kikongwe na chakakavu. Kuna kituo cha Afya cha Magoma. Pamoja na miradi hii ya vituo vya afya tuliyokuwa nayo ya kila Tarafa na inavyoendelea, tunaomba sana, vituo vya afya za zamani, vikongwe na vichakavu, viboreshwe ili wananchi wetu waweze kupata huduma. Kwenye hili la Vituo vya Afya, siyo tu majengo, pamoja na hivyo vifaa tiba, lakini tuna changamoto kubwa sana ya watumishi kwenye sekta ya afya na kwenye sekta ya elimu. Tunawaomba sana TAMISEMI tulingalie hili kwa uzito wake liweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho ni la usimamizi wa Serikali za Mitaa. Tunaendelea kusema, Wabunge wote ni mashahidi, muda tunaotumia Majimboni ni mdogo sana, muda mwingi tupo kwenye vikao vya Bunge karibu nusu ya mwaka, tupo huku Bungeni. Wanaotusaidia kufanya kazi vizuri ni Waheshimiwa Madiwani. Naiomba Serikali, tuangalie namna ya kuboresha maslahi ya Madiwani wetu. Fedha wanayopata, kiwango cha posho yao ni kidogo na kimekaa kwa muda mrefu. Tuna Madiwani karibu 4,500; Serikali ikiamua kutenga shilingi bilioni 30 kwa mwaka, tunawaongezea nguvu hawa Madiwani wanafanya kazi yao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia na Wenyeviti wetu wa Serikali za Mitaa, naomba nao tuangalie namna ya kuweza kuwaongezea uwezo waweze kufanya vizuri.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kutoa mchango wangu kwenye bajeti muhimu sana hii kwa mustakabali wa nchi yetu. Kama muda utaniruhusu, ninayo mambo matatu.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, tumeipongeza Serikali, inafanya kazi nzuri ya kuitangaza nchi yetu na kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza kwenye nchi yetu, lakini ni ukweli usiofichika kwamba hatujafanya kazi nzuri kwenye kufufua viwanda vilivyokufa. Hasa viwanda vilivyokuwa vikimilikiwa na Umma na tukavibinafsisha na viwanda hivi vingi ni viwanda muhimu sana. Bahati mbaya sana kule Korogwe kuna Kiwanda cha Tembo Chipboard, ni kiwanda muhimu sana, na kimetelekezwa muda mrefu. Mheshimiwa Naibu Waziri aliniahidi humu ndani atakuja kukitembelea, mwaka umekwisha sijamwona. Naomba niishauri Wizara tuongeze nguvu kwa kushikana na Msajili wa Hazina na Wizara za Kisekta.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kuhusu NDC, Shirika letu la maendeleo. NDC lilikuwa ni shirika muhimu sana na nadhani bado ni shirika muhimu. Lilianzishwa kwa Tangazo la Serikali Na. 90 la mwaka 1969, na limeendelea kuwepo chini ya utaratibu wa Sheria ya Mashirika ya Umma. Hata hivyo kuendelea kuwepo kwa NDC leo, mkazo wake hasa ni maamuzi ya Baraza la Mawaziri, Waraka Na. 6 wa Baraza la Mawaziri wa Mwaka 1996.

Mheshimiwa Spika, waraka ule ulieleza kwamba Shirika liendelee kubaki Serikalini, limilikiwe asilimia mia moja na Serikali, liendelee kufanya miradi hii muhimu ya kimkakati ya kusaidia viwanda vingine. Ni ukweli kwamba, hali na utendaji wa NDC bado hauridhishi. Mheshimiwa Waziri baadaye atakapokuwa anafanya majumuisho kesho, nangetamani kujua, kwa sasa NDC in miradi mingapi? Ni mingapi ambayo inafanya kazi? Ninyi kama Wizara mtuambie, hivi kweli mnaridhika na namna NDC inavyofanya kazi zake? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, moja ya njia nzuri ya kuvutia na kushawishi wawekezaji ni kuwahakikishia utulivu kwenye nchi yetu lakini kuwahakikishia kwamba nchi yetu inafuata utawala wa sheria. Hakuna mwekezaji anaweza kuja kuwekeza kwenye nchi ambaye ana wasiwasi na utawala wa sheria unavyotekelezwa kwenye nchi. Nchi yetu inafuata utawala wa sheria, lakini siku za karibuni kumekuwa na matukio ambayo yanafanywa na baadhi ya Taasisi za Serikali yanayopelekea nijaribu kuamini kwamba pengine taasisi hizi zinakoelekea ni kutokutii utawala wa sheria kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, yapo mazingira ambayo ningeweza nikatoa mfano, lakini naomba nitoe mfano kwenye eneo moja tu. Jana wakati namaliza research yangu hii kwa ajili ya kuchangia leo, ndugu yangu Mheshimiwa Shabiby aliniambia, kama unachangia kesho na mimi nimo. Sasa nataka naye pia anisikilize vizuri.

Mheshimiwa Spika, hapa nataka nitolee mfano sakata linaloendelea la Twiga Cement na Tanga Cement. Hapa nataka nioneshe tu madhara ya kisheria ambayo yanaweza kuleta taswira mbaya kwa wawekezaji.

Mheshimiwa Spika, nitalisema kwa kirefu, naomba unisadie, maana muda hautoshi. Mwezi Oktoba, 2021 Kampuni ya Scancem International na Kampuni ya AfriSam. Scancem International ni subsidiary company ya kampuni yenye hisa nyingi kwenye Kiwanda cha Twiga Cement; na AfriSam ni Kampuni yenye hisa nyingi, asilimia 68 kwenye Kiwanda cha Tanga Cement.

Mheshimiwa Spika, mwezi Oktoba, Mwaka 2021 walitoa joint statement kwamba wamemaliza terms na makubaliano ya kuhamisha hisa za AfriSam kwenda Scancem. Tarehe 2 Novemba, Scancem akaiandikia FCC kuomba approval. FCC wakapokea, wakachakata, na FCC wakaridhia kuhamisha hisa hizi kutoka kwa AfriSam kwenda kwa Scancem lakini walitoa masharti. Yapo kadhaa ambayo FCC waliyatoa, na nimeyasoma vizuri kwenye major analysis report ya FCC yenyewe.

Mheshimiwa Spika, wapo wadau ambao hawakuridhika. Wadau watatu wakaenda kufungua shauri kwenye Baraza la Biashara. Mdau wa kwanza ni Scancem yenyewe akifungia shauri kutokuridhishwa na masharti aliyowekewa na FCC. Mdau wa pili ni Kampuni ambayo inafanya biashara kwa jina la Chalinze Cement na mdau wa tatu ni Tanzania Consumers Protection Associations. Wakafungua shauri kwenye Baraza la Ushindani, shauri linasikilizwa. Mwezi Septemba tarehe 23 Mwaka 2022 Baraza la Washindani likatoa uamuzi kwamba baada ya kupima hoja za pande zote, na kwa kutumia major analysis report yenyewe ya FCC, Baraza la Ushindani likazuia kwamba acquisition hii ya shares za AfriSam kwenda kwa Scancem isimame.

Mheshimiwa Spika, cha kushangaza, uamuzi wa Baraza ukishatolewa kuna namna mbili tu, aidha kuomba review warudishe kwenye Baraza lenyewe au kukata rufaa kwenda Mahakama ya Rufaa. Hayakufanyika. Mwezi Desemba, 2022 Scancem wanaandika tena FCC kuomba kupewa approval ya kufanya acquisition ya hizi shares za AfriSam. Tarehe 11 Februari, 2023 FCC anatoa notice watu wapeleke maoni.

Mheshimiwa Spika, cha kushangaza Baraza hili ni la kwetu, tumeliunda kwa sheria. Utaratibu wa ku-challenge uamuzi wa baraza hili upo. Kwanini utaratibu haukufuatwa? Wameacha, wanakuja ku-file application nyingine mpya.

Mheshimiwa Spika, moja ya jambo ambalo Baraza lilizingatia ni measure analysis report ya FCC ambayo ilionesha kwamba Scancem na AfriSam waki-merge watakuwa na 42.27 ya market share kwenye biashara ya cement, kitu ambacho ni hatari na ni kinyume na kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Ushindani. Pia hakuna aliyekata rufaa, mwisho wa siku watu wamekuja kivingine.

Mheshimiwa Spika, jambo hili linatia mashaka sana. Kinachotia mashaka zaidi, mwezi Machi mwaka huu, Taasisi nyingine ya Wizara hii, BRELA ikai-deregister Chalinze Cement ambayo ndiyo challenger mkubwa wa hili jambo, wakitoa sababu kwamba haja-file annual returns.

Mheshimiwa Spika, mimi ni kiongozi, najua suala la annual returns ni suala la kisheria, siwezi kulikataa, lakini hivi ni kweli? Mtuambie, makampuni yote tunayo BRELA sasa hivi yamekidhi? Yana-file annual returns kwa wakati? Mheshimiwa Waziri ukija tunataka tujue, maana kunakuwa na harufu ya jambo ambalo siyo zuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na uamuzi huu, mimi binafsi sikatai acquisition, sikatai ku- merge, ni mchakato wa kawaida kwenye biashara kwa ajili ya kuyafanya makampuni yaendelee kufanya kazi vizuri, lakini kwenye jambo hili, kuna maswali lazima tujiulize, mbona kuna kulazimisha sana Twiga kuinunua Tanga Cement? Mbona jambo hili halikutangazwa na halikuwa wazi? Walikaa wakakubaliana; Twiga Cement amekuwa registered kwenye stock exchange, akatangaze, watu waje, kuwe na ushindani. Jambo la pili, wakiungana hawa, hii asilimia ambayo kisheria inakataza ya ku-monopolize biashara hii, ninyi mnalionaje kama Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, sisi watu wa Tanga ni wahanga wakubwa sana wa mambo ya namna hii; ni wahanga wa hizi merge, ni wahanga wa hizi acquisition, ni wahanga wa wabinafsishaji, ni wahanga wa uuzaji wa Mashirika na Makampuni, kwa namna ambayo inakuwa haijanyooka vizuri.

Mheshimiwa Spika, hofu yetu sisi tunaotoka Mkoa wa Tanga, Waziri anajua na Serikali inajua, kwamba eneo la Kiwanda cha Tanga Cement ndiyo kiwanda pekee kime-deposit vya kutosha raw materials za kuzalisha cement kuliko sehemu nyingine yoyote kwenye nchi yetu. Tanga ndiyo inaongoza kuwa na deposit kubwa ya clinker ambayo kwenye uzalishaji wa cement huwa kunainahitajika content yake, ni karibu asilimia 95. Huyu Twiga hana deposit ya namna hiyo. Tuna hofu, anapomchukua huyu, usalama utakuwepo? Biashara hii itaendelea? Brand ya Tanga Cement itaendelea kuwepo? Ndiyo hofu yetu. Tunasema haya, hofu hii siyo kufikirika, yametukuta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Korogwe tulikuwa na Kiwanda cha Mrwazi Kamba, aka-merge na kiwanda kingine, aliishia kufungua mashine za Mrwazi Kamba, akaenda kufanya shughuli nyingine. Tanga tulikuwa na Kiwanda cha Amboni Plastic, kikanunuliwa na Kampuni nyingine ya Dar es Salaam mnaijua. Kilipoishia, iko wapi ambayo ni plastic yetu leo Tanga? Haipo, imekufa. Hii ndiyo hofu yetu. Lazima Serikali mjiridhishe ili mtutoe sisi wenzenu kwenye hii hofu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, nini kifanyike kwenye eneo hili? Moja, kama nchi tuiambie Jumuiya ya Kimataifa, tunaheshimu Mfumo wa Utawala wa Sheria. Uamuzi uliotolewa na Baraza la Ushindani, uheshimiwe. Tunaweza kufanya merger au kufanya acquisition kwenye viwanda hivi kwa kutumia taratibu ambazo zitatutoa kwenye eneo la kutokuheshimu uamuzi wa Mahakama zetu, tunaweza kutafuta watu wengine, tunaweza kuangalia mabadiriko kwenye market shares, tunaweza kuangalia mabadiliko kwenye considerations ya hiyo transfer inayotakiwa kufanyika. Tukifanya hivyo, tutakuwa salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile ushauri wa pili kwenye eneo hili, kama Tanga Cement iko registered kwenye stock exchange, kuna public individuals wanayoiyona hisa mle, kuna shida gani kutangaza huu mchakato ukaenda vizuri? Utangazwe, tuondoe usiri na malalamiko ambayo yalikuwepo. Kwa sababu ukitangaza, faida zake, jambo litakuwa wazi, watu watashindana, tutapata mwekezaji anayeweza kutoa fedha nzuri itakayosaidia kuongeza kodi ya Serikali. Pia akitoa hela ya kutosha, ni rahisi kuwa serious na biashara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mauziano yaliyokuwa yamefanyika ambayo FCC iliyabariki na Baraza likayakataa, wanataka kuuza hisa moja kwa shilingi 3,100, jumla kwa hisa zote ni shilingi bilioni 137 na point kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Serikali, tunawaomba sana, vyombo vyetu vya Serikali na taasisi zetu za Serikali, zisitumike kama sehemu ya kuharibu utawala wa sheria kwenye nchi yetu. Kubwa, zingatieni maslahi ya Taifa, zingatieni maslahi ya walio wengi, zingatieni maslahi ya nchi yetu. Tunachohitaji hapa ni kazi hii iende. Sisi hatutaki kuona Tanga Cement inakuja kufikia mahali inafungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami nitoe mchango kwenye bajeti hii ya Wizara ya Nishati. Nianze kwa kuungana na wenzangu waliotangulia kusema kukutakie kila la heri katika jambo hili kubwa na zuri ambalo liko mbele yako. Tuko pamoja na wewe na tunakuombea heri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, watendaji wa Wizara hii na taasisi zao zote. Sisi sote ni mashahidi wa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya. Miaka kadhaa nyuma iliyopita tulikuwa tukikutana kwenye Bunge hili kujadili Bajeti ya Wizara ya Nishati tulikuwa tunatumia muda mwingi kwenye eneo la REA, lakini leo kuanzia kwenye hotuba ya Waziri, taarifa ya Kamati lakini hata Michango ya Wabunge inatambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa kwenye uzalishaji wa umeme kwenye maeneo mengine na kwenye vyanzo vingine. Leo tutazungumzia gesi, umeme wa upepo, umeme wa jua na vyanzo vingine mbalimbali. Niwapongeze Wizara kwa maono hayo ni jambo zuri tunaliunga mkono endeleeni nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina mchango kwenye maeneo mawili. Eneo la kwanza ni eneo la usambazaji wa umeme vijijini lakini eneo la pili nitazungumza kidogo kuhusu gesi.

Mheshimiwa Spika, kama kuna miradi ambayo imesaidia kuipa heshima Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwenye nchi hii ni pamoja na mradi wa kusambaza umeme vijijini. Wananchi wamefurahi ni mradi unaogusa maisha yao moja kwa moja, ni mradi unaokwenda kubnadilisha maisha ya watu wetu kule vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwenye eneo hili mimi nilitaka nizungumze tu kuhusu Jimbo la Korogwe Vijijini. Sisi Korogwe vijijini tuna vijiji 118, vijiji 54 havijapata umeme kabisa. Tulikubaliana kwamba vijiji hivi vitapata umeme kupitia mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili. Kwa bahati mbaya sana baada ya zoezi kufanyika na kutafuta wakandarasi kuna lots tano ambazo zilikosa wakandarasi ikiwemo lot moja ambayo ilikuwa ina Wilaya za Korogwe, Mkinga pamoja na Pangani. Tukachelewa kwa muda mrefu lakini baadae wizara, Serikali na REA wakatusaidia tukapata mkandarasi na tukaamini kwamba kazi ya kupeleka umeme kwenye vijiji inakwenda kuanza kwa kasi na wananchi wetu wapate umeme.

Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya sana tukapata mkandarasi ambaye kwa kweli uwezo wake ulikuwa si wa kurudhisha na hivyo hajaifanya kazi hii Vizuri. Kipekee nishukuru sana Kamati yetu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa kutembelea eneo la Korogwe kama eneo la kujifunza. Walipofika Korogwe waliona kazi aliyoifanya mkandarasi yule. Katika vijiji 54 mpaka Kamati inakwenda ilikwenda kuwasha umeme kwenye vijiji viwili na vijiji vilivyokuwa vinakaribia kuwa tayari na maeneo mengine yote kulikuwa hakuna kazi iliyofanyika. Jambo hili lilitusikitisha sana na limewaumiza sana watu wa Koropgwe na limewachelewesha watu wa Korogwe kupata huduma ya umeme

Mheshimiwa Spika, lakini nimshukuru Mheshimiwa Waziri, baada ya Kamati kutoka tumekaa vikao kwa maelekezo yake Mheshimiwa Waziri na kwa usimamizi wake kwa kweli tumeanza kuona ile speed ya yule mkandarasi imeanza kubadilika. Katika vijiji 54, vijiji sita tayari tumekwishawasha umeme, vijiji viwili wanasubiri ratiba ya Mbunge tukawashe umeme kwa wananchi na kuna vijiji 21 tayari nguzo zimekwisha simikwa na kazi inaendelea. Pia yako makubaliano ambayo tumekubaliana na mkandarasi huyo chini ya REA na ninyi wenzetu wa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachoomba niwashauri kwenye eneo hili la REA katika maeneo matatu.

Mheshimiwa Spika, ushauri wa kwanza, makubaliano tuliyokubaliana kwenye vikao vyetu na yule mkandarasi ayatimize, na ayatimize kwa kasi; na tukiona hayaendi kama tulivyokubaliana tunaomba msisite kuchukua hatua nyingine za kisheria ili kazi zikamilike na wananchi wa Korogwe waweze kupata umeme.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, tumesema kuhusu vitongoji. Mimi Korogwe tuna vitongoji 610. Kwenye hotuba yako Mheshimiwa Waziri kwenye ukurasa wa 36 umesema vizuri kwamba tunahitaji shilingi trilioni 6.7 ili kukamilisha kazi ya kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote ambavyo havina umeme. Fedha hii ni nyingi sana, na wewe mwenyewe umesema tukienda kwa utaratibu wa kawaida tunaweza kuchukua miaka 20. Hata hivyo, kwenye kitabu chako umetuahidi kwamba mnakamilisha mpango wa kupeleka umeme kwenye vitongoji hivi angalau ndani ya miaka mitano kazi iwe imekamilika.

Mheshimiwa Spika, ninamwomba Mheshimiwa Waziri kazi hiyo waifanye kwa kasi. Kuna vijiji ambavyo vina vitongoji vikubwa na vina hadhi hata ya kuwa vijiji havijapata umeme. Kama shida ni fedha kaeni Serikalini huko wekeni utaratibu na ifanyeni hii kama mradi kama ilivyo miradi mingine. Kama tulivyo na mradi wa kupeleka vijijini tuwe pia na mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji vipate umeme tuwe tumemalizana na jambo la umeme kwenye vijiji na kwenye upande wa vitongoji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ambalo nilitaka nimshauri Mheshimiwa Waziri na wizara na hili kwa kiasi mmeanza kulifanyia kazi ni hii namna ya kupata wakandarasi. Utaratibu uliozoeleka na ambao umekuwa ukitumika mkandarasi anapatikana kwa njia ya ushindani. Mnazingatia vigezo vya kifedha na vigezo vya kitaalamu kwa maana ya vigezo vya kiufundi. Huo ndio utaratibu ambao umekuwa ukitumika muda mrefu na kiukweli ndio ambao umehusika kutuchelewesha kufika hapa tulipofika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, tumeona maelekezo yako kwa REA kwamba vigezo hivi viwili visiwe vigezo pekee vya mkandarasi kupata kazi ya kupeleka umeme vijijini. Pamoja na kuangalia uwezo wa kifedha, uwezo wa kitaaluma na uwezo wa kiufundi umewambia REA waangalie historia ya Mkandarasi, utendaji kazi wake kwenye miradi mingine ambayo tayari alishaifanya huko nyima au ambayo anaendelea kuifanya. Ninashukuru nimesikia angalau REA wamesema kwa saa ili mkandarasi apewe kazi nyingine au mpya afike angalau asilimia 60 au 80. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachoomba jambo hili lisiwe maneno likasimamiwe vizuri ili litusaidie kuendelea kupata wakandarasi wazuri ambao watafanya kazi vizuri ya kupeleka umeme kwenye maeneo ya vijiji vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo nilitaka kulichangia kidogo ni eneo la gesi. kipekee tumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kukubali na kufufua tena ndoto za watanzania kufanya kazi ya utafutaji na uza.ishaji wa gesi ndani ya nchi yetu. Manufaa ya gesi ni makubwa, tangu Mheshimiwa Rais alipoamua mwaka 2022, nchi yetu sasa imeanza kukaribia kuingia kwenye ramani na kwenye nchi za uchumi wa gesi na mafuta. Tunampongeza sana Mhe shimiwa Rais kwa jambo hili kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niseme, jambo hili limesemwa vizuri na hata kwenye hotuba Mheshimiwa Waziri amelieleza vizuri. Halikufikia maamuzi haya kwa bahati mbaya jambo hili ni la muhimu sana na lina sababu. Sababu ya kwanza ni Mheshimiwa Rais mwenyewe kutengeneza mazingira wezeshi na mazingira rafiki ya uwekezaji kwenye nchi hii hasa kwenye eneo la gesi, tunampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili, jambo la gesi halikwepeki. Duniani sasa hivi gesi ni sekta inayokua kwa kasi. Sekta ya gesi inakuwa kwa zaidi ya asilimia 7.5 kwa mwaka sio jambo la kudharau. Vile vile, mahitaji ya gesi yamekuwa ni makubwa sana. Hata hivyo, kwa tafiti na taarifa tulizonazo tuna gesi za kutosha lakini pia tuna faida ya jiografia yetu. hapa tulipo ni rahisi kutoa gesi hapa kwa urahisi zaidi na kuipeleka maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachoomba nishauri mambo mawili kwenye eno hili la gesi. kwanza, Mheshimiwa Waziri umesema kwenye hotuba yako ukurasa wa 50 kwamba mnaelekea kukamilisha kazi kudurusu mkataba kifani. Niwaombe sana jambo hili lifanyike kwa haraka ni jambo muhimu. Mkataba huu utatusaidia kutuwekea uwazi wa sisi tunafaidika nini? Nini wanafaidika wenzetu lakini pia itatuondolea uwezekano wa yeyote anayekuja kwenye Serikali au kwenye nafasi za Serikali kuamua anachokitaka kwa sababu tayari mkataba huu unao mwongozo wa kunufaika na mapato haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili nataka nishauri. Ukisikiliza michango humu ndani, ukamsikiliza Mheshimiwa Waziri, ukawasikiliza watendaji wa Wizara kuhusu jambo la gesi linasemwa kwa matarajio makubwa na faida kubwa na watu wana matumaini makubwa. Vile vile, gesi hii kuna hatua. Niwaombe jambo moja tu la muhimu sana, jiandaeni kama Serikali kufanya expectation management. Watu huko wanajua matrilioni, mabilioni yanakuja lazima wajue kuna hatua za kwenda, kuna hatua za kufuatwa mpaka uchimbaji unaanza na kunufaika moja kwa moja kunaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake, wanafanya kazi nzuri, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitumie nafasi hii kuzungumza mambo machache; kule Korogwe tuna barabara inaitwa Korogwe – Dindira – Bumbuli – Soni, ni barabara ya kilometa 77. Kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010 ambayo ninayo mkononi hapa, kwenye ukurasa wa 48 kulikuwa na ahadi ya kufanya usanifu kwenye barabara hii. Kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015, kwenye ukurasa wa 58 kuna ahadi ya chama chetu kwenda kutengeneza barabara hii kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipoingia kwenye Bunge lililopita, kwa maana ya Mkutano wa Kumi na Nne, niliuliza swali, Mheshimiwa Waziri akaniambia wametenga shilingi milioni 130 kwa mwaka huu wa fedha unaoisha Juni kwa ajili ya usanifu, lakini mpaka sasa hivi hela zile hazijafika, na usanifu umeshafanyika kwenye kilometa 20 za kutoka Soni kwenda Bumbuli, bado kipande cha kutoka Bumbuli – Dindira – Korogwe na ahadi hii imekuwa ni ya muda mrefu kwa watu wa Korogwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia kitabu cha Mheshimiwa Waziri, nimeona kwenye ukurasa wa 181 kuna hela, bilioni sita, wametenga kwa ajili ya barabara pale, wamesema kuanza matengenezo ya lami. Hata hivyo, nilipokwenda ndani zaidi kwenye kitabu, kwenye ukurasa wa 275 wametenga shilingi milioni 770 kwa ajili ya ukarabati, lakini wameweka kwenye ukurasa wa 317 wametenga shilingi milioni 140 kwa ajili ya usanifu. Kwa ukubwa wa kilometa zilizobakia, shilingi milioni 140 haiwezi kutosha kukamilisha shughuli ya usanifu kwenye barabara ile, hata ile 130 ambayo bado haijafika ikija haiwezi kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba matengenezo ya barabara hii ni muhimu, lakini kwa kuwa watu wa Korogwe wamekuwa na kiu ya barabara hii kwa muda mrefu na ni ahadi ya chama chetu; ni ahadi ya viongozi wa Serikali akiwemo Mheshimiwa Rais, akiwemo Mheshimiwa Waziri Mkuu, nimwombe Mheshimiwa Waziri, kama hatuna mahali pengine pa kupata fedha ya kukamilisha usanifu ili tuanze kujiandaa kwenda kujenga, basi hizi 770 tupeleke kwenye usanifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu tumefanya matengeneo na nimpongeze Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Tanga, Enineer Ndumbaro, anafanya kazi nzuri sana, sisi Wabunge wa Mkoa wa Tanga tunaisifia kazi yake, anafanya kazi nzuri sana. Mwaka huu tumefanya matengenezo, sehemu iliyobakia ni maeneo machache yaliyobaki, nina hakika hizi milioni 140 na zile milioni 60 nyingine wametenga zinaweza kutosha kumaliza hii kazi. Hebu hizi milioni 770 tupeleke kwenye usanifu ili kazi ya usanifu ikamilike, halafu tuendelee na kutafuta hela kwa ajili ya kutengeneza barabara kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ya Old Korogwe kwenda mpaka Magoma ambayo inakwenda kuunganisha mpaka na wenzetu wa Mkinga, ni barabara muhimu, lakini haijawahi kufikiriwa kuwekwa kwenye kiwango cha lami. Tunaomba sana Serikali iikumbuke hii barabara. Pia nawakumbusha watu TANROADS wameweka alama za X kwenye nyumba za watu na kuna wengine wamekaa miaka mingi kama watu wa pale maeneo ya Kerenge Kibaoni waende wakapewe elimu juu ya hatma ya makazi yao pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipongeze sana Shirika la Reli kwa kazi kubwa ya kufufua hii reli, reli ya kutoka Tanga kwenda mpaka Moshi na sehemu ya Tanga- Same imeshakamilika. Ninachoomba tu, SGR wakati ukifika watukumbuke, lakini kwa sasa hivi yale maeneo ambayo kuna makazi ya muda mrefu, watuwekee vivuko ili wananchi waweze kuvuka kutoka upande mmoja wa reli kwenda upande mwingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Nditiye na kaka yangu Engineer Ulanga wamefanya kazi kubwa kule Kizara tulikuwa na shida ya mawasiliano, lakini bado yako maeneo nimeyapeleka kwao maeno ya Lewa, Lutindi, Makumba na Kata ya Mkalamo, tunaomba watupelekee huduma ya mawasiliano kwa ajili ya watu wetu pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, muda sio rafiki sana. Kuna jambo limezungumzwa hapa na kiti chako kimeshalisemea. Tunazungumza yapo malalamiko kwamba kwa nini Wakala wa Ndege amehamishwa kwenda kwenye Ofisi ya Mheshimiwa Rais? Lazima tukumbuke nchi yetu inaongozwa kwa mujibu wa sheria za nchi yetu aliyepewa dhamana ya kuongoza Taifa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hawa walio chini yake wanamsaidia na hata ukiosoma Presidential Affairs inaeleza, hakuna dhambi kwa Rais kuamua kazi ipi ya Serikali isimamiwe chini ya Wizara ipi au ofisi ipi siyo dhambi. Ni vibaya kusema kwamba Rais amefanya makosa au ana nia ovu, sheria inamruhusu, hakuna sheria inayovunjwa ni utaratibu wa kawaida. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu kwenye bajeti hii muhimu sana kwa maisha ya Watanzania na maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametupa uzima, lakini na mimi kipekee nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri, lakini kipekee sana niipongeze sana Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri ambayo inaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye bajeti ambayo imewasilishwa kuna ongezeko la fedha kwenye upande wa fedha za maendeleo kwa asilimia 13.7. Jambo hili ni jambo kubwa, ni jambo zuri, tunaipongeza Serikali kwa kuwa tunajua tunaongeza nguvu ya kwenda kutatua changamoto tulizokuwanazo kwenye sekta mbalimbali zinazosimamiwa na Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe mchango kwenye maeneo matatu. Eneo la kwanza ni reli, eneo la pili barabara nae neo la tatu ni bandari.

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa reli niipongeze Wizara, lakini nilipongeze Shirika la Reli kwa kazi kubwa na kazi nzuri inayofanyika kwa upande wa reli. Tumeshuhudia ukarabati mkubwa kwenye reli yetu ya zamani; reli ya Dar es Salaam mpaka Moshi, reli ya Moshi – Arusha, lakini pia na ile ya kutoka Mwanza inayokwenda mpaka kwa wenzetu wa Uganda. Kazi hii ni kubwa, kazi hii ni nzuri, tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na tunapopongeza sio kwamba tunapongeza tu, tunapongeza kwa sababu kazi tumeiona na kuna sababu za kupongeza. Sio tu kwenye kukarabati hii reli ya zamani, lakini hata ukusanyaji wa mapato kwa shughuli zinazosimamiwa na Shirika la Reli umeongezeka kutoka bilioni 30 mpaka bilioni 50 sio jambo dogo tunawapongeza sana, lakini kubwa kwa upande wa reli tunaendelea kuipongeza Serikali na Wizara kwa kazi kubwa ya ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Standard Gauge alipoingia Mheshimiwa Rais kulikuw na hofu, kulikuwa na maneno, wengine walikuwa na hisia kwamba pengine miradi mikubwa ya kimaendeleo ambayo ameikuta kasi ya utekelezaji wake itapungua. Mheshimiwa Rais amechukua nchi akakuta kuna vipande vile viwili, lot zile mbili ya kwanza na ya pili, lakini leo tunapozungumza kazi inakwenda vizuri kuna mikataba imesainiwa, tumeona kazi imeanza kufanyika. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuhangaika na miradi hii mikubwa ambayo aliikuta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo machache ya kushauri kwa upande wa reli. Niwashauri sana wenzetu wa reli, Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo juu ya reli ya kutoka Tabora kwenda Kigoma inayokwenda mpaka DRC. Ni reli muhimu sana kwa uchumi ukiangalia kwamba DRC ni eneo muhimu sana kiuchumi na kwenye soko. Tuwaombe sana maagizo yale ya Mheshimiwa Rais myafanyie kazi kwa haraka ili kazi ya reli kwa kipande hiki ianze tuweze kuliwahi soko hilo la DRC. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini eneo la pili, tumefufua reli ya zamani, tumefanya ukarabati mkubwa, yapo maeneo mengine ambayo bado, ikiwemo reli ya kutoka Kilosa – Malinyi ambayo muda mrefu iliachwa. Ni reli muhimu kuongeza thamani na kazi ya reli ya SGR, lakini pia ukumbuke reli hii ndio kuna makutano kati ya reli ya kati na reli ya TAZARA. Tungeomba sana Wizara muweke kwenye mipango yenu jambo hili liweze kufanyika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho la kushauri kwenye upande wa reli, hii kazi nzuri mnayofanya ya kufufua reli hii ya zamani, yako maeneo ya reli yaliachwa, yako maeneo ya reli yalikuwa hayafanyiwi kazi wananchi wetu waliingia wakafanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo ikiwemo shughuli za biashara. Natoa mfano wa eneo la Mombo kule Korogwe Vijijini, niwaombe sana wenzetu wa reli yale maeneo ni muhimu. Kwa yale maeneo ambayo hakuna madhara kwa wananchi wetu kuendelea kufanya shughuli za kujipatia kipato ruhusuni wananchi wetu wafanye shughuli za kujipatia kipato tuweke utaratibu mzuri wa namna gani watu wetu watatumia maeneo haya kujipatia kipato na sio kuwaondoa kabisa ili tuendelee kuwapa Watanzania mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao za kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ninalotaka kuchangia ni eneo la upande wa barabara; wiki mbili zilizopita niliuliza swali Bungeni kuhusu barabara ya kutoka Korogwe – Dindira – Bumbuli mpaka Soli; na yale majibu niliyopewa nilisema kama majibu ni haya tukifika kwenye bajeti hatutaelewana hapa ndani. Kipekee kabisa nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri, nimesoma hotuba yako kwenye ukurasa wa 162 nimekuta umetenga fedha shilingi bilioni moja ya kuanza maandalizi ya kuanza ujenzi wa lami wa barabara ya kutoka Korogwe – Dindira – Bumbuli mpaka Soli, nikupongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nisingeiona hii hali ingekuwa tofauti hapa leo, lakini nikupongeze niseme tu kwamba, jambo hili tumelisubiri muda mrefu. Ni ahadi ya Chama cha Mapinduzi kwa zaidi ya chaguzi mbili. Umefika wakati sasa wa kukiheshimisha chama chetu kwa kutekeleza ahadi hii kwa Watanzania ili wananchi wa Korogwe na Lushoto waendelee kuwa na imani na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni barabara hii muhimu sana ya kutoka Korogwe – Mashewa – Bombo Mtoni – Mabokweni na kwenda mpaka Tanga. Barabara hii ni barabara muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu, lakini kwa ulinzi na usalama wa nchi yetu. Hii ni barabara mbadala ambayo mtu aliyetoka Kenya akipita Horohoro sio lazima aende Tanga, aje Muheza kuja Korogwe kwenda Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha. Kupitia barabara hii mtu anayetoka Kenya akitoka Horohoro anaweza kupita barabara hii ni barabara mbadala. Ni muhimu sana kwa ulinzi na uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, Wizara mlituahidi kwamba, mtatenga shilingi bilioni mbili kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii, mpaka sasa kuna ukimya mkubwa. Wakati wa kuhitimisha bajeti yako Mheshimiwa Waziri ningefurahi kusikia nini kinachoendelea kwenye barabara hii kulingana na umuhimu wake mkubwa iliokuwanao kwa ajili ya uchumi wa watu wa Tanga, Kilimanjaro, Arusha, lakini na uchumi na ulinzi na usalama wa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho napenda kuchangia ni eneo la bandari, kipekee niipongeze sana Serikali. niipongeze Mamlaka ya Bandari na watendaji wake kwa kazi nzuri mnayoifanya, kwa miaka zaidi ya sita bandari imekuwa ikijiwekea lengo la makusanyo ya shilingi trilioni moja kwa mwaka mmoja wa fedha, lakini kwa miaka zaidi ya sita hatujawahi kufika wala kukaribia, tumejitahidi sana bandari imeishia kwenye shilingi bilioni 800. Nimesoma hotuba yako Mheshimiwa Waziri, nimeona tuna bilioni mia tisa kasoro kidogo mpaka mwezi Aprili. Nina uhakika kazi ikifanyika vizuri kwa mwezi huu wa tano na mwezi wa sita inawezekana kwa mara ya kwanza tukafikia mipango na malengo tuliyojiwekea ya kufika angalau shilingi trilioni moja kwenye mwaka mmoja wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaongeze sana bandari kwa kazi hii nzuri ambayo mmeifanya. Tunajua kazi hii ni kubwa, lakini endeleeni kuifanya tunawategemea bandari ni eneo muhimu katika mapato na uchumi wan chi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia niipongeze Mamlaka ya Bandari. Mmefanya kazi nzuri kwenye bandari ya Tanga kwenye kuongeza kina na kupanua eneo lile la kufanyia shughuli za bandari, mmefanya kazi nzuri sana na sisi tunawapongeza watu wa Tanga kwa kazi mliyoifanya. (Makofi)

Ombi langu kwenu watu wa bandari, baada ya kazi hii nzuri mliyoifanya na mnayoendelea kuifanya ya kuboresha Bandari ya Tanga, sasa ni wakati muhimu mje na mpango mahususi wa masoko namna gani ya kuongeza mizigo inayopita kupitia Bandari ya Tanga, inayoingia na inayotoka kupitia Bandari ya Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatuoni sababu kwa nini mkonge wa Korogwe usafirishwe kwa gari mpaka Dar es Salaam upelekwe bandarini, upelekwe kwenda kutafuta masoko nje, hatuoni sababu. Ni wakati sahihi sasa mjitahidi kuongeza kuitangaza na kutengeneza mpango wa masoko kwa ajili ya bandari ya Tanga ili bandari ya Tanga iendelee kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine la pili kwa upande wa bandari. Tuna mfumo wetu wa Single Window System, unafanya kazi, unatusaidia kuondoa na kuingiza shehena kwenye maeneo yetu ya bandari na maeneo yetu ya mipakani, lakini kumekuwa na changamoto. Ni wakati sasa Serikali iangalie namna ya kuboresha mfumo huu ili tusihangaike na network inatupotezea muda mrefu inatuchelewesha kuweza kuongeza muda wa kusafirisha bidhaa zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mara nyingi system inasumbua na system ikiwa chini maana yake uondoaji wa shehena unachelewa. Ni wakati sasa wa kuangalia namna nzuri na mkakati mahususi wa kuboresha system hii ili mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kwenye system hii sehemu kubwa ya uchakataji wa taarifa zote iko centralized makao makuu. Ni wakati pia wa kuangalia kwenye bandari kama ya Tanga, bandari kama ya Mtwara, sio lazima taarifa zichakatwe makao makuu, tufanye decentralization ya huu mfumo ili na kwenye bandari husika Mtwara, Tanga, taarifa zichakatwe, sio wachakate Dar es Salaam wamalize watume, watu wa Tanga wakati mwingine inachelewesha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nashukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya Eneo la Pori la Akiba Kigosi Kuwa Hifadhi ya Taifa Kigosi pamoja na Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji wa Hadhi Sehemu ya Eneo la Pori la Akiba la Igalla Kuwa Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki (Minamata Convention on Mercury)
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana kunipa nafasi niweze kuchangia na kwa ujumla mambo mengi yameshazungumzwa na Wabunge wengine waliochangia, lakini nitumie nafasi hii kwanza kabisa kusema naunga mkono maazimio yote yaliyoletwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuunga mkono maazimio yaliyoletwa na Serikali, pia nitumie nafasi hii kuipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa wanayoifanya hasa watu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ulinzi mkubwa wa rasilimali zetu, hata ongezeko la tembo mpaka wanakuja kwenye makazi ya watu sasa hivi ni matokeo ya kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya kazi kubwa mliyoifanya ya kuhifadhi na tembo wamekuwa wengi basi mtusaidie kwenye yale maeneo kama kule Korogwe tumeathiriwa sana na tembo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaunga mkono, nichangie kwa upande wa maazimio haya mawili ya kubadilisha hadhi Mapori ya Akiba ya Ugalla na Kigosi kuwa Hifadhi za Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ziko faida nyingi sana kupandisha hadhi mapori haya na tunajua kwamba Hifadhi ya Taifa ni hatua ya juu kabisa ya uhifadhi kwa maana kwenye Hifadhi ya Taifa haturuhusu shughuli nyingine za kibinadamu, kwa hiyo kwa mapori haya kupandishwa hadhi kuwa Hifadhi ya Taifa tutakuwa tumeimarisha ulinzi wa rasilimali zetu, ikiwemo wanyama na baionuwai nyingine kwenye maeneo haya ya mapori.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaipongeza sana Wizara na tunaunga mkono azimio hili kwa sababu ni jitihada za kwenda kuongeza na kuimarisha ulinzi wa rasilimali zetu, lakini pia iko faida nyingine ya kupandisha hadhi mapori haya na kuwa Hifadhi ya Taifa. Faida nyingine kubwa ni kwenda kusaidia kuongeza mchango kwenye Pato la Taifa, lakini pia kwenda kugusa maisha ya watu wetu, hasa kwenye maeneo ambayo yanapakana na hifadhi hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo nyuma tulikuwa tunapiga kelele kidogo baadhi ya watu kwenye mambo kama ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Chato, sasa kwa kazi kubwa inayofanywa na Serikali sasa hivi ya kuimarisha miundombinu kama ujenzi wa viwanja wa ndege, kama reli ya SGR, kama ujenzi wa barabara, lakini pia kufufuliwa kwa shirika letu la ndege ni sehemu ya kutusaidia kwenda kuongeza pato kwa maana inakwenda kuchocheo utalii kwenye hifadhi hizi ambazo zitakwenda kuanzishwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi naunga mkono maazimio hayo, lakini naomba nishauri kwenye maeneo mawili, TANAPA ina hifadhi 19 na jambo hili limesemwa sana na tunaomba tuliweke msisitizo kidogo, tukichukua azimio tulilopitisha jana na haya mawili ya leo na yakienda kupita na hifadhi hizi zikianzishwa tutakuwa na jumla ya hifadhi 22 na hifadhi zinazoweza kujiendesha ni hifadhi tano. Kwa hiyo, unaweza ukaona huo mzigo wa kuendesha hifadhi nyingine ulivyokuwa mkubwa kwa TANAPA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yale majibu mazuri sana ya kitaalamu aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri wa Maliasili jana, lakini tunaomba tushauri vitu viwili, kitu cha kwanza, ni lazima Wizara iisimamie TANAPA vizuri na iwaelekeze waongeze Mkakati madhubuti wa kutangaza masoko ili kusaidia hifadhi hizi mpya zinazoanzishwa tusichukue muda mrefu sana zikaendelea kuwa tegemezi, ziweze kuanza kuingiza mapato vizuri na ziweze kuweza kujiendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili ni kwenye mzigo wa kodi, lilisemwa jana, lakini hata mama yangu Mheshimiwa Lulida amelizungumza hapa. TANAPA wanalipa kodi nyingi, TANAPA wanalipa asilimia 15 wanatoa asilimia 15 ya gawio kwenda Serikalini, malipo ya asilimia tatu kwenda kwenye tourism development levy, wanalipa skills development levy, lakini pia wanalipa cooperate tax, lakini hayo yote siyo shida ile miradi wanayofanya kwa ajili ya kusaidia jamii ambazo zinapakana na Hifadhi za Taifa na yenyewe inakuwa inatozwa kodi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimuombe sana Mheshimiwa Waziri tunaunga mkono azimio hili, ni azimio zuri litatusaidia kuimarisha maliasili zetu, litatusaidia kuongeza pato la Taifa lakini...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: ...salama nipongeze mkakati wa kuweza kutangaza vivutio vyetu ili waongeze utalii kwenye maeneo yetu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri, lakini na kazi wanayoifanya yeye na Manaibu Waziri.

Mheshimiwa Spika, nina mambo machache sana leo ya kuzungumza, mambo kama mawili tu. Jambo la kwanza ningeomba kuchangia kwenye kilimo cha mkonge, kwa mwaka 2014 - 2018 kwenye mkonge tumezalisha tani 190,649. Katika hizo Mkoa wa Tanga peke yake umezalisha tani 106,221 na katika Mkoa wa Tanga Wilaya inayoongoza kwa kuzalisha mkonge ni Wilaya ya Korogwe hasa Halmashauri ya Korogwe. Hata hivyo, tumekuwa na changamoto kadhaa kwenye zao la mkonge, changamoto kubwa ya kwanza ni usimamizi usioridhisha wa taasisi inayosimamia zao la mkonge. Pia ushiriki mdogo wa taasisi zetu za utafiti kama ile ya pale Mlingano kwenye kusaidia kuendeleza zao la mkonge.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tumekuwa na wakulima wadogo wengi kule Korogwe na Mkoa mzima wa Tanga, lakini tuna changamoto kubwa sana. Wakulima walio wengi hata mbegu wanaokota kutoka kwenye mashamba ya mkonge ya muda mrefu kwenda kupanda kwenye mashamba yao. Mbegu hizi zinafanya mkonge huu usiweze kuwa na muda mrefu wa kuvunwa lakini tungeweza kuvitumia vizuri vyuo vyetu vya utafiti na taasisi za utafiti kama pale Mlingano tungeweza kuwa na mbegu bora na wakulima wetu wangelima na wangeweza kuvuna mkonge kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, inawezekana changamoto kubwa inayotusumbua ni fedha. Kwenye zao la mkonge kwa miaka mingi tunapata service levy ya 0.3%, lakini kwa mujibu ya Sheria ya Fedha kwenye mazao haya ya biashara tunapaswa pia kuwa na ushuru wa mazao produce cess lakini kwa mujibu wa Sheria ya Fedha produce cess anayepaswa kuilipa ni mnunuzi.

Mheshimiwa Spika, sasa wakulima hawa wakubwa wa mikonge ambao wanazalisha singa wenyewe mnunuzi wanamkuta nje, ambapo kule nje wanamkuta wakala hakuna nani ambao; kwa hiyo ni vigumu sana kupata produce casse wanapoleka mkonge kule nje; na hata halmashauri zetu zimekuwa zikikosa sana mapato kwa sababu hii.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia vizuri kama tungekuwa tunapata produce cess 2014 mpaka 2018 tungepata zaidi ya bilioni tisa kwenye produce cess peke yake. Kwenye service levy tumepata takriban shilingi milioni sita na kitu. Nilikuwa naiomba sana Serikali tuangalie namna, hapa hatuombi kuibua kodi mpya, hii kodi ipo kwa mujibu wa sharia. Changamoto tuliyonayo ni namna ya kupata fedha hizi; kwa sababu mnunuzi anayepaswa kulipwa yuko nje ya nchi na hajumo ndani ya nchi.

Mheshimiwa Spika, tuna mfumo mpya sasa hivi; na ninampongeza sana Mheshimiwa Mkuu wetu wa Mkoa wa Tanga, ametusadia sana na ametusaidia kupata haki na faida kwa wakulima wadogo wa mkonge. Tuna wakulima wadogo wa mkonge ambao wanauza mazao yao ya mkonge kupitia vyama vyao vya ushirika na mnunuzi anapatikana kwa kushindanishwa kwenye mnada. Sasa tunapopata mnunuzi anayeshindanishwa kwenye mnada ananunua mazao ya wakulima hawa wadogo wa mkonge yule mnunuzi analipa produce cess kwa sababu yeye anakuja kununua ndani; lakini hawa wakulima wakubwa wanaopeleka nje hawalipi, hatimaye hii ita-discourage hawa wanunuzi wanaokuja kununua mazao ya wakulima wadogo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mnzava.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, mkonge; pamoja na mchango wangu wa kuzungumza naomba nishauri Serikali kwa Wizara ya Kilimo na Fedha kukaa pamoja ili kuweka kwenye Finance Bill kipengele cha namna ya kutoza produce cess kwa wakulima wote wakubwa wanaosafirisha nje mkonge ili tusiwavunje moyo wanunuzi wanaokuja kununua mkonge wa wakulima wadogo. Pia fedha hizi zitasaidia utatuzi wa changamoto za zao la mkonge.

Mheshimiwa Spika, chai; kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa pembejeo kwenye zao la chai. Jambo linalowalazimisha wakulima kukopa pembejeo kwa wenye viwanda na kuwaathiri kwenye bei. Ushirika katika chai uimarishwe , pia tuanzishe soko au mnada wa chai hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, umwagiliaji; ili kuwaondoa katika umaskini wananchi wa kata 10 za Tarafa ya Mombo ni kutekeleza Mradi wa Umwagiliaji wa Bonde la Mto Mkomazi. Bwawa linaloweza kusaidia kilimo cha umwagiliaji kwenye hekta zaidi ya 5,000.

Mheshimiwa Spika, Bodi ya Mkonge, kumekuwa na udhaifu mkubwa wa usimamizi wa mkonge kwa sababu ya uwezo mdogo wa Bodi ya Mkonge. Nashauri bodi iangaliwe upya. Pia Serikali ifuatilie utaratibu uliotumika kutoa mashamba ya mkonge. Pia namna mali za Bodi ya Mkonge zilivyouzwa au kugawanywa ili kujua Bodi ilikuwa na mali gani, zimekwenda wapi na kwa utaratibu upi?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, hoteli zote zilizokuwa za Serikali zilizopewa, zilizokodishwa au zilizouzwa zifuatiliwe mikataba yake na utekelezaji wa mikataba kwa kuangalia hali za hoteli hizo na utendaji kazi wake kwani hoteli nyingi zinaonekana kuwa na hali mbaya na haziingizii faida Serikali na nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, TFS iendelee kuimarisha ushirikiano wake na jamii kwa kuondoa migogoro iliyopo kati yake ni vijiji kama kule Korogwe kwenye Hifadhi ya Nilo na Msitu wa Chang’andu, Kata ya Kwalukonge.

Mheshimiwa Naibu Spika, TFS na Wizara kuendelea kuacha kiwanda cha mazao ya misitu cha TAMISO CHIPBOARD ambacho bado kina mashine nzuri kimeendelea kuchezewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, utetezi wa TFS na Wizara kuwa kiwanda hicho kinaangaliwa na Msajili wa Hazina sio sawasawa kwani hata uanzishwaji wa kiwanda hiki ulikuwa maalum kwa ajili ya mazao ya misitu ya shamba la miti la Shume na Gologolo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuendelea kukitelekeza kiwanda hiki ni matumizi mabaya ya fedha za nchi na kufifisha nia na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kazi nzuri ya kupambana na ujangili kumekuwa na ongezeko kubwa la tembo na wanyama wakali. Je, mamlaka zinazohusika zimejiandaaje kupambana na ongezeko hilo?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara ya Nishati kwa kazi kubwa wanayofanya hasa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini (REA). Hata hivyo kasi ya utekelezaji wa mradi huu hasa kwenye Wilaya ya Karagwe na Jimbo la Korogwe Vijijini sio ya kuridhisha. Kwenye mradi huu kwenye Awamu III mzunguko wa kwanza Korogwe ilipangiwa vijiji 16 mpaka sasa umeme umewashwa kwenye vijiji saba tu.

Mheshimiwa Spika, tulileta maombi ya kupelekewa umeme kwenye vijiji 67 katika Mradi wa REA, awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza. Ni vyema Wizara ituambie baada ya bajeti hii tutapata umeme kwenye vijiji hivyo vyote au hapana?

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na shida ya kuunganisha umeme kwa wakati, viko Vijiji vya Kulasi, Kibaoni na Mswaha Majengo vimesimikwa nguzo tangu mwaka 2018 mwezi Oktoba, lakini mpaka sasa umeme haujafika katika vijijji hivyo. Mkandarasi anasema tatizo ni tofauti ya transformer kati ya size inayotamkwa kwenye mkataba ambayo ni 33 kv na size ya line iliyopo ambayo ni 11 kv. Tofauti hii haijafanyiwa kazi muda mrefu na kusababisha malalamiko.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri alipofanya ziara Korogwe tarehe 19 Mei, 2019 alitoa maelekezo kuwa Kijiji cha Mahenge kipelekewe umeme. Umeme huo unatoka Kijiji cha Kerenge Kibaoni, Jimbo la Korogwe Vijijini lakini kuna vitongoji viwili vya Antakae na Mianzini vinapitiwa na umeme huo ukienda Mahenge. Naomba sana vijiji hivi visirukwe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kama kijana wa Kitanzania kiongozi nasimama kwa uchungu sana kwa yanayoendelea ndani ya Bunge letu. Tunapofanya siasa na kuchafua sura ya Taifa letu badala ya kulitetea na kuliweka vizuri Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, muda ni mchache, nizungumze mambo machache. Jambo la kwanza nizungumze nafasi ya haki za binadamu kwenye mahusiano ya Kimataifa. Nakubaliana kabisa kwamba haki za binadamu zina nafasi kubwa kutuweka kama Taifa kwenye sura nzuri kwenye ulimwengu huu, kwenye mahusiano yetu na nchi nyingine na Mataifa mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu ambacho tunasahau, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache sana ambazo zinatii na kufuata haki za binadamu. Ni miongoni mwa nchi chache sana ambazo haki za binadamu hazitajwi tu, tumeziweka kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sura ya Kwanza, sehemu ya tatu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika…

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hayo…

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Kwenye nchi yetu tunazo sheria zilizotuwekea utaratibu, tunayo institutional and legal framework ya namna… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, muda hautoshi.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Hakuna mtu ametoa taarifa, Mheshimiwa Salome naomba unyamaze. Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa naomba ukae nimeshasimama, naomba ukae. Waheshimiwa Wabunge tujifunze kuheshimu mamlaka…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Nasema hivyo kwa sababu, nisikilizeni. Mheshimiwa Susan Lyimo amechangia dakika zake tano hakuna mtu nimemruhusu kusimama, Mheshimiwa Lulida amechangia hakuna mtu amesimama na huyu mchangiaji wa CCM atachangia bila mtu kusimama. Mheshimiwa Timotheo Mzava. (Makofi)

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa hoja yangu ni hii, kwamba kwenye nchi yetu tunayo Katiba na tunazo Sheria za Haki za Binadamu na namna ambavyo mtu atakuwa anahisi haki za binadamu zimevunjwa, aende kwenye vyombo vya sheria kwenda kufuata haki hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kushauri vitu viwili; cha kwanza niishauri Serikali. Niiombe Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje semeni juu ya haya mambo, tusiache watu wakachafua nchi yetu. Mheshimiwa Kabudi ameenda Geneva, ametoa taarifa nzuri na amesifiwa lakini huku ndani watu hawajui.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili nataka kushauri, kwa kuwa tunayo legal na institutional framework ya namna ya ku-deal na mambo ya haki za binadamu, niwashauri wenzangu, Watanzania wote twende kwa namna hiyo, tuache kuzunguka kwenye maofisi huko mara kwenye Mabalozi, tunao utaratibu wa kisheria na kikatiba wa namna ya ku-deal na vitu vya namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze jambo la pili kwenye diplomasia ya uchumi. Diplomasia ya uchumi ni dhana pana na inawezekana tunapata shida sana kuielewa, niwapongeze sana Mabalozi wa nchi yetu ambao wanatuwakilisha kule nchi. Balozi wetu wa China, Balozi wa Urusi wanafanya kazi kubwa, matokeo tunayoyaona kwenye utalii sasa hivi ni matokeo ya kazi kubwa wanayoifanya kwenye diplomasia ya uchumi. Hata kitendo cha Zimbabwe kukubali tupeleke mahindi tani zaidi ya 700,000 kwenye ziara ya Mheshimiwa Rais ni matokeo ya diplomasia ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wasichoelewa ni kitu kimoja, Sera yetu ya Mambo ya Nje, Toleo la Mwaka 2001 imejisimika kwenye diplomasia ya uchumi, lakini haina maana kwamba kwa sababu ya diplomasia ya kiuchumi tumeacha vitu vingine na hata sera ile imesisitiza kwamba tunaendelea kuimarisha misingi na kanuni za sera yetu ya asili ile ya mwanzo ambayo ilitokana na Serikali ya Awamu ya Kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa kanuni za kwenye Sera yetu ya asili ya Mambo ya Nchi za Nje pamoja na kwamba ilikuwa ni kwa ajili ya kuangalia ukombozi wa nchi nyingine, ilikuwa ni kulinda uhuru wa Taifa hili. Kuja kwa sheria za kwenye Sekta ya Madini, mabadiliko tuliyoyafanya ni ishara ya kulinda uhuru wa Taifa kwenda kutafsiri diplomasia ya uchumi ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri tu Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje iendelee kutoa ushirikiano mkubwa kwenye mikataba na Mataifa mengine, kwenye mikataba ya wawekezaji ili katika kufanyia kazi mambo hayo, tujitahidi kuhakikisha kwamba na zile dhana zote zinazohusiana na mambo ya diplomasia na uhusiano wa mambo ya nje zinazingatiwa vizuri kwa kuondoa mikwaruzano na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze sana Serikali, tangu 2015 mpaka sasa tumeanzisha Balozi zaidi ya saba, mpaka juzi tumeanzisha Balozi nyingine ya Cuba. Kukubaliwa kuanzisha balozi kwenye nchi nyingine, yenyewe ni ishara kwamba tuna mahusiano mazuri na nchi nyingine. Hii dhana inayojengwa kwamba tuna mahusiano mabaya, watu wanatupotosha. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sana Serikali, waendelee kusimamia mahusiano na nchi nyingine, waendelee kusimamia diplomasia ya Tanzania kwenye Mataifa mengine. Sisi tunamwamini Mheshimiwa Profesa Kabudi, Mheshimiwa Dkt. Ndumbaro na tunamwamini Mheshimiwa Rais, wafanye kazi kwa niaba ya Watanzania, nchi yetu ipate sura nzuri mbele ya ulimwengu na dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nitumie nafasi hii kwanza kabisa kumshukuru Mungu lakini pia kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Naibu Waziri na Watendaji wao Wizarani wanafanya kazi kubwa, wanafanya kazi nzuri sana hongera sana kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja kwa mujibu wa tafiti mbalimbali duniani moja ya njia bora kabisa ya kuondoa kama sio kupunguza migogoro ya ardhi ni kupima na kupanga matumizi bora ya ardhi. Hii ndio moja ya njia bora kabisa pamoja na kwamba tunakubaliana kwamba kwa mujibu wa sheria zetu Planning Authority ni kule kwenye Serikali za Mitaa, lakini Wizara ndio yenye jukumu la kusimamia kutekeleza sera kwenye Sekta ya Ardhi. Naomba sana pamoja na changamoto za kifedha na za kibajeti watutafutie mkakati maalum wa kupima na kupanga maeneo yetu. Tume ya Mipango ya Ardhi inafanya kazi nzuri, lakini bado uwezo wake ni mdogo na imebaki kuwa kama waratibu tu.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kwenye mashamba yasiyoendelezwa. Nitumie nafasi hii kwa dhati kabisa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, tangu ameingia amefanya kazi ya kufuta hati za mashamba ya baadhi ya wawekezaji ambao hawayaendelezi vizuri na hata kule kwetu Korogwe, hili pia limefanyika pamoja na maboresho yaliyofanyika kwenye mashamba yale sita ambayo yalifutwa, bado alichokifanya Mheshimiwa Rais kinawasaidia sana watu wetu na sisi watu wa Korogwe tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ninayo mashamba mengine kule na nimeshamwambia Mheshimiwa Waziri zaidi ya mara moja na namwamini sana baba yangu na naikubali sana kazi yake, kama pale Wizarani kuna watu wanakwamisha yasifike kwa Mheshimiwa Waziri hebu aingie ndani aangalie kuna nini huko, kuna shamba la pale Mwakinyumbi, Hale. Nimekuja juzi kwenye Bunge lakini hii nazungumza ni mara ya tatu kama sikosei.

Mheshimiwa Spika, kuna shamba linaitwa Kwashemshi, kuna mwekezaji anasema yeye ni mwekezaji wa Mkonge, anakodisha kwa watu wengine, miaka miwili iliyopita alikuwa anakodisha kwa wananchi walime mahindi kule ndani kwa sababu eneo kubwa halijalimwa mkonge. Mwaka huu ameamua mpaka na kuwafukuza wananchi amechukua mtu binafsi amekuja analima mahindi kwenye shamba hilo, wananchi hawana maeneo.

Mheshimiwa Spika, mimi ni muumini ambaye naamini kabisa sio sawasawa kila ardhi ya mwekezaji tukaichukua tukagawa kwa wananchi, hatuwezi kuwa nchi ya namna hiyo, lakini lazima tukubaliane kama mtu amepewa ardhi haitumii kwa mujibu wa masharti aliyokabidhiwa masharti yake ya umiliki, wahukue hatua. Hili suala nimelisema muda mrefu, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aingie, najua kwake mara naambiwa halijafika, mara limefika likarudi, sielewi kinachoendelea hapo, hebu aangalie Mheshimiwa Waziri hapo kwenye Wizara, kuna mtu atakuwa anacheza na hivi vitu, kuna shamba linaitwa shamba la Mwakinyumbi.

Mheshimiwa Spika, huu ni mwaka sijui wa ngapi tunalalamika na hili jambo. Marehemu Profesa Majimarefu amepiga kelele sana humu ndani mpaka Mwenyezi Mungu amemchukua, hatujui kinachoendelea kwenye mashamba haya. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kwa unyenyekevu mkubwa na kwa kazi yake anayoiamini awasaidie watu wa Korogwe waweze kupata maeneo, lakini pia kazi zifanyike vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri jambo lingine hasa kwa niaba ya vijana wote lakini na Watanzania kwa ujumla, sasa ni wakati muafaka wa kuwa na sera ya nyumba. Ni wakati muafaka kama Taifa kuwa na sera ya nyumba, hebu Wizara walifanyie kazi hili jambo tuweze kufikia mahali pazuri.

Mheshimiwa Spika, yamesemwa hapa na nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi anayoifanya, ile kazi tuliyoikuta inafanyika Kilombero, Ulanga na Malinyi ilikuwa ni kazi nzuri sana nimpongeze yeye lakini niipongeze na ile timu iliyokuwa inasimamia ule mradi. Mheshimiwa Waziri kwenda kugawa hati ni sehemu ya namna ya kusadia kutatua changamoto za migogoro ya ardhi kwa watu wetu, hakuna kosa. Korogwe pia tukipima tutamwita Wziri aje atugawie hati na sisi tutapokea.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri anafanya kazi nzuri, sina maneno mengi, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nami nitumie nafasi hii kukishukuru sana Chama changu cha Mapinduzi na wananchi wa Jimbo la Korogwe Vijijini kwa kura nyingi na za heshima walizotoa kwa chama chetu na kuniwezesha nami kuwa mwakilishi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma vizuri mapendekezo ya Mpango, nimesoma vizuri mpango huu, naipongeza Serikali kwa kazi kubwa na hatua kubwa ambayo tumepiga mpaka sasa. Ila nilipokuwa nasoma Mapendekezo ya Mpango huu wa Awamu ya Tatu kwenye ukurasa wa 87 nimekutana na vipaumbele pale viko vitano. Ukisoma kuanzia kipaumbele cha kwanza, cha pili na cha tatu, huoni namna ambavyo unaweza ukaikwepa sekta ya kilimo kwenye kuendeleza na kukuza uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri sana Serikali, kwenye suala la kilimo, tunayo mambo mengi sana ya kufanya na mengi yameshazungumzwa, mimi naomba nizungumzie sana eneo la soko. Ni lazima Serikali ijitahidi kuweka uhakika wa masoko kwa wakulima wetu wanaolima kwenye nchi yetu hii. Tukiweka uhakika wa masoko tutasaidia viwanda vyetu, tutatengeneza ajira, tutaongeza pato kwa wale wakulima wanaolima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tulikuwa tunamwuliza Waziri Mkuu kuhusu mkakati tulionao kwenye mazao ya kimkakati, nikatoa mfano wa zao la mkonge. Wananchi wameitikia na wanalima sana, lakini tusipokuwa na uhakika wa soko kwa ajili ya mazao haya, mwisho wa siku wananchi watakuja kuishia kupata hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya njia ya kuweka uhakika wa soko ni kutengeneza viwanda na kushawishi wawekezaji kuwekeza kwenye sekta ya viwanda. Tunavyo viwanda kwa mfano kwenye zao la mkonge, tulikuwa na viwanda vya magunia, sasa hivi havifanyi kazi vizuri. Asubuhi kuna mtu amezungumza hapa kwamba wale wawekezaji ikiwezekana wanyang’anywe lakini ni lazima tujiulize hivi viwanda vya magunia vilikwama wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya magunia ni makubwa sana, lakini uzalishaji wa magunia ni mdogo, kwa nini? Ni gharama za uzalishaji. Siyo hivyo tu, pia magunia yetu yanakumbana na ushindani kutoka kwenye magunia yanayozalishwa kwa kutumia mazao mengine na bidhaa nyingine kama jute. Ukiangalia India na Bangladesh, wao wana subsidy kwenye jute na wanajitahidi sana kuwekea mfumo mzuri wa kununua mazao yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia East Africa Community, Sheria za Ushuru wa Forodha zinatoa nafuu ya kodi kwa bidhaa ambazo zinaingia kwa ajili ya kuchukua mazao na kutoa bidhaa na kuzipeleka nje kwa ajili ya ku-export. Haya yote ukiangalia yanafanya magunia ya jute yanakuwa na bei rahisi wakati magunia yanayozalishwa na mkonge yanakuwa na bei kubwa. Ukienda kwenye ushindani hatuwezi kupata faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze jambo linguine, tumejiwekea malengo, tumepiga hatua kidogo kwenye umwagiliaji na tumejiwekea malengo mpaka 2025 tufike hekta 1,200,000. Naiomba Serikali, lazima tuangalie miradi mikubwa ya umwagiliaji itakayotusaidia kuweza kuhudumia eneo kubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo tulikuwa nao Tanga, Bwawa la Mkomazi, mradi mmoja tu una uwezo wa kuhudumia hekta zaidi ya 6,000, lakini kwa zaidi ya miaka 10 wananchi wamekaa na matumaini wanasubiria miradi hiyo haitekelezwi. Naomba tuweke nguvu kwenye maeneo ya namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni la miundombinu. Kilimo kinafanyika vijijini, lakini miundombinu ni mibovu sana. Leo tunasema tuongeze uzalishaji kwa kuongeza maeneo ya kulima, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo na Waziri wa Kilimo wanajua, kwenye chai peke yake kwa mwaka, zaidi ya kilo milioni nne tunazipoteza, zinachelewa kufika kiwandani kwa sababu ya miundominu na zinapotea. Thamani yake ni karibu shilingi bilioni 2.8 kwa sababu ya miundombinu. Naungana na Mheshimiwa Nditiye, tunahitaji kuwa na nguvu na mkakati wa ziada kwenye suala la miundombinu, kutafuta fedha kuiongezea TARURA ili wananchi wetu wapate uhakika wa kupeleka mazao kwenye masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nipate fursa ya kuchangia maazimio haya mawili yaliyoletwa mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa nami niungane na wenzangu kutoa pole kwa Mheshimiwa Rais na Watanzania kwa ujumla kwa msiba mzito ambao ulitufika kama taifa wa kuondokewa na mpendwa wetu Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, maazimio haya yamekuja kwa wakati sahihi na ni jambo sahihi na ni jambo muhimu na kubwa sana kufanywa na Bunge lako Tukufu. Katika miaka sita ambayo Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amehudumu kama Rais wa nchi hii amefanya mambo makubwa, amefanya mabadiliko makubwa sana kwenye taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukisema tuanze kueleza kazi nzuri na njema alizofanya Dkt. Magufuli, hata muda huu haunitoshi kusema yote mazuri aliyoyafanya. Lakini kama Mbunge na kama Mbunge kijana, nianze kabisa kwa kutambua mchango na thamani kubwa ambayo Dkt. Magufuli aliitoa kwa vijana wa taifa hili kwa kuwateua kwenye nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya nchi yetu. Mheshimiwa Dkt. Magufuli aliwaamini sana vijana, aliwapa nafasi za kufanya kazi na kuitumikia nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika,inawezekana yako maeneo tumemuangusha kidogo lakini kwa sehemu kubwa vijana aliowateua walifanya kazi nzuri ya kumsaidia na kuleta uongozi kwenye taifa letu. Sisi kama vijana tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa imani hiyo kubwa kwa vijana. Amewatengeneza watu wengi kuwa viongozi na kuweza kutoa mchango kwenye taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kubwa zaidi alilofanya Dkt. Magufuli ni kutusaidia kukamilisha ndoto kubwa tulizokuwa nazo kama taifa kwa miaka mingi. Kwa muda mrefu tumekuwa na ndoto ya kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi yetu lakini tulikuwa tukisuasua kwenye utekelezaji wa jambo hili. Dkt. Magufuli kwenye kipindi chake amesimama imara jambo hili limefanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuishia kuhamishia tu makao makuu, alihakikisha kwamba Wizara za Serikali zinapata majengo mazuri na ya kudumu kwenye eneo la Dodoma ili Serikali iweze kufanya shughuli zake vizuri hapa Dodoma. Ni muhimu sana kuendelea kuenzi mchango huu. Pia amefanya kazi kubwa kwenye kusimamia rasilimali za taifa letu. Tulibadilisha sheria kwenye usimamizi wa madini na nchi yetu imeongeza thamani na imeongeza mapato kutoka kwenye rasilimali tulizokuwa nazo kama taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi nzuri alizofanya Dkt. Magufuli, lakini kwa mara ya kwanza kama kijana wa Kitanzania nimeona na kusuhudia kitu cha tofauti. Nimeona na kushuhudia baadhi ya watu wakifurahia kifo na kusema maneno yasiyokuwa mazuri. Kwa umri wangu mdogo, kwa nilivyolelewa kwa utamaduni wetu si jambo zuri sana kufurahia kifo cha mtu mwingine. Lakini pia si jambo zuri kukosoakosoa mtu akiwa ameshatangulia mbele ya haki. Ninawaomba Watanzania, Dkt. Magufuli ameifanya kazi yake vizuri, ameimaliza safari yake, amefunga kitabu chake. Tumpe heshima anayostahili, tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu amhifadhi mahali pema peponi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuondoka kwa Dkt. Magufuli tumempata mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kipekee kabla ya kumpongeza Mheshimiwa Samia ni lazima Watanzania tujipongeze kama taifa. Tumepita kwenye kipindi ambacho pengine kuna watu walikuwa wanatuangalia kama tutavuka salama au hatutavuka salama. Lakini leo tunapozungumza kwa uimara wa Katiba iliyotengenezwa na waasisi wa taifa letu, kwa uimara wa sisi Watanzania na kupendana kwetu, kwa uimara wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, kama taifa tunavuka salama na tunavuka vizuri. Tunayo sababu ya kujipongeza na kujivunia Watanzania, ni jambo kubwa ambalo tunaweza tukaliona kama ni jambo la kawaida, lakini ni jambo kubwa sana kuvuka kwenye kipindi kama hiki tukiwa salama na tukiwa tumeendelea kushikamana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kuendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Samia kwa kupata nafasi ya kuwa Rais wa Nchi yetu. Mheshimiwa Samia ana uzoefu mkubwa kama ilivyosemwa na aliyewasilisha hoja ya Azimio la Kumpongeza. Ana uzoefu mkubwa kwenye kuongoza Serikali ya nchi yetu, ana uzoefu mkubwa kwa uongozi wa Serikali kwa pande zote mbili za Muungano, na hili ni jambo la kipekee na muhimu sana. Tunampongeza kwa kupata nafasi ya Urais. Tuna matumaini kwamba ataifanya kazi hii vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Samia ni mchapakazi. Kama wako watu ambao wanafikiri baada ya kuondoka kwa Dkt. Magufuli mambo yatalegalega, wanafikiri watapata nafasi ya kuja kuiibia na kuifisadi nchi yetu, kwa mama Samia nafasi hiyo haipo. Ni mama mwadilifu anayependa taifa lake, mama mzalendo anayeichukua rushwa na mchapakazi wa kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 15 ya mwezi Februari tulikuwa Korogwe kwenye ziara na Mheshimiwa mama Samia akiwa Makamu wa Rais. Tulikuwa na daraja linasumbua akiwa mama kwa muda mrefu, tulipomueleza akatoka palepale akafanya mawasiliano na Wizara na TARURA wakasema hawana fedha. Akawaambia hata kama hakuna fedha jengeni kivuko ambacho akina mama wanaokwenda kupata huduma za afya hawatateseka. Leo ninapozungumza mkandarasi yuko site ameshashusha vifaa na kazi inafanyika; ni ufuatiliaji wa mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema kwamba mama Samia Suluhu Hassan si mtenda miujiza. Kama ambavyo tumetoa ushirikiano kwa Dkt. Magufuli, nawaomba Watanzania tumuunge mkono Mheshimiwa Rais, nawaomba tumuombee, nawaomba tushirikiane naye ili mama huyu aweze kuifanya kazi vizuri aende mbali zaidi kuanzia pale alipotuacha Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na ninaunga mkono maazimio yote mawili. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu kwenye bajeti ya Wizara ya Maji. Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, aliyetujalia uzima na ametuwezesha kuendelea kuwepo ndani humu na kuendelea kuwatumikia Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa nimpongeze sana ndugu yangu Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso kwa kuwa Waziri wa Maji, lakini pia kwa kazi kubwa wanayoifanya yeye na wataalam wake wote kwenye Wizara ya Maji. Wanafanya kazi kubwa sana, nami ni muumini wa kumpongeza mtu anapofanya vizuri. Wanafanaya kazi kubwa na nzuri, tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bajeti hii ya mwaka huu, nitumie nafasi hii kutoa ushauri kwenye baadhi ya maeneo machache. Pamoja na kazi nzuri wanayoifanya kwenye Wizara ya Maji na Taasisi zao zote, tumeanzisha RUWASA, RUWASA inafanya kazi nzuri na ni moja ya chombo ambacho kinakwenda kuwakomboa sana watu wetu hasa sisi watu wa vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maboresho machache ninayoshauri tuyafanye kwa upande wa RUWASA ili iendelee kufanya kazi zake vizuri. Eneo la kwanza Mheshimiwa Waziri, nilisema mwaka jana na leo narudia tena. Tuiimarishieni RUWASA kwa kuweka Bodi za Manunuzi, hata kama hatuwezi kwenye Wilaya lakini basi tuwe na Bodi za Manunuzi za RUWASA kwenye mikoa yote. Haiwezekani RUWASA Mkoa wa Tanga kwa mfano, manunuzi wakitaka kufanya mpaka tutegemee Bodi ya Manunuzi ya TANGA - UWASA, ambayo ina majukumu yake, ina mambo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi tunachelewa na miradi yetu inachelewa kutekelezwa kwa sababu ya kutokuwa na Bodi za Manunuzi. Kila mkoa kwenye Ofisi za RUWASA tupate Bodi ya Manunuzi, kuwe na Mtaalam wa Manunuzi ili manunuzi yafanywe na RUWASA wenyewe tusitegemee Mamlaka nyingine hizi za maji. Huo ni ushauri wangu kwenye eneo la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili Mheshimiwa Waziri, sehemu kubwa ya kazi za maji tunafanya kwa kutumia force account, tunatumia wale watu wetu tunaita local-fundi. Hao mafundi wanaofanya kazi ni mafundi wa chini kabisa ambao hawana mitaji mikubwa na hata miradi wanayopewa ni miradi midogo, tuziboreshe na Ofisi za RUWASA kwenye ngazi ya Wilaya. Waweke Wahasibu pale, haiwezekani fundi wa mradi wa milioni 15 anayelipwa labour charge, aki-raise kabarua kake ka kuomba alipwe milioni tatu atoke Lushoto, atoke Mlalo aende Tanga Mjini kwenda kufuata malipo yake ya fedha, haiwezekani. Nawaomba tuziboreshe hizi Ofisi za Wilaya, kuwe na Wahasibu na Wataalam pale ili waweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Bodi za Watumia Maji, kama tumeweza kwenye Serikali kuajiri wataalam wa kilimo karibu kwenye kila kata, tunashindwaje kuwa na Mtaalam wa Maji kwenye kila kata ambaye ameajiriwa na Serikali. Sehemu kubwa tunatumia mafundi wale local ambao tunao wanashirikiana na wananchi wenyewe. Naiomba Wizara wafikirie kuajiri watu wa kwenda kufanya kazi za maji kwenye kata zetu, tuwe na Mtaalam wa Wizara, tuwe na Mtaalam wa Serikali aliyeajiriwa na anayelipwa ili kuwa na ufanisi mzuri wa kutekeleza majukumu yao kwenye yale maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ninalotaka kushauri kwa ujumla ni kwenye eneo la Sera ya Maji. Maisha yanabadilika na yanakwenda kasi sana, maendeleo yetu yanakwenda kwa speed kubwa, Sera yetu ya Maji inatwambia kufikisha maji mita 400, nadhani tunapoelekea tunapaswa tuangalie kufikisha maji kwenye nyumba za Watanzania. Miji yetu inakuwa kwa kasi, vijiji vinakuwa kwa kasi, kuna haja ya kuingalia vizuri Sera hii ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ushauri huo wa jumla, niende hasa kwenye mambo ambayo yanawagusa Wanakorogwe. Tunao mradi wa Mwanga – Same – Korogwe, mradi huu umechelewa sana na Mheshimiw;a Waziri ni shahidi. Nimpongeze kwa hatua alizochukua za kuvunja mkataba wa Mkandarasi na kutafuta namna nyingine ya kufanya ile kazi. Pamoja na hilo lakini bado speed ya kazi ile siyo nzuri sana na hairidhishi. Ninachotaka tu Mheshimiwa Waziri akija kuhitimisha atuhakikishie kwamba ni kweli huu muda aliotuambia kwamba mradi utakamilika ni kweli utakamalika? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huu mradi kukamilika kwake ndiyo kuwapa maji wananchi wa Jimbo la Korogwe Vijijini hasa Kata za Mkomazi na Mkumbara ambao ndiyo wapo mwishoni mwa mradi huu. Mradi huu umechelewa kwa muda mrefu, tulitamani sisi tupate maji kutoka hata kwenye Mto Pangani au Mto Ruvu ambao unapita pale Mkomazi, lakini kila tukijaribu kutoa hayo mawazo tunaambiwa haiwezekani kwa sababu kutakuwa na double allocation of resources.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa watuambie kama huu mradi bado sana na kama hakuna uhakika na muda huu, waturuhusu na watutafutie fedha tuchukue maji kutoka kwenye mito tuliyokuwa nayo, ipo mito mingi na maji mengi ya kutosha, tupeleke maji kwa watu wa Mkomazi na watu wa Mkumbara kuliko kusubiri mradi huu mpaka muda ambao haujaeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumezungumzia Miradi ya Miji 28 na moja kati ya maeneo ambayo Waziri amesema yanakwenda kunufaika na mradi huu ni eneo la Mji wa Korogwe ambalo ni Jimbo la Korogwe Mjini. Mheshimiwa Waziri anajua kwa sababu tulifanya ziara naye, chanzo cha maji cha mradi huu kupeleka maji Korogwe Mjini na kupeleka Handeni, kupeleka na Muheza na Pangani kinatoka pale Korogwe, kwenye Kata ya Mswaha eneo ambalo vijiji vyake vyote havijapata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachomwomba Mheshimiwa Waziri atuhakikishie watu wa Korogwe, tulishaomba kuwa sehemu ya mradi huo, sasa wanapochukua maji kuwapelekea Korogwe Mjini, Muheza na Handeni, hivi vijiji hivi wasivisahau. Kama Mheshimiwa Waziri anavyosema kwamba anapowadhuru wengine asitupite, basi wasiwapite wale wananchi. Tumesema muda mrefu lakini hatujajua kama walitukubalia, walituingiza kwenye mpango au hawajatuingiza. Kwa kuwa tunabmatumaini mradi unakwenda kutekelezwa sasa, tunaomba Waziri atupe ahadi na uhakika wa Serikali kuwa wananchi hawa watanufaika na mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna bwawa ambalo nimeshawahi kumwambia Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara, Bwawa la Mayuyu ambalo linapatikana kwenye kule Kata ya Kerenge. Bwawa hili lilikuwa likitoa huduma ya maji kwa wananchi wetu, liliharibiwa na mafuriko, wakatuahidi kwamba wanatafuta fedha na kuna wakati wakasema wamepata fedha kutoka kwa wenzetu wa Misri, lakini mpaka leo bado kupo kimya. Namwomba Mheshimiwa Waziri anapokuja kwenye majumuisho atuambie tu ili tujue lini wananchi wa Kerenge na watu wa Mayuyu wanakwenda kupata ile huduma ya bwawa ili kurudisha huduma ya maji na kuendeleza shughuli za kiuchumi kwenye maeneo yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema nimeangalia bajeti ya Waziri vizuri na nimeisoma nimeona kwenye ukurasa 219 mpaka 220 ametenga fedha kwa ajili ya Vijiji vya Wilaya ya Korogwe kupata maji. Tunayo miradi ya kutosha pale, tunayo miradi mingi, lakini sehemu kubwa fedha hizi ni fedha za kuanzia na ni fedha ambazo hazitoshelezi na ceiling tuliyopewa ni ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Wizara ya Maji, lakini pia Serikali, ipo haja ya kuangalia namna ya kuongeza bajeti ya maji ili miradi hii iweze kukamilika. Tunamwomba Waziri atusaidie hilo ili wananchi wetu waweze kupata huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nimshukuru sana Mwenyezi Mungu anayetupa uzima na aliyetuweka kuendelea kuwatumikia Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa kabisa, tangu nimekuwa Mbunge inawezekana leo ikawa mara ya kwanza kuchangia bajeti nikiwa na masikitiko, na ninaomba Mungu anisaidie isirudie tena iishie kwenye bajeti hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ni muhimu sana kwa ajili ya uchumi wa nchi yetu. Kule Korogwe tunayo barabara ya kutoka Korogwe – Dindira – Bumbuli – Soni, ni barabara ya kilometa 74. Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010 kwenye ukurasa wa 48 ilitoa ahadi kwa watu wa Korogwe kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii, ikaenda miaka kumi hatukufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwaka 2015 tukahuisha ahadi hii kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM, na tukasema baada ya upembuzi kukamilika tutakwenda kuanza ujenzi, kwenye ukurasa wa 49 na ukurasa wa 56 wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015. Tukafanya usanifu kwenye kilometa 21 za kutoka Soni mpaka Bumbuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, 2015 kuja 2020 tukaahidi kwenye ilani, lakini pia na fedha zikawa zinatengwa. Na kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020, juzi tumetoka kwenye Uchaguzi, ukurasa wa 66 tumewapa taarifa Watanzania kukamilisha kazi ya upembuzi yakinifu wa barabara ile. Na kwenye ukurasa wa 77 tukatoa ahadi ya kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekwenda kwenye bajeti za Serikali kwenye Wizara hii. Bajeti ya mwaka 2018/2019 hii ninayo hapa, tulitenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Bajeti ya 2019/2020, hii hapa, tulitenga fedha; bajeti ya mwaka 2020/2021 kwenye ukurasa wa 98 Mheshimiwa Waziri aliahidi kwamba kwenye bajeti ile tunatenga shilingi milioni 840 kuanza maandalizi ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo kwenye bajeti ya mwaka 2021/22 Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake, ukurasa wa 12, anasema:-
“Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili 2021, mkataba wa kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Barabara ya Soni – Bumbuli – Dindira – Korogwe (km 74), ulikuwa umesainiwa. Aidha, fedha za mradi huu mara baada ya Mhandisi Mshauri anayefanya kazi hii kuwasilisha hati za malipo.”

Mheshimiwa Naibu Spika, imeishia hapo. Hiki ni nini? Naomba Waziri akija atuambie, tumesema upembuzi yakinifu umekamilika na kwenye bajeti iliyopita ambayo tunaimalizia mwaka huu tumetenga fedha ya kuanza maandalizi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami. Leo unakuja kuniambia kwamba tunakwenda kukamilisha kazi ya upembuzi yakinifu; kipi ni kipi? Watu wa Korogwe waelewe kipi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa Korogwe wameumia kwa muda mrefu, wamekuwa na ahadi hii kwa muda mrefu. Mheshimiwa Waziri nakuomba, kwanza mtuambie ssa status ya barabara hii ni ipi? Lakini mpango sasa wa kutekeleza Ilani hii ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2020 kama tulivyoahidi ukurasa wa 77 ni upi? Ili watu wa Korogwe wajue. Ni barabara muhimu, ni barabara ya kiuchumi. Mazao yetu yanaharibika kwa sababu ya barabara hii. Ninakuomba Waziri akija kwenye majumuisho atuambie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, amesema kaka yangu, Mheshimiwa Kitandula, kuhusu barabara ya Mabokweni – Bombomtoni – Kwashemshi – Korogwe, ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais. Ni maombi ya kwetu Wanakorogwe, ni maombi ya viongozi wetu wa dini, ni maombi ya wadau wengi wa maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ni barabara muhimu sana kwa uchumi. Na hii ni barabara mbadala kama mtu anatoka nchi jirani siyo lazima aende Tanga Mjini, anaweza kupita barabara hii akaenda Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha na mikoa mingine. Lakini kwenye bajeti hii jambo hilo halipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba kujua kutoka kwa Mheshimiwa Waziri sasa ni lini mpango wa barabara hii, ni lini barabara hii itatengenezwa ili kuweza kuleta maendeleo kwa watu wa Jimbo la Korogwe na Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Waziri, tunao utaratibu wa kupandisha hadhi barabara zetu kutoka kuwa barabara za wilaya kule kwenda kuwa barabara za mikoa na Kitaifa. Na tunafanya hivi kwa sababu tunaamini TANROADS ina uwezo mkubwa wa kifedha na wa kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa miaka karibu mitano hatujafanya jambo hili. Sisi Tanga tumepitisha barabara na kwenye Wilaya ya Korogwe tunazo barabara nne muhimu; iko barabara ya kutoka Mombo – Mzeri, barabara ya kutoka Msambiazi – Rutindi, Kwetonge – Bombomtoni na Makuyuni – Zege – Mpakanani. Tumeshamaliza taratibu zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, wewe ndio Mwenyekiti wa kamati ile. Tunaomba mtupandishie hadhi barabara hizi zifanyiwe ukarabati vizuri, wananchi wetu wapate maendeleo. Nakushukuru sana. (Makofi)


Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu kwenye hoja muhimu sana kwa Taifa letu, lakini pia kwa maisha na mustakabali wa watoto wetu na vijana wetu.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kwa kukiri na kutambua mchango na kazi kubwa iliyofanywa na Serikali, kuendelea kuongeza Bajeti ya Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kila mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka fedha 2017/2018, mikopo ilikuwa ni billioni 427.5. Mwaka wa fedha uliopita na mwaka wa fedha tuliyonao mikopo ni billioni 570, ni hatua kubwa sana. Pamoja na hayo bado tuna changamoto na changamoto ni hii ambayo imeletwa na hoja na Mheshimiwa Ezra.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana bajeti iliyopita ya 2021 tulikuwa na billioni 570 na kwa takwimu za Bodi wenyewe wanufaika walikuwa ni laki moja elfu sabini na saba na mia nane tisini na mbili. Mwaka huu wa fedha tulionao bajeti ni ileile bilion 570 na matarajio ni wanufaika haohao laki moja sabini na saba mia nane tisini na tatu, anaongezeka mnufaika mmoja.

Mheshimiwa Spika, changamoto tuliyonayo wenzetu Serikalini hasa Bodi na Wizara ya Elimu walipaswa wawe wameiyona. Kilichotokea hapa ni nini? Mwaka jana wanufaika tuliyokuwa nao wanufaika wapya walikuwa ni elfu sabini mia sita na tisa. Wanufaika waliokuwa wakiendelea ni laki moja na elfu saba na miambili na themanini na tatu. Mwaka huu kwa Bajeti hii hii kwa taarifa za Bodi itawalazimu kuwapa wanufaika wanaoendelea laki moja na thelathini na tano mia nane tisini na tatu. Maana yake ni kwamba kwa idadi hile wanufaika wapya wanaoanza mwaka wa kwanza wanashuka kutoka elfu sabini mpaka wanufaika elfu arobaini na mbili. Kuna tofauti ya wanafunzi wanufaika zaidi ya elfu thelathini ambao tunatarajia hawataweza kupata mikopo kwa Bajeti tuliyokuwa nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vijana elfu thelathini ni wengi na ni nguvu kazi kubwa sana kwa nchi yetu. Kama Taifa hatupaswi kukubali hata kidogo vijana hao wakashindwa kunufaika na mikopo hii na kushindwa kupata elimu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto ni kwamba tuna vyanzo viwili tu vya fedha kwa ajili ya vijana wa vyuo vikuu. Kwanza ni pesa inayotoka kwenye Bajeti, pia pili ni marejesho yanayofanyika kutoka na wanufaika huko nyuma. Nishauri, ushauri wa muda mfupi kabisa, Serikali na Mheshimiwa Ezra, nimshauri kwenye maazimio, ni lazima Serikali ituletee mpango wa dharura ya namna ya kuwasaidia hawa vijana zaidi ya elfu thelathini ambao tunaamini kama tukifanya takwimu vizuri sio thelathini wataongezeka kwa sababu udahili unaongezeka na watu wanaongezeka. Serikali ilete mpango wa dharura, ni namna gani vijana hawa ambao tayari vyuo vimefunguliwa, wanakwenda kupata fedha za mikopo ya kuwasaidia kuweza kufanya masomo yao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili tulikuwa tunataka tushauri, kama ambavyo amesema Mheshimiwa Hasunga, la kwanza ni lazima Serikali na sisi kama nchi, Wizara na Bodi tufanye tathmini upya ya utaratibu wa utoaji wa mikopo, utendaji kazi wa Bodi ya Mikopo, vigezo na masharti yote katika kuzingatia suala la utoaji wa mikopo. Lazima tufanye tathmini ya kitaifa ya muda mrefu kwamba mfumo huu tulionao unaweza kutufikisha au unakwenda kutukwamisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, ufanyike uchunguzi, itengenezwe tume au kupitia Kamati ya Bunge, ufanyike uchunguzi wa vigezo vinavyotumika kutoa mikopo kwa watoto wetu, kwa sababu malalamiko ni mengi, vigezo vipo lakini kwa uhalisia kwenye macho ya faida ya kibinadamu hatuoni kama vinafanya kazi vizuri. Ufanyike uchunguzi wa kina wa vigezo vilivyotumika kwa miaka mitano mpaka miaka kumi, vigezo vilivyotumika, idadi na aina ya wanufaika walionufaika na mikopo ya elimu ya juu ili tujiridhishe kama Taifa kama tuko kwenye sehemu salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia sehemu nyingine tukafanye uchunguzi wa utaratibu wa urejeshaji wa mikopo hii na kiasi cha kinachorejeshwa, kinachoripotiwa na matumizi yanayotumika kwa ajili ya kutengeneza msingi mzuri kwa huko mbele tunakokwenda.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Ezra, jambo hili ni la dharura, lazima twende na mpango wa dharura kama Bunge na kama nchi tuwasaidie vijana wetu. Nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nimshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ameendelea kutujaalia uzima na kutuwezesha kuifanya kazi hii ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na mimi kwa kuungana na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Timu yenu yote mnafanyakazi nzuri sana na kazi yenu inatubariki sana; tunawapongeza tunawatia moyo muendelee na kazi hiyo. Mheshimiwa Waziri kwenye Wizara yako siyo ninyi tu Wizarani hata ukienda kwenye taasisi zenu sisi wa vijijini tunabarikiwa na kazi nzuri sana inayofanywa na wenzetu wa RUWASA. Mkurugenzi Mkuu anajitahidi anafanyakazi vizuri. Kule Tanga sisi Injinia wetu wa Mkoa anafanyakazi nzuri na kipekee sana Meneja wetu wa RUWASA wa wilaya na timu yake nzima. Kwenye kazi huweza kuwa kuna changamaoto lakini kijana yule anajitahidi anafanyakazi nzuri muendelee kumtia moyo sisi tunamtegemea na anaifanyakazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kumpongeza Waziri na timu yake, napenda nitumie nafasi hii katika kuchangia hotuba hii ya Bajeti ya Wizara ya Maji, kumpongeza sana sasa sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa mambo makubwa mawili; jambo la kwanza kwa kujiongeza na kutafuta fedha nje ya utaratibu wetu; fedha kwa ajili ya UVIKO, zimetusaidia sana kwenye upande pia wa sekta ya maji. Jambo la pili, kipekee ninampongeza sana Mheshimiwa Rais na Serikali yake; kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwenye ule ukurasa wa 10 mpaka Mwezi Aprili, wizara imepokea fedha kwa asilimia 95 ya matarajio tuliyoyaweka kwenye bajeti. Tunavyosema mama anaupiga mwingi wako watu wengine wanakuwa na mashaka mashaka na wengine wanakuwa na maswali. Kunawezi kuwa na changamoto za ndani, za kitaifa lakini haiondoi ukweli kwamba mama anaupiga mwingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwenye hili nitafanya tu rejea ya maeneo machache. Tumepokea fedha kwa asilimia 95 mpaka Mwezi Aprili, 2022. Nimekwenda kutafuta hotuba za bajeti za Wizara ya Maji, nikachukua na maandiko mengine, mwaka 2017/2018 mpaka mwezi Machi, 2018 fedha za maendeleo zilitoka kwa asilimia 12.3, matumizi ya kawaida ilitoka asilimia 73. Mwaka 2018/2019 mpaka mwezi Machi, 2019 fedha za matumizi ya kawaida zilikuwa asilimia 68, fedha za maendeleo zilitoka kwa asilimia 51; nimekwenda Mwaka 2019/2020 matumizi ya kawaida tulipewa kwa asilimia 70 mpaka mwezi Machi, matumizi ya maendeleo kwa asilimia 74. Lakini mwaka uliopita 2021 Mpaka mwezi Aprili, 2020 zilizotoka kwenye bajeti zilitoka kwa asilimia 72 kwa matumizi ya kawaida na asilimia 53.4 kwa matumizi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumza kwenye bajeti hii Wizara imepokea fedha kwa asilimia 95. Huu ndio ushahidi kwamba mama anaupiga mwingi sana. Kizuri zaidi sio tu kwenye kutoa fedha; sisi wote ni mashahidi, fedha zinatolewa kazi inafanyika na kazi inaonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikichukua mfano wa Jimbo la Korogwe Vijijini tuna miradi zaidi ya mitano ambayo imekamilika; na miradi sita ambayo ipo kwenye hatua mbalimbali inaendelea sasa hivi na miradi minne tunatarajia kusaini mikataba wiki inayokuja na nina miradi mitano iko kwenye hatua mbalimbali za manunuzi hakika mama anaupiga mwingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo kwa kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Rais lakini na Serikali yake, na kwa hiyo kwa pongezi hizi mimi sina mambo mengi; nina maombi tu machache nikukumbushe wewe na wenzako wa Wizarani ili kazi iweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi ule wa maji wa Vuga – Mlembule pale Mombo ni wa muda mrefu umeshatoa fedha. Kuna uzito kidogo kwa upande wa ule mradi wa kule Lushoto, ambako ndiko kwenye chanzo cha maji. Tusaidie kuongeza nguvu mradi huo ukamilike tuwape huduma ya maji watu wa Mombo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu la pili, nimeona kwenye ukurasa wa 56, umesema vizuri sana kuhusu Mradi wa Maji wa Miji 28, na umesema tayari kila kitu kimekamilika tunasubiri kusaini utekelezaji wa miradi hii ukaanze. Naendelea kukumbusha Wizara yako, katika ile miradi ya miji 28 ambayo inaanza sasa kwa fedha kutoka India; kuna miji ya Muheza kwa akina Hamis, Handeni na Korogwe Mjini chanzo chao maji kiko pale Jimbo la Korogwe Vijijini Kata ya Mswaha. Ninakuomba sana kama tulivyokuwa tumeomba tangu mwanzoni tutakwenda kwenye utekelezaji, vile vijiji vilivyojirani na kile chanzo msikisahau vijiji vya hii Kata ya Mswaha viweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni mradi wa maji wa Mwanga – Same – Korogwe. Umeusema vizuri sana kwenye ukurasa wa 55 wa hotuba yako, na umeeleza changamoto ulizokutana nazo na hatua tulizochukua. Mimi nikuombe, baada ya kupitisha bajeti hapa hebu kaongeze nguvu jambo hili likamilike ili mradi huu ukamilike watu waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maombi hayo matatu ombi la nne, tulizungumza na Mheshimiwa Waziri kuhusu Bwawa la Mayuyu, na ulikuwa umeniahidi kwamba kesho ungekwenda kufanya ziara, na watu wa Korogwe wanakusubiri. Ninakuomba sana tuliangalie tuwajali wale watu bwawa lile ni bwawa muhimu ndilo wanalolitegemea kwa ajili ya kupata huduma za maji na huduma nyingine kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa nane ambayo haimo kwenye ule mradi wenu wa EP4R; na huko nyuma tumekuwa tukihudumiwa sana kwenye miradi yetu midogo midogo iliyo mingi kupitia mradi wa PbR. Tunajua program ya PbR ndiyo inakwenda mwishoni PbR5 ndiyo ya mwisho mradi una-Phase Out. Tunawaomba sana Wizarani mtusaidie kupata mradi mwingine wa aina hii au mtuunganishe na wenzetu wale wengine ambao wako kwenye EP4R na sisi tuweze kupata huduma za miradi hii midogo midogo ili wananchi wetu waweze kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, Mheshimiwa Waziri unatambua changamoto niliyonayo kwenye Kata za Mkomazi, Mkalamo, Magambo Kwalukonge na Mpale. Kata hizi zinachangamoto kubwa ya vyanzo vya maji. Tumeamua na ninyi Wizarani mliamua kutusaidia mradi mkubwa kutoka kwenye maji ya Mto Ruvu. Mkatuahidi kututafutia mshauri kwaajili ya kuja kufanya kazi ya usanifu na upembuzi yakinifu. Tunaomba mchakato huu uharakishwe kidogo, tumeusubiri kwa muda mrefu ili mambo yaende vizuri ili tumalize maeneo haya machache, tuunganishe na yale maeneo mengine makubwa ambayo watu wa Korogwe wanapatia huduma ya maji ili mambo yao yaweze kwenda kuwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninakushukuru sana kunipa nafasi. Ninaunga mkono hoja ninawatakia kila la kheri katika kutekeleza bajeti mtakayopitisha. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu kwenye hotuba ya bajeti ya Wizara hii muhimu sana kwa maisha ya Watanzania. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya. Hakika Mheshimiwa Rais katika wakati wake ameonesha namna nzuri na namna bora ya kuzilea na kuzisaidia Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuteuliwa kuwa Waziri kwenye Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mchango kwenye maeneo machache. Eneo la kwanza ni eneo lenyewe la Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 145 (1), inaeleza kuwepo kwa vyombo mbalimbali kwenye maeneo ya Serikali za Mitaa. Vile vile ibara ya 146 (1) inaeleza madhumuni ya kuwepo kwa Serikali za Mitaa ikiwa ni kurudisha madaraka kwa wananchi na vyombo hivi viweze kuwashirikisha wananchi. Sasa sisi Tanzania kwenye mfumo wa Serikali za Mitaa tume-buy mfumo wa wenzetu wa British mode. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye British mode, moja ya tabia yake ni kuwa na double accountability. Kwa maana watendaji wetu wanakuwa accountable kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa, lakini at the same time wanakuwa accountable kwenye Serikali Kuu. Kwenye mazingira ya namna hii, kama kusipokuwa na proper coordination, lazima kutakuwa na kigongano kati ya mamlaka hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ombi langu kwa TAMISEMI, mwaka 2019 tulianza mapitio ya kuboresha sera ya ugatuaji wa madaraka, lakini mpaka leo kumekuwa na ukimya. Mheshimiwa Waziri ukija kwenye majumuisho utuambie, tumefikia wapi kwenye zoezi la kuboresha Sera ya Ugatuaji wa Madaraka? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, kwa sababu, tayari kuna double accountability, ni lazima wenzetu wa Serikali Kuu wakubali kuwa flexible ili kuweza kuchukua mawazo ya wananchi katika kutekeleza ile azma ya kurudisha madaraka kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba wenzetu wa TAMISEMI, mnafanya vitu vizuri, lakini kuna maeneo ambayo hamtutendei haki. Serikali za Mitaa siyo za kupokea tu maelekezo, lazima zishirikishwe; na katika kushirikisha lazima muwe flexible kusikiliza na mawazo ya waliokuwa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano wanataka kujenga masoko, unatoa mfumo mmoja wa kujenga masoko nchi nzima. Aliyekwambia Soko la Korogwe linafanana na Soko la Sumbawanga ni nani? Aliyekwambia jiografia ya Korogwe na ya Sumbawanga inafanana ni nani? Haiwezekani, lazima tuangalie mazingira halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, tumemsikia Mheshimiwa Rais akisema mara kadhaa kwamba, kugawa maeneo ya utawala ni gharama kubwa. Nami nakubaliana naye, lakini moja ya chombo muhimu kwenye Serikali za Mitaa ni mamlaka ya kwenye Kijiji kwa maana ya Halmashauri ya Kijiji na Mkutano wa Kijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaotoka vijijini, vijiji vinakua. Ukiwaona maeneo mawili tofauti kwa vijiji yamekua, yanaanza kuwa na msigano, na shughuli za maendeleo hazifanyiki vizuri. Tunaomba mumshauri Mheshimiwa Rais, kuna gharama kubwa kutangaza mikoa mipya, kutengeneza Halmashauri mpya, lakini hata kutengeneza vijiji! Hakuwezi kuwa na gharama kubwa namna hiyo! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vijiji vimekuwa ni vikubwa, vinahitaji kugawanywa ili wananchi wasogezewe huduma karibu na waweze kufanya shughuli za maendeleo. Kule Korogwe Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja na aliahidi kwamba atatoa vijiji vipya, lakini mpaka leo kumekuwa na ukimya. Tunaomba muishauri mamlaka ili mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni vituo vya afya. Sera yetu inasema tuwe na vituo vya afya kila Kata, tuwe na zahanati kila Kijiji. Tukaona utekelezaji wake umekuwa mgumu tukasema, tuwe na vituo vya afya vya kimkakati na vya Tarafa. Nimeahidiwa vituo vya kimkakati tangu mwaka 2020 hapa, mpaka leo sijaona hata kimoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alipoingia tu kwenye Wizara ametuita, amekaa vikao na Wabunge, yale tuliyoyasema siyaoni yakiwa reflected kwenye bajeti hii. Vituo hivi tunavipata lini? Vinajengwa wakati gani? Tumewaahidi wananchi, tunakwenda kwenye uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kwenye mikopo ya akinamama, vijana na watu wenye ulemavu ya asilimia 10. Ninaungana kabisa na alichokisema Mheshimiwa Rais. Pia nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa mawazo na maelekezo aliyoyatoa jana. Naomba niwashauri, mnapoenda kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais, muongeze. Tukipeleka fedha hizi kwenye mfumo wa kibenki, tutafanikiwa kwenye lengo moja la kuhakikisha tunakuwa na utaratibu mzuri wa utoaji na urejeshaji, lakini bado hatutakuwa na utaratibu mzuri wa kuziwezesha jamii zetu kubaki na matokeo baada ya kumaliza kufanya mrejesho wa hiyo mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna haja ya TAMISEMI kutoa maelekezo kuziunganisha idara; Idara ya Maendeleo ya Jamii, Idara ya Kilimo, Idara ya Mifugo, Idara ya Biashara, ili mikopo hii inapotolewa, itolewe kulingana na mazingira halisi ya biashara kwenye maeneo yale, ili baada ya kumaliza kurejesha marejesho ya mkopo huu, wananchi hawa waone biashara hizi zikiendelea, tuone matokeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotusumbua sasa hivi kwenye kurejesha pia, hakuna mipango mizuri na elimu nzuri ya kuzitumia hizi fedha. Tukiziunganisha idara hizi; Idara ya Kilimo, Idara ya Mifugo, Idara ya Maendeleo ya Jamii, tutafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, nikuombe sana Mheshimiwa…

(Hapa kengele ililia kushiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa nakuongezea dakika moja umalize jambo la mwisho.

MHE. TIMOTEHO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, naipongeza Serikali kwa ajira ambazo imetangaza. Ukisoma ripoti ya CAG, alifanya tathmini kwenye Halmashauri 23 tu, lakini upungufu ulikuwa ni asilimia 35, karibia watumishi 10,000 kwenye Idara ya Elimu peke yake. Hawa walimu 13,000 wanakwenda kuishia kwenye hizo Halmashauri 23 tu. Tuna Halmashauri 184. Tukifanya tathmini kwa nchi nzima, upungufu huu ni mkubwa sana kwa watumishi wa elimu na watumishi wa afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ajira hizi, bado hazitoshi. Tunaomba wekeni mikakati zaidi ili tupeleke watumishi kwenye maeneo yetu, lakini siyo kuajiri tu wapya, vile vile na mlinganisho na msawazo wa watumishi hasa kati ya Halmashauri za Mijini na Halmashauri za Vijijini. Halmashauri za Vijijini zimechoka kuwa sehemu za watu kupatia ajira na kuondoka kwenda kukaa maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nitoe mchango wangu kwenye bajeti hii muhimu sana. Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema ambaye anatujalia uzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nitumie nafasi hii kumpongeza kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa namna alivyotoa jicho la uhakika kwenye sekta ya kilimo. Kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na watendaji wote wa Serikalini wakiongozwa na katibu Mkuu. Kiukweli Mheshimiwa Bashe, sisi vijana tunajifunza kwako na kwenu, na tuna imani kubwa na ninyi, na tunaridhika na kazi nzuri mnayoifanya. Kwa sababu hiyo nitakuwa na mambo madogo tu mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni la umwagiliaji. Kipekee sisi wananchi wa Korogwe tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri. Tumeimba muda mrefu habari ya Bonde la Mkomazi. Tumekuwa na hadithi nyingi, wewe ni shahidi tangu ukiwa Naibu Waziri na mwenzako Mheshimiwa Mgumba, lakini mwaka jana 2022 uliniahidi ukasema, mdogo wangu tunatenga fedha, tunarudia upembuzi yakinifu na usanifu, na mwaka unaofuata tutakwenda kwenye ujenzi. Hakika mkataba umesainiwa na nimeona kwenye bajeti ukurasa wa 25 umenihakikishia kwamba kwenye bajeti hii ujenzi wa skimu hiyo unakwenda kuanza kwenye mwaka wa fedha unaokuja. Nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninawashukuru Mawaziri hawa kwa usikivu wao. Nimekaa nao kawenye vikao akaniambia nimwandikie, nikamwandikia. Kwenye bajeti, nimeyaona mabonde yale ya Magoma. Ukarabati wa skimu ile ya Chekerei, skimu ya Magila na eneo lile la Mayuni kule Mapangoni nimeona, nawashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili la umwagiliaji sina cha kuchangia, zaidi nawashukuru sana. Tunaomba tu kazi hizi ziende kwa speed ili tuweze kuwanufaisha wakulima wetu na wananchi wa Korogwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni eneo la kilimo cha zao la mkonge. Sisi watu wa Mkoa wa Tanga ndio tunaongoza kwa uzalishaji wa Mkonge kwenye nchi hii. Unaposema Mkoa wa Tanga unaongoza kwenye uzalishaji, anayeongoza ni Wilaya ya Korogwe hasa Korogwe Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa namna walivyorudisha matumaini ya wananchi wa Korogwe na Mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla kwenye zao la mkonge. Tulijengewa dhana kwamba mkonge ni zao la wakulima wakubwa wenye fedha nyingi, wenye maeneo makubwa ya kulima, lakini imani mliyoijenga kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga, imani mliyoijenga kwa wananchi wa Korogwe na wakulima wa mkonge, imewarudisha watu wa Tanga na watu wa Korogwe kwenye kilimo cha mkonge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mwaka 2020 nchi yetu tumezalisha Mkonge tani 37,022, lakini katika hizo wakulima wadogo walizalisha tani 26,000. Mwaka 2021 tumealisha tani 39,484, wakulima wadogo wamezalisha tani 24,000. Mwaka 2022 uliopita, tumezalisha tani 48,351, wakulima wadogo wamezalisha tani 22,000. Kwa miaka hii mitatu iliyopita, jumla kama nchi tumezalisha tani 124,858.39, na katika hizo wakulima wadogo mchango wao ni tani 73,420 sawa na asilimia 58.8. Kwa takwimu hizi huwezi kubeza mchango wa wakulima wadogo kwenye uzalishaji wa zao la mkono. Kwenye hotuba yako umesema na kwa mujibu wa takwimu za Bodi ya Mkonge wakulima wenye mkonge mdogo ambao haujapita miaka miwili wakulima wadogo sasa hivi wenye mkonge mdogo hawajaanza kuvuna, wana hekta 3,545. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema nini? Uzalishaji huu moyo huo wa wakulima wadogo ili uende vizuri naomba tuzingatie mambo mawili. Jambo la kwanza; mkonge kama mkonge majani hayani maana, maana ya mkonge ni nyuzi baada ya kusindika. Wakulima wadogo wanachangamoto kubwa sana ya mashine za kusindika mkonge kule Korogwe na AMCOS zile tano kuna mashine za kuchakata mkonge za Sasalana nilisema mwaka jana tunashukuru wamejirekebisha wanakwenda vizuri. Lakini wakulima wana uhitaji wa mashine ukiangalia uzalishaji huu, ukiangalia idadi ya eneo la mashamba mapya waliyokuwa nayo wakulima wetu na kazi wanayoifanya sasa baada ya miaka miwili kutakuwa na crisis kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana Mheshimiwa Waziri, alihaidi kwenye Bunge hili kwamba wanakwenda kununua mashine mbili kubwa za kuchakata mkonge wa wakulima kila tukiulizia tunaambiwa manunuzi bado ningetamani baadae ukija utuambie kwenye eneo hili Mheshimiwa Waziri mmefikia wapi? Lakini Mheshimiwa Waziri, wakulima wadogo kupitia AMCOS zao walitaka kuchukua mikopo kwenye taasisi za kifedha lakini mpaka leo taratibu zimekuwa ngumu wanakwama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana tumesema hapa Mheshimiwa Waziri kwani hii Benki ya Kilimo ni kwa ajili ya kina nani? Kwanini Benki ya Kilimo iisiingie kusaidia AMCOS zetu hizi? Benki ya kilimo isibaki na wakulima wakubwa tu tuwasaidie AMCOS, tutumie benki ambazo ziko tayari, tuwe na madirisha. AMCOS zikopeshwe wakulima wapate mashine ili waende wakasindike mazao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo jingine bodi imegawa mashamba na nimesoma vizuri kwenye hotuba yako mmesema mmeishagawa hekta zaidi ya 3,829. Ombi langu na watu wa Korogwe tunaomba kwenye kugawa mashamba pamoja ya kwamba ardhi hii ni ya nchi nzima wapeni kipaumbele watu wa Korogwe kwenye yale maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho ni kwenye mkonge. Mwaka jana tumesafirisha nje tani 32,627 sawa na asilimia 67.5 lakini kwa miaka mitatu iliyopita nyuzi za mkonge zinakwenda nje ni zaidi ya asilimia 71 ya uzalishaji wa mkonge wote. Kupeleka nyuzi za mkonge nje ni kuuza ajira za watu wetu, kupeleka nyuzi za mkonge zote hizi asilimia 71 nje ni kupunguza kodi tunapata kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali Mheshimiwa Waziri tunao watalamu wa uchumi, tunao watu wanafanya economic intelligence hivi tunashindwa kwenye kujifunza tunakopeleka mkonge? Wanazalisha nini? kwa ajili ya soko lipi? Tukafanya mikakati ya kuwavutia wawekezaji kuja kufunga mashine na viwanda Tanzania vya kuchakata mkonge, tusafirishe matunda ya mwisho siyo kusafirisha nyuzi. Tukisafirisha nyuzi tunapoteza ajira za watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimwia Waziri, mwaka jana kwenye hotuba ukurasa wa 165 na 166 ulisema vizuri sana kuhusu kuielekeza Bodi ya Mkonge kuongeza nguvu ya kuvutia matumizi ya magunia na nyuzi za mkonge naku– discourage bidhaa zile nyingine zinazoharibu soko la mkonge. Bahati mbaya mwaka huu kwenye hotuba yako sikuiona na bahati mbaya sana kwenye nchi yetu kuna viwanda nane vinavyoshulika na mazao ya mkonge kwa maana ya nyuzi za mkonge. Lakini leo tunapozungumza viwanda hivi nane vinavyofanya kazi vizuri ni viwanda vitatu tu kati ya viwanda vile nane na idadi ya uzalishaji wake ninayo hapa. Mheshimiwa Waziri siyo jambo zuri viwanda vinaendelea kufa, vinaendelea kupungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulijifunza kwenye COVID, ikitokea tuna majanga tujifunze kwenye vita ya Urusi, ikitokea kuna majanga masoko ya nje hayafanyi vizuri hatma yetu ni nini? Hatma ya wakulima wetu ni nini? Ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili moja ya jambo linalo–discourage uzalishaji wa vifaa vya mkonge kwenye nchi yetu ni sheria tulizokuwanazo na usimamizi wa sheria tuliyonayo. Sheria ya Forodha ya Afrika Mashariki ina ruhusu msamaha wa kodi kwa nyuzi za plastiki…

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: …ni vizuri watu wa uvivi inawasaidia lakini tukazikague ili zitumike kwa matumizi yaliyokusudiwa na zisiende zaidi ya hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nitoe mchango wangu kwenye Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Awali ya yote nianze kwa kumpongeza sana kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna alivyoamua kutoa mwelekeo wa jinsi anavyotaka sekta hii ifanye kazi, lakini namna anavyotaka Watanzania wanufaike na sekta hii ya uhifadhi, lakini pamoja na utalii kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda nitakwenda haraka kwenye maeneo matatu. Eneo la kwanza, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu yote ya Wizara na taasisi zao zote kwa kupata imani ya Mheshimiwa Rais kuendelea kuongoza Wizara hii. Mheshimiwa Waziri nimesema nimpongeze kwa sababu, yako mambo mawili nataka kumshauri yeye na wenzake kwenye Wizara.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza Mheshimiwa Waziri, nimekupongeza ili nikushauri. Pamoja na kuwa Waziri wa Wizara hii, Wizara hii ni muhimu, taasisi za uhifadhi zinafanya kazi kubwa na kazi nzuri. Nakuomba usiwe Waziri tu, ukawe baba na ukawe mlezi wa Wizara hii. Ukawe baba na ukawe mlezi wa watumishi wa sekta na taasisi zote zinazosimamiwa na Wizara yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ninalotaka kumshauri Mheshimiwa Waziri, kwa miaka kadhaa tumekuwa na changamoto kidogo kwenye Wizara hii. Kila ukija uongozi yanakuja mambo mapya, zinakuja kauli mpya, inakuja mikakati mipya; nakuomba kwenye awamu yako uache alama. Katengeneze mifumo ya uhakika itakayoweza kufanya kazi kwenye Wizara hii, hasa kwenye eneo la sekta ya utalii ili utalii uweze kufanya vizuri ulete matokeo kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ninalotaka kulizungumza ni kuhusu wanyama wakali na waharibifu. Changamoto hii ni kubwa sana na iko kwenye maeneo mengi. Ni changamoto ambayo inawatesa na kuwaumiza sana wananchi wetu, malalamiko na manung’uniko ya wananchi yamekuwa makubwa. Ukienda Korogwe, zaidi ya kata nane tembo wanaharibu mazao ya wananchi, tembo wanaua na wanaharibu mali za wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natambua, nathamini na kupongeza juhudi kubwa inayofanywa na Serikali. Imefanyika kazi kubwa sana kuanzisha vituo vya Askari, kuongeza Askari wa Doria, kununua magari, kununua pikipiki, lakini kubwa sana ni utayari wa Serikali kuendelea kulipa kifuta machozi kwa wananchi wetu. Mambo haya ni makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo haya ambayo Serikali imefanya, bado tatizo hili ni kubwa, lazima kama nchi na Serikali mjue yako mambo lazima tuendelee kuyafanya. Jambo la kwanza nishauri, Wizara hii iwe serious kwenye shughuli ya kuongoa shoroba zetu. Pili, mapitio ya Wanyama, mapito ya wanyama yaweze kutambulika vizuri na yasilete madhara kwa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili. Tujifunze kwenye nchi nyingine teknolojia mbalimbali za namna ya kukabiliana na hali hii ili tuwasaidie wananchi wafanye kazi zao kwa amani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, Mheshimiwa Waziri amesema, moja ya changamoto na sababu kubwa ya changamoto hii ni ongezeko kubwa la watu na ongezeko kubwa la shughuli za kibinadamu. Kwa mujibu wa Taarifa za Sensa, mwaka 2022 tulikuwa na watu milioni 44 na ukiangalia idadi ya watu mwaka 2022 ukilinganisha na sensa ya mwisho 2002 nyuma yake, ongezeko lilikuwa ni la asilimia 2.7. Sensa ya mwaka 2022 tumefika Watanzania milioni 61,741,000 na wastani wa ongezeko la watu kwa mwaka kwa mujibu wa Taarifa za Sensa ni asilimia 3.2. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ongezeko hili siyo dogo. Unaweza kutumia ongezeko hili kuvuta picha ya miaka 10 inayokuja hali itakuwaje? Miaka 20 inayokuja hali itakuwaje? Tukiendelea kupiga kelele hapa bila kuweka mikakati madhubuti hatuwezi kumaliza jambo hili.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali; Wizara ya Ardhi, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Kilimo tukae pamoja tuweke mpango wa kupanga nchi hii. Haiwezekani tukalima kila mahali, haiwezekani tukachunga kila mahali, haiwezekani tukajenga kila mahali, lazima tuje na mkakati wa Kitaifa wa kupanga nchi yetu ili mambo haya yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho ninalotaka kuchangia siku ya leo ni zoezi la kuhamisha watu kwa hiyari kutoka kwenye Hifadhi, Eneo la Ngorongoro. Nakushukuru Mheshimiwa Waziri amelisema vizuri kwenye hotuba yake na ametoa tamko kwamba halijasitishwa na hakuna mabadiliko yoyote. Ninamshukuru sana na ninampongeza kwa jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka mwezi Novemba mwaka 2022 na kwenye Taarifa ya Kamati tumesema, kaya ambazo zilikuwa zimeshahama ni 489, watu 2,629 na mifugo 14,000, lakini tunapozungumza tangu wakati huo wa Novemba, tayari kuna kaya 1,524 zimejiandikisha na ziko tayari kuhama ambazo hizi kaya zina watu 8,715. Hizi kaya zina mifugo 32,842 pamoja na tamko ambalo amelitoa Mheshimiwa Waziri. Nafurahi kwamba nachangia wakati Waziri Mkuu, ambaye ndio Mtendaji Mkuu wa shughuli za Serikali akiwa ndani ya ukumbi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri anasema jambo hili halijasimama na hakuna mabadiliko, lakini tangu tumemaliza awamu ya kwanza ya kuhamisha watu kutoka Ngorongoro ni miezi sita. Mlikuja kwenye Kamati mwezi wa Pili na mwezi wa Tatu mkasema mna mipango ya kutafuta fedha. Tumekaa miezi sita, fedha hazijapatikana? Kwa nini zoezi hilo haliendelei? Sawa ametuambia kwamba jambo hili lipo na halijabadilika, lakini haiwezekani kwa zoezi kubwa, kwa zoezi muhimu kama hili ambalo Bunge hili tulilibariki, nchi hii imelikubali, inakwenda kuiokoa na kulinusuru eneo la Hifadhi ya Ngorongoro tukakaa miezi sita tunasubiri. Tunasubiri nini miezi sita? Hizi kaya zaidi ya 1,000 zipo tayari zinasubiri. Zinasubiri kwa muda gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inawezekana jambo hili likawa siyo la maliasili peke yake. Nimesema nimefurahi kwa sababu Waziri Mkuu yupo. Tunapokwenda kuhitimisha bajeti hii ya maliasili Serikali ituambie. Pamoja na kauli kwamba kazi hii inaendelea na jambo hili halijabadilika, mtuambie tumekwama wapi? Ni kwa nini jambo hili haliendi mbele? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, athari ya jambo hili ni kwamba likipoa, yanaanza mambo mengine ya ajabu ajabu. Mmeona watu wamekwenda mpaka Ulaya kuanza kushitaki, wameanza kulalamika, tumerudishwa nyuma. Inawezekana labda kuna mtu anataka kuhujumu hili zoezi. Kama hakuna mtu anataka kuhujumu suala la kuhamisha watu Ngorongoro tukiwa tunahitimisha bajeti hii, Wizara, Serikali kwa ujumla mtuambie. Msituambie tu maneno kama zoezi linaendelea, mtuambie mmefika wapi? Kama kuna changamoto, ni nini? Tunataka kuona zoezi hili likikamilika ili tuendelee na hatua nyingine za mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi ili Kuruhusu Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu wa Kigosi na Azimio la Bunge la Kuridhia Kurekebisha Mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, niongeze mchango kwenye hoja zilizoko mbele yetu leo. Kwa pekee kabisa niungane na wenzangu kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya ya kujali Maisha ya wananchi wa nchi hii. mazimio haya ni Ushahidi wa moja kwa moja wa Mheshimiwa Rais namna anavyowajali na kuwapenda na kuwasikiliza Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kazi nzuri ambayo wameifanya kwenye kuchakata na kuandaa mazimio haya ambapo kufikia hatua hii kuja kujadiliwa ndani ya Bunge lako. Mwisho kwenye pongezi nikupongeze wewe mwenyewe na nikushukuru kwa namna ulivyotoa uongozi mzuri uongozi imara kwenye jambo hili mpaka tumefika hapa tulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesimama niongeze mchango kidogo na nianze kwa kuwaambia Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako Tukufu Kamati yako ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi Maliasili na Utalii inayofanya kazi kwa niaba ya Bunge lako kulisimamia na kuishauri Serikali kwa upande wa Wizara ya Ardhi na Wizara ya Maliasili na Utalii. Kwenye jambo hili imefanya kazi hii kwa umakini mkubwa sana. Imefanya kazi hii kwa kuangalia na ku-balance maslahi makubwa ya Taifa na kuangalia Maisha ya wananchi wa nchi ya Tanzania. Niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge tuunge mkono mazimio haya na kuwasaidia watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nitoe mchango kwenye maeneo hayo mawili. Eneo la kwanza kwenye eneo hili la Ruaha kama tulivyosema tunaipongeza Serikali kwa kazi hii nzuri lakini kwenye mchakato wa jambo la Ruaha nimejifunza mambo makubwa mawili ambayo naomba Serikali niishauri. Moja, nimejifunza kwamba Elimu kwa watu wetu juu ya tunayoyafanya kwa ajili ya Maisha yetu lakini kwa ajili ya nchi yetu ni jambo muhiu sana. Niiombe sana Serikali si kwenye jambo hili, siyo kwa mamlaka ya maliasili peke yake lakini Elimu kwa wananchi wetu ni jambo muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo nimejifunza, Serikali inafanya kazi kubwa inafanya kazi nzuri. Niwaombe Serikali iendelee kukubali kuwa na moyo huu mzuri wa kutafakari na kufikiria Maisha ya watu wetu wanaotoka kwenye jambo hili la Ruaha. Kwenye kazi iliyofanywa na Timu ya Mawaziri Nane mapendekezo yaliyotolewa kwenye kushughulikia jambo la Ruaha moja ya jambo nililojifunza yako baadhi ya maeneo machache ambayo taarifa zilizotumika kufikia maamuzi yale hazikuwa zimekaa sahihi kule uwandani kule chini kwenye ardhi. Naishukuru Serikali kwa busara yake baada ya kuona kuna haja ya kuongeza vitu vya ziada Serikali imefanya hivyo na leo tumefika hapa kuja kwenye haya maazimio. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaombe sana Serikali nitoe mfano tu wa kule Tanga kwenye eneo la Kaka yangu Mkinga, kwa Mheshimiwa kaka yangu Kitandula, Wilaya ya Korogwe kuna eneo kule kwenye Mto Umba, eneo la Bonde la Umba kuna eneo kwenye Kata ya Mwakijembe, kuna eneo kwenye Kata ya Kalawani kwenye Wilaya ya Korogwe taarifa zilizotumika tunaamini wataalam wakienda uwandani watakuja na picha kamili ya kusaidia kutatua mgogoro huu na kuwanufaisha wananchi kama vile wananchi wa Ruaha wanakwenda kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyohivyo na kwenye Kata ya Magambo kwa Lukonge kwenye Jimbo la Korogwe Vijijini kwenye Kijiji kile cha Magamba kwa Lukonge eneo la Chang’andi. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri wa Maliasili tutume tena timu yale maeneo ambayo bado wataalam wetu hawajarudi kwa mara ya pili, wakafanye uhakiki wa hali iliyopo kule chini pia tujitahidi kuongeza kasi ili maeneo yale yote ambayo yalipitiwa na Timu ya Mawaziri nane kazi ambayo mmewaachia wakuu wa mikoa ifanyike ikamilike ili tufunge mambo haya mogogoro hii iwe imekwisha na itakuwa ni utatuzi wa kudumu kwa migogoro hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la pili eneo la Hifadhi ya Kigosi, nirudishe tu historia kidogo kwa Neema ya Mungu nilipata nafasi ya kuwa sehemu ya Bunge la 11 mwaka 2019 nikiwa Mjumbe wa Kamati, ndiye niliweka mezani Taarifa ya Kamati kuhusu maoni kuhusu kupandisha hadhi eneo la Hifadhi ya Ugalla na Hifadhi ya Kigosi kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, kama kuna kazi ngumu tuliwahi kufanya kwenye Bunge hili ilikuwa ni kazi ya kupandisha Kigosi na kupandisha Ugalla. Wabunge wa maeneo haya walikuja wakilia walikuja wakilalamika wanaomba maeneo haya yasipandishwe hadhi ili wananchi wao wapate maeneo ya kufanya shughuli zao kwa sababu ya mazingira na sababu mbalimbali jambo hili halikuwezejana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee tumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa hiki kilichokuwa kinafanyika sasa. Kimekuwa ni kilio cha muda mrefu sana cha watu hawa kimekuwa ni kilio kikubwa cha Wabunge na wananchi wa maeneo haya. Ninaamini jambo hili linalokwenda kufanyika linakwenda kuwafanya wananchi wa maeneo yanayokaribiana na eneo la Kigosi yanayonufaika na eneo la Kigosi kurudisha moyo wa kuendelea kuipenda na kuithamini Serikali. Ninaomba jambo hili likasimamiwe vizuri lifanyike vizuri ili mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho ninaushauri kwenye maeneo madogo matatu; moja tuna hifadhi nyingi sana za Taifa lakini hifadhi zetu nyingi hazifanyi vizuri na kwenye uhifadhi, Hifadhi ya Taifa ndiyo hatua ya juu kabisa ya uhifadhi ambayo kwenye hatua hiyo shughuli za kibinadamu haziruhusiwi kabisa. Ni wakati sasa kama nchi tufanye tathmini sahihi kuhusu hifadhi zetu za Taifa zipi zinafanya vizuri, zipi ambazo tunaweza tukazibadilisha baadaye kupata mapori ya akiba ili mambo yaweze kwenda vizuri. Lakini kama yako maeneo ya kupandisha na kwenyewe pia yaendelee kupandishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili kama nilivyosema tuongeze kasi kwenye kukamilisha utatuzi wa migogoro yale maeneo ambayo Kamati ya Mawaziri nane imefika.

Mheshimiwa Spika, jambo la nne niishauri Wizara, mambo yanayokwenda kufanyika na mazimio haya yanatusaidia kupunguza migogoro kati ya wananchi na hifadhi wananchi na Serikali. Lakini hii peke yake haitoshi Mheshimiwa Waziri ni wakati sasa na Mheshimiwa Rais alishasema na ametoa maelekezo kalitafakarini upya namna ya kuliboresha na kuliimarisha Jeshi Usu ili kulipa elimu zaidi kulipa weledi zaidi na kulifanya liwe rafiki na wananchi tupunguze migogoro kwenye haya maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ni wakati wa kwenda kuliunganisha Jeshi hili, leo tunakwenda kuirudisha Kigosi ambayo ni kubwa sana, moja ya sababu tutaipandisha wakati huo na mambo ya kiusalama pia yalikuwepo. Tutampa TFS kufanya kazi lakini tusipoliimarisha jeshi hili tunahitaji utunzaji na uangalizi zaidi wa weledi na taaluma wanaopewa watu wa misitu ili mambo yaweze kwenda vizuri. Tukaliimarishe Jeshi Usu ili mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho nishauri, narudia tena kwa mara nyingine na nitaendelea kurudia hili. Kama nchi tukajidhatiti kwenye eneo la mipango ya matumizi bora ya ardhi. Siyo kweli kwamba tuna uhaba mkubwa kiasi hicho wa maeneo ya kufanya shughuli maeneo ya kulima, maeneo ya kuchunga na maeneo mengine. Moja ya changamoto tuliyonayo hatujatengeneza mipango vizuri ya matumizi ya maeneo yetu. Kuna ranch nyingi lakini ng’ombe wanaletwa maeneo ya kwenda kufuata malisho lakini ranch tunazo nyingi. Niombe sana Serikali jambo hili tukalipe uzito kwa wakati tuliokuwa nao ili mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hojanakubaliana na mazimio yote mawili nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kutoa mchango wangu kwenye bajeti kuu ya nchi yetu.

Nianze kwa kumpongeza kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri anayofanya ya kujenga na kuimarisha uchumi wa nchi yetu. Kipekee nimpongeze Mheshimiwa Waziri kaka yangu Dkt. Mwigulu, kazi yake ni njema, yeye na timu yake na niseme tu kwamba hatuna mashaka na uwezo wako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nichangie bajeti kwenye maeneo mchache. Eneo la kwanza ni kwenye hali ya makusanyo. Nimeona kwenye ukurasa wa 19 Mheshimiwa Waziri ameeleza hali ya makusanyo. Na kwa ninavyomfahamu alivyo bingwa wa namba ameweka fedha tu hakuweka asilimia. Mimi nikajipa kazi ya kwenda kwenye asilimia nikajikuta makusanyo ambayo tumeshakusanya mpaka anawasilisha taarifa ile Aprili, 2023 tuko kwenye asilimia 78. Niwapongeze kwa kazi hii nzuri lakini kwa mahitaji ya nchi yetu bado tuna haja ya kuongeza nguvu zaidi kwenye makusanyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, niwaombe Waheshimiwa Wabunge na Watanzania tuungane na Mheshimiwa Waziri. Suala la kusisitiza umuhimu wa ulipaji wa kodi sio suala la Waziri peke yake na wala si suala la Serikali peke yake. Hakuna nchi inayoweza kuwezeshwa bila watu kulipa kodi. Sisi kama viongozi tuungane pamoja kuhamasisgha ulipaji wa kodi kwenye nchi yetu ili tuendelee kutengeneza maendeleo ya kwetu sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo yako maeneo mawili naomba nitoe ushauri, eneo la kwanza nimeona kwenye ukurasa wa 107 Mheshimiwa Waziri ameeleza kuanza kutoza shilingi 20 kwa kilo ya saruji inayotoka nje na inayozalishwa ndani. Ukisema shilingi ishirini maana yake kwa mfuko mmoja unakwenda kuongeza shilingi elfu moja. Leo hii hatujaongeza tozo hii bei ya saruji ni kubwa na malalamiko ya watu wetu ni mengi, maeneo mengi watu wanashindwa kufanya kazi ya ujenzi kwa sababu ya bei hii ya saruji. Tukaliangalie vizuri jambo hili, sioni kama litakwenda kuwasaidia sana Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia watu watafanya ulinganisho, unakwenda kutoza shilingi 20 kwa kilo moja ya saruji lakini wakati huo huo kwenye ukurasa wa 97 unakwenda kutoa msamaha wa VAT kwenye gaming odds na kwenye gaming software. Jana amesema vizuri sana ndugu yangu Mheshimiwa Jerry Silaa, jambo hili si zuri. Tunaomba mkaliangalie vizuri kama Serikali na ikiwezekana kwenye finance bill marekebisho yafanyike ili tuliondoe jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho ambalo nataka nichangie ni kwenye upatikanaji wa fedha za kigeni. Mheshimiwa Waziri amesema vizuri kwenye ukurasa wa 50 na 51 wa hotuba yake, kwamba nchi nyingi ziliingia kwenye changamoto ya kuwa na upungufu wa fedha za kigeni ikiwemo nchi yetu. Lakini umeeleza jitihada na hatua ambazo Serikali inafanya ikiwemo kuongeza uzalishaji ili tupunguze kuagiza bidhaa kutoka nje, ninawapongeza wa hatua hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwenye eneo hili, pamoja na hii ya kuongeza uzalishaji na kupunguza kuagiza bidhaa liko eneo ambalo tunaweza kutengeneza fedha nyingi za kigeni kwenye nchi yetu, na si eneo lingine, ni kwenye eneo la sekta yetu ya utalii. Sekta ya utalii inaweza kutuingizia fedha nyingi za kigeni kwenye nchi yetu. Na bahati nzuri amesema mwenyewe kwenye hotuba yake. Niungane naye kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuamua kufanya kazi ya kutangaza utalii wa nchi yetu kwa vitendo. Matokeo ya Royal Tour yameonekana, amesema mwenyewe kwamba tumeongeza fedha za kigeni kutoka dola 1,310,000 mwaka 2021 hadi dola 2,527,000.7 mwaka 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ninayoiona hapa, tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa Royal Tour, tunampongeza kwa maneno au tunampongeza kwa dhati ya mioyo yetu na kwa kazi ambazo tunazifanya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo changamoto; mwaka 2019 wakati wa kupitisha bajeti ya mwaka 2019/2020 tulifanya marekebisho kwenye Finance Bill. Marekebisho tuliyoyafanya tukaleta utaratibu mpya wa taasisi za uhifadhi kukusanya fedha, akina TANAPA, Ngorongoro kwamba fedha zao zikusanywe moja kwa moja kwenye mfuko mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna shida na jambo hilo limefanyika lakini tangu tumeanza jambo hili changamoto zimekuwa ni nyingi. Tukaja na mawazo ndani ya Bunge hili kwamba pamoja na makusanyo haya kwenda moja kwa moja tuhakikishe tunaweka retention kwa taasisi hizi ili ziweze kujiendesha, shughuli za uhifadhi ni za gharama, zina dharula nyingi, wazo hilo halikusikilizwa. Wakati wa kupitisha bajeti ya mwaka 2021/2022 kamati ya bajeti ikashauri kama retention imeshindikana basi angalau muweze kutoa hali ya miezi miwili au mitatu mbele kama OC kwa taasisi hizi, mpaka leo imeshindikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunapozungumza leo, hali ya taasisi za uhifadhi ni mbaya. Tunakwenda kwenye high season hawana fedha, miradi ya barabara imesimama, OC haziendi. Hiyo high season tunakwenda nayo namna gani, tunatengenezaje fedha? Tunaomba Mheshimiwa Waziri walete utaratibu mpya, tutoe retention kwa taasisi hizi. Wakishindwa retention basi OC za taasisi hizi wa akina TANAPA, Ngorongoro, TAWA zitoke mapema, ikiwezekana awe na advance ya miezi mitatu. Tembo wanasumbua wananchi taasisi hazina fedha, majangili wanarudi kwa kasi taasisi hazina fedha lazima tuziwezeshe taasisi hizi ziweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho Mheshimiwa Waziri akija atuambie, wakati wa bajeti ya Wizara ya Maliasili tulisema lakini hatukupata majibu. tumekwama wapi kwenye zoezi la kuhamisha watu kwa hiari kwenye hifadhi ya Ngorongoro? Zaidi ya miezi saba zoezi limesimama. Kama unataka kunusuru hifadhi ile ni lazima tuhakikishe, tunahamisha watu na watu wamekubali, wamejiandikisha, wamesimamisha shughuli zao tumekwama wapi? Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha atuambie... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Niungane na wenzangu kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, vijana wenzangu, kwa uteuzi wa kuongoza Wizara hii. Tunawafahamu vizuri, tufahamu uwezo wao na tuna matumaini makubwa sana na wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda niende harakaharaka, muda ukiruhusu nitakuwa na mambo matatu. Jambo la kwanza ni kilimo cha umwagiliaji. Kilimo cha Umwagiliaji kinaongeza tija, kinaongeza eneo la kulima na kinaongeza vipindi na misimu ya kulima. Ninazo takwimu kuanzia mwaka 2015 mpaka sasa tumeongeza hekta ngapi kwenye kilimo cha umwagiliaji, lakini kwa sababu ya muda sitaki kuzitoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona malengo ya Mheshimiwa Waziri, ameweka malengo ya kuongeza hekta elfu tisini na tano na tano kwenye mwaka wa fedha huu unaokuja. Jambo hili litawezekana kama mambo makubwa mawili yatafanyika. Jambo la kwanza ni lazima kama nchi tukubali kutafuta fedha zaidi nje ya bajeti zetu tulizokuwanazo kwa ajili kugharamia kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni kuhakikisha tunasimamia na kutekeleza miradi mikubwa itakayo-cover eneo kubwa. Kwenye eneo hili niwe specific kabisa kwenye eneo la Bwawa la Mkomazi. Bonde la Mto Mkomazi na Bwawa la Mkomazi. Tumesema sana, tumefanya vikao vingi, ni ahadi ya chama chetu kwenye uchaguzi na Mheshimiwa Waziri alitoa maelekezo kwa watu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji. Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha nataka kusikia nini kinakwenda kufanyika na wakati gani kuhusu Bwawa la Mkomazi, pamoja na urafiki na kazi anayoifanya nisiposikia kitu cha kuwaridhisha watu wa Korogwe, nitakuja kushika Shilingi.

Mheshimiwa Spika, siyo tu Mkomazi kuna Bwawa la Kwamkumbo tunayo ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri ameshatoa maelekezo hatujaona kinachoendelea, tumekwama wapi? Ukija kwenye majumuisho nitapenda kujua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ili niweze kuzungumza kwenye suala zima la zao la mkonge, Mheshimiwa Waziri nimeona umesema malengo yetu ni kutoka tani 36,698 kwenda mpaka tani 60,000 kwenye mwaka wa fedha unaokuja, naomba kukumbusha jambo, hatuwezi kufikia haya malengo kama hatutaendelea kuwajali na kuwathamini wakulima wadogo wadogo, mchango wa wakulima wadogo ni mkubwa sana kwenye zao la mkonge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2019 kwenye tani tulizozalisha, mchango wa wakulima wadogo ni asilimia 24, mwaka 2020 ni asilimia 30 na mwaka 2021 ni asilimia 37. Lakini wakulima wanachangamoto, Mheshimiwa Waziri tumehamasisha, Waziri Mkuu amefanyakazi nzuri, lakini bado kuna changamoto kubwa kwa wakulima wadogo wadogo. Mashine za kuchakata mkonge imekuwa ni changamoto. Tumeleta kampuni kule Sisalana imechukua mitambo kuwa ya katani wanawazalishia wakulima wetu. Gharama ya uchakataji ni kubwa sana inawaumiza wakulima wetu, lakini mitambo ile ni mibovu inafanya tunapata mkonge mchache lakini pia hata ubora wa mkonge wenyewe unapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema sana, ninashauri mambo matatu kwenye jambo hili. Jambo la kwanza, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo Naibu wako alikuja Korogwe, Bodi ya Mkonge waliunda Kamati ya kupitia zile gharama, wameenda wamekwama wanasema subiri Mkuu wa Mkoa aseme. Bodi ya Mkonge ndiyo yenye dhamana ya kusimamia mkonge kwenye nchi hii. Tunawaomba toeni tamko juu ya bei halali inayofaa kulipwa na wakulima wetu wadogo wa mkonge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili Mheshimiwa Waziri tununue mashine, Bodi na Wizara nunueni mashine za kuchakata mkonge muwape wakulima wetu. Jambo la tatu Mheshimiwa Waziri bado wakulima wetu wanamadai na Kampuni ya Katani. Mlichukua mitambo ya katani akapewa NSSF akaenda Kampuni ya Sisalana, lakini ukweli ni kwamba kwa mujibu wa Waraka Na. 31 wa 2005 wa Baraza la Mawaziri, Katani alipaswa kutengeneza kampuni ili wakulima wetu wadogo wadogo wawe hisa kwenye kampuni hizo kwenye zile AMCOS tulizokuwa nazo, mambo hayo hayakufanyika. Leo umechukua mitambo umempa Sisalana anawahujumu wananchi wetu, anawahujumu wakulima wetu. Mashine ambayo ilitakiwa izalishe ichakate mita 100 kwa siku leo wanachakata mita 60. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini cha kufanya Mheshimiwa Waziri, Wizara ya Kilimo ninyi ndiyo wasimamizi wa sera kwenye eneo la kilimo. Kaeni na Msajili wa Hazina tupitie ule mchakato ulivyokuwa, tutoe hizi mashine kwa Sisalana tuwape wananchi, tuwape wakulima wadogo kwenye AMCOS zao wasimamie. Pia mnaweza mkatusaidia kuwa wasimamizi wa mazungumzo kati ya AMCOS zetu na Benki ili wakulima wetu kupitia AMCOS zao wakopeshwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hakuna hatari kubwa kwenye zao la mkonge kama kutenganisha mchakataji na mzalishaji. Mchakataji akiwa hana uchungu na mazao ya mkulima atamkwamisha, na ndicho kinachofanyika, kampuni hii kwa sasa inawahujumu wananchi wetu. Mheshimiwa Naibu Waziri umeenda umewaambia wachimbe kisima wachakate mkonge mwingi kwa siku, watoe mkonge ulio bora Zaidi, mpaka leo hakuna kilichofanyika. Sisi ndiyo tuna dhamana kusimamia mkonge Wizara ya Kilimo, tusiwaachie watu wakacheza na mkonge wa wakulima wetu, watawakatisha tamaa, wataacha kulima, tutarudi nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni upande wa chai.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mbunge, muda wako umemalizika.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unipe dakika moja nimalizie. Bodi ya Chai isiwasahau wakulima wa Usambara kama inavyofanya kwa wakulima wa Mafinga na Nyanda za Juu Kusini, kiwanda cha Mponde tumekisubiri kwa muda mrefu ni wakati sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu kwenye Muswada huu wa Sheria muhimu ulioko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kushukuru na kumpongeza sana mtoa hoja kwa maana ya Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kazi nzuri na usikivu mzuri waliokuwa nao kusikiliza na kukubali na kuthamini maoni na michango ya Waheshimiwa Wabunge. Kipekee sana niipongeze sana Kamati yetu ya Bajeti imefanya kazi nzuri na kwa hakika imefanya kazi kubwa kwa niaba ya Bunge lako hili. Tunawapongeza sana kwa kazi nzuri waliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi hii nzuri waliyoifanya nimeona nichangie kwenye maeneo tu machache; na sehemu kubwa ni pongezi kwa sababu kazi kubwa imefanyika ya kurekebisha Muswada huu tofauti na vile ambavyo ulikuwa umesomwa kwa Mara ya Kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, kwani kwenye Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Simu, marekebisho yaliyofanyika, na haswa ule ushauri wa Kamati wa kuweka ukomo wa vile viwango, ni jambo kubwa sana na inatusaidia hata wananchi wetu wanaona ni namna gani ambavyo pamoja na kwamba tunazihitaji kodi kwa ajili ya maendeleo, lakini wakati huo pia tunaendelea kuzingatia namna ya kupunguza huu mzigo kwa wananchi wetu. Niwapongeze sana kwa jambo hilo zuri ambalo tumelifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kwenye mabadiliko ya Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta, Sura ya 220, amesema hapa Mheshimiwa Kakunda na Mheshimiwa Kigwangala; Mheshimiwa Waziri jana amesema hapa kwamba hela hizi hazitaguswa, zitakwenda moja kwa moja. Ili jambo hili liwe na tija ambayo inakusudiwa ni lazima tuliwekee utaratibu ambao uko wazi zaidi tofauti na ilivyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tukubaliane Mfuko wa Barabara umefanya kazi kubwa na unafanya kazi nzuri, lakini kwa kuwa tuna chanzo cha fedha cha kueleweka kwa ajili ya shughuli za TARURA, ni lazima tufikirie na tukubaliane kuanzisha mfuko maalum kwa ajili ya barabara za vijijini. Tukianzisha mfuko huu maalum maana yake ni kwamba, fedha hizi zikipatikana; huko zinakopatikana na huko zinakokatwa, zitakwenda moja kwa moja kwenye mfuko huu kufanya kazi ambayo imekusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo linaweza kuja kuwa jambo la baadaye huko tunakokwenda, lakini kwa sasa tukiwa bado hatujaenda kufanya mabadiliko ya sheria kwenda kuanzisha mfuko huo, Mheshimiwa Waziri kwanza tukaangalie kwenye zile kanuni, tukaziboreshe ili kwa sasa pia kanuni zile ziseme wazi kuhusu mapato haya na mgawanyo wake tunaokwenda kuongeza kwenye ule mfuko wetu wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nizungumze kuhusu marekebisho ya Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa. Nilichangia hapa na nimesema nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa usikivu, nimeona mmesema mmeamua kuondoa mapendekezo ya marekebisho mliyokuwa mmeyaleta yale, tunawashukuru sana, ni jambo zuri, mnakwenda kutusaidia, lakini tutakuwa hatujafika mwisho wa jambo letu, lazima huko mbele ya safari tuangalie namna ya kufikisha jambo hili kwenye hatua ya mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichokuwa tunakisema hapa, kabla ya 2014 Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Kifungu cha 16 (7), kilikuwa kinasema tu kwamba Service Levy inayolipwa, italipwa hivyo hivyo kwa kiwango hicho hicho, kwa wenye viwanda ndiyo utakuwa ushuru wa viwanda. Mwaka 2014 yakafanyika marekebisho tukaongeza pale kwamba, cooperate entity ambayo imelipa Service Levy haitalipa produce cess. Tukawa na mgongano hapo kidogo, sisi wengine tukaenda kutengeneza sheria ndogo ili itusaidie kuweza kukusanya. Yalipokuwa yanakuja marekebisho haya ambayo yalikuwa yanapendekezwa mwanzoni, yangefanya zile sheria ndogo zisiweze kufanya kazi, tungeweza kuzifunga mikono. Kwa hiyo, naishukuru Serikali kwa kuondoa yale mapendekezo, tumebaki tulivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tupate suluhu ya mwisho ya jambo hili mbele ya safari huko tukakirebishe hiki kifungu cha 16 (7). Tuynakirekebisha kwa sababu gani? Wenzetu wa Wizara ya Kilimo ndiyo wanasema sana hoja hii kwamba, hawa wenzetu wasilipe tozo mbili mbili, kwamba asilipe Service Levy, pia akaja akalipa na Produce Cess, lakini hizi ni tozo mbili tofauti, zinalipwa na watu wawili tofauti na kwa namna tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Sheria ya Fedha anayelipa Produce Cess ni mnunuzi, anayelipa Service Levy ni huyu ambaye anafanya shughuli pale kwa huduma anazozifanya. Changamoto ambayo inakuja, wako baadhi ya wazalishaji ambao wanunuzi wao hatutakuja kukaa tuwajue kwa kuwa wanajua wenyewe wanakokwenda kulipata soko; na wanunuzi wengine hawatakuja kuingia kwenye hii nchi, watapelekewa mzigo huko huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ikibaki hivyo, Halmashauri nyingine zitashindwa kupata fedha kwa sababu wanunuzi hawapo. Mmeandoa yale marekebisho, siyo by law itakwenda kutekelezeka, lakini ziko Halmashauri ambazo ili ushuru huu waukusanye, ni lazima wakatengeneze sheria ndogo ambazo zitazuia mazao haya yasitoke kwenye mamlaka ya Halmashauri kabla ya kupewa kibali na Halmashauri na kibali hicho kisitoke kabla ushuru huu wa mazao haujalipwa. Hao watafanya vizuri. Wasipotengeneza hiyo, hakuna watakachokipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa usikivu wake, lakini nashauri ni lazima tunakokwenda mbele ya safari tuone namna ya kukiboresha zaidi kifungu hiki ili kuondoa aina yoyote ile ya utata ambayo inaweza ikajitokeza. Sisi kwa mfano Mkoa wa Tanga sasa hivi itakuwa ni rahisi tu, mabadiliko aliyoyaondoa by law yetu itafanya kazi, tutaendelea kukusanya mapato yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nampongeza Mheshimiwa Mtoa Hoja, mabadiliko ni mazuri na marekebisho ni makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)