Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Timotheo Paul Mnzava (51 total)

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na naishukuru Serikali kwa kazi waliyoifanya. Pamoja na majibu hayo nina maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa barabara hii kwa mara ya kwanza kabisa iliwekwa kwenye Ilani mwaka 2010 na mwaka 2015 na kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hii Serikali haioni iko haja sasa ya kutenga fedha zaidi na kuongeza kasi ya utekelezaji ili tujenge barabara hii isivukwe na muda wa Ilani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wananchi wa Korogwe Vijijini wamekuwa wakisubiri utengenezaji wa barabara hii kwa hamu na kwa muda mrefu, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili kuongozana nami kwenda Korogwe akaone hali ya barabara hii na kutoa neno la matumaini kwa wananchi wa Jimbo la Korogwe Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Timotheo, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Timotheo kwa sababu amekuwa anafuatilia sana mambo mbalimbali kuhusu eneo lake, nampongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maswali yake, kwa ufupi nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kama ilivyo kawaida kwamba Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kufanya maboresho ya barabara katika eneo lake. Kwa hiyo, nimuahidi tu tutaendelea kutenga fedha kadri tunavyopata bajeti ili tuendelee kuboresha barabara katika eneo hili. Niliwahi kutembelea katika eneo hili lakini nakubalia nitakuja kwa sababu zipo changamoto nyingi ili nije kuona pia na maeneo mengine. Ahsante sana.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kazi kubwa inayofanywa na TARURA inapunguzwa faida au kufifishwa faida yake kutokana na ukosefu wa fedha za kujenga madaraja muhimu. Wananchi wa Korogwe wamekuwa wakipata shida ya muda mrefu ya Madaraja yao ya Mbagai, Makondeko na Mswaha. Serikali haioni kwamba iko haja ya kuweka jicho maalum kwenye bajeti inayokuja kwa ajili ya madaraja kwenye barabara ambazo zinatengenezwa na TARURA?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Korogwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge, ni Mbunge mpya lakini anafanya kazi kubwa sana ya kutetea wananchi wake wa Korogwe. Jambo la pili ni kwamba huu mpango mkakati ni wa kudumu na ndiyo maana imeanzishwa TARURA ili wataalam wetu hawa wakilala, wakiamka wafikirie barabara zetu za vijijini na mijini. Kwa hiyo, naomba tu aamini kwamba kazi hii inaendelea kufanyika vizuri na huu ni mwaka wa bajeti na bajeti ya barabara hizi inabidi ianzie katika vikao vyao vya ndani kuanzia kwenye mtaa, kijiji, halmashauri yao na hatimaye hapa Bungeni. Sisi kama Serikali tupo tayari kushirikiana na wananchi wa Korogwe na Mheshimiwa Mbunge wao ili kuhakikisha kazi hii inafanyika vizuri na kuondoa kero zilizopo pale.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kama ilivyo Igalula kumekuwa na changamoto kubwa ya mawasiliano kwenye Jimbo la Korogwe Vijijini hususan kwenye Kata za Kizara, Makumba, Kalalani, Mkalamo, Elewa na Lutindi na Mheshimiwa Naibu Waziri anafahamu changamoto hizi. Ni lini Serikali itatoa utatuzi wa changamoto hizi zinazowakabili watu wa Korogwe Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikiri kwamba nilishatembelea Korogwe Vijijini na hilo eneo alilolitaja Mheshimiwa Mbunge nililiona, ni kweli kwamba kuna mnara wa mawasiliano lakini hauna nguvu ya kutosha. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba nitatuma wataalam kwanza wakaongeze nguvu kwenye hicho kijiji cha kwanza alichokitaja halafu na nitatoa orodha nyingine kesho aangalie vijiji vingine ambavyo tumeviorodhesha kwa ajili ya kuimarisha mawasiliano maeneo hayo.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri alifanya ziara kwenye hili na anazungumza eneo ambalo analifahamu. Pamoja na majibu yake mazuri ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza mradi huu ulibuniwa muda mrefu sana na ni mradi ambao una uwezo wa kuhudumia eneo kwa maana hekta karibu zaidi ya hekta 5000 na tathmini ambayo unasema ilifanyika ya usanifu uliofanyika ulifanyika muda mrefu.

Je, Serikali iko tayari sasa kuharakisha mapitio ya usanifu upya ili kujua gharama halisi kwa mazingira tuliyokuwanayo sasa na kwa namna ya kutekeleza mradi huu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili tunayo Skimu ya Songea na Makalala kule Magoma, lakini pia skimu ya Kwamkumbo pale Mombo ambapo wananchi wamekuwa wakiathirika wakati mvua maji yakiwa mengi yanaenda kwenye mashamba ya wakulima na kuharibu mazao na kusababisha hasara kubwa.

Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari, kuwatuma wataalam wa umwagiliaji waende kwenye maeneo haya na kuona namna ya kutatua changamoto hizi za wananchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anataka kufahamu Serikali kuharakisha mchakato wa kuweza kupitia upya tathmini ya mradii huu. Kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tangu siku zile nilivyofika mimi katika bonde hili na kufika bwawa lile tayari tushawaelekeza viongozi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro wanalifanyia tathmini upya bwawa lile ili kujua gharama halisi na kuanza utekelezaji kwa mipango ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu athari ya mafuriko katika skimu hizi tatu alizozitaja za Skimu ya Songea na Makalala, kwamba nitumie nafasi hii kwanza kuwaelekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro kwenda haraka katika mabwawa haya kufanya tathmini na kuona namna gani tunaweza kujenga miundombinu ile yamatuta kwa ajili ya kukinga mafuriko ya athari ya mabwawa haya.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ni miongoni mwa halmashauri ambazo zilielekezwa kuhamisha Makao yake Makuu ya halmashauri kutoka Mjini kwenda kwenye maeneo yake ya utawala, lakini kuna changamoto kubwa sana ya barabara haswa kwa wananchi wa Tarafa ya Bungu barabara ya kutoka Makuyuni Kwemshai na barabara ya Makuyuni, Zege Mpakayi.

Je, Serikali iko tayari sasa kuwa na mkakati maalum wa kusaidia uboreshaji wa miundimbinu ili wananchi hawa waweze kufika kiurahisi kwenye maeneo ya Makao ya halmashauri mpya zilizoanzishwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa kwanza nimpongeze kwa namna anavyohangaika na barabara za eneo lake na nimshukuru alinipa ushirikiano wa hali ya juu nilivyotembelea maeneo haya na maeneo mengine ambayo hakuyataja.

Mheshimiwa Naibu Spika, na niseme tu labda ni kwa kutoa kumbukumbu sahihi kwa mvua ambazo ambazo ziliathiri Mkoa wa Tanga zilikuwa ni kubwa sana kiasi kwamba urejeshaji wa maeneo ambao tumeyafanya hadi sasa tumetumia bilioni 7.8 kurejesha eneo la Tanga peke yake kwa mvua za mwezi Octoba peke yake na nikubaliane na yeye kwamba sasa tumefanya tena kwenye uratibu huu wa mvua zilizonyesha kuanzia Octoba kuja Januari kwa upande wa Tanga pia kumbukumbu kwamba kuna mahitaji makubwa ikiwepo maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge umeyataja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumetambua maeneo yote yenye shida hizi ikiwepo maeneo uliyoyataja na tunafanya utaratibu wa kuwa na fedha tena kama tulivyofanya Awamu ya I ya mvua za mwezi Octoba tutakwenda kufanya kazi kubwa kufanya marejesho ya maeneo haya ambayo nayataja kwa sababu nafahamu eneo la kwako pia ndiyo limekumbwa na maporomoko ya udongo wananchi wamepata athari kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunatambua hivyo na tutakuja kufanya uharaka wa kurejesha maeneo hayo uliyoyataja,ahsante sana.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kabla sijauliza maswali ya nyongeza, niruhusu niendelee kuwapa pole wananchi wa Jimbo langu la Korogwe Vijijini na Mkoa mzima wa Tanga kwa mafuriko makubwa yaliyotupata siku chache zilizopita. Tunaendelea kutumaini juhudi ya Serikali kurejesha miundombinu yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; moja ya sababu ya nchi tunazoshindana nazo kwenye soko la mazao ya viungo na mazao ya bustani kufanya vizuri ni wao kuwa na mamlaka za kusimamia mazao haya. Je, ni lini Serikali yetu itaona umuhimu wa kuanzisha Mamlaka ya Kusimamia Mazao ya Viungo na Mazao ya Biashara?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wananchi wa Tarafa ya Bungu, Wilaya ya Korogwe, ni wakulima wakubwa na wazuri sana wa mazao ya viungo na zao la chai, lakini tumekuwa na changamoto kubwa sana ya bei kwenye zao la chai. Je, ni upi mkakati mahususi wa Serikali wa kuhakikisha kwamba wanaboresha bei ya zao la chai ili kuweza kuwaletea tija wananchi na wakulima wa zao la chai nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mnzava kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kutumia nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba Wizara ya Kilimo inafahamu umuhimu wa kuanzishwa kwa taasisi itakayosimamia mazao ya horticulture na mazao ya viungo. Hivi sasa tunapitia mfumo na muundo wa Wizara kupunguza idadi ya bodi na kuanzisha mamlaka chache ambazo hazitazidi tatu, mojawapo ikiwa ni Mamlaka ya Maendeleo ya Mazao ya Horticulture.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwenyezi Mungu akijaalia hivi karibuni Bunge hili litapokea sheria ambayo itaonesha mabadiliko ya muundo wa taasisi mbalimbali ndani ya Wizara ya Kilimo ili kuipa sekta hii nafasi inayostahili kwa sababu ni subsector ndogo katika Sekta ya Kilimo inayokua kwa kiwango kikubwa sana na inahitaji attention inayostahili. Kwa hiyo nimtoe hofu kwamba tuko katika hatua za awali na kabla ya kufika Bunge lijalo la Bajeti tutakuwa tumeshaanzisha Mamlaka ya Mazao ya Horticulture.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la chai; ni kweli kama Serikali hatua tunazochukua mojawapo sasa hivi tuko katika hatua za mwisho za kuanzisha a primary market katika eneo la Dar es Salaam ili tuwe na mnada wa kwetu hapa Tanzania. Tumesha-earmark eneo na sasa hivi tuko katika hatua za awali kutengeneza utaratibu ili chai yetu badala ya kwenda kuuziwa katika soko la Mombasa sasa ianze kuuziwa katika soko la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tutatumia mfumo wa TMX ili kuwaruhusu wanunuzi duniani waweze ku-bid. Mchakato huu unawahusisha Sekta Binafsi ambao wamewekeza katika chai ili kuhakikisha kwamba zao la chai linapata soko na bei ya uhakika. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge tunaamini kwamba ndani ya muda mfupi tutaanzisha soko la kwetu ndani ya Tanzania na chai yetu itauziwa hapa na itapunguza gharama na kumpatia mkulima bei nzuri.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni Wilaya ya Korogwe zimeathiri kwa kiasi kikubwa miundombinu ya maji na kusababisha shida ya upatikanaji wa maji.

Je, Mheshimiwa Waziri anasema ni upi mkakati maalum na wa dharura wa Serikali kurekebisha miundombinu hii na kurudisha miundombinu hii na kurudisha huduma ya maji kwa wananchi wa Korogwe Vijijini kama wanavyofanya wenzenu kwenye upande wa barabara?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni uhai. Namwomba Mheshimiwa Mbunge tukutane leo saa 7.00 ili tujue namna ya kuweza kuwasaidia wananchi wa Korogwe.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, pamoja na majibu ya matumaini ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, moja ya changamoto kubwainayochelewesha kukamilika kwa wakati kwa miradi yah ii ya REA ni tofauti ya size ya transfoma iliyopo kwenye mikataba ya kVA 33 na ukubwa na laini ambazo wanachukulia ule umeme. Jambo hili limesababisha kuchelewa kwa Miradi ya REA ya kukamika kwenye Jimbo la Korogwe Vijijini, kwenye vijiji vya Kulasi na vijiji vya Mswaha Majengo, nguzo zimesimama kwa zaidi ya miezi sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itatoa maelekezo kwa REA kuharakisha utatuzi wa changamoto hizi ili wananchi hawa waweze kupata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika Jimbo la Korogwe Vijijini zipo kata tano ambazo vijiji vyake vyote katika kata hizo havijafikiwa na huduma ya umeme. Kata za Kizara, Foroforo, Kararani, Mpale na ya Mswaha. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, uko tayari kuwahakikishia wananchi wa kata hizi kuiwapa kipaumbele na kupata umeme kwenye mwaka wa fedha unaoanza Julai mwaka huu?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi la Mheshimiwa Mnzava, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Mnzava, pampja na kwamba si Mbunge wa muda mrefu, lakini kafanya mambo makubwa sana kwenye jimbo lake hata nilizotembelea. Baada ya kusema hayo basi napenda nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mnzava.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, ni kweli, katika Kijiji cha Kurasi Kibaoni pamoja na Mswaha Majengo, kuna transfoma zilifungwa za kVA 33, lakini tumeshamwelekeza mkandarasi kuanza kushusha kutoka kVA 33, kwenda kVA 11 kuanzia Jumamosi iliyopita. Kwa hiyo, vijiji viwili vya Kulasi pamoja na Mswaha vimeshaanza kupelekewa umeme na vitapata umeme mwisho wa wiki hii. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Mnzava katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kweli zipo kata tano ambazo zilikuwa hazijapata umeme katika Jimbo la Korogwe Vijijini na kati ya kata tano tayari kata moja ya Mswaha- Majengo imeshaanza kupelekewa umeme. Zimebaki kata nne ya Foroforo pamoja na Kirarani ambazo nazo zinaanza kupelekewa umeme kuanzia Julai mwaka huu na kufikia Juni, mwakani nafikiri zitakuwa zimepatiwa umeme. Nimpongeze sana Mheshimiwa Mzava, aendelee kutupa ushirikiano.

Mheshimiwa Naibu Spika, na nilipotembelea tarehe 22 kwa Mheshimiwa Mnzava, Kijiji cha Mkalekwa pamoja na Welei vilipelekewa umeme na nikaagiza Kijiji cha Kulasi nacho kiwashwe umeme. Kimeshawashwa umeme tangu tarehe 28 mwezi uliopita. Kwa hiyo, nashukuru sana Mheshimiwa Mnzava tuendelee kushirikiana. Ahsante sana.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kama ilivyo kwa barabara hii ya Lupiro – Malinyi, barabara ya Korogwe – Dindira – Bumbuli mpaka Soni iliahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, lakini pia kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ilikamilika. Napenda kujua, ni lini sasa kazi ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami itaanza ili kuwasaidia wananchi wa Korogwe na Lushoto kwenye eneo la usafiri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mbunge ambaye ameuliza barabara ya Korogwe hadi Soni ni lini itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wabunge wawe na imani na Serikali hii ya Awamu ya Tano kwani kwanza ni ahadi za viongozi wetu wa kitaifa Mheshimiwa Rais lakini pia zimetajwa katika Ilani. Naomba tuanze bajeti na nina hakika hizi barabara ambazo tunaziulizia zimo, kwa sababu tumeahidi tutatengeneza hizi barabara kwa kiwango cha lami. Nashauri Waheshimiwa Wabunge wawe na imani kwamba barabara hizi zitajengwa ikiwa ni pamoja na barabara ya Korogwe kwenda Soni. Ahsante.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na Serikali kwenye ujenzi wa hospitali na vituo vya afya, kama alivyokiri Mheshimiwa Naibu Waziri, ni kweli bado kuna uchakavu mkubwa wa vituo vyetu vya afya.

Napenda kujua kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, ni upi sasa mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba tunamaliza kabisa ukarabati wa vituo vyote vichakavu na vikongwe vikiwemo Vituo vya Afya vya Mombo, Bungu na Magoma katika Wilaya ya Korogwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mnzava, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imefanya kazi kubwa sana katika ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati na pia imefanya kazi kubwa sana katika kukarabati vituo vya afya ili kuwezesha kutoa huduma bora kwa wananchi. Ni kweli pia kwamba bado kazi ipo na inahitajika kufanyika zaidi na Serikali inatambua kwamba bado kuna vituo vya afya ambavyo ni chakavu na vinahitaji kukarabatiwa vikiwemo vituo vya afya vilivyopo katika Jimbo la Korogwe Vijijini kwa Mheshimiwa Mnzava.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka huu, Serikali imetenga shilingi bilioni 11 na imeshaainisha hospitali 43 za Halmashauri kwa ajili ya ukarabati na kuongeza majengo ambayo yanapungua ili yaweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Pia mchakato wa kuandaa na kuainisha vituo vya afya chakavu vikiwemo vya Korogwe Vijijini, unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mnzava kwamba vituo vyake pia vitaingizwa katika orodha hiyo ili kadri ya upatikanaji wa fedha viweze kukarabatiwa na kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake lakini nina nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ahadi ya ujenzi wa bwawa na miundombinu ya umwagiliaji kwenye eneo hili ni ya muda mrefu tangu wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano aliuhisha ahadi hiyo wakati wa kampeni zake za mwaka 2020. Eneo hili lina maji mengi ambayo yanaleta mafuriko kwenye Kata zaidi ya tano. Kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri kwenye majibu yake ni sehemu ya mpango kabambe, swali langu nataka kujua, ni lini ahadi hii itatekelezwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Wilaya ya Korogwe inaongoza kwa fursa na mazingira mazuri ya kilimo cha umwagiliaji. Serikali haioni sasa ni wakati sahihi kuboresha skimu zilizopo kwenye Tarafa za Magoma na Mombo ikiwemo Skimu ya Kwamkumbo ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri waliitolea ahadi wakati wa ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu Februari, 2021?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya Mheshimiwa Mnzava, Mbunge wa Korogwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini tutaijenga Skimu ya Mkomazi, commitment ya Wizara na Serikali ni kwamba katika kipindi cha miaka hii mitano kwa maana ya plan ya 2025, Skimu ya Mkomazi ni moja kati skimu ambazo Serikali itazijenga. Nataka nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba hii ni moja kati ya skimu tutakayoipa priority kwa sababu kila mwaka maafa yanayotokea na upotevu wa maji katika eneo hilo ni makubwa sana kuna potential kubwa ambayo na sisi tunafikiri kwamba ni muhimu tukaifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi tuliyoitoa tukiwa katika ziara na Mheshimiwa Waziri Mkuu ipo palepale. Tuliahidi kwamba baada ya mvua hizi wataalam wetu wa Wizara ya Kilimo kwa maana ya wataalam wa Tume ya Umwagiliaji watapeleka vifaa kwa ajili ya kwenda ku-repair ile skimu ambayo ilikuwa imeathirika. Ahadi ile ipo palepale, naomba avumilie, Inshaallah, hivi karibu wataalam wetu watakwenda.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu haya ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kuna haja ya kukaa nae baadaye tuangalie hizi takwimu vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na majibu hayo ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, moja ya sababu kubwa ya upungufu wa watumishi kwenye Halmashauri za Vijijini kama ilivyo Halmashauri ya Korogwe au kama ilivyo kwenye Jimbo la Mlalo kule kwa ndugu yangu Shangazi, sababu kubwa ni kwamba watumishi wanaenda kule, wakipata ajira wanahama. TAMISEMI mmekuwa mkipitisha uhamisho wa watumishi wakati mwingine bila kuzingatia maoni ya wakurugenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kujua ni lini sasa TAMISEMI mtakubali kuzingatia maoni ya Wakurugenzi kutoa watumishi mbadala kabla ya kuwahamisha waliopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wakati mwingine tunaweza kupunguza shida ya upungufu wa walimu kwa kusawazisha Ikama ndani ya halmashauri yenyewe. Kwa mfano Halmashauri ya Korogwe zaidi ya miaka mitatu kifungu cha moving allowance hakijawahi kupat afedha. Inasababisha ugumu katika kusawazisha Ikama ya watumishi ndani ya halmashauri yetu. Ni lini Serikali itakuwa tayari sasa kutoa fedha ya kutosha kwenye vifungu hivi vya uhamisho ili kuweza kusababisha Ikama ndani ya Halmashauri yenyewe? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tumekuwa na changamoto ya upungufu wa watumishi katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa ikiwemo Halmashauri ya Korogwe. Lakini kama ambavyo nimetangulia kutoa m ajibu ya msingi kwamba Serikali imeendelea kuweka jitihada za kutosha kuhakikisha kwamba tunaendelea kuongeza watumishi katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni kweli tumekuwa na changamoto kubwa sana ya watumishi hasa wanaokuwa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa maeneo ya vijijini kuomba uhamisho wengi wao wakiomba kuhamia mijini. Ofisi ya Rais TAMISEMI na Serikali kwa ujumla imeendelea kuhakikisha inazingatia Ikama katika maeneo ya vijijini na imeendelea kuhakikisha inasimamia kwa karibu uhamisho wa watumishi hasa kutoka vijijini kwenda mijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba si kweli kwamba TAMISEMI imekuwa kila siku inapitisha maombi ya uhamisho kwa watumishi wote wanaoomba. Mara kwa mara tumekuwa tunachuja sababu za msingi ambazo zinasababisha baadhi ya watumishi kukubali lakini watumishi walio wengi kutokukubaliwa kupata uhamisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili Serikali imeweka utaratibu sasa. Ofisi ya Rais TAMISEMI tutaenda kuzindua mfumo wa kielektroniki ambao sasa maombi ya uhamisho yatapitishwa kwa njia ya kielektroniki na yatawezesha sasa kuchuja kwa uhakika zaidi hamisho zote ambazo zinaombwa na itawezesha sana watumishi wetu katika maeneo ya vijijini kubakia kufanya kazi katika maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili tutakwenda kuwa na mikataba ya watumishi wanaoajiriwa. Watumishi wengi wamekuwa wakiajiriwa maeneo ya vijijini, wakifika na kupata cheque number wanaanza kufanya jitihada za kuhama. Sasa kabla ya kuajiriwa tutahakikisha tunakuwa na mikataba kwamba baada ya kupangiwa kwenye vituo hivyo ni lazima wakae angalau miaka mitatu au mitano kabla ya kuanza kuomba vibali vya uhamisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii itatuwezesha sana kuhakikisha watumishi wetu katika maeneo ya vijijini wanabaki na kutoa huduma ambazo zinakusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na ugumu wa kusawazisha watumishi kwa maana ya ikama katika maeneo yetu, ni kweli na Serikali imeendelea kutenga fedha za matumizi mengineyo kwa awamu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha kuhakikisha yale maeneo ambayo yana watumishi wengi lakini maeneo mengine yana watumishi wachache tuweze kufanya usambazaji wa ndani ya halmashauri. Hili pia tumeendelea kusisitiza Wakurugenzi katika Serikali za Mitaa kutenga bajeti za uhamisho wa ndani katika halmashauri zao ili waweze kuhakikisha mgawanyo wa watumishi ndani ya halmashauri unazingatia ikama na angalau unakuwa reasonable.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutaendelea kutenga fedha kuhakikisha msambao huu pia unakuwa wenye tija zaidi. (Makofi)
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri tuishukuru Serikali kwa kazi ambayo imeanza kwenye vile vijiji vichache viwili ambavyo vilikuwa vimepitiwa na umeme mkubwa, lakini kwa hivi vijiji 47 kwa kuwa tunategemea Mradi wa REA, kazi hii Mheshimiwa Naibu Waziri imekuwa na changamoto kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kupata majibu ya Serikali sasa ni lini kazi za kupelekea umeme kwenye vijiji hivi vyote vilivyobaki itaanza na kukamilika kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa Jimbo la Korogwe?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili kwenye Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko ule wa Kwanza tulipeleka umeme kwenye vijiji, lakini maeneo mengi ya vijiji bado hajafikiwa na kwenye mzunguko huo wa pili tunafikiria kupeleka kwenye kilometa moja kwenye kila kijiji.

Ni upi mpango sasa wa Serikali kwa vile vijiji vya mzunguko ule wa kwanza na ule mzunguko wa pili kukamilisha maeneo yote ya vijiji ili wananchi wa vijiji vyetu waweze kupata huduma hii ya umeme? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika majibu ya msingi kwamba upelekaji wa umeme kwenye vijiji vyote 49 na hivyo viwili tayari kazi imeanza, itakamilika ifikapo Septemba, 2022 na niseme ni kwa Korogwe Vijijini peke yake lakini katika maeneo yote ambayo vile vijiji tulikuwa hatujavipelekea umeme tayari kazi hizi zimeanza na tutahakikisha kwamba ndani ya huo muda tuliousema ambao maximum ni Disemba, 2022 vijiji vyote kama 1,500 vilivyobakia vitakuwa vimepata umeme na tutahakikisha kwamba kila mtu anapata manufaa ya umeme huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika swali la pili ni kweli kwamba mpaka sasa hatujatosheleza kupeleka umeme katika vitongoji vyote kwenye maeneo yote, lakini maendeleo ni hatua, tulianza hatuna kabisa, sasa tumepeleka robo, baadaye nusu, sasa kwenye vijiji tunaenda kumaliza. Niwaahidi tu Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali inayo nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba katika vitongoji pia tunafikisha umeme kwa kadri inavyowezekana, na kama tulivyokuwa tunasema kwenye vitongoji tunapeleka kupitia hiyo REA, lakini huko mradi maalum wa kupeleka umeme kwenye vitongoji unaoitwa densification, lakini pia TANESCO ni jukumu lao la kila siku kuhakikisha wanapeleka umeme katika maeneo hayo, ni wahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tutaendelea kupeleka umeme katika maeneo yote ya nchi yetu ya Tanzania.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru pamoja na majibu mazuri sana kutoka kwa Mheshimiwa Waziri naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Jambo la kwanza jambo hili limekuwa ni la muda mrefu sana na Mheshimiwa Waziri atakuwa shahidi wa jambo hilo pamoja na ahadi hii nzuri ulioitoa Mheshimiwa Waziri ningependa kujua uko tayari baada ya Bunge hili uongozane na mimi kwenda kuzungumza na wananchi wa Hale uwape matumaini ya kuharakisha jambo hili ili wapate ardhi kwa ajili ya kufanya shughuli zao za kilimo?

Mheshimiwa Spika, Swali la pili Wilaya ya Korogwe sehemu kubwa ya ardhi yake ni mashamba makubwa ya wawekezaji wa chai na wawekezaji wa mkonge na maendelezo yake hayaridhishi sana na jambo hili limefanya wananchi wetu kukosa maeneo ya kufanya shughuli za kilimo hasa vijana wamekosa maeneo ya kujiajiri. Je, Serikali iko tayari kukaa pamoja na wawekezaji hawa pamoja na umuhimu wa uwekezaji wao kwenye maeneo haya lakini tufanye mazungumzo ya kuona namna gani ya kumega maeneo kwa ajili ya kuwapa vijiji ili wananchi wapate sehemu ya kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo suala la kilimo? (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Mnzava Mbunge kijana machachari wa Korogwe kama ifuatavyo: -

Kuhusu swali la kwanza, kwenda anauzoefu anajua akiniita naenda tulishaenda na nitakuja na huko na nitafanya yale ambayo tulifanya sehemu nyingine ambazo ulinipeleka. Kwa hiyo, wananchi wasiwe na wasiwasi Mheshimiwa Mnzava akinihitaji kwangu mimi ni agizo nakwenda tu na Waheshimiwa Wabunge wote kama kuna matatizo kama haya mkiniambia ndiyo inanisaidia kupata kazi maana mkinituma ndiyo napata uhalali wa kuja. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mnzava nakuja. (Makofi)

Swali lake la pili; ni kweli una mashamba mengi na ni kweli kwamba kwenye mashamba mengi najua wakati ule wenye mashamba wanapomiliki hasa Kanda hii ya Kaskazini wananchi walikuwa wachache sasa wananchi wameongezeka sana. Kwa hiyo nataka ukitoka hapa muulize Mheshimiwa Mbunge wa Same hapa Mama Kilango akufundishe namna alivyofanya na mpaka na mimi nikaenda kule na moja ya shamba wananchi wakarudishiwa ekari 300. Kwa hiyo uwezekano huo upo kwa sababu mifano tunayo tutakaa na wenye mashamba wanajua kabisa wanataka kuishi vizuri na majirani wao, hawakatai.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge aniorodheshee hao wenye mashamba ni watu gani halafu tupange ratiba tuzungumze nao wanajua hali halisi na wenyewe wanataka kuishi vizuri na wananchi wanaowazunguka kwa hiyo hilo tutafanya, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Serikali iliahidi kufanya mapitio ya usanifu wa ujenzi wa bwawa la umwagiliaji kwenye eneo la Mto Mkomazi kule Korogwe, lakini mpaka leo ahadi hiyo bado haijatekelezwa: -

Napenda kujua, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo ikiwa ni maandalizi ya ujenzi wa bwawa hilo, kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwa watu wa Korogwe?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mnzava. Tulifanya ziara akiwepo Mheshimiwa Waziri Mkuu katika Jimbo lake na tuliahidi kupeleka wataalamu.

Nataka tu nimwambie kwamba Wizara ya Kilimo imepatiwa fedha kwa ajili ya Tume ya Umwagiliaji, OC tumeshapokea. Sasa moja ya eneo ambalo wataalam wetu na wasanifu wanakwenda kulifanyia kazi ni eneo hilo. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie tu kwamba kabla ya mwaka huu wa fedha kwisha usanifu wa bwawa hilo utakuwa umekamilika na tutaliingiza katika plan. (Makofi)
MHE. TIMETHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Barabara ya Magokweni - Maramba – Daluni – Mashewa Mpaka Korongwe ni barabara muhimu sana kwa uchumi na ulinzi na usalama wa nchi yetu; na kumekuwa na ahadi za viongozi za muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, nataka kujua, ni lini Serikali itatengeneza barabara hii kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mnzava, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge atakuwa shahidi, baada ya Bunge tulilomaliza hii barabara, nimeitembelea kuanzia Mabokweni mpaka Korogwe na hasa kutokana na umuhimu wa hii barabara.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha. Hata hivyo, kitu tunachokifanya sasa hivi kwa jinsi ilivyopita kwenye miinuko tutaanza kwanza kujenga barabara katika hali zile zenye changamoto ngumu kujenga vipande vifupi vifupi kwa njia ya lami ili njia ipitike kwa muda wote wakati Serikali inatafuta fedha kujenga barabara yote kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, ninataka kujua ni lini Serikali itakamilisha mradi mkubwa wa maji wa Mwanga, Same, Korogwe ili kusaidia usambazaji wa maji kwenye vijiji vya Kata ya Mtomazi na Mkumbara katika Wilaya ya Korogwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni mradi mkubwa ambao umeshachukua muda mrefu lakini Wizara tunaendelea kutekeleza tunaamini ndani ya muda wa usanifu tunakwenda kukamilisha wa phase hii ambayo tupo. Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana na hongera kwa kuendelea kufuatilia mradi huu muhimu. (Makofi)
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana; pamoja na majibu ambayo nina uhakika hayatawafurahisha wala kuwaridhisha watu wa Korogwe naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, jambo hili ni la muda mrefu sana na muwekezaji huyu hana uwekezaji wowote ambao ameufanya kwenye eneo lile, wapo wafanyakazi wa zamani wanadai, lakini pia wapo wawekezaji wengi wanajitokeza wanakitaka kiwanda hiki.

Nataka Serikali iniambie ni lini sasa zoezi la kurudisha kiwanda hiki rasmi itakamilika ili kuwezesha uwekezaji mwingine?

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili; kwa kuwa kuna malalamiko ya madai waliokuwa wafanyakazi kwenye eneo lile na kiwanda hiki ni muhimu kwa uchumi kwa watu Korogwe. Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari baada ya Bunge hili, Wizara ya Viwanda inayosimamia Sera, Ofisi ya Msajili wa Hazina na watu wa Maliasili waliokuwa wanakisimamia kiwanda hiki, tufanye ziara kwenda Korogwe tukazungumze kule namna nzuri ya kukikwamua kiwanda hiki kiweze kuwasaidia watu wa Korogwe? Nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Thimotheo Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Thimotheo Mnzava kwa vile ambavyo anafuatilia sana maendeleo ya jimbo lake hususan katika sekta ya viwanda.

Mheshimiwa Spika, ni kweli jambo hili limekuwa la muda mrefu kama alivyosema tangu mwaka 2018 na kimsingi kama unavyojua kwa viwanda vyote ambavyo vilikuwa vimebinafsishwa kulikuwa na mikataba ambayo lazima Serikali iwe na uhakika inavyofanya urejeshwaji wake ili kusiwe na matatizo mengine ya kuingia utata kati ya wawekezaji hawa. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu za kisheria zikikamilika mapema iwezekavyo uwekezaji mpya katika kiwanda hiki utafanyika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la lake pili, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge sisi kama Wizara ya Viwanda na Biashara, Serikali ina nia ya dhati kuhakikisha tunakwamua au tunaendeleza sekta ya viwanda. Tutaambatana baada ya Bunge hili tutawasiliana ili tuweze kufanya ziara na kuongea na wananchi wa Korogwe Vijijini ili tuone namna gani ya kusaidia kufufua kiwanda hiki muhimu kwa ajili ya maendeleo ya Jimbo la Korogwe Vijijini. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru pamoja na majibu ya Serikali naomba kuuliza swali dogo moja tu la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kazi kubwa sana iliyofanywa na Serikali ya kuboresha bandari ya Tanga na kwa sababu bandari ya Tanga kuwa na eneo dogo, ujenzi wa bandari kavu kwenye eneo la Korogwe ni jambo muhimu sana. Ni lini sasa Serikali itafanya hiyo tathmini ili kuwezesha bandari kavu kwenye eneo la Mji wa Korogwe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Kwa sasa Serikali inaboresha na imewekeza sehemu kubwa sana kuboresha bandari ya Tanga ili kuweza kupokea mizigo na kusafirisha mizigo mingi. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi tulikuwa bado eneo la Korogwe halijabainishwa kuwa eneo la kujenga bandari kavu, na ndiyo maana Serikali imesema baada ya kupata hilo wazo la Mheshimiwa Mbunge ambaye kazi yake kubwa pia ni kuishauri Serikali tumelichukua na tutafanya tathmini ili tuone kama eneo hilo litafaa kujenga bandari kavu ambayo itakuwa na tija na endelevu, ahsante.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Kama alivyosema, kituo hiki ni kikongwe, hakuna ufinyu wa eneo. Kwa kuwa kutoka kituo hiki mpaka kituo kingine cha hadhi kama hii ni kilomita 50: Serikali haioni sasa ni vizuri kwa dharura ikawaonea huruma watu wa Bungu, angalau kuwajengea jengo la upasuaji au jengo la mama na mtoto ili kuwasaidia wananchi hasa akina mama na watoto? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; wakati tukiwa tunasubiri hizo fedha na taratibu nyingine zote zikamilike, wananchi hawa wanateseka: Ni lini Serikali itapeleka gari la uhakika la wagonjwa ili kuwasaidia wananchi wa Bungu, kutoka Bungu kwenda mpaka Korogwe Mjini kilomita 50 kupata matibabu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kituo hiki cha Afya cha Bungu kiko katika eneo lenye ukubwa wa ekari mbili, lakini standards zetu za vituo vya afya ni angalau ekari kumi na Serikali imefanya tathmini kwa aina ya uchakavu mkubwa wa kituo kile cha afya, haitakuwa na tija kuweka fedha za kukarabati kituo kile. Ni vema kujenga kituo cha afya ambacho kitaendana na ramani za kisasa. Bahati nzuri kituo hicho kinajenga ndani ya Kijiji kile kile cha Bungu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimtoe shaka Mheshimiwa Mbunge kwamba kituo cha afya kitajenga katika kijiji kile na Halmashauri itaanza kutenga fedha katika mwaka ujao wa fedha mpaka kitakapokamilika.

Mheshimiwa Spika, pili, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kununua magari ya wagonjwa. Niwahakikishie Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe pia itapelekewa gari la wagonjwa ndani ya mwezi ujao. Ahsante.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Serikali ilituahidi kwamba mwezi wa Saba tungepata consultant kwa ajili ya Bwawa kubwa la Mkomazi, lakini mpaka leo kuna ukimya. Je, ni lini ahadi hii itatekelezwa?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mnzava, kuhusu Bwawa la Mkomazi yeye mwenyewe anafahamu hivi karibuni timu ya Wizara ya Kilimo ilikuwepo kule na tatizo lililokuwepo katika suala la Mkomazi, design iliyokuwa imefanyika toka awali na zile skimu zilizoko maeneo yale ilikuwa ina makosa. Kwa hiyo, wataalam wa Wizara wamefanya kazi ya kwanza kwa ajili ya kwenda kutembelea na kuangalia na nimuahidi tu yeye na wananchi wa jimbo lake, kwamba next financial year ya 2023, Bwawa la Mkomazi litakuwa kwenye miradi itakayojengwa na Wizara ya Kilimo kwa ajili ya eneo hilo na skimu zote zilizoko katika ukanda ule ambazo ziko saba.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa zaidi ya miaka Sita wananchi wa Korogwe wanalia na shamba la Mwakinyumbi lililotelekezwa na Serikali imekuwa ikituahidi lakini hakuna matokeo. Mheshimiwa Waziri ni nini sababu inayoifanya Serikali ishindwe kulifuta shamba la Mwakinyumbi na kuwarudishia wananchi wafanye shughuli za uzalishaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mnzava Mbunge wa Korogwe swali lake kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli juu ya shamba hilo ambalo limetajwa na Mheshimiwa Mbunge taarifa zimeshafika Wizarani na taratibu za kiutawala kwa ajili ya kulitwaa shamba hilo na kulirudisha kwa wananchi zinaendelea na tutakapo kuwa tayari tutakupa taarifa za kina juu ya jibu la maombi ya wananchi wa Korogwe.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kama ilivyo kwa hospitali kongwe, tuna vituo vya afya vikongwe na chakavu sana kama Kituo cha Afya cha Gungu kilichopo Korogwe. Ni lini Serikali italeta mkakati wa ukarabati na kuboresha vituo vya afya vya siku nyingi na chakavu ili kuwapa huduma wananchi wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshemiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mnzava Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba Serikali imefanya tathmini ya vituo vya afya chakavu vyote nchini kote na mpango unandaliwa kuhakikisha vinakarabatiwa na vinakuwa bora kwa ajili ya utoaji wa huduma za afya. Kwa hiyo, kituo hicho pia kitapewa kipaumbele. Ahsante.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kuhusu ujenzi wa barabara ya kutoka Maramba kwenda Humba kwenda Mlalo. Ni ipi kauli ya Serikali juu ya kipande cha kuunganisha kutoka Maramba - Mashewa kwenda Old Korogwe mpaka Korogwe Mjini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara aliyoainisha ipo kwenye mpango wa kukamilisha usanifu wa kina wa barabara aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge inayoanzia Old Korogwe hadi Mabokweni kama nimemwelewa. Nadhani ndiyo hiyo barabara; ipo kwenye ukamilishaji wa kufanya usanifu ili iweze kuanza kwa kiwango cha lami baada ya kukamilisha usanifu. Ahsante.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kama tutakwenda na majibu haya mpaka wakati wa bajeti, hali itakuwa tete hapa. Pamoja na hayo naomba kuuliza swali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umekuwa ukifanyika kwa awamu na tayari kipande cha kwanza kimekamilika na kipande cha pili kiko asilimia 81. Serikali haioni sasa ni vizuri kuanza pia ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami, kwa awamu kwa vipande tukianza na bajeti inayokuja mwaka 2022/2023?

Mheshimiwa Spika, Pamoja na ahadi hizo za barabara ya lami, Serikali imekuwa ikijitahidi kutenga fedha kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa barabara hii pamoja na barabara ile ya Korogwe - Magoma kwenda mpaka Maramba. Lakini matengenezo yamekuwa yamekuwa yakifanyika kwa kuchelewa sana lakini pia kifusi kinachowekwa kinakuwa hakina ubora unaoendena na mazingira tuliyokuwa nayo. Na hivi tunavyoongea sasa hivi barabara ya kwa Shemshi haipitiki kwa sababu vifusi havijasambazwa; ni nini kauli ya Serikali juu ya wakandarasi hawa wanaofanya kazi chini ya kiwango na kuwasababishia wananchi wetu matatizo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFRY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inafanya usanifu wa kina wa barabara hii yote aliyoainisha Mheshimiwa Mbunge, ya kutoka Soni, Bumbuli, Dindira hadi Korogwe ili gharama halisi iweze kufanyika na tuone kama kutakuwa na ulazima wa kuwa na loti moja ama mbili. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa tukishakamilisha usanifu wa hiyo barabara tuona namna ya kuanza kuijenga hiyo barabara; na ni azma ya Serikali kuijenga barabara yote hii kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, na kuhusu barabara aliyoitaja ya pili, ambayo inaanzia Korogwe, Bombo Mtoni, Maramba hadi Mabokweni, barabara hii inapita kwenye sehemu nyingi ya miinuko. Kwa kawaida arabara kwa kawaida nyingi ambazo zinapita kwenye miinuko zinaoshwa na mvua, tumewaagiza mameneja, wa mikoa waweze kuainisha maeneo yote korofi, ili tutafute namna ya kudhibiti maeneo yote yaliyo bondeni na kwenye miinuko ili tuweze kutafuta utaratibu muhimu wa kuweza kudhibiti hayo maeneo ikiwa ni pamoja na kuweka lami nyepesi ama zege ama strip za mawe ambazo tunahakika barabara hizi zitakuwa na uwezo wa kuitika kwa muda mrefu bila kuitika.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tangu mwaka 2019 mpaka sasa watu watatu wamethibitika kufa kwa sababu ya tembo kwenye kata za Mkomazi na kata za Mkumbara kule Korogwe Vijijini na sasa hivi tunapozungumza hali ya uharibifu wa mazao ni kubwa sana. Ni upi mkakati madhubuti wa Serikali kuhakikisha kwamba tunawasaidia wananchi wetu kudhibiti tembo na wanyama wengine wasiendelee kuathiri mazao lakini na maisha ya wananchi wetu? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Timotheo Mnzava Mbunge wa Korogwe Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali la yote nimpongeze Mheshimiwa Mbunge. Ni kweli wiki iliyopita tu tulikuwa tuna changamoto ya tembo ambao walivamia katika maeneo ya mashamba ya katani na mashamba ya mipunga, lakini tulipeleka askari.

Changamoto iliyopo ni kwamba wale askari walikuwa ni wachache. Lakini nimuahidi Mheshimiwa Mnzava wananchi wa Korogwe zoezi linalofuata sasa hivi ni kwamba tumeamua kutafuta askari wa ziada ambao tutakuwa tunawaajiri kwa muda ili kuongeza nguvu katika maeneo ambayo yana changamoto ya wanyama wakali ili hawa wananchi katika kipindi cha mwezi wa nne mpaka wa saba waweze kuvuna mazao yao bila tatizo. Hili naliweka ni commitment ya Serikali tunaenda kulitekeleza mara moja.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, ni upi mkakati wa Serikali kuhakikisha unaharakisha na kukamilisha kupelekwa kwa umeme kwenye vijiji vya Wilaya ya Korogwe kwa sababu mkandarasi wake anasuasua sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mnzava, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli mkandarasi anayepeleka umeme kwenye Wilaya ya Korogwe pamoja na nyingine mbili anazembea sana na tumekubaliana achukuliwe hatua na itakapofika katikati ya mwezi huu kama atakuwa hajafikia yale makubaliano tuliyofikia basi hatua stahiki zitachukuliwa ikiwemo pamoja na kuvunja mkataba wake ambao ameshindwa kuutekeleza kwa wakati.
MHE. TIMETHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ukizingatia kwamba kazi ya upembuzi na usanifu ulikamilika muda mrefu: Ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kuijenga kwa lami barabara ya kutoka Korogwe – Dindira – Bumbuli mpaka Songwe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mnzava, Mbunge wa Korogwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema ni kweli barabara hiyo ni muhimu na ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tusubiri bajeti tutakayoisoma, naamini kuna mapendekezo ya kuianza kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami. (Makofi)
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushuru. Wananchi wa Kata ya Mazinde kwa kushirikiana nami Mbunge wao tumeshirikiana kujenga Kituo cha Polisi mpaka boma limekamilika. Je, ni lini Serikali itatusaidia kumaliza Kituo hicho cha Polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, kupitia bajeti ya mwaka 2023/2024, tutaona uwezekano wa kupata fedha kutoka Mfuko wa Tuzo na Tozo kukamilisha Kituo cha Mazinde ambacho Mheshimiwa Mbunge amekizungumzia.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Bei hii inayosemwa imepanda sasa ilikaa zaidi ya miaka mitano bila kupanda, wakati kwenye Soko la Dunia bei ilikuwa ikipanda ukiacha kile kipindi cha Covid-19: Ni upi mkakati wa Serikali sasa angalau kufanya mapitio kila mwaka ili kuhakikisha kwamba tunawasaidia wakulima wa nchi hii wakiwemo wakulima wa Tarafa ya Bungu kule Korogwe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Moja ya njia ya kusaidia kupanda kwa bei ya chai ni kuwa na mnada wa kwetu Tanzania. Mheshimiwa Waziri, Serikali ilituahidi tangu mwaka 2019, ukiwa Naibu Waziri, kuanzisha mnada wa chai Tanzania, lakini mpaka leo mnada huo haujaanzishwa: Ni nini kauli ya Serikali juu ya kuanzisha mnada wa chai ndani ya nchi yetu ya Tanzania?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei iliyodumu kwa kipindi cha miaka mitano ni bei ya shilingi 312. Kikao cha wadau kilichofanyika mwanzoni mwa mwaka huu ndicho tulichobadilisha bei na kuipeleka kuwa shilingi 366 kwa maana ya bei ya chini ya chai. Sasa hivi katika baadhi ya maeneo, hasa maeneo ya Nyanda za Juu Kusini wakulima wanauza chai grade one mpaka shilingi 420. Kwa hiyo, mabadiliko ya bei yamefanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ambalo tunalifanya kwenye eneo la bei, Serikali inapitia mfumo mzima wa uchakataji na importation ya chai kutoka nje ili kuvifanya viwanda vya ndani na kuongeza consumption ya matumizi ya chai ya ndani na kuvipunguzia baadhi ya tozo mbalimbali. Mtaona kwenye bajeti itakapokuja Wizara ya Fedha, mtaona mabadiliko katika eneo hilo ili kuvifanya viwanda vya blending vya ndani viweze kutumia zaidi chai ya ndani na kupunguza importation ya chai kutoka nje na kuvitengenezea soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mnada. Nataka nilihakikishie Bunge lako, ni kweli, dhamira ya Serikali toka mwaka 2019 ilikuwa ni kuanzisha mnada, lakini nilihakikishie Bunge lako kwa uwezo wa Mungu, mwaka huu mnada utaanza. Tumeshakamilisha masulala ya miundombinu, tumeshakamilisha eneo la maabara, tumeshakamilisha mwongozo, na sasa hivi tuko hatua za mwisho kwa ajili ya kusajili ma-broker wa Kimataifa ambao watashiriki kwenye trading kwa sababu, uuzaji wa chai una utaratibu wake.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Je, ni lini Serikali itakikarabati Chuo cha Ufundi Music ambacho kiko Korogwe ambacho ni kikongwe na kimechakaa sana?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava Mbunge wa Korogwe kama ifuatavyo:
-

Mheshimiwa Spika, tunafahamu uwepo wa chuo hiki cha FDC pale Korogwe, na katika nchi yetu tuna vyuo 54 vya FDC ambavyo vingi sana ni vya muda mrefu. Tumeanza kufanya ukarabati tangu mwaka 2020/2021 katika bajeti ile na tumeweza kuvikia vyuo 35 kufanya ukarabati pamoja na upanuzi. Nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, katika bajeti yetu hii ya 2023/2024 tunakwenda kuvifikia vyuo 21 vilivyobaki kikiwemo na hiki cha Korogwe.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Kata ya Mpare yenye vijiji vinne na chanzo kizuri cha maji hakuna kijiji hata kimoja chenye maji. Ni lini Serikali itatatua changamoto ya maji kwenye Kata ya Mpare?

Swali la pili, mradi wa maji wa Goha, Mkumbara mkandarasi wake amekuwa akisuasua na kwa muda mrefu kazi zimesimama. Pamoja na maelekezo uliyotoa Mheshimiwa Waziri hakuna kinachoendela. Ni nini kauli Serikali juu ya mradi huu? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayofanya, lakini kubwa ambalo nataka nimhakikishie hasa katika hii Kata ya Mpare katika bajeti yetu hii ambayo tunakwenda 2023/2024 tumezingatia ombi lake katika kuhakikisha wananchi wanapata maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya mradi huu ambao Mkandarasi ana suasua nilishafanya ziara Korogwe, moja ya maelekezo ambayo tumeyatoa mkandarasi yule aondolewe mara moja pale site na kazi ile tutaifanya kupitia wataalam wetu na kuweza kukamilisha kazi kwa wakati. (Makofi)
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Pamoja na kutengewa fedha, shilingi milioni 900 hali ya hospitali ile ni mbaya na fedha hiyo ni ndogo. Serikali iko tayari kuwaahidi wananchi wa Handeni Mjini kwamba itaendelea na utaratibu wa kupoteza fedha hizi kila mwaka ili hospitali hii ifanyiwe ukarabati yote? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Wananchi wa Handeni Mjini, kama walivyo wananchi wa Korogwe Vijijini, wamejenga sana zahanati, maboma yamesimama na hayajakamilika; Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inayamalizia na kuyakamilisha maboma yote ya zahanati nchini ambayo wananchi wameyajenga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya nyongeza, la kwanza kwamba fedha ni ndogo; fedha hii inatengwa na Serikali kuhakikisha wanafanya ukarabati wa yale majengo ambayo yalikuwepo toka zamani. Kwa mfano, nikisema kwenye Hospitali hii ya Handeni Mjini, wao walitaka kujenga hospitali mpya kabisa ya wilaya, lakini fedha iliyotengwa ilikuwa ni kwa ajili ya ukarabati wa majengo yaliyopo. Tutaendelea kutafuta fedha na kuhakikisha kwamba tunaendelea kupeleka fedha kwenye Halmashauri hizi kwa ajili ya ukarabati zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili la kumalizia zahanati, nyote ni mashahidi humu ndani, katika majimbo yetu na Halmashauri zetu, Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imekuwa ikileta fedha shilingi milioni 50 za kumalizia zahanati na tutaendelea kutafuta fedha, na kadri ya upatikanaji wa fedha hizo basi tutaendelea kuleta katika majimbo hayo kuweza kumalizia zahanati ambazo zimejengwa kwa nguvu ya wananchi.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu ya Serikali nina mswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, barabara hii ni mihimu sana, ndiyo barabara fupi na rahisi kuunganisha Kijiji cha Msomela Kijiji cha mfano, na barabara kubwa ya Segera - Arusha. Sasa kwa sababu ya umuhimu huo;

Je, ni lini Serikali itakubali kuipandisha hadhi barabara hii iwe barabara ya Mkoa ihudumiwe na TANROADS, barabara hii pamoja na zile barabara nyingine kama ile ya Msambiazi - Lewa - Lutindi na barabara ya Kwetonge – Tonge – Kizara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Mvua zinazonyesha sasa hivi Korogwe zimeathiri sana barabara zetu za changarawe;

Je, Serikali iko tayari kuwapa TARURA fedha za dharura ili wakatusaidie kurekebisha hali ya barabara zetu kwenye maeneo ambayo yameathiriwa na mvua?
NAIBU WAZIRI, 0FISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikubaliane na Mheshimiwa Mnzava kwamba barabara hii ni muhimu sana na barabara hii pia imetajwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025 Ibara ya 55(c)(4) katika ukurasa wa 77. Hivyo ni kipaumbele cha Serikali kuhakikuisha barabara hii inajengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kupandisha hadhi taratibu ziko wazi za kisheria, inatakiwa wao kule waaanze katika vikao vyao vile vya DCC itoke pale ipite katika kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa, na ikitoka kwenye Bodi ya Barabara ya Mkoa waende wapitishe kwenye RCC na iwasilishwe kwa Waiziri mwenye dhamana na TANROADS ambaye ni Waziri wa Ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili; fedha za dharura kwa TARURA, tayari Serikali inaliangalia hilo na tayri ilikuwa bajeti yao TARURA wao kwa mwaka ya dharura ilikuwa ni bilioni 11. Hivi sasa tunaangalia namna ya kuweza kuwaongezea fedha Kwenda mpaka bilioni 43 ili kuhakikisha kwamba wana fedha ya kutosha ya dharura kwa ajili ya ujenzi wa barabara wakati wote; ije mvua lije jua barabara ziwe zinapitika na ndiyo maana Serikali pia imeiongezea TARURA bajeti kubwa sana kutoka bilini 226 mpaka bilioni 776.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; moja ya njia ya kutoa bei nzuri isiyotetereka ya zao la mkonge ni kuwa na nyuzi bora, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri. Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi yake ya kununua mashine za kuchakata mkonge, ili mazao ya mkonge, nyuzi zinazochakatwa ziwe na ubora ukizingatia kwamba, tuna changamoto kubwa ya uhaba wa mashine?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; katika kuimarisha soko la ndani, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, Serikali ilitoa agizo la kuzuia uingizaji wa kamba na nyuzi za plastic, lakini mpaka leo hali bado sio nzuri. Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya kudhibiti uingizaji wa nyuzi na kamba za plastic kwenye nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya maeneo ambayo tunatilia mkazo ni kuwa na teknolojia sahihi ya kuzalisha bidhaa mbalimbali, ikiwemo nyuzi zinazotokana na mkonge. Katika jitihada hizo tumeshaweka bajeti kwa ajili ya kununua mashine hizo za kisasa ambazo ziliahidiwa, lakini zaidi kupitia taasisi zetu za ubunifu, TEMDO, kuna mashine inaandaliwa ambayo nayo itasaidia kuchakata mkonge, ili kupata nyuzi bora na zenye tija kwa ajili ya kuhakikisha tunapunguza uingizaji wa nyuzi mbadala za plastic kutoka nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuzuia uingizaji wa nyuzi za plastic kama unavyojua ni kweli, bado mahitaji ni makubwa zaidi ya bidhaa hii kuliko uwezo wa kuzalisha wa ndani, kadri tunavyoendelea kuimarisha uzalishaji wa nyuzi za mkonge naamini tutapunguza hilo gap na pale tutakapokuwa tumejitosheleza, maana yake hii marufuku itaisha ili kuhakikisha hatuagizi tena nyuzi za plastic kutoka nje, nakushukuru. (Makofi)
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, pamoja na kutengewa fedha kwenye bajeti, bado hakuna hatua yoyote ambayo imeanza mpaka sasa.

Ni lini Serikali itaanza taratibu za ujenzi wa barabara ya lami ya kutoka Korogwe – Dindila – Soni mpaka Bumbuli? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, barabara hii anayoitaja Mheshimiwa Mbunge tumeitengea bajeti, kwa maana ya utekelezaji wa mwaka huu wa fedha, tayari tender documents zinaendelea kuandaliwa ili barabara hiyo iweze kutangazwa kwa ajili ya kuanza ujenzi. (Makofi)
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa, kwenye nchi yetu majira yanatofautiana: Je, Serikali haioni umuhimu wa kuiruhusu na kuielekeza TARURA juu ya muda wa kutangaza na kutekeleza miradi kwa kuzingatia majira ya maeneo husika? (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, TARURA inatangaza kazi zake hizi kote nchini mara baada tu ya bajeti yao kuidhinishwa. Ni kama hivi sasa bajeti ya Shilingi bilioni 776 imeidhinishwa na Bunge lako Tukufu, hivyo katika mwaka mpya wa fedha unaoanza mwezi Julai mwaka huu 2023, ndipo kazi zote zitaanza kutangazwa.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, ujenzi wa barabara za lami kilometa tatu kwenye Mji wa Mombo ni ahadi ya Serikali iliyotolewa na Mgombea wa Urais wa Chama cha Mapinduzi mwaka 2015 na ikarejewa mwaka 2022. Kazi inayoendelea haiathiri ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami, nataka kujua, ni lini ahadi hii ya Serikali kwenye Mji wa Mombo itatekelezwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Wilaya ya Korogwe ni eneo muhimu sana kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo, kilimo cha mkonge lakini Tarafa ya Bundi kilimo cha chai: Ni lini Serikali itaiingiza Wilaya ya Korogwe kwenye mradi ule mahususi wa miundombinu kwenye maeneo ya uzalishaji na maeneo ya kilimo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Timotheo Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini, la kwanza hili kwamba barabara hii ya lami ni ahadi ya Serikali, nikiri kwamba ni ahadi ya Serikali na kwamba tutaendelea kuipa kipaumbele kwa sababu iliahidiwa na Kiongozi Mkuu wa Nchi alipopita katika eneo la Mombo. Tutaendelea kutafuta fedha na tutaona ni namna gani katika mwaka wa fedha huu tunaoenda kuuanza ni nini kinaweza kikafanyika na Serikali kuweza kuendelea kutekeleza ahadi hii ya viongozi wakuu wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili kwamba kule kuna uzalishaji mkubwa kuingiza katika miradi mbalimbali mingine, nimtoe mashaka, Korogwe vijijini ipo katika mradi ule wa bottleneck removal ambao unakwenda kujenga madaraja na vivuko mbalimbali katika maeneo tofauti hapa nchini, ikiwemo kule kwake Mheshimiwa Mnzava, Korogwe Vijijini. Najua alichokuwa anataka ni kwamba Mkoa wa Tanga wawekwe katika Mradi wa Agri-connect, lakini mradi huu wa Agri-connect upo katika Southern Highlands, mikoa yetu ya nyanda za juu kusini tu, na wao Korogwe wapo katika hii bottleneck removal kwa vijijini; kwa Korogwe Mjini, kwa Dkt. Kimea kule, wamo katika TACTIC na Tanga Mjini vile vile wapo katika TACTIC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya ukarabati na matengenezo ya barabara mbalimbali kule Korogwe Vijijini.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali ambayo ni ya jumla sana, naomba kuuliza swali dogo moja tu la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, maeneo ambayo yanataka kumegwa kutoka kwenye vijiji ambavyo nimevitaja ni maeneo makubwa na tayari pande zote za vijiji zina miundombinu muhimu kama vile shule na zahanati na kuna ahadi ya viongozi wakiwemo Mheshimiwa Waziri Mkuu. Ni lini, Serikali itavigawa vijiji hivi ili kurahisisha shughuli za maendeleo na kuwasogezea wananchi huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kama ambavyo ametoka kusema Mheshimiwa Mnzava hapa, kwamba kama maeneo haya tayari yana miundombinu muhimu kwa ajili ya kukidhi vigezo vile vinavyotakiwa kuwepo kwa ajili ya kugawa vijiji vipya, basi tutatuma timu katika maeneo hayo ili kuweza kufanya tathmini hiyo na kisha baada ya thathmini hiyo tutakaa na wataalam pale kwetu Ofisi ya Rais - TAMISEMI na kisha kuona ni namna gani tunaweza kuwapatia vijiji hivyo kwa sababu tayari maeneo hayo yameshakidhi vigezo vile vinavyotajwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Serikali kwa muda mrefu sana imeahidi kuhusu ujenzi wa bwawa kwenye Bonde la Mto Mkomazi. Je, ni lini ahadi hii sasa itaanza kutekelezwa rasmi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo Mnzava, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli utekelezaji wa mradi wa Bonde la Mto Mkomazi umekuwa ni wa muda mrefu na Mheshimiwa Mbunge amekuwa akifuatilia sana, nataka nimhakikishie mbele ya Bunge lako Tukufu ya kwamba ifikapo mwezi wa Saba taratibu za awali za kumpata mshauri mwelekezi zitafanyika ili kazi ya usanifu na upembuzi yakinifu uanze na baada ya hapo tutaanza utekelezaji wa mradi huu mkubwa ambao wananchi wa Korogwe wanausubiri kwa hamu kwa sababu unagusa zaidi ya Kata 11 na una manufaa makubwa sana. Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge tutaanza mwezi wa Saba mapema kabisa kumpata mshauri mwelekezi. (Makofi)
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza vituo hivi vitatu vya Bungu, Magoma na Mombo ni vituo vya muda mrefu na vinahudumia eneo kubwa; ni lini sasa hiyo tathmini inafayofanya na Serikali itakamilika ili Serikali ipate nafasi ya kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya maboresho?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, vituo hivi nilivyovitaja karibu kila kituo kimoja kinahudumia tarafa nzima, kata zaidi ya tisa. Zipo kata ambazo tumeziainisha kwa ajili ya vituo vya kimkakati; ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya vituo vya mkakati kwenye Jimbo la Korogwe Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba vituo hivi vya afya vitatu ni vituo vya siku nyingi na Serikali tayari tulishapeleka wataalamu kufanya tathmini ili kuona majengo yanayohitajika, lakini na gharama ambazo zinazohitajika. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakamilisha mapema iwezekanavyo ili Serikali iweze kutafuta fedha kwa ajili ya kwenda kuongeza majengo yanayopungua katika vituo hivi.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu na vituo vya afya vya kimkakati, Serikali imeshaainisha maeneo yote nchini kote ambayo yanahitaji vituo vya afya vya kimkakati ikiwemo kwenye Jimbo la Korogwe Vijijini na fedha zinatafutwa kwa ajili ya ujenzi kwa hatua kadri ya upatikano wa fedha, ahsante sana.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Kwa kuwa, shughuli nyingi za maendeleo zinazofanyika vijijini zinafanywa na wananchi wenyewe na vijiji vingi ni vikubwa kiasi kwamba kumekuwa na mivutano. Serikali haioni kwamba ni wakati sahihi sasa angalau wa kufanya mgawanyo wa vijiji ili shughuli za maendeleo vijijini ziendelee kufanyika vizuri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mnzava, mchakato wa kuanzisha maeneo ya utawala ya Mikoa, Wilaya, Tarafa, Kata na Vijiji ni mchakato unaofanywa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na taratibu zilizopo. Wao wanatakiwa waanzishe wenyewe mchakato ule kupitia vikao vyao na kama ni katika ngazi ya Wilaya wanalipitisha kwenye DCC kisha inakwenda Mkoani kwenye RCC na ndipo mapendekezo yanaletwa.

Mheshimiwa Spika, lakini kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi, kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele katika kuyaendeleza yale maeneo ambayo ni mapya ya kiutawala.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naishukuru Serikali kwa kazi ambayo imefanyika kwenye barabara hii.

Nina maswali mawili ya nyongeza; swali la kwanza; barabara hii ni muhimu sana, barabara hii pamoja na barabara za Kwetonge – Donge - Kizara, barabara ya Mombo - Mzeri, barabara ya Makuni - Zege Mpakani zimeunganisha Wilaya ya Korogwe na Wilaya ya jirani.

Ni lini Serikali itatimiza ile ahadi yake ya kuzipandisha hadhi barabara hizi kuwa kwenye hadhi ya barabara za mkoa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, barabara nyingi zinazosimamiwa na TARURA ni za changarawe na udongo na zinahitaji matengenezo ya mara kwa mara. Serikali haioni sasa ni wakati sahihi kununua vifaa kwa TARURA kila mkoa ili matengenezo madogo madogo ya barabara yafanywe na TARURA wenyewe kwa kutumia wataalam wao wa ndani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, najibu maswali mawili ya Mheshimiwa Timotheo Mnzava; la kwanza hili la barabara hii kupandishwa hadhi, barabara ambazo ametaja Mheshimiwa Mnzava taratibu ziko wazi kwa mujibu wa sheria. Vikao vile vya kisheria lazima vikae, wanaanza kwanza wao kwenye DCC vinatoka vinakwenda kwenye Bodi ya Barabara ya Mkoa na kisha wanamuandikia Waziri mwenye dhamana ya barabara hizi za mikoa yaani TANROADS kuomba kupandisha hadhi. Tutafuatilia kuona maombi hayo yamefikia wapi kwa ajili ya kuweza kupandisha hadhi barabara hii kwa wenzetu wa Wizara ya Ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la mitambo, TARURA kuweza kununua mitambo. Tayari mkakati wa Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kutoa fedha kwa wenzetu wa taasisi ya TARURA kuweza kununua mitambo hasa katika maeneo ambapo upatikanaji wa mitambo ni mgumu. Tayari mpango huu umeanza kufanya kazi kule visiwani Mafia. Maeneo mengine ni pembezoni mwa nchi yetu ambapo tayari wameanza na kadri ya upatikanaji wa fedha tutazidi kufanya hivyo ili mitambo ile iweze kutumika wakati wa dharura.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, vijana waliokuwa wanatekeleza zoezi hili, walilifanya katika namna isiyo ya kistaarabu, namna ya kinyanyasaji na ya kuwaumiza na ya kuwaharibia na ya kuwafilisi katiba wajasiriamali wetu. Nataka nijue kama haya yalikuwa ni maelekezo ya Serikali?

Swali la pili, kwa sababu maeneo yote ambayo yameathirika kuanzia Bwiko – Segera – Hale, yana maeneo ambayo yanafaa kwa shughuli za kibiashara kwa kuzingatia taratibu za kiusalama. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amesema shida ni vibali na mpangilio, Serikali iko tayari kutoa maelekezo kwa TANROADS Mkoa wa Tanga ili tukae nao waone namna ya kuwapanga vizuri wajasiriamali hawa kwenye barabara ili Watanzania wapate nafasi ya kujipatia riziki na kipato chao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wote wa Serikali wanatakiwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu. Kama hilo lilitokea kwa upande wa Korogwe wakati zoezi hilo linafanyika, si maelekezo ya Serikali na halikubaliki kwani Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejipambanua kutoa haki na watumishi wa Serikali kuwatumikia wananchi kwa heshima na siyo kwa kuwanyanyasa ama kwa namna nyingine yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama hilo lilitokea hayakuwa maelekezo ya Serikali. Pengine nitumie nafasi hii kuwaelekeza Mameneja wote na watumishi wote wa Wizara ya Ujenzi, kuhakikisha kwamba wanatoa huduma kwa watumishi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu pia kwa kuheshimu haki na heshima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge kwamba kama yako maeneo ambayo yanastahili na yanaweza kupewa vibali, basi nimwombe Mheshimiwa Mbunge na nimuagize Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga, waweze kukutana na Mbunge na wananchi ili waweze kuainisha maeneo ambayo wanadhani yanaweza yakapata vibali ili mradi tu hayataathiri usalama na shughuli za kawaida za kutumia barabara ya TANROADS, ahsante. (Makofi)
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, kwa zaidi ya miezi miwili sasa Viwanda vya Chai vya Ambangulu na Dindira vimefungwa na wananchi hawana maeneo ya kupeleka chai. Ni nini Kauli ya Serikali kuwasaidia wananchi hawa, ili waweze kuendelea na shughuli zao za kilimo na uzalishaji? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ni kweli tunafahamu changamoto ambayo Mheshimiwa Mbunge ameieleza na kwamba, Wizara ya Kilimo tumeshawaandikia wawekezaji wote akiwemo mmiliki wa Kampuni ya Mohamed Enterprise kwanza kufungua hicho kiwanda.

Mheshimiwa Spika, pili, tunaendelea na mazungumzo kama ambayo tunafanya katika Halmashauri ya Lupembe kuhakikisha kama ameshindwa uendeshaji. Maana yake viwanda hivi sisi kama Serikali tutakuwa tayari kumlipa fidia ili kuvirejesha kwa wananchi ili waweze kuviendesha wenyewe kupitia vyama vya ushirika. Ahsante sana.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, Serikali iliahidi na ikawaambia wananchi watumie nguvu zao kuhakikisha wanajenga kituo cha afya, wamejenga wameweka wodi mbili pamoja na OPD.

Je, kwa kuwaambia hivyo Serikali haioni kwamba inawasumbua wananchi na kuwakatisha tamaa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa kuwa wamekwisha kujenga sehemu ambayo ni ndogo na Kata ya Solwa ina wakazi 32000; je, Serikali itawafidia kujenga sehemu nyingine kwa gharama zote za Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Solwa kwamba Serikali inathamini sana kazi kubwa waliyofanya kwa nguvu zao kwa ujenzi wa Jengo la OPD na wodi.

Mheshimiwa Spika, kwa standard za Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa sasa zahanati pia zinakuwa zina wodi, lakini sababu kubwa eneo ni dogo, ekari 1.5 ni ndogo sana kujenga kituo cha afya kwa sababu tunatazama miaka 50, 100 ijayo. Kwa hiyo, niwahakikishie kwamba zahanati hiyo ambayo wamejenga itasajiliwa, itaanza kutoa huduma kama zahanati na kuendelea kutoa huduma hizo, lakini Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kujenga kituo cha afya katika eneo ambalo Mkurugenzi ameelekezwa kulitafuta kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya, ahsante.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati kwenye maeneo ya Mashoa na Vugiri kwa sababu haya yamekidhi vigezo na tumeyaainisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kwamba kila mwaka wa fedha kila bajeti inapotengwa tunatenga vituo vya afya vya kimkakati na vinaendelea kujengwa kwa awamu nchini kote. Kwa hiyo, tutahakikisha kwamba katika Jimbo la Korogwe Vijijini pia tunatenga fedha hizo kwa ajili ya kujengo vituo hivyo vya afya vya kimkakati.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itakamilisha Mradi wa Maji wa Mwanga – Same – Korogwe ili kuzisaidia Kata za Mkomazi na Mkumbara ambazo ziko mwishoni mwa mradi huo? Nakushukuru (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mnzava, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi Mheshimiwa Waziri Jumaa Aweso alikuwepo Kilimanjaro na alikuwa kule kwa ajili ya kuhakikisha kwamba miradi ya maji iliyoko katika Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na Tanga inakamilika kwa wakati. Nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwa niaba ya wananchi wake, miradi hii itakamilika ndani ya mwaka huu wa fedha.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Moja ya njia ya kutatua changamoto ya barabara iliyoulizwa kwenye swali la msingi ni kutumia barabara mbadala ambayo ni ya kutoka Korogwe kupita Dindila – Bumbuli mpaka Soni. Kwenye bajeti Mheshimiwa Waziri aliahidi kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Mpaka leo kuna ukimya, ni ipi kauli ya Serikali juu ya jambo hili?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakiri Mheshimiwa Mnzava amekuwa akifuatilia barabara hii ambayo ni mbadala kama alivyosema. Ni kweli na kwenye bajeti hii ya Mwaka wa Fedha 2024/2025, tumetenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mnnzava pamoja na wananchi wake, kwamba kwa vile tumeiweka kwenye bajeti maana yake ni kipaumbele kwa upande wa Serikali na tuko kwenye hatua za kutekeleza bajeti hii. Kwa hiyo, fedha zitakapopatikana tutaijenga barabara hii ili iweze kuwahudumia wananchi lakini pia iwe kama mbadala wa ile barabara ya kwenda Bumbuli kutokea Lushoto. Ahsante sana.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, yako maeneo ya vijiji ambayo mpaka sasa hayaunganishiwi umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 badala yake wanaunganishiwa kwa shilingi 320,000. Mfano ni eneo la Manyata Kata ya USA River kule Arumeru Mashariki. Je, nini kauli ya Serikali juu ya jambo hili?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Wilaya ya Korogwe mpaka sasa kazi ya kuunganishiwa umeme wa kilometa mbili, pamoja na ujenzi wa vile vitongoji 15 haijaanza. Ni lini kazi hii itaanza kwenye Wilaya ya Korogwe, Jimbo la Korogwe Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la kwanza la hili eneo la Manyata - USA River, maeneo yote ya vijiji, umeme unaunganishwa kwa shilingi 27,000 labda isipokuwa maeneo haya ni maeneo ya mamlaka ya Mji mdogo ambayo yanatambulika kama mitaa.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, niendelee kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wote kuwa, maeneo yote ya vijijini, ada ya kuunganisha umeme ni shilingi 27,000. Kwa hiyo, tutaangalia eneo hili la Manyata ambalo lipo USA River, kama wanachajiwa zaidi ya hapo na ni eneo la vijiji, basi tutachukua hatua ili kuhakikisha wanarudi kwenye shilingi 27,000; lakini kama ni eneo ambalo liko kwenye Mamlaka ya Mji Mdogo, basi ndiyo maana ada yake inakuwa ni shilingi 321,000.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na mkandarasi ambaye yupo Korogwe, tayari Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu alitoa maelekezo kwa mkandarasi kutoa commitment ya kumaliza mradi kwa wakati kwa sababu alikuwa anasuasua. Tayari imeshafanyika hivyo na ndani ya wiki hii tutasaini na mkandarasi ili aanze kupeleka umeme katika kilometa mbili kwenye Jimbo la Mheshimiwa Mbunge, ahsante.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, ni upi mpango wa Serikali kuharakisha utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28 ili Kata za Mswaha na Mji wa Korogwe na maeneo mengine, yatatue changamoto kwa wakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, Mradi wa Miji 28 kwa upande wa Mkoa wa Tanga, unaojumlisha Handeni, Muheza, Korogwe pamoja na Pangani wenye jumla ya shilingi 170,000,000,000 umefikia wastani wa 32%. Juzi nilikuwepo kule nimetoa maelekezo kwa wakandarasi kuharakisha mradi huu kwa sababu hakuna changamoto ya kifedha. Kwa hiyo sisi kama Serikali tumeelekeza mradi huu usiwe nyuma ya wakati ili wananchi wa maeneo hayo wapate huduma ya maji safi na salama, ahsante sana.